Search This Blog

Thursday, 2 June 2022

SHETANI MSALABANI - 5

 







    Simulizi : Shetani Msalabani

    Sehemu Ya Tano (5)



    Ilipoishia



    Anaamua kumfuata Lightness nyumbani kwao ili amtambue! Kwani anadhamiria kupambana naye iwe kwa heri ama shari kutokana na kile anachojua ni ubazazi aliofanyiwa na rafiki yake Lightness ambaye tayari amegeuka kuwa adui.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Songa nayo sasa…





    Anatoka chumbani ili aondoke kwenda kwa adui yake. Anapofika sebuleni anakutana na sura ya Lightness ambaye anaingia sebuleni kwa rafiki yake akiwa na shauku ya kutaka kujua kile kinachoendelea ambacho anashindwa kuelewa kwanini rafiki yake kipenzi ambaye wameshibana ameamua kumficha mahusiano mapya jambo lililosababisha kupokea lawama toka kwa shemeji yake Bosco. Flaviana anashindwa kuzitawala hisia zake na kijikuta akimpokea Lightness kwa matusi na maneno makali ya kuumiza. Lightness anaduwaa bila kujua rafiki yake amepandwa na pepo wa aina gani!.



    ‘Mnafiki mkubwa we, unajifanya rafiki kumbe ‘snichi’. Leo utanitambua nakwambia’.

    Yalikuwa ni maneno ya Flaviana huku akiwa na hasira kama simba jike aliyejeruhiwa, anamfuata Lightness ‘amvagae’ kitendo kinachomfanya Lightness amuulize swahiba yake amepandwa na wazimu gani.



    Ugomvi mkubwa sana unazuka pale ndani huku matusi yakimfyatuka Flaviana bila kizuizi. Lightness anashushiwa kichapo kikali kinachomfanya aanze kulia huku akipiga mayowe kuomba msaada. Kipigo kinazidi, Lightness anashindwa kujizuia hivyo anaamua kutoka ‘nduki’ ili aepuke makonde mazito toka kwa bondia mpya wa uzito wa juu mwenye hasira za mbogo.



    Flaviana anammkimbiza Lightness ili ahakikishe anamshikisha adabu hadi amkome. Lightness hakumbuki kama alikuja na gari ila anachoona ni njia ya uchochoro yenye kona nyingi.



    Wakati riadha ile ya mbiyo ndefu ikiendelea, breki ya matusi kinywani mwa Flaviana ilikuwa imekatika, hivyo maneno yalitoka bila ‘gonga’. Tukio lile linashuhudiwa ‘laivu’ bila chenga na majirani pamoja na wapita njia ambao wanalipokea kwa hisia tofauti. Wengine wanaamua kuacha shughuli zao na kufuatilia mkasa huo ili waone mkanda mzima.



    Vita vile vya panzi ikawa sherehe kwa kunguru. Waandishi wa habari nao tayari wameshaanza kufanya yao bila makosa wakifuatilia na kuona jinsi jitihada za Flaviana kumtia mikononi adui yake zikikwama pale anapoteleza na kuangukia katika kidimbwi kidogo cha maji machafu. Flaviana anainuka kwa haraka na kukuta tayari adui yake alishatokomea.



    Kuangaza anakutana na umati wa watu wakishuhudia igizo hilo ambalo unaweza kuliita ‘komedi’ lakini utakuwa hujakosea kama ukiliita ‘tragedy’. Wakati huo wengine walijua Flaviana yuko kazini katika tasnia yake ya filamu, wakati wengine wakijua lile sio igizo bali ni shughuli pevu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Flaviana anajisikia vibaya kuuona umati wote ule ukimshuhudia kile anachofanya. Anaamua kuangaza huku na kule kama anaweza kuona ‘taxi’ ili apande kuepuka kuzongwa na mapaparazi pamoja na mashuhuda kibao jambo linalogonga mwamba kwani hakuna taxi maeneo yale. Anaamua kupanda bodaboda iliyokuwa jirani na kumuamuru dereva ampeleke kwake. Bila kupoteza muda dereva anaendesha kwa mwendo wa kasi hadi nyumbani kwa Flaviana huku akiacha watu wakimsindikiza kwa macho hadi anatokomea.



    Flaviana anafika kwake, anaingia ndani huku akihema kwa nguvu. Anapitiliza moja kwa moja chumbani ambapo anasimama mbele ya kioo. Anashangaa kuona jinsi ‘make~up’ ya tope ilivyokolea wakati akifanya zile ‘’aksheni’. Mbaya zaidi anagundua kuwa ‘kisketi’ chake kifupi alichokuwa amevaa kimechanika vibaya kiasi cha ‘kufuli’ kuonekana wazi~wazi. Anagundua kuwa amefanya kituko ambacho kimeharibu taswira ya maisha yake na kuleta tafsiri mbaya ambayo haitafutika akilini mwa watu. Anatamani angekuwa na uwezo wa kurudisha nyuma gurudumu la wakati ili asahihishe makosa aliyofanya, lakini anagundua kuwa hana nafasi hiyo.



    Anaamua kwenda bafuni kuoga, kisha anarudi chumbani. Anachukua simu yake ya mkononi na kupanda kitandani. Anafungua sehemu ya ujumbe mfupi wa maneno, anakutana na ujumbe toka kwa Bosco akimweleza kuwa anashukuru kwa maamuzi mapya aliyoamua kufanya, ya kuanzisha mahusiano na mwanaume mwingine. Anamtakia kila la kheri katika mahusiano yake mapya. Ujumbe ule unamuumiza sana moyo Flaviana kiasi cha kuanza kulia kwa huzuni huku akimpigia simu Bosco amweleze ukweli jambo linalokwama baada ya kupiga simu ya Bosco mara kadhaa bila kupokelewa. Mara simu yake inaita, anaangalia kutaka kujua kama ni Bosco ndiyo anapiga ile simu, kuangalia ile simu anaona ni namba asiyoifahamu. Anaacha kupokea kutokana na kutokuwa na furaha.



    Mawazo yanamwelemea kiasi cha kujikuta anapata maumivu makali ya kichwa. Anaangalia mahali ambapo huwa anaweka dawa, anachukua dawa za kutuliza maumivu na kumeza kisha anapanda kitandani ajaribu kama anaweza kubahatisha kupitiwa na usingilizi atulize akiili yake iliyovurugika. Licha ya kuhangaika kwa muda mrefu, usingizi unagoma jambo linalomkwaza mwanadada huyo na kusababisha atamani …kuleeewa…kuleeewaaa ili apunguze mawazo ila anaogopa kwani hajawahi kutumia pombe aina yoyote katika maisha yake. Anafikiria pia anaweza kunywa pombe na kulewa halafu akajikuta analeta ‘majanga’ yanayoweza kuongeza tatizo badala ya kuleta suluhu.



    Anaangalia saa yake kubwa ya ukutani iliyoko pale chumbani ili kujua muda. Saa inamuonesha ni saa kumi na mbili na dakika tano jioni. Anakumbuka kuwa hakula chochote zaidi ya kifungua kinywa alichopata asubuhi, japo hajisikii njaa wala hana hamu ya kula kitu chochote zaidi ya kuhisi kiu ya maji inayomfanya aamke kuyafuata maji ya kunywa yalipo na kuikata kiu yake na kurudi pale kitandani.

    Anawaza jinsi atakavyoweza kuipata faraja katika wakati ule ambao aliihitaji kuliko wakati mwingine wowote. Anaamua kuwasha redio na kuweka nyimbo ‘laini’ zinazomfanya aanze kumkumbuka mpenzi wake Bosco ambaye amekuwa mtu muhimu sana kwake katika kipindi chote tangu wamekuwa pamoja. Hafikirii kama itakuja kutokea siku moja wanaweza kutengana kutokana na jinsi ambavyo wamekuwa wakipendana.



    Anaamua kufungua sehemu ya barua pepe, anakutana na barua pepe aliyotumiwa na Bosco akieleza jinsi alivyohuzunishwa ha kitendo cha usaliti alioufanya Flaviana kwa kujiingiza katika mahusiano na mwanaume mwingine, ujumbe unaomfanya Flaviana atoe machozi kwa vile anavyohukumiwa kwa kosa ambalo hakufanya yeye. Anajibu ile barua pepe kwa kumweleza Bosco ukweli wote ili aweze kunusuru penzi lake ambalo linaonekana kuyumbishwa na dhoruba kali. Anamaliza kutuma ule ujumbe na kufungua mtandao wa twitter kisha anamtumia Bosco ujumbe kueleza masikitiko yake kwa tukio baya lililojitokeza ambalo limemchafua sana.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Anamaliza kumtumia ujumbe Bosco katika mtandao wa twitter kisha anaanza kusoma ujumbe aliowahi kumtumia Bosco katika ukurasa wake. Anasoma ujumbe mmoja baada ya mwingine, huku akitafakari maneno yale matamu ambayo Bosco alimwandikia. Anaendelea kupitia ujumbe ili angalau moyo wake upate kufarijika na maneno matamu ya upendo toka kwa Bosco ambayo. Anajua jinsi mpenzi wake anavyojua kutoa maneno ambayo yenye mvuto hasa pale anapoelezea mapenzi yao na kumsifia.



    Anafika katika ujumbe ambao ulitumwa takribani miezi miwili iliyopita ambao amekuwa akiusoma mara nyingi tangu ulipotumwa, kwani alikuwa akiusoma alimkumbuka sana Bosco na kumfanya azidi kutambua umuhiu wake maishani mwake.



    Anausoma ujumbe na kurudia mara kadhaa. Ujumbe unasomeka hivi;-











    Flaviana My love,

    You are so great. You are among those great women in the world.

    Nafasi yako ni kubwa hakuna wa kubeza. Utu wenye heshima, hekima na busara ni miongoni mwa sifa lukuki zinazokufanya kuwa mwanamama imara wa Kiafrika kama chuma cha pua!, ambapo siku zote umekuwa ukiueleza ulimwengu jinsi ya kupenda, tambua kuwa wewe ni kile kitu bora na cha thamani sana ambacho nilikusudia kutokukikosa maishani japo ni bahati kubwa, kwani wema na sifa zako zitanichukua maisha yangu yote kuuelezea ulimwengu unielewe ninachoelezea.



    Wakati huu ambao uko mbali nami, ukiwa maelfu ya maili toka hapa nilipo huku tukiwa tumetenganishwa na bahari, maziwa, milima, mabonde, tambarare na miamba, navuta taswira ya mke wangu mtarajiwa ambaye umekuwa TUNU maishani. Siwezi tu kueleza upweke uliopo moyoni mwangu kwa wakati huu bali pia jinsi gani inavyonigharimu missing the smell of your skin`………………………………



    Mbele yetu naona taswira kubwa sana ya maisha yetu ya siku za usoni na zijazo hapo baadaye sana, naamini hiyo ndiyo picha ya uhalisia wa maisha ambayo tunayahitaji na kuyaandaa. Nakuombea sana kwa Mwenyezi Mungu akusaidie uweze kujitinza hadi pale ahadi yetu itakapokamilika ili tufunge pingu za maisha, tukio takatifu litakaloleta furaha ya dhati katika maisha yetu na kufanya tushuhudie mibaraka ya pekee ambayo Mungu ameamua kutumiminia, na kuleta furaha sio kwetu tu, bali kwa jamaa, ndugu na marafiki na kutufanya tuwe wenye shukrani za dhati kwa hayo yote. By the way, nimekuandalia zawadi very special. Hii ni zawadi ya maisha ambayo pia itakuwa kumbukumbu ya milele milele na milele…...



    Tuzidi kumuomba Mungu azidi kutulinda na kututunza na azidi kutupatia hekima. Tambua NAKUPENDA MOYO WANGU, kamwe huwezi kutengana na mwili huu isipokuwa mauti pekee………………………………………………………………..



    ’Hope we are going to have another very happy moment in our live, even more than before.’

    JITUNZE.



    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ************

    Flaviana anamaliza kusoma maneno hayo yanayomchoma sana kutokana na kile anachokipitia kwa wakati ule kisha anafunga kompyuta yake. Anaangalia muda na kugundua kuwa muda umeenda na tofauti na alivyodhani. Saa inamuonesha kuwa sasa yapata saa tatu na nusu usiku. Anaamka na kuamua kumimina chai, anachukua na vipande vichache vya mkate kisha anakula na kukaa sebuleni kwaajili ya kuangalia filamu kama alivyozoea. Anaangalia filamu inafika katikati, filamu inakosa mvuto kwake kutokana na msongo alionao. Anazima televisheni na kwenda kulala.



    Anajikuta yuko juu ya kinara kirefu sana. Akiangalia chini anoana nyumba zinaonekana ndogo kutokana na umbali toka pale alipo hadi chini. Anashangaa na kujiuliza amefikaje pale. Akiangalia haoni ngazi ambayo anaweza kuitumia kushuka chini. Anajaribu kuangalia mbele, nyuma, kushoto, na kulia huenda atapata msaada lakini matumaini hayaonekani kwani anaona mawingu tu ambayo yako umbali wa sentimeta chache sana toka pale alipo.



    Wakati akitafakari bila kupata jibu, mbele yake anaona ndege ya abiria ikipita kwa mbali sana. Kwa umbali ule alijua hata angepaza sauti yake kuita aombe msaada wala sauti yake isingeweza kusikika. Anaamua kuita kwa nguvu japo anajua zoezi lake haliwezi kufanikiwa. Anasitisha zoezi la kuita pale anapoona ile ndege tayari imefika mbali sana na kutokomea machoni mwake. Anaanza kuangua kilio cha huzuni kubwa kinachodumu kwa muda mrefu.



    Baadaye ananyamaza na kufuta machozi kwa kutumia kiganja chake cha mkono na kuanza kutafakari maisha yake tangu alipokuwa na umri mdogo ambao tayari alikuwa anajitambua. Anakumbuka mambo mengi aliyojifunza toka kwa wazazi wake katika umri ule. Anakumbuka jinsi mama yake alivyokuwa akImweleza kuwa anapaswa kumwomba msaada Mwenyezi Mungu anapokuwa na tatizo ili Mwenyezi Mungu amsaidie. Anakumbuka pia jinsi walivyokuwa wakipata shida pale nyumbani, walimwomba Mungu akaonesha njia.



    Wazo linamjia amwombe Mungu ili amsaidie kwa njia ya kipekee huku akifikiria kuwa, Mwenyezi Mungu atatuma malaika waje wamshushe katika kinara kile. Kabla hajaomba wakati akifikiria jinsi Malaika watakavyokuja kumnyakua, anasikia muungurumo wa ndege. Sauti ya muungurumo ilikuwa inasikika kwa mbali lakini kadri muda unavyokwenda, ndivyo sauti hiyo ilivyosikika kwa karibu zaidi hatimaye inatokeza helikopta upande wa kushoto ikija pale alipo Flaviana. Tukio hilo linaleta matumaini makubwa sana kwa Flaviana ambaye anaanza kutabasamu huku akiishuhudia ile chopa jinsi inavyokaribia.



    Anaanza kupunga mikono ishara ya kuomba msaada baada ya kuona chopa hiyo imekaribia sana maeneo yale. Punde chopa inafika karibu kabisa, kutazama vizuri anamuona Bosco ndiye aliyekuwa rubani. Furaha isiyo kifani inamjaa moyoni mwake na kujiona yuko salama. Anaanza kuita kwa nguvu ;

    ‘Boscoo…. Boscoo, mpenzi wango Bosco’. Bosco anageuka kumwangalia Flaviana ambaye uso wake umejaa furaha.

    Furaha ya Flaviana inatoweka ghafla anaposhuhudia ille chopa ikimpita huku ikiongeza mwendo bila kuonesha dalili zozote za uokozi. Haamini kama Bosco anaweza kumpita hivihivi bila kumuokoa wakati akiwa amechoka na mwenye njaa bila matumaini yoyote.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Anaanza kulia huku akiitazama ile helikopta ikipotelea kwenye mawingu. Anaona haimpasi tena kuendelea kuishi kwani hana msaada. Alitegemea Bosco amsaidie lakini amemuacha solemba. ‘Yanipasa nini mimi kuendelea kuishi wakati niliyetegemea anisaidie amenicha….’ Ni manung’uniko ya Flaviana huku akilia kwa uchungu. Dakika ziliendelea kusonga, Flaviana bado anaendelea kulia na kuzidi kupoteza matumaini. Anaangalia chini anaona ni mbali sana, akiandalia juu anaona mbalamwezi na nyota ziking’aa. Akiangalia pande zote haoni msaada. Baridi kali inaanza, anakunja mikono yake na kujikunyata huku akitetemeka. Nguvu zinamwishia na hewa inakuwa nzito hivyo anapumua kwa taabu. Anajua tayari huo ndiyo mwisho wake umefika kwani anaona jinsi hali ile inavyomuelemea.



    Anajua kuwa hana dakika nyingi za kuendelea kuishi. Anatamani aache ujumbe lakini haoni sehemu ya kuuandika. Mara wazo linamjia aandike pale juu ya mnara ili hata kama akifa, ujumbe ule ubaki pale. Anajaribu kufikiria kitu cha kuandikia kwa dakika zile chache za maisha yake zilizobaki. Anachukua pini aliyokuwa nayo na kuamua kujitoboa ili damu itoke aitumie kuandika asije kuondoka duniani wakati bado hajaacha ujumbe ambao alikuwa anaukusudia kwa mpenzi wake Bosco.

    Damu hazitoki licha ya kujitoboa mara kadhaa. Anaamua kuikandamiza ile pini kwa nguvu pajani mwake huku akilia sana kwa maumivu makali anayoyapata. Anaichomoa pini na kuiichomeka tena katika paja lake kisha kuitoa tena. Anaina damu zinatoka kidogo sana jambo linalomfanya aamue kujikwaruza kwa nguvu huku akutoboa sehemu ilipo mishipa ya damu katika mkono wake wa kushoto. Awamu hii anafanikiwa, damu zinaanza kutoka kwa wingi. Anaanza kuchovya ile damu kwa kidole chake kisha anaanza kuandika ujumbe kwa shida sana huku hali yake ikiwa ni mbaya sana. Mara anashindwa kuendelea kupiga magoti wakati akiendelea kuandika ule ijumbe, anajikuta anaisiwa nguvu na kuanguka kifudifudi.



    Anajua tayari safari imewadia kwani tayari ameanza kuhisi hali ambayo siyo ya kawaida. Anajaribu kunyoosha mkono wake ili aendelee kuandika huku akiwa amelala pale chini, jitihada zinakwama. Ghafla kaupepo mwanana kanavuma hivyo kanampatia nguvu kidogo angalau za kujivuta. Anaanza kufanya jitihada za kunyanyuka ili angalau apate kukaa wakati akimalizia dakika zake za upendeleo alizopewa.



    Wakati akifanya zile jitihada za kujisgeza apate kujinyanyua pale chini, ghafla anafika sehemu iliyoinama na kuanza kubingilita akielekea kuanguka chini. Anafanya jitihada za kujizuia lakini inashindikana anajikuta akiwa hewani toka juu kwenye kinara kuitafuta ardhi. Hapati picha chini palivyo mbali aliposhuhudia wakati ule yuko pale juu ya kinara. Anajua anakufa kifo kibaya sana ambacho anaona hakikumstahili, aliona bora angefia pale juu ya kinnara kuliko kwenda kugawanyika kama glasi iliyopasuliwa sakafuni na kuvunjika vipande vipande.



    Anaamua kusali dua ya mwisho, ili ikiwezekana basi Malaika waje kumdaka na kama itashindikana ikiwa malaika wako mbali sana, basi Mwenyezi Mungu amsamehe dhambi zake na kumuweka mahali pema peponi. Anaposema amina, anajikuta ametua kwenye turubai kubwa ambalo lilikuwa limekingwa ili asianguke chini. Haamini macho yake kujiona yuko salama. Anaamka na kuangaza anaona watu wengi washika pembeni mwa lile turubai. Wale watu wanashusha lile turubai, mmoja anamkaribia na kumshika mkono akinyanyua. Kuinua macho yake anamwona ni mpenzi wake Bosco. Anaanza kulia kilio cha furaha huku haamini yale yote yaliyomkuta. Bosco anamfuta machozi kisha anambeba kumpeleka nyumbani. Wakati Bosco amembeba akiwa njiani kuelekea nyumbani, ghafla anateleza wanaanguka chini kama magunia ya mihogo. Anapotua pale chini, Flaviana anashtuka na kugundua alikuwa anaota.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Usingizi unapaa kwa muda mrefu. Akipata usingizi unakuwa wa mang’amung’amu. Hali hiyo inaendelea kusumbua sana usiku ule hadi inafika mida ya asubuhi kunapambazuka. Anaamka akiwa na njaa kuliko kawaida. Anaandaa kifungua kinywa na kuketi mezani kuanza kula. Wakati akiendelea kula, anasikia mlango wa sebuleni ukigongwa, anaingia Lightness, akifuatiwa na Zawadi pamoja na watu wengine wawili mmoja amevaa sare za jeshi la polisi wakati mwingine za kawaida. Wanajitambulisha wale watu wawili kuwa ni maafisa wa jeshi la polisi na kueleza kilichowaleta ni kumchukua ili aende kituo cha polisi cha kati kwa ajili ya kutoa maelezo kuhusiana na tukio la kumshambulia Lightness alilolifanya.



    Anaongozana nao hadi kituo cha polisi ambako ‘anatupwa ndani’ kwa kosa la kumtishia maisha Lightness na kumshambulia kwa kumpiga na kumtukana. Habari zinazagaa kuhusiana na tukio la Flaviana kuswekwa ‘lupango’ kiasi cha kutawala vichwa vya habari katika vyombo mbalimbali vya habari.



    Machallo anapata habari kuwa Flaviana yuko kituo cha polisi. Anavaa vizuri kuhakikisha amependeza, kisha anaamua kwenda kituoni kumuona huyo mpenzi wake wa kughushi. Kwakuwa tayari anajua ameshakuwa maarufu, anaona hapaswi kupanda matatu, wala bodaboda. Anaamua kwenda kukodi gari katika kampuni ambalo hukodisha magari. Anakodi gari aina ya lexus na kuanza safari hadi kutuoni ambako anafikia kudakwa na mapaparazi ambao wanamhoji kuhusiana ma mahusiano yake na mwanadada Flaviana. Anajifanya kama hataki kuongea lakini mwishowe anaamua kufunguka. ‘Nimekuja kumwona mpenzi wangu na kufanya taratibu za kumwekea dhamana’ anaeleza Machallo wakati kamera za waandishi wa wa habari zikimulika tukio na vinasa sautii vikiwa vimewekwa sambamba na mdomo wa Machallo.



    Maswali yanaulizwa na mapaparazi hao kuhusiana na mahusiano ya wawili hao ambayo yaliwekwa wazi na Flaviana, pia wanamuuliza kuhusiana na sekeseke lililotokea kati ya Flaviana na rafiki yake Lightness.

    ‘Inasemekana, ugomvi kati ya Flaviana na Lightness ulisababishwa na kitendo cha wewe kuwa na uhusiano na Lightness huku mkimzunguka Flaviana, unalisemeaje hili?’ anauliza mmoja wa mapaparazi huku akisogeza kinasa sauti jirani na mdomo wa Machallo.



    ************

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    :: Je nini kitaendelea hapo? nini hatma ya Machallo?





    :: Safari ndio kwanza imeanza, hapo ndipo utajua maana ya ‘SHETANI MSALABANI’ hakika si ya kukosa endelea kufuatilia kujua.



    MWISHO

0 comments:

Post a Comment

Blog