IMEANDIKWA NA : GLOBAL PUBLISHERS
*********************************************************************************
Simulizi : Kitanzi, Kisu Na Bastola
Sehemu Ya Kwanza (1)
ANATEMBEA akiwa anapepesuka kwa ulevi uliomjaa kichwani. Amelewa chakaliii, pombe zikimdanganya na kumfanya asiwe na hofu hata kidogo kukatiza kona hatari za mitaa ya Songasonga.
Laiti kama angekuwa na akili zake timamu asingediriki hata kuwaza kupita peke yake usiku huo kwa kuwa anazijua vema sifa za mtaa wake.
Roba za mbao, ubakaji na mara nyingine kesi za mauaji ndiyo mambo makubwa yanayozifanya hata serikali za mitaa na wilaya ziuangalie kwa jicho la tatu pekee mtaa huo. Lakini usiku wa leo, saa nane hiyo, Dedan Magesa anapita bila wasiwasi wowote, mkononi akiwa amekumbatia kopo la pombe ya kienyeji maarufu kama mataputapu.
“Muuuvu bichii geliatu weiii. Muuuvu bichii geliatu weiii,” alijiimbia wimbo wake aliokuwa akiurudiarudia kiitikio tu tena kwa sauti mbaya ya kilevi kinachotia kichefuchefu hata kukisikiliza.
Taratibu Magesa aliyoyoma akipita karibu kabisa na kona na vichochoro kadhaa vyenye sifa mbaya sana za uhalifu. Kama vile mkono wa Mungu ulikuwa juu yake siku hiyo, alifika nyumbani salama salimini. Akafungua na kufunga mlango wa chumba chake kwa umakini mkubwa kisha akajitupa kitandani kwa nguvu na kulala fofofo akiwa na viatu na nguo zake zote. Kwa mbali kabisa, moyo wake ulilia na kuomboleza.
“Uko wapi mpenzi wangu, kwa nini umeniacha peke yangu leo? Ina maana hukunipenda hata kidogo kiasi cha kuamua kunifanyia hivi?
“Najua sitampata msichana mwingine mzuri kama wewe...Ooh Carolina! Nini nimefanya hadi kustahili adhabu hii?”
***
Asubuhi iliyofuata, Dedan aliamka kama kawaida yake na kufungua ofisi yake, kibanda kidogo pembezoni mwa nyumba kubwa aliyopanga, akiuza vifaa vya simu, kuchajisha simu, kutengeneza na kuingiza nyimbo kwenye simu kwa kutumia kompyuta.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kwa maisha ya kujinyima na kutopenda starehe, kazi yake hii ilimnufaisha kiasi cha angalau kujikimu kimaisha na pengine kumfanya hata asiwaze kabisa kufikiria kufanya kazi nyingine yoyote.
Tofauti na siku nyingine, siku hiyo ilianza vizuri sana kwa upande wake, alipata wateja wengi kupita kiasi. Kama mjasiriamali mwingine mzoefu, alifanya kazi zake kwa umakini mkubwa na kuhakikisha wateja wake wanavutiwa na huduma zake kwa kuongeza ukarimu na kuongea lugha yenye bashasha na hata ikamlazimu kuwajua na kuwaita kwa majina wateja wake ambao walijipanga kwa michapo ya hapa na pale huku akiendelea kuwahudumia.
Hakika mtu yeyote alijisikia huru kukaa kwenye benchi dogo lililopo pembeni ya kibanda cha Dedan, akipiga soga na kupoteza muda, akinywa kahawa au pengine akijiunga na kikundi cha vijana wachache kwenye vikao visivyo rasmi wakibadilishana mawazo ya siku.
Ndiyo, kila mtu hulalamikia ugumu wa maisha wa siku hizi, kiasi cha furaha au jambo jema kutokea kwa nadra sana na pengine lisitokee kabisa hata kufikia mtu kukushirikisha walau punje ya neema yake.
Umasikini ulisababisha kila mtu ajifungie peke yake kwa uchoyo akila matunda ya kazi zake. Hivyo, iwe asubuhi, mchana au jioni, wakazi wa Mtaa wa Songasonga hukutana kwa unyonge si kwa jambo lingine, bali kuzungumzia mawazo dhaifu ya siasa za kupindua nchi na mara nyingine wakisimuliana hadithi za nani kafanya nini, lini na wapi!
Kwa kifupi Dedan alikuwa ndiyo kitovu cha mkusanyiko wa watu katika mtaa mzima wa Songasonga. Kwa sababu hiyo na sifa nyingine kedekede, alitokea kupendwa na kila rika kiasi cha kujulikana vizuri na kila mtu mtaani kwake.
Japokuwa alionekana mwenye furaha kubwa machoni mwa watu siku hiyo, ndani ya moyo wake kwa kificho alikuwa amebeba maumivu makali kiasi kwamba kama hali hiyo ingemkuta mtu mwingine kwa hakika asingekuwa hata na nguvu ya kusimama na kuongea kwa furaha mbele za watu.
Siku zote Dedan aliamini katika kuyamaliza matatizo yake yeye mwenyewe bila kuathiri mwenendo wa shughuli zake au wa watu wengine. Akaamua kutowashirikisha kabisa ndugu wala marafiki zake majonzi na matatizo yake. Mara nyingine aliweza hata kulala na njaa bila kusema wala kuomba msaada kwa mtu yeyote.
Huenda misimamo hiyo ndiyo sababu kubwa iliyomfanya ajikaushe muda wote huo, akiigiza kucheka na watu hali moyoni akilia kwa sauti akimuwaza mpenzi wake, hapana, aliyekuwa mpenzi wake, zamani
“...ooh! Carolina, maisha gani nitaishi bila wewe? Naumia…naumia, ee… Mungu naomba nirudishie Caro wangu.”
Tenzi zilipokwamia hapo alitamani kupiga kelele na kulia kwa nguvu. Huenda angepunguza maumivu walau kwa kiasi kidogo, si ndiyo wanavyosema hao wanaojiita wanasaikolojia, eti kulia kunapunguza msongo wa huzuni na kulainisha mrundikano wa dukuduku lililofungamana rohoni. Waongo wakubwa!
Kinyume na wote hao yeye aliamini kulia si punguzo wala suluhisho la matatizo yake, hasahasa tatizo la mapenzi. Alihakikisha kwamba hatoi mwanya wa hata chozi moja kumdondoka wala kumlengalenga kutoka machoni mwake. Mwanaume rijali hamlilii demu bwana!
TARATIBU zimwi la upweke likamzonga na kuushinda kirahisi ustahimilivu wa moyo wa Dedan. Kama mfungwa kwa mawazo yake akajikuta hajielewi kabisa. Kichwani akiwaza mara ya kwanza alipoongea na Caro kwa njia ya simu
“Mungu wangu! Msichana mrembo wa ajabu huyu,” alisema moyoni Dedan. Akakumbuka pia alipoamua kumfungulia kurasa mpya za mapenzi ndani ya kuta za moyo wake.
Alikumbuka vyema kila zuri walilofanya pamoja, wakicheza baharini na kurushiana mito kitandani. Walilishana chakula na kubusiana kimahaba.
Lakini hayo yote yalitoweka ghafla baada ya kukumbuka sauti kali ya Carolina kwenye simu ikimtosa bila huruma na pasipokuwa na sababu yoyote. Akasikia sauti nyingine ya mwanaume wake wa sasa ikimchimba mkwara kwamba atakiona cha mtemakuni endapo atajipendekeza kwa hali yoyote ile kumtafuta Carolina.
“Hapana,” alijishtukia akiweweseka kwa sauti ya ukali mbele ya mteja wake mkubwa, Salima ambaye muda mwingine alikuwa akimsemesha huku akimkabidhi simu yake ya mkononi kwa ombi la huduma ya kuchajisha lakini bila mafanikio.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ooh! Samahani sana Salima, ulikuwa unasema nini?” Dedan aligutuka kutoka katika vita ya nafsi na kushusha pumzi ndefu akimwomba Salima arejee maongezi yake ya awali.
“Dedan, mzima kweli leo wewe?” Salima aliuliza baada ya kugundua hali ya kubabaika ya Dedan.
“Mi mzima tu...lete stori,” kwa uchangamfu Dedan aliongea kiasi cha kumshawishi Salima aamini kwamba kila kitu kilikuwa sawasawa.
“Hata hivyo, siku zote ni nzuri kwa Dedan, ni kama anaishi katika ulimwengu wa pekee, japo ni maskini mwenzangu, anaonekana haumizwi na kitu. Shida hizi anazichukulia kama changamoto kwa kupigana kwa nguvu zake zote kupata maendeleo tofauti na vijana wengi wa rika lake.
“Kweli ninatamani sana niwe na mwanaume kama huyu. Hapana si kama, bali ni huyu huyu…Mh! Lakini namwogopa kumuanza, sijui atanichukuliaje? Mtu mwenyewe ni mwingi wa shughuli! Ila nitamwambia kesho asubuhi nikija kuchukua simu yangu.
“Nitamtumia meseji nzuri ya mapenzi. Nimejaribu kumfanyia mambo mengi ilimradi azisome hisia zangu, lakini mtu mwenyewe wala haoni,” aliwaza Salima huku akiwa amesimama na kujichekesha na kuweka tabasamu pana mbele ya Dedan aliyekuwa akimtazama tu bila kuona chochote.
Mawazo yake yalikuwa mbali, kama vile ana macho lakini haoni na ana masikio lakini hasikii.
“Usiku mwema Dedan,” aliongea Salima kwa huruma na upole baada ya kugundua ameshindwa kulinasa windo lake kwa siku hiyo.
Mbinu alizofundishwa na kungwi wake, Bi. Hamdani wa Masasi hazikufua dafu mbele ya Dedan.
Alitamani amrukie na kumbusu kwa nguvu ili amjulishe hisia zake, lakini alihofia akiamini ataonekana msichana malaya kama si aliyekosa maadili mema.
“Nitasubiri nafasi yangu, sitaki niharibu yote niliyoyaanza. Kwa Dedan nitakuwa mwanamke mstaarabu, mwema na mwaminifu daima naamini atanipenda tu,” alijiapiza na kujiondokea zake moyoni akilia na kumlaumu mwanaume huyo kwa kutojua windo lake.
“Usiku mwema Dedan…usiku mwema mpenzi wangu...” chochote asichokisema kwa sauti kumwambia Dedan moja kwa moja, aliamua kukimalizia kwa kuongea kwa sauti ndogo akitumaini ipo siku atamjibu na kumuuliza mambo mengi wakiwa kama mke na mume.
Baada ya kuhakikisha amemaliza na kuweka vizuri kila kitu, Dedan aliitazama saa juu ya kioo cha simu yake iliyoonesha namba ishirini na moja, ikiashiria saa tatu usiku kwa urekebisho wa saa ishirini na nne za siku moja.
Alifunga vyema ofisi yake kisha akatokomea huko vichochoroni ambako aliwahi kusikia vinauzwa hivyo vinavyopoteza mawazo, eti pombe!
“Hakuna muda mzuri wa kuamua kuwa chakari kama huu,” Dedan alijisukuma kwa mara ya kwanza kwenye vilabu vya pombe za kienyeji.
Aliamini atalewa kwa gharama ndogo sana huku akifanikiwa angalau kuvuka makali ya upweke kwa usiku huo wa kwanza akilala akiwa anajua kabisa hataishi na Caro wake tena.
***
Asubuhi aliamka na kujinyoosha na kupiga miayo mfululizo. Alionekana mwingi wa uchovu kutokana na pombe kali za jana yake. Ghafla alijishangaa machozi yakimbubujika. Alitaka kuamka, lakini akashindwa. Jasho jingi lilimtoka mwilini huku mapigo ya moyo yakienda kwa kasi ya ajabu. Kama mzigo alidondoka chini na kupoteza fahamu.
Jasho jingi lilimtiririka na kufuatiwa na maumivu makali ndani ya kifua chake. Mapigo ya moyo yalimuenda kwa kasi na kusimama kwa mara moja. Ghafla nguvu zake zilimuishia akadondoka na kuzirai akiwa peke yake chumbani.
Salima alitembea haraka akielekea dukani kwa Dedan. Moyoni akiwa na malengo makuu mawili, kuichukua simu yake aliyoiacha kwenye chaji usiku wa jana yake na kumfungukia Dedan kuhusu dukuduku aliloliweka rohoni kwa muda mrefu.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Njiani kote moyo wake ulimdunda kwa kasi akihofia ni nini Dedan atamjibu kama atamwambia hisia zake. Kile kiroho cha nighairi leo nimwambie kesho kilizidi kuisumbua nafsi yake.
Akaona kama kila siku ataendelea kuogopa na kuishia kusema atamwambia kesho, basi kwa hakika hatamwambia daima na zaidi ataendelea kuumia tu na kesho zisizofika.
“Leo lazima kieleweke,” Salima alijipa moyo huku akijiangalia vizuri kuanzia juu mpaka chini jinsi alivyopendeza. Akahakikisha anatembea mbali na barabara akihofia vumbi la magari lisije likamchafua.
Hakuwahi kujisikia hali hii kwa mwanaume yeyote kabla hajakutana na Dedan, lakini siku hiyo alishindwa kabisa kujizuia kujipodoa na hata kupitiliza. Asubuhi alipokuwa bafuni alitumia takriban nusu saa kuhakikisha alikuwa msafi kila kona ya mwili wake.
Hata alipokuwa chumbani mwake, alijishangaa akitumia muda mwingi kucheza mchezo wa vua vaa kwa kila aina ya nguo mpaka alipoipata suruali yake adimu aliyoiandaa rasmi kwa tukio muhimu kama hilo.
Kwa kuwa alikuwa mgeni wa mavazi ya kubana, alijishangaa baada ya kuona ukubwa wa hipsi zake na jinsi zilivyojichora vema nje ya suruali. Alitembea huku akijiangalia kila hatua aliyoipiga.
Juu alivaa kiblauzi cha pinki kilichoendana vizuri na rangi ya ngozi yake ya kahawia. Kifua chake kilikuwa wazi sehemu kubwa na kukifanya kivutie maradufu huku kichwani akiwa amevaa wigi la rangi nyeusi akizifunika nywele zake zisizoijua saluni kwa muda mrefu.
Ilikuwa wazi kwamba uzuri wake siku zote ulijificha kutokana na jinsi alivyokuwa akijiweka, lakini siku hiyo hata yeye mwenyewe alijishangaa na kujikubali kwamba wakiitwa warembo kumi hakika na yeye ataitika.
Njiani kila mtu alikuwa akimuangalia kwa mtazamo mpya. Yeye pia alionekana akiupenda sana muonekano huo. Akazidisha mikogo na kujifanya kama ameizoea hali hiyo japo moyoni alijaa aibu tele kwa ugeni wa kila alichokivaa siku hiyo.
Akiwa njiani alifungua kipochi chake na kutoa kioo kidogo akihakikisha poda na rangi aliyoipaka mdomoni imesambaa vizuri. Akajilazimisha kutabasamu ili kuondoa mikunjo yoyote ya huzuni kwenye uso wake japokuwa haikuwepo.
Akiwa anakaribia kona ya mwisho kutokea kwenye kibanda cha Dedan, Salima alibana kwenye kona na kuhema kwa nguvu. Akajipulizia marashi kwa mara ya mwisho. Akajitokeza na kuanza kutembea taratibu huku akiangalia ni wapi alipo Dedan ili amroge kwa muonekano wake alioenda nao siku hiyo.
Kwa mbali, alishangaa kuona kibanda kimezungukwa na watu wengi ambao bila shaka walikuwa wateja wa Dedan, kwani wengi huwa na mazoea ya kuacha simu na betri zao usiku mzima kwenye chaji kwa ahadi ya kwenda kuzichukua siku itakayofuata.
Salima alishangaa kuona mpaka saa nne, bado ofisi ya Dedan ilikuwa haijafunguliwa. Alihisi kuna walakini kwani kwa jinsi alivyomjua Dedan, hakuwahi kumwona hata siku moja akikosa kufungua ofisi yake mapema pasi na sababu maalumu.
“Pengine anaumwa!”alistaajabu Salima huku akiukaribia umati uliojaa nje ya duka la kijana huyo ili angalau ajue nini kilichokuwa kikiendelea.
“Huyu jamaa vipi leo? Kuna mtu anayepajua nyumbani kwake? Sisi tunachelewa kazi zetu bwana!” Hayo ndiyo maneno aliyosikia yakisemwa na watu walioshindwa kuvumilia huku wengine wakidiriki kuyapuuza mema yote waliyofanyiwa na Dedan kwa kumtuhumu huenda akawa amewatia changa la macho na kutoroka na fedha na simu zao.
Presha ikaanza kumpanda Salima. Akapitiliza bila hata kupiga hodi na kuingia moja kwa moja hadi ndani ya nyumba kubwa yenye vyumba vingi vilivyotenganishwa na varanda nyembamba.
Akahesabu vyumba kuanzia mkono wa kulia na kugonga mlango wa chumba cha tatu. Akagonga tena na tena bila mafanikio.
Hofu ikaanza kumpanda kadiri alivyokosa majibu ya hodi zake. Akachungulia kwenye kitasa akaona ufunguo ukiwa ndani ya kitundu cha mlango.
Je, Dedan amepatwa na nini?CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Akahisi huenda Dedan alijifungia kwa makusudi kabisa na pengine alikuwa amelala na mwanamke mwingine ndiyo maana alishindwa kumfungulia mlango. Hasira na wivu vilimjaa Salima, akaanza kujilaumu kwa kila kitu alichojisumbua kwa ajili ya Dedan kwa siku hiyo. Nguvu za miguu zilimuishia, akajikuta akikaa chini na kuuegemea mlango wa chumba cha Dedan akilia. Machozi yalimtoka mpaka yakamkauka kwa mapenzi yaliyozidi kipimo. Kwa mara ya kwanza katika maisha yake, akawa hajitambui kabisa. Akawa kama mtu aliyechizika, huku mapenzi yakiwa ndiyo sababu kubwa ya uchizi wake.
Akaona hapana, ni lazima ahakikishe ukweli wa kile alichokuwa akikiwaza. Akajibanza pembeni kwenye kona akitega sikio juu ya ubao wa mlango akikusudia kusikiliza kila tendo lililokuwa likifanyika mle chumbani.
Japokuwa kulikuwa kumetawala ukimya wa hali ya juu, lakini kwa upande wake alisikia sauti kubwa zikitoka chumbani tena kwa ufasaha kabisa. Aliisikia sauti ya huyo mwanamke aliyeamua kumpachika jina la malaya na ile ya Dedan zikisemezana kwa maneno ya faragha kana kwamba walikuwa kwenye mapenzi mazito sana. Kwa sikio lake alimsikia vyema huyo malaya akizungumza kwa lugha laini na kwa sauti ya kubana pua.
Wakati huo akili ya Salima ilikuwa ikimpeleka kama aliyokuwa akitaka mwenyewe, ilimtoa kutoka kwenye ulimwengu wa uhalisia na kumtupa sehemu mbali kabisa kwenye ulimwengu wa dhahania ambao laiti kama ungepewa jina ungeitwa Ulimwengu wa Watu Wenye Wivu wa Kipumbavu. Ulimwengu ambao wenye wivu usio na maana wote wangekutana huko na pengine kuanzisha serikali huku Salima akiwa rais wao. Akawa akiwaza kitu na mara moja kinakuwa kweli, sawa sawa na kuwaza bahari na ghafla mbele yako inatokea.
Macho ya Salima yakaanza kujaa ukungu huku machozi yakimlengalenga kwa hasira na wivu, ingawa hakuwa mpenzi wa Dedan rasmi, lakini aliumia sana. Alijihisi kama vile alikuwa akiibiwa mali yake. Siku zote alitamani kuwa mwenye haki juu ya mwili na akili ya Dedan na siyo mwanamke mwingine yeyote. Aliamini amezaliwa si kwa ajili ya mwanaume mwingine zaidi ya Dedan Magesa. Moyo wake ulikuwa huko na daima aliapa kulipigania penzi lake.
Alijikuta akiwaza mambo mengi ambayo kiukweli yote yalikuwa ya kuhisi tu na laiti kama angejua yaliyomkuta Dedan huko chumbani hakika nafsi yake ingemsuta kwa kumuhukumu kwa uongo bila kujua ukweli; na hata kama ingekuwa kweli kwamba Dedan alikuwa na mwanamke chumbani kwake, yeye Salima alikuwa ni nani mpaka aingilie maisha yake? Hakuwa mpenzi wake, wala rafiki yake. Alikuwa mteja wake tu hapo dukani, sasa kwa nini ajifanye anajali sana?
Alifikia kipindi akawa hawezi kabisa kuuzuia uchizi wake, akasimama na kurudi nyuma hatua kadhaa na kuurukia kwa nguvu mlango ambao tayari ulikuwa umeshaanza kuliwa na mchwa. Mlango ukajiachia kwa kukatika katikati huku vipande viwili vikining’inia kwenye bawabu,“ lolote na liwe,” aliwaza Salima.
Ilimchukua dakika kadhaa kuzinduka katika bumbuwazi alilokuwa nalo. Hakukuwa na huyo mwanamke malaya aliyekuwa akimuwaza wala hakukuwa na Dedan hapo kitandani, ila kuna kitu mfano wa mtu upande wa pili chini ya kitanda.
“Ni nini…Ah! Ni nani… Dedan! Dedan! Nini tena? We Dedan!” Salima alijikuta akipiga makelele yaliyochanganyika na kilio baada ya kumuona Dedan akiwa hajitambui huku akitokwa na mapovu mdomoni.
***
“Mimi ni Salima unanikumbuka?”
“Mmm...”
“Mimi ni mpenzi wako Salima, haunikumbuki?”
“Mmm…”
“Jana tu nilikukumbusha jina langu, kwa nini unanisahau jamani!”
“Mmm…”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kila alichokiongea alijibiwa: “Mmm…” Mpaka akachoka, akaamua kukaa kimya akimwangalia tu.
Hakuna rafiki wala ndugu yake hata mmoja aliyejua kama anaishi na mwanaume. Aliifanya siri kubwa moyo wake ukawa sanduku pekee la kuihifadhi.
Pamoja na furaha yake mpenzi wake hakuwa na uwezo wa kufanya kitu chochote. Siku nzima alishinda amekaa au amelala kitandani kama zezeta...
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment