Simulizi : Kitanzi, Kisu Na Bastola
Sehemu Ya Pili (2)
SALIMA alishtuka kutoka usingizini baada ya kuhisi alimsikia Dedan akitamka maneno ambayo hakuwa na uhakika nayo.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Akaamka kitandani na kumsikiliza kwa makini kama ni kweli Dedan ndiye aliyekuwa akiyatamka maneno yale. Akagundua kuwa kweli alikuwa yeye.
Alipomsikia mara ya pili na ya tatu, akagundua moja kwa moja kwamba, Dedan hakuongea maneno yale kwa bahati mbaya. Ni wazi kuwa alianza kurudiwa na kumbukumbu zake. Salima alifurahi kidogo alipomsikia kijana huyo kwa ufasaha zaidi akitamka ‘Caro,’ neno ambalo bila shaka lilikuwa jina la mwanamke.
“Caro!” Salima alistaajabu kimoyomoyo huku akimuangalia Dedan aliyekaza macho akiliangalia pazia lililokuwa likiyumbishwa kila upande na upepo uingiao ndani kupitia dirisha.
Awali, Dedan alikuwa akitamka neno moja tu, “mmm’’ kila alipokuwa akiulizwa swali. Ajabu ni kwamba neno hilo limebadilika ghafla kwa usiku mmoja na kuwa Caro. Kwa wakati huo kila alipokuwa akiulizwa kitu alitamka jina hilo huku machozi yakimtoka hali iliyosababisha Salima ahisi kuna uhusiano mkubwa kati ya Dedan na Caro.
“Labda ni ndugu yake,” aliwaza kwa wasiwasi huku akishindwa kuzizuia hisia zake kwamba huenda Caro alikuwa ndiye chanzo cha Dedan kuwa katika hali ile na labda ilikuwa bora aendelee kukaa kimya tu asije akayaibua mambo mengi ambayo yalikuwa yametulia.
Salima alitambua kuwa ni lazima afanye utafiti binafsi kuhusu huyo mwanamke Caro. Aliamini lazima kutakuwa kuna kitu kati ya wawili hao.
Akawa kama anakumbuka kitu fulani, akainuka na kulivuta sanduku moja kutoka chini ya uvungu wa kitanda akafungua zipu yake na kulitazama ndani. Aliviweka pembeni vyeti na picha za Dedan na kupekuapekua kila upande akilenga kutafuta kiashiria chochote kuhusu namna gani Caro na Dedan walikuwa wakifahamiana.
Alitafuta mpaka akachoka, hakukuwa na cheti wala karatasi iliyokuwa na jina la Caro. Alitazama kila mahali akijitahidi kukumbuka kama kuna kitu cha Dedan alikiweka mahali pengine zaidi ya hapo, kwani tangu wahamie hapo alihakikisha kukitunza kila kitu cha Dedan bila ya kuvifungua ili kama mwenyewe atapona ampatie vitu vyake vikiwa salama.
Kwa wasiwasi aliokuwa nao alikubali kwa siku hiyo kuivunja kanuni aliyojiwekea na kupekua vitu vya Dedan bila ya ruhusa yake. Akainama na kulivuta furushi jingine. Ndani yake akatoa chaja, vifaa vya umeme, simu mbovu na nzima, vyote vikiwa ni vifaa vya dukani kwa Dedan.
Alipoziona simu ndipo akaikumbuka simu ya Dedan ambayo wala hakuwahi kuifikiria kwa muda wa takriban miezi mitatu tangu Dedan alipoanza kuumwa. Akaiwasha na kushusha pumzi akisubiri utitiri wa meseji uanze kuingia.
***
Side alikuwa akimfuatilia kwa karibu sana msichana huyo aliyekuwa adimu sana kuonekana mitaani, alihakikisha anaijua vema nyumba aliyokuwa akiishi. Alipomwona akiingia chumba kimoja kati ya vile vya mkono wa kulia, akatabasamu na kuingia ndani ya gari lake aina ya Toyota Hilux na kuondoka eneo lile.
Huku akiendesha gari, Side aliipokea simu yake iliyokuwa inaita na kuiweka loudspeaker.
“Vipi? “ sauti nzito ilisikika kutoka kwenye simu.
“Bro, nimeshapajua anapokaa,” Side alijibu huku akitabasamu kana kwamba alikuwa amefanikisha jambo muhimu sana.
“Kweli?”
“Huamini kesho nikupeleke?”
“Duh! Kweli dogo we ni noma aisee, njoo basi haraka unipe fulu stori.”
“Nipo njiani nakuja usiende sehemu yoyote kaka,” aliongea Side huku mikono yake ikiwa bize na kuzungusha usukani wa gari akikwepa vidimbwi vilivyojazana katikati ya barabara.
***
Baada ya muda, simu ya Dedan iliunguruma mara mbili kuashiria meseji mpya imeingia. Akatulia kimya asiifungue akitaka meseji zote ziingie kwanza ili aanze kuzisoma taratibu.
Alihesabu moja mpaka ishirini haikuingia meseji nyingine, akaamua kufungua na kuisoma. Cha ajabu haikuwa na jina la mtumaji na ilikuwa fupi sana isiyoonesha hali, dhamira wala jinsia ya mtumaji. Iliandikwa tarakimu ‘90’.
Salima aliisoma mara nyingi bila kuijua maana yake kiundani, akaipuuza na kuanza kuzisoma meseji nyingine zilizokuwepo ndani ya simu hiyo tangu awali. Akagundua meseji nyingi zilitumwa kwa namba ileile iliyotuma meseji muda ule. Akiwa haamini alichokigundua ghafla simu yake ikaanza kuita, alipoiangalia aliona namba ile
aliyotumiwa ujumbe.
Ilikuwa kama vile mpigaji alikuwa akiiangalia simu yake muda wote, maana kama isingekuwa hivyo angewezaje kujua kama ujumbe wake umefika kwa mtu aliyemtumia?
Salima alikuwa makini, alitafakari kwanza kabla ya kuipokea simu ile kwa vile ndiyo kwanza alikuwa ameanza kuzisoma meseji zilizokuwa zimejazana kwenye simu ya Dedan.
Aliamini kwamba ni vyema kama angejua kwanza jambo lolote kuhusu mpigaji simu huyo kabla hajaipokea na kuongea naye akihofia asije akajianika yeye na Dedan wake kwa watu wabaya ambao huenda kwa njia moja ama nyingine walishiriki kumfanya jamaa yake huyo kuwa katika hali ile.
Kwanza alimtazama mgonjwa wake ambaye alikuwa ameshaanza kusinzia kwa uchovu wa chai na mihogo ya kukaanga aliyokuwa amemlisha, kisha akaipokea ile simu na kusikilizia sauti ya mpigaji.
“Haloo!” sauti ya kike ilisikika…
“Halo Dedan!” mpigaji aliendelea kuita huku Salima akiwa amejikausha.
“Haloo, mimi ni Carolina. Najua nimekuumiza sana kwa yote niliyokufanyia, tafadhali naomba unisamehe mpenzi wangu, haikuwa dhamiri yangu kukuumiza. Please Dedan naomba unijibu basi,” aliongea msichana huyo kwa huzuni huku kwikwi na kilio vikisikika kwa mbali.
Baada ya kulisikia jina la Caro, Salima akahisi kama vile alikuwa akitaka kupasuka kwa jinsi alivyovimba kwa hasira. Ule uchizi na jazba alizokuwa nazo zamani zilianza kumpanda kichwani na kujikuta akishindwa kujizuia kwa ghadhabu alizokuwa nazo.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Msichana huyo akasonya na kukata simu kwa kuizima kabisa huku mishipa ya damu ikiwa imemsimama kichwani.
“Hakuwepo wakati unaumwa, leo anajifanya anakupigia simu akiomba msamaha. Kama yeye mwanamke kweli tutaona kama atakupata. Eti oooh! Mimi Carolina mpenzi wako, anajua nimekugharamia vingapi? Mbona hakujitokeza siku zote hizo. Anachezea moto, we muache tu!” Salima aliongea kana kwamba alikuwa akimwambia Dedan badala ya Carolina mwenyewe.
Kipindi chote hicho Dedan alikuwa amelala, lakini alipolisikia jina la Carolina likitajwa na Salima akashtuka na kukaa kitandani akimkazia macho bila kuyafumba huku akihema kwa kasi kama amekutana na jinamizi.
Salima aliogopa kumuona Dedan katika hali ile, akamfuata na kumbembeleza taratibu hatimaye akalala tena kitandani. Salima alishindwa kujizuia kustaajabu jinsi Caro alivyouteka moyo wa Dedan, yaani hata katika hali ile ya kutojielewa, lakini alimkumbuka vizuri kiasi cha kumtajataja kila mara.
***
Ilipofika saa tano juu ya alama, Side alikuwa tayari ameshafika kwa John Chakos kumpa kila kitu alichokuwa akikifuatilia asubuhi na mapema ya siku hiyo.
Ndani ya chumba kizuri katika Hoteli ya Toptown Wild Wind mwanaume mrefu mwenye rangi ya kitasha alitokea kutoka maliwatoni akiimba kwa mikogo huku akiwa na kitaulo tu.
Alimtazama Side aliyekuwa amekaa kwenye sofa bila wasiwasi akiitazama sehemu ya jiji zima la Dar kupitia dirisha kubwa la kioo kwa mwonekano wa juu. Ilikuwa ni ghorofa ya kumi na saba.
Mtu yeyote anayepanga vyumba vya hoteli hiyo kwa vyovyote vile huwa na utajiri wa mabilioni ya fedha kiasi kwamba haimuumi kulipa laki sita kwa siku moja kama gharama ya kukaa hotelini hapo.
Japo Side ni mtoto wa mjini kiasi cha kulijua vyema Jiji la Dar na vichochoro vyake, lakini siku hiyo alikubali kutolewa ushamba kwa kuingia katika hoteli yenye hadhi kama hiyo.
John Chakos ni mmoja kati ya matajiri wachache walionufaika kwa kuwatumia wasichana wachache wa tabaka la chini kwa biashara ya ngono. Kwa mujibu wa uchunguzi wake, Side alibaini kuwa wasichana wachache walioonekana warembo, hupangiwa kulala na wageni mbalimbali wa kiume wajao nchini kwa malipo ya kiasi fulani cha fedha.
Kwa donge nono, Side alipewa kazi ya kuhakikisha kila mara alikuwa akiwatafuta wasichana hao kutoka mitaani. Alianza kazi yake taratibu na sasa amekuwa mzoefu na mwenye mafanikio makubwa.
Alikuwa akipiga picha za wasichana kadhaa na kuzinadi kwa bosi wake, ikiwa picha ya mrembo mmoja ilikubaliwa basi lilikuwa ni jukumu lake kumfuatilia na kumpeleka kwa bosi wake kwa kumlaghai kwa pesa kidogo.
Siku hiyo Side alikuwa amekwenda kukabidhi ripoti ya uchunguzi wake wa awali kuhusu mmoja wa wasichana warembo aliyekuwa akimfuatilia kwa muda mrefu. Tofauti na wasichana wengine ambao Side alikuwa akiwapeleka kwa bosi wake, msichana huyo alionekana kuzitawala fikra za bosi wake, Mr. John Chakos. Alimuulizia kila mara na kumtaka aharakishe kukamilisha ripoti yake na kumpelekea chumbani mwake tofauti na utaratibu wa kawaida.
Kiasi fulani machale
yalimcheza Side na kuanza kuhofia juu ya hatima ya msichana huyo aitwaye Salima Rajab.
HAKUWAHI kuwa na rafiki wala ndugu aliyepajua alipokuwa akiishi tangu ahamie kwenye mtaa huo mpya.
“Huyu atakuwa ni nani?” aliwaza Salima.
Kengele ya hatari ikalia kichwani mwake, akausogelea mlango na kufungua kidogo akichomoza kichwa chake kwanza ili kutotoa mwanya wa mtu huyo kuchungulia ndani ya chumba chake ambacho pasipo ubishi kilikosa hadhi ya kuitwa chumba, ingawa Salima mwenyewe alifanya hivyo ili kumficha Dedan asionekane.
“Habari yako,” alisema mwanaume mrefu kidogo mwenye kila sifa ya kuitwa bosi au mkuu wa kitengo fulani kwa jinsi alivyovalia kiofisi na haiba yake.
“Sa…salama tu…nikusaidie nini?” alisema Salima kwa kigugumizi.
“Naitwa Saidi Hamis Kibona, eee.. Wewe ni Salima?”
“Haa...hapana haa..no, ni mimi, unashida gani?” kwa woga Salima alijikuta akikataa na kukubali kwa pamoja.
“Usiwe na hofu dada yangu, mimi ni wakala kutoka kwenye Kampuni ya kigeni iliyoingia nchini Tanzania. Mmm… Mara nyingi tumekuwa tukitembelea nchi kadhaa tukifanya sanaa ya urembo na wasichana mbalimbali hasa tunaowaona wana vigezo.”
“Kwa hiyo nikusaidie nini?”
“Kama nilivyokwambia awali, huwa tunafanya kazi na msichana tunayemwona ana vigezo, eee.. Salima nadhani bahati hii imekuangukia wewe.”
“Mbona sikuelewi! Hebu kwanza niambie jina langu umelijuaje?”
“Kwani una wasiwasi gani, nimeuliza nikatajiwa au kuna ubaya wowote dada yangu?”
“Hapana sikuwa na maana hiyo,” alijibu Salima akiwa bado na wasiwasi mkubwa.
“Usijali Salima, nadhani utanielewa vizuri, kwa sasa naomba nikupe fomu hii ambayo ina maelekezo yote kuhusu historia na jinsi kampuni yetu inavyofanya kazi zake.”
Side alifungua begi lake na kutoa bahasha ndogo akamkabidhi Salima.
“Maelekezo yote yapo humo. Tafadhali yasome taratibu na kama umevutiwa kufanya kazi na sisi, tuwasiliane,” alisema Side na kuondoka.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Salima alipokea bahasha ile kwa mshangao na kurudi chumbani kwake, lakini akaona siyo vizuri mgeni aondoke bila kumsindikiza. Akajitanda kanga mabegani na kutoka nje haraka akimuwahi Side.
“Ngoja nikusindikize mgeni,” alijibaraguza Salima kwa aibu baada ya nafsi yake kumsuta kwani awali hakuweza kumchangamkia wala kumkaribisha ndani kwa ukarimu, lakini hata kumsindikiza pia asiweze! Aliona siyo picha nzuri kwa mgeni huyo na pengine angeweza hata kuikosa kazi nzuri kutoka katika kampuni hiyo kwa kuwa tu hakuwa mkarimu kwa mtu huyo.
Side aligeuka na kumtazama Salima aliyemkimbilia. Wakatembea wakiongozana bila ya kuongea jambo lolote kimyakimya mpaka nje ya nyumba. Kwa mshangao Salima alimuona Side akiutoa ufunguo na kufungua mlango wa gari moja zuri na kuingia ndani yake.
“Salima, nafasi ni chache sana fanya maamuzi haraka sana hata leo jioni nijulishe kama umevutiwa na kazi yetu,” alisema Side huku akiwasha gari lake na kuondoka, moyoni akifurahi kwa mtego aliomtega Salima.
Watano kati ya wasichana aliokwisha wakabidhi kwa Mr. Chakos walikuwa wepesi sana kuwapata. Kwa maisha mabovu waliyokuwa wakiishi, hakupata tabu kunasa kwani wengi walipotajiwa tu kiwango cha fedha watakazolipwa waliruka kwa furaha bila kujali wangedhalilishwa kwa kiasi gani. Pesa ilikuwa na thamani hapa kuliko hata uhai wa mtu katika jiji hili na Side alilijua hilo fika.
Salima tu ndiye aliyekuwa tofauti na wasichana wenzake na kumfuata kwa njia ya kawaida kungesababisha kumpoteza msichana huyo. Kutokana uzuri wa sura na hata umbo lake.
***
Salima aliifungua haraka bahasha hiyo, akasoma na kuvutiwa na hadhi na mshahara mkubwa wa kazi hiyo. Akafurahi kuona hatimaye angeweza kupata fedha za kumtibia Dedan na kufanya mambo mengi ya kimaendeleo. Moyoni mwake alikubali kuajiriwa na kampuni hiyo akaitafuta simu ya Dedan na kuiwasha akidhamiria kumtaarifu Side ili asije akaipoteza nafasi ya kazi hiyo adimu.
Alipoiwasha simu mara meseji ziliingia kwa fujo, zote zikiwa zimetumwa na Caro moja ilisomeka kwa tarakimu ’91.’
“Huyu mwanamke mchawi hizi namba ana maanisha nini!” alistaajabu Salima na kuzipuuza.
***
Side akiwa na wasiwasi kama mtego wake utanasa au lah, alisimama kama punguwani akipiga hatua mbele na nyuma huku macho yake kila saa yakiiangalia saa yake ya mkononi.
Alitaka amalize kila kitu kabla hajampeleka Mr. John Chakos kuhakiki makazi ya Salima. Alitaka amshtukize bosi wake na pengine kwa kutaka kuonekana mfanyakazi bora kwa kukamilisha kazi zake mapema.
Kwa muda wote huo alikuwa akiisubiri simu kutoka kwa Salima kwani kwa mkwara aliomuonesha msichana huyo, isingekuwa rahisi kutobabaika na kuamini kwamba alikuwa hatanii kuhusu kazi hiyo.
Majira ya saa tano na nusu asubuhi, Dedan aliamka akihisi maumivu makali ya tumbo. Laiti kama angekuwa na ufahamu basi angetambua kwamba alisumbuliwa na njaa kali.
Kila siku alikuwa akilishwa na kufanyiwa kila kitu na Salima. Bado hakuwa na kumbukumbu kuhusu kitu chochote katika maisha yake na mbaya zaidi hata kutembea na kuongea ulikuwa mtihani.
Ingawaje alikuwa hakumbuki vitu vingi sana, lakini tabia ya asili ya kibinadamu ilimfanya kuwa na utambuzi juu ya matendo yote ambayo huleta maumivu na yale yaletayo furaha, kwa hiyo alilia kwenye maumivu na kutabasamu au kucheka kwenye furaha.
Kwa mara ya kwanza Dedan akasimama na kutembea akikisogelea kiberiti kilichokuwa juu ya meza, akatoa njiti moja na kuisugua upande wenye baruti. Huenda jambo hilo alijifunza kwa kumuona Salima alipokuwa akiwasha moto kila alipokuwa akitaka kupika. Moto ukawaka huku ile njiti ya kiberiti ikiwa mkononi mwake.
Iliwaka huku moto ukishuka taratibu na kuongeza joto kwenye vidole vyake. Kwa maumivu ya kuungua akaitupa njiti ile chini kwa bahati nzuri ilizimika pasipo kuunguza kitu chochote.
Kwa kiasi fulani mwanga wa kumbukumbu za kale ukapita akilini mwake. Siku hiyo akaanza kutambua kwamba kuna kitu kuhusu yeye hakijui. Akaangaza macho yake kila kona ya chumba kile kama mgeni huku akikosa majibu ya maswali kibao aliyokuwa nayo kichwani.
Akastaajabu yeye ni nani na alikuwa akifanya nini humo ndani! Kanga na nguo za kike zilizokuwa zimesheheni humo chumbani, kwa kiasi fulani zilimuogopesha. Hisia zake zikamtuma kwamba kulikuwa na mwanamke aliyekuwa akiishi, mwanamke huyo ni nani? Alijiuliza.
Kitu ambacho pengine mwanadamu wa kawaida hukichukilia pasipo na uzito kwenye nyumba, ‘mlango,’ kwa Dedan mtazamo wake ulikuwa tofauti sana juu ya kifaa hicho muhimu kiasi kwamba alipouona tu aliutambua mara moja. Mbao nne zilizounganishwa pamoja, bawaba na kitasa chenye tundu la ufunguo ndiyo vilikuwa vitu muhimu sana kwa muundo wa milango mingi ya uswazi.
Kwa Dedan, mlango haukuwa njia ya kutoka nje na kuingia ndani tu. Hata katika ulimbukeni aliokuwa nao, bado aliuona mlango kama alama ya tumaini baada ya kiza cha utumwa na ufungwa. Ndani kulikuwa ni kizuizi chenye upweke wakati nje ilikuwa ni uhuru na furaha hatimaye.
Haya yote alijifunza alipokuwa mvulana mdogo sana. Shangazi yake Bi. Tabia alikuwa akimfungia mara kwa mara ndani, mchana na usiku bila kutoka nje huku adhabu kubwa aliyopewa na shangazi yake huyo ikiwa ni kuchomwa na moto mikononi.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mambo hayo yote aliyavumilia kwa kuwa hakuwa na mzazi aliyekuwa hai kumtetea. Kwa hiyo aliishi katika mazingira hayo mpaka siku moja alipoweza kutoroka kwa kuufungua mlango kuelekea kwenye uhuru na furaha ya kuwa nje aliyokuwa akiitamani siku zote.
Nje ya mawazo hayo, Dedan aliutazama ule mlango kwa muda kisha akaukimbilia haraka, akauzungusha mkono wa kitasa na kujaribu kufungua, lakini haukufunguka. Akauvuta kwa nguvu; haukufunguka pia. Moyoni alijua halikuwa jambo rahisi kwani hata alipokuwa mtoto mdogo, pindi alipofungiwa mlango na shangazi yake alikuwa akitumia waya au msumari kuchokonoa tundu la mlango mpaka ufunguke.
Akaanza kuutafuta waya au msumari ndani ya chumba hicho, kwa bahati nzuri akaupata msumari mkubwa wa bati. Akausuguasugua ardhini na kuufanya bapa kisha akaupenyeza kwenye tundu la kitasa na kuanza kuchokonoa taratibu huku akiwa amefumba macho yake kana kwamba alikuwa akivuta hisia.
Kwenye mawazo yake aliiona sura mbaya ya shangazi yake ikimkaripia, hofu ikaanza kujijenga taratibu huku kila kitu ndani ya chumba hicho kikigeuka na kuwa kama vile cha shangazi yake huyo. Kwa mara nyingine mlango ukawa alama ya uhuru kwa Dedan, kwa muda huo alitaka sana kuwa huru tena.
Akajitahidi kuchokonoa kitasa hicho na mara kikazunguka na kichuma cha loki kikajiachia na kurudi ndani kadiri alivyokuwa akiunyonga msumari huo.
Akaufungua mlango na kutoka nje kwa kupita koridoni hadi nje ya nyumba. Njiani akikutana na sura tofauti za watu wengi wakimtazama na kumshangaa kwa jinsi alivyovaa vibaya na jinsi uso wake ulivyomvimba kwa usingizi na njaa.
Akakatiza mitaa kama chizi kwa bahati mbaya alikoswakoswa na magari mengi barabarani.
Tangu alipofika asubuhi, alikuwa akitolewa chumba kimoja na kupelekwa chumba kingine. Alishangaa sana alipoingia kwenye chumba kidogo chenye mvuke wenye joto kali kiitwacho ‘Sauna’, aliambiwa mvuke huo humsafisha mtu kuzidi hata maji ya kawaida ambayo tumezoea kuyaoga.
Kisha akapelekwa chumba cha ‘massage’, humo alikandwakandwa na warembo wenye mikono laini utadhani mikono yao haifanyi kazi nyingine yoyote zaidi ya hiyo, kwani kwa jinsi mikono yao ilivyokuwa laini hakuna aliyeonekana kuwa na uwezo wa kushika shoka na kukata kuni au hata kusugua majungu yenye ukoko na masizi.
Akapelekwa chumba kingine ambacho kwa huduma alizozipata humo alikitambua kama saluni ya kike. Humo alisetiwa nywele na kufanyiwa ‘facial’, ‘manicure’ na ‘pedicure.’
Kwa mambo hayo Salima alijikuta akisahau kabisa kuhusu Dedan ambaye kwa wakati huo alikuwa akitembea toka mtaa mmoja hadi mwingine bila kuelewa mahali alipokuwa akielekea au hatari iliyokuwa ikimkabili.
Wasichana wengi wazuri na warembo walimzunguka kila mmoja akifanya kazi fulani katika mwili wake. Alitumia muda mwingi sana akistaajabu, jinsi gani urembo wa mwanamke ulivyokuwa na gharama! Alishukuru tu kwamba kila kitu kilikuwa kikilipwa na kampuni hiyo aliyoitambua kwa jina la ‘Serenity’ .
Kwa muda wote huo Madam Flaviana alikuwa amekaa pembeni ya Salima akimtazama kana kwamba alizidi kuwa mpya kwa kadiri alivyokuwa akipambwa. Ilisemekana kuwa mwanamke huyo alikuwa na uwezo wa kumpima mtu kwa kumtazama tu na kujua haraka vipimo vyote vya nguo yake, kuanzia ukubwa wa kiuno, urefu, mpaka upana wa mabega.
Inawezekana kabisa Madam Flaviana alikuwa akimtazama Salima kwa lengo hilo, lakini kuna kitu cha ajabu ambacho Salima alihisi baada ya kumtazama jinsi Madam Flaviana alivyokuwa akimuangalia, lakini alipuuzia na kukaa kimya.
“Salima, unajua kama wewe ni mrembo sana?” alisema Madam Flaviana huku akimwangalia Salima kuanzia chini mpaka juu.
“Mbona mi wa kawaida sana,” Salima alijibu kwa aibu kidogo.
Ukweli ni kwamba Salima hakujali sana urembo kama wasichana wengine kiasi cha kujijua na kujua watu wengine wanamuonaje. Alikuwa msafi na mzuri wa asili asiyependa kuupoteza muda wake mwingi mbele ya kioo, hivyo hakuwa akijifahamu kama ni mzuri kiasi hicho cha kusifiwa na Madam Flaviana, kilicho kuwa akilini mwake wakati huo ni harakati za kutoka kimaisha tu.
“Oke, twende nikakuchagulie nguo,” alisema Madam Flaviana bila kutaka kuendeleza ubishi kwa mtu ambaye haifahamu thamani ya uzuri wake. Alichowaza akilini ni kumtumia kwa manufaa ya kampuni yao haramu. Salima kwao alikuwa ni kama ndege mjinga asiyejua thamani ya mlio wa sauti yake, hilo lilikuwa jambo la kujivunia kwa Madam Flaviana, akapenda abakie hivyohivyo.
Akiwa katika chumba kilicho sheheni nguo mbalimbali, alichaguliwa nguo moja baada ya nyingine na kutakiwa kuzijaribu. Nyingi zilikuwa fupi, zenye kubana. Kila mara alivyotoka kwenye chumba cha kubadilishia nguo na kuvaa nguo nyingine, Madam Flaviana alionekana kumuangalia sana bila kusema chochote zaidi ya kumkabidhi nguo mpya badala ya ile ya mwanzo na kumtaka aendelee kuzijaribu.
Hatimaye zoezi hilo la kuchosha lilimalizika kwa Salima na kuvaa nguo moja iliyombana sana kisha wakaelekea kwenye mgahawa kwa ajili ya chakula cha mchana.
Kila kitu kilikuwa kipya sana kwa Salima, akafundishwa jinsi ya kuketi kistaarabu, jinsi ya kula kwa kutumia uma na kisu, akafundishwa jinsi ya kufungua shampeni na kuzungumza kwa staha na haiba za kike. Yote alionekana kuyashika haraka sana kiasi cha kumfurahisha Madam Flaviana.
“Mama yangu!” Salima alishtuka baada ya kugundua kuwa muda mrefu ulikuwa umepita tangu amuache Dedan peke yake. Akasimama na kutaka kuondoka kama mtu aliyechanganyikiwa.
“Salima nini tatizo?” aliuliza Madam Flaviana baada ya kugundua kubadilika ghafla kwa hali ya Salima.
“Nimemuacha mgonjwa peke yake tangu asubuhi nilipokuja huku, nilipitiwa na kumsahau kabisa, sijui hali yake itakuwaje maana hawezi hata kusimama na kula mwenyewe.”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Usihofu sana, hii ni saa nane tunaweza kumuwahi kwa gari langu. Twende haraka,” aliongea Madam Flaviana kisha wote wakaondoka.
Wasiwasi ulimjaa sana Salima, akaona hata gari lenyewe lilikuwa halikimbii kwa kasi aliyokuwa akiitaka, lakini alijikaza na kuvumilia bila kuteremka. Kimoyomoyo alisali sala zote bila kujali dini wala lugha aliyoitumia ilimradi tu sala hizo ziweze kumfanya Dedan awe mzima mpaka saa atakayofika.
“Usihofu Salima, utamkuta tu akiwa mzima,” alisema Madam Flaviana kwa huruma huku akiuzungusha usukani na kuongeza spidi kila ilipompasa kufanya hivyo.
“Madam, hujui tu Dedan ana umuhimu gani kwangu ndiyo maana unasema kirahisi hivyo,” aliongea Salima huku machozi yakimtoka bila kujua kama alilitaja jina la Dedan kimakosa katika maneno yake aliyoyasema.
“Kwani mgonjwa wako anaitwa Dedan? Mmm...ni nani yako?” Madam Flaviana alimuuliza maswali mfululizo Salima.
“Aahh...ni mpenzi wangu tu,” aliongea Salima kwa kigugumizi baada ya kujishtukia kwamba alilitaja jina la Dedan kimakosa.
“Oooh! pole sana, kwani anaumwa nini?”
Kwa swali hilo Salima akawa kimya akijishauri kumwambia au kutomwambia Madam Flaviana, hata hivyo aliamua kumsimulia ukweli wote kwani kwa hali ilivyokuwa asingeweza kuyazuia maswali kutoka kwa mwanamke huyo kwa wakati huo kwa kuwa alijikoroga mwenyewe kwa kumtaja Dedan mbele yake. Alihisi asingekuwa muungwana kwa kuficha kila kitu mbele ya Madam Flaviana ambaye alijitolea kumpeleka kwa gari lake mpaka nyumbani kwake bila hiyana.
Basi Salima alijikuta akimsimulia Madam Flaviana mwanzo mpaka mwisho kuhusu Dedan na yeye. Akamwambia kila kitu bila kuficha. Akabainisha pia hata dhumuni la kuamua kufanya kazi katika kampuni hiyo, ilikuwa ni kwa ajili ya mpenzi wake aliyekuwa akihitaji tiba na matunzo.
Madam Flaviana alishindwa kulizuia chozi lisimdondoke mara baada ya Salima kuhitimisha simulizi yake kwa kusema alikuwa akimpenda sana Dedan kiasi cha kufanya kitu chochote ili awe naye.
Madam Flaviana alimuonea huruma sana msichana huyo mdogo ambaye maisha hayakuwa mazuri sana kwa upande wake. Akaishia kumwangalia tu moyoni akitamani amuokoe na janga ambalo yeye pamoja na kampuni yake walikuwa wamemwandalia, lakini akasita na kuamua kumuacha tu katika bumbuwazi alilokuwa nalo kwa kuhofia kuwa kama angemwambia angesababisha hata uhai wake yeye mwenyewe kuutia mashakani kwani alimjua vyema Mr. John Chakos. Mwanaume mtanashati sana ambaye ukatili wake ulijificha vyema nyuma ya uzuri wa sura na umbo lake.
Madam Flaviana mwenyewe alikuwa kama mmoja wa wasichana waliokuwa wa kwanza kabisa kuuzwa katika biashara hiyo, ndiyo maana hakukuwa na mtu wakumshangaa kwa nini alikuwa mrembo sana.
Tuseme bahati tu ilikuwa upande wake. Uzuri wake ulimletea mafanikio makubwa na kujuana na watu wengi kutoka nchi mbalimbali. Pengine hiyo ndiyo ilikuwa salama yake kwani kampuni ingepata hasara kubwa kama ingemwachisha kazi baada ya umri wake kumtupa mkono kwa kuhofia kupoteza mtandao wa marafiki na wateja ambao Madam Flaviana aliutengeneza. Kwa kugundua hilo wakampandisha cheo na kuitwa ‘Madam’ ama ‘Bibi Mkuu,’ kazi yake ikiwa ni kuwafunza ustaarabu mabinti wapya na kuhakikisha wanatii sheria na taratibu zote za kazi yao huku akiripoti maendeleo ya kila msichana aliyekuwa akiishi kwenye lile jumba.
Kwa miaka kumi na mbili aliyoishi katika kampuni ya ‘Serenity’ alipata kushuhudia mambo ya kutisha sana yakiwatokea wote ambao walikuwa wakikaidi kanuni za kazi na kutaka kutoa siri za kampuni hiyo nje.
Kwa kifupi hata yeye mwenyewe alishapoteza marafiki wengi sana aliokuwa nao katika jumba la ‘Serenity’.
Hakuna mtu wa nje aliyekuwa akifahamu vizuri nini kilichokuwa kikiendelea ndani ya kuta za jengo hilo ambalo yeye aliliona kama ‘Danguro la kimataifa.’
“Kwa hiyo vipi! Kama Caro atakuja kumfuata bwana ‘ake, wewe utafanyaje?” aliuliza Madam Flaviana huku akikata kona ya kuingia vibarabara vya uswahilini.
“Sipo tayari kumuachia, labda nisiwe hai,”
“Nilishawahi kupenda kama wewe Salima, sishangai hata kido…”
“Ishia hapohapo!” Salima alisema akimkatiza usemi Madam Flaviana na kushuka haraka akikimbilia moja kwa moja hadi ndani ya nyumba. Macho yake yakakutana na mlango wa chumba chake ukiwa wazi huku kila kitu ndani ya chumba chake kikionekana isipokuwa Dedan.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment