Simulizi : Jaha
Sehemu Ya Tano (5)
Kama unachochote waweza kuwapa udi wazee wakua-chie hapa. Bila hivyo utapelekwa mahakamani na kisha mahabusu huko gerezani”
“Gerezani!
Kwa kosa gani sasa hadi nipelekwe huko?”
“Hujui kosa lako? Ni kuingia humu kwa sababu ya uta-peli.
Hulijui kosa lako?”
“Hilo jambo dogo sana hata hakimu hawezi kunitia nda-ni. Elfu ishirini tu!”
“Angalia, watu wengi waliomo jela si kweli wote wali-hukumiwa na kutiwa hatiani. Kuna wengi walitiwa ndani na kesi zao kutelekezwa hivyo wana miaka mingi gerezani pasipo kusikilizwa wala kuhukumiwa. Isitoshe hawajawahi hata kufanya chochote na wengi wao ni wezi wa kuku. Iwe wewe kwani ni nani? Una mjomba wa kukutoa?”
“Naishi na shangazi yangu hapa mjini na hata sifahamu kama anataarifa hii.”
“Umekwisha.
Ngojea asubuhi ifike uchukuliwe maelezo na utwaliwe mahakamani na huko hutatoka.
Nchi hii sheria ni pesa.
Kama unayo pesa basi wewe ni mfalme utaonja pepo.”
“Ha!
Sawa bwana.
Mungu anajua itakavyokuwa na iwe.
Nina imani nitatoka.
Wewe atakutoa nani katika janga hili?”
“Nitatoka tu.
Mi nishazoea huku ni nyumbani.
Nitakwenda lakini siku chache nitatoka kwani kesi yan-gu haitapata shahidi.
Nafahamu wote ambao huwakwapua wengi wao si wa-kazi wa mjini hapa ni wapita njia.
Hawana muda wa kufatilia kesi.”
Mazungumzo yao yalikatishwa na askari aliyefungua mlango na kumsukumiza mtuhumiwa mmoja aliyeka-matwa wakati wa doria akiwa na bunduki tayari kufanya uhalifu. Anlisukumizwa ndani na alidondoka chini pali-po tapakaa mtondoo. Kimya kilitawala na kila mmoja alibaki kimya akitafakari kilichotokea.
Saa ziliyoyoma na kisha asubuhi iliwadia. Carolina naye aliishika njia kuelekea kilipo kituo cha Polisi cha mjini kati. Wakati huo alikata shauri la kutoa maelezo na msimamo wake kuwa alimsamehe aliyempora na kisha kuendelea na maisha yake. Alijua fika kuwa, awapo na kesi ingemlazimu kupoteza muda mwingi kufatilia kesi ambayo haina manufaa kwake. Ilimchukua nusu saa kuwasili kituo cha polisi. Moja kwa moja aliingia katika chumba cha mapokezi na kumkuta dada mmoja akiwa zamu.
“Karibu nikusaidie.” Alinena askari wa zamu mapokezi.
“Asante.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Jana nilikuja hapa kutoa maelezo kuhusu kuporwa kwangu mkoba. Mtuhumiwa alikamatwa na yupo hapa sasa. Jana niliombwa nije asubuhi ili kuangalia hatua itakayofuata.”
“Sawa.
Jana ulichukuliwa maelezo ya kutosha?”
“Hapana.
Niliandikisha tu hapa mapokezi, sijachukuliwa maele-zo.”
“Subiri nikuitie askari atakayeshughulikia jambo hili.”
“Hapana!
Nilikuwa na wazo.”
“Wazo gani hilo?”
“Nimeamua kumsamehe.
Mwacheni aende zake.
Kama anaweza kujifunza atakuwa kajifunza.
Dunia itamhukumu.”
“Hapana dada.
Huo si uamuzi wa busara.
Mtuhumiwa lazima afikishwe mahakamani.
Kama kuachiwa huru aachiwe huko huko.”
“Sawa nimekuelewa.”
“Naomba pita chumba cha upelelezi utamkuta askari atachukua maelezo yako.”
Carolina aliingia chumba cha askari mpelelezi na kuchukuliwa maelezo. Baada ya muda alitakiwa kusubiri nje ya chumba hicho kujua uamuzi utakaofuata. Askari mpelelezi alitoa agizo la kumwita Tora Miembe ili ahojiwe. Wakati askari mpelelezi akitoa amri ya kuletwa Tora, Carolina alisikia kwa mbali na kisha alihisi kuwa jina hilo si la kawaida ndani ya visiwa vya Zanzibar. Alistaajabu alichokiona wakati huo. Aliona ni sura ya aliyemtamani kumpata wakati huo. Hakika, alikuwa ni Tora aliyechoka wakati huo. Alionekana mnyonge asiye furaha usoni kwake. Mwili wake ulichoka, miguuni alikuwa peku huku suruali yake ikining’inia kama pulizo. Askari alimsindikiza kuelekea chumba cha mpelelezi. Akiwa katika mawazo ya kukumbuka, aliwaza jinsi Sudi alifanya hapo kitambo na jinsi alivyoonekana wakati huo. Huruma ilimjia akajikuta akimwita Tora kwa sauti.
“Tora!
Ni wewe?”
Machozi yalimtoka na kisha kwikwi iliziteka pumzi zake kwa uchungu. Hakutarajia kumwona Tora sehemu hiyo kwa urahisi. Alihisi pengine alifanya kosa lile lile la awali alilomfanyia yeye la kumbaka pasipo aibu.
Tora naye hakuamini macho yake. Alipoiona sura ya Carolina alihisi kunamuujiza unatokea. Alijaribu sana kutafakari mengi kwa sekunde chache na kisha kupunga mkono kwa Carolina akitabasamu kwa furaha. Askari hakuwa na wakati wa kusubiri zaidi ya kumfokea na kumtaka awahi kuelekea ilipo ofisi ya mpelelezi. Ali-chukuliwa na kisha kuwasilishwa katika ofisi ya mtaa-lamu mpelelezi. Mahojiano yalianza;
“Unaitwa nani?” Askari mpelelezi alihoji.
“Tora.”
“Tora Mkojo!
Una jina moja, ulijizaa mwenyewe?”
“Hapana afande.
Naitwa Tora Miembe.”
“Umri wako?”
“Miaka ishirini na tano.”
“Kabila lako.”
“Sijui”
“Pumbavu.
Huna kabila?
“Mtanzania. Mimi Mtanzania toka Tabora.”
“Mwenda wazimu nini.
Hujui tofauti ya kabila na utaifa wako?”
“Najua. Kabila langu mi sijui. Baba ni mp…”
“Kweli wewe ni zumbukuku heri ya mbuzi!
Mbuzi! Tangu lini kabila likawa Mp..?”
“Mi najua hivyo.
Sijui kabila langu.”
“We si M.........!?
Basi acha niishie hapa.
Kazi gani unafanya hapa mjini?”
“Sina kazi.”
“Huna kazi!
Sema jambazi.
Kwani upo hapa kwa nini?
Si wizi?”
“Hapana afande.
Mi sio mwizi, si bahati tu nipo hapa.”
“Tutajua ukweli punde.
Inaonesha wewe ni jambazi sugu.
Bunduki iko wapi?”
“Sina bunduki na siijui afande.”
“Haya tuendelee.............,....!
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Askari mpelelezi alimchukua maelezo Tora wakati huo. Alieleza yote yaliyojiri na kisha askari mpelelezi alihi-timisha mahojiano na Tora kwa kumuuliza;
“Una ndugu wa kukusaidia?”
Tora alinyamaza kidogo kisha alipatwa na jawabu la kumtaja Carolina kama ndugu yake.
“Ndiyo, nina ndugu”
“Anaitwa nani?”
“Carolina.”
“Nani yako?” Tora alisita kidogo kisha aliendelea.
“Dada yangu.”
“Anaishi wapi?”
“Sijui anapoishi lakini yupo nje hapo.”
“Hupajui anapoishi eee?”
“Tunaishi naye Kiembe Samaki.” wakati huo alidan-ganya.
“Askari wa zamu. Naomba niitie mtu aitwaye Carolina hapo nje.”
Aliitwa Carolina na alielekea ofisi ya mpelelezi. Akiwa na wasi wasi nini kingetokea wakati huo. Mawazo yali-uteka mwili akiwaza nini kingetokea. Alijikaza akaingia ndani ya chumba cha mpelelezi;
“Naomba keti hapo.”
Mpelelezi alimwonesha pahala pa kuketi na aliketi. Tora alimkodolea macho Carolina na kutaka kumsemesha. Alitafuta namna ya kumpatia ujumbe ili akubali kweli ni dada yake. Wazo la kumbaka Carolina kichwani mwa Tora lilitawala na wakati huo alihisi kuwa tayari alipatikana na hatia ya kweli. Endapo Carolina angekataa kuwa kaka yake ingekuwaje? Askari mpelelezi aliendelea kudadisi;
“Wewe ndiye nimechukua maelezo yako muda mfupi uliopita kuwa uliibiwa?”
“Ndiyo ni mimi.”
“Haya, nieleze unamfahamu huyu?”
“Ndiyo namfahamu.”
“Unamfahamuje?” Carolina aliingiwa na wasiwasi huku Tora akiwa kamkazia macho na kutamka maneno ki-moyomoyo kwa ishara ya mdomo “kaka”. Caro aliiona midomo ya Tora ikiwa inatamka kimyakimya neno hilo na kisha aliongea.
“Kaka yangu.”
“Una mpango gani naye.
Unataka tumpeleke mahakamani?”
“Sijui kwani kafanya nini?”
“Muulize atakueleza.”
Tora alidakia na kusema yote yaliyomtokea. Carolina alisikitika na kumwomba askari mpelelezi watete naye kidogo. Wakati wakitoka nje Tora alijawa na hofu kuwa Carolina angeweza kuyatapika maovu aliyomfanyia hu-ko nyuma.
“Carolina, ulionesha kuwa ni mgeni hapa mjini.
Imekuwaje umejuana na huyu.
Imekuwaje huyu ni kaka yako wakati maelezo yako ni wazi umetoka Bara, tena huyu ni..?”
“Sikiliza afande.
Mimi ni mfanyabiashara.
Huyu ni kaka yangu ambaye tuliishi naye huko Nzega. Isitoshe nimelelewa na familia yake hivyo ni kaka yan-gu. Sikutegemea kumwona wakati huu ingawaje kuna jambo alifanya nyumbani dhidi yangu.” Askari alidakia;
“Alifanya nini?”
“Alin..................! aliniacha!”
“Ulitaka kusema jambo. Alitaka kufanyaje?”
“Hapana. Aliondoka na kuahidi atarudi mapema hajarudi hadi leo.” Carolina alificha ukweli.
“Sasa, utamsaidiaje?”
“Nakusikiliza wewe, kwani unajua uzito wa jambo hili.”
“Hapana njia hapa.
Ni hadi upelelezi ukamilike ndio nitapata la kuongea.
Nataka kumwandalia hati ya mashitaka afikishwe maha-kamani.”
“Hatafungwa?”
“Hapana. Hawezi kufungwa kwa kosa hilo. Unachotaki-wa kufanya ni kumwekea mdhamana na baada ya hapo atakuwa nje hadi kesi yake itakapo malizika.”
“Naomba usimpeleke mahakamani.
Tulimalize hapa hapa, kwani hakuna jambo dogo maha-kamani. Likifika huko itakuwa usumbufu sana.”
“Kwa hiyo, unasemaje?”
“Kama kuna njia ya mkato naomba tuchague hiyo tum-saidie atateseka sana.”
“Nakusikiliza wewe.
Mimi sina pingamizi.
Hili jambo zito, inahitaji tufanye mchakato wa kuelewe-ka ingali mapema.”
“Sawa. Niambie unataka nini?”
“Una laki mbili hapo, tumalize mambo!”
“Ndugu yangu, laki mbili!”
“Ndiyo!
Pesa hiyo kidogo sana.
Hebu fanya ninachokuagiza.
Na kama tunakubaliana niwekee kwenye F-Pesa.
Namba yangu ya simu hii hapa.”
Alimtolea kadi ya namba ya simu na alimsisitiza. Caro-lina alitoka na alielekea palipo kibanda cha simu cha F-Pesa alifanya mchakato wa kuiingiza pesa hiyo na alifa-nikiwa. Huku mpelelezi wa polisi alirejea chumbani na kumkuta Tora akiwa na wasiwasi na ghafla alidakia;
“Amekwambiaje dada?
Ananitoa?”
“Tulia hapo.
Wasiwasi wa nini?
We subiri upate maelekezo!”
Punde ujumbe wa simu uliingia kwenye simu ya mpele-lezi huyo kumjulisha kuwa alipokea pesa shilingi laki mbili. Alifahamu kuwa ndizo pesa alizoomba kupewa na Carolina ili asimtayarishie Tora hati ya mashitaka na kumpeleka mahakamani. Aliandaa karatasi ya maelezo mafupi na punde aliingia Carolina. Askari alimtaka Tora kusaini na Carolina pia ili kuonesha uhalali wa utendekaji wa jambo hilo. Baadaye alimwelekeza Tora kwenda kuchukua vitu vyake na kusaini katika kitabu cha kumbukumbu ya vitu vya watuhumiwa. Carolina alitaka kuambatana na Tora wakati huo alisahau kilichomfikisha pale kituoni.
“Carolina, nakuhitaji ofisini uje.” Aliingia ofisini kwa mpelelezi na aliketi
“Swala la huyu jamaa aliyekupora, unasemaje?
Uko tayari twende mahamani?”
“Hapana, sina muda wa kupoteza kufatilia hilo.”
“Kwa hiyo?”
“Mfutie jalada aende zake.”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Gharama ya kufuta jalada unailipa wewe ama nani ata-lipa?”
“Acha alipe mwenyewe na ndugu zake.”
“Hatujui ndugu zake waliko.
Yeye yupo tayari kwenda mahakamani anavyoonekana. Kama haupo tayari kwenda mahakamani lipa hiyo gha-rama. Ni pesa kidogo tu shilingi elfu hamsini.”
“Basi nitakuwekea kwenye F-pesa.”
“Haya hakuna shida usiache.
Nakutakia muda mwema.”
“Haya asante.”
Wakati huo Carolina aliondoka na kuelekea alipomwa-cha Tora kasimama. Jinsi alivyochafuka na mwili wake kudhoofu alikaa juu ya jiwe akingojea. Alipomwona Carolina akimwelekea alinyanyuka. Wakati huo aliwaza jinsi gani angefanya ili Carolina aweze kumwamini na kumsamehe. Alipiga magoti na kuanza kuomba msama-ha;
“Nisamehe Caro.” Wakati huo Carolina hakuongea jam-bo zaidi ya kumtazama.
“Caro nisamehe.
Najua mimi nilikukosea sana lakini umenilipa fadhila. Nisamehe”
“Usijali Tora.
Naomba nyanyuka.
Hustahili kunipigia magoti mimi.
Najua mimi ni kijakazi wako, kama ilivyokuwa hapo awali. Nyanyuka naomba.”
“Asante Caro kwa kunitoa.
Nashukuru sana Mungu atakulipa.
Naomba unisamehe!”
“Nisha kusamehe kitambo.
Nafahamu maisha ni mzunguko na Mungu ndiye anajua kila jambo juu ya mwanadamu.
Nishakusamehe, nyanyuka”
Akiwa hayaamini maneno yaliyotoka kinywani mwa Carolina, Tora alinyanyuka na kumkumbatia kisha alilia sana. Hakika hakufahamu baadaye kuna nini. Hakujua Carolina kuwa alishakuwa shetani na bedui asiye mfano. Alifahamu kuwa Carolina bado alikuwa kijakazi mwenye shida na pesa. Swali alijiuliza, ni nini alikifanya Carolina hadi yeye aliruhusiwa kumtoa Korokoroni. Alijiuliza ni nini kilimfikisha Zanzibar Carolina wakati huo ama ni ndoto na si ukweli ulitokea hapo. Aliwaza cha kumfanyia kilicho chema hata hakupata. Hakika, alijipotezea muda wake wakati huo na alizidi kustaajabu ya firauni.
“Tora, dunia ni duara. Kumbuka mimi ni binadamu ka-ma binadamu wengine. Ninapaswa nikusamehe kwa yote. Wakati wote lazima ufahamu, ulitendalo leo kwa mwenzio laweza kukukuta kesho, hivyo jitayarishe. Ka-tika maisha yako jitahidi sana kumheshimu kila mtu. Haijalishi ni mtoto, mzee na hata kijana wala usijali jin-sia na hata tabaka atokalo mtu. Ni heri kuwa maskini wa mali, lakini uwe na moyo wa utu. Na wakati wote pesa isitumike kama fimbo ya kuonea wanyonge kwani pumzi sote hupewa pasipo ubaguzi. Naomba tekeleza hayo. Mimi nakupenda sana na ndio maana leo Mungu kapenda zaidi katukutanisha.”
“Asante Caro! Asante sana!”
“Unaelekea wapi sasa?” Carolina alihoji.
“Naishi Kiembe Samaki kwa Shangazi yangu na huko ndio naelekea. Naomba twende sote.”
“Hapana.
Siwezi kwenda huko nina mambo mengi ya kufanya.”
“Unaishi wapi na unafanya nini hapa visiwani?
Ulikuja lini?”
“Mbona maswali mengi Tora?
Tutaongea zaidi vuta subira.”
“Hapana Caro.
Twende kwa shangazi angalau akuone.
Umenisaidia sana.
Bila wewe sijui ingekuwaje.
Naomba twende!”
“Nimesema siwezi kwenda.
Nipe muda zaidi tutaenda tu.
Nafahamu hanijui na wala si nduguye iweje lazima anione. Naomba nenda kamtoe wasiwasi afahamu kuwa upo na si vinginevyo. Atakuwa anakutafuta sasa.”
“Nijulishe angalau basi unakokaa angalau nikutafute baadae nipafahamu.”
“Ninakoishi utapafahamu.
Chukua namba yangu ya simu utapajua.
Nakupenda usijali!’ aliongea kwa hadaa huku akitaba-samu. Tora alitabasamu na kisha aliafiki kwa furaha.
“Asante sana Caro!
Nakupenda sana ujue!”
“Usijali, tuko pamoja.” Tora alianza kuondoka. Hakuwa na chochote mfukoni wakati huo. Carolina alimtazama na kisha aliita;
“Tora!.... Tora!”
“Naam Caro!” Huku akiwa amesimama.
“Naomba urudi mara moja kuna kitu nimekumbuka.” Alirudi huku hofu imemkaa.
“Ndiyo Carolina! Nimerudi.” Carolina alimwangalia Tora kisha kutikisa kichwa.
“Utafika kwa miguu huko uendako?”
“Ndiyo! Nitafika tu Caro.
Sina jinsi yoyote ya kufanya hadi hapa.”
“Hapana! Naomba nikupatie nauli uwahi kufika.”
“Nitashukuru sana kwa hilo.”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Carolina alichomoa pesa na kumpatia. Alimpatia pesa taslimu shilingi laki moja na nusu kama matumizi yake. Tambaza lilimshika Tora kupokea noti kumi na tano za elfu kumi kumi toka kwa aliyekuwa kijakazi wa kulipwa elfu kumi kwa mwezi. Alishikwa tutwe pia kuwa mkimya akimkodolea macho Carolina.
“Asante Carolina!
Pesa hizi zote umenipa, wewe utabaki na nini?”
“Usijali Tora.
Najua mwenyewe, si juu yako kuhoji hilo.”
Caro alipanga kukaa Zanzibar kwa muda wa juma moja na aliona vema kama angeweza kuanzisha duka la jumla arudipo mjini Nzega. Alikata shauri kufanya biashara ya nguo za kike kwa wakubwa na watoto. Hakupenda ku-wahudumia wanaume katika biashara yake kwa jumla ya maisha yake.
Carolina alipanda gari na kurejea ilipo hoteli ya EI Fad-hili. Aliishi hapo siku hiyo akiwa na mawazo mengi. Alijaribu kutafakari yaliyomtokea siku hiyo na hakuamini kilichokuwa kikiendelea. Alifikiri Mungu alimfungulia njia ya kumpata Tora kwa njia hiyo. Tora alikuwa tayari kawasili nyumbani na alimsimulia shangazi yake yaliyokuwa yamempata ambapo alisikitika kwa kile kilichompata. Alimshukuru Carolina ingawaje hakuwahi kumtia machoni. Alimwomba Shangazi yake amsaidie simu ya mkononi kumjuza Carolina kuwa alifika salama.
“Hallo Caro!” Tora aliongea.
“Ndiyo!
Nani mwenzangu?”
“Tora anaongea!”
“Okay!
Habari za muda?”
“Nzuri sana. Nimefika salama.
Asante sana kwa msaada wako.
Shangazi yangu kafurahi sana na angependa kukuona.”
“Usijali Tora.
Muda upo wa kutosha usiwe na shaka wangu.
Tutapanga muda ukifika.”
“Asante sana!
Naomba kesho nijue unapokaa.
Ikiwezekana uje hapa umjue shangazi yangu.”
“Usijali, kesho nitakupa ramani na utafika.”
“Asante sana. Tena na tena asante!” Tora alikata simu na Carolina aliendelea na shughuli zake pale hotelini.
Iliwadia siku iliyoitwa kesho katika miadi yao. Tora alimwomba Shangazi yake ampatie simu ili awasiliane naye na kwenda kupafahamu mahali ambapo Carolina aliishi mjini Zanzibar. Alijiuliza maswali mengi sana wakati huo, je Caro kweli alimpenda na kamsamehe kwa dhati wakati huo ama alikuwa na kitu kingine rohoni kinamkereketa? Hakupata jawabu na aliiahidi nafsi yake kuwa mwanamke siku zote husahau mapema kila jambo, hivyo atakuwa kasamehe na kusahau. Carolina alimwelekeza na kumjuza alipatikana wapi na ndipo aliianza safari kuelekea hotelini. Nini kilitokea hapo?
Alipofika na kukiona chumba alimoishi Carolina, mshi-tuko ulimshika Tora. Alimtazama mkononi alikuwa na simu mbili ikiwemo aliyompora Mputa mutu ya Kongo. Akiwa kajilaza kitandani, Tora alimtazama kwa jicho la kuiba na tamaa zikimjaa kichwani.
Malaika watoa roho waliishawishi nafsi yake aende kwa Carolina kujivinjari. Siku hiyo haikuwa rahisi, alikuwa na mizunguko mingi hasa kuhusu maandalizi ya safari ya shangazi yake. Alihakikisha shangazi yake anaondoka kwenda Tanga hata kwa bei ya kuruka. Alifanikiwa kumsafirisha kesho yake na alielekea Tanga kwa mafanikio.
Moyoni mwake Carolina alijiita mshindi na alipanga kumpa zawadi Tora kwa alichokuwa amemtendea. Ilipo-pita siku hiyo, kesho yake haikuwa mbali. Tora aliwasili katika hoteli ya EL-Fadhili na moja kwa moja alielekea kilipo chumba cha Carolina.
“Caro! Caro! Tora alisikika akiita. Hapo alimwita Caro-lina ambaye alikuwa kachukuliwa na usingizi wa asubu-hi.
“Mh! Tora, umekuja tayari. La!
Kweli umebadilika sana siku hizi.”
“Kwani ilikuwaje hapo awali hadi useme nimebadilika?”
“Ulikuwa huzingatii muda, mvivu na wakati mwingine mwongo kuzidi kiasi.”
“Hapana Caro.
Ulikuwa ni utoto tu, lakini sasa nimekua.”
“Hata mimi naona umekua!
Lakini sijui kama akili pia imekua unaweza kuni.........! Tora alidakia kwa haraka.
“ Umeshaanza sasa Caro.
Tangu lini umekuwa mwongeaji kiasi hiki?”
“Ulinifundisha mwenyewe. Hukumbuki?”
“Nilikufundisha kufanya nini?
“Ulinifundisha ku.........!” Tora alimziba mdomo.
“Mbona unaniziba mdomo!
Acha niongee, kwani unamwogopa nani!
Una kimada hapa kama kawaida yako!”
“Hapana.
Najua utasema hivyo.
Nishaacha kitambo utoto huo.
Je naweza kujumuika nawe hapo?
“Ili iweje?”
“Iweje kwani?
Kwani unafanya nini?”
“Napumzika!
Kwani vipi?”
“Utaweza?”
“Nitaweza nini?”
“Kukaa kitandani!
Kwani unadhani kufanyaje?” Tora alicheka na kumsogelea Carolina. Hakuwa katika hali ya kujitambua na alilewa.
Siku hiyo Tora alifurahi sana. Alifurahi na kusahau yote wakati huo. Hakujua kama alifanya dhambi na adhabu yake aliipata papo hapo.
“Caro, nakupenda sana.
Naahidi nitakuoa mara moja.
Nakupenda sana.”
“Hayo maneno tu Tora!
Unaweza kunioa mtu kama mimi kijakazi, a house girl!”
“Usijali hayo.
Mapenzi ni kitu tofauti na vyote uvionavyo na kuvidha-ni. Neno, nakupenda ndilo sahihi zaidi, unaonaje?”
“Sawa, sikukatazi kunipenda.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mimi sikupendi Tora!
Nakuchukia sana!”
“Kwa nini hunipendi” Tora alihoji
“Hujui kwa nini sikupendi?
Sikupendi kwa sababu uli...............!
“Acha basi kunikumbusha ya zamani.
Yameshapita tusahau tugange yajayo.”
“Kidonda changu hakiwezi kupona.
Ulinitesa sana na unaendelea kunitesa hadi leo.
Mla muwa husikia utamuwe bali karaha hubaki kwa mtupa maganda. Wewe ushakula muwa na maganda nilitupa mie. Mwenyeshibe siku zote hamkumbuki mwenye njaa, basi ulishiba na kutosheka. Leo tena umekumbuka kuituliza njaa yako kama fadhila kwa wema wangu. Nimekutoa polisi kwa wema wangu na kwa gharama zangu. Leo hujanilipa fadhila zaidi yake umenilipa hisia iliyoyaumiza maisha yangu. Umenilipa fadhila ama unajilipa na kujipongeza kwa ujinga wangu?” Carolina alitokwa na machozi huku akizizima kwa uchungu.
“Usiongee hayo yote Carolina!
Nakupenda sana!
Unaiumiza nafsi yangu, hata nashindwa nisemeje.”
“Ni heri ushindwe kusema Tora.
Wewe ni fedhuli, bedui na baradhuli usiyemfano.
Iweje unifanye ulivyofanya na leo tena nimetenda wema na unanilipa makombo, huna haya?
We hayawani usiye haya.
Naomba nikome, nishapona ugonjwa huo.”
“Caro nakupenda!”
“Hunipendi!
Najua hunipendi!”
“Amini ninachosema.
Chochote utakacho nifanye, nitakifanya amini.”
“Chochote Tora utastahamili?
Nimeshasema chochote kuwa sikupendi, sikutaki inga-waje unaonesha kunipenda. Familia yako imenifanyia mengi maovu. Imeniandalia kaburi tangu alfajiri hadi kiama. Wewe ulianza unyama huo, baba yako kauende-leza na wengine wengi kuustawisha tena leo umeufufua ulikuwa umekufa. Sina furaha, nina simanzi maishani.”
“Baba yangu! Nini?” Tora alihoji kwa mshangao.
“Nafahamu umesikia.
Sijui mwisho wangu utakuwa lini ingawaje nahisi muda si mwingi nitatoweka ulimwenguni.”
“Kwa nini unasema hivyo?
Kuna tatizo kwani?”
“Kama kweli unanipenda, nitafahamu leo.
Je, ukinikuta nateseka njiani utanisaidia?”
“Ndiyo Caro, ntakusaidia.”
“Je, nikiwa mzima mwenye furaha si utafurahi?”
“Ndiyo!
Lazima nifurahi kwani nakupenda.”
“Je ukiambiwa naugua nimelazwa na nakaribia kukata roho utafanyaje?”
“Nitakuja kukuona na kukusaidia.”
“Utanisaidiaje Tora?”
“Kwa njia yoyote ile usitoe uhai wako.”
“Naomba niulize, ikitokea nikapatwa na ugonjwa wa kunitoa duniani na ukaambiwa tukiugawana tutaishi utaafiki?
“Kama hauui kwa muda nitakubali.
Lakini.......!”
“Lakini nini?”
“Basi tu! Nakupenda!”
“Utajua ukweli baadae.
Unionavyo si dhahabu.
Najua ni asili yenu wengi wenu.
Tora nakukaribisha sana katika maisha yangu ya huzuni. Sina msaada wa dhati, baba alizaa akakulea na akanilea nami lakini ndiye chanzo cha haya.”
“Carolina, una nini wewe?”
“Subira yavuta heri, mara zote mvumilivu hula mbivu lakini haraka haraka huzaa karaha na asiye mvumilivu uozo huwa halali yake. Tora siku nyingi zimepita pasipo kufahamu ukweli wa yote. Mimi ni m.................! Caro-lina aliangua kilio na Tora aliingiwa kiwewe cha kutaka kujua.
“Caro, nini?
Ongea basi nijue una maana gani?”
“Amini Tora ninayosema.
Sikupendi na hata sitakaa nikupende.
Mimi nishakufa siku nyingi ingawaje kivuli changu ndi-cho kinaishi.
Baba yako..... Baba!...! Carolina aligugumia.
“Ushakufa!
.........Baba yangu!.........
Sikuelewi.”
“Utaelewa Tora.
Mimi ni ......! alilia kwa uchungu.
Mimi ni mwathirika Tora.
Baba yako ali....................!
Kilio kilimkaba Carolina na aligumia kwa kwikwi iliyomnyang’anya pumzi yake. Tora aliposikia hayo ali-shikwa na tambaza akashindwa hata kuongea. Jasho jembamba lilimtoka kisha alitoka pasipo kuongea jambo na kuanza kukimbia akielekea mjini kati huku akili si yake tena.
Kweli Tora aliingia kikaangoni kwenye mafuta ya moto yaliyomkausha na kumuunguza kabisa.
Pasipo kuendelea na hofu, Carolina alifanya ununuzi wa bidhaa alizokuwa amekusudia kununua kwa ajili ya biashara yake aliyoipanga. Akiwa ameambukizwa virusi, Tora hakuweza kuyazuia machozi yake kumdondoka kila wakati pale Carolina alipomjia akilini mwake. Aliwaza na kuwazua wakati huo pengine angeenda kulipa kisasi kwa kumnyonga na amkatishe maisha yake. Alitapatapa pasipo hoja ya msingi, hakujua atafanyaje wakati huo kwani kitumbua kiliingiwa mchanga. Alikata shauri kwenda kumtoa uhai Carolina kesho yake kwa kuandaa mazingira ya kuonesha alimpenda. Hakujua dhamira yake kama ingefanikiwa ama ingegonga mwamba. Kilimtokea nini hapo?
Kesho yake asubuhi na mapema, Carolina aliianza safari yake kurejea Nzega. Hakuweza kukwama popote wakati akimwacha Tora akiendelea kusambaza vimelea hivyo ndani ya kisiwa cha Zanzibar. Kwa kuwa maisha hubadilika, je Carolina aliishije baada ya kurudi katika mji wa Nzega? Je Tora aliwaza nini wakati huo wa matatizo?
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kiama
HAKUNA KIUMBE AFAHAMUYE kiama kitakuwa lini. Wakati wote kila mmoja hutoa mtazamo wake kuhusu wazo hilo. Kama ilivyo ada, dunia haina mtu ambaye anayo lazima yoyote juu yake kuwa bora au duni. Awe mkumbukwa au msahauliwa, mashuhuri au vingine katika ulimwengu pasipo hiari yake yeye kutaka kuwa hivyo. Kwa kweli hali iwavyo tajiri, jamali au vingi-nevyo, hata kama ni Rais, anayo lazima ya kujitafutia na pia kupata riziki katika muda wote wa maisha yake. Lakini tu iwe kwa nja halali.
Ilikuwa hivyo pia kwa Carolina. Kama kiungo kilicho bora katika mchanganyiko wa chakula na vyote vili-wavyo kwa viungo duniani, chumvi ilikuwa ni lazima kupata. Hivi ndivyo maisha ya mrembo huyu yalivyo-kuwa. Hii ilifanana na juhudi zake za lazima kutafuta maisha ambayo yangempendeza yeye mwenyewe na kumfanyia heshima mbele za watu wengine. Aliishi kwa kadri ya mazingira yalivyo mkabili na utashi wa moyo wake ulivyomwagiza.
Kitendawili kilichokuwa kigumu huteguliwa na mtegaji mwenyewe. Hii haina maana kuwa aliyetegewa ali-shindwa kupata jawabu, lakini ni kutokana na mtazamo wa mawazo na desturi ya kukariri mfumo fulani wa ku-jibu. Hivyo ndivyo hasa ilionekana fikra yake Carolina. Aliamini kuwa, moja mara moja jibu lake ni moja na kwa nini moja na moja iwe mbili wakati mwonekano sehemu zote ni sawa. Na pengine ingewezekana kuwa moja na moja hufanya kumi na moja badala ya mbili. Falsafa yake ilimruhusu kwa yeyote kujibu atakavyo kadri ya wakati, uelewa pamoja na mazingira yake. Mfano, yeye alipoulizwa mtaka cha uvunguni... mara zote alijibu... sharti abinue kitanda na si lazima kuinama. Wakati wote pia alipenda kujibu alipoulizwa... mchelea mwanakulia, “hushikwa na huruma” na si hulia yeye kama alivyowahi kujibu. Wakati akiwa shule ya msingi aliwahi kujibu kuwa “zimwi likujualo hukatisha maisha mara moja.” Hakuwahi kuafiki wakati huo kuwa zimwi likujualo halikuli likakwisha.
Kwa kuwa maisha ni kitendawili kikubwa kisicho na mteguaji kama vile Carolina, hakutaka kuwa mtumwa wa mawazo ya waliomtangulia. Aliona vema kuyaanza maisha ya kuishi kama mfanyabiashara. Wakati huo ali-fahamu nini kingemkabili hapo baadae kama si mauti. Alifahamu dunia ni moja ya njia ya kupita ili kutekeleza maagano ya Muumba. Shida ni sehemu ya maisha na ugonjwa aliokuwa nao ni mpango wa Mungu aliyeamua kuwafundisha wanadamu ubaya wa zinaa.
Carolina hakujua lolote kuhusu biashara wakati huo. Alijipa moyo kuwa jembe halimtupi mkulima na hata biashara haigombi. Biashara yake ilimpatia matumaini ya kuishi wakati akisubiri hatima ya maisha yake hasa akingojea siku ya kifo chake.
Thamani ya mtu wakati huo kutokana na mtazamo wa Carolina ilitokana na jinsi yeye alivyoweza kujitegemeza mwenyewe. Aliamini kuwa kijakazi yeyote ambaye humtegemea bwanake aliyemwajiri, maisha yake wakati wote ni ya mashaka na hana uamuzi pia uhuru wa fikra zake. Wakati akiyawaza hayo, alibubujikwa na machozi akiziangalia mbingu huku kainua mikono yake juu akiashiria kuomba jaha iliyopotea duniani. Aligundua na kufahamu kuwa ulimwengu ulikuwa na thamani lakini wakazi wake walikuwa wametokwa na utukufu na kuishi kama mapepo wasio na matarajio.
Katika jumla ya maisha yake, Carolina alijaliwa kumiliki duka lenye thamani kubwa. Alijipatia watu wengi wa kumuunga mkono katika biashara yake, si wake, waume, vigoli na hata watu wa mataifa mbalimbali waliofika hapo walilazimika kufika dukani kwake kujipatia mavazi na mahitaji muhimu.
Hakuwahi wala kuwaza juu ya kuuza nguo za kiume kama ishara ya kutotamani kukaa na wanaume karibu naye. Kweli mabadiliko katika maisha humbadilisha mtu pengine kumpandisha kwenye kilele cha sifa kama si kumteremsha na kumzika katika kaburi la sahau. Kwake yeye alikwea kilele cha sifa na alijikusanyia marafiki wengi ambao walivutwa na utajiri wake.
Kweli mikono mitupu hailambwi, shoga yake Carolina aliyeitwa Tasira ambaye awali alifanya naye kazi katika nyumba ya kulala wageni, alikuwa ni binadamu wa kwanza kuvutwa na umaarufu wa Carolina. Hakuna wa-kati huu aliyefahamu kuwa Carolina aliathirika zaidi ya daktari aliyempima, Pachoto hawara aliyemkimbia na pengine Mzee Miembe. Kwa alivyobadilika wasifu wake, hakuna yeyote aliyeweza kunyanyua kinywa chake kumteta wala kunena lolote kuhusu yeye. Na hata kama mtu angesema kuhusu kuathirika kwa Carolina, yeye kwanza ndo angeonekana mgonjwa na si Carolina. Vipimo vya macho vilitosha kuwahakikishia wanaume kuwa Carolina ni mrembo asiye na mfano.
Kama ilivyo, cheo ni dhamana, hakika usidharau mwenye shida ukadhani hatapata tunu asilani. Tasira hasa ndiye alikuwa rafiki wa mashaka kwa Carolina. Kwa jinsi walivyokutana, Carolina hakumtupa na alimsikiliza sana wakati huo. Alikuwa hajui mlango wa kanisa wala msikiti katika jumla ya maisha yake zaidi ya kufahamu makazi ya waganga wa kienyeji alioamini ndio haswa walimsafishia nyota yake na kumfanya mwenye bahati.
Ukweli wa elimu katika chochote ni jambo la msingi, na pesa bila daftari hutumika bila habari. Baada ya mwaka mmoja katika biashara yake, Carolina hakuwahi kuhi-fadhi pesa yoyote benki na wala hakuwa na kumbukum-bu yoyote ya mapato na matumizi. Alichofahamu alitu-mia pesa kadri ya uwezo wake na akili yake ilivyomtu-ma pamoja na kuwahonga wanaume wakati huo.
Haikumchukua muda Carolina kufilisika na ilistahili afunge duka lake. Kwa kuwa alikuwa na roho ya paka alijikaza kisabuni akimtafuta mchawi wake ni nani. Tasira rafiki yake alimfanya aujue ukweli wa kufilisika kwake;
“Carolina, binadamu wanakijicho sana!
Wamekuroga tayari!
“Kwa lipi Tasira?”
“Huoni kinachoendelea sasa.
Tangu utoke Zanzibar umekuwa na mafanikio lukuki. Leo je, mali ziko wapi?”
“Hata mimi sijui kimetokea nini.
Inawezekana kweli ikawa hivyo.”
“Sasa una mpango gani kunusuru hili?”
“Kwa kuwa watu wenye hila wamefanya dawa ili kuha-misha utajiri wako. Watu hawapendi kuona mwanamke akimiliki utajiri wakati wao wanateseka. Na je ulishawahi kuota ndoto yoyote ihusuyo pesa.”
“Mara nyingi sana, nimekuwa nikiota hivyo.”
“Unaona, tayari wamekuroga. Changamka sasa kila kitu kitaharibika na isitoshe bado hawajakumaliza kabisa.”
Akiwa amemshawishi Carolina hadi kuunyosha moyo wake, alimshauri kwenda kwa Mgonezi. Alikuwa ni mtu ambaye Tasira alimtumia kutafsiri ndoto za bahati yake. Isitoshe angepatiwa dawa itakayomfanya arudishe mali zake zote
Kweli mwenyenacho huongezewa na mwenye kidogo hunyang’anywa chote. Alipofika kwa mganga huyo Mgonezi, Carolina alielezwa kuwa kuna wachawi hu-chukua utajiri wake hivyo alistahili kufanyiwa zindiko ili angalau arudishe utajiri wake. Kwa kuwa walimfahamu sana Tasira, Mganga huyo alikutana na Tasira kabla ya kwenda na Carolina. Siri zote kumhusu Carolina alizifahamu, kilichotokea wakati akielezwa ndoto yake kilikuwa ni jambo lisilotabirika.
Wakati wanaingia nyumbani kwa mganga huyo, walisi-kia sauti ikitokea kwenye mtungi palipo simbi za mgonezi mpiga ramli. Sauti iliyotoka ilisema;
“Chausiku, hatupendi waungwana uitwe Caroli-na,.Unaiacha bahati yako.
Wewe ni binti mwenye bahati kubwa sana.
Mafanikio lukuki duniani. Ulipata bahati kubwa na ma-fanikio lukuki duniani, hasa kule ulikokuwa na kujitajirisha. Jina lako limekupotezea bahati pamoja na utajiri mkubwa. Karibu sana ! ................... (sauti iliendelea) Waungwana tayari wameijua shida yako. Una majonzi na masikitiko tangu kuzaliwa kwako. Yote hiyo ni mizimu yako ilikasirika baada ya familia yako kutotii agizo la Milembe ndiyo maana unapata misukosuko ya kila namna. Kwa sasa, hatutakudai pesa yoyote, lakini tunaomba fanya tutakayokuagiza kufanya, hapo utafanikiwa......... UMESIKIAAA!
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
(Iliendelea tena )... mtoto wetu atakupatia dawa nyeusi na nyeupe kama ishara ya kutakasa nyota yako. Baada ya hapo kesho nenda benki yoyote nchini utapata pesa ya mkopo na dhamana yako itakuwa duka lako. Utayaona mafanikio ukiagiza bidhaa. Utatakiwa kuleta pesa yote kwa waungwana mara utokapo benki na tutakupatia masharti ya kuzitumia pesa hizo. Ahsante, tekeleza hayo !
Akiwa hafahamu ukweli kuhusu hili wala lile, Carolina alihisi matatizo yake yamepata mtatuzi. Aliitikia hata pasipo kuhoji kuwa aliafiki. Waliondoka na Tasira kure-jea kule alikokuwa amepanga maeneo ya Uzunguni hapo mjini Nzega. Hakuchelea kwenda kumwona meneja wa benki ili kuchukua fomu za kuombea mikopo. Alitimiza sharti la dhamana na kesho yake asubuhi kabla ya saa tano alipata pesa ya mkopo kutoka benki. Alipata shilingi milioni mbili taslimu.
Hakika jambo usilolijua ni kama usiku wa giza. Carolina hakufahamu janja iliyotumika kwa kuwa nyumba aliyoishi mganga huyo tapeli bwana Kamugamu ilikuwa na vyumba viwili mbali na sebule. Chumba kimoja kilikuwa ni sehemu alipojificha yule aliyetoa sauti. Ukuta ulitobolewa na kupitisha bomba lililo fungwa waya ndani yake na kipaza sauti. Pale tu alipoongea toka upande huo sauti ilitokea kwenye mtungi upande walikokuwa wameketi Carolina, mganga pamoja na Tasira.
Wakati akienda kwa Kamugamu, sharti la kwanza lili-kuwa atoe noti moja ya shilingi elfu kumi ichomwe moto katika chungu cha dawa ili yapatikane majivu yaliyochanganywa dawa itakayotumiwa kumchanja Carolina. Aliambiwa kuwa, atawekewa pia dawa sehemu za utupu wake na mtaalamu Kamugamu. Alijulishwa kuwa nuksi yake mbali na mizimu ilitokana na mwanamume wake wa kwanza kukutana naye. Alitoa rai hiyo kwani alifahamu kuwa Carolina alibakwa. Hapakuwa na pingamizi lolote kwani Carolina aliafiki na kumruhusu Kamugamu afanye alivyoweza. Kiu cha Kamugamu kwa kumtamani Carolina kilimfanya afanye kinyume na matakwa yake. Alijua kuwa ndege mjanja hunasa kwenye tundu bovu. Alitimiza lengo lake lililomuita katika kundi la marehemu aliyehai baada ya kuvunga anamtakasa.
Wakati amebakia na shilingi milioni moja na sehemu, alipewa masharti atakayoyatekeleza ili kupata bahati yake. Kwa pesa alizozipata ilibidi atoe shilingi laki saba aende nazo mjini ili kujinunulia nguo za kuvaa awapo dukani kwake. Alipaswa anunue kila kitu cheusi, mion-goni mwa alivyonunua ni hijabu nyeusi, mtandio, Soksi, viatu, shanga, saa, miwani, cheni, kidani pamoja na he-reni; vyote vilikuwa vyeusi.
Baada ya kununua vitu hivyo alipaswa pesa alizobakiza azipeleke kama malipo ya zindiko la bahati kwa mgan-ga. Pesa aliyokuwa amebakiza wakati ule ndiyo ilistahili anunulie bidhaa chache kwenye maduka ya watu mbalimbali. Alishauriwa kila duka anunue nguo mbili na alitakiwa azipange dukani kwake. Kwa kufanya hivyo kungemfanya yeye akusanye bahati za wote alionunua nguo kwao na bahati yote itamhamia yeye. Alitakiwa pia, mara afanyapo mauzo ya siku ya kwanza, zile pesa ampelekee Kamugamu kama shukrani ndipo aendelee na biashara yake. Angepata mafanikio lukuki kama yalivyokuwa maneno ya Kamugamu kama angefata masharti aliyotakiwa kuyaabudu.
Maagizo yote aliyatekeleza kama alivyoagizwa. Kweli hakuwa na hili wala lile kuhusu uongo wa Kamugamu. Alitumia shilingi laki moja pekee katika shughuli zake za mavazi, wakati akiwa amebakiza shilingi laki sita Carolina alimkabidhi pesa yote tapeli wake. Alipatiwa dawa aliyoahidiwa ili kuendelea na biashara yake. Ka-mugamu alimwamuru kuwa waungwana walitaka aka-fungue duka saa tano asubuhi na si saa moja na awe amevalia mavazi yake na kuoga dawa ile aliyoelekezwa. Alishauriwa kuwa wakati anaoga achanganye kwenye maji vuguvugu, aliahidiwa kupata bahati ambayo hata-kaa asahau milele.
Kwa hila aliyoitumia Kamugamu, aliwatafuta watu alio-shiriki nao kufanya utapeli huo. Aliwagawia kiasi chote cha fedha alichopatiwa na Carolina ili waende kununua nguo pale dukani kwake. Kila mmoja alienda kwa waka-ti wake. Wote walifanya hivyo na mauzo ya Carolina ya siku ile yalikuwa laki saba na aliongeza elfu hamsini iliyokuwa imeuzwa jana yake na zote alizibeba kumpe-lekea mganga wake.
Wakati Kamugamu alipata fedha sawa na thamani ya nguo alizonunua, maisha yake yalizidi kustawi. Fumbo mfumbie mjinga kama Carolina mwerevu angeng’amua. Tofauti na alivyoahidiwa na mganga wake, mauzo ya dukani kwa Carolina yalizidi kushuka siku hadi siku. Alikuwa hata hafikishi shilingi laki moja kwa kutwa. Aliingiwa na wasiwasi na alikosa hamu. Wakati huohuo watu wengi waliompita dukani kwake walimshangaa kuvalia kwake mavazi meusi kila mara. Wakati huo pia alishindwa kumfuata Kamugamu. Wakati alipokata shauri kumwendea alimjulisha pengine alikosea masharti akachanganya na pesa alizokuwa ameuza jana yake jambo ambalo alilifanya. Kwa hilo aliamini ni kweli na aliishia kushusha pumzi.
Ilimchukua miezi mitatu zaidi pasipo kurejesha riba benki alikokopa pesa za kufungulia duka. Hali hiyo iliendelea akiwa hana pesa kabisa. Kwa kuwa wanaume mara hii walifahamu kuwa Carolina hakuwa na kitu, walitumia mwanya huo kutaka kujineemesha naye. Hakika haikuwa neema zaidi ya kuukwaa moto wa kifuu. Benki ilitaka kumfilisi na hapakuwa na chochote cha kuchukua, kwani hata mwenye nyumba alikopanga maeneo ya Uzunguni aliamua kumfurusha wakati aliposhindwa kulipa kodi ya nyumba.
Wasaa huo wa kuteseka baada ya kufilisika kwa Caroli-na, kulipokelewa kwa shangwe na baba mmoja ambaye ni mfanya biashara katika mji huo wa Nzega. Bwana Fursad Mgemo ndiye aliamua kumnusuru Carolina. Akijisemea rohoni kwake kuwa kuvuja kwa pakacha nafuu ya mchukuzi, aliamua kulilipa deni lote alilodaiwa Carolina kule benki;
“Carolina, wewe ni binti mrembo.
Hustahili kupata tabu na sisi tupo.
Naomba ukubaliane nami kuwa mke wangu.
Nitakutafutia nyumba ya kuishi katika mji huu.
Nitalipa gharama zote kwa mwaka mzima.”
“Sina pingamizi na hilo.
Naomba kama kweli utakuwa na wazo la dhati kunisai-dia utafanya hivyo.” Carolina aliomba.
Akiwa ameitelekeza ndoa yake na familia ya watoto wa-tatu, Fursad Mgemo hakufahamu kama Carolina aliishi na virusi. Naye Carolina hakutaka kufanya chochote zaidi ya kuangalia televisheni na kuandaa chakula pengine kumliwaza Fursad. Wakati Fursad akiwa safarini kibiashara sehemu mbalimbali nchini na hata nje ya nchi, huku nyuma majirani waliomzunguka walimnyemelea na hakusita kuwapatia walichokihitaji bila shaka yoyote. Ilikuwa juu yao kung’amua. Kwa tabia zao za kudoweana wake, wakazi wa mtaa huo walichukua siku chache sana kuingiwa na maradhi yaliyowahakikishia tiketi ya kuwatwaa safari yao ya mwisho katika uso wa dunia.
Watu wengi walimdowea Carolina. Achilia mbali made-reva, wakatisha tiketi na wafanyabiashara pia watumishi wengi wa kada mbalimbali serikalini walimnyemelea mama Fursad na kuufuata msiba uliowashinda kuuhimi-li. Kwa kuwa siku za mwizi ni arobaini, pia penye moshi pana moto, siku ilifika ambayo Fursad hawezi kuisahau maishani mwake. Ilikuwa ni siku ile Fursad alishikwa na homa kali iliyomfanya apatiwe kitanda hospitalini ambako pia aliwahi kulazwa Carolina akiwa na Pachoto. Wakati huo alikuwa amekaa hospitalini zaidi ya siku nne. Alikuwa akihudumiwa na daktari tofauti na aliyemhudumia Carolina wakati huo. Daktari wa awali alikuwa hajarudi toka safarini huko Kilimanjaro alikokuwa ameenda kimasomo.
Siku ya tano ndiyo ilimfanya Fursad kushtuka na kuujua ukweli wa mambo. Ilikuwa ni siku ya kuufahamu ukwe-li, ni siku ambayo chozi adimu ya jaha ilimtoka machoni kwake kwa kuufahamu ukweli. Pachoto na Carolina wote kwa pamoja walikutana kila mmoja na kiambata wake. Pachoto alimpeleka mkewe hospitalini hapo wakati Carolina alimpeleka mumewe na wote wakiwa waathirika na Carolina ndiye aliyewaazimisha tatizo hilo.
Daktari alikuwa amechukua vipimo vya Fursad na mke wa Pachoto vyote kwa pamoja na alivishughulikia. Ilihi-taji Pachoto na Carolina kumwona daktari kuwapatia ukweli kuhusu afya za wagonjwa wao. Kwa kuwa Pa-choto alitoka kidogo wakati huo, saa aliyorejea hakufa-hamu kama kumejiri chochote wodini. Carolina alitangulia kwenda kumwona daktari ambapo Pachoto alipofika tu mkewe alimjulisha kuhusu wito wa daktari na mara moja alielekea palipo ofisi hiyo. Mambo yalianza kuharibikia hapo.
Walipokutanisha macho yao mule kwa daktari, Pachoto hakuwa na neno; hata Carolina alibaki akibubujikwa na chozi akimhurumia Pachoto pamoja na familia yake. Alipotaja nambari ya mgojwa wa Pachoto Carolina ali-shituka na alifahamu fika kuwa dada huyo tayari aliathirika. Vile vile Pachoto alifahamu kuwa Fursad naye alikuwa mwathirika lakini hakufahamu nani alimwambukiza. Pachoto alishikwa hasira na kumkaba Carolina shingoni jambo lililofanya kutokea vurumai pale hospitalini.
Kila mmoja hakufahamu kilichotokea. Alipochoropoka toka mikononi mwa Pachoto, Carolina aliondoka zake na kutokomea kule ambako ni kitendawili. Hakumwaga mtu wakati huo zaidi ya kuacha maswali mengi yasiyojibiwa. Hakuna yule ajuaye kule ambako Carolina alielekea alipoona mambo yamefikia kikomo hasa kuogopa kuumbuka.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Daktari aliwaeleza wagonjwa lililowasibu na kisha ali-wapatia ushauri nasaha. Alisisitiza kuwa kila mmoja ilimpasa kuchukua hadhari kwani hawafahamu hatima ya maisha ya dunia hii. Pia kuugua ugonjwa uliowakabili ni jambo la kibinadamu. Yampasa kila aliyehai kuwa mwaminifu dhidi ya mwenzi wake. Ngao ya mwisho ni kuiomba serikali na watu wake kuandaa misingi bora ya sheria na mifumo sahihi ya ajira ili kuweza kulinda maadili na ustawi wa taifa. Kwani, nini chanzo cha ukimwi kama maisha kwa wote hayashawishi makengeza ya uovu kwa kupoza machungu na makali ya maisha yetu?
TAMATI
0 comments:
Post a Comment