Search This Blog

Thursday, 2 June 2022

MIRATHI YA KAKA - 2

 







    Simulizi : Mirathi Ya Kaka

    Sehemu Ya Pili (2)



    ILIPOISHIA........

    Punde si punde Kishoka alirudi na kunipa funguo zangu. Aliponikabidhi niliondoka zangu kuelekea mitaani huku nikimuacha yeye yupo hapo nyumbani.

    SASA ENDELEA.......

    Wakati wa jioni nikiwa narudi nyumbani nilipitia sokoni kununua matunda, nikiwa sokoni nilimuona msichana mmoja, msichana huyo alikuwa anafanana sana na yule niliyemuona  kule ufukweni. Siyo kwa sura tu, bali mpaka mavazi aliyokuwa amevaa siku ile ufukweni.

                Nilimsogelea na kumwambia dada mambo naye akanijibu poa. Baada ya kuisikia sauti yake nilibaini kitu, sauti hiyo haikuwa na tofauti na sauti ya msichana aliyekuwa akinizingua kule ufukweni, yaani sauti ileile ya mwanadada niliyekutana naye nikaanza kumuita asikubali hata kunisubiri.

    Sauti yake hiyo iliyokuwa nyororo kiasi kwamba hata kama ulikuwa na homa ukiisikia tu unapata afueni. Sauti ambayo husemekana inauwezo wa kumtoa chura mtoni aisikiapo.

                Nilijikakamua na kumuuliza kama alikuwepo ufukweni jana yake. Akakanusha kanu na kusema yeye huwa hana kawaida ya kwenda ufukweni. Nilimuuliza tena kama ananifahamu mimi naye akasema ilikuwa ndiyo mara yake ya kwanza kuniona. Niliamua kuachana naye baada ya kukumbuka usemi wa wahenga usemao kuwa duniani wawili wawili.

                Lakini sura yake, nguo alizokuwa amevaa pamoja na sauti yake havikuwa na tofauti hata kidogo na yule msichana  wa ufukweni. Nilibaki kuwaza huku nikiendelea na safari yangu ya kurudi nyumbani.

                Nikiwa njiani simu yangu ya kiganjani ilianza kuita, nikaitoa mfukoni na kuangalia namba ya aliyekuwa ananipigia. Nilibaini kuwa kumbe alikuwa ni Kishoka, nilibonyeza kitufe cha kupokelea kisha nikamsikiliza alichokuwa anasema.

                “Kaka uko wapi?” Aliniuliza nami nikamjibu nipo njiani kuelekea nyumbani. Baada ya kumjibu hivyo aliniambia kuwa msichana aliyezuru kwetu asubuhi alikuwa kaja tena na alikuwa ananisubiri. Nilimwambia nipo karibu kufika kisha nikakata simu na kuirudisha mfukoni.

                Nililazimika kuongeza mwendo kama si kuanza ‘kutroti’ ili nimuwahi mgeni wangu niliyeambia ananisubiria, mgeni ambaye tangu jana alikuwa ananizingua kule ufukweni. Wakati mwingine woga flani ulianza kuniingia kutokana na maajabu aliyokuwa ananionyeshea tangu asubuhi.

                Nilipofika mita chache kutoka kwenye geti la nyumba yangu simu yangu ilianza kuita tena, nilipoiangalia namba niliikumbuka. Namba hiyo ndiyo iliyokuwa imetumiwa na msichana huyo kunipigia asubuhi akidai miadi yetu iwe jioni.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

                Niliipokea na kusikiliza kilichokuwa kinasemwa, mwanadada huyo alilalamika sana akidai nimechelewa. Nilimwambia avute subira kidogo kwani mimi nilikuwa tayari nipo getini kwa wakati huo.

    Msichana huyo alikataa katakata kuningoja akidai kwamba nimechelewa, muda aliokuwa ameutenga kwa ajili ya miadi yetu ulikuwa umeisha.

                Huku nikifungua geti nilijitahidi kumsihi anisubiri japo kwa muda wa dakika sifuri kwani nilikuwa nipo getini, hata hivyo aliendelea kushikilia msimamo wake akidai ndiyo anaondoka ndani na hawezi kurudi tena.

    Kauli hiyo ndiyo aliyomalizia kuongea kisha akakata simu. Huku nimeshikilia simu mkononi nilifunga geti na kuelekea ndani haraka haraka kumwahi mgeni wangu ambaye alikuwa kacharuka kuondoka.

                Nilijipa matumaini kwamba ningekutana naye nje ya nyumba akielekea getini ama ningekutana naye mlangoni. Na kama ningekutana naye basi ningejaribu kumbembeleza ili arudi tena ndani japo dakika tatu ndipo aende zake, lengo langu ni kutaka kumuona kwenye mwanga ili nimfaidi, nikishamuona basi hata aende zake.

                Mpaka nafika mlangoni sikukutana na mtu, nilifungua mlango na kuingia ndani nikijua kuwa mgeni wangu huyo alikuwa kanielewa na kuamua kunisubiri. Wakati nafungua mlango jicho lilikuwa ‘busy’ kuangalia kwenye sofa ili nimuone mgeni wangu.



    Tofauti na matarajio yangu, jicho langu halikuona chochote kwenye sofa, kulikuwa ni kweupe. Hapakuwa na mgeni wala Kishoka lakini tv ilikuwa inawaka na redioni ilikuwa inasikika ZBC radio ikiunguruma kwa mbaali, kituo cha radio ambacho mimi na Kishoka hupenda kukisikiliza kila wakati. Hata kama tv iwe imewashwa, midundo ya ZBC radio ilikuwa ikisikika kwa chini chini.

                Ndivyo ilivyokuwa hapo sebuleni kwa wakati huo, lakini aliyekuwa akisikiliza radio wala kuangalia tv sikumuona. Nilijaribu kumwita Kishoka lakini hakuniitikia, nikaamua kwenda mpaka kwenye chumba chake kumwangalia, niliukuta mlango umefungwa, nikajaribu kugonga lakini sikujibiwa.

                Nilijaribu kuusukuma mlango nao ukafunguka, nikaangalia chumbani humo lakini sikuona mtu, nikaamua kurudi tena sebuleni nikidhani nitakuta mabadiliko, nilipofika nilikuta hali ni ileile kama ya awali, hapakuwa na Kishoka wala mgeni.

                Nilipata wazo la kumpigia simu Kishoka ili nimuulize alipo, nilipopiga simu  ilianza kuita mpaka ikakata. Mlio wa kupokelea wa simu hiyo ulisikika ukiita kwenye chumba changu. Nikabaki nikijiuliza kuwa Kishoka kaenda kufanya nini chumbani kwangu, vilevile kwa nini sasa alikuwa hapokei simu? Nilijiuliza kimoyomoyo baada ya simu kuita bila kupokelewa.

    Niliamua kwenda mpaka chumbani kwangu kuona alichokuwa anakifanya Kishoka kiasi kwamba mpaka anaichunia simu yangu. Nilianza kuhisi kuwa huenda alikuwa anafanya kamchezo kachafu na mgeni wangu kwani naye kwa mambo hayo alikuwa hajambo, alikuwa havumi tu lakini yumo.

    Lakini bado kuna kitu kilikuwa kinanichanganya, katika kumbukumbu zangu wakati natoka mlango ulikuwa umefungwa na funguo nilikuwa nazo, hiyo simu ya Kishoka ilifikafikaje chumbani kwangu? Kishoka mwenyewe alikuwa kaingiaje huko chumbani wakati funguo nilikuwa nimeondoka nazo? Au asubuhi nilisahau kuufunga mlango? Nilibaki na maswali ambayo majibu yake yangepatikana baada ya kumhoji Kishoka.

    Shauku ya kutaka kujua alichokuwa anakifanya Kishoka humo chumbani kwangu ilinikaa rohoni. Nilikuwa nikiwaza mambo mia kidogo kabla ya kufika mlangoni;

    ‘huyu Kishoka yuko peke yake au yupo na  huyo mgeni, maana mpaka naingia ndani sijakutana naye wakati mara ya mwisho kuongea naye kwenye simu nilikuwa nimekaribia getini kwangu. Angekuwa ni mtokaji basi ningekutana naye walau karibu na geti kama siyo mlangoni.’

    Nilipofika mlangoni nilibaini kuwa mlango ulikuwa haujafungwa bali ulikuwa umerudishiwa tu. Nilizidi kujiuliza kuwa umefunguliwaje wakati kipindi naondoka funguo niliondoka nazo? Nilizidi kuduwaa.

    Mara nilikumbuka kuwa wakati natoka mlango sikuufunga mimi bali aliufunga Kishoka.

    ‘Kama alikuwa amesahau kuufunga au alikuwa ameuacha kwa makusudi basi atakuwa kaingia kiulaini, lakini kaingia kufanya nini chumbani kwangu? Bila shaka Kishoka anafanya matusi na mgeni wangu chumbani kwangu.’ Mawazo yangu yalianza kunituma vile kwa wakati huo.

    Ndipo nilipouona mwanga wa taa ikiwaka chumbani, nikazidi kujawa na ghadhabu.

    ‘Wamewasha hadi taa utadhani ni chumbani kwao, hizi sasa ni dharau. Kwa nini asimpeleke chumbani kwake?’ Nilizidi kujisemea kimoyomoyo.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

     ‘Lakini Kishoka huwa hana kawaida ya kuingia chumbani kwangu kama sipo, na hata kama angekuwa na kawaida hiyo asingefanya hivyo kwani alikuwa kanipigia simu muda si mrefu kunijuza kuwa kuna mgeni wangu ananisubiri nami nikamwambia nipo njiani.’ Nilizidi kuwaza huku masikio yakiwa makini kusikilizia chumbani kama kuna mihemo ama miguno ya watu wakifanya matusi.

    Lakini suala la Kishoka kusahau kuufunga mlango wangu ama kuacha kwa makusudi lilikuwa haliniingii akilini hata kidogo kwani alikuwa ni mtu mwaminifu sana. Sasa aliingiwa na ibilisi gani mpaka akaamua kutofunga mlango wangu. Na kama alikuwa kafunga aliingiaje wakati funguo nilikuwa nazo na nilikuwa sina kawaida ya kuziacha? Funguo nilikuwa natembea nazo utadhani pete ya ndoa kwa mwanandoa mwaminifu!

    Nilizidi kujiuliza maswali teletele huku nikiusogelea mlango. Nilipousukuma mlango nilizidi kuchanyikiwa baada ya kukiona kisu kilichokuwa kimetapakaa damu kikiambaa ambaa pale mlangoni kunako tambala la kufutia miguu.

    Nililazimika kuingia kwa tahadhari kubwa wakati chumba kilikuwa ni changu, chumba ambacho nilikuwa nimeshakizoea kiasi kwamba hata liwemo giza totoro lakini swichi ya taa sitashindwa kuiwasha. Siku hiyo nilijikuta nikinyata wakati taa ilikuwa inawaka!

                Kwa mwendo wa kunyata niliuvusha mguu wangu wa kwanza pale mlangoni huku ukifuatiwa na mguu wa pili. Nilijaribu kuangaza mbele usawa wa mlango lakini sikuona chochote kigeni zaidi ya kabati langu la nguo na meza ya  kujipodolea yenye kioo kikubwa cha kuweza ujiona nusu mwili; yaani kuanzia kiunoni kwenda juu.

                Wakati huo nilikuwa sijaangalia upande wa kulia wa chumba changu, upande ambao kitanda changu cha sita kwa sita kilipokuwa, si unajua tena mambo ya mila na desturi kitanda sharti kiwe pembeni!

    Niligeuka mzima mzima huku nikitupia jicho langu pale kitandani. Jicho lilipotua kitandani nilijikuta nikibaki mdomo wazi huku nikikodoa macho bila ya kupepesa.

                Lahaula! Mambo yaliyokuwa yametendeka juu ya kitanda changu ni vioja, nilishindwa kuelewa ni nani aliyefanya unyama huo usiokuwa na breki hata kidogo. Nguvu zilianza kuniishia, nikabaki nimeduwaa huku nisijue la kufanya. Sikutegemea kabisa kukuta tukio la kutisha na la umafia namna ile likiwa limetendeka kwangu, tena juu ya kitanda changu.

                Tukio jenyewe lilikuwa ni la mauaji ya kutisha, kichwa cha Kishoka kilikuwa kimetenganishwa na kiwiliwili chake. Kisu kilichokuwa mlangoni kikiwa kimetapakaa damu nadhani ndicho kilichotumika kumchinja mpangaji wangu, yaani Kishoka.

    ‘Chinjachinja ni nani sasa kama siyo yule mgeni wangu? Na kama ndiyo yeye, kajificha wapi sasa wakati sijamuona akitoka?’ Nilizidi kuchoka.

    ‘Kumbe msichana huyo ni hatari! Sioni mtu mwingine wa kufanya kitendo kama hiki zaidi yake, atakuwa ni huyohuyo!’ Nilizidi kunena kimoyomoyo huku nikiisogelea maiti ya Kishoka, maiti ambayo ilikuwa haitamaniki kutokana na  kutenganishwa kikatili, kichwa na kiwiliwili havikuwa pamoja tena.

                Wakati nikitafakari hatua ya kuchukua kwa wakati huo, nilishangaa baada ya kuona watu wawili wanaingia mpaka humo chumbani kwangu utadhani ni kwao vile, wote walikuwa na jinsia ya kiume. Sijakaa sawa wakanipiga ‘henzapu’ na kuniambia nipo chini ya ulinzi.

                Pumzi zilianza kuniishia, nikajikuta nikipumua kwa shida huku kifua changu kikianza kubana. Sijakaa sawa nikaanza kuhisi kama kizunguzungu na kuhisi kama nataka kuanguka. Mpaka hapo nilipoteza ‘network’ na kujikuta sijitambui hata kidogo.



                                        **********************

    Fahamu zilinijia kama mtu aamkapo kutoka usingizini. Kitanda nilichokuwa nimelalia si kile nilichokizoea, kitanda chenye godoro la Dodoma ambacho ni futi sita kwa sita.

    Kitanda nilichokuwa nimekilalia kwa wakati huo kilikuwa ni tatu kwa sita,

    ‘piga ua hiki siyo kitanda changu.’ Nilijikuta nashikilia msimamo huo.

                Huku nikipepesa macho niligundua kitu kingine, humo ndani kulikuwa na vitanda lukuki vilivyokuwa vinafanana. Harufu ya dawa nilianza kuisikia, hapo ndipo nilipong’amua ya kuwa nipo hospitali.

                Huku nikipiga miayo, nilitaka kupeleka mkono wangu wa kuume usoni kujaribu kupangusa tongotongo endapo zipo, mkono uligoma kwenda. Nikaanza kujiuliza ni kwa nini mkono wangu unang’ang’ania kwenye chuma cha kitanda?CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

                Kabla sijaangalia kilichokuwa kinakwamisha mkono wangu wa kulia kunyanyuka, nilitaka kutumia mkono wangu wa pili kusafisha macho yangu, nao ulikuwa mzito kiaina.

    Huku maruweruwe yakififia kwenye mboni za macho yangu, niliinua kidogo kichwa changu kuangalia kilichokuwa kinaufanya mkono wangu wa kushoto uwe mzito kunyanyuka. Ndipo nilipojionea sindano kubwa ikiwa imeunganishwa na mrija wa plastiki ambao unaelekea kwenye nguzo ya chuma iliyokuwepo karibu na kitanda nilichokuwa nimelazwa.

                Nilipoufuatilia mrija huo mpaka ulipoishia nilijionea drip ya maji imetundikwa, huku maji hayo yakitoja taratibu na kuingia kwenye mrija huo kisha kuteremka mpaka kwenye mkono wangu.

                ‘Nimetundikiwa drip ya maji, ni nini kimenisibu mpaka nikafikishwa hapa?’ Nilibaki nikijiuliza bila kupata majibu ya swali langu hilo.

                Wazo la kuangalia kilichokuwa kinaufanya mkono wangu wa kulia ung’ang’nie huko kwenye chuma cha kitanda lilinijia, nikageuza shingo yangu kiasi kwamba mpaka nikaweza kuona kwenye chuma cha kitanda nilichokuwa nimelalia. Moyo uliruka baada ya kukiona kilichokuwa kimeufanya mkono wangu ugande  kwenye chuma hicho.

                ‘Nimefungwa pingu! Ni kosa gani nililofanya mimi mpaka nikafikia hatua ya kulazwa hospitali huku nikiwa nimefungwa pingu. Mimi siyo jambazi na wala huwa sina fikra za kuja kuwa, sasa iweje leo nifungwe pingu mithili ya jambazi aliyeshindikana kisha akakamatwa kwa bahati mbaya?’ Fukuto la maswali mengi lilizidi kukisumbua kichwa changu na akili yangu kwa ujumla.

                Katika kuangaza angaza niliwaona askari wawili waliokuwa wamekaa karibu yangu huku mmoja akiwa ameshikilia mtutu.

     ‘Ama kweli huu ‘msala’ si wa kitoto, nimewekwa chini ya ulizi kwa silaha za moto, hivi nimefanya kitu gani mimi?’ Nilijaribu kuwaza na kuwazua ili nifahamu kilichokuwa kimenisibu lakini ikawa ‘holla’.

                Nilijikakamua na kuamua kuwauliza hao hao waliokuwa wameniweka chini ya ulizi.

    “Samahani afande, hivi ni tukio gani nililofanya mpaka mmeniwekwa chini ya ulinzi ndani ya hospitali?” Nililibwaga swali hilo kwa maafande hao ambao sura zao zilikuwa zimekunja ndita si mchezo.

                “Unajifanya hujui urichokitenda? Acha kuuriza maswari yasiyokuwa na tumbo wara mgongo mura.” Alisikika askari ambaye alikuwa kashikilia cha moto huku rafudhi yake ikinidhihirishia waziwazi kuwa ni mtu wa Mara, yaani mkurya. Tena alinijibu kwa sauti ya ukali utadhani kanishika ugoni kwa mkewe.

    Niliamua kujinyamazia kwa kuhofia kupewa mikong’oto na maafande hao walioonekana kupinda kuzidi maelezo. Alama za mia moja kumi na moja zilizokuwa zimejichora kwenye mapaji ya nyuso zao kwa kukunja ndita zilikuwa zinanitisha.



    Nilitulia na kuamua kuvuta kumbukumbu mwenyewe ili niweze kung’amua kilichotokea na kuniweka matatani kiasi kile. Kumbukumbu zangu zilianza kuniijia kwa mbaali, nilijaribu kuwa makini ili niweze kuyakumbuka matukio yote yaliyokuwa yametendeka tangu asubuhi kwenye mizunguko yangu.

                Nilikumbuka jinsi nilivyoshuhudia kioja cha mwanadada wa asubuhi, mwanadada aliyekaribishwa na Kishoka akakataa kuingia ndani kisha nilipoenda kumwangalia sikumkuta. Kumbukumbu zilizidi kutiririka sasa kwenye fikira zangu, nikakumbuka jinsi nilivyoachana na kioja cha dada huyo na kuondoka zangu.

                Ratiba nzima ya mizunguko yangu nilifanikiwa kuikumbuka kwa marefu na mapana, niliendelea kukumbuka nilivyopigiwa simu na Kishoka wakati narudi nyumbani akaniambia kuwa mgeni wa asubuhi ananisubiri.

    Mpaka nilipofika getini na kuongea naye dada huyo kwa njia ya simu akiniaga kuwa anaondoka kwa madai ya kuchoka kunisubiri, licha ya kumbembeleza kwa kumwambia kwamba nilikuwa getini lakini bado mwanadada huyo aligoma kunisubiri.

                Mpaka naingia ndani kwangu sikuweza hata kumuona japokuwa nilitegemea ningekutana naye. Kumbukumbu ziliendelea kutiririka mpaka nilipoingia chumbani kwangu na kumkuta Kishoka kauawa juu ya kitanda changu.

                Wakati nikitafakari la kufanya watu wawili waliingia na kuniweka chini ya ulinzi. Hapo ndipo kumbukumbu zangu zilifikia kikomo, sikukumbuka tena kilichoendelea zaidi ya kujikuta nipo kwenye mahakama ya magonjwa, sehemu ambayo magonjwa yote yanayowasumbua binadamu hushtakiwa na kutolewa hukumu, yaani namaanisha hospitalini.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

                ‘Sasa nimeelewa, nitakuwa ninadhaniwa kumuua Kishoka. Muuaji atakuwa ni yule mwanamke, lakini lazima nishakiwe mimi kutokana na mazingira ya kifo chenyewe; kweli leo nimeamini kuwa akamatwaye na manyoya ndiye mwizi wa kuku.’ Nilijisemea kimoyomoyo baada ya kukumbuka mkanda wa tukio zima.

                Nilianza kujuta kumfahamu msichana huyo, nilijilaumu mno kwa kumsemesha kule ufukweni siku niliyoanza kumuona. Kama nisingemsemesha huenda yasingetokea haya, ama kweli siku zote busara huja baada ya kutenda.

                ‘Hivi tukio hili ni la kweli au naota?’ Niliendelea kuwaza.

    ‘Lakini hii siyo ndoto, hii ni ‘laivu’, tena ni ‘laivu’ bila chenga.’ Nilijikuta nikijijibu mwenyewe.

                Niliamua kumwachia Mungu kwani yeye ndiye mweza wa yote, yeye ndiye alikuwa anajua suluhisho la kesi iliyokuwa inanikabili, kesi ya mauaji ambayo sikuhusika nayo hata kidogo. Nilijipa matumaini kuwa maadamu sina hatia basi Mungu atakuwa na mimi.

                “Afande, kama vipi richukue maerezo maana tayari rimeshazinduka.” Alisikika afande aliyekuwa ameshikilia bunduki akimwambia mwenzake ambaye alikuwa kashika faili mkononi.

    “Hamna tabu afande, hata mimi nilikuwa ninalifikiria hilo kichwani mwangu.” Alijibu afande huyo



    Mara nilimuona afande huyo aliyekuwa kashikilia faili mkononi akivuta kiti chake na kusogea karibu kabisa na pale nilipokuwa nimelaza kichwa changu. Alifungua faili lake huku akiwa kashikilia kalamu mkononi.

                Alianza kunihoji maswali kuhusiana na tukio zima la mauaji ya Kishoka, kila aliponiuliza nilimjibu, kila nilipomjibu aliandika kwenye karatasi iliyopo kwenye faili lake.

    “Mnaishi wangapi katika hiyo nyumba?” lilikuwa ni baadhi tu ya maswali niliyokumbana nayo kutoka kwa kachero huyo. Swali hilo nililijibu kwa kusema kuwa tunaishi wawili tu katika hiyo nyumba, yaani mimi na Kishoka.

    Mara aliniuliza uhusiano wangu na Kishoka, nami nilimjibu kuwa Kishoka ni mpangaji wangu katika nyumba yangu niliyorithi kutoka kwa marehemu kaka yangu, kaka James ambaye alikufa kifo cha kujiua mwenyewe kwa kujifyatulia risasi kichwani baada ya kumuua aliyekuwa mpenzi wake pamoja na jamaa aliyemfuma akilamba asali ya mapenzi kwa mpenzi wake huyo..

                “Sasa kwa nini umeamua kumuua Kishoka?” Askari huyo alinifyatulia swali jingine. Nami nilimjibu bila kusita wala kujing’atang’ata kwamba mimi sijaua.

    “Kama wewe hujaua, ni nani aliyemchinja Kishoka ilhali mnaishi wawili tu katika hiyo nyumba?”

                Nilijitahidi kuwa makini sana katika maelezo yangu ili nisijikanganyekanganye halafu nikaonekana nimeua kweli. Niliamua kumtaja muuaji, nikasema kuwa ni msichana fulani ambaye alianza kunifanyia vioja tangu juzi nilipokutana naye ufukweni. Nilieleza jinsi mambo yalivyokuwa kati yangu na mwanadada huyo kule ufukweni.

                Nilipoulizwa jina lake na mahali alipokuwa anaishi niliishia kusema sina nijualo juu yake. Nilijaribu kurudia tena kutoa maelezo jinsi nilivyokutana na msichana huyo, sikuwa namfahamu hata kidogo, lakini yeye alidai kuwa ananifahamu na kwa kunithibitishia hilo alinitajia hadi jina langu. Hakuishia hapo tu, aliongeza kuwa mpaka kwangu alikuwa anapajua hivyo akaniahidi atanitembelea kesho yake asubuhi.

                “Ilipofika kesho yake asubuhi kweli alikuja?” Aliendelea kuhoji askari huyo huku akionekana kunisikiliza kwa makini sana.

    “Ndiyo alikuja lakini vilikuwa ni vioja vitupu!”

    “Uliweza kuonana naye na mkaongea nini?” Aliniuliza afande nami nikaanza kumdadavulia vile ilivyojitokeza tangu msichana huyo anafika pale getini, akakaribishwa na Kishoka lakini akakataa kuingia ndani.

                Niliendelea kueleza jinsi msichana huyo alivyopotea kimazingara tusimuone alikoelekea. Nilizidi kuweka wazi kila kilichojitokeza mpaka wakati nilipokikuta kichwa cha Kishoka kikiwa kimetenganishwa na kiwiliwili chake. Nilimalizia kwa kusema kuwa muuaji si mimi bali ni huyo msichana ambaye kwa vyovyote vile si binadamu wa kawaida.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

                Askari huyo aliyakataa katukatu maelezo yangu na kuniambia kuwa mimi ni muongo na hayo maelezo yangu hayawezi yakanifikisha kokote, akasema jeshi la polisi haliamini ushirikina wala mazingazi. Akanitaka nieleze ukweli ili aone ni jinsi gani ataweza kunisaidia. Nilimwambia ukweli wangu ndiyo huo na sikuwa na maelezo mengine zaidi ya hayo.

                Afande huyo nilimuona akifunga faili lake na kuniambia nijiandae kwenda kuozea jela. Alichodai ni kwamba laiti kama ningeeleza ukweli basi angeweza kunisaidia.

                                     

                                            ************************



    Nikiwa rumande machozi yalizidi kunitiririka bila kukauka utadhani chemichemi za mto Naili, chemichemi ambazo hutiririka bila kukauka misimu yote; iwe masika ama kiangazi. Mifereji ya machozi ilikuwa inatiririka kutoka machoni ikipitia mashavuni mpaka kwenye kidevu.

                Harufu mbaya ya humo kwenye ‘gheto’ la watuhumiwa ilinifanya nipige chafya mara kwa mara. Nilijaribu kujikaza kiume nijizuie kulia lakini cha ajabu machozi  yalizidi kunitoka. Nilikuwa sijawahi kuswekwa rumande hata siku moja tangu kuumbwa kwa misingi ya dunia.

                Siku niliiona kama haiendi, masaa nayo yalikuwa kama yamesimama. Tangu saa tano za asubuhi baada ya kuruhusiwa hospitali niliingia humo,  mpaka muda huu ambao nilikuwa nauhisi ni kama saa tisa za jioni nilikuwa nimeiva sawasawa. Kwa muda mchache huu ambao nilikuwa nimekaa ndani nilikuwa  najiona kama nimekaa mwezi mzima.

                Mawazo kibao yalikuwa yametawala kichwa changu; niliwaza biashara zangu zitasimamiwa na nani, zaidi ya yote kilichokuwa kinaniumiza kichwa ni hatima ya kesi yangu iliyokuwa inanikabili, kesi ya mauaji.

                Ilipofika usiku nilizidi kuipata freshi, tena ni freshi ya mwaka. Sulubu iliyokuwemo kwenye ‘gheto’ la watuhumiwa haielezeki, yaani ni sulubu ya kufa mtu. Hapo ndiyo nilianza kuamini kuwa kweli rumande siyo kanisani ama msikitini.           

                Mbu walinishambulia si mchezo, nilijaribu kuwaua mmoja baada ya mwingine lakini wakawa hawaishi wala kupungua, suala la kupata usingizi walau dakika moja lilikuwa ni ndoto; tena ndoto yenyewe ni ndoto ya kuota mchana kweupe.

                Siyo mbu peke yao walionipa kero usiku huo, kunguni na viroboto nao walizidi kuleta adha katika mwili wangu.

    ‘Kama rumande ya polisi tu hali ndiyo hii, kule gerezani sasa hali ikowaje?’ Nilizidi kutafakari huku nikiwa ‘buzy’ kupambana na wadudu hao wasiyokuwa na chembe ya adabu hata kidogo.

                Niliwatumbua kwa hasira kila nilipowabahatisha wakigema damu yangu, lakini nao ndiyo kwanza walizidi kuongezeka utadhani walikuwa wakialikana.

    ‘Kwa mtindo kama huu kufikia asubuhi nitakuwa nimepoteza lita kadhaa za damu katika mwili wangu. Lakini chanzo cha mateso haya yote ni yule msichana  aliyemuua mpangaji wangu Kishoka.’ Niliendelea kunung’unika peke yangu. Manung’uniko ambayo hayakuzaa matunda ya wokovu wa kesi yangu hata kidogo.

                Hayawi hayawi mwisho yakawa, jogoo la kwanza nililisikia likiruka ‘bonanza’ kuashiria alfajiri inawadia. Mara nilisikia jogoo la pili na hatimaye la tatu. Kulionekana kupambazuka huku nikiumaliza usiku kwa kuutoboa, yaani namaanisha sikusinzia hata sekunde moja zaidi ya kupepesa macho pale ilipobidi.

                Ikawa asubuhi, siku ambayo sikujua itaishaje. Nilitegemea kupandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza ili kusomewa shauri lililokuwa linanikabiri. Lakini mambo yakawa sivyo.

    Mara mlango ulipofunguliwa niliwaona askari wawili waliokuwa wameshikilia bunduki kila mmoja wamesimama mlangoni kisha wakanitaka nitoke. Nilipotoka walinifunga pingu mikononi kisha wakanitanguliza mbele mpaka kwenye chumba kimoja katika kituo hicho kisha mahojiano yakaanza upya.



    Nikiwa rumande machozi yalizidi kunitiririka bila kukauka utadhani chemichemi za mto Naili, chemichemi ambazo hutiririka bila kukauka misimu yote; iwe masika ama kiangazi. Mifereji ya machozi ilikuwa inatiririka kutoka machoni ikipitia mashavuni mpaka kwenye kidevu.



    Mahojiano hayo yalichukua takribani masaa mawili na nusu, hata hivyo hapakuwa na kipya zaidi ya kurudia kuulizwa maswali niliyokuwa nimeulizwa hata kule hospitali. Pia katika mahohjiano hayo yaliambatana na vitisho lukuki vya kunitaka nikiri kuwa nilimuua Kishoka. Hata hivyo niliendelea kushikilia msimamo ya kuwa sijaua.

    “Wewe ni muuaji ila unajifanya ni mbishi, mbona ripoti ya postimotamu imeonyesha kuwa wewe ndiyo umeua?”

    “Hapana afande, mimi sijamuua Kishoka. Maelezo niliyoyatoa ndiyo yana ukweli wote.”

    “Mbona kwenye kisu kilichotumika kumuulia marehemu tumeona alama za vidole vyako, vilevile kwenye mwili wa marehemu alama za vidole vyako zipo?”

                Hilo nalo lilikuwa ni neno. Nilishtuka sana kusikia hivyo. Ukweli ni kwamba wakati naingia chumbani kwangu sikujaribu hata kukigusa kisu kilichotumika kumchinja Kishoka. Isitoshe hata mwili wake sikuugusa; sasa jambo la alama zangu za vidole kuonekana kwenye kisu hicho na kwenye mwili wa marehemu lilizidi kunichanganya. Wakati mwingine nilihisi huenda ni mitego tu ya makachero hao ili kumfanya mtu aropoke kama kweli katenda kitendo hicho.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

                “Hilo ni jambo geni kwangu, kile kisu sikuwahi hata kukigusa zaidi ya kukitumbulia macho. Hata mwili wa Kishoka sikuwahi kuugusa zaidi ya kuukodolea macho, sasa alama za vidole vyangu zilifikafikaje kwenye kisu na maiti ya Kishoka?”

    “Unatuuliza tena sisi! Naona wewe huna jipya ila ni ubishi tu unaokusumbua. Kesho faili lako tunalipeleka mahakamani kwani uchunguzi wetu sisi umeshakamilika.” Alimalizia kuongea askari huyo aliyekuwa amevaa nguo za kiraia kisha akaamuru nirudishwe rumande.

    Baada ya mahojiano hayo nilirudishwa tena rumande. Kilichokuwa kinasubiriwa pale ni kufika asubuhi nyingine kisha nipelekwe mahakamani kujibu shauri lililokuwa likinikabili.

     Nilisweka tena ndani na kuanza kuburudika na adha ya humo. Joto la kufa mtu nilikuwa linanisumbua kwa wakati huo. Hamkuwa na mkeka wala busati hivyo nililazimika kujilaza kwenye sakafu.

    Ilipofika jioni mbu walicharuka tena. Ikawa tafrani mtindo mmoja, usiombe mbu wa rumande ndugu msomaji, wanauma mpaka kwenye nyayo. Nahivi sikuwa na shuka wala blanketi, heheee, nakwambia nilikoma kuringa.

    Asubuhi nyingine ilifika japokuwa kwa shida sana. Mbavu zote zilikuwa zikiniuma kutokana na kulala kwenye sakafu usiku kucha. Mikononi na niguuni vilikuwa vimejitokeza vipele vingi kutokana na kutafunwa na mbu usiku mzima.

    Mara mlango wa selo ulifunguliwa kisha nikawaona askari watatu wakinitaka nitoke. Nami bila ubishi nilitoka. Nilipotoka tu hawakunichelewesha, wakanifunga pingu kisha wakanipeleka sehemu ambako kulikuwa na karandinga.

                Waliniamru nipande nami nikajitoma bila ya ubishi. Safari ya kuelekea mahakamani ilianza. Gari lilitoka mbio utadhani lipo katika mashindano, tulitumia takribani dakika kumi kufika mahakamani.



    Tulipofika mahakamani tuliwakuta watu kibao, baadhi yao niliwatambua, walikuwa ni wakazi wa mtaani kwetu. Nilianza kuhisi kuwa taarifa za kesi yangu zilikuwa  zimetapakaa sana huko mtaani.

                Kamera za mapaparazi nazo zilizidi kunisonga wakati naingia mahakamani. Nilijaribu kujifunika usoni ili nisipigwe picha lakini haikusaidia chochote. Nilipelekwa mpaka sehemu ya kukaa watuhumiwa wakati wanasubiri kupandishwa kizimbani.

                Mara ilisikika sauti... ‘koooort!’, sauti hiyo iliashiria kufunguliwa kwa mahakama. Watu wote walisimama ili kutoa heshima katika mahakama kama ilivovyo ada, muda mfupi waliketi na kesi zikaanza kusikilizwa.

                Kesi yangu ndiyo ilikuwa ya kwanza kutajwa. Nilipandishwa kwenye kizimba kisha nikaulizwa dini yangu. Nilipotaja dini yangu nikapewa kitabu kitakatifu cha dini husika na kuanza kuapishwa.

                Baada ya kuapishwa nilisomewa shitaka langu na kuambiwa sitakiwi kujibu chochote kwani mahakama hiyo ilikuwa haina uwezo wa kuendesha kesi ya mauaji. Baada ya hapo nilitolewa kizimbani na kurudishwa rumande nikasubiri jalada la kesi yangu lipelekwe mahakama kuu. Lakini rumande niliyopelekwa kwa mara hii haikuwa ile ya kule kituoni bali ni rumande ya magereza.

                Nilikaa mahabusu katika rumande hiyo kwa siku kadhaa nikisubiri tarehe ya kutajwa kwa kesi yangu kwa mara ya pili ambayo ilitakiwa kuhamishiwa mahakama kuu, mahakama ambayo huwa na uwezo wa kuendesha kesi za mauaji.

                Kawaida ya sheria za nchi yetu ni kwamba, mshtakiwa yeyote wa kesi ya mauaji hutafutiwa wakili na serikali kama hana uwezo wa kumlipa wakili. Wakili huyo humsaidia kusimamia kesi yake mpaka mwisho.

                Hicho ndicho kilichotokea kwenye kesi yangu hiyo. Nilitafutiwa wakili ambaye alikuwa ni wakili kutoka kwenye taasisi moja inayosimamia haki za binadamu.

                Nikiwa nasota kwenye rumande ya magereza nilipokuwa nimepelekwa baada ya kutoka mahakamani, wakili alinifuata na kuanza kujadiliana nami jinsi ya kunisaidia katika kunitetea kwenye kesi iliyokuwa ikinikabili.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

                “Hebu nieleze ukweli wako wote ili nijue ni jinsi gani nitakusaidia.” Alisikika wakili Jonas Mlyanyama kwa sauti iliyokuwa imejaa upole na yenye kubembeleza.

    “Kusema kweli sikuhusika kabisa na kifo cha Kishoka.”

    “Ilikuwaje, hebu niambia A mpaka Z bila kuficha kitu chochote.”

                Nilianza kumweleza tukio zima lilivyokuwa. Nikamweleza jinsi msichana wa kule ufukweni nilivyokutana naye na kuweka miadi ya kunitembelea kesho yake nyumbani kwangu.

                Sikuishia hapo, niliendelea kusimulia jinsi mauzauza yalivyoanza kujitokeza kwa mwanadada huyo pale alipokuja nyumbani na kukatalia getini baada ya kwenda kuambiwa na Kishoka apite ndani. Hata Kishoka alipokuja kuniambia kuwa mgeni huyo kakataa kuingia ndani bali ananitaka niende kulekule getini, nilienda lakini sikumkuta.

                Niliendelea kumhadithia kizaazaa hicho wakili Jonas Mlyanyama huku akiwa kanisikiliza kwa makini kabisa. Hatimaye nilimaliza maelezo yangu kwa kueleza jinsi nilivyoikuta maiti ya Kishoka ikiwa imelazwa juu ya kitanda changu.

                “Nimeambiwa kwamba alama za vidole vyako zilionekana kwenye mwili wa marehemu na kwenye kisu kilichotumika kumuua marehemu, ulikigusa kisu au ile maiti?”

    “Hapana wakili sikugusa chochote hapo, na ndiyo maana nakuambia kwamba kesi hii ipo kimazingara. Hata mimi nashangaa kuonekana alama za vidole vyangu.”

                Wakili Jonas Mlyanyama alivuta pumzi kisha akazishusha. Wakati natoa maelezo wakili huyo alikuwa ‘busy’ kuandika maelezo yangu kwenye kitabu alichokuwa amekuja nacho.

                Pamoja na kuwa ‘busy’ wakili huyo alionekana kuwa makini sana kunisikiliza kila nilichokuwa nakinena. Pia hakuacha kuhoji maswali pale ilipolazimu. Alikuwa na maswali mengi utadhani mgambo wa kata.

                Alinipa moyo na kuniambia kuwa kwa vile nilikuwa sijafanya kosa hilo kama nilivyokuwa nimeshtakiwa, Mungu angetusaidia na mwisho wa siku tungeibuka kidedea.



    Baada ya maongezi hayo yaliyochukua takribani saa moja wakili huyo aliondoka zake na kuniacha nikirudishwa rumande kusubiri siku yingine ya kusomwa kesi yangu.

                Niliendelea na msoto wa rumande. Kila siku mlo mmoja kwa siku huku chakula chenyewe kikiwa ni ugali wa dona na maharage yenye uozo. Maisha hayo nilikuwa sijawahi kuishi hivyo ilikuwa ni vigumu sana kuyazoea.

                Hata hivyo sikuwa na jinsi, nililazimika kujikaza kisabuni huku nikisubiri kudura za Wahidi ziniokoe katika hilo janga. Ilikuwa inauma sana hasa pale nilipofikiria jinsi uhusiano wangu ulivyokuwa na mpangaji wangu Kishoka ambaye nilikuwa natuhumiwa kumuua.

                Tuliisha kwa ushirikiano mkubwa kama ndugu wa damu ilhali tulikuwa tumekutana ukubwani tu huku kila mmoja akiwa na meno thelathini na mbili; yaani akiwa mtu mzima.

                Sikuhusika na kifo chake, lakini nilikuwa nikishtumiwa ya kwamba nilimuua. Kwa mtindo huo kwa nini sasa roho isiniume? Ilikuwa ni zaidi ya uchungu.

                Siku ya kupandishwa kizimbani kwa mara nyingine tena iliwadia. Asubuhi asubuhi mimi na mahabusu kadhaa tulisweka kwenye karandinga la askari magereza huku ulinzi ukiwa umeimarishwa. Safari ya kuelekea mahakamani ilianza.

                Mara baada ya kufikishwa mahakamani tulishushwa huku tukilindwa kwa silaha za moto, siraha nzito nzito za kivita. Mapaparazi nao walikuwepo kama kawaida yao, wakaanza kutusonga ili wapate picha za kwenda kutuuzisha sura runingani na magazetini.

                Licha ya kukaripiwa na askari magereza waliokuwa wametutanguliza, mapaparazi hao walizidi kukomaa ‘kutufotoa’ na kamera zao. Tukaingia mpaka mahakamani tayari kabisa kwa kuanza kusomewa mashtaka yetu kila mmoja kwa awamu.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

                Mimi ndiyo nilianzia kupandishwa kwenye jukwaa la watuhumiwa kisha nikaapishwa kama zilivyo taratibu za mahakama kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

                Baada ya kuapishwa kizimbani kesi yangu ilitajwa. Hata hivyo jaji Aneth Mwalukwa aliiahirisha tena kesi ili kusubiri jalada la kesi kutoka kwa mkurugenzi wa mashtaka. Kesi yangu ilipelekwa mbele kwa muda wa majuma matatu.

    Niliteremshwa kizimbani na kurudishwa kwenye sello ya hapo mahakamani kusubiri mahabusu wengine wamalize kusomewa mashtaka yao kisha turudishwe rumande.

                Baada ya mahabusu wengine kumaliza kusomewa mashtaka yao tulirudishwa rumande ya magereza huku gari tulilokuwa tumepakizwa likikimbia kwa kasi.



    Tukiwa njiani moyo wangu ulizidi kuumia kwa kupotezewa muda kwa kesi ambayo sijashiriki wala kuifanya. Akili yangu yote ilikuwa kwenye hatima ya hiyo kesi. Mpaka tunafika kwenye ngome ya gereza nilikuwa nimezama kwenye mawazo mazito. Nilighutushwa na sauti ya mlango wa karandinga ulipokuwa ukifunguliwa ili tushuke. Tulishuka na kuswekwa kwenye gheto la watuhumiwa kuendelea na msoto.

                Wiki mbili zilikatika nikiwa rumande, niliziona ni nyingi sana. Hali yangu kiafya ilizidi kuwa mgogoro kila siku iliyoenda kwa Mungu. Kudhoofu huko hakukutokana na ugonjwa bali mawazo, aiseeeh! Acha kabisa kitu mawazo, tena mawazo ya kesi ya mauaji ambayo hukushiriki hata kuitenda. Kila wakati nilijikuta nikichoka kabisa.

                Wakili wangu alinitembelea tena siku moja kabla ya siku ya kwenda mahakamani. Tuliongea mawili matatu huku akinipa moyo kwa kuniambia nitashinda tu na haki itatendeka kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu.

                “Halafu mbona umekonda sana?” Lilikuwa ni swali la Jonas Mlyanyama baada ya kuongea mambo yetu muhimu yaliyokuwa yanahusiana na hiyo kesi yangu.

    “Mawazo kaka, unajua kesi hii inanipa wakati mgumu sana katika kichwa changu.” Nami nilimjibu.

    “Acha kuwaza sana ndugu yangu, kwanza hii kesi mimi hainipi presha hata kidogo. Hapo tutashinda tu.” Alisikika wakili Jonas akiniambia.

                Maneno yake hayo niliyaona kama ya kunifariji tu ili niache kuwaza, lakini hatari iliyokuwa mbele yangu ilikuwa kubwa mno. Piga ua kifo cha kunyongwa kilikuwa kinaninyemelea. Suala la kuokoka lilikuwa adimu kama kaburi la baniani.

                “Najaribu kujikaza lakini najikuta nikiwaza tu, kila nikikaa mawazo yananijia, hata usingizi nashindwa kupata, chakula nacho hakipandi hata kama kwa kukilazimisha.”

    “Usijali ndugu yangu, amini nakwambia Mungu yupo na atakusaidia.” Ilikuwa ni sentensi ya mwisho kutoka kinywani kwa wakili Jonas Mlyanyama.

                Bila ya muda kupotea tayari nilikuwa mbele ya askari aliyekuwa akilalama kuwa tumetumia muda mwingi kwa kupiga soga kama tumekutana sokoni.

                Alinipeleka moja kwa moja kwenye ‘gheto’ la watuhumiwa lililokuwepo gerezani hapo. Nikawakuta mahabusu wenzangu ambao tulikuwa tumeshaanza kuzoeana.

    Tuliendelea kupiga stori za hapa na pale. Hata hivyo mimi mawazo yangu yote hayakuwa pale hata kidogo. Nilikuwa nikiwaza mambo lukuki kwa awamu, mara namuwaza Kishoka, mara nawaza kesi yangu itakavyokuwa.

    Wakati mwingine taswira ya msichana aliyenisababishia matatizo hayo ilinijia kichwani mwangu; msichana ambaye mimi ndiyo nilikuwa nikiamini kwa asilimia mia tano kuwa ndiye alihusika na kifo cha Kishoka.

                Hali ya rumande ndugu yangu wee acha tu. Hata kama kungekuwa na masofa pamoja na runinga mimi nisingeweza kuyafurahia kwani uhuru hamna.

                Ilipofika mida ya jioni vijana wawili waliletwa kwenye ‘sello’ tuliyokuwemo. Mahabusu mmoja akaninong’oneza kuwa vijana hao walikuwa wameifanya rumande kuwa ni maskani yao.

                Kukatisha mwezi hawajaswekwa humo ilikuwa ni vigumu kwao. Kila waliporudi uraiani baada ya kumaliza kutumikia adhabu za vifungo walizokuwa wakipewa, vijana hao walifanya makosa tena na kurudishwa rumande.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

                Niliwashangaa sana baada ya kuambiwa kuwa walikuwa na kasumba hiyo. Sehemu mbaya kama ile wao walikuwa wakiifurahia! Ama kweli kila shetani na mbuyu wake. Nilipojaribu kuuliza kipi hasa ambacho huwafanya waione rumande kama maskani niliambiwa kuwa ni ugumu wa maisha.

                Kumbe huo ndiyo ulikuwa ni mfumo wao wa maisha, si unajua tena huko kula ni bure na kulala ni bure! Kwao siku zilisonga kwa mtindo ule.

                Hata hivyo mimi niliona ni ujinga na umbumbumbu uliokuwa ukiwasumbua. Mbona kuna shughuli kibao huko uraiani ambazo wangefanya zingewapatia riziki ya halali.

                Vijana hao niliwafananisha na mazuzu ambao mishipa ya fikra ilishakatika kichwani mwao. Rumande siyo sehemu ya kukimbilia kama una akili yako timamu.



                                        *************************



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog