IMEANDIKWA NA : NYEMO CHILONGANI
*********************************************************************************
Simulizi : Hili Ni Jiji La New York
Sehemu Ya Kwanza (1)
Kila Mmarekani alikuwa na shauku ya kuitazama timu yao ya mpira wa kikapu ya York Buckets ambayo ilikuwa ikitarajiwa kushiriki mashindano ya klabu ya mpira wa kikapu ambayo yalitarajiwa kufanyika nchini China wiki ijayo. Kwa wakati huo hakukuwa na ushabiki wa timu moja tena, mashabiki wale ambao walikuwa wakiishabikia La Lakers, Chicago Bulls na timu nyingine wakaunganisha nguvu zao kwa kuipa kampani timu ya York Buckets.
Idadi kubwa ya Wamerekani hasa wale ambao walikuwa wakipenda mchezo wa kikapu wakawa na bendera nyingi za New Buckets mikononi mwao. Waandishi wa habari hawakuwa mbali, kila wakati walikuwa wakirusha mazoezi ambayo yalikuwa yakifanyika katika uwanja wa mazoezi ambao ulikuwa katikati ya jiji la New York, The Margedonians.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ingawa Waingereza mara kwa mara walikuwa wakiitangaza timu yao ya mpira wa kikapu ya The Buffalloes lakini wakaonekana kuanza kupigwa vikumbo na vyomba vya habari vya Kimarekani kama CNN, ESPN na Independient ambavyo vilikuwa vikirusha mambo mengi kuhusiana na timu hiyo ya New Buckets.
Mashabiki wa mpira wa kikapu duniani wakaonekana kupata msisimko wa mashindano hayo ambayo yalikuwa yakitangazwa kwa nguvu zote duniani. Wachezaji wa klabu mbalimbali za mpira wa kikapu duniani ambazo zilikuwa zimefuzu katika mashindano hayo wakaanza kusafiri kuelekea nchini China ndani ya jiji la Shanghai kwa ajili ya kushiriki mashindano hayo ambayo yalionekana kusisimua zaidi ya mchezo wa soka.
Wamarekani wakaungana muunganiko ambao uliwashangaza hata wao wenyewe, mapenzi na timu zao wakayaweka pembeni na kuungana pamoja na mashabiki wa timu ya New Buckets. Kitu ambacho walikuwa wakikihitaji kwa wakati huo ni heshima tu, waliamini kama New Buckets ingeweza kuchukua ubingwa basi ingekuwa ni heshima kubwa katika nchi yao.
Timu ya New Buckets ambayo ilichukua ubingwa wa nchi hiyo katika mchezo wa kikapu ndiyo ilikuwa ikionekana kuwa bora katika msimu huo. Katika michezo yao yote ambayo walicheza, hawakupoteza mchezo hata mmoja, hiyo ikiwa ni pamoja na kuzipiga timu kongwe kama Chicago Bulls na La Lakers.
New Buckets ikaonekana kuwa timu bora ambayo ilivunja historia na kuweka rekodi zao wenyewe. New Buckets ndio ambayo ilivunja rekodi ambayo ilidumu kwa miaka mia moja na ishirini ambayo iliwekwa na timu ya Huphilinghton kwa kucheza michezo yote katika ligi bila kufungwa.
Siku zikaendelea kukatika na hatimae kufikia siku ambayo wachezaji wa timu ya New Buckets walitakiwa kuanza safari yao ya kuelekea nchini China kwa ajili ya mashidano ya klabu za dunia katika mchezo wa kikapu. Watu zaidi ya elfu saba walikuwa wamekusanyika katika uwanja wa ndege wa John F. Kennedy kwa ajili ya kuiaga timu hiyo ambayo kwa kuiangalia kwenye televisheni, ilionekana kuwa na mvuto kwa staili yao nzuri ya uchezaji.
Wachezaji wote ambao walikuwa wakiichezea timu hii walionekana kuwa bora. Kulikuwa na Phillip Mc Kenzie, huyu alikuwa na urefu zaidi ya futi saba. Mwili wake ulikuwa umejazia kupita kawaida. Kila siku kichwa chake kilikuwa kikipendezeshwa na nywele zake ambazo alikuwa akizisuka. Kazi yake kubwa uwanjani ilikuwa ni kuzuia mipira ambayo ilikuwa ikitakiwa kuingizwa katika goli lao.
Katikati kulikuwa na mchezaji ambaye alikuwa akiogopwa kutokana na kasi yake ya kupeleka mashambulizi. Huyu alikuwa Fredrick Tunbull, mzungu aliyekuwa na uraia wa nchini Canada. Fredrick alionekana kuwa moyo wa timu ya New Buckets kutokana na kusababisha pointi nyingi katika lango la maadui.
Ukiachilia wachezaji hao na wengine, pia kulikuwa na mchezaji ambaye alionekana kuwa mwiba mkali zaidi kwa timu pinzani, huyu alikuwa Williams Jnr, mtoto pekee wa Detective Daniel Kurt. Williams ndiye mchezaji ambaye alikuwa akiogopewa zaidi kuliko mchezji yeyote, yeye alikuwa maalumu kabisa katika kuipatia pointi New Buckets.
Asilimia tisini na nane ya mipira ambayo alikuwa akiilega golini ilikuwa ikizaa pointi ambazo zilikuwa zikiwaacha mbali wapinzani. Halikuwa jambo la kushangaza kwa kumuona Williams akifunga pointi tisini hadi mia moja kwa kila mchezo.
Williams ndiye alikuwa mchezaji bora wa ligi hiyo ambayo hujulikana kama NBA nchini Marekani. Kazi yake kubwa ya kufunga ndio ambayo ilikuwa ikimpa umaarufu mkubwa katika mchezo huo. Kuwa na mchezaji kama Williams katika timu hiyo, hakukuwa na wasiwasi kabisa ya kupata ubingwa huo wa dunia ambao ulikuwa unakwenda kufanyika nchini China wiki moja ijayo.
Williams alikuwa na urefu wa futi nane huku mwili wake ukiwa mwembamba. Kichwani, nae alikuwa akipendelea kusuka nywele zake huku masikioni mwake akivaa vieleni vidogo ambavyo alikuwa akivinunua kwa gharama kubwa.
Williams alikuwa mtoto wa Detective Daniel Kurt, mzungu ambaye alizaa na mwanamke wa Kiafrika kutoka nchini Ghana. Maisha ya Williams yalikuwa zaidi nchini Marekani kuliko kwa mama yake nchini Ghana. Alilelewa na baba yake lakini mara nyingi alikuwa akisafiri mpaka nchini Ghana kwa ajili ya kumuangalia mama yake.
Kila siku kilio chake kilikuwa juu ya wazazi wake ambao walikuwa wametengana. Alikuwa akitamani sana kuwaona wazazi wake hao wakirudiana na kuishi pamoja kama zamani. Alihitaji kuwa karibu na wote wawili hata zaidi ya mtu yeyote.
Williams hakutaka kuzificha hisia zake, kila alipokuwa akihojiwa na waandishi juu ya familia yake, aliwaeleza wazi kwamba angependa sana siku moja wazazi wake hao waishi pamoja kama ilivyokuwa zamani. Williams alikuwa akiumia moyoni kila alipokuwa akiwaona marafiki zake wakipiga picha pamoja na wazazi wao wote wawili, moyoni alijiona kama kutengwa.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Katika maisha yake ya mahusiano, Williams alikuwa na msichana mmoja, Celine Kerms. Msichana huyu alionekana kuwa kila kitu kwake, yeye ndiye ambaye alikuwa faraja yake, alimpenda na kumthamini, alimsikiliza katika kila kitu ambacho alikuwa akimwambia.
Celine ndiye ambaye alikuwa mshauri mkuu wa Williams. Kila siku alikuwa akimpa furaha kitu ambacho kilimsukuma kumpa ahadi ya kumuoa mara tu atakaporudi kutoka nchini China huku akiwa ameshika kombe la klabu Bingwa la Dunia.
“Do you love me? (Unanipenda?)” Celine alimuuliza Williams huku macho yake yakionekana kama mtu aliyekuwa amelia kwa kipindi kirefu.
“Yes. I love you baby. You are everything to me. You are my Queen, my Angel. You are my everything (Ndio. Ninakupenda mpenzi. Wewe ni kila kitu kwangu. Wewe ni malkia wangu, malaika wangu. Wewe ni kila kitu changu)” Williams alimwambia Celine katika kipindi ambacho alikuwa akimuaga uwanja wa ndege.
Celine bado alikuwa akihuzunika. Kwa siku moja tu ambayo hakuwa akimuona Williams kwake ilikuwa shida, hakujua angeishi vipi katika kipindi hicho ambacho alikuwa akielekea nchini China ambapo angekaa kwa muda wa mwezi mmoja.
Wakakumbatiana. Machozi yakaanza kutoka machoni mwa Celine na kutiririka mashavuni mwake mpaka mgongoni mwa Williams. Waliendelea kukumbatiana kwa muda wa dakika mbili huku waandishi wa habari wakilipiga picha tukio lile.
“Dont cry baby. I will come back baby and be with you again (Usilie mpenzi. Nitarudi na kuwa nawe tena)” Williams alimwambia Celine.
“I love you (Ninakupenda)”
“I love you too (Ninakupenda pia)”
Wakaachana na wachezaji wote wakatakiwa kuelekea katika ndege ya kukodi ambayo ilikuwa imeandaliwa kwa ajili yao. Kila mchezaji alionekana kuwa na furaha kwenda kushiriki mashindano hayo japokuwa katika mioyo yao walikuwa wakipata wakati mgumu sana hasa kila walipokuwa wakiwaangalia wapenzi wao ambao ilitakiwa kuwaacha ili kutokuharibu uwezo wao mara wawapo uwanjani.
Wote wakaingia ndani ya ndege huku kila tukio likirushwa moja kwa moja na vituo vingi vya televisheni duniani kikiwepo CNN. Mara baada ya kuingia ndani ya ndege, ndege ikawashwa na safari ya kuelekea nchini China kuanza.
Celine hakutaka kuondoka, alibaki akiiangalia ndege ile mpaka katika kipindi ambacho ilikuwa ikipaa. Alibaki akipunga mkono wake hewani kama ishara ya kumuaga mpenzi wake aliyekuwa akimpenda kwa moyo wake wote. Mara baada ya ndege kupotea machoni mwake, Celine akaanza kulifuata gari lake la kifahari la Aston Martin na kisha kuondoka uwanjani hapo.
*********
Watu zaidi ya elfu tano walikuwa wamekusanyika katika uwanja wa ndege wa Shanghai kwa ajili ya kuipokea timu ya mpira wa kikapu ya New Buckets. Picha mbalimbali za wachezaji wa New Buckets zilikuwa zimeshikwa na mashabiki ambao walikuwa wamekusanyika uwanjani hapo.
Ingawa timu ya Bufalloes kutoka nchini Uingereza ilikuwa imepokelewa na idadi kubwa ya watu lakini timu ya New Buckets ilikuwa imefunika katika idara ya mapokezi. Wachezaji wakaanza kuteremka kutoka katika ndege huku watoto wadogo walioshika maua wakiwa wamesimama pembezoni mwa ngazi za kushukia.
Viongozi mbalimbali wa mpira wa kikapu nchini China wakafika mahali hapo na kuanza kusalimiana na wachezaji hao na kisha kuingia garini na safari ya kuelekea katika hoteli ya Xuai kuanza. Ni ndani ya dakika ishirini tu, walikuwa wakiteremka katika basi hilo kubwa na kisha kuanza kuingia hotelini.
Muda wote wachezaji wa New Buckets walikuwa wakionekana kuwa na furaha. Machoni walionekana kuwa na uhakika kwamba walikuwa wanakwenda kuuchukua ubingwa huo. Wakajiandaa kwa kwenda bafuni kuoga na baadae kula chakula cha usiku.
Usiku mzima Williams alikuwa akiongea na Celine kupitia simu yake ya mkononi. Moyoni alijisikia faraja, kuongea na mpenzi wake kwa wakati huo kulionekana kumfariji kupita kawaida. Ni masaa kadhaa yalikuwa yamepita pasipo kumuona lakini alikuwa amemkumbuka kupita kawaida.
Kila alipokuwa akizidi kuongea nae na ndivyo ambavyo taswira ya sura ya Celine ilivyozidi kukaa kichwani mwake. Wote walikuwa wakipendana kupita kiasi, kila mtu alikuwa na kiu ya kumuona mwenzake haraka iwezekanavyo. Hiyo ndio ilikuwa siku ya kwanza lakini ikaonekana kuwa siku ngumu sana katika maisha yao.
Hawakuzoea kabisa kukaa mbalimbali. Walikwishazoea kwamba kila wanapokuwa nyumbani, basi hukaa pamoja huku wakati mwingine hata mazoezini, Celine akielekea huko kumuona mpenzi wake. Mapenzi ndio ambayo yalikuwa yamewatawala maishani mwao. Kitu ambacho walikuwa wakikifikiria kwa wakati huo ni ndoa tu.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/Walihitaji sana kuoana na hatimae kutengeneza familia moja moja yenye furaha na amani. Walifanya sana mchezo mchafu, lakini kila walipokuwa wakifanya, hawakuonekana kuwa huru mpaka pale ambapo wangesimama mbele ya kanisa na kuvarishana pete vidoleni mwao.
“Sitoweza kukaa hivi kwa muda wa mwezi mzima mpenzi, ni lazima nipande ndege nikufuate” Celine alimwambia Williams.
“Usifanye hivyo mpenzi. Naamini hata kama utakuja hautopata nafasi ya kuonana nami kwani muda mwingi tutakuwa kambini ambako haruhusiwi kuingia mtu yeyote zaidi ya wahusika” Williams alimwambia Celine.
“Maisha magumu mpenzi. Maisha bila kukuona yamekuwa magumu sana” Celine alimwambia Williams.
“Usijali mpenzi. Tutakuwa tukiwasiliana mara kwa mara. Hasa nitakuwa nikitumia mtandao wa Skype kama kuna kitu nitataka kukuonyeshea. Naomba usijali mpenzi. Kila kitu kitakuwa sawa” Williams alimwambia Celine.
“Sawa mpenzi. Nakupenda sana”
“Nakupenda pia” Williams alisema na kisha kuagana.
Akapanda kitandani na kulala chali. Macho yake yaikuwa yakiangalia juu huku mikono yake ikiwa chini ya kichwa chake. Mawazo yake kwa wakati huo yalikuwa yakimfikiria mpenzi wake, Celine. Usingizi ukaonekana kuwa mgumu kupatikana.
Alijaribu kuuvuta usingizi lakini wala haukupatikana. Mawazo yake yalikuwa juu ya Celine tu. Kwa jinsi ambavyo alivyokuwa akimkumbuka, angeweza kutoroka kambini kama tu mashindano hayo yangekuwa yakifanyika nchini Marekani hasa katika jiji la New York kama mwaka uliopita.
Williams alikuja kupata usingizi saa kumi kasoro alfajiri. Saa moja na nusu, simu ya mezani iliyokuwa chumbani kwake ikaanza kuita, moja kwa moja akajua kwamba kwa wakati huo alitakiwa kuamka na kuungana na wenzke katika chumba maalmu kwa ajili ya kifungua kinywa.
“Nimemkumbuka sana mpenzi wangu” Williams alimwambia Shelton.
“Kama mimi tu. Yaani hadi mwezi ujao naona muda mrefu sana” Shelton alimwambia.
Kila mchezaji alkuwa amemkumbuka mpenzi wake. Mapenzi yalionekana kuwakamata sana na hii ilitokana kwamba wachezaji wengi walikuwa na umri mdogo. Walitumia muda wa dakika arobaini hadi kumaliza kunywa chai na kisha kwenda katika uwanja wa mazoezi.
Zaidi ya mashabiki elfu moja walikuwa wamekusanyika katika uwanja huo kwa ajili ya kuangalia mazoezi ya timu ya New Buckets. Wachina hawakutaka kuwaona wachezaji hao kupitia katika televisheni zao tu, kwa wakati huo walitamani sana kuwaona ana kwa ana.
Kila shabiki akaonekana kufarijika. Kuwaona Williams, Shelton, Tunbull, Phillip na wachezaji wengine kulionekana kuwafariji kupita kawaida. Ingawa Wachina walikuwa na timu yao ambayo ilikuwa ikiiwakilisha nchi yao lakini wengi wao mapenzi yao yalikuwa juu ya timu ya New Buckets.
“Naomba tufanye mazoezi ya nguvu, kushinda kwetu kombe hili itakuwa ni zawadi nzuri sana kwa wapenzi wetu. Tujitahidini sana kufanikisha lengo lililotuleta huku” Kocha aliwaambia katika kipindi ambacho mazoezi yalikuwa yamekwisha.
“Ndio kocha” Wote waliitikia.
Siku ziliendelea kukatika mpaka kufikia siku ambayo mashindano hayo yalipokuwa yakianza. Kila timu ilionekana kuwa ngumu kwa kuwa zilikuwa zimefanya maandalizi ya kutosha. Timu ya New Buckets ikaonekana kufanya vizuri, ilifanikiwa kushinda kwa pointi nyingi katika kila mchezo.
Walianzia mzunguko, wakaja kumi na sita bora. Baadae wakaingia robo fainali hadi nusu fainali. Mwisho kabisa wakaingia fainali ambako wakakutana na timu ngumu kutoka Humberg City ya Ujerumani. Siku hiyo ndio siku ambayo ilionyesha uwezo halisi wa Williams.
Alifunga zaidi ya pointi mia moja kumi na tano hali iliyopelekea kuvunja rekodi ambayo ilikuwa imewekwa miaka ya nyuma kwa kufunga pointi nyingi. Mwisho wa mchezo, New Buckets ilishinda kwa pointi zaidi ya mia moja hamsini.
Kelele za shangwe zilikuwa zikisikika ukumbini katika kipindi ambacho timu hiyo ilipokuwa ikikabidhiwa kombe. Ulikuwa ni ushindi wa kihistoria kwani New Bucket ilikuwa imecheza mechi zote bila kufungwa wala kusuluhu. Wachezaji wote wa New Buckets wakaitwa katika hoteli ya Shi Hong ambako huko sherehe kubwa ikafanyika.
“Wamarekani wanatusubiri. Hatutakiwi kiu ya ushindi wetu tuimalizie hapa” Kocha aliwaambia.
“Itakuwa vizuri zaidi. Ushindi huu ninautoa kwa mpenzi wangu mpendwa, Celine. Kombe hili ni zawadi ya heshima kwake” Williams aliwaambia huku akionekana kuwa na furaha.
“Na mimi pia ninautoa ushindi huu kwa mpenzi wangu. Najua alikuwa akiniangalia katika kipindi ambacho nilikuwa nikiokoa mipira. Nampenda sana mpenzi wangu, Rebecca” Phillip aliwaambia na wachezaji wote kuanza kucheka.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kila mmoja alikuwa akiongea lake kwa wakati huo, ushindi huo kwao ulionekana kuwa wa thamani kubwa kwa wapenzi wao. Hakukuwa na mtu aliyejua kwamba baada ya hapo maisha ya furaha yasingepatikana tena katika maisha yao, maisha ya maumivu makali ndio ambayo yangefuata baada ya hapo. Vicheko ambavyo walikuwa wakicheka ndani ya ukumbi ule vingegeuka na kuwa vilio vikubwa ambavyo visingeisha katika maisha yao yote. Kama wangejua ni kitu gani kingefuata baada ya hapo, kusingekuwa na mtu yeyote ambaye angefurahi wala kusafiri kuja nchini China.
Kila mmoja alikuwa na furaha katika kipindi ambacho walikuwa wakiingia ndani ya ndege yao tayari kwa kuanza safari ya kurudi nchini Marekani. Muda wote nahodha wa timu hiyo, Bruce alikuwa amelishika kombe lile ambalo walikuwa wamelinyakua.
Wachina zaidi ya elfu nane walikuwa wamefika katika uwanja wa
ndege ule kwa ajili ya kuiaga timu hiyo. Katika kipindi chote cha mwezi mmoja wa mashindano, wachina walionekana kuridhika kuwaangalia wachezaji wale ambao kila siku walikuwa wakiwaona katika televisheni tu.
Mwenyekiti wa chama cha mpira wa kikapu nchini China, Bwana Sha Jung akaanza kuagana na makocha pamoja na benchi lote la ufundi la timu ile na kisha kuingia ndani ya ndege. Wala hakukuwa na muda wa kupoteza, ndege ikawashwa na kisha kuanza kutembea katika ardhi ya uwanja ule na baada ya dakika moja, ikaanza kupaa.
Ndani ya ndege, Williams alikuwa amekaa pamoja na Phillip huku muda wote stori zao zikiwa ni kuzungumzia mapenzi tu. Kila mmoja alijaribu kumueleza mwenzake namna ambavyo alivyokuwa akimpenda mpenzi wake. Yalikuwa yamebakia masaa ishirini na tatu kabla ya kuwaona wapenzi wao ambao walikuwa wakiwazungumzia mahali hapo.
Kelele zilikuwa nyingi ndani ya ndege, wengine walikuwa wakiimba huku wengine wakicheza. Walionekana kuwa na furaha kubwa kupita kiasi. Mara kwa mara Williams alikuwa akiichukua simu yake na kufungua sehemu ya picha na kisha kuziangalia picha za Celine.
Moyoni alikuwa akijisikia furaha. Alimkumbuka sana mpenzi wake hata zaidi ya alivyowakumbuka wazazi wake. Alitamani afike jijini New York, ateremke ndani ya ndege na kisha kuanza kupiga hatua kumfuata mpenzi wake ambaye aliamini kwamba angekuwa uwanjani hapo akimsubiri.
“Nimemkumbuka sana Celine” Williams alisema huku akiiangalia picha ya Celine kwenye simu yake.
“Muda mrefu sana tumekaa mbali nao. Unajua sijawahi kukaa mbali na Rebecca namna hii” Phillip alimwambia Williams.
Safari bado ilikuwa ikiendelea kama kawaida huku kelele zikiendelea kusikika ndani ya ndege. Kila mtu alikuwa akiongea lake kwa wakati huo. Picha mbalimbali zilikuwa zikipigwa ndani ya ndege hiyo kama picha za ukumbusho hapo baadae.
Williams akasimama na kisha kuanza kuwapiga picha watu wote waliokuwa ndani ya ndege hiyo. Kwake ilikuwa ni picha za kumbukumbu ambazo katika kipindi atakachostaafu mpira wa kikapu basi ataweza kuziangalia na kukumbuka mambo mengi ya nyuma.
“Picha themanini” Williams alimwambia Phillip huku akiizima simu yake.
“Kumbukumbu nzuri. Nitazichukua baadhi ya picha tutakapofika” Phillip alimwambia Williams.
Waliendelea kupiga stori kiasi ambacho baada ya masaa mawili, watu wote walikuwa wamechoka na hivyo kuvilalia viti vyao. Safari bado ilikuwa ikiendelea, baada ya masaa mawili, wote wakashtuka mara baada ya kusikia sauti ya kike ikiwaambia kwamba walitakiwa wafunge mikanda yao tayari kwa ndege hiyo kutua.
Wote wakakurupuka na kuanza kufunga mikanda yao. Wakavipandisha vidirisha kwa juu ili kuona walikuwa wamefika katika nchi gani. Kila mmoja akaonekana kushtuka, sehemu ambayo walikuwa wakiiona katika wakati huo ilikuwa tofauti na jinsi ambavyo walivyokuwa wakifikiria.
Ndege ilikuwa ikitua katika msitu mkubwa ambapo ulikuwa umezunguka lami ile ambayo ilitumika kuwa kama uwanja wa ndege. Hakukuwa na nyumba ya aina yoyote ambayo ilikuwa ikionekana machoni mwao zaidi ya miti minene na mirefu tu.
Kwa mbali walikuwa wakiona milima mirefu huku ukungu ukiwa umetawala katika milima hiyo. Kila mmoja akaonekana kuogopa, wakaonekana kuchanganyikiwa kwani hakukuwa na mtu ambaye alielewa mahali pale walipokuwa.
Ndege ikasimama, kila mtu alibaki akichungulia dirishani huku wakitaka kuona ni kitu gani kingeendelea baada ya hapo. Watu zaidi ya themanini waliokuwa na bunduki mikononi wakaonekana wakitoka katika msitu ule mkubwa. Wachezaji wakaonekana kuogopa.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mmoja kati ya marubani wa ndege ile akatokea mahali hapo na kisha kuanza kuufuata mlango na kuanza kuufungua. Hakukuwa na mtu ambaye alithubutu kuuliza kitu chochote kile kwani bunduki aina ya AK47 ilikuwa ikionekana katika mikono yake.
Mara baada ya mlango kufunguliwa, baadhi ya watu wale ambao walikuwa nje ya ndege ile wakaanza kuingia ndani ya ndege ile. Kila mmoja mchezaji alionekana kuogopa zaidi, nyuso za watu wale hazikuonekana kuwa na huruma hata mara moja.
“This is your destination (huu ni mwisho wenu)” Mwanaume mmoja ambaye alionekana kuwa kiongozi wa kundi lile la watu aliwaambia.
“You have to stay calm. If u ask anything, I will pull my trigger (Mnatakiwa mtulie. Kama mkiuliza kitu chochote, nitakwenda kuvuta kitufe cha bunduki)” Mwanaume yule aliwaambia.
Amri ikatolewa kwamba wote walitakiwa kuweka mikono yao kichwani na kisha kusimama na kuanza kutoka nje. Hawakutakiwa kutoka na kitu chochote kile zaidi ya nguo ambazo walikuwa wamezivaa. Hakukuwa na ubishi wowote kile ambacho waliambiwa ndicho ambacho walikitekeleza.
Wote wakajipanga mstari na kuanza kuusogelea mlango ule na kuteremka ngazi. Eneo ambalo walikuwa wamefika mahali hapo lilionekana kuwa eneo la hatari. Miti mirefu na minene ambayo ilikuwa ikionekana mbele yao ilikuwa ikiwaogopesha.
Hawakujua ni nchi gani ambayo walikuwepo kwa wakati huo, na wala hawakujua ni bara gani ambalo walikuwepo kwa wakati huo. Mara baada ya wote kuteremka, wakaamriwa kuunga mstari mmoja ambao ulitakiwa kuwafuata watekaji watatu ambao walianza kuingia msituni huku watekaji wengine wakiwa kwa nyuma.
Williams hakuwa na amani, furaha yote ambayo alikuwa nayo katika kipindi cha nyuma ikaonekana kufutika moyoni mwake. Alibaki akijisikia uchungu moyoni, hakujua kama angeweza kutoka salama katika mikono ya watekaji wale na hatimae kuonana na mpenzi wake, Celine.
Walizidi kutembea zaidi na zaidi mpaka kufika katika eneo ambalo lilionekana kutisha zaidi. Nyumba mbili ambazo zilikuwa ni magofu zilikuwa zikionekana mbele yao huku mapipa makubwa yakionekana katika eneo lile. Michirizi ya damu zilizoganda ilikuwa ikionekana vizuri machoni mwao.
Kwa jinsi ambavyo picha ile ilivyoonekana mbele yao, hakukuonekana kuwa na dalili zozote za kutoka salama. Wote wakaamriwa kuvua nguo zao na kubakia na bukta ambazo walikuwa nazo, hakukuwa na ubishi wowote ule, wakatekeleza kile ambacho walikuwa wameambiwa.
Baada ya hapo, wakaamriwa kuingia ndani ya nyumba moja na kisha kufungiwa huku wakitaarifiwa kwamba kulikuwa na mtu ambaye alikuwa akitarajiwa kuingia masaa machache yajayo kwa ajili ya kuangalia kama kazi yake ilikuwa imefanyika kikamilifu.
Wote wakabaki ndani ya gofu lile huku watekaji wote wakiwa wamekwenda nje. Wakabaki wakiangaliana tu, nyuso zao zilikuwa zikionyesha wasiwasi mkubwa. Hawakujua sababu ambayo iliwapelekea kutekwa na kupelekwa katika msitu ule ambao haukuwa ukionekana kuwa na amani hata kidogo.
“Why are we here? (Kwa nini tuko hapa?)” Bruce, nahodha wa timu hiyo aliuliza.
“I dont know. Who knows? (Sifahamu. Nani anafahamu?)” Kocha wa timu hiyo, Peters alijibu na kuuliza.
Hakukuwa na mtu aliyejibu kitu chochote. Maswali yale yalionekana kuwa magumu kwa kila mmoja. Hawakujua mpango wa utekaji ule ulianzia wapi, hawakujua wale marubani ambao walikuja nao walikuwa wamekwenda wapi. Kila mmoja akaonekana kuchanganyikiwa.
“We must get out of here (Ni lazima tuondoke hapa)” Shelton aliwaambia.
“How? (Kivipi)
“We have to fight against them. How do you see? (Inabidi tupigane nao. Mnaonaje?)”
“How? They got guns and we have nothing, how can we fight them? (Kivipi? Wana silaha na sisi hatuna kitu, tutapigana nao vipi?)” kocha Peters aliuliza.
Walikuwa wakiendelea kujadili ni kwa namna gani wangeweza kutoka katika mikono ya watekaji wale na kurudi nchini Marekani. Mpaka giza linaingia, hakukuwa na mtu ambaye aliujua ni kwa namna gani wangeweza kuondoka katika eneo lile.
Giza lilikuwa kubwa ambalo hawakuwahi kuliona katika maisha yao yote. Milio ya wanyama wakali kama dubu, simba ilikuwa ikisikika masikioni mwao. Uoga ambao walikuwa nao mioyoni mwao ukazidi kuongezeka zaidi. Kila mmoja aliona kwamba hata kama wangeweza kutoroka mahali hapo wasingeweza kufika mbali kutokana na msitu huo kujaa wanyama wakali.
Usiku ule kwao ulikuwa usiku wa tabu kuliko kipindi chote katika maisha yao. Mbu walikuwa wakiwauma huku joto likiwa kali sana. Muda wote walikuwa na kazi ya kufukuza mbu tu. Miili yao ambayo haikuzoea kabisa kung’atwa na mbu siku hiyo ilikuwa ni siku ya mateso sana.
Usiku mzima walikuwa macho huku miili yao ikizidi kuvimba. Akili zao zilikuwa zikifikiria utajiri ambao walikuwa wakimiliki katika maisha yao. Hawakuwahi kulala katika sehemu ambayo ilikuwa na mateso makali ya mbu kama eneo lile. Mpaka mwanga unaanza kuchomoza, mwili wa kila mmoja ulikuwa umevimba.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Watekaji watatu wakafungua mlango wa gofu lile na kuingia ndani. Wachezaji wote ambao walikuwa wamekaa karibu na mlango wakaamriwa kusogea mbali kabisa na mlango ule. Wakaanza kuhesabiwa na watekaji wale ambao walikuwa wameingia ndani ya gofu lile.
“Samahanini” Paul alisema huku akisimama.
“Kuna nini?”
“Hivi hapa ni wapi na kwa nini tuko hapa?” Paul aliuliza maswali mawili mfululizo.
Mtekaji mmoja akaonekana kuwa na hasira baada ya kulisikia swali lile. Akaanza kumsogelea Paul mpaka pale aliokuwa amesimama na kuanza kumwangalia kwa macho yaliyojaa hasira ambayo yalionekana kumuogopesha Paul. Mtekaji yule akaanza kuikoki bunduki yake.
“Paaa .... Paaaa .... Paaa... ” Milio ya risasi ikasikika.
Hapo hapo Paul akaanguka chini huku damu zikimtoka kifuani. Kila mchezaji alionekana kuogopa. Watekaji wengine zaidi wakafika ndani ya gofu lile kwa kudhani kwamba wachezaji wale walikuwa wamewazidi nguvu watekaji wenzao na kuanza kuwashambulia.
Walipoingia mule macho yao yakatua kwa Paul ambaye alikuwa akirusha miguu yake huku na kule na baada ya sekunde chache, akatulia tu. Nyuso za watekaji wale zikaonekana kuwa na furaha, kitendo cha Paul kupigwa risasi kilionekana kuwa kitendo kilichowafuhisha sana.
“Kama kuna mtu mwingine atajaribu kuuliza swali lolote, hatutosita kuupoteza uhai wake” Mtekaji yule aliwaambia huku akionekana kukasirika.
Mwili wa Paul ukabebwa na kupelekwa nje ya gofu lile. Kila mchezaji alionekana kuumia hawakuamini kama wangeweza kumpoteza Paul, kijana mcheshi kuliko yeyote katika timu ile. Walimwangalia yule mtekaji ambaye alikuwa amempiga risasi Paul, kila mmoja alitamani kuchukua bunduki na kumfyatulia kama alivyomfyatulia Paul.
Wachezaji wale wakashindwa kuvumilia, machozi yakaanza kutiririka mashavuni mwao. Mioyo yao iliumia kupita kawaida, hawakuamini kama safari ile ya kuelekea nchini China ndio ingekuwa safari ya mwisho kwa Paul.
Saa mbili kamili asubuhi wakaanza kusikia miungurumo ya gari kutoka nje. Kila mmoja akawa na shauku ya kutaka kujua ni mtu gani ambaye alikuwa akiingia kwa wakati ule. Walijua fika kwamba huyo ndiye mtu ambaye alikuwa nyuma ya mpango ule wa kutetwa kwao.
Kila mmoja alitaka kumfahamu mtu huyo ni nani. Wakabaki kimya ndani ya gofu lile mpaka katika kipindi kile ambacho mtu huyo akaaingia pamoja na watekaji wale. Kila mmoja alionekana kushtuka, hawakuamini kama mtu yule ambaye alikuwa ameingia ndani ya gofu lile ndiye ambaye alikuwa nyuma ya mpango wa kutekwa kwao.
Walimfahamu vilivyo mtu yule. Aliwaonyeshea ushirikiano mkubwa sana katika kipindi ambacho walikuwa nchini Marekani. Hawakuamini kama mtu huyo angeweza kufanya kitu kama kile. Kila mmoja akaonekana kuwa na hasira nae, wakaonekana kumchukia.
“Karibuni sana...” Mwanaume huyo aliwaambia huku tabasamu pana likionekana usoni mwake.
****
Habari za kutekwa kwa ndege iliyokuwa imebeba wachezaji wa klabu ya mpira wa kikapu ya New Buckets ilionekana kumshtua kila aliyezisikia. Dunia ikaonekana kutetemeshwa na taarifa ile ambayo kuanzia muda hiyo ndio ilikuwa habari ambayo ilitawala vyombo vyote vya habari duniani.
Hakukuwa na mtu ambaye alielewa kitu kilichotokea mpaka marubani wale kuhusika katika utekaji wa ndege ile. Hawakuelewa kitu chochote kama wale marubani ambao walikuwa wameipeleka ndege ile nchini China huku ikiwa na wachezaji, wote walikuwa wametekwa na kufungwa ndani ya choo cha wafanyakazi katika uwanja wa ndege wa Hong Kong.
Taarifa zile zikafikishwa katika meza ya kamati ya mchezo ule wa mpira wa kikapu nchini Marekani, kila mmoja akaonekana kuchanganyikiwa. Haikuwa rahisi sana kuiamini taarifa ile, uongo ndio ambao ulikuwa ukikisiwa kwa wakati huo. Halikuonekana kuwa jambo rahisi kwa ndege yoyote kutoka nchini Marekani kutekwa kirahisi namna ile.
Kikao cha dharura kikawekwa na bodi ya mchezo huo nchini Marekani. Ni watu kumi tu ndio ambao walikuwepo ndani ya kikao hicho. Kikao kilionekana kuwa kizito na kigumu, kila mmoja alionekana kuchanganyikiwa, hawakujua ni kwa namna gani wangeweza kuliazungumzia tukio lile ambalo kadri muda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo lilivyozidi kuvitawala vyombo vya habari.
“Impossible.. (Haiwezekani)” Hilo ndilo lilikuwa neno lililoongewa na wanakamati wote katika bodi ile.
Kikao hakikukwenda vizuri kama ilivyotakiwa kutokana na kila mmoja kutokuamiani kama kweli ndege ile ilikuwa imetekwa. Kitu ambacho walikuwa wakikitaka kwa wakati huo ni kupata taarifa za kina kutoka nchini China na kujua ni kitu gani kilikuwa kimeendelea kule.
Kwa haraka haraka simu zikapigwa na Mwenyekiti wa Chama cha mpira wa kikapu nchini China, Bwana Ting Chung ambaye akathibitisha kutekwa kwa ndege ile. Bado hali ilionekana kuwa tete, hakukuwa na mtu ambaye alifahamu sehemu ndege ile ilipotua.
Wamarekani wakajaribu kuwasiliana na viwanja vingi vya ndege duniani ili kujua kama kuna uwezekano wa ndege ile kutua huko lakini jibu lilikuwa ‘hapana’. Serikali ya nchini Marekani haikutaka kuliacha suala hilo kwa shirikisho la mchezo huo, NBA. Kitu kilichofanyika ni kutumwa wapelelezi wa shirika la kipelelezi la F.B.I kwa ajili ya kuangalia sehemu ambayo ndege ile ilikuwa imepelekwa.
Kazi haikuwa rahisi kama ilivyotarajiwa na watu wengi, wapelelezi walitumia siku tano, hakukuwa na dalili zozote za kujua sehemu ambayo ndege hiyo ilikuwa na uwezekano wa kutua. Wapelelezi hawakutaka kukata tamaa jambo ambalo liliwafanya kufanya upelelezi zaidi na zaidi lakini bado hali ilikuwa ile ile, ndege haikuonekana.
Familia za ndugu wa wachezaji ambao walikuwa wamesafiri kuelekea nchini China kwa ajili ya kushiriki mashindano yale walikuwa wamebaki na huzuni kubwa mioyoni mwao. Hawakuwa na uhakika kama kweli wangeweza kukutana na ndugu zao kwa mara nyingine. Hali ile ilionekana kuwatisha, kuchukua muda mrefu kwa wapelelezi wa shirika la F.B.I kulionekana kila dalili za kushindwa kwa upelelezi ule.
Celine hakuwa na raha. Kila alipokuwa akimfikiria mpenzi wake, Williams alibaki akilia tu. Kila siku alikuwa akiangalia picha za mpenzi wake huyo, moyoni aliumia kupita kawaida. Celine alionekana kukata tamaa, hakuwa na uhakika wa kuonana na mpenzi wake huyo.
Bwana Kurt alionekana kuwa katika wakati mgumu, mtoto wake, Williams kuwa miongoni mwa wachezaji ambao walikuwa wametekwa kulionekana kumuumiza kupita kawaida. Alichokifanya kwa wakati huo ni kumpigia simu mzazi mwenzake, Latifa aliyekuwa nchini Ghana kwa ajili ya kwenda kufarijiana nae nchini Marekani.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Bi Latifa alionekana kuchanganyikiwa, hakuamini kile ambacho alikuwa akikisikia katika vyombo vya habari. Wala hakutaka kuendelea kukaa nchini Ghana, alichokifanya ni kuchukua viza, kukata tiketi na kisha kuanza safari ya kuelekea nchini Ghana.
Njia nzima Bi Latifa alikuwa na mawazo, alimpenda sana mtoto wake, Williams, alikuwa tayari kitu chochote kitokee katika maisha yake lakini si kumpoteza kijana wake. Alimpenda sana Williams hata zaidi ya jinsi alivyojipenda yeye mwenyewe, Williams alikuwa kila kitu katika maisha yake.
Kila alipokuwa akiangalia magazeti ambayo yalikuwa ndani ya ndege ile, alikuwa akiumia. Picha za wachezaji mbalimbali zilikuwa zikionekana katika magazeti yale huku picha ya mtoto wake ikiwa kubwa zaidi kutokana na kuwa na umaarufu mkubwa zaidi ya wengine.
Katika maisha yake yote aliyopitia, safari hiyo ya kuelekea nchini Marekani ndio ilikuwa safari ya majonzi kuliko safari zote. Macho yake yalikuwa mekundu kutokana na kulia kwa muda mrefu. Mpaka ndege inatua uwanja wa ndege wa John F Kennedy nchini Marekani, Bi Latifa alikuwa akilia tu.
Akaanza kupiga hatua kuelekea chini. Mara alipotoka nje ya uwanja ule na macho yake kutua katika uso wa mtalaka wake, Bwana Kurt, kilio kikaanza upya. Kumuona mtalaka wake huyo kulimkumbusha taswira ya mtoto wake kipenzi.
Akaanza kumfuata, alipomkaribia, wote wakakumbatiana. Celine ambaye alikuwa pembeni yao akaanza kulia zaidi, kumuona mama wa mpenzi wake kulionekana kumuumiza. Bi Latifa alikuwa amefanana sana na Williams kiasi ambacho kila alipokuwa akimwangalia alikuwa akimkumbuka mpenzi wake.
Wote wakaanza kuelekea nje ya jengo la uwanja ule na kisha kuanza kulifuata gari lao. Waandishi wa habari wakatokea mahali hapo na kuanza kuwapiga picha ambazo waliamini kwamba zingeuza sana magazeti siku inayofuata. Wote wakaingia garini na kisha safari ya kuelekea Westbury kuanza huku ikiwa ni saa kumi na moja jioni.
Kama fedha kwake halikuwa tatizo kabisa, alikuwa akimiliki kiasi kikubwa cha fedha kilichokuwa zaidi ya dola za Kimarkani bilioni kumi na sita. Kwake maisha hayakuonekana kuwa na tatizo lolote lile, alinunua kitu chochote ambacho alikuwa akikihitaji katika maisha yake.
Alimiliki nyumba tano ambazo zilikuwa ziimemgharimu fedha nyingi. Nyumba ambayo alikuwa ameinunua katika jiji la Atlanta lilimgharimu kiasi cha dola za kimarekani Milioni sitini. Hiyo ndiyo nyumba ambayo alikuwa akiishi katika kipindi hicho ingawa alikuwa na nyumba tano katika miji mbalimbali kama Washington, New Orleans, Chicago na sehemu nyingine.
Mzee huyu, Robinson, alikuwa na vitega uchumi mbalimbali ndani ya nchi ya Marekani na nje ya nchi hiyo. Yeye ndiye ambaye alikuwa akimiliki kiwanda cha kutengeneza karatasi pamoja na kiwanda cha kinywaji cha Fantastic. Mzee huyu hakuwa na vitega uchumi hivyo tu, bali alikuwa akimiliki kiwanda kikubwa cha kutengeneza magazeti ya The Independent ambayo yalikuwa yakitoka kila siku ya Jumatano nchini Marekani.
Ingawa alikuwa na fedha nyingi na za kutosha lakini Bwana Robinson hakuwa na kitu kimoja ambacho alikuwa akikihitaji katika kipindi chote cha maisha yake, UMAARUFU. Mara kwa mara alikuwa akifanya mambo mengi kama kujitangaza, alikuwa akisaidi watoto yatima huku akitembelea wagonjwa katika hospitali nyingi nchini Marekani huku lengo lake kubwa likiwa ni kutangazwa na hatimae kuwa maarufu.
Umaarufu kwake ulionekana kuwa mbali, kila siku alikuwa akihitaji sana kuupata na kujulikana na watu wote duniani. Ingawa alikuwa akifanya mambo mengi, alikuwa akiandikwa mara chache sana katika vyombo vya habari na kisha kusahaulika. Alitamani kuwa na umaarufu mkubwa kama aliokuwa nao Bill Gates, Nyemo Chilongani pamoja na matajiri wengine, kilio chake kikubwa ambacho alikuwa akikililia kila siku ni kuwa maarufu na kujulikana.
Hapo ndipo ambapo alikuja kupata wazo la kununua timu ya mchezo wa ‘NFL’ nchini Marekani, timu ya Reegoot Palace. Hapo ndipo alipokuwa akiamini kwamba umaaruu ambao alikuwa akitaka ndipo ambapo ungepatikana kutokana na mchezo huo kupendwa sana na Wamarekani wengi.
Alijitahidi kununua wachezaji wegi katika klabu hiyo na kuwalipa vizuri. Timu hiyo ilipoanza kufanya vizuri nae ndipo ambapo akaanza kujulikana na kusikika masikioni mwa watu. Jambo hilo likaanza kumfurahisha kupita kawaida, kila mwandishi ambaye alikuwa akitumia muda wake kumtangaza, alikuwa akimlipa kisiri siri.
Muda uliizidi kwenda mbele mpaka katika kipindi ambacho akaamua kununua timu ya mpira wa kikapu ya Boston Five. Ingawa ilikuwa timu ya chini, akaanza kununua wachezaji wengi na wakubwa kwa ajili ya kuifanya timu hiyo kuwa na jina kubwa. Baada ya kupata wachezaji wengi wazuri, timu hiyo ikaanza kufanya vizuri na jina lake kuanza kutangazwa katika ulimwengu wa michezo.
Ni ndani ya miaka miwili, asilimia 90 ya watu duniani walikuwa wakimfahamu Bwana Robinson. Kwake ikaonekana kuwa faraja kubwa kiasi ambacho akaamua kuwalipa fedha zaidi wachezaji wote ambao walikuwa wakicheza katika timu yake ya Boston Five.
Tayari umaarufu ambao alikuwa akiutaka alikwishaupata, sasa alikuwa akihitaji kitu kimoja tu, heshima michezoni. Ni kweli kwamba alikuwa ameandaa timu nzuri, lakini katika timu hiyo bado alikuwa akihitaji mafanikio. Alikuwa akihitaji timu hiyo ichukue vikombe kama zilivyokuwa timu nyingine. Ingawa alikuwa na wachezaji waliokuwa na kila aina ya sifa lakini bado walikuwa wakizidiwa uwezo na wachezaji wa timu ya New Bucketts,
Bwana Robinson akaonekana kukasirika, chuki juu ya timu ya New Bucketts ikaanza kuingia moyoni mwake, hakuonekana kuipenda kabisa timu hiyo. Kila siku alikuwa akitamani kuiona timu yake ikiwa juu ya timu zote ambazo zilikuwa zikishiriki katika ligi ya mpira wa wa kikapu ya NBA.
Alijiona kuna kitu cha muhimu ambacho alikuwa akitakiwa kukifanya kwa wakati huo. Alijiona kuwa na sababu zote za kuiangamiza timu hiyo na ifutike katika uso wa dunia ili kuiachia timu yake ya Boston Five itawale mchezo huo.
Kitu ambacho alikifanya katika kipindi hicho ni kuwasiliana na rafiki yake mkubwa ambaye alikuwa akiishi nchini Thailand. Lengo lake kubwa katika kipindi hicho ilikuwa ni kuilipua ndege ambayo wachezaji wa timu ya New Bucketts wangeitumia katika kipindi ambacho wangeelekea nchini China kwa ajili ya mashindano ya dunia ya mpira wa kikapu.
Wiki moja ilikuwa imebakia hata kabla ya timu ya mpira wa kikapu ya New Bucketts kusafiri kuelekea nchini China. Mipango ikaanza kufanywa kwa haraka haraka huku ikiwa chini ya Mzee Kalaway ambaye alikuwa nchini Thailand.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kitu alichokifanya mzee Kalaway ni kuwasiliana na kundi la waasi nchini humo, kundi la Lampang ambalo lilikuwa likiogopwa sana na watu wote waliokuwa wakiishi katika bara la Asia. Mzee Kalaway akaikabidhi kazi hiyo mikononi mwa Lampang. Kazi hiyo ilionekana kuwa rahisi sana katika kundi hilo hivyo wakaamua kufanya kila kitu kitakachowezekana kukamilisha kazi haraka iwezekanavyo.
“Ila alibadilisha maamuzi. Amesema msiilipue ndege. Itekeni na kuipeleka kati msitu mkubwa wa Chian Rai” Mzee Kalaway alimwambia mkuu wa waasi hao wa kundi la Lampang, Mekong.
“Usijali. Kazi itafanyika katika kipindi ambacho watakuwa wakirudi” Mekong alisema.
“Sawa. Hakuna tatizo”
*****
Kila mchezaji alionekana kushtuka, hawakuamini kama kweli Bwana Robinson angekuwa nyuma ya lile tukio ambalo lilikuwa likiendelea. Kila mmoja alionekana kuwa na hasira juu ya mzee Robinson ambaye uso wake muda wote ulikuwa umetawaliwa na tabasamu pana.
Bwana Robinson akaanza kuwaangalia wachezaji wote kana kwamba alikuwa akiwakagua, alipoona ameridhika, tabasamu lile likaongezeka usoni mwake. Kazi kubwa ambayo alikuwa amempa mzee Kalaway ilionekana kukamilika bila kuwa na tatizo loote lile.
“Who wants to go back home? (Nani anataka kurudi nyumbani?)” Bwana Robinson aliuliza.
Hakukuwa na mtu yeyote aliyelijibu swali lile. Kila mmoja alionekana kukasirika, kitendo ambacho alikuwa amekifanya Bwana Robinson kilionekana kuwakasirisha. Walimwangalia kwa macho makali huku kila mmoja akionekana dhahiri kukasirika.
“Who wants to go back home? (Nani anataka kurudi nyumbani?)” Bwana Robinson aliuliza swali lile kwa mara ya pili.
Mkono ukaonekana kuwa hewani, Bwana Robinson akaangalia vizuri ili kufahamu mtu ambaye alikuwa amenyoosha mkono, alikuwa Simpson, mchezaji wa akiba wa timu hiyo. Bwana Robinson akaanza kupiga hatua, bado tabasamu lilikuwa likiendelea kuwa usoni mwake.
Alipomfikia Simpson, akaanza kumwangalia kuanzia juu hadi chini. Simpson akaanza kubadilika kiasi ambacho mpaka akaanza kujuta sababu iliyomfanya kunyoosha mkono. Bwana Robinson hakutaka kuongea kitu chochote katika kipindi kile ambacho alikuwa akimwangalia Simpson.
“Did you go to church last month? (Ulikwenda kanisa mwezi uliopita?)” Bwana Robinson alimuuliza Simpson.
“Yeah”
“What did your teacher say in Sunday School Service? (Mwalimu wako wa shule ya Jumapili alisemaje?)” Bwana Robinson aliuliza.
“He taught us about forgiveness (Alitufundisha kuhusu msamaha)” Simpson alijibu huku akionekana kuwa na wasiwasi.
Tabasamu lile lililokuwa usoni mwa Bwana Robinson likaongezeka zaidi na zaidi, alionekana kufurahia majibu aliyokuwa akiyatoa Simpson. Akaupeleka mkono wake katika kiuno chake, akatoa bastora yake na kuanza kuiangalia.
“You have to go home (Inabidi uende nyumbani)” Bwana Robinson alimwambia Simpson.
Kila mchezaji akaonekana kushangaa, hawakuamini kama Simpson angeweza kupata nafasi kama ile ambayo alikuwa amepewa. Simpson akaanza kupiga hatua kuufuata mlango wa kutokea katika gofu lile huku akionekana kutokujiamini.
Waasi wale ambao walikuwa karibu na mlango wa kuingilia ndani ya gofu lile wakampisha. Simpson akaanza kuelekea nje ya gofu lile. Bwana Simpson akaanza kupiga hatua kuwafuata wale waasi ambao walikuwa pale karibu na mlango ule na kiasha kuanza kuwaambia kitu kwa sauti ya chini.
Mara waasi wale wakatoka mahali pale na kisha kuelekea nje. Ni ndani ya sekunde ishirini tu, milio ya bunduki ikasikika. Kila mchezaji akajua fika kwamba Simpson ndiye ambaye alikuwa amepigwa risasi. Bwana Robinson akaonekana kutabasamu zaidi, kifo cha Simpson kilionekana kumfuraisha.
“But he wanted to go back home. I showed him the shot cut to get there (Lakini alitaka kurudi nyumbani. Nimemuonyesha njia ya mkato kufika huko)” Bwana Robinson aliwaambia wachezaji wale na kuendelea.
“We are strangers in this world...Heaven is our home. Did your pastors tell you that? (Sisi ni wageni katika ulimwengu huu....Mbinguni ndiko nyumbani kwetu. Wachungaji zetu walikwishawahi kuwaambia hivyo?)” Bwana Robinson aliwaambia na kuwauliza.
Bwana Robinson alionekana kuwa na roho ya kinyama hata zaidi ya waasi ambao walikuwa mahali pale, hakuonekana kuwa na huruma hata kwa mtu mmoja. Hakutaka kumuacha mtu yeyote mahali pale, alitaka kumuua kila mchezaji ambaye alikuwa ndani ya gofu lile.
Bado alihitaji kila kitu kiendelee kuwa siri, kama angethubutu kumuacha mtu yeyote hai na kisha kurudi nchini Marekani basi ni lazima angepata matatizo ya kufungwa jela kiungo cha maisha au kunyongwa. Alitakiwa kuwaua wote, na hilo ndilo lengo lake kubwa ambalo alikuwa nalo.
Kwa sababu alikuwa amekwishajulikana kuwa yeye ndiye ambaye alikuwa katika mipango yote ile, basi alikuwa na sababu ya kufanya kila kitu kilichowezakana ili tu kusiwe na mtu yeyote ambaye angekuja kuufahamu ukweli. Bwana Robinson wala hakukaa sana ndani ya gofu lile, alichokifanya ni kuondoka kuelekea nje ya gofu lile pamoja na wale waasi.
Kila mchezaji alionekana kuumia kwa kile ambacho alikuwa amekiona, idadi yao ilikuwa imezidi kupungua. Waliingia ndani ya gofu lile wakiwa watu ishirini na nane, ila kwa sasa walikuwa wamebakia ishirini na sita hasa baada ya Paul na Simpson kuuawa kwa kupigwa risasi.
Wote wakasogeleana na kuanza kuongelea njia ambazo zingewafanya wao kutoroka ndani ya gofu lile. Kwa jinsi hali ilivyokuwa ikiendelea, waliona dhahiri kwamba kulikuwa na uwezekano wa wao wote kuuawa katika gofu lile. Hawakujua ni kwa jinsi gani wangeanikiwa kutoroka ndani ya gofu lile, ila walichokifanya ni kupanga mipango tu.
“Tutaanzaje?” Bruce, nahodha wa timu ile aliuliza.
“Tupigane nao. Nina uhakika kwamba tutawashinda na kutoroka” Phillip alijibu.
“Hilo suala linaweza kuwa gumu Phillip. Hatujui wako wangapi mpaka sasa na pia huko nje wako wangapi. Ila nafikiri nina wazo” Bruce aliwaambia.
“Wazo gani?” Ryan aliuliza.
“Kama kweli tunataka kupigana, basi ni lazima tuanze na wale ambao wanaingia ndani. Mmoja wetu atajificha na wengine tutakuwa tunaangalia jinsi mchezo utakavyokuwa. Lakini subirini. Mbona naona na hiyo inakuwa ngumu!” Phillip alifafanua na kuukosoa ufafanuzi wake.
“Wazo lako zuri Bruce. Ila inabidi kuwe na watu wanne nyuma ya mlango” Wiliams alimwambia.
“Yeah. Hilo wazo zuri sana. Na kama tukiwashinda, tuchukueni silaha zao na sare zao” Bruce alisema na wote kukubaliana.
Mpango wao ambao walikuwa wameupanga haukutakiwa hata mara moja kufanyika mchana hivyo wakasubiri mpaka giza liingie. Kila mmoja alionekana kuwa na presha, giza ndicho kitu ambacho walikuwa wakitamani kuliona kwa wakati huo.
Dakika kwao zilikuwa zikisogea kwa taratibu sana tofauti na siku nyingine zote. Kila mmoja akajiweka tayari kwa mapambano, hawakutaka kuendelea kukaa katika gofu lile ambalo lilikuwa limejaa mbu wakali. Walichokitaka kwa wakati huo ni kuondoka na kurudi nchini Marekani ambako wangeelezea kila kitu kilichokuwa kimewapata.
Dakika kwao zilionekana kwenda taratibu sana tofauti na siku nyingine, walitamani kufanya kile ambacho walikuwa wamekipanga kukifanya kwa haraka iwezekanavyo. Hawakuwa tayari kulala usiku ndani ya gofu lile, kwa siku zile mbili ambazo walikuwa wameishi ndani ya gofu lile zilionekana kuwatosha kabisa.
Usiku ukaingia, kila mmoja akajiweka tayari. Williams, Phillip, Bruce na Ryan wakaelekea nyuma ya mlango kwa ajili ya kuwavamia wale waasi ambao wangeingia ndani ya gofu lile. Wala hazikupita hata saa moja, mara mlango ukasikika ukifunguliwa.
Ufunguaji wa mlango ulionekana kuwa wa tofauti sana wakati mwingine. Mlango ulifunguliwa taratibu sana kana kwamba mfunguaji hakutaka mtu yeyote kusikia. Wote waliokuwa nyuma ya mlango wakajiweka tayari kwa ajili ya uvamizi.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mlango ulipofunguka wote, mwanaume mmoja akaingia. Mkononi hakuwa na tochi wala silaha yoyote ile. Kwa kasi ya ajabu, Williams akamvamia na kumpiga roba. Mwanaume yule alijitahidi kukukuruka katika mikono ya Williams lakini hakuweza kujinasua.
“Chukueni silaha” Williams aliwaambia huku akiwa ameendelea kumkaba mwanaume yule.
“Hana kitu”
“Unasemaje?”
“Hana silaha” Ryan alilirudia jibu lake kwa mara ya pili huku Williams akiwa bado amempiga roba mwanaume yule..
******
Dunia haikuonekana kutulia, kutekwa kwa wachezaji wa timu ya New Rocketts kulionekana kuanza kuleta matatizo. Ukaribu kati ya nchi ya China na Marekani ukaonekana kuanza kuyumba na baada ya muda basi ungomvi mkubwa ungeonekana kuanza kutokea.
Maneno ya chini chini yakaanza kusikika, Wamarekani walikuwa wakiwalaumu Wachina kwa kila kitu kilichotokea. Wachina ambao walikuwa wakiishi nchini Marekani hasa wale waliokuwa wakiishi katika mji mdogo wa China Town wakaonekana kuwa katika wakati mgumu.
Kila siku Wamarekani walikuwa wakiingia katika mji huo na kufanya fujo ambazo kwao zilionekana kama kuwa kisasi. Serikali ya nchi ya China ikaingilia kati, raisi wa nchini China Bwana Tueng Peng akasafiri mpaka nchini Marekani kwa ajili ya kuongea na rais wa nchi hiyo.
Kikao cha dharura kikawekwa na wote kuafikiana kuweka wapelelezi makini ambao wangeweza kujua ni mahali gani ndege ile ilipokuwa imepelekwa. Kila kitu kikakubaliwa, taarifa juu ya maamuzi yale zikatangazwa katika vyombo vya habari huku Wamerekani wakitakiwa kuacha fujo katika mji wa China Town.
Wapelelezi waliokuwa na uwezo mkubwa ambao walikuwa wamekwishastaafu wakarudishwa kazini kwa ajili ya kupeleleza mahali ambapo ndege ile ilipopelekwa kwa kuamini kwamba huko ndipo kila kitu kingekuwa rahisi kwao. Miongoni mwa wapelelezi ambao walikuwa wamestaafu na kurudishwa kazini alikuwa Bwana Samuel Thomas ambaye mara zote alikuwa akihitaji kuitwa kwa jina la Sam.
Sam ndiye ambaye alikuwa mpelelezi aliyekuwa akiaminiwa katika kazi ya upelelezi kuliko mpelelezi yeyote yule nchini Marekani. Upelelezi wake mkubwa wa kujua mahali ambapo Saddam Hussein alipokuwa amejificha, kujua sehemu ambayo Osama Bin Laden alipokuwa amejificha ndicho kitu kilichopelekea kuaminiwa na kuonekana kuwa mpelelezi aliyekuwa na uwezo mkubwa.
Mpelelezi Sam hakuwa na sifa hizo tu. Kwa kipindi chote ambacho alikuwa amefanya kazi zake za upelelezi alionekana kuaminika sana kwa kuwa makini kazini. Alifanya upelelezi katika kila kitengo mpaka pale alipopeleleza na kugundua kwamba Iraq, Syria na Palestina walikuwa wakitengeneza silaha za Nyuklia.
Kila mtu alikuwa akimuamini Bwana Sam, katika kipindi chote cha kazi yake hakuonekana kushindwa na upelelezi wowote ule, alikuwa akikamilisha kila kitu na hata kama ushahidi ulikuwa ukihitajika basi alikuwa akiuleta kama uthibitisho.
Mara baada ya kukabidhiwa kazi hiyo, kitu cha kwanza alichokifanya ni kusafiri kuelekea nchini China kwa ajili ya kuanza kazi yake. Kila kitu ambacho kilikuwa kikifanyika kwa kipindi hicho kilikuwa kikifanyika kwa siri kubwa sana, raia wa kawaida hawakujua kama mpelelezi Sam alikuwa tayari amekwishafika nchini China kwa ajili ya kuanza kazi ambayo alikuwa amepewa na serikali kuu ya Marekani.
****
Alizaliwa katika familia iliyokuwa imejaa dhiki kubwa kama familia nyingi zilivyokuwa nchini Thailand. Kamwe hakuwahi kumuona baba yake ambaye aliuawa katika maandamano yaliyokuwa yamefanyika nchini humo mwaka 1999 kwa kumtaka rais wa nchi hiyo Bwana Zukeng aachie madaraka.
Katika maisha yake alikuwa akilelewa na mama yake ambaye alikuwa akimpa kitu chochote alichokuwa akikihitaji. Vijana wengi wa mtaani walikuwa wakimtenga kutokana na umasiki mkubwa ambao alikuwa nao. Akajikuta akipoteza marafiki na hata ndugu ambao alikuwa akiwaamini.
Alifanya kazi mbalimbali kwa ajili ya kujikwambua na maisha ambayo yalikuwa magumu sana. Hapo ndipo alipoamua kuanza kufanya biashara ya kusafiri katika miji mbalimbali kwa ajili ya kununua matunda na kuyaleta Bangkok. Biashara hiyo kidogo ikaonekana kuanza kuyabadiisha maisha yake.
Baada ya miezi miwili, mambo yakaanza kubadilika hasa mara baada ya serikali kutaka kulisafisha jiji la Bangkok. Watu wote ambao walikuwa wakifanya biashara mbalimbali wakatakiwa kuacha kufanya biashara hizo. Kijana huyo, Gong Paa hakuwa na cha kufanya zaidi na yeye kufunga biashara yake.
Maisha ambayo alikuwa akiishi zamani ndio yakawa yamekwisharudi kwa mara nyingine, tena kwa kipindi hiki yalikuwa makali hata zaidi ya kipindi kilichopita. Kila siku Gong akawa mtu wa kwenda huku na kule kwa ajili ya kutafuta fedha kwa ajili ya kumtunza mama yake pamoja na kujitunza yeye mwenyewe.
Kila kitu kikaonekana kubadilika hasa mara baada ya mama yake ambaye alikuwa ndugu na rafiki pekee aliyebaki kuanza kuumwa ugonjwa wa moyo ambao ulikuwa umeanza kuvimba. Gong hakutaka kumuona mama yake akipata shida kiasi ambacho kilimfanya kuangaika zaidi na zaidi.
Hospitalini kulikuwa kukihitajika kiasi kikubwa cha fedha ili mama yake aweze kutibiwa na kupona kabisa. Fedha hazikupatikana kwa sababu zilikuwa kiasi kikubwa sana. Akaanza kumtibia mama yake kwa kutumia dawa za asili za mizizi nyumbani, hiyo wala haikusaidia kwani baada ya miezi mitatu, akafariki dunia.
Hili lilikuwa ni pigo kubwa maishani mwake, hakuamini kama mwanamke ambaye alikuwa amemlea katika kipindi chote tayari alikuwa amefariki. Maisha ya upweke yakaanza kumtawala. Muda mwingi alikuwa akikaa ndani akilia, hakuamini kama kweli asingeweza kumuona mama yake tena katika maisha yake yote yaliyobakia.
Baada ya kukaa kwa kipindi fulani, nchi ikaanza kuingia katika matatizo, waasi wakajitokeza kwa ajili ya kuchukua uongozi wa nchi hiyo baada ya kuona uongozi uliokuwa madarakani ukiyumbayumba. Vijana wengi walikuwa wakiliunga mkono kundi hilo la waasi kiasi ambacho fujo zikaanza kutokea mitaani.
Nchini Thailand, amani yote ikapotea, watu walikuwa wakiuawa mitaani na wengi kujeruhiwa. Mara baada ya kuona mambo yanakuwa makubwa kadri siku zilivyozidi kwenda mbele, Umoja wa Mataifa ukaingilia kati. Mwenyekiti wa Umoja huo Bwana Koffi Annan pamoja na baraza lake wakaa chini na kuamua kuyapeleka majeshi yao nchini Thailand.
Kidogo amani ikaonekana kurudi tena huku waasi wakirudi msituni kwa ajili ya kujipanga tena. Vijana wengi nchini Thailand walikuwa wakitekwa na kupelekwa msituni kujiunga na jeshi hilo ambalo lilikuwa likiongezeka kadri siku zilivyozidi kwenda mbele. Gong akawa mmoja wa vijana waliojiunga na kundi la waasi hao.
Huku wakiwa wamefika idadi ya watu elfu hamsini, msitu ukavamiwa na wanajeshi wa Serikali iliyokuwa madarakani, waasi wengi wakauawa na wengine kukimbia. Hapo ndipo wale waasi waliosalimika kuanza kujikusanya upya.
Kwa sasa malengo yao yalikuwa yamebadilika, hawakutaka kupigana kwa ajili ya kuutaka uongozi wa nchi hiyo, wao walikuwa wakielekea mijini kuwateka watoto wa viongozi na matajiri na kisha kuhitaji kiasi kikubwa cha fedha. Kwa hatua hii ambayo walikuwa wamefikia, tayari walikuwa wamejiingizia kiasi kikubwa cha fedha kiasi ambacho hata vijana wale wakaanza kulipwa vizuri.
Kama kulikuwa na tukio lolote ambalo lilikuwa likitakiwa kufanyika hasa kwa shughuli za utekaji, kundi hili ilikuwa likihusika vilivyo huku tayari wakiwa wamekwishalipwa kiasi ambacho kilitakiwa kulipwa. Mpaka katika kipindi ambacho ndege waliyokuwa wachezaji wa timu ya mpira wa kikapu ya New Bucketts ilipotekwa, Gong alikuwa miongozi mwa watekani wale.
Ingawa alikuwa amehusika lakini kwa wakati huu Gong hakuonekana kuupenda utekaji huu. Kitu cha kwanza alikuwa akipenda sana mchezo wa mpira wa kikapu huku timu hiyo ya New Bucketts ikiwa ndio timu ambayo alikuwa akiipenda kuliko timu yoyote ile.
Kila siku katika maisha yake alitamani sana kwenda nchini Marekani kuiona timu hiyo ikicheza huku akitamani hata vitabu vyake na nguo zake ziwe na saini ya wachezaji wa timu hiyo. Kutekwa kwa wachezaji wale na kuletwa mule akaona kabisa kwamba ni lazima wachezaji wale wote wangeuawa.
Hakutaka kabisa kuliona jambo hilo lilkitokea kitu ambacho kikamfanya kutafuta namna ya kuwatorosha wachezaji hao. Hakujua ni kwa namna gani alitakiwa kufanya lakini akaona ni lazima awaokoe kwa gharama yoyote ile hata kama ingemgharimu maisha yake.
Usiku wa siku hii ndio ilikuwa siku ambayo alikuwa ameipanga kuwaokoa wachezaji hao. Baada ya saa mbili usiku kuingia, moja kwa moja akaanza kuelekea katika gofu lile huku akihakikisha hakukuwa na mtu yeyote ambaye alikuwa akimuona.
Mikononi wala hakuwa na silaha kutokana na kuogopa kuhisiwa vibaya na wachezaji wale. Alipoufikia mlango, akaufungua taratibu na kuingia ndani. Alipoingia, akashtukia akipigwa roba kali.
“Chukueni silaha” Williams aliwaambia huku akiwa ameendelea kumkaba Gong.
“Hana kitu”
“Unasemaje?”
“Hana silaha” Ryan alilirudia jibu lake kwa mara ya pili huku Williams akiwa bado amempiga roba Gong.
Gong akatamani kuongea kitu, roba ile ilimfanya kushindwa kuongea zaidi ya kuanza kurusha rusha miguu yake huku na kule. Tayari alikwishaona kwamba kama asingefanya kitu basi ni lazima angeuawa huku akijiona. Kwa kutumia nguvu zake, akaanza kuitoa roba ya Williams huku akijiyumbisha huku na kule.
Akafanikiwa kuitoa roba ile kwa kumrusha Williams mbele yake kwa kumpitishia mgongoni mwake. Kila mchezaji akaonekana kuogopa kwani walijua kwamba ni lazima Gong angetoka nje na kuwaamia wenzake kile ambacho kilikuwa kimetokea.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kooo... kooo ... koooo...” Gong akaanza kukohoa huku akijishika shingoni mwake.
Akayainua macho yake na kuanza kuwaangalia wachezaji wale, kila mmoja alionekana akiwa na wasiwasi. Katika hali ambayo ilionekana kuwashangaza, Gong akaanza kutoa tabasamu pana. Kutokana na kutojua lugha ya kingereza, akaanza kuonyesha vitendo ambavyo vilimaanisha kwamba alikuwa mahali hapo kuwasaidia kuondoka ndani ya gofu hilo.
“I got him (Nimemuelewa)” Williams aliwaambia wenzake.
Kilichofuatia hapo ni kuanza kupanga namna ya kuondoka mahali hapo huku Gong akiendelea kuwaambia kwa vitendo. Wote ishirini na saba wakatoka kwa kunyata huku wakiinama inama. Wakaanza kuelekea katika kichaka ambacho kilikuwa pembeni ya gofu lile na kisha kuanza kukimbia porini.
Kila mchezaji alionekana kushangaa, hawakuamini hata kidogo kama kazi ingekuwa rahisi namna ile. Huku wote wakiwa wakikimbia porini wakiongozwa na Gong, wakashtukia milio ya risasi ikianza kusikika nyuma yao. Walichokifanya ni kuanza kuongeza kasi kuelekea porini zaidi.
Idadi kubwa ya waasi ilikuwa nyuma yao ikiwakimbiza. Milio ya risasi ikaendelea kusikika zaidi na zaidi. Ni ndani ya sekunde thelathini tu, mchezaji mmoja baada ya mwingine akaanza kuanguka chini baada ya kushambuliwa na risasi. Mpaka kufikia mwendo wa kilometa mbili, ni wachezaji watatu tu ndio ambao walikuwa wamebaki pamoja na Gong.
“Phillip.... make hurry... (Phillip fanya haraka)” Williams alimwambia Phillip.
“Williams. Am tired. I reather die (Williams. Nimechoka. Bora nife)” Bruce alimwambia Williams.
“Bruce, lets get out of here (Bruce, tuondoke mahali hapa)” Williams alimwambia Bruce ambaye alikuwa ameinama.
“Just go Williams. I cant move my leg. Let me die Williams (Nenda tu Williams. Siwezi hata kuunyanyua mguu wangu. Niache nife tu)” Bruce alimwambia Williams.
“I cant let you die (Siwezi kukuacha kufa)” Williams alimwambia Bruce, akamfuata na kisha kumbeba begani mwake na kuendelea na safari yao ya kuelekea wasipopafahamu.
Bado waasi hawakuonekana kuridhika, walikuwa wakiendelea kuwakimbiza wachezaji ambao walikuwa wamebakia pasipo kujua kwamba Gong alikuwa miongoni mwa wale wachezaji. Waliendelea kuachia risasi ambazo zilikuwa zikiwakosa kwa kupiga katika miti.
Baada ya mwendo wa kilometa tano, wakafika katika mto ambao ulikuwa ukikatiza porini pale ulioitwa Ram Nam. Hawakujua kama kina kilikuwa kirefu au la, wakajitosa katika mto ule na kuanza kuogelea. Williams hakutaka kumuacha Bruce, aliogelea nae kuuvuka mto ule mpaka ng’ambo ya pili.
“Williams....stop (Williams... simama)” Phillip alimwambia Williams ambaye akasimama na kumuweka Bruce chini.
Damu zilikuwa zikimtoka Bruce mdomoni kutokana na risasi ambazo zlikuwa zimemuingia mgongoni. Williams akaonekana kushangaa kwani hakujua kama katika kipindi ambacho alikuwa amembeba Bruce, ndicho kilikuwa kipindi ambacho alikuwa amepigwa risasi tatu za mgongoni.
“Let me die Williams (Acha nife Williams)” Bruce alimwambia Williams.
“Pleaseeee. Dont leave us (Tafadhali. Usituache)” Williams alimwambia Bruce huku machozi.
“I have to die Williams. Please....tell Gloria... she is the girl of my dreams and always will be (Inabidi nife Williams. Tafadhali... mwambie Gloria.... yeye ni msichana wa ndoto zangu na siku zote atakuwa)” Bruce alimwambia Williams huku akiivua pete iliyokuwa kidoleni mwake na kumkabidhi.
“This is a symbol of my love (Hii ni alama ya upendo wangu)” Bruce alimwambia.
“Pleaseeee.... dont leave us.... (Tafadhali... usituache....)” Williams alimwambia Bruce lakini kuanzia hapo, Bruce hakufumbua mdomo wake, alikuwa amekwishakufa.
Williams akaonekana kuchanganyikiwa. Akaanza kumtingisha Bruce lakini wala Bruce wala hakuweza kuamka. Phillip akamuinua Wlliams. Kila mmoja akaonekana kuumia, ni kweli walikuwa wamewapoteza wachezaji wengine lakini kwa Bruce ilionekana kuwaumiza zaidi.
Hata kabla hawajafanya kitu chochote, mara milio ya risasi ikaanza kusikika tena. Waasi walikuwa wamekwishaufikia mto ule na walikuwa wamekwishaanza kuuvuka. Hawakuwa na jinsi, walichokifanya ni kuuacha mwili wa Bruce na kuanza kukimbia huku wakiwa wamebakia watatu.
“Rest In Peace Bruce (Pumzika kwa amani Bruce)” Williams alisema huku akikimbia na machozi yakimtoka.
Furaha ya maisha yao ikaonekana kuingia doa, kutekwa kwa mtoto wao , Williams kulionekana kuwaumiza vichwa kupita kawaida. Muda mwingi walikuwa wakikaa ndani ya nyumba yao, hawakutaka kutoka nje kwa kuhofia waandishi wa habari ambao mara nyingi walikuwa wakilandalanda nje ya nyumba yao.
Wakasahau kila kitu kuhusiana na talaka ambayo walikuwa wamepeana kipindi kirefu kilichopita, kwa wakati huo wakaamua kuunganisha nguvu zao katika kupeana moyo na kufarijiana kwa kile ambacho kilikuwa kimetokea katika kipindi hicho.
Mara kwa mara walikuwa wakiangalia taarifa za habari katika vituo mbalimbali vya televisheni. Kwao, waliiona serikali ya nchi hiyo kutojali kitu chochote kile, waliiona serikali kupuuzia kile ambacho kilikuwa kimetokea japokuwa mara kwa mara wananchi wenye hasira kali walikuwa wakipiga kelele na hata kuandamana kutaka serikali ichukue hatua muda wowote ule.
“Moyo wangu umeumia. Moyo wangu umepata kidonda ambacho sidhani kama kuna siku kitakuja kupona” Bi Latifa alimwambia Bwana Kurt ambaye wala hakuwa na sura yoyote yenye tabasamu au furaha yoyote ile.
“Kama watashindwa, haina budi mimi kama mimi nisafiri hadi nchini China kwa ajili ya kuangalia kile kilichokuwa kimetokea. Kamwe sitoweza kubaki nyumbani na wakati sijui kitu gani kimemtokea mwanangu” Bwana Kurt alisema.
“Kama ukienda huko, na mimi nitakwenda pamoja nawe” Bi Latifa alimwambia.
“Hapana mpenzi. Baki nyumbani unisubiri” Bwana Kurt alimwambia Bi Latifa.
Jina la mpenzi ambalo alikuwa ameitwa Bi Latifa likaonekana kumtia moyo, hakuamini kama mtalaka mwenzake huyo kuna siku angelitamka jina hilo ambalo alikuwa akilitamka katika miaka kadhaa iliyopita, kwake akaonekana kufarijika kupita kawaida, ila kutokana na hali waliyokuwa nayo katika kipindi hicho, faraja ile ikapotea ghafla.
“Na mimi ninataka kujua kuhusu mtoto wangu pia. Utakwenda vipi peke yako, nataka kuwa ubavuni mwako mpenzi, nataka tuendelee kufarijiana mpaka pale kila kitu kitakapokuwa tayari” Bi Latifa alimwambia Bwana Kurt.
Bwana Kurt hakujibu chochote kile, alitamani sana kuelekea nchini China ili kujua ni kitu gani ambacho kilikuwa kimetokea nchini kule mpaka ndege waliyopanda wachezaji akiwepo mtoto wake, Williams kutekwa na kutojulikana mahali ilipo mpaka kipindi hicho.
Wakakubaliana kwa pamoja kwamba siku inayofuata ni lazima wasafiri mpaka nchini China kujua ni kitu gani ambacho kilitokea na kama ikiwezekana basi waanze kufanya utafiti ili kujua mahali ambapo ndege hiyo ilipokuwa imepelekwa.
Siku iliyofuata wakafuatilia taratibu zote za safari na kisha kukata tiketi katika shirika la American Airways na safari ya kuelekea nchini China kuanza mara moja. Ndani ya ndege walikuwa wamekaa katika daraja la juu kabisa, hawakuona sababu yoyote ya kupata usumbufu, walihitaji kukaa peke yao kwa ajili ya kuvipumzisha vichwa vyao ambavyo wala havikuwa vimetulia kabisa.
Ndege ilitumia masaa ishirini na saba mpaka kufika nchini China ambako wakateremka na kuanza kuelekea katika hoteli ya Binshung ambayo ilikuwa kaskazini mwa jiji la Shanghai. Wakachukua chumba kimoja na kisha kulala huku wakiisubiri siku inayofuatia kuanza kazi yao ya kujua ni kitu gani ambacho kilikuwa kimetokea.
****CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kazi ilikuwa kubwa sana mbele yake, hakuhitaji kufanya haraka hata mara moja, alihitaji kuifanya kwa utulivu mkubwa sana mpaka kuona anaikamilisha. Alichokifanya mpelelezi Sam mara baada ya kuamka ni kuanza kuelekea katika uwanja wa ndege wa Shanghai kwa ajili ya kupata ratiba nzima ya siku ambayo ndege ile ilipokuwa imeondoka uwanjani hapo.
Kupata ratiba nzima ya siku hiyo wala haikuwa kazi kubwa sana, akaipata na kuanza kurudi hotelini. Alichokifanya katika kipindi ambacho alikuwa njiani ni kununua magazeti kadhaa ambayo yalikuwa yameandika kuhusu utekaji ule na kurudi nayo.
Akaanza kulipita gazeti moja baada ya jingine, alipohakikisha ameyaelewa, akalifungua begi lake na kutoa karatasi kubwa ambalo lilikuwa limechorwa ramani nzima ya dunia. Akaanza kuiangalia ramani ile huku akiitupia macho ramani ya nchi ya China.
“Kwa kuwa marubani walikuwa wametekwa na kufungiwa chooni, basi ni lazima ndege hiyo ilipoanza kupaa ilikuwa ikipaa kuelekea katika upande ambao ndege yoyote iliyotaka kuelekea Ulaya inapoelekea. Isingeweza kupaa na kuelekea upande mwingine, kwani kama wangefanya hivyo basi ni lazima watu hasa wale wanaoongoza ndege kushikwa na wasiwasi. Kwa hiyo, kwa namna moja au nyingine ndege hii imeweza kutekwa na kupelekwa nchini Thailand, Vietnam, Malaysia au hata India” Sam alikuwa akiongea na bosi wake simuni.
“Kweli inawezekana ndege kupelekwa katika nchi hizo? Mbona zinaonekana hazina historia yoyote ya mambo ya fujo?” Bosi aliuliza.
“Ngoja nikwambie kitu. Nchi hizi ndizo zinaongoza kuwa na misitu mikubwa duniani. Achana na Marekani ya Kusini ambako kuna msitu mmoja mkubwa, nchi hizi ndizo zina misitu mingi sana. Unakumbuka matukio yaliyotokea nchini India katika kipindi kile cha Ghandhi? Unakumbuka wale viongozi waliotekwa na kupelekwa katika misitu ile nchini India na kuuawa? Utasemaje kuhusu Malaysia, nchi ambao inaongoza kuwa na misitu ambayo ina miti minene. Unalikumbuka lile basi lililowabeba wanachuo wa chuo kikuu cha Malaysia na kisha kupelekwa katika moja ya misitu hiyo na kuuawa kikatili kwa kukatwa vichwa vyao?” Sam alimuuliza bosi wake.
“Nakumbuka kila kitu” Bosi alijibu.
“Sawa sawa. Unakumbuka miaka miwili iliyopita watoto wa viongozi na matajiri walivyokuwa wakikamatwa na kupelekwa katika misitu mikubwa nchini Thailand na watekaji kuhitaji kiasi fulani cha fedha? Unakumbuka au haukumbuki?” Sam aliuliza.
“Nakumbuka”
“Safi sana. Ninafikiri hata ndege hiyo itakuwa imetekwa na kupelekwa katika moja ya nchi hizo. Amini hilo mkuu” Sam alimwambia bosi wake.
Ukimya ukatawala kwa muda fulani kuashiria kwamba bosi alikuwa akijifikiria kitu fulani. Baada ya muda fulani, kikohozi cha kizushi kikaanza kusikika kutoka kwake. Maneno ambayo alikuwa ameongea Sam yalionekana kuwa na ukweli asilimia mia moja.
“Kwa hiyo utaanza na nchi gani?”
“Kazi rahisi sana”
“Kazi rahisi. Unasemaje kazi rahisi na wakati inaonekana kuwa ngumu” Bosi aliuliza kwa mshangao.
“Unaniamini?”
“Ndio. Nakuamini”
“Basi amini ninavyokwambia kwamba kazi rahisi sana”
“Sawa” Bosi aliitikia kiunyonge kwani kwake tayari kazi ilionekana kuwa ngumu kwa kuona kwamba Sam asingeweza kwenda katika misitu ya nchi zote kwa ajili ya kutafuta mahali ndege iliyotekwa na kupelekwa.
“Nipe masaa matano tu, nitakwambia ndege umepelekwa nchi gani?”
“Una uhakika?”
“Asilimia mia tatu hamsini”
“Sawa”
****
Bwana Robinson alikuwa ndani pamoja na kiongozi wa waasi wale. Walikuwa wameweka kikao cha dharura namna ya kuwaua wachezaji wale pasipo yeyote kusalimika. Kitu ambacho alikuwa amekiangalia ni ulinzi wa maisha yake tu.
Ingawa maamuzi yangetolewa kwa haraka sana na kikao kumalizika lakini wakajikuta wakitumia hadi masaa matatu ndani ya chumba hicho huku Kalaway akiwa pembeni akiendelea kuwasikiliza huku nae mara chache akichangia kile alichokuwa akikifahamu.
Uamuzi ukaafikiwa kwamba usiku huo ndio ulikuwa usiku wa mwisho kwa wachezaji wale kuvuta pumzi za dunia hii, walitakiwa kuuawa kwa stali ya kuchomwa moto ndani ya gofu lile, hayakutakiwa kuonekana hata majivu yao.
Huku giza likiwa limekwishaingia na kwa mbali sauti ya jenereta likisikika, mara ghafla wakasikia sauti za milio ya bunduki. Kwa kasi ya ajabu, wote wakachomoka kutoka ndani ya chumba kile na kwenda nje kuona ni kitu gani ambacho kilikuwa kikiendelea mahali hapo.
Mara ya kwanza walidhani kwamba kundi la wanajeshi wa serikali ya Thailand walikuwa wamevamia msituni hapo na kuanza kushambuliana na risasi na waasi wale, lakini walipoyatuliza vizuri macho yao, wakawaona waasi wakianza kukimbia kuelekea msituni huku milio ya risasi ikiendelea kusikika.
“Kuna nini?” Mekong alimuuliza mmoja wa waasi wale.
“Wanatoroka” Muasi mmoja alisema na kisha kuendelea kukimbia kuelekea msituni.
Kila mmoja akaonekana kushtuka ila kwa Bwana Robinson akashtuka zaidi kuliko wenzake. Kwa kasi ya ajabu nae akaanza kukimbia kuelekea msituni. Kwa kila mchezaji ambaye alikuwa akipigwa risasi alikuwa akihesabu.
Idadi kubwa ya wachezaji walikuwa wamepigwa risasi na walikuwa wamebakia wachezaji watatu tu ambao walikuwa wakikimbia kwa kasi kuelekea msituni zaidi. Bwana Robinson akawaona waasi wale kama hawakuwa na shabaha hali ambayo ilimpelekea na yeye kuchukua bunduki yake na kuanza kushambulia.
Muda ulikuwa ukizidi kwenda huku umbali wa wao kukimbia ukizidi kuongezeka, wale wachezaji watatu ambao walikuwa wamebakia bado hawakuwa wamepatikana japokuwa kwa mbali walikuwa wakiwaona wakizidi kukimbia.
Wakafika katika mto Ram Nam, wakajaribu kuangalia huku na kule, kwa kutumia msaada wa mwezi, wakafanikiwa kuwaona wachezaji wale wakiwa ng’ambo ya pili. Wakaanza kuwashambulia kwa risasi kwa mara nyingine huku nao wakianza kuvuka mto ule.
Bwana Robinson akaonekana kuchanganyikiwa zaidi na zaidi, hakuelewa ni kitu gani ambacho alitakiwa kukifanya. Kumuacha hai mchezaji yeyote kwake ilionekana kuwa hatari kubwa sana ya kufungwa jela maisha au adhabu ya kunyongwa.
Yeye ndiye alikuwa wa kwanza, yaani alikuwa kama kamanda mkuu ambaye alikuwa akiwaongoza waasi wale. Walipofika ng’ambo ile, ni mwili wa Bruce tu ndio ambao ulikuwa ukionekana mbele yao. Kwa hasira ambazo alikuwa nazo kwa kipindi hicho, akaumiminia risasi tatu za kichwa na kisha kuendelea na safari ya kuwakimbiza wengine.
****
Williams, Phillip na Gong bado walikuwa wakikimbia kwa mwendo wa kasi kuelekea mbele zaidi. Milio ya risasi ambayo walikuwa wakiisikia iliwafanya kuongeza kasi zaidi na zaidi. Ingawa wote walikuwa wamechoka kupita kawaida, lakini hakukuwa na mtu yeyote ambaye alikuwa radhi kusimama.
Walikimbia zaidi na zaidi kwa umbali kama kilometa kumi, wakaamua kutafuta kichaka na kujificha kwa tahadhari kubwa. Walijiona kuwa na kila sababu ya kuvuta pumzi kabla ya kuendelea na safari ya kuelekea wasipopafahamu.
Walikaa katika kichaka kile kwa dakika tano, wakaendelea na safari yao ya kuelekea msituni zaidi. Kila mmoja alijua kwamba waasi wale walikuwa wamekata tamaa ya kuwakimbiza kwa umbali ule pasipo kuwakamata, hivyo wakaamua kupunguza mwendo na kukimbia kwa kasi ya kawaida.
“Tuombe Mungu tukute kijiji chochote kile” Williams alimwambia huku wakiendelea kukimbia zaidi.
“Naona bado mbali sana mpaka kukifikia kijiji chochote” Phillip alimwambia Williams.
Ingawa hakukuonekana kuwa na dalili za kijiji chochote kile lakini bado waliendelea kukimbia zaidi na zaidi. Walitamani waongee na Gong na kuwaeleza kule ambako alikuwa akielekea pamoja nao lakini tatizo lilikuwa ni kutokuelewana kwa lugha zao.
Mpaka inafika saa kumi Alfajiri, hakukuwa na dalili za kijiji chochote kile mbele yao. Bado miti mikubwa na mirefu, nyasi nyingi na ndefu zilikuwa zimetapakaa katika eneo lote ambalo walikuwa wakilitumia.
Baada ya kuendelea kwa mwendo mrefu, wakafika katika sehemu ambayo ilikuwa na uwazi mkubwa kama mita mia tatu na ishirini. Wakaliangalia vizuri eneo lile, wakagundua kwamba lilikuwa ni shamba kubwa la mpunga.
Kila mtu akawa na uhakika kwamba tayari walikuwa wamefika katika eneo ambalo kulikuwa na uhakika kwamba kuna makazi ya watu karibu na lile shamba. Walichokifanya ni kuendelea mbele huku kila mmoja akitegemea kukikuta kijiji chochote mbele yao.
Walikuwa wakikimbia kwa matumaini makubwa mioyoni mwao, ila kadri walivyozidi kukimbia, hawakuona dalili zozote za kijiji. Wakaonekana kukata tamaa, wakatamani kupumzika kwa muda kabla ya kuendelea na safari ya kusonga mbele zaidi.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kwa mbali nyuma yao wakaanza kusikia vishindo kadhaa vya watu wakija kule ambapo walipokuwa. Moja kwa moja wakafikiria kwamba watu hao walikuwa wale waasi ambao walikuwa wakiwakimbia, wakaanza kukimbia tena, kwa kasi zaidi ya ile ya mara ya kwanza.
Mawazo yao yalikuwa sawa sawa na uhalisia wa mambo. Milio ya risasi ikaanza kusikika upya. Kasi zao zikaongezeka zaidi, kila mmoja alikiona kifo kikiwa karibu nae. Wakafika katika sehemu ambayo kulikuwa na barabara imekatiza, kila mmoja hakujua waivuke barabara na kuendelea na safari yao au waanze kuifuatilia barabara ile mpaka huko itakapoishia.
Walichokubaliana ni kuivuka barabara ile na kusonga mbele zaidi. Mwanga wa mwezi ambao ulikuwa ukiwasaidia sana kuona mbele ukaanza kufifia na hatimae kupotea kabisa, mbele yao wakaanza kuliona giza nene.
Wakaanza kukimbia kwa hisia. Waliendelea kukimbia zaidi na zaidi, mara ghafla Phillip akaanguka chini na kuanza kulia kama mtoto mdogo. Kelele zile zikawafanya Williams na Gong kusimama na kuanza kurudi nyuma.
“Kuna nini?” Williams aliuliza huku Phillip akiwa chini akilia.
“Mguu wangu” Phillip alijibu huku akiugulia kwa maumivu makali.
“Umefanya nini?”
“Maumivu. Uangalie” Phillip alimwambia Williams.
Hakukuwa na kupoteza muda tena, kwa haraka sana Williams akainama na kuanza kuuangalia mguu wa Phillip. Mguu ulikuwa umebanwa na mtego wa wa chuma wa kunasia wanyama porini, damu zilikuwa zimeanza kumtoka.
Kila ambavyo Phillip alivyojitahidi kuutoa mguu wake katika mtego ule wa chuma na ndivyo ambavyo maumivu yalivyozidi kuongezeka zaidi na zaidi. Mtego ulikuwa mgumu kutoka mguuni mwa Phillip, mfupa wa mguu wake ukaonekana kama kuanza kuvunjwa kadri alivyojaribu kujinasua.
“Usilazimishe kuutoa mguu..... kadri unavyoulazimisha na ndivyo unavyozidi kuuma” Phillip alimwambia Williams.
Mara vishindo vya watu vikaanza kusikika tena kutoka kule walipotoka. Kila mmoja akaonekana kushtuka, hawakuamini kama waasi wale walikuwa wamekwishawafikia. Williams alitamani kukimbia lakini hakuona kama lingekuwa jambo jema kumuacha Phillip mahali pale peke yake.
“Endelea na safari Phillip. Acha mimi nife huku porini” Phillip alimwambia Williams huku akilia kama mtoto.
“Haiwezekani. Kama watakuua, acha watuue wote. Siwezi kukuacha Phillip” Williams alimwambia Phillip huku nae akianza kulengwa na machozi.
“Ondoka Williams. Endelea na safari. Niache nife peke yangu mahali hapa” Phillip aliendelea kumwambia Williams.
“Haiwezekani. Sitoweza kukuacha. Kama watakuua, niko tayari kufa pamoja nawe” Williams alimwambia Phillip.
Alichokiongea Williams ndicho ambacho kilichotokea, hakutaka kuondoka mahali hapo, aliona ni afadhali auawe mahali pale pamoja na Phillip kuliko kumuacha. Aliukumbuka urafiki wao mkubwa ambao ulianzia toka walipokuwa watoto, walisoma wote na kucheza pamoja, ilionekana kuwa ngumu kumuacha Phillip porini pale.
“Ninakufa leo Williams. Sikujua kama mwisho wa maisha yangu ungekuwa huku porini. Sikutarajia katika maisha yangu kwamba kuna siku nitakufa porini na kisha ndege kuula mwili wangu. Sikutarajia Williams” Phillip alimwambia Williams maneno ambayo yalionekana kumchoma.
“Kama ndege wataula mwili wako, acha waule wangu pia, ila kukuacha mahali hapa peke yako, hakika haitowezekana” Williams alimwambia Phillip huku akimshika mkono na wote wakilia.
Gong alikuwa pembeni akitetemeka, hakujua afanye nini kwa wakati huo. Ni kweli kwamba alitamani kuondoka kukiepuka kifo lakini kila alipokuwa akifikiria kwamba alikuwa pamoja na wachezaji ambao alikuwa akiwapenda sana katika maisha yake, aliona ilikuwa bora kuuawa pamoja nao.
Kwa kipindi kirefu alikuwa akihitaji saini zao, hakutarajia kama kuna siku ambayo angekutana nao ana kwa ana. Muda wote moyo wake ulikuwa ukimlaumu Mungu kwa kumkutanisha na watu hao katika kipindi kigumu kama kile.
Alijua kwamba kama wangesalimika na kuendelea na safari yao, basi kungekuwa na uhakika wa yeye kuhama nchini Thailand na kuhamia nchini Marekani bila matatizo yoyote yale. Kitu ambacho alikuwa akitakiwa kukifanya ni kutoa msaada kwa kila ulipohitajika.
Sekunde ziliendelea kwenda mbele na hatimae wale watu ambao walikuwa wakiwakimbiza kukaribia. Walisikia vishindo vile vya watu vikiwa vimewakaribia kabisa. Watu zaidi ya kumi wakaingia katika kichaka kile na kusimama mbele yao huku nao wakionekana kuchoka kwa kukimbia kwa muda mrefu.
“Mlifikiri mngeweza kutukimbia zaidi? Mmeshindwa. Mko katika mikono yetu” Sauti ya mwanaume mmoja ilisikika. Hata kabla hawajaongea chochote kile, wote wakapigwa na vitako vya bunduki usoni, wakapoteza fahamu pasipo kujua ni kitu gani kiliendelea baada ya hapo.
Mpelelezi Sam hakutaka kubaki hotelini, mara baada ya kukata simu, moja kwa moja akaanza kuelekea nje ya hoteli ile ambapo akakodi teksi ambayo ikaanza kumpeleka mpaka katika uwanja wa ndege wa Shanghai.
Mara baada ya kuteremka garini, moja kwa moja akaanza kupiga hatua kuelekea ndani ya jengo hilo. Hakutaka kuelekea katika sehemu ya watu wanapokaa kusubiria ndugu zao ambao walikuwa wakiingia na ndege uwanjani hapo, bali alipokwenda yeye ni katika idara ya ulinzi katika uwanja huo.
Akatoa kitambulisho chake na moja kwa moja kuruhusiwa kuingia ndani ya chumba hicho. Akaanza kuongea na mkuu wa kitengo kile cha usalama huku akionekana kutaka kufahamu mambo mengi zaidi kuhusiana na ratiba nzima ya siku ile ambayo ndege ilikuwa imetekwa.
Alipoelezwa kila kitu, akawaulizia marubani wale ambao walikuwa wametekwa na kufungiwa katika vyumba vilivyokuwa ndani ya uwanja huo huku wakiwa wamewekewa gundi ya karatasi midomoni mwao na watekaji wale.
Mpelelezi Sam akaanza kupelekwa katika chumba maalumu ambacho walikuwa wamewekwa marubani wale wakisubiri safari yao kuelekea nchini Marekani kwa ajili ya kuelezea kila kitu ambacho kilikuwa kimetokea.
Sam akaingia ndani ya chumba kile, marubani wote wakasimama na kuanza kumsalimia. Amani ikaanza kuonekana nyusoni mwao, kumuona Mmarekani mwenzao akiingia ndani ya chumba kile kulionekana kuwafariji.
“Kuna vitu vichache ningependa kufahamu kuhusu watekaji” Sam aliwaambia.
“Vitu gani?” Kenneth aliuliza.
“Kuhusu hawa watekaji. Hivi mliweza kuwaangalia nyusoni mwao?” Sam aliwauliza.
“Ndio” Benard alijibu.
“Mnavyohisi watakuwa ni watu wa nchi gani?” Sam aliuwaliza.
Swali lile likawafanya wote kuanza kuangaliana usoni, hawakujua watoe jibu gani. Si kwamba jibu hawakuwa nalo, hapana, walikuwa nalo ila lilionekana kuwachanganya vichwani mwao. Sam akabaki akiwaangalia tu, kitu alichokuwa akisubiri mahali hapo ni jibu la marubani hao ili ajue wapi pa kuanzia.
“Tatizo watu wa huku Asia wamefanana sana” Kenneth alijibu Sam.
“Kivipi?”
“Mimi kama mimi sifahamu kama wale walikuwa ni wachina, Wathailand, Wataiwan au Wamalaysia. Yaani nawaona wamefanana sana hata kuwatofautisha siwezi” Kenneth alimwambia.
“Ina maana hata hamuwezi kujua kabisa?” Sam aliuliza.
“Inawezekana wakawa Wathailand. Lugha yao haikuwa ngeni kuisikia masikioni mwangu” Huth ambaye alikuwa amekaa kimya alijibu.
“Kumbe mliwasikia walivyokuwa wakiongea?”
“Ndio, ila hatukuwa tukiwaelewa. Waliingia ndani ya chumba chetu cha kubadilishia nguo kwa ajili ya safari ya kurudi nchini Marekani, wakatuweka chini ya ulinzi, baada ya kuongea wenyewe kwa wenyewe, wakatuvutisha vitambaa ambavyo vilikuwa na sumu kali puani mwetu, baada ya hapo hatukelewa ni kitu gani kilichoendelea” Huth alisema.
“Kwa hiyo mna uhakika kwamba wanaweza kuwa Wathailand?” Sam aliwauliza huku akitaka uhakika zaidi.
“Ndio” Kenneth alijibu.
Mpelelezi Sam hakutaka kupoteza muda wake mahali hapo, alichokifanya ni kuondoka ndani ya chumba kile kurudi katika ofisi ya mkuu wa ulinzi mahali pale na kisha kumuaga. Safari ya kuelekea katika hoteli aliyofikia ikaanza huku akiiona kazi yake kuanza kukamilika.
Akaingia ndani ya chumba kile na kujilaza kitandani. Akaanza kuwaza namna ambavyo angeweza kusafiri mpana nchini Thailand ambako huko aliona dhahiri kuwa na kazi kubwa mbele yake. Alihitaji kuifanya kazi kwa haraka sana na kuimaliza yote. Kamwe hakutaka kuichafua sifa yake ambayo alikuwa amejiwekea, alihitaji kuendelea kuheshimika katika Shirika hilo la kipelelezi la F.B.I
Baada ya kujilaza kwa muda fulani pale kitandani, akasimama na kuichukua simu ya mezani na kuomba kupiga simu ya Kimataifa, baada ya muda wa sekunde chache simu ikaanza kuita. Wala haikuchukua sekunde nyingi, sauti nzito ikaanza kusikika kutoka upande wa pili.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Umefikia wapi?” Bosi wake alimuuliza hata kabla ya salamu.
“Kwanza ningependa kujua mpaka sasa ni masaa mangapi yamekatika toka nilipoomba muda kutoka kwako” Sam aliuliza huku akionekana kuwa na furaha.
“Ulisema nikupe masaa matano. Mpaka sasa ni saa moja na nusu ndilo limekatika. Kwa hiyo yamebakia masaa matatu na nusu” Bosi alijibu.
“Sawa sawa. Kama nilivyokwambia kwamba kazi haikuwa ngumu ndivyo ambavyo nilivyo ilivyotokea. Kazi ilikuwa ndogo sana na niliifanya ndani ya dakika tano tu. Ila ninachotaka kukifanya sasa hivi ni kusafiri kuelekea nchini Thailand” Sam alisema.
“Umepata taarifa kwamba wapo huko?”
“Ndio”
“Kwa hiyo unataka kusafiri lini?”
“Leo. Nataka ndani ya saa moja nianze safari. Kitu cha msingi ninaomba uwasiliane na wahusika ili kila kitu kikamilike” Sam aliwaambia.
“Sawa”
Sam akatulia kitandani, baada ya nusu saa, akasikia mlango ukigongwa, alipokwenda kuufungua, mwanaume mmoja alikuwa amesimama mlangoni huku akiwa na bahasha ya kaki iliyokuwa ngumu. Akamkabidhi bahasha ile ambayo ilikuwa na dokumenti zote za vibali vya kuingia nchini Thailand.
Baada ya dakika arobaini na tano alikuwa ndani ya ndege ya shirika la Fly Emirates akisafiri kuelekea nchini Thailand. Kutokana na umbali kuwa mdogo na ndege kuwa na uwezo mkubwa, ni ndani ya masaa mawili tu wakawa wamekwishafika katika uwanja wa Bangkok nchini Thailand.
Moja kwa moja akachukua bajaji ya kukodi na kisha kutaka kupelekwa katika hoteli moja ya hali ya juu iliyokuwa katika jiji hilo. Walitumia dakika ishirini, bajaji ikasimama mbele ya hoteli moja kubwa ambayo ilikuwa na maneno makubwa yaliyokuwa yakisomeka THE BAVARIANS ambayo ilikuwa ikimilikiwa na Bwana Henrick, raia wa Uingereza ambaye alikuwa akijihusisha na mambo ya kuuza magari, meli na hata ndege, alikuwa dalali mkubwa aliyekuwa akijulikana kila sehemu.
Akachukua chumba kimoja cha hali ya juu na kisha kuanza kujipanga ni kwa namna gani angeanza kazi ambayo ilikuwa mbele yake. Akainuka na kuanza kwenda mbele ya kompyuta yake, website ambayo aliifungua ilikuwa GOOGLE. Akaanza kuangalia mambo mengi kuhusiana na nchi hiyo. Akaangalia misitu, idadi ya watu na makazi yao pamoja na mambo mengine.
Ingawa kulikuwa na misitu mingi nchini Thailand, lakini kulikuwa na msitu mmoja ambao ulikuwa mkubwa zaidi ya misitu yote, msitu huu uliitwa Chian Rai. Akaanza kuangalia vizuri picha ya msitu ule, kwa muonekano tu ulionekana kuwa msitu mkubwa sana.
“Nafikiri watakuwa huku. Na kama nikiwakosa huku, nitatumia uzoefu wangu kuwapata” Sam alisema.
Swali ambalo lilikuja kichwani ni kwa jinsi gani ambavyo angekwenda ndani ya msitu ule. Moyoni alikuwa na hofu, historia ya msitu ule ilikuwa imekwishamuogopesha kupita kawaida. Miti mirefu na minene, wanyama wakali pamoja na matukio mengi ya kutisha ambayo yalikuwa yakitokea kule yalikuwa yakimuogopesha.
Kesho asubuhi hakutaka kuendelea kubaki chumbani pale, alichokifanya ni kuondoka kuelekea katika sehemu ambayo ilikuwa na idadi kubwa ya bajaji. Alichokifanya ni kukodisha bajaji moja na kuanza kumplekeka kule alipotaka kwenda.
“Nitawezaje kuingia ndani ya msitu huo mkubwa?” Sam alimuuliza dereva Bajaji.
“Ni rahisi sana hasa kwa ninyi wageni. Unachotakiwa kukifanya ni kwenda kwa mzee mmoja ambaye anaujua vizuri sana msitu huu, ukifika kwa mzee huyo atakuuzia ramani nzima ya msitu huu” Mwendesha Bajaji alimwambia.
“Ila ningependa kama ningeweza kupata mtu wa kwenda nae huko”
“Sijui kama utapata. Hakuna kijana yeyote ambaye anatamani kuingia ndani ya msitu huu. Kila mtu anaogopa kutokana na wanyama wakali ambao wako msituni huu. Kuna majini na mambo mengi ya kishirikina kutokana na ibada za kichawi ambazo mara kwa mara hufanyika ndani ya msitu huu” Kijana yule alimwambia.
“Lakini si unaweza kuingia na kutoka salama?”
“Hiyo inawezekana kwa asilimia kumi, Watu wengi kutoka katika nchi za Ulaya ambao walijaribu kuingia ndani ya msitu huu wala hawakurudi, walipotelea huko huko, mbaya zaidi hata miili yao haijulikani ilipo” Kijana yule alisema maneno yaliyoonekana kuanza kumtisha Sam.
“Kwa hiyo huyo mzee huwa hatoi kinga kwa kila anayemuuzia ramani?”
“Hapana. Kazi yake kubwa ni kuuza ramani tu. Una rozari?” Kijana yule aliuliza.
“Hapana”
“Basi wewe ndiye utakuwa katika wakati mgumu sana. Kidogo ungekuwa na ile ingekusaidia japokuwa watu wengi wa huku hatuiamini hata kidogo” Kijana yule alisema.
“Kwani wewe imani yako ipo wapi hasa?”
“Imani yangu ipo kwa Budha. Ninampenda Budha, ninamuabudu usiku na mchana, ananiwezesha kufanikiwa katika maisha yangu, yeye ndiye mungu wangu wa kweli. Siamini katika Biblia wala Koran. Ninaamini katika kitabu chetu kitakatifu ambacho kiliandikwa na mungu wetu, Budha” Kijana yule alimwambia.
Hata kabla maneno hayajaendelea zaidi, wakawa wamekwishafika katika eneo la nyumba ya mzee Tong, mzee ambaye alikuwa akihusika na ugawaji ramani kwa kila mtalii ambaye alikuwa akitaka kuingia ndani ya msitu ule.
“Unasemaje?” Mzee Tong aliuliza huku akionekana kushtuka.
“Nataka kuingia msituni”
“Hapana. Njoo mwezi wa sita. Sasa hivi huko hali si ya amani hata kidogo. Jana damu zilimwagika huko, mungu amekasirika, kama ukitaka kuingia ndani ya msitu huo, wewe ingia lakini mimi wala sihusiki na maisha yako” Mzee Tong alimwambia.
“Basi ninahitaji ramani mzee wangu”
“Hapana. Hata ramani siwezi kukuuzia mpaka utakapofika mwezi wa sita, mwezi ambao amani itakuwa imetawala” Mzee Tong alisema.
“Na vipi kuhusu damu hizo zilizomwagika?”
“Kuna watu walipigwa risasi, hakuna anayejua, ila hali iliyotokea ilitangazwa katika nyumba zetu za ibada na miungu yetu kukasirika. Msitu mzima unalindwa, kama ukiamua kuingia, kamwe hautorudi huku, na kama ukirudi, basi hautoweza kuishi maisha marefu, utakufa tu na kama ikitokea haujafa, hakika maisha yako yatakuwa ya shida, miungu yetu itakuwa ikikusumbua kila siku” Mzee Tong alimwambia Sam ambaye alikuwa akimsikiliza kwa umakini mkubwa.
“Kwa hiyo watu hao waliowapigwa na risasi hawakuuawa na hayo mashetani?”
“Watakuwa wameuawa tu. Yaani hata kama zile risasi hazikuwaua basi mashetani watakuwa wamewauwa tu”
“Nitaingia tu, hata kama sitokuwa na ramani, nitaingia, sina rozari lakini naamini Mungu wangu wa Mbinguni Atanilinda” Mpelelezi Sam alisema na kuanza kuingia ndani ya msitu huo kwani aliona kila alivyozidi kuongea na yule mzee ndivyo ambavyo alizidi kumuogopesha.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kipindi hiki kilikuwa ni kipindi cha masika, Wathailand wengi walikuwa wakiendelea na kilimo cha mpunga ambao ulikuwa ukiingiza kiasi kikubwa cha fedha katika kipindi hicho. Tani za mpunga zilikuwa zikivunwa nchini Thailand na kuuzwa kwa bei ya juu katika masoko mbalimbali duniani.
Mchele ambao ulikuwa ukivunwa nchini Thailand ulikuwa mchele bora ambao ndio ulikuwa ukiongoza kwa ubora katika kipindi hicho. Watu wengi kutoka sehemu mbalimbali duniani walikuwa wakifika nchini Thailand kwa ajili ya kununua mchele huo ambao wengi walikuwa wakiuona kufaa kwa matumizi mengi.
Pamoja na kuwa na mashamba makubwa ambayo yalikuwa yakilima mpunga lakini pia kulikuwa na wezi ambao wizi wao mkubwa walikuwa wakiufanya mashambani hasa nyakati za usiku. Mara kwa mara wezi walikuwa wakijikusanya pembezoni mwa mashamba ya mpunga na kisha kuvamia.
Wakulima walikuwa wakipata hasara kubwa sana kutokana na kiasi kikubwa cha mpunga kuibwa. Hapo ndipo walipoamua kuanzisha ulinzi mkubwa katika mashamba yao. Wakulima walionekana kuwa na hasira kupita kawaida, hawakuonekana kuwa na masihara kwa kila mwizi ambaye walikuwa wakimkamata.
Wezi mbalimbali walikuwa wakiuawa mashambani na wengine kukamatwa na kuuawa maporini tena kwa vifo vibaya na vya aibu. Tayari sheria ilikuwa mikononi mwa wakulima, waliwaua wezi kwa staili waliyoitaka.
Serikali ikapewa taarifa juu ya mauaji ambayo yalikuwa yakifanyika mashambani. Hakukuwa na kiongozi yeyote ambaye aliongea kitu chochote kile kwani wakulima walionekana kuwa watu waliokuwa na hasira kali.
Mpaka katika kipindi ambacho Williams, Phillip na Gong walipokuwa wakipita katika shamba kubwa la mpunga, wakulima walikuwa wamejificha pembeni ya shamba hilo huku wakiwa na bunduki mikononi mwao.
Walikuwa na uhakika asilimia mia moja kwamba Wiliams na wenzake walikuwa wezi ambao mara kwa mara walikuwa wakifika mashambani kwao na kuwaibia mpunga. Walichokifanya mara baada ya kuwaona wakipita kwa kasi ya ajabu shambani, ni kuanza kuwakimbiza.
Williams na wenzake walikuwa wakikimbia kwa mwendo wa kasi kuelekea mbele zaidi, kadri wakulima walivyokuwa wakizidi kuwakimbiza na ndivyo ambavyo walizidi kuongeza kasi zaidi na zaidi.
Ikafika hatua ambayo Williams na wenzake wakawa wamepotea machoni mwao, wakaanza kuwatafuta katika kila kona bila mafanikio. Walichokifanya ni kuanza kuangalia ndani ya vichaka ambavyo vilikuwa karibu na eneo lile walilokuwepo.
Kama bahati kwa upande wao, Williams na wenzake walikuwa wamejificha ndani ya kichaka kile. Kutokana na kuchoka pamoja na hasira kali ambazo walikuwa nazo wakawapiga na vitako vya bunduki nyusoni mwao na kisha kuondoka nao.
****
Williams aikuja kupata fahamu baada ya dakika ishirini kupita. Kitu cha kwanza alichokifanya ni kuangalia katika kila upande mahali pale alipokuwa. Bado giza lilikuwa limetawala mahali pale kiasi ambacho akajiona kuanza kuogopa.
Vikoroboi pamoja na chemli zilikuwa zikiendelea kuwaka mahali pale kitu ambacho kilimfanya kuweza kuwaona baadhi ya watu ambao walikuwa wakionekana kuwa kama walinzi. Huku akionekana kuwa na uchovu, Williams akainuka.
Akashindwa kuisogeza miguu yake kutokana na mnyororo mkubwa ambao ulikuwa umefungwa miguuni mwake. Akaangalia huku na kule, Phillip na Gong bado walikuwa wamepoteza fahamu. Williams hakuelewa ni kitu gani ambacho kilikuwa kimetokea mpaka kujikuta akiwa mahali hapo, ila baada ya dakika chache, kumbukumbu zikaanza kumrudia kichwani mwake.
Hakuelewa hata mara moja kwamba watu ambao walikuwa wamewapiga na vitako kule porini walikuwa wakina nani, mawazo yake bado yalikuwa yakiwafikiria wale watekaji ambao walikuwa katika mikono yao katika masaa machache yaliyopita.
Hakuwa na uhakika kama wale walikuwa ni watekaji au watu wengine. Katika kila swali ambalo alikuwa akijiuliza alikosa jibu kabisa. Moyo wake ulikuwa ukiogopa kupita kawaida, sala yake ilikuwa ikiendelea moyoni kwamba watu wale wasije kuwa watekaji wale ambao walikuwa wamewatoroka.
Wala hazikupita dakika nyingi, Phillip akaarudiwa na fahamu. Kitu cha kwanza alichokuwa amekifanya ni kuanza kupiga kelele kutokana na mguu wake ambao bao ulikuwa katika maumivu makali ambayo yalikuwa yamesababishwa na kubanwa na mtego wa wanyama ambao alikuwa ameukanyaga porini.
Mguu wake ulikuwa katika maumivu makali sana, aliuhisi mfupa wa mguu wake kuwa kama umevunjika. Akaanza kuyapeleka macho yake huku na kule, alionekana kutokuifahamu sehemu ambayo alikuwepo kwa wakati huo.
“Tuko wapi?” Phillip alimuuliza Williams.
“Bado sijafahamu hata kidogo. Hii sehemu inaonekana kutokuwa na amani na maisha yetu” Williams alimjibu Phillip.
Gong akashtuka kutoka katika usingizi mzito wa kupoteza fahamu. Nae akaanza kuangalia katika kila kona mahali pale walipokuwa, sehemu ile ikaonekana kuchanganya kupita kawaida. Akawaangalia Williams na Phillip, alitamani kuongea kitu lakini akakumbuka kwamba hasingeweza kuelekeweka.
Hakukuwa na mtu aliyekwenda kuwaona mahali pale walipokuwa mpaka inaingia asubuhi. Muda wote huo walikuwa macho huku kila mmoja akionekana kuwa na hamu ya kutaka kufaham mahali pale walipokuwa.
Wanaume wawili ambao walikuwa na miili iliyojazia wakafika mahali pale huku mikononi wakiwa wameshika mikuki, wakaanza kuwaangalia kwa macho yaliyojaa hasira na kisha kumfuata Gong ambaye walijua fika kwamba wangeelewana nao baada ya kuona kwamba alikuwa Mthailand mwenzao.
Waliongea nae kwa sauti ya kukaripia, Gong akajaribu kuwaambia mambo mengi ambayo yalikuwa yametokea katika kipini ambacho walikuwa wametoroka kutoka katika mikono ya waasi wale. Hasira zote ambazo walikuwa nazo zikaonekana kupotea, wakaanza kuwaonea huruma.
Walichokifanya ni kuwafungua minyororo ile ambayo ilikuwa imefunga miguu yao na kisha kuwaingiza katika nyumba ambayo waliamini kwamba kungekuwa na usalama zaidi.
Hapo ndipo maisha yao mapya yalipoanza. Kila siku walikuwa wakishinda ndani, hawakutakiwa kutoka kutokana na usalama wa maisha yao kuwa mdogo. Kila kitu ambacho walikuwa wakikihitaji walikuwa wakiletewa ndani ya chumba hicho, tayari mioyoni mwao walikuwa wameanza kujisikia amani.
****
Mpelelezi Sam akaanza kuingia ndani ya msitu ule ambao ulikuwa ukitisha sana kutokana na mambo mbalimbali ya kishirikina ambayo yalikuwa yakiendelea kutokea ndani yake. Katika kila hatua ambayo alikuwa akipiga, moyo wake ulikuwa ukisali sala mbalimbali za kumuomba Mungu aweze kumlinda na kufanikiwa kutoka salama katika msitu ule pasipo kupata tatizo lolote lile.
Dhumuni lake bado lilikuwa moyoni mwake, bado alikuwa akihitaji mahali ambapo wachezaji wa timu ya mpira wa kikapu ya New Bucketts walipokuwa msituni humo. Tayari alikuwa na uhakika wa asilimia zote kwamba wachezaji wa timu ile walikuwa wamepelekwa ndani ya msitu ule na kufanywa mateka.
Msitu ulionekana kutisha kupita kawaida, japokuwa muda ulikuwa ni mchana lakini hakukuwa na mwanga wa kutosha msituni mule. Mwanga wa jua ulikuwa unazuiliwa na miti mikubwa na mirefu ambayo ilikuwa imechanua kwa juu na kuyafanya majani yake kutawala kwa juu.
Kwa kuuangalia tu, msitu ule wala haukuonekana kuwa na amani yoyote ile, chembechembe za damu zilikuwa zikionekana katika baadhi ya maeneo hali ambayo ilikuwa ikionekana kumtisha Sam. Bado alikuwa akiendelea kupiga hatua huku bunduki yake ikiwa mkononi mwake tayari kwa kitu chochote kile cha hatari ambacho kingetokea.
Aliendelea kupita vichakani na sehemu mbalimbali lakini wala hakukuwa na dalili zozote zile za kuwepo kwa ndege ile ambayo ilikuwa imetekwa. Hakukata tamaa, bado alikuwa akiendelea kuitafuta zaidi na zaidi lakini bado hali ilikuwa ile ile. Akaonekana kukata tamaa, masaa mawili ambayo alikuwa ametumia msituni mule yakaonekana kumchosha kupita kawaida, alichokipanga mahali hapo ni kuamua kurudi kule alipotoka.
Hapo ndipo Sam alipochanganyikiwa kupita kawaida. Kule ambapo alikuwa ametokea kulionekana kuwa tofauti na jinsi ambavyo kulivyokuwa hapo mwanzo, kulionekana ubadilika kwa kiasi kikubwa sana. Kitu kilichokuwa kimemshangaza ni mto ambao alikuwa ameuona hatua kama hamsini kutoka pale alipokuwa amesimama.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alijua fika kwamba alipokuwa akiendelea kupiga hatua wala hakukuwa na mto wowote ule, sasa kwa nini kulikuwa na mto ambao hakuwa ameuona kabla? Hali ile ikaonekana kumchanganya, tayari akaona kwamba mauza uza yalikuwa yameanza kumpata.
Kelele za watu zikaanza kusikika masikioni mwake, akaanza kuangalia kila upande kuona kama kulikuwa na watu lakini hakuweza kuona kitu chochote kile. Hofu ikaanza kumshika, akaishikilia vizuri bunduki yake.
Wala hazikupita dakika nyingi, upepo mkali ukaanza kuvuma. Hali hiyo ndio ambayo ilimuogopesha zaidi. Kelele za watu wasiionekana pamoja na upepo ule vikaonekana kumchanganya zaidi. Hofu ikamuingia zaidi, alichokifanya mahali hapo ni kuanza kukimbia kuelekea mbele zaidi.
Sam akaanza kukimbia bila kuangalia nyuma, akaruka mashimo na kupita katika vichaka mbalimbali, hakutaka kusimama sehemu yoyote ile, alizidi kukimbia zaidi na zaidi. Tayari mahali hapo hakukuonekana kuwa na amani hata kidogo, mauza uza yale ya kishirikina yakaonekana kumuogopesha zaidi.
Alikimbia mpaka kufika sehemu ambayo ilikuwa na njia mbili kubwa. Njia moja ilikuwa imejaa miba mikali na mirefu lakini njia moja ilikuwa ya kawaida ambayo ilikuwa na nyasi fupi fupi. Sam akaanza kuziangalia njia zile, akaamua kuichagua njia ile ambayo ilionekana kuwa bora kwake.
Akaanza kukimbia tena kuelekea mbele zaidi, kwa kila hatua ambayo alikuwa akipiga kuelekea mbele, nyuma kulionekana kubadilika jambo ambalo ilimpasa kuendelea mbele zaidi na si kurudi nyuma. Alikimbia mpaka kufika sehemu ambayo ilikuwa na idadi kubwa ya watu ambao walikuwa wakicheza ngoma huku wakiwa watupu.
Sam akaanza kuwaangalia watu wale ambao walionekana kutokumuona. Kutokana na sehemu ile kuwa ya wazi, akaamua kujificha katika kichaka kidogo kilichokuwa pembeni. Akaanza kuwaangalia watu wale kwa macho yaliyojaa wasiwasi, walionekana kutisha machoni mwake.
Huku akiwa amejificha kichakani pale, akajikuta akianza kusimama na kuanza kuelekea kule ambako kulikuwa na idadi kubwa ya watu wale. Hali ile ilionekana kumshangaza kupita kawaida, hakuwa na lengo lolote la kwenda kule ambako kulikuwa na watu wale ambao walikuwa wakicheza ngoma mbalimbali, sasa ni nani ambaye alikuwa akimvuta kuelekea kule ambako walikuwepo wale watu ambao walikuwa wakicheza ngoma.
Kadri muda ulivyokuwa ukizidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo alizidi kuvutwa zaidi na zaidi mpaka kufika katikati ya kundi lile la watu. Akayapeleka macho yake katika kila upande, macho yake yakatua katika nyuso za wazungu ambao walikuwa na ndevu nyingi.
Akaanza kuwaangalia watu wale, wengine alionekana kuwatambua, walikuwa baadhi ya watu wale ambao walikuwa wameingia katika msitu ule na kutoonekana kabisa. Hapo ndipo hofu ilipomshika zaidi na zaidi, tayari akajiona kuwa mfu ambaye kamwe asingeweza kurudi jijini New York na kuelezea kama tayari alikuwa ameikuta ile ndege au la.
“God will save my soul from them (Mungu ataiokoa nafsi yangu kutoka kwao)” Mpelelezi Sam alisema huku watu wale wakimwangalia kwa nyuso zilizojaa tabasamu
****
Bwana Robinson pamoja na kundi lile la waasi bado walikuwa wakiendelea kuwatafuta Williams na wenzake lakini hawakuweza kufanikiwa kuwapata. Bwana Robinson akaonekana kuchanganganyikiwa kupita kawaida, kila wakati alikuwa akirusha vitu kwa hasira. Alijua fika kwamba kama asingefanikisha kuwaua watu ambao walikuwa wamebakia basi ilikuwa ni lazima taarifa ifike nchini Marekani na hivyo siri yake kuvuja.
Hakutaka jambo hilo litokee hata mara moja, hakutaka mtu yeyote afahamu kile ambacho kilikuwa kimeendelea, kitu ambacho alikuwa akikihitaji mahali hapo ni kuwauwa wale wachezaji ambao walikuwa wamebakia. Kwa upande mwingine aliwaona walinzi wa kundi lile kuwa na uzembe mkubwa sana, ilikuwaje watu watoroke na wakati walikuwa wamemarisha ulinzi katika sehemu zote nje ya gofu lile?
Bwana Robnson alionekana kukasirika kupita kawaida jambo ambalo wakati mwingine alikuwa akimfokea Mekong sana kwa kutokuwaambia vijana wake kuimarisha ulinzi mkali mahali pale na wakati kila kitu kilikuwa kimepangwa kama kilivyotakiwa kuwa.
Walizunguka msituni kwa masaa zaidi ya mawili lakini wala hawakufanikiwa kuwapata, hawakuonekana kukata tamaa, waliendelea kuwatafuta zaidi na zaidi. Hapo ndipo walipogundua kwamba kulikuwa na kijiji katika msitu ule ambacho wala hakikuwa mbali kutoka pale ambapo walikuwepo. Walichokiamua mahali hapo ni kuanza safari ya kuelekea katika kijiji hicho huku tayari ikiwa imetimia saa tatu asubuhi.
Walipita katika mashamba ya mpunga, wakapita katika mabonde mpaka kufika sehemu ambayo wakaanza kukiona kijiji kwa mbali. Wakaanza kupiga hatua kuelekea katika kijiji kile huku kila mtu akiwa na uhakika kwamba watu ambao walikuwa wakiwatafuta walikuwa katika kijiji kile.
Bunduki ambazo walikuwa nazo walizificha, hawakutaka zionekana na mtu yeyote kwani walijua kama ingetokea watu kuziona bunduki zile wasingefanikiwa kukipata kile ambacho walikuwa wamekusudia kukipata.
Baada ya dakika kadhaa wakafika katika kile kijiji ambako wakaanza kuulizia. Kila mtu ambaye alikuwa akiwauliza walitoa jibu ambalo hawakulipenda, sijui. Kikafika kipindi ambacho wakaonekana kukata tamaa kwa kuona kwamba mateka wao hawakuwa katika kijiji kile. Wakaanza kupiga hatua kuendelea na safari yao ya kuwatafuta, huku wakiwa wameanza safari ya kusonga mbele zaidi, kijana mmoja akaanza kuwakimbilia huku akiwaita.
Alipowafikia, kwa kuwa alikuwa hafahamu lugha ya Kingereza, akaanza kuongea na Mekong, baada ya sekunde kadhaa, tabasamu pana likaonekana katika uso wa Mekong. Bwana Robinson akaanza kuwasogelea, tayari alijua kwamba kulikuwa na kitu kilizungumziwa mahali hapo, hivyo nae alitaka kukifahamu.
“They are here (Wapo hapa)” Mekong alimwambia Bwana Robinson.
“In this village? (Ndani ya kijiji hiki?)”
“Yeah!” Mekong aliitikia.
Hakukuwa na muda wa kupoteza, wote kwa pamoja wakaanza kupiga hatua kurudi kijijini. Wakaziandaa bunduki zao tayari kwa kuwafyatulia mara tu ambapo wangewatia katika macho yao. Bunduki zikakokiwa vizuri na kitendo ambacho kilikuwa kimebaki katika bunduki zile ni kuziruhusu risasi tu.
Walipofika, wakaanza kuelekea katika nyumba ya mwenyekiti wa kijiji kile, walipoifikia nyumba ile wakaomba kuonana na mwenyekiti wa kijiji kile ambaye akaitwa. Mwenyekiti akaonekana kuanza kutetemeka, watu wale ambao walikuwa wamesimama mbele yake tayari alikuwa amepata taarifa kuhusu wao.
Mekong akaanza kuongea nao, mwenyekiti akakataa katakata kama alikuwa amewaona watu hao ambao walikuwa wakiuliziwa mahai hapo. Tayari jibu lile likaonekana kuwakasirisha, japokuwa walikuwa wamefika mahali pale kwa amani na upendo lakini wakaanza kubadilika. Walichokifanya ni kumnyooshea bunduki zao.
Hofu ya mwenyekiti wa kijiji ikazidi kuongezeka, tayari aliona kama angeendelea kukataa basi ni lazima watu wale wangemfyatulia risasi mfululizo na hivyo kuwa mwisho wa kuvuta hewa ya dunia hii. Akawaambia waingie ndani na kuwachukua watu ambao walikuwa wakiwahitahiji.
Bwana Robinson na wenzake wakaanza kuingia ndani, wakaelekezwa katika chumba ambacho walikuwepo Williams, Phillip na Gong. Wakaanza kupiga hatua kuufuata mango ule, walipoufikia, Mekong akaupiga teke na kuingia ndani huku kila mmoja akiona kwamba walikuwa wamefanikisha kile ambacho ambacho walikuwa wakikihitaji, kuwakamata wachezaji waliobakia na kisha kuwaua.
“There they are (Wale pale)” Mekong alimwambia Bwana Robinson huku Williams na wenzake wakionekana wakiwa vitandani wamelala.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Je nini kitaendelea?
Je huo ndio utakuwa mwisho wa Williams na Phillip?
ITAENDELEA.
0 comments:
Post a Comment