Search This Blog

Tuesday, 14 June 2022

JAHA - 4

 





    Simulizi : Jaha

    Sehemu Ya Nne (4)





    Alipomaliza kupaka unga sehemu alizohisi zinhemnasa alirejea kwa mkubwa aliyekuwa tayari kapanga na kuamua kusherehekea mavuno ya jasho yake. Hakufahamu lolote kuhusu kile kilichoendelea. Carolina alifahamu kuwa, mbunge huyo angeukwaa mkenge bila shaka yoyote pale tu atakapokaa naye karibu. Lilikuwa jambo gumu kwa mheshimiwa na hata mtu yeyote kutonaswa katika mtego huo.

    Alipoingia chumbani kama ilivyokuwa matarajio yake, Carolina alitimiza lengo lake pasipo shida yoyote. Ilim-chukua dakika tano hadi kumi ambapo mheshimiwa alipotelewa na fahamu. Alilewa na kulala usingizi fofofo. Hakuwa katika hali yake ya dunia hali ambayo ilimfanya Carolina kupekua na kuchukua nyaraka nyingi alizozipenda. Jumla ya nyaraka hizo ilisadikika zilisheheni siri nyingi za kifisadi katika idara na Wizara nyeti nchini. Alifahamu angejichumia pesa lukuki kutokana na vielelezo hivyo. Carolina alifanikiwa kwa kiwango kikubwa sana kutekeleza kusudio la roho yake pale alipoweza kutoweka na nyaraka huku kazificha tumboni kwenye blauzi yake. Alirudi ndani ya chumba alimolala Mputa bwanake aliye mkodi kwa pesa nyingi.

    Achilia mbali siri nyingi zilizofichua hali ya ufisadi nchini, kulikuwemo pia nyaraka za siri kuhusu familia ya mheshimiwa huyo. Kulikuwemo pia barua nyingi zilizokuwa zinamkashifu na kumtaka atilie maanani ahadi zake kule lilipo jimbo lake. Walitishia wananchi wake kutomchagua awamu nyingine hasa endapo angeshindwa kutekeleza azma ya kuhamia jimboni na kutoka huko Dar-es-salaam kuliko makazi yake. Je Kitufya alikubaliana na hali ama nini kilimtokea?

    Nyaraka alizozichomoa Carolina alizificha kwenye mkoba wake aliokuwa kaubeba wakati wa safari. Baada ya kuzihifadhi nyaraka zake alijisafisha na kuendelea na ratiba yake iliyomlenga kumteka Mputa pasipo fahamu yake. Walilala pamoja usiku kucha huku mheshimiwa Kitufya akiwa hana fahamu wakati wote.

    Ilipofika saa kumi na moja na nusu alfajiri wakati mhe-shimiwa Kitufya akiwa hajazinduka, Carolina na Mputa waliianza safari kuelekea jijini Dar-es-salaam. Kwa Carolina safari hiyo ilikuwa kama ya kipofu kwani hakuwahi kufika jijini Dar-es-salaam zaidi ya kuangalia kipindi cha runinga kilichorushwa na kituo kimoja kuihusu Bongo.

    Kweli msafiri kafiri, Carolina alikuwa kafiri wakati huo. Alimbembeleza sana Mputa akijua mwisho wa safari kitakuwa kilio chake. Alipanga kumfanyia hiana ambayo asingekaa aisahau maishani mwake. Hakuwaza kuhusu utu wala utukufu kwa wanaume walioitesa roho yake. Aliwaza na kuamua kuwa, kila mwanamume atampatia adhabu yake pale tu ajipendekezapo kumsemesha na kumchombeza. Hakika alidhamiria kulipiza kisasi kwa visa vyote vilivyochangia kuharibu maisha yake.

    Carolina na Mputa waliendelea na safari ao kuelekea Dar-es salaam. Huku nyuma alikokuwa akihudumu vyumba katika mji wa Nzega kuliendelea harakati za kumpekua Babu yake Tasira mzee Gainda. Hakika mambo yalizidi ugumu na hakuna yule ambaye hakufa-hamu kuwa mzee huyo alikuwa bedui na bazazi mkub-wa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wakati akipekuliwa nyumbani kwake, kilichowashan-gaza wengi katika nyumba zake zote tatu, zilikuwa zi-meunganishwa na handaki ambapo ndani yake kulikuwa na masanduku mawili ambamo walijionea viroja.

    Hakuna yeyote aliyeamini wala kutegemea wangekuta vipande vya masikio pamoja na viganja vya mikono ya zeruzeru katika sanduku la kwanza. Wakistaajabu hayo, sanduku la pili lilipofunguliwa, hakuna aliyebaki kuta-zama kilichojiri. Wakati huo walikutana na mwili wa kichanga zeruzeru kilichokuwa kimekaushwa. Hali hiyo ilifanya umati uliokuwepo hapo kushikwa na simanzi pamoja na uchungu usiopimika. Hakika mzee Gainda alikuwa ni bedui mkubwa asiyekifani. Tasira pia hakuwa na cha kuongea zaidi ya kushikwa bumbuwazi. Ni kweli alikuwa zumbukuku juu ya maisha aliyoyaishi babu yake.

    Mahali pale palikuwa na ushahidi uliodhahiri kuwa Jinasa aliuawa. Nguo zake, baiskeli, simu pamoja na kofia aliyoipenda kuivaa vilikuwemo mafichoni humo. Polisi hawakuwa na jinsi ya kufanya zaidi ya kuchukua vielelezo hivyo kama ushahidi wakumfunga Gainda.

    Kwa hali aliyokuwa nayo huko hospitalini, mzee Gainda hakutumainiwa kupona punde. Hakupata fursa hata ya kusomewa shitaka lake. Alifariki na pingu zake zikiwa mikononi. Alikufa kwa msongo wa mawazo, aibu pamo-ja na maumivu yaliyoukabili mguu wake. Kwa kuwa alitakiwa kuzikwa, hakujitokeza mtu zaidi ya ndugu zake. Baada ya nduguze kuusitiri mwili wa mzee Gainda ikawa ndilo hitimisho la ubedui wake katika uso wa dunia hii. Kweli palipo na moshi kuna moto na siku za mwizi ni arobaini.

    Baada ya hayo kujiri, kilitokea nini kwa Carolina



    Usiku wa giza



    FAHARI NA MAJIGAMBO ni mateso. Huchochea mtu kuingia katika majaribu magumu. Katika matendo baada ya matendo mbalimbali na katika mabadiliko baada ya mabadiliko mapya. Wakati uleule, muda ulikuwa ukuta, ulimzuia Carolina kutenda kadri alivyowaza hapo awali.

    “Mutu ya Kongo” Mputa akiambatana na mrembo mwi-ba Carolina, alianza kuinusa Dar-es-salaam kwa madaha. Kwa kuwa ilikuwa mchana kweupe, Carolina alifurahi sana kuona mandhari ya jiji hilo lenye joto na gasia za aina mbalimbali. Wakati wote aliwaza na kukumbuka maneno ya sifa yaliyotawala masikio yake kuusifu mji huo. Kweli Dar es salaam ni jiji, alijiambia alipojionea msongamano mkubwa wa magari ya kila aina maeneo ya Ubungo karibu na stendi ya mabasi ya mikoani.

    Alivyojiona fahari pale awali ndani ya roho yake, wakati huu alijishusha na alijiona mnyonge kutokana na mwonekano wake. Roho yake ndiyo ilionesha kushindwa lakini alijitahidi kuwa jasiri. Alikuwa mtu wa kuduwaa huku na kule. Alistaajabu alivyoona mabinti warembo wenye kila hali wakiwa na nguo za kushangaza. Ingawa walikuwa warembo, baada ya muda aling’amua kuwa hawakuwa ahali za watu wangali hawajapata wa kuwaweka ndani. Hapakuwa na sababu zaidi ya kuijiwa na usemi usemao vijana wa kiume walikuwa bado wapowapo kwanza. Kilichomchosha wakati huo ni jinsi mabinti walivyokuwa wamevaa nusu uchi kitu ambacho maishani mwake hakugusia kukifanya. Alijaribu kutazama mazingira yote na kuona kila msichana ama mwanamke aliye pita mbele ya mboni zake alikuwa kavaa suruali ama nguo nyepesi iliyoonesha maungo yake hadharani.

    Ama kweli, mji huo ulioneka kuwa na harakati za kila namna. Alistaajabu kuona msongamano wa watu alipo-katiza barabara itokayo Ubungo kwenda Posta ambapo walipitia Manzese, Magomeni na hadi kule kuliko ofisi za mashirika mbalimbali ya kujitegemea na ya serikali. Walikuwa maeneo ya Posta wakati huo. Carolina hakuo-na jengo lolote fupi zaidi ya kushangaa asiyotarajia kama angeyaona Tanzania. Alijua kweli ilikuwa jiji la Dar-es-salaam.

    Wakati akijishusha na kuwaza kuwa alikuwa hatakiwi katika mji huu, alibashiri kuwa walihitajika wastadi kuishi hapa hasa wale wenye elimu ya kutosha. Alikosa jawabu kila alipolinganisha maisha yake yaliyokuwa yamempandisha juu ya mlima wa umashuhuri na yale ayaonayo kwa macho. Hakutegemea kama angalikuja siku moja kuja potea katika bonde la sahau sehemu am-bayo hakuweza kufahamika na yeyote yule.

    Ilikuwa hoteli moja waliyoipenda kufikia wakati hu. Hoteli hiyo ilikuwa ya kifahari ambayo akili ya Carolina haikuwahi hata kuwaza kuwa atakuja kupepesa kope zake ndani yake. Hoteli hii iliitwa STERING DE’ HOME. Mahala hapo palikuwa na kila hali ya kumchan-ganya Carolina. Alizoea wakati wote kusikia hoteli maarufu kama Moven Peak na hata Kilimanjaro na Africana. Yote wakati huu yalifutika masikioni mwake na kuamini hoteli aliyofikia ilikuwa ni ya kisasa isiyo na ulinganifu na chochote.

    Kwa kuwa chumba walichopatiwa kilikuwa na hadhi ya kidiplomasia, kulikuwa na kila kitu ambacho binadamu bora alistahili kuwa nacho. Achilia mbali televisheni, simu pamoja na kiyoyozi, chumba kilisheheni jokofu na vinywaji, ngamizi na mitandao mbalimbali ya mawasi-liano ya kileo viliunganishwa.

    Carolina alikuwa mbumbumbu asiyefahamu kitu zaidi ya kuwasha na kuzima televisheni. Wakati huu walitaka wajipatie walau chakula cha mchana ndipo wasaa ambao Carolina alistaajabu na kuliita jiji la Dar-es-salaam ni la kifisadi. Kilicho mshangaza zaidi wakati huo, ilikuwa ni taratibu zilizotumika kupata huduma ndani ya hoteli hiyo. Mputa alikuwa na macho meupe juu ya mambo yote isipokuwa hilo zito toka kwa Carolina. Alifanya kila agizo la kisasa kujipatia huduma mule ndani pasipo hata ya kukutana na mhudumu ndani ya hoteli hiyo. Milango yote ilikuwa ya kielektroniki iliyotumia kadi kufunguka.

    Kwa kuwa alifahamu vyakula kwa kiasi kidogo, ilibidi ataje chipsi kuku ambayo haijakaushwa sana. Ombi lake liliambatanishwa na ombi la Mputa kuwa yeye alitaka Chaza waliokaushwa na chakula cha Kitaliano kijulika-nacho kama Spanish Omlet. Mputa alibahatika kupata elimu ya kutosha ya kidunia. Aliomba apatiwe vyakula hivyo kupitia mfumo wa kisasa ulioandaliwa na hoteli hiyo. Kweli mfumo ulikuwa sawa na pepo ambayo bina-damu huiwaza na kuifikiri ndotoni.

    Kwa kuwa walichoka, wote wawili pasipo hadhari wa-liamua kupumzika baada ya kujipatia kinywaji na kule-wa. Siku ya pili asubuhi waliamka hawana hali. Mputa alitakiwa kufika bandarini wakati asubuhi siku iliyofua-ta. Alipekua nyaraka zote zilizohitajika na kufunga safari kuelekea bandarini. Wakati huo hakuwa msafara mmoja na kiambata chake Carolina. Alimwacha chumbani amepumzika akiangalia kipindi cha Habari Maalumu kuhusu mchakato wa kesi za kifisadi zilizohusu Benki kuu ya Taifa.

    Hapakuwa na haja ya yeye Mputa kushughulikia moja kwa moja magari aliyoagizwa. Ilivyokuwa imezoeleka, madalali walitumika kufanya taratibu zote za utoaji mi-zigo pale bandarini. Alimpata dalali mmoja mzee Chou-za ambaye ni mkongwe bandarini hapo. Mzee Chouza alimtaka Mputa ampatie nyaraka na pesa taslimu dola mia tano. Alimuahidi arudi baada ya saa tatu ndipo ata-kuta mambo yote yako sawia.

    Kwa kufahamu jinsi ilivyo bandarini hapo, Mputa haku-wa na ubishi wowote. Alitoa pesa hizo na kwenda zake mitaani. Alichokifanya alienda katika duka la kubadili-shia pesa lililopo maeneo ya Mchikichini ili kujipatia fedha za Kitanzania kwa matumizi yake ya kawaida. Hakika siku hiyo alifanikiwa kubadilisha pesa pasipo usumbufu wowote.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Aliporejea bandarini, aligundua na kufahamu kuwa ali-tendewa hila. Hakumkuta mzee Chouza wala yeyote aliyefanana naye. Alipouliza wote aliowauliza hawa-kumfahamu mzee huyo. Alipotakiwa kumwelezea mzee huyo hali na jinsi alivyo mwonekano wake ndipo walimtambua na kumfahamisha kuwa, mzee huyo hujulikana sana kwa jina la mzee wa Bandari. Walimshauri asubiri kwa muda wa nusu saa ambapo walimjulisha kuwa Mzee huyo alienda kuliko ofisi za mapato kupata kibali na kulipia ushuru kwa gharama nafuu.

    Pasipo kufahamu nini kingejiri, Mputa alisubiri hadi dakika arobaini zaidi ndipo mzee wa bandari alirejea. Alikuwa na kila kitu mkononi. Alimtaka avumilie hadi kesho ndipo atakabidhiwa mzigo wake. Ilimlazimu Mputa alipe pesa zaidi ya dola elfu tatu kwa shughuli yote pamoja na madereva wa kusaidia kuendesha magari hayo kwenda mjini Goma. Mputa hakukaidi, alifahamu siri ya mchezo. Aliahidi kutoa pesa zaidi japo angetekelezewa na kufanikisha shida yake ndani ya muda mfupi. Baada ya hapo alirejea kule hotelini alikomuacha Carolina kiambata chake kuisubiri kesho iwadie.

    Ilivyostahili ya Mputa kupenda starehe, alimchukua Carolina usiku ule na kwenda kwenye ukumbi wa sta-rehe ili kujivinjari naye. Hakika hakuwa na staha. Katika harakati hiyo alikutana na kila aina ya fedhuli wa mji waliochenguka na wajihi wake. Kwa kutokuwa na staha, wanaume katika ukumbi wa Dar Jealing walimchombeza Carolina. Walishindana kumjazia mapesa wakati ule ambao Mputa alielekea kutabawali. Kijana aliyemvutia sana Carolina alikuwa mwanamuziki ambaye jina lake alijulikana sana kama BAZ-KO. Wakati Carolina akielekea msalani, BAZ-KO alimfuata hukohuko ili atimize haja zake. Carolina alifahamu fika na kwa makusudi alikata shauri kuwa yeyote na aje atapata zawadi yake. Hivyo hakumkataa mwanamume yeyote aliyeitwa kujiunga naye katika shida zilizonyong’onyeza furaha zake. Siku hiyo iliisha na walirejea hotelini.





    Siku ya agano ilipowadia, Mputa alirejea bandarini kujua hatima ya safari yake. Hakika alizungushwa sana wakati huo hadi Mputa aliamua kutoa mlungura na ndipo kazi yake ilifanikiwa. Kwa hila waliyonayo madalali wa bandari, mzee Chouza alipopatiwa nakala za nyaraka zilizohusu magari, alikodisha vijana ambao walitumika kung’oa kila kilichokuwa cha thamani kilichofungwa kwenye magari hayo. Walifungua taa za pembeni, vioo vya pembeni, redio, ngamizi na chochote kilichoonekana cheye kutoathiri kutembea gari wakati huo. Chouza alimpatia taarifa Mputa akisema;

    “Mzee, kazi uliyonikabidhi nimekamilisha.

    Naomba malipo yangu kama tulivyoahidiana.” Mzee Chouza alimtaka Mputa kummalizia pesa yake.

    “Usiwe na shaka.

    Naomba mzigo wangu nikabidhi kwanza ndipo nami nikupatie haki yako. Gari zangu ziko wapi?” Mputa alihoji.

    “Una wasiwasi?

    Ondoa shaka kijana wangu.

    Umri huu bado huniamini mwanangu.

    Kweli makubwa, pamoja na kuwa nimefanya kazi hii kwa miaka ishirini na tano sasa bado huamini kazi yan-gu!”

    “Hapana, shida muzee yangu!

    Kanuni ya kazi, kisayansi zaidi ni lazima kuangalia uone ndipo hela ifuate. Naomba fanya nisemavyo.”

    “Shika nyaraka.

    Nifuate nikukabidhi gari zako.” Waliongozana wote.

    Alipokabidhiwa magari hayo. Mputa alitokwa na ma-chozi akilaani ubedui uliofanywa.

    “Mzee, mbona hata gari baadhi haziwaki?

    Angalia hii gari ya tatu, haiwaki na hata vitu vyake vingi vimeng’olewa, kulikoni!”

    “Hapana kijana wangu.

    Mali hizi zimefika bandarini zikiwa kama uonavyo.

    Hakuna kilichofanyika hapa cha kuhujumu mali yako.”

    “Tusitaniane mzee.

    Iweje gari hizi nimezipandisha mwenyewe kwenye meli Japan zikiwa salama na zina kila kitu na spea ndani yake leo uniambie zimepokelewa hivi ilivyo. Angalia, hati ya kupokelea hapa bandarini inaonesha vitu vyote vimefika salama. Na meneja katia saini yake hapa kuthibitisha kufika kwake. Muzee mimi nasema vitu vyangu vipatikane hapa. Itatimuka vumbi mzee!” Alipayuka kwa jazba watu wengi wakimsikiliza.

    “Tulia kijana.

    Usipige kelele watatushangaa kijana.

    Kwa nini uwafaidishe watu?”

    “Acha ushenzi wako mzee.

    Bandari gani wizi njenje.

    Kwa nini tusiseme.

    Sitatumia bandari hii tena.

    Acheni utapeli mtafungwa.

    Hii si haki bali ni wizi.

    Nani ameiba kama si uongozi mnaendekeza.

    Acheni ushamba!” Mputa aling’aka.



    Aliendelea kuyakagua magari yake, baadhi yalishindwa hata kuwaka kutokana na mifumo yake kuharibika. Yalikuwa hayana taa, redio na mifumo ya viyoyozi vil-ing’olewa. Ilimlazimu kuanza kununua upya baadhi ya vipuri ili kuyawezesha magari hayo walau kutembea hadi mjini Goma kuliko kituo cha Umoja wa Mataifa kinachojihusisha na maswala ya wakimbizi.

    Wakati akijiandaa kesho yake waanze safari hakupenda kumwacha Carolina jijini Dar-es-salaam. Alitaka waambatane naye kurudi mjini Nzega pengine hadi Goma. Kweli Mputa alidhamiria kumchukua Carolina awe mkewe wa pili. Jinsi maisha yalivyokuwa matamu jijini hapo, Carolina alihisi siku zilikimbia sana. Hakutaka kuondoka na alijua hata kama aneondoka asingepata pesa za kutosha kwa kulipwa na Mputa. Alipanga kumfanyia hila Mputa kwa njia aliyomfanyia mbunge kule Dodoma na kumfanya afanye kile alichokuwa akikihitaji.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kwa kuwa alimzoea sana Carolina, Mputa hakuwa na wasiwasi wowote kuhusu yeye. Stahiki aliyomtunuku Carolina ilikuwa ndiyo hasa adui yake mkubwa. Kweli kikulacho ki nguoni mwako na zimwi likujualo halikuli likakwisha. Carolina alipanga kummaliza Mputa, si kumtoa roho yake zaidi ya kumfanyia hiana. Mkobani mwake Mputa alisheheni dola elfu tano alizokuwa akitaraji kumnunulia mkewe gari ndogo ya kutembelea. Haikuwa rahisi kutimiza ndoto zake hizo. Ilikuwa usiku mmoja kama alivyozoea kubarizi na Carolina kama mkewe. Hakika aliukwaa mkenge. Hakufahamu kama alinusishwa madawa ya kulevya yaliyomlegeza na kum-lewesha na ndipo aliporwa thamani zake zote ikiwemo zile pesa alizopanga kumnunulia gari mkewe.

    Ilikuwa jambo rahisi wakati huo kwa alivyokubuhu Car-olina. Alifahamu kajipatia pesa za kutosha kuyategeme-za maisha yake katika jiji hilo lililo na kila aina ya uchafu na dhahabu. Alitoroka kutoka pale hotelini baada ya kuchukua tax barabarani na kumtaka dereva ampeleke katika moja ya hotel zenye bei nafuu maeneo ya Kinondoni. Haikuwa tabu kwa dereva huyo kumfikisha kadri alivyoomba. Wakati huo alichostaajabu ni pale Kinondoni makaburini, aliwaona kina dada wenye mvuto na warembo wakiwa wamejianika kuinadi miili yao. Hakuamini macho yake majira hayo ya saa saba za usiku. Alijiita mwenye staha kwani hakufikia hatua ya kujianika kama chaza juu ya jiwe akisubiri mabwana kuunadi mwili wake. Ingawa aliifanya kazi hiyo, alihisi bado aliifanya kwa staha.

    Carolina aliamini kuwa, heshima ya mtu hutokana na pesa aliyonayo mwenyewe. Wakati huo Carolina alijio-na mwenye staha isiyokifani. Kibindoni mwake alikuwa tayari na zaidi ya milioni tano za Kitanzania achilia mbali masurufu aliyojilipa mwenyewe kwa kuhifadhi chenji walizorudishiwa baada ya matumizi mbalimbali katika safari yote. Wakati huu aliwaza hata kufika asipotarajia kufika kwa kiburi cha pesa yake. Kama mmea uotapo na kufuata ulipo mwanga, Carolina alitaka kufahamu sehemu aliko mbaya wake aliyeyatesa maisha yake na kumtia kiwewe maishani. Hakuwa mwingine bali ni kijana Tora aliyeanza kumtibulia furaha zake.

    Usiku wote Carolina hakulala usingizi ukamjia. aliwaza sana muda wote akijisemea kimoyomoyo;

    “Carolina mie.

    Bahati dume ndiyo hii nimeipata.

    Ni wasaa wa kumtafuta Tora mbaya wa roho yangu.

    Hapa na Zanzibar si mbali sana.

    Yanipasa kumtafuta ili niweze kuulipa uchungu alioni-sababishia hadi leo najutia. Ngoja kupambazuke niianze safari yangu. Atajutia uamuzi wake.”

    Carolina alikesha akiziangalia pesa zake. Aliwaza na kuwazua na kukata shauri kuwa hapatakuwa shaka alihitimisha safari ya Mputa. Hakuhisi wala kuhofu kama atatafutwa na kupatikana jijini Dar es salaam kwa jinsi mji ulivyokuwa na vurugu nyingi.

    Akiwa amefikishwa usiku ule pale Kinondoni na dereva wa taxi, alibahatika kupatiwa namba za simu. Alim-womba bwana yule ili apatapo dharura angemtafuta na kumpeleka popote alipostahili kupatembelea. Alimwahidi kuwa, atampigia ili ampeleke bandarini kesho yake asubuhi ili aweze kuelekea Zanzibar kwenda kumtafuta kijana Tora. Alitekeleza jambo hilo asubuhi sana hata kabla ya saa kumi na mbili za asubuhi. Alijua wakati huo kuwa, Mputa Mkongo alikuwa bado kalewa madawa aliyoyanusa na kuyalamba pasipo hadhari yoyote.

    Wakati Mputa amezinduka, ilikuwa tayari saa tatu kaso-ro robo asubuhi. Wakati huo Carolina alikuwa tayari ameshapanda boti kwenda Zanzibar. Alipozinduka ali-kanganyikiwa baada ya kumkosa. Mkoba wake pamoja na simu yake ya mkononi vyote havikupatikana. Alifa-hamu fika ameingizwa chuo kikuu kama wabongo wali-vyopaita jijini hapo. Hakuchelea kulia ingawaje alibaha-tika kupata fedha zilizokuwa zimehifadhiwa na dereva wake Makonya. Wakiwa na Carolina, Mputa alimkabid-hi dereva wake kiasi cha dola elfu mbili mapema. Pesa hizo hakika zilikuwa mwokozi wa safari yake kwani alipaswa kuanza safari majira ya saa tano yeye pamoja na msafara wa madereva walioendesha magari aliyoyafuata.

    Mputa alifahamu jinsi Carolina alivyokuwa limbukeni wa mjini. Alifahamu ya kuwa, bila shaka atakuwa ame-rudi mjini Nzega ama atarudi Nzega baadae kidogo na atampata kwa urahisi. Alichojilaumu ni pale aliposhind-wa kufahamu shetani gani alimwingia hadi alisahau kupata picha yake, na hata ushahidi hakujaliwa kuupata. Hakuwa na janja, Carolina alitoweka na simu yake ili kumnyima mawasiliano. Mputa aliuahidi moyo wake kutorudia tena udhaifu huo.

    Tokea pale na baadaye, Carolina alishawishi bahati kubwa ya ajabu kumuandama. Bahati aliyoishawishi sasa ilitokana na machozi yaliyowatoka wengi ndipo aliponufaika yeye. Aliongelea maisha ya jaha wakati wote. Alipowasili bandari ya Zanzibar hakujua aelekee wapi. Aliwaza na kuwazua kisha jawabu likavamia fikra zake. Wakati huo aliamua kuwasiliana na madereva wa taxi ili wampeleke hoteli yoyote iliyokuwa karibu na maeneo hayo.

    “Kaka habari yako?” alimsabahi mwendesha taxi.

    “Salama dada. Karibu usafiri.”

    “Asante. Nahitaji unipeleke hoteli yoyote yenye staha na usalama hapa mjini. Nahitaji kupumzika.”

    “Mara yako ya kwanza kufika mjini hapa? Maana inao-nekana si mwenyeji hapa Zanzibari.” Dreva taxi alihoji.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ndiyo! Mi mgeni, natokea bara. Nimekuja hapa mara moja ki biashara pekee.”

    “Sawa! Naomba nikupeleke hoteli moja iitwayo El Fad-hili, ama Kikombo Inn. Chagua moja.”

    “Hapana, nipeleke unakopapenda zaidi nami nitapapen-da.”

    “Basi twende nikupeleke El Fadhili. Ni pazuri, patulivu na pia usalama upo. Ni hoteli yenye hadhi.”

    “Haya endesha twende.” Gari liliondoka kuelekea ilipo hoteli.

    Walitumia dakika chache kufika ilipo hoteli hiyo. Caro-lina alipapenda sana hata alimshukuru sana aliyempele-ka. Dhamira yake ilikuwa hai kumpata Tora. Fikra zote zilitawaliwa na sura ya Tora. Aliwaza na kuwazua wakati wote wapi angempata kwa urahisi ingali ni mgeni katika mji wa karafuu. Wakati wote alijitahidi sana kuvuta kumbukumbu ya mazungumzo yaliyokuwa yakitawala pale kwa Mzee Miembe kuhusu Zanzibar. Hakupata jawabu na majina ya sehemu zote yalimtoka wakati huo. Aliamua kuelekea kuupoza mwili bafuni kwa kuoga na kisha usingizi mzito ulimchukua.

    Wakati akiwa katikati ya usingizi alijiwa na ndoto am-bayo hakuwa amewahi kuota hapo awali. Akiwa ndotoni alikutana na Tora. Aliota ameamka na kuelekea bandarini katika usiku huo wa ndoto. Akiwa kaushika mkoba wake wenye nakshi mkononi pamoja na viatu mchuchumio alikaza mwendo kuelekea alipokuwa amesimama. Tora alionekana bandarini akikata tiketi kwenye kilango cha boti ziendazo Tanga.

    Wakati anakiburi cha pesa alimfikia Tora alipokuwa kasimama. Kwa nyuma alimshika bega akiwa mkinya. Tora aligeuka na kuduwaa kwa sekunde chache ndipo aliita kwa mshangao;

    Carolina!......

    Duh!

    Kweli milima haikutani lakini kwa binadamu ni lazima.

    Kulikoni! ........siamini macho yangu.

    Nahisi naota, tena ndoto ya mchana.

    ....... Hivi ni wewe?

    Wakati wote huo Carolina alikuwa haongei chochote. Alimkazia macho Tora kwa jicho la huba pia dharau ndani yake. Ndoto ya Caro iliendelea kumuwewesesha usiku huo.

    Ndotoni mwa Caro Tora naye alikumbuka kilichomfiki-sha Zanzibar kilikuwa ni nini? Alijua kuwa ni juu ya Carolina. Ghafla alihisi Carolina amemfuata kulipiza kisasi ndipo ilibidi ampigie magoti hata bila haya kwenye unasi. Alisema;..Ca.....Carolina ! Nisamehe kwa yote niliyokutendea.......Nafahamu moyo wako hata mwili niliusononesha sana. Utakuwa na taathira rohoni mwako.. Tafadhali naomba sana nielewe na wala usinid-harau.

    Akiwa ndotoni Carolina alitokwa na chozi mfululizo huku akimshika mkono Tora kumnyanyua pale alipokuwa amepiga magoti. Alimhakikishia Tora usalama na msamaha wake kwa fumbo kali aliposema;.... “Tora, nimeshakusamehe tayari... Nilishakusamehe tangu siku ile ya unyama wako kwangu, yote niliyasamehe na kumwachia Mungu... kumbuka adui yako mwombee njaa lakini mimi naamini kuwa adui yako mwombee neema na usimlipize ubaya ili ajionee mwenyewe neema ya Mungu ilivyo. Nimeshakusamehe Tora!”

    Hatimaye ndoto ilimsafirisha katika ulimwengu wa ma-haba. Alimkumbatia Tora na kisha walibarizi wote. Chumba kizima kilijaa kelele toka ndotoni mwa Caroli-na. Mhudumu aliyekuwa karibu na mapokezi aielekea palipo mlango wa Caro akabisha hodi na kuugonga kwa nguvu.





    “Hee!

    Vipi mbona mnasumbua wengine?

    Acheni utoto bwana.

    Watu wengine bwana!”

    Baada ya mlango kuwa umegongwa, Caro alishtuka na kusikiliza sauti iliyogonga mlangoni. Alinyanyuka ku-elekea mlangoni akifungua kwa hadhari. Alikutanisha macho uso kwa uso na msichana mhudumu na kumhoji.

    “Kulikoni usiku huu anti?”

    “Unapiga makelele sana hata wateja wengine unawakera. Kwani una bwana mnagombana naye humu ndani ama kuna nini?”

    “Nisamehe anti.

    Sina mtu yeyote ndani niko peke yangu.

    Ni ndoto tu imenikumba wakati huu.

    Wala sikujua kama kweli nimepiga makelele, nisa-mehe!”

    “Hapana shida.

    Hiyo ni ishara mbaya, Mwombe mola wako kisha ulale kamwe hutaota tena. Usiku mwema!”

    “Asante anti.

    Usiku mwema nawe pia!”

    Carolina alirejea kitandani kwake na kujitupa. Hakuu-funga mlango wakati huo alijisahau. Aliamua kuushika mkoba wake na kuziangalia pesa zake na kisha anashik-wa na shauku ya kuzihesabu. Ghafla aliwaza kuwa in-aweza kutokea siku moja akaibiwa pesa zote na kukosa cha kufanya. Ingawaje hotelini hapo walisisitiza kuwa kama mtu ana mali za thamani alitakiwa kukabidhi kwa wahusika la sivyo tatizo litokeapo asilaumiwe yeyote. Carolina aliamua kuzilalia pesa zake. Baadhi aliziweka uvunguni kwenye gazeti na kiasi fulani ndani ya bahasha na zingine zilibaki kwenye mkoba.

    Nini kilimkumba Carolina wakati huo? Hakika hakuota wala kutabiri kilicho mkuta hapo baadaye. Aliwaza sana usiku ule kuhusu ndoto iliyomkabili na alijiuliza;

    “Nini hiki sasa?

    Inawezekana nikampata Tora muda mfupi huu uliopo?

    Sijawahi kumwota hata kuweweseka juu yake.

    Mbaya zaidi nimwote na….. ah!

    Hata kelele …. kiasi hiki.

    Hakika haitawezekana.

    Hii ni ishara mbaya kwangu.

    Sitaweza kumpata inawezekana.

    Ikiwezekana nitamshukuru Mungu!” Alijiwazia kisha alijiegesha kuingoja asubuhi kuwadia.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ilivyofika saa kumi na moja aligutushwa na sauti zitokazo misikitini. Ni sauti zilizoalika waumini wa dini ya kiislamu kuhudhuria ibada na kumwabudu Muumba wao. Alijua fika tayari ni saa kumi na moja na aliamka na kuanza kujiandaa kwa mizunguko ya siku hiyo. Haikumchukua muda ikatimu saa moja kisha alielekea mapokezi na kumweleza dada wa mapokezi kuhusu uwepo wake hapo. Alimtaka amtunzie chumba kwani atakuwepo hapo kwa kipindi cha siku tatu zaidi akikusanya mzigo wa biashara ili apate kufungua biashara yake arudipo Nzega. Dada wa mapokezi hakuwa na hiana, alimkubalia na kumtunzia chumba kisha aliteremka kuelekea mgahawani kujipatia staflahi yake hasa chai aliyoipenda. Alipendezwa sana na watu wa mji huo. Alipokewa na kila macho yenye staha kisha alistahi nafsi yake.

    Wakati akimalizia kikombe cha chai, wazo lilimjia baada ya kuwasikia jirani aliokuwa karibu nao wakizungumza kuhusu miji ndani ya Zanzibar. Alisikia wakizungumza kuhusu mji wa Forodhani, Kiembe Samaki, Michenzani na Chambani. Alitafakari na jibu lilimjia kuwa sehemu ambayo Tora alikuwa akipazungumzia kuwa ni kwa shangazi yake ni Kiembe Samaki. Alinakili jina hilo kwenye karatasi na kisha alitoweka na kuelekea mjini katikati kufanya manunuzi ya vitu alivyovitafuta. Wakati akinunua vitu alifanya kila mbinu kulipa asijulikane pesa anakozitoa. Hakuwa na hili wala lile kama kuna wakora tayari walinusa na kugundua ugeni wake na pia kufahamu kuwa katika mkoba wake kulikua na pesa.

    Walimtia alama akilini mwao na kuanza kumfatilia kote kule aendako. Wakati akipandisha mizigo yake kwenye taxi, ghafla alihisi mkoba wake ukikwapuliwa. Alipo-geuka alikutana na kibao kilichomfanya ashikwe jelezi na kudondoka chini pembezoni mwa barabara. Mkoba ulianza kuota miguu kama si mbawa mikononi mwa mkora mmoja aliyekuwa akikimbilia pikipiki ili kukwe-pa shari. Raia wema hawakukosa wakati huo. Waligun-dua uovu huo na kumtia mbaroni mhusika na kisha wa-limtaka Carolina kuandamana nao hadi kituo cha polisi kati kwenda kutoa maelezo. Caro alifikiria sana wakati huo. Hakuamini hata siku moja kama visiwani Zanzibar kuna wakora wenye uchu wa kupora na kupokonya ama-li za wengine.

    Iliwachukua muda mfupi sana kukamilisha kuandikisha maelezo ya awali hapo kituoni. Carolina alitakiwa kurudi kituoni kesho yake ili kupatiwa taarifa sahihi kuhusu kufunguliwa kwa jalada na hati ya mashitaka juu ya mtuhumiwa kabla ya kumpeleka Mahakamani. Carolina alirejea hotelini akiwa na maumivu ya jicho ambayo yalitokana na kibao cha mkora mpora pesa. Hakuwa na la kufanya wakati huo. Aliamua kwenda kulala na ilipotimu saa nane alihisi maumivu yakimzidi na kisha alikata shauri kwenda hospitali kuangalia kama aliumia na kipigo hicho. Alichunguzwa na daktari na hapakuwa na jeraha kubwa. Alishauriwa kuiangalia hali yake na kisha atumie dawa ya maumivu na ya kuchua sehemu alipopigwa kwani hali ingerejea kawaida. Alirejea hotelini kuisubiri kesho ifike aelekee kituo cha polisi kufahamu kinacho endelea.

    *****

    Wakati huo Tora hakuwa na habari wala hisia juu ya uwepo wa Carolina Visiwani. Hakuwaza hata kuwa kuna siku ataonana naye akiwa kisiwani Zanzibar. Aliwaza na kuamini kuwa Carolina hawezi kufika Zanzibar kwani hakuwa na ndugu na hata hakuwahi kugusia kuihusu mji huo. Wakati huo alikuwa kaagizwa na Shangazi yake kwenda kumkatia tiketi ya kwenda Tanga. Hii ilikuwa kama ndoto ya Carolina ilivyomtuma usiku mmoja uli-okuwa umepita.

    Tora aliukaza mwendo wake kuelekea Bandarini kukata tiketi ili shangazi yake apate kusafiri kwenda Tanga kumwona mdogo wake. Alibahatika kufika salama mae-neo ya bandari ingawaje alipatwa na tashwishi. Alipati-wa tiketi na alipojaribu kutoa pesa aliyokuwa kapewa na shangazi yake, hakuweza kuiona pesa hiyo. Jambo hilo liliwakera wakatisha tiketi na wakalazimika kumtia chini ya ulinzi kwa msaada wa polisi na kwenda naye hadi kituo cha Polisi cha mjini kati kwa tuhuma za utapeli. Haikuwa rahisi kwa Tora kusikilizwa wakati huo ingawa alijaribu sana kujitetea wakati akitiwa mbaroni. Hakuwa na jinsi alitiwa korokoroni na watuhumiwa wengine akiwemo mkwepuaji wa Carolina.

    Uliingia usiku Tora akiwa korokoroni akingojea hatima yake. Alifahamu hakuwa na msaada zaidi ya kumtege-mea Mungu wake ili kupata haki yake. Ilikuwa vigumu kuamini na hakutarajia kuwepo siku ambayo angeweza kutiwa mbaroni na kisha kuswekwa korokoroni. Aliwaza sana usiku huo akijitahidi kutopumua kwa nafasi kwani harufu ya mikojo na vinyesi walivyojisaidia wenzake viliondoa hewa safi na kujaa harufu yenye kukera. Hakustahimili hali wakati huo zaidi ya kushikwa na kichefuchefu. Aliona usiku ni mrefu akiingojea asubuhi ili kuchukuliwa maelezo. Aliwaza sana wakati wote kule ambapo pesa husika ilienda hasa baada ya kuikosa mifukoni mwake. Aliishia kubashiri na kujenga hisia kuwa, pesa hiyo yawezekana kabisa ilikwapuliwa alipokuwa katika mbanano ndani ya kipanya ambacho alipanda akiwa amesimama akielekea bandarini. Alijaribu kuvuta hisia, kamwe hakufaulu kupata jawabu. Kutahamaki alipokuwa akijiwazia ugomvi ulivuma ndani ya selo hiyo kati ya mmoja wa tapeli mkwepuaji alipokutana na ambaye aliwahi kumkwapua mtaani na kumnakili sura yake. Vurugu zilizidi na walipigana wakati ambapo Tora alikata shauri kuamua ugomvi huo. Alifanikiwa kuwatuliza ingawaje katika vurugu hizo mtondoro ulimwagika na kutapakaa katika sakafu ya selo hiyo na kufanya wote waliotiwa mbaroni kusimama na kujibanza pembezoni mwa ukuta kama mijusi. Tora alitokwa na machozi kisha aliendelea kufanya mazungumzo na mporaji wa Caro wote wakiitafuta kesho angalau wafahamu ambacho kingejiri;

    “Sheikh!

    Unaitwa nani rafiki” Tora alihojiwa

    “Naitwa Tora, we nani?”

    “Mi naitwa Jeba Matata.

    Una tatizo gani hadi uko hapa?”

    “We acha tu.

    Sikutegemea kama nitaingia humu.

    Imetokea tu.”

    “Ulitegemea nani aingie humu.

    Nioneshe mmoja aliyetegemea kuingia humu.”

    “Hapana, si hivyo.

    Katika maisha yangu, sijawahi kufikiri kuingia humu. Leo nimepatikana.”

    “Mbona unakuwa na maneno mengi.

    We sema, kwa nini uko humu?

    Maneno mengi eti hustahili wala hukuwaza ni historia upo hapa tayari sema?”

    “Nilikuwa bandarini mapema leo kumkatia shangazi yangu tiketi ya usafiri kwenda Tanga. Wakati nimepati-wa tiketi nililazimika kutoa pesa. Isivyobahati, sikuikuta hiyo pesa mfukoni mwangu na hapo ndipo mambo yaliponigeuka. Kilichonishangaza hata kusikilizwa sikusikilizwa, haya ni maajabu sana katika nchi hii na sijui itakuwaje.”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Shilingi ngapi ulitakiwa kulipa?”

    “Ni hela kidogo tu wala si nyingi.”

    “Kidogo shilingi ngapi?

    Mbona unakuwa kichwa maji wewe?

    Ukiulizwa jibu swali.

    Inavyoelekea, omba usifikishwe mahakamani.

    Ukifikishwa hutatoka na utatiwa hatiani kwa sababu ya ubwege wako. Mi nimekuuliza ni shilingi ngapi unajibu lingine, angalia.”

    “Ni hela kidogo kama elfu ishirini na tano hivi.”

    “Hiyo hela kidogo!

    We mwendawazimu nini.

    Nilifahamu kitambo kuwa utakuwa na akili timamu. Pesa yote hiyo ni kidogo? Nyingi kwako ni ngapi?”

    “Si hivyo kaka.

    Nina maana ni kidogo kwani hata kama iliibiwa ningei-pata mara moja kama ningepata wasaa wa kurudi nyum-bani. Angalia pesa kidogo inanitesa hivi leo.”

    “Acha ushamba wako.

    Pesa kidogo kama hiyo!

    Pesa nyingi sana hiyo na aliyekupora amepata mtaji wa siku kazaa. Kidogo kwako kwa maskini kama mimi hiyo ni pesa nyingi sana. Natamani hata ningekupora mimi.”

    “Kwani wewe ni mporaji wa pesa za watu?”

    “Nani kakwambia mimi ni mporaji.

    Umejuaje?”

    “Kwa ulivyonieleza punde.”

    “Mi si mporaji bali ni mtafutaji.

    Nawe ndiye tapeli?

    Unatapeli hadi bandarini mwanangu!

    We kiama mwanangu!”

    “Kamwe huo si msimamo wangu.

    Sijawahi kudokoa vya mtu nina hakika na hilo.”

    “Sema haki ya nani! Hujawahi?”

    “Ndiyo! Sijawahi.”

    “Basi utakuwa na tatizo akilini mwako.

    Kwani cha mtu ni nini?

    Si lazima kiwe pesa ama chochote cha kubeba.

    Yaweza kuwa hata mabinti wa jirani zako?

    Hujui hilo ndilo udokozi mkubwa?

    Wakati mwingine watu hubaka na hata kumtia mimba mtoto wa jirani, hilo ni udokozi kwani hujapewa kuwa naye kisheria. Tena ninyi vijana gubegube, sharo-sharo hamna simile wala subira. Angalia mambo si vile ufiki-riavyo. Nakuomba ujue kuwa polisi, jela na mahakama vipo kwa kila mmoja ingali muda tu hutofautiana.”

    “Inatosha basi.

    Hebu nieleze pia, kwa nini uko humu na naona una ngeo kila pahala?”

    “Ngeo hizi zisikutishe sana.

    Hii ni alama ya mzalendo mtafuta mali na ni ishara ya mwanamume wa shoka. Ulitaka niwe kama wewe mrembo? Usiombe kwenda gerezani, watakuoa Manya-para.”

    “ Hujanijibu bado.”

    “Hiyo ni rahisi sana.

    Mi mjasiriamali.

    Wakati wote kazi yangu ni kukusanya vilivyosahaulika na wenyewe. Jana nilikusanya mali ya mwenyewe akiwa hajaisahau nikatiwa mikononi.”

    “Kitu gani ulikusanya cha mwenyewe. Uliiba?”

    “Nimeshasema mimi si mwizi bali ni mjasiriamali.

    Wezi hawapo tena nchi hii.

    Tumebaki wajasiriamali za watu waliozisahau.

    Nilikusanya mkoba wa dada mmoja mjini kati hapo akawa kaniona na wavimba macho wakanitia mbaroni.

    Nashukuru sijapoteza uhai kwa kipigo kwani walikuwa na hasira.”

    “Lazima wawe na hasira.

    Wanatafuta mali kwa jasho, iweje mwingine ale kwa feni?”

    “Hakuna yule alaye kwa feni hapa.

    Huoni ni kazi ngumu kupora cha mtu.

    Walao kwa feni ni wale viongozi wenye matumbo am-bao hujichotea vyao mapema baada ya wavuja jasho ku-toa kodi zao. Hao ndio wezi hawafanyi kazi lakini huku-sanya na kutia kapuni bila haya. Si wavuja jasho bwa-na.”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kwa hiyo itakuwaje sasa?” Tora alihoji.

    “Itakuwaje ki-vipi?”

    “Kitu gani kinafuata baada ya hapa?”

    “Mahakamani!

    Kama unachochote waweza kuwapa udi wazee wakua-chie hapa. Bila hivyo utapelekwa mahakamani na kisha mahabusu huko gerezani”

    “Gerezani!

    Kwa kosa gani sasa hadi nipelekwe huko?”

    ITAENDELEA 

0 comments:

Post a Comment

Blog