Search This Blog

Sunday, 19 June 2022

KIVULI CHEUSI - 2

 





    Simulizi : Kivuli Cheusi

    Sehemu Ya Pili (2)



    Wakati ambao alikuwa anataka kukata roho, Omary alikuwa anataka kumshika Moses kwa hasira akaambulia kuipokonya picha aliyoishika Moses. Picha ya kivuli cheusi. Roho ya mauti ikatwaa roho yake na kumlaza usingizi wa milele Omary.

    Ukawa mwisho wa Omary Kibanga.

    Moses alipoyakumbuka yote hayo, akabaki akicheka kilevi. Hivyo ndani ya chumba hicho hakukaa sana, dakika chache baadaye ikawa sawa na hakuwa hata na chembe ya kilevi, pombe ikamkatika. Moses akawa katikati ya mitaa ya kigogo mburahati akitafuta nyumba nyingine ya kujificha. Kule akawa amehama na kila kilicho chake.



    XXXXX



    Maeneo ya kijitonyama ilipo bar ya GQ, Kulikuwako na pilika pilika za kila aina. Mvua iliyokera haikukoma kunyesha na kusababisha mazingira kuwa machafu kama yalivyokuwa. Vidimbwi vya maji machafu vilikanyagwa na magurudumu ya magari, tope zito likawarukia wapita njia waliokosa uvumilivu wa kusubiri mpaka mvua iishe.

    Mmoja wa wapita njia hao, alishushwa kutoka kwenye bajaji na kukumbana na dhahama hiyo. Kiatu chake cha kufuta, kikarushiwa tope zito kisha gari likaendelea kutembea taratibu kama mwanamke mwenye maringo ajitingishaye. Mtu huyu alilitazama gari lile huku akimtusi dereva wake. Akamlipa dereva ujira wake na kukimbilia ndani ya pub hiyo.

    Saa 4:26 asubuhi, watu walikuwa wengi sana. Aliangaza huku na kule, akaipata nafasi moja iliyo mafichoni karibu na tawi la mti. Akatembea taratibu kwa mwendo ambao si wake. Nani ambaye angefahamu haukuwa wake kama alikuwa amebadilika kiasi hicho? Aliibuka kutoka mafichoni kwake kigogo akiwa amepunguza vitu viwili ambavyo vilikera wasichana. Kwanza kitambi pili unene ulioanza kumnyemelea. Alitumia wiki chache tu za kufanya hivyo.

    Alibadilika kiasi kwamba hakuna ambaye angemkumbuka. Alikuwa mwembamba mwenye kifua kipana cha mazoezi na mwili ulioenda hewani. Nywele zake akanyoa tofauti kama alivyozoeleka. Sasa alinyoa kipara kilichong'arishwa kwa mafuta. Ndevu chache za bandia zilizotengeneza O kwenye mdomo wake, hakuna atakayekubali kuwa huyo alikuwa maeneo hayo wiki chache zilizopita. Akajihifadhi ndani ya suti nzito ya gharama. Hakika Moses akapendeza hata akajipenda alipotazama muonekano wake mpya. Suti hiyo ilimbana na kuwa kama mmoja wa wanamitindo jukwaani akinadi aina ya nguo mpya.

    Alikaa huku tabasamu likiendelea kung'ang'ania juu ya mdomo wake. Akachomoa kasha la sigara na kuivuta moja mara baada ya kuipachika mdomoni. Huyo ndiye Moses mwenye kila hila za kulipiza kisasi. Alifanya kazi kwa muda mrefu, akitegemea ipo siku angeanza harakati zake huku akitafuna taratibu fedha zake. Utajiri mwingine mkubwa wa fedha, ulitunisha akaunti yake kutoka kwenye kampuni ya baba yake.

    Aliendelea kuangaza angaza huku na kule akimtafuta Eva. Akajisema alipokuwa akimtafuta bila mafanikio yeyote.

    "Haiwezekani awe amehama bar"

    Akaendelea kuvuta taratibu moshi wa baridi uliokuwa ukitoka kwenye sigara. Kama ujuavyo wahudumu wa kwenye bar zetu za Tanzania, zikachukua dakika nyingi mpaka Moses alipofuatwa kusikilizwa.

    "Nikusaidie nini kaka?"

    Moses si kwamba hakumuona au hakusikia alichoulizwa, ila msichana huyo alikuwa si mgeni kwake. Msichana huyo ndiye alikuwa akimtafuta. Akajiuliza "ina maana amenisahau? Au haujanifahamu?"

    Eva akarudia kwa kuudhika "kaka nakusubiri wewe"CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Moses akasema "niletee Ndovu ya moto"wakati ambao Eva alikuwa anaondoka, Moses akapata nafasi ya kuzungumza "ningeomba ukirudi unipe dakika zako tano naahidi kukulipa"



    Moses hakuwa msanii wa kubadilisha taswira yake pekee hata lafudhi haikutofautiana kabisa na mfaransa. Ungesema labda ni mkazi wa Rwanda au nchi zilizotawaliwa na mfaransa. Lakini ukweli ni kwamba lugha hiyo aliisomea chuoni kutokana na kukuza uhusiano mzuri wa biashara katika kampuni ya baba yake.

    Si kifaransa pekee alikiweza kireno, kichina hata kwa kukuandikia. Huyo ndiye Moses aliyelelewa na kukuwa katika familia ya Mzee Joram Utonga. Mzee ambaye kwa miaka mingi Moses alifahamu kuwa ndiye baba yake mzazi.

    Haikuwa hivyo.

    Mzee Utonga alilazimika kumlea baada ya mkewe bi Matopi kunyang'anywa uhai na risasi iliyofumua vibaya kichwa chake. Haijulikani ni nani aliyemuua kwa sababu ushahidi ulikosekana. Mzee Utonga alimfahamu muuaji japo hakuwa na uwezo wala sauti ya kumuadabisha muuaji huyo. Moses akaelezwa asili na ukweli wa maisha yake na Utonga mwenyewe alipokuwa akiyapigania maisha yake kutokana na risasi iliyopenya moja kwa moja na kukifumua kifua chake. Damu nyingi zilimuangukia mikononi Moses. Utonga akatamka kwa shida sana

    "mali na kila kitu ni vyako urithi huu nimekuandika we.." hakuweza kumalizia neno lake lakini alifanikiwa kueleza kila kitu, akayafunga macho yake kistaarabu. Moses alilia kwa uchungu sana. Alilia kilio ambacho si rahisi kwa mtu wa kawaida kumbembeleza anyamaze. Alilia si kwa sababu Mzee Utonga amefariki, alilia kwa sababu ni yeye aliyesababisha kifo hicho.

    Eva akarudi na kinywaji huku furaha ya kumnasa afrikast asubuhi asubuhi ikizidi kutanua papi zake na kuunda kitu kilichoitwa tabasamu. Eva alimkaribisha

    "karibu " Moses aliyejitambulisha kwa jina la Frank, hakujibu ahsante zaidi ya kwenda katika hila yake moja kwa moja.

    "Unakaa wapi vile?"

    "Kigogo mbuyuni" Eva akajibu bila kufahamu furaha gani aliyompa Moses. kazi ya kutafuta windo lake. Moses alimaliza kile alichopanga kukisema.

    "Nahitaji kukaa na wewe jioni ya leo katika ile bar ya jirani na kituo cha kwenda mburahati" akatoa noti 5 za shilingi elfu kumi na kusema kwa ushawishi "tafadhali!"

    dhiki ikamlaghai Eva akaingia katika mtego wa Moses akakubali bila hiyana. Hata hivyo hakumkumbuka kabisa.

    XXXXX



    Vannesa alipokea taarifa za mtu aliyekufa huko Keko Magurumbasi. Inspekta Jafari Hiza ndiye alimpa taarifa hizo kwa hali ya kuchanganyikiwa sana. Zilikuwa ni habari za kushitua, lakini zilikuwa ni ambazo zinaweza kumpa mwanga katika uchunguzi wake. Watu walikuwa ni wengi kama ilivyo sehemu yeyote yenye tukio la kushangaza.

    Vannesa alipata shida kujipenyeza kati kati yao mpaka alipofika kwa Jafari Hiza. Hakukuwa na salamu, picha yenye kivuli cheusi ikawekwa mkononi mwake.

    "muuaji ni mmoja na lile tukio la msichana Bertha kule kijitonyama"

    ilikuwa sauti ya Jafari Hiza iliyozibua masikio yake kwa furaha.

    "maiti yako wapi?"

    Akaongozwa mpaka ilipo maiti ya kijana Omary. "amekufa kistaarabu" vannesa akataka kucheka akaishia kutabasamu. Akaendelea "hajatema povu wala damu? Ni ajabu"

    Inpekta Jafari Hiza akaongea kwa kuhuzika "vannesa sipo tayari kufanya kazi na mtu mwenye mzaha kama wewe naomba ujaribu kuwa serious wakati mwingine" alinyamaza kama aliyejaribu kuangalia huku na huko, kisha akasema kwa utaratibu sana “.. unafanya kazi na jeshi la polisi kwa usiri naomba uiheshimu nafasi hii uliyopendelewa” bado Vannesa akacheka kama hakuambiwa kitu. Baadaye Vanessa akaongea kwa hasira “si nafasi ya upendeleo kufanya kazi na jeshi zembe lenye tama ya pesa kam la polisi. Jeshi lililojaa rushwa na uhaini wa hali ya juu. Sipo hapa kwa ajili ya maslahi ya polisi ali kwa ajili ya roho za raia wema naomba unielewe kwa hilo hiza” kisha kaitazama picha ile, haikuwa na tofauti na ile aliyo nayo ofisini kwake. Akaachana nayo.

    Akaungana na watu wawili watatu waliojikusanya kimakundi kujaribu kusikiliza kama angepata lolote la maana, lakini hakuna lililomsaidia. Alipotaka kuondoka, akavutwa na mtu mmoja aliyekuwa akilia sana kuliko hao waliokuwa wakishangaa. Yeye alikuwa ni kijana aliyekuwa akielekea katika utu uzima. Uso wake ulikomaa kiasi cha kukadiria hajapoteza miaka 45 basi angefikisha 50 kabisa. Alionekana kuwa alikuwa na mengi ya kuzungumza kuliko watu walivyolichukulia swala hilo kiuwepesi. Jicho la mtu wa kawaida lingemuona yeye kaguswa tu kama wengine ambao wangekuwa wamefiwa. Ndio maana askari uchwara walimpita lakini Vannesa aliyebarikiwa ushushu, akamfuata kabisa.

    "Habari yako kaka?"

    huyo aliyekuwa akilia, akalivuta kamasi laini na kufuta chozi lililomdondoka. Akamtazama aliyemsalimia, 'binti mrembo' akajinong'oneza, kabla hajajibu salamu ya Vannesa.

    "si nzuri kama uonavyo"

    Vannesa akakaa kitako pembeni ya mtu huyo.

    "naitwa Vannesa" yule mtu alimtazama Vannesa kwa kumsahili juu mpaka chini, kwa macho yaliyolowa machozi. "mimi si polisi wala mwandishi wa habari" vannesa alijaribu kujitetea kumtoa hofu "unajua hiki kifo cha Kibanga kimenishangaza sana. Lakini hakuna la maana nililopata zaidi ya kusikia kuwa alichukua msichana wa mtu?" alitia hila zake ili apate chochote kutoka kwa huyo mtu.

    Yeye alijulikana kwa jina la Mfaume, mfagizi na aliyehusika kusafisha vyumba vya nyumba hiyo. Mfaume akahamaki kwa hasira "Waache unafki" kikohozi laini kikampitia na kamasi alilivuta, kisha akaendelea. "Omary alikuwa hana tabia za wasichana hata kidogo. Nimekaa naye miaka 10 katika hii biashara tangu keko machungwa mpaka hapa. Mpaka niliwahi kuhisi huyu kijana jogoo hapandi mtungi ila kijana wa watu yupo safi" kilio kikaanza upya. Hakuna lolote aliloongea Mfaume, la kumjengea picha Vannesa katika kuanza upelelezi wake.

    Vanessa akaendelea kudadisi."Ina maana ameuwawa na mwendawazimu gani" akajitia kuweka hasira katika sauti yake "Hata amuue kijana mpole kama Omary?"

    Mfaume akavuta kamasi, kisha akamuinamia Vannesa. "sikiliza dada yangu hawa polisi watahangaika tu, lakini muuaji amekwisha ondoka na sidhani kama ni rahisi kumpata."

    Mapigo ya moyo wa Vannesa yalimuenda kasi kwa furaha, kupata lile alilotarajia. Akatega ufahamu wake wote aweze kupata picha halisi.

    Akahoji "ina maana muuaji unamfahamu?"

    Mfaume akatingisha kichwa, huku akitabasamu kuonesha alimaanisha alichozungumza.

    XXXXXCHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Jirani na kituo cha daladala ziendazo kigogo mburahati na ruhangwa, kulisimama taksi moja aina ya chaser mayai, yenye rangi ya maziwa. Vioo vilivyopandishwa mpaka juu , viliashiria kuwa kipupwe cha kutosha kilipuliza ndani ya gari hilo. Yule ambaye alikuwa kama mteja kwenye gari hiyo, alishusha mguu wa kwanza, hatimaye wa pili mara baada ya kumlipa ujira wake dereva huyu mzee aliyechoka. Gari lilipoondoka, mteja alionekana kuwa nadhifu kuliko wakazi wa kitongoji hicho. Yeye alivaa suruali iliyokolea upanga kwa moto wa pasi shati iliyobana kifua chake na tai ya teksido.

    Alikuwa Moses, nyuma ya miwani ya transparent, alipendeza. Kila jicho lilikuwa upande wake. Kabla hajavuka, Moses alishikwa shati. Alipogeuka kumtazama aliyemshika, alikuwa Eva.

    "Frank!?"

    Moses alishitushwa sana kumuona Eva akiwa amewahi kiasi hicho. Mshituko mwingine uliongezwa na jina aliloitwa. Nadhani alikwishasahau hata kuwa ni yeye ndiye alimdanganya jina hilo. Baada ya sekunde chache alikumbuka hila zake. Alikumbuka kisasi na roho ya mauaji ikamuingia na kuuchukulia uzuri wa Eva kama kinyago. Tabasamu laini lile linalowachanganya wengi, likamponyoka Moses na kumlaghai Eva.

    "sikutegemea kama ungewahi kiasi hiki." Akamshika mkono Eva, "twende tena ni heri umewahi" Moses alisimamisha taksi nyingine na kumuongoza Eva ndani. Eva alishitushwa, haikua hivyo kama walivyoahidiana asubuhi pale GQ. Akauliza "mbona umebadilisha sehemu?"

    ilimchukua muda Moses kujibu. Lakini lengo na dhumuni hakuhitaji kusumbua maficho yake mapya kwa sasa. Aliwaza endapo angempeleka mbali, huko ndipo ungefanyika msako wa muuaji anayeacha kivuli cheusi.

    "Tupeleke kinondoii"

    Dereva aligeuza gari na kuelekea alipoagizwa. Moses alikumbuka njia ya kuelekea katika apartment moja nzuri sana maeneo ya Masaki. Mmiliki wake alikuwa ni mholanzi fulani ambaye alimfahamu vizuri. Alifahamu michezo yake michafu aliyoicheza na kumfanya yeye kumiliki apartment kama hizo kumi pembezoni mwa ufukwe wa bahari. Hivyo alikuwa na hakika kwa lolote baya lingetokea, ingebidi mholanzi huyu kumfichia siri hiyo nzito.

    Wakaegesha pembezoni mwa jumba la kifahari. Jumba lililomezwa na bustani iliyotota ukijani uliovutia macho. Alimlipa dereva elfu 10, huyu alikuwa ni wa pili alimtoa pale kinondoni a kumfikisha Masaki ilipo apartment hiyo.

    Mchezo wake ulikuwa ni ule ule kubadilisha madereva, kupoteza ushahidi. Urefu wa njia na foleni za hapa na pale, ziliwatosha Eva na Moses kuwa wapenzi. Eva akahoji kwa bumbuwazi

    "sasa mpenzi" huku akiendelea kushangaa kila kona ya bustani na wafanyakazi waliosimama wakiwatazama wageni hao. Eva akaendelea "kama una nyumba nzuri kiasi hiki? Kwa nini usiwe na gari ya kutembelea?"

    Si kwamba hiyo ilikuwa ni nyumba nzuri pekee kwa Moses. Alikuwa nazo nne zilizobebana na kuitwa ghorofa. Moja ya kijitonyama nyingine upanga na mbili za bunju ambayo moja ndiyo anayoipenda zaidi. Alikuwa na magari ya kifahari ya kutosha. Hivyo alitabasamu tu na kumuona Eva ni mmoja kati ya wasichana waliokosa elimu ya kutosha kutokana na kushindwa kutambua tofauti ya nyumba na apartment ya kukodisha. Walikaribishwa kwa bashasha kutoka kwa wahudumu waliohakikisha usafi wa nyumba hiyo ukiwa ni wa hadhi ya kimataifa. Moses alivaa pama kubwa na kuwa kama mtalii huku akiwa amemshikilia Eva kiuno chake. Hakika wakaonekana kuwa wapenzi wa kudumu wa muda mrefu.

    Wakajitoma ndani.

    Huko walikaribishwa na kipupwe cha kiyoyozi kilichomfanya Eva aone hakika maisha ndio hayo. Moses alifahamu kila kona ya nyumba hiyo, hakuwa mgeni kufungua hiki na kile. Akaitoa chupa ya mvinyo wa dodoma. Eva akaropoka “Anha! Dompo!"akiwa ameishika chupa yake "Naipenda sana"

    waliinywa hiyo kisha chupa ya pili wakaimaliza na ya tatu. Eva akawa hoi kwa kilevi aliposhikwa kidogo na Moses, akaita jina la Frank kwa huba.

    Moses akambeba na kuingia naye chumbani. Huko kitu kilichofanyika, hakikufaa kutazama. Kichwa kilinyofolewa, mikono na miguu vikatenganishwa na kiwiliwili. Alikichukua kichwa hicho na kukihifadhi ndani ya friji la chumbani hapo. Mkononi akamuwekea picha aliyotembea nayo siku hiyo, ilikuwa ni picha ya kivuli cheusi. Moses akatokomea baada ya kukamilisha zoezi lake. Alijua sasa kilichobaki ni mke wa Raymond. Mwanamke aliyesababisha kifo cha mama yake, Bi furahiya.

    "Lazima nimuanze yeye ile huyu mshenzi ajue nipo siriazi"

    Moses hakufahamu kuwa hakumaliza kufuta kumbukumbu ya taswira yake ya uzee katika kichwa cha Mfaume. Akacheka sana kwa furaha alipokuwa akitazama taarifa ya habari akiwa ndani ya bar yenye mazingira machafu katika guest aliyolala huko kigogo mburahati. Taarifa iliyokuwa ikitangaza tukio la kuuwawa kwa kwa muhudumu wa nyumba ya kulala wageni na muuwaji akihusishwa katika matukio ya mauaji ya wasichana wawili.

    XXXXX



    Majira ya saa 3:15 asubuhi, ndipo Andrew kiongozi wa wahudumu wa apartment aliyoichukua Moses akakosa uvumilivu. Ilipita siku moja bila mtu yeyote kufungua mlango.

    "si mwanamke wake wala yeye mwenyewe" alikuwa Baraka, msaidizi wa Andrew. "kitu cha ajabu na kushangaza zaidi, kuna harufu kali inatokea chumbani"

    Haikuwa kawaida kwa Andrew kupoteza uvumilivu haraka kiasi hicho. Lakini kengele ya hatari ikagonga kichwani mwake. Kengele ya kuhisi kumetokea jambo ambalo si la kawaida. Akavunja masharti ya kazi yake.

    Kazi yake haikumruhusu kuingia ndani ya nyumba endapo kuna wateja. Labda kwa ruhusa maalumu au baada ya kutoka na kwenda kufanya usafi. Harufu kali ya uvundo, ikampa wasiwasi kila mfanyakazi wa apartment hiyo.

    Andrew alichukua ufunguo wa ziada, akatekenya kitasa nacho kikalegea. Harufu ikawapokea kwa kero na hali ya kutofahamu kitu gani kimetokea ndani ya nyumba hiyo. Andrew akifuatiwa na Baraka walienda moja kwa moja mpaka chumbani. Harufu ikawa nzito hata ikawafanya wazibe pua zao. Wakaingia ndani ya chumba hicho, taswira ya dimbwi dogo la damu lililoanza kukauka likataka kumkimbiza Baraka. Kutokana na kukosa uvumilivu, Baraka akaita Mama kwa sauti ya juu kama vile hakuimeza miaka thelathini na nne duniani. Kiwiliwili kilichogawanyishwa mikono na miguu yake iliyowekwa pembeni kikawaadhibu Andrew na Baraka kwa uoga. Jasho jingi likawatoka hakuna aliyemuongelesha mwenzake.

    "kichwa kiko wapi?"

    likawa swali la kwanza kwa Andrew tangu wafike katika chumba hicho. Baraka akaona michirizi ya damu iliyoelekea moja kwa moja mpaka kwenye friji ndogo ya chumba hicho. Yeye mwenyewe akalifungua alichokutana nacho, kikamfanya apoteze fahamu.

    Dakika chache baadaye Andrew ndiye aliwaita mapolisi baada ya kumtafuta kwa muda mrefu mmiliki wa apartment hiyo McCuthbert bila mafanikio. Simu zake zote ziliita bila kupokelewa. Polisi walikuja huku Inspekta Jafari Hiza akiwemo. Yakawa mauaji mengine ya kushitua zaidi. Tena huenda haya yalikuwa makubwa kuliko yaliyopita. Akampa taarifa rafiki yake wa karibu Vannesa. Kwa kuwa waandishi wengi walikuwepo, basi Vannesa akaendesha gari, hakika ulikuwa ni mwendo wa mwendawazimu. Dakika kumi tu zikamfikisha hapo.

    Wengi walimfahamu Vannesa na walizoea kumuona kwenye matukio makubwa, haswa kama hayo. Akaondokea kuwa mwandishi aliyejulikana na askari wengi kwa kazi ya uandishi bila kufahamu kuwa kulikuwa kuna kazi kubwa zaidi ya hiyo. Wakampa njia alipotaka kupita.

    Ushirikiano alipouhitaji.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Akaelekea moja kwa moja kwenye chumba kilichofanyika mauaji. inspekta Jafari Hiza akamkabidhi picha ya kivuli cheusi iliyokutwa ndani ya friji pamoja na kichwa

    "Unasema huyu nae amekatwa kichwa?"

    Vannesa alihamaki kwa mshangao wa hasira. Haikuwa kawaida kwa Vannesa kuwa katika hali hiyo. Ni nani ambaye hamjui Vannesa anayependa kucheka hata kwenye misiba? Basi leo Jafari Hiza alimshangaa.

    "Naomba kukiona kichwa cha huyo msichana"

    Akaletewa kichwa cha Eva. Sura ya Eva haikumpotea hata kidogo. Alikumbuka vyema alivyokuwa akimuhoji katika tukio lile la Bertha kijitonyama. Damu yake ikaanza kuchemka. Ilichemka kwa kuwa alifahamu kuwa muuaji anajua anachokifanya. Akaanza kuingiwa na hisia muuaji huyu labda si mtanzania kamili. Mtanzania aliyezaliwa Tanzania hawezi kuwa na akili za kuua kiakili kiasi hicho.

    Ushahidi wa kwanza ukawa umefutika bila kupata chochote cha maana kutoka kwake. Akamwambia Jafari

    "namfahamu huyu msichana aliyeuawa"

    "unamfahamu?"

    Inspekta hakufahamu kabisa kama huyo ni Eva. Jafari Hiza amekuwa msahulifu katika mambo mengi sana, ndio maana akauliza tena

    "ina maana tunaweza kumpata muuaji?"

    "kifo chake kinazidi kutupa ugumu wa kumpata muuaji"

    Vannesa akaondoka akiwa amechanganyikiwa. Kifo cha Eva kikazidi kumchanganya na kumfanya amchukie zaidi muuaji huyo. Akaelekea bar fulani aliyoipenda huko maeneo ya kinondoni. Alichoamini bila kuushitua ubongo wake kwa kinywaji kikali, basi asingekuwa sawa wala kupata chochote katika tafakuri zake.

    Akaingia ndani ya bar hiyo maarufu kwa watu maarufu na kama hukuwa nazo, basi usingeweza kumudu gharama za bar hiyo. Hivyo kwa sababu hiyo, ikafanya bar hiyo ya caribean kuwa na wateja wachache waliopata huduma za hadhi yao. Vannesa akajipachika pembezoni mwa ukuta huku akitazama orodha ya vinywaji

    XXXXX



    Baada ya kufanya mauaji ndani ya apartment ile, Moses alitoka na kuelekea upanga siku iliyofuata mara baada ya kutoka katika guest aliyopanga kama amekurupushwa. Huko alienda moja kwa moja kwenye nyumba aliyoishi McCuthbert. Mholanzi aliyemiliki apartment nyingi hapa mjini. Moses alifahamu fika endapo askari watakuja kumuhoji McCuthebert, basi angeharibu mipango yake. Mipango ya kulipaza kisasi kwa kumtaja kuhusika na mauaji hayo ndani ya apartment yake.

    Hakutaka hilo litokee.

    Ndio maana akausaliti urafiki walio nao kwa muda mrefu na kumpokonya uhai wake kwa sumu kali ya nyongo ya mamba. Alitokomea huku akiwa amebadilisha muonekano alioingia nao ndani ya ofisi ya bosi huyo wa kiholanzi.

    Alitafakari mengi juu ya Raymond kutokana na bugudha ya kelele kusumbua tafakuri zake, sehemu sahihi aliyoamua kwenda ikawa ni kinondoni katika bar ya Caribean. Aliupenda utulivu wa eneo lile pamoja na huduma zake. Alipofika huko akachagua sehemu pweke ambayo angekaa peke yake huku akitafakari jinsi ya kumuangamiza Raymond.

    Muhudumu akaifuata orodha ya vinywaji, huku akiwa amechagua mvinyo kutoka dodoma (dompo) leo hakuhitaji kabisa kulewa. Kabla hajafanya chochote wala ajamimina funda lolote kinywani mwake. Alihisi kusimamiwa mbele yake. Alipouinua uso wake kumtazama mtu huyo hakuwa mwingine zaidi ya Vannesa....

    XXXXX



    Kifo cha Bertha na muendelezo wa vifo vingine vya ghafla, vilimchanganya sana Raymond. Maswali mengi aliyojiuliza "ni vipi kifo cha Bertha kiungane na vifo vya hawa wengine?" taarifa za vifo hivyo alizipata kutoka kwa Inspekta Jafari Hiza.

    Yeye ndiye aliyempa taarifa za kifo cha Omary yule muhudumu wa nyumba ya kulala wageni, yule msichana muhudumu wa GQ pub na hata mmiliki wa apartment McCuthbert. Hao wote aliambiwa kuwa muuwaji ni mmoja na aliyemuua binti yake, Bertha. Raymond akawatafakari maadui zake wengi, kati ya wote aliyewaogopa alikwishawamaliza. Aliwamaliza wote kwa mkono wa kijana wake aliyemuamini sana. Kijana aliyependa kumuita simba. Jina la kijana huyu mwenye nguvu na aliyetokea kumuamini sana ni huyu huyu Moses.

    Akiwa katika tafakuri nzito huku machozi yakiwa karibu kumtoka, ndipo alipomkumbuka simba wake. Aliuhitaji ulinzi wake, aliamini akilindwa na yeye hakuna baya litakalompata. Alikumbuka vitisho alivyovipata kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kwake kama 'KIVULI CHEUSI' mtu huyo huyo ndiye anayeendeleza mauaji na kuacha picha yenye kuonesha ujumbe wa kivuli cheusi. Akapata tabasamu mara baada ya kutafakari juu ya kijana wake.

    Akajisemea "atapambana na simba"

    Aiinua simu yake ya kiganjani na kuanza kumtafuta Moses, kijana wake aliyemuita Simba. Alipoipiga simu ya Moses haikupatikana.

    "huyu mtoto kwa pombe!" kisha akacheka "nitamtafuta kesho nimkate pombe zake kwa supu ya kuku aipendayo huku tukizungumza biashara mpya"

    Wakati huo ulikuwa usiku wa saa 2:20, alipata chakula cha usiku pamoja na mkewe huku akimkumbusha jambo juu ya simba.

    "Yule anafaa mume wangu" Bi Furahiya akagongea nyundo juu ya msumari wa tafakuri ya Raymond. Kesho asubuhi bado Simba hakupatikana. Ndani ya wiki mbili na siku zote Simba hakupatikana.

    Akakata tamaa ya kumpata Simba.

    Raymond hakufahamu Simba ambaye ndiye Moses ndiye alikuwa akiisaka roho yake usiku na mchana. Ndiye kivuli cheusi aliyemuua Bertha. Alimfahamu Moses muda mrefu kutokana na urafiki wake pamoja na Carlos lakini hakumtilia manani, kupitia Bertha akaanza kufikiria kufanya naye kazi. Mwanzo alikuwa haupendi uhusiano wa Bertha na Moses, lakini baadaye aliuridhia. Alimpenda Moses kwa kuwa alionesha ukomavu wa misuli, nguvu pamoja na akili.

    Alishitushwa katika kifo cha Bertha kwa kuwa hakumuona Simba msibani. Hilo halikumtisha wala kumtia wasiwasi Raymond. Lakini kutokupatikana kwake siku zote alizomtafuta, zikamfanya ahisi huenda Simba alishauawa. kitu pekee alichokiweka kichwani mwake ni kuwa Simba ameshakufa. Akapoteza tumaini la kumkomoa KIVULI CHEUSI, Akapanga jipya la kufanya kulinda himaya yake.

    ******



    Asubuhi Vannesa alijikuta akiwa kitandani, ndani ya chumba cha hoteli juu ya kitanda chenye mashuka meupe pekee.

    "nipo wapi?"

    Alitazama kila kona ya chumba cha hoteli hiyo na kuona nguo za kiume.

    "Nimelala na mwanaume?"

    Jasho likamtoka, jasho la uoga. Akainua shuka zito jeupe alilojifunika nalo, alijikuta mtupu.

    "Mungu wangu nimetembea naye?"

    Alipokuwa akiendelea kujiuliza alisikia mtu akikohoa kutokea bafuni. Kiwiliwili kilichoongozwa na kifua kipana mbele kikajitokeza mbele yake. Alikuwa ni kijana mwenye mvuto usoni akiwa amepambwa na tabasamu. Alikuwa akimtazama kwa viulizo vingi lakini Moses alikuwa tayari kumjibu yote ambayo angemuuliza.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/-

    Moses akaendelea kujifuta taratibu na taulo zito la hoteli hiyo. Tabasamu bado likiwa usoni mwake, alimuuliza

    "Umeamkaje Vannesa?"

    Alinyanyuka na kumsogelea kitandani alipokaa.

    "Nimekuagizia supu ya kukata hangover uliyonayo"

    kitu pekee ambacho vannesa alimuuliza mara baada ya kupata sauti yake ni kuwa

    "Wewe ni nani?"

    Moses alicheka kwa kebehi akamwambia

    "Vannesa kazi yako ya uandishi wa habari ni mbaya sana" alichukua suruali akawa anavaa "kila kitu unahoji, jana tulikuwa wote kwenye ile bar ya caribean tulizungumza mengi unanishangaza yote niliyokujibu jana leo unaniuliza upya"

    Muhudumu wa hoteli aliileta huduma kama alivyoagizwa. Supu ya samaki sato na pilipili nyingi iliyochanganywa na ndimu. Vannesa alishangaa sana, alishangaa kwa kuwa supu hiyo ndiyo ilikuwa pendeleo lake kubwa alipokuwa akihisi uchovu mara baada ya kunywa kiasi kikubwa cha pombe. Akauliza tena

    "Umejuaje kama mimi ni mpenzi wa supu ya aina hii?" Tabasamu la Moses halikutosha kuwa jibu. Akamwambia "umeshanieleza yote jana tulipokuwa tunakunywa Caribean huna haja ya kurudia."

    Vannesa akajihoji kwa mashaka. "Nimekwisha mueleza yote? Yapi?" ukawa mtihani mkubwa kwa Vannesa kukumbuka vyote ambavyo alikwishaongea mbele ya Moses. Lakini ukweli ni kwamba, Vannesa hakumueleza lolote kuhusiana na uchunguzi wa mtu anayejiita kivuli cheusi.

    Moses alikaa chumbani hapo naye akizimua kwa pombe alizozikuta ndani ya friji dogo la hapo chumbani. Vannesa akavutiwa na huduma aliyoipata kutoka kwa Moses. Ni siku nyingi zimepita bila kuwa na mwanaume, hivyo alijihisi faraja kuwa karibu na Moses.

    Hivyo hivyo ikawa kwa Moses.

    Penzi alilopata usiku kutoka kwa Vannesa, likamrudisha katika kumbukumbu zake na Bertha. Wakiwa wanatazamana kwa muda mrefu bila huyu kumuongelesha mwenzake na huyu akiendelea kumtazama tu mwenzake bila kuzungumza chochote, ukafika wakati ambao kila mmoja akamuhitaji mwenzake tena. Vannesa akaliweka pembeni bakuli la supu na kumkaribia Moses.

    Hakika Vannesa alikuwa ni mtundu aliyefuzu michezo ya mapenzi. Akampagawisha tena Moses kwa kumlamba masikio, mabusu motomoto ya mdomoni na kila sehemu. Moses akaapa kumpenda Vannesa milele. Wakatoka kwenye kochi na kumtupia Vannesa juu ya kitanda, kitanda nacho kikawapokea kwa bembelezo mathubuti. Walitumia muda mwingi kushikana hapa na pale mpaka kila mmoja aliporidhika kumridhisha mwenzake.

    Simu ya kiganjani ya Vannesa ikapata uhai. Juu ya kioo jina la mpigaji alikuwa Jafari Hiza kama alivyomuhifadhi katika kitabu cha namba zake za simu. Alimuacha Moses kitandani na kuelekea bafuni kuzungumza na simu hiyo. Wasiwasi ukiwa juu ya tafakuri za Moses. Tangu aanze kazi hii ya mauaji akiwa peke yake, hakukiamini hata kivuli chake mwenyewe. Hivyo hakutaka aharibu mipango yake kwa uzembe kidogo. Alinyanyuka mpaka karibu na mlango wa bafu kusikiliza maongezi ya simu aliyoipokea Vannesa.



    *&****



    Kwa muda mrefu InspektaJafari Hiza alivutiwa na Vannesa. Alishindwa kumueleza ukweli kwa kuwa hakujua pendeleo halisi la Vannesa. Alikaa nae kwa muda mrefu tangu kisa cha NENDA NA MOYO WANGU, mpaka kisa hiki cha muuaji anayejiita Kivuli cheusi.

    Moyo wake ulisumbuka alipoliona tabasamu la Vannesa mara kwa mara. Kila alipotamani kuweka hoja yake mezani, mdomo ulikuwa mzito. Kuna wakati aliishia kumsifia tu na kumtamani zaidi. Ila usiku wa leo alichoka kuvumilia. Ulikuwa ni usiku mrefu sana kwa Inspekta Jafari Hiza. Aliota ndoto nyingi nzuri kuhusu Vannesa. Lakini hii iliyomkatisha usingizi majira ya saa 3:15 asubuhi, ilikuwa ni mbaya sana.

    Ilikuwa ndoto ambayo inamuonesha Vannesa akiwa njiani kisha vumbi fulani lililokuja mithili ya kisuli suli likammeza. Vumbi hilo likiwa limejigeuza mithili ya nyoka mkubwa mweusi.

    Ndoto hiyo ndiyo iliyomfanya aipige simu ya Vannesa asubuhi asubuhi. Maongezi yao yakawa yanasikika na mtu wa tatu. Mtu ambaye hawalali usiku na mchana wakimtafuta. Mtu ambaye anawaumiza kichwa na kujiita kivuli cheusi.

    "Habari yako Vannesa?"

    sauti ya Vannesa ikawa ya kichovu "Kwanini asubuhi asubuhi" aliongea kana kwamba kuna kitu alichokuwa akihofia. Akaendelea "Kuna tukio? Ameuua tena?" wakati huo Moses hakuwa bado hajasikia chochote. Alipokuja kusikia ni wakati ambao maongezi yalikuwa yamefika tamati. Neno la mwisho alilolisikia ni sauti ya kuhamanika iliyomtoka Vannesa.

    "Nipo kwenye hatari!?" sauti ilikuwa imeweka pozi kwa muda "Nitakuwa mwangalifu usijali Jafari"

    Jafari Hiza aliikata simu kisha akaibusu huku tabasamu likiwa kwenye papi zake. Akajisemea kwa sauti ya chini "Nakupenda sana Vannesa, leo jioni nitakueleza kiasi gani nakupenda"

    akajinyanyua kitandani na kuelekea nje kusafisha kinywa.

    *****

    Vannesa alipotoka bafuni baada ya mazungumzo hayo, alimkuta Moses akivuta sigara. Moses alijua kuigiza haswa. Akaizima sigara yake na kumpa kumbatio la haja Vannesa. Vannesa akalihisi joto la kimahaba kutoka kwenye kifua cha Moses. Vannesa akaonesha kumuhitaji tena Moses, lakini Moses aliuhitaji upweke. Upweke ambao ungempa fursa ya kutafakari njama zake juu ya kumuangamiza Raymond. Alimsihi Vannesa "Nisikilize tafadhali" penzi la Moses likamchanganya sana Vannesa. Hakusikia chochote alichoambiwa zaidi ya kuhema zaidi kimahaba na kuonesha uhitaji wa penzi la Moses tena kwa mara ya tatu. Moses akajaribu kumzuia Vannesa "Mpenzi sikia kwanza" Vannesa alipoonesha utulivu, Moses akazungumza

    "Huu ni wakati wa mimi kuelekea ofisini, tafadhali tukutane jioni bado nakuhitaji pia zaidi."

    Vannesa akaonesha kumuelewa zaidi Moses. Baada ya kujiandaa kwa pamoja na kila mmoja kuchukua bajaji moja na Waliachana maeneo ya posta ambapo Vannesa alihamishia ofisi yake hapo.

    Moses akaelekea katika hoteli ya new afrika jirani na ofisi ya Vannesa. Hakujua kwa nini aliamua akae jirani na ofisi hiyo. Aliagiza mvinyo mtamu wa st anna. Akainywa taratibu huku akipasha joto mapafu yake kwa sigara kubwa. Tafakuri zake zikazama katika mauhusiano ya ghafla aliyoyaanzisha na Vannesa. Msichana aliye na kila dalili za upelelezi.

    "Nipo kwenye hatari?" akaikumbuka sauti ya Vannesa akizungumza na mtu asiyemfahamu akiwa bafuni.

    Aliyatafakari mazungumzo hayo kwa muda ndipo akapata jibu kwanini ameamua kuja kukaa new afrika karibu na ofisi ya Vannesa. Mazungumzo hayo ndio sababu ya kutaka kumfuatilia kwa ukaribu Vannesa na kutaka kufahamu nini anachokificha Vannesa katika maisha yake halisi. Akapiga funda moja la kinywaji chake.

    Kisha akatabasamu. Alitabasamu mara baada ya kuyapinga mawazo yake. Mawazo aliyoyatamka kwa sauti iliyosikika "Vannesa hafai kufa mapema. Nahitaji kumjua zaidi"

    Ofisini, mawazo ya Vannesa yalikuwa juu ya Moses. Yeye alikuwa ni msichana ambaye aliogopwa na wengi. Wengi waliomtamani Vannesa waliogopa kumueleza hisia zao. Kazi yake ikamfanya kujitenga na mapenzi. Mapenzi yakamchukia na kumkinaisha kwa kuwa alikuwa busy na kazi. Hata alipokuwa akiwaza kuhusu Moses, bado ungedhani alikuwa akitafakari jinsi ya kumkamata muuaji.

    Alipotabasamu ndipo aligundua kuwa hayupo peke yake katika chumba cha ofisi aliyopo. Kicheko kikubwa ndicho kilimshitua na kumfanya apoteze furaha yake. Alipotazama mbele ya meza yake ya mstatili, alimuona Naima akiwa anapasuka kwa kucheka yeye pia akacheka kwa tuo kana kwamba hakutaka kucheka.

    Naima alizungumza huku bado kicheko kikiwa kimembana. "Dada Vannesa" alishakatazwa kumuita bosi. Vannesa alipenda kuishi na Naima kama mdogo wake wa kuzaliwa na mama mmoja. Naima akaendelea kuuliza "vipi mbona umesahau hata kunisalimia? Tabasamu halijabanduka usoni mwako tangu uingie ofisini leo" Ilikuwa ni hali ya kushangaza lakini fikra juu ya Moses ndizo zilimchanua na kuwa mng'avu. Hakuacha kutabasamu hata alipoambiwa hivyo.

    "Niambie basi kama umeshakikamata Kivuli cheusi na mimi nifurahi?"

    Naima alijikaribisha katika kiti kilichopo mbele ya meza hiyo. Neno kivuli cheusi, likabadilisha kabisa taswira ya Vannesa. Taswira iliyojizaa upya ni ile ya hasira. Mistari fulani juu ya paji la uso ikajitutumua na kufanya uwe uso unaochukiza.

    Hakucheka tena.

    Naima akalifahamu hilo vannesa alipozungumza

    "umenikumbusha jambo"

    Naima naye aliacha kucheka, akaingiwa na shahuku ya kufahamu.

    "Jambo lipi?"

    "Huyu mshenzi amemuua shahidi mkubwa wa kesi hii"

    "Mungu wangu" Naima akaishika midomo yake kwa kustaajabu, akauliza "ina maana yule Eva amekufa?"

    "Ndiye huyo"

    Vannesa alinyanyuka na kutaka kuondoka. Naima naye alinyanyuka "kwa hiyo umepanga kufanya nini?"

    "Naelekea kwenye eneo lake la kazi, pale sitakosa pa kuanzia" vannesa pamoja na Naima wakiwa nje ya ofisi, Vannesa akamalizia "Nitaenda pia katika apartment ambayo huyu msichana ameuawa, niliziona kamera katika nyumba ile, hivyo nitapata chochote kutoka hapo pia"

    Naima akastaajabu ufanyaji kazi wa Vannesa. Kifua chake kikapanda na kushuka kwa kuwa ni jambo lilohitaji umakini sana kugundua kamera ndogo ndogo zilizofichwa ndani ya nyumba ile. Ufuatiliaji wa kesi kama hiyo ukahitaji Pia ujasiri na hekima ya kumfahamu muuaji.

    Vannesa na Naima wakaagana mara baada ya Vannesa kutekenya ufunguo wa gari na kuligeuza kuelekea kijitonyama. Mwendo ulikuwa wa wastani huku akiendelea kutafakari namna ya kumkamata muuaji huyo. Muuaji aliyemkosesha usingizi. Mauaji yake yalimfanya aone kuwa muuaji huyo alifahamu alichokuwa akikifanya. Alimuona muuaji kama mtu mwenye akili za ziada na aliyehisi kufuatiliwa kwa ukaribu.

    Akiwa amekipita kituo cha mwenge akaendelea kutafakari huenda pia kuna anayehusika katika jeshi la polisi

    "Ndio" akajinong'oneza "iweje aweze kuua mashahidi ambao wataniwezesha kumpata muuaji?"

    akaanza kuuondoa uaminifu kwa jeshi la polisi. Akatafakari mishahara midogo wanayoipokea inaweza ikawafanya kupokea rushwa za kuwarubuni na wao wakazitoa siri zote. Akaendelea kuamini kuwa ni mmoja kati ya mapolisi hao anamfahamu muuaji na kutoa siri zote. 'eva amekwisha uawa. Omary pia ameuawa' hapo akamkumbuka pia na mfaume.

    Akaiegesha gari yake pembezoni mwa pub ya GQ, kuna gari aina ya IST nayo ikaegeshwa mbali kidogo.

    Vannesa alikwishaiona.

    Alihisi muda mrefu ikimfuatilia sasa hakujitia tena uzembe naye akataka kuanza kumfuatilia yeye anayemfuatilia. Akaingia ndani ya pub ya GQ na kuelekea moja kwa moja kaunta. Akapokelewa kwa tabasamu na msichana aliyenyuma ya nondo za kaunta hiyo.

    "Naitwa Vannesa"CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Nakukumbuka Afande" alijibu haraka haraka yule msichana "nikupe nini" Vannesa hakupenda kuitwa Afande ndio maana akatabasamu kwa hasira. Akampinga kabla hajaagiza sprite.

    "Mimi sio afande ila nahitaji kufahamu jambo"

    "Jambo lipi hilo dada Vannesa?"

    Msichana yule wa kaunta aliitwa Zainabu. Vannesa akaieleza shida yake juu ya kumtambua muuaji wa Eva. Zainabu alionesha kuna jambo alikuwa akilifahamu, akamueleza Vannesa yote kuhusu Moses wa kikongo aliyezungumza lafudhi ya kifaransa. Alieleza jinsi alivyo, hata kuahidi kumfahamu endapo angemuona mara ya pili.

    Zainabu akawa ametimiza furaha ya Vannesa na kumfanya kuondoka. Gari ya Vannesa ilipokuwa ikiipita gari ambayo alihisi ilikuwa ikimfuatilia, alimshuhudia mvulana akibadilishana mate na msichana fulani mwenye asili ya kiarabu. Akairudisha barabarani gari yake na kurudi Masaki kwenye apartment ya McCuthbert.

    Huko alifuata mkanda wa video uliorekodi matukio yote ya mgeni aliyeingia ndani ya nyumba hiyo. Japo dhumuni la kamera hizo, zilikuwa kupiga picha za watu ambao walitaka kufanya uhalifu kwa wageni watakaolala ndani ya nyumba hiyo. Vannesa akaiendesha gari yake kwa uangalifu zaidi. Alifuatilia kuitazama gari ile aliyoiacha pale Gq, haikuwepo.

    Wasiwasi huo ukamshitua kuitazama kila gari na chombo cha usafiri. Ndipo vinyweleo vikamsimama alipohisi bajaji iliyokuwa ikimfuatilia kwa muda mrefu, ikiambatana naye kila alipokuwa anaenda mara alipokiacha kituo cha bamaga sheli.

    Hata alipofika jirani na apartment aliyokuwa anaifuata, hakushuka. Aliichunguza bajaji ile ilipokuwa inaelekea. Haikusimama kama alivyotarajia. Bajaji ile iliendeshwa na mzee wa makamo aliyesahau matumizi ya kiwembe juu ya kidevu chake. Bajaji ikampita pale pale na kutokomea.

    Vannesa alishuka na kuiendea apartment ile. Ikawa rahisi kwa kuwa alikutana na mke wa McCuthbert, alifahamiana naye siku ya msiba wa mumewe. Akaieleza shida yake na hakukuwa na kikwazo. Kwa kutumia kompyuta ya mapajani, walizitoa cd ndani ya kamera zile na kuzichomeka kwenye deki ya kompyuta. Picha iliyoonekana ndani ya cd ile ikamfanya Vannesa kuhamaki. Hasira zikampanda na kumfanya aropoke

    "Haiwezekani"CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog