Search This Blog

Sunday, 19 June 2022

HARUFU YA KIFO - 5

 





    Simulizi : Harufu Ya Kifo

    Sehemu Ya Tano (5)



    Joshua akajengeka kama muuaji, asiyekuwa na huruma.

    Macho yake aliyokutanisha na Isabela, yalitangaza dhahiri kuwa alikuwa hafai kuitwa mwanadamu maana alipewa jukumu la kuitetea na kuilinda haki ya raia yeyote lakini yeye akajichagulia watu wa kuwatendea haki.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hata yeye anastahili kuwa katika orodha hii!!!” Isabela alijisemea huku akiwa ameuma meno yake kwa hasira.

    Mara ya mwisho kukutana na Joshua alikuwa na miaka 21 sasa ana miaka 27. Hakuwa na uwezo wa kujinunulia walau chakula lakini sasa alikuwa na pesa za kutumia.

    Isabela yule wa miaka 6 iliyopita si huyu tena!!!! Isabela alikuwa amebadilika.



    ***

    Kifo cha mlinzi wa getini katika nyumba ya marehemu Aby kilichotokea masaa machache baada ya kifo cha James ambaye alikuwa swahiba wa Aby na siku chache baada ya kifo cha mwanamke aitwaye Zuwena jijini Mwanza. Vilizua utata wenye utata ndani yake.

    Mlinzi hakuachiwa ujumbe wowote lakini mwanamke wa Mwanza aliachiwa ujumbe wa bado watano, kisha James akaachiwa ujumbe wa bado wanne.

    Sasa ameuwawa mlinzi katika geti la Abdul.

    Na haijulikani ni wapi alipo huyo Abdul!!



    Gasto aliunganisha matukio haya na kuamini kuwa kupatikana kwa Abdul ambaye kwa namna moja au nyingine alikuwa amenusurika kufa kunaweza kuleta mwanga!!

    Akina mama nyumbani kwa Abdul walikiri kuwa yule msichana mwenye baibui hakuwa akijulikana kwao, na wao walidhani kuwa alikuwa amekuja na wale polisi.

    Hakika alikuwa amewatoka kizembe!!



    Taarifa zilisambaa kila mahali juu ya mwanamke mwenye baibui akiwa na rangi ya chungwa. Mwanamke huyu aliyetambuliwa sauti yake na askari mwenye sura mbaya aliyezungumza naye dakika chache kisha akatoweka huku Sajenti Joshua akikiri kuyatambua macho yake.

    Mkuu wa jeshi la polisi alitoa tamko rasmi la upelelezi yakinifu huku akiahidi kumtia mikononi mwanamke huyu ambaye sasa alibebeshwa kesi za mauaji zisizopungua nane.

    Picha mbalimbali za kinamama wa dini ya kiislamu waliovaa mabaibui zilipamba kurasa za mbele za magazeti mengi lakini hakuna hata picha moja iliyokuwa ya muhusika.

    Hakuna picha iliyokuwa ya Isabela.



    Taarifa za kutafutwa kwake, alizisikia akiwa hotelini akipata kifungua kinywa. Taarifa zile hazikumshtua bali kumpa umakini zaidi juu ya hatua anazotakiwa kuchukua ili kumaliza zoezi lake bila kujulikana.

    Lakini taarifa iliyomgusa zaidi ni juu ya kifo cha Abdul kwa kujinyonga. Isabela akasita kidogo kisha akapumua kwa nguvu zaidi. Aliamini kuwa akimpata Abdul ndipo atapata utatuzi wa kuweza kumaliza orodha yake pasi na kikomo.

    Nani amemuua Aby sasa!!! Alijiuliza Isabela bila kupata jawabu. Inawezekana amejiua kweli ama!!!

    Hakuamini hata kidogo, huyo Abdul alivyokuwa na roho mbaya na jasiri kupitiliza asingeweza kuamua kuchukua hatua ya kujitia kitanzi kirahisi namna ile!!!

    Hapana haiwezekani!! Alikataa.



    Baada ya kumaliza kutumbua mazagazaga mengi, alilipia na kutoweka pale akiwa hana wasiwasi hata kidogo. Na wakati huu akiwa hana baibui, bali alikuwa amevalia kama wasichana wengi wa Dar es salaam ambavyo huwa wanavaa.

    Hatua kwa hatua, mguu wake ukamfikisha katika nyumba ya kupanga. Ambayo ilikuwa na wapangaji wengi sana huku wengi wao wakiwa na watoto wadogo. Hili lilidhihirishwa na vinyesi vya hapa na pale na nguo nyingi za watoto zilizojaza kamba ya kuanikia nguo.

    “Katotoooo!!!.” Isabela aliita, mtoto mmoja akamsogelea. Isabela akamfuta futa kichwani huku akimuuliza maswali.

    “Baba Swebe yuko wapi..”

    “Baba Swebe…”

    “Eeeh!! Baba Swebe yule mrefu yupo?”

    “Baba Swebe hayupo alihamia kuleee”

    “Wapi?”

    “Kule hivi…ile nyumba nyeupe ile hapo hapo” alitoa maelekezo hayo yule mtoto ambaye alionekana kuwa mjanjamjanja.

    Isabela alipenyeza chochoro hadi akaifikia nyumba aliyoelekezwa.

    “Samahani mamdogo..ba Swebe nimemkuta?.” Aliuliza huku akijitia kujiamini sana.

    “Yupo hapo mlango wa kwanza.”

    “Asante sana.” Alimaliza Isabela huku akiuendea mlango na kugonga akaruhusiwa kuingia.

    Bila hiyana akaingia ndani. Aliyemtegemea akamkuta.

    Hasira zikampanda sana. Akajaribu kuzidhibiti, zikamshinda akaanza kutetemeka.

    Mzee wa umri wa miaka sitini alikuwa anatetemeka kitandani, alikuwa amepata kumjua aliyeko mbele yake. Alijaribu kujichekesha lakini hakujibiwa tabasamu lake.

    Alitaka kupiga kelele lakini ghafla mambo yalibadilika. Mshangao ukachukua nafasi yake!!!!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Isabela alikuwa akimtazama mzee huyu wa makamo kwa jicho lililojaa chuki. Baba Swebe alijaribu kujichekesha lakini Isabela hakujaribu kufanya kosa lolote.

    Nia yake haikuyumbishwa na mzee aliyekuwa mbele yake mzee ambaye miaka sita iliyopita alimjengea imani na heshima kubwa huku akiamini ni yeye pekee ambaye atamkomboa katika Maisha yake. Safari ya kutoka kijijini Malimbwe huko Kahama hadi kulifikia jiji pendwa la Dar es salaam haikuwa safari fupi.

    “Usome kwa bidii mwanangu…huko mjini uwe makini sawa!!!.” Sauti ya upole kabisa ya mama mwenye upendo ilimsihi mtoto wa kike aliyekuwa analia sana, dalili za kutangaza ukiwa atakaokumbana nao huko atakapokuwa. Mwanaume wa makamo aliyeonekana kutofautiana na wanaume wengine hapo kijijini alikuwa akimbembeleza yule msichana asilie sana kwani hapo ni nyumbani na wazazi wake atawakuta kila siku.

    Binti alijaribu kujikaza asilie lakini machozi na kilio cha kwikwi vilisikika kwa mbali. Mama hakuwa na la kusema, wakaisogelea barabara, binti akaigeukia nyumba yao ya matope akaiaga kwa kuitazama na chozi kuidondokea ardhi kavu iliyowanyima mazao kwa muda mrefu.

    Ardhi ikalipokea chozi lile kwa ulafi, ikalimeza kama ilivyommeza mzazi wa kiume wa binti huyu likatoweka usoni pa dunia. Gari ikapigwa mkono ikasimama, binti akabeba kiroba chake kidogo akapanda garini akiwa ameongozana na mzee huyu mtanashati. Mama akapunga mkono binti naye akapunga gari ikatoweka.

    Mama akabaki mpweke, yule binti aliyemzoea akawa ameondoka na mwanaume huyu mtanashati kwa ajili ya kwenda kumsomesha.

    Mwanaume huyu hakuwa na undugu wowote na familia ya binti huyu, lakini mwanaume huyu alikuwa rafiki kipenzi wa marehemu baba wa binti.

    Walidumu katika urafiki kwa miaka mingi wakati huo mwanaume huyu akiitwa Justin na marehemu akiitwa Samson. Baadaye Samson akapata mtoto, jina lake likawa baba Chausiku, baada ya mwaka mmoja na yeye Justin akapata mtoto, akaitwa Swebe na yeye akawa maarufu kwa jina la baba Swebe.

    Ukaribu huu ukajenga undugu. Mzee Samsoni alipofariki baba Swebe alikuwa jijini Dar es salaam, tayari alikuwa amehamishia makazi huko.

    Alipokuja msibani, alizungumza faragha na mama Chausiku na kumsihi kuwa ameamua kumsomesha Chausiku ili siku moja aje kumkomboa kimaisha.

    “Kwa hiyo nitakuja kumchukua na kwenda naye mjini akasome huko.”

    “Utakuwa umenisaidia sana shemeji yangu!!! Yaani Mungu akubariki sana.” Mama Chausiku alitoa shukrani zake za dhati, baba Swebe akazipokea.

    Baada ya miezi mitatu ya kusubiri, sasa baba Swebe alikuja na kumchukua Chausiku. Safari ya kuelekea mjini.

    Chausiku kwa mara ya kwanza anaingia jijini. Lengo likiwa kusoma.

    Nyumbani kwa baba Swebe, Chausiku anamkuta mke wa baba Swebe lakini huyu hakuwa mama yake na swebe, huyu alikuwa ni binti tu. Tena ambaye hata hakuonyesha dalili za kuwa amezaa.

    Swebe naye hakuwepo nyumbani. Chausiku hakuuliza!!!!

    Ile shule aliyoitegemea haikuwepo tena. Kwanza akageuzwa kijakazi. Kama hiyo haitoshi akageuzwa mwili wa kufanyia mazoezi ya kupigwa na baadaye walipomchoka wakamtafutia kazi. Kazi ya uhausigeli. Kazi ambayo Chausiku aliona ni afadhali atakuwa akilipwa pesa na mwisho wa siku apate nauli ya kurudi kijijini kwa mama yake.

    Hiyo nayo haikuwa kazi bali mtego, mtego ulionasa kilaini.

    Yaliyomtokea Chausiku miaka hiyo, leo hayataki kufutika hadi hapo tu atakapolipiza kisasi. Sasa alikuwa mbele ya Baba Swebe. Mzee mnyama kabisa, hakuwa Chausiku tena bali Isabela.

    Roho ya unyonge ya Chausiku ilikuwa imeenda likizo wakati baba Swebe akijaribu kuudhibiti usingizi wa ghafla uliomnyemelea. Isabela alikuwa akimsubiri asinzie ili aweze kutimiza lengo lake.

    Jicho la baba Swebe lilimtoka pima, alishuhudia kisu kikali kikitolewa katika mkoba wa Isabela. Alitamani kukimbia lakini alikuwa na usingizi mzito. Alitamani kupiga kelele lakini na mdomo nao ulikuwa kama umewekewa gundi

    “Chausiku….Chausiku….we……” Hakufanikiwa kuimaliza kauli yake, maumivu makali yakautenganisha uhai wake na dunia. Uhai ukaenda kutalii katika pepo nyingine. Utalii wa milele.

    Ule uchungu wa miaka sita iliyopita ukawa umepungua kidogo!!!

    Uchungu wa kupoteza kila kilicho muhimu katika Maisha yake.

    “Kilaaniwe kizazi chako chote kama ulivyoniletea laana hii.:” Alizungumza Isabela huku akitoweka kutoka katika chumba kile.

    Hakuwa na walau tone la damu!!!!

    Bila shaka hakuwa mgeni katika kuua.

    Nyuma aliacha ujumbe wake kuwa ‘BADO WAWILI’



    ****



    ****

    Kijasho chembamba kiliwatoka Gaston na Kejo. Ile kesi waliyokuwa wakiipeleleza ikaonekana kuwa ngumu zaidi kutokana na jinsi mtiririko wa matukio ulivyokuwa.

    Alikuwa ni Gasto ambaye alimpigia simu Kejo kumwelezea juu ya kifo cha baba Swebe na kisha kuachiwa ujumbe wa bado wawili.

    Ujumbe huu uliwapagawisha maaskari hawa na kujiuliza mbona namba tatu imerukwa, hapa Gasto akaamini kabisa kuwa kujinyonga kwa Abdul hapakuwa pa burebure palikuwa na sababu na huenda ni huyu alikuwa kati ya wanne waliokuwa wamebaki, lakini kujinyonga kwake kukasababisha namba moja irukwe.

    Kuna siri kubwa sana hapa si bure!!!

    Alisema Kejo na Gasto akaunga mkono hoja!!

    Wakaamua kujipanga tena upya kutafuta namna ya kuweza kukabiliana na huyo mwanadamu anayeua kadri anavyopenda!!

    Tena anaweka na orodha!!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ilikuwa saa kumi jioni, kila mtu alikuwa kwenye pilikapilika za kurejea nyumbani hii ilitokana na tatizo kubwa la usafiri jijini Dar es salaam.

    Sio kila mtu alikuwa salama, wapo wengine muda huo hawakuwa wakijua lolote lile juu ya harakati hizo kwani walikuwa ni wagonjwa vitandani. Wenye magari yao binafsi hawakuwa na hofu ya kutokwa jasho, tatizo kwao lilikuwa ni foleni ndefu za jijini Dar. Kwa wale wajanja wa mjini walijua vichochoro vya kupita ili wawahi kufika huko waendako.

    Ilikuwa ngumu sana kugundua kwamba alikuwa ni padri wa kanisa fulani hapo jijini kwa jinsi alivyokuwa amevaa, suruali ya kitambaa kigumu nzuri sana ikisindikizwa na fulana iliyouonyesha vyema mwili wake wa mazoezi. Tabasamu jepesi liliuvaa uso wake na kumfanya avutie kumtazama. Mwendo wake haukuwa kero kabisa kwa atakayetaka kumtazama, na ungetamani kumsihi asiingie katika gari dogo aina ya Vitara ilimradi u uendelee kumtazama lakini haikuwezekana. Huenda hakujua kama anatazamwa na watu wengi hasahasa akina dada. Wengi wa wasichana waliomtazama walivutiwa kimapenzi lakini ni mmoja tu ambaye hakujali utanashati wa bwana huyu. Huyu alikuwa kila mara akiitazama saa yake na punde baada ya padri yule kuwasha gari yake naye aliingia katika taksi na kutoweka. Kuelekea anapojua mwenyewe.

    Hakuna aliyemjali!!!

    Wakati yule msichana anaondoka liliingia gari jingine akashuka msichana ambaye aliwasahaulisha waliokuwa na mawazo ya kumtazama padri. Sasa walimtazama binti huyu ambaye kwa neno moja tu ungeweza kumuita mrembo!! Hakika alikuwa mrembo haswaa.

    Sasa ilikuwa zamu ya wanaume nao kumthaminisha na kutamka wanayoyaweza. Wasichana walijifanya hawamuoni huku kimoyomoyo wakikiri kuwa alikuwa ameumbika.

    Moja kwa moja aliingia katika kituo kile cha afya. Haikuonekana kama alikuwa na ugonjwa wowote ule, alikuwa amenawiri na mwenye afya.

    Labda amekuja kusalimia mgonjwa wake!!! Waliwaza hivyo wale waliokuwa wakimtazama.

    Alijongea kwa mwendo wa madaha hadi akaifikia sehemu ya mapokezi. Alikuwepo kijana mrefu, jicho la matamanio likatua katika kifua cha yule dada.

    “Dokta Temba yupo ofisini kwake!!!.” Aliuliza kwa sauti nyororo isiyohusisha kubana pua.

    “Aaah!! Ametoka kidogo lakini muda si mrefu anarejea.” Alijibu huku akifumbata mikono yake na kuisuguasugua midomo yake. Dalili za uoga.

    “Aaah!! Unaweza kumsubiri hapo, amesema hachelewi.” Alizidi kujiumauma.

    Yule binti hakujibu kitu, akajisogeza pale kwenye benchi akakaa, harufu yake ya manukato ya bei ghari ikameza harufu kali ya madawa kwa muda.

    Dakika zikaanza kuhesabika huku mikao ikikaribia kuisha, maana tayari alishakunja nne, alikuwa ameinama tayari, alisimama kwa muda, alichuchumaa, alijaribu kusinzia na bado dokta Temba hakutokea.

    Yalikuwa yamepita masaa manne, na ilikuwa saa mbili usiku.

    Yule kijana aliyemwambia yule binti kuwa dokta atarejea mapema aibu zikawa zimemshika, akajiuliza ataanza vipi kumweleza yule binti kuwa aondoke na kurejea kesho baada ya kuwa amempotezea masaa mengi kiasi kile.

    Akiwa katika kujiuliza hayo alisikia simu ya pale mapokezi ikitoa mlio, akaisogelea na kuitazama kisha akapokea.

    Sauti nzito upande wa pili ilikuwa inaongea. Kwa amri ilizokuwa inatoa yule kijana mrefu aliamini kuwa ni askari hata kabla hawajajitambulisha.

    “Ndio..aliondoka saa za jioni jioni…kama saa kumi….ndio….eeeh!! hapana…..hakunieleza,…kwani vipi?” Alisikika akihoji na kuhojiwa. Baada ya hapo akakata simu. Hofu ikawa imemtawala.

    “Mh!! Dokta sijui amekuwaje??” Alizungumza kijana mrefu binti akamsikia akasimama.

    “Kwani vipi?.” Aliuliza yule binti.

    “Polisi wamepiga simu wameniuliza maswali, siwaelewi.” Alijibu huku akilazimisha lile tabasamu lake litokeze.

    Hakujibiwa kitu chochote yule binti mrembo akatoweka.

    Hakumuaga mtu.

    Akajichukulia nafasi ndani ya taksi akaamuru apelekwe Magomeni.

    Huko alijifungia chumbani kwake alipokuwa amepanga kwa muda, akaanza kufanya tafakuri.

    Usingizi ukampitia bila hata kuvua viatu. Aliposhtuka alfajiri akaiendea luninga na kuiwasha.

    Kilikuwa kipindi cha magazeti.

    “Padri auwawa gesti, damu yake yatumika kuandika maneno BADO MWINGINE.”

    Binti akasimama wima na kutaka kukimbia baada ya kuishuhudia picha ya dokta Temba. Wasiwasi ukamjaa. Akatamani kupiga kelele za kuomba msaada lakini akajizuia huku akikibana kichwa chake ili akili ikae sawasawa.

    “Nani huyo amemuua padri.” Alijiuliza hakupata jibu.

    Hofu ikachukua nafasi, akaanza kutetemeka.

    Inamaana kuna maadui zangu wengine pia ni maadui kwa watu wengine? Alijiuliza binti huyu aliyezaliwa kwa jina la Chiku na sasa alikuwa na jina jipya la Isabela.

    Jibu halikupatikana mara moja. Akajiuliza mara nyingi zaidi, bado hakupata jibu sahihi.

    Roho ilimuuma sana kwa kuikosa roho hii ya Padri ambaye pia ni daktari. Dokta Temba.

    Isabela alikuwa na kila sababu za kuumia moyoni kwani kwa kumpata padre huyu angeweza kupata mwanga zaidi wa kulipiza kisasi chake cha miaka takribani sita iliyopita. Isabela aliamini kuwa padre atakuwa amekufa kifo chepesi sana tofauti na unyama aliokuwa amemtendea akishirikiana kiukaribu kabisa na baba Swebe ambaye sasa ni marehemu.

    Marehemu baba Swebe bila huruma, mara tatu alimlazimisha Chiku ambaye ni Isabela wa sasa kutoa mimba. Mimba alizokuwa akizipata si kwa bahati mbaya bali makusudi ya akina baba Swebe. Padre Temba kwa kuweka pembeni utumishi wake na kujali zaidi pesa alikubali kushiriki katika kitendo hichi cha kinyama.

    Isabela alifumba macho yake na kuuma meno yake kwa hasira alivyokumbuka jinsi padre alivyokuwa anamnasa vibao huku akimlazimisha kujitanua aweze kuingiza vyuma na kuua kwa maksudi kiumbe kilichoingia maksudi. Daktari huyu hakuwa na huruma kama ambavyo anasimama mbele ya altare na kuitangaza injiri. Alikuwa ni mkatili. Na hakuwa na upole hata kidogo, damu iliyokuwa ikimtoka Isabela kwake haikuwa mali kitu.

    “Au kwa kuwa huna mtoto eeee!!! Mbona wanitenda hivi?.” Kauli hii Isabela aliitoa baada ya kuwa anaandaliwa kuitoa mimba ya pili. Mimba kutoka kwa bwana yuleyule bwana anayehusudiwa na baba Swebe, bwana anayetumia pesa zake kumbadili padre kuwa muuaji.

    Padre hakujibu kitu badala yake alitoka nje na kisha akarudi na mipira ambayo Isabela hakuweza kuifahamu mara moja lakini ni kama aliwahi kuona watoto wakiitumia kutengeneza manati za kuwindia ndege.

    Padre alikuwa ameukunja uso wake na kufanana na mcheza sinema anaecheza kipande cha jambazi kuu. Padre Temba alikuwa amegeuka kuwa kiumbe hatarishi.

    Kipigo alichopokea siku hiyo, kamwe hakuweza kukisahau. Padre alimpiga sana na baada ya kipigo hicho mimba ikatoka yenyewe bila kutumika njia haramu za kutoa mimba.

    “Ndio ulitaka hivyo eeeh!!! Safi sana hujanisumbua kukushika shika mwili wako mchafu huo. Pumbavu!!! Unantukana mimi kuwa sina mtoto…hayawani!!!.” Alitukana yule Padri huku akijipangusa mikono yake. Isabela alikuwa hoi.

    Baba Swebe alikabidhiwa mzigo wake akaondoka naye. Wakati huo Isabela alikuwa na miaka 21 tu!!!

    Katika makabidhiano ya pesa Isabela hakuhusishwa hata kidogo.

    Isabela akiwa amesimama bado alikuwa anatetemeka sana kwa hasira. Hasira za kukikosa roho padre huyo muonevu. Padre aliyejivika ngozi a kondoo huku ndani akiwa mnyama mkali asiye na huruma.

    Hasira za kumkosa padre Temba zikamsukumia katika filamu nyingine matata kabisa. Wahusika wakiwa yeye na padre ambaye sasa naye ni marehemu. Muuaji akiwa hajulikani.

    Siku hiyo Isabela aliamua kujishusha mpaka mwisho akaenda kumtembelea padre wakati huu akiwa na cheo chake cha udaktari. Isabela alijitahidi kuunda tabasamu ili amvutie padre, hilo kidogo lilisaidia kumtega bwana huyu.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Isabela baada ya kuwa amejenga urafiki sasa alimueleza yule padre shida yake. Akajaribu hadi kutoa machozi akilaani vitendo anavyofanyiwa na bwana mkubwa wake, alilaani kila kitukinachomtokea Maishani. Alihitaji padre yule amsaidie walau nauli tu aweze kurejea kijijini kwa mama yake. Isabela alizidi kujieleza kuwa hakuwa na mzazi wa kiume na katika tumbo la mama yake alikuwa wa pekee!!!

    Maneno ya Isabela yalionekana dhahiri kumgusa padre huyu wa kizungu aliyeishi Tanzania kwa miaka mingi sana, akiwa na jina la father Tembel, kanisa alilopangiwa la waswahili wakashindwa kuliita jina hilo kwa ufasaha, Tembel, Tembel, Tembel hatimaye akawa Temba na sasa alifahamika zaidi kwa jina la Temba. Wasiomjua walijiuliza sana iweje mzungu aitwe jina la wachaga?? La!! Hakuwa mchaga. Asili yake ilikuwa Kualalumpar Malaysia.

    Huku akiwa katika uso wake uleule uliojawa majonzi. Alisimama aauendea mlango akaufunga vyema akarejea na kuwa nyuma ya Isabela, akamshika mabega na kuanza kumbembeleza. Isabela alijisikia kupata faraja sana kwa upendo aliokuwa ameuonyesha padre huyu. Kutoka moyoni akawa ameanza kumsamehe kwa maovu yote aliyomtendea hapo kabla.

    Akiwa katika kusamehe alishtuka mkono wa padre ukipenya kaika matiti yake. Alipojaribu kushtuka na kugeuka alikutana na uso wa padri ukiwa umebadilika tena na kuwa kama wa bwana mkubwa ambaye humjaza mimba bila kuwa na malengo ya kupata mtoto. Machale yakamcheza. Akataka kupiga kelele akakutana na kiganja kilichokomaa cha mzungu huyu.

    Sauti haikutoka. Akiwa katika kutapatapa gauni lake likanyanyuliwa juu. Maskini binti kutoka kijijini hakuwa hata na ujanja wa kuvaa skin taiti kwa ndani. Akafanya zoezi la kubakwa kwake kuwa jepesi zaidi. Bila shaka Temba hakutegemea kama itakuwa rahisi kiasi kile. Lakini ilikuwa hivyo Isabela akabakwa. Mtu aliyemwamini Isabelani ni kimbilio kuu la mwisho na mwenyewe akamfadhaisha. Akapoteza tumaini!

    Akawa amedhalilishwa tena!!!!

    Hadi mtu wa Mungu????

    “Unanitukana kuwa mimi sina mtoto…shenzi kabisa” Mzungu yule alimkaripia Isabela. Kwa kukumbushia maneno ya miezi kadhaa nyuma kipindi alipokuwa akimfanyia ‘Abortion’. Huenda maneno yale yalimuumiza sana.

    “Na ole wako uende kumwambia mtu..! Si unamjua bosi wako? Atakuua!!” Alitishia mzungu.

    Isabela akashusha gauni lake akatoweka akiwa analia.



    Si jambo geni mgonjwa kutoka chumba cha daktari akiwa analia au anatembea kwa kuchechemea. Utajuaje labda kachomwa sindano ama ana fangasi. Au analia kwa majibu aliyopewa.

    Ndivyo ilivyokuwa kwa Isabela, alitoka akiwa anachechemea na kutokwa machozi. Hakuna aliyejali.

    Kumbukumbu hizo zilimfanya Isabela aangue kilio upya kama vile amefiwa na ndio kwanza anapewa taarifa. Hakika ilikuwa hali ya kusikitisha.

    Baada ya kuugulia kwa muda mrefu, Isabela alipitiwa na usingizi.

    Kesho yake asubuhi Isabela akashindwa kuendelea na harakati zake. Ile maiti ya Padre Temba isingeweza kujibu swali lake hata moja.

    Akapata wazo. Wazo la kuachana na kisasi. Akae atulie afanye mambo yake kwani mlolongo alioupanga tayari ulikuwa umevurugika. Yule aliyetakiwa kutoa taarifa rasmi sasa alikuwa maiti

    Nitaishi wapi sasa?? Lilikuwa swali.

    Wakati akiwaza haya mara akakumbuka jambo moja muhimu zaidi ambalo lilimfanya atabasamu.

    Hakika alikuwa amebaki mtu mmoja tu katika orodha. Isabela akajipa imani kuwa huyu ndiye muuaji wa padre pamoja na bwana Abdul. Kwa sababu ni hawa wangeweza kufichua maovu yake iwapo wangehojiwa.

    Na bila shaka kwa kuziondoa roho zao angekuwa amejisafisha na kuwaweka kimya kwa muda mrefu.

    Jambo hili likamtia hasira na kuamua kufanya tukio la mwisho ambalo aliamini lingemweka katika amani ya milele.

    Isabela akaamua kumkabili adui yake!!

    Aliutaka ukweli tu japo ungemuweka matatani sana.



    *****



    Majira ya saa mbili na nusu usiku Isabela alipiga hatua akiwa amevaa ushungi ambao ulifanikiwa kuiziba sura yake kwa kiasi fulani, akapita maeneo kadha wa kadha ambayo aliamini ingewezekana kukutana na mbaya wake.

    Hakika alifanikiwa kumuona japo alikuwa amezungukwa na watu watatu wakiwa wanasaidia kunywa pombe.

    Isabela alimfahamu vyema bwana yule ambaye licha ya uzee wake bado aliyapenda sana mambo ya ujana. Akajiweka katika meza moja ambayo ilikuwa katika kiza kiasi fulani, akaagiza soda akatulia bila kuharakisha kuinywa akawa anatazama upande ambao alikuwepo bwana Joshua!!

    Walikuwa wanacheka kwa furaha zote!! Akawahesabia bia moja baada ya nyingine. Akahesabu hadi walipoanza kulewa.

    Isabela hakuwa mtu pekee ambaye alikuwa akimtazama Joshua, kuna jicho jingine lilikuwa likimtazama pia.

    Ilipotimu saa nne na nusu, Isabela akaona ulikuwa wakati muafaka wa kutimiza azma yake, akaupekua mkoba wake na kukutana na kisu chake kikubwa kabisa.

    Akakiweka vyema katika namna ambayo anaweza kukifikia upesi. Akakisia sekunde ngapi atatumia kukitoa na kukitumia.

    Akatoweka eneo lile na kuendelea kuzurura huku na kule.

    Kile kitendo chake cha kuagiza soda na kutojishughulisha kunywa kilimfurahisha yule kijana ambaye naye pia alikuwa akimtazama Joshua.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hivyo alimsindikiza kwa macho hadi alipofika gizani, akaachana naye!!

    Baada ya hapo aliendelea na zoezi lake la kumtazama mzee Joshua.

    Wakati huo walikuwa wameanza kusahau juu ya mauaji yaliyokuwa yakienda kwa namba, hali ilikuwa shwari huku wakijidanganya kuwa huenda katika kamatakamata yao walifanikiwa kumtia nguvuni muuaji.

    Kejo akaendelea na shughuli zake jijini Mwanza huku Gasto naye akiendelea na mambo yake, sasa alikuwa akimlinda mzee wake dhidi ya watoto wa kike wa mjini ambao walikuwa wakimpeleka puta mara kwa mara na kujikuta akigombana na mkewe ambaye ni mama yake Gasto Mushi.

    Sasa alikuwa akingojea mzee wake alewe aweze kumchukua na kumrudisha nyumbani.

    Kuna muda alikuwa anaacha kumtazama mzee wake huku naye akijikita katika kunywa bia zake mbili zilizokuwa mezani na wakati mwingine akichezea simu yake.

    Alipoyanyanyua macho yake alikutana na tukio lililomsisimua, yule msichana aliyekuwa ameketi bila kunywa soda kisha akapotelea gizani alikuwa akitembea kwa mwendo wa kasi kuelekea katika meza aliyokuwa amekaa mzee Joshua. Alikuwa akijiamini kabisa.

    “Ahaa kumbe kimada wa mzee!!” alijisemea Gasto.

    Yule binti akafika na kuinama mahali alipokuwa ameketi mzee Joshua.

    Hasira zikampanda Gasto na kuona mzee wake hajakoma tabia yake hiyo ya kupenda ngono.

    Alimuona yule binti akiwa anamnong’oneza kitu mzee wake, Gasto akavuta subira aone nini hatma ya kisanga kile. Huku kichwani akikiri kuwa hatakubali kuona mzee wake akiondoka na msichana yule.

    Mara akamshuhudia mzee wake akikodoa macho kwa mshtuko, na katika sekunde zile zile akamuona yule binti akijipekua kidogo.

    Mara kisu kikubwa!!!

    “Nooooooo!!” alipiga kelele Gasto, lakini alikuwa hajawahi kuliko yule binti. Kisu kikazama katika mgongo wa mzee Joshua. Akapiga mayowe.

    Binti akageuka na kutaka kutimua mbio, Gasto akaruka viti vinne katika mwendo wa kasi akamfikia na kumchabanga teke mbavuni, kisha akamwongeza teke jingine usoni.

    Binti akalainika.

    Mzee Joshua alikuwa akigumia kwa maumivu, kisu kikiwa kimezama katika mwili wake.

    Hakika kilikuwa kizaazaa cha nguvu…

    Simu za dharula zikapigwa.

    Baada ya muda msaada ukapatikana….



    ****



    Mzee Joshua alijua kuwa lazima atakufa, binti akatoa maelezo yake juu ya mkuu huyo ambaye alikuwa mpepelezi wa kawaida miaka sita iliyopita na sasa akiwa katika ngazi ya uinspekta.

    Alielezea maasi yake, alivyomnyima haki yake ya msingi huku akizidi kusaidia katika manyanyaso. Isabela alisema mengi huku akielezea juu ya Lameck ambaye alimfanyisha utumwa wa ngono, Abdul aliyejinyonga akiwa muunganishaji wa mpango huo akisaidiana na Zuwena ambaye wakati huo alikuwa akiishi jijini Dar. Padre aliyembaka na kumsababishia matatizo ya kizazi, mzee Swebe ambaye alimtoa kijijini, Karama mpenzi wake wa enzi hizo aliyemtumia kisha kumtelekeza pasipo na msaada, na kubwa zaidi ni James kijana ambaye alijiingiza naye katika mahusiano huku akijifahamu fika kuwa ni muathirika wa gonjwa hatari la Ukimwi!! Akamwambukiza kisha kumcheka kuwa ni marehemu mtarajiwa.

    Isabela aliyasema haya yote huku akiwa anatabasamu! Alitabasamu kwa sababu alikuwa ametimiza kile ambacho alimuahidi yule mama ambaye alimpa hifadhi hadi kuwa kama alivyo na kubarikiwa katika kisasi chake cha damu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wakati mzee Joshua, akiiaga dunia. Isabela alikuwa anatabasamu katika nguo za wafungwa akiwa amepewa hukumu ya kunyongwa hadi kufa!!

    Hakuwa na la kuogopa kwanza alikuwa mgonjwa wa Ukimwi!! Pili alikuwa hana jingine la kufanya duniani!!

    Labda mbele ya safari kama angekutana tena na roho zile!



    TOA MAONI YAKO NA USHAURI!!!!



    MWISHO

0 comments:

Post a Comment

Blog