Search This Blog

Sunday, 19 June 2022

MJI TULIVU ULIONIPA UGONJWA WA MILELE - 3

 





    Simulizi : Mji Tulivu Ulionipa Ugonjwa Wa Milele

    Sehemu Ya Tatu (3)





    MKE wangu bila kujua kuwa mumewe nilipitia njia za mkato katika kusababisha ile mimba ipatikane alinisihi sana twende kumpa zawadi yule daktari ambaye alituwezesha hadi nikapona na kuweza kumjaza mimba.

    Nafsi ilinisuta sana siku tuliyofunga safari hadi kwa daktari kwa ajili ya kumpatia zawadi ambayo haikuwa stahiki yake.

    Lakini ningeanza vipi kukataa mbele ya mke wangu?

    Kama ningekataa kwenda basi nilitakiwa pia kuwa tayari kumweleza kuwa ile mimba chanzo ni nguvu za giza.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Sikuwa tayari!!

    Kwa daktari napo zikanitoka pesa taslimu shilingi laki tano kama asante kwa daktari, akatupongeza huku akimsihi Nyambura ajitahidi kuhudhuria kliniki mara kwa mara ili aweze kuimarisha afya yake na ya mtoto ambaye hajazaliwa bado.

    Kwa sababu aliyetusaidia ni daktari yule basi tukaamua pia kliniki kufanyia kwake.

    Pesa zikaendelea kukatika tu!

    Roho iliniuma sana kuiona ile nusu milioni ikiteketea kwa mtu asiyehusika nayo hata kidogo.
    Ujauzito ulipofikisha miezi mitatu, mama yangu akahamia rasmi nyumbani kwangu kwa ajili ya kufanya uangalizi wa karibu kabisa kwa mkamwana wake. Jambo hili lilinifurahisha sana, mama yangu alikuwa mtu wa kujali siku zote.

    Kabla sijaoa aliwahi kuniambia kuwa hata nikikukataza kuoa kabila fulani lakini ukaamua kuoa kwa sababu zako mwenyewe nitampenda kwa dhati mkeo!!

    Sasa yalikuwa yanatimia.
    Siku tatu za mama kukaa pale nyumbani, aliniita siku moja na kunieleza kuwa alipoingia tu pale ndani na kutazamana na Nyambura amesisimka vibaya mno, vinyweleo vimemsimama na amekosa raha kabisa. Kauli ya mama ilinishtua sana, nikajisemea kuwa utu uzima dawa labda mama ametazamana na kile kiumbe ambacho kimepatikana kwa sababu ya nguvu za giza.

    Lakini sikuwa tayari kukiri kuwa kuna tatizo mahali, nikaendelea kupigana hii vita dhidi ya wanaonitazama na dhidi ya nafsi yangu mwenyewe!

    Nilimwondoa mama hofu kabisa na kumweleza kuwa aondoe mashaka hakuna kitu kibaya kinachoendelea pale.

    “Joshua wewe ni mwananngu wa kumzaa kabisa wala sijapewa na mtu kumlea…. Nimekwambia nilichohisi. Sasa usije ukayabeba na kuyapelekwa kwa mkeo akaanza kunichukia. Wewe ni mtu mzima sawa baba!” alinieleza mama huku akinishika shika bega langu kirafiki kabisa.

    Nilijisikia hatia sana, nikaamini kuwa chanzo cha mama kusisimka ni kitendo cha mimi kwenda kwa mganga na kufanikiwa kupata uwezo wa kumpa mimba mke wangu.

    Nisingeweza kumwambia mama, zaidi nilikuwa naombea tu isijekuwa kituko mtoto atakapozaliwa… niliombea iwe heri tupu.

    Lakini nilijionya kuwa si kila uombalo hutimia kama lilivyo!
    Mama aliendelea kuwa karibu kabisa na Nyambura, akimpa ushauri wa hapa na pale na wakati mwingine kumpikia pale anapopatwa na hamu ya kula.

    “Nyambura, ulinidekeza sana ulipokuja kule kijijini wakati naumwa… sasa ni zamu yako. Yaani nidekee kuliko anavyodeka mtoto wa mwisho, wewe ndo mkamwana wangu wa pekee….” Niliwahi kumsikia mama akimwambia Nyambura, nilifurahi sana kuona mama anaelewana vizuri kabisa na mke wangu.

    Miezi sita ikakatika, mama akanijia tena kwa mara nyingine safari hii ilikuwa ni ndoto. Akanisimulia ile ndoto ilikuwa inatisha lakini niliamua kuipokea kama ndoto, alinieleza kuwa aliona katika ndoto mke wangu anazaa lakini nilipotaka kumchukua mtoto akamkatalia na kumpa mwanaume mwingine. Ukazuka ugomvi na mwisho wa siku yule mtoto akaanguka chini na kupasuka kichwa akavuja damu hadi akafa mimi nikakamatwa na kupelekwa polisi kwa kesi ya kushiriki katika mauaji…

    Kwa mara nyingine nilijichekesha na kumwondoa mama hofu. Nilimwambia anaota ndoto hizo kwa sababu anawaza sana juu ya mapokeo ya mjukuu wa kwanza.

    “Usijisikie vibaya mwanangu, mimi nakueleza kwa sababu tu nakupenda na sitaki siku moja nikwambie eti niliwahi kuota, ni bora niiseme tu hii ndoto ijiondokee zake” aliniambia mama yangu kwa upendo mkubwa.

    Kisha akaelekea chumbani kwa Nyambura kumjulia hali.

    Hofu ikaanza kunikaribia hasahasa kulingana na haya maneno ya mama na njia nilizotumia kumpata mtoto yule mtarajiwa. Lakini nilijipa moyo kuwa ndoto itabaki kuwa ndoto tu haiwezi kuwa na madhara yoyote.

    Nikaendelea kufanya kazi kwa bidii ili kutengeneza kipato kikubwa kwa ajili ya familia yangu.

    Hatimaye ikatimia miezi tisa, mke wangu akajifungua salama kabisa mtoto wa kike!!

    Mtoto alikuwa mwenye afya tele, nisiwe mwongo mtoto alimfanana sana mama yake.

    Ilikuwa ni furaha kubwa sana kwetu, hasahasa mama ambaye alimnyanyua juu mjukuu wake kwa mara ya kwanza. Akamuombea dua kabla ya kumkabidhi kwa mama yake.

    Tukamuita mtoto Agness, jina la hayati mama yake Nyambura.

    Juma moja likapita nikaona nisifanye mzaha kusubiri kupigiwa simu na mganga, nikaamua kwenda mwenyewe kwa sababu mizimu ilihitaji kitu kutoka kwangu baada ya kunifanikishia kupata mtoto.

    Nilimkuta mganga akiwa anatabasamu, kabla sijasema lolote akanipa hongera kwa kupata mtoto wa kike.

    Nilishangaa amejuaje juaje? Lakini sikumuuliza akanikaribisha ndani nikaketi na kumweleza nia yangu.

    Akanieleza kuwa mizimu inapokea zawadi na kuzungumza na marafiki siku ya ijumaa usiku pekee, hivyo natakiwa kufika pale siku ya ijumaa nisikie mizimu inasema nini.

    Siku ile ilikuwa ni jumatano, nikamuachia mganga posho kidogo na kuahidi kuwa nitafika hiyo ijumaa.

    “Hata jina mlilomchagulia ni jema sana…. Agness naamini mizimu italipokea vizuri!” alinieleza wakati ananiaga….. nilishtuka sana kuwa mganga huyu amekuwa mwepesi sana kugundua kila kinachoendelea katika maisha yangu.

    Je? Haitakuwa hatari sana kwangu pindi wakiamua kumdhuru mtoto wangu!! Nilijiuliza kwa mashaka huku nikiondoka.

    ______

    Niliona siku kama haziendi kabisa, nilitamani kumalizana na mizimu kabisa ili niwe huru na mambo yangu hasahasa kumlea mtoto wangu na ndoa kwa ujumla.

    Ikawa usiku ikawa mchana ikawa usiku tena kukakucha, ijumaa ikafika.

    Niliwahi sana ofisini na kufanya shughuli zangu zote za muhimu, nikawagawia watu majuukumu. Na mwisho wa siku nikaondoka majira ya saa kumi, nikawasili nyumbani majira ya saa kumi na moja. Nikamwona mama na Nyambura wakifanya mazoezi ya kutembea, nikautazama ule upendo wa mama yangu kwa Nyambura nikamshukuru Mungu kwa kunipa mama yule.

    Nikaingia ndani na kubadili nguo kisha nikaaga kuwa naenda kuonana na wadau fulani kuna jambo kubwa tunataka kulifanya hivyo tunaenda kujadiliana. Kibindoni nikiwa nimebena pesa taslimu shilingi milioni tatu.

    Niliamini mizimu itaomba pesa.

    Nyambura alinisihi sana nisiende anatamani niwe pembeni yake, lakini haikuwezekana nisingeweza kuacha wakati ndo siku pekee ya kuzungumza na mizimu.

    Nilimbembeleza hadi nikaondoka, nikambusu Agness shavuni na kuondoka.

    Moja kwa moja hadi kwa mganga!

    Mganga alinipokea vyema, akaniambia niliache gari nyumbani kwake na sisi twende kwa miguu akasema si mbali sana, na hata kama ni mbali hatuwezio kwenda kuipigia mizimu kelele kwa kuitembelea tukiwa na gari.

    Hapo ilikuwa ni saa tano usiku safari ilipoanza.

    Tulitembea kwa mwendo wa saa zima hadi kulifikia eneo la tukio, lilikuwa ni shamba kubwa ambalo lilikuwa halina mazao yoyote, tukajongea hadi pale, mganga yule akaanza kupiga manyanga yake huku akizungumza lugha nisiyoijua.

    Mwisho zikaanza kusikika ngurumo na mwanga mkali kutoka katika mti mmoja katika lile shamba. Nilikuwa natetemeka sana, hapo kabla sikuwahi kukutana na mizimu……

    Sasa leo naja kuzungumza nayo!

    “Mizimu imeshuka tayari… sasa nakuacha uzungumze nayo. Hili halinihusu mimi….” Mganga aliniaga huku akitaka kuondoka, nikamzuia.

    “Sasa lugha nitaielewaje…” nilihoji kwa mashaka

    “Ni Kiswahili, kuwa makini katika kujibu tafadhali usije kuiudhi mizimu… ukiwaudhi umeniua na kujiua wewe mwenyewe na ukoo wako.” Alinionya.

    Nikabaki kungoja, ule mwanga ukaanza kufifia kiasi kisha kikatoka kibabu kizee kikiwa na mkongojo.

    “Kijana wangu Joshua.. karibu katika ulimwengu wetu…” alizungumza kikongwe yule.

    “Nimeagizwa kama mwakilishi, nimeambiwa kuwa tayari umepata kile tulichokuahidi… na sasa ni zamu yetu kukuona wewe ukitimiza ahadi yako.” Nikatikisa kichwa kukubali, kikongwe yule akaendelea.

    “Sogea… sogea hapa…” aliniamrisha. Nikasogea hadi alipokuwa, akanionyesha bahasha fulani nyekundu, akaniambia niiokote.

    Bahasha ile haikuwepo hapo kabla!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Wazee wameandika kila kitu. Utasoma na kama kuna maswali utamuuliza aliyekuleta hapa kisha akatuita nasi tukashuka.” Alimaliza kisha mwanga ule ukang’ara ukinimulika machoni, ngurumo zikasikika na ulipotoweka ule mwanga yule kikongwe hakuwepo.

    Nilitishika sana kwa sababu yale yalikuwa mauzauza taslimu.

    Nikiwa nimeganda pale na bahasha yangu alifika yule mganga akanishika mkono tukaondoka… moja kwa moja hadi nyumbani kwake.

    Alinionya nisiseme lolote kuhusu kilichotokea hadi tutakapofika nyumbani, hivyo njia nzima kila mmoja alikuwa kimya.

    Hatimaye tukafika!

    Tukaifungua bahasha na kuisoma vyema nini matakwa ya mizimu.

    Nilirudia kuisoma mara mbilimbili hakuna kilichobadilika, walichohitaji ndo kile nilichokuwa nakiona pale katika maandishi yale machache.

    Niliishiwa nguvu, tumbo likaanza kuunguruma na kichwa kuniuma sana.

    Nikampa yule mganga asome upya na kunielewesha. Na yeye akaona vile nilivyoona mimi!

    Kichwa kikazidi kuuma, sikuamini hata kidogo kuwa niliposema kuwa nitatoa zawadi yoyote ingewezekana kuwa hii waliyoomba.

    Nilitamani nyakati zinisaidie kwa kurudi nyuma ama kunifanya niwe ndotoni ili niamke na kuachana na maono haya.

    Lakini hapakuwa na ndoto!

    Maandishi yalikuwa yameandikwa kwa kalamu nyekundu iliyokolea.

    Halikuwa ombi bali amri!
    *****************


    NILIRUDIA tena kuisoma karatasi ile iliyoandikwa kwa wino mwekundu, na mganga naye akarudia kuisoma.

    Nilichanganyikiwa sana….

    Mganga akanisihi niende nyumbani nikafikirie kwa kina kisha tutaonana siku inayofuata kwa sababu nilipewa siku saba za kufanya utekelezaji basi zinatosha sana kwa ajili ya kutuliza akili kufikiria kwa kina na kufanya maamuzi yaliyo sahihi.
    Nilimweleza kuwa siwezi hata kuendesha gari nahisi nikiendesha nitapata ajali, akaniambia kama inafaa basi nilale nyumbani kwake.

    Nikamweleza haitawezekana kwani mke wangu hawezi kulala bila mimi kurejea nyumbani.

    Akafikiri kwa muda kisha akanifanyia msaada mmoja, akaniendesha hadi nyumbani kisha yeye akarejea nyumbani kwake kwa kutumia usafiri wa pikipiki.

    Kweli nilimkuta Nyambura hajalala alikuwa sebuleni anatazama runinga.

    Aliponiona akanifuata na kunikumbatia huku akinipa pole kwa uchovu.

    “Mbona unatetemeka hivi?” aliniuliza.

    “Kichwa kinaniuma sana ghafla… sijui malaria hii?” nilitoa jibu la uongo.

    Nyambura akanishika kiuno akanikongoja hadi chumbani, akanivua shati na viatu, kisha suruali yangu na mwisho akanipeleka hadi bafuni tukaoga pamoja, huku akinipa pole kedekede na kunifariji.

    Mke wangu alikuwa ananipenda sana jamani!

    Alinifariji sana hadi nikasahau kuwa nina balaa linanikabili, masharti kutoka kwa wazee wa mizimu.

    Tulilala akiwa amenikumbatia, alipopitiwa na usingizi nikajitoa katika mikono yake na kuanza kutafakari upya juu ya maombi ya wazee.

    Maombi ambayo sikuwahi kufikiria hata kidogo kuwa mizimu ingeweza kuomba.

    Nilijisahau kabisa na kuwa muoga wa kutoa kafara ama zawadi yoyote inayohusisha damu, mizimu ikanikubalia nami nikajitapa kuwa siwezi kushindwa kutoa zawadi nyingine watakayohitaji.

    Nilijua watahitaji pesa!

    Haikuwa!

    “Kampuni yangu iwe yao, na pesa zilizopo benki ni mali yao na nisiziguse kuanzia dakika hiyo niliyopokea barua…” nilikumbuka baadhi ya maneno katika ile barua.

    Milioni mia moja na sabini!!

    Nilikikumbuka kiwango cha mwisho cha pesa nilichokiacha katika akaunti ya kampuni, halafu ilikuwa kiherehere changu tu, kuhamishia pesa kutoka katika akaunti yangu binafsi kwenda kwenye akaunti ya kampuni.

    Sasa pesa zote zile ni mali ya mizimu, na si pesa tu bali kampuni yote kiujumla. Na kati ya hizo pesa katika kampuni, milioni mia moja nilikuwa nimekopa benki kwa kuweka dhamana hati ya nyumba yangu niliyokuwa nimejenga.

    Pagumu hapo!

    Nilipagawa nikaketi kitako, nikaminyaminya kichwa changu huenda nikapatwa na fikra mpya lakini hakuna nilichoambulia. Ukweli ulibaki uleule kuwa nilikuwa katika mtihani mmoja mzito sana na nilikuwanazo siku saba tu za kufanya utekelezaji.

    Nikajaribu kukumbuka labda kuna sehemu ambayo inahusu kipingamizi katika barua ile lakini haikuwepo, hivyo lile halikuwa ombi bali amri.

    Kutambua kuwa ile ni amri kulinifanya nikanyong’onyea zaidi….. Mizimu ilikuwa imenikamata pabaya mno.

    Sikuwa na njia mbadala ya kufanya jambo lolote.

    Nilipitiwa na usingizi baadaye hata sikumbuki ilikuwa saa ngapi.

    Asubuhi majanga yakaendelea.
    Mama Agy alikuwa anaumwa mgongo. Alipiga mayowe kadri maumivu yalivyokuwa yanazidi.

    Mama akatoka mbio kuja kumtazama, huku akinihimiza kumpeleka hospitali.

    Nilimbeba mama Agy hadi katika gari, mama akambeba Agy mwanangu, nikaendesha kuelekea hospitali. Tayari nilikuwa nimempigia simu daktari yule yule aliyemsimamia Nyambura hadi alipojifungua.

    Wauguzi walimpokea Nyambura na kumkimbiza katika wodi ya wazazi, huko alifanyiwa vipimo na kilichofua hapo ni pesa moja baada ya nyingine.

    Hadi siku inaisha na Nyambura kupata nafuu na kuruhusiwa kurudi nyumbani nilikuwa nimetumia kiasi cha shilingi laki mbili kasoro senti chache.

    Akiba iliyobaki ilikuwa shilingi laki moja na nusu pekee.

    Hii ndo pesa iliyokuwa mfukoni, kumbuka kuwa mizimu ilitopa tamko kuwa sitakiwi kutoa walau senti tano katika akaunti ya kampuni yangu.
    Nilianza kutetemeka, hasahasa nilipokumbuka kuwa sitaruhusiwa na mizimu kutoa walau senti tano katika akaunti yangu. Na pia sikutakiwa kusimamisha shughuli za ofisi.

    Jioni majira ya saa kumi na mbili baada ya kumrejesha Nyambura nyumbani, simu yangu iliita na ilikuwa ni namba binafsi ya katibu muhtasi wangu.

    Alinieleza mambo kadhaa juu ya siku nzima ya ofisini, kwa sababu ilikuwa ni siku ya jumamosi ofisi yetu ilikuwa inafungwa saa saba mchana.

    Akanieleza kuwa siku ya jumatatu kuna pesa tunatakiwa kuingiza kwenye akaunti ya kituo kimoja cha runinga kwa ajili ya kulipia tangazo ambalo huwa linarushwa katika kituo chao.

    “Ni shilingi ngapi?” nilimuuliza.

    “Ni laki saba wametupunguzia awali walisema milioni moja.” Alinijibu.

    Nilisikia kama lugha za kichina zinaniingia masikioni na nisielewe zina maana gani hata.

    Laki saba? Naitoa wapi mimi…. nilijiuliza

    Ni kweli ilikuwa ni pesa ndogo sana katika milioni mia moja sabini zilizokuwa katika akaunti.

    Lakini siruhusiwi kuzitoa ama la nizitoe na kukutwa na mabalaa makubwa.

    Mfukoni nilikuwa na shilingi laki moja na nusu.

    Nikamweleza katibu muhtasi kuwa nimemuelewa, tukaagana akakata simu.

    Wazo la kukopa likanijia kichwani mwangu.

    Nikamfikiria Revo, kweli akanikopesha shilingi laki tano.

    Lakini haikufaa kitu, matatizo yalikuwa mengi sana, nikajikuta hadi jumatatu inafika nikiwa na shilingi laki nne tu.

    Nilijitahidi kutoa matumizi yaleyale ya siku zote nyumbani kwangu kwa sababu sikutaka mtu yeyote agundue kuwa kuna utofauti.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nilikuwa naugulia ndani kwa ndani.

    Mtoto nilikuwa nampenda na aliniletea heshima lakini kwa hali ilivyokuwa nikajikuta taratibu natamani nyakati zirudi nyuma ningoje muujiza wa Mungu tu niweze kupata mtoto.

    Lakini shida ni kwamba nyakati haziwezi kurudi nyuma kamwe. Tayari nilikuwa nimejiingiza katika janga la mizimu, njia ambayo hata haikuhitaji kiwango chochote cha elimu kutambua kuwa haikuwa njia sahihi.

    _____
    UBAYA wa mawazo ni kwamba unaweza kuwaficha wengine lakini sio kuuficha mwili wako uliokubeba, ukiwaza sana mwili nao unanyauka.

    Naam! Nikaanza kupungua, zilikuwa ni siku chache tu lakini nilionekana dhahiri kuwa sikuwa sawa hata kidogo.

    Nikiwa bado natafakari ni kitu gani nitafanya, Nyambura mke wangu ananipa rungu jingine katika utosi wangu.

    Ananipa nambari za mtu nimuwekee kiasi cha shilingi milioni nne, amchukulie mzigo katika biashara waliyokuwa wanafanya ili aendelee kumzungushia asijekusahaulika katika biashara hiyo aliyokuwa anafanya..

    Akanieleza kuwa anatamani angeenda benki kujichukulia pesa katika akaunti yake lakini hajioni kama yupo sawa.

    “Usijali mke wangu, wewe haujawa wa kutembea bado… nitakufanyia usijali.” Nilimjibu huku moyo wangu ukipiga kwa nguvu sana kana kwamba nilikuwa nimekamatwa ugoni.

    Hiki nini Mungu wangu!! Nilijiuliza baada ya kujifungia chumbani, kama laki saba ya matangazo ilikuwa mbinde kuipata, vipi kuhusu hii milioni nne?

    Machozi yakaanza kunitoka, jasho nalo halikubaki nyuma.

    Nilikuwa mwenye hofu!
    Siku zikasogea na hatimaye zilibaki siku mbili sawa na masaa arobaini na nane kabla sijakutana na wazee na kuwakabidhi kampuni yao pamoja pesa zote katika akaunti.

    Ahadi yangu ilikuwa inanihukumu mchana kweupe!

    Nilichanganyikiwa sana, nikaiona dunia inanionea, nilitamani kumshirikisha mtu lakini ingesaidia nini na mizimu imesema hilo sio ombi bali ni lazima.

    Mara kwa mara mama alinieleza kuwa kuna jambo nawaza na linanipelekesha puta sana akanisihi nimweleze lakini sikuwa na ujasiri huo nikaishia kumpiga danadana tu!

    Hatimaye siku ya tukio ikawadia!!
    NAKUSIHI

    Kamwe usitoe ahadi wakati ukiwa na hasira pia usitoe ahadi wakati umechoka na ninakukumbuka kuwa usifanye maamuzi wakati una furaha kubwa.

    Kwa asilimia tisini ahadi hizo utazijutia! Hata kama hautajuta mbele ya watu….

    Moyoni utakuwa shuhuda!


    ***************


    Kila mtu hufanya makosa katika Maisha, lakini haimaanishi kuwa lazima yamgharimu maisha yake yote.

    Wakati mwingine watu wema hufanya uchaguzi usio sahihi (mbaya) hii haimaanishi kuwa ni watu wabaya, ila inamaanisha kuwa ni Binadamu.

    Kubali kukosea na ujifunze kukosolewa! "


    KABLA ya kwenda kwa mganga nilimpigia simu na kumueleza kuwa kama inawezekana aiombe mizimu inivumilie kwa siku walau nne mbele kwa sababu bado mwanasheria wangu alikuwa anaandaa nyaraka maalumu kwa ajili ya kuuza hisa zangu kwenda kwa mtu mwingine.

    Nilimueleza kwa kirefu sana huku nikiwa natetemeka, akaniambia kuwa atanipigia baada ya muda.

    Ikawa hivyo, akanipigia baada ya robo saa kupita akanieleza kuwa ili aende kuzungumza na mizimu hawezi kwenda mikono mitupu. Akanitajia mahitaji ya kwenda kuonana na mizimu.

    Akanitajia mbuzi mweusi, mafuta ya nazi lita moja, nazi saba na makorokoro mengine mengi.

    “Ambavyo ni sawa na shilingi ngapi?” niliuliza kinyonge huku kichwa kikiwa kinaniuma sana, kwa wakati ule kitu chochote kiitwacho pesa kilikuwa kinaniumiza sana kichwa!

    Kila ikitajwa pesa nakum,buka masharti ya mizimu iliyonipa mtoto juu ya kampuni yangu.

    “Laki moja na elfu ishirini.” Alinijibu kwa sauti kavu kabisa.

    Nikakata simu huku kijasho chembamba kikinitoka.

    Nikafikiria ni wapi tena pa kukopa.

    Nikatafuta majina katika simu yangu na hatimaye nikampigia bwana mmoja kutoka katika mojawapo ya makampuni niliyowahi kufanyanayo kazi. Ni bwana ambaye tulikuwa tunaheshimiana sana, hata kama hatanipatia pesa ninayohitaji lakini anaweza kunipa walau nusu yake.

    Nikamweleza shida yangu ya pesa, nikataja kiasi kuwa nina haja na shilingi laki tano.

    Akaniahidi kuwa atanitumia ndani ya saa moja, akatimiza ahadi yake!!

    Nikatuma kiasi alichohitaji mganga ili aniombee kwa mizimu niongezewe siku, kiasi kilichobaki nikafanya matumizi ya nyumbani.

    Jioni kabisa mganga akanieleza kuwa mizimu imenielewa na imenipa hizo siku tano nilizoomba zaidi ya hapo hapatakuwa na muda wa ziada.

    Nilishukuru sana, nikamtumia elfu hamsini kama shukrani.

    Akanieleza kuwa haikuwa shughuli nyepesi hata kidogo kuishusha mizimu ili imsikilize.
    Walau amani yangu ilirejea japokuwa haikuwa amani ambayo ingedumu kwa siku nyingi.

    Kutambua kuwa mizimu imenielewa basi hata tabasamu bandia usoni niliweza kulipachika.

    Baada ya kuhemea vitu kwa ajili ya nyumbani, nikarejea katika makazi yangu, nilimkuta mama amelala kwenye mkeka sebuleni, sikutaka kumsumbua nikanyemelea hadi chumbani niweze kumshtua kidogo mke wangu na tuweze kutaniana kidogo. Kwani ni siku nyingi nilikuwa sijamtania kwa sababu ya ule msongo mkubwa wa mawazo

    Nilinyemelea hadi mlangoni, nikamsikia mke wangu anazungumza na simu.

    Nilitulia pale mlangoni nikisubiri amalize kuzungumza, mazungumzo yake hayakunishangaza sana kwa sababu alikuwa anazungumzia masuala ya paspoti huku pia akijadili kuhusu nauli na mtu ambaye alikuwa anazungumza naye. Nikatambua kuwa alikuwa anazungumza na wafanyabiashara wenzake, sema kuna jambo jipya nililisikia, aliuliza kuwa akisafiri na mtoto mchanga haitakuwa na madhara?

    Sijui upande wa pili ulijibu nini…CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mazungumzo haya yakanikumbusha kuhusu pesa ambazo Nyambura alikuwa ameniomba nimtumie mtu wanayefanyanaye biashara na nilikuwa sijafanya hivyo bado!

    Mwili ukaingiwa uvivu!

    “Sasa Nyambura anataka aanze kusafiri na Agy mapema hivi…” niliwaza, kisha nikatulia alipomaliza kuongea nikagonga mlango….

    Akaitikia nikafungua na kuingia.

    Macho yangu na ya Nyambura yakagongana… nikasisimka vibaya mno.

    Msisimko huu ukanikumbusha ule msisimko ambao mama yangu mzazi alinieleza kuwa aliwahi kuupata siku ya kwanza kutazamana na Nyambura wakati akiwa mjamzito.

    Kuna nini? Nilijiuliza…..

    Lakini mara zote hizi nilikuwa najitupia lawama mimi mwenyewe kuwa huenda kisa cha yote haya ni yule mtoto wa mizimu. Nilimkumbatia na kumbusu kisha nikambusu na mtoto, nikampatia Nyambura zawadi niliyomnunulia mjini. Akashukuru kwa kunibusu.
    Baadaye kidogo nikamsikia mama anaimba nikatambua kuwa ameamka tayari nikamuaga Nyambura kuwa naenda kumsalimia mama.

    Mama aliponiona nikiwa nimevaa fulana aliniita kwa ukaribu zaidi, akanisihi niketi, hapo hata salamu yangu hajajibu.

    “Una nini Joshu mwanangu, zungumza na mimi… mimi ndiye mama yako. Wala hauna mama mwingine…..una tatizo gani” alinihoji, nikiwa bado sijapata neno la kusema akaendelea.

    “Huu sio mwili wako baba, umekonda sana Joshua. Unawaza nini.. hebu niambie mwanangu. Ni mimi niliyekubeba miezi tisa tumboni mwangu, nikawa mkweli kwako hata wakati ninakulea sasa umekuwa mtu mzima hebu nawe kuwa mwaminifu kwangu. Una nini?” alinihoji zaidi

    “Mama ni biashara tu haziendi vizuri lakini eti kusema kuna kitu nakuficha. Walaa!” niliongopa huku nafsi yangu ikiingia katika mfadhaiko mkubwa sana.

    Kumdanganya mama!!

    Lakini ningefanya nini unadhani….

    Mama akanitazama kwa huruma, kisha akaniambia kuna kitu anataka kunipatia.

    Akainuka na kujikongoja hadi jikoni, akarejea akiwa na kibakuli. Akanipatia.

    Nikafunua na kukutana na mlenda pori.

    Zawadi hii ya mama ikawa imenikumbusha mbali sana. Enzi ambazo nilikuwa naishi maisha magumu kupita kawaida pamoja na familia yangu.

    “Nilijitahidi sana niwe nachuma mboga hiyo ili mle muishi, nilikuwa muaminifu sana kwenu! Ni Mungu tu ndiye shahidi ikiwa nyie mtakataa kushuhudia hilo, siku ambapo mboga ilikosekana niliwalaza miguuni mwangu nikawaambia ukweli kuwa siku hiyo tunalala njaa mvumilie.

    Nilikuwa mkweli sana Joshu! Mkweli kwa sababu mimi ni mama yenu niliyewazaa….. kula huo mlenda Joshu na kama ukiendelea kuwa mkaidi kwangu, mi nitamuachia Mungu! Haupo sawa mwanangu.” Alimaliza mama akaniacha pale, nilijaribu kunywa ule mlenda lakini haukupita kooni.

    Mama alikuwa amenisema na kuugusa sana moyo wangu.

    Lakini nitaanzaje mimi kumweleza mama kuwa nilienda kwa waganga na sasa nadaiwa??

    Mgogoro wa nafsi ukanichukua, ukanikabaa koo na kuanza kunipiga makonde mazitiomazito mfululizo!

    Niliteseka sana!

    ___
    Siku iliyofuata nilienda kwa mwanasheria wa kampuni yangu na nikamueleza nia yangu ya dhati ya kuuza asilimia 90 ya hisa zangu.

    Alishangaa sana ni taarifa ambayo hakutarajia kuisikia kutoka katika kinywa changu, yaani kwa jinsi nilivyopambana hadi kuifikisha kampuni katika kilele kile cha mafanikio eti ghafla ninauza hisa zote.

    “Joshua unataka kuhama nchi nini?” aliniuliza, nikabaki kujichekesha tu.

    “Halafu umepungua balaa… una matatizo yoyote rafiki yangu”

    “Tatizo langu ndo hilo moja tu, ninahitaji kuuza hisa za kampuni yangu hivyo nahitaji uniandalie uthibitisho wa kisheria juu ya jambo hili.” Nilimjibu bwana yule, akabaki kuniangalia hata asinimalize.

    Nikaondoka nikiwa nimemsisitiza kuwa jambo hilo lisizidi siku mbili.

    Akakubali….
    ____
    Niliporejea nyumbani majira ya saa mbili usiku, nilimkuta mama sebuleni. Haikuwa kawaida yake kuwa macho hadi muda huo.

    “Nilikuwa nakusubiri Joshua..” aliniambia punde tu baada ya kukanyaga pale sebuleni.

    “Joshua mwanangu, sina amani katika nafsi yangu na ninadhani nikiendelea kuishi hapa nitaugua na kukuletea shida wakati mkeo ana mtoto mnalea sitaki niwe mzigo.” Alisita akanitazama, kauli yake ikanifanya nisogee na kuketi jirani naye na kumuuliza kulikoni.

    “Joshua mwanangu mimi ni mama yako halali, nimekulea hadi ukajitambua, nakujua kuliko wewe unavyodhani unajijua… kuna tatizo unalo linakukabili na hutaki kunishirikisha mimi mama yako, nimekosa amani kabisa na kuona kuwa sina stahiki tena katika maisha ya mwanangu. Naomba unipatie nauli Joshua mimi asubuhi nitarudi kijijini….” Mama alizungumza huku sauti yake ikikwama kwama katika mirindimo iliyoashiria kuwa yupo katika hatua za mwisho kabisa kuelekea kuangua kilio.

    Mungu wangu! Yaani mama alie mbele yangu na sababu nikiwa mimi!? Nilihamanika vibaya mno.

    Nilijisikia vibaya sana kwa kauli ile ya mama yangu, nikajiona jinsi gani simtendei mama yangu mzazi haki.

    Kusema nimpe nauli aondoke nadhani hii ingemuongezea mawazo labda angeondoka pale na wazo kuwa mimi na mke wangu tulikuwa tumemchoka tayari. Kitu ambacho si kweli kabisa.

    Nikasema sasa liwalo na liwe, nikamshika mama mkono na kumwita nje.

    Akanifuata akiwa mnyonge kabisa.

    “Ni kweli mama nina tatizo. Tena ni tatizo kubwa sana mama, na ninakueleza wewe kama madhara yatatokea ujue nimefanya kwa ajili yako mama, sikutakiwa kukueleza.” Nikasita na kutazama anga, niliposhusha kichwa nikazungumza bila kumtazama mama usoni.

    “Mama unaamini katika ushirikina?” nikamtupia swali la ghafla.

    “Najua upo ila siamini kama ni njia sahihi.” Alinijibu.

    “Umewahi kushiriki?”

    “Mdogo wako alipokuwa bado mdogo alishikwa na magonjwa ya ajabu ajabu baba yako akashauri tukampeleka katika hizo tiba za asili, sijui kama nazo ni ushirikina.”

    Aliponijibu vile na mimi nikamsimulia kwa ufupi juu ya sakata langu la kukosa mtoto katika njia za kawaida na hatimaye kukimbilia njia za kishirikina.

    Mama hakushtuka aliendelea kuniskiliza, nikamweleza hadi nikafikia mafaniko ya kupata mtoto sanjari na ahadi yangu kwa mizimu.

    Sasa ahadi inanisulubu.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mama alinitazama kwa sekunde kadhaa kisha akanikumbatia kwa nguvu.

    “Asante sana mwanangu kwa kunijali.”

    “Naomba unipatie nauli, kesho nirudi kijijini nikazungumze na wazee wa kwetu waiambie mizimu yetu ikazungumze na hiyo mizimu ikiwezekana wabadili malipo hayo wanayotaka. Hiyo mizimu iliyokupa mtoto ni mizimu ya wapi?” mama aliniuliza. Sikuwahi kusikia majina ya mizimu ile, labda kutokana na hofu yangu, ama kukosa umakini.

    “Mama hauoni kama mizimu itachukia?” nilimuuliza. Sasa nikiwa mdogo kabisa mwenye aibu kubwa.

    “Ni heri kujaribu kuliko kubaki kimya, hiyo waliyokupa ni adhabu na sio zawadi wanayotaka, wewe utamlea viipi mtoto bila kuwa na kazi?? Nitawasihi sana, kama ni mizimu inayofahamiana kila kitu kitakuwa sawa mwananangu.”

    Alinijaza nguvu mama, nikashangaa nilikuwa wapi kumweleza juu ya hayo siku zote.

    Nikampatia nauli ya kutosha.

    Asubuhi akamuaga mama Agy na kuondoka.

    Mimi nikaingia katika pilikapilika za hapa na pale, jioni nikapiga simu niwasiliane na mama…. Kwa sababu niliamini amefika tayari.

    Simu yake haikuita kabisa!

    Nikajaribu tena na tena…..

    Hali ilikuwa ileile, mwisho nilipigiwa mimi simu na nambari mpya.

    Nikapokea nikidhani ni mama…

    “Joshua, ni nini umemsababishia mama yako hiki? Sina la kukusaidia safari hii sasa!” ilikuwa ni sauti tulivu ya yule mganga wa jadi. Akamaliza na kukata simu

    Kusikia mganga yule akitaja jina la mama yangu, nikaishiwa nguvu!
    JIFUNZE!!


    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog