Simulizi : Harufu Ya Kifo
Sehemu Ya Nne (4)
Mkojo ukasogea kwa kasi Isabela akajaribu kubana miguu, ukapenya kidogo lakini chupi ikaumeza. Akaanza kutetemeka, akaamini ni yeye alikuwa anatafutwa!!!
"Nimekwisha kabla sijamaliza!!!" alisema kwa sauti ya chini, alitamani kumwondoa yule mlinzi ambaye sasa alikuwa maiti lakini muda haukuruhusu.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Askari walizidi kuligonga geti kwa mikono yao iliyokomaa kimazoezi huku wengine wakitumia virungu.
Isabela alibaki akiwa ameduwaa asijue nini cha kufanya, tayari alikuwa ameua na maiti ilikuwa pembeni yake. Alitamani kuzirudisha sekunde nyuma ili ajitoe hatiani lakini haikuwezekana.
“Hivi huyo Baraka hasikii…we Baraka wewe???” Sauti kutoka ndani ya nyumba ilisikika, sauti ile ilikuwa inaamrisha. Isabela aliamini kuwa baada ya amri hiyo inayotolewa kutofanyiwa kazi kitakachofuata ni huyo anayeamrisha kutoka nje kushuhudia kulikoni. Jambo hili Isabela hakutaka litokee maana mipango yake yote ingeharibika.
Kama alivyotegemea ndivyo hivyo ilivyotokea vishindo vilianza kusikika kwa mbali vikizidi kusogea.
“Nikizubaa nimekwisha!!!!” alijisemea Isabela kisha akafanya kitendo cha ghafla, akalisogelea geti akafungua kibati kidogo akachungulia.
“Fungua!!!” wakaamrisha askari. Isabela hakushtuka kwani aliutambua uwepo wao eneo hilo, alichofanya ni kufungua kama alivyoamrishwa. Wakati akifanya hivyo yule mwanamke aliyekuwa anafoka kwa sauti kali kutoka ndani alionekana nje.
“Shkamoo….” Isabela alisalimia kwa uoga wa kuigiza.
“Sogea pembeni!!!” Alifoka askari mmoja, Isabela aliponyanyua macho yake kumtazama wakajikuta wakishangaana kwa muda huku kila mmoja akijaribu kuvuta kumbukumbu ni wapi alimuona mwenzake hapo kabla. Yule askari alionekana kuwa amepoteza kumbukumbu upesi sana hivyo hakuendelea kuangaliana na Isabela kwani baibui lake lilikuwa limemficha sana, aliingia ndani akiwafuata wenzake.
“Mwenye nyumba yuko wapi?.” Aliulizwa Isabela. Akajibu kwa ishara akimuelekezea kidole mwanamama aliyekuwa amesimama kwa mbali, hakuwa akigomba tena.
Mlinzi naye alikuwa amelala kwa utulivu kama vile akishtuliwa kidogo ataamka.
Baada ya kuwa amemrushia madaraka mwanamke huyo ambaye wala hakuwa akimfahamu, askari wote walielekeza macho yao kwa mama yule wa kiarabu.
Uzembe wa hali ya juu!!!!
Askari wote hawakumtilia maanani Isabela. Wote kama msafara wa kumbikumbi waliingia ndani. Wote wakihitaji kuzungumza na mama wa kiarabu.
Isabela alizitumia sekunde hizo chache kutoka nje. Huko palikuwa pametulia huku askari wawili wakiwa wametulia garini.
Isabela alitembea kwa mwendo wa kasi, alitamani kukimbia akihisi kuwa mauaji aliyoyafanya yatashtukiwa lakini alihofia kuwa huenda kuna mtu anamtazama anaweza kumshtukia.
“Wewe…..njoo hapa!!!.” Isabela alisikia sauti ikimwita kutokea kichochoroni. Alipogeuka likutana na jezi ya askari. Hofu ikamkumba maradufu. Akawa anatetemeka dhahiri akiamini kuwa huenda askari yule alikuwa amemshtukia.
Askari yule alikuwa ana bunduki kwapani. Alikuwa mweusi na hakuwa akitabasamu.
“Shkamoo…” Isabela alisalimia. Yule askari hakujibu badala yake akatoa tabasamu kubwa lililoruhusu meno yake meusi kuonekana huku mwanya usiokuwa na faida mdomoni nao ukifichuka.
“Unaenda wapi mtoto mzuri eeh!!.” Askari yule aliyekuwa anatisha alimuuliza Isabela kwa sauti iliyokoroma. Macho yake yalikuwa yanatangaza uchu…uchu mkubwa. Isabela alipoligundua hilo alipunguza presha.
“Naenda sokoni nimetumwa…” Alijibu kwa kusitasita.
“Unaitwa nani?.”
“Rebeka!!!.” Alidanganya.
“Aaah!! Sasa si unaenda halafu unarudi au??.” Aliuliza yule askari. Isabela akajibu kwa kichwa akimaanisha ndio.
“Aaah!!....” Kabla hajaendelea zaidi akasikia kipenga cha dharula kikipigwa. Mara moja akamsahau Isabela aliyejipachika jina la Rebeka. Akatimua mbio.
Isabela naye akatimua mbio. Alijua tayari mambo yameharibika huko nyuma.
Baibui lake alilipandisha hadi usawa wa magoti, hivyo akawa katika nafasi ya kukimbia vizuri.
Baada ya dakika chache alikuwa kwenye taksi akimtafakari Joshua Mathayo bila kumsahau Abdul Mangesho.
****
MIAKA SITA ILIYOPITA
Kesi yake aliyotegemea itachukuliwa uzito kwa jinsi suala lilivyokuwa wazi, ilipuuziwa. Kila siku alijibiwa majibu yanayokatisha tamaa waziwazi. Elimu yake ya darasa la saba ilimfanya anyanyasike. Kila mtu alijua kuwa alikuwa ametendewa unyama waziwazi lakini aliyemtendea unyama alikuwa akijumuika na marafiki wakinywa bia na nyama za kuchoma huku akijitapa kuwa hakuna wa kumbabaisha jijini Dar es salaam. Na kweli huenda kauli zake hizo zilikuwa na ukweli ndani yake. Kwani hata yule mpelelezi mashuhuri aliyesifika kwa roho yake mbaya alikuwa amelegezwa msimamo wake na kuwa kama bwege tu!!
“Joshua leo sitaweza kuja mwambie huyo mjinga..labda jumapili.” Ndiyo majibu aliyokuwa anayatoa mtu mzito huyu kwa mpelelezi huyu aliyeitwa Joshua Mathayo, mpelelezi aliyekuwa amekabidhiwa kesi ambayo ilikuwa ya kuweza kumpelekea mtuhumiwa kuhukumiwa kifungo cha Maisha ama miaka thelathini. Lakini kwa kuwa mtendwa alikuwa ni mtoto yatima, mtoto asiyekuwa na kwao. Mtoto asiyejua ladha ya mapenzi ya baba na mama.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ilikuwa ni kwa sababu mtendwa ni mfanyakazi wa ndani asiyejulikana hata katika mishahara ya wafanyakazi serikalini.
Mtendwa alikuwa ni Isabela John. Ndio maana haikupewa uzito hata kidogo.
Matusi aliyotukanwa na Joshua yalikuwa yanamuumiza, badala ya kuwa mshtaki sasa akawa kama mshtakiwa.
Taratibu akaanza kukata tamaa na hatimaye akatoweka. Hakwenda tena kituoni na hata uraiani hakuonekana.
Kwa kuwa alikuwa ni yule yule mpweke Isabela. Hakuna aliyejali.
Hata wangemkumbuka angewasaidia nini?? Hakuwa na lolote katika jamii.
WAKATI ULIOPO
Isabela alikuwa akizitafakari kauli za Joshua miaka sita iliyopita na kumchukulia kati ya watu walioweka kauzibe asiweze kutendewa haki zake za msingi.
Joshua akajengeka kama muuaji, asiyekuwa na huruma.
Macho yake aliyokutanisha na Isabela, yalitangaza dhahiri kuwa alikuwa hafai kuitwa mwanadamu maana alipewa jukumu la kuitetea na kuilinda haki ya raia yeyote lakini yeye akajichagulia watu wa kuwatendea haki.
“Hata yeye anastahili kuwa katika orodha hii!!!” Isabela alijisemea huku akiwa ameuma meno yake kwa hasira.
Mara ya mwisho kukutana na Joshua alikuwa na miaka 21 sasa ana miaka 27. Hakuwa na uwezo wa kujinunulia walau chakula lakini sasa alikuwa na pesa za kutumia.
Isabela yule wa miaka 6 iliyopita si huyu tena!!!! Isabela alikuwa amebadilika.
***
Kifo cha mlinzi wa getini katika nyumba ya marehemu Aby kilichotokea masaa machache baada ya kifo cha James ambaye alikuwa swahiba wa Aby na siku chache baada ya kifo cha mwanamke aitwaye Zuwena jijini Mwanza. Vilizua utata wenye utata ndani yake.
Mlinzi hakuachiwa ujumbe wowote lakini mwanamke wa Mwanza aliachiwa ujumbe wa bado watano, kisha James akaachiwa ujumbe wa bado watatu.
Sasa ameuwawa mlinzi katika geti la Abdul.
Na haijulikani ni wapi huyo Abdul yupo!!
Gasto aliunganisha matukio haya na kuamini kuwa kupatikana kwa Abdul ambaye kwa namna moja au nyingine alikuwa amenusurika kufa kunaweza kuleta mwanga!!
Akina mama nyumbani kwa Abdul walikiri kuwa yule msichana mwenye baibui hakuwa akijulikana kwao, na wao walidhani kuwa alikuwa amekuja na wale polisi.
Hakika alikuwa amewatoka kizembe!!
Taarifa zilisambaa kila mahali juu ya mwanamke mwenye baibui akiwa na rangi ya chungwa. Mwanamke huyu aliyetambuliwa sauti yake na askari mwenye sura mbaya aliyezungumza naye dakika chache kisha akatoweka huku Sajenti Joshua akikiri kuyatambua macho yake.
Mkuu wa jeshi la polisi alitoa tamko rasmi la upelelezi yakinifu huku akiahidi kumtia mikononi mwanamke huyu ambaye sasa alibebeshwa kesi za mauaji zisizopungua nane.
Picha mbalimbali za kinamama wa dini ya kiislamu waliovaa mabaibui zilipamba kurasa za mbele za magazeti mengi lakini hakuna hata picha moja iliyokuwa ya muhusika.
Hakuna picha iliyokuwa ya Isabela.
Taarifa za kutafutwa kwake, alizisikia akiwa hotelini akipata kifungua kinywa. Taarifa zile hazikumshtua bali kumpa umakini zaidi juu ya hatua anazotakiwa kuchukua ili kumaliza zoezi lake bila kujulikana.
Lakini taarifa iliyomgusa zaidi ni juu ya kifo cha Abdul kwa kujinyonga. Isabela akasita kidogo kisha akapumua kwa nguvu zaidi. Aliamini kuwa akimpata Abdul ndipo atapata utatuzi wa kuweza kumaliza orodha yake pasi na kikomo.
Nani amemuua Aby sasa!!! Alijiuliza Isabela bila kupata jawabu. Inawezekana amejiua kweli ama!!!
Hakuamini hata kidogo, huyo Abdul alivyokuwa na roho mbaya na jasiri kupitiliza angeweza kuamua kuchukua hatua ya kujitia kitanzi kirahisi namna ile!!!
Hapana haiwezekani!! Alikataa.
Baada ya kumaliza kutumbua mazagazaga mengi, alilipia na kutoweka pale akiwa hana wasiwasi hata kidogo. Na wakati huu akiwa hana baibui, bali alikuwa amevalia kama wasichana wengi wa Dar es salaam ambavyo huwa wanavaa.
Hatua kwa hatua, mguu wake ukamfikisha katika nyumba ya kupanga. Ambayo ilikuwa na wapangaji wengi sana huku wengi wao wakiwa na watoto wadogo. Hili lilidhihirishwa na vinyesi vya hapa na pale na nguo nyingi za watoto zilizojaza kamba ya kuanikia nguo.
“Katotoooo!!!.” Isabela aliita, mtoto mmoja akamsogelea. Isabela akamfuta futa kichwani huku akimuuliza maswali.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Baba Swebe yuko wapi..”
“Baba Swebe…”
“Eeeh!! Baba Swebe yule mrefu yupo?”
“Baba Swebe hayupo alihamia kuleee”
“Wapi?”
“Kule hivi…ile nyumba nyeupe ile hapo hapo” alitoa maelekezo hayo yule mtoto ambaye alionekana kuwa mjanjamjanja.
Isabela alipenyeza chochoro hadi akaifikia nyumba aliyoelekezwa.
“Samahani mamdogo..ba Swebe nimemkuta?.” Aliuliza huku akijitia kujiamini sana.
“Yupo hapo mlango wa kwanza.”
“Asante sana.” Alimaliza Isabela huku akiuendea mlango na kugonga akaruhusiwa kuingia.
Bila hiyana akaingia ndani. Aliyemtegemea akamkuta.
Hasira zikampanda sana. Akajaribu kuzidhibiti, zikamshinda akaanza kutetemeka.
Mzee wa umri wa miaka sitini alikuwa anatetemeka kitandani, alikuwa amepata kumjua aliyeko mbele yake. Alijaribu kujichekesha lakini hakujibiwa tabasamu lake.
Alitaka kupiga kelele lakini ghafla mambo yalibadilika. Mshangao ukachukua nafasi yake!!!!
Isabela alikuwa akimtazama mzee huyu wa makamo kwa jicho lililojaa chuki. Baba Swebe alijaribu kujichekesha lakini Isabela hakujaribu kufanya kosa lolote.
Nia yake haikuyumbishwa na mzee aliyekuwa mbele yake mzee ambaye miaka sita iliyopita alimjengea imani na heshima kubwa huku akiamini ni yeye pekee ambaye atamkomboa katika Maisha yake. Safari ya kutoka kijijini Malimbwe huko Kahama hadi kulifikia jiji pendwa la Dar es salaam haikuwa safari fupi.
“Usomee kwa bidii mwanangu…huko mjini uwe makini sawa!!!.” Sauti ya upole kabisa ya mama mwenye upendo ilimsihi mtoto wa kike aliyekuwa analia sana, dalili za kutangaza ukiwa atakaokumbana nao huko atakapokuwa. Mwanaume wa makamo aliyeonekana kutofautiana na wanaume wengine hapo kijijini alikuwa akimbembeleza yule msichana asilie sana kwani hapo ni nyumbani na wazazi wake atawakuta kila siku.
Binti alijaribu kujikaza asilie lakini machozi na kilio cha kwikwi vilisikika kwa mbali. Mama hakuwa na la kusema, wakaisogelea barabara, binti akaigeukia nyumba yao ya matope akaiaga kwa kuitazama na chozi kuidondokea ardhi kavu iliyowanyima mazao kwa muda mrefu.
Ardhi ikalipokea chozi lile kwa ulafi, ikalimeza kama ilivyommeza mzazi wa kiume wa binti huyu likatoweka usoni pa dunia. Gari ikapigwa mkono ikasimama, binti akabeba kiroba chake kidogo akapanda garini akiwa ameongozana na mzee huyu mtanashati. Mama akapunga mkono binti naye akapunga gari ikatoweka.
Mama akabaki mpweke, yule binti aliyemzoea akawa ameondoka na mwanaume huyu mtanashati kwa ajili ya kwenda kumsomesha.
Mwanaume huyu hakuwa na undugu wowote na familia ya binti huyu, lakini mwanaume huyu alikuwa rafiki kipenzi wa marehemu baba wa binti.
Walidumu katika urafiki kwa miaka mingi wakati huo mwanaume huyu akiitwa Justin na marehemu akiitwa Samson. Baadaye Samson akapata mtoto, jina lake likawa baba Chiku, baada ya mwaka mmoja na yeye Justin akapata mtoto, akaitwa Swebe na yeye akawa maarufu kwa jina la baba Swebe.
Ukaribu huu ukajenga undugu. Mzee Samsoni alipofariki baba Swebe alikuwa jijini Dar es salaam, tayari alikuwa amehamishia makazi huko.
Alipokuja msibani, alizungumza faragha na mama Chiku na kumsihi kuwa ameamua kumsomesha Chiku ili siku moja aje kumkomboa kimaisha.
“Kwa hiyo nitakuja kumchukua na kwenda naye mjini akasome huko.”
“Utakuwa umenisaidia sana shemeji yangu!!! Yaani Mungu akubariki sana.” Mama Chiku alitoa shukrani zake za dhati, baba Swebe akazipokea.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya miezi mitatu ya kusubiri, sasa baba Swebe alikuja na kumchukua Chiku. Safari ya kuelekea mjini.
Chiku kwa mara ya kwanza anaingia jijini. Lengo likiwa kusoma.
Nyumbani kwa baba Swebe, Chiku anamkuta mke wa baba Swebe lakini huyu hakuwa mama yake na swebe, huyu alikuwa ni binti tu. Tena ambaye hata hakuonyesha dalili za kuwa amezaa.
Swebe naye hakuwepo nyumbani. Chiku hakuuliza!!!!
Ile shule aliyoitegemea haikuwepo tena. Kwanza akageuzwa kijakazi. Kama hiyo haitoshi akageuzwa mwili wa kufanyia mazoezi ya kupigwa na baadaye walipomchoka wakamtafutia kazi. Kazi ya uhausigeli. Kazi ambayo Chiku aliona ni afadhali atakuwa akilipwa pesa na mwisho wa siku apate nauli ya kurudi kijijini kwa mama yake.
Hiyo nayo haikuwa kazi bali mtego, mtego ulionasa kilaini.
Yaliyomtokea Chiku miaka hiyo, leo hayataki kufutika hadi hapo tu atakapolipiza kisasi. Sasa alikuwa mbele ya Baba Swebe. Mzee mnyama kabisa, hakuwa Chiku tena bali Isabela.
Roho ya unyonge ya Chiku ilikuwa imeenda likizo wakati baba Swebe akijaribu kuudhibiti usingizi wa ghafla uliomnyemelea. Isabela alikuwa akimsubiri asinzie ili aweze kutimiza lengo lake.
Jicho la baba Swebe lilimtoka pima, alishuhudia kisu kikali kikitolewa katika mkoba wa Isabela. Alitamani kukimbia lakini alikuwa na usingizi mzito. Alitamani kupiga kelele lakini na mdomo nao ulikuwa kama umewekewa gundi
“Chiku….Chiku….we……” Hakufanikiwa kuimaliza kauli yake, maumivu makali yakautenganisha uhai wake na dunia. Uhai ukaenda kutalii katika pepo nyingine. Utalii wa milele.
Ule uchungu wa miaka sita iliyopita ukawa umepungua kidogo!!!
Uchungu wa kupoteza kila kilicho muhimu katika Maisha yake.
“Kilaaniwe kizazi chako chote kama ulivyoniletea laani hii.:” Alizungumza Isabela huku akitoweka kutoka katika chumba kile.
Hakuwa na walau tone la damu!!!!
Bila shaka hakuwa mgeni katika kuua.
Nyuma aliacha ujumbe wake kuwa ‘BADO WAWILI’
****
Kijasho chembamba kiliwatoka Gaston na Kejo. Ile kesi waliyokuwa wakiipeleleza ikaonekana kuwa ngumu zaidi kutokana na jinsi mtiririko wa matukio ulivyokuwa.
Alikuwa ni Gasto ambaye alimpigia simu Kejo kumwelezea juu ya kifo cha baba Swebe na kisha kuachiwa ujumbe wa bado wawili.
Ujumbe huu uliwapagawisha maaskari hawa na kujiuliza mbona namba tatu imerukwa, hapa Gasto akaamini kabisa kuwa kujinyonga kwa Abdul hapakuwa pa burebure palikuwa na sababu na huenda ni huyu alikuwa kati ya wanne waliokuwa wamebaki, lakini kujinyonga kwake kukasababisha namba moja irukwe.
Kuna siri kubwa sana hapa si bure!!!
Alisema Kejo na Gasto akaunga mkono hoja!!
Wakaamua kujipanga tena upya kutafuta namna ya kuweza kukabiliana na huyo mwanadamu anayeua kadri anavyopenda!!
Tena anaweka na orodha!!
Ilikuwa saa kumi jioni, kila mtu alikuwa kwenye pilikapilika za kurejea nyumbani hii ilitokana na tatizo kubwa la usafiri jijini Dar es salaam.
Sio kila mtu alikuwa salama, wapo wengine muda huo hawakuwa wakijua lolote lile juu ya harakati hizo kwani walikuwa ni wagonjwa vitandani. Wenye magari yao binafsi hawakuwa na hofu ya kutokwa jasho, tatizo kwao lilikuwa ni foleni ndefu za jijini Dar. Kwa wale wajanja wa mjini walijua vichochoro vya kupita ili wawahi kufika huko waendako.
Ilikuwa ngumu sana kugundua kwamba alikuwa ni padri wa kanisa fulani hapo jijini kwa jinsi alivyokuwa amevaa, suruali ya kitambaa kigumu nzuri sana ikisindikizwa na fulana iliyouonyesha vyema mwili wake wa mazoezi. Tabasamu jepesi liliuvaa uso wake na kumfanya avutie kumtazama. Mwendo wake haukuwa kero kabisa kwa atakayetaka kumtazama, na ungetamani kumsihi asiingie katika gari dogo aina ya Vitara ilimradi u uendelee kumtazama lakini haikuwezekana. Huenda hakujua kama anatazamwa na watu wengi hasahasa akina dada. Wengi wa wasichana waliomtazama walivutiwa kimapenzi lakini ni mmoja tu ambaye hakujali utanashati wa bwana huyu. Huyu alikuwa kila mara akiitazama saa yake na punde baada ya padri yule kuwasha gari yake naye aliingia katika taksi na kutoweka. Kuelekea anapojua mwenyewe.
Hakuna aliyemjali!!!
Wakati yule msichana anaondoka iliingia gari nyingine akashuka msichana ambaye aliwasahaulisha waliokuwa na mawazo ya kumtazama padri. Sasa walimtazama binti huyu ambaye kwa neno moja tu ungeweza kumuita mrembo!! Hakika alikuwa mrembo haswaa.
Sasa ilikuwa zamu ya wanaume nao kumthaminisha na kutamka wanayoyaweza. Wasichana walijifanya hawamuoni huku kimoyomoyo wakikiri kuwa alikuwa ameumbika.
Moja kwa moja aliingia katika kituo kile cha afya. Haikuonekana kama alikuwa na ugonjwa wowote ule, alikuwa amenawiri na mwenye afya.
Labda amekuja kusalimia mgonjwa wake!!! Waliwaza hivyo wale waliokuwa wakimtazama.
Alijongea kwa mwendo wa madaha hadi akaifikia sehemu ya mapokezi. Alikuwepo kijana mrefu, jicho la matamanio likatua katika kifua cha yule dada.
“Dokta Temba yupo ofisini kwake!!!.” Aliuliza kwa sauti nyororo isiyohusisha kubana pua.
“Aaah!! Ametoka kidogo lakini muda si mrefu anarejea.” Alijibu huku akifumbata mikono yake na kuisuguasugua midomo yake. Dalili za uoga.
“Aaah!! Unaweza kumsubiri hapo, amesema hachelewi.” Alizidi kujiumauma.
Yule binti hakujibu kitu, akajisogeza pale kwenye benchi akakaa, harufu yake ya manukato ya bei ghari ikameza harufu kali ya madawa kwa muda.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Dakika zikaanza kuhesabika huku mikao ikikaribia kuisha, maana tayari alishakunja nne, alikuwa ameinama tayari, alisimama kwa muda, alichuchumaa, alijaribu kusinzia na bado dokta Temba hakutokea.
Yalikuwa yamepita masaa manne, na ilikuwa saa mbili usiku.
Yule kijana aliyemwambia yule binti kuwa dokta atarejea mapema aibu zikawa zimemshika, akajiuliza ataanza vipi kumweleza yule binti kuwa aondoke na kurejea kesho baada ya kuwa amempotezea masaa mengi kiasi kile.
Akiwa katika kujiuliza hayo alisikia simu ya pale mapokezi ikitoa mlio, akaisogelea na kuitazama kisha akapokea.
Sauti nzito upande wa pili ilikuwa inaongea. Kwa amri ilizokuwa inatoa yule kijana mrefu aliamini kuwa ni askari hata kabla hawajajitambulisha.
“Ndio..aliondoka saa za jioni jioni…kama saa kumi….ndio….eeeh!! hapana…..hakunieleza,…kwani vipi?” Alisikika akihoji na kuhojiwa. Baada ya hapo akakata simu. Hofu ikawa imemtawala.
“Mh!! Dokta sijui amekuwaje??” Alizungumza kijana mrefu binti akamsikia akasimama.
“Kwani vipi?.” Aliuliza yule binti.
“Polisi wamepiga simu wameniuliza maswali, siwaelewi.” Alijibu huku akilazimisha lile tabasamu lake litokeze.
Hakujibiwa kitu chochote yule binti mrembo akatoweka.
Hakumuaga mtu.
Akajichukulia nafasi ndani ya taksi akaamuru apelekwe Magomeni.
Huko alijifungia chumbani kwake alipokuwa amepanga kwa muda, akanza kufanya tafakari.
Usingizi ukampitia bila hata kuvua viatu. Aliposhtuka alfajiri akaiendea luninga akaiwasha.
Kilikuwa kipindi cha magazeti katika luninga.
“Padri auwawa nyumba ya kulala wageni, damu yake yatumika kuandika maneno BADO MWINGINE.”
Binti akasimama wima na kutaka kukimbia baada ya kuishuhudia picha ya dokta Temba. Wasiwasi ukamjaa. Akatamani kupiga kelele za kuomba msaada lakini akajizuia huku akikibana kichwa chake ili akili ikae sawasawa.
“Nani huyo amemuua padri.” Alijiuliza hakupata jibu.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment