Search This Blog

Thursday, 2 June 2022

SHETANI MSALABANI - 3

 







    Simulizi : Shetani Msalabani

    Sehemu Ya Tatu (3)



    Ilipoishia



    Machallo anashukuru kwa ukubali ule, anakaa huku akitafakari wakati mgumu alionao kueleza hisia zake kwa yule mwanadada. Alijua kitendo kile kilihitaji ujasiri wa hali ya juu. Anajua kuwa hakuna jambo lingine



    Songa nayo sasa…





    Japo anavaa moyo wa ujasiri, tayari ameshasahau maneno yote aliyopangilia kumwambia mwanadada yule ambayo amekuwa akiyarudiarudia kwa wakati Fulani ili yamkae vizuri akilini kwani aliamini yalikuwa ni silaha tosha ya kufanya mashambulizi ya hatari ambayo yangemletea ushindi kwa asilimia zaidi ya tisini na tisa nukta tisa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ‘Flaviana’ Machallo anamwita yule mrembo jina.

    ‘Aabe!’ anaitika Flaviana huku akimtazama na kumkazia macho tayari kwa kusikiliza kile Machallo anachotaka kumwelezea.

    ‘Naitwa Machallo, ni mfuatiliaji mzuri sana wa filamu zako. Hakika unajua kukitendea haki kipaji ulichopewa’ ni maneno toka kwa Machallo.

    ‘Nafurahi kukufahamu Machello’ anajibu Flaviana.

    ‘ni Machallo sio Machello’ anamsahihisha Machallo.

    ‘Nashukuru kukufahamu Machallo, pia asante kwa kufuatilia kazi zangu. Mi naamini bila wewe mimi sio kitu’ anaendelea kuelezea zaidi Flaviana kuwa anaamini kipaji cha uigizaji alipewa na Mungu ili aweze kugusa maisha ya watu wengi.

    Furaha yake kubwa siyo mafanikio makubwa ya kiuchumi aliyoyapata na anayoendelea kuyapata katika tasnia ya filamu, bali ni aina ya mtu anayetaka kuwa na jinsi anavyogusa maisha ya watu kwa namna tofauti.

    Machallo anagundua kuwa Flaviana ni mtu wa watu, anawathamini sana watu wanaothamini kile anachofanya. Jambo kubwa linalomfurahisha ni ule ukarimu na uchangamfu ambao ameuonesha Flaviana tofauti na mawazo yake yalivyompelekea awali kulingana na hadhi na mafanikio aliyonayo Flaviana.

    Wakati wakiongea maongezi ya hapa na pale, kabla Machallo hajafunguka, anakuja mwanadada mrembo ambaye sio mgeni sana machoni mwa Machallo kwa jinsi anavyomtazama na kuvuta kumbukumbu. Anafika pale walipokaa, anampatia Flaviana ufunguo wa gari na kumweleza kuwa amesumbuka kidogo kupata sehemu nzuri ya kupaki gari ndiyo maana amechelewa kufika tangu Flaviana alipomwacha ‘garini’.

    Anakaa na kumsalimia Machallo, bila kumfahamu huku akiwa na shauku kutaka kumfahamu. Kabla hajauliza, Flaviana anamtambulisha Machallo kuwa huyo dada ni rafiki yake kipenzi anaitwa Lightness. Kisha anamgeukia Lightness na kumwambia kuwa yule kaka anaitwa Machallo, ni shabiki wake mkubwa sana wa filamu zake. Ameamua kujumuika nao ili wapate fursa ya kuongea machache.

    Machallo anaamua kueleza kile anachokifahamu kuwa anakumbuka alishawahi kumwona Lightness katika moja ya filamu alizowahi kuangalia ila hakumbuki haswa jina la ile filamu inaitwaje!

    ‘Sijawahi kucheza filamu hata moja’ anabainisha Lightness huku akiongeza kuwa, huyo Machallo aliyemwona ni dada yake ambaye ni mwigizaji maarufu sana.

    ‘Watu wengi hushindwa kututofautisha wanapotuona, jinsi tunavyofanana’ anaongezea Light huku akieleza kuwa yeye alishawahi kushiriki kuwania taji la Miss Tanzania japo hakunyakua, ila alifarijika taji hilo liliponyakuliwa na rafiki yake kipenzi Flaviana. ‘Niliamini ushindi wa Flaviana ni ushindi wangu’ ni kauli ya Light.

    Wanaagiza chakula, Machallo anapata bahati ya kuambiwa na Flaviana aagize chakula anachopenda. Anaagiza, baada ya muda chakula kinaletwa wanaanza kula huku wakiiendelea na mazungumzo. Fursa ile ilikuwa ni adhimu sana maishani mwa Machallo, anajiona tayari ameshakubaliwa na kupewa nafasi ndani ya moyo wa yule mwanadada wa ndoto yake. Anaenda mbali zaidi kifikra na kujiona ameshakuwa ‘nyota’ kwa bahati ile iliyomtembelea siku ile.



    Kibarua bado hajakikamilisha. Suala ambalo linamfanya afikirie jinsi anavyoweza kufunguka, somo lipate kueleweka kwa mwanadada huyo ambaye hachoki kumwangalia huku akimshusha na kumpandisha bila kuona dosari.

    Anapanga mashambulizi kimoyo-moyo

    ‘Moja… mbili.. tatu…’ mmmh!, eeeh!. Maneno yanakwama kutoka. Anaamua kuanza kwa swali kwa Light huku akivuta kasi na kupanga gia ya kumwingilia malaika Flaviana.

    ‘Lightness, una ‘boyfriend’?’ anauliza huku akimtazama macho ya aibu iliyochanganyikana na woga kwa mbali.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ‘Sina, nina marafiki tuu. Bado sijafikiria wala kuamua kufanya uchaguzi sahihi kwa sasa japo wanaokuja ni wengi’. Anafafanua Lightness.

    Anakaa kimya kidogo, kisha anafikiria jinsi ya kuanza kutema ‘swagga’ kwa Flaviana. Kabla hajafikia muafaka aanzie wapi, anapata swali la uchokozi toka kwa Flaviana.

    ‘Mbona mimi hujaniuliza kama nina ‘boyfriend’ au sina?’.

    Machallo anajibu

    ‘najua lazima utakuwa naye, msichana mzuri kama wewe ukose boyfriend?’

    jibu hilo lilitolewa na Machallo makusudi akimtaka Flaviana abainishe ukweli kama anaye au hana. Kabla hajatamka neno lolote, simu yake ya kiganjani inaita hivyo anaamua kuipokea.

    Wakati Flaviana akiendelea na maongezi ya simu, Lightness anarudisha swali kwa Machallo akitaka kujua kama ana ‘girlfriend’. Anabainisha kuwa hana, ila kwa muda mrefu amekuwa akimsaka msichana mwenye sifa za kipekee azipendazo bila mafanikio. Anaendelea kufafanua kuwa, ameshamwona mwenye sifa anazohitaji. Kilichobaki ni kumweleza hisia zake toka moyoni ili naye asikilize moyo wake kama anaweza kutoa nafasi.

    Maongezi hayo yanakatizwa na Flaviana ambaye amemaliza kuongea kwa simu, anamtaka Light waondoke kwenda mahali ambapo kuna mtu walikuwa wamepanga miadi wakutane mida ile. Wanamuaga Machallo na kuondoka kitendo kinachomfanya Machallo ajilaumu na kutoamini kile anachokishuhudia. Anashindwa kuamini kama ni kweli Flaviana anaondoka au ni mauza-uza anayoyaona.

    Machallo anabaki kimya huku akiwasindikiza marafiki hao kwa macho hadi anahakikisha wametokomea mbele yake. Anaamua kuondoka pale alipokaa huku akiwa na furaha kidogo iliyochanganyika na huzuni tele kwa kushindwa kuitumia fursa ile kukamilisha mpango wake.



    Lightness na Flaviana wanafika mahali lilipo pakiwa gari lao. Wakati wakifungua gari na kuingia Light anamuuliza Flaviana kama anafahamiana na yule kaka (Machallo) kwa muda mrefu. Flaviana anamwambia kuwa hiyo ndiyo ilikuwa mara ya kwanza kuonana naye

    ‘Nilipofika ‘canteen’ nikamwona kaja na kuomba akae pale nilipokaa. Nikamkubalia, hapo ndipo akaanza kujitambulisha kwangu ndiyo nikamfahamu. si unajua tena ukiwa maarufu……………?’ ni maneno ya Flaviana



    Machallo anajiona ni mwanaume asiye na maarifa, hilo ni suala jingine ambalo anaahidi ndani ya moyo wake kuwa atapambana nalo kwa nguvu kuhakikisha analikabiri hadi anashinda.

    Anafika chumbani, anavua suti yake na kuitundika katika ‘stendi’ maalumu ya kutundikia nguo iliyopo pale chumbani. Anaketi kitandani akiwa na bukta ndogo. Anatafakari yaliyotokea pale uwanja wa mawindo na kujiona ameshindwa kumfyatua risasi swala aliyenona!

    Anafungua simu yake ya mkononi kuangalia sehemu alipohifadhi picha. Anaangalia picha ya mwanadada huyo ambaye amepata bahati kukutana naye.

    Licha ya kushindwa kutimiza kusudi lake anaamua kujipongeza kwa jitihada zile alizofanya kwani anagundua haikuwa rahisi kujivisha ujasiri ule kukutana na mlimbwende yule ambaye alipokuwa akimtazama toka chini hadi juu hakuona dosari.





    *************

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ni semista ya pili baada ya kufunga chuo kwa mapumziko. Maisha ya Machallo yanabadilika. Anakuwa mtu wa kujiweka katika hadhi ya juu na kupenda kusalimiana na kila anayekutana naye, pengine kujitambulisha ili kusudi lake kuwa maarufu lipate kutimia. Ameshakwaruzana na Selike kutokana na kupishana mienendo kufuatia mabadiliko ya tabia yaliyojitokeza kwa Machallo. Hilo linamfanya asijali, hadi ahakikishe anatimiza azma yake.

    Alitumia fursa kutumia mitandao ya kijamii ya facebook, twitter, instagram na mingine akitafuta umaarufu.

    Kama hiyo haitoshi, alitumia muda wake kufungua wavuti (blog) yake ili kuhakikisha watu wengi wanaitembelea na kusoma habari zake ili atii kiu yake. Kujenga ukaribu na watu maarufu lilikuwa ni jambo alilotamani sana, aliitumia vizuri fursa alipoipata. Alihakikisha anapokutana na mtu maarufu, lazima ajitambulishe kwake.

    Jitihada za kumuweka karibu mwanadada Fllavi bado ziliendelea japo zilikabiri changamoto ‘kibao’



    Unafika wakati ambao wanachuo wanapata fursa ya kuchagua viongozi wao katika serikali ya chuo. Machallo anaona ni fursa nzuri kwake kuingia katika kinyang’anyiro hicho ambacho kitamfanya awe maarufu pindi atakapopata madaraka. Anachukua fomu na kugombea miongoni mwa nafasi nyeti pale chuo.



    Kampeni zilianza, anajitahidi kujinadi kwa sera ambazo anaamini zitamweka katika nafasi ile anayowania. Bahati inakuwa mbaya kwake, anashindwa kupata ile nafasi baada ya kushindwa wingi wa kura na hashimu wake ambaye alikuwa na nguvu kubwa katika sera zenye mvuto. Jambo hilo linamnyima furaha, anajiona ana bahati mbaya kama ‘analala na bundi’ jambo linamchelewesha kufika katika kilele cha ‘umaarufu’.



    Mtiririko wa mambo hayo yote yanamfanya atumie gharama kubwa sana katika mavazi, vyakula pamoja na vitu vingi alivyohitaji ambavyo alijua vingemweka katika tabaka la juu. Anajikuta katika wakati mgumu ambapo anataka kuishi maisha ya juu huku uwezo wake kifedha ni mdogo.

    Suala la kumpata Flaviana amweleze la moyoni limekuwa shughuli pevu kushinda awali. Jitihada za kutafuta namba yake ya simu zinaendelea, anabahatika kupata namba ambayo anajaribu kupiga, inaita bila kupokelewa. Jaribio la kupiga ile namba linaendelea mara kwa mara bila mafanikio.



    Unafika wakati ambao hawezi kuendelea kungoja kwani njaa na kiu ya mafanikio inazidi. Anapata wazo, kujichanganya katika makundi pindi watu wanapokuwa ‘wakipiga stori’ ili kuhakikisha anayateka mazungumzo na kujijengea jina.

    Zoezi halikuwa rahisi kwani ni mara chache watu walikuwa wavumilivu kusikiliza mazungumzo yale jinsi alivyokuwa akijipeperushia bendera.

    Katika harakati, siku ya siku anafumania kundi la wanachuo waliokaa katika ‘vimbweta’ wakijadili habari za mpira kuhusiana na watani wa jadi Simba na Yanga. Anajichanganya katika lile kundi kuanza kuchangia mada. Wakati maongezi yakiendelea, linapita gari aina ya prado. Ambalo linaonekana kama gari analopenda kulitumia Flaviana mara nyingi.

    Mmoja wao anauliza kama lile gari sio la Flaviana. Machallo anadakia

    ‘siyo lenyewe’

    Anaona hiyo haitoshi anaamua kujifagilia

    ‘Flaviana ni demu wangu, popote alipo lazima anitaarifu’

    maneno yale yalimsababisha Machallo ashambuliwe kwa vicheko vya dharau na kejeli huku maneno ya kashfa yakimfuata. Anashindwa kuvumilia kwa fedheha anayopata, anaondoka eneo lile huku akiendelea kuzomewa na kutaniwa. Kitendo kile kinamkosesha amani kwa muda na kumvunja moyo kuendelea kuvamia makundi. Anaanza kufikiria jinsi anavyoweza kufanya ili akamilishe ndoto yake.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Jitihada zinashindwa kuzaa matunda hadi mitihani inapoanza, wakati ambao anakuwa ‘bize’ kiasi cha kukosa muda wa kufanya jitihada zozote zinazoweza kumkutanisha na Flaviana wala kumfanya maarufu.

    Semista ya pili inaisha baada ya mitihani kumalizika na chuo kinafungwa tayari kwa likizo ndefu.



    Wakati wa likizo ulikuwa ni muda mzuri kwake kujipanga ili chuo kinapofunguliwa aweze kuwa na mafanikio katika ndoto yake kubwa. Anatambua kuwa hawezi kumpata Flaviana katika kipindi hicho cha likizo, kwani husafiri kwenda Daresalaam katika kipindi chote cha likizo.



    Anapata nafasi ya kufanya ‘field’ katika shule maarufu sana isiyokuwa ya serikali ya Knowledge Springs iliiyoko jijini Mwanza. Field yake inakuwa na mafanikio makubwa kuanzia majuma machache tangu aanze, kutokana na kutokea kupendwa sana sio tu na wanafunzi, bali waalimu pamoja na baadhi ya wazazi waliosikia sifa zake.



    Kadri siku zinavyoyoyoma, anajikuta maarufu sana katika mazingira yake ya kazi kutokana na tabia njema na mwenendo uliotukuka wa maadili mazuri ya ualimu. Jambo hili linamtofautisha na vijana wengine ambao huonesha utovu wa nidhamu pindi wanapokuja kufanya field pale shule, huanzisha mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi.



    Kutokana na uwezo wake mzuri kufundisha darasani, wanafunzi waliweza kuelewa sana somo la baiolojia alilokuwa akifundisha. Somo lilitokea kupendwa hata na wanafunzi ambao walilichukia na kuliona gumu. Uongozi wa shule unaamua kuweka makubaliano ya kumlipa Machallo ilii aweze kufundisha vipindi vya ziada na kumpangia kufundisha madarasa mengi. Anakubali na kujituma. Kiasi cha pesa anachopata kinamsaidia kwa kiasi kikubwa sana katika kumudu gharama za maisha.



    ‘Anajibana’ na kutumia sehemu kubwa ya fedha anayopata kuanzisha kipindi cha redio mara moja kwa juma, kila siku ya jumamosi kuanzia saa nne asubuhi. Kipindi kinachodumu kwa muda wa dakika 45 akifundisha somo la baiolojia.

    Kipindi kilikuwa na mafanikio makubwa sana baada ya kupata wasikilizaji wengi ambao asillimia kubwa walikuwa ni wanafunzi ambao walikuwa wakituma barua pepe, ujumbe mfupi wa maneno na kupata fursa ya kupiga simu wakati wa kipindi kuuliza maswali na kutoa maoni.



    Bahati inakuwa nzuri upande wake pale anapopata udhamini toka kwa kampuni kubwa inayojihusisha na uchapaji wa vitabu. Anaingia nao mkata, wanamchapia kitabu cha baiolojia ambacho alikuwa ameshamaliza kukiandika, alichoanza kukiandika mwaka mmoja uliopita. Kitabu kinakamilika, anaanza kukinadi kwa wanafunzi shuleni anakofundisha na shule nyingine za jirani pamoja na redioni anapofanya kipindi. Wengi wanatokea kukipenda sana kile kitabu kwa jinsi kilivyo ‘nondo’ jambo linalomfanya Machallo afanikiwe kuuza nakala nyingi ndani ya majuma machache. Mauzo yanapelekea akaunti yake ya benki kuanza ‘inapumua’ baada ya kutengeneza na kuendelea kutengeneza kiasi kikubwa cha pesa kutokana na ujasiriamali huo. Kwakuwa pesa ipo sasa, anatafuta nyumba yenye nafasi na kuondoka kwenye chumba kimoja allichokuwa amepanga. Maisha yake yanabadilika kiuchumi, japo bado anatafuta wigo wa soko la kubwa zaidi la kitabu chake ili kiuzwe katika mikoa yote Tanzania jambo litalomletea manufaa makubwa zaidi.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kwa mafanikio aliyopata anawakumbuka ndugu zake kwa kuwalipia ada wanaosoma, kumwongezea mama yake pesa kwa ajili ya kulima shamba pamoja na mambo mengine ya msingi.



    Wakati akiendelea na mambo hayo yote, bado suala lake la kujipanga kuhakikisha chuo kikifunguliwa hafanyi makosa lilikuwa endelevu. Awamu hii anadhamiria lazima awe na mahusiano ya kimapenzi na mwanadada Flaviana jambo litalomfanya apate nafasi ya kuonekana katika mitandao mbalimbali inayotembelewa na watu duniani kote, pia vituo vya redio, televisheni hata magazeti jambo ambalo lingempa umaarufu wa kufumba na kufumbua.



    Anajihahidi kuangalia filamu, kusoma vitabu mbalimbali pamoja na kutembelea mitandao mbalimbali ya intaneti ili kupata uelewa na maarifa ya kutosha na mbinu zitakazofanikisha mpango wake. Anajikuta anatokea kuipenda filamu inayoitwa ‘love doesn’t cost a thing’. Anagundua muhusika katika filamu ile alikuwa na shauku ya kuwa maarufu akaona jinsi alivyofanya akafanikiwa kujizolea umaarufu, jambo lililompa moyo na kumfanya aamini kuwa anaweza bila kujali changamoto na misukosuko atayokumbana nayo.



    Anakuja mdogo wake wa mwisho wa kiume anayeitwa Babuu toka nyumbani kwao kuishi naye hapo jijini Mwanza wakati akitafuta fursa ya ajira, kwani alikuwa amemaliza kidato cha nne na kusomea kozi inayohusiana na ‘graphics designing’, uandaaji wa picha za video pamoja na ufundi wa kompyuta.



    Machallo anadhamiria kununua gari la kutembelea. Jambo ambalo aliamini lingemfanya awe tabaka la juu, japo hakuwa na uhakika sana kama angeweze kulijaza mafuta na kuhakikisha analifanyia matengenezo siku za mbeleni.

    Anaamua kumshirikisha mdogo wake wazo hilo, Babuu anaona ni jambo zuri ila alishauri kuwa lingekuwa jambo zuri zaidi endapo kiasi hicho cha pesa kingewekezwa katika biashara ambayo ingeingiza faida kuliko gari kwa wakati ule ambalo llingehitaji gharama nyingi za mafuta na matengenezo.



    ‘Unafikiri tunaweza kufanya biashara gani nzuri hapa mjini?’ anauliza Machallo. Babuu amshauri afungue ofisi itayohusika na kutoa huduma ambazo amezisomea jambo litalompa fursa ya ajira badala ya kukaa tu pale kwa kaka yake.



    Machallo anaona ni jambo jema, japo anatamani sana kumiliki gari. Anakubaliana na wazo la mdogo wake na kuamua kufungua ofisi maeneo ya Malimbe~Nyegezi, jirani na chuo cha Mt. Agustino anakosoma.



    Ofisi inaendelea vizuri, pesa ya kuendeshea maisha inapatikana bila wasiwasi. Babuu anajituma sana na kuonesha uaminifu mkubwa, jambo linamfanya Machallo azidi kumpenda na kumwamini sana mdogo wake. Anaamua kumweleza mambo yake mengi bila kuacha kumweleza shauku yake kumpata Flaviana.





    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Likizo imeisha, chuo tayari kimefunguliwa. Ni nafasi nzuri sasa kwa Machallo kuanza zoezi lake la kumpata Flaviana. Anadhamiria kumuwinda kwa nguvu ili kuhakikisha anapata nafasi ya kumweleza hisia zake.



    Siku hazigandi, ila ugumu wa kumpata Flaviana unazidi kwani Flaviana yuko ‘busy’ sana semista hii kuliko iliyopita. Mara kadhaa aidha baada ya Machallo kumvizia Flaviana anapotoka katika mhadhara, maktaba au anapotoka sehemu moja kwenda nyingine huomba nafasi kumtaka Flaviana ampe nafasi dakika chache ili amwambie jambo lakini mara zote Flaviana amekuwa akimwambia kuwa hana muda kwa wakati ule.



    Masomo yanazidi kushika kasi kiasi cha kumfanya Machallo akose nafasi. Ndoto yake inakuwa mbali sana kiasi cha kujiona anakosa kutimiza `dhamira yake maishani.



    Inafika siku ya Jumapili, Machallo anakutana na Flaviana ‘super~market’ kubwa na maarufu sana jijini Mwanza iliyoko jirani na kipitashoto chenye sanamu ya samaki.

    Hii imetokea kama bahati kwa Machallo, ambaye amesubiri pale kwa takribani saa tatu tangu alipofika maeneo ya jirani na eneo la tukio tangu saa tatu asubuhi. Alifahamu ratiba, katika siku za jumapili mrembo huyo hufika pale kununua mahitaji yake.



    Wakati akiwa mle ndani akinunua mahitaji, Machallo anamsogelea huku akitabasamu.

    ‘Mambo mrembo?’ anatoa salamu Machallo.

    Flaviana anaitikia ile salamu kwa uchangamfu huku akitaja jina la Machallo kwa ufasaha.

    Anashangaa kidogo kuwa mrembo alikuwa akimkumbuka jina. ‘nakumbuka tulionana……. Wapi vile?

    Anajaribu kukumbuka bila mafanikio, anaamua kuuliza. Bila kuchelewa Machallo anajibu kwa kujiamini

    ‘Chuo, St. Augustine. Tulikutana kwa mara ya kwanza canteen tukala chakula pamoja, ulikuwa na rafiki yako Lightness’. Flaviana anakumbushwa.



    ‘nambie… za siku?’ anauliza Flaviana.

    ‘njema’ anajibu Machallo, anaendelea kumweleza kuwa amekuwa akihitaji fursa ya kuongea naye kwa muda mrefu ila Flaviana amekuwa ‘busy’ sana kiasi cha kumfanya akose nafasi hiyo.



    Flaviana anafafanua kuwa amekuwa na mambo mengi sana tangu miezi kadhaa iliyopita, kuna mambo mengi anayofanya huku akiendelea na masomo kwa wakati mmoja jambo linalomfanya awe bize kiasi kile.



    Machallo anaamua kupiga moyo konde na kueleza lililoko moyoni mwake bila kumung’unya maneno kwani alijua ile ni nafasi adhimu ambayo ameipata kwa bahati wala isingeweza kujirudia.



    ‘Sina sababu ya kuficha mambo wala kuishi na maumivu moyoni mwangu. Napenda niweke bayana jambo ambalo limekuwa likinitesa kwa muda mrefu sasa’ Anamweleza Flaviana.

    ‘Eleza nakusikiliza’ ni sauti ya Flaviana baada ya kuona ukimya kidogo.



    ************

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    :: Machallo atafanikiwa kusema ya moyoni?? vipi kuhusiana na Flaviana atakubaliana kweli na machalo?? nini hatma ya Machalo katika simulizi hii??



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog