Search This Blog

Thursday, 2 June 2022

SHETANI MSALABANI - 1

 





    IMEANDIKWA NA : ABEL H. SAMIDA



    *********************************************************************************



    Simulizi : Shetani Msalabani

    Sehemu Ya Kwanza (1)



    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Machallo anajiunga na chuo kikuu cha Mt. Agustino kilichopo jijini Mwanza, jiji mashuhuri katika Afrika ya Mashariki lenye miamba mingi. Anaanza kufanya udahili pale chuo. Zoezi la udahili linakamilika, anapata ratiba na utaratibu mzima wa pale chuo ambao alipashwa kuufuata kwa kipindi chote anapokuwa pale chuo. Anajitahidi kuuzoea na kuendana nao kisha anaanza kuuuzoea taratibu kadri siku zinavyokwenda.



    Muda unayoyoma, masomo yanazidi kuchanganya na mambo mengi ya pale chuoni yanadhihirika kwa Machallo. Anajikuta katika wakati mgumu kwani anaona kuna mambo mengi yanayoendelea pale chuo, yanayompelekea katika mazingira ambayo siyo rafiki mzuri kwake. Anajiuliza kama anaweza kujitawala na kuyashinda mambo yaliyo kinyume na maadili yaliyomjenga kutokana na mazingira aliyoishi muda mrefu. Anakumbuka shule ya sekondari ambako alisoma, shule yenye wanafunzi wa jinsia moja (wavulana). Hakuwa amezowea kusoma na kujichanganya karibu na wasichana, jambo lililokuwa tayari limemjengea woga kwa jinsia tofauti na yake na kujikuta mwenye aibu anapokuwa karibu na viumbe hao.



    Pale Hosteli anaishi na wenzake watatu akiwemo Selike, Gibsoni na Gamba, lakini wanajikuta wana matabaka yaliyojengeka kulingana na vitivo wanavyosoma. Machallo na Selike wako kitivo kimoja (kitivo cha elimu) ambao wanajikuta wako karibu zaidi wakishirikiana mambo mengi na kujenga urafiki mkubwa sana. Gamba pamoja na Gibsoni wako vitivo tofauti, Gamba anasoma kitivo cha Sheria wakati Gibsoni akisoma kitivo cha Uongozi wa Biashara. Hawa wawili hawakuwa karibu sana wala haukuwepo ukaribu kati yao na akina Machallo na Selike. Kila mmoja aliona kitivo anachosoma ni bora kuliko kitivo anachosoma mwingine jambo linalowafanya Machallo na Selike wadharaulike mbele ya Gamba na Gibsoni kwa ajili ya dhana kwamba kitivo wanachosoma ni duni. Jambo hilo halina nguvu kiasi cha kuwasumbua hawa waalimu walioko mafunzoni.



    Selike anakuwa maarufu kiasi pale chuoni, hasa katika kozi anayosoma tofauti na Machallo ambaye alikuwa hafahamiki. Selike anachaguliwa kuwa mwakilishi wa darasa jambo linalomfanya afahamike kwa kila mtu anayesoma katika lile darasa ambalo lilikuwa na watu ‘utitiri’ Machallo anaamua kutoa hisia zake wakati wamekaa chumbani akiwa na Selike mida ya jioni baada ya vipindi kumalizika.

    ‘umetokea kuwa maarufu sana ndani ya kipindi hiki kifupi’ anaeleza machallo huku akiendelea

    ‘..yaelekea una nyota ya kupendwa na watu’. Anaeleza Selike. ‘Nahisi uongeaji ndio unaochangia, si unajua tena mi mtoto wa uswazi, tantalila za kutosha!’ anajibu Selike huku akitabasamu na kuinuka kuelekea kabatini kuchukua kompyuta mpakato yake kuiweka ipate chaji.

    Mazungumzo yanaendelea hadi unafika wakati muafaka kwa ajili ya kupata chakula cha usiku. Wanatoka kuelekea ‘Canteen’ ambako huwa wanapata chakula.



    Wanafika sehemu ya chakula pale canteen, Selike anaitwa na mwanadada ambaye anafahamika kwa jina la Maunda aliyekaa na rafiki zake wawili. Selike anafika, anaketi katika moja ya kiti kilichokuwa wazi pale kando ya meza.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya salamu Maunda anafanya utambulisho kuhakikisha Machallo anawafahamu wale rafiki aliokaa nao bila kuacha kumtambulisha Machallo kwa rafiki hao. Wakati zoezi la utambulisho likiendelea, Joyce anamwita muhudumu kwa ishara akimtaka aje pale alipokaa. Muhudumu anafika na kusimama kando ya Joyce. ‘Msikilize kaka hapa chakula anachohitaji umhudumie’. Joyce anamweleza yule muhudumu.

    ‘Wali samaki’ anajiongeza Machallo kabla hajaulizwa na mhudumu. Mhudumu anaondoka kwenda kumletea chakula Selike.

    ‘Mlikuja wawili, mbona mwenzio ameenda kukaa peke yake?’ Ni sauti ya Joyce akimuuliza Selike. Kabla Selike hajajibu swali hilo, Maunda anarudisha chakula kwenye sahani ambacho alikuwa amechota kwa kijiko kwa ajili ya kubugia, anafuta mdomo wake kwa tishu kisha anaeleza jambo kuhusiana na swali la Joyce. Anaeleza kuwa anamfahamu huyo kaka aliyeambatana na Selike. Mara nyingi huwa anajitenga, usipomkuta peke yake basi atakuwa na Selike. Mara chache sana utamkuta amekaa na watu tena ni wavulana tuu. Anaweka bayana kuwa hajawahi kumwona akiwa amekaa na wasichana au akiongozana na msichana.



    ‘Au domo zege?’ anachomekea Joyce, kauli inayowafanya waangue kicheko huku Msope, Joyce na Maunda wakigeuka kumwangalia Machallo katika kona aliyokuwa amekaa. ‘Hivi ana ‘girlfriend’?’. Anauliza Msope ambaye amekuwa kimya kwa muda huku akimtazama Selike kwa makini.

    ‘Vipi unataka awe boyfriend wako nini?’ Ni Selike anamjibu kwa mtindo wa swali kwa lengo la kumtaka Msope afunguke

    ‘Inaelekea anapenda wanaume wapole huyu… kama yeye alivyo’ anadakia Joyce kabla Msope hajajibu, huku akimsonda.

    Maunda anaeleza wazi kuwa Msope sio mpole kama wanavyomdhania. Yeye anamfahamu, anaongea kama chiriku kwani amekuwa rafiki yake kwa muda mrefu.

    ‘Msope anaongea sana, hata hivyo leo nashangaa amekuwa sio mwongeaji kama siku zingine’. Anaeleza Maunda.



    Wakati huo wakipiga soga huku wakipata chakula, Machallo anawatazama kwa macho ya wizi-wizi toka katika kona aliyokaa. Japo yuko mbali kiidogo kiasi cha kutosikia mazungumzo yao, anahisi kuna kitu wanamzungumzia hasa pale walipogeuka na kumwangalia alipokaa wakati wa majadiliana yao. Anajisikia vibaya, sio kwa sababu anahisi amezungumziwa bali kwa kile kilichowafanya wamzungumzie. Anajua dhahiri kuwa walimzungumza kutokana na yeye kujitenga na kukaa peke yake. Anataka aweze kuyashinda mazoea hayo mabaya yaliyomjengea tabia ambayo haimpi uhuru, kwani kukaa na wasichana sehemu moja ulikuwa ni mtihani uliomfelisha mara nyingi sana, jambo ambalo halipendi hata kidogo. Anatamani awe aina ya mwanaume bora anayejiamini na mwenye umaarufu kwa watu wengi zaidi badala ya kuwa duni asiye na mvuto wala thamani kwa wengine kama fikra zake zilivyompelekea.



    Anamaliza kula chakula. Anaingiza mkono wake katika mfuko wa suruali yake na kutoa simu yake ya mkononi. Anafungua sehemu ya ujumbe mfupi wa maneno kisha anamtumia ujumbe rafiki yake Machallo

    ‘natangulia room’.

    Anaondoka kwenda chumbani huku kichwani akiwa na mawazo mazito akiwaza namna ya kushinda hulka yake iliyojenga tabia ambayo inamnyima uhuru na furaha kwa ujumla. Anafika chumbani, anasimama mbele ya kioo kikubwa kilichopo pale chumbani kuanza kujitathmini. Anajiona kuwa ni mwanaume bora, mwenye umbo zuri lenye mvuto na kila sifa inayomfanya kuwa bora kuliko vile alivyo.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Anavuta taswira ya rafiki yake Selike na wanaume wengine pale chuoni ambao wana umaarufu mkubwa kuliko yeye, anagundua kuwa wengi wao hawana sifa kama zile anazozishuhudia katika taswira yake mbele ya kioo anachotazama. Uzuri wa umbo la kiume lililojengeka na kumfanya kuwa na mvuto kwa baadhi ya wanawake ambao mara kadhaa walishamsifia kwa nyakati tofauti linamfanya ajione anastahili kuwa aina ya mwanaume anayotaka. Lakini bado anajua iko kazi kubwa na ngumu ya kujenga fikra za kujiamini na kubomoa zile za kutojiamini, aibu na woga.



    Anaketi na kuchukua simu yake ya mkononi ambayo ina huduma ya mtandao wa intaneti, anafungua ajifunze mambo yatayomfanya awe mwenye kujiamini na kuondoa hofu kwa watoto wa kike. Anafungua katika mtandao wa google na kuandika kile anachokikusudia kujifunza. Yanakuja matokea mengi, anachagua yale anayoona yanaelekeza vizuri kile anachokusudia kujifunza. Katika kuperuzi anakutana na mbinu zinazomfurahisha na kumfanya ajifunze kwa makini kuwa aina bora ya mtu anayohitaji. Maelezo yanaenda mbali zaidi kiasi cha kugusa uhalisia wa maisha yake anaona kuwa mwandishi wa ule mtandao alidhamiria kuandika kwa ajili yake kutokana na kuainisha sababu zinazomfanya awe vile, ambazo zina uhalisia mkubwa kwake.



    Anadhamiria kuanza kuyafanyia kazi mashauri aliyosoma katika wavuti ile ambayo aliamini yatakuwa ni msaada mkubwa kwake kuweza kuondokana na kuishinda kabisa ile hali duni aliyokuwa nayo kisaikolojia. Anajua haitakuwa kazi ndogo wala haiwezi kutokea kwa siku moja, ila ingechukua muda na kuhitaji uvumilivu mkubwa. Lakini anajihakikishia,

    ‘lazima nifanikiwe kwani maisha ni mapambano kujenga kile ninachokikusudia maishani, kukitunza na kukilinda. nisipopambana, kujenga wala kukilinda ninachokikusudia, kile nisichokusudia kitachukua nafasi kama silka na kutawala maishani’



    Selike anamaliza kula wakati ambao akina Maunda na wale rafiki wengine walishamaliza. Anaamua kuaga na kuondoka huku akiwaacha akina Maunda pale wakisuburi waletewe bili. Anafika chumbani na kumkuta Machallo akiwa ‘bize’ na simu yake ya mkononi. Anamuuliza kama anawasiliana na watu kupitia mitandao ya kijamii, Machallo anamweleza kwamba alikuwa akiperuzi habari katika mtandao. Hakutaka kumweka bayana kwa wakati ule kuhusiana na jambo linalomsumbua akilini kutaka kuzishinda fikra zake zinazomwangusha.



    Selike anamweleza Machallo kuwa waende darasani kwa ajili ya kujisomea.

    ‘Najisikia ovyo leo’. Machallo anatoa udhuru

    ‘……….haina shaka, pumzika’. Anaeleza Selike huku akikusanya vitabu vyake vya rejea na kumuaga rafiki yake, kwenda darasani. Anapotoka, kabla hajamaliza kufunga mlango anakumbuka kumweleza Machallo jambo ambalo alipaswa amwambie. Anarudi ndani kumweleza Machallo kuwa, walipokuwa ‘canteen’ kupata chakula yule aliyemwita alikuwa ni Maunda. Alijua siyo mgeni machoni mwa Machallo hivyo alijua bila shaka Machallo anamfahamu japo alikuwa na wasiwasi huenda hawafahamu wale rafiki wengine waliokuwa wameambatana naye. Hivyo anaamua kumfahamisha Machallo kuwa, aliyekaa jirani naye (Selike) anaitwa Joyce, anasoma kitiivo cha Mawasiliano ya Umma, wakati yule aliyekaa jirani na Maunda anaitwa Msope, yuko kitivo cha Elimu. Wote ni mwaka wa kwanza.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ‘Kuna kitu nimekisikia kwa masikio yangu mawili toka kwa Msope, ngoja nikupe mchapo huenda ni zali la mentali!’ anaeleza Selike.

    ‘lipi hilo kaka?’ anauliza Machallo kwa hamaki akitaka kujua kilichojiri.

    ‘Msope amekusifia sana, anasema wewe ni mwanaume wa kipekee ambaye uko tofauti sana na wengine. Mpole, mwenye kujiamini, pia uko ‘serious’ na mambo. Anapenda sana awe karibu nawe ila anasema tatizo anakosa namna ambayo anaweza kukuweka karibu’. Ndivyo anavyomalizia Selike na akifungua mlango kuondoka kwenda kujisomea huku akisisitiza

    ‘mi nimefikisha ujumbe kama nilivyosikia’.



    Maneno yale yanapokelewa kwa furaha moyoni mwa Machallo. Anagundua kuwa, yeye siyo duni machoni mwa akina dada warembo kama alivyokuwa akidhania awali. Suala linarudi pale pale alipokuwa anafikiria,

    ‘kujiamini na kuondoa woga’.



    Lakini maneno yale yalitoka kinywani mwa Selike ili kupoza mambo. Alihisi huenda machallo alijisikia vibaya alipokaa peke yake ‘canteen’ kitu kilichommbadili ‘mudi’ na kumfanya ashindwe kujumuika naye kujisomea jambo ambalo halijazoeleka kwa marafiki hao. Aliamini maneno yale yangemfanya ajione wa thamani mbele ya wengine, hasa akina dada ambao huwakwepa kama ukoma!



    Machallo anaendelea kutafakari huku akifungua mtandao wa intaneti kuendelea kujifunza zaidi baada ya kusitisha kwa muda wakati akisikiliza maongezi toka kwa rafiki yake Machallo kabla hajaondoka kwenda kijisomea. Anafungua historia ya mwigizaji mkubwa na mashuhuri sana duniani ambaye alikuwa ‘bongo lala’ almaarufu kama ‘kilaza’ darasani wakati akisoma. Anavutiwa sana pale anaposoma kuwa alikuwa ni mtu wa aibu sana na mwoga asiyejiamini. Alipoingia katika tasnia ya uigizaji, mwalimu wake alimfundisha na kumsaidia jinsi ya kujiamini na kuificha hofu aonekane shujaa pale anapoigiza. Machallo anajikuta akitokea kuvipenda vipengele vinavyoelezea jinsi ya kuwa mtu unayejiamini vilivyoainishwa pale na kudhamilia kuvifanyia kazi ili abadilishe mazoea yake ambayo tayari yalishajenga tabia iliyokomaa. Anamaliza kujisomea katika wavuti ile, anafunga huduma ya mtandao na kuchukua filamu inayoitwa ‘Famous’ iliyoigizwa na muigizaji huyo nguli ambaye ametoka kusoma habari zake kwenye mtandao kisha anaanza kuitazama

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya kuitazama filamu hiyo iliyodumu kwa takribani saa 2, Machallo anajikuta akitokea kuipenda sana na kutamani awe na tabia iliyojengwa katika uhusika aliouvaa Elvin, mwigizaji mashuhuri ambaye ndiye nyota katika ile filamu. Anazima televisheni kisha anajipumzisha kitandani huku akitafakari hili na lile yote yakiwa yanalenga kumfanya awe mtu bora. Wakati akiendelea kutafakati, taratiiibu usingizi unamnyemele na kumpitia. Anashtuka usiku wa manane, kutazama saa, inamuonesha ni saa nane usiku. Ukimya umetawala sio tu pale chumbani ambapo kila mtu alishalala, bali hata nje ambako palikuwa na utulivu kuashiria kila kiumbe alikuwa tayari ameshalala isipokuwa bundi na popo ambao ndiyo mida yao ‘kuvinjari’



    Usingizi unapaa kwa muda, anaamua kuchukua simu yake na kufungua sehemu ya mtandao wa intaneti ili aendelee kujisomea zaidi na kukazia maarifa juu ya kile alichojifunza. Hizi zilikuwa ni jitihada katika harakati zake za kuitawala akili yake na kuiongoza kufanya yale anayokusudia bila kukatishwa na fikra dhaifu. Dakika zaidi ya arobaini za kuperuzi mtandao wa intaneti zinakoma pale anapochoka na kuamua kuiweka simu yake pembeni na kuvuta shuka tayari kwa ‘kuuchapa’ usingizi.



    Anaamka asubuhi na mapema. Anaenda kufanya mazoezi ya viungo kama ilivyo desturi yake na kurudi kwa maandalizi ya kuanza ratiba ya masomo katika siku ile. Anapoingia chumbani anamkuta Selike akinyoosha nguo zake yakiwa ni maandalizi ya kuingia darasani. Anamueleza jinsi alivyofurahishwa na ujumbe wa Msope siku iliyopita huku akiulizia zaidi habari za Msope. Selike anaahidi kumweleza kinagaubaga baadaye, kwa wakati huo anamtaka akaoge haraka ili waweze kuwahi vipindi kwani muda umeenda sana, wamebakiza dakika chache kabla vipindi havijaanza.



    Wanamaliza maandalizi na kuingia darasani mahsusi kuanza vipindi. Awamu hii Machallo anaamua kuvaa moyo wa ujasiri na kujitahidi kuficha aibu zake mfukoni ukiwa ni mwanzo wa jitihada zake za awali kuhakikisha anajenga aina ya tabia anayoikusudia.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Darasani katika ukumbi wa mihadhara anakaa karibu na mabinti. Jirani upande wa kushoto amekaa na binti ambaye anaonekana yuko tayari kwa ajili ya mhadhara. Machallo anaamua kutumia sekunde chache zilizobaki kabla ya mhadhara kuanza, awasiliane na yule binti. Anamsalimu, dada anaitikia. Machallo anaenda mbali zaidi ya salamu kwa kumuuliza maswali ya udadisi kutaka kujua A B C D kuhusu huyo dada. Dada anakuwa mzito kujibu, jambo linalomjengea Machallo dhana ya kukata tamaa na kutaka kuachana na maongezi yale. Anahisi huenda yule dada anamchukulia Machallo sio wa hadhi yake. Wazo lingine linamjia kuitikia sauti inayotoka ndani inayomtia moyo kwa kumwambia yeye ni mwanaume hodari mwenye hadhi ya kimataifa hivyo asijenge fikra za kukataliwa.



    Anaamua kuanza upya au kama vijana wa siku hizi wanavyosema ‘kupanga swagga’.

    “…..unanukia vizuri!” Anamsifia yule dada.

    ‘Asante’ dada anajibu kwa bashasha tele!.

    Chezea Machallo wewe…..!!??’

    Machallo anadhamiria kumuuliza swali yule mrembo, anapofumbua mdomo wake kuanza kuzungumza, anakatishwa na sauti ya Mhadhiri ambaye alikuwa tayari kwa ajili ya kuanza Mhadhara unaodumu kwa saa moja.

    Saa moja la mhadhara linaisha, machallo anaamua kutafuta fursa ya kupiga soga na yule kigoli. Bahati mbaya yule dada alishaondoka mapema bila yeye kujua hivyo mpango mzima unakwama.





    ************

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    :: Unavyodhani nini kitaendelea hapo?



    :: Huu ni mwanzo tu wa simulizi hii kali na ya kuvutia



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog