Search This Blog

Thursday, 2 June 2022

SHETANI MSALABANI - 4

 







    Simulizi : Shetani Msalabani

    Sehemu Ya Nne (4)



    Ilipoishia



    Napenda niweke bayana jambo ambalo limekuwa likinitesa kwa muda mrefu sasa’ Anamweleza Flaviana.

    ‘Eleza nakusikiliza’ ni sauti ya Flaviana baada ya kuona ukimya kidogo.



    Songa nayo sasa…





    ‘Nimekuwa nikifikiria kuwa na mpenzi mwenye sifa na vigezo stahiki ninazohitaji nikagundua kuwa wewe ndiye mwanamke wa pekee ambaye unakidhi vigezo hivyo. Naomba nafasi ndani ya moyo wako nikuoneshe penzi la dhati nililonalo’ anaongea Machallo kwa hisia kali huku akimwangalia Flaviana machoni. Flaviana anabaki kimya, akiwa anayaangalia macho ya Machallo ambayo yanamshuhudia mateso anayoyapata Machallo kumkosa mtu muhimu maishani mwake.



    Machallo anaendelea kumweleza Flaviana kuwa, lengo lake sio kumchezea wala kumpotezea muda. ‘napenda tujenge penzi bora, tuwe vielelezo ili ulimwengu ushuhudie tukio hili takatifu ambalo litaleta amani, furaha na upendo mioyoni mwetu kwa kipindi chote kiliichobaki cha maisha yetu pindi tutakapokuwa pamoja’ anahitimisha Machallo.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ‘Nimekuelewa Machallo. Naheshimu sana hisia zako, napenda nikueleze ukweli ambao utakuweka huru. Tayari nina mpenzi, nampenda sio taratibu na tayari nimeshampa roho yangu, ninaishi ndani yake naye anaishi ndani yangu hivyo nafasi ni moja, wala sina nyingine’. Anaeleza Flaviana huku akiendelea na zoezi la kuchagua mahitaji.



    Kauli ile inaupasua moyo wa Machallo, anajiona ‘amepoteza’. Japo anajifariji kuwa ana nafasi ya mwisho kujaribu bahati yake. Anambembeleza Flaviana ampe nafasi moyoni mwake, jitihada zinazogonga mwamba kwa kukutana na msimamo wa Flaviana asiyetaka kuyumbishwa katika penzi lake kwa mtu anayempenda.



    ‘Naomba nafasi niwe rafiki yako, unijue mimi ni mtu wa namna gani na nia yangu kwako. Pengine inaweza kusaidia kubadili maamuzi na kukusaidia kukupeleka katika chaguo bora zaidi’. Anasema Machallo zikiwa ni jitihada zake za mwisho.



    Ombi lake linasubirishwa, kwani Flaviana ameshaanza maongezi, akiwasiliana na mtu kwa simu huku zoezi lake la kuchagua mahitaji likiendelea. Alikuwa akichagua mahitaji kwa mkono mmoja huku mwingine umeshika simu aliyoweka sikioni huku kuwasiliana na mtu. Mahitaji aliyohitaji alikuwa akiweka katika kitoroli ambacho Machallo alijikuta akimsaidia kukisukuma huku akimfuata kule anakoelekea kama ‘bodu gurd’. Flaviana anamaliza kuchagua mahitaji , anaelekea sehemu ya kufanya malipo iliyoko jirani na mlango wa kutokea huku machallo akimfuata nyuma na toroli lenye mahitaji aliyochukua.



    Flaviana anatoa kadi na kuichanja katika mashine maalumu iliyopo pale ili kufanya malipo kisha anapewa risiti. Baada ya kukamilisha, anatoka nje kuelekea kwenye gari alilopaki nje ya ‘supermarket’ wakati mtu maalumu kwa kusaidia wateja kubeba mizigo anampokea Machallo toroli, anaipanga mizigo vizuri katika boksi na kuipeleka kwenye gari, Flaviana anafungua ‘buti’ yule kaka anauweka mzigo kwenye buti kisha anafunga ule mlango wa buti.



    Wakati huo Machallo amesimama hapo pembeni akishuhudia kinachoendelea huku shauku yake kubwa ikiwa ni kuona Flaviana anamaliza kuongea kwa simu ili asikie jibu la ombi lake. Anahamaki na kubaki mdomo wazi pale anaposhuhudia Flaviana anaingia kwenye gari, na kumpungia mkono ishara ya kumwambia kwaheri kisha anawasha gari na kuendesha akiwa ameshika usukani kwa mkono mmoja wakati mkono mwingine ukiwa umeshika simu ambayo ilikuwa bado iko sikioni akiendelea na mazungumzo na mtu.



    Maumivu makali ya moyo yanamtesa Machallo, anaamua kuondoka pale kuelekea katika kituo zinapopaki bodaboda. Anakodi kupelekwa nyumbani, akiwa mnyonge mwenye mawazo mengi. Anaona tayari ndoto yake imekufa, wala hana nafasi tena ya kuishi aina ya maisha ya ndoto yake ambayo imejengeka akilini mwake kwa muda mrefu. Anapatwa wazo, afikirie namna nyingine inayoweza kumpa umaarufu.



    Siku zinaenda bado jawabu halijapatikana. Mitihani nayo inaanza, anakuwa bize na masomo na kushindwa kujua njia sahihi atayomfanya akamilishe ndoto yake kwa wakati ule.





    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Ni semista ya pili katika ule mwaka wa pili wa masomo pale chuo. Ofisi ya Machallo inazidi kupata umaarufu kwa kazi nzuri zinazofanyika. Wanachuo, wahadhiri na watu wengine hupenda kupeleka kazi zao pale ofisini ili zifanyike. Kazi zilifanywa kwa uaminifu na kwa wakati uliopangwa bila usumbufu.



    Inafika siku ya ijumaa, mida ya mchana, Babuu yuko bize sana pale ofisini. Anakuja mteja, mwanadada, anatoa compyuta mpakato yake na kuelezea tatizo ili irekebishwe.



    Babuu anatoa daftari maalumu kwa ajili ya wateja ambao huandika taarifa zao wanapoleta kazi zifanywe pale ofisini. Anamaliza na kumweleza kiasi cha pesa ambacho atalipia, yule dada analipa kiasi kile cha pesa na kuuliza muda ambao kazi itakuwa imekamilika. ‘Uje kesho mida ya saa nne asubuhi itakuwa tayari’ anamjibu Babuu.



    Dada anaondoka zake, Babuu anaendelea na kazi aliyokuwa anaifanya. Baada ya kumaliza ile kazi aliyokuwa akiifanya anagundua tayari muda ulikuwa umeenda sana zikiwa zimebaki dakika chache ufike muda wa kufunga ofisi hivyo anaamua kuondoka na ile kompyuta aliyoleta yule dada ili akifika nyumbani apate nafasi ya kuifanyia matengenezo.



    Muda wa kufunga unafika, anafunga na kuondoka. Anafika nyumbani, baada ya kupumzika na kupata chakula cha usiku anaamua kuianza kazi ya kuitengeneza ile kompyuta ya mteja ili siku inayofuata apate nafasi ya kufanya kazi zingine na pindi yule dada akifika akute iko tayari kwa wakati waliokubaliana.



    Anaifungua ile kompyuta na kuiwasha. Anaona picha ya Flaviana mwanadada ambaye anausumbua sana moyo wa kaka yake. Anafungua mafaili yaliyomo mle ndani anaona yanamhusu Flaviana. Anakuta picha za Flaviana pamoja na mambo mengi yanayomhusu mwanadada huyo.



    ‘Hii laptop itakuwa ya Flaviana bila shaka’ anajisemea. Kabla hajaanza zoezi la kuitengeneza ile kompyuta, anamwita kaka yake ambaye yuko chumbani kisha anamweleza kuwa anahisi ile kompyuta ni mali ya Flaviana kutokana na mambo aliyoyaona mule ndani yanamuhusu Flaviana. Machallo anaangalia ili kujiridhisha kama anachoambiwa kina ukweli au Babuu ameamua kumtania kwa kujua anampenda Flaviana. Anagundua kuwa ni kweli, ile kompyuta itakuwa mali ya mwanadada huyo bila shaka.



    Anaona mambo mengi yanayomhusu Flaviana na maisha yake kwa ujumla, familia, chuo, Marafiki pamoja na tasnia za Mitindo, filamu na urembo. Anaziona filamu anazozipenda Flaviana ambazo amezihifadhi pamoja na zile alizowahi kuigiza.

    Anachukua ‘external hard disk’ yake na kuhamishia baadhi ya vitu toka katika kompyuta ya Flaviana. Zoezi linakamilika kisha anachukua ‘moderm’ na kutumia kompyuta ya Flaviana kuingia kwenye huduma ya mtandao wa intaneti.



    Anaona orodha ya wavuti mbalimbali alizotembelea Flaviana. Anafungua sehemu ya barua pepe na kugundua ilikuwa iko wazi. Anasoma barua pepe za Flaviana, anasoma barua pepe ambazo ametuma mpenzi wake Flaviana pamoja na picha. Katika kuendelea kupekua, anaiona barua pepe ambayo alimtumia Flaviana kama majuma mawili yaliyopita.



    Wakati akiendelea kusoma barua pepe moja baada ya nyingine, anakutana na barua pepe inayomfanya ashindwe kuzuia hisia zake. ‘Enheeee….!!!’ Anaonesha kufurahishwa na kile anachokiona. Anachukua kalamu na karatasi kisha ananakiri kitu toka katika ile barua pepe anayosoma. ‘nini hicho kaka?’ anauliza Babuu kwa shauku ya kutaka kujua.

    Machallo anamweleza kuwa ameliona neno la siri la wavuti ya Flaviana toka kwenye ile barua pepe, lililotumwa wakati Flaviana alipokuwa akibadili neno la siri.



    Machallo anamweleza Babuu kuwa, amedhamiria kumpata Flaviana. Hivyo alipanga atumie kila njia ili ampate kwakuwa jitihada nyingi zilifanyika bila kuzaa matunda, aliona ile ni fursa nyingine ambayo inaweza kuleta matokeo chanya kama akiitumia kikamilifu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Anamshauri mdogo wake amsaidie ili atume ‘post’ kwenye wavuti ya Flaviana kuelezea kuwa wao ni wapenzi. Babuu anashauri bora wabadili neno la siri ili Flaviana asiweze kuingia tena katika ile wavuti.

    Babuu anaingia katika wavuti, anaenda sehemu ya kubadili neno la siri, anaweka neno la siri la awali kisha anaweka neno la siri jipya na kuthibitisha. Neno la siri linatumwa katika anwani ya barua pepe ya Flaviana. Anafungua kisha anaifuta hiyo barua pepe yenye neno jipya la siri katika kikasha cha ujumbe ili Flaviana asiweze kuisoma na kulipata neno la siri jipya.



    ************





    Machallo anamwambia mdogo wake achukue picha ya Flaviana katika kompyuta ya Flaviana aunganishe na picha yake (Machallo) kwenye kompyuta yake kwa kutumia majo ya ‘program’ ya kompyuta mahususi kwa ajili ya kazi hiyo ili ionekane kama wamepiga hiyo picha pamoja. Babuu anafanya zoezi hilo huku Machallo anabuni maneno ya kuandika watakayoyatuma kwenye wavuti hiyo. Baada ya muda mfupi Babuu anamaliza kazi wakati ambao Machallo anamaliza kazi yake pia.



    Machallo anachukua kompyuta mpakato yake, anahakikisha ile picha imehifadhiwa tayari kwenye kompyuta hiyo kisha anaingia nayo chumbani wakati akimwacha Babuu akianza zoezi la kuitengeneza kompyuta ya Flaviana. Machallo anafika chumbani na kukaa kitandani huku akiiweka kompyuta yake tayari kwa zoezi lake. Anaingia katika mtandao wa intaneti, anaingia kwenye wavuti ya Flaviana na kuiweka ile picha na yale maneno aliyobuni.



    Anajua sasa adhma yake inaenda kutimia kufuatia tukio hilo litakaloleta taswira mpya katika maisha yake. Anamaliza kutuma kisha anayapitia yale maneno aliyobuni na kuyaweka katika mtandao kwa mara nyingine;



    “Halloo Dunia..,

    Leo nafungua ukurasa mpya ambao unaleta taswira mpya katika maisha yangu.



    Napenda kuweka wazi tukio hili maalumu ambalo linagusa maisha yangu na kuyafanya yawe na maana sana kwa wakati huu kuliko kipindi kingine chochote cha maisha yangu.



    Namtambulisha kwenu Machallo Mussa (niliyepiga naye picha hapo juu) kuwa ndiye chaguo la moyo wangu.

    Ni tukio ambalo pengine, linaweza kuchukuliwa kwa hisia tofauti ila ninachojua kwa sasa, kuna kitu special ninachopata toka kwake ambacho sitarajii kukikosa katika kipindi chchote cha maisha yangu.



    Najiona nimekamilika sasa, maisha yamekuwa na maana zaidi ya vile ninavyoweza kueleza. Naahidi kumpenda leo, kesho na hata milele.



    Mwenyezi Mungu bariki PENZI hili linalomea katika mioyo yenye rutuba”.





    Ni usiku wa manane, macho ya Machallo ni makavu. Hana hata chembe ya usingizi, anawaza jinsi tukio hili litakavyo leta taswira mpya. Anawaza umaarufu ambao unaenda kupatikana kupitia njia ya panya aliyoigundua ili azima yake ipate kutimia. Tafakuli zinafikia ukingoni pale anapoianza ku~abiri kuelekea katika bandari ya asubuhi njema.



    Asubuhi kunapambazuka, siku mpya ya jumamosi. Babuu anakuwa wakwanza kuamka kabla ya Machallo, anaanza kufanya maandalizi kuelekea kazini zoezi linaloendelea hadi majira ya saa mbili asubuhi. Machallo bado amelala, Babuu anaamua kumwamsha ili amuage tayari kwa kuondoka.

    Baada ya Babuu kumuaga Kaka yake anaamua kuondoka kuelekea kazini aweze kufungua ofisi tayari kuanza kazi huku nyuma akiwa amemuacha Machallo bado anaendelea kulala kutokana na usingizi mwingi.

    Simu ya Machallo inaita mara kadhaa lakini kutokana na usingizi alionao anashindwa kuisikia.



    Ni majira ya saa nne na dakika ishirini na mbili asubuhi, Machallo anaamka, anajinyoosha na kufikicha macho yake huku anapiga miayo!. Anatandika kitanda na kwenda ‘uani’ kupunguza maji mwilini. Baada ya muda mfupi anarudi chumbani. Anaanza kufanya usafi wa jumla kama ilivyo desturi yake katika siku za jumamosi. Mara simu yake inaita, kuangalia ni namba ya Babuu. ‘Nambie dogo’ anaiipokea ile simu, na kuelezwa kuwa afungue redio Vibes Fm kuna habari inarushwa hewani mida ile ataisikia.

    Anafungua redio na kukuta habari inaisha. Anagundua ni habari ya mahusiano yake na Flaviana aliyoandika kwenye mtandao.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Anafungua kituo kingine maaruufu kinachorusha matangazo yake toka jijini Mwanza na kusikika Tanzania pamoja na nchi jirani. Kipindi ni dondoo za magazeti na Mitandao. Anasikia muhtasari wa habari zitakazosomwa, miongoni mwa habari hizo anasikia habari ya Flaviana kufunguka juu ya mahusiano yake na mpenzi wake wa sasa, aliyoituma katika wavuti yake.



    Habari ile inamdhihirishia Machallo kuwa amefanya kazi nzuri ambayo itakamilisha kusudi lake kubwa la kuwa mtu maarufu kwa kupata nafasi kuandikwa katika mitandao na kuonekana katika televisheni pamoja na vyombo vingine vya habari.





    Anafungua mtandao wa facebook kupiitia simu yake ya mkononi ambako aliweka ile picha yake akiwa na Flaviana katika ukurasa wake na kuandika maneno yanayoonesha kuwa wawili hao ni wapenzi. Anakuta ‘comments’ nyingi pamoja na ‘likes’ pia wengine wame ‘share’. Ni habari ambayo imegusa sana hisia za watu, kila mmoja alisema alilojisikia kusema.



    Wakati akifanya zoezi la kufungua intaneti alikuwa akiendelea kuitegea sikio ile habari iliyokuwa ikitangazwa redioni. Mtangazaji akabainisha kuwa amejaribu kupiga simu ya Flaviana ili aweze kufanya naye mahojianao kidogo kwa njia ya simu aelezee kuhusiana na tukio hilo bila kupokelewa. Habari anaisha, anaendelea na shughuli za usafi ambazo alikuwa amekatisha kwa muda wakati akisikiliza ile habari.











    Ikiwa ni mida ya saa sita mchana Babuu akiwa ofisini akiendelea na kazi, anafika yule dada aliyeacha kompyuta yake siku iliyopita.

    ‘kaka mambo?’ anamsalimia Babuu.

    ‘poa dada, mzima? Anajibu Babuu na kutaka kumjulia hali.

    ‘sijambo’ anaitikia yule dada. Babuu anaitoa ile kompyuta kisha anampa yule dada, ambaye anaikagua na kugundua imesha tengemaa. Anairudishia katika begi kisha anaanza kuondoka ‘asante’ anashukuru huku akiondoka.

    ‘karibu tena’ anajibu Babuu.



    Yule dada anaingia katika gari yake aliyokuwa amepaki pale pembeni, anachukua simu yake ya kiganjani na kubofya akitafuta namba ya simu ya rafiki yake Flaviana. Anaipata na kupiga ambapo simu inaita bila kupokelewa.



    Anaamua kwenda nyumbani kwake ambako anaamini atamkuta. Anaendesha gari kwa muda wa robo saa tayari anafika nyumbani kwa Flaviana.`

    ‘Wooow! Lightness…karibu mpenzi’ ni sauti ya Flaviana akimkaribisha rafiki yake ndani.

    ‘yaelekea umetoka kuamka muda simrefu’ anauliza Lightness.

    ‘jana nilichelewa kulala baada ya kutoka kushoot ile movie, nikaanza kuangalia movie mpya iliyotoka’. Anajibu Flaviana.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Lightness anamkabidhi rafiki yake ile kompyuta.

    ‘asante mwaya’ nataka niingie kwenye mtandao ili nipost trailer ya filamu mpya iliyotoka’ ni maneno ya Flaviana akimwambia Lightness.



    Wanaendelea na mazungumzo, baada ya muda mfupi simu ya Lightness inaita. Ni dada yake amempigia akimtaka arudi nyumbani mara moja kuna dharula imejitokeza bila kumwambia suala lenyewe. Anamuaga Lightness na kumuahidi atarudi baadaye akipata nafasi.



    Wakati yuko kwenye gari kuelekea nyumbani, simu yake inaita. Ni Bosco, mpenzi wake Flaviana.

    ‘hallo shem’ anaitikia Lightness.

    ‘mbona Flaviana hapokei simu yangu?’ anauliza Bosco kwa ukali. Lightness anahisi kitendo cha kutokupokea simu alichokifanya Flaviana kimemkwaza Bosco, japo anajua kuwa Flaviana hawezi kuacha kupokea simu ya kipenzi chake. Anamwambia huenda Flaviana alikuwa bafuni anaoga wakati Bosco akimpigia simu, sababu ambayo haimwingii akilini Bosco.

    ‘Wewe na huyo msaliti mwenzio lenu moja’ anafoka Bosco.

    ‘Mbona sikuelewi shem?’ anauliza Lightness kwa mshangao.

    ‘sawa jifanye hunielewi, ila mwambie huyo shetani wa kike nashukuru sana kwa alichonifanyia’ anahitimisha Bosco na kukata simu.



    Lightness anajiuliza maswali mengi bila majibu. Anashangaa shemeji yake kumtolea maneno makali vile bila kuelewa sababu. Furaha inakwenda likizo, anajikuta mwenya huzuni mithili ya mtu ‘aliyetendwa’.



    Anafika nyumbani.

    ‘una tatizo gani mamii?’ Anauliza Zawadi, dada yake Lightness alipomwona Laghtness anaingia sebuleni akiwa hana furaha. Lightness anakuwa kimya huku akipitiliza chumbani kwake. Zawadi anahisi huenda kitendo cha kumwita Lightness arudi nyumbani wakati akiwa na mambo yake kimemkwaza. Anaamua kumuacha kwa muda ili baadaye kidogo aende kuongea naye, kwani anampenda sana mdogo wake na hapendi kumkwaza wala kumwona akiwa katika hali ya huzuni. Alipenda kumfanya mdogo wake mwenye furaha na amani muda wote kwani amemlea tangu mdogo tangu wazazi wao walipofariki.



    Lightness anafika chumbani na kujitupa kitandani huku ana msongo wa mawazo. Anaamua kumpigia simu rafiki yake Flaviana ili amuulize kama kuna tatizo kati yake na Bosco na amwambie kile kilichojiri, jambo linalokwama baada ya simu ya Flaviana kutopokelewa.

    Wakati akitafakari, simu yake inaita. Anaangalia namba inaonekana ni namba asiyoifahamu. Anapokea na kusikia sauti ya mtu aliyejitambulisha kwa jina la Madadi akijitambulisha kuwa ni mwandishi wa habari katika gazeti la kila siku la ‘mwanahabari; akimtaka kufahamu kuhusiana na tukio jipya linaloendelea la mahusiano mapya kati ya rafiki yake Kipenzi Flaviana na mpenzi wake wa sasa.

    ‘sielewi unachoniuliza’ anajibu Lightness kwa jazba huku akikata simu.



    Zawadi anaingia chumbani kwa Lightness, anamkuta akiwa bado katika hali ya huzuni.

    ‘Naomba unisamehe mdogo wangu, sikujua kama nIngekukwaza kukuita wakati una mambo yako ya msingi’ ni maneno ya Zawadi akiomba radhi kwa mdogo wake huku akipaza sauti ya upole. ‘Hapana dada, siyo hilo. Kuna jambo jingine…’ anajibu Lightness. ‘lipi hilo?’ anauliza Zawadi akitaka kujua.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Lightness anamweleza dada yake jinsi alivyoambiwa maneno ya utata toka kwa Bosco akimshutumu kwa mambo asiyoyajua.

    ‘Kwani hujuwi chochote kuhusiana na suala la usaliti alioufanya rafiki yako kwa Bosco?’ anauliza Zawadi .

    ‘Sijuwi, ila sidhani kama kuna jambo Flaviana anaweza kunificha’ anafafanua Lightness.



    Zawadi anamfungulia Lightness wavuti, anaangalia na kusoma zile habari ambazo zinamshitua Lightness.

    ‘Mbona Flaviana hajawahi kunidokeza kuhusiana na suala hili?’ anauliza Lightness kwa mshangao. Zawadi anamuuliza Lightness kama anamfahamu huyo mpenzi mpya wa Flaviana, anakiri kuwa hadhani kama alishawahi hata kumwona.

    Kutokana na kumbukumbu kufutika kama alishawahi kukutana naye, kwani kwa kawaida hukutana na watu wengi sana hivyo inamuwia vigumu kuwakumbuka wote.



    Hali ya sitofahamu inaendelea kumkumba Lightness ambaye anashindwa kuelewa kwanini rafiki yake amekuwa msiri kwake kiasi kile kwa jambo lile wakati huwa wanawekana wazi kwa kila kitu.









    Flaviana anafungua tovuti yake, anakutana na kitu kipya ambacho kimepokelewa kwa ‘comments’ nyingi kuliko kitu chochote alichowahi kuandika tangu afungue tovuti ile.



    Anaisoma ile habari na kujikuta akipiga mayowe bila kujizuia asiamini kile anachoona katika mtandao wake. Anaangalia simu yake pale alipokaa anaikosa, anaangalia kabatini bila mafanikio. Anachukua mkoba wake kuangalia, anaiona. Anaona ‘missed calls’ nyingi pamoja na ujumbe mfupi wa maneno. Anaamua kumpigia simu Lightness kwanza kabla hajaangalia missed calls na kusoma ujumbe mfupi wa maneno. Simu ya Lightness inaita bila kupokelewa kwani alikuwa ameingia ‘uani’ hivyo simu aliiacha kitandani pale chumbani.



    ‘Anajua upuuzi alioufanya ndiyo maana hataki kupokea simu yangu, atanitambua leo’. Anajisemea Flaviana huku akikaa kwa ajili ya kuingia kwenye mtandao kwa ajili ya kufanya jitihada za kufuta ile habari ambayo anaona sio kwamba imemfedhehesha tu, bali imemchafua vilivyo.

    Anaingiza neno la siri, anaona ujumbe ukieleza kuwa amekosea neno la siri. Anaamua kuingiza neno la siri kwa mara nyingine, matokeo anayopata ni yaleyale jambo linalomshangaza na kumfanya asielewe kile kinachoendelea.

    Anaamua kuingiza neno la siri alilokuwa akitumia awali kabla hajabadilisha lakini bado anagonga mwamba. Anagundua kuwa kuna mchezo mchafu uliofanywa na rafiki yake Lightness.



    Hasira na chuki juu ya Lightness vinampanda Flaviana kiasi cha kulia mithili ya mfiwa. Anaamua kumfuata Lightness nyumbani kwao ili amtambue! Kwani anadhamiria kupambana naye iwe kwa heri ama shari kutokana na kile anachojua ni ubazazi aliofanyiwa na rafiki yake Lightness ambaye tayari amegeuka kuwa adui.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    ************

    :: Machallo atafanyaje kukabiliana na mchezo aliokwishaufanya?? nini hatma yake baada ya kutafuta umaarufu kwa njia ya mkato?? Atajulikana kama yeye ndio aliofanya hivyo??

0 comments:

Post a Comment

Blog