Simulizi : Harufu Ya Kifo
Sehemu Ya Tatu (3)
Kisha wakaletewa ujumbe uliokutwa katika pesa walizokamatwa nazo. Wakati wanazitazama Gasto alikuwa akiwatazama machoni, hakuna alichokiona katika macho yao, ni aidha hawakujua lolote kuhusiana na ujumbe ule ama la walikuwa wakiushangaa pia na kuuona wa kawaida.
“Sijawahi kuona kitu kama hicho.” Mmoja alisema na mwenzake ambaye alikuwa katika chumba kingine alisema vilevile.
Huu ulikuwa mtihani mkubwa sana kwa askari hawa!!
Jijini Dar bwana Marko hajui lolote kuhusu ujumbe wa BADO SITA, na huku Mwanza walevi wanakiri kuwa ni mara yao ya kwanza kuona ujumbe wa BADO TANO.
Balaa juu ya balaa!!
*****
Maelezo ya awali baada ya mahojiano yakafikishwa kwa mkuu wa upelelezi ambaye aliyawasilisha kwa Inspekta Omari.
Maelezo haya yakamfanya inspekta awaite tena wapelelezi wale ofisini kwake, akawaelezea juu ya ukweli fulani kutoka kwa walevi. Ni kweli kuna gari ipo pale kituoni na katika gari ile ilikutwa maiti ambayo ilikuwa na jeraha la kupigwa risasi.
Wapelelezi wakavutiwa nataarifa ile, wakamuhitaji mmiliki wa gari ile ambaye alitajwa kama mume wa marehemu. Walimuhitaji kwa sababu waliamini lipo la kumuuliza na yeye akajibu.
Siku iliyofuata Ramadhan alikuwa katika chumba cha mahojiano akihojiwa na Kejo maswali mepesi mepesi huku akingojewa mpelelezi mwingine ili waweze kwenda sawa.
Baada ya dakika chache mlango ukafunguliwa, Gasto akaingia akiwa amechangamka akipiga miluzi kwa mbali.
Akafika na kuchukua nafasi kisha macho yake na ya Rama yakakutana ana kwa ana. Wakatazamana kwa muda, Gasto akang’amua kuwa sura ile aliwahi kuiona mahali, lakini ni wapi? Hilo likawa swali, alitaka kumuuliza lakini alisita kwa sababu aliamini swali hilo litampa mwanga katika maelezo yake ya awali. Kama alitaka kudanganya atagairi na kusema ukweli ama kubadilisha muelekeo wa uongo wake kitaalamu.
Gasto akatulia.
Rama akaanza kujieleza kila kitu alichokuwa anajua kuhusu tukio lile na pia akijieleza yeye alikuwa wapi wakati tukio linatokea.
Rama alijieleza bila kutetereka kuwa alikuwa njiani akitokea jijini Dar es salaam kuja Mwanza ndipo tukio hilo lilitokea, akakumbushia juu ya simu aliyopokea kutoka kwa rafiki yake na kumweleza juu ya gari lake kuonekana mahali, baada ya hapo ukaingia ujumbe kutoka kwa mkewe, ujumbe mfupi kabisa. “UMENIUA MUME WANGU” akawaonyesha ujumbe ule kisha akaendelea mbele zaidi hadi hatua yake ya kwenda moja kwa moja eneo la tukio na kulikuta gari likiwa pweke pembezoni mwa barabara. Akaufungua mlango na kisha kukutana na maiti ya marehemu mke wake. Hapa macho ya Rama yakalengwa na machozi. Hakuna aliyejihangaisha na huzuni hiyo.
“Unasema Dar ulikuwa umeenda msibani?” Gasto aliuliza
“Ndio nilikuwa msibani afande.” Alijibu Rama.
Ni hapa ambapo Gasto alikuwa akingoja, akaikumbuka sura hii aliiona msibani siku ya kifo cha pili kikiambatana na ujumbe. Gasto akakiri kuwa yule bwana alikuwa hadanganyi hata kidogo.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Unadhani kwa nini mkeo alikutumia ujumbe huo wewe na si mtu mwingine?” aliuliza Kejo.
“Hata sifahamu hadi dakika hii, nilimpenda sana mke wangu yaani…” akaishia hapo akatupa mikono huku na kule. Sasa alikuwa analia.
Wapelelezi wale wakaendelea na maswali lakini hakuna hata moja lililowapa mwanga kuwa yawezekana Rama anahusika katika kifo cha mkewe na pia ujumbe ambao aliachiwa mkewe wa ‘BADO WATANO’ kisha ujumbe huo ukakwapuliwa na vibaka katika mkoba.
Rama akaruhusiwa kuondoka!!
Akaendelee na mazishi ya mkewe huku kiza kikitanda katika akili yake, hakujua ni kipi kimemsibu mkewe hadi auwawe kikatili hivyo.
“Nani huyu anayetuma ujumbe huu, na ni kitu gani anataka sasa. Hizo roho nyingine tano ni za nani sasa.” Wapelelezi walijiuliza bila kupata jibu la mara moja.
Kesi ikaanza kuwa ngumu kwao!!
****
BAADA YA SIKU TATU
DAR ES SALAAM
UKUMBI maarufu wa lango la jiji ulikuwa umezizima kwa mziki mzito wa taarabu, ukiwa kwa nje ungeweza kudhani palikuwa na pilika pilika za watu kuucheza muziki ule. Lakini haikuwa vile, ukumbi ulikuwa na watu wachache sana na kila mmoja alikuwa amejikita katika kunywa kinywaji kilichoendana na haja zake. Wengine walijidunga vinywaji baridi huku wengine wakiburudika kwa pombe mbalimbali.
Wasichana walikuwa na wanaume wao huku wakiwa wamevaa mavazi ya kupendeza kulingana na eneo lakini yalikuwa ya aibu kuu iwapo wangeonekana hivyo mchana kweupe.
Machangudoa na mashoga walianza kuingia majira ya saa nne usiku ambapo ukumbi ulikuwa umechachamaa, wale walevi walikuwa wamechanganyikiwa tayari na kufanya yale matendo ambayo pombe zimewatuma. Mashoga walijifanya kama watoto wa kike huku watoto wa kike machangudoa wakisaka wateja kwa nguvu zote. Marashi yao ya kuvutia yalizidi kufanya mahali hapo kuwa sahihi kabisa kuketi.
Changudoa mmoja naye alikuwa katika harakati za aina yake, tofauti na wenzake waliotaka mteja yeyote yule ilimradi pesa ipatikane, huyu alikuwa akimuwinda kijana mmoja ambaye alikuwa amejikita katika kunywa pombe yake bila kuwa na mtu pembeni yake.
Changudoa yule alijibaraguza na kujifaragua huku na kule, kisha akajiweka pembeni ya yule jamaa ambaye hakujali ujio ule. Ni kama alikuwa anautarajia au alikwishauzoea.
Changudoa alizidi kujishaua hatimaye yule kijana ambaye alikuwa ameanza kulewa kidogo akageuka kumtazama. Yule changudoa akatabasamu, wigi lake lililoziba macho yake kidogo lilimpendeza haswa. Na lile tabasamu likamfanya awe bidhaa inayonunulika upesi sana sokoni.
Mara yule kijana akaanza kumchombeza alipogundua kuwa hakuwa na mtu ambaye alikuwa anammiliki. Yule changudoa akaweka ngumu lakini baadaye akakubaliana na yule mlevi. Alifanya hivyo ilimradi tu kumhadaa yule kijana asijue lengo lake.
“Lakini hatulali na kama ni kulala bei inabadilika. Itakuwa themanini.” Changudoa alitoa masharti yake.
“Themanini kitu gani, nitakupa mia kamili.” Mlevi anayejitambua akapandisha dau.
Kijana aliyelewa akamkokota hadi nje, akampungia dereva taksi mkono, akasogea na gari yake, akawachukua hadi nyumba ya kulala wageni ya Mikumi. Hapo tayari msichana alikuwa amepokea nusu ya pesa alizotarajiwa kulipwa.
Wakaongozana kama wapenzi wa siku nyingi, changudoa akionekana kulewa zaidi ya yule mwanaume ambaye alijaribu kumkokota hapohapo akizidiwa na uchu na kutamani wafike ndani afanye alilokuwa anataka.
Chumba kikalipiwa wakaingia ndani.
Walipojifungia tu! Mambo yakabadilika. Yule changudoa aliyeonekana kuwa mlevi kupita yule mwanaume, akachangamka na kuwa kama ambaye hakunywa pombe hapo kabla.
Mlevi ambaye alionekana hakuwa mgeni kabisa na mambo ya kununua msichana kwa ajili ya kujiburudisha kingono, alikuwa anaondoa nguo zake kwa papara huku akionekana kuzidiwa kabisa na matamanio.
Wakati mlevi akijishughulisha na kuondoa nguo zake, binti na yeye alijishughulisha katika jambo moja tu.
Akaliondoa wigi lake upesi kisha akamgeukia yule mlevi. Mlevi akiwa uchi akakutanisha macho ana kwa ana na yule binti ambaye asingeweza tena kumuita changudoa.
Pombe zikayeyuka kutoka katika kichwa cha yule mlevi, akataka kukimbia lakini akimbilie wapi iwapo yule changudoa alikuwa mlangoni na mbaya zaidi alikuwa amemwonyesha bunduki? Hakuwa na tabasamu hata kidogo na hasira ilikuwa ikimchemka waziwazi.
“James….tulia kama ulivyo kisha piga hatua mbili nyuma na ukae kitandani kwa umakini kabisa unisikilize kama itabidi. Na uwe uchi hivyo hivyo usiiguse hata nguo moja, tukimaliza kuzungumza nitakupa ulichokilipia” Yule dada alinong’ona huku akiwa makini kwa kila hatua ambayo yule bwana alipitia.
“Isabela….Isa… lakini kwani….” Alijaribu kuzungumza yule mlevi huku akiwa amenyanyua mikono kama anayesihi jambo fulani..
“Kaa kitandani James kabla sijakufyatua.” Alikanya tena yule binti ambaye mapaja yake yalikuwa wazi kabisa na kitovu kikiwa nje. Sasa hakuwa legelege tena mwenye macho ya kumtega mwanaume, sasa alikuwa amekumbwa na hasira kali iliyowiva katika uso wake, alikuwa na kila dalili ya kuua iwapo aliye mbele yake asingeyasikiliza maneno yake na kuyatii.
“Kumbe unanikumbuka vizuri James kiburi, James jeuri. Asante nilidhani nitapoteza muda kujitambulisha sana. Kama umenikumbuka jina basi nadhani unajua nipo hapa kufanya nini…au ulidhani kuwa hatutakutana tena James” Alisema huku akiwa hajapoteza muhimili wake wala shabaha katika silaha aliyokuwa ameikamata. Mdomo wa bunduki ulichungulia kichwa cha James.
James alikuwa akitetemeka tu na bila shaka alikuwa anajutia kujiingiza katika tamaa za kutaka kushiriki penzi la changudoa asiyemfahamu nia yake. Lakini hapakuwa na muda wa kujuta tena, huyu aliyekuwa mbele yake hakuwa changudoa na ni heri angemuita mzuka ama mzimu kwa sababu alitokea katika mazingira ambayo hakuyatarajia.
“Unajisikiaje kuwa wanne katika orodha yenu ndefu, maana baada ya wewe atafuata mwingine kisha watabaki watatu wanaojifanya wajuaji sana. Na wenyewe nitawauliza kama ninavyokuuliza, halafu wewe umepata raha sana yaani hadi umenipapasa na kunibusu mdomoni aaargh ptuuuuuuu!!” akatema mate chini yule binti aliyeitwa Isabela..
James kimya alikuwa amenyanyua tu mikono juu huku akionekana kuwa hana ujanja wowote wa ziada. Alikuwa amekamatika.
“James unadhani unastahili kuishi? Unadhani unatakiwa kuitwa mwanadamu.” Aliuliza Isabela huku akitetemeka kwa hasira. James hakujibu kitu alibaki kuduwaa tu huku nafsi ikimsuta kwa yote yaliyotokea.
Akamkumbuka marehemu Lameck Magiri, marehemu Karama akawakumbuka, Temba, Justin, Zuwena Ally na Rama, Kokubanza na …..na yeye mwenyewe. Kwa hiyo alitakiwa kuuwawa ama vipi. Kabla hajapata mstakabali mzuri na wa uhakika mara alishtukia akikanyagwa teke kali kifuani, akaangukia kitandani. Akiwa hajategemea shambulizi lile mara alivamiwa pale kitandani akajaribu kufurukuta hakuweza. Akarusha miguu huku na kule katika namna ya kujitetea lakini hali ilikuwa tete. Adui alikuwa amejipanga vyema.
“Isabela utaniua…Isaaa…..” alilalama James pasi na mafanikio.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
*****
ASUBUHI mfanyakazi wa gesti ile ya Mikumi, akakutana na maajabu. Mteja alikuwa amelala hadi saa tano na hakuwa ametoa taarifa juu ya kuendelea kukitumia chumba kile. Mlango ulikuwa umerudishiwa vizuri na mteja alikuwa amejifunika shuka.
Mfanya usafi akaulizia mapokezi iwapo amuamshe ama vipi. Wakamwomba amuamshe ili aweze kujua nini kinaendelea. Kama anaendelea ama ndo amepitiwa bahati mbaya.
Akatii amri, akakifungua tena chumba akaanza kuita kwa sauti ya chini pasi na majibu yoyote, akapiga hatua na kuanza kumtikisa tikisa lakini hakusema chochote.
Mfanya usafi akaenda kutoa taarifa tena. Safari hii waliongozana watu watatu. Wakajaribu pia bila mafanikio yoyote kumwita huku wakimtikisa..
Hili likawa tatizo, mmoja akaamua kumpima mapigo ya moyo……walipobaini ya kuwa mteja wao alikuwa maiti tayari walibanana wote kwa pamoja waweze kupita katika mlango mmoja.
Doh! Maiti ni kitu kingine hakuna aliyetaka kuwa ndani ya kile chumba tena. Mbio mbio hadi mapokezi ambapo mkuu wao alikuwepo.
Taarifa ikatolewa polisi, wakafika baada ya saa moja wakaingia chumbani na hakika wakakuta mfu kitandani.
Wakiwa wamevaa mipira mikononi wakamgeuza kidogo kuona iwapo kuna jeraha.
Badala ya jeraha wakakutana na kikaratasi kikubwa lakini chenye maandishi machache, maandishi ambayo serikali ilikuwa imeanza kutikiswa nayo.
“BADO WATATU.”
Askari wakashtuka, walikuwa wameshuhudia kifo ambacho kina utata ndani yake, simu za upepo zikafanya kazi taarifa ikatolewa makao makuu ya polisi. Idadi ya wataalamu ikaagizwa kwenda eneo la Magomeni kwa ajili ya kuibuka na jibu la nini kinaendelea huko.
Baada ya dakika chache eneo lilikuwa limezingirwa na maaskari wenye sare na wasiokuwa na sare za kazi.
Marehemu alikufa kwa kukosa hewa muda mrefu. Alikuwa na alama za vidole za mwanamke.
Taarifa zikatumwa makao makuu.
Simu ikapigwa jijini Mwanza ambapo muuaji aliaminika kuishi huko na tayari alikuwa amekamatwa.
Kejo na Gasto Mushi wakapewa taarifa kuwa mauaji mengine yametokea na ujumbe wa sasa ni ‘BADO WATATU’
Wakachanganyikiwa wapelelezi hawa kisha wakakiri kuwa walikuwa wakipambana na adui ambaye alijua kuzipanga vyema karata zake. Kilichowaduwaza zaidi ni namba iliyotajwa…mwandiko uleule lakini sasa ni BADO WATATU….hii iliwashangaza maana walingojea kupata majibu kuwa ameua na sasa ameandika BADO NNE.
Hofu ikatanda kuwa huenda kabla ya mauaji hayo kuna tukio la mauaji jingine lilikuwa limefanyika.
Swali likabaki kuwa wale walevi na yule mlokole Dar wanahusika vipi katika hili. Wanaua vipi wakati wapo rumande??
****
WAKATI wapelelezi wakihaha jijini Mwanza, huku jijini Dar es salaam katika nyumba moja, mtu na mkewe walikuwa katika majadiliano mazito.
Majadiliano haya yalitokana na taarifa ya kifo cha James Bwire.
Mwanamke aliichukulia kiwepesi kama matukio mengine ambayo huwa yanatokea na kupotea lakini mwanaume sasa akili ilikuwa inafanya kazi katika uwezo usiokuwa wa kawaida kuhusisha matukio haya.
“Yaani mimi wasije tu wakaniulia mwangu” mweanamke alisema kama analaumu.
“Nilimwambia aachane nah ii kesi akabisha akadai kuwa anataka kufanya kazi. Mimi ningeweza vipi kumzuia sasa?” mwanaume naye alijibu katika namna ya kujitoa katika hatia.
“Lakini mume wangu wewe ni mkuu kwake, si ungeweza kutumia amri…”
“Mama Gasto, mwanao ni mbishi sana na unamjua tangu zamani, mbishi halafu anapenda kususa. Pale ningesimamia msimamo tu angekususia hadi wewe na mwisho ungesema mimi mbaya.” Alijitetea inspekta Seleli ambaye ni baba mzazi wa Gasto. Mama akanywea huku akikiri kuwa mzee hakuwa na kosa hata kidogo.
Mama Gasto alikuwa wa kwanza kusinzia akimwacha mumewe akihangaika kuusaka usingizi. Lakini sio hicho tu kilichomkosesha usingizi lakini lilikuwepo jinngine la ziada.
Mzee Seleli alikuwa akiwaza juu ya mlolongo wa vifo hivyo, havikushabihiana tu kwa sababu ya ujumbe ule ambao ulikuwa unaachwa lakini hata hawa watu waliokumbwa na umauti walikuwa wanahusiana katika jambo fulani. Lakini jambo hilo lilitokea kitambo sana lisingeweza kuwa na madhara kwa wakati huu.
“Wala hawezi kuwa Chausiku…” alijipinga kichwani mwake akibishana na hisia zake juu ya Chausiku. Hakutaka kujipa imani kuwa anaweza kuhusika katika mauaji.
“Labda kama kuna mtu anamlipia lakini kihivihivi sidhani…” alienedelea kuhangaisha kichwa chake bila jibu sahihi.
Kwa kuwaza kuwa hiki kinaweza kuwa kisasi ama mauaji yaliyokusudiwa, Seleli akamuwaza mwanaye Gasto ambaye alikuwa mstari wa mbele katika upelelezi huo. Mzee Seleli akamuhofia kuwa iwapo muuaji atajua kuwa anafuattiliwa anaweza kumuua kama namna ya kutoa onyo.
Mapigo ya moyo ya mzee Seleli yakaenda kasi huku akijisikia hali fulani ya kumuhofia muuaji japo alikuwa hajaamua kushika uamuzi mmoja kuwa yawezekana Chausiku anahusika.
*****
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wakati awali tukio hili likichukuliwa kuwa litaweza kushughulikiwa mara moja na kisha muuaji kupatikana na kufikishwa mbele ya sheria, hivi sasa mambo yalikuwa magumu.
Muuaji alizidi kuua, anaua Mwanza, wakimfuata mwanza anaua jijini Dar es salaam.
Kejo na Gasto maaskari wapelelezi waliopewa jukumu la kutambua nani muuaji walikuwa wamepagawa na kuchanganyikiwa kabisa. Hakika walilazimika kuchanganyikiwa kwa sababu huenda adui tayari alishatambua kuwa anatafutwa hivyo alikuwa katika tahadhari kuu.
Ilihitajika nguvu nyingine ya ziada kukabiliana na adui huyu asiyejulikana.
Gasto askari mpelelezi kutoka jijini Dar es salaam alitakiwa kurejea jijini Dare s salaam wakati Kejo alitakiwa asimamie na kuunda timu ya oparesheni msako jijini Mwanza ili kuwezesha kukamatwa kwa muuaji asiyefahamika anayeua kwa kujisikia huku akiweka wazi namba ya watu ambao anataka kuwaua.
Aliua jijini Dar bwana Lameck Kagiri, kisha akaua tena msibani bwana Karama, Mwanza akauwawa mwanamama Zuwena huku mumewe Rama akiwa anashutumiwa kumuua. Kumuua katika namna isiyosimulika. Anamuuaje mtu wakati yeye alikuwa safarini!!
Huu ukawa ni utata!!
Gasto akarejea jijini Dar es salaam kukabiliana na maiti ya bwana James ambaye aliuwawa katika nyumba ya kulala wageni huku akiachiwa ujumbe wa bado wanne.
Katika kazi zake za upelelezi akakiri kuwa huu ulikuwa upelelezi wenye changamoto ya hali ya juu sana!!
Gasto akapanda ndege na baada ya dakika kadhaa alikuwa akiranda randa katika jiji la Dar es salaam.
Tatizo likiwa halijatatuliwa!!!
Sasa hao wanne ni akina nani? Na kwa nini wanauwawa. Na ni nani anayewaua!! Mbaya zaidi amevuka namba moja! Au ndo ameua tayari….
Asubuhi ya siku iliyofuata alipitia vyema faili lililokuwa na taarifa juu ya kifo cha bwana James, akaguswa na taarifa ya muhudumu wa nyumba ile kuwa bwana James aliingia na mwanamke ambaye alifanania na changudoa.
Lakini asubuhi alikutwa akiwa pekee tena maiti.
Gasto aliomba kukutanishwa na muhudumu yule. Kisha akayasikiliza tena maelezo yake ambayo yalikuwa kama alivyoyaandika.
“Ukikutana na huyu mwanamke ambaye inasemekana ndiye muuaji unaweza kumtambua.”
“Akivaa kichangudoa lazima nitamtambua tu maana nilivutika kumtazama jinsi alivyokuwa anayumbayumba.” Alijibu muhudumu yule wa kiume kwa kujiamini. Kisha akaelezea muonekano wa changudoa yule aliyeingia na marehemu chumbani, maelezo yote yale hayakumjengea picha yoyote ile ambayo aliwahi kuiona mahali, lakini kwa kiasi yalimjenga na kumweka katika tahadhari iwapo atamuona mahali.
Afande Gasto alitoa maombi kwa inspekta wake juu ya kuhitaji kufanya mahojiano kadhaa katika nyumba ya marehemu James huenda kuna kisasi chochote wanachofahamu juu ya hili, na huenda huo ukawa mwanzo mzuri katika kufuatilia nyayo za huyo muuaji ambaye hajajionyesha hadharani.
Inspekta akabariki ombi la Gasto, akapewa mamlaka. Akawapa amri askari kadhaa kuongozana naye katika upelelezi huo.
Mzee Seleli ambaye ni Inspekta pia na baba mzazi wa Gasto alisikia juu ya harakati hizi za mwanaye, akatamani sana kumzuia lakini mwanaye alikuwa ameamua kufanya kazi na hakutaka litokee jambo lolote la kumrudisha nyuma.
Mzee huyu alifikiria kwa makini sana juu ya maelezo ya mwanaye juu ya mwonekano wa binti ambaye anasadikika kumuua James katika chumba cha kulala wageni. Mzee Seleli aliizungusha akili yake akimfikiria huyo binti ambaye anasadikika kuua, alijaribu kujichora sura yake lakini akaishia kupata maluweluwe.
Hakufanania na huyo Chausiku ambaye yeye alikuwa anamuwaza kuwa huenda anahusika katika vifo hivyo vyenye utata. Gasto alimshangaa sana mzee wake kwa jinsi alivyokuwa akiulizia juu ya sura ya hayo binti, lakini kwa sababu hata yeye alikuwa ni askari pia hakujali.
“Lakini Gasto ungejiweka mbali na mabo haya muujai anaonekana kuwa amejipanga na anajua mbinu zenu zote.” Mzee Seleli alimwambia mwanaye.
“Baba hivi uoga huu umeuanza lini, mbona unasimamia kesi nzito zaidi ya hii lakini unaonekana kuwa na wasiwasi tangu kesi hii inapoanza halafu mzee nakumbuka hata siku ya kwanza tulipogundua ujumbe katika mwili wa hayati mzee Lameck ambaye nui swahiba wako yuligoma kabisa kuturuhusu kuendelea na upelelezi, kwani kuna nini?” Gasto alihoji.
“Sijawahi kuwa muoga mwanangu, tatizo unampa presha mama yako!!! Gasto mama yako, wewe ni mwanaye wa pekee mambo ya familia ni ya familia ujue.” Alionya mzee Seleli.
Gasto akapuuzia.
*****
Mwanamke aliyekuwa amevaa hijabu zuri la rangi nyeusi alikuwa anatembea kwa haraka sana baada ya kushuka kutoka katika bajaji, alionekana kama mtu aliyekuwa amesahau kitu cha muhimu sana huko alipokuwa anaenda, urefu wa hijabu ulimzuia kutembea harakaharaka hivyo akalazimika kulikunja ili mwendokasi wake uongezeka.
Alifika na kusimama mbele ya geti kubwa jeusi maeneo ya Kibamba nje kidogo ya jiji la Dar es salaam.
Alitaka kugonga hodi lakini akasita, alikuwa anaikaribia shari kubwa sana, alikuwa anajaribu kucheza pata potea. Aliamini kwa asilimia zote kuwa kwa wakati huo na lengo lake alikuwa sahihi kabisa.
"Je kama Abdul yupo!!!" alijiuliza mwanamke huyu huku akiwa katika kuganda pale nje.
"Hata hivyo hatanitambua nikiwa na baibui hili!!!" alijipa matumaini na kisha akabonyeza kengele. Ilichukua sekunde kadhaa mlango ukafunguliwa.
Mlinzi akafungua kitundu akachungulia. Kisha akafungua mlango.
"Karibu sana dada karibu!!!" mlinzi alimkaribisha.
Macho ya mwanadada huyu yalikwepa kumtazama mlinzi alihofia huenda atamkumbuka, licha ya kwamba amevaa vazi hilo. Kwani haikuwa mara ya kwanza kuonana naye na tangu wakati ule alikuwa ni yeye bado katika geti hilo kama mlinzi. Enzi ambazo hataki kuzikumbuka tena.
"Wapo ndani??"
"Wapo dada zake na bosi na shemeji zake"
"Yeye mwenyewe yupo wapi??"
"Mh!! alitoka tangu jana na hajarudi hadi sasa hivi" alijibu mlinzi huku akijinyoosha viungo vyake.
Jibu hilo lilimpa faraja sana mawanamke huyu aliyekuwa hapo siku kadhaa nyuma aliwahi kufika katika nyumba hiyo na kumkuta mlinzi huyo huyo.
Hofu ya mlinzi kumtambua siku ile ndiyo ilikuwa imemrudisha. Hakutaka kutambuliwa na mtu yeyote kabla ya kutimiza haja zake hivyo mlinzi alikuwa amejiingiza katika hatia asiyoijua.
Isabela alitaka mauti ya Abdul yafanyike hapo hapo nyumbani kwake, lakini alihitaji kuzungumza naye kabla hajafikia hatua ya kumuangamiza hivyo kama mlinzi anayemtambua asipokuwepo basi kazi ingekuwa rahisi zaidi.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Isabela alijisogeza mahali mlinzi alipokuwa huku akijidai kutafuta mtandao kwa njia zote, ni kama alikuwa anaongea na mtu na hawaelewani vizuri.
Mtego wake ulinasa vyema akawa karibu na mlinzi na kwa kitendo cha dakika mbili tayari mlinzi alikuwa amenusa unga ambao Isabela alikuwa anataka aunuse. Taratibu akakaa chini na kuanza kupambana na usingizi, jaribio likashindikana akasinzia, Isabela akachomoa kisu haraka haraka akamchanja kidogo tu, katika mkono wake, sumu iliyokuwa katika ncha ikaenda kusalimiana na damu. Wakati anamalizia kukihifadhi kisu akasikia kengele inagongwa na baadaye geti likaanza kugongwa kwa nguvu.
"Mungu wangu au ni Aby amerejea!!! naumbuka leo.....ila la nammaliza hapa hapa" alizungumza na nafsi yake Isabela.
Taratibu akasogeza pua yake kuchungulia, hakuwa Aby kama anavyodhani lilikuwa gari la polisi na baadhi ya polisi wakiwa wamevaa sare zao walikuwa wanasubiri kufunguliwa geti.
Mkojo ukasogea kwa kasi Isabela akajaribu kubana miguu, ukapenya kidogo lakini chupi ikaumeza. Akaanza kutetemeka, akaamini ni yeye alikuwa anatafutwa!!!
"Nimekwisha kabla sijamaliza!!!" alisema kwa sauti ya chini, alitamani kumwondoa yule mlinzi ambaye sasa alikuwa maiti lakini muda haukuruhusu.
Askari walizidi kuligonga geti kwa mikono yao iliyokomaa kimazoezi huku wengine wakitumia virungu.
Isabela alibaki akiwa ameduwaa asijue nini cha kufanya, tayari alikuwa ameua na maiti ilikuwa pembeni yake. Alitamani kuzirudisha sekunde nyuma ili ajitoe hatiani lakini haikuwezekana.
“Hivi huyo Baraka hasikii…we Baraka wewe???” Sauti kutoka ndani ya nyumba ilisikika, sauti ile ilikuwa inaamrisha. Isabela aliamini kuwa baada ya amri hiyo inayotolewa kutofanyiwa kazi kitakachofuata ni huyo anayeamrisha kutoka nje kushuhudia kulikoni. Jambo hili Isabela hakutaka litokee maana mipango yake yote ingeharibika.
Kama alivyotegemea ndivyo hivyo ilivyotokea vishindo vilianza kusikika kwa mbali vikizidi kusogea.
“Nikizubaa nimekwisha!!!!” alijisemea Isabela kisha akafanya kitendo cha ghafla, akalisogelea geti akafungua kibati kidogo akachungulia.
“Fungua!!!” wakaamrisha askari. Isabela hakushtuka kwani aliutambua uwepo wao eneo hilo, alichofanya ni kufungua kama alivyoamrishwa. Wakati akifanya hivyo yule mwanamke aliyekuwa anafoka kwa sauti kali kutoka ndani alionekana nje.
“Shkamoo….” Isabela alisalimia kwa uoga wa kuigiza.
“Sogea pembeni!!!” Alifoka askari mmoja, Isabela aliponyanyua macho yake kumtazama wakajikuta wakishangaana kwa muda huku kila mmoja akijaribu kuvuta kumbukumbu ni wapi alimuona mwenzake hapo kabla. Yule askari alionekana kuwa amepoteza kumbukumbu upesi sana hivyo hakuendelea kuangaliana na Isabela kwani baibui lake lilikuwa limemficha sana, aliingia ndani akiwafuata wenzake.
“Mwenye nyumba yuko wapi?.” Aliulizwa Isabela. Akajibu kwa ishara akimuelekezea kidole mwanamama aliyekuwa amesimama kwa mbali, hakuwa akigomba tena.
Mlinzi naye alikuwa amelala kwa utulivu kama vile akishtuliwa kidogo ataamka.
ABDUL ni nani? Na Isabela anaitafuta orodha hii kwa sababu gani??
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment