IMEANDIKWA NA : GLOBAL PUBLISHERS
*********************************************************************************
Simulizi : Mirathi Ya Kaka
Sehemu Ya Kwanza (1)
Kiza kinene kilikuwa kimetanda pande zote za dunia, sikuelewa kama nipo peke yangu ama tupo wengi kutokana na kutoona umbali hata wa sentimita moja mbele yangu.
Nilifikicha macho na kutazama huku na kule,CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
‘Mungu wangu! Nipo wapi huku, nimefikaje na nimefika saa ngapi?’ Nilishindwa kupata jibu.
Nilikodoa macho kwa nguvu kama mtu aliyeshikwa ugoni; bado nilikuwa sioni chochote mbele ya mboni za macho yangu zaidi ya weusi wa giza totoro lililokuwepo.
Niligeuka kushoto sikuona chochote, nikageuka kulia pia sikuona chochote. Niliamua kugeuka mzimamzima, bado sikupata picha hata kidogo, moyo wa woga ulianza kuniingia, nikataka kukimbia lakini nikashindwa.
Nilipojaribu kunyanyua mguu wangu wa kuume nipige hatua kuelekea mbele, mguu ulikuwa mzito.
Ndipo nilipogundua kuwa nguvu zimeniishia, viungo vyote vya mwili nilivihisi vimelegea; vilikuwa vimekufa ngazi kabisa. Nilibaki nikitetemeka palepale, nikajaribu kufumbua kinywa changu angalau nipige yowe la kuomba msaada. Hata hivo nilijikuta nikishindwa kuongea, nikaishia kumung’unyamung’unya maneno utadhani anaongea bubu vile. Kinywa kilikuwa kizito kufumbuka.
Kijasho chembamba kilianza kunitoka, nikajikuta nimelowana chepechepe mwili mzima utadhani nimemwagiwa maji. Ghafla nikadondoka chini mzimamzima, nikaanguka puu kama gunia la mtama liangukavyo linapotupiwa chini hasahasa na mtu mzembe ama aliyechoka kubeba.
Nilianza kuona mwanga mweupe, mwanga huo ulikuwa ni mkali mara kumi zaidi ya ule wa radi; mwanga huo ulizidi kujirudiarudia.
Ghafla mwanga ulisitisha kumulika; mara nikamuona mtu mbele yangu, mtu huyo alikuwa amevaa kanzu iliyong’aa japokuwa gizani. Nilijaribu kuinua kichwa changu nimwangalie huenda nitang’amua kuwa ni nani.
Nilijikuta nikipigwa na butwaa baada ya kuinua macho yangu kwani nilimuona mtu huyo ni wa ajabu mno. Ni miaka ishirini na saba sasa tangu nizaliwe lakini sijawahi kuona mtu mrefu namna hii hapa chini ya jua. Nilijaribu kukifuatilia kiwiliwili chake ili nione kichwa chake kilipoishia .
Niligundua kuwa mtu huyo alikuwa ni mrefu kuzidi maelezo kwani nilishindwa kuuona mwisho wake.
Sijakaa sawa mtu huyo akapotea, nilibaki nikiwaza bila kupata jawabu. ‘Nitasalimika kweli leo?’ Nilijiuliza kimoyomoyo bila kutoa sauti. Nikaangaza pande zote, giza lilikuwa bado lipo palepale. Nilijaribu kuinuka ili nikimbie, hata hivo nilishindwa kwa vile mwili ulikuwa bado hauna nguvu.
Sauti za ngurumo kama za radi zilianza kusikika kwenye ngoma za masikio yangu. Zilizidi kujirudiarudia kabla ya kusindikizwa na tetemeko kubwa la ardhi. Nilihisi ardhi yote inatikisika, woga ukazidi kuongezeka. Mapigo ya moyo wangu yakaanza kwenda kasi zaidi.
‘Nitapona kweli leo?’ Huu ni mfano wa baadhi ya maswali yaliyokuwa yanaisumbua akili yangu kwa wakati huo. Nilikosa majibu ya maswali yangu, nikaishia kujisemea kuwa Mungu yupo.
Tetemeko lilikoma ghafla, pakawa shwari tena, lakini giza lilikuwa lipo palepale. Mvua kubwa ilianza kunyesha, mwanga na miungurumo ya radi nilizidi kuvishuhudia.
Nilibaki nimeduwaa baada ya kugundua kuwa pale nilipokuwa silowi licha ya mvua kubwa kuendelea kunyesha. Hakuna hata tone moja la maji lililokuwa likinifikia utadhani nilikuwa chini ya mwamvuli, nilizidi kuchanganyikiwa.
Hata kwa chini maji hayakunigusa hivyo nyayo zangu zilikuwa kavu. Lakini mvua nilikuwa naishuhudia ikinyesha, tena ni bonge la mvua.
Nilibaini kuwa kumbe nilikuwa nipo juu ya kilima baada ya mwanga wa radi kumulika. Lakini hapakuwa hata na mwamvuli juu yangu licha ya kutoangukiwa na tone hata moja.
Mara niliona kitu kama shuka jeupe kikishuka kutoka angani. Nilikisubiri kwa hamu kitu hicho ili nione ni nini kitatokea.
Woga ulianza kupungua. Siyo kwa kuwa nilikuwa nimeyazoea mazingira; la hasha! Ulipungua kutokana na kukata tamaa nikijua kuwa kuokoka kwangu ni asilimia 0.0025. Nilijipa uhakika wa kupoteza uhai endapo kudura za Mwenyezi Mungu zisingechukua nafasi.
Kitu hicho kilizidi kuteremka taratibu, tena kilikuwa wima mithili ya kitambaa cha sinema. Japokuwa giza lilikuwa limetanda angani kote, kitu hicho kiling’ara na niliweza kuushuhudia mng’ao wake. Shauku ya kutaka kuona kitakachotokea ilizidi kunishika, moyo wa woga haukuwepo tena kwa wakati huo.
Kitu hicho kilianguka chini, moshi mwingi niliushuhudia kilipokuwa kimeangukia. Moshi uliendelea kutoka mahali hapo lakini kitu hicho mfano wa shuka kilikuwa hakionekani tena.
Kufumba na kufumbua niliwaona watu katikati ya moshi huo, nikashindwa kujua idadi yao kamili kwa sababu walikuwa wanatembeatembea bila ya kutulia. Licha ya moshi mwingi kutanda eneo hilo, watu hawa walionekana ‘live’ tena bila chenga.
Nilizidi kuchanganyikiwa nilipoanza kuwatambua baadhi yao, kilichokuwa kinanishangaza ni kwamba kila niliyemtambua alikuwa kashatangulia mbele ya haki tukamzika, yaani namaanisha alishakufa kitambo.
Mtu wa kwanza kumtambua alikuwa ni mzee Mboma, alionekana akitembeatembea huku uso wake ukiwa umeghubikwa na huzuni.
‘Ni mambo gani haya jamani?’ Nilibaki nikijiuliza.
Ni mwaka mmoja sasa tangu tumzike mzee Mboma. Kifo chake kiliwashtua watu wengi sana pale mtaani, na siyo mtaani kwetu peke yake; bali nchi nzima ilisikitishwa na kifo cha mzee huyo kutokana na umashuhuri wake.
Ukianza kuongelea waasisi wa chama kilichotukomboa kutoka kwenye utawala wa kikoloni hutomuacha mzee huyu. Alikuwa ni mwanasiasa mkongwe ambaye alionyesha uanaharakati wake katika kupigania uhuru wa nchi yetu na Afrika kwa ujumla.
Mzee huyo alitegemewa sana pale mtaani kwetu kwa ushauri na kusuluhisha migogoro kutokana na busara zake. Kitendawili kilijitokeza kufuatia habari za kifo chake, mpaka waleo bado hakijateguliwa.
Hakufa kwa ugonjwa wala hakuuliwa na mtu yeyote. Kwa kweli kifo chake kilizua gumzo kwenye vyombo vya habari; kujiua kwa kujinyonga bila kujulikana sababu ni fumbo tosha ambalo halijafumbuliwa mpaka sasa.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alijinyonga mishale ya saa kumi jioni kwa kutumia kamba ya usumba palepale nyumbani kwake. Hakuacha waraka wowote kuelezea sababu zilizopelekea kuchukua uamuzi wa kujinyonga. Hata mkewe hakuwa na hili wala lile juu ya kifo chake. Watu wengi huwa hawaamini kuwa alijinyonga, lakini ukweli ndiyo huo.
Basi kitendo cha kumuona mzee Mboma katika kundi lile kilinifanya nizidi kutaharuki.
‘Kwani mtu akifa huwa anarudi tena duniani?’ Hili ndilo swali lililofuatia baada ya kuvuta kumbukumbu za mzee huyo aliyekuwa na busara sambamba na hekima mithili ya hayati baba wa taifa, mwl. Julius Kambarage Nyerere.
Sijakaa sawa nikamtambua mtu mwingine, mtu aliyekuwa muhimu sana na mhimili katika maisha yangu. Nilitamani kumkimbilia ili nikamsabahi kwa kumkumbatia. Nilijisahau kabisa kuwa awali nilishindwa kujongea japo ile hatua moja. Nilikosa jinsi baada ya kubaini kuwa hali yangu ilikuwa bado iko vilevile, viungo vya mwili wangu vyote vilikuwa havina nguvu mfano wa mtu aliyepooza.
Nilitaka kumuita lakini nikaishia kugugumia kwani sikuweza hata kukifumbua kinywa changu. Nilimung’unya mung’unya maneno utadhani bubu anayelalamika.
Kushindwa kwenda kumkumbatia ndugu yangu huyo wa damu kuliniumiza sana moyoni. Nilishindwa kupata uhakika ya kwamba na yeye alikuwa kaniona au la! Tatizo hata kuongea kwenyewe sikuweza, japo ningemuita kwa sauti natumai angenisikia.
Mtu huyu si mwingine bali alikuwa ni kaka yangu James, ndugu wa damu tumbo moja japokuwa baba tofauti. Mtu aliyeonyesha umuhimu mkubwa sana baada ya wazazi wangu kufariki.
Hakupenda kabisa kuniona nikihangaika ama kusumbuliwa na shida yoyote katika dunia hii, siyo siri alinipenda sana kaka James.
Upendo ulioshibishwa na udugu wetu ndiyo ulionifanya nimuone mtu muhimu sana chini ya jua. Kila msaada niliomuomba alinisaidia, iwe wa kifedha ama wa kimawazo.
Kwa kuwa hata vikombe hugongana kabatini; siwezi kusema kwamba mimi na James hatukuwa tukikoseana. Pindi tulipokoseana tulisameheana bila kujali ukubwa ama udogo wa kosa jenyewe. Msamaha wetu ulikuwa wa kweli pindi tuliposameheana. Hakika tuliishi maisha ya amani na furaha siku zote, vicheko na matani ya kawaida vilitawala kila tulipokuwa pamoja.
Hata kilipotokea kifo chake sikuweza kujikaza, niliumia sana moyoni mpaka nikafikia hatua ya kupoteza fahamu. Fahamu ziliniijia baada ya masaa matano, nilipozinduka nikashangaa kujikuta nipo hospitali. Niliangaza huku na huko bila mafanikio ya kumuona nesi wala daktari zaidi ya wagonjwa wenzangu waliokuwa wamelala katika vitanda vyao kila mmoja.
Kumbukumbu za kifo cha kaka James zilinifanya nishindwe kuutambua umuhimu wa drip ya maji niliyokuwa nimetundikiwa na kuanza kukimbia kwenda kumzika kaka yangu mpendwa, ndugu yangu wa pekee aliyekuwa mtegemewa katika maisha yangu.
James alichukua uamuzi wa kujiua kutokana na kusalitiwa na mwanamke ambaye alikuwa ni mchumba wake, mwanamke ambaye alimwamini kupita maelezo; akamnunulia nyumba ya kifahari pia na gari zuri la kifahari. Wakaanza mikakati ya kuoana wakaishi pamoja kwenye hilo jumba la kifahari waendelee kuponda mali wakiamini kabisa kuwa kufa kwaja.
Moyo wa James uligongomewa mwiba wa sumu alipomkuta mwanamke huyo yupo na kibwana kingine.
Kibaya zaidi mwanamke huyo baada ya kufumwa alijibu utumbo kwa James na kumwambia hamtaki tena wala hana mpango wa kuolewa nayeye.
Mpaka naingia kaburini mwanamke huyo nitakuwa namfananisha na nyoka ndumilakuwili, tena mwenye sumu kali. Hii yote ni kutokana na kupoteza dira ya maisha yangu kwa kuiangusha nguzo niliyokuwa nimeegemea ambayo ni kaka James.
Mwanamama huyo ilibidi amweleze bayana James kuwa hakuwa na mapenzi ya dhati kwake. Pia alizidi kujifaragua kuwa alijifanya anampenda ili amchune kisawasawa. Baada ya kuridhika kuwa amemchuna vya kutosha ; pesa, nyumba pamoja na gari , mwanamke huyo aliamua kusema ‘byebye’ kwa kaka James na kukitangaza rasmi kimjamaa alichokuwa nacho kuwa hicho ndiyo kimume chake kitarajiwa.
Maneno kama yale yenye kejeli za kila namna yalimkasirisha sana James. Hasira ziliuzidi uwezo wake wa kufikiri, na ndipo alipoamua kufanya mauaji ya kinyama kwa mwanamke huyo pamoja na kimjamaa kile kwa kuwatwanga risasi kila mmoja.
Alipomaliza kufanya tukio hili, moyo wa woga ulimwijia hatiye ukauzidi uwezo wa kuamua. Akaona suluhisho la tatizo lake ni kujimaliza hata yeye pia. Ndipo alipoamua kujifyatua risasi ya kichwa na kufa papo hapo.
Nikiwa bado nimeukodolea macho umati wa watu waliokuwa wamefariki kitambo, akiwemo kaka yangu James, machozi yalizidi kunitiririka mithili ya mto usiokauka kila msimu. Nguvu za kumsogelea nazo sikuwa nazo, nikabaki nikisaga meno na kutikisa kichwa huku niking’ata kidole changu cha shahada na kuendelea kutikisa kichwa. Kufanya hivyo kote hakukusaidia chochote, mambo yalikuwa bado yako palepale, sikuweza kuongea wala kunena chochote.
Nilipumua kwa nguvu, sijakaa sawa nikamtambua mtu mwingine. Nilishindwa kujizuia baada ya kumuona mtu huyo, nikajikuta nikitabasamu.
Kutabasamu kwangu hakukuashiria kuona mlango wa wokovu kwa tatizo lililokuwa likinikabili; tukio lenye maajabu, vitisho na mikikimikiki ya kila aina. Kumuona tena huyo jamaa ndiyo kulinifanya nitabasamu kwani nilikumbuka visa na vituko alivyokuwa akivifanya kipindi cha uhai wake.
Jamaa huyu ni Patrick, Patrick Chibehe; kijana wa kihehe aliyetia fora kwa madeni pale mtaani kwetu. Walipokusanyika watu watano basi watatu au wanne walikuwa wakimdai.
Ulevi wake wa pombe ya kienyeji ijulikanayo kama mabonge ndiyo uliomfanya awe na madeni lukuki. Wakati mwingine alidiriki kuuza hata nguo alizokuwa amevaa kisha kubaki kifua wazi au kubaki na kaputura tu ili apate pesa ya kununulia pombe.
Vituko alivyokuwa navyo wakati wa uhai wake ndivyo vilivyonifanya niachie tabasamu likifuatiwa na kutikisa kichwa. Nilikumbuka jinsi alivyotuingiza mjini kwa kutuuzia TV moja watu watatu tofauti.
Kumbukumbu zilizidi kunijia jinsi kijana huyu alivyopoteza uhai wake kimzaha mzaha. Aliamua kujinyonga kwa kutumia mkanda wa suruali yake baada ya kuambiwa kuwa wadai wake tumemshitaki kituo cha polisi. Aliona njia pekee ya kujiokoa na hilo janga ni kujinyonga.
Kwa kweli nilishindwa kabisa kuamini kwa hicho nilichokuwa nakiona, nikabaki nikijiuliza kwa nini kila niliyemtambua katika kundi hilo alishakufa. Nilianza kufikiria kuwa labda hata wale wengine ambao nilikuwa siwatambui katika hilo kundi walikuwa wameshakufa.
‘Kwa hali kama hii huenda hata wazazi wangu nitawaona.’ Wazo hilo lilinijia baada ya kuwaona mzee Mboma, kaka James pamoja na Patrick.
Niliendelea kukodoa macho walipokuwa watu hao, nikazidi kuumia kutokana na vilio walivyokuwa wakivitoa. Nikazidi kujiuliza;
‘Watu husema kuwa mtu akifa huenda kupumzika kwa amani, mbona sasa hawa wanalia?’ Nilikosa jibu kabisa.
Nilikomaa kuangaza angaza nikijipa moyo ya kwamba huenda nitamtambua mtu mwingine, hasahasa shauku yangu ilikuwa ipo kwa wazazi wangu waliofariki kitambo nikiwa bado nipo darasa la tatu. Pamoja na kukodoa kwangu macho niliambulia kapa, sikufanikiwa kuwaona baba yanga na mama yangu katika kundi hilo.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Katika harakati za kuhangaika kutafuta mtu mwingine ambaye ningeweza kumfahamu kutoka kwenye hilo kundi, nilimuona mtu ambaye aliamsha machungu ndani ya mtima wangu. Donda lililokuwa limeanza kupona moyoni mwangu sasa lilitoneshwa tena na kitendo cha kumuona mtu huyu, tena lilitoneshwa kwa msumari wa moto.
Niliyasikilizia maumivu hayo yazidiyo maumivu ya mwanamke anayeumwa na uchungu wa kujifungua, hasa uchungu wa mimba ya kwanza.
Marehemu Anna, aliyekuwa kipenzi cha moyo wangu, ndiye niliyemuona kwa wakati huo. Naye alikuwa analia kama walivyokuwa wanafanya wale wengine katika hilo kundi. Nilivuta na kushusha pumzi, nikakodoa macho pima zaidi ya vile nilivyokuwa nimekodoa mwanzo huku mdomo ukiwa wazi!
‘Ama kweli leo ndiyo leo, ngoja nisubiri hatima yake.’ Niliwaza kimoyomoyo huku mdomo ukiendelea kuwa wazi, kamasi pamoja na machozi vilianza kunitoka hata sikuwa na muda wa kuviondoa badala yake nilizidi kuviachia vitiririke mpaka basi.
Mrembo Anna, niliyezoea kumuita ‘queen’; msichana aliyekuwa amefanikiwa kuuteka moyo wangu kwa kiasi kikubwa, siku hiyo alikuwepo mbele yangu. Msichana niliyemuamini kiasi kwamba niliapa kumzika endapo asingenizika. Tena aliniahidi kunitunzia zawadi adimu, zawadi ambayo wasichana wengi wa siku hizi wamepungukiwa, zawadi ya usichana wake ama bikira yake. Hakika nilikuwa naingojea kwa hamu kubwa.
Zawadi hiyo alikuja kuipoteza pasipo yeye kutaka; siku ambayo alimsindikiza dada yake kwenye ‘birthday’ ya mpenzi wake. Walipofika huko mambo yalikuwa ndivyo sivyo; alitokea kijana mmoja ambaye alimtaka kimapenzi.
Anna hakuwa tayari kwa vile alikuwa akinipenda na kunithamini pia. Hakutaka kabisa kunisaliti wala kumzawadia kidume mwingine yeyote tunu adimu kama ile. Kikombe kile kilikuwa ni halali yangu kukivunja.
Kwa kuwa mazingira yenyewe yalikuwa hatarishi, msimamo wa Anna haukuzaa matunda yoyote. Kijana huyo aliamua kutumia ubabe baada ya sera zake kugonga mwamba, na kweli alifanikisha. Aliamua kumbaka Anna, kitendo ambacho kiliyavunja maagano yetu.
Baada ya Anna kunieleza habari hizo, habari ambazo zilileta msiba mkubwa ndani ya moyo wangu, nilimuomba anipe muda wa wiki mbili kabla ya kutoa uamuzi wangu juu ya hiyo hujuma ya tunu yangu. Vilevile nilitoa shinikizo la kwenda kupima virusi vya ukimwi baada ya miezi mitatu.
Wakati tukisubiria miezi mitatu ikamilike ili tuende kupima VVU, nilipokea taarifa za kifo cha mpenzi Anna, taarifa ambazo zilionekana kuuchoma moyo wangu mkuki wenye sumu kali.
Anna alipoteza uhai wake baada ya majaribio ya kuitoa mimba aliyoipata siku aliyobakwa. Kabla mauti hayajamfika aliandika ujumbe uliosisitiza kuwa ataendelea kunipenda hata huko aendako.
Anna sasa alikuwa yupo mbele yangu, nilitaka kumnyoshea mikono nimuite japo kwa ishara. Hata hivyo nilishindwa kutokana na kukosa nguvu katika mikono yangu.
‘Sasa Anna atajuaje kuwa nipo karibu yake, tena nimemuona!’ Nilizidi kuchanganyikiwa huku nikiwaza vile.
Bila kutegemea nilimuona akinisogelea, moyo wangu ulianza kufarijika kidogo kidogo. Nikaanza kujipa matumaini ya kwamba huenda nitapata kuongea na Anna wangu.
Nilimsubiria kwa shauku kubwa. Alinisogelea hadi akanikaribia, sasa alikuwa yupo umbali wa kama mita tatu hivi kutoka nilipokuwa. Alizidi kutoa kilio cha kuomboleza, nikaanza kumuonea huruma mpenzi wangu wa tangu zamani, tulikuwa tukipendana ila kifo ndicho kilichotutenganisha.
Alifungua kinywa chake na kuanza kunena,
“mpenzi wangu Brighton, najua nilikukosea sana, na siyo wewe peke yako bali hata jamii kwa ujumla. Huko tuliko tunateseka sana, tena mimi nateseka mara mbili ya wenzangu. Kawaambie binadamu huko duniani kuwa kuua ni dhambi kubwa mno, adhabu yake ni kali kupita maelezo.” Aliongea kwa masikitiko makubwa huku akionekana ni jinsi gani alivyokuwa anaugua moyoni.
Nilitaka kumuuliza swali, tatizo nilikuwa bado siwezi kuongea. Nilibaki nimemwangalia bila ya kupepesa macho. Aliendelea kunihubiria,
“adhabu yangu imekuwa tofauti na za wengine kwa sababu niliua mara mbili, nilikiua kiumbe kilichokuwamo tumboni mwangu kisha na mimi nikajiua. Japokuwa uhai niliupoteza baada ya kupoteza damu nyingi nilipotoa mimba, kitendo hicho kilinifanya nihesabike kuwa nilijiua; kosa ambalo ni la kuua.
Usijaribu kabisa kuua wala kujiua. Yeyote afanyaye hivyo makazi yake ni hii sehemu tuliyopo. Brighton; kazidi kutenda mema duniani ili siku zako zitakapoisha ukapumzike kwa amani na siyo kwa mateso kama tunavyopumzika sisi.”
Ghafla mwanga kama wa radi ulitokea alipokuwa amesimama Anna. Ukali wa mwanga huo ulinifanya nifumbe macho. Nilipigwa na bumbuwazi baada ya kufumbua macho kwani sikumuona Anna wala lile kundi la wale kina mzee Mboma. Nilishangaa kujiona nipo kitandani kwangu kwenye chumba changu. Kumbe ilikuwa ni ndoto tu.
Nilikukuruka huku nikihema. Kumbe nilikuwa nimepiga yowe kwa nguvu kabla ya kughutuka, yowe hilo nililolitoa bila kujijua lilimfanya mpangaji wangu atoke chumbani kwake na kuja kwenye mlango wa chumba changu kufahamu kulikoni. Nikiwa bado nahema nilisikia mlango ukigongwa, nilijikaza na kuuliza ni nani aliyekuwa anagonga.
Sauti ya Kishoka ilisikika ikinijibu, taratibu niliinuka kwenda kufungua mlango baada ya kung’amua kuwa mgongaji wa mlango ni mpangaji wangu.
Baada ya kumfungulia aliniuliza,
“kulikoni kaka, mbona umepiga yowe kwa nguvu sana, ni nini kimekusibu?”
“Kaka mimi nilikuwa nimelala, wakati nimelala nikaota ndoto lakini siikumbuki!” Hilo ndilo lilikuwa jibu langu kwa swali la Kishoka.
“Basi utakuwa umeta ndoto ya kutisha sana maana makelele uliyokuwa unapiga yalikuwa siyo ya kawaida.” Aliniambia kwa sauti iliyojaa kila aina ya upole.
“Ndoto niliyoota ni ya kutisha lakini sikumbuki jinsi ilivyokuwa, isitoshe huwa sina kawaida ya kuota mchana.” Nilimalizia kwa kushusha pumzi huku akili yangu ikijaribu kurudisha kumbukumbu nyuma.
Kumbukumbu zilianza kunijia kwa mbaali sana, zikawa zinakuja na kuondoka utadhani ‘network’ ya simu zilizochakachuliwa, simu zinazouzwa na matapeli chini ya mnara. Katika kukumbuka nilianza kukumbuka kuwa nimemuona marehemu Anna ndotoni.
Akili yangu sasa ikawa ‘busy’ zaidi ya ‘customer care’ wa mtandao wa simu wenye wateja lukuki wanavyokuwaga. Nilizidi kuvuta kumbukumbu juu ya ndoto niliyoota, ndoto ya kutisha ambayo nilikuwa nimeiota muda mfupi uliopita nilipokuwa nimelala, ndoto ya mchana.
Mara nikaikumbuka yote, nikaanza kumsimulia Kishoka ndoto hiyo ilivyokuwa, nilimsimulia mwanzo mpaka mwisho.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nikamsimulia jinsi ndoto yangu ilivyokuwa imetawaliwa na watu waloikufa kitambo, tena vifo vyao ni vya kujiua kila mmoja. Kipenzi changu Anna, Kaka James, mzee Mboma, Patrick pamoja na watu wengine lukuki ambao sikuweza kuwatambua niliwashuhudia kwenye hiyo ndoto .
Kishoka akaniambia kuwa hiyo ni ndoto tu kama zilivyo ndoto zingine. Alianza kwa kunifafanulia tafsiri ya neno ndoto; akaniambia ndoto kwa jina jingine huitwa njozi ama ruya.
Aliendelea kuniambia kuwa ndoto ni mkusanyiko wa mawazo makuu yaliyokuwa yametawala katika kichwa cha muotaji kipindi hajalala ama siku za nyuma. Akili inapokuwa imepumzika wakati mtu yupo usingizini kichwa huweza kukumbuka matukio hayo na kuyaundia picha ambayo huwa kama tukio halisi.
Maelezo ya Kishoka hayakuniingia akilini kabisa, nikamkubalia tu ili turudi kwenye pointi yetu ya msingi, yaani fasiri ya ndoto niliyokuwa nimeota. Nilimuuliza ndoto hiyo ina maana gani?
Hata hivyo alinijibu kuwa yeye siyo bwana njozi, lakini alivyokuwa anahisi ni kwamba akili yangu itakuwa imetawaliwa sana na kuwawaza watu wawili, watu ambao hata kwenye ndoto hiyo nilikuwa nimewaota, yaani marehemu kaka James pamoja na mpenzi wangu wa zamani marehemu Anna.
Kuondokewa na watu hawa katika maisha yangu kulikuwa kumeniathiri sana kisaikolojia na ndiyo maana nikawaota. Hivi ndivyo Kishoka alivyoning’amua.
Nilimuuliza kuhusu mzee Mboma, Patrick na wengineo ambao sikuwatambua; sikuwa na mawazo sana juu yao, wengine nilikuwa sijawahi hata kuwaona. Sasa kwa nini nao waonekane kwenye ndoto yangu? Kweli sikatai kuwa kifo cha mpenzi wangu na kaka yangu kilikuwa kimeniathiri sana kisaikolojia, lakini siyo hao wengine, sasa kwa nini nao niwaone?
Jibu alilonijibu Kishoka ni kwamba hakuna mechi isiyokuwa na washangiliaji, pia akaongezea kuwa hakuna ‘muvi’ inayochezwa na kinara peke yake, lazima pawepo na wahusika waalikwa. Hivyo wahusika wakuu wa ndoto yangu walikuwa ni Anna na James, wengine wote walikuwa wahusika wadogowadogo. Mpaka hapo nilikuwa nimemuelewa kwa kiasi fulani.
Aliniacha na kwenda zake, nikiwa bado nipo kwenye kitanda changu cha sita kwa sita, niliendelea kuitafakari ndoto ambayo nilikuwa nimeiota muda mfupi uliopita. Maneno ya Anna yenye ujumbe mzito yalizidi kujirudia kichwani mwangu.
Niliangalia saa yangu ya mkononi, nikaona masaa yanayoyoma, saa kumi na nusu ilikuwa inaelekea. Wazo la kwenda ufukweni kupunga upepo lilinijia, nikaenda kuoga kwanza kabla ya kuanza safari yangu ya kuelekea ufukweni. Baada ya kuoga ‘nilitupia pamba’ za kufa mtu mwilini mwangu; kaputura ya jinzi na fulana yenye mikono ya kuishia mabegani.
Nilienda kwenye ‘dressing table’ langu kisha nikajipulizia marashi, nikaanza kwenda nilikokuwa nimekusudia kwenda. Nikiwa njiani nilizidi kuumiza pua za watu waliopita karibu yangu kwani marashi niliyokuwa nimejinyunyiza yalikuwa na harufu kali.
Huku nikitembea taratibu nilianza kuisikia harufu ya bahari, mara nikaanza kuukanyaga ufukwe. Nikiwa naambaa ambaa kandokando mwa bahari, nilimuona mwanadada amekaa mbele yangu. Nilianza kumfuata ili nikampe ‘hai’, na ikibidi tupigepige soga kubadilishana mawazo.
Nilipomkaribia akainuka, hapo ndiyo niliweza kuushuhudia uzuri aliojaaliwa na Muumba. Kichwani nywele ndefu, kifuani maziwa yaliyojaa kiasi, kiunoni palikuwa pamekatika kidogo kisha pakafuatiwa na wowowo la wastani.
Nilizidi kukoshwa na hipsi zake sanjari na mguu wake wa bia. Mwanadada huyo alikuwa kavaa kipedo pamoja na kitopu. Kwa jinsi alivyokuwa ametokelezea nilijikuta nikivutiwa naye kabla hata sijaanza kuongea naye.
Kabla sijafika alipokuwa nilimuona kajinyosha kisha akaanza kuchapa lapa, bila kujishauri mtu mzima nilijikuta nikiropoka kwa nguvu,
“samahani dada, naomba kuzungumza na wewe kidogo.”
Licha ya kutanguliza neno la kiungwana, yaani samahani, mwanadada huyo hakusimama wala hakugeuka kunitazama.
Nilianza kumfuata kwa nyuma nyuma, nilipoanza kumfuata nilishangaa kumuona anaanza kukazana. Nilishindwa kuelewa ni kwa nini alikuwa muoga kiasi hicho, nilimuita tena kwa mara ya pili lakini aliendelea kunichunia.
“Wewe dada, inamaana hujanisika au hujanielewa?” Hilo ndilo swali nililomtwanga huku nikimfuatia kwa nyuma.
Kwa mara ya kwanza niliisikia sauti yake nyororo, sauti yenye kuweza kumtoa nyoka pangoni ama kumtoa sungura kwenye kichuguu. Sauti yake adimu ni moja ya sauti ambazo huaminika kuvuta mvua mpaka ikanyesha hata kama ni kiangazi.
“Utanisamehe kaka yangu kwa sababu nina haraka kwelikweli, ila usijali, nitakuja kwako kesho asubuhi!” Alinijibu bila ya kugeuka kuniangalia.
Niligutushwa na kauli yake hiyo, kauli ya kwamba atakuja kwangu kesho asubuhi. Akili yangu ilianza kuwaza mara mbilimbili bila kupata jibu.
‘Nimeiona sura yake kwa macho yangu mawili ya damu na nyama, tena mchana kweupe lakini sijamfahamu, sasa iweje yeye awe anapafahamu mpaka nyumbani kwangu?’ Nilizidi kuwaza.
Nilimuuliza kama anapajua ninapoishi naye akasema anapajua. Nikamuuliza kama ananifahamu mimi, akanijibu kuwa ananifahamu, tena kwa kukata mzizi wa ubishi alinitajia hadi jina langu,
“wewe si unaitwa Brighton mdogo wake na marehemu James!” nilizidi kuchoka.
Chaajabu maongezi yetu yalikuwa yanafanyika huku tukiwa tunatembea, yeye yupo mbele na mimi nipo nyuma, nikajaribu kumbembeleza ageuke ili nimuangalie kwa makini huenda na mimi ningemtambua lakini hakukubali.
‘Huyu mrembo mbona simuelewi? Anadai ananifahamu, kwa nini sasa asisimame japo kidogo tusalimiane? Kama ananifahamu kweli na pia anapafahamu ninapoishi, kwa nini asisimame japo dakika sifuri tukasabahiana kisha akaendelea na safari yake?’ Niliwaza na kuwazua huku nikiendelea kuchapa lapa nikiwa nyuma ya mlimbwende huyo.
Nilitembea kwa takribani dakika kumi nikimfukuzia msichana huyo lakini alikuwa hajakubali kunisubiri au kugeuka kuniangalia. Hakutaka kabisa kunielewa kwani kujikomba kwangu kote ilikuwa ni sawa na kumuimbia kiziwi ama kummulikia kipofu.
Niliamua kuachana naye huku nikijipa matumaini kuwa kesho siyo mbali,
‘tena si kasema mwenyewe kuwa atakuja kunako anga zangu? Hahaaaa!’ Nilijikuta nikiangua kicheko cha dharau huku nikigeuka nyuma kuanza kurudi ufukweni.
Nilitafuta mahali palipokuwa pametulia ili nijipumzishe, nieendelee kufurahia upepo murua unaovuma bila bughudha kandokando ya bahari.
Mawazo ya ndoto ambayo nilikuwa nimeiota masaa machache kabla ya kwenda ufukweni yalianza kupotea. Nikaanza kuamini usemi wa baadhi ya watu wanaodai kwamba ufukweni ni sehemu ya kupotezea mawazo na kutuliza akili. Kwa wakati huo usemi huo nilikuwa siutilii shaka hata kidogo.
Kichwa changu sasa nilianza kukiona ki chepesi, uzito kiliokuwa nao mara baada ya kugutuka kutoka ndotoni nikawa siuhisi tena. Niliamua kuanza kurudi nyumbani kwani machweo nayo yalikuwa yamewadia.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ilikuwa ni asubuhi, kwa muda huo nilikuwa nipo kwenye meza ya chakula nikipata kifungua kinywa; supu ya kuku na mikate ya boflo.
Mara nilisikia kengele ya getini ikinijuza kuwa kuna mgeni pale getini. Nilimuomba Kishoka aende kumsikiliza mgeni aliyekuwa anapiga hodi kule getini kwani mimi nilikuwa ninakula wakati yeye alikuwa hali. Naye bila ubishi aliondoka na kwenda getini.
Punde si punde alirudi, akaja na taarifa iliyosema kwamba mgeni aliyekupo pale nje kakataa kuingia ndani hivyo ananitaka niende tukaongee palepale nje. Nilipomuuliza Kishoka mwonekano wa mgeni huyo upoje, alinieleza jinsi alivyokuwa. Mwonekano wa mgeni huyo kwa mujibu wa maelezo ya Kishoka ulionekana kuendana na mwonekano wa msichana niliyekuwa nimemuona jana yake kule ufukweni.
“Umemuuliza jina?” Nilimuuliza tena Kishoka.
“Ndiyo nimemuuliza.”
“Akakwambia anaitwa nani?”
“Alichonijibu ni kwamba nije nikuambie kuwa mlionana naye jana kule ufukweni na mkapeana miadi ya kuonana leo asubuhi.”
Nilifurahi sana kusikia kuwa mrembo wa jana aliyejifanya kudengua kaingia kwenye anga zangu mwenyewe.
Niliinuka na kuachana na supu yangu haraka kisha nikaenda moja kwa moja mpaka getini kumwangalia mgeni huyo. Nikiwa naelekea huko getini nilijaribu kujifutafuta midomo yangu ili kuondoa mabaki ya boflo na mchuzi wa supu ya kuku.
Nilifika mpaka getini, nikafungua geti na kuangalia pale nje, cha ajabu sikuona mtu yeyote. Nikaanza kujiuliza mgeni aliyekuwepo hapo kaenda wapi? Kusema kakaa sana mpaka akachoka kusubiria huo ni uongo kwani ulikuwa haujapita muda mrefu sana tangu Kishoka aingie ndani kuniita, sikujua alikokuwa kaelekea.
Hata kama angekuwa kaghairi kunisubiri akaondoka, haiwezekane nisimuone wakati njia ya kutoka kwangu kuingia kwenye barabara ni ndefu kiasi, ni kama mita mia moja kutoka kwenye geti la nyumba yangu mpaka kufika kwenye barabara kuu.
Nilijaribu kuangaza kwenye njia lakini sikuona mtu. Nikaamua kurudi ndani kuendelea kushambulia boflo zangu na supu yangu ya kuku.
Wakati namalizia zoezi nililokuwa nalo, zoezi la kupata kifungua kinywa, simu yangu ya mkononi ilianza kuita. Niliangalia namba iliyokuwa inanipigia lakini nilishindwa kuitambua, yaani ilikuwa ni namba ngeni ambayo haijahifadhiwa katika simu yangu. Taratibu nilibofya kitufe cha kupokelea kisha nikapeleka simu sikioni.
Sauti nyororo ilisikika kwenye spika za simu yangu, sauti iliyokuwa ikijitambulisha kuwa ni mtu niliyeongea naye jana kule ufukweni. Nilipomuuliza yuko wapi aliniambia yupo nyumbani kwao hivyo miadi yetu angependa iwe muda wa jioni.
Nilijaribu kumuuliza kama alikuwa kaja nyumbani kwangu muda mfupi uliopita, naye aliniambia hajaja. Pia aliongezea kuwa mpaka muda huo ananipigia simu alikuwa bado yupo kitandani wala hajaachana na shuka.
Kwa kweli nilianza kuchanganyikiwa upya, Kishoka alipoenda kufungua geti alimkuta dada aliyedai kuwa nilionana naye jana kule ufukweni, huyo aliyenipigia simu naye alijitambulisha kuwa nilikuwa naye ufukweni siku iliyopita.
Nilishindwa kuelewa jinsi mambo hayo yalivyokuwa yakienda,
‘ufukweni mimi niliongea na msichana mmoja tu, msichana ambaye alikuwa hataki hata kugeuka kunitazama. Sasa mbona wamefika wasichana wawili wanaodai tumeonana ufukweni?’ Niliendelea kuumiza kichwa nikiwaza juu ya tukio hilo la kushangaza na kustaajabisha.
Hata hivyo nilishindwa kupata jibu. Niliishia kubetua mabega huku akili yangu ikizidi kuchoka kutokana na maajabu hayo. Niliamua kuachana na suala hilo, nikaingia chumbani kwangu kujiandaa ili nitoke kuelekea katika mizunguko ya kila siku kwani tayari nilikuwa nimeshamaliza kustaftahi.
Wakati nikiwa chumbani mlango wa chumba changu ulianza kugongwa. Nami nilienda kufungua ili nimuone aliyekuwa anagonga. Nilimkuta Kishoka yupo pale mlangoni.
“Kaka umesema ulipoenda getini hukumuona yule shori, mbona mpaka sasa hivi bado yupo?” Lilikuwa ni swali la Kishoka aliloniuliza baada ya kufungua mlango.
Taarifa hiyo ilizidi kunishtua, nikaanza kujawa na wasiwasi na hofu fulani. Hata hivyo nilijikaza kiume na kumwambia Kishoka tuende wote mpaka getini tukahakikishe kama kweli kuna mtu.
Tuliondoka kuelekea getini, tulipofika hatukuona mtu yeyote, tuliangalia njiani lakini hatukuona hata dalili za mtu kuondoka getini muda mfupi uliopita. Tulibaki tukiangaliana bila kuongea chochote. Tukio hilo lilikuwa geni kabisa nyumbani kwetu.
Pale getini hapakuwa na sehemu ya kusema kwamba labda mtu huyo alikuwa anajificha, palikuwa ni peupe kabisa. Sasa hata Kishoka naye alianza kuigiwa na wasiwasi.
Kutoka hapo getini sikutaka hata kurudi ndani. Nilimwambia Kishoka akaufunge mlango wa chumbani kwangu kisha anichukulie funguo zangu zilizokuwa zikining’inia kwenye mlango wa chumba changu, naye akaenda.
Punde si punde Kishoka alirudi na kunipa funguo zangu. Aliponikabidhi niliondoka zangu kuelekea mitaani huku nikimuacha yeye yupo hapo nyumbani.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment