IMEANDIKWA NA : GLOBAL PUBLISHERS
*********************************************************************************
Simulizi : Mama Yangu Adui Yangu
Sehemu Ya Kwanza (1)
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
WASWAHILI wanasena uchungu wa mwana aujuae mzazi, lakini kwa mama yetu ilikuwa kinyume. Sikuamini mama yetu mzazi kuwa chanzo cha matatizo ya familia yetu, pengine hata mimi kushindwa kufikia ndoto zangu za kusoma hadi chuo kikuu na kuishia kidato cha nne huku nikifeli vibaya.
Mwanzo sikuelewa lolote kwa vile nilikuwa na akili za kitoto na kuona kila kitu kiko sawa. Lakini nilikuja kuufahamu ubaya wa mama baada ya kuingia kwenye ndoa ambayo ilighubikwa na utata mkubwa na hapo ndipo nilipoyaona makucha ya mama. Ni mama yangu lakini kama asingekuwa mzazi wangu sijui tungefikishana wapi.
Mambo aliyonitendea mama yangu, kama mzazi aliyenizaa kwa uchungu, hakutakiwa kunifanyia kamwe . Lakini kama sitatanguliza shukurani nitakuwa mwizi wa fadhila. Waswahili wanasema mnyonge mnyongeni haki yake mpeni.
Kwanza kabisa lazima nitangulize shukurani zangu za dhati kwa mama yangu mzazi, kwa kunizaa na kunilea, pia kunipa elimu aliyonikadiria mwenyewe. Hiyo ni hatua kubwa sana katika maisha ya mwanadamu anayopitia akiwa mikononi mwa wazazi wake. Kabla sijafunguka akili nilimuomba Mungu katika maisha yangu aniwezeshe uwezo wa kulipa hata robo ya yote aliyonifanyia mama yangu, japo nilijua ni kazi kubwa. Toka nikiwa binti mdogo nilijua mama yangu ndiyo kila kitu kwa vile alijitoa kwa ajili yetu.
Maisha yote tuliishi na mama yetu, sikubahatika kumuona baba, nilielezwa alifariki mama yangu akiwa na ujauzito wangu wa miezi sita, kwa hiyo sura ya baba yangu niliiona kwenye picha tu. Siku nilipojua siri ya kifo cha baba nilikuwa hoi. Nimeamini nyuma ya mioyo ya watu kuna siri kubwa, ndiyo maana huwezi kujua dhamira ya mtu. Namuomba Mungu asinipe moyo wa mama.
Najua unataka kujua kwa nini mama yetu alituzaa ili ageuke adui yetu namba moja, kwa vile tuko pamoja naomba ungana nami ili siku moja ukubaliane na kauli yangu ili kina mama wenye roho kama ya mama yangu wabadilike.
Naitwa Mwaija mtoto wa mwisho katika familia ya marehemu mzee Salmini. Japokuwa sikubahatika kumuona baba yangu naambiwa nilifanana naye sana. Katika familia ya watoto watano, wa kike wanne na wa kiume mmoja. Baada ya kumaliza elimu yangu ya sekondari kidato cha nne nilipata mchumba wa kunioa.
Ukweli mchumba wangu hakuwa mgeni kwangu, ni mwanaume wangu niliyeanza naye urafiki tangu nilipokuwa kidato cha pili. Mwanzo tulifanya mapenzi ya siri japokuwa kati ya dada zangu, mmoja alimfahamu baada ya siku moja kuniona naye kwa mbali. Aliponiuliza nilijaribu kumficha lakini aliponibana nilimweleza ukweli. Basi ikawa kila siku nikikutana na mpenzi wangu lazima nimpelekee dada zawadi.
Ahadi yetu ilikuwa nikimaliza kidato cha nne tuoane, japokuwa mwanzo nilikuwa na ndoto za kufika chuo kikuu, lakini mazingira ya nyumbani yalinifanya nipoteze mwelekeo wa masomo na kuyabadili mawazo yangu yote kuhamishia kwa mpenzi wangu ambaye muda mwingi baada ya masomo nilikwenda kwake.
Hata matokeo ya kidato cha nne yalipotoka na kuonesha nimefeli vibaya sikushtuka kama wengine waliofikia hatua ya kutaka kujiua. Kwangu ilikuwa sawa kwa vile niliamini kabisa muda ule ulikuwa muafaka kwa mimi kuolewa na Beka.
Baada ya matokeo nilimfuata mwenzangu na kumweleza ule ndiyo ulikuwa muda muafaka wa yeye kuja kujitambulisha rasmi nyumbani.
Siku nilipomtambulisha hakuwa mgeni kwa dada, baada ya kuondoka mpenzi wangu, familia yangu ilitaka kujua anafanya
kazi gani. Niliwaeleza ni dereva wa teksi.
Teksi yake au ameajiriwa? mama aliniuliza.
Ameajiriwa.
Sasa akifukuzwa kazi mtakula nini?
Mama mbona umekimbilia kufukuzwa kazi kuliko yeye kununua yake?
Atawahi! Mwanangu hawa dada zako wamekosa nini hapa nyumbani?
Mama wao hawakupenda kukaa nyumbani bali mapenzi ya Mungu.
Hata kama kazi ya Mungu, lakini toka warudi nyumbani wana tatizo gani?
Hawana matatizo, lakini wao ndiyo hawataki kuolewa tena.
Hawataki kuolewa kwa sababu wanaume wasio na uwezo ni mzigo kwa familia tu, kesho akifukuzwa kazi nikulishe mimi?
Mama ni kuniombea kwa Mungu nifanikiwe.
Kwa kazi kama hiyo nakuomba uachane na wazo hilo, mama alinikata maini.
Mama siwezi kuachana na wazo hilo kwa vile nitakayeolewa ni mimi.
Kama una uamuzi wako, sawa olewa kwa amri yako.
Mama nipo tayari kuishi maisha yoyote ndani ya ndoa, tutaishi hivi mpaka lini tunajazana nyumbani hata heshima hatuna.
Kwa hiyo umefanya vibaya kwenye mtihani ili uolewe?
Mama uliniambiaje?
Nilikuambia nini?
Mama si uliniambia huna hela za kunisomesha tena?
Ndiyo umefeli kiasi hicho?
"Lakini matokeo yalipotoka mama si ulisema afadhali, leo hii umenigeuka?"
"Kote huko tunazunguka, kifupi huwezi kuolewa na kabwela."
"Lazima nitaolewa," nilimpinga mama.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Mimi na wewe nani kamzaa mwenzie? kama wewe umenizaa utaolewa."
Kwa kweli kauli ya mama ilikuwa mkuki moyoni mwangu, nilitegemea mimi kupata mume angefurahi kuliko kuendelea kujazana nyumbani. Lakini ilikuwa tofauti na mawazo yangu, alipenda tujazane huku nyumba yetu ikiwa na sifa mbaya ya kuitwa danguro. Iliitwa hivyo kutokana na dada zangu kubadili wanaume kila kukicha, kila mwenye fedha ndiye aliyependwa.
Baada ya mama kunikatalia niliwafuata dada zangu na kuwaeleza maneno ya mama, nao nilishangaa kuwa upande wake kwa kumuunga mkono kwa kunieleza;
"Mwaija umekosa nini mpaka ukimbilie kuolewa na dereva wa teksi?"
"Dada, ndiye chaguo langu."
"Muda wa kujichagulia haujafika, unatakiwa kuchaguliwa mwanaume."
"Dada hata siku moja siwezi kuchaguliwa, mkinilazimisha nitatoroka."
"We toroka, yakikufika usirudi."
"Sawa."
Siku ile nililia usiku kucha na kutishia kujiua kama watanikataza kuolewa na Beka, vitisho vyangu vilifanya walegeze masharti kidogo. Mama alikubali niolewe, japo ilionesha kwa shingo upande. Kwangu sikujali kwa vile niliamini maisha yangu yalinitegemea mimi mwenyewe baada ya kutimiza miaka kumi na nane nilitakiwa kuwa na uamuzi wangu bila kuingiliwa na mtu.
Ilikuwa tofauti na nilivyodhania harusi yangu ingedoda kutokana na kuwa na vipingamizi. Lakini maandalizi ya harusi yangu yalikuwa makubwa sana. Mama na dada zangu walishirikiana kwa hali na mali, katika kicheni pati nilipata vitu vya zaidi ya milioni nne.
Siku nne kabla ya harusi nyumbani kwetu ilikesha rusha roho mfululizo. Harusi yangu ilitikisa mtaa kwani ilikuwa tofauti na za wenzangu. Baada ya ndoa nilihamia kwa mume wangu Beka aliyekuwa akikaa Tandika Maguruwe.
Sikuamini ushirikiano nilioupata kwa mama na dada zangu muda wote nikiwa mgeni wa ndoa. Nilijikuta nikiyasahau yote yaliyopita ya kukatazwa kuolewa na mwanaume kabwela. Kwa vile nyumbani hakukuwa mbali toka Temeke Mikoroshoni mpaka Maguruwe ilikuwa haipiti siku mbili au tatu bila mama kuja kunijulia hali.
Miezi sita baada ya ndoa yangu nilipata ujauzito, kwa furaha ya kuwa katika hali hiyo nilikwenda kumwambia mama.
"Mama sipo vizuri."
"Kivipi?"
"Nina wasiwasi nina ujauzito."
"Ujauzito?" mama alishtuka.
"Ndiyo."
"Umejuaje?"
"Baada ya kupima leo asubuhi na kujiona kweli nina mimba."
"Mmh! Sawa."
"Mbona kama hujafurahi?"
"Mwanangu unabeba ujauzito wakati maisha ya mumeo unayajua!"
"Mama maisha ya mume wangu na ujauzito wangu vinaingiliana vipi?"
"Mwanangu mtoto anatakiwa malezi."
"Mama mume wangu mbona ana maisha mazuri tu, hatujawahi kulala na njaa hata siku moja."
"Mwanangu maisha nayajua mimi mama yako, mwanzo utayaona mazuri baadaye mtafikia hata kipande cha muhogo unakitafuta. Ulitakiwa upitishe hata mwaka ndipo ubebe ujauzito, wewe miezi sita tu, unakimbilia nini unafikiri kuzaa raha?"
"Mama mbona wasichana wa umri wangu wengi wamezaa."
"Usiishi kwa kuangalia jirani bali maisha yako mwenyewe."
"Lakini mama kwani tatizo lipo wapi?"
"Ulitakiwa uniulize kuliko kukimbilia kubeba ujauzito."
"Sasa haya makubwa, suala la kubeba ujauzito nije kutaka ushauri kwako?"
"Basi tuachane na hayo, vipi mumeo?"
"Namshukuru Mungu, sasa hivi kidogo mambo yanamwendea vizuri amenunua kiwanja."
"He! Kanunua kiwanja?"
"Ndiyo, mbona umeshtuka?"
"Hapana, kanunua wapi?"
"Charambe."
"Mmh! Mbona nje ya mji?"
"Mama siku hizi hakuna nje ya mji madamu magari yanafika."
"Ameisha anza kujenga?"
"Bado."
Kwa vile muda ulikuwa umekwenda nilirudi nyumbani kuwahi kuandaa chakula cha mchana. Nikiwa nyumbani nilijawa na mawazo mengi kutokana na kauli ya mama kuhusiana na ujauzito wangu.
Niliamua kuipuuzia na kuendelea na mambo yangu huku nikipanga baadhi ya mambo yangu nisimshirikishe mtu yeyote katika familia yangu.
Niliendelea kumshukuru Mungu kwani maisha yaliendelea vizuri tofauti na wasiwasi wangu kutokana na maneno ya mama.
Siku moja nikiwa nimekaa na mume wangu aliniambia kitu ambacho kilikuwa faraja kwangu.
"Mke wangu, Mungu kanijalia kumpata mke mwenye mapenzi yake kweli mwenye nyota ya bahati."
"Kwa nini mume wangu?"
"Huwezi kuamini kila ninachokifanya sasa hivi kinafanikiwa tofauti na zamani. Wiki ijayo tunaanza ujenzi wa nyumba yetu."
"Usiniambie!" nilifurahi sana.
"Nilikuwa na wazo la kununua gari, lakini nimeshauriwa kwa vile gari nimeachiwa kama langu, basi nianze kwanza nyumba kisha gari."
"Tutajenga nyumba kubwa au?"CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Tutasimamisha kwanza vyumba viwili mambo mengine yatafuata."
Maneno ya mume wangu yalikuwa faraja sana kwangu baada ya kujiona kumbe nami ni mmoja wa viumbe wenye bahati. Niliendelea kumuomba Mungu maisha yasibadilike tuendelee kufanikiwa. Lakini alinionya kitu kimoja suala letu la kujenga nisimwambie mtu.
"Hata mama?" nilishtuka kusikia vile.
"Mtu yeyote, hata wazazi wangu sijawaambia, watajua siku tukitaka kuhamia kwetu, binadamu hawaaminiki."
"Mmh! Sawa."
"Narudia siri hii ni yangu mimi na wewe tu."
"Nimekuelewa mpenzi wangu."
"Si kujenga tu, chochote cha kwetu iwe siri yetu sawa mpenzi?"
"Sawa mpenzi wangu."
Baada ya kuachana na mume wangu nilijikuta njia panda kutokana na kauli yake ya kufanya mambo yetu kwa siri. Nilijiuliza itakuwaje ikiwa nilikuwa tayari nimeshamwambia mama kila kitu pia nilimuahidi kumpeleka tunapojenga. Nilipanga kufanya siri huku nikimuomba mama naye asimwambie mtu hata dada zangu ili ibakie siri sirini.
Wiki iliyofuata tulianza kuchimba msingi wa nyumba, mwisho wa wiki hiyohiyo ndiyo niliyompeleka mama kwenye kiwanja chetu. Kabla ya kumpeleka nilimweleza kuhusiana na kauli ya mume wangu kuwa hakupenda mambo yetu kila mtu ayajue.
Nilimuomba mama siri ya kwenda kule ibakie moyoni mwake ili mume wangu asinione msaliti.
Tuliongozana hadi kwenye saiti yetu, tulipofika alishtuka sana hatua tuliyofika. Nyumba ilikuwa imeanza kunyanyuka, ilikuwa tayari ipo katika kozi tatu. Mume wangu alipanga baada miezi mitatu tuwe ndani mwetu.
"Mmh! Hongera," aliguna kabla ya kutoa pongezi.
"Mama mbona umeguna kwanza?"
"Walaa, umenisikia vibaya."
Baada ya mama kupaona tunapojenga tulirudi nyumbani, tukiwa njiani mama alinipa moyo huku akiniombea kwa Mungu tumalize nyumba yetu haraka ili nasi tukae kwetu. Nilimshukuru mama yangu kwa dua zake.
Niliagana na mama na kurudi nyumbani na siri yangu moyoni, nilimuomba Mungu mama naye awe msiri ili kuongeza uaminifu katika ndoa yangu. Siku zilikatika huku mama akizidi kuja kunitembelea na kunipa maadili ya ndoa. Kwa kweli nilijivunia kuwa na mama mwenye mapenzi ya kweli na familia yake.
Siku moja nilikuwa nikitoka ndani, niliponyanyua mguu kuvuka mlango nilihisi kizunguzungu kikali. Nilijitahidi nisianguke, japo mbele nilikuwa sioni nilishika ukuta na kukaa chini. Kilichoendelea sikujua mpaka niliposhtuka na kujikuta nipo Hospitali ya Temeke nikiwa nimelazwa tena naongezwa damu.
Nilishtuka kuwa katika hali ile, nikiwa bado nipo kwenye maswali magumu yasiyo na majibu, aliingia muuguzi na kusogea kitandani kwangu na kunisemesha.
"Vipi dada?"
"Poa," nilijibu kwa sauti ya kutaka kujua nimefikaje pale.
"Pole."
"Asante," nilijibu huku macho yangu yakiwatazama mama na dada zangu waliokuwa wakisogea kwenye kitanda.
"Mwaija," mama aliita.
"Abee mama."
"Pole mama."
"Asante."
"Pole Mwai," dada zangu nao walinipa pole.
"Asante."
"Vipi unaendeleaje?"
"Hata najua! Sielewi nimefikaje hapa na pia naumwa nini!" kwa kweli nilikuwa sijui lolote zaidi ya kushikwa na kizunguzungu na kujitahidi nisianguke na kukaa chini zaidi ya hapo sikujua kitu.
"Pole sana," mama alinipa pole baada ya kusikia maelezo yangu.
"Asante."
Baada ya muda alikuja mume wangu na ndugu zake, wote walinipa pole. Jioni ya siku ile nilimaliza kuongezwa damu na kuweza kuzungumza na waliokuja kuniona. Jirani yangu mama Saidi ndiye aliyeniokota na kunieleza kilichotokea siku ile.
"Basi shoga nilipotoka ndani nilikukuta umelala pembeni ya mlango wako ukiwa umepoteza fahamu na chini ulikuwa umetoka damu nyingi kama kachinjwa mbuzi."
"Mungu wangu!"
"Basi ikabidi niwaite dada zako pia nilimpigia simu mumeo, bahati nzuri walifika wote kwa pamoja na kukuleta huku."
"Mmh! Nashukuru dada yangu sijui bila wewe ingekuwaje?"
"Tumshukuru kwa kila jambo."
"Mmh! Una maana nimetoka damu nyingi?"
"Ndiyo, ulifanya nini?"
"Nifanye nini zaidi ya kukaa chini, jamani mimba haijatoka?" nilishtuka baada ya kujua ujauzito wangu unaweza kuwa umetoka.
"Kwa kweli sijui, kwani daktari anasemaje?" jirani yangu aliniuliza.
"Sijazungumza naye chochote wala sijamuona, mtu wa kwanza alikuwa ni muuguzi."
Baada ya majirani zangu kuondoka alikuja mama na kukaa pembeni yangu na kunishika mkono kama ananikanda kuonesha kuna kitu anataka kuniambia. Sikuwa na haraka nilitulia kumsikiliza mama alitaka kusema nini.
"Mwaija," mama aliniita kwa sauti ya chini.
"Abee mama."
"Unajisikiaje?"
"Kwa kweli kama nilivyokujibu mwanzo sijui lolote, sijui nimekujaje na sasa nipo kwenye hali gani."
"Kwani daktari amesemaje?"
"Bado sijazungumza naye na wala sijamuona."CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mara aliingia daktari na kusogea kwenye kitanda akiwa na muuguzi.
"Samahani, naomba kumhudumia mgonjwa."
Mama na ndugu zangu walitoka nje ya wodi na kuniacha peke yangu. Baada ya kutulia daktari alianza kunipima mapigo ya moyo na kuandika kwenye kadi yangu, kisha alimuomba muuguzi aondoe chupa ya damu iliyokuwa imekwisha.
Baada ya kuondoa sindano mkono, aliniuliza:
"Unajisikiaje kwa sasa?"
"Kwa kweli sijui chochote."
"Lazima ujue, ilikuwaje ukaletwa hospitali na hali uliyokuja nayo ukiwa hujitambui na sasa hivi."
"Nina imani sasa sijambo kwa jinsi nilivyoelezwa."
"Kichwa vipi?"
"Kimetulia."
"Kizunguzungu?"
"Sina."
"Hebu kaa," nilifanya nilivyoelekezwa na mganga.
"Unajisikiaje?"
"Uchovu tu na njaa."
"Nina imani unaendelea vizuri."
"Eti dokta nasikia nimetoka damu nyingi sehemu za siri, mimba yangu haijatoka?"
"Kwani ilikuwaje mpaka ukatokwa na damu nyingi kiasi kile?"
Nilimueleza ilivyokuwa mpaka kuwepo pale hospitali.
"Si kweli inawezekana ulipigwa na kitu tumboni na kusababisha kuharibu ujauzito wako."
"Mungu wangu mimba yangu imetoka," nilianza kuangua kilio kama mtu niliyefiwa. Ilibidi daktari na muuguzi waanze kazi ya kuninyamazisha. Ilikuwa kazi ngumu kuninyamazisha, mpaka mama alipofuatwa na kuja kunikemea kwa maneno makali ambayo yalinifanya ninyamaze, lakini moyoni niliumia kupoteza mtoto wangu niliyepanga kumlea kama mboni ya jicho langu.
Baada ya kupata matibabu niliruhusiwa kutoka hospitali na kurudi nyumbani. Mama alitumia muda mwingi kuniasa kuacha kuendelea kulia baada ya ujauzito wangu kutoka.
"Mwaija, kuendelea kulia ni uchuro unaweza ukafunga kizazi usizae tena."
Mmh! Kauli ya mama ilinitisha sana na kumhakikishia mama sitalia tena japo niliamini ingechukua muda kusahau.
Siku nazo zilisonga, maisha yaliendelea huku nikiendelea kufurahia maisha ya ndoa yangu japokuwa ujauzito ambao ungeongeza ukoo ulitoka. Nayo mapenzi ya mama yangu yalikuwa makubwa sana, ilikuwa haipiti siku mbili au tatu bila kuja kunijulia hali, japokuwa nami nilikuwa nikienda mara mojamoja tofauti na yeye ambaye kila mara alikuja kwangu.
Ajabu siku zote alizokuja hakutaka kuonana na mume wangu, niliendelea kumshukuru Mungu kutuongozea maisha yetu. Mwaka ulikatika huku suala la ujenzi likiwa limekwama, huwezi amini nyumba ilikomea kozi ya tano.
Maisha nayo yalianza kuwa magumu, biashara nazo ziligoma kiasi cha siku nyingine kulalia chai na kipande cha mkate. Kwa kweli nilianza kuona aibu ya mama kuja kushinda nyumbani kwani sikuwa na kitu. Ili kuficha aibu ile niliingia madeni kwa ajili ya kumpikia chakula nikiamini hali ile ni ya mpito tu.
Lakini kila kukicha ilikuwa afadhali ya jana, kuna kipindi mume wangu alirudi bila hata senti tano. Kuomba msaada nyumbani niliona aibu kwa vile yangetimia waliyoyasema. Lakini siku zote penye moto huwezi kuzuia kufuka moshi.
Pamoja na kufanya siri lakini hali yangu ilionekana, kwani nilianza kupungua mwili kutokana na kukosa kula.
Siku moja mama alipokuja kwa kweli sikuwa na ujanja, sikuweza kwenda kukopa kama kawaida yangu, madeni ya awali nilikuwa sijalipa pia ilikuwa siri yangu na sikutaka mume wangu ajue.
Ajabu siku ile mama hakukaa sana, alipotaka kuondoka alinipa elfu hamsini, kitu kilichonishtua na kunifanya nihoji:
"Za nini mama?"
"Mwaija unauliza za nini, maisha yako sasa yapo sawa?"
Kwa kweli nilishindwa kujibu kitu, moyo wangu uliingiwa aibu na kujua nimeumbuka mtoto wa kike na kumpa nafasi mama yangu kusema. Nilibakia nimeinama chini kama mwana mwari kwa vile maneno yalikauka mdomoni.
"Mwaija," mama aliniita huku akinishika kichwani.
"A..a..bee mama."
"Usijali ni sehemu ya maisha, najua sasa hivi mpo katika hali ngumu, lakini Mungu ataleta heri zake kila kitu kitakwenda vizuri."
"Na...nashukuru sana mama."
"Usihofu mwanangu ukizidiwa usione aibu kuja kuomba msaada."
"Nashukuru mama yangu."
"Na nyumba yenu imefikia wapi?"
"Mmh! Mama wee acha tu, mbona mwaka huu wetu."
"Kwa nini?"
"Yaani ulipoona tumeongeza kozi mbili tu, yaani malengo ya mume wangu yameyeyuka kama donge la barafu. Mpaka muda huu alipanga tungekuwa nyumbani kwetu."
"Mipango ya Mungu yote ya mpito, endeleeni kumuomba atakusikilizeni."
Kwa kweli nilizidi kumshangaa mama, nilitegemea angeniporomoshea maneno, lakini siku ile alikuwa mpole. Baada ya kunikabidhi fedha ile aliondoka na kuniacha nikiwa na maumivu makali moyoni mwangu, huku nikijiuliza hali ile itaendelea mpaka lini.
Fedha niliyopewa na mama nililipa sehemu ya madeni na kununua mchele na sukari ambavyo niliamini vingetusaidia hata kama hatuna kitu tunaweza kuchemsha na chumvi na chai ili kudanganya tumbo.
Hali ilikuwa ileile, mume wangu kila aliporudi alitia huruma kwani biashara ilikuwa ngumu kila kukicha, kilichokuwa kikimshangaza kila alipofikisha hesabu ya bosi wake biashara ilikata. Siku nyingine hata hesabu ya bosi ilikuwa haitimii. Wakati siku za nyuma baada ya ndoa yangu alikuwa akiingiza zaidi ya mara tano ya hesabu ya bosi wake, kitu kilichofanya maisha yetu yabadilike ghafla.
Siku moja baada ya chakula cha usiku tukiwa tumekaa sebuleni mume wangu aliniita.
"Mwaija."
"Abee mume wangu."
"Nilikuambia nini?"
"Kuhusu nini?" nilishtuka kidogo.
"Nilikwambia nini kuhusu siri yetu ya ndani?"
"Nisimwambie mtu."
Mume wangu kwa nini tufikie huko, kwa nini nisiende nyumbani kuomba msaada?
Tutaomba mpaka lini?
Kwani hali hii itakuwa ya kila siku?
Mi nafikiri we ungerudi kwenu, na mimi nihangaike nijuavyo. Nikirudi katika hali yangu ya kawaida tutaendelea na maisha yetu.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hapana naomba jukumu hili niachie kwanza mimi, nikishindwa nitakwambia.
Nilimbembeleza mume wangu, akanielewa. Sikutaka kupoteza muda, nilijifunga kitenge na kwenda nyumbani kumweleza mama na kumsikiliza atanisaidiaje. Njia nzima nilikuwa nikijiuliza, mama kweli atakubali kutulipia chumba kwa miezi sita zaidi ya laki tatu?
Wazo la kuambiwa nirudi nyumbani nililiogopa kwani hata kama tungelipiwa chumba bado tusingekuwa na fedha za kula. Nilijikuta nikichanganyikiwa kiasi cha kupitiliza nyumbani mpaka niliposhtuliwa na dada zangu waliojua nina safari zangu nyingine kumbe nilikuwa naenda palepale.
***
Wee Mwai vipi, safari ya wapi? Maana unapita kama hutujui, dada alinishtua katika lindi la mawazo nikiwaza hali yetu ya maisha ilivyobadilika ghafla na kutufanya tupoteze mwelekeo.
Mungu wangu! nilishtuka na kuufunika uso kwa mikono.
Unashtuka nini nawe hukutaka kuja nyumbani?
Dada yangu wee acha tu, mbona mwaka huu nitakuwa kichaa.
Kwa sababu gani?
Tutazungumza baadaye, mama yupo?
Yupo sebuleni anakula raha zake, si unajua mama yako anapenda raha kama paka wa Kiarabu, dada alitania.
Anakunywa? niliuliza kutaka kujua kama mama anakunywa bia.
Aache! Jioni hii wakwe zake wameshamletea yupo sebuleni kajaa tele kama pishi la mchele.
Kabla sijaondoka dada alinishangaa kwani miguu ilikuwa imejaa vumbi, nywele zilikuwa timtimu. Wakati mume wangu alipokuwa anarudi nilikuwa naosha vyombo kisha ndiyo niingie bafuni kuoga. Lakini aliyonieleza
yalinichanganya, nilikumbuka kujifunga kitenge chini, juu nilikuwa na gauni la kulalia ambalo tangu niamke nilikuwa sijalivua.
Wee Mwai! dada aliniita kama kuna kitu kimemshtua.
Vipi dada?
Mbona sikuelewi?
Kivipi dada?
Unajiona upo sawa? nilijua ni kutokana na nilivyokuwa siku ile.
Nilijikuta nikishtuka na kujikagua, hali niliyokuwa nayo ilinishangaza. Lakini sikutaka kuonesha kushangaa kulingana na uzito wa tatizo lililokuwa kichwani mwangu.
Aah! Dada wee acha tu, nilimjibu huku nikielekea ndani kwani sikutaka maswali zaidi ya kuzungumza na mama ili nijue atanisaidia vipi.
Ubishi wako! Ona unavyozeeka, unatufanya dada zako tuonekane kama wadogo zako.
Sikutaka kumjibu, niliachana na dada ambaye alionekana alikuwa katika mkao wa mtoko. Kwa kweli maisha ya dada zangu sikuyafurahia hata kidogo. Baada ya dada zangu wawili kufiwa na waume zao pia mmoja kuachika katika mazingira ya utata, hakuna aliyekubali kuolewa tena, wote waliishi maisha ya kutumia miili yao kama vitega uchumi.
Katika vitu Mungu alivyotujalia watoto wote wa kike tulifuata umbile la mama. Mama yetu alikuwa na umbile la Kitutsi. Mweusi asilia pia ana shepu ya mvuto. Hilo ndilo lililowafanya wanaume wenye fedha zao kumiminika nyumbani kama kwenye kituo cha akina dada poa.
Japokuwa hali ile ilifanya maisha yetu yawe mazuri kidogo lakini ilishusha hadhi ya nyumba yetu kwa kutufanya wote tuonekane machangudoa. Aibu niliiona mimi peke yangu lakini mama na dada zangu waliiona ile hali ni ya kawaida.
Nilipoingia ndani nilimkuta mama amenyoosha miguu kwenye meza na pembeni yake kulikuwa na bia iliyokuwa imebakia robo kwenye chupa, kwenye glasi kulikuwa na bia nusu. Aliponiona naingia aliyaondoa macho kwenye runinga alipokuwa akiangalia taarab.
Karibu mwanangu.
Ahsante mama yangu.
Upo sawa? mama alinishtukia.
Mmh! Ha..ha..pana.
Tatizo nini mziwanda wangu?
Mama mbona mikosi imezidi kuniandama.
Tatizo nini? Mama alisema huku akiteremsha miguu kwenye meza na kukaa vizuri kunisikiliza.
Kabla ya kuzungumza lolote, nilimuona akinishangaa kwa kuanza kuniangalia kwa kunipandisha na kunishusha. Alituliza macho kwa muda usoni kwangu kisha alitikisa kichwa na kuchukua chupa ya bia iliyokuwa imebakia robo
na kuijaza kwenye glasi kisha aliinywa yote na kuniangalia tena kama vile bia aliyokunywa ilimfanya anione vizuri.
Mwaija mama, mama aliniita akiwa kama ananishangaa.
Abee mama,
Una tatizo gani mwanangu, maana kila kukicha la leo linazidi la jana.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
MAMA wee acha tu mwanao nakuwa chizi sasa hivi."
"Tatizo nini?"
"Mama kama ulivyosema kila kukicha ya jana yanakuwa na afadhali kuliko ya leo, mume wangu hana kazi."
"Etii!" mama alishtuka.
"Amenyang'anywa gari."
"Tangu lini?"
"Wiki ya pili sasa."
"Tatizo nini?"
"Siku hizi bundi ametua kwenye nyumba yetu, kazi imekuwa ngumu, hesabu ya tajiri imekuwa haifiki mwenyewe kaamua kuchukua gari lake."
"Mlipokuwa na gari nanga ilipaa, sasa hivi hana gari itakuwaje?"
"Mama yote tisa kumi kodi ya nyumba huu mwezi wa pili sasa."
"Kodi ya nyumba imefanya nini?"
"Tokea mwezi jana tulitakiwa kulipa lakini mpaka leo hii hatujalipa na hatujui tutalipa lini."
"Kwani mumeo hana akiba hata kidogo?"
"Hata senti tano nyekundu hana."
"Kwani ana mawazo gani?"
"Mama hana yoyote zaidi ya kutaka nirudi nyumbani."
"Ili?"
"Ili ajipange kimaisha."
"Kwa hiyo ukirudi nyumbani, anakuwa amekuacha au?"
"Hapana siyo kuniacha bali kuja kupumzika ili ajipange upya."
" Kwa hiyo kula yako ihamie kwangu?"
"Sasa mama kwa hiyo unataka nitafute pa kwenda?" kauli ya mama ilinichefua sana.
"Siyo pa kwenda, ila uamini mimi mama yako naona mbali, haya niliyaona mapema lakini ukanibishia."
"Mama huu si wakati wa kubishana, nimefuata msaada."
"Rudi nyumbani, hapa kwenu huwezi kufukuzwa."
"Mama shida yangu si kurudi nyumbani."
"Eeh! Shida gani?"
"Nilikuwa naomba utukopeshe fedha tulipe kodi, mume wangu akipata kazi atarudisha."
"Hiyo kazi atapata lini?"
"Mungu atasaidia kwani naye anahangaika."
"Mwanangu kwa ushauri wa mumeo ungekubaliana naye."
"Mama, kwa nini tuendelee kujazana nyumbani?"
"Hivi katika ndugu zako ambao hawana wanaume nani mwenye shida?"
"Mama siyo shida, bali heshima."
"Kifupi sina uwezo wa kifedha zaidi ya kuiunga mkono kauli ya mumeo kuwa urudi nyumbani ili ajipange. Kumbuka kuendelea kuwa karibu naye atazidi kuchanganyikiwa mtoto wa watu na kumfanya azidi kuongeza matundu ya mkanda wa suruali."
"Kwa hiyo mama?"
"Rudi nyumbani."
"Mamaaa," sikukubaliana na mama.
"Unatakaje?"
"Kwa nini usitukopeshe tukalipe kodi tutakulipa mume wangu akipata kazi."
"Hivi wewe na mumeo nani mwenye kauli ya mwisho?"
"Mume wangu."
"Kama yeye amesema wewe urudi kwenu ameona mbali, hivyo basi rudi nyumbani kwenu ili kumpa nafasi mumeo kutafuta kazi kwa utulivu. Kama utalazimisha utasababisha kijana wa watu aibe ili mpate chakula, mwisho wake kuuawa au kufungwa."
Nilijikuta nikiangua kilio ambacho niliamini lazima kitamshawishi mama kubadili uamuzi wake. Lakini mama aling'ang'ania msimamo wake wa mimi kurudi nyumbani. Kwa upande wa pili nilikubaliana na mama kwani hata kama tungelipa kodi bado chakula kingekuwa shida, hivyo ningezidi kumchanganya akili mume wangu.
Japokuwa sikupenda kurudi nyumbani, ilibidi nikubaliane na mama kwa shingo upande kwa kuamini aliyonieleza yalikuwa yana umuhimu kukubaliana nayo.
"Kwa hiyo mama kwa kipindi hiki mume wangu utamsaidiaje?"
"Mwaija unachekesha, nimsaidieje wakati ana ndugu zake?"
"Mama yule ni sawa na mwanao mpaka nakuomba msaada nina sababu zangu."
"Mwanangu nawe king'ang'anizi haya unataka shilingi ngapi ukampe huyo mumeo?"
"Hata laki mbili kwa ajili ya kujikimu kimaisha wakati anatafuta kazi."
"Nitakupa laki," mama alisema huku akinyanyuka na kuelekea chumbani kwake.
Baada ya muda alitoka na laki mkononi na kunikabidhi huku akisema:
"Mwanangu we nd'o mwanamke wa kwanza kumhonga mwanaume badala ya kuhongwa wewe."
"Mama simhongi, kumbuka yule ni mume wangu."
"Kwa hiyo unarudi lini kwa mumeo?"
"Atakaponieleza nirudi."
"Umeisha kula?"
"Ndiyo mama."
"Mumeo umemwacha wapi?"
"Nyumbani."
"Basi muwahi."
Niliagana na mama na kurudi nyumbani kwangu, njiani niliwaza mambo mengi kuhusiana na kushindwa kumshawishi mama kunipa fedha za kulipia pango.
Kitu kilichokuwa kigumu moyoni mwangu ni kutengana na mume wangu kipenzi. Lakini hali iliyotutokea ilinifanya nisiwe na jinsi na kukubaliana na kilichoamuliwa.
Nilipofika nyumbani nilimkuta mume wangu kajilaza mikono ikiwa bado kichwani kuonesha jinsi gani kichwa kilikuwa katika wakati mgumu. Nilimwangalia mume wangu ambaye sikuwahi kumuona kwenye hali ile siku za nyuma.
Moyo uliniuma na kujiuliza upepo gani mbaya uliotukuta na kufikia hatua ile. Kila kitu tulichokifanya kilikuwa kibaya, afya zetu zilidhoofu kwa mawazo na chakula cha kulambalamba ili kuipitisha siku, japokuwa nyumbani walikuwa na uwezo lakini kuomba kila siku niliona aibu.
Nilisimama mlangoni kabla ya kuingia chumbani na kumuangalia mume wangu kwa uchungu huku moyo ukiniuma bila kujielewa, nami machozi yalianza kunitoka na kuweka michirizi mashavuni.
Maumivu yalikuwa makubwa kuliko kawaida, niliwaza mengi. Nilikiangalia chumba chetu kisha nilimwangalia mume wangu ambaye bado alikuwa kwenye dimbwi la mawazo, hata nilipoingia hakushtuka. Moyo uliniuma na kuamini hakuna kitu kibaya duniani
kama umaskini na kifo, kwani niliona ulivyokuwa ukiyatenganisha maisha yetu ya mume na mke kwa muda bila kujua itachukua muda gani kuwa tena pamoja na mume wangu.
Nilijikuta nikipata wazo la ghafla na kunifanya nimwite mume wangu kwa sauti.
"Bekaa," sauti yangu ya juu ilimfanya ashtuke na kunitazama.
Uso wake ulikuwa umetandwa na machozi, macho yalikuwa mekundu mishipa ya kichwa ilimsimama. Mume wangu alikuwa akitia huruma, nami nilijikuta nikitokwa machozi zaidi.
"Unasemaje?" aliniuliza huku akinitazama.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Mume wangu kwa nini tusiuze baadhi ya vitu vyetu vya ndani ili tulipe kodi ya nyumba wakati tukisubiri mambo yawe mazuri?"
"Wazo zuri mke wangu, lakini tukiuza vitu vyote na bado mambo yasiwe mazuri itakuwaje?"
"Ina maana mpaka muda wa kudaiwa tena utakuwa hujapata gari?"
"Mke wangu lazima nikuambie ukweli, si kwamba gari nimenyang'a nywa wiki mbili zilizopita bali nina mwezi wa tatu sasa."
"Mume wangu, uongo huo!" kauli ile ilinishtua na kuona mume wangu ananidanganya.
"Kweli mke wangu, muda wote nimeishi kwa kuungaunga, kila kukicha maisha yanazidi kuwa magumu. Ndiyo maana nikaona kwa nini nikutese wakati familia yako ina uwezo ni bora nikuache ukapumzike kwenu ili nijipange upya kuliko kuendelea kukutesa."
SIKU zilizidi kukatika bila kupata taarifa za mume wangu yupo wapi.
Mama alinieleza niendelee na maisha yangu ikibidi hata kutafuta mwanaume kwa wakati ule wa kuniliwaza wakati namsubiri mume wangu.
Japokuwa kulikuwa na wanaume wengi walionimezea mate lakini sikuwa tayari kujidhalilisha. Niliiheshimu ndoa yangu pia mwenyewe nilijiheshimu, sikutaka kuwa na sifa mbaya kama dada zangu. Siku nazo zilikatika bila kupata taarifa za mume wangu.
Sikuchoka kwenda kuuliza kwao na kijiweni kwake labda kulikuwa kuna mtu ana taarifa zake. Kila nilipouliza majibu yalikuwa yaleyale, hawakuwa na taarifa zozote.
Nilijikuta nikianza kuzoea taratibu maisha ya peke yangu na kuamua kujichanganya kama zamani huku moyoni nikiwa na swali lisilo na jibu, mume wangu amekwenda wapi?
Hata kama angekuwa amekwenda kutafuta maisha bado alitakiwa kuniaga kwa vile mimi ndiye nilikuwa mkewe na mtu wake wa karibu. Miezi minane ilikatika bila kujua mume wangu yupo wapi huku nikizidi kuwa katika mtihani wa wanaume walionitaka kimapenzi huku mama na dada zangu wakitumika kunikuwadia.
Kuna mwanaume mmoja aliahidi kama nikimkubali basi angeninunulia gari. Najua angekuwa mtu mwingine angekubali kwa vile hakuwa na mawasiliano na mumewe aliyeondoka bila kuaga.
Lakini kwangu sikuwa hivyo labda ningepata taarifa ya kifo cha mume wangu tena niwe na kithibitisho, hapo ndipo naweza kubadili mawazo na kwa mwanaume muoaji si wa kunichezea kwa vile ana fedha zake mwisho kila mwenye fedha kuugeuza mwili wangu kama dekio.
Baada ya kukaa muda mrefu nilipata wazo la kutafuta kazi. Wazo langu nilimueleza dada ambaye alinieleza atamwambia bwana yake mmoja aliyekuwa na cheo kwenye kampuni moja mjini.
Baada ya kumweleza, alimwuliza nilikuwa nina ujuzi gani, kwa kweli sikuwa na ujuzo wowote zaidi ya elimu ya kidato cha nne tena niliyefeli. Lakini alikubali kunipatia kazi katika duka moja la Supermarket ambalo aliniahidi kunipa jibu baada ya wiki.
Nilimuomba Mungu nipate kazi ili niwe bize nisiwe na wazo baya la kujiingiza katika umalaya wa kuugawa mwili wangu kama pipi. Siku moja tukiwa sebuleni na mama pamoja na dada zangu tukiangalia na kusikiliza muziki wa taarab kwenye video, zikiwa siku nne kabla ya kupata jibu la kuanza kazi, tulisikia sauti ya gari likisimama nje ya nyumba.
Hakuna aliyekuwa na mawazo nalo kwa kujua kama mgeni wetu atapiga honi au kugonga mlango kwa vile marafiki za dada zangu wengi walikuwa wenyeji pale.
Niliwaona kina dada wakitazamana, nilijua kila mmoja alikuwa akijiuliza labda ni mgeni wake, kwa vile hawakuwa na bwana wa siku zote, aliyewahi ndiye aliyepata nafasi ya kuwa na mmoja wa dada zangu.
Mara mlango uligongwa, wote tuliondoa macho kwenye video na kuangalia mlangoni.
"Karibu," dada mkubwa alikaribisha.
Tukiwa tunaangalia mlangoni, sikuamini kumuona mume wangu Beka akiingia. Jamani hata nilivyoamka sijui, nilijikuta nikimkumbatia kwa nguvu na kufanya wote tuanguke chini.
"Yoyooo mume wangu."
Ajabu nyingine baada ya mume wangu kuingia, mama alipata mshtuko na kudondoka toka juu ya kochi mpaka chini. Kwa kweli sikuelewa ule ulikuwa mshtuko wa nini.
Niliamini kabisa huenda mama naye hakutegemea kumuona mkwewe ambaye alikuwa amempoteza zaidi ya miezi minane ameonekana tena akiwa katika hali nzuri. Ilibidi tuingie kwenye kazi ya kumhudumia mama aliyekuwa amepoteza fahamu.
Baada ya kuzinduka aliomba tumuingize chumbani kwake, tulifanya vile mara moja. Baada ya dakika chache, niliwaacha dada zangu nikatoka kwenda kwa mume wangu aliyerudi kama maji jangwani.
Kabla sijazungumza lolote dada zangu nao walitoka, tulijikuta mimi na dada zangu tukiwa na hamu ya kuzungumza na mume wangu.
"Jamani shemeji za siku?" dada yangu alimuuliza.
"Nzuri tu."
"Mmh! Naona mambo si mabaya."
"Kiasi."
"Jamani basi niacheni nizungumze kwanza na mume wangu," niliingilia kati baada ya kuona wananizuia hamu yangu kwa mume wangu.
Dada zangu walinipisha, lakini kabla ya kuondoka walimpiga mzinga shemeji yao.
"Shem makoo makavu," wakimaanisha wanataka kunywa.
Mume wangu bila kusema kitu aliingiza mkono kwenye mfuko wa juu wa shati na kutoa elfu kumi na kuwapatia.
"Mambo si hayo," walishukuru na kuondoka na kuniacha nikiwa na shauku ya kuzungumza na mume wangu. Nilimwangalia kama ndiyo siku ya kwanza ya ndoa yetu.
"Jamani mume wangu karibu," nilimkaribisha na kumshika kwa kumuogopa.
"Asante," alijibu kwa sauti ya chini.
"Jamani Beka mbona sauti ya chini unaumwa?"
"Hapana."
"Uchovu wa safari?'CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Wala, nipo sawa."
"Sasa tatizo nini?"
"Basi tu, sasa Mwaija naomba tuzungumze nje kwa vile mi si mkaaji."
"Kwa nini tusizungumzie chumbani kwetu."
"Hakuna tatizo."
Tulitoka hadi nje ya nyumba kubwa na kuelekea kwenye chumba changu kilichokuwa banda la uani. Tuliingia chumbani kwetu ambako nilikuwa nimepatengeneza kama nilikuwa naishi na mtu, muda wote chumba changu kilikuwa kwenye hali ya usafi.
"Karibu mume wangu," nilimkaribisha kwa heshima zote.
"Asante," bado asante yake haikuwa na uchangamfu.
"Mume wangu mbona huoneshi furaha kuwa karibu yangu, au hujanikumbuka?"
"Kwa kweli najitahidi lakini inashindikana."
"Nini?"
"Najua hata nikikueleza huwezi kunielewa, lakini ipo siku Mungu akijalia tukionana nitakueleza na utanielewa."
"Kitu gani mume wangu?"
"Nina mambo mengi lakini siwezi kukueleza ila naomba nitakachokifanya ukipokee."
"Kitu gani mume wangu."
"Mwaija nakupenda sana na naamini mpaka nakufa sitampata mwanamke aliyenipenda kama wewe."
"Mume wangu mbona unasema aliyekupenda kwani mi nimekufa si nipo?" kauli yake ilinishtua.
"Ndiyo maana nikasema kila nitakachokisema itakuwa vigumu kunielewa."
"Beka mbona leo sikuelewi?"
"Najua hutanielewa ila elewa sina jinsi lazima iwe hivyo."
"Beka! Una nini?"
"Narudia tena katika maisha yangu mpaka naingia kaburini sitapata tena mwanamke kama wewe."
"Beka au umesikia nimeolewa?"
"Hapana, sijasikia chochote kibaya kwako ndiyo maana nasema sitapata mwanamke mzuri na mwenye heshima kama wewe katika maisha yangu."
"Kwa hiyo unarudi ulipokuwa na kuniacha nyumbani?"
"Hapana, nina imani unayajua maisha yetu yalivyokuwa?"
"Ndiyo mume wangu."
"Kilichotokea mpaka kutengana unakijua?"
"Ndiyo mume wangu, baada ya maisha yetu kubadilika na kuwa magumu."
"Unajua baada ya miezi sita mimi ningekuwa wapi?"
"Mume wangu mi nitajuaje wewe ungekuwa wapi?"
"Unajua sababu ya mama yako kuanguka nilipoingia?"
"Hata sijui."
"Basi kama tungekuwa pamoja leo hii ningebakia jina."
"Ungebakia jina? Una maana gani?"
"Mwaija naomba nikueleze kilichonileta kwenu."
"Kipi mume wangu?"
"Nimeamua kuachana na wewe."
"Sijakuelewa, kuachana kivipi?"
"Leo nimekuletea talaka yako."
"Talaka yangu! Kivipi?" nilishtuka na kushindwa kumuelewa mume wangu alikuwa anamaanisha nini.
"Mwaija, nakuacha huku nakupenda sana tena sana, lakini talaka nitakayokupa ni usalama wa maisha yangu."
"Beeka, nilitaka kukuua?"
"Walaa!"
"Sasa usalama upi?"
"Kwa leo hutanielewa."
"Nieleze nitakuelewa tu mume wangu."
"Ipo siku lakini siyo leo."
"Sasa unaniacha ili iweje?"
"Kila kitu mama yako anajua."
"Mama anajua nini?" jibu la mume wangu lilinishtua sana.
"Mwaija mama yako anajua kila kitu juu ya talaka hii."
"Anaijua kivipi?"
" We kamuulize."
"Ndiye aliyesema unipe?"
"Nikiondoka muulize mama yako atakujibu kila kitu tena kwa kirefu."
"Beka mbona sikuelewi, mara kujua kilichomuangusha mama, mara nimuulize mama kuhusu talaka yangu mbona sikuelewi?"
"Majibu ya maswali yote anayo mama yako, ila kila kilichopo hapa ni mali yako na sehemu ya kiwanja cha Charambe nitakiuza na kukupa haki yako. Siwezi kukudhulumu hata senti tano kwa vile ni haki yako."
"Beka umesikia maneno gani mabaya juu yangu? Au umeambiwa na mimi nilijiunga na dada zangu kufanya mchezo mchafu?" nilijikuta nikijitahidi kubashiri sababu ya kupewa talaka.
"Wala sivyo unavyodhania, hujafanya na nina amini huwezi kufanya."
"Umesikia nina mwanaume?"
"Hapana."
"Sasa kosa langu nini mpaka unaniacha mume wangu?"
"Huna kosa ila mama yako anajua kila kitu."
"Beka kwa nini aniambie mama yangu wakati wewe upo? Kama kuna kosa niweke wazi mume wangu, japokuwa naamini sina kosa kwako."CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Nimekwambia siku yoyote tukionana nitakueleza sababu ya talaka, naamini hutakasirika na utakubaliana nami kwa uamuzi wangu huu."
"Beka nimekaa muda gani kukusubiri? Nimejitunza kwa ajili ya ndoa yetu, nimevumilia mangapi leo hii nakuona mume wangu furaha yangu unaigeuza kilio? Beka umepata mwanamke mwingine? Nipo tayari kuishi uke wenza lakini siyo kuniacha Beka, bado nakuhitaji katika maisha yangu," nilimpigia magoti mume wangu ili abadili uamuzi.
"Hata mimi nakuhitaji tena sana."
"Sasa kwa nini unaniacha mume wangu, kama kuna kosa niambie ili nami nijitetee."
"Mwaija huna kosa."
"Jamani! Kama sina kosa, kwa nini unaniacha? Beka ni unyama gani unaonifanyia? Nimekusubiri kwa muda mrefu huku kila siku nikikuombea kwa Mungu ufanikiwe. Leo nimekuona kicheko changu kimegeuka kilio?
"Beka mume wangu nionee huruma, nimeteseka kwa miezi minane sijui upo wapi, unatokea na kunipa talaka, hii ni haki? Beka mume wangu hebu rudisha moyo nyuma. Naomba usijifikirie wewe peke yako, nifikirie na mimi mume wangu," niliendelea kupiga magoti mbele ya Beka ambaye naye alikuwa akitokwa na machozi huku mishipa ya kichwa ikiwa imemsimama.
Beka aliinama na kulia kilio cha kwikwi, kitu kilichonifanya ninyamaze na kumnyamazisha mume wangu.
"Beka usilie mume wangu, niambie tatizo nini, kama kuna uwezekano tulitatue."
"Mwaija," aliniita huku akinitazama, macho yakiwa mekundu.
"Naam mume wangu."
"Mwaija nakupenda zaidi ya sana, lakini lazima nikuache ili pawepo na usalama wa maisha yetu."
"Usalama upi? Mbona sikuelewi?"
"Kwa leo hutanielewa, naomba nikuachie mzigo wako mi niondoke."
"Mzigo gani Beka?"
"Talaka yako."
"Beka unasema kweli au unatania?"
"Sijawahi kukutania," Beka alisema huku akiingiza mkono kwenye mfuko wa shati na kunipa karatasi.
Niliipokea nikiwa siamini, niliifungua na kuisoma, kweli ilikuwa talaka moja. Nilipatwa na mshtuko na kuanguka chini.
***
Nilipozinduka nilijikuta nipo chini nimelazwa, pembeni walikuwepo dada zangu.
"Vipi Mwaija?"
"Beka yupo wapi?" niliwauliza kwanza mume wangu.
"Amekuja kutuita na kutueleza umepatwa na mshtuko, tumeingia ndani na kukuta umepoteza fahamu, baada ya huduma ya kwanza umezinduka."
"Beka yupo wapi?" niliendelea kumuulizia mume wangu.
"Baada ya kutuita tulijua tutakuwa naye ndani, lakini kumbe yeye ameondoka. Beka ni mwanaume muuaji mkubwa sikutegemea," alisema dada mkubwa kwa hasira.
Macho yangu yalitua kwenye mkono wa dada na kumuona ameshikilia karatasi, nilinyanyuka na kumpokonya ile karatasi na kuisoma, nilikuta kweli ni talaka yangu.
"Jamani kosa langu nini mpaka nipewe talaka?" niliuliza huku nikiangua kilio.
"Sasa unatuuliza sisi wakati mlikuwa wenyewe ndani?" dada alionesha kunishangaa.
"Dada kwani kawaambia sababu ya kunipa talaka?"
"Hajatuambia kitu zaidi ya kutuita na kutueleza kuwa umeanguka. Lazima wewe unajua sababu ya kupewa talaka."
"Dada zangu hata sijui chochote, basi ameamua tu, yaani kujizuia siku zote kwa ajili yake, matokeo yake kunipa talaka. Kweli hii ni halali?" niliuliza kwa uchungu huku nikiendelea kulia.
"Sasa mdogo wangu sisi tutajuaje? Wewe ndiye uliyetakiwa kutuambia sababu."
"Najua ninyi ndiyo mmeniponza na kuonekana nami nina wanaume wa nje," niliwalaumu dada zangu.
"Koma weee, upuuzi wako na mtalaka wako isikufanye utuvunjie adabu," dada zangu walinijia juu.
"Laki.." nilikatwa kauli.
"Funga domo lako, alikuja akakufumania?"
"Hapana."
"Sasa kwa nini utulaumu, kwani wakati anakuoa na sasa, kipi kimebadilika hapa kwetu?"
Niliona hakuna msaada wowote kwa dada zangu, niliendelea kulia mpaka mama alipokuja na kunikemea.
"We mtoto mbona unaleta uchuro?"
"Mama inauma, kosa langu nini la kupewa talaka?"
"Wewe Mwaija kipi cha ajabu kwani wewe ni wa kwanza kuachwa. Kipi kimepungua kwako toka aondoke huyo mwana haramu wako, hukulala na njaa wala kulala nje."
"Mama inauma mtu nimsubiri siku zote atokee na kunipa talaka, hii ni halali kweli? Si bure kuna kitu tu mama," nilimlalamikia mama huku nikiendelea kulia.
"Kama unajua huna kosa achana naye, huenda keshaoa huko alipokwenda. Amekuja kuachana na wewe. Unajuaje pengine mwanamke aliyempata alimdanganya hajaoa."
"Lakini mama mbona mume wangu kaniambia eti wewe ndiye unayejua sababu ya talaka yangu?"
"Nini! Mimi niijue talaka yako?" kauli yangu ilionesha kumshtua sana mama.
"Ndiyo mama."
"Sasa haya makubwa! Yaani mimi nijue sababu ya talaka yako wakati mnapeana mimi sikuwepo?"
"Hapana, ila mume wangu kasema wewe unajua sababu ya mimi kupewa talaka."
"Mumeo ndiyo kakwambia hivyo?"
"Ndiyo, kasema nikuulize wewe."
"Hii ajabu! Mwenye kutoa talaka asikwambie, mimi nitajuaje? Huoni huo ni ukosaji wa adabu anaofanya mumeo? Shukuru Mungu kupewa talaka, ni wazi yule mwanaume alikuwa hakufai na pia hakuwa na mapenzi nawe."
"Hapana mama, mume wangu namfahamu vizuri kuna kitu mama unakijua ila unanificha, yeye si mwendawazimu kusema hivyo."CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Nikufiche ili iweje?"
"Eti, halafu nini kilichokuangusha wakati alipoingia mume wangu mpaka ukapoteza fahamu?"
"Mwaija! Swali gani hilo?" niliona mama akinibadilikia.
"Mama kuna ubaya gani kukuuliza?"
"Ulitaka nife ufurahi?"
"Mama mi nifurahie kufa kwako?" nilimshangaa mama.
"Sasa hilo ni swali gani?"
"Basi mama yamekwisha, lakini bado talaka yangu naamini kuna kitu si bure."
"Mumeo asituchanganye, upuuzi wake usitugombanishe bure kuwa makini mwanangu."
"Mmh! Sawa nitajua tu," ilibidi nikubali ili yaishe kwani hapakuwa na ushahidi wa moja kwa moja.
"Hilo ndilo neno."
Baada ya kusema vile mama alitoka nje na kuniacha peke yangu, wakati huo dada zangu walikuwa wameshatoka kitambo na kuniacha na mama. Chumba nilikiona kichungu niliitazama upya talaka yangu huku nikitokwa machozi, haikuwa na mabadiliko yoyote zaidi ya kuandikwa nimeachwa kwa talaka moja.
Siku hiyo nilishinda chumbani kwangu nimejilaza kifudifudi nikiwa nimelalia mto nikiendelea kulia. Nilijitahidi kuvuta kumbukumbu katika maisha yangu ya ndoa kama kuna kosa lolote nililowahi kumkosea mume wangu hata kwa siri kufikia kuamua kunipa talaka.
Baada ya kutafuta kwa muda, sikubaini kosa nililomtendea mume wangu wala kuliwaza, maneno ya mume wangu yalinirudia kichwani kuhusu sababu ya fumbo la talaka yangu. Maneno yalijirudia kichwani mwangu kama mtu aliyekuwa akisikiliza redio.
"Unajua baada ya miezi sita mimi ningekuwa wapi?"
"Mume wangu mi nitajuaje wewe ungekuwa wapi?"
"Unajua sababu ya mama yako kuanguka nilipoingia?"
"Hata sijui."
"Basi kama tungekuwa pamoja mpaka leo hii ningebakia jina."
"Ungebakia jina? Una maana gani?"
"Mwaija naomba nikueleze kilichonileta kwenu."
"Kipi mume wangu?"
"Nimeamua kuachana na wewe."
"Sijakuelewa, kuachana kivipi?"
"Leo nimekuletea talaka yako."
"Talaka yangu! Kivipi?" lilikuwa neno lililonishtua sana.
"Mwaija, nakuacha huku nakupenda sana tena sana, lakini talaka nitayokupa ni usalama wa maisha yangu."
Nikarudia yale maneno kwa sauti ya chini kama namwambia mtu.
"Miezi sita mume wangu angekuwa wapi? Na...na sababu ya mama kudondoka! Kudondoka..mama...i..i...naashiria nini? Kwani kuna nini kati ya siri ya talaka na mama? Mmh! Eti kunipa talaka ni usalama wa maisha yake...mmh! Amesikia nimeathirika?... Mungu wangu lazima kuna mtu amekwenda kumpa uongo mume wangu kuwa nimekuwa malaya na kutembea na mtu aliyeathirika. Mmh! La...la...kini mbo...mbo...na ameuliza kuanguka kwa mama? Jamani hii talaka ina nini, sikubali lazima nimtafute Beka anieleze kiundani...aa...au mama alimtaka mume wangu kimapenzi? Jamani mbona sipati jibu, jamani naweza kuwa kichaa bure."
Nilijikuta nikikosa jibu na kukifanya kichwa kisitulie, kwani kilikuwa kikiniuma kama kidonda kila nilipolazimisha kuwaza kitu kilichokuwa hakina jibu.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment