Search This Blog

Sunday, 19 June 2022

MJI TULIVU ULIONIPA UGONJWA WA MILELE - 4

 





    Simulizi : Mji Tulivu Ulionipa Ugonjwa Wa Milele

    Sehemu Ya Nne (4)





    Baada ya kupokea simu ile na kugundua kuwa mpigaji alikuwa ni yule mganga wa jadi na alikuwa ananieleza kuwa kuna jambo baya ambalo limemtokea mama kwa sababu yangu, nikajua wazi kuwa yawezekana kile kitendo cha kumshirikisha mama juu ya mambo yanayonikabili ndo chanzo cha wazi kabisa cha yeye kukumbwa na balaa lolote lililomkumba. Lakini niliomba sana hilo balaa lisijekuwa eti ni kifo kwa mama yangu.

    Nilimsihi sana yule mganga anieleze nini kimemsibu mama yangu, akanieleza kuwa mizimu imemchukua na itakuwa tayari kumrejesha ikiwa tu nitatimiza ahadi yangu, lakini vinginevyo nitakuwa nimemtoa mama yangu kafara.

    Akanilaumu kuwa nimeikasilisha sana mizimu kwa kumshirikisha mama yangu juu ya jambo linaloendelea.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
    Damu ilichemka sana kusikia hivyo, nikaituliza akili yangu na kujiuliza ni kipi nitafanya.

    Mama ndo mtu pekee ambaye alikuwa akinifariji hasahasa nikiwa nimezidiwa na mawazo kama hivyo, sasa naambiwa kuwa amechukuliwa na mizimu.

    Licha ya kujaribu sana kuituliza akili bado nilikuwa katika mchecheto.

    Nilichukua simu yangu na kumpigia mwanasheria wangu kumsihi anifanyie hima sana juu ya zile nyaraka za kuhakikisha kuwa hisa zimeuzwa.

    “Joshua!” mwanasheria aliniita baada ya kuwa nimezungumza naye na kumsihi. Nikamuitikia, akanieleza kuwa kama ninaweza nionane naye usiku huohuo kuna maswali anahitaji kuniuliza ili aweze kukamilisha vizuri zile nyaraka bila dosari yoyote.

    Laiti kama angekuwa ananiitia mambo mengine hata nisingeweza kwenda, lakini kwa sababu ilikuwa ni juu ya nyaraka zile muhimu niliamua kwenda.

    Tukakutana katika mgahawa mmoja tulivu sana usiokuwa na kelele na vurugu za hapa na pale.

    Yule mwanasheria ambaye kiumri alikuwa ananizidi alinitazama kwa muda bila kuuliza chochote, kisha akaniuliza kuhusu ndoa yangu kama imetulia na ni salama.

    Nikamjibu kuwa kila kitu kipo sahihi kabisa.

    “Joshua mdogo wangu, nahitaji tuzungumze kirafiki tafadhali usinijibu kana kwamba mimi ni adui yako.” Alinisihi kwa upole.

    “Ndugu, niulize maswali juu ya mkataba na sio vinginevyo..” nilimfokea kidogo. Akatabasamu kisha akapiga funda moja la bia aliyokuwa amenunua kabla sijafika.

    “Mkeo ana biashara gani anazofanya na Revo?” aliniuliza swali ambalo sikujua lilikuwa na mantiki ipi.

    Sikumjibu na nilizidi kupagawa kwa sababu huyu bwana nilimwona akinipotezea muda wangu angali mimi nina tatizo kubwa sana.

    Nilikuwa nahema juu juu huku hasira nazo zikichukua nafasi katika nafsi yangu, kitendo cha yule bwana kuzungumza juu ya mke wangu kikanifanya nikumbuke kuwa alikuwa ameniomba shilingi milioni nne na hadi wakati huo nilikuwa sijampatia na sikuwa na dalili hizo,

    “Joshua… sina maana mbaya kukuuliza hivyo. Naomba tu unijibu.” Alinisihi.

    Nilijitahidi hasira zangu zisije zikavuka mpaka na kumvunjia heshima yake.

    Nikamjibu kuwa hakuna biashara yoyote kati ya mke wangu na Revo.

    “Na unadhani kwa nini Revo aliuza hisa zake ghafla baada ya wewe kumtolea mahari Nyambura?”

    Hili swali likanilainisha kidogo, ni swali ambalo kama jibu lake lingepatikana basi lilimaanisha kuwa kuna mahusiano kati ya Revo kuuza hisa zake na mahusiano yangu na Nyambura.

    “We umewaona wapi Revo na Nyambura?” nikauliza, sasa nikirejea juu ya lile swali la kwanza Nyambura ana biashara gani anafanya na Revo.

    Mwanasheria akanitajia mazingira ambayo amewahi kuwaona Nyambura na Revo akauelezea uhusiano baina yao tangu niliposafiri na unavyoendelea hadi wakati huu ambao nina matatizo.

    “Unavyosema juzi umewaona, unamaanisha juzi kabla hajajifungua mtoto ama akiwa na mtoto?” nilimuuliza kwa namna fulani ya kumsuta uongo nikijifanya namuamini sana Nyambura wangu.

    “Juzi katika maana halisi ya juzi, na hakuwa na mtoto, si mara moja wala mara mbili.. nadhani ni mara tatu. Wanakutana katika baa fulani iliyojificha mtaani kwetu… ni baa ambayo huwa napenda kujificha hapo nakunywa bia kwa amani kuliko kwingine ambapo nitasumbuliwa na marafiki wapenda ofa.” Alinijibu kwa utulivu sana huku akijiamini mno.

    Sasa sikuwa na hasira tena bali wingi wa maswali pasi na majibu.

    “Kwa hiyo kaka unadhani wanafanya biashara gani?” nilijikuta natokwa na swali la kipuuzi.

    Akatabasamu kisha akapiga funda moja la kinywaji chake.

    Hakunijibu!!

    “Huwa wanakuwa watatu wakati mwingine wanne, sidhani kama ni biashara ndogo. Ila we si ulinambia mkeo anafanya biashara?? Labda ndo hiyo?”

    “Hapana, hawezi kufanya biashara na Revo halafu asinishirikishe, anaujua urafiki wetu vyema, na Revo hawezi kuacha kunishirikisha juu ya hilo.” Nilipinga.

    “Unaonyesha unapenda sana kuamini kwa asilimia mia eeh!” alihoji kwa kebehi kiasi fulani. Nikagundua alichomaanisha.

    “Siwezi kujua anyway, ila nimeona tu nikushirikishe kama mdogo wangu, uzuri ni kwamba ukimwambia mkeo kisha akanichukia atakuwa anamchukia mtu ambaye hamjui na hata Revo akijua nimekwambia akachukia haitafaa chochote maana sisi wanasheria tunachukiwa sana na tunapendwa vilevile, mimi ni mwanasheria wako!” alimaliza akapiga funda moja la mwisho na kutaka kunyanyuka. Nikamsihi asiondoke.

    Nilikuwa nahitaji sana kusikia zaidi kutoka kwake.

    Yaani kwa ufupi nilikuwa hoi kimawazo, huku nawaza juu ya mizimu na upande wa pili nikiwaza kuwa eti yawezekana mke wangu ana mahusiano ya kimapenzi na rafiki yangu wa karibu kiasi kile??

    “Kaka tafadhali naomba uniambie basi unahisi kuna nini ukiniacha hivi kaka nitagongwa na gari mimi, nimechanganyikiwa kaka yaani kuna mambo yananiendea kombo kiasi kwamba ninajiona nina kitu kama jini la mitihani nimetupiwa…” nilimsihi

    “Kwani unahisi mkeo anaweza kujihusisha kimapenzi na Revo ama alikuwa akijihusisha naye hapo kabla hujamuoa ama?” alinihoji, wakati huohuo akampungia muhudumu mkono na kuongeza kinywaji kingine.

    Nikafarijika kuwa ataendelea kubaki zaidi.

    “Kaka, sina walau hata hisia potofu kidogo tu dhidi ya mke wangu, nimekuwa naye kiuaminifu sana na ninaamini ananipenda.” Nilimjibu nikiwa namaanisha.

    “Aisee! Umesema kuwa huwa anasafiri mara kwa mara kwa shughuli zake za kibiashara, je? Umewahi kufuatilia walau tiketi za mabasi na ndege ambazo anatumia?”

    Lile lilikuwa swali zito sana na nikajiona ni mzembe sana kutofuatilia nyendo za mke wangu eti kisa tu naamini kuwa ananipenda.

    “Haya basi nambie na wewe ni kwanini unauza hisa za kampuni, tena unauza zote tisini, unayemuuzia simjui unanilazimisha tu kuandaa makubaliano. Joshua ni nani anayekulazimisha kuuza hisa zako najua hauuzi kwa hiari yako mwenyewe… ni mkeo ama?” alipouliza vile akanikazia macho yake nikakosa ujasiri wa kuendelea kumtazama.

    Nafsi ilikuwa inanisuta.

    Nilikosa cha kujibu. Nilitamani kumweleza ukweli lakini kwa yaliyomtokea mama yangu. Nilihofia kuyakuza zaidi nikimsimulia na mwanasheria.

    “Kesho makubaliano yatakuwa tayari, kumbuka kama unanidanganya mimi unajidanganya mwenyewe. Mimi ni mwanasheria mteja wangu akiniongopea balaa huja kwake si kwangu…”

    Alimalizia maneno yale kisha akainuka na kuondoka zake hata bia yake hakuimalizia.

    _____CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Maneno ya mwanasheria wangu yalikuwa yameniletea ugonjwa mpya uitwao mashaka, nilikosa kujiamini… nikimtazama mke wangu machoni namwona asiyekuwa na hatia lakini busara za mwanasheria nazo zilikuwa na makali yake katika upande wa kuishtua akili yangu.

    Usiku huu niliporejea nyumbani nikawa namuwaza mke wangu, namuwaza rafiki yangu Revo, namuwaza mwanasheria na maneno yake lakini zito zaidi nikimuwaza mama yangu mikononi mwa ile mizimu inayotaka kuimiliki kampuni yangu na kila kitu kilichomo.

    Niliyafumba macho yangu, nikaanza kulijengea picha wazo la kwanza.

    Nyambura na Revo!

    Nikafikiria jinsi ambavyo huwa tunacheza bafuni huku tukiyaacha maji yamwagike pasi na jambo la msingi. Ananigusa huku nami namgusa kule.

    Nikajitoa pale bafuni kisha nikamuweka Revo.

    Yaani Revo naye anamgeuza nyuma Wambura na kumuuliza hii alama hapa mgongoni ulikuwaje?

    Nilijiuliza huku nikipambana kuidhibiti ghadhabu yangu.

    Lakini si ana mke kabisa Revo! Halafu mkewe mrembo haswa kuliko hata huyu Nyambura, sasa kama wana mahusiano kweli… kampendea nini?

    Nilizidi kuumia kichwa nikiyakosa majibu kabisa.
    Nikiwa ningali katika mawazo mazito kabisa, Nyambura mke wangu akanitikisa nakuniambia kuwa kuna mambo kadhaa anahitaji kuzungumza na mimi.

    Nilimweleza kama inawezekana tuzungumze asubuhi akakataa akasema ni lazima iwe usiku uleule!

    Nikakubali japokuwa niliamini kuwa sikuwa tayari kumsikiliza kwa umakini.

    Akaanza kwa kunikumbusha juu ya zile pesa alizoomba nimsaidie kuweka kwenye nambari aliyonipatia, nikazuga kushtuka na kumtaka radhi kuwa nilisahau.

    “Sawa achana na hilo, nahitaji kuzungumza juu ya mama.” Akasema kisha akasita.

    Ile kutaja jina mama, moyo wangu ukalipuka vibaya sana. Nikaingiwa na ganzi na ubaridi ukitambaa katika mwili wangu.

    “Nilizungumza na mama kabla hajaondoka!” akaweka mkato tena, kisha akaendelea, “Kwanini umemfukuza mama?” akanirushia swali la ghafla.

    “Nani? Mimi?” nikatokwa na swali la kizembe. Nyambura hakusema kitu akaniacha nibabaike.

    “Mimi nimemfukuza mama? Nani kakwambia? Ni mama kakwambia mi nimemfukluza?” nikabaki kujiuliza na kujipa majibu katika namna ya kutaharuki.

    “Baba Agness…” akaniita kwa utulivu, akaendelea baada ya mimi kuitika, “Ulinieleza kuhusu historia yako, na mama pia alinieleza juu ya hilo. Leo hii umekuwa mtu mzima unamficha mama mambo yako, mimi je? Si ndio utaniua kabisa kwa kunificha siri zako?” aliuliza katika namna ya kulalamika.

    Nilikuwa nimekamatika!

    “Tazama! Unadhani sikuoni unavyokonda kila siku, unadhani sioni kuwa hauna raha wala amani? Nayaona yote haya…. Lakini mimi ni uchafu tu mbele yako, hata nikiuliza najua hautanijibu, kama mama yako mzazi umemkatalia katakata je mimi mpita njia!” aliendelea kulaumu, sasa alikuwa amejinyanyua na kuegemea mkono wake akinitazama vizuri.

    “Ni nini chanzo cha kuapa kanisani kuwa sasa mimi ni ubavu wako rasmi, nakuaje ubavu wako! Nakuaje kiungo katika mwili wako ikiwa siyajui maumivu yako? Sijui hisia zako… sijui unachopitia!!” alishindwa kuendelea sasa machozi yakaanza kumtiririka.

    Looh! Nilichanganyikiwa kupita awali, nikaanza kumbembeleza lakini Nyambura katukatu hakutaka kunisikia.

    “Joshua! Nalala sebuleni, naomba usinifuate huko, na kesho usiku nitalala kitandani ikiwa tu aidha mama amerejea hapa! Au utanipa nafasi mimi kama mke wako kujua nini unapitia… la sivyo! La sivyo Joshua …..” akaiacha hewa sentensi yake akaondoka zake.

    Kama ni mpambano wa masumbwi, nilikuwa nimepigwa ngumi mfululizo nazipangua halafu nikajisahau nikatoa mikono na nikaingizwa pigo moja mahususi liitwalo ‘uppercut’, huu ni mtindo wa ngumi ambapo mpinzani wako anaikunja ngumi yake na kisha anairusha kwa kutokea chini inatua katika kidevu chako.

    Pigo hili linaweza kuvunja taya ya mlengwa!

    Nami nilivunjwa vibaya, nikabaki kama tahira kitandani.

    Moyo wa kike ukanivaa, nikaanza kulia kana kwamba nimefiwa!

    Ama! Yalikuwa yamenifika Joshua mimi.
    JIFUNZE!

    KATIKA mahusiano ya kimapenzi, hususani ndoa. Mahusiano mengi huanza katika namna sahihi kabisa ya tatu jumlisha tatu jibu ni sita, lakini kuna nyakati katika ndoa mahesabu hayo hubadilika, mmoja ataiona ile sita ni tisa na mwingine ataiona sita ni sita. Na kila mmoja akiamini kuwa yupo sahihi!

    Ni hapa FUKUTO huanzia!
    *************


    Asubuhi ilipowadia Nyambura alikuwa ameninunia na hata hakunisalimia wala kunibusu kama ilivyokuwa kawaida yake siku zote.

    Na macho yake yalikuwa yamevimba sana.

    Bila shaka alilia usiku kucha!

    Niliondoka pale nikiwa sina la kufanya, niliona uamuzi sahihi wa kuniweka mimi salama ni kuwapa mizimu kile walichokuwa wanahitaji ili mama yangu aweze kurejea salama mikononi mwangu. Kwani kwa kitendo cha mama kuonekana tu basi Nyambura naye angetabasamu na kunielewa.
    Siku iliyofuata nikiwa tayari na zile nyaraka muhimu, nilienda hadi kwa yule mganga nikampatia na kumweleza kuwa kila kitu sasa kipo tayari ila watatakiwa kufanya uhakiki wa kisheria ili ile kampuni iwe yao.

    Nikaongezea kuwa wafanyakazi sijawaambia jambo lolote ili kutoyumbisha utendaji kazi wao, mganga akapokea ile hati ya umiliki na kunieleza kuwa ataiwasilisha kwa wazee yaani mizimu.

    “Lakini masuala ya kibenki hamna namna lazima tukabidhiane benki hukohuko sasa hii itakuwaje? Mizimu itafika benki?” nilimuuliza yule mganga.

    Swali langu likamshtua sana hadi mi mwenyewe nikafahamu kuwa amebabaika. Akajirekebisha baada ya muda kidogo kwa kuanza kuchekacheka.

    Akanieleza kuwa mizimu haishindwi kitu, atawasilisha kisha majibu atanieleza kwenye simu.

    “Vipi kuhusu mama yangu sasa…” nilihoji jambo lile la msingi ambalo nd’o lilinisukuma kumlazimisha mwanasheria kufanya kila awezalo kampuni itolewe katika umiliki wangu kwa asilimia tisini.
    Niliondoka kwa yule mganga kichwa chini mikono nyuma, kila hatua niliyopiga nilikuwa nakumbuka jinsi nilivyotokwa jasho hadi kufanikiwa kuimiliki ile kampuni. Nikafikiria ni mara ngapi nilianguka na kuinuka tena, watu wangapi waliniunga mkono hadi kufanikiwa kuifungua ile kampuni.

    Niliyakumbuka majibu ya mkato niliyokuwa napewa pale BRELA (Ofisi inayohusika na usajili wa makampuni), lakini bado nilikuwa mnyonge na kufuata walichohitaji.

    Hata pesa ya mtaji haikuwa inajitosheleza, tukahangaika na Revo hadi tukalikamilisha lile jambo ambalo liliniacha nikiwa na uzito wa kilo hamsini na tano kutokea sitini na nne nilizokuwanazo.

    Halafu leo hii napoteza kila kitu kwa mkupuo.

    Sasa sina kampuni tena!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nilijiweka pembeni ya barabara na kuanza kulia bila kukoma. Nililia huku nikikumbuka kumlaumu Mungu kwa kunipa mitihani mikubwa kuliko uwezo wangu wa kuitatua.

    Nililia sana mpenzi msikilizaji…. Na ninakusihi hata wewe ukikabiliwa na tatizo.. usijikaze jiweke mahali na ulie kwa kiasi utakachohisi nafuu.

    Kilio ni tiba, hupunguza msongo wa mawazo mwilini na kulifanya tatizo kubwa lililopo walau lipungue makali.

    Nilifika nyumbani, tofauti na ilivyo kawaida sikumkuta mke wangu nyumbani, haikuwa tarehe ya kumpeleka mtoto kliniki labda ningeweza kusema ameenda hospitali.

    Ameenda wapi sasa? Nilijiuliza huku nikijilaza kitandani.

    nikiwa nasumbuliwa na maumivu makali ya kichwa, nikapokea simu kutoka kwa mwanasheria wangu.

    “Acha nionekane mnafiki na mchonganishi lakini kama mbele ya Mungu nitapata thawabu kwa kukueleza ukweli mdogo wangu basi acha niabike duniani.” Alianza kuzungumza bila hata kunipa salamu.

    “Kulikoni kaka…” nilimuuliza kinyonge.

    “Nipo hapa nakunywa bia.. mkeo na wenzake wana kikao kidogo sijui ndo kikao cha biashara?” aliniuliza katika namna ya kunisanifu.

    “Wapo wawili tu leo, yupo na mfanyabiashara mpya kabisa sijawahi kumuona…. Kutana nami jioni nikupe swali moja ambalo mimi sina majibu wewe ndo unayo. Ila akirudi nyumbani usimuulize sana juu ya alikuwa wapi…. Aisee mkeo kiboko yaani ana mtoto mdogo ila bado anapiga bia kama maji!!” alizidi kunichanganya mwanasheria.

    Akamaliza akaniaga na kukata simu, sasa kichwa kilikuwa katika maumivu makali kupita maumivu yote niliyowahi kupitia.
    Yaani mke wangu ninayemuamini kupita wanawake wengine duniani ukimweka kando mama yangu, leo hii kuna hila anafanya juu yangu…. Yaani yawezekana ananisaliti?

    Nilihamanika vibaya mno. Nikaenda kujitazama kwenye kioo na kushuhudia macho yangu yakiwa mekundu sana.

    Nilitambua wazi kuwa mke wangu akinikuta pale nyumbani kisha nikamuuliza swali lolote halafu akaniongopea basi naweza kujikuta nambamiza vibaya sana.

    Nilikuwa katika kiwango cha juu kabisa cha ghadhabu! Na nisingeweza kujiongoza kwa namna yoyote ile.

    Naweza kuua! Niliwaza.

    Nikaamua kuondoka pale nyumbani hadi jioni kabisa nilipokwenda kukutana na mwanasheria.

    Kabla sijafika kwa mwanasheria nikapigiwa simu na yule mganga, akanieleza kuwa hakuna muda wa kupoteza mizimu imemtuma mtu wao ambaye wamemvika ubinadamu atafika kwa ajili ya kukamilisha taratibu zilizobaki kisheria ili kampuni iwe mikononi mwa mizimu.

    Mganga akanisisitiza kuwa natakiwa kuacha chochote ambacho nilikuwa nafanya na wakati huohuo niende Posta maeneo ya City Garden kwa ajili ya kukutana na wajumbe kutoka kambi ya mizimu.

    Maneno yale yakanifanya nikabadili uelekeo na kwenda Posta kukutana na wajumbe ambao mganga alinielekeza kuwa walikuwa wamevaa nguo nyeupe wote aina ya suti.

    Hivyo nilipofika tu niliwaona, nikaenda hadi walipo.

    Walikuwa wanazungumza Kiswahili kibovu kabisa chenye lafudhi ya kongo, waliniuliza maswali kadhaa nami nikawajibu, nilipotakiwa kuweka sahihi yangu nikaweka.

    Kisha wakanitaka wakati uleule niwapeleke ilipo kampuni yangu, nikatii.

    Tukaongozana hadi ofisini.
    Wakatazama nyaraka kadha wa kadha, kisha wakanieleza kuwa mizimu imewaagiza kunielekeza ni wapi mama yangu mzazi alipo.

    Wananipa maelekezo mara moja na nitatakiwa kufanya utekelezaji mara moja.

    Wakanieleza kuwa ninatakiwa kusafiri hadi katika wilaya ya Tunduma mkoani Mbeya, niende hadi mpaka wa Tanzania na Zambia na huko nitakabidhiwa mama yangu akiwa hai kabisa na baada ya hapo nitaendelea na maisha yangu.

    Hakuna nilichopinga, kwanza nilikuwa ninawaogopa sana na pili nilitaka haya mambo yaishe upesi niendelee na maisha yangu hata kama ni ya kimasikini lakini sio ya mashaka kwa kiwango hicho.

    Wakati mmoja akinipa maelekezo yale, mwingine alikuwa amekalia kiti ambacho nilikuwa nakikalia mimi kama mkurugenzi mtendaji wa kampuni. Alikuwa anazunguka kwa kujinafasi.

    Anajinafasi katika mali niliyoichuma kwa jasho sana.

    Ningefanya nini?

    “Hiyo gari unayoendesha sio ya kampuni?” aliniuliza na lafudhi yake ileile.

    Nikatikisa kichwa kukataa na kudai kuwa ni mali yangu.

    Wakacheka na kunong’onezana. Sijui hata walisema nini.

    “Tukitoka hapa tunaenda benki, utatoa pesa yote kama ilivyo katika akaunti, pesa hiyo itapelekwa kwa mizimu kwa ajili ya kubarikiwa kisha itarudishwa kwenye akaunti…” walinielekeza.

    Nikatii!

    Wakati tunatoka ilikuelekea benki, simu yangu ikaita.

    Alikuwa ni mke wangu ananipigia.

    Ile kuliona jina la mke wangu, mapigo yangu ya moyo yakapiga vibaya mno nikawa nimekumbuka na ujumbe kutoka kwa mwanasheria juu ya mke wangu kuonekana mahali akiwa anakunywa pombe huku akiwa na mtoto. Nilitaka kuipuuzia kwa sababu nilikuwa naendesha gari lakini hakuacha kupiga alifanya hivyo tena.

    Alipopiga kwa mara ya tatu nikapokea kwa sababu nilijua kuna tatizo, mke wangu si mtu wa kupiga simu zaidi ya mara mbili na kuendelea kupiga tu hata isipopokelewa.

    Nikaipokea na kumsikiliza.

    “Baba Agness mume wangu upo wapi?” aliniuliza huku sauti yake ikisikika kama mtu ambaye anakaribia kulia.

    “Naendesha gari naelekea posta Kariakoo mara moja, vipi?” nilimjibu huku nikiwa makini barabarani.

    “Nahitaji kukuona sasa hivi!” aliniambia bila kuongeza neno.

    “Dah! Nyambura, kuna jambo la kiofi…”

    “Hakuna cha jambo la kiofisi, muda huu nahitaji kukuona kisha utaendelea na jambo hilo. Waambie watu unaoenda kuwafanyia hilo jambo kuwa unahitaji kuonana na mkeo kwanza.” Alinisihi na kuzidi kunichanganya. Hawa watu wametumwa na mizimu, na mizimu inamshikilia mama yangu, sasa inakuwaje niwape kero nyingine? Je wakimuua mama yangu?

    Mama anayenipenda kuliko huyu Nyambura anayenisaliti kwa kushiriki mapenzi na rafiki yangu Revo!

    Nilijiuliza kisha nikaweka katika mzani na kuchukua maamuzi.

    Sitaenda kwa mke wangu, nitamalizana na hawa watu kwanza kwa masilahi ya mama yangu.

    “Nyambura nitaonana nawe baada ya dakika arobaini tafadhali.” Nilimsihi na kukata simu.

    Hakupiga tena!

    Tulifika hadi benki, wao wakaketi mahali pa kusubiria huduma, mimi nikapanga foleni kuelekea katika dirisha tayari kwa kuzichota zile pesa, nilikuwa natetemeka sana nilipofikiria milioni mia moja na sabini inaweza kufanya nini katika maisha ya kawaida tu.

    Nikatambua kuwa ni pesa nyingi sana naenda kuzipoteza kwa sababu ya ujinga wangu tu wa kuupinga utendaji kazi wa Mungu na kuamua kuingiza mambo ya waganga wa jadi katika ndoa yangu.

    Walikuwa wamebaki watu watano kabla haijawa zamu yangu kuchota pesa.

    Mwanamke mwenye baibui akasimama pembeni yangu, alikuwa amejiziba hadi usoni yakabaki macho tu.

    “Samahani!” alisema kwa sauti ya chini. Sikuju kama anasema na mimi.

    “Samahani Joshua.” Sasa alinitaja, nikageuka kwa mashaka.

    “Noo! Usinitazame we angalia mbele tu….. naomba uje hapa uwe kama unanisaidia kujaza hii fomu. Kuna ujumbe wako muhimu tafadhali nakuomba..” alinisihi. Sikushawishika, nilijua ni mizimu inanipima.

    “Joshua njoo, ni ujumbe kutoka kwa mke wako.” Aliposema vile moyo ukapiga kwa nguvu. Nikaamua kuthubutu nikaenda alipohitaji niende.

    Akawa anajaza fomu ya kuomba mkopo kwa kuzuga.

    “Mke wako amesema usifanye lolote lile unalotaka kufanya, nenda ukaonane naye kwanza. Tafuta sababu yoyote ile ambayo itasababisha usifanye unalopaswa kufanya… zingatia ni mkeo amesema. Yule pale nje katika pikipiki.” Akamalizia kwa kuniambia uelekeo alipo mke wangu, nikageuka na kutazama.

    Kweli alikuwa ni mama Agy akiwa na Agy mgongoni!

    Nilipagawa sana na kujiuliza ni nini hiki kinatokea katika maisha yangu.

    Hadi nafika dirishani na kukabidhi matakwa yangu kwa muhudumu bado sikujua lipi nifanye ama lipi nisifanye.

    nilipomkabidhi na kuanza kuishughulikia alinitazama na kuniuliza kuwa ni kwanini nimeamua kutoa pesa zote. Nilimtazama sikumjibu!

    Akafanya alichostahili kufanya.

    Nikasema pesa ni makaratasi acha wazichukue wanipe mama yangu!

    Nikakabidhiwa kiasi kile...

    Lakini sikutoka ndani ya benki salama bin salmini kabla hakijazuka kizaazaa cha funga na fungua mwaka!
    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
    **************




    Nyambura aliendelea kulia nilipomkaribia kumuuliza alinisukuma na kudai kuwa nikae mbali naye.

    Kwa sababu na mimi nilikuwa nimepagawa nilirejea katika kochi, nikatulia.

    Akalia hadi aliponyamaza.

    Akamuita yule mwanadada anayeitwa Mariam Sumra!

    Akamnong’oneza huku akipambana na kwikwi za kilio.

    “Amesema si hapa labda pengine!” alinieleza, kitu alichosema sikukielewa kabisa.

    “Nani? Aah! Mbona mnanichanganya jamani!” nililalamika.

    Nyambura akamuita tena kwa ishara, mwanadada akaenda kwa unyenyekevu kabisa. Akanong’ona tena..

    Yule dada akaomba maelekezo zaidi, alipoelewa akaondoka kuelekea jikoni.

    Aliporejea alikuwa ana chupa ya mvinyo katika mkono wake mmoja na mkono mmoja akiwa na glasi.

    Alifikisha hadi kwa Nyambura!

    Nikazubaa, sikuwahi kumwona nyambura akinywa kilevi cha aina yoyote ile… kulikoni leo anakunywa mvinyo.

    Dada yule alipotaka kummiminia katika glasi Nyambura akakataa…

    Akaishika chupa na kuanza kuigida kwa fujo hadi yule dada akawahi kumpokonya ile chupa.

    “Nyambura inatosha mama… inatosha….” Alimsihi huku akimzuia kuendelea kunywa.

    Nyambura akasimama ghafla, akaichukua ile glasi na kuirusha ukutani ikapasuka vipande vipande.

    Ebwana eeh! Nilichachawa nikahisi Nyambura anakumbwa na wendawazimu mbele yangu…..

    Nilitaka kumkabili nimzuie lakini yule mwanamama akanizuia, akanisihi nikae kuwa kila kitu atamaliza.

    “Tuondoke hapa!” Nyambura akamweleza Mariam Sumra!

    “Ni wapi sasa unapendelea…. Tafadhali kuwa mtulivu Nyambura, tulia kila kitu kitakuwa sawa kama nilivyokueleza hapo kabla. Nakuomba sana uniamini, niamini Nyambura!” Mariam alimsihi kwa nidhamu ya hali ya juu. Hakujishughulisha kabisa na ile glasi iliyopasuka vipande vipande.

    “Twende ofisini kwangu!” Nyambura alitoa maelekezo.

    Mariam akanigeukia na kunitazama kama nimesikia alichosema Nyambura.

    Nikawa kama msukule nikafuata kile kinachotakiwa hata nisijue nini kinaendelea.

    Tulimchukua Agness aliyekuwa amelala bado, tukaingia garini na kuondoka.

    Moja kwa moja hadi ofisini, hapo tayari giza lilikuwa limeingia.

    Nyambura akachagua twende katika ofisi yangu!

    Tukaenda, nikataka kuketi katika kiti cha wageni akanizuia na kunisihi nikalie kiti changui.

    Nilipoketi akazungumza.

    “Nakupenda sana Joshua. Nafsi yangu inajua, mwili wangu unajua, na ulimi wangu haudanganyi!”

    Akasita, chozi likamtoka!

    Mariam akawahi kumpatia kitambaa, Nyambura akakikataa.

    Sasa alikuwa anayumbayumba kiasi, bila shaka sasa pombe zilikuwa zimeanza kukikung’uta. Akaketi na kunitazama kwa muda.

    “Je unaweza kuzungumza sasa….” Mariam alimuhoji Nyambura.

    “Na wewe upo tayari kusikiliza?” naye Nyambura akanihoji mimi ghafla, nikatikisa kichwa kukubali.

    Wakati wote huu nilikuwa najiuliza kuwa inamaana Nyambura amejua kila kitu nilichokuwa nafanya, kuhusu kwenda kwa mganga na mengineyo ya kutaka kuwamilikisha kampuni yangu ikiwa ni makubaliano kwa kunipa mtoto.

    Wazo hili lilinifanya nijisikie aibu na kukosa ujasiri wa kufanya lolote lile.

    Sikuwa najiamini, hivyo nikabaki kuwa msikilizaji tu.

    Nyambura akasimama na kufika ukutani, akaigusa kalenda huku akitembeza kidole chake hadi akaifikia tarehe aliyoihitaji.

    Tarehe kumi na tano!

    Akaitaja kisha akanigeukia.

    Akanitazama kwa jicho kali.

    “Joshu…a… Na.. nakup..en..nda!” akabwabwaja maneno haya huku mwili wake ukilainika na kutua chini kama mzigo hakuna aliyewahi kumdaka.

    Hapo sasa ikawa hekaheka tena.

    Hekaheka ya kumpepea Nyambura, lakini hakuna kilichosaidia.

    Tukalazimika kumuwahisha hospitali.

    “Alikuwa anataka kusema nini?” nilimuuliza Mariam ambaye kwa mara nyingine alikuwa akiendesha ile gari.

    Mariam akadai kuwa anachotaka kukisema Nyambura anakijua yeye mwenyewe Nyambura.

    Jibu lake lilinivuruga sana.

    “Na wewe ni nani hasa, maana sielewi.”

    “Mimi ni Mariam Sumra, nielewe hivyo.” Alinijibu kwa mkato huku akiongeza umakini barabarani.

    Safari ya kumpeleka Nyambura hospitali.
    Wakati safari inaendelea, simu yangu iliita.

    Kutazama ilikuwa nambari mpya, nikapokea upesiupesi nikitarajia kuwa watakuwa wale wavaa nguo nyeupe wanataka kunipa maelezo mengine, nami nilikuwa tayari kujitetea.

    “Joshua mwanangu, haujambo!” ilikuwa ni sauti ya mama yangu mzazi.

    Nilipagawa sana.

    “Mama.. mama upo wapi? Upo wapi mama?” nilimuuliza.

    “Nipo Morogoro ila sijui panaitwaje hapa hata. Nimeazima simu ya mtu tu, naomba umtumie pesa humu nifanye nauli kurudi Dar es salaam Joshua! Yaliyonikuta ni makubwa…” alizungumza mama kwa sauti iliyotia huruma sana. Nilimjua mama yangu vyema ni mtu wa kujikaza lakini hadi kuongea kama anavyoongea basi kuna jambo zito.

    Mwili ukaingiwa ganzi.

    Nikamsihi abaki na ile simu nampigia kumpa maelekezo zaidi.

    Nilipokata simu nikaanza kupambana kutafuta majina katika simu yangu, nilikuwa nimechanganyikiwa sana nisijue ni jina la nani natafuta.

    “Nani huyo mama? Au!” aliniuliza yule binti bila kuonyesha kushtuka.

    Nikamjibu ndiye.

    “Mchezo unaelekea ukingoni.” Akazungumza kwa sauti ya chini.

    “Mchezo? Mchezo gani?” nilimuuliza.

    “Mtumie mama anachotaka umtumie….” Alijibu kitu kingine.

    Wakati nazama katika taharuki mpya, akamalizia kunijibu.

    “Kila kitu anajua Nyambura sio mimi.”

    “Na mama anasema yupo Morogoro, wakati walisema yupo Zambia sijui.” Nilijiuliza huku nikihisi kuna mchezo nachezewa.

    “Joshua hizi nyakati huwa haziepukiki, nyakati za kugeuzwa gunia!”

    “Gunia?”, “Gunia kivipi?”

    “Kila mmoja anakufanyia mazoezi, kila mmoja anakupiga na wala hauwezi kurusha ngumi hata moja. Kwani gunia linapenda kufanywa vile?” alinijaza katika fumbo nikashindwa kuelewa maana yake ya moja kwa moja.

    Nilipojaribu kupiga simu ambayo awali mama aliitumia haikuwa inapatikana tena.

    Huku mama hapatikani, na miguuni mwangu Nyambura akiwa amepoteza fahamu.

    Haya yakiwa hayajanichanganya vizuri, Agness akaamka na kuanza kulia kilio kitakatifu!

    Bila shaka alikuwa akihitaji titi la mama yake.

    Muunganiko wa haya mambo ukanifanya nami niaanze kulia kama mtoto mdogo tena.

    “Acha ujinga Joshua! Bembeleza mtoto….” Mariam Sumra mwenye tabia nisizozielewa alinipa kauli iliyonitikisa.

    Mbona kama naye ananigeuza gunia!? Nilijiuliza.

    Nikataka kumkaripia lakini nikaona ni heri niendelee kumbembeleza mwanangu.

    Kadri safari ilivyokuwa ndefu nikaanza kugundua jambo jingine lisilokuwa la kawaida hata kidogo.

    Hapakuwa na safari ya kuelekea hospitali, tulikuwa tunaelekea mahali nisipopajua kabisa.

    Kwanini tuelekee huku!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mariam Sumra! Ni wapi tunaelekea?” nilimuuliza.

    “Mbembeleze mtoto Joshua…. Acha upuuzi.” Alinijibu.

    Nadhani jibu lake lilizua kimya ambacho hata Agness mtoto wangu alikigundua, akanyamaza kimya ghafla!

    Hali ilikuwa tete!!


    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog