Search This Blog

Sunday, 19 June 2022

HARUFU YA KIFO - 2

 





    Simulizi : Harufu Ya Kifo

    Sehemu Ya Pili (2)



    “Mama Wanka, usilie sana mwisho ukakufuru. Mungu aliye hai atajibu na si lazima iwe sasa hata kama itapita miaka usiache kumtukuza kwa kukuletea mtihani huu ili utambue kuwa yu hai na anakupitisha katika majaribu ili umsahau yeye ama uendelee kumkimbilia. Nenda na amani, ilimradi nipo hai kwa uweza wake.” Marko alimwambia mkewe, siku ambayo alikuwa akihamishiwa katika gereza la mahabusu la Segerea. Maneno hayo yalimjenga mkewe kiimani lakini katu hayakumwondoa katika majonzi.

    Karandinga ikafunguliwa na Marko akaingizwa ndani kwa kosa na kesi asiyoifahamu.

    Akamlilia Mungu wake kimyakimya!! Kisha akatabasamu kidogo kabla ya kusema kwa sauti ya juu kidogo.

    “Mungu hakika upo hai, nilikuomba unijaribu imani yangu. Nawe umejibu!! Sitakufuru kamwe!”

    “Fala wewe unaenda kufia segerea na huo unafiki wako” askari magereza alimtupia tusi na kebehi.

    Marko akatabasamu tena!!!



    ****



    Manyunyu yaliitawala anga ya jiji la Mwanza, wakazi wengi walikuwa aidha wamejikinga katika vibanda vilivyokuwa maeneo hayo huku wengine wakiisikilizia hali ile ya hewa majumbani kwao. Katika nyumba moja ya kifahari watoto wadogo kama kawaida walikuwa wakichezea maji yanayoletwa na mvua. Hii kwao ilikuwa faraja sana.

    Mwanamama mmoja asili ya kihindu ama kiarabu alikuwa amekunja sura yake waati aielekea nje ambapo watoto wale walikuwa wanacheza, alifika kwa hasira akamkamata mmoja na kumnasa kibao mgongoni kama namna ya kuwaonya wengine. Kisha akazidi kugomba.

    Aliwaongelesha kwa lugha ambayo waliifahamu wao pekee, kisha akatoa msonyo wa nguvu. Watoto wakanywea na kuingia ndani kiuoga. Mama alipotaka kuufunga mlango mara kengele ya mlangoni ililia kumaanisha kuna mtu alikuwa anahitaji kufunguliwa geti.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mama yule akapandwa na jazba na kuhisi mbonyeza kengele alikuwa akifanya maksudi ili amchoshe tu. Akauendea mwamvuli akauchanua na kisha kujifunika, akavaa makubadhi miguuni akaliendea geti kwa mwendo wa kuinamainama.

    Akafika akakifunua kibati kilicholiziba tundu dogo.

    “Nini shida?” akauliza huku akitazamana na sura ya mwanamke ambaye angefaa zaidi kuitwa binti.

    Binti alionyesha ishara ya kutaka kuonana na yule mama, taratibu akaliendea geti akalifungua.

    “Mama Kassim…” yule binti akamuita mama yule.

    “Ni mimi unasemaje?”

    “Nina shida na wewe kama itawezekana….”

    “Shida gani wewe mtoto. Zungumza”

    “Unapenda nijieleze nikiwa hapahapa ama kidogo waweza kuzungumza name pembeni.” Aliomba yule binti.

    “Zungumza nakusikiliza.” Alijibu katika namna ya kumaliza mazungumzo upesi na hasahasa kutoyatilia maanani.

    “Ni kuhusu mume wako aliyekulaghai kuwa yupo msibani hadi leo.” Alisema yule binti kisha akawa kama anayetaka kuondoka. Ilikuwa zamu yake kucheza na akili ya yule mama mweupe.

    “Binti unasema?” alihamanika!!

    “Siwezi kuzungumza nikiwa nimesimama hivi na tena mahali hapa. Ni hatari akinikuta.” Alisema huku akitazama kushoto na kulia kama mwivi. Hii yote ni kucheza na akili ya yule mama.

    Mama yule ambaye alikuwa amejitanda ushungi alimtazama yule binti kwa umakini kisha akatega sikio kumsikiliza. Ni kama bado hakuwa tayari kwa mazungumzo ya kirefu zaidi.

    “Kama haiwezekani basi mi naondoka.” Akasema huku akitaka kutoweka.

    Ni hapa lilipotokea jambo ambalo hakuliota kama laweza kutokea kirahisi hivyo. Yule mama naye alikuwa ana ratiba ya kutoka hivyo akamuomba kama inawezekana waondoke naye katika gari lake. Huku wakizungumza



    Binti akafanya ama kujishauri ili asionekane kuwa mwenye papara sana na kisha akakubali na kisha huku akisifia kuwa walau hapo atakuwa na amani na maneno yake.

    Maneno ya kidaku!!



    Baada ya dakika kumi, binti mgeni alikuwa pamoja na mama mnene mwarabu ama muhindi katika gari kubwa aina ya Toyota VX. Nyeusi!!

    Safari ikaanza kutokea maeneo ya Nyakato Sokoni kuelekea Sahara katikati ya jiji la Mwanza. Binti alikuwa mkimya wakati yule mama akihangaika na gari.

    “Ehe baba Kassim kafanya nini.” Aliuliza yule mama. Wakati huu foleni iimewazuia kuendelea, yalikuwa ni majira ya jioni jioni. Mama alionekana kuwa na kiherehere cha kujua nini kinatokea kwani alikuwa na mashaka na safari ya mumewe kwenda msibani kumzika mtu aliyemuita rafiki yake wa karibu, kwa jina Lameck Kagiri!!

    Binti alijishauri kidogo kisha akazungumza kwa kifupi!! Wakati mama akitarajia kuwa sasa aneenda kupewa umbea ambao utamwezesha kumtuhumu mumewe akakutana na jibu la ajabu!!

    “Amekuua.” Alijibu bila hofu huku akitazama mbele. Kana kwamba hasemi neno lolote na yule mama.

    Mama akashangaa kisha akaumaliza mshangao wake katika swali.

    “Ameniua kivipi, sema acha kuyumbisha maneno binti.” Alikaripia yule mama. Sasa akadhani kuwa mumewe aidha alikuwa muathirika wa virusi vya Ukimwi na alikuwa amemwambukiza tayari.

    “Muuaji kabisa amekuua yule.” Alijibu tena bila kumalizia kauli yake. Sasa alitabasamu lakini akiwa anaangalia mbele vilevile.

    Sasa yule mama mweupe akahisi kuwa yule binti atakuwa na matatizo ya akili!! Akafikiria kutumia lugha ya ukali na ikiwezekana kumshusha yule binti kutoka katika gari.

    Mama yule akataka kusema neno mara yule binti akamwonyesha kitu kinachotisha na ambacho hakutegemea kukutana nacho kwa wakati huo.

    Vioo vyeusi vilivyofungwa kwa sababu ya baridi sasa ni heri vingefunguliwa maana yule mama alikuwa anatokwa jasho huku akitazamana na mdomo wa bunduki ambayo ilikuwa imekamatwa vyema mkononi mwa yule binti. Sasa hakuwa anatabasamu na hakuwa akingalia mbele tena!! Alikuwa anamtazama yule mama machoni!!

    “Ukitikisika tu nalipua bila uoga wowote. Nalipua kichwa chako” Alikaripia yule binti. Mama akatulia tuli lakini asingeweza kujizuia kutetemeka.

    Binti akampa yule mama amr amtumie mume wake ujumbe katika simu yake.

    Mama akatii huku akiwa anatetemeka akalazimishwa kuandika maneno fulani mafupi kwenda kwa mume wake. Akafanikiwa kumaliza kwa tabu kutokana na kukoseakosea, alipomaliza akautuma ujumbe ule kama alivyoambiwa!!



    *****



    SIMU YA Ramadhan Uwesu iliita kwa muda mfupi kisha ikakata. Rama akaitazama kisha akapiga kite cha hasira. Hakuna kitu alikuwa akichukia katika simu kama tabia ya kubipu ama kubipiwa.

    Mbaya zaidi aliyekuwa amembipu alikuwa ni mwanaume mwenzake. Wakati akiidhibiti fedheha yake mara yule mtu alibipu tena.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Rama akatokwa na tusi zito la nguoni. Waliokuwa wamemzunguka wakastaajabu bila kuhoji kitu chochote. Hakujua kama alitokwa na tusi lile kwa sauti ya juu, yeye kwa mawazo yake lile tusi alikuwa amelitoa kimoyomoyo.

    Akabonyeza simu yake na kuanza kusikiliza nini kimemsibu huyo mtu anayembipu. Sasa alikuwa ameamua kumpigia kwa kujilazimisha.

    “Oya Kessy eeh sina hela bwana unasemaje?” alijitahidi kuidhibiti sauti yake isitangaze jazba aliyokuwanayo.

    “Ahaa! We vipi bwana, nilikwambia kuna siku litakubumia hilo gari lako. Pole bwana.”

    “Unamaana gani Kessy. Sema basi mi sina hela kwenye simu.” Alilalamika Rama. Aliona kama huyo Kessy alikuwa hajui thamani ya pesa katika simu.

    “Nimekupita hapo Igoma, ama ni waifu maana..” Kessy akiwa katika kujibu, Rama akakata simu kisha akatoa tusi jingine zito zaidi, safari hii kwa kukusudia kabisa. Midomo ilikuwa inamtetemeka.

    Akaitazama simu yake kwa ghadhabu kama kwamba huyo Kessy asiyekuwa na hoja yoyote ya msingi angeweza kumwona kupitia kile kioo na akome kabisa kubipu, lakini badala ya Kessy ukaingia ujumbe.

    Ramadhan akaufungua upesi akidhani ni Kessy ametuma ujumbe kama haueleweki apate nafasi ya kumtukana huenda ghadhabu yake itapungua. Na alijua lazima atakuwa ni Kessy!!

    “Kessy mbona ana mambo ya kijinga hivi.” Alilalamika Rama huku akiwatazama watu waliomzunguka kama vile na wao wanamjua huyo Kessy ambaye anaonekana kumvuruga akili yake, na wao wakamtazama kama wanangoja awasimulie juu ya huyo Kessy na wao wastaajabu na kutoa ushauri ikiwezekana.

    “….Nimemuua nimemuua kivipi sasa…..tena ameandika …he! Huyu jamaa mwehu kweli. Mi nimekuwa mume wake…” Alimalizia kwa sauti ya chini huku akisikitika. Sasa aliweza kucheka kidogo.

    Rama aliitazama simu yake akihamisha macho yake kutoka kwa watu ambao aliamini hawana msaada kwake. Mara akaduwaa, hakuwa ameuelewa ujumbe ule barabara lakini sasa alianza kuelewa nini kimeandikwa katika simu yake.

    Maajabu haya! Ilikuwa namba ya mkewe ambayo awali aliona kuwa ni ya Kessy kutokana na kupagawa na kuwa mtumwa wa hasira. Hivi alisahau kuwa hasira hasara?.

    Ujumbe ulitumwa na mkewe na ulitumwa kuja kwake.

    “Umeniua mume wangu..” ulisomeka hivi bila kuwa na neno la ziada.

    Akarejea kuusoma kisha akabofya namba ya mkewe aweze kumuuliza iwapo alimaanisha kutuma ujumbe ule na kama hakumaanisha. Simu haikuita mara ya kwanza, akajaribu kupiga tena haikuita.

    Akaguna! Kisha akajaribu kupiga tena mara nyingine. Hali ileile simu haikuita!!

    Akazungumza peke yake kwa sauti za chinichini hakuna aliyemsikia!!

    Wakati anazungumza mwenyewe simu nayo ilizungumza, sauti ya kike!! Rama akaiweka sikioni akidhani ni mkewe, alkini aliambulia kukutana na maneno haya.

    “Mteja wa simu unayempigia hapatikani kwa sasa taf…” akakata simu kabla haijamaliza kumwimbia nyimbo hizo.

    Ni hapa ndipo alipoukumbuka umuhimu wa Kessy, yule bwana ambaye alimbipu na kisha akampigia akiwa ametaharuki haswaa. Wakashindwa kuelewana.

    Mwanzoni alimchukulia kama mpuuzi asiyejielewa kabisa. Lakini muunganiko wa ujumbe kutoka kwa mkewe ambaye hapatikani kwenye simu ukamvuruga kabisa.

    Sasa ikawa zamu yake kuhangaika kumpigia. Simu ikaita kitambo kidogo kisha ikapokelewa.

    “Bwana Kessy…hivi nanii..”

    “Samahani Rama nipo naendesha gari mida basi kaka…” alijibu Kessy kisha akakata simu bila kutambua Rama ana shida gani.

    Rama alijaribu kupiga mara kwa mara Kessy asipokee.

    “He huyu Kessy jamani mbona hapokei simu ama!!” alizungumza tena huku akiwashangaa watu wa pembeni yake. Sasa ilikuwa zamu yake kuonekana mjinga kwa kauli zake za kugeuka huku na kule. Mwanzoni alisema Kessy ni mjinga sasa anasema Kessy hapokei simu!!

    Akiwa anaduwaa bado, Kessy alimbipu. Akampigia upesi, Kessy akamwelezea juu ya gari yake kuonekana maeneo ya Igoma ikiwa barabarani imeegeshwa pembeni kama vile ni mbovu. Na mbele imewekea ngao ndogo ya kuitambulisha kuwa ina hitilafu.

    “Sasa mbona hapatikani huyu mama Kassim sasa.” Aliuliza kipumbavu Rama.

    “He! Kaka mambo ya mkeo kutopatikana sasa mimi nitayajuaje aisee.” Alijibu kwa sauti iliyofedheheka. Hakutarajia swali lile.

    Ramadhan hakuwa na jingine la kuongezea akakata simu lakini akiwa na maswali lukuki.

    Wakati huo walikuwa wameufikia mzani wa mwisho kabla ya kuingia jiji la Mwanza akitokea Dar es salaam katika mazishi ya bwana Lameck Kagiri, mfanyabiashara mwenzake ambaye alikutwa amekufa ofisini kwake.

    “Suka eeh hebu kaza mkono bwana mke wangu sijui kimemsibu nini.” Alileta hoja hiyo.

    “Hee yaani matatizo ya mkeo nd’o yatusababishe tuongeze mwendo baada ya kusafiri vyema kuanzia Dar acha hizo Rama.” Aliingilia kati jamaa mwingine ambaye alikuwa kama amesinzia lakini kauli ya Rama ikamgutusha.

    Rama akamtazama kwa jicho kali yule mzee aliyemkata kauli. Mzee yule alikuwa amegeukia upande mwingine tayari hakuweza kuiona hali ile. Dereva akatii ombi la Rama akaongeza mwendo wa gari, wakaipita Nyegezi kwa fujo kisha ndani ya dakika kadhaa walikuwa Mwanza mjini katikati, wakaifuata barabara ya kuelekea Igoma inayojulikana kama barabara ya Nyerere.

    Walipofika Mabatini, mmoja akashuka na mwingine akashuka Barnaba, hatimaye wakabaki watatu katika gari. Hawa walikuwa mashuhuda wa tukio la kustaajabisha na ni hawahawa waliotakiwa kuisaidia polisi kwa upelelezi zaidi.

    Kweli gari lilikuwa limeegeshwa kandokando ya barabara ya ya Nyerere kuelekea Kisesa na Magu. Halikuwa na uhai wowote na hakuna aliyejihangaisha nalo aidha kulitengeneza ama kuliosha.

    Rama akastaajabu, akili yake ikawaza kuhusu wizi. Akaweka makisio kuwa gari yake ilikuwa katika jaribio la kuibiwa.

    Lakini mbona imeegeshwa kistaarabu kabisa na kibao cha kuonyesha kuwa ina hitilafu kimepachikwa kwa mbele.

    Au njama!!! Akajiuliza.

    Hili likawa tatizo jingine ambalo alijaribu kukabiliana nalo kichwani mwake huku akizidi kulikaribia gari lake akiwa pamoja na yule mzee ambaye alikuwa ana macho kama anasinzia.

    Ramadhani akajaona ni ujinga kuliogopa gari lake, akauendea mlango wa upande wa dereva akaufungua.

    Lahaula! Mwili wa aliyekuwa mke wake mpenzi mama wa watoto wake watatu ukaanguka. Badala ya kujishughulisha kuwahi usianguke akatokwa na yowe la hofu huku akiruka mbali.

    Akauachia mwili ule mnene na mzito!!

    Mwili wa yule mwanamke mweupe ukatua chini kama gunia la mkaa. Kisha damu ikatapakaa kwa fujo ardhini. Ilikuwa ni picha ambayo iliwavutia watu wengi, wakakimbilia kwa fujo eneo lile lakini walipoufikia mwili ulioharibiwa vibaya kwa risasi. Wakasita kupiga hatua ya ziada. Wengi waliuogopa!!

    Taarifa zikasambaa kama upepo na watu wakazidi kumiminika eneo la tukio. Mwishowe wanausalama wakafika baada ya barabara kuzibwa kabisa na umati uliokuwa ukishangaa mwili wa mwanamke yule.

    Walifika wakiwa wamechelewa sana na mwili ulikuwa upo kama ulivyokuwa awali, Ramadhani akiwa amechanganyikiwa kabisa asijue nini cha kufanya na mzee mwenye macho ya kusinzia akiwa ametoweka tayari polisi waliusaili kabla ya kupiga simu kadhaa za upepo na baadaye wakazungushia wigo wa kuzuia raia wasiweze kulisogelea eneo la tukio. Baada ya muda lilifika gari la wagonjwa likauchukua mwili wa marehemu huku wakiwa wamevaa mipira mkononi kuzuia kuacha alama za vidole katika miili yao.

    Hali ilikuwa tete sana na hakuna ambaye alikuwa ana jibu watu walibaki kuweka unabii huku kila mmoja akisema alikuwa na mashaka na uwepo wa gari lile maeneo yale kwa muda mrefu vile. Hakika ilitatanisha kumbe muda wote ule kulikuwa na maiti ndani ya gari.

    Mahojiano yalifanywa kwa watu kadhaa ambao walikiri kuliona gari lile maeneo yale lakini hawakuwa na mchango zaidi ya kukiri ni kweli waliliona gari.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hata mwanaume mmoja ambaye alitambua fika kuwa kuna dada mmoja alikuwa ndani ya lile gari aliogopa kusema lolote kwa kuhofia mambo ya kuchukuliwa kwa ajili ya kusaidia upelelezi huku akiwa anasota rumande.

    Hivyo akakaa kimya bila kusema neno.

    Baadaye gari lile liliondolewa na kupelekwa kituo cha polisi cha MWATEX kwa hatua nyingine za kichunguzi. Polisi waliandamana na bwana Rama ambaye alikuwa mmiliki halali wa gari lile.



    ****



    KATIKA baa ya Ndama, iliyopo pembezoni kidogo mwa kata ya Igoma jijini Mwanza, mlevi mmoja alikuwa ameanza kulewa na kujikuta akisakata mayenu katika namna ambayo awali ilifurahisha wateja na kuwafanya watabasamu lakini baadaye ikazua kero kutokana na mlevi yule kuanza kusukasuka wateja katika miondoko yake ya kilevi, mara avunje chupa mara atukane matusi ya nguoni. Mara akanyage viti kwa fujo!!

    Muhudumu wa kike alipojaribu kumuelewesha alikumbana na matusi makubwa zaidi. Na ikifikia hatua muhudumu wa baa akachukia baada ya kutukanwa basi ujue ametukanwa matusi mazito mno. Matusi asiyostahili kutukanwa mwanadamu yeyote yule.

    Muhudumu mwingine wa kiume akaingilia sakata lile la kumdhibiti yule mlevi asiendelee kuwabughudhi wateja wastaarabu, lakini hapa napo kikazuka kizaazaa kingine, yule mlevi akadai anaingiliwa uhuru wake na wahudumu wale. Akaanza kuporomosha matusi huku akimtishia yule muhudumu kuwa iwapo ataendelea kumsumbua sumbua basi atamshtaki kwa meneja wake na kumpotezea kibarua chake. Maneno ambayo hayakuwa na tija sana maana yule kijana alikuwa kazini.

    Martin Kejo alikuwa analishuhudia sakata hili akiwa katika kona moja yenye gizagiza aliyojibanza na Rose ambaye ni mpenzi wake wa siku nyingi.



    Walikuwa wamepotezana muda mrefu kidogo na juma hilo la kuonana lilikuwa juma la starehe. Walienda ufukweni walenda disko na leo walikuwa Ndama hoteli. Kejo alimtazama yule bwana tangu alivyoingia kistaarabu na sasa akawa amevurugika na kufanya vurugu. Jamaa akakiri kiuhakika kuwa pombe sio chai.

    Akazidi kumtazama zaidi hadi aliposimama na kuanza kucheza, hapa yeye na Rose walicheka huku wakigonga viganja vya mikono yao. Alikuwa amewafurahisha.

    Mara wakatazamana tena baada ya mlevi yule kuanza kusumbua wateja mara aanguke huku mara avunje chupa. Hali hii hawakuipenda hata kidogo, lakini Kejo alichukizwa zaidi na yale matusi ya nguoni ambayo yule mlevi alianza kumtukana muhudumu wa kike, yalikuwa matusi ambayo ni kama alikuwa akitukanwa Rose wake na pia mama yake wa kumzaa. Hapa Kejo alifanya tabasamu hafifu ambalo Rose analifahamu vyema kabisa, ni tabasamu la hasira.

    “Achana naye hebu!” Rose aliwahi kumwonya Kejo kabla hasira yake haijamtuma kwingine. Alimjua vyema mpenzi wake huyo.

    Kejo hakujibu kitu, akapiga funda moja la pombe yake kisha akaendelea kutazama upande ambapo tukio lile lilikuwa linaendelea.

    Mara yule mlevi alianza kupambana na muhudumu wa kiume kimabavu huku akimshikia chupa na kumtishia kumjeruhi.

    Katika harakati hizi mara yule mlevi katika kujibizana na yule kijana muhudumu, mara akatokwa na neno baya ambalo lilizidi kumkera Kejo.

    “Hapa hata waje askari siondoki hapa hizi ni starehe zangu.”

    Kejo akalisikia neno hili Rose naye akalisikia, akamtazama Kejo usoni. Tabasamu la Kejo lilikuwa limetanuka zaidi.

    Hasira kali sana!! Zaidi ya awali

    “Ngoja nimrudishe akili zake hapa mara moja kama atakuwa tayari kurejea.” Kejo alisema huku akisimama. Rose hakufanya jitihada za kumzuia kwani alikuwa akimfahamu fika mpenzi wake yule akikasirika anakuwa mtata sana. Hakawii kumcharukia na kumzushia kesi yoyote ile.

    Halafu kingine alikuwa sahihi kuingilia vurumai ile mbele yake kwa sababu alikuwa askari mtiifu wa jeshi la wananchi Tanzania. Haijalishi yu ndani ya gwanda ama la! Inapohitajika msaada anautoa bila kusita.

    Kejo alitokea ukumbini katika mwendo wa kunesa asionyeshe ukakamavu wowote, alimtazama yule muhudumu wa kiume kijasho kilikuwa kinamtoka kupambana na yule mlevi. Kejo akasita na kumtazama vyema yule mlevi kisha akakiri katika nafsi yake kuwa yule bwana alikuwa mkakamavu sana na mtu wa mazoezi. Kejo akatabasamu tena alipomtazama muhudumu alivyokuwa anahema juu juu. Hakika alikuwa amefikwa!!

    Baadhi ya wateja walikuwa wameanza kusimama huku wengine wakiwa wamenuna, hawakupendezwa na kile walichokuwa wanakiona mbele yao.

    “Unaonaje ukitoka nje ya ukumbi bosi unatusumbua huku wateja wengine” alisema Kejo huku akimtazama yule mlevi machoni.bado alikuwa anatabasamu.



    Yule mlevi akamgeukia Kejo na kuanza kumvurumishia mvua ya matusi huku akiwatishia kuwapiga wote kwa pamoja. “Yaani nitawakunjakunja niwachape vibao ohooo!!” aling’aka

    Aliwatishia wote kwa pamoja Muhudumu wa kiume na huyo mteja aliyeleta malalamiko kwake ya kupigiwa kelele. Kejo!!

    Kejo alimpa onyo la pili lakini bado alipuuzia na kutaka kumkabili kwa kutumia chupa. Hapa Kejo akashtuka na kujirusha pembeni kidogo kisha akaurejesha umakini wa watu na kuzidi kulitazama lile tukio. Huyu hakuwa lelemama kama yule muhudumu aliyetolewa kijasho!!

    Kejo akarusha mguu wake ukanyooka vyema akaidokoa ile chupa ikaanguka chini na kupasuka kisha bila kuushusha vyema chini akajizungusha kwa mguu mwingine teke likatua barabara katika mbavu za yule mlevi. Halafu akajirusha nyuma akasimama kilegelege kama hakuna kitu kilichotokea kabisa.

    Ilipendeza kutazama!!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mlevi akaanza kuhaha huku na kule akitafuta silaha nyingine, Kejo hakutaka kupoteza wakati na kujitoa jasho bure. Akamvamia tena na kumtwisha ngumi nzito begani, mlevi akatokwa na yowe la uchungu.

    Watu wakashangilia, mara akatokea mwanaume mwingine na kujitia kumsaidia yule mlevi huku akidai kuwa anachofanya Kejo ni uonevu. Kejo akamtishia kama anampiga teke kisha akamshushia ngumi ya haja mbavuni, akalia kwa uchungu huku akilainika kwenda chini.

    Mara Kejo akajizungusha tena akalichomoa shati lake nadhifu, akachomoka na pingu na baada ya dakika moja wale jamaa wawili walikuwa wameunganishwa mikono yao kwa pingu.

    Wakati watu wakiduwaa Kejo alitoa kitambulisho na kukipunga hewani na kuwafanyia ishara watulie katika viti vyao.

    Wateja wakapiga makofi huku wakitabasamu na kusimuliana juu ya tukio ilhali wote walilishuhudia moja kwa moja wakati linatokea.

    Kejo aliwatwaa watu wake kisha akaongozana na Rose.

    “Tukalale zetu washanichafua wajinga hawa.” Kejo alimweleza Rose huku wakichukua taksi ambayo iliwapeleka moja kwa moja hadi kituo cha polisi Mwatex ambapo hao walevi wangehifadhiwa hapo kisha kuachiwa asubuhi. Pombe zikiwa zimewaisha kichwani.

    Baada ya kuwafikisha Kejo aliondoka upesiupesi akiwapa maelezo machache askari waliokuwa zamu kuwa jamaa hao hawakuwa na kesi ya kujibu badala yake waadabishwe kidogo kwa kulala katika mahabusu chafu.



    Akatoweka na kumkwapua Rose wakarejea katika taksi kwa safari yao ya kuelekea Nyakato sokoni. Ni huku Rose alikuwa amepanga chumba na kuishi peke yake, usiku huu alitegemea kulala na Kejo.

    Taksi iliondoka kwa mwendo wa kasi ya kawaida na vile ulikuwa ni usiku hapakuwa na foleni kabisa wakawahi kufika Nyakato.

    Walipofika walikuta umati wa watu katika nyumba ambayo walikuwa wakiifahamu kuwa ni nyumba ya kipekee ambayo walikuwa wakiishi waarabu ama vyovyote vile lakini nd’o iliitwa nyumba ya uzunguni. Watu walikuwa wamesambaa huku na kule hali ambayo haikuwa ya kawaida kabisa katika nyumba hiyo.

    Kejo na Rose hawakuulizana licha ya wote kukazia macho eneo lile.



    Wakati wanafungua mlango waweze kuingia ndani afande Kejo akapigiwa simu. Ilikuwa ni namba mpya.

    “Kituo cha polisi Mwatex, afande Kejo. Kesho alfajiri uwahi hapa kituoni.” Sauti iliunguruma, akatii, akatambua kuwa alitakiwa kwenda kuelezea juu ya watu wale aliowatupa pale kituoni, hilo halikumtisha hata kidogo.

    Wakajichoma ndani. Usiku ukamalizika kwa wao kufurahisha miili yao.



    ALFAJIRI kama alivyoamriwa afande Kejo aliwahi kituoni na kukuta maelezo ya wapi alipokuwa akihitajika, upesi akaingia katika ofisi ya mkuu wa kituo. Ni huku alitarajia kupewa maelezo kadha wa kadha juu ya nini kinaendelea.

    Afande hakutegemea kama alichokuwa anaitiwa ni juu ya wale walevi wawili aliowatupa rumande kwa kosa la kuvunja amani mtaani. Kama wangekuwa ni hao wala asingeweza kuitwa katika ofisi ya mkuu wa kituo.

    Lakini jambo lenyewe lilikuwa hilo. Ajabu!!

    Mkuu wa kituo inspekta Omari Omari, alimweleza jambo la kustaajabisha ambalo limekutwa kwa walevi wale ambao bado haijajulikana kama wana mahusiano kiurafiki ama kindugu ama la!

    Inspekta alimweleza juu ya vifo viwili vyenye utata vilivyotokea jijini Dar es salaam, kifo kilichotokea ofisini na kingine kilichotokea makaburini. Vikiwa ni vifo vya namna ya tofauti lakini vilivyokuwa na ujumbe unaofanana.

    Kejo alitikisa kichwa na kukiri kuwa taarifa ile alikuwa nayo yote kama ilivyo, akilini alistaajabu sana kuulizwa kitu alichokuwa anakijua.

    “Na ujumbe ule unaosema ‘BADO SITA kwa upande mmoja na BADO SABA kwa upande mwingine’ ndo kitu kilichosababisha matukio yale kushabihiana, lakini cha kustaajabisha sasa, ujumbe uleule umekutwa kwa walevi hawa. Ujumbe umeandikwa BADO TANO’.Hii ina maana gani afande eeh! Inamaana hawa walevi ndio wauaji? Ama jiji letu linamtunza muuaji??” aliuliza Inspekta Omari huku akiuma uma kalamu yake.

    Kejo alistaajabu, hakutegemea hata kidogo kuwa yawezekana jambo hili likawa limefikia huku, yaani ujumbe hatari kama ule kukutwa kwa walevi katika baa ndogo tu jijini Mwanza? Ilistaajabisha sana.

    Kejo akaelezea tukio zima la kukutana na walevi wale baa akiwa na mpenzi wake akajieleza kinagaubaga jinsi alivyoamua kuvaa kofia yake ya kazi baada ya walevi wale kuleta vurugu na kutishia kuvunja amani katika eneo lile.

    “Haukuhisi kitu chochote kutoka kwa hawa walevi ama tuseme huyo mlevi aliyekuwa analeta vurugu afande?” inspekta alihoji.

    “Kikubwa ambacho niliona kwa macho yangu na kukiri ni kuwa yule mlevi alikuwa ni mtu wa mazoezi sana na laiti kama asingekuwa amelewa basi angeweza kuwa mtu hatari, hakuna jingine nililoliona.” Alijibu bila kutetemeka afande Kejo.

    Inspekta Omari akakuna kichwa chake kisha akamruhusu Kejo aondoke lakini asikae mbali sana anaweza kuhitajika muda wowote.

    Kejo akasimamana kupiga saluti kikakamavu kisha akatoka nje ya ile ofisi.

    Alipotoka nje, inspekta Omari akanyanyua mkonga wa simu yake na kupiga simu jijini Dar es salaam.

    Alikuwa akitoa maelezo ambayo amepewa na Kejo!!



    *****



    ASKARI mpelelezi Gasto Mushi alikuwa akistafutahi huku akisikiliza mirindimo ya muziki uliokuwa ukitoka katika mojawapo ya spika zilizokuwa katika mgahawa wa Jitegemee maeneo ya Kurasini jijini Dar es salaam, muziki ule uliifanya chai yake ya maziwa iwe tamu zaidi, chapatti za kumimina zitelemke vizuri zaidi na pia ile juisi iliyokuwa pembeni yake izidi kutamanisha ilhali alikuwa hajaionja bado.

    Simu yake mkononi ilivyoita ndipo ladha nayo ikapungua, akajiuliza juu ya kunawa kisha ajipapase mifuko yake na kuitoa ile simu.

    Kwa mara ya kwanza akapuuzia, lakini ilivyoita tena akaitua chapati chini akachukua kitambaa chake akajifuta juu juu kisha akaitoa simu.

    Inspekta!! Jina lilisomeka hivyo.

    Upesi kikakamavu kama mpiga simu alikuwa anamuona akaipokea.

    “Jambo afande!” akatoa salamu.

    “Njoo ofisini kwangu upesi.” Aliamriwa pasi na maelezo marefu.

    Akazitazama chapati mbili na juisi yake roho ikamuuma kuziacha lakini hakuwa na ujanja. Akasimama na kuliendea bomba akanawa kisha akafanya malipo kamili. Halafu akairukia pikipiki yake na kuitia moto akatoweka kuelekea katika kituo cha polisi Chang’ombe wilaya ya Temeke jijini Dar es salaam.

    Akafika na kuingia moja kwa moja katika ofisi ya mkuu wa kituo hicho kilichopo maeneo ya Temeke jijini Dar es salaam baada ya kuwasabahi marafiki zake wawili watatu.

    “Ni utata mwingine. Ama la ni jibu limepatikana lakini dah.” Akasema inspekta huku akimtazama kijana wake ambaye anakiri kuwa ni mchapakazi.

    “BADO TANO” akasema kisha akamtazama Gasto Mushi machoni, na kisha akaendelea, “Jijini Mwanza hiyo” alimalizia.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ujumbe umepatikana Mwanza? Ujumbe wa bado tano” aliuliza Gasto huku akijiweka sawa katika kiti kilichokuwa mbele ya meza ya bosi wake.

    “Tena ujumbe huu umepatikana kwa walevi, hakuna cha maiti wala nini, sasa sijui kama ndo walikuwa wanaenda kuua ama vipi. Yaani kama walikuwa wanaenda kuua aisee hii kesi imemaliziaka na wanafia jela” Inspekta aliendelea kisha akamweleza kila kitu alichoambiwa na inspekta kutoka jijini Mwanza juu ya ujumbe ule.

    “Wanaweza kuwa wanafahamiana na huyu mlokole ama?” alijiuliza Gasto bila kumshirikisha Inspekta, yaani ni kama alikuwa akiongea mwenyewe juu ya Marko. Inspekta naye alikuwa akijiuliza alichojua mwenyewe hivyo hakusema lolote.



    “Jiandae, kesho uende Mwanza hatuwezi kuchezewa mchezo wa kitoto na walevi sisi. Vyombo vya habari vikianza tu kufuatilia jambo hili tayari wanalichafua jeshi, wapumbavu sana hawa watu wa magazeti yaani hapa watashupalia mpaka basi. Vile wana uhuru wa kuandika basi hatutapumua, hebu tulizimishe jambo hili kabla halijawa komavu.” Inspekta alimweleza Gasto kisha akasimama akimaanisha kuwa ahitaji majibu zaidi. Gasto kusikia habari za waandishi akaikumbuka kauli ya inspekta Seleli.

    Gasto akashusha pumzi na yeye upesi akasimama na kusaluti.



    SIKU iliyofuata majira ya saa nne asubuhi askari huyu kijana alikuwa akingoja tangazo la ndege aliyokuwa amekatiwa tiketi aweze kuingia na kuondoka. Kichwani mwake alikuwa akiifurahia kazi yake kwa mara nyingine tena alikuwa amekabidhiwa kesi ambayo ilikuwa inaumiza kichwa na hakika alipenda kuumia kichwa.

    Akaombea kuwa huyo askari mwingine aliyewakamata hao walevi na yeye awe mchangamfu na anayependa kuumiza kichwa.



    TANGAZO likasikika, akaingia katika mstari wa kupekuliwa kisha akaingia ndani zaidi katika ukumbi wa kusubiri muda ufike, na baada ya nusu saa tayari alikuwa amezima simu yake na kuingia ndani ya ndege tayari kwa safari ya kuelekea jiji la Mwanza, kikazi!!

    Tena kazi aliyoipenda yeye mwenyewe.



    Kejo alifika uwanjani mapema kabla ndege haijatua, na ilipotua akabofya namba za mgeni wake. Wakafanikiwa kuonana, wote walikuwa wachangamfu na maumbo yao yalirandana kwa kiasi kikubwa.

    Wakapeana salamu mbili tatu kisha wakaingia katika daladala, wakaanza safari ya kuelekea kituoni huku wakiongea kwa uchangamfu kama vile ni marafiki wa miaka mingi.

    Huku wakapokelewa na inspekta Omari.

    Akazungumza nao kwa kirefu, kisha akawakabidhi rasmi kesi ile. Watafute ufumbuzi.

    Hatua ya kwanza ilikuwa kuwahoji wale walevi ambao sasa akili yao ilikuwa timamu. Wakabanwa kidogo ili waseme wanaufahamu vipi ule ujumbe na zile pesa nyingi walizokutwa nazo ni wapi walikuwa wamezitoa.

    Hapa wakaamua kukiri kuwa wao ni vibaka na walikwapua mkoba mahali na huku wakazikuta pesa zile.

    Walijieleza kwa kirefu sana wakielezea juu ya gari aina ya Toyota Vx ambalo lilikuwa limeegeshwa maeneo ya Igoma kwa muda mrefu bila ya mwenyewe kuonekana, wao wakaendelea kuvizia wafahamu kama kuna chochote waweze kukwapua, wakangoja hadi pale kilipozuka kizaazaa pale ambapo ndani ya gari ulikutwa mwili wa mwanamke akiwa amekufa.

    Ni hapa walipopata nafasi ya kukwapua mkoba. Wakataja mali walizozikuta ndani ya mkoba ule, wakataja simu ambayo walikiri kuwa waliiuza usiku uleule na vitu vingine kama vitambulisho ambavyo walidai kuwa walivitupa baada ya kupekua na kukutana na pesa. Wakaelezea mahali ambapo walivitupa vile vitambulisho.

    Kisha wakaletewa ujumbe uliokutwa katika pesa walizokamatwa nazo. Wakati wanazitazama Gasto alikuwa akiwatazama machoni, hakuna alichokiona katika macho yao, ni aidha hawakujua lolote kuhusiana na ujumbe ule ama la walikuwa wakiushangaa pia na kuuona wa kawaida.

    “Sijawahi kuona kitu kama hicho.” Mmoja alisema na mwenzake ambaye alikuwa katika chumba kingine alisema vilevile.

    Huu ulikuwa mtihani mkubwa sana kwa askari hawa!!

    Jijini Dar bwana Marko hajui lolote kuhusu ujumbe wa BADO SITA, na huku Mwanza walevi wanakiri kuwa ni mara yao ya kwanza kuona ujumbe wa BADO TANO.

    Balaa juu ya balaa!!

    Walevi wakarudishwa katika selo zao tofauti.

    Gasto na Martin Kejo walitumia muda kidogo tu kutambua kuwa kuna gari ilikutwa imetelekezwa na ndani yake alikuwa mwanamke mweupe ameuwawa kwa kupigwa risasi.

    Ina maana nani sasa alimuua!!

    Hilo likabaki kuwa swali.



    ***GASTO MUSHI na MARTIN KEJO katika upelelezi wa kesi ya aina yake…waliokamatwa hawajui lolote kuhusiana na makosa waliyotajiwa!!!

    Hakuna anayeujua ujumbe wala kujua nani aliyeuandika……

    Ujumbe huu kila ukionekana haunekani hivihivi..unaondoka na uhai wa mtu!!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    UTATA!!!!



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog