Simulizi : Shetani Msalabani
Sehemu Ya Pili (2)
Ilipoishia
Saa moja la mhadhara linaisha, machallo anaamua kutafuta fursa ya kupiga soga na yule kigoli. Bahati mbaya yule dada alishaondoka mapema bila yeye kujua hivyo mpango mzima unakwama.
Songa nayo sasa…
***********************
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Sekunde, saa, siku, juma na miezi ilisonga. Jitihada za makusudi zinazidi kufanywa na Machallo kuhakikisha anapambana na hali yake duni kifikra. Matokeo yanaonekana, anajikuta tayari ameanza kupiga hatua na kujenga uwezo kidogo wa kujiamini na kupambana na hali yake licha ya vikwazo lukuki anavyokumbana navyo. Anagundua kuwa zile wavuti alizotembelea na vitabu mbalimbali alivyosoma vimemfanya awe bora zaidi na aimarike kifikra. Anatokea kukipenda sana kitabu chenye kichwa ‘Saikolojia ya Kujitambua’ kilichoandikwa na Habel Samida ambacho kimekuwa na msaada mkubwa sana kumfanya ajitambue zaidi ya awali na kutambua nguvu, vipaji, uwezo na uimara ulioko ndani yake na namna ya kuviendeleza.
Inafika siku ya jumamosi, mwisho wa juma. Siku ambayo kila mtu huwa na pilika za mambo yake binafsi kwani huwa hakuna ratiba ya masomo. Machallo anashinda chumbani akiwa peke yake. Anasimama mbele ya kioo kilichopo pale chumbani na kujaribu kufanya ‘reharsal’ ya kila aina ya tabia anayotaka kuijenga.
Anasimama akiwa amevaa vizuri, mbele ya kioo akitamka maneno na kuonesha ishara kwa mikono yake akijaribu mambo mengi anayotaka kushindana nayo. Anavuta taswira yuko kwenye ukumbi wenye maelfu ya watu, yeye ndiye mtu maalumu anayetoa hotuba pale. Anafanya hivyo huku akijitazama kwenye kioo kilicho mbele yake. Anagundua amekuwa bora zaidi, anajiona imara kama chuma cha pua mwenye uwezo wa kusimama popote bila aibu wala hofu.
Baada ya majaribio mengi, anahamia katika suala lingine ambalo ni nyeti sana moyoni mwake. Suala hilo sio jingine, ni mahusiano yake ya kimapenzi na binti ambaye macho yake yamemwona na moyo ukamchagua. Ni mzuri wa sura, umbo hata tabia. Wanaume wengi hutokea kuvutiwa naye kwa sifa lukuki alizonazo ila suala la kumweleza bayana huwa zito kwani wengi wao hujikuta midomo imejaa maji!
Anaamini akimpata mlimbwe huyo, atakuwa ametimiza ndoto yake kubwa ‘kuwa maarufu’ iliyojengeka tangu akiwa mdogo. Aliamini kuwa na yule dada kungemfanya aikamilishe hiyo ndoto yake kulingana na hadhi na nafasi aliyonayo huyo dada katika jamii. Anainuka kusimama mbele ya kioo kujaribu ‘staili’ ambayo inaweza kuwa nzuri kwake, jinsi atakavyokwenda kumweleza mwanadada wa ndoto yake yanayotoka moyoni. Anajaribu kwa mara ya kwanza, anahisi hiyo siyo namna nzuri, anajaribu tena. Awamu hii anaona ameboresha maneno ni mazuri ila tatizo mavazi aliyovaa hayana hadhi ya kusimama mbele ya ‘mchumba’. Anaamua kufungua begi lake ambalo hulitumia kutunza nguo. Anachagua nguo ambazo anaona ni nzuri zaidi ya zingine na akivaa anahisi anapendeza. Nguo zimejikunja, hivyo anaamua kuzinyoosha ili avae aweze ‘kutokelezea’ tayari kwa kuanza mazoezi ya kumvutia kasi mwanadada ambaye ametokea kumpenda. Anamaliza kuzinyoosha, anavaa na kuhakikisha amechomekea vizuri kwa ustadi. Anasimama vizuri ajitazame kwenye kioo huku akiachia tabasamu matata na kuvuta picha yuko na yule mlimbwende ambaye ametokea kumfanya teja wa mapenzi.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Flaviana,
Wewe ni mwanamke ambaye una sifa lukuki, za kipekee ambazo siwezi kuuelezea ulimwengu na kuzimaliza kwa dakika hizi chache….
Kwa sifa hizo, unastahilii kuwa na aina ya mwanaume ambaye atajali nafasi uliyonayo na kukufanya bora zaidi siku zote ujione umependelewa na Mwenyezi Mungu.
Mimi ni chaguo sahihi kwako. Najua hunifahamu kwa karibu, ila naomba unipe nafasi uone mimi ni mtu wa namna gani!
Usije kunifikiria na kunichukulia kama maleghuni ambao siku zote wao hubananga”.
Anajisemea Machallo huku anashuhudia kijasho chembamba kikimtoka anapomaliza kutamka yale maneno, kitendo kinachoashiria kuwa ile siyo shughuli ndogo hata mara moja.
Anapanga mikakati kabambe kuhusu namna atakavyokutana na huyo kiumbe adhimu na ‘kumtemea madini’ ambayo anaamini ni Tanzanite. Wakati amekaa na kutafakari hayo, anafika Selike pale ndani. Anagundua, kuwa kuna jambo zito linalomkabiri rafiki yake kipenzi. Kwakuwa alijua, lolote linalomgusa Machallo linamgusa hata yeye, anaamua kumuuliza kinachomsibu hadi awe anatapatapa katika bwawa la mawazo kiasi kile. Bila kusita, Machallo anafunguka kueleza lile lililoko moyoni mwake na dhamira yake ya dhati.
Anaeleza kuwa, anafikiria jinsi atakavyompata yule ampendaye awe sehemu ya maisha yake. Jambo ambalo linamfanya Selike aulize kwa shauku kubwa kutaka kujua moyo wa rafiki yake umetua wapi!
Machallo anabainisha kuwa anampenda msichana ambaye amedhamilia kumpata awe naye maishani. Furaha yake itakamilika pindi atakapofanikiwa kwani akili yake, moyo, mwili, damu, maji na mifupa yake ilikuwa inamshuhudia umuhimu wa kiumbe huyo maishani mwake. Hapati picha mateso atakayopata akimkosa.
Wakati akieleza hayo Selike yuko makini anasubiri afahamishwe ni nani hasa ambaye anaunyanyasa moyo wa rafiki yake ili aone namna ya kumsaidia rafiki yake ahakikishe anapata shemeji mwema.
‘Flaviana ni chaguo langu sahihi’ anasema Machallo huku akishusha pumzi ndefu.
“ni Flaviana yupi?” Selike anajiuliza.
Maana yeye anamfahamu Flaviana mmoja tu pale chuo. Ni dada maarufu sana sio tu pale chuo, bali katika jiji la Mwanza, Tanzania bara na visiwani, pamoja na Afrika Mashariki na kati kwa ujumla. Hadhani kama anaweza kuwa Flaviana huyo anayemfahamu yeye, anajua huenda ni Flaviana mwingine. Kuondoa mkanganyiko anaamua kumuuliza Machallo ili apate uhakika.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Selike anashindwa kujizuia, anacheka kwa dharau baada ya kuambiwa kuwa ni Flaviana huyohuyo anayemfahamu. Kicheko hicho kinatosha kumfanya Machallo agundue kuwa rafiki yake anaamini kwamba hizo ni ndoto za Alinacha, kwani hawezi kumpata mrembo huyo kutokana na mafanikio makubwa na umaarufu alionao katika tasnia ya Filamu (Bongo Movie), kuwa mwanamitindo anayefanya vizuri, pia kuwahi kutwaa taji la ‘Miss Tanzania’.
Selike anaweka bayana kuwa huyo dada sio wa hadhi yake!
‘…not your stuff, anyway!’
Anaamua kumweleza Machallo asijisumbue kumfikiria mwanadada huyo, anaweza kuumia na kuambulia maradhi ya moyo bure! Ni bora atulize moyo wake amtafute wa hadhi yake. Kauli hiyo haina nguvu kiasi cha kumkatisha tamaa Machallo.
‘Naamini kitu chochote ambacho mtu atakidhamiria kwa dhati na kufanya jitihada za makusudi bila kukata tamaa kinawezekana. Ndivyo ninavyoamini itatokea…’ Anasisitiza Machallo.
Anamuhakikishia rafiki yake kuwa lazima ampate.
‘Yangu macho….., ila nakuahidi, kama utaweza kumpata Flaviana, siku hiyo mi ntavua nguo na kutembea uchi chuo kizima! Tena mchana kweupeee…’ anaongea Selike kwa kebehi,
Kauli inayomfanya Machallo amwambie Selike ‘wapinge’ (njia ya kuweka makubaliano) ili siku ikitokea, avue nguo kweli na kutembea uchi.
Wanamaliza kupinga, Selike anaenda kabatini na kuchukua glasi. Anamimina juisi na kumpa Machallo huku naye akichukua glasi nyingine na kujiwekea. Anatafuta filamu nzuri ambayo anaweza kuangalia. Anamuuliza Machallo filamu ambayo angependa waangalie. Machallo anamweleza kuwa aweke filamu yoyote nzuri ila iwe ‘love story’. Anaangalia katika ‘droo’, anapata filamu inayoitwa ‘Gharama ya penzi’
Wanaangalia ile filamu nzuri yenye mikasa ya kimapenzi inayosisimua wakati Machallo akiwa amekaa chini huku akikodolea macho TV, lakini mawazo yake hayako pale. Alikuwa akimfikiria Malkia wake mwenye hadhi kuwa malkia wa ulimwengu ambaye ametokea kumkaa akilini kuliko kitu chochote.
Anajisikia vibaya kuwa ‘dissappointed’ na rafiki yake ambaye hayuko upande wake kumtia moyo. Potelea mbali…. Anakusidia kusonga mbele bila kukatishwa tama na maneno ya rafiki yake. ‘lazima azma yangu itimie bila kujali vikwazo’ anajisemea moyoni.
********************
Kadri siku zinavyokwenda ndivyo njaa ya umaarufu inamzidia kiasi cha kuwaza sana kile anachoweza kufanya apate kukidhi njaa yake. Hilo ndilo lengo lake kubwa linalomfanya amfikirie sana Flaviana. Alijua akimpata huyo manzi, umaarufu utakuwa ni ‘wakufikia’.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Maneno ya kumkatisha tama yaliyotolewa na rafiki yake Selike yanajirudia akilini mwake. Anafikiria sifa alizonazo yule ‘mamiito’ anakubaliana na kauli ya Selike kuwa sio wa hadhi yake. Lakini bado dhamiri yake inamtuma arushe nyavu ili aweze kumnasa kiumbe huyo.
Ni jumatatu, ratiba ya chuo inaendelea kama ilivyo ada. Akili ya Machallo imetawaliwa na fikra za kuwa maarufu na kumpata Flaviana. Anadhamiria kujitutumua amfuate kumweleza hisia zake. Alifahamu kuwa Flaviana huwa anapenda kwenda kupata chakula ‘canteen’ maalumu kwa ajili ya wahadhiri na wanachuo wenye uwezo mkubwa kifedha kwani bei ya vyakula na vinywaji pale ni kubwa kuliko sehemu zinigine. Anatambua uwezo wake kifedha sio mkubwa. Kiasi cha fedha alichonacho ni kidogo hivyo alitambua akienda pale kupata huduma ya chakula na kinywaji wakati akimsubiria Flaviana, atakuwa ametumia kiasi kikubwa cha fedha, ambacho kitamharibia bajeti yake siku za usoni ataishiwa pesa.
Anaamua kutojali hilo huku akiwa tayari hata kula mlo mmoja ilimradi afanikiwe mpango wake mahususi. Anaangalia muda, anagundua bado haujafika ule muda muafaka ambao Flaviana hufika pale ‘canteen’ kupata chakula cha mchana.
Anaendelea na masuala mengine huku akisubiria muda muafaka ufike. Muda unafika, anataka kughairi kwenda lakini anajipa moyo. Anarudi chumbani kwanza kujiangalia kwenye kioo. ‘you are so great’ anajisemea wakati akijiangalia kwenye kioo kushuhudia ‘alivyotupia’ suti yake nyeusi ambayo ni moja tu aliyonayo. Anakumbuka kuwa alipewa na shangazi yake katika sherehe aliyofanyiwa na familia yake ikiwa ni kumpongeza kupata nafasi ya kujiunga na chuo kikuu, kitendo kilichoipa heshima kubwa sana ile familia kwani, katika ukoo mzima yeye ni mtu wa kwanza kugusa elimu ya chuo kikuu.
Anakumbuka asubuhi alipulizia manukato ‘pafyumu’ lakini anaamua kufungua kabati tena kuchukua manukatu na kujipulizia kwa mara nyingine kisha anaamua kuelekea uwanja wa mawindo. Anapotoka, kufika nje anakumbuka hakutengeneza nywele zake vizuri. Anaamua kurudi ndani na kuchukua ‘brashi’ anazitengeneza vizuri nywele zake zilizonyolewa na kuachwa fupi zikipendeza. Sasa anajiamini baada ya kujiridhisha, anatoka kwenda kuianza shughuli.
Kufika ‘VIP canteen’ anaangaza macho huku na kule kuona kama Flaviana ameketi mahali, bila kumwona. Wakati akifanya zoezi hilo alikuwa makini asije kuonekana mshamba kwa jinsi anavyoshangaa.
Anaamua kwenda sehemu ya mbele , ambako anakaa karibu na TV kubwa iliyowekwa ukutani. Kumaliza kuketi tayari muhudumu ameshafika na kuanza kumuuliza anachohitaji. Wakati muhudumu anauliza, tayari Machallo amemuona mwanadada ambaye anajua ni Flaviana akiingia mule ndani kwa mwendo wa madaha!. Jambo hilo linamfanya atumbue macho huku mawazo yote ameyahamishia kule anakotazama.
Anashituka kidogo anapoguswa begani huku akisikia sauti inamuuliza ‘kaka nikuhudumie nini nakuuliza?, ni muhudumu akiuliza. Anageuka na kumwangalia mhudumu usoni huku macho yake akiyapepesa kwa haraka
‘Juisi ya parachichi’ anajibu kwa haraka huku akijibaraguza baada ya kugundua kuwa muhudumu amekuwa akimuuliza mara kadhaa bila kujibu baada ya kuwa ‘amepitiwa’ pindi alipomwona yule kigoli wakati anaingia.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Muhudumua anaondoka ili akamletee mteja wake kile alichoagiza. Machallo anatupa jicho tena kuangalia yule mrembo ameketi maeneo gani baada ya kukatishwa na muhudumu zoezi lake la kumsindikiza kwa macho kuona pale atakapokaa. Kuangalia kule alikokuwa anaelekea kuketi yule mrembo, anamuona, loh! Kumbe amemfananisha ‘bhana’.
Mawazo yanamtawala, huku shauku ya kumwona Flaviana na kupata nafasi ya kuongea naye inatanda. Anamwangalia tena yule dada ili ajiridhishe kama sio Flaviana kweli. Anagundua siyo kwa mara nyingine.
Saa yake inamuonesha ni saa saba na nusu mchana, ikiwa imebaki nusu saa kufika saa nane muda ambao ana kipindi. Anaamua kujitoa ‘muhanga’ hata kama atakosa kipindi lakini lazima amsubiri Flavana hadi amwone.
Anaendelea kunywa juisi huku akiwaza na kuangaza macho yake yashuhudie tukio muhimu, pindi Flaviana anapoingia ‘mjengoni’.
Muda unazidi kwenda bila kumtia machoni Flaviana. Anawaza huenda alishafika pale kupata chakula na kuondoka kabla yeye hajafika. Au pengine siku hiyo Flaviana hajafika chuo. Lakini anakumbuka alipoangalia ratiba kozi anayosoma Flaviana, aliona ana kipindi kuanzia saa sita mchana hadi saa saba kamili, hivyo alijirishisha kuwa atakuwa bado hajafika pale kula chakula kabla yeye hajafika. Anawaza mengi, mwishowe anakata tama kumsubiri. Anaamua kuondoka. Anaenda ‘kaunta’ kulipa bili. Anatoa noti ya shilingi elfu kumi anamkabidhi mhasibu.
Wakati akisubiria chenji akaangaza katika lango kuu la kuingilia ‘kantini’, anamuona kiumbe aliyekua akimsubiria kwa takribani saa moja na dakika zipatazo arobaini na saba anaigia. Kumwona, moyo ‘unampasuka’ kiasi cha mapigo ya moyo kuongezeka kwa kasi. Anamsindikiza kwa macho hadi alipokwenda kuketi. Anaamua kumfuata ili apate nafasi ya kuongea naye amweleza lililomo ‘uvunguni’ mwa moyo wake.
Anasahau kuwa amekuwa akisubiria chenji anaondoka.
‘kaka chukua chenji yako’ ni mhasibu aliyekuwa akimweleza Machallo ambaye alikuwa ameanza kuondoka.
Machallo anarudi, anachukua chenji na kuelekea alipokaa yule malaika. Anafika na kumsalimia huku akimtolea tabasamu zito linalochimba ‘vijisima’ vidogo mashavuni mwake. Flaviana anaitikia kwa uchangamfu bila hiyana. Anaomba aketi pamoja naye kwa maongezi mafupi, Flaviana anakubali na kumruhusu. Machallo anashukuru kwa ukubali ule, anakaa huku akitafakari wakati mgumu alionao kueleza hisia zake kwa yule mwanadada. Alijua kitendo kile kilihitaji ujasiri wa hali ya juu. Anajua kuwa hakuna jambo lingine muhimu zaidi ya jitihada za kuvaa moyo wa ujasiri ili aanze kumtemea madini yule manzi.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
*************
::: Je machallo ataweza kutupa kete kwa flaviana?? itakuwaje sasa atakubaliwa?? nini hatma ya Machallo?
:: Safari ndio kwanza imeanza, hapo ndipo utajua maana ya ‘SHETANI MSALABANI’ hakika si ya kukosa endelea kufuatilia kujua.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment