Search This Blog

Sunday, 19 June 2022

MJI TULIVU ULIONIPA UGONJWA WA MILELE - 5

 





    Simulizi : Mji Tulivu Ulionipa Ugonjwa Wa Milele

    Sehemu Ya Tano (5)





    Kadri safari ilivyokuwa ndefu nikaanza kugundua jambo jingine lisilokuwa la kawaida hata kidogo.

    Hapakuwa na safari ya kuelekea hospitali, tulikuwa tunaelekea mahali nisipopajua kabisa.

    Kwanini tuelekee huku!

    “Mariam Sumra! Ni wapi tunaelekea?” nilimuuliza.

    “Mbembeleze mtoto Joshua…. Acha upuuzi.” Alinijibu.

    Nadhani jibu lake lilizua kimya ambacho hata Agness mtoto wangu alikigundua, akanyamaza kimya ghafla!

    Hali ilikuwa tete!!

    _____
    KAMA nilivyohisi kuwa hakuna safari ya hospitali ilikuwa hivyo, hatukwenda hospitali badala yake gari lilisimama mbele ya nyumba fulani ya kifahari. Honi ikapigwa na geti likafunguliwa…

    Gari lilipoingia tu, Nyambura akajigeuza.

    Mariam Sumra akachukua maji na kumwagia, fahamu zikarejea akiwa anapepesa macho huku na kule.

    “Mtoto wangu yupo wapi?” akaulizia, lakini kabla sijamjibu tayari Aggy alisikia sauti ya mama yake akaanza upya kulia.

    Nyambura akamchukua na kumpa alichohitaji.

    Titi akanyonya!

    “Nyambura hili jambo linatakiwa kumalizika sasa!” Mariam alimsihi.

    “Asante kwa kuja katika maisha yangu kwa wakati sahihi dada Mariam. Nadhani machache umejionea na kuyasikia..” alizungumza huku akimlaza Aggy ambaye tayari usingizi ulikuwa umempitia.

    Wakati huo tulikuwa katika sebule iliyosheheni samani za kutosha.

    “Umemsikia vizuri Joshua ambaye hadi sasa anamlilia mama yake na kukonda kwa sababu yake… Joshua mbinafsi asiyebadilika tabia yake.” Alizungumza tena kwa sauti ya chini akiwa anatazama dari.

    “Dada Mariam, aliyekutuma uje katika maisha yangu awali nilimchukia lakini sasa natamani kumuona najisikia kwa mbali naanza kuwa mwanamke!” aliweka kituo na kunitazama. Hapo sielewi lolote lile.

    “Nafsi yangu haitachoka kukiri kuwa ninampenda sana mume wangu na baba halali wa mtoto wangu wa pekee Agness.” Akakohoa kidogo na kuendelea, “Lakini bila ujio wako dada Mariam nisingejali kama ninampenda ama la. Alichotakiwa kupata alistahili….. nadhani nilikwambia kuwa mambo mengine sitakueleza wewe pekee bali nitakueleza siku moja mbele ya mume wangu na siku hii ni leo.”

    Nikaketi vizuri kusikiliza hukumu niliyotaka kusomewa ambayo ingenipa mwangaza wa haya niliyokuwa napitia.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ni tarehe kama ya leo, tarehe ambayo ilinifanya nianze kumchukia Joshua….. hii tarehe mama yangu mzazi aliaga dunia. Sitabadili msimamo wangu kuwa aliyemuua mama yangu ni Joshua ambaye sasa ni mume wangu…” akasita na kunitazama nami nikamtazama nikiwa na viulizo vingi.

    “Nimekuwa jasiri sasa, na nimekubaliana na matokeo, Joshua wewe haukuwa wa kuninyima mimi nauli pekee ya kwenda kumzika mama yangu, ukaacha mama yangu azikwe na manispaa ya mji wa Musoma. Sidhani kama ungejisikia ahueni ama ungekuwa na moyo wa kusamehe kama ungetendwa hivi! Ni kweli unaweza kujitetea kuwa ulikuwa hunifahamu, lakini ni mara mbili nimekujia nikiuweka wazi moyo wangu kwako ili unisaidie… haukunifaa kitu”

    “Mama yangu aliniuma sana Joshua, niliumia sana kwa sababu niling’atwa mbu sana usiku ule sikumwambia yeyote shida yangu bali wewe. Sijui hata ulinionaje…. Mimi sikuwa najirahisisha kwako na nilikueleza vile nafsi yangu imenituma. Badala yake ukanisaliti na kuniacha niingie katika janga baya kabisa, janga la kuuza mwili wangu ili nipate kula, nikapoteza vyeti vyangu katika namna nisiyoelewa…. Ulivyo mtu wa kupuuzia mambo yasiyokuhusu haukujali kuona ninaitwa Neema! Haukujali kuniona nikiwa bikira angali nina umri mkubwa na nimepitia mengi, ukajidanganya kwa faida yako mwenyewe.

    Jitazame ulivyokonda sasa, jitazame ulivyoaibika katika lolote ulilopitia. Unadhani nayafurahia haya Joshua, sifurahii hata kidogo lakini nataka upate somo katika maisha yako kuwa ni heri utende wema na uliyemtendea akupuuze kuliko kuacha kabisa.

    “Mariam Sumra, kama hajajitambulisha kwako huyu ni mke wa mwanasheria wako. Hujui lolote hata kuhusu watu wako wa karibu, unajijali wewe tu Joshua. Kama mke wa rafiki yako humjui ni mangapi haujali kuhusu wanadamu wenzako?

    Nd’o maana hata siku ile haukujali yule rafiki yangu ambaye ni changudoa alipogongwa na gari.. ukasema huyu ni changudoa acha tu afe!

    Kwa sababu changudoa hana damu sio?

    Mariam Sumra ameagizwa na mumewe kwa ajili yako, huyu ni mwanasaikolojia… na hakika bila huyu sidhani kama ningehairisha nilichohitaji kufanya. Ametumia ushawishi mkubwa sana kunifanya nighairi kile ambacho nilitaka kufanya juu yako ili nihakikishe moyo wako unatoboka matundu mengi kama ulivyokuwa wangu

    Ulikuwa haujateseka inavyofaa Joshua, haujateseka walau nusu ya nilivyopanga tangu siku ile nilipoivaa pete kidoleni kuwa wewe ni mume wangu. Haukuwa mume wangu bali adui uliyekubali kuishi karibu na mimi nitimize matakwa yangu.

    Hauna tatizo la kizazi na haujawahi kuwa nalo, hakuna mganga hata mmoja hapa ila ni faraja yangu kuwa umelala makaburini na kupelekeshwa inavyotakiwa. Japokuwa huo ulikuwa ni mwanzo tu.

    Joshua! Mimi nilibadilika na kuwa kiumbe wa ajabu sana kuanzia pale niliposhuhudia wadogo zangu wawili wakinusurika kufa kwa njaa.

    Na wakati huohuo unajisifu kwangu kuwa umetoka familia ya kimaskini na ulipata tu msaada kutoka kwa watu wema ukasomeshwa na kuikomboa familia yako.

    Leo hii kusaidia wenzako unadhani ni mojawapo kati ya mitihani migumu kabisa.”

    Akasita kisha akamtazama Mariam Sumra.

    “Da’ Mariam hebu imagine, licha ya yote haya lakini… lakini… hebu tufanye mfano wewe Mariam utajisikiaje mume wako akiwa anafanya mambo pasipo kukushirikisha?”

    “Nitajisikia vibaya na sina umuhimu kwake!” alijibu Sumra.

    “Sasa Joshua ambaye mimi na yeye ni wamiliki wa kampuni, akafanya hila na kutaka kuuza hisa zake karibuni tisini bila kunishirikisha, huyu ni mwanaume kweli? Eeh! Ni mwanaume ambaye unanishauri kila siku kuwa nimsamehe kwa sababu yeye ni mwanadamu??” alifoka Nyambura kiasi cha kuanza kutetemeka. Hapa sasa nilijikaza na kuzungumza.

    “Nyambura… ina maana,aah! Ina maana hujui kuhusu hawa wanaume….niliokuwanao pale benki?”

    Akanikata jicho la chuki huku akiwa bado anatetemeka.

    “Ningewajua ningekuvizia benki kukupokonya hii bahasha, huna huruma wewe mwanaume, una mtoto mdogo unauza hisa kimyakimya una mpango wa kunikimbia ama?” alinihoji, sasa alikuwa amesimama wima mbele yangu.

    Nyambura alikuwa ameiva kwa hasira na alikuwa ananitisha mno. Hapo sasa nikakiri kuwa wanawake wa kutoka mkoa wa Mara sio wa mchezo hata kidogo.

    “Nyambura mke wangu..” nilipotamka vile sikuweza kumaliza kabla hajaninasa kibao kikali usoni na kisha akaanza kulia huku mimi naugulia maumivu.

    “Unaendelea kuwa mwongo na mnafiki mkubwa katika ndoa yetu, unaendelea kuutoboa moyo wangu Joshua, kwa nini lakini? Maria Sumra ungeniacha, ungeniacha usingenizuia!” alilalama zaidi.

    “Nyambura nisikilize kwa sekunde tafadhali..” nilimsihi na sikusubiri jibu lake.

    Sasa kama ni uchi tayari nilikuwa uchi nimevuliwa nguo zote. Sikuona haja ya kufichaficha lolote lile.

    Nikamueleza Nyambura pamoja na Mariam Sumra juu ya maagizo kutoka kwa mizimu!

    Nikawaeleza juu ya masharti yao kuwa nikipata mtoto wanahitaji zawadi, na zawadi waliyoichagua ni kampuni yangu na pesa yote ya akiba iliyomo.

    “Nyambura! Nilishindwa hata kukusaidia kila kiasi cha pesa kwa sababu hiyo mizimu ilinikataza mke wangu, hapa nina madeni kila kona kwa sababu sina chanzo cha pesa. Na pale tulikuwa katika makabidhiano kwa sababu wamemshikilia mama yangu mzazi.” Nikaishia pale na kumsubiri Nyambura aseme neno.

    Si Nyambura peke yake bali hata Mariam Sumra hili jambo la mizimu kuhitaji pesa zote katika kampuni lilikuwa geni kabisa. Nyambura akaanza kuhaha akiniuliza maswali ya kizembe ambayo majibu yalikuwa wazi tayari.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Milioni mia moja sabini? Mungu wangu! Wanataka kuniwekea dhambi ya kudumu hawa watu…. Nooo! Hayakuwa maelewano haya hata kidogo… na hapo kabla wamechukua pesa ama?” alinitupia swali.

    “Ndio nilitoa kama milioni zisizopungua nne kwa ajili ya shukrani….”

    “Uuuuwi! Mungu wangu, pesa pekee niliyoichukua kwako ni ile ya daktari tu pale hospitali… na ipo ndani hadi leo. Mimi sio tapeli Joshua….. what’s going on sasa… mbona wameingiza tamaa katika jambo lisilowahusu!” aliendelea kubabaika.

    Akaichukua simu yake akapiga namba ambazo alizijua yeye.

    Sisi tukabaki kimya kabisa.

    Kwa kimya kile tuliweza kuisikia simu hata ilivyopokelewa.

    Aliyepokea simu alikuwa ni mwanaume, lakini zaidi ya kusema ‘halo’ hakusema neno jingine la ziada.

    Ikasikika sauti ya mwanamke.

    “Mama Agness wapeni wanachokitaka hawa watu… wataniua!” ilikuwa ni sauti ya mama yangu mzazi.

    Tumbo la kuhara likanishika!

    Awali ulikuwa mchezo wa kuigiza ila sasa kila mmoja aliitambua kuwa ni vita rasmi.

    Kama mchezo wa kuigiza ulinigalagaza huku na kule nikabaki hoi, vipi kuhusu hii vita kamili?

    Niliulizia choo kilipo, nikatimua mbio nisije kuzua balaa!

    Huku nyuma Agness akashtuka usingizini na kuanza kutokwa na kilio...


    *************


    BAADA ya kutoka maliwatoni kujistiri maumivu yangu ya tumbo nilirejea sebuleni pale nilipowaacha Mariam Sumra mke wa mwanasheria wangu pamoja na Nyambura mke wangu.

    Nyambura alikuwa anaongea vitu visivyoeleweka. Alikuwa amepagawa zaidi….

    Simu ikapigwa tena na safarihii aliipokea Mariam Sumra. Alizungumza kwa takribani dakika sita hivi kabla hajakata simu na kutugeukia.

    “Inatakiwa bahasha yenye dola!” alitamka akinitazama mimi kisha akamgeukia Nyambura.

    “Noo! Hatutawapatia….” Alipiga kelele Nyambura.

    “Nyambura, wamemshikilia mama yenu… huyo ndiye mama pekee mliyebakiwa naye hamna mwanamke mwingine wa kumuita mama. Nyambura sahau kabisa kuhusu mafarakano yako na mumeo, fikiria kuhusu mama aliyekuwa nawqe bega kwa bega katika uzazi wako.” Mariam Sumra sasa alizungumza akimkazia macho Nyambura.

    Maneno yale yalimyumbisha sana Nyambura, akaonekana kutamani kusema kitu lakini hakuweza kusema, bila shaka alikuwa akitamani nyakati zitupatie maajabu kwa kurejea nyuma ili asifanye yote aliyoyafanya? Ama labda ili asikubali kuolewa na mimi? Ama labda asikubali kuusema ukweli ulivyo!

    Sikujua anawaza nini.

    “Tutawapatia bahasha wanayohitaji.” Hatimaye na mimi nilizungumza.

    Nyambura akanitazama huku akinionea haya, akanisogelea na kunikumbatia.

    “Yuda msaliti!” nilijisemea kimoyomoyo huku nikimtazama mwanamama huyu kama shetani!

    Lakini sikudumu katika fikra za kumtazama kama shetani kwa sababu ndiye mwanamke pekee aliyenizalia mtoto.

    Mtoto wangu hajazaliwa na shetani! Nilijirekebisha.

    “Nisamehe Joshua wangu, sijawahi kupanga hata siku moja iwe hivi. Hata kama ningekuwa na kisasi kikubwa zaidi kwako lakini sio kufikia hatua ya utapeli wa aina hii. Nimesalitiwa Joshua….” Alizungumza huku nikiyahisi machozi yakichuruzika na kunilowanisha.

    “Niwapigie simu kuwa tunaipeleka bahasha?” aliuliza Mariam huku akiwa tayari na simu mkononi.

    “Naomba nizungumze nao..” aliomba Nyambura lakini Mariam alidai kuwa huu haukuwa muda wa mazungumzo bali vitendo.

    Nikamweleza kuwa awaambie kuwa tunawapelekea bahasha kama ilivyo.

    Akanyanyua simu na kuwapigia, wakatoa maelekezo yao. Wakahitaji niende peke yangu, na kwa namna yoyote ile Nyambura asionekane kuwa karibu na eneo la tukio.

    Walitoa vitisho zaidi kuwa nikithubutu kuleta ujanja wowote ule basi nijiandae kumsafirisha mama yangu kwenda kijijini akiwa katika jeneza.

    Kitisho hiki kiliniingia zaidi!

    Nikakubalianana Mariam abaki na Nyambura pamoja na mtoto na mimi niende kuwapa ile bahasha yao wanipatie mama yangu!

    Makutano haya tulikubaliana yafanyike Morogoro, ni huko nitapewa mama yangu na kuondoka naye salama kabisa.

    Nilitoweka siku iliyofuata nikambusu Aggy katika paji la uso na mama yake nikambusu shavuni, nikamsihi Nyambura awe mtulivu kabisa kila kitu kitaenda sawa na asifanye lolote baya kwa sababu yupo Agy asiyejua nani mbaya kati ya baba na mama anatutegemea wote kama wazazi wake.
    _______
    MOROGORO, Tanzania
    Nilipokelewa katika kituo cha mabasi ukiwa ni kama ugeni wa kawaida kabisa. Nilishangaa watu hawa walikuwa wanajiamini kiasi gani kuwa siwezi kuambatana na askari katika safari yangu.

    Walikuwa wanaojiamini mno. Walinichukua katika taksi yao, safari ikaanza, tulipita kona kona kadhaa kwa zaiddi ya dakika ishirini kabla hatujaingia katika hoteli yenye hadhi ya wastani palepale Morogoro lakini sikuwa naifahamu mitaa tuliyokuwa.

    Niliingizwa katika chumba kimoja, na kwa mara nyingine tena nikakutana na wale wavaa suti wenye lafudhi ya kikongo.

    Walinitazama kwa jicho la chuki kali.

    Na walipoanza kuzungumza nilibaki kustaajabu.

    Walikuwa wanaongea Kiswahili safi kabisa na sio kile kibovu chenye mahadhi ya kongo.

    Duh! Nilibaki kuduwaa, kumbe walikuwa wanaichezea akili yang utu muda wote ule.
    Wakaiomba bahasha, nami nikaweka ngumu nikasema ninamuomba mama yangu.

    Mvaa suti mmoja akasimama na kunirushia kibao, nikawahi kutega mkono nikawa nimekipangua.

    Hawa watu vipi? Nilijiuliza.

    Nilichohitaji nikaletewa.

    Kweli walikuwa wanamshikilia mama yangu mzazi, hawakuwa wamemdhuru hata kidogo lakini alikuwa na hofu kuu, nadhani kuna vitisho walikuwa wamempatia.

    Nilipomuona mama yangu nikawa tayari kuitoa bahasha, nikawakabidhi wakaifungua na kuzihesabu dola zile zilizokuwa katika mafungu mafungu.

    Nyuso zao zikang’ara kwa matabasamu mazito.

    Hapo sasa wakaanza kuzungumza maneno mabaya sana juu ya Nyambura, wakasema mengi ya kutisha, kama ni siasa basi walikuwa wamemchafua kiasi cha kukosa hadhi ya kupigiwa kura hata moja.

    Yote haya sikujali japokuwa waliyasema mbele ya mama yangu.

    Walipomaliza kuhesabu na kuhakikishakuwa sio feki, wakaturuhusu kuondoka kwa amani huku wakitusihi kuwa wao sio mashetani bali mke wangu ndiye shetani mkubwa.

    Wakati nataka kuondoka wakahesabu noti mbili za dola mia moja na kunipatia wakidai ni nauli.
    Tulishuka ngazi nikiwa nimekabwa na kitu kooni ambacho nilijua nikikiruhusu kitoweke basi niwe tayari kuangua kilio.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Tuliondoka pale mapokezi tukipishana na watu kadhaa ambao sikuwatilia maanani bali nilikuwa makini kuzishusha ngazi nisije nikaporomoka.

    Tulipofika nje niliinama ukutani, jasho likinitoka nikaanza kulia sana. Nililia mama akawa ananibembeleza kuwa niwe mwanaume upya!

    Alisema mengi ya kunipa nguvu lakini moyoni nilikuwa nimekufa ganzi.

    “Nyambura siso shetani kama walivyomuita wao, Nyambura amefanywa kuwa shetani. Nani aliyemfanya kuwa shetani hili ni swali wapaswa kujiuliza…” akasita na kunitazama huku akinifuta machozi.

    “Hata wewe kwa sasa unaelekea kuwa shetani, usijiruhusu hata kidogo kufika huko. Humchukua mwanadamu dakika chache sana kuwa shetani na kisha akadumu katika ushetani na asiweze kubadilika kamwe.”

    Maneno ya mama yakanipatia jibu kulingana nay ale maelezo ya Nyambura awali, ni mimi nilimfanya yeye kuwa shetani. Nilijaribu kufikiria ni namna gani nitaweza kuishi na mwanamke aliyenifanyia haya yote….

    Nikakosa kujiamini kabisa.

    Nisingeweza kulala kitanda kimoja na Nyambura.

    Siku hiyohiyo tulisafiri na mama kurejea jijini Dar es salaam. Mji ambao sikujua utanipokea vipi hasahasa kuonana ana kwa ana na Nyambura mke wangu.

    Masaa manne yakapita na hatimaye nilikuwa pamoja na mama tukiufungua mlango wa kuingilia nyumbani kwangu.

    Kimya kilikuwa kikubwa sana……

    Hatua ya kwanza tu kuingia sebuleni, kuna mwili ulikuwa umejilaza hovyo kabisa.

    Kidevu kikijibwaga katika meza ya kioo, huku akiwa amepiga magoti!

    Nini hiki? Nilijiuliza, mama yeye alishtuka na kupiga kelele.

    Licha ya kelele hizo bado mwili ule haukutikisika.

    Sura yake ni mimi pekee niliyeweza kuifahamu, mama hakuifahamu kabisa.

    Mariam Sumra!

    Tulihaha huku na kule kumtafuta Nyambura na mtoto lakini hatukuziona dalili zozote zile.

    Hapa sasa hofu kuu ikatanda.

    Ni kitu gani kimetokea?? Hili likibaki kuwa swali kuu….

    Mariam Sumra akaendelea kusujudu pale sakafuni na kidevu kikijibwaga mezani!


    ************


    NUKUU

    MKE/MUME ni kitu kingine. Awali unapoingia katika mahusiano ya kimapenzi mwenzi wako anakuwa kama mtu wa ziada kwako ambaye hata akikumbwa na jambo inakuwa mbali na wewe, baada ya muda mnaanza kufanana mitazamo, na hapo unajihisi huwezi kufanya lolote la maana bila yeye… unaamua kuingia katika ndoa. Damu zinakutana na mnakuwa mwili mmoja.

    Mwenza wako anageuka kuwa ndugu yako wa karibu zaidi wa kila siku……

    Ukifika wakati huu, waweza kufanya lolote kwa ajili yake.

    Umewahi kusikia watu wanakuwa vichaa kwa sababu ya mapenzi? Umewahi kusikia wanaojinyonga kwa sababu ya mapenzi?

    Haya yote hutokea wakati mwili wako umeungana na wa mwenza wako!

    HII NI SEHEMU YA KUMI NA SABA….
    Nilikimbia huku na kule kutafuta muafaka wa jambo nisilolijua kabisa. Nilishika simu nikaicha, mama naye alikuwa amechanganyikiwa akiulizia ni wapi Nyambura atakuwa ameenda. Sikuwa na jibu la kumpatia….

    Kwa sababu yeye mwenyewe alifahamu fika kuwa tulikuwa wote Morogoro na sasa tupo jijini Dar es salaam.

    Nilifahamu fika kuwa mimi nikionyesha kuchanganyikia na mama naye aonyeshe kuchanganyikiwa basi patakuwa hapakaliki pale ndani, nikatulia na kuchukua tena simu yangu nikajisahaulisha kama kuna lolote ambalo limetokea.

    Sasa niliweza kupata mtu wa kumpigia.

    Mume wa Mariam Sumra ambaye ni mwanasheria wangu!

    Simu ilipokelewa upesi sana.

    “Nilitaka kukupigia simu muda huu huu!” alianza kuzungumza bila salamu yoyote. Nikamsikiliza.

    “Simpati Nyambura hewani, sijui kama upon aye?”

    “Nyambura? Wa nini?” nikamrushia swali.

    “Upon aye?” aliendelea kuuliza badala ya kujibu.

    “Hapana! Kuna tatizo lolote?” nikarusha tena swali.

    Hapohapo bila kutarajia chochote, ghafla mama akanipokonya ile simu.

    “Mje mtusaidie tumekuta mtu ni mwanamke ndani ya nyumba yetu, hatujui kama amekufa ama ni mzima. Na mke wa mwanangu hayupo, nje mtusaidie jamaniii!” alizungumza upesi upesi mama akiwa amechanganyikiwa sana.

    Ni tukio ambalo sikulitarajia kabisa na lilizua mshikemshike.

    Alipomaliza akanipatia simu huku akinilaumu kuwa ninazunguka zunguka mbuyu badala niseme shida inayotukabili.

    Sikumlaumu mama!

    Niliporejea kumsikiliza mwanasheria alinisihi nimweleze ukweli nini kinatoke.

    Nikamweleza hali kwa ufupi kama ilivyokuwa inaonekana machoni pangu. Lakini sikumgusia juu ya safari yangu ya Morogoro!

    Akasema anakuja pale nyumbani.

    Sisi tulibaki mbali kabisa na mwili wa Mariam Sumra, mama alikuwa ananionya kabisa nisiusogelee mpaka polisi wafike.

    Yeye alijua niliyekuwa nazungumza naye anahusika na mambo ya kipolisi.
    Baada tya dakika kumi na tano na ushee, pikipiki ilisimama mbele ya nyumba yangu. Geti lilikuwa wazi nikasikia vishindo vya mtu akija mbiombio.

    Nikaufungua mlango na kumtazama kwa mbali mwanasheria wangu akitimua mbio.

    Ama! Mapenzi ni kitu cha ajabu sana.

    Usiombe yakakumeza na kukutupa katika mji unaoamini ni tulivu kupita yote.

    Hii ilikuwa mara yangu ya kwanza kumuona mwanasheria huyu akiwa na hofu kubwa kiasi hiki.

    Alipofika akanisalimia mimi ‘SHKAMOO’ kisha akamwambia mama yangu ‘HABARI ZA KAZI’

    Nilijikuta nachekea mbavuni, baada ya muda mrefu kupita nikiwa sina hata tabasamu.

    “Amekuwaje mke wangu eeh! Amekuwaje jamani?” alihoji.

    “Kama nilivyokueleza katika simu mkuu. Hakuna ajuaye.. wote tumeingia muda huu.”

    “Hata mama nawe haukuwepo?” alimtupia swali mama.

    Mama hakujibu!

    Mwenye mke akamsogelea mkewe.

    Akamgusa hapa na pale….CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Anapumua!!” alisema….

    “Nini kimemtokea jamani eeh!” sasa alikitoa kichwa pale mezani na kumnyoosha sakafuni.

    Sasa hata mimi niliweza kuona akiwa anapumua.

    Hapakuwa na muda wa kupoteza zaidi, tukakubaliana kumpeleka hospitali.

    Nilijikaza na kuendesha gari kwa sababu mwanasheria alikuwa amepagawa zaidi.

    Tukiwa katika gari alikuwa akirudia rudia maneno ambayo awali niliyachukulia kuwa ya kawaida sana lakini alipozidi kuyarudia nikaanza kupatwa na hasira.

    Alikuwa akisema, ‘Joshua unajua mkeo ni shetani eeh! Shetani kabisa huyu mwanamke, sijui hata ulikosea nini ukaoa shetani.’

    Anatulia kidogo ananikumbusha tena kuwa mke wangu ni shetani.

    Hasira zikanikaba, lakini nikapambana nisije kufanya jambo lolote la kishenzi.

    Hii hali ya kukasirika baada ya mke wangu kuitwa shetani ilinifanya nitambue kuwa licha ya haya yote yaliyotokea, alama za penzi zito la Nyambura zilikuwa katika sehemu kubwa tu ya moyo wangu licha ya hayo yote yaliyotokea.

    Unaweza kunishangaa sana na kusema kuwa laiti kama ingelikuwa ni wewe usingelichukia kabisa.

    Ni kweli kwa sababu si wewe uliyeshuhudia penzi zito na la dhati kabla ya mkasa huu!!

    Tulifika hospitali, tukasaidia kumshusha Mariam Sumra!

    Akapokelewa na wauguzi akaingizwa wodini.

    Baada ya kutoa maelekezo na sisi kupewa maelekezo sasa tulibaki nje kusubiri kitakachojiri.

    Mwanasheria akaanza tena kusema vibaya juu ya Nyambura.

    Nikaona huyu bila kumwonyesha makucha sekunde si nyingi atanivuruga upya akili yangu.

    “Brother! Achana na masuala ya Nyambura na ushetani wake, unapomzungumzia Nyambura kama shetani unamzungumzia mke wangu wa ndoa, mama wa mtoto wangu mmoja. Unaposema ni shetani ni kipi mkeo alifuata kwa Nyambura kama sio shetani kumfuata shetani mwenzake? Wote ni mashetani tu, shetani mmoja yupo wodini amepoteza fahamu, shetani mwenzake anazurura popote anapojua yeye. Acha kumsema Nyambura hivyo tafadhali….” Niliwaka!!

    “Joshua acha baba…. Yaishe tupo matatizoni, na wewe baba mwingine acha kusema ushetani wa mtu usiyemjua…. Hivi mnajua Nyambura mnayemuita shetani alinitolea damu nyingi sana alipokuja kuniuguza kijijini, bila yeye ningeweza kufa. Hakutaka sifa zozote hajatangazia mtu… hebu mtunzie na haya mazuri yake basi…. Hata kama ni shetani basi tuyatunze katika mioyo yetu.” Mama alitusuluhisha.

    Yakaishia pale.

    Lakini sikutaka tena kuwa jirani na mwanasheria nikaketi mbali kiasi.

    Nusu saa baadaye majibu yalitoka kuwa Mariam Sumra alilishwa madawa ya kuleta usingizi, hakuwa na tatizo lolote zaidi ya pale.

    Huduma zikaendelea kutolewa hadi mjajira ya saa kumi jioni tukaondoka pale.

    Niliendesha gari hadi nyumbani kwa mwanasheria, wakati huo maelezo ya Mariam Sumra hayakufaa kitu chochote.

    Kwa sababu alidai kuwa Nyambura hakumweleza mpango wowote aliokuwanao.

    Tulipowashusha, mwanasheria alinifikia na kunipigapiga begani kisha akajutia kauli zake.

    Nikamwambia yamekwisha kabisa.

    Tukaondoka na mama hadi nyumbani, tukiwa kimya kabisa katika gari.
    Tulifika na kuikuta nyumba ipo kama vile tulivyoiacha. Hii ilimaanisha kuwa Nyambura hakuwa amerejea.

    Niliufungua mlango na kuingia pale ndani….

    Mara mama akapiga mayowe, nikaruka mbele kukwepa hatari yoyote ambayo ingejitokeza.

    Nikageuka na kumtazama mama alikuwa anatazama chini…..

    Damu!!

    Palikuwa na alama za damu ambazo hazikuwepo hapo kabla.

    Kutazama vizuri ulikuwa ni mchirizi wa damu…..

    Sijui pale tulipouona ndo ulikuwa unaanzia ama ulikuwa unaishia…

    Mchorizi ule ulikuwa unatokea chumbani ama kuelekea huko.

    Mapigo ya moyo yakaanza kufukuzana tena……

    Nini hiki?

    Tulijiuliza, nikatimua mbio mpaka chumbani bila uoga wowote ule.

    Matatizo yalikuwa lukuki sana sasa sikuwa naogopa lolote lile.

    Niliingia na kuufuata mchirizi ule.

    Nikainama uvunguni, mama naye akinifuata nyuma hapakuwa na mauaji wala hapakuwa na mtu yeyote yule.

    Tulibaki kustaajabu.

    “Bahasha hiyo ina damu..” mama aliona na kusema, nikageuka na kutazama upande alionionyesha.

    Kweli kulikuwa na bahasha yenye damu.

    “Mama wamemuua Agy wangu!!” nilianza kulia sasa.

    “Agy! Umejuaje?” alinibambika swali lililokatisha kilio changu, kwa sababu nilikuwa nalilia kitu nisichokijua.

    Nikaiokota ile bahasha huku nikitetemeka.

    Nikaifungua na kukuta ndani kuna kipande cha barua.

    Nikatoa huku nikiomba Mungu pasije kuwa na masharti ya kipesa kwa ajili ya kumkomboa mwanangu.

    Sikuwa na pesa kabisa, hivyo mwanangu angeweza kuuwawa.

    Safari hii sikuwaza sana juu ya Nyambura!

    Kutazama ulikuwa ni mwandiko wa Nyambura, mwandiko niliouzoea pindi tulipokuwa ofisini.

    Nikaisoma kwa sauti mama awe shuhuda kwa kusikia.
    NYANBURA ANAANDIKA!!

    Joshua, mume kipenzi kabisa.

    Ndugu yangu pekee, na baba halali wa mtoto wetu!

    Niligundua kuwa nakupenda sana lakini nilikuwa nimechelewa, tayari nilikuwa nimeharibu kwa kutunza kisasi kisokuwa na tija.

    Kisasi cha kipuuzi!

    Umeteseika nimeona kwa macho, nami ninateseka moyoni hakuna anayeweza kuona.

    Nikiulizwa peponi nini maana ya pendo la dhati nitajibu Joshua, hata wakihitaji orodha ya wanaume wa uhakika niliowahi kukutana nao jibu litakuwa Joshua.

    Yaliyopita yamepita! Wewe ni baba bora sana ambaye unastahili kupata mwanamke safi asekuwa na visasi katika nafsi yake.

    Lakini ni mwanaume ambaye haustahili kutendewa haya yaliyotokea kwako.

    Nimeona na kwa dakika za mwisho nimejaribu walau kupigania kidogo kilicho chako walichotaka kukupokonya,

    Ulipishana nami katika hoteli Morogoro.

    Usingeweza kunijua, nilikutazama na kuuona uso wako ulivyosononeka kwa haya yaliyotokea, niliona jinsi ulivyokonda kwa mawazo.

    Nilimuona mama yetu alivyokuwa anakusikitikia.

    Niliingia ulipokuwa na niliua!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ndio niliua….

    Kuhusu niliuaje na niliua wangapi? Haya hayana tija lakini kwa sababu walikiuka makubaliano yetu niliona hawa ndo wanafaa kuadhibu na sio wewe Joshua.

    Mimi ni binti imara kabisa kutoka mkoani Mara, nimepitia suluba zote na pale mtu anapokiuka tulichokubaliana nipo radhi hata kuua.

    Narudia tena niliua na nimeirejesha bahasha iole kwako. Sikutoa hata noti moja.

    Halali yangu ipo katika akaunti yangu, ulinilipa mshahara mzuri sana unanitosha kuanza maisha mapya nikiwa namlea mtoto wako.

    Kama nisipokamatwa mapema basi mwanao akifikisha miaka minne, nitamleta kwako.

    Lakini kama ukisikia nimekamatwa mapema tafadhali usiache Agness akatua katika mikono ya watu wabaya.

    Mchukue wewe uliyesota kumpata!

    Mchirizi huo wa damu usikushangaze sana…

    Nimejikata maksudi na kuiacha damu hii iishi nawe katika nyumba yako milele yote.

    Nawapenda sana!

    Nakusihi sana usiyafuatilie tena mambo haya kwa namna yoyote kwa sababu yatakuumiza kichwa.

    Naomba msamaha mimi kwa niaba ya wote nilioshirikiana nao.

    FUNUA GODORO MUDA HUU!!
    Nyambura Joshua!!
    Barua iliishia pale, nami upesi nikafunua godoro.

    Macho yangu yakakutana na ile bahasha niliyoipeleka Morogoro.

    Nilijikuta natokwa na kilio huku moyo wangu ukiuma sana, nilitamani Nyambura angerejea tena katika maisha yangu!!

    Lakini Nyambura hakujulikana ni wapi alipo…..
    _____
    Baada ya muda nikaendelea na shughuli zangu katika kampuni yangu ambayo ilikuwa imeacha kufanya kazi kwa sababu wafanyakazi hawajalipwa mishahara yao.

    Siku niliyoingia ofisini kwangu, nilijikuta natabasamu tu, nilikuwa nimewakumbuka wale matapeli waliodai kuagizwa na mizimu….

    Nikatambua kuwa hata wao huko walipo kuzimu watakuwa wakikumbuka wananicheka sana.

    Nikatulia katika kiti changu cha kuzunguka, nikaanza kuandika majina na madhara katika akili yangu.
    NYAMBURA: Sitakaa niwaamini wanawake katika maisha yangu hasaha katika sekta ya mapenzi, sikuwaza kuoa tena. Mpaka hivi sasa sitaki ushauri!!
    REVO: akili yangu haikuwa na nafasi tena kwa ajili ya rafiki wa dhati, hata mwanasheria aliyenisaidia bado sikutaka kumwamini sana. Ikiwa naye alimuita mke wangu shetani, ipo siku nami anaweza kuniita baradhuli.
    MGANGA: Sitathubutu kwenda kwa waganga wa jadi tena, ni waongo na wanafiki wakubwa.
    Majina haya yalinitosha sana kwa wakati ule.

    Na niliapa kuwa hata wanasaikolojia wahamie nyumbani kwangu na wengine waje kuishi ofisini kwangu hawataweza kulitibu gonjwa langu la kihisia juu ya marafiki na mapenzi.

    “Ama hakika Nyambura ulikuwa ni mji tulivu, mji bora kabisa niliowahi kuishi lakini gonjwa uliloniachia ni la milele nitadumu nalo….”
    JIFUNZE:
    KATIKA maisha kuna nyakati huja katika maisha ya watu wengine, nawe utaziona na kuishia kusema yamemtokea fulani. Lakini halahala litokealo kwa jirani yako hata nawe laweza kukutokea. Majaribu shida na mateso tumeumbiwa wanadamu!!!

    Jifunze kupitia uyaonayo ili ujiandae kuyakabili yakija kwako…..
    MWISHOO!!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
    #TAFADHALI USIPITE BILA KUTOA MAONI SIKU HII YA LEO!!
    ASANTENI SANA kwa kuwa nami mwanzo hadi mwisho

0 comments:

Post a Comment

Blog