Simulizi : Kitanzi, Kisu Na Bastola
Sehemu Ya Tano (5)
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wakaingizwa ndani ya lifti na kupelekwa hadi ghorofa nyingine, huko wakakabidhiwa kwa Madam Bernadeta na kupewa nguo zenye rangi sawa kisha wakapelekwa kwenye jukwaa kubwa ambalo ndani yake kulikuwa na wasichana wengi wakiwa na nguo kama zao.
Kwa harakaharaka, Carolina na Sonia wakajua kwamba tayari wamerudishwa tena kutumika ndani ya jumba la Serenity kwa kuwa hawakuwa wageni ndani ya mazingira hayo.
Wakati huo, Sonia alikuwa akitokwa na machozi mfululizo kwa kuwa alimkumbuka sana mume wake Side na watoto wake ambao mpaka siku hiyo hakujua nini kilichokuwa kikiendelea kwa upande wao.
Wakati huohuo, Carolina alikuwa akiwaza jinsi ya kumpata Salima msichana ambaye aliongea naye siku chache zilizopita. Moyoni mwake alijua kama akionana na msichana huyo basi kila kitu kinachomhusu Dedan atakifahamu.
“Niambie, unamfahamu Salima?” Carolina alimuuliza Julieth bila kutoa salamu yoyote ya kiungwana.
“Salima! Unamaanisha Caro?” aliuliza Julieth.
“Mimi namfahamu kwa jina la Salima tu na si vinginevyo.”
“Kwani mnafahamiana?”
“Sijawahi kumuona hata siku moja. Naomba unioneshe kama yupo hapa tafadhali.”
“Tangu leo asubuhi sijamuona… labda nikupeleke kwenye chumba chake,” alisema Julieth na kumuongoza Carolina huku Sonia naye akifuatia kwa nyuma.
“Hiki ndiyo chumba chake,” alisema Julieth huku akiufungua mlango wa chumba cha Salima bila kubisha hodi.
Wakiwa wanajishauri waingie au wamsubiri, mwenyeji wao awakaribishe, mara wakasikia kicheko kikali kikitoka ndani ya chumba hicho. Walipoingia walimkuta Salima akirukaruka juu ya kitanda chake huku masikioni akiwa na ‘headphone’ alizozichomeka kwenye ‘ipod’ yake. Ni wazi kwamba alikuwa akisikiliza na kucheza nyimbo fulani kwa fujo.
Salima alipowaona, akaacha uchizi aliokuwa akiufanya na kuteremka kitandani kisha kwa mashauzi akamfuata Julieth na kumtazama kwa madaha kabla ya kufanya vivyohivyo kwa Carolina na Sonia.
“Caro, una nini leo? aliuliza Julieth kwa mshangao baada ya kuhisi mabadiliko makubwa kwenye tabia ya Salima tofauti na alivyokuwa akimfahamu.
“Kwani vipi! Hawa akina nani?” Salima aliongea kwa dharau huku macho yake yakitua kwenye uso wa Carolina na kumuangalia kwa muda huku akisubiri jibu la swali lake.
“Hawa ni wageni wako. We wasikilize mwenyewe bwana!” Julieth alijibu kwa hasira na kutaka kuondoka, lakini aliamua kusubiri asikilize kitu gani wasichana hao walitaka kuongea na Salima au Caro kama alivyokuwa akiitwa.
“Mimi naitwa Carolina, tuliongea wote kwenye simu siku chache zilizopita,” aliongea Carolina kwa sauti ya chini baada ya kubaini kamera iliyokuwa imetegwa kwa kificho pembeni ya ua, akahisi lazima kutakuwa na kinasa sauti mahali fulani karibu na waliposimama.
“Carolina? Mbona mimi sikufahamu,” Salima alijibu kwa sauti na harakaharaka bila ya kuipa nafasi akili yake ifikirie.
“Tulikuwa tumuongelee Dedan. Bado haujakumbuka?” Carolina alisisitiza.
“Sikia dada, mimi sikukumbuki hata kidogo…naomba tusipotezeane muda. Kama hauna kitu cha msingi, ondoka.”
“Lakini…wewe si ndiyo Salima?”
“Hapana, mimi naitwa Caro,” aliongea Salima na kuvaa headphone zake huku akiendelea kucheza wimbo aliokuwa akiusikiliza.
Carolina alivunjwa nguvu na kauli hiyo ya Salima kwa kuwa alimtegemea msichana huyo kama mtu pekee atakayeweza kumsaidia kukutana na Dedan wake kwa mara nyingine.
***
Afande John akiwa kwenye haraka, alikatiza wodi ya watoto, Muhimbili akielekea kwa daktari mkuu wa kitengo hicho, Dr. Denis Mtima ambaye alimpeleka moja kwa moja mpaka kwenye chumba walicholazwa watoto wa Side. Watoto ambao walinusurika kifo kwenye ajali mbaya ya moto.
Mengi yalikuwa yakiongelewa kuhusiana na tukio hilo, lakini ukweli ulikuwa ndani ya mioyo ya watoto hao ambao kama walikuwa wamerudiwa na fahamu basi watawataja wahusika wote pamoja na chanzo cha moto ule.
Kwa mujibu wa daktari huyo, watoto hao walikuwa wameanza kupata nafuu na kuweza kuongea, hivyo hiyo ilikuwa ni nafasi pekee ya afande John kuwauliza maswali ili kujua nini kilichokuwa kimetokea siku ile.
“Hamjambo watoto wazuri?” aliongea afande John huku akiwapatia pipi na chokleti watoto wale ambao walikuwa wamelala kwenye vitanda tofauti. Wakapokea na kushukuru.
“Eti mama na baba wapo wapi?” aliuliza Habida, mtoto wa kwanza wa Side na kumfanya mwenzake aitwaye Safia ageuze shingo yake haraka na kumtazama afande John kwa makini.
“Baba na mama wanakuja sasa hivi. Wamenituma niwaletee hizo zawadi kwanza,” aliongea afande John huku moyo wake ukimuuma kwa kuongea uongo.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Akafungua mkoba wake na kutoa picha za watu kadhaa. Akawaonesha wale watoto picha moja baada ya nyingine akitaka wachague picha za watu waliowahisi kuwaona siku ya tukio. Picha ya kwanza kuchaguliwa ilikuwa ya Dedan na baada ya kuchambua picha nyingine ilionekana picha ya Henry.
Wa kwanza kushtuka alikuwa ni Safia ambaye alipoitazama picha ile alifumba macho kwa woga na kugeuza shingo yake kana kwamba aliiona taswira mbaya ya ‘Lusifa’ mwenyewe.
Baada ya kugundua hilo, afande John akaigeuza picha hiyo haraka na kuirudisha kwenye mkoba wake ili asiwaumize watoto hao walioonekana kupitia maumivu makali tofauti na umri wao.
Kwa kitendo cha watoto hao kuiogopa picha ya Henry, tayari afande John aligundua kuwa mtu huyo hakuwafanyia jambo jema watoto hao tofauti na Dedan ambapo walipoiona picha yake walitazama bila woga wowote.
Akawageukia tena watoto wale na kuanza kuwahoji. Walisimulia kila kitu kilichowatokea ikiwemo jinsi Henry alivyowachukua shuleni kwao kwa kujifanya mjomba wao.
Pia wakasimulia walivyopelekwa nyumbani na kufungwa kamba ambapo chumba cha pili walisikia sauti ya baba yao, yaani Side akilia kwa uchungu kabla ya baadaye kusikia mlio wa kuogofya ambao afande John alitambua kuwa walikuwa wakimaanisha mlio wa risasi.
Mwisho kabisa wakaelezea jinsi moto ulivyowaka na kuwazingira kila kona.
“Aliyeyafanya yote hayo ndiye huyu?” aliuliza afande John kwa mara nyingine huku akitoa picha ya Henry na kuwaonesha watoto wale jambo ambalo liliwashtua sana na kuwafanya wapige kelele kwa nguvu.
“Afande, mahojiano gani hayo ya kuwatisha watoto kiasi hicho? Naomba uondoke mara moja!” Dk. Denis aliongea kwa jazba akimtimua afande John.
Kwa kutambua hilo, afande John akatekeleza agizo la daktari bila ubishi kwa kuwa alitambua fika kuwa watoto wale walikuwa bado kwenye mfadhaiko kwa yote yaliowatokea, hivyo kama Dk. Denis asingemkataza angeweza kuwasababishia presha na matatizo mengine.
Afande John aliondoka mara moja katika wadi hiyo, safari hii angalau alikuwa na uhakika kuwa amepata mahali pa kuanzia.
“Hallow afande Prisca! Umepata chochote?” aliongea afande John kupitia simu yake ya mkononi huku akitembea kuelekea mahali alipoipaki pikipiki yake.
“Ndiyo mkuu, wengi kati ya hawa wasichana waliopo pichani, wamewahi kuripotiwa wamepotea mitaani mwao. Sasa sijui kama walitoroka makwao kwa makusudi au vipi?” alizungumza afande Prisca ambaye ni afisa upelelezi kitengo cha uhalifu kwa njia ya mtandao.
“Mh…Hapo kuna tatizo, nakuja sasa hivi,” alijibu afande John na kuondoka hospitalini hapo.
Kwa mbali Henry aliyekuwa amejibanza kwenye foleni za wagonjwa, alimtazama afande John akiondoka. Akaishusha kofia yake chini zaidi na kuficha sehemu kubwa ya uso wake kisha akaingia ndani ya hospitali ileile aliyotoka afande John, mkononi mwake akiididimiza bastola yake aina ya ‘revolver’ ndani ya mifuko ya koti lake.
Bila kutiliwa mashaka na mtu yeyote, Henry akaingia mpaka kwenye varanda kuu na kuelekea chumba walichokuwamo watoto wa Side.
***
Akiwa mwenye kukosa tumaini, Carolina alimtazama Salima kuanzia chini mpaka juu kana kwamba hakutaka amsahau kabisa katika kumbukumbu zake.
Katika kutazama huko, mara akagundua kidoa chekundu katika kiganja cha mkono wa Salima. Ghafla akamfuata na kumshika mkono wake akikitazama kidoa kile kilichofanya kipele kidogo juu ya mshipa wake wa damu.
Kwa hasira Salima akamsukuma Carolina na kumtaka aondoke chumbani kwake mara moja.
Kwa tahadhari ya kutoharibu mipango yake, Carolina alitoka nje ya chumba cha Salima akiongozana na Sonia na Julieth ambao wote walipigwa na butwaa wakiwa hawajui maana ya kitendo alichokifanya Carolina.
“Wewe una uhakika kama yule ndiye Salima?” aliongea Carolina kwa ghadhabu akimwangalia Julieth usoni kana kwamba alidanganywa na kupelekwa kwa mtu mwingine mbali na Salima.
“Ndiye yeye mwenyewe…kama huamini waulize wote humu ndani.” Julieth alijitetea baada ya kuona uso wa Carolina ukiwa umefura hasira.
“Umeshawahi kumuona Salima akiwa katika hali ile au amebadilika?”
“Salima ni mpole na mwenye aibu nyingi, leo amebadilika sana, hata mimi mwenyewe amenishangaza.”
Kwa jibu hilo la Julieth, tayari Carolina alielewa kuwa huenda msichana huyo alikuwa amechomwa sindano ya dawa za kulevya ‘Ecstasy 33’ iliyomfanya apoteze haiba na kumbukumbu zake za awali. Carolina alilijua hilo kwa kuwa hata yeye mwenyewe alishawahi kuchomwa sindano hizo na mtu ambaye si mwingine zaidi ya Dr. Church; Mkemia hatari ambaye kipaji chake alikitumia vibaya kwa kuumiza kundi fulani la watu na kujinufaisha mwenyewe.
Miaka kadhaa iliyopita, Mzee huyo aliajiriwa na ‘Serenity,’ huku kazi yake kubwa ikiwa ni kutumia dawa zake kwa msichana yeyote aliyeonekana kutoendana na taratibu za ‘Serenity,’ hasa katika suala la kutumika kimapenzi.
“Bila shaka Salima ni msichana mwenye msimamo sana kiasi cha kudungwa madawa. Kwa sasa sina la kufanya. Itanilazimu nimsubiri mpaka atakapopata ahueni,” Carolina alijisemea kimoyomoyo akikumbukia jinsi alivyokuwa akichomwa sindano hizo kila mara alipovunja kanuni za jumba hilo.
Akajiangalia mikononi na kuona alama za makovu ya sindano zile yakiwa yameanza kufifia. Akashusha pumzi kwa nguvu akitafakari jinsi ya kutoka ndani ya jengo hilo akiwa na Dedan, mwanaume aliyedhamiria kumpata kwa hali yoyote.
***
Wakati huo Dedan alikuwa akipata huduma nzuri tofauti na wenzake. Yeye alipata nafasi ya kuwa karibu zaidi na Madam Flaviana. Wakazungukia kila kona ya jumba la ‘Serenity’ isipokuwa upande wa vyumba vya wasichana waliowekwa tayari kwa ajili ya kuuzwa kwa wanaume Wakizungu.
Kwa hali hiyo, Dedan akawa kama mmoja wa wafanyakazi wa karibu wa madam Flaviana huku mwanamke huyo akiwa makini kutomkutanisha na Salima wala Caro akiepuka kuharibu mipango yao.
***
Henry bila kusuasua, aliufungua mlango wa chumba walichokuwemo watoto wa Side huku mkono wake wa kulia ukiishika vyema bastola yake. Akaingia ndani na kutupa macho yake juu ya vitanda na kuwaona watoto wote wawili waliokuwa wamelala kwa kujifunika kwa mashuka mwili mzima.
Akakenua meno yake na kuwafuata taratibu huku akiufunga mlango kwa nyuma. Akajongea mpaka kwenye kitanda cha mtoto wa kwanza na kufunua shuka kwa kutumia mdomo mrefu wa bastola yake, akitumaini hapo atakiona kichwa cha mtoto mmoja wapo ili amuulie mbali lakini badala yake akauona mto.
Alipofunua shuka lote alikutana na mito na mashuka yaliyopangwa vizuri na kufanya shepu kama ya watu waliolala. Kabla hajafanya chochote alishtukia mdomo wa bastola ukimgusa nyuma ya kichwa chake.
“Taratibu rusha bastola yako pembeni na uinue mikono juu. Ukijaribu kufanya chochote nakufumua ubongo wako,” ilisikika sauti ya afande John.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kivyovyote huyu mtu atakuwa anajua vyema kuitumia bastola yake. Hapa sina ujanja zaidi ya kutii maagizo yake,” Henry alijionya mwenyewe kimoyomoyo na kufanya kama alivyoagizwa.
Kufumba na kufumbua Henry alishtukia yupo chini huku mikono yake ikiwa imefungwa pingu kwa nyuma. Pamoja na mwili wake wa miraba minne, Henry hakuwa na ujanja wowote mbele ya afande John.
Kwa mshangao, Henry akabaki akistaajabu jinsi ambavyo afande John alirudi hospitalini hapo haraka kiasi kile, wakati kwa macho yake alimshuhudia akiondoka? Baada ya dakika chache, askari wengine walifika katika eneo hilo na kumpeleka Henry kituoni kwa ajili ya mahojiano.
***
Siku zikazidi kuyoyoma huku Salima akiwa amebakiza siku tatu kabla ya ujio wa Prince Khalfani; mgeni ambaye yeye na Julieth walipangiwa kuwa naye katika kipindi chote cha ziara atakayoifanya nchini.
Mr. Chakos na Madam Flaviana chini ya usimamizi wa Madam Bernadeta, walikesha wakifanya kazi kuhakikisha Salima au ‘Caro’ kama walivyomwita anakuwa katika afya nzuri na kupatiwa mafunzo yote muhimu ilimradi asiwaangushe wakati wa ziara hiyo. Wakahakikisha anakariri vyema maneno mengi ya kiarabu na kuelewa baadhi ya tamaduni zake.
Baada ya kuhakikisha kila kitu kinaendelea vizuri wakakaa kimya wakisubiri ugeni huo.
“Madam Flaviana, amekuja kunifuata mimi au?” alijiuliza Salima kwa shauku kwani zilikuwa zimepita siku nyingi bila kuonana naye.
Salima aliingia ndani na kusimama kwa furaha baada ya kumuona Madam Flaviana pembeni ya Madam Bernadeta.
Moyoni aliamini Madam Flaviana atakuwa na habari mpya kuhusu mpenzi wake, Dedan. Akahisi huenda atakuwa amepatikana.
“Caro, nina habari nzuri na mbaya, ipi nianze kukwambia kwanza?” Madam Flaviana alimuuliza Salima bila uso wake kuonesha alama yoyote ya furaha.
“Aaah…anza na habari njema kwanza,” Salima aliongea kwa wasiwasi hasa baada ya kumsikia Madam Flaviana naye akimuita kwa jina la ‘Caro’ na si Salima kama ilivyokuwa zamani.
Kauli ya habari nzuri na mbaya ilizidi kumtia hofu Salima.
“Baada ya wiki mbili kutoka sasa, kuna ugeni kutoka Uarabuni utafika nchini kwa ziara binafsi ya kibiashara na kampuni yetu. Kwa niaba ya ‘Serenity’ tumekuchagua wewe kuwa mwenyeji wao kipindi chote watakapokuwa katika ziara yao… Hongera sana Caro,” alisema Madam Flaviana akirudia tena kutumia jina hilo Caro badala ya lile la Salima, akaachia tabasamu pana huku Madam Bernadeta na Julieth wakimpigia makofi.
Kipindi chote hicho Salima alitulia kimya, maswali mengi kuhusu uhusika wake kwenye hiyo ziara yalitawala akilini mwake huku akishangazwa kwa jinsi gani hiyo ilikuwa habari nzuri!
“Usiwe na wasiwasi hautakuwa peke yako. Kipindi chote utakuwa na shoga yako Julieth. Mwenzako ana uzoefu sana,” Madam Flaviana alisema huku akimwangalia Julieth ambaye alikuwa amesimama nyuma ya Salima huku uso wake ukiwa umejikunja kwa kutajwa kama msindikizaji wa Salima.
“Na habari mbaya ni ipi?” Salima aliuliza kwa hofu akimtazama Madam Flaviana machoni kana kwamba alitegemea kusoma macho yake zaidi ya kusikiliza.
“Jamani naomba mtupishe,” aliongea Madam Flaviana, mara moja Julieth na Madam Bernadeta wakatoka nje na kumuacha yeye (Madam) na Salima.
Madam Flaviana alijua fika kuwa lazima abuni uongo mpya ambao Salima hatoweza kuugundua kwa haraka kwa kuwa, awali yeye ndiye aliyemdanganya Salima kwamba Dedan alikuwa amechukuliwa na Caro jambo ambalo halikuwa sahihi.
Mbaya zaidi Salima alishaongea na Caro mwenyewe, kwa hiyo isingekuwa rahisi kumdanganya Salima kuwa Dedan bado alikuwa kwa Caro.
“Habari mpya ni kuhusu Dedan,” alianza kuongea Madam Flaviana kwa umakini mkubwa.
“Dedan! Vipi amepatikana?” Salima alijikuta akiuliza kwa hofu kwani tayari kichwani mwake alishajiwekea kuwa hiyo ndiyo habari mbaya kama alivyotahadharishwa.
“Ndiyo amepatikana na ni mzima wa afya, lakini…”Madam Flaviana alinyamaza kidogo na kumtazama Salima kwa kuibia akitarajia kumuona akiwa ameanza kuchanganyikiwa jambo ambalo lilikuwa sahihi.
“Siku zote tulizodhania alikuwa kwa Caro kumbe alikuwa na mwanamke mwingine anayeitwa Sonia. Kibaya zaidi ni kwamba, Sonia ndiye mke wake wa ndoa na wana watoto wawili siku nyingi.
“Kwa kifupi Dedan alikuwa na uhusiano na wanawake wawili, ambao mmoja tu ndiye uliyemtambua, yaani Caro.” alisema Madam Flaviana kwa umakini mkubwa ili asije kukosea.
Siku zote msema uongo hupaswa kuwa na kumbukumbu nzuri ili asije akajisahau na kuchanya madawa. Kwa hilo, Madam Flaviana alijipanga kutofanya makosa kwani alishakariri kila neno alilopanga kumwambia Salima na kuhakikisha analirudiarudia kabla ya kukutana na Salima siku hiyo.
“Sina haja ya huyo mkewe wala watoto wake, Dedan yupo wapi?” Salima aliuliza kwa hasira kidogo kwani alishaanza kuhisi kuumizwa na kila neno ambalo Madam Flaviana alikuwa akiliongea kuhusu Dedan.
“Ubaya ni kwamba mimi mwenyewe nilijitahidi kumtaka Dedan angalau aongee na wewe yeye mwenyewe, lakini alikataa na kusema kuwa hakufahamu na mbaya zaidi amenipa ujumbe huu akitegemea kuwa baada ya kuusoma, hautamsumbua tena,” aliongea Madam Flaviana huku akimkabidhi Salima bahasha ndogo.
***CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya kushinda siku nzima ya jana yake wakiwa na uchovu uliopindukia, siku hiyo waliamka wakiwa na nguvu kama kawaida. Kwa mara ya kwanza Sonia naye alianza kuhisi maumivu shingoni mwake, akajua kwamba Madam Flaviana hakutania kuhusu kuwawekea vipandikizi ndani ya miili yao.
Akageuka na kumtazama msichana aliyejitambulisha kwa jina la Caro na kumuongelesha.
“Caro, unamfahamu Dedan?” aliuliza Sonia kimasihara baada ya kuhisi huenda Caro aliyewahi kusimuliwa na Side alikuwa ndiye huyo.
“Ndiyo namfahamu. Nafahamu pia kuhusu Salima msichana aliyekuwa akiishi naye baada ya wewe kumsababishia Dedan matatizo.”
“Jamani Dedan wangu ana matatizo gani! Yupo wapi?” alinong’ona Caro kwa simanzi kubwa huku machozi yakianza kumtiririka.
“Tulitekwa wote na kuletwa hapa, lakini sijui amewekwa sehemu gani!”
“Unataka kusema Dedan yupo hapa Serenity! Alipatwa na matatizo gani?”
“Kwani wewe hujui? Nimeambiwa alikuwa zezeta, lakini alipona akiwa kwa huyo Salima ambaye naye nimesikia ameletwa hapa Serenity kama msichana wa kuuzwa.”
“Unasemaje! Dedan alikuwa zezeta?” alihoji Caro huku machozi yakimtiririka kwa kasi, safari hii yakifika hadi mashavuni mwake. Hakutegemea kama Dedan angefikia hali hiyo baada ya kummwaga enzi zile.
Akakosa hoja na kubaki akijilaumu kwa yote aliyomfanyia Dedan, hata hivyo alitamani kupata nafasi ili amuombe msamaha kwa kitendo alichomfanyia na kuamini angesamehewa kwani alijua alikuwa na sababu ya msingi ya kufanya vile.
***
“Umefanya kazi nzuri sana Madam,” Mr. Chakos alimpongeza Madam Flaviana huku akimmiminia ‘wine’ kwenye glasi yake.
“So nini kinafuata?” aliongea Madam Flaviana huku akiipokea glasi kutoka kwa Mr. Chakos na kuonja kidogo.
“Njoo uangalie, nilichokigundua,” Mr. Chakos alimvuta Madam Flaviana mpaka upande wenye kompyuta moja kubwa na kuicheza video aliyorekodi muda mfupi uliopita. Kwenye video ile, Salima alionekana akitembea kwenye korido huku macho yake yakiziangalia kamera zilizotegwa kwenye dari kana kwamba alikuwa akifahamu uwepo wa vifaa hivyo.
“Angalia na hii,” Chakos alibofya ‘kipanya’ cha kompyuta yake na kuicheza video nyingine ambapo ndani yake walionekana Caro na Sonia wakiongea kwa kunong’ona kana kwamba walikuwa wakijua uwepo wa kinasa sauti ndani ya chumba chao.
“Dirty bitch (mbwa jike mchafu)! Lazima Caro alimwambia Salima kuhusu jambo hili, si unakumbuka siku ile Caro ndiye aliyeongea naye mara ya mwisho kwenye simu?” alifoka Madam Flaviana.
***
Ndani ya chumba chake, Salima alikuwa amejifungia kimya akitafakari jinsi gani Dedan aliweza kufanya mambo hayo yote kwa muda mfupi. Ujumbe aliopewa ulijieleza vizuri kama Madam Flaviana alivyomwambia, lakini hakuamini moja kwa moja kama maneno hayo yaliandikwa na Dedan mwenyewe.
Akiwa na hasira zilizochanganyika na wivu, Salima alifikiria jambo moja tu ambalo ni kuondoka ndani ya jengo la Serenity na kuhakikisha anamsaka Dedan popote alipo ili angalau amsikie akitamka maneno hayo kwa kinywa chake mwenyewe.
Akasimama na kuweka nguo zake kwenye begi bila kujali kamera iliyokuwa ikimmulika.
Baada ya kumaliza zoezi hilo, akafungua mlango wa chumba chake na kuanza kutembea kwa kujiamini akielekea kwenye korido na hatimaye kuteremka kwa lifti mpaka chini na kufika nje.
Akavuka vizingiti vyote na kutembea kuelekea kwenye geti kubwa lililotenganisha ulimwengu wa nje na mle ndani.
Kwa hasira alizokuwanazo, hakujali chochote, akazidi kukaribia geti hilo, lakini ghafla kitu mfano wa sindano kikamchoma mgongoni, Salima akajikuta akilegea ghafla na kudondoka chini kama mzigo, ‘puuh’.
***
Kufanya kazi kwa bidii ndiyo sababu iliyomfanya Mkuu wa Upelelezi amkabidhi kesi ile Afande John. Alijua baada ya siku chache watuhumiwa watakuwa wamepatikana kwa kuwa alimuamini sana kijana wake huyo tofauti na maaskari wengine.
Bila hiyana, Afande John naye alilichukua jukumu hilo na kuanza kulifanyia kazi ambapo kwa muda mfupi tu alifanikiwa kupata taarifa za watu wawili ambao ni: Henry ‘Ze Deader’ yaani yule muuaji wa Side, na mtu mwingine ambaye alionekana mara moja tu akiwa na marehemu, wakimaanisha Dedan.
Kwa maelezo ya watu wachache aliowafanyia mahojiano, Afande John alifanikiwa kufika hadi kwenye kichaka ambacho awali alifungiwa Dedan na Sonia na kugundua kamba zikinin’ginia kwenye magome ya miti miwili. Baada ya kuchunguza, aligundua kuwa mahali hapo watu wawili walikuwa wamefungwa kabla ya kuhamishwa ama kutorokea sehemu nyingine.
Kama kawaida yake, Afande John akatoa kitabu chake na kuchora michoro aliyoifahamu yeye mwenyewe.
Ghafla wazo likamjia. Kwa kasi ya ajabu akairukia pikipiki yake na kuiwasha kana kwamba alikuwa akiwahi jambo fulani alilolikumbuka. Akiwa njiani, aliiacha barabara ya lami na kuingia ya vumbi ambayo haikuwa ikielekea sehemu yoyote nyingine zaidi ya kwenye jengo moja kubwa la ghorofa lenye fensi ya ukuta mrefu kupindukia.
Akasimamisha pikipiki yake na kuificha mita chache karibu na jengo lile. Akaitoa mfukoni ile kadi aliyoichomoa kwa yule mhalifu aliyekurupushana naye usiku wa jana yake na kujaribu kuifananisha na alama iliyopo kwenye kadi hiyo na ile aliyoiona kwenye lile geti. Akaitazama na kubaini kuwa alama zile zinafanana.
“Kumbe herufi ‘s’ ni kifupi cha neno ‘Serenity’!” Afande John alistaajabu kimoyomoyo. Moja kwa moja akatambua kuwa kwa vyovyote yule mtu aliyekurupushana naye alikuwa akifanya kazi ndani ya jengo hilo. Kwa kutumia simu yake ya kisasa akaandika neno ‘Serenity’ akidhamiria kutafuta maana yake kwenye mitandao akiamini huko atapata maelezo sahihi kuhusu kampuni hiyo na shughuli zake.
Baada sekunde chache za kuperuzi kwenye kurasa za ‘google,’ alibaini kuwa jengo hilo lilijihusisha na masuala ya kukuza vipaji vya urembo na lina matawi mengi duniani.
Alipojaribu kuchimba zaidi kuhusu watu wanaoiendesha kampuni hiyo, kurasa ziligoma kufunguka na kuhitaji anuani ya barua pepe na ‘pasiwedi’ ili kuweza kufunguka.
“Kwani kuna siri gani humu!” alijisemea Afande John huku akiingiza anuani yake ya barua pepe na ‘pasiwedi’ akijaribu kama kurasa hizo zingefunguka.
Taratibu kurasa mpya ilianza kufunguka kwenye simu yake huku zikionekana baadhi ya picha za wasichana kadhaa warembo wakiwa katika pozi tofauti. ‘Akazidownload’ haraka picha hizo na kuzihifadhi ndani ya simu yake, lakini zaidi ya hapo hakufanikiwa kupata kitu chochote ndani ya kurasa hizo, aliona maandishi mekundu yaliyosomeka: MEMBERS ONLY (Wanachama pekee)!
Baada ya jitihada za kuzifungua kurasa zile kugonga mwamba, Afande John aliketi hapo kwa muda kidogo akiangaza kila kona ya jengo hilo lililokuwa kimya sana.
Kwa kujificha akapiga picha chache na kupotea eneo hilo moyoni akiweka azma ya kufuatilia zaidi namna kampuni hiyo inavyoendeshwa.
***CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Salima akiwa hajielewi alibebwa na kukokotwa na mabaunsa walioonekana kujizatiti katika kazi yao. Wakapita naye karibu kabisa na mahali walipofungiwa akina Sonia.
Moja kwa moja wakambwaga juu ya kitanda cha chumba ambacho ndani yake walionekana Madam Flaviana na mzee mmoja wa Kizungu aliyejulikana kwa jina la Dr. Church kisha wakaondoka.
Haraka Dr. Church alifungua begi lake na kuchukua sindano, kisha akaifyonza dawa iliyokuwa ndani ya chupa moja wapo na kumchoma Salima kwenye mshipa wa kiganja chake na kutulia kwa muda.
“Itasaidia kweli?” aliuliza Madam Flaviana ambaye kipindi chote hicho alikuwa kimya akimwangalia Dr. Church alipokuwa akifanya vitu vyake.
“Hii ni moja kati ya dawa zangu chache zilizonigharimu sana katika ugunduzi wake, nimeipa jina la ‘Ecstacy 33’ kutokana na uwezo wake wa kumfanya mtu asahau mambo yote ya awali na kukubali kila kitu atakachoamrishwa kufanya. Sibahatishi katika hili, kama utakuwa tayari tutamjaribu mtu wako baada ya saa moja.” alisema Dr. Church kwa kujiamini tena kwa Kiswahili fasaha.
Kwa maelezo yake, dawa hiyo aliigundua kwa kutumia dawa za kulevya aina ya ‘Ecstasy’ ambayo ina uwezo wa kumfanya mtu asahau mambo na kumchangamsha saa zote.
Dr. Church alichoweza kukifanya ni kuiweka dawa hiyo katika kiwango sahihi cha dozi huku akiichanganya na kemikali nyingine zilizokuwa na uwezo wa kumfanya mtu kuwa katika hali hiyo kwa muda mrefu tofauti na ‘ecstasy’ ya kawaida.
Kwa hiyo, baada ya muda mfupi ujao, dawa hiyo ingeweza kumfanya Salima amsahau Dedan na kukubali kufanya kila kitu atakachotumwa na Madam Flaviana hasa wakilenga kufanikisha kumtumia katika ziara ya Prince Khalfani kutoka Falme za Kiarabu.
***
“Caro, kwa nini kila mara ukiongea unataka tuzungumze kwa sauti ya chini kwani kuna nini?” aliuliza Sonia kwa kunong’ona baada ya kila mara kuzuiwa na Caro kuongea kwa sauti ya kawaida.
“Shh! kuna vinasa sauti na kamera ndani ya jengo zima,” alijibu Caro bila kumtazama Sonia.
Bado moyo wake ulikuwa na donge zito kwa aliyoyasikia muda mfupi kuhusu Dedan. Ghafla wakasikia vishindo vya watu vikipita karibu na chumba walichomo, kwa sauti za hatua zao Caro aligundua mara moja kuwa watu hao walikuwa wakielekea upande wao, jambo ambalo lilikuwa sahihi. Kufumba na kufumbua wanaume watatu wenye miraba minne waliingia ndani ya chumba hicho. Kwa uoga Sonia alijikuta akimkumbatia Carolina.
“Tufuateni mara moja!” alitoa amri mmoja wa wanaume hao aliyeonekana kama kiongozi wao.
Bila kukaidi, Caro alisimama na kuanza kutembea akiwafuata watu wale huku Sonia naye akifuatia kwa nyuma kama vile mbwa amfuatavyo chatu hali akijua hatoweza kupona.
********
“Ni mbinu za kikazi, siwezi nikakueleza. Cha msingi naomba unijibu maswali nitakayo kuuliza,” afande John aliyeyusha swali la Henry kwa kuhamisha mada.
“Haya uliza!” Henry alijibu kwa hasira baada ya kuona hakupata jibu zuri kutoka kwa afande John.
“Serenity inajihusisha na nini?”
“Come on! Afande John, nilidhani unajua kuhusu hilo, kwani hujui kama Serenity inawauza wasichana kwa wageni wa kizungu wanaokuja nchini?”
“What! Mimi nilitambua inahusika katika shughuli za urembo na kuwapromoti mamiss.”
“Wasichana wote wanaoonekana kama mamiss hutumikishwa kingono, Serenity ni danguro kubwa linalojiendesha kwa kivuli cha masuala ya urembo, hakuna lolote!”
“Mh! unauhakika na unachokiongea?”
“Yah, asilimia mia mbili,”
“Mmiliki wake ni nani?”
“afande mimi nawafahamu watu wawili tu; Mr. Chakos na Madam Flaviana lakini mmiliki wake nimewahi kusikia kuwa anajulikana kwa jina la Mr. George.
Hakuna mtu yeyote ambaye amewahi kuuona uso wake, hata Mr.Chakos mwenyewe hajawahi kuonana naye hata siku moja. Wanasema kuwa yeye ndiye hutafuta amtakaye na siyo wewe umtafute yeye. Mara zote Mr. George huongea kwa simu kwa sauti tofautitofauti au hutuma ujumbe kwa njia ya mtandao kwa watu maalumu tu. Kwa hiyo kumtafuta ni sawa na kuitafuta njia ya mauti,” alisema Henry ambaye maelezo yake yalizifanya nywele za afande John zisimame kwa hofu.
Mara nyingi nywele zake zinaposimama na kwa mtindo huo, afande John hukosa amani kwa kuwa hujua kuna hatari inamnyemelea, hatari yake kwa wakati huo ilikuwa ni hilo suala la Serenity.
***
NDANI YA UWANJA WA NDEGE, MAHALI FULANI
Waarabu wawili waliovalia suti na miwani myeusi walionekana kuteremka ngazi za ndege moja iliyoonekana kutua muda mchache uliopita. Mavazi na mienendo yao ilionekana wazi kuwa ni walinzi wa mtu au kitu fulani cha gharama. Kwa umakini mkubwa wakaangalia kila upande kisha mmoja wao akajongea mbele kidogo ambapo hapo walionekana Mr. Chakos na Madam Flaviana wakiwa na kundi la wasichana warembo waliokuwa wakitabasamu muda wote isipokuwa wasichana wawili pekee ambao ni Sonia na Carolina.
Baada ya Mwarabu yule aliyeonekana kama bodigadi kuwaona wenyeji wake, akatoa ishara kwa yule mwingine ambaye alichomoa simu yake na kupiga mara moja. Sekunde chache baadaye walionekana kuteremka Waarabu wengine ambao idadi yao ilifikia wanaume kumi na moja. Wengi walionekana kuvalia kanzu na vilemba vichwani isipokuwa mmoja tu kati yao ambaye alivalia kizibao cha rangi ya kahawia, miwani ya jua na kanzu nyeusi kiasi cha kuonekana nadhifu kuliko wote waliokuwa hapo.
“Bila shaka yule ndiye mgeni wao,” alisema Henry aliyejificha ndani ya gari la vioo vya tintedi akimwambia afande John ambaye alikuwa bize akiliangalia tukio zima kwa darubini yake huku akivuta lenzi yake kuelekea upande waliosimama warembo wale. Kwa umakini mkubwa akapiga picha kadhaa za wasichana hao kwa kubonyeza kitufe fulani cha darubini hiyo ya kisasa na kusevu ndani yake kama picha za mnato.
“Unaweza kumtambua mmojammoja kama nikikuonesha picha zao?” aliuliza afande John baada ya kumaliza kuchukua picha ya kila mrembo aliyekuwa katika kundi lile.
“Yah,” alijibu Henry huku akiangalia kwa makini nje ya kioo chake.
Yule Mwarabu nadhifu kuliko wote alionekana kujongea mbele na kuongea kwa muda na Mr.Chakos kisha wakapeana mikono na kukumbatiana kwa furaha kabla ya kila mmoja kumbusu mwenzake shavuni kama desturi ya Waarabu ilivyo.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya kitendo hicho Kwa unyenyekevu, Mr. Chakos na Madam Flaviana waliwaongoza wageni wao mpaka kwenye msururu wa magari ya kifahari yaliyoegeshwa nje ya uwanja huo na kuwabeba wageni hao wakielekea kuponda raha ndani ya jengo la Serenity.
Kila msichana aliyekuwa uwanjani hapo alipangiwa gari atakaloingia na kuketi akiwa na mgeni wake kabla ya baadaye kununuliwa na wageni hao ambao kwa huduma ya kila mrembo watapaswa kulipa fedha zisizopungua dola elfu mia tano kwa siku.
Wakati wakielekea Serenity, Sonia alikuwa ameketi siti ya nyuma kabisa na Mwarabu mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Awadh Sayeed. Muda wote Awadh alionekana kumsumbua Sonia kwa kumpapasapapasa kila mara.
Wakati mwingine alitumia nguvu kutaka kumvua blauzi yake kitendo ambacho Sonia alikichukia na kubaki akijisitiri mwili wake huku machozi yakimtoka.
Bila kujali, Awadh aliendelea kumnyanyasa mrembo huyo huku akionekana kuvutiwa na kitendo alichokuwa akikifanya.
Kuna wakati alimshika na kumpiga makofi huku akimtanua miguu yake kwa nguvu ili amalize haja zake humohumo kwenye gari, lakini Sonia alibana miguu yake kwa kadiri alivyoweza asiruhusu kudhalilishwa.
Walipofika Serenity, wengi kati ya waarabu hao waliondoka na warembo hao huku kila mmoja akielekea katika vyumba maalumu ambavyo vilikuwa tayari vimeandaliwa kwa ugeni huo.
Bila kupoteza muda Awadh aliyeonekana kuvutiwa na Sonia alikuwa wa kwanza kumbeba msichana huyo na kuingia naye ndani ya chumba chake tayari kwa kutekeleza azma yake mbaya.
Kwa mbali Carolina aliyekuwa akiingia chumbani kwake na Mwarabu mwingine aliyejitambulisha kama Omar Kareem, alimuona Sonia akihangaika kujinasua maungoni mwa Mwarabu huyo, moyo wake ulimuuma sana kwa kitendo kile lakini katika mazingira hayo hakuwa na cha kufanya zaidi ya kutafakari jinsi ya kuyaepuka matatizo yake kwanza kabla ya kumsaidia mwenzake.
***
Salima alionekana kuvinjari na Prince Khalfani kwa mtindo wa pekee. Mara alimkumbatia na kumbusu, mara alisimama na kuzungusha kiuno chake laini akicheza ala za kiarabu na mara nyingine aliongea kwa lugha laini na Prince Khalfani ambaye muda wote huo alikuwa mtulivu sana kama vile buibui atuliavyo akisubiri mdudu ajipeleke katika utando wake aanze kumshambulia.
***
Wakati mambo yote yakiendelea kama yalivyopangwa, Madam Flaviana na Mr. Chakos wote walikuwa makini kuhakikisha hakuna kitakachoharibu ugeni wao.
Wakakaa kwenye kompyuta zao wakiangalia kila kitu kinachofanyika katika vyumba hivyo. Katika kuonesha kwamba suala hilo lilikuwa na umuhimu, Mr. George mwenyewe alipiga simu kuulizia kila kitu kilichokuwa kikiendelea.
Wakati mwingine yeye mwenyewe ndiye alikuwa akitoa maelekezo ya nini kifanyike, wapi na wakati gani.
***
Carolina akiwa chumbani na Omar, alivua nguo zake taratibu na kuvaa mavazi mepesi ya usiku kama alivyotakiwa kufanya. Wakati huo Omar alikuwa kitandani ameegemea kitanda chake akivuta sigara yake kwa pupa huku akimtazama Carolina kwa jicho la husuda, Carolina alilishtukia na kuzidisha manjonjo.
Akili ya Carolina muda huo ilifanya kazi haraka sana kwani kadiri muda ulivyozidi kuyoyoma, ndivyo alivyozidi kupata wasiwasi juu ya rafiki yake Sonia ambaye kwa muda huo alikuwa katika wakati mgumu na Awadh.
Harakaharaka lakini kwa mpangilio, Carolina aliuchomoa udi wake ndani ya boksi maalumu, akauwasha kisha akaanza kuufukiza chumba kizima kama wafanyavyo watu wa Pwani.
Taratibu akajongea mahali alipolala huku akilipandisha gauni lake taratibu kana kwamba alijitoa kumpatia mwili wake.
Lakini kadiri alipokuwa akimsogelea ndivyo Omar alivyozidi kutetemeka kwa hofu, mara akadondoka kitandani kama gogo huku akitoa sauti ya kukoroma kana kwamba alipitiwa na usingizi mzito.
Baada ya zoezi hilo, Carolina alikimbilia bafuni ghafla na kunawa uso wake huku akijiziba pua kuuepuka moshi wa udi uliotanda ndani ya chumba hicho. Haraka pasipo kupoteza muda aliuzima udi ule ambao vielelezo vyake vilionesha kuwa ulitengenezwa kwa sumu aina ya ‘Carbon Monoxide.’ Sumu ambayo huanza kwa kulegeza fahamu za mtu kisha kufuatiwa na usingizi mzito kabla ya kifo.
Kama mzimu, Carolina akazima taa na kurudi taratibu mpaka kwenye mabegi ya Omar. Akachambua nguo zake akitafuta simu au kifaa chochote cha mawasiliano ambapo kwa bahati aliipata simu ya kisasa ‘Smart Phone’ ambayo aliiwasha na kutuma ujumbe mfupi kwa mtu aliyemfahamu mwenyewe.
***
“Sikilizeni, nimetumiwa meseji ya hatari kutoka kwa afande Beatrice. Haya kaeni tayari kwa kuvamia!” alisema Afande John akiwaambia makachero wenzake ambao tayari walikuwa wameishaizingira ngome ya ‘Serenity.’
“Samahani kidogo, Beatrice ndo nani?” Henry alishindwa kujizuia na kuamua kuuliza baada ya kusikia jina la afande Beatrice likitajwa kama mtu aliyetuma ujumbe wa hali ya hatari muda mfupi uliopita.
“Ni afisa upelelezi ambaye alijipenyeza ndani ya Serenity bila kujulikana,” alijibu afande John lakini jibu hilo lilizidi kumwacha Henry njia panda badala yake akauliza tena.
“Nini? Ina maana kumbe mlikuwa mnaifuatilia hii inshu kwa muda mrefu? Hivi huyo Beatrice ni nani humo ndani?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ni siri za kikazi. Kukusaidia tu ni kwamba, ‘Beatrice’ siyo jina lake halisi kwa hiyo usijisumbue kufikiria kama unamfahamu au la. Hima tuoneshe njia,”
“Tuelekee huku,” aliongea Henry na kuingia kwenye mtaro wa majimachafu uliopita chini ya ukuta na kuibukia ndani ya uzio wa jengo hilo nyuma yake akifuatiwa na makachero ambao wote waliingia huku macho yao yakiwa makini kuangalia kila upande tayari kukabiliana na adui yeyote.
Kwa namna fulani waliweza kupenya hadi ndani kabisa ya jengo hilo bila kuonekana kwa kuwa kulikuwa na giza nene sana usiku huo. Mwanga pekee ulioonekana hapo ni ule uliotokana na taa zilizoonekana kutokea vyumba vya ghorofani na juu ya ukuta wa fensi ile ndefu.
***
Akiongozwa na hisia zake, Carolina alitoka chumbani kwake na kupita koridoni haraka kisha akaingia bila hodi ndani ya chumba alichokuwemo Sonia na yule Mwarabu Awadh.Wote walishtuka baada ya kumuona Carolina akiwa amesimama mbele yao. Aliyeshtuka zaidi alikuwa ni Awadh ambaye kwa wakati huo alikuwa kama alivyozaliwa.
“Maadha turidu (unataka nini)?” Awadh alifoka kwa kiarabu huku akimtazama Carolina kwa hasira.
“Laashakka (hakuna shaka),” alijibu Carolina kwa kiarabu pia huku akavifungua taratibu vifungo vya gauni lake jepesi akijaribu kumlaghai Awadh kwa mwili wake kana kwamba alikuwa na nia ya kufanya mapenzi ya watu watatu.
Wakati huo Sonia aliyekuwa amejikunja pembeni ya kitanda, akikikumbatia kipande cha nguo yake ambacho ndiyo pekee kilichokuwa kimebakia kumsitiri maungo yake, alibaki akimshangaa rafiki yake asijue kusudio lake.
Taratibu fahamu za Salima zilianza kumrudia. Aliweza kukumbuka kila kitu kilichokuwa kimetokea. Mbali na kumbukumbu hizo pia alimkumbuka Dedan na Carolina. Wasiwasi ulianza kumjaa kila mara alipowaza uwezekano wa Dedan kurudiana na msichana huyo ambaye muda huo ndiyo kwanza alianza kumkumbuka kuwa aliwahi kuonana naye mara kadhaa alipokuwa ‘Serenity.’
Akiwa katika mawazo hayo, mara mlango wa wodi aliyolazwa ulifunguliwa. Ndani yake akaingia Dedan aliyeongozana na Carolina. Ikawa kama vile Salima alivyowaza. Kweli Dedan alikuwa mikononi mwa Carolina tena huku wakionekana wenye furaha juu ya maisha yao mapya, japokuwa walijitahidi kuificha hali hiyo mbele ya Salima.
“Salima unaendeleaje?” Carolina alitangulia kuuliza baada ya kumuona Dedan akisitasita kumsalimia Salima ambaye hakujibu chochote zaidi ya kufumba macho yake huku machozi yakimlengalenga.
“Salima, najua uliteseka sana juu yangu kiasi cha kujiingiza katika matatizo makubwa ili unisadie. Kwa moyo wangu wote, naomba radhi kwa hilo. Nipo tayari kurudisha wema wako kwa kukupatia chochote utakacho, tafadhali niambie nikupe nini ili angalau nirudishe nusu ya fadhila zako,” aliongea Dedan akijitahidi kuikaza sauti yake huku akijaribu kutoathiriwa na machozi ya Salima.
“Naomba unipe kitanzi, kisu au bastola!” alijibu Salima kwa hasira.
“Una maanisha nini Salima?” aliuliza kwa mshtuko Dedan.
“Baada ya kupitia yote haya unadhani nitaishije? Si ni bora niukatishe uhai wangu kuliko kuishi kwa fedheha? Najua haukunipenda hata kidogo na najua siwezi kuubadilisha moyo wako ukanipenda mimi kama unavyompenda Carolina. Nyote wawili mna maisha mapya mbele yenu na mnapendana kwa dhati je, mimi nitabaki na nani? Niache nijiue,” aliongea Salima na kuangua kilio kikubwa.
Dondoo:
-Kwa msaada wa Carolina, Salima aliweza kupatiwa kazi na nyumba ya kuishi, lakini mbali na yote hayo bado upendo wake kwa Dedan ulikuwa palepale. Kitu cha ajabu ni kwamba Salima alianza kubadilika kitabia. Alianza kukopi kila kitu kutoka kwa Carolina, kuanzia muonekano wake hadi utembeaji. Moyoni akitarajia kuuteka moyo wa Dedan.
-Carolina na Dedan walishtukia tabia ya Salima, ili kuepuka kumuumiza msichana huyo, wakahamisha makazi yao na kuelekea mkoani Arusha ambapo walianza maisha mapya kwa kufunga pingu za maisha na kuishi kwa raha mustarehe kama mume na mke.
-Sonia alifanikiwa kukutana na watoto wake na kuanza maisha mapya. Kutokana na akiba ya fedha aliyoiacha mumewe, Sonia aliweza kuanzisha biashara mbalimbali jijini na kuweza kujikimu.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
-Mr. Chakos na Madam Flaviana wote wawili walitupwa jela na kutumikia kifungo cha miaka 40 kila mmoja kwa makosa ya mauaji, utumwa na kukwepa kodi. Polisi nao wakiongozwa na Afande John bado walikuwa wakiendelea kumtafuta Mr. George wakiwa na matumaini ya kumtia nguvuni.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment