IMEANDIKWA NA : EMMY JOHN
PEARSON
*********************************************************************************
Simulizi
: Harufu Ya Kifo*********************************************************************************
Sehemu Ya Kwanza (1)
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
UMATI wa watu ulikuwa mkubwa haswa. Nyuso za wana umati zilitawaliwa na faraja badala ya majonzi, furaha badala ya huzuni. Na vicheko badala ya vilio.
Muziki uliendelea kupiga kwa sauti za juu nyimbo za kuhamasisha juu ya wokovu na ahadi tele juu ya mbingu. Wasikilizaji walikuwa wengi lakini walijali sana mdundo kuliko maneno yaliyohusiwa katika nyimbo hizo. Wengine walitikisa vichwa huku na kule huku wengine wakitikisa miguu yao ilimradi tu kuusindikiza wimbo ule ambao baadhi ya mashairi yalionekana kufahamika kwa watu wengi na baadhi walionekana kuyakariri na kisha kufuatisha katika kuyaimba bila kuyatilia maanani.. Labda kwa sababu walihudhuria matukio kama hayo mara kwa mara au huenda mitaani haikupita wiki moja kabla hazijapigwa nyimbo hizo.
Hivyo walizizoea!!
Wahudumu waliokuwa wamevaa nguo nyeupe za kufanana zikiwa na nembo ya hoteli kubwa ya kifahari, waliendelea kupita huku na kule kuhakikisha kuwa nyuso zile za umati zinaendelea kutabasamu kwa kuwapatia maji ya kunywa yaliyokuwa katika makopo maalumu. Wakati wengine wakigawa maji wengine walizikusanya sahani za chakula ambazo zilikuwa zimetumika tayari.
Kwa jinsi mambo yalivyokuwa yanaenda hakika ilimlazimisha mkaaji wa pale kujikuta tu akitabasamu. Mambo yalipangwa yakapangika!! Shughuli ile ni kama ilikuwa imepangwa vile!!
Hakika huduma zilikuwa bora.
Mara muziki ukakatika ghafla na kipaza sauti kikaanza kurindima katika namna ya kutoa taarifa. Mzungumzaji alikuwa mwanaume mnene mfupi na tumbo kubwa!!
“Jamani tusikilizane!!...bila shaka kila mmoja amefurahia chakula sasa ratiba inayofuata ni kuuaga mwili wa marehemu, utaratibu utakuwa kama ifuatavyo. Wataanza wanandugu wa karibu kabisa wa marehemu hawa wataambatana na wanafamilia, kisha baada ya hapo watafuata wanawake na mwisho wanaume watafunga zoezi hili. Tafadhali tufuate utaratibu jamani ili kila mmoja apate nafasi ya kumuaga mpendwa wetu ambaye ametangulia katika haki kutuandalia makazi.” Alimaliza mzee mfupi mwenye kipara cha haja na kitambi cha wastani ambacho hakikuwa cha dhiki. Alisoma maandishi yale kama yalivyokuwa yameandikwa katika karatasi na hakujihangaisha hata kidogo kuumiza kichwa chake!! Utaratibu huu alianza nao na sasa alikuwa anaendelea nao.
Kipaza sauti kilizimwa kisha muziki ukaendelea tena. Muziki ule ule wa kusisitiza wanadamu wapunguze madhambi na kusisitiza juu ya wokovu.
Ama kwa hakika msiba huu ulihudhuriwa na watu sana wa kaliba tofauti tofauti. Watoto, vijana na wazee bila kuwasahau wanawake.
Aliyepoteza uhai alikuwa mtu wa watu haswa. Alikuwa ni tajiri na alikuwa anajitolea mara kwa mara kuwasaidia wale waliomwomba iwapo anacho. Na hata kama hana angeweza kukuongoza mahali ambapo unaweza kukipata.
“Ama kweli wema hawadumu!” mzee mmoja alisema baada ya kuuaga mwili wa marehemu. Kisha akafanya ishara ya swala ya kiislamu!! Akaondoka zake huku akitikisa kichwa.
“Yaani kweli akafia ofisini kwake doh! Dunia gunia kweli.” Mwanamama wa makamo naye alilalamika kivyake. Hakuna aliyemjibu na hata hivyo hakuhitaji jibu!!
“Sijui hata kama kombe la Kagiri litaendelea.” Kijana mwingine mwenye umbo la kimichezo kutoka katika kona nyingine ya umati alimnong’oneza mwenzake.
“Dah halafu kweli ujue mzee alikuwa anasimamia vizuri sana…” yule kijana alijibiwa na mwenzake kisha wakajilazimisha kutabasamu. Huku wakielekea upande mwingine wa umati, bila shaka walikuwa wanajaribu kuikwepa kamera iliyoanza kuwamulika kutokea mahali fulani.
Wakati vijana wale wakihamia upande mwingine kuna mwanaume mmoja aliyekuwa amevalia kofia ya pama na pensi iliyouzidi mwili wake akiwa ameyaziba macho yake kwa miwani nyeusi alikuwa makini kutazama kila kitu kilichokuwa kinaendelea katika msiba huo. Yeye hakusema neon lolote lakini kichwani alikuwa na mambo mengi sana. Hakuna ambaye angeweza kuyatatua bali yeye mwenyewe.
Hata ulipofika wasaa wa kuondoka kuelekea makaburini, alijipakiza katika pikipiki yake na kuungana na msafara, yeye akawa kati ya watu wa mwanzo kabisa kufika eneo la tukio. Akaiegesha pikipiki yake mahali salama, akaifunga vyema kiusalama!!
Maeneo ya Kinondoni makaburini.
Hata alipofika maeneo yale alijiweka katika pembe ambayo angeweza kushuhudia mambo mengi ikiwezekana yote ambayo yanatokea katika shughuli ile. Labda yangemfaa katika utatauzi wa haja yake.
Kila mtu alijikita katika jambo lake na hakuna ambaye alijihangaisha kujiuliza yeye ni nani na anafanya nini pale. Pilikapilika ziliendelea za kuandaa lile kaburi ambalo kama ni nyumba basi ingekuwa ya kifahari sana. Hakika liliandaliwa nalo likaandalika. Kama nilivyosema awali shughuli hii ni kama iliandaliwa mapema!!
Laiti marehemu angepewa nafasi walau ya kuamka mara moja atazame mahali ambapo atahifadhiwa kwa siku ile basi angelala kwa hiari yake huku akiwashukuru wale wabunifu wa kaburi lile. Lakini haikuwezekana ainuke tena, tayari alikuwa maiti.
Maiti ambayo ilikuwa inaondoka lakini huku nyuma ikiacha maswali mengi, lakini si maswali pekee bali na utata ndani yake!!CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Utata uliofanywa siri na wale walioujua kijuujuu.
Kweli waliamua iwe siri ilimradi tu yasizuke maswali mengi hapo baadaye!! Na siri hiyo hawakuipa uzito hata kidogo, maana ilionekana kuwa siri ya kawaida.
Kama ilivyokuwa upande wa kuaga huku napo ratiba ilionyesha kuwa wanandugu ndio watakaotangulia kumwaga michanga katika kaburi. Kisha watu maalum na baadaye wanawake na mwisho wanaume!
Kiongozi wa kidini alichukua nafasi yake akaanza kuwasisitiza watu juu ya kujiandaa kabla siku ya kiama haijafika. Aliwakumbusha kufanya toba na kusameheana huku wakiweka akilini jambo moja kuwa hakuna aijuaye siku wala saa. Maneno aliyoyasema yaliigusa kila nafsi na hivyo kuzua kimya kinene, hata yule kijana mwenye kofia ya pama alijikuta akishtushwa na kuguswa haswaa na maneno yale. Haikuwa mara ya kwanza kuyasikia maneno yale lakini uwasilishaji wa kiongozi huyo wa kiroho uligusa katika namna ya kipekee, kijana mwenye kofia ya pama akajikuta katika kuijutia nafsi yake na akakumbuka kuwa na muda mrefu sana bila kuhudhuria nyumba za ibada!
“Bwana Lameck Kagiri ametangulia leo, nasi hatujui kesho yetu itakavyokuwa. Leo tunamuombea Lameck lakini nasi kesho tutafukiwa hivi hivi. Wanadamu sisi ni mavumbi na mavumbini tutarudi. Basi kwa muda huu kila aaminiye kuwa Mungu aliye hai anasikiliza kilio chake basi aungane nami katika sala hii kwa ajili ya marehemu ndani ya jeneza” Ukafika muda wa kuomba dua ya mwisho kwa ajili ya marehemu ndani ya jeneza. Kila mmoja akajikuta akiweka ishara za imani yake. Huku wengi wakifumba macho.
Kijana mwenye kofia ya pama akiwa vilevile katika hatia akafumba macho yake ambayo yalikuwa yamefunikwa na miwani nyeusi ya jua. Aliamini kuwa hata kwa siku hiyo kumkumbuka Mungu italeta maana sana kuliko kuendelea kuwa dhambini.
Sala ikachukua dakika takribani kumi kabla ya kumalizika na kila mmoja kujibu kwa sauti kubwa hivi ‘AMEN’.
Hapo mwili ukaingizwa kaburini huku mama mmoja mwenye asili ya kizanzibari akilia kwa uchungu mkubwa huku watoto wawili wa kike na mmoja wa kiume wakiungana naye katika kilio hiki. Pembeni walikuwepo watu wengine wasiokuwa na uchungu kwa ajili ya kuwabembeleza wafiwa hawa!
Hawa ndio walikuwa ndugu wa karibu kabisa wa marehemu Lameck Kagiri. Mke na watoto wake watatu.
Wakati familia ikijongea katika kaburi kwa ajili ya kutupa michanga kwa ishara ya kukubaliana na kauli ya mwanadamu ni mavumbi na mavumbini atarudi mara kijana mmoja ambaye alikuwa anaenda kuambatana na wanandugu wa karibu alianza kupiga kelele akilalamika kuwa anapatwa na maumivu makali ya tumbo ghafla, alilia kwa sauti kuu huku akijisongasonga huku na kule kama namna ya kujaribu kukabiliana na maumivu yale. Mwanzoni alivumilia kweli kiume lakini sasa alilia mithiri ya mtoto mdogo kabisa.
Ukiona mtu mzima analia amini kuwa amefikwa!! Huyu bwana alikuwa analia kwa uchungu mkubwa!! Waliomsikia kilio chake walibaki kumpapasa huku na kule na kumuuliza maswali magumu ambayo hakuweza kuyajibu.
Kijana mwenye kofia ya pama alishuhudia tukio la kijana yule kulalamika, na alimuona tangu wakiwa katika kuaga mwili wa marehemu, na hata katika pitisha pitisha macho hapa na pale katika ibada ya kumwombea marehemu aliweza kumuona japo hakumtilia maanani kama ambavyo hakuwatilia maanani watu wengine ambao hakuwa na mashaka nao.
Macho yake yalijikita zaidi katika kutazama wanawake hasahasa waliojivika hijabu na nikabu. Aliamini kuwa katika hijabu na nikabu anaweza kujihifadhi mwanaume ambaye anaweza kuhatarisha jambo lolote, ama anaweza kuwa msaada kwake katika kupata ufumbuzi wa siri ambayo alikuwa anakabiliana nayo.
Tukio la kuumwa tumbo lilionekana la kawaida na akataka kuyapitisha macho yake. Lakini akavutika jinsi mwanaume yule alivyokuwa akijikunja kunja.
Bora angekuwa mnyonge angeweza kumtafsiri kama ‘mtoto wa mama’, lakini huyu alikuwa mkakamavu sana. Japo alikuwa ndani ya vazi la suti bado alionekana kuvimba kifua haswa.
Maumivu ya tumbo ndo yampeleke vile? Alijiuliza kijana mwenye kofia ya pama kisha akajiuliza iwapo huyu anaweza kuwa kati ya anaowahitaji. Akaamua kufuatilia kwa ukaribu!
Akaruka na kulipita kundi la watu, hatimaye akafika jirani kabisa na yule kijana ambaye alikuwa katika sekunde za mwisho kabisa kujaribu kupambana na hali iliyokuwa inaendelea katika mwili wake. Alikuwa anakosa muhimili na kuwaegemea watu waliokuwa jirani naye, sasa alianza kurusha mikono huku na kule mithiri ya mtu mwenye kifafa. Watu waliogopa hali hii wakaanza kurudi nyuma kumkwepa, alinyoosha mkono kama anayeomba msaada lakini hakuweza kunena lolote.
Mara akaanza kutokwa na mapovu, macho yaliyokuwa yamepoteza nuru mara yakafumbuka waa! Waliomkaribia kwa mara nyingine wakatimua mbio huku yowe la hofu likiwatoka
Kiongozi wa kiroho alikuwa katika wakati mgumu, alibakia kaburini peke yake na hapakuwa na dalili yoyote ya utulivu. Alijaribu kutumia kinywa chake kuwatuliza watu lakini hakuna aliyekuwa msikivu tena.
Alibaki akiwa ameduwaa, kitabu cha kidini mkononi na michanga mikononi. Ni kama alikuwa ameamriwa kuganda na kubaki vilevile.
Umati ulikuwa umezagaa haswa.
Yule kijana akajitupa chini kwa nguvu, macho yakiwa yamekodolewa vilevile. Na mara yakabenjuka, boliti nyeusi ikapotea njia na kukimbia kuelekea inapojua yenyewe.
Waa!! Macho yakawa meupe pee!! Alitisha kumtazama. Na ni kama alikuwa anatokwa na uhai, ulimi nao ukamtoka kama mbwa mwenye hasira ka kung’ata. Akinamama wakatimua mbio huku wakipokezana namna ya kushtuka. Kanga ziliwaanguka na umoja ukatoweka rasmi. Mikoba yao ikawa mizito, wale wenye miili minene walifurahisha kuwatazama jinsi walivyokuwa wakikimbia na kudundika kama wanamaanisha kufurahisha watu, lakini walikuwa katika kuokoa uhai wao kutoka katika hofu wasioyoijua hata kidogo.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wanawake bwana!!
Mara kijana mwenye kofia ya pama akafika, akaduwaa kidogo lakini hakuruhusu hali ile ya kuduwaa iendelee. Akamvamia yule mtu na kumkamata vyema shingo yake iliyokuwa ikijilazimisha kugeuka katika namna isiyokuwa ya kawaida kwa mwanadamu yeyote. Kwa namna aliyomkamata ni kama alikuwa akijaribu kumtoa uhai, watu waliokuwa wamesaliwa na ujasiri kidogo walipiga mayowe kumtuhumu yule bwana kuwa ni muuaji!!
Akasimama upesi, akakabiliana na umati uliokuwa katika mchanganyiko wa hofu, uoga na kupagawa. Akajipekua na kuibuka na kitambulisho. Akaitoa kofia yake ya pama.
“Polisi kutoka kituo cha kati, muwe na amani..kuna tatizo hapa. Tulieni msipagawe!” Aliongea upesi upesi huku akikipunga kitambulisho chake hewani, hakuna aliyejihangaisha kukisoma. Kusikia neno polisi liliwatosheleza, na hata namna alivyokuwa amenyoa nywele zake ulikuwa ushahidi tosha.
Wakaachana naye, wale waliokuwa wamekimbia wakaanza kurejea huku wengine wakiondoka moja kwa moja. Huku wengine waliposikia kuwa yule ni askari wakatoweka kimyakimya kuukwepa ushahidi!!
Askari yule mpelelezi akawa makini, akatoa glovu katika pensi yake kubwa kumzidi, wakati anatoa mara bunduki ndogo nayo ikamtoka bahati mbaya ikaanguka.
Wacha wee! Umati ukapagawa na kupiga mayowe ya hofu. Wale waliokuwa wamejivika ujasiri na wao wakakodoa macho.
Yule askari akawa mwepesi kuificha tena bunduki ile akavaa glovu zake, na kisha moja kwa moja akaingia katika mifuko ya suruali ya yule mhanga wa tumbo ambaye alikuwa ametulia tuli. Mapovu yakiendelea kumtoka mdomoni
Moyo ukaripuka kwa mchanganyiko wa wasiwasi na furaha baada ya kuweza kukisoma kikaratasi kile. Kama alivyohisi awali alikuwa sahihi lakini akajutia uzembe wake. Kuna msichana alikuwa pamoja na kijana yule tangu wakiwa nyumbani kwa marehemu lakini sasa hakumuona pale, ni sura hii alitakiwa kuitambua ili aweze kuanza upelelezi wake. Ni sura ile inahusika na kikaratasi kile!!
Akakisoma tena vyema kikaratasi kilichokuwa ndani ya suruali ile ya yule bwana, mwandiko uleule na ujumbe uleule.
Lakini ukiwa na tofauti kidogo tu katika namba.
“BADO SITA.” Ulisomeka hivi, wakati ule uliokuwa katika mfuko wa shati la marehemu Lameck kagiri ambaye mwili wake ulikuwa umeingizwa kaburini lakini ukiwa bado haujafukiwa ulisomeka ‘BADO SABA’.
Ujumbe huu ulibaki kuwa siri!! Siri kwa wachache waliouaona!! Wakapuuzia na sasa ujumbe huu unapatikana katika mwili mwingine. Siku ya maziko ya Lameck Kagiri.
Muuaji alikuwa anahesabu kurudi nyuma, na alikuwa makini huku akiwa na uhakika na kitu alichokuwa anafanya.
Sawa alikuwa anaua!! Lakini huu ujumbe alihitaji nani ausome haswa. Maana mtu hawezi tu kuandika bila kuwa sababu ya kufanya hivyo, tena ni katika tukio zito kabisa la mauaji, hapa lazima palikuwa na jambo.
Ajabu ni kwamba Inspekta anayeheshimika sana alikuwa akilipuuzia. Inspekta Seleli hakujali kabisa na ni yeye aliyewasihi Gasto na wenzake wasitilie maanani kile kiujumbe.
“Waandishi wa habari si mnawafahamu, jambo dogo watafunga misafara hapa na kusumbuana kila kukicha tena vile wamepewa uhuru nd’o hatupumui. Utawasikia ooh!! Gaidi laua jeshi la polisi lafumbia macho. Hawana maana hao.” Gasto aliyakariri maneno ya Inspekta Seleli akayapima uzito wake na kuyaona kuwa kwa namna moja yana maana lakini kwa namna nyingine yalikuwa ya kujitia uzembe.
Sasa limetokea jingine, ujumbe wa mauaji!!
Kijasho chembamba kikamtoka Askari mpelelezi Gasto Mushi. Mkazi wa Kahama ambaye alikuwa jijini Dar es salaam kikazi. Akilitumikia jeshi la wananchi Tanzania.
Hakumshirikisha yeyote kuhusiana na jambo hilo bali alikitunza kile kikaratasi katika mojawapo ya mifuko yake kisha akawapisha watoa huduma ya kwanza ambao walikuwa tayari eneo hilo baada ya kupigiwa simu!!
Haya yote yalitokea ndani ya dakika tano tu!
Mazishi yakaendelea…..huku wazikaji wakiwa na hofu juu ya tukio lililotokea. Wengine wakiwa wametoweka jumla na kujiepusha na jambo hilo. Mchungaji naye hakuzungusha maneno mengi kwa sababu tayari mwili ulikuwa kaburini. Familia ilimwaga michanga kisha kaburi likasakafiwa na mafundi waliokuwa wakingoja muda ufike wa kufanya hivyo.
Wakati wanatoka makaburi ya Kinondoni mtu mmoja mwenye kiherehere na kupenda kujua mengi tayari alikuwa na taarifa kutoka hospitali. Wazikaji wakasimama wakamzunguka awape taarifa ya kilichoendelea huko hospitali.
Karama Nassoro alikufa hata kabla ya kufikishwa hospitali. Na kwa taarifa zaidi ni kwamba inawezekana alikufa palepale makaburini. Sumu kali inayoua mara moja iliondoka na uhai wake, hivyo ni aidha alikufa kwa kunywa ama kunyweshwa sumu.
Mpekunuzi akatoa taarifa, kila mmoja akaondoka akiwa na lake kichwani. Wengine wakidai kuwa huenda cheo alichopandishwa kazini basi wabaya watu wamemroga!! Wapo wengine waliosema huenda alikuwa muathirika wa Ukimwi na alikuwa akibadilisha damu mara kwa mara. Ilimradi tu kila mtu na lake!!
Msiba ule ukawa wa aina yake kuwahi kutokea!!
Wakasimuliana vijiweni na katika familia zao.
*****
KIFO cha Lameck Kagiri, diwani mstaafu na mwalimu mkuu katika shule ya sekondari ya Zimbu iliyopo jijini Dar es salaam kilionekana kuwa cha kawaida sana kwa wakazi wa jiji. Wengi wakiegemea upande wa umri wake hivyo wakahusisha matatizo ya mkandamizo wa damu aidha mkandamizo wa juu ama chini.
Lakini kukutwa kwa alama za vidole katika mikono yake, usoni na kidogo begani mwake hii ilimaanisha kuwa aliguswa kabla hajapoteza uhai. Hivyo kwa polisi hakikuwa kifo cha kawaida hata kidogo!!
Ilikuwa aidha Lameck alikufa kwa kuzibiwa hewa asipumue ama vinginevyo lakini sio kwa kifo cha maradhi ya kawaida.
Alama za vidole zikapimwa na kugundulika kuwa ni za mwanamke. Mwanamke asiyefahamika ubini wake. Hili nalo likawa tatizo jingine. Inspekta Seleli anawaambie vijana wake kadhaa wasahau na wasijihusishe juu ya habari ya kifo kile kutokuwa kifo cha kawaida. Japokuwa aliyekufa alikuwa ni Lameck, swahiba wa Inspekta lakini bado hakutaka suala hilo lichukuliwe uzito. Naam!! Wakatii amri. Na kuamua kusahau. Lakini Gasto hakusahau kirahisi. Alitaka kuthibitisha kuwa kile hakikuwa kifo cha kawaida.
Anaamua kuhudhuria mazishi.
Wakati imeruhusiwa Lameck azikwe linatokea tukio jingine, hili la sasa ni sumu kali sana, inayoua upesi.
Hii ikaondoka na uhai wa Karama Nassoro, rafiki na kama ndugu katika familia ya marehemu mzee Lameck.
Cha kustaajabisha alama za vidole katika mwili huu zilikuwa za mwanaume, lakini ujumbe ulikuwa uleule na mwandiko uleule. Tofauti ilikuwa moja tu. Namba.
Huku ikiwa ni sita na huku kwingine ikiwa ni saba.
Ni Gasto tena sasa akiwa yeye kama yeye anaamua kulivalia njuga suala hili, anafikisha ripoti yake kwa Inspekta Seleli, ukaribu wao huwa wanauweka mbali linapokuja suala la kazi.
Gasto anaelezea juu ya kifo cha Karama Nassoro katika namna ya kushangaza, hawezi kuwa alijia bali aliuliwa na muuaji yule alikuwa palepale msibani. Gasto akaenda mbali zaidi na kuelezea juu ya kumwona marehemu akiwa karibu sana na msichana ambaye hakuonekana tena baada ya mauaji.
“Mara yako ya mwisho kumuona alikuwa na marehemu nyumbani au hata makaburini.” Aliuliza Inspekta.
“Waliandamana kotekote lakini wakati anaugulia tumbo hakuonekana tena.”
“Na hao madaktari wanaodai kuwa pipi nd’o kitu chake cha mwisho kula!! Uliiona?”
“Hapana, sikuiona. Ujue sikuwa nafahamu litakalojiri hivyo nilikuwa naangaza huku na kule, huenda walipeana bila mimi kuona.” Alijibu tena kwa nidhamu.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Gasto!!..lakini si tulisema hili jambo linaishia pale ama labda hukunisikia vizuri bwana mdogo!!” aliuliza kipole sana Seleli huku akijikuna kwa kutumia kalamu yake.
Gasto akakosa cha kujibu kwa muda kisha akazungumza,
“Nilienda kumzika bamdogo Lameck.”
“Kwa hiyo kwa sasa unataka nini katika hii kesi”
“Kama ni sawa niendelee kufuatilia nijue kuna nini hapa katikati.” Alijibu kikakamavu. Inspekta akamtazama katika namna ya kumwonea huruma huku macho mengine kama yakimkataza kufanya hicho alichotaka kufanya.
“Mh! Haya jaribu tuone lakini sikushauri hata.” Alimaliza kwa kubetua midomo yake.
Gasto alishamzoea tayari, hakutikiswa! Akaandaliwa na kukabidhiwa rasmi jukumu hilo la upelelezi huku akitakiwa kufikisha taarifa kwa Inspekta wa kituo chake.
Bwana Mathias!!
Kila upelelezi huwa una mahali pake pa kuanzia na yule anayekumbwa katika upelelezi aidha anakuwa muhusika ma la! Hii haijalishi na inaitwa kuwasaidia polisi upelelezi.
Marko alikuwa ni mmoja wa wahanga wa maafa haya ya upelelezi, ni yeye ambaye alama za vidole kutoka kwa marehemu zilimtaja kuwa aligusana naye kwa mara ya mwisho, hivyo hata kama ni pipi basi ni yeye anayejua kuwa nani alimpa. Kiuhalisia hakuwa muhusika wa jambo lile lakini alitetemeshwa na iwapo kuna lolote aweze kusema. Lakini hakuwa akijua lolote na zilikuwa zimepita siku tatu tangu augulie mahabusu huku dhamana ikifungiwa. Kisa kosa la kushiriki mauaji.
Marko alihusisishwa na kesi ya mauaji. Mauaji ya watu wawili. Tena akafanywa aonekane kuwa yeye ni mtu wa kutisha sana pale ambapo alishutumiwa kuwa na mtandao mpana wa kigaidi akishirikiana na waasi kutoka jamuhuri ya kidemokrasia ya kongo ambao wanasadikika kumiliki sumu kali zinazoangamiza ndani ya sekunde. Marko alipagawa.
Mke wake alilia sana huku akisema neno moja tu kuwa mume wake alikuwa mcha Mungu. Na wala asingeweza kufanya tukio lile hata kwa kulazimishwa.
Mama huyu hakuwa akidanganya, Marko alikuwa mcha Mungu, na hata biashara yake ya kuuza machungwa na pweza aliifanya kwa uaminifu mkuu. Vijana mtaani wakamzoea kwa jina la baba mchungaji.
Mama yule alikumbushia hata kitendo cha mume wake huyo ambaye hakuwa amemtolea mahali, cha kurejesha pochi yenye pesa taslimu laki nne za kitanzania iliyosahauliwa na mteja katika kibanda chake cha mchana machungwa, usiku pweza.
Lakini nani angeziamini ngonjera za mama yule ambaye badala ya kuitwa mke wa mtuhumiwa aliitwa muhusika msaidizi katika kesi.
Serikali haikutaka kuelewa kitu kwa sababu haikuwa na dini, na sheria haipingwi kwa imani isiyoonekana. Maneno ya mama yule yakapita katika sikio hili na kwa kasi ya ajabu yakatokea katika sikio jingine.
Marko akaendelea kusota ndani, hakupinga kuwa hakumshika mkono marehemu Karama lakini alipinga vikali kuhusika katika kumlisha kitu chochote kibaya. Alionyeshwa ujumbe ambao ulikutwa katika mifuko ya suruali ya marehemu Karama katika namna ya kushtukizwa iwapo atatambua lolote lakini Marko alionekana kutoutambua ujumbe ule hata kidogo. Ujumbe wa ‘BADO SITA’.
Lakini licha ya hayo hakuweza kuachiwa huru, huku ikidaiwa kwamba upelelezi unaendelea bado. Kipigo alichopokea, laiti kama angekuwa anahusika kweli asingeweza kustahimili. Lazima angeusema ukweli.
Ule uvumilivu wake na msimamo ukazidi kuwatia mashaka na kuzidi kuamini kuwa alikuwa na dalili za kigaidi.
“Mama Wanka, usilie sana mwisho ukakufuru. Mungu aliye hai atajibu na si lazima iwe sasa hata kama itapita miaka usiache kumtukuza kwa kukuletea mtihani huu ili utambue kuwa yu hai na anakupitisha katika majaribu ili umsahau yeye ama uendelee kumkimbilia. Nenda na amani, ilimradi nipo hai kwa uweza wake.” Marko alimwambia mkewe, siku ambayo alikuwa akihamishiwa katika gereza la mahabusu la Segerea. Maneno hayo yalimjenga mkewe kiimani lakini katu hayakumwondoa katika majonzi.
Karandinga ikafunguliwa na Marko akaingizwa ndani kwa kosa na kesi asiyoifahamu.
Akamlilia Mungu wake kimyakimya!! Kisha akatabasamu kidogo kabla ya kusema kwa sauti ya juu kidogo.
“Mungu hakika upo hai, nilikuomba unijaribu imani yangu. Nawe umejibu!! Sitakufuru kamwe!”
“Fala wewe unaenda kufia segerea na huo unafiki wako” askari magereza alimtupia tusi na kebehi.
Marko akatabasamu tena!!!
****CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
**LAMECK na KARAMA wanakufa vifo tofauti lakini wanakutwa na kitu kingine kinachosababisha vifo vyao vionekane kusheheni utata….wanakutwa na ujumbe..huyu BADO SABA na huyu BADO SITA.
**Askari mpelelezi GASTO MUSHI anavalia njuga hili jambo, anataka kujua kulikoni vifo hivi.
**Inspekta Seleli anajaribu kumkanya Gasto lakini hiyo ni kazi bure…
**Marko aliyemgusa marehemu Karama kwa mara ya mwisho anatiwa hatiani…lakini anasimamia msimamo kuwa ahusiki….nani sasa muhusika kama huyu ahusiki??
****TUKUTANE TENA !!***
TOA MAONI YAKO!!!
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment