Search This Blog

Sunday, 19 June 2022

KIVULI CHEUSI - 1

 







    IMEANDIKWA NA : STALLONE JOYFULL



    *********************************************************************************



    Simulizi : Kivuli Cheusi

    Sehemu Ya Kwanza (1)



    Panga boi lilikuwa linazunguka taratibu, bila kuleta dalili yoyote ya ubaridi. Sifahamu kama ilikuwa ni udogo wa chumba, ama ni hali ya hewa ya jiji la Dar es salaam? Lakini hiyo haikumsumbua mlalaji huyu mgeni, katika kitongoji duni cha keko magurumbasi. Kitongoji kilichobeba vibaka wa simu, makahaba na zile biashara haramu; kama uuzwaji wa bangi na pombe aina ya gongo, zilipatikana kwa wingi. Kijana wa mapokezi katika nyumba ya kulala wageni, yeye alipokea bakshishi ndogo kutoka kwake mgeni huyo. Jumamosi yake kijana huyo wa mapokezi, ikaelekea kuisha vizuri jioni ile ya saa kumi na mbili. Yeye mgeni huyo alihifadhiwa ndani ya kofia kuukuu, akatoa masharti ya kutomuelekeza mgeni yeyote chumbani kwake, Akidai kuwa, hakuna anayemfahamu; hivyo hakuna atakayekuja kumtafuta. Hiyo haikuwa tatizo, kijana Yule aliitikia kwa kichwa; haraka haraka tabasamu jepesi la kiushawishi likipita juu ya papi zake. Elfu arobaini alizisunda kibindoni, nyongeza mara nane ya bei ya kawaida. Binafsi aliiona bahati ya ngekewa, iliyomdondokea zaidi ya nyota ya jaa. Akampatia ufunguo mgeni huyo asiyeeleweka. Macho yake mgeni yakiwa yaqmehifadhiwa nyuma ya miwani mikubwa meusi na mwendo wake kama anayechechemea. Yeye mgeni huyo, aliuchukua ufunguo aliopewa na kuondoka. Ufunguo wenyewe, ulining’inizwa kwenye kibao kilichoandikwa namba ya chumba na kulifuata korido lililopanga vyumba kwa nambari zilizofuatana kimpangilio. Baada ya kuhesabu vyumba vyote, alisimama mbele ya chumba ambacho ufunguo wake, alikuwa nao yeye. Aliufungua mlango na kujitoma ndani. Hakutaka kuwasha taa, kwa sababu mwanga hafifu wa jua lililoashiria kudondokea magharibi, ulimtosha kukiona kitanda. Alilala vile vile kama alivyoingia. Kitanda kikamlaki kama kilivyowalaki wengine. Kunguni waliifurahia damu yake, viroboto nao

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    wakamchoma choma. Hakujisumbua kukishusha Chandarua, hivyo mbu walicheza gombania goli katika sikio lake. Mara akaamka ghafla, aliamka sio kwa sababu ya usumbufu wa chumba hicho duni bali ni mlio wa simu iliyoingia ghafla, saa tano ya usiku. Muda ulikuwa umeenda kasi sana. Juu ya simu likuwa ni namba ya Bertha, mpenzi wake. Alijiuliza ni nani atakuwa anaitumia namba hiyo. Baada ya kuipokea, aliifahamu sauti iliyoongea kwa hali ya kuchanganyikiwa. Yeye aliongea kiutulivu na kumchota akili yule aliyewehuka upande wa pili. Baada ya maongezi aliyoyafanya katika simu hiyo iliyoingia punde, Alijinyanyua kitandani na kurudi maeneo ya kijitonyama sayansi nyuma ya kanisa. Eneo ambalo alikuwa akiishi mpenzi wake aitwaye Bertha. Baada ya kumaliza shughuli iliyompeleka, Alitumia taksi iliyompeleka na kumsubiri umbali wa mita zipatazo mia kutoka katika nyumba ya mpenzi wake, baada ya kumlipa dereva pesa yake ya kumleta na kumuomba amsubiri kwa dakika chache kisha alipomaliza ilimrudisha mpaka Buguruni na yeye kuamua kuchukua taksi nyingine mpaka keko magurumbasi. Sasa akawa anautafuta usingizi akiwa na bia nane kichwani. Bia alizozinywa katika ile klabu ya usiku maarufu kwa jina la kimboka by night. Hapo kulikuwako na madada poa waliouza miili yao kama ndafu ya shereheni. Usingizi ukamkubali. Licha ya usumbufu wa kunguni na mbu wa usiku alioupata, unadhani hata alijigusa? Lah! Aliyafurahia maficho yake. Japo usingizi ulimpaa jirani na alfajiri. Hali hiyo ilisababshwa na jinamizi la mawazo lililokuwa likimnyonga. Mwanga hafifu wa jua la alfajiri uliojipenyeza katika dirisha la chumba chake, ndio uliyomfanya aamke kivivu huku akitanguliza kitambi chake kilichoanza kujichomoza. Hatua zake zikiwa nzito kuubeba mwili mfupi kiasi uliobeba kifua kipana na kitambi cha bia na nyama choma; zote kwake zilikuwa kheri, mpaka alipokifikia kioo kilichopachikwa ukutani. Akashituka! Nadhani alianza hata kuisahau sura yake. Aliyasahau macho yaliyokosa nguvu ya kope za juu na kusababisha kuwa kama anayetaka kusinzia. Hata hivyo haikua sura ngeni aliyokuwa anatazamana nayo. Akakumbuka kuwa macho hayo yalikuwa ya kawaida. Macho yaliyomuwezesha kumpora Bertha kutoka kwa rafiki yake, Yesaya. Kidevu chake kikatawaliwa na msitu wa ndevu, Lakini hiyo haikuwa sababu ya kuisahau miaka ishirini na nne aliyoifukia kwa kula na kunywa kwa anasa. Aligeuza macho kukitazama kitanda alicholalia. Godoro jembamba kama ngozi ya tembo, likamdhihaki. Akajitusi mama yake mzazi kwa hasira, Kisha kicheko kisicho na ladha yoyote ya raha kikauharibu uso wake. Akili yake ikaanza kutafakari yaliyotokea asubuhi ya siku ya jana, iliyomfanya apahame Osterbay na kuja kujificha huku vichochoroni, Keko Magurumbasi. Ulimi wake ukapata nguvu ya kuinua matamshi kadhaa “Bertha” aliita jina la msichana aliyefanya urafiki wake na Yesaya kuangamia. Msichana waliyesoma wote chuo cha mlimani, kitivo cha sheria. Msichana aliyeiiba nafsi yake na kuiyumbisha yumbisha kama mawimbi ya bahari. Aliikumbuka siku ya kwanza Bertha alipowasili chuoni hapo akitokea Nyegezi Mwanza. “Anha! Kumbe na wewe ni msukuma? Mimi ni mwenzio bwana, naitwa Moses” akalikumbuka Tabasamu lililoacha uchi kinywa chake na kuonesha meno yaliyojipanga na kufanya mpangilio sahihi katika kinywa cha Bertha. Kwa mara ya kwanza Moses alikiri kuushika mkono wa malaika ‘laivu’ waliposalimiana kwa kushikana mikono. Ila Bertha sasa si Bertha tena, ingefaa utangulize jina jipya, kabla hujaamua kumuita Bertha. Bertha kwa sasa aliitwa marehemu. Maiti yake yalifichwa na Moses ndani ya chumba chake mwenyewe Bertha. Chini ya kitanda na kuhifadhiwa kwa kuviringishwa ndani ya mkeka. Hakika aliuwawa kinyama. Moses alifanya unyama zaidi ya mnyama. Unyama aliomfanyia binadamu mwenzake hauelezeki kwa maneno machache pekee ya kitabu. Shingo yake Bertha haikutenganishwa na kiwili wili wakati alipochinjwa kama kuku na kisu kilichopoteza makali kwa kukatiwa nyanya na vitunguu, mpaka masoksi machafu aliyoingizwa mdomoni ili Bertha asitoe sauti. Japo si Bertha pekee aliyekuwa maiti ndani ya nyumba yake. Rafiki yake Pamela pia, alipoteza roho yake kwa kutaka kutoa ushahidi polisi. Yeye aliuwawa kikawaida kwa sumu aliyoinywa ndani ya maji ya baridi, ilikuwa ni sumu kali sana. Nyongo ya mamba waliovuliwa kutoka katika ziwa Tanganyika. Ilisagwa na kuwa unga baada ya kukaushwa sana. Pamela aliipoteza roho yake kwa kiu ya maji ndani ya dakika kumi tu. Baada ya kufanya yote hayo, Moses alikumbuka kufanya jambo. Alikaa uelekeo ambao mwanga wa taa ulimpiga na kutumia kamera yake aina ya Kodak, kukipiga kivuli chake mwenyewe. Baada ya kuridhika na picha aliyoipata, akatumia mashine ndogo ya kusafishia picha hiyo, alikuwa nayo. Baada ya kusafisha, picha ikatoka vile alivyotaka. Akatabsamu kwa kebehi, kisha nyuma ya picha hiyo akaandika maandishi haya ‘KIVULI CHEUSI’ akaiweka picha hiyo pembeni ya kichwa cha Bertha, alichokiweka ndani ya friji.



     “Si kawaida ya Bertha kuchelewa kufungua mlango” Alijinong’oneza, baada ya kusonya muda mfupi uliopita. Pamela aligonga mlango muda mrefu, bila dalili yoyote ya kuja kufunguliwa. Alijishauri aondoke, lakini alikumbuka kuwa Bertha alimtumia ujumbe kuwa, anamualika katika sherehe. Sherehe yake ya kuvalishwa pete ya uchumba na mpenzi wake, Moses. Hivyo aliamua kujikaribisha baada ya kuona kuwa mlango ulikuwa wazi. Mara tu alipoingia ndani, alipigwa na butwaa. Alijiuliza nini kimetokea kwa Bertha, miguu yake ikalakiwa na damu nzito, iliyoanza kuganda pale sebuleni. Alihisi miguu ikikosa nguvu ya kukibeba kiwiliwili chake. Kizunguzungu kikampepesua, akastahimili kiukakamavu asidondoke. Mapaja yakalowana kwa mkojo uliomchuruzika kiuwoga. Hakika hali ya sebule ilitisha. Macho yakavutwa na matone ya damu, yaliyodondoka mpaka kwenye friji. Alijikokota taratibu kwa mwendo wa kuvizia, mpaka kwenye friji hilo. Alipolifungua friji, hakuamini alichokiona. Kilikuwa ni kichwa cha Bertha. Mdomoni akiwa na matambara machafu. Wakati huo, ndipo kile kitu alichokuwa akikizuia kwa muda mrefu, kikampiga mtama. Alianguka na kuzimia papo hapo. Zilipita dakika nyingi, mpaka alipoanza kuhisi kichwa kikimuuma kupita kiasi. Hakujuwa amezimia kwa muda gani na pia alikwisha sahau, kilichomfanya ajikute kaibusu sakafu kama anayekisujudia kichwa cha rafiki yake mrembo, Bertha. Friji lilikuwa wazi hivyo kichwa cha Bertha kilikuwa juu kikionekana. Ulikuwa ni usiku mzito uliomuogopesha kuendelea kutazama hali ya nyumba ya Bertha. Muda wote nyumba ilikuwa kimya na giza likimzomea. Aliamua kupiga simu kituo cha polisi, kwa kutumia zile namba zilizotolewa kwa ajili ya usalama wa raia. Kwa kuwa simu yake haikuwa na salio, aliamua kutumia simu ya Bertha. Simu ambayo aliipata pembezoni mwa kochi kubwa kwa msaada wa mwanga utokao kwenye friji. “Habari yako?” ilijibu sauti ya upande wa pili, baada ya kuita kwa muda mrefu bila kupokelewa. Pamela aliongea kwa pupa, bila mpangilio wa mtu wa pili kumuelewa vizuri. “We!! dada embu tulia!” ilikoroma sauti ile, Pamela akatii. kisha sauti ya upande wa pili ilivuta tafakuri na ilipopata uhai, ikasema “Unasema mauaji?” kabla sauti ile haijamaliza, Pamela alidakia tena “Rafiki yangu Bertha, wamemuua kinyama. Kichwa chake” sauti ile, ambayo Pamela aliifahamu vizuri, ikapata tena uhai. Pamela hakuweza kuigundua, kutokana na papara zake na kuchanganyikiwa. “Unasema mauaji yametokea hapo nyumbani kwa rafiki yako?” Pamela akajibu kiutulivu huku akiwa analia “ndiyo afande” Pamela alichukuwa jukumu la kumuelekeza mtu aliyekuwa akiongea naye, bila kuulizwa. “Sawa usimueleze mtu yeyote mpaka tutakapofika hapo” Pamela alipoitikia, sauti ile ilitoa onyo la mwisho “kumbuka! usimwambie mtu yeyote mpaka tutakapofika hapo. Hata wazazi wake wala mtu wake yeyote wa karibu usimwambie, hiyo ni kutokana na usalama wako. Pia usiende popote” kisha yule mtu, alikata simu. Pamela aliendelea kusubiri kwa dakika arobaini na tano zaidi. Muda wote bado hakuwasha taa wala kujigusa. Alitetemeka kiasi cha kuhisi joto kali, licha ya kiyoyozi kilichokuwa , kikifanya kazi yake kiufasaha kikibadilisha hali ya hewa kwa fujo. Alikwisha jikojolea mara mbili kwenye kochi alilokalia akakauka. Choo kilikuwa ni cha ndani, vipi aingie akutane na muuaji kajibanza? Alijiuliza. Akiwa katika lindi la mawazo, ndipo aliposikia kitasa kikishikwa na mlango kufunguliwa. Kutokana na giza nene, hakuweza kumuona aliyeingia. Mapigo ya moyo yalimuenda mbio sana, jasho likamtiririka kwa wingi. Kivuli kile cheusi kilichojitoma ndani ya nyumba bila hodi, kikawasha taa. Macho ya Pamela yakamtoka pima baada ya kumuona aliyeingia. Alikuwa ni Moses. “Shemeji” kilio kikaanza upya “Wamemuua rafiki yangu, amewakosea nini jamani yoo!! Wamemuua Bertha jamani ” Moses akamkumbatia Pamela na kumliwaza kinafki. Walikaa kwenye kochi, huku Pamela akimuhadithia Moses yote tangu Bertha alipomtumia ujumbe uliomfanya yeye kuja hapo. “Aliniambia upo naye, leo ulikuwa ukimvisha pete ya chumba” Pamela alimshitua Moses. Moses akamtusi Bertha

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    kimoyomoyo. Ni yeye Moses ndiye alimdanganya hivyo ili apate njia rahisi ya kumuua. Pamela akaendelea kumueleza mpaka alipopoteza fahamu baada ya kukiona kichwa cha Bertha ndani ya friji. Moses hakuoneshwa kushitushwa na hadithi hizo zote zilizosindikizwa na kilio. Alinyanyuka na kuelekea jikoni. Pamela alikuwa huru kwa kuwa aliaamini sasa ana mtu wa kumlinda. Lakini laiti angejua, asingethubutu kuiuza roho yake kwa mkopo. Alimwambia Moses “Nimewataarifu polisi, lakini naona wanachelewa” sauti ilimfikia Moses jikoni, naye akajibu “Umefanya vizuri” kisha Moses alikuja na bilauri ya maji ya baridi yaliyotoka kwenye friji ya jikoni. “Ahsante shemeji umejuaje nilikuwa na kiu? Yaani sijatoka kwenda popote kwa uoga” aliyafakamia maji hayo, bila kujua hila za Moses. Moses alimtazama huku akimcheka kimoyo moyo. Moses akajinong’oneza. “Kufa Malaya wewe, kamsalimie mbwa mwenzio” dakika tano zilikuwa nyingi. Tumbo lilianza kumsokota Pamela. Pamela alilia kwa uchungu huku akimtazama Moses aliyekuwa akitabasamu. Pamela Akagundua kuwa maji aliyoyanywa yaliwekwa sumu. Alijuwa kuwa, Moses alipanga kummaliza ili ushahidi upotee. Aligundua kuwa hata aliyemuua Bertha ni yeye Moses kasha hata sauti ile kwenye simu akaikumbuka. Akiwa katika kuugulia, alimwambia Moses “kwa nini unatuua Moses? Kumbe ni wewe ndiye uliyepokea simu yangu? Kwanini Moses unafanya hivi? Tumekukosea nini?” Moses alicheka kifedhuli, akamwambia neno moja ambalo liliisindikiza roho ya Pamela katika umauti “Pole Pamela, ni ujinga wako ndiyo umekuponza. haukuwa katika njama hizi, lakini ni upuuzi wako. Nililazimika kuidaiveti namba ya Bertha ila nimpate ninayemkusudia. Sikujuwa kama wewe ungekuwa wa kwanza kukiona kifo cha Bertha na harakati hizi haziishii hapa naapa kukiangamiza kizazi chake chote, na umsalimie kuzimu uendako” si maneno yote ambayo Pamela aliyasikia, kwa sababu tayari alikwisha funga macho na roho kuiacha mwili. Moses alicheka kwa kejeli baada ya kuzikusanya simu zote mbili, simu ya Pamela na Bertha kisha kutokomea nazo baada ya kuacha picha ile yenye ujumbe wa kivuli cheusi nyuma ya picha aliyojipiga

    mwenyewe.



    Bertha alipendelea sana kunywa supu wakati ambao anaamka, hakuna mtu ambaye alikuwa halifahamu hilo. Ndio maana aliweka oda ya kutengenezewa supu ya ulimi na chapati mbili, katika pub iliyo jirani na nyumbanin kwake. Hicho ndio kilikuwa kifungua kinywa chake mara kwa mara. Ilikuwa ni baada ya oda aliyoiacha jana alipoitembelea Pub hiyo, akiwa na Moses. Pub inayojulikana kama GQ.

    Wapishi na wahudumu wa pub hiyo, walikwishazoea kumpelekea mpaka nyumbani kwake. Walimthamini kutokana na kuwa mteja wao mkubwa na kumfanya wa muhimu kwao. Leo ikawa zamu ya Eva kupeleka supu.

    “mwambie atusamehe sana, tulikosa ndimu” mpishi mkuu wa jiko, alisikika kwa mbali. Eva alijibu huku akiendelea kutembea “huo ni uzembe jamani, kila inapofika zamu yangu hamkamilishi breakfast yake, Mimi namuogopa jamani”

    Eva akazipita nyumba tatu, ndipo akaifikia ya Bertha. Hakushangaa kukuta geti lipo wazi, lakini alistaajabu kukuta mlango ukimzomea na nzi wengi wakimlaki kwa shangwe. Alibisha hodi mara tatu kana kwamba aliukuta mlango ulikuwa umefungwa. Ukimya ukamfanya kujikaribisha ndani huku akiwa ananyata akiendelea kuita

    “Dada Bertha nimekuletea….” Mdomo wake ukakosa stamina na kuropoka neno “mamaaaaa!!!!!” baada ya kuangusha sahani iliyobeba bakuli la supu na chapati. Hakuingia zaidi ndani kwa kile alichokiona. Akatoka mbio bila kutazama alipokuwa akienda. Alikwisha jikwaa mara tatu na kupiga yowe, alipokuwa akikimbilia getini huku akitazama nyuma GQ alipaona mbali. Hakika Eva alipendeza kuwa mwanariadha, Kisigino kilibaki sentimita chache kigonge kisogo kwa kukimbia.

    Alienda mpaka kwa mpishi mkuu bila kujali hasara aliyosababisha ya kulikwapua sinia lililojaa maini na chapati za mteja.

    “Mungu wangu…. “muhudumu mwenzie alibwatuka, baada ya kushindwa kulizuia sinia lisianguke akahamanika kwa fadhaha “..Eva!!”. Aliye angusha sinia alimfuata Eva mpaka jikoni akipokimbilia.

    “Amekufa?” mzee huyo wa jikoni alibwatuka kwa butwaa. Hata Yule aliyekuwa akimjia kwa jazba naye aliuliza kwa kuhamanika “Bertha amekufa?” Eva alionekana kuchanganyikiwa kupitiliza

    “Mimi jamani sifahamu ila nyumba yake haitamaniki, Kila sehemu damu na nilimuona amejilaza chini niliogopa kutazama kama ameshakufa au lah!”

    Eva hakujuwa kuwa Yule aliyemuona ndani ya nyumba ya Bertha, hakuwa Bertha bali ni Pamela. Mpishi mkuu wa jikoni alimuamuru Bosco yule mhudumu wa vinywaji, akaangalie nini kimemkuta Bertha. Kama kuna msaada wowote unahitajika, inabidi waitaharifu polisi.

    “sawa babu bonge”

    Bosco alijibu huku akitoka yeye na Eva mpaka nyumbani kwa Bertha. Bosco hakuamini alichokikuta kwa Bertha. Ilikuwa ni harufu ya uvundo wa damu, iliyoanza kunuka. Aliziba pua yake na kuingia ndani. Alimuacha Eva nje, akitetemeka kwa uoga.

    Mwili wa Pamela uliojilaza sakafuni haukuwa na damu zaidi ya mapovu yaliyomtoka, kutoka mdomoni. Bosco hakuitaji ushaidi wa daktari, kumuhakikishia kuwa aliugusa mwili tu, roho haikuwepo tena ndani yake

    “Huyu siyo Bertha” Bosco akasema kwa nguvu.

    “Sasa atakuwa nani bwana?” Eva alisema huku akichezesha chezesha miguu yake kwa uoga.

    “Sijuhi ni nani? Na hizi damu ni za nani? Maana huu mwili hauna jeraha lolote” alisema Bosco. Jambo lililomvuta Eva kuingia ndani na kuangalia alichokuwa akikisema Bosco. Bosco yeye alikwisha ona damu zilizochuruzika mpaka kwenye friji, hivyo wakati Eva anaingia na yeye alikuwa amekwisha fungua mlango wa friji na kukiona kichwa cha Bertha kilichong’ata matambara machafu.

    Damu zilizoanza kuganda shingoni mwake, miguu ikamkosea adabu Bosco, akadondoka kama mtoto aliyeanza kujifunza kutembea. Ilikuwa ni hali inayotisha. Eva alishitushwa na kuzimia huko kwa Bosco, akavutwa kukitazama kilichomfanya Bosco adondoke. Alipoona! yeye akatapika, alitapika sana mpaka akaitapika nyongo. Mkojo ulimtoka na machozi kumchuruzika asijue ni hatua ipi ya kuichukuwa. “Berthaaa” alipiga mwereka alipotaka kukimbia, kumbe alimkanyaga Bosco aliyedondoka. Alijiinua na kukimbia hovyo kurudi GQ.

    XXXXX

    Moses aliirudia taswira yake ile ile aliyokuja nayo jana, kofia ya kizee vijana wakaiita pama miwani mikubwa iliyobebwa na mashavu yake pamoja na jino moja la dhahabu. Taswira iliyomfanya aonekane mzee kwa kuvaa midabwada na mandevu ya bandia yaliyochafua kidevu chake. Alipanga hila za kutoka katika Guest hiyo ya vichochoroni, asigundulike na mtu wapi aelekeako. Ni Yule kijana mroho wa mapokezi, ndiye aliufahamu ugeni wa Mzee huyo aliyejiandikisha katika kitabu cha wageni kwa jina la Mussoline. “Mzee anayenuka umasikini lakini mwenye pesa nyingi” Alijisemea hivyo Yule kijana. Moses alipopita pale mapokezi akiwa katika mwendo wake ule ule wa kuchechemea, Yule kijana alimsimamisha.

    “mzee umedondosha kitambulisho chako”

    Moses alikuwa ameshampita pale alipokuwa anafagia. Yule kijana alikuwa ameshakisoma kile kitambulisho na kuitazama picha ya muhusika.

    “Sio mzee mussoline” alijisemea.

    Moses alimshukuru na kumuondoa wasiwasi “nashukuru sana kijana wangu. Hiki ni kitambulisho muhimu sana” Moses hakujuwa Yule kijana alikwisha kisoma, Alimuuliza

    “sasa babu, huyo pichani ni nani?” Moses alishituka lakini hakumuonesha wasiwasi. Alimjibu kwa hekima, baada ya kikohozi kifupi kumpitia “mwanangu..” kisha kama aliyekuwa akivuta hisia juu ya jambo Fulani, akazungumza kwa unyonge “mwanangu mpendwa na wa pekee Fredy. Amekufa katika kifo cha kusikitisha sana. Ndio maana nimekueleza ni kitambulisho cha muhimu kwa kuwa ni ukumbusho wa pekee unaonifanya nihisi ninaishi naye mpaka sasa” Moses aliongeza hila zake kwa kujifanya akivuta kamasi na kuyafuta machozi ya uongo na kweli kwa kitambaa. Alimuuliza

    “kijana, unaitwa nani tena?”

    yeye kijana akajibu “pole sana mzee, mimi naitwa Omary au alimarufu kama Kibanga”

    Moses na Omary wakaagana kuwa wangeonana jioni wazungumze mengi. Safari ya Moses ilikuwa ni kwenda katika ofisi za baba yake Bertha, akiwa katika Taswira ile ile. Kabla ya kwenda aliingia katika kibanda kimoja cha TTCL na kutumbukiza sarafu kadhaa na kuzungusha nambari za Mzee Raymond baba yake Bertha.

    Alizifahamu.

    “Raymond Chilambo nikusaidie nini?” sauti katika spika ilikoroma baada ya kuita kidogo tu. Moses alicheka kimoyo moyo baada ya kusikia sauti iliyopwaya kutoka upande wa Raymond. Yeye alijibu

    “kivuli cheusi, naitafuta roho yako kwa udi na uvumba ” kisha Moses alikata simu

    XXXXX



    Bosco ndiye alipewa jukumu la kuitaarifu polisi. Alipiga simu ya mkuu wa kituo cha Osterbay, inspekta Nyaluto.

    “Tupo njiani, ahsante kwa taarifa”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nyaluto hakuwa mwenye maneno mengi, aliikata simu baada ya kuelekezwa eneo lilipotokea mauaji hayo. Kifo cha Bertha kikawa gumzo katika maeneo yote ya Kijitonyama. Hata wasiomjua walipozisikia habari za kifo cha kinyama alichofanyiwa mrembo huyo, wakinamama kanga ziliwavuka kuelekea alipokuwa akiishi Bertha. Huyu akasikitika, Yule vinyweleo vikamsimama wengine walishika midomo yao. Kuna walioshindwa kuyazuia machozi yasiwaadhiri, kwa huruma waliyolaaniwa nayo wanawake, hata yakawadondoka.

    Nani basi ambaye asingeshituka kusikia “kichwa chake kimekutwa ndani ya friji, kikiwa kimetafuna soksi?” ilikuwa ni habari ya kusikitisha, iliyowavuta pia na waandishi wa habari. Waandishi wakataka kufahamu kuhusu maiti nyingine iliyopatikana ndani ya nyumba hiyo. Maiti iliyoonekana kuwa na kichwa chake, isiyo na jeraha lolote lililovuja damu. Kikawa kitendawili kwao Bertha ni yupi na huyu anayevuja mapovu ni nani? Hakuna ambaye aliifahamu familia ya Bertha, hivyo hakuna ambaye alitoa wazo la kumtaarifu ndugu au jamaa yeyote wa karibu na Bertha.

    Jeshi la polisi lilikuwa eneo la tukio, kupima hiki na kukiokota kile. Mwili wa Pamela uliwekwa ndani ya mfuko maalumu baada ya kupigwa picha kadhaa. Inspekta Nyaluto alikuwa karibu na Bosco kumuuliza hili na lile

    “Sasa huyu ndiye Bertha?”

    Bosco akajibu kwa hakika “hapana, ila kichwa mlichokikuta kwenye friji ndiyo cha Bertha”

    “Kiwiliwili cha Bertha kiko wapi sasa?”

    Ukimya wa Bosco ukamsuta Inspekta Nyaluto, akajuwa kuwa, Bosco hakuwa akijuwa lolote. Punde askari mmoja alisikika akipiga yowe kutoka katika chumba cha Bertha. Ni Harufu ndiyo iliyomvuta kudadisi kulikuwa na nini dani ya mkeka uliofungwa kwa nyaya za umeme. Mkeka huo aliutoa kutoka chini ya uvungu.

    “kiwiliwili chake kipo huku”

    kidole chake akakielekezea chini ya uvungu. Askari walifanya kazi hiyo pamoja na inspekta mwingine Jafari Hiza. Inspekta aliyeaminika sana katika kutatua matatizo mbalimbali yaliyoonekana kuyashinda uwezo wa jeshi la polisi.

    Wengi hawakung’amua.

    Hawakufahamu siri inayompa kiburi juu ya utatuzi wa kesi nzito kama hizo. Kulikuwa na msichana, mpelelezi binafsi anayeshughulika na kesi mbalimbali kwa kivuli cha uandishi wa habari. Inspekta wa polisi, Jafari Hiza alimfahamu vyema na kumtumia yeye katika kesi mbalimbali.

    Yeye alijulikana kwa jina la Vannesa.

    Katika kesi hii ya mauaji, iliyogundulika asubuhi ya jumatano yenye hali ya ubaridi na mawingu yaliyoleta unyevunyevu alikuwepo pia. Jafari Hiza alimnong’oneza “hizi kesi za mpenzi kumuuwa mpenzi zinaelekea kukupenda sana Vanessa” kama kawaida yake, tabasamu likamponyoka. Muda mwingine unaweza usielewe alitabasamu nini. Lakini uzuri wa Vanessa ulimfanya aonekane anatabasamu hata kama hajatabasamu.

    Huyo ndiyo mwanamke aliyemfanya mwandishi aliyekunwa na njaa iliyomsumbua tumbo hata akadiriki kumfuatilia Vanessa kwa ukaribu na kuibuka na mkasa mzima ambao yeye mwandishi huyo, aliamua auite NENDA NA MOYO WANGU. Mkasa ule ambao vannesa alionekana kushinda kesi ya kumtetea kijana masikini, aliyesemekana amemuua mtoto wa kigogo wa umoja wa mataifa.

    Vanessa alimtafuta mtu wa kwanza kugundua mauaji, ndani ya nyumba ya Bertha. Haikumchukua muda mrefu kuoneshwa Eva aliyekuwa hajiwezi kwa kulia. Alimtazama kwa tuo kabla ya kumpatia leso ya kujifuta machozi. Vannesa alikuwa simple kama wasemavyo watoto wa mjini. Kalamu na daftari lake kujitia mwandishi kweli na miwani yake ya kisomi kaishusha kiasi.

    “Naitwa Vanessa” alijitambulisha

    “Naitwa Eva” kilio kikapamba moto

    “Naomba unyamaze nina maswali machache ninataka kukuuliza”

    “Lakini afande mimi sijaua” Maneno hayo ya kiudhaifu yakamponyoka Eva. Vanessa alicheka kwa huruma na kumwambia

    “Usiogope, mimi sio afande ndio maana sijajitambulisha kama Afande Vanessa. Naomba uwe huru kuzungumza na mimi. Mimi ni mwandishi wa habari kutokea gazeti la ngurumo” alitoa kitambulisho cha kugushi hata hivyo Eva hakusumbuka kukitazama. kisha Vannesa aliendelea

    “Naomba nifahamu wewe unamfahamu vipi Bertha” Haikuwa shida kwa Vannesa kuuliza moja kwa moja kwa kutamka jina la Bertha, jina lake alikwisha ambiwa na wakazi wawili watatu wambea walioponyokwa na maneno wasiyoulizwa na mtu ambaye hawamfahamu. Ili mradi ilikuwa ni siku ya majonzi, kila mtu alizungumza lake analolijua kumuhusu Bertha. ‘alikuwa mpole, masikini dada wa watu’ alimsikia mmoja akisema . Huyu naye “aliongea na kumchangamkia kila mtu” wa mwisho kabla hajamuita Eva, ndiye akalitaja jina la Bertha “halafu Bertha ni mgeni, hapa hana hata wiki tatu. Yule jamaa yake aliyekuwa naye jana hapo GQ simuoni? ina maana hana taarifa” pia habari hiyo ilimsukuma haswa afanye mahojiano na Eva.

    Ilimsukuma kufanya mahojiano na Eva kwa kuwa alisikia pia kuwa mtu wa kwanza kugundu mauaji hayo ni mfanyakazi kutoka katika pub ambayo jana alikuwako Bertha. Pili mtu ambaye alikuwa naye jana ni mwanaume ambaye inasadikika kuwa leo hayupo katika tukio hili.

    Akaanzia hapo kupekenyua.

    XXXXX



    Raymond Chilambo aliipokea simu hiyo akiwa njiani kuelekea nyumbani kwa Bertha. Ilikuwa ni simu nyingine iliyoingia na habari mbaya sana kwake. Simu nyingine baada ya ile ya kwanza iliyompa taarifa juu ya kuuwawa kwa mtoto wake. Hivyo kila namba ngeni kwake aliipokea kwa hudhuni, ila ambayo anaifahamu hakujisumbua kupokea. Alifahamu fika ni wambea ambao wanataka kumpa umbea wa hapa na pale. Pole na kujikaza kama mwanaume, yeye aliuita umbea. Aliuita hivyo kwa kuwa aliamini alikuwa na maadui wengi kuliko marafiki. Marafiki wanaoibuka wakati wa matatizo yake na kujifanya wakimpa pole.

    “Raymond chilambo, nikusaidie nini” aliipokea hivyo Sauti ya upande wa pili ikakoroma. “unasema?” aliuliza kwa mshituko bila kufahamu kuwa simu ilikuwa imeshakatika. Aliishia kuhakikisha kama simu ilikuwa hewani “halo halo…” akaambulia patupu. ‘kivuli cheusi?’ akajinong’oneza.

    “baba Bertha unasemaje?” Bi Furahiya aliuliza. Raymond hakufahamu kuwa mawazo yalimfanya aweze kuongea kwa sauti, hata kwa ile sauti ya kujinong’oneza. Raymond alichanganyikiwa sana.

    Hivyo hakujibu chochote.

    Bi Furahiya ndiye alikuwa akiendesha gari, hivyo gari ilienda kwa mwendo wa kawaida sana. Raymond alihisi machozi yakimtoka kila akikumbuka jinsi alivyompenda binti yake. Hakuwa mtoto wake wa pekee, ila kwa Bi Furahiya alikuwa ni wa kwanza na wa pekee. Alikuwa na watoto wakubwa wawili wa kiume ambao aliwapata akiwa sekondari. Aliwakataa kutokana na ugumu wa maisha. Hivyo hakujua taswira zao za ukubwa wala hakuwa na uhakika kama walikuwa hai tena.

    Walifika eneo ambalo Bertha alikuwa akiishi. Umati mkubwa wa watu ulimfanya adondoshe chozi. Bi Furahiya alilia kwa uchungu zaidi hata kuwashitua wale wengine ambao walikuwa eneo lile. Mmoja mmoja alisikika akisema “ni ndugu yake” Mwingine akapatia kubashiri “huenda akawa ni mama yake”

    Wakati ambao Raymond na Furahiya wanaingia eneo hilo, maiti zilikuwa zimeshatolewa eneo la tukio na kupelekwa mochwari. Vanessa alikwisha kunakili hili na lile alilolipata kutoka kwa Eva, Inspecta Nyaluto alikwisha ondoka na Inspekta Jafary Hiza na askari wengine hawakukaa sana, nao walikwisha rudi katika ofisi zao. Walibaki askari wachache waliokuwa wakipekua nyumba hiyo kutazama kama kutakuwa na lolote litakalowasaidia kumpata muuaji. Raymond na Bi Furahiya wao walielekea hospitali walipoelekezwa kuwa miili ya watoto hao, imepelekwa.

    Simu ya Raymond ikaita tena. Raymond aliipokea bila kuongea chochote. Kama walikuwa wakitegana upande wa pili nao haukujibu kitu mpaka simu ilipokatika. Hapo wasiwasi ukamvaa Raymond na uwoga ukamtetemesha. Akaona si jambo la kulinyamazia, ni heri amueleze mke wake.

    XXXXX



    Moses baada ya kutoka Kwenye kibanda cha simu, alienda bar ya jirani kuivua midabwada aliyoiona kama mzigo kwake. Aliingia katika bar moja ya jirani na kiwanja cha mpira wa miguu huko karume, soko maarufu la mitumba. Hakuna ambaye aligundua hila zake. Aliingia katika bar hiyo kama mteja wa kawaida aliiagiza supu aipendayo, na bia ya baridi. Akiwa katika hali ile ile ya uzee aliyechoka, akanyanyuka na kwenda maliwatoni. Aliporudi mwendo ule wa kuchechemea haukuwepo. Ni nani angefahamu kijana huyu mzuri aliyehifadhiwa katika moja ya suti nadhifu, ndiyo Yule mzee mchafu aliyeagiza supu akiwa na lijimfuko lake lililowavuta wengi, kudhani huenda amebeba kinyesi? Mfuko ule ule ndiyo ulihifadhi suti hiyo na kiatu mchongoko kilichong’ara kwa rangi nyeusi.

    Alitembea vizuri na kuwavutia kila aliyekuwemo mahali pale. Kwa bahati mbaya aliyoidhamiria, aliipita meza aliyokaa mwanzo na kwenda kaunta. Akaiagiza bia ya moto, akiwa na tabasamu laini lililomfanya muhudumu amtazame mara ya pili. Hakika alikuwa ni kijana ambaye si mfupi sana wala mrefu wa kutisha lakini mwenye uso wa mvuto. Uso wake bapa ulinyimwa ndevu, kutokana na usafi alionao. Ni vipele vichache ndivyo viliathiri kidevu chake. Aliinywa haraka haraka huku akionekana mzoefu wa maji.

    Huyo ndiye Moses mwenye chuki kubwa na ukoo wa Chilambo. Chuki iliyomfanya atumie hila nyingi, hata zikamfanya ajidumbukize katika mahusiano na Bertha ili aweze kumnasa kila aliyehusika katika njama za mauaji ya familia yake. Hakujali ni nani alihusika ama hakuhusika ila kulipiza kisasi kulihusu ukoo mzima ili moyo wake uridhike. Alipokumbuka tukio lile alilolishuhudia mwenyewe kwa macho yake, aliiagiza konyagi chupa kubwa akaifakamia hata jirani yake akaogopa.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hasira zikampanda alipomkumbuka Raymond. Akataka kuzungumza naye, ndipo alipoamua kumpigia simu. Alimpigia simu wakati ule ambao Raymond na Bi Furahiya walikuwa njiani wakielekea hospitali. Simu iliita, ikapokelewa, lakini Raymond hakuongea chochote. Naye hakuthubutu kuongea. Si alifahamu kuwa Raymond aliitambua vyema sauti yake? Sasa iweje aharibu njama zake? Alizisikia pumzi nzito za Raymond zikipanda na kushuka. Simu ilikuwa hewani kwa nusu dakika mpaka alipoamua kuikata. Funda la pili, likaifuta pombe yote ndani ya chupa na kuondoka zake kwenda alipopajua yeye.



    Baada ya kutoka hospitali, Raymond na Bi Furahiya walielekea nyumbani. Ilikuwa ni karibu na jioni hivyo foleni haikuwa kubwa sana. Walipofika nyumbani walipokelewa na mlinzi wa getini, Majura.

    “Majura niache kidogo, leo sipo sawa”

    Alitamka Raymond, baada ya kusimamishwa na Majura pale getini. Ilikuwa ni kawaida kwa Raymond, kumuuliza Majura kama kuna mgeni yeyote aliyekuja. Siku hiyo haikuwa siku muafaka ya kumuuliza hayo. Alifahamu fika ni lazima wageni wangekuwa ni wengi kuhani msiba. Msiba ulimchanganya, lakini sauti iliyokoroma kama ‘kivuli cheusi’ Sauti iliyojitambulisha wakati alipopokea simu yake kutoka kwenye simu ya kibandani, ikamtisha zaidi.

    Alipopita sebuleni, aliwaona watu kadhaa waliokuwa wakilia kwa uchungu, yeye akawapita kama hakuwaona. Aliingia chumbani kwake kivivu, baada ya kuitikia pole zao kwa kichwa. Hakuvua chochote kutoka katika mwili wake mara alipoona kitanda, alijitupa hivyo hivyo na viatu bado vikiwa mguuni. Akazama kwenye tafakuri nzito, mkono ukiwa kichwani. Aliingalia taa kubwa yenye nakshi za kuvutia kama ingeweza kutoa jibu lolote kati ya maswali yaliyomsumbua. Lakini mawazo yake hayakuwa katika chumba alicholaza mwili wake. Aliukumbuka mchana ambao aliipokea ile simu. Mara baada ya kuisikia kauli iliyosema “naitamani roho yako” kisha ikakatwa ndiyo ilimuumiza kichwa. Kisha jina la ajabu likajirudia rudia kichwani mwake kama mwangwi “kivuli cheusi” kama angekuwa akihesabu basi angeshindwa kutoa idadi kamili ya alivyolitamka jina hilo akijaribu kuvuta kumbukumbu.

    Simu yake ikapata uhai baada ya muda. Haikutokea namba wala jina la mpigaji, kwenye kioo iliandikwa UNKOWN CALLER. Akaipokea akiwa anajua fika ni simu nyingine ya kitisho.

    “Nani mwenzangu” hakujitambulisha.

    Sauti upande wa pili ikajibu “Najua unanifahamu fika ni mimi Kivuli cheusi” Raymond aliongea akiwa anatetemeka katika sauti yake

    “Unahitaji nini? Kama Roho yangu njoo uichukue niachie familia yangu”

    “umepata ujumbe wangu kutoka kwa Majura”

    “Majura?” Raymond akauliza kwa jazba. Sauti ile upande wa pili ilijibu kwa kicheko cha dharau na kisha kukata simu. Raymond hakujijua kuwa ameshasimama na kukizunguka chumba chake mwenyewe mara ngapi, alichokitambua yeye ni kuwa yupo nje akimfuata Majura, mbio.

    “Majura ulikuwa unasemaje?” alimuuliza.

    Majura alitoa boksi moja kubwa lililonakshiwa na kumpatia Raymond “pole sana bosi kwa matatizo. Aliileta babu mmoja, huku akisisitiza ni ya muhimu sana uipate usiku wa leo” alisema. Akili ya Raymond haikuwa katika kusikiliza hadithi za Majura. Alikwishalifungua boksi lile muda mrefu, kilichokuwemo ndani ya boksi kikamfanya kupoteza fahamu.

    Kama asingekuwako Majura karibu yake, basi kisogo cha Raymond kingeisalimu ardhi iliyojaa changarawe. Umapepe wa Majura ukamfanya aropoke.

    “Nisaidieni jamaani!!!!!” Kila mtu aliyeisikia sauti ya Majura, alitoka mbio kuelekea getini.

    XXXXX



    Vanessa ni mwanamke wa ajabu sana. Aliwashangaza wengi katika uvutaji wake wa sigara. Alizivuta zile sigara kubwa zilizoitwa ‘cigar’ Katika ulabu alipendelea haswa zile wine tamu tamu, kama sweet anna na sinzano. Huyo ndiye mpelelezi aliyekataa kujiunga na kikosi maalumu cha usalama wa taifa na kubaki kama mwandishi wa habari wa kujitegemea.

    Siyo kwamba hakufuatwa, hata Raisi mwenyewe aliwahi kupoteza dakika zake na kumuandikia barua ya kumomba ajiunge na kikosi hicho. Alikataa bila sababu, lakini sababu aliijuwa mwenyewe. Vanessa aliupenda uhuru wa kufanya kazi zake binafsi. Hakutaka mtu wa kumshinikiza afanye hiki na kile. Kazi yake ya kwanza iliyomletea umaarufu huo ni ile kutoka katika kisa cha Nenda na moyo wangu iliyomuhusu kijana anayeitwa Ramon kama nilivyoeleza hapo mwanzo. Magazeti yalimuandika kwa kumtukuza na hata waandishi wengi wa riwaya wakamtaja katika riwaya zao kama mwanamke wa chuma. Akawashinda wanaume katika mapigano na hata upeo wa kufikiria.

    Leo alikaa ofisini kwake nyuma ya kiti kikubwa kinachozunguka kama tiara. Glass ya sinzano ilikuwa mkono wa kulia, sigara ikashikwa mkono wa kushoto. Kichwa kikaegemea kiti kikiwa katika tafakuri nzito. Aliwaza kuhusu mauaji ya kutisha.

    Mara akakumbuka kitu.

    Aliinama kwenye meza yake iliyojaa picha mbali mbali za maiti ya Bertha na Pamela. Akauvuta mtoto wa meza hiyo, kisha kuibuka juu na bahasha iliyohifadhi kitu Fulani. Vanessa aliiangalia bahasha iliyohifadhi nakala moja ya picha ile ya kivuli cheusi aliyojipiga Moses.

    Wakati akiitazama picha ile, simu yake ya mezani ikapata uhai.

    “Vanessa” ilikuwa ni sauti ya Inspekta Jafary Hiza

    “habari yako Hiza?”

    “salama, umepata majibu yeyote juu ya mpigaji wa picha hiyo?” Hiza aliuliza

    “hapana na bado najiuliza kwanini mtu huyu ameamua kuuacha ushahidi huu kama sehemu ya kuendeleza mauaji yake” alisema Vanessa

    “sawa, pia majibu ya Postemoterm kuhusu ule mwili wa yule binti mwingine tuliyemkuta pale sebuleni”

    Vanessa akauliza “yule aliyeibusu ardhi akielea juu ya mapovu?”

    “Acha mzaha Vanessa, Majibu yametoka na yanasema kuwa, alikunywa sumu kali iliyomnyang’anya uhai wake” Inspekta Hiza alihitimisha hivyo na kuikata simu mara baada ya kuagana. Vanessa akabaki akiwa hajaelewa jambo.

    Alijidumbukiza kwenye tafakuri nyingine nzito, hata pombe iliyoanza kumkolea, ikimsaliti na kubaki mweupe. ‘ina maana alianza kufa yeye au Bertha? Ni nani alikuwa wa kwanza kuuwawa? Ni nani alikuwa mlengwa wa mauaji haya?’ alijiuliza Vanessa akiishirikisha nafsi yake.

    Alisimama akakizunguka chumba chake. Akaongeza kinywaji kwenye glass akakifuta chote. Alienda pale, akarudi kitini alipotaka kukaa wala hakukaa, alikuwa akiwaza tu. Ghafla alitabasamu, tabasamu lililochanua na kuufanya uso wake kuwa mzuri na kuonesha taswira ya umalaika. Hakika Vanessa alipendeza akicheka katika raha. Mashavu yake yakabonyea na kujenga dimples. Alimuita katibu muhtasi wake, alieyemchukulia kama mdogo wake. Yeye aliitwa Naima, mtoto wa kitanga. Binti aliyeiacha shule kutokana na shida za kuilima ardhi iliyonuna kustawisha mazao yake. Aliyetundikwa mimba kabla hajalimaliza darasa la saba na siku ya kujifungua mtoto wake alikataa kutoka akiwa hai. Alifia tumboni baada ya kukosa pumzi. Kipindi hicho Naima alikuwa na miaka kumi na nane.

    Alikutana na Vanessa katika harakati zake za kutafuta maisha, alikuwa akiuza mchicha, sukuma wiki na mnafu. Ni nani ambaye hakutokwa na mate alipomtazama Naima? Ni nani ambaye, hakuacha kumsifia alipotazama kifua chake kilichotuna kiuchokozi na kufanyiza mfano wa matiti kifuani mwake? Alikuwa na kiuno kilichobeba mapaja manene na mguu uliofaa kuitwa wa bia. Huyu ndiye Naima mwenye asili ya kiarabu kutoka Tanga, hakutumia mkorogo wowote katika weupe wake.

    “nimepata wazo” alimwambia Naima

    “wazo gani?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “kuhusu haya mauaji”

    “mauaji ya hawa mabinti wawili waliouwawa huko kiitonyama?” Naima alimuuliza.

    “ndiyo. Nimepigiwa simu na Hiza, amenieleza kuwa huyu mmoja” Vanessa alikuwa akiongea huku ameshika picha ya Pamela, akiwa ameyalalia mapovu. “ameuwawa kwa sumu. Hivyo inavyoonyesha, huyu alikuwa wa pili baada ya huyu wa kwanza aliyekatwa kichwa” macho yakamtoka pima Naima na kubaki mdomo wazi. Hakujuwa ni vipi Vanessa akili yake ilifanya kazi haraka hata kutambua hayo yote bila kumfahamu muuaji.

    “Inawezekana huyu msichana hakuwa katika njama hizi, ila kihere here chake kilifanya hata akaupoteza uhai” alinyamaza akiyameza mate kwa raha huku akitabasamu kama kawaida yake

    “inawezekana huyu aliingilia harakati za muuaji na kutaka kuitoa siri ya mauaji haya”

    Naima kicheko kikamponyoka na kumwambia Vanessa “sielewi wewe ni binadamu wa aina gani, nimeanza kukuogopa”

    Vannesa akaendelea kumwambia “na ndio maana hata pale eneo la tukio, hatukukuta simu. Inawezekana simu zingetuwezesha kupata ushahidi mwingi. Zilipofuatiliwa namba zilizokuwa zikiingia katika simu ya huyu Bertha..” akashika picha ya Bertha “hakuna historia yeyote. Hivyo inaonekana huyu muuaji kuna mchezo mchafu ameucheza na hawa watu wa mitandao kama sio hawa wajanja wa it”

    XXXXX



    Raymond alipokuwa akikimbizwa hospitali, aliipata nafuu. Gari ilikuwa ikienda kasi sana akiwa mapajani mwa Bi Furahiya. Alijishika kichwa na kumtazama mkewe. “niko wapi?”

    Bi Furahiya alishituka kumuona mumewe ameamka, alifurahi sana na kumwambia dereva asimamishe gari. Wote waliokuwemo walishangaa na kumshukuru mungu kwa pamoja.

    “mungu mkubwa!!!”

    Raymond alitoa amri yakurudishwa nyumbani kwa kuwa alijiona hakuwa na tatizo la kumpeleka hospitali.

    “sawa baba Bertha kama ni hivyo, lakini ilikuwa muhimu wewe kwenda kufanyiwa check up..”

    “Nimeshasema ulikuwa ni mshituko wa kawaida” Raymond akafoka.

    Raymond alikumbuka kila kitu kilichotokea na kuwahadithia kila kitu. Aliwahadithia Bi Furahiya na kaka yake Nyato Chilambo, kuhusu ujio wa lile boksi na alichokiona ndani yake. Boksi lililonakshiwa, lililomfanya apoteze fahamu. Kwa kuwa Bi Furahiya alifahamu yote yanayoendelea, alianza kupatwa na hisia mbaya. Alitetemekwa na mwili sanjari na mapigo ya moyo yaliyomuenda kasi zaidi. Alitamani kulia machozi hayakutoka. Alibaki kuwa mnyonge akisubiri litakalotokea.

    Walipokuwa njiani, ndipo gari yao ilipata pancha na kuwalazimu wakae zaidi ya nusu saa eneo hilo la barabara iliyosuswa kupitiwa na magari mara kwa mara. Milango ilikuwa wazi, upepo ukiwapiga. Bi Furahiya alimpatia Raymond barua iliyoandikwa kwa damu. Barua hiyo iliandikwa na Moses. Barua yenye vitisho na masharti ya kuogofya.

    Raymond aliisoma huku akitetemeka na moyo kumuenda kasi zaidi. Alitoa onyo. Yeyote aliyeyasikia hayo, asitoe habari hiyo kwa yeyote. Wote wakatii. Tairi likarekebishwa na kuwekwa la spare.

    Safari ya kurudi nyumbani ikaendelea

    XXXXX



    Moses alijirudisha katika mavazi yake yale yale ya kuudhi na taswira ya kishamba iliyomzeesha. Alienda mpaka nyumbani kwa Raymond, kisha akakirudia chumba chake kilichochoka na kuhifadhi kunguni viroboto na kila aina ya wadudu, katika ile guest ya bei nafuu huko Keko magurumbasi.

    Kukaa kwake keko magurumbasi, Si kwamba hakuwa na pesa hata aamue kukaa katika chumba kama hicho. Pesa alikuwa nazo nyingi, tena nyingi zilizomkinaisha. Urithi wa kampuni ya baba yake, Mzee Utonga usingemtosha kweli? Usingemtosha kuishi katika hoteli zenye hadhi ya nyota tano? Ale vinono huku akisaza akiwa amezungukwa na walimbwende wenye hadhi ya juu? Mivinyo ya gharama na vyakula vya kutoboa amana ya mwenye kubipu starehe?

    Hakuna ambaye hakumjua Moses kipindi yupo chuoni. Huyo ndiye Moses aliyejiita Musolline pale mlimani. Aliyeuvaa umasikini hata akauzoea, akaupenda na aliutamani pale alipokuwa mbali nao. Umasikini uliomuhifadhi mbali na mkono wa polisi pamoja na wale aliowaweka katika harakati zake za kulipiza kisasi.

    Alifanya haraka kurudi mafichoni kwake, baada ya kutimiza njama zake. Maficho yaliyomkumbatia kwa kunguni, mbu, viroboto na patasi, waliomganda hapa na pale. Kwa hali ya ulevi, mara moja moja sana; walionesha kumgasi na kujipiga makofi yasiyo na madhara hata ya kuuwa mbu. Jinamizi la kisasi, lilimsukuma kuanza mauaji kwa mpenzi wake. Bertha mpenzi wa kujilazimisha. Hiyo yote ikiwa ni njama ya kutuma salamu kwa wahusika. Alimuonea huruma sana Yesay kwa kuwa aliumiza hisia zake siku alipomsaliti na kumchukua msichana wake. Bertha kwao kulikuwa na pesa lakini alikuwa na tamaa ya pesa nyingi zaidi. Moses alikuwa nazo za kumchanganya Bertha hata akamsaliti Yesaya wake waliotoka mbali. Bertha hakujua njama za Moses akajisifia kwa wenzake kila alipopita pamoja na Moses.

    Moses aliulalia mkono wake akitafakari safari zake za tangu asubuhi, mpaka sasa usiku wa manane akiwa amelewa bwii. Aliikumbuka safari yake ya kwanza, alipoenda katika ile bar. Aliingia kama Mzee aliyechoka na kuagiza supu ya kuku na chapati mbili pamoja na bia ya baridi. Akacheka

    “Niliwaweza kweli” kwa sauti ya chini akasema “Tangu lini nikanywa bia ya baridi mimi?” hakukuwa na wa kumjibu, hivyo alicheka zaidi. Ilishangaza sana alipocheka kwa nguvu hata kikohozi kilichokuwa kikishitua shitua, sasa kikaachia na kujirusha katika kidevu chake. Alijifuta mdomo kwa mkono wake. Mara alibana pua yake, akiiga sauti fulani ya kike. “shenzi nilijuwa tu huyu babu hawezi kurudi tena” alimuiga yule muhudumu katika ile bar alisimama huku akipepesuka pepesuka kwa ulevi. Hakika alilewa. Alienda kushoto akarudi kulia, lakini alikuwa imara akapiga breki asiibusu ardhi.

    Sakafu iliyopoteza hadhi ya kuitwa sakafu kwa mashimo mashimo yaliyojichimba baada ya cement kumomonyoka. Alisonya, kisha akabeua na kuanza tena kucheka. Aliikumbuka safari yake ya kwenda nyumbani kwa Raymond Chilambo na kukutana mlinzi aliyemfahamu fika, “bwana mdogo, Majura” akajisemea.

    Aliporudi kutoka kumpa mzigo ule Majura, mzigo uliomuangusha na kumfanya Raymond kupoteza fahamu ndipo akapata wazo, wazo la kuangamiza tena. Alitaka kuangamiza, ili alinde uhuru wake. Ndani ya moyo wake alihisi kabisa hayupo huru na mtu ambaye alihatarisha maisha yake alikuwa ni Omary Kibanga yule muhudumu wa nyumba ya kulala wageni.

    Tukio lile la kuokota kitambulisho alijua fika lingemtia katika wakati mgumu endapo serikali ingefikia uamuzi wa kutangaza kumtafuta muuaji wa bertha kupitia katika vyombo vya habari. Alikuwa na hakika hakuna mwenye picha yake, wala taswira; hivyo isingekuwa rahisi kutambulika.

    "lakini, lakini.." akiwa katika kuwaza akawakumbuka wahudumu wa pub ya GQ. Eva ndiye muhudumu wa mwisho kumuhudumia yeye na Bertha. Huyo ndiye angeharibu harakati zake za kulipiza kisasi. Katika jeshi la polisi, walikuwako vijana walio na uwezo mkubwa wa kuchora picha kwa kuhadithiwa tu jinsi mtu alivyo. Eva ana uwezo mkubwa wa kuwaongoza vijana hao na sura yake kupatikani.

    "Nimuanze nani?" akajiuliza huku akiangalia saa yake. Ilikuwa yapata saa 12:30 usiku. Uhakika wa kumuanza Eva ukapotea. "lazima leo nifute ushahidi wa mmoja" akajisemea huku akifika eneo la maegesho ya bajaji na kuichukua mojawapo ya bajaji nyingi zilizojipanga hapo. Bajaji hiyo hakupenda kuichukua moja kwa moja mpaka keko magurumbasi yalipo maficho yake, Alitumia bajaji tatu mpaka kufika hapo kwenye nyumba ya kulala walala hoi. Mtu wake wa kumtoa kafara ndio kwanza alikuwa anapasha mapafu moto kwa kahawa.

    Tabasamu laini likamponyoka Omary.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nadhani moyoni mwake alipendezwa na utembeaji wa mzee huyu mchafu. Kwa hila za moses na jinsi alivyopenda kubadilisha muonekano wake, ugoro ukamzoea na kumpenda. Meno yake yalikwisha chafuka na kufanana na wazee kabisa. Akalijibu tabasamu la Omary kwa kuonesha meno yake machafu. Meno ambayo kuna wakati alilazimika kulitoa lile jino la dhahabu na kubaki kama pengo

    "ha! Babu! Kumbe una. pengo?" Moses akacheka kicheko cha kuudhi. kicheko alichokitia na kikohozi kikavu. Kikafanana kabisa na kicheko cha kizee. Akafanikiwa kumlaghai Omary, akamjibu

    "Mjukuu wangu una maswali mengi"

    "Ah! Babu unajua siku zote nimekaa na wewe sijawahi kukuona ukiwa na pengo"

    Moses akijitia kusikilizia maumivu ya kiuno, Omary akaendelea "Nikajua wazee wa kitongoji washakung'oa" wakacheka kwa pamoja Moses akamlaghai Omary, Omary nae akajaa kwenye hila za Moses.

    "nina kiu ya kahawa mjukuu wangu"

    Omary kwa upendo, akajibu haraka haraka "anha babu! Lipo birika zima siwezi kumaliza lote acha nikumiminie"

    Sekunde ya kugeuka, likawa kosa kwa Omary. Moses alitoa ule unga wa sumu ya nyongo ya mamba na kuimwaga ndani ya kikombe cha kahawa aliyokuwa akiinywa Omary. Omary akageuka na kikombe cha kahawa na kumpatia Moses. Moses akakohoa kiasi huku akimtupia jicho la wizi Omary. Omary akakifakamia kikombe chote na kukifuta pale pale. Moses naye akainywa kahawa yake funda moja na kuingiza mkono wake ndani ya mfuko wa koti kuukuu na kuibuka na picha ambayo alipiga kivuli chake. Picha ambayo aliipiga mara baada ya kumuua Bertha na Pamela. Alikuwa nazo nyingi mara baada ya kujipiga na kutoa nakala nyingi.

    Dakika tatu zikawa nyingi, Omary naye alijinyonga tumbo macho yakamtoka kama anayekufa saa yeyote. "Babu nakufa" Moses akacheka pia na kumwambia kwa hasira "Pole kwa kujua siri yangu unakufa kwa kufuta ushahidi"

    Wakati ambao alikuwa anataka kukata roho, Omary alikuwa anataka kumshika Moses kwa hasira akaambulia kuipokonya picha aliyoishika Moses. Picha ya kivuli cheusi. Roho ya mauti ikatwaa roho yake na kumlaza usingizi wa milele Omary.

    Ukawa mwisho wa Omary Kibanga.

    Moses alipoyakumbuka yote hayo, akabaki akicheka kilevi. Hivyo ndani ya chumba hicho hakukaa sana, dakika chache baadaye ikawa sawa na hakuwa hata na chembe ya kilevi, pombe ikamkatika. Moses akawa katikati ya mitaa ya kigogo mburahati akitafuta nyumba nyingine ya kujificha. Kule akawa amehama na kila kilicho chake.



    XXXXX

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog