Simulizi : Jestina
Sehemu Ya Tatu (3)
Asubuhi ilifika na Alwin alikuja kuchukuliwa na profesa na safari ya kuelekea kwao ilianza, wazazi wake hawakuamini kama mtoto wao kapona hasa baba ake na kujikuta akimtwanga swali "miliioni saba laki sita hamsini na tano elfu mia mbili thalathini na moja gawa kwa mbili, jibu lake ngapi". "milioni tatu laki nane ishirini na saba elfu mia sita na kumi na tano" alijibu Alwin bila kusita na profesa akathibitisha jibu hilo. Kwa mara nyingine tena ndani ya miaka kumi furaha ilirejea ndani ya nyumba ya Mr Kelvin kwa kumpata mwanae Alwin. Machozi yaliwatoka wanafamilia hao huku wakikumbatiana kwa furaha iliopitiliza.
Asubuhi ilifika na kila mtu aliingia katika mishemishe zake, "oyaa Frank bado hajaamka" Jay aliuliza. "nahisi atakuwa bado maana jana nahisi kanywa nyingi sana" James alijibu, "nenda kamcheki basi" Jay aliongea na James aliondoka kuelekea chumba alicholala Frank. Baada dakika mbili James alirudi mbio huku akihema kwa nguvu, "oyaa nini wewe" Jay aliuliza. "Frank... Fra...nk" alijibu huku machozi yakimtoka, Ilibidi Jay na wengine wakimbie kuelekea chumba alicholala Frank. Wote walipigwa na butwaa baada kukuta damu zikiwa zimetapakaa chumba kizima huku mwili wa Frank ukiwa hautamaniki hata kuangalia. Jay alitoa simu na kuripoti polisi, haukupita muda gari ya polisi ilifika pamoja na gari ya kubebea wagonjwa. Mwili wa Frank ulitiwa kwenye gari na kupelekwa hospitali kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Inspecta Hans ndie aliekabidhiwa kesi hiyo, "habari yako kijana mimi naitwa Inspecta Hans na ndie ninae shughulikia kesi hii" alimwambia Jay ambae alionekana kuchanganyikiwa "hebu nieleze kila kitu bila kunificha". "ukweli inspector Frank alikuja jana usiku akiwa na majeraha kadhaa kichwani huku akipiga kelele kuwa amemuona Jestina". "Lakini Jestina si ameshakufa muda mrefu sasa" aliongea Inspector Hans lakini lengo lake ilikuwa ni kujaribu kutafuta ukweli kwa sababu kesi ya Jestina aliifungua tena. "mimi simjui Jestina ndio nani" alijibu kwa kitete huku akiangalia chini. "asante kwa ushirikiano wako nikikuhitaji tena nitakutafuta" aliongea inspector Hans na kuinuka kisha akamfata James ambae alikuwa kafunikwa shuka na mkononi akiwa na kikombe cha kahawa..CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"habari yako kijana naitwa Inspecta Hans" alijitambulisha, "mimi naitwa James na ni rafiki mkubwa wa Frank", "Ok James naomba unieleze tukio lilitokea jana". Na yeye alieleza kama alivyoeleza Jay na pia alipoulizwa kuhusu Jestina alisema vile vile na waliobaki wote walisema vile vile.
Baada kumaliza kuwahoji alirudi kituoni kwa ajili ya kuendelea na harakati nyingine, lakini wazo lilimjia aende kwa Alwin huenda angepata pa kuanzia. Bila kuchelewa alitoka na kuelekea kwa Mr Kelvin. "habari za saa hizi mzee wangu na samahani kwa usumbufu, kwa jina naitwa inspecta Hans nina maswali mawili matatu kwa ajili ya Alwin" alijitambulisha na kueleza shida yake. Mr Kelvin ni muelewa sana alijua hilo litakuwa ni swala la usalama hivyo alimwita Alwin na kumwambia nia ya inspecta. "karibu inspecta na jiskie huru kuniuliza chochote na nakuahidi nitakupa ushirikiano" alieleza Alwin na kukaa kwenye kiti. "sawa kijana, nimekuja hapa kwa jambo moja tu. Profesa Alexander Harison alinipa kazi ya kufatilia kesi ya Jestina lakin kazi hii siwezi kuifanikisha bila msaada wako na najua ntakuwa nimekutonesha kidonda lakini naomba unisamehe kwa sababu nimesubiri kwa muda wote uliokuwa huko sawa" aliongea Inspecta.
"hapana Inspecta hujatonehsa kidonda, yaliopita yashapita tugange yajayo" alijibu Alwin huku akitabasamu. Kwa mtu wa kawaida angeweza kusema yuko sawa lakini kwa mtu wa mafunzo kama Inspecta Hans tabasamu hilo lilitafsiri mambo mawili moja lilikuwa ni chuki na pili kisasi. "sawa, sasa jana kumetokea kifo cha kijana mmoja anaeitwa Frank, nadhani unamjua". "ndio namfahamu vizuri", "ok, mpaka sasa kifo chake ni cha utata huku wenzake wakidai kuwa kimesababishwa na Jestina" aliongea. Alwin alitabasamu kidogo "unajua inspecta damu ya mtu haipotei bure, na huo ni mwanzo tu wamebakia kumi na tisa na leo usiku atakufa mwengine" alijibu Alwin huku machozi yakimtoka. "sasa anaefaanya mauaji haya ni nani" aliuliza inspector, "Jestina" Alijibu Alwin na kuachia tabasamu kubwa. Inspector akaona hakuna haja ya kuendelea kuuliza maswali , aliaga na kuondoka.
Hofu ilianza kutawala katika mioyo ya wale walioshiriki katika kifo cha Jestina kwa njia moja ama nyingine. Mazishi ya Frank yalifanyika huku wengi waliomjua walikwenda akiwemo Alwin ambae alioneka kutokuwa na huzuni kabisa. Baada ya kumaliza watu walianza kutawanyika, ila wakati Alwin anaondoka alishikwa bega na alipogeuka "Alwin unanikumbuka" aliuliza inspector Hans. "samahani mbona sijawahi kukuona" alijibu na kumfanya inspecta ashangae kidogo, "leo asubuhi nilikuja kwenu na tukaongea mambo fulani kuhusiana na kifo cha Jestina" alifafanua labda alihisi huenda akawa amesahau lakini bado Alwin alishikilia kuwa hamjui na kuomba aondoke zake. Inspecta alimruhusu huku akiwa na maswali mengi sana kichwani ambayo yalikosa majibu "ikiwa huyu yule sie Alwin sasa atakua nani" alijiuliza mwenyewe. Kwa mchana huo hali ilikuwa shwari kabisa, usiku ulianza kuingia na kila mtu akawa anamalizia biashara zake ili arudi nyumbani kwa ajili ya mapumziko.
Sara ni miongoni mwa watu waliokuwa wakimalizia shughuli zao, "Sara kwa heri tutaonana kesho" Bety alimuaga huku akitoka katika chumba cha kubadilishia nguo na kuondoka. Ghafla hali ya hewa ilianza kubadilika humo ndani, Sara alihisi kama kuna mtu mwengine humo ndani. "Sara....sara" alisikia sauti ikimuita lakini mtu hakumuona, alifunga kabati lake ambalo lilikuwa na kioo mbele. Alipoangalia vizuri aliona kuna mtu amesimama nyuma yake lakini alipogeuka hakumuona, sasa wasiwasi ulianza kumuingia moyoni. Mara akaanza kusikia vicheko na vilio, woga ulimpata na kuanza kukimbia kuelekea mlango wa kutokea lakini ghafla taa zikazimika na kumfanya ajikwae na kuanguka chini kama mzigo. "sara....sara.....sara" alisikia tena sauti ikimwita, "we nani" aliuliza kwa sauti ya kilio. "mimi ni kifo chako" alijibiwa na kuzidi kutetemeka, Sara alinyanyuka kutoka chini na alipogeuka aelekee mlangoni ndipo akamuona mwanamke amesimama mbele ake.
"wewe ni nani" aliuliza huku akiokota mbao pembeni, "leo hunijui si ndio" alijibiwa na kwa mbali sauti hio ikagonga kwenye ngoma za masikio yake. "lakini usijali nitakwambia" alijibiwa na ghafla akapotea na kutokea nyuma yake, "geuka" aliambiwa Sara na kuanza kugeuka taratibu na macho yake yakatuwa usoni mwa Jestina na hapo ndipo akamtambua lakini kabla hajafanya kitu alichezea kibao kizito na kuanguka chini "nisamehe Jestina" aliomba sara. "wewe hukunionea huruma na kuamua kuniziba mdomo si ndio" Jestina alijibu huku machozi ya damu yakimtoka. "sasa nataka nikuonyeshe maumivu niliyoyapata siku ile" aliendelea kuongea na ghafla Sara akawa hatoi sauti kwa sababu mdomo wake ulizibwa na kitu kama kipande cha nyama iliyooza. Kutokana na harufu kali ya kipande hicho Sara alianza kuhisi kutapika lakini matapishi hayakutoka kabisa, hali ilizidi kuwa mbaya huku yakianza kutokea puani na kumfanya akose pumzi. Jestina alikuwa mbele ya binti huyo ambae siku ile anabakwa yeye ndie alimziba mdomo ili asipige kelele. Haukupita muda Sara aliaga dunia kutokana kukosa pumzi muda mrefu, kama kawaida Jestina aliandika kwenye ukuta kwa damu "AMELIPA" kisha akatoweka eneo hilo..CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Siku ya pili wale waliofika kazini mapema walishudia mwili wa sara ukiwa upo katika hali mbaya sana na pia kulikuwa na harufu kali ya kinyesi. Taarifa zilitolewa polisi na haukupita muda walifika sehemu ya tukio na kufanya kazi yao ikiwemo kuwahoji marafiki wa karibu na binti huyo. Baada ya hapo walirudi kituoni kuendelea na majukumu mengine lakini inspector Hans bado alikuwa njia panda asijue la kufanya. Sasa hofu iliongezeka kwa wale wote waliohusika na kifo cha Jestina "unajua mtu wangu sisi tulikosea sana" Jay alimwambia James. "oyaa acha uoga wewe lazima kuna mtu atakuwa anatufanyia uhuni tu" James alijibu. "inawezekana ikawa Alwin au maana tokea atoke hospitali ya vichaa mauaji yameanza" Jay aliongea. "kama vipi tumuibukie asilete mambo ya kijinga" James aliongea kwa hasira na wakakubaliana hivo. Safari ya kuelekea kwa kina Alwin ilianza na kwa sababu walikuwa na usafiri walifika mapema.
"Alwin yupo" Aliuliza Jay bila hata kutoa salamu, "nipo niwasaidie nini" Alwin alijibu mwenenyewe baada kuzitambua. Walimuomba atoke nje na yeye bila kupinga alitoka, "dogo sikia unajifanya mjanja si ndio" James alihoji kwa hasira. "kwani vipi mbona siwaelewi nyinyi" alijibu bila wasiwasi. "kama hutuelewi basi ngoja tutakuonesha" Jay alijibu na kumpa ishara James waondoke.
"James" Alwin aliita, alipogeuka akamuonesha ishara kwa kupitisha mkono katika shingo akimaanisha ni zamu yake usiku wa siku hio. Lakini alipotezea na kuondoka zake bila hata kugeuka nyuma, Alwin alirudi ndani moja kwa moja alikwenda chumbani kwake. "vipi wameshaondoka" Aliuliza Alwin, "ndio" alijibu Jestina akirudi katika umbo lake la kike. Huo ni mchezo wamekubali kuucheza huku Jestina akiitumia nyumba hiyo kama ngome yake na mtu yeyote atakaekuja kwaajili ya kesi yake basi hujibadilisha na kuwa Alwin. Na hicho ndicho alichokifanya siku ile alivyokuja Inspector Hans kwaajili ya mahojiano. Bado vifo vyote viwili vilibakia kuwa ni gumzo, daktari alieifanyia uchunguzi miili hiyo alikuja na majibu yale yale tu "yoyote aliefanya mauaji haya si kiumbe wa kawaida".
************************************
"Matt mwanangu kwanini uliamua kufanya ushenzi ule"
"Ah ni ushundani tu ndo ulionipelekea kufanya vile"
"sasa umeona madhara yake nimetumia mabilioni ya mapesa kuwahonga majaji na wanasheria waifute kesi ile"
"najua mzee, ila usijali kila kitu kipo sawa na muda si mrefu nitarudi nyumbani"
Hayo yalikuwa ni mazungumzo ya Matt na baba yake kwa njia ya simu, baada kufanya tukio lile ilibidi Matt asafirishwe na kesi ile iuliwe kwa aina yoyote. Sasa anataka kurudi akiamini miaka aliokaa nje ya mji wake ingetosha watu kumsahau na hata wenzake walikata mawasiliano nae kwa sababu aliondoka kimya kimya bila kuwataarifu wenzake chochote. Ni baada tukio lile alilomfanyia Jestina, Matt alisafirishwa na baba yake na kupelekwa Ufaransa.
"Baba naskia Alwin kapona" aliuliza Miryam, "ndio mwanangu kapona kabisa" Profesa Alexander Harison alijibu." Ah basi mimi namaliza mtihani wangu wiki ijayo baada ya hapo nitakuja, lakini usimwambie kitu Alwin" aliongea Miryam kwa furaha sana. Miryam hakuweza kuendelea kusoma Mashvile baada lile tukio na lilisababisha kifo cha Jestina pamoja na kichaa cha Alwin. Na baada baba yake kugundua hilo aliamua kumsafirisha kwa ajili ya kwenda kumalizia masomo yake nchini China na huo ndio ulikuwa mwaka wake wa mwisho wa masomo. Lakini haikupita hata siku moja bila kumuombea uzima Alwin.
Bado inspecta Hans alikuwa njia panda maana aliona kama Alwin anamchezea mchezo mchafu, baada kufikiria sana bila kupata majibu aliamua kwenda nyumbani kwa Profesa Alexander Harison kwa ajili ya kuripoti alichokiona. Safari yake ilikuwa ni ya dakika kumi tu, alipofika alikaribishwa ndani na kuomba kuonana na Profesa. Haukupita muda aliambiwa aingie katika ofisi, "samahani kwa kuja bila taarifa" aliomba msamaha kwanza, "bila samahani". "ukweli kuna jambo linatitaza, kwa sababu jana nilienda kuongea na Alwin lakini nilipokutana nae msibani alisema hanifahamu na wala hatujaongea kitu" alieleza, " wakati unaongea nae majibu yake yalikuaje" aliuliza profesa. "yalikua yenye chuki ndani yake na baadhi yalikuwa ya mkato" alijibu. "Alwin hana majibu ya mkato, ni kijana ambae majibu yake yanaheshima" aliongea profesa na kumshtua kidogo inspecta Hans ambae sasa alishaanza kuamini kama hakuongea na Alwin, sasa swali lilikuwa aliongea na nani kama si Alwin. "na kuhusu mauaji yanayotokea, mpaka sasa ripoti zinasema kuwa si ya kawaida" alijikaza na kuendelea kuongea. "naweza nikaziona picha za miili yao" aliuliza profesa. "ndio" kisha akatoa fail na kumkabidhi profesa..CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Profesa aliziingiza kwenye mashine fulani hivi kama projecta na kuzima taa zote katika ofisi yake kusababisha kigiza fulani hivi, kisha akaiwasha ile mashine na zile picha zikawa zinaonekana ukutani. Lakini aliganda kidogo akiangalia alama za kucha katika miili yote miwili na kubaini kuwa alama hizo zimepigwa katika mtindo mmoja. Haraka alifungua droo na kutoa picha ya ile michoro alioandikwa Alwin kipindi ambacho allikuwa hayuko sawa na kuanza kulinganisha. "unaona kitu gani hapo inspecta" aliuliza profesa, "mi naona michoro tu" alijibu. "angalia kwa makini" alisisitiza profesa ndipo inspecta Hans aliposimama na kusogea kwenye ukuta na kuanza kuzichunguza kwa makini sana. Aligundua kuna maandishi fulani hivi lakini alishindwa kuyasoma "naona kama maandishi hivi" aliongea inspecta. "ndio katika miili yote miwili kuna jina limeandikwa lakini katika lugha ya kale ya wenyeji wa Mashvile na jina hilo ni JESTINA" aliongea profesa na kumfanya Inspecta kutumbua macho kama mtu aliesakamwa na tonge la chakula kwenye koo. "unataka kunambia kuwa muuaji ni JESTINA au vipi" aliuliza kwa sintofahamu, "ndio inspecta muuajai ni Jestina, hivi umewahi kusikia kama kuna ulimwengu wa watu waliodhulumiwa" alijibu profesa na kuuliza. "ah mi hizo story huwa nazisikia tu lakini siamini kabisa" alijibu inspecta huku akitabasamu, "basi kuanzia leo ndio uamini kama kweli huo ulimwengu upo na mtu akifa kifo cha kudhulumiwa basi hupita hapo kwanza na hukaa kwa muda wa miaka kumi. ikiwa ndani ya kipindi hicho kutakuwa na mtu duniani ambae anaamini mtu huyo amedhulumiwa na haki haijatendeka basi hupata uwezo wa kurudi duniani kuja kuwalipa wale waliomdhulumu" aliongea na kufafanua Profesa "inspecta kazi yako imekwisha sasa kwa sababu hakuna utakalofanya kumzuia Jestina asilipe kisasi. Wewe kazi yako itakuwa ni kushuhudia tu mauaji hayo" aliongea profesa na kuonekana kama kufunga kikao hicho.
*****************************
Sauti za huba ziliskika ndani ya chumba kimoja katika hoteli kubwa katika mji wa Mashvile, "James niahidi kama utanioa". "niamini wewe ni wangu na kesho nakupeleka nyumbani nikakutamblishe kwa wazazi wangu" James alijibu huku akionekana kunogewa na penzi la mschana huyo, ndani ya chumba hicho taa zilikuwa zimezimwa isipokuwa taa moja nayo ilikuwa ikitoa mwanga hafifu sana na kukifanya chumba hicho kipendeze. Kuna wakati James alifunga macho kwa raha alioipata, alipofungua alijkuta akimuachia mpenzi wake na kuruka pembeni. Hiyo ni baada kuona sura ya Jestina badala ya mpenzi wake, "James unanini mbona umenikata stimu" aliongea mwanamke huyo kwa kudeka. "ah hamna kitu" alijibu kwa kujibabaisha na kurudi kitandani ili aendelee na mchezo, wakati akiendelea kufanya hivo aliangalia dirishani na kumuona Jestina akimuangalia. "mama" alipiga kelele huku akimsukuma mpenzi wake kwa nguvu na kusababisha ajigonge kichwa kwenye kona ya kitandana na kuanza kutoka damu nyingi na mwisho alitulia tuli. Kicheko kikali kiliskika na kufuatiwa na maneno "na bado utajuta kuzaliwa" kisha kimya kikatawala ndani ya chumba hicho. Alipoona hali imerudi kuwa ya kawaida alimsogelea mpenzi wake na kumtikisa lakini wapi, muda mrefu alikuwa kashapoa. Woga ulimpata na kuamua kuvaa na kuondoka eneo hilo na kuuwacha mwili wa mpenzi wake ukiwa umetapakaa damu.
Asubuhi mapema akiwa kwao, gari ya polisi ilifika na kuonyesha waraka wa kukamatwa James, hakukuwa na jinsi zaidi ya kukubali na kufikishwa kituoni. Alihojiwa kidogo lakini hakutaka kuonyesha ushirikiano, hivo ikatoka amri awekwe mahabusu mpaka atakapokuwa tayari kusema. Masaa yalikatika na hatimae usiku ulifika bila kukubali kuongea chochote. Akiwa kajilaza kwenye kigidoro kidogo, "James...James...hahaha" aliskia sauti ikimwita lakini hakumuona mtu. "Jestina dadangu naomba unisamehe, ujinga tu ulikuwa ukinisumbua" alianza kuomba msamaha huku akilowanisha suruali yake. "mpumbavu mkubwa wewe nani dadaako, kuna mtu anaeweza kumshika dadaake ili abakwe" Jestina alijibu kwa hasira na kumtokea mbele yake. "mamaaaa nakufa" James aliruka huk akipiga kelele, lakini ghafla Jestina akatoweka na kumtokea nyuma yake.
Aliinua mkono wake na kumtandika kucha za mgongo na kumfanya apige ukwenzi wa maumivu. Kwa kweli James alijua hicho ndio kiama chake maana kila alivojaribu kujitetea ni kama alikuwa akichochea moto. Jestina aliendelea kumrarua mpaka alipohakikisha amemmaliza kabisa, kuhakikisha haishi tena alikpiga kucha za koromea na kulikata. Kama kawaida yake aliacha ujumbe na kutoweka, siku ya pili asubuhi maaskari waliripoti kifo cha James. Wengi walishtuka hasa waliohusika kwa namna moja au nyingine katika kifo cha Jestina. Hali hiyo haikuwatisha wao tu bali mpaka watu wengine ambao hawakujua chochote juu ya matukio hayo. Kila kukicha vyombo vya habari vilitangaza mauaji mapya yanayofanyika hukua ikiaminika kuwa muuaji ni mtu ambae amebobea na anauwa kwa sababu ya kulipa kisasi. Kama kawaida inspeta Hans alirikodi tukio hilo katika mafaili yake na kuondoka. Sasa hakuumiza sana kichwa kwa sababu alishajua muuaji sikiumbe wa kawaida..CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Upande wa Alwin hali yake ilizidi kutengemaa na sasa mwili wake ulishaanza kurudi na vidonda vidogo vidogo vilishaanza kukauka. Familia yake ilifurahi lakini haikuwa hivyo kwa familia ya Jestina ambayo bado walikuwa ni wenye majonzi sana hasa kwa kumpoteza mtoto wao pekee. Hilo lilimuathri sana mama yake na kupelekea baadhi ya wakati kuzimia kutokana na msongo wa mawazo. Hata baba yake pia ilimathiri na kupelekea kudhoofika kimwili japo si sana. Siku hiyo Alwin alipanga kwenda kuwatembelea ili kuwajulia hali, aliondoka kwao asubuhi mapema na kuelekea kwa Mr Hendrix. Alipofika alikaribishwa ndani vizuri na mfanya kazi kisha akaenda kuitwa Mr Hendrix. Alifurahi sana alipomuona Alwin na kumkumbatia "Mungu ashukuriwe kwa kukupa uzima mwanangu" aliongea huku akijizuia machozi yasitoke. "asante, habari za siku nyingi" Alwin aliuliza, "kama unavoziona mwanangu, kwa kweli tokea Jestina atutoke maisha yetu yamekuwa magumu sana sijui hata kwanini Mungu ametutenda kiasi hichi" Alijibu Mr Hendrix na wakati huu alishindwa kuyazuia machozi na kuyaacha yatiririke kuonyesha machungu alokuwa nayo.
"hapana mzee wangu usiseme hivo, Mungu hajawatenda ila amekupeni mtihani kama alivowapa wengine tu ili kukupimeni imani. Yeye ndie aliewapa Jestina na yeye ndie aliemchukua kwani kuna ubaya gani mtu kuchukua kilichochake. Nyie jueni tu kama Jestina amepumzika lakini hatopata amani ikiwa bado mtaendelea kumlaumu Mungu kwa kifo chake" Alwin aliendelea kumliwaza Mr Hendrix ambae alikuwa akilia kama mtoto mdogo. "mwangu we huujui uchungu nlokuwa nao, kifo cha Jestina kimepelekea mpaka mamaake kupata maradhi ya kuanguka. Ukweli Alwin naogopa kumpoteza mke wangu" Alwin alivyosikia hivo alishtuka kidogo na kuomba kwenda kumuona. Bila kinyongo Mr Hendrix aliongozana nae mpaka chumbani, alimkuta akiwa amelazwa huku akiwa amewekwa drip. Alwin alisogea mpaka pembeni yake na kukaa kwenye kiti "habari yako mama" aliongea kwa sauti ya chini. "nashkuru sijui wewe Alwin" alijibu mama huyo japo kwa tabu kidogo. "pole kwa yote yaliotokea", "asante mwanangu, kwanini lakini" alijibu huku akilia. ""pole kwa yote yaliotokea", "asante mwanangu, kwanini lakini" alijibu huku akilia. "yote ni kazi ya Mungu na kama tunavojua kazi ya Mungu haina makosa cha msingi mamaangu kukubaliana kama Jestina hayupo tena nasi" Alwin aliongea huku akimshika mkona mama Jestina kwa ajili ya kumliwaza.
"kwanini waliamua kumfanyia ukatili mwanangu, aliwakosea nini" aliendelea kuongea huku machozi yakimtoka. "usijali mama wote waliohusika na kifo cha Jestina watalipa kutokana na dhambi waloifanya" Alwin aliongea huku hasira zikizidi kumpanda lakini alijitahidi kuzizuia. "nakuahidi mama nitakuletea Jestina mwengine, nipe muda tu mpaka mambo fulani yakamilike" aliongea Alwin na kumfanya mama huyo aachie tabasamu kwa mbali. Waliongea mambo mengine mengi huku kwa muda wakisahau machungu yote ya mambo yaliotokea. Baadae Alwin aliaga na kuondoka na kurudi kwao, moyo wake ulifarijika sana kuonana na familia ya Jestina. Hata wazazi wake waligundua furaha alokuwa nayo na wala hawakujali kumuuliza chochote kile.
***************************
Baada ya kifo cha James waliitana karibu wote wale waliohusika na kifo cha Jestina, "jamani natumai mtakuwa mnajua nini kilichotukutanisha hapa" Jay aliongea baada kikao hicho kilichokuwa na waschana sita na wavulana kumi na moja. "tumeshazika wenzetu watatu, na hatujui atafuata yupi" aliendelea kuongea. "lakini kwa nini tulishiriki kitendo kile" aliongea mschana mmoja alieitwa Christina, "hakuna muda wa kulaumiana saa hivi jambo lile ndo lilishatokea kilichobaki ni kutafuta suluhishi kwa hili linalotukabili sasa hivi" aliongea kijana mwengine alieitwa Mark. "lakini wewe, James, Jay na Matt ndo mloyataka" aliongea mschana mwengine alieitwa Jesca. Walianza kulumbana huku kila mmoja akitafuta wa kumtupia lawama, "sasa mukigombana hivo ndio mtafikia suluhisho, hebu acheni upuuzi wenu" alifoka Jay na wote wakanyamaza kimya. "cha msingi hapa ni kumjua muuaji ni nani" aliongea Jay na kuwashangaza wote. "kivipi wakati muuaji ni mzimuwa Jestina" alijibu Jesca, "kwanza subiri niwaambie kitu, mimi hasa siamini kama mtu akifa anarudi tena duniani eti akiwa mzimu" aliongea Jay. "cha msingi hapa kwanza tuanze kumfatilia Alwin kila anachokifanya, mi nahisi kama si yeye anaefanya mauji basi atakuwa anamjua muuaji ni nani" Aliongea Jay kwa kujiamini.
"oyaa we umekunywa mchana wote huu mtu wangu" aliongea kijana mwengine alieitwa John, "unadhani boya kama yule anaweza kufanya mauaji, hivi we unadhani kuuwa ni kitu cha mchezo" aliendelea kuongea. "hivi nyie hamjiulizi kwanini mauaji haya yameanza baada Alwin kutoka hospitali ya vichaa, kwanini kipindi chote cha miaka kumi hakujatokea matukio kama haya" aliendelea kuongea Jay na sasa maneno yake yalianza kuleta maana ndani ya vichwa vya wenzake. "hapo kidogo inaanza kugonga ndani ya kichwa changu" aliongea Mark kisha akaendelea " sasa tunafanyaje". "hapo ndio kwenye shughuli yenyewe, inabidi tuanze kufanya uchunguzi chini kwa chini mpaka tuapate ukweli" aliongea Jay na kisha wakaanza kupanga mipango ya kuanza kufanya uchunguzi huku kila mmoja akipewa jukumu lake. Baada ya maongezi ya muda mrefu waliagana na kila mtu alikwenda zake kwao.
**************************
.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Jesca akiwa chooni anaoga ghafla moshi ulianza kutanda chumbani kwake, na ulipotoweka alianza kuhisi maji ni mazito sana na alipoangalia vizuri alijikuta anaoga damu. Alipiga kelele kwa nguvu huku akitoka mbio chooni, alianza kusikia sauti za ajabu ajabu zikinong'ona. "we nani" aliuliza kwa nguvu, "Jesaca siku yako ndio leo" aliiskia ikimjibu, "utalipa kwa ulichokitenda" yalizidi kusikika maneno. "unadhani mi nakuogopa, kama unajiamini jitokeze mbele yangu" aliogea kwa kejeli. ghafla taa zikazimika na kuwaka, mbele yake alisimama Jestina huku damu nyingi zikimtoka. Sasa Jesca aliamini kama ule ni mzimu, alianza kupiga kelele huku akikimbilia mlangoni kwa ajili ya kutoka lakini mlango haukufunguka. "nimekoma nisamehe Jestina" alianza kuomba msamaha, "siku ile wakati unafurahia tukio lile hukujua kama ulikuwa unakosea" Jestina alijibu huku akimsogelea na kumkaba koo. Jesca alianza kutapatapa huku akijaribu kupiga kelele lakini hazikutoka. Kwa nguvu Jestina alimrusha ukutani na kumbamiza, alimsogelea na kumtandika makucha mara kadhaa. Jesca alipoona hali mbaya, alijinyanyua na kukimbilia dirishani. Kwa nguvu alijirusha na kuvunja kioo, kwa vile chumba chake kilikuwa gorofani alianguka mpaka chini na kupasuka kichwa na hapo ndio ukawa mwisho wa Jesca. Hali ilirudi kuwa shwari na Jestina alitoweka huku akiacha ujumbe anaouwacha mara zote baada kufanya mauaji.
Kishindo kiliskika na majirani pamoja na wazazi wa Jesca walitoka lakini hali waliokutana nayo iliwafanya washangae, Jesca alikuwa chini huku damu nyingi zikitapakaa sehemu alioangukia. Simu zilipigwa polisi na muda si mrefu walifika eneo la tukio, Inspector Hans alifika kuchelewa lakini alifanikiwa kuona mwili kabla haujapelekwa maabara kwa ajili ya uchunguzi zaid. Aliwahoji wazazi wa Jesca kama wanajua lolote kuhusiana na kifo cha Jesca lakini walikuwa hawajui chochote. Basi baada taratibu zote kufanyika mwili wa Jesca uliingizwa kwenye gari na kupelekwa hospitali kwaajili ya uchunguzi zaidi. Vifo hivo viliendelea kuacha gumzo kwa watu wote, hasa watu wa usalama maana kila walipojaribu kuchunguza waliishia kwenye mambo ya mizimu jambo ambalo wengi hawakukubaliana nalo. "jamani sisi tunaonekana wapumbavu sana" aliongea mkuu wa kituo cha inpector Hans, "tukimuacha huyu muuaji atasababisha kuachishwa kazi" aliendelea kuongea.
"mnajua sisi wote tulikosea mwanzo" aliongea inspecta Hans na kuwashangaza wote, "unamaana gani kusema hivo?" aliuliza mkuu wao kwa mshangao. "nina maana kuwa mauaji yote haya yanahusiana na kesi iliyotokea miaka kumi iliopita" aliendelea kufafanua inspector. "Kwahiyo unamaanisha haki haikuyendeka katika kesi ile au" aliuliza kwa hasira mkuu wake. "kwa kweli mkuu sasa itabidi heshima nieke pembeni sasa maana unataka kunifokea bila msingi, kesi ile ulikabidhiwa wewe na ushahidi wa kutosha kuwa Jestina alibakwa na mwanaume zaidi ya mmoja akiwemo mtoto wa mheshimiwa waziri mkuu Matt, lakini kwa tamaa zako binafsi ukala pesa na kukanusha ushahidi badala yake ukasema kuwa aliebaka ni Alwin. ulifanya hivo makusudi kwa kuelewa kuwa Alwin asingeweza kusema lolote kwa sababu alirukwa na akili. Sasa vyote vinavyotokea leo ujue na wewe umehusika. Na kama nilivokwambia nimekukera basi fanya unalotaka" alimaliza kuongea Inspector Hans na kutoka katika chumba hicho cha mikutano.
***********************************
(miaka kumi iliyopita)
"asante sana inspector kwa kufika hapa japo nimekushtua" aliongea baba yake Matt, "kwa wewe muheshimiwa hata kama ningekuwa nimelala basi ningeamka na kuja" aliongea inspectar Brandon. "sasa inspecta ni hivi kuna kesi umepewa uisimamie lakini kwa bahati mbaya sana kesi hiyo na mwanangu anahusika" aliongea Waziri mkuu ambae ndio baba yake Matt, "una maanisha kijana wetu Matt anahusika na kifo cha Jestina" aliuliza inspecta kwa mshangao. "ndio inspecta, sasa nataka unisaidie kitu kimoja", "kitu gani hicho". "nataka hiyo kesi ife na ikiwezekana ushahidi upotee kabisa au tafuta yoyote tu umbambikizie" aliongea waziri huku akisogeza bahasha iliovimba. "lakini unajua muheshimiwa kazi hiyo ni ngumu sana" aliongea inspecta huku akiimezea mate ile bahasha. "ah halafu ukifanikiwa kufanya hivyo nitaandika barua rasmi upandishwe cheo" aliongea waziri na kuzidi kutia tamaa inspecta Brandon. kuskia hivo aliinuka haraka na kuchukua ile bahasha kisha akasema "usijali mzee nitahakikisha kesi inakwisha mara moja" na kuondoka. Waziri alitabasamu na kujisemea "hakuna kinachoshindikana mbele ya pesa".
Inspecta Brandon alirudi kituoni huku akipanga jinsi ya kuizima kesi hiyo, alikuwa na mawazo mengi sana kichwani hasa alipofikiria kupandishwa cheo. Alitumia mbinu zote anazozijua mpaka akafanikiwa kupotosha ukweli wa kesi hiyo na kumsingizia Alwin kuwa ndie aliefanya jambo lile. Habari za kukanushwa kesi hiyo zilimfikia profesa Alexander Harison, alisikitishwa sana lakini hakukuwa na njia nyingine ya kufanya zaidi ya kukubali tu. Wakati wote huo Alwin alikuwa hospitali hajitambui kwa maneno mengine alikuwa amerukwa na akili. Na kutokana na hilo kesi hio ilifungwa moja kwa moja na hivyo Matt na wenzake kuwa huru. Baada ya tukio hilo ndipo waziri mkuu akaamua kumuondoa kwa muda mtotot wake huku Inspecta Brandon akipandishwa cheo na kuwa mkuu wa kituo chake jambo ambalo hata wenzake hawakujua limetokeaje lakini hakuna alieuliza.
***********************
(baada miaka kumi).CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Profesa tayari wameshaakufa wanne lakini bado hakuna aliekuwa tayari kukubali kuhusika na kifo cha Jestina" alisema Alwin wakati akiwa anaongea na profesa. "tulia kijana madhali hawataki kusema wacha Jestina alipe kisasi kwa kuwauwa mpaka pale watakapokubali kusema ukweli" Aliongea profesa huku akitabasamu. Maongezi yao yaliendelea kwa muda mrefu sana mpaka mwisho walikubaliana wakutane baada wiki moja kujadili tena swala hilo. Baada ya hapo kila mmoja aliondoka na kuelekea nyumbani kwake, lakini Alwin alipita makaburini na kuzuru kaburi la Jestina. "natumai umepumzika kwa amani mpenzi wangu, usijali watalipa kwa kile walichokufanyia" aliongea Alwin na kuweka ua juu ya kaburi la Jestina na kisha akaondoka zake. Jay na wengine waliendelea kumfatilia Alwin wakiamini yeye ndie muuaji na Alwin tayari alishawashtukia hivo kupita kaburini kwa Jestina ilikuwa ni kuwachanganya wanaomfatili pasi na kujua kumbe wao pia wanafatiliwa na Alwin.
"unajua mke wangu Alwin kabadilika sana siku hizi" aliongea Mr Kelvin kumwambia mkewe, "kivipi mbona mi namuona yupo kawaida tu. "hapana mke wangu mi nakwambia tena Alwin kabadilika sana tokea atoke hospitali ya vichaa" alisitiza Mr Kelvin. "mhh haya lakini mi namuona kawaida tu isipokuwa siku hizi kachangamka sana tafauti na zamani" aliongea mama Alwin huku akiachia tabasamu akionesha kufurahishwa na mabadiliko ya Alwin. Wakati wakiendelea kuongea Alwin aliingia na kuwasalimia, waliitika kwa pamoja na baadae Alwin akaenda zake chumbani kwake.
Kwa upande wa inspecta Hans baada ya kutoka kwenye kikao alikwenda nje na kutulia huku akili ikitafakari mengi sana, akiwa dimbwi hilo la mawazo aliskia akiitwa na alipogeuka alikutana na mkuu wake wa kituo inspecta Brandon. "nifuate ofisini" aliongea na kuondoka, bila kusita aliinuka nae akamfuata nyuma mpaka walipofika ofisini. "bwana mdogo chunga kauli zako" hayo ni maneno ya kwanza yaliotoka kinywani mwa inspecta Brandon, "wewe hapa kituoni unaongea vile kama nani" aliendelea kuongea kwa hasira. "samahani mkuu, ule ndio ukweli we unadhani dunia bila haki ipo sawa. Hata waliokufa nao wanataka haki zao, we ulielewa fika kama Matt na wenzake wako hatiani lakini ukaibaitilisha kesi na kumuuzia Alwin. Natamani huo mzimu siku moja ukutembelee na wewe uone machungu ya kudhulumiwa" alijibu inspecta Hans bila woga wowote ule. "sasa unaonekana umeota mapembe si ndio" aliongea inspecta Brandon, "kama ndivyo unavofikiri sawa tena makubwa sana" alijib inspecta Hans na hakusubiri neno jingine kutoka kwa mkuu wake aliondoka maana hata yeye hasira zilishaanza kumpanda. Alimuacha mkuu wake akiwa ni mwenye mawazo tele lakini akaona bora apotezee tu.
Kifo cha Jesca kiliwachanganya wengi miongoni ya waliotenda kosa lile, wapo walioomba usiku usiingie maana walijua Jestina hufanya mauaji yake usiku. Lakini kwa vile hatuwezi kuzuia masaa basi muda uliyoyoma na hatimae kiza kikaana kutanda angani, hatiame usiku uliingia lakini kulikua na mvua kali sana iliondamana na ngurumo pamoja na radi. Usiku huo ulivo ulitosha kuwatisha wengi sana, Mark ndo alikuwa akitoka zake mihangaikononi kwake kuelekea nyumbani kwao ghafla akiwa njiani umeme ukazima.
Hali hiyoilimshtua kidogo Mark lakini akajipa moyo kuwa ameshaakaribia nyumbani kwao, hivyo basi alianza kukazana huku akiangalia pande zote kama kuna kitu ama mtu anamfuata. Nyumba yao ilikuwa imejitenga kidogo kutoka katika makazi ya wtu wengine, aliacha njia kubwa na kuingia njia ndogo ambayo ilikuwa nampeleka mpaka kwao. Wakati akikazana kwa mbali mbele yake akaona kama mtu kapita mbio. Moyo ulianza kumuenda mbio maana alishaanza kuziona dalili za mauzauza, akiwa anatetemeka ghafla alihisi kama kitu kimepita nyuma yake. Aligeuka kwa kasi lakini hakuona kitu, alipogeuka tena mbele kwa mbali akaona mtu akiwa anakuja upande wake taratibu . Kidogo alipata matumaini na kuanza kukazana kumfata yule mtu. Lakini alivomkaribia mwili ulimsisimka na kuhisi kama hakuwa mtu wa kawaida lakini alipiga moyo konde na kunyongea kwa mendo wa haraka. Ghafla tochi yake ilizima, na ilivowaka alikutana sura ya ajabu sana mbele yake. Aliruka na kuiangusa tochi pembeni, japo kulikuwa na baridi lakini kijasho kilianza kumtoka kwa wingi. "maumivu...." alisikia sauti ikitamka neno hilo kwa sauti a kuning'ona, "leo utahisi maumivu nilioyapata" sauti hiyo iliendelea kuongea huku ikizidi kuwa kali. "unataka nini lakini" aliuliza Mark kwa woga, "nataka roho yako" alijibiwa na wakati huu sauti aliifahamu vizuri sana kama ilikuwa sauti ya Jestina..CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Aliokota tochi yake na kuanza kukimbia, lakini hakufika mbali alishtukia akichezea kofi zito la uso lililomfanya aanze kuona mawenge kidogo na kuanguka chini. Mark alijua kuwa huo ndio ulikuwa mwisho wake, "nisamehe Jestina" alianza kuomba msamaha kwa kilio huku damu zikimoka mdomoni. "leo unalia mshenzi mkubwa wewe, siku ile ulikuwa ukicheka" Jestina aliongea na kumnyanyua Mark. Sasa alifanikiwa kumuona uso kwa uso, macho yalimtoka Mark asijue nini la kufanya. Wakati akiendelea kutumbua macho alirushwa kwa nguvu, kabla hajakaa sawa alichezea makucha kadhaa ya mgongo na kumfanya apige kelele za maumivu. "nimekoma naomba unisamehe" aliongea huku akisimama, "nikusamehe kweli, hivi unajua ni maumivu kiasi gani niliyapata siku ile" Jestina alijibu na kumtokea Mark mbele na kumkaba, kisha sura yake ilianza kubadilika na kuwa ya kutisha sana huku damu nyingi zikichuruzika kutoka machoni mwake kama machozi. Mabadiliko hayo yaliambatana na harufu kali sana ya kuoza, kwa nguvu alimpiga Mark na chini kiasi cha kushndwa kuinuka. "leo utakiona cha moto mpumbavu mkubwa wewe" aliongea Jestina na kisha akamfungua mdomo Mark na kumtia funza. Yeye alikaa pembeni akimuangalia kwa jinsi funza wanavomteketeza Mark. Hawakuwa funza wa kawaida kwani punde baada ya kutiwa mdomoni walianza kutoboa sehemu mbalimbali za mwili wa Mark na kusababisha maumivu makali sana. Mark alipiga sana kelele lakini hakuna msaada wowote alioupata mpaka mwisho alitulia tuli na kuaga dunia. Jestina alipotea eneo hilo akiacha ujumbe wake wa kawaida.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment