Simulizi : Dunia Rangi Rangire
Sehemu Ya Pili (2)
Asubuhi na mapema walianza tena safari, walisafiri mchana kutwa. Walipita sehemu iliyokuwa kama jangwa, haikuwa na miti isipokuwa miba na miamba hadi wakafika katika msitu mkubwa. Ilipotimu saa tano usiku walifikia nyumba iliyokuwa katikati ya msitu mnene, Moris akamwambia Kibe,
"Tumefika, nisubiri hapa, niende nikaangalie kama huyu jamaa yupo".
Geti lilikuwa limefungwa, akaamua kupanda ukuta ili aweze kuingia ndani, aliporuka ukuta akakutana na mbwa wakali, wale mbwa wakaanza kubweka huku wakitaka kumrarua.
Lio akiwa chumbani kwake, akachukua bastola yake, akahakikisha kuwa ina risasi, akaenda dirishani kuchungulia nje, akaona jamaa aking'ang'ana kupambana na mbwa, akaamua kutoka kupitia mlango wa nyuma, akanyata hadi alipomfikia yule jamaa, akamwwekea bastola ya kisogo na kumwambia,
"Leo utajua kilichomtoa Kanga manyoya". Moris aliposikia sauti ya Lio, akacheka,
"hahaha, Lio, Lio, Lio"
Lio baada ya kugundua kuwa mtu aliyevamia nyumba yake ni boss wake, naye akacheka kisha akamwambia,
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Boss, una bahati niliamua kutoka, maana nilitaka niiachie risasi nikiwa ndani, bahati hukuwa katika tageti, imekuaje unafika saa hizi, halafu unaruka ukuta?"
Moris akavuta pumzi ndefu kisha akasema,
"Nilijua umelala, naninavyokujua huwa ukilala kuamka ni shughuli pevu, ndiyo maana nikaamua kuruka ukuta, hawa mbwa kidogo wanitoe roho."
"wanakufahamu hawa, walikuwa wanakutisha tu ili na mimi nitoke huko ndani, hujanijibu kuwa wafanya nini hapa saa hizi?"
"Kuna dogo nimemleta, afanye kazi huku."
"Kila idara mbona ina watu wa kutosha?"
"Mweke kule kwenye vinu, baadaye ukiona kuwa ni kijana mwaminifu, unaweza ukamhamisha na kumpeleka kitengo kingine, huyo dogo nimemtoa kwa mkuu, yeye ndiye aliyeniambia nimlete".
"Sasa yuko wapi?"
"Nimemwacha hapo nje ya geti, yupo garini"
Morisi akafungua geti na kwenda kuingiza gari, walipofika ndani, Morisi akamwambia Lio,
"Lio, huyu ndiyo dogo mwenyewe, anaitwa Kibe, Kibe huyu anaitwa Lio, atakuwa boss wako hapa, yeye ndiye msimamizi wa shughuli zote huku."
Baada ya Kibe kusalimiana na Lio, Lio akamwambia,
"Natumaini utakuwa mchapakazi mzuri, maana huwa sipendi watu wavivu, kama wewe ni mvivu, ujue kazi za huku hazikufai," Kibe akajibu,
"Kazi ndiyo niliyoifata huku, kwa hiyo ni jukumu langu kufanya kwa bidii hilo lililonileta hapa."
Lio akamgeukia Moris, "Huko mlikotoka si mmekula?"
Moris akatabasamu kisha akasema,
"Kwani wewe ni mgeni wa barabara ya kujia huku? huo mgahawa au hoteli itakuwa inaendeshwa na nyani au sokwe? Maana hao ndiyo waliojaa njia yote."
"Haya boss, nilifikiri mmepika huko njiani, ngoja niangalie cha kufanya."
Lio akaenda jikoni kwake na kurudi akiwa amebeba sahani mbili zilizojaa wali na nyama, moja akampa Moris na nyingine Kibe, akawaambia, "Hiki ndicho kilichopo, kwanza ni bahati tu niliamua kupika kingi, msiposhiba mtajazia na maji."
"Tutashiba na hii nyama ni aina gani?" hayo yalikuwa maneno ya Moris.
"We kula, usitake kujua ni aina gani ya nyama, ulifikiri tunafuga huku?".
"Nafahamu kuwa hakuna mfugo hapa, nilitaka tu kujua ni aina gani ya nyama pori?"
"Hiyo ni nyama ya swala"
"Ooh! ndiyo maana tamu sana, bado umebakisha nyingine?"
"Una maana gani, si nimekuambia hakuna chakula kingine zaidi ya hicho?"
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Namaanisha kuwa kama una akiba ya nyama ya swala anigawie kesho nikiondoka nipeleke kwangu."
"Hiyo utapata, lakini imekaushwa."
"Safi sana, hiyo ndiyo nzuri, ukiipika hiyo uiunge vizuri na tui zito la nazi halafu upate na ugali mlaini na pilipili, hapo utatolewa mezani"
"Hahaha, unapika mwenyewe? Au kuna shemeji anayekupikia?"
"Shemeji atoke wapi bwana, nilipokuwa mdogo mama yangu alinifunza kupika, kwa hiyo nafurahia kupika nikitumia ujuzi nilioupata toka kwa mama yangu."
Wakati wote huo Lio alipokuwa anaongea na Moris, Kibe alikuwa kimya huku akimchunguza Lio alivyo, Lio alikuwa pandikizi la mtu, mweusi na alikuwa na mapengo, meno matatu au manne ya mbele hayakuwepo, halafu alikuwa ametoboa sikio la kushoto na alikuwa amevaa hereni, mkono wake wa kushoto alikuwa amechora nge.
Kibe akaanza kuingiwa na wasiwasi baada ya kumwangalia na kumchunguza Lio kwa muda, akawa na mawazo kuwa pengine hawa watu wanajihusisha na biashara haramu maana kama ingekuwa halali, kwa nini inafanyika katikati ya msitu mnene, ila hakutaka kuonyesha hofu yake maana japo hajakaa na Lio kwa muda mrefu, roho yake haikuwa na imani dhidi ya Lio, alimuona kuwa ni mtu ambaye anaweza kumtoa mtu roho.
Baada ya kumaliza kula, Kibe akaonyeshwa sehemu ya kulala, huku akiambiwa kuwa kesho yake ndiyo atapelekwa katika kituo chake cha kazi. Baada ya kupanda kitandani, akafumba macho na kuomba mizimu ya kwao imlinde na chochote kibaya. Asubuhi na mapema, Lio alimwamsha Kibe, akamwonyesha maji ya kunawa uso, kisha akapewa uji.
"Kaka Moris yuko wapi?" Kibe alimuuliza Lio.
"Ameondoka kitambo sana, amesema anataka awahi kufika mjini maana kuna kazi nyingi sana zinamsubiria, maliza uji haraka twende maana saa zinakwenda. Alipomaliza kunywa uji, Lio akamwambia Kibe atoke waende, wakapanda gari aina ya Land Rover kisha wakaelekea juu mlimani, Kibe akamuuliza Lio,
"Hicho kituo cha kazi kipo mbali sana?".
"Ukienda kwa gari siyo mbali sana, ila kwa mguu ni mbali kiasi".
"Sasa nikishaanza kazi, nitakuwa nafikaje huko kwa wakati? Kama mtu akienda kwa mguu ni mbali."
"Utakuwa unakaa hukohuko pamoja na wenzako."
Walipofika juu mlimani, Kibe akaona nyumba zilizojengwa kwa miti na kuezekwa kwa nyasi, kisha akaona watu wasiyopungua kumi, kila mmoja akiwa na kinu na mtwangio mkononi huku wakitwanga. Lio akasimamisha gari, akamwambia Kibe kuwa ashuke maana hapo ndipo atakapofanyia kazi.
Wale watu walipoona gari limesimama, wakaacha kutwanga na kulifuata lile gari, kijana mmoja aitwae Twalibe, akamsalimia Lio kasha Kibe, akamuuliza Lio,
"boss, leo mbona umetutembelea asubuhi asubuhi kuna nini?" Lio akafungua mlango wa gari akashuka akasema,
"Nimewaongezea mtu mwingine maana nimeona kazi zinawalemea".
"Tutashukuru sana boss, ndiye huyu?"
"Yah, ndiye huyu anaitwa Kibe, Kibe hawa ni wafanyakazi wenzako, watakuonyesha namna ya kufanya kazi na mtakapo maliza kazi jioni, watakuonyesha sehemu ya kulala, Twalibe, si kuna vinu vya akiba?"
"Ndiyo boss, vipo, ashindwe tu mwenyewe".
"Haya mpeleke umwonyeshe vinu vilipo, kazi iendelee, nitarudi jioni kuangalia mlipofikia".
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Lio akarudi katika gari kisha akaondoka. Twalibe akampeleka Kibe chumba ambacho vinu vimewekwa, wakachukua kinu kimoja na mtwangio wake, Kibe akamuuliza Twalibe,
"Ni kitu gani kinatwangwa?" Twalibe akamjibu,
"Kuna majani fulani huwa yanaletwa hapa kila jioni, kazi yetu ni kuyatwanga kisha jioni boss analeta mengine na kuchukua yale yaliyotwangwa, twende nikakuonyeshe yalipo ili uanze kazi."
Kibe akapelekwa chumba kingi kilichojaa magunia yaliyojaa majani, wakachukua gunia moja na kuelekea sehemu ile ambayo wenzao walikuwa wakiendelea kufanyia kazi.
Wakati wanaendelea kufanya kazi, Twalibe akamuuliza Kibe,
"Kwani wewe umetokea wapi?."
Kibe akamjibu, "nimetokea kijiji kiitwacho SISI KWA SISI, ulishawahi kukisikia?"
"Hapana, mie nimekulia mjini , sijawahi kufika kijijini."
"Kwani ulikosa kazi nyingine huko mjini hadi uje kufanya kazi huku porini?"
"Mie sijasoma, kama mtu umesoma na una vyeti vyako, hapo ndiyo utapata kazi za ofisini, ila watu kama sisi, kazi za mikono ndiyo saizi yetu, si umewahi kusikia kwa mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe?"
"Sawa, sasa haya majani yana kazi gani?"
"Mie sijui na sitaki kujua, ninachojua ni kuwa mwezi ukiisha Napata mshahara, kama haya majani wanauza au la, wanajua wenyewe."
Kibe akaamua kutouliza maswali zaidi, alijua kuwa wakati utafika ambapo majibu ya maswali yanayomtatiza atayapata.
Walifanyakazi hadi muda wa chakula cha mchana ulipofika. Wakati wanaendelea kula, Kibe akamuuliza Twalibe,
"Hiki chakula tunatakiwa tulipie?"
"La hasha, chakula na malazi ni juu ya muajiri, boss hapendi wafanyikazi wake wapate tabu".
"Na mshahara ni mzuri au kiasi kidogo tu".
"Kwa mtu ambaye hana kisomo na ukilinganisha na kazi tunayofanya, zinatutosha kusukuma maisha yetu, ila kwa yule ambaye hana mpangilio wa maisha anaweza kusema hazimtoshi."
Kadiri siku zilizoendelea, Kibe alizidi kuwa na shauku ya kujua yale majani wanayotwanga kila siku yana kazi. Akaamua kujenga mazoea na kijana mmoja kati ya wale waliokuwa wanakuja jioni kuchukua yale majani waliokuwa wakiyatwanga, aliyekuwa anaitwa Fabian. Siku moja baada ya kumaliza kazi, Fabian na wenzake waliwasili kuchua mzigo wa siku hiyo, Kibe akamfata Fabian,
"Mambo vipi Fabi?"
"Ooh mtoto wa sisi kwa sisi, bado upo tu hapa hujaenda kujipumzisha?"
"Nani kakuambia mie rafiki yako?"
"Acha hizo mtu wangu, urafiki si wa kuambiwa, huanza tu wenyewe bila kutambua."
"Nilikuwa tu nakutania, mambo poa kama uonavyo tunawajibika"
"Unajua Fabi, kuna mambo yanasumbua akili yangu, na nafikiri pengine wewe unaweza kunipatia majibu"
"Kama nitakuwa na jibu nitakuambia, ni nini hicho kinachokusumbua?"
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Hebu twende tukakae chini ya ule mti pale," Wakaenda hadi katika mti mkubwa wa Mkwaju , wakakaa katika magogo yaliyokuwa chini ya ule mti. Kibe akakohoa kidogo kisha akasema,
"Kwanza nakuomba uniapie na kuniahidi kuwa haya nitakayokuuliza hutamwambia mtu yoyote," Fabian akamwangalia Kibe kwa sekunde kadhaa bila kusema kitu kasha akatabasam na kusema,
"Kwani unataka kuua mtu hadi uniapishe?"
"Nipo serious Fabi, kuna saa ya utani lakini huu siyo utani,"
"Sawa, naapa kwa jina la Mwenyezimu na jina la Mama yangu aliyenizaa, utakalonieleza litaishia hapa."
"Sawa, jambo lenyewe ni kuhusu hii kazi tunayoifanya."
"Una maana gani ukisema kazi tunayoifanya?"
"Ninamaanisha haya majani tunayoyatwangwa kila siku, yana kazi gani?"
"Nani aliyekutuma kuulizia mambo yasiyokuhusu?"
"Kuuliza siyo ujinga na hakuna aliyenituma, tafadhali kama wajua niambie."
Fabian akakaa kimya kitambo bila kusema kitu huku akitafakari kuwa amwambie Kibe au la na je akumuambia, ataweza kuchunga ulimi wake bila kumwambia yeyote? Kibe alipoona Fabian hasemi chochote, akamwambia,
"Nilifikiri wewe ni rafiki yangu wa kufa na kuzikana ila naona huna imani na mimi, tusahau kama nilikuuliza swali kama hilo."
"Umeniuliza swali ambalo kwangu ni gumu sana na majibu yake siyo rahisi kama unavyofikiria."
"Nilifikiria utanipatia majibu ya mambo yanayo nitatiza kumbe sivyo, nitatafuta majibu toka kwa mtu mwingine."
Baada ya Kibe kusema hayo, akanyanyuka toka pale alipokuwa amekaa na kuondoka. Fabian alipoona Kibe amesimama na kuondoka naye akasimama na kupiga hatua za haraka ili kumfikia, alipomfikia akamshika bega na kusema,
"Nipe muda nitafakari uliyonieleza, ila usije ukamwambia yeyote kuwa umeniuliza swali kama hilo, sawa?"
"Poa, mie sina shida hapo utakapona umefikiri vya kutosha utaniambia."
Fabian akawafata wenzake na kumalizia kupakia mizigo katika gari kasha wakaondoka. Baada ya Kibe kuachana na Fabian, alijaa mawazo, alikuwa akiwaza Fabian alivyosema, na kujiuliza kuwa Fabian alikuwa na maana gani alipomuambia,
‘usifikiri ni jibu rahisi kama anavyofikiria’, ina maana ninavyo hisi kuwa kuna biashara haramu inayofanyika hapa ni kweli?, 'eeh Mungu nipe ujasiri na uwezo wa kufumbua mafumbo kama alivyokuwa mfalme Suleiman'.
Siku ile Kibe alichelewa kwenda kulala baada ya kula chakula cha usiku, alikuwa anawaza namna ya kumshawishi Fabian ili amtegulie kitendawili kile lakini hakupata jibu. Kesho yake Kibe alikuwa wa kwanza kufika katika kituo chao cha kazi, nia yake ilikuwa kuchunguza yale majani wanayotwanga kila siku kama anaweza kuyatambua.
Wakati anaendelea kuchunguza wazo likamjia kuwa pengine yale yalikuwa majani ya bangi, moyo ukamwenda mbio baada ya kukumbuka kuwa kuna siku alihisi harufu ya bangi pale karibu na wanapolia chakula, alipofuatilia akagundua kuwa aliyekuwa akivuta hiyo bangi alikuwa boss wao, Lio. 'kama hii ni bangi, kwa nini inatwangwa?', Kibe aliwaza. Baada ya wenzake kuwasili wakaanza kumtania,
"Imekuaje leo umewahi hivyo?, unafikiri utapandishwa cheo na kwenda kule katika kitengo cha kuchemsha?" Huyo alikuwa kijana aliyeitwa Omondi, akaendelea kumwambia Kibe,
"Wenzako tumekaa miaka mingi hapa lakini hakuna kubadilishwa idara wala nini". Kibe akamwambia,
"Kila wakati huwa nachelewa, leo na mimi nimeamua niwahi, si unajua kuwa ada ya mja hunena , muungwana ni vitendo, hivyo nataka boss ajue kuwa nimekuja hapa kwa shughuli moja tu, 'kazi'.
Wakati wanaendelea na kazi, Kibe akawa anafikiria Omondi alivyosema, 'unafikiri utapelekwa kitengo cha kuchemsha?'.
Wafanyakazi wenzake walikuwa wakiongea na kucheka, huku Kibe akijiuliza, 'hivi bangi inachemshwa?, na kama inachemshwa, inachemshwa ili ifanyiwe nini?'. Wakati wa chakula ulipofika, Kibe akamwona Moris, ilikuwa mara ya kwanza kumuona toka siku ile walipoachana pale kwa Lio, akaenda kumsalimia. Moris akamuambia,
"Yaelekea umeshazoea mazingira".
"Nashukuru nimezoea, je umewahi kumwona Dada Teresia?".
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Nina muda sijaonana nae ila mkuu Bwana Kanjubai alionana nae juzi, akamwambia mwisho wa wiki hii atakwenda kijijini kwenu hivyo kwa kuwa nilikuwa na safasi ya kuja huku, akaniambia nikuone kama una pesa za kuwatumia wazee wako unipatie ili kesho kutwa Alhamisi Teresia akija kumuona Bwana Kanjubai, ampatie".
"Nitakupa kabla hujaondoka."
"Sawa, fanya hivo maana sina muda mrefu hapa, nataka leo hii hii nirudi mjini."
Kibe akakimbia kwenda katika makazi yao kuchukua pesa za kuwatumia wazazi wake.
"Kama utamwona dada Teresia, mwambie awape wazazi wangu salamu zangu."
Kibe alimwambia Moris baada ya kumkabidhi pesa za kuwatumia wazazi wake. Moris akaondoka na kwenda kwa Lio, alipofika akamkuta akipika chakula cha mchana, akamwambia,
"Sasa Lio, mie nataka nirudi maana huu mzigo unatakiwa kama itawezekana, kesho usiku uwe umewasili visiwa vya Komoro."
"Boss, subiri walau msosi uive ule ndiyo uondoke."
"Hapana, hata hivyo nimechelewa, kwani kuna shida yoyote ambayo unahitaji usaidizi?"
"Kwa sasa hakuna ila wakati mwingine utakapokuja, naomba uniletee mifuko ya kupakia mzigo maana iliyopo inakaribia kwisha."
"Hilo halina shida, mafuta taa, asidi na vimiminika vingine vipo vya kutosha?"
"Afadhali umenikumbusha, haidrokloriki asidi, imepungua na ile kama unavyojua ndiyo muhimu zaidi ili kufanya mzigo uwe wa daraja la kwanza, ethanol japo haijapungua saana niyakuongeza pia."
"Poa, hayo nimeyasikia, ikiwezekana kesho usiku hivyo vitu vitaletwa hapa, na usisubiri hadi malighafi ipungue, kuna soko jingine mkuu anafuatilia, hiyo dili ikikubali utafurahi mwenyewe."
"Shaka ondoa boss, unajua hizi shughuli zetu zinatakiwa kujipanga kimaisha wakati muda haujayoyoma".
"Una maana gani? ,usiniambie umeanza kuingiwa baridi."
"Hahaha, mimi Lio, The Lion of Juda, niingie baridi, hilo halitowahi tokea, mie ni mkongwe katika hizi shughuli, nilichokuwa namaanisha nikuwa, twajua ya leo, yakesho hatuyajui hivyo mtu unatakiwa upigane leo ili kuijenga kesho".
"Kwani siku hizi, busara unazitoa wapi?"
"Usitake nicheke boss, kama nisingekuwa na busara unafikiri Mkuu angeniweka sehemu nyeti kama hii?, hapa panatakiwa akili na busara na ujanja pia."
"Ila si unajua kuwa unapoingia katika hizi kazi, ni ngumu kutoka?, na kama ukiamua kutoka huo ndiyo mwisho wa kula ugali hapa duniani?"
"Mbwa hafundishwi kunusa boss, hilo nalitambua kama kiganja change."
"Poa kama walitambua hilo,ngoja mie niwahi,nitakuja baada ya siku mbili, ila kesho hizo malighafi zinazohitajika zitaletwa."
"Poa, safari njema, siku ukija nakuomba uniletee walau kreti mbili za bia."
"We si umezoea kunywa gongo, ukinywa bia siutalazwa hospitali?"
"Utani huo boss, we fanya hivyo ikiwezekana uniongezee na chupa moja ya whiski."
"Poa, kwaheri ila usiwe unakunywa tu pombe hadi usahau jukumu lililokuweka hapa."
"Shaka ondoa, boss."
Moris alipofika mjini, bwana Kanjubai akamuambia ajiandae kwa safari ya kuelekea visiwa vya Anjuani.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Sasa boss, nitatumia usafiri gani?" Moris alimuuliza Kanjubai.
"Kwani wewe iko sahau kuwa nimenunua boti mpya juzi juzi? hiyo ndiyo utatumia, utaandamana na vijana wa kazi, nawe pia usisahau bastola yako, you know just in case yakiharibika, uwe na silaha ya kujitetea."
"Sawa, na huyo jamaa wa huko Anjuani umeshawasiliana naye? Maana nataka
nikifika tu kama mipangilio itakuwa sawa nataka nigeuze."
Je haya ni majaani gani na ni mzigo gani unaopelekwa Visiwa vya Anjuani?..je Moris atafanikiwa?...je nini kitamtokea Moris?....
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment