Search This Blog

Thursday, 2 June 2022

MIRATHI YA KAKA - 3

 







    Simulizi : Mirathi Ya Kaka

    Sehemu Ya Tatu (3)



    ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA....

    Wakili wa serikali bwana Charles Ngonyani alimtazama hakimu na kumwambia,

    “Nimemaliza!” aliongea na kwenda kuketi.

    SASA ENDELEA.......         

                Ilifika zamu ya wakili wa upande wa utetezi kumuhoji shahidi aliyekuwa kizimbani. Wakili huyo bwana Jonas Mlyanyama alisimama na kusogea karibu na kizimba cha shahidi wa upande wa mashitaka sajenti Bakari Mlongo.

                “Umesema mlipoingia chumbani mlimkuta mtuhumiwa anazunguka zunguka huku kisu kikiwa kinaambaa ambaa sakafuni, si ndiyo?” Mlyanyama alimhoji shahidi huyo.

    “Ndiyo!” alijibu na kumsikiliza wakili wangu aendeleee kuongea

    “Nikiiambia mahakama tukufu ya kwamba mteja wangu alikuwa katika kustaajabu baada ya kulikuta tukio hilo limefanyika katika chumba chake nitakuwa nakosea?”

    “Ndiyo utakuwa unakosea kwa vile alama za vidole zilionekana kwa mtuhumiwa baada ya kuchukua vipimo, yote hayo yatakuja kuelezewa na mtaalamu wetu wa mambo ya picha na alama za vidole ambaye tulikuwa tumeambatana  naye siku hiyo.”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

                “Na ikiwa labda mtuhumiwa alikishika kisu pamoja na mwili wa marehemu wakati tukio limeshafanyika ikiwa kwa kutokujua au kutokana na kuchanganyikiwa na hali ya tukio lilivyokuwa?”

    “Kwenye vipimo hatukuona alama zingine zaidi ya alama za mtuhumiwa tu.”

                “Huyo aliyewapigia simu kituoni kuwapasha taarifa za tukio alikuja kituoni?”

    “Hapana!”

    “Mlichukua namba yake ya simu baada ya kumaliza kuongea naye?”

    “Hatukuweza kuchukua namba yake ya simu kwa sababu alipiga kwenye simu ya mezani.”

                “Mpaka jalada la  upelelezi wa kesi hii linakamilika mtu huyo aliwahi kufika kituoni japo mara moja nanyi mkapata kumfanyia mahojiano juu ya tukio hilo?” Wakili Jonas Mlyanyama alimtwanga swali hilo tena shahidi wa upande wa mashitaka.

    “Hapana!”

    “Sasa mimi naiambia mahakama kuwa mteja wangu hakuua bali mwanamke huyo ndiye mbaya na huenda ndiye aliyeua au anafahamu mwanzo mpaka mwisho juu ya mauaji ya Kishoka.”

    “Siyo hivyo, mtuhumiwa ni yule pale kizimbani kwa sababu hata alama zake zilionekana kwenye mwili wa marehemu na kwenye kisu kinachosadikika kutumika kumchinja marehemu.”

    “Sasa kwa nini mtoa taarifa wa awali asijitokeze kituoni kutoa maelezo na kuwa tayari kuja kutoa ushahidi mbele ya mahakama?”

    “Kwa kweli hilo siwezi kujua ni kwa nini hajaonekana kituoni.”

    “Basi kubaliana na mimi ya kuwa yule ndiyo mhalifu.”

                Sajenti Bakari Mlongo alionekana kuwa na kigugumizi hatimaye akaganda mithili ya cd kongwe iliyochakaa. Wakili wangu bwana Jonas Mlyanyama alimwambia hakimu hana la zaidi la kumuuliza shahidi huyo.



    Hatimaye shahidi wa pili kutoa ushahidi aliwadia. Shahidi aliyefuatia alikuwa ni Sajenti Majaliwa Mbogo, askari ambaye yupo katika kitengo cha kupima alama za vidole ambaye pia alikuwa ameambatana na kikosi kilichokuja kwangu siku ya tukio.

                Sajenti Mbogo baada ya kuapishwa alikumbushwa saa na siku ya tukio na mwendesha mashtaka bwana Charles Ngonyani.

                Sajenti Mbogo alieleza kuwa siku hiyo alikuwa kwenye kituo chake cha kazi kama ilivyo ada. Ndipo alipopata wito kutoka kwa mkuu wa kituo hicho na kuambiwa kuna mauaji yametokea kwenye nyumba yangu. 

    “Tueleze ilikuwaje baada ya kuambiwa hivyo na mkuu wako wa kituo.”

    “Agizo lililokuwa limetolewa pale ni kwenda kunako eneo la tukio, na ndicho kilichofuata.”

    “Mlipofika eneo la tukio mlikuta nini?” Mwendesha mashitaka aliendelea kuuliza maswali ya kuweza kumuongoza shahidi huyo aendelee kutoa ushahidi.

                Maelezo ya Sajenti Mbogo hayakutofautiana sana na yale ya shahidi aliyekuwa ametangulia. Mwisho shahidi huyo alieleza jinsi matokeo ya vipimo vya alama za vidole yalivyonihusisha kuwa nilimuua Kishoka.

                Hatimaye mwendesha mashitaka alimaliza kutoa muongozo kwa shahidi huyo kisha akamwambia mheshimiwa Jaji kuwa amemaliza na akaenda kuketi.

                Wakili wangu aliinuka tena na kusogea kwenye kizimba ambacho shahidi huyo alikuwa amesimama. Alipofika akaanza kumuuliza maswali kama ilivyoada.

    “Natumaini wewe upo kwenye kitengo cha kupiga picha na kupima alama za vidole kwa muda mrefu katika jeshi la polisi?”

    “ Ndiyo.”

    “Kama mimi nikishika kitu kisha mkaja kupima alama zangu za vidole si zitaonekana?”

    “Ndiyo.”

    “Nikiiambia mahakama kwamba mteja wangu alishika mwili wa marehemu pamoja na kisu baada ya kukuta tukio limeshatokea chumbani kwake kwa kutokujua madhara yake ama kutokana na kuchanganyikiwa unaweza ukakubaliana na mimi?”

    “Hapana sitakubaliana na wewe.”

    “Kwa nini?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kwa sababu hatukuona alama za vidole vya mtu mwingine zaidi.”

    “Mimi nitaiambia mahakama tukufu kwamba mteja wangu alishika sehemu hiyo hiyo aliyokuwa ameshika muuaji na ndiyo maana hazikuonekana alama za mtu mwingine.?”

    “Haiwezekani, siyo rahisi kumshika mtu mpaka kumuua usimguse sehemu kubwa ya mwili. Ingekuwa mtuhumiwa aliyepo kizimbani hajafanya hilo tukio basi alama za vidole za mtu wa kwanza zingetapakaa mwili mzima wa marehemu.”

    “Je, mtu kama kavaa ‘groves’ mikononi alama zake huonekana akishika sehemu?”

    “Hapana.”

    “Basi muuaji alikuwa kavaa groves wakati anaua na ndo maana alama za vidole hazikuonekana!”

    “Hapana, muuaji ni yule pale kizimbani maana ndiyo tulimkuta eneo la tukio.”

    “Shahidi aliyekutangulia amesema kwamba mtu aliyetoa taarifa za awali juu ya kifo cha kishoka hakujitokeza hata kidogo zaidi ya kupiga simu tu kituoni, unaweza kuniambia kwa nini hakutaka kujitokeza?”

    “Kwa kweli siwezi kujua.”

    “Nikikwambia kuwa hajajitokeza kwa kuwa alikuwa ni mharifu na huenda aliogopa kuja kuumbuka utakubaliana na mimi?”

    “Hapo siwezi kusema chochote kwa sababu sijui sababu zilizomfanya asijitokeze kituoni.”

    “Basi huyo akipatikana na kufanyia mahojiano kikamilifu huenda akawa na maelezo ya kutosha kuwasaidia katika upelelezi wa kesi hii na huenda mtambaini muuaji halali wa Kishoka na siyo mteja wangu.” Aliunguruma bwana Mlyanyama.

                Mpaka hapo Sajenti Majaliwa Mbogo hakuwa na la kuongea. Wakili wangu alimtazama jaji na kumwambia kamaliza maswali ya kumuuliza shahidi huyo. Baada ya kusema hivyo akaenda kuketi.

                Jaji aliiahirisha kesi na kutaja tarehe nyingine ambayo ingeendelea kusikilizwa. Nilitolewa kizimbani na kupelekwa kwenye karandinga la magereza tayari kabisa kwa kurudishwa mahabusu.



    Ilikuwa ni kesi iliyonipa wakati mgumu sana kwa kipindi chote nilichokuwa mahabusu nikisubiri hatima yake. Kila wakati nilikuwa siishi kuwa na wasiwasi mithili ya mbuzi wa shughuli.

                Wasiwasi pamoja na kuwaza huko kulizidi kuifanya afya yangu izidi kuwa mgogoro zaidi ya vile ilivyokuwa awali. Niliiona kesi inapelekwa polepole sana, nikawa natamani bora nihukumiwe ili nijue moja, kama kusubiri kunyongwa ama kuponea kwenye wokovu wa ngamia kupenya kwenye tundu la sindano.

                Pamoja na maneno ya wakili wangu bwana Jonas Mlyanyama ya kunitia moyo na kunihakikishia kuibuka kidedea katika kesi hiyo, bado nilikuwa naona kama ananikebehi na kunipa faraja za kijinga kwa vile niliamini kabisa kuwa hata yeye alikuwa anauona ugumu wa kesi yangu ulivyokuwa.

                Kibaya zaidi sikuwa hata na shahidi ambaye angesimama kizimbani na kujaribu kunitetea. Kesi yenyewe ilikuwa imejaa utata mtupu. Hata wewe mpenzi msomaji uliona wapi alama za vidole zionekane kwenye kitu ambacho hukuwahi hata kukishika? Huo ni utata, kama siyo kubambikiwa basi ni kiini macho.

                Tarehe ya kusikilizwa tena kesi yangu iliwadia. Siku hiyo tena upande wa mashitaka ulitakiwa kupeleka mashahidi wake wawili. Shahidi wa kwanza kupanda kizimbani kutoa ushahidi alikuwa ni Daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu Kishoka.

                Akiwa kizimbani huku akiongozwa na mwendesha mashitaka, daktari huyo alieleza jinsi alivyoupokea mwili wa marehemu Kishoka na kuufanyia uchunguzi. Baada ya hapo alitoa maelezo ya ripoti ya postimotam kabla ya kuwasilisha nakala ya ripoti hiyo kwa Jaji.

                Wakili wangu hakuwa na maswali mengi sana ya kumuuliza shahidi huyu hivyo hakutumia muda mrefu sana kumhoji alipokuwa kwenye kizimba cha kutolea ushahidi.

                Ripoti ya daktari huyo ilikiri kuwa kweli Kishoka aliuawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali mpaka akapoteza uhai wake.

                Baada ya shahidi huyo kutoa ushahidi, upande wa mashitaka ulitakiwa kupeleka shahidi mwingine. Shahidi aliyekuwa ameandaliwa ni mmoja wa askari waliokuwa wamekuja nyumbani kwangu kuja kunikamata baada ya kupewa taarifa za kifo cha Kishoka.

                Nilimuona mwendesha mashtaka ambaye ni wakili wa serikali akisimama na kumwambia jaji kuwa shahidi aliyetakiwa kupanda kizimbani haonekani na huku alikuwepo wakati mahakama inaanza.

                “Hata hivyo kuna shahidi mwingine kajitokeza ambaye ni muhimu sana katika kesi hii. Mtu mwenyewe ni yule mwanamke aliyetoa taarifa za awali kituo cha polisi kuhusiana na kifo cha Kishoka.” Nilimsikia mwendesha mashtaka akimwambia jaji.

                Moyo ulinilipuka puu baada ya kusikia kauli hiyo. Tumbo langu likachemka ghafla huku maswali mia mia nikijiuliza ya kuwa huyo mtu aliyetoa taarifa kituoni akinisingizia kuua ni nani.

                Hata hivyo kwa upande mwingine nilifurahi ili nimuone mtu huyo mwenye moyo wa kinyama na roho ya kishetani kwa kunisakizia kwesi ya mauaji ilhali sikuua.

                Baada ya jaji kuruhusu shahidi huyo apande kizimbani, nilimuona dada mmoja akiinuka na kuanza kutembea mwendo wa maringo kuelekea kwenye kizimba cha kutolea ushahidi.

                Kitendo cha kumuona mwanadada huyo kilinifanya nianze kuhisi kupumua kwa shida huku mwili wangu ukianza kuishiwa nguvu. Pumzi zilizidi kubana, ghafla nilijiona nikianguka mzima mzima huku macho yangu yakipoteza upeo wa kuona. Kabla sijafika chini niliacha kujitambua na kupoteza fahamu ghafla.



     “Brighton, unajisikiaje?” Ilikuwa ni sauti ya wakili wangu bwana Jonas Mlyanyama aliyekuwa kaketi pembeni mwa kitanda nilichokuwa nimelala.

    “Mh! Wakili, hapa nipo wapi?” Nilijikuta nikiuliza swali na siyo kutoa jibu baada ya kumfahamu mtu niliyekuwa naongea naye.

    “Hapa upo kwenye hospitali ya magereza, ulianguka ghafla leo asubuhi wakati ukiwa kizimbani.” Alinijibu bwana Mlyanyama.

                Baada ya kuniambia hivyo kumbukumbu zilinijia kwa kinagaubaga. Hapo ndiyo nilikumbuka tukio zima lilivyokuwa, hata hivyo nikapata shauku kubwa ya kumuuliza wakili wangu jinsi mambo yalivyokuwa kule mahakamani.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

                Wakati mimi ninashauku hiyo, yeye naye alikuwa na shauku ya kujua ni kitu gani kilinifanya nipoteze fahamu nilipokuwa pale kizimbani. Kila mmoja akawa na hamu ya kusikia maelezo kutoka kwa mwenzake.

                Nilishusha pumzi ndeefu kisha nikamwambia bwana Mlyanyama,

    “hivi nilianguka mpaka chini kabisa?”

    “Ndiyo! Kwani ilikuwaje?”

    “Kaka, ni mambo ya ajabu niliyoyaona mle mahakamani!”

    “Mambo gani hayo?” Aliniuliza wakili huyo kwa upole kabisa huku akikaa mkao wa kula kisikia kilichonifanya nianguke na kuzua gumzo mahakamani hapo.

                Ndipo nilipoamua kumpasulia kile nichokuwa nimekiona mahakamani.

    “Yule msichana aliyeinuka kutoa ushahidi ndiyo muuaji kaka.” Nilimwambia wakili wangu kwa sauti ya kunong’ona.

    “Muuaji ki vipi?” Naye alihoji kwani somo lilikuwa bado halijamwingia akilini.

    “Yule ndiyo msichana mwenye mauzauza niliyekusimulia.”

    “Yule uliyeonana naye ufukweni kisha kesho yake akawa anagonga geti lakini mkienda kumfungulia mnakosa?” Alizidi kuhoji wakili Jonas Mlyanyama.

    “Haswaah! Wala hjakosea kaka. Sasa kitendo cha kumuona msichana huyo moyo wangu ulishtuka ghafla mpaka nikaanza kujihisi napata shida kupumua. Baada ya hapo sikujitambua tena.”

                Mpaka hapo wakili wangu akawa ameshakifahamu kilichonifanya nizirai huku nikiwa kwenye kizimba. Nilipotupia jicho kwa wakili Mlyanyama nilimuona kajishika tama huku akionekana kuwaza kwa kina, baada ya hapo akashusha pumzi ndeefu iliyoashiria mtu kuchoka ama kukata tamaa.

                “Kwa kweli hii kesi inautata sana. Tangu niwe wakili sijawahi kukutana na kesi yenye kizaazaa kiasi hiki. Pamoja na kukaa katika kazi hii kwa miaka zaidi ya kumi na mitano hii ndiyo mala ya kwanza kukumbana na kesi ngumu kama hii. Ama kweli hii ni kali, tena ni kali ya karne.” Alisikika bwana Jonas Mlyanyama.

    “Ehe, baada ya kuanguka nini kiliendelea?” Nikazidi kudodosa.

    “Kesi yako imeahirishwa, itapangwa tena pale afya yako itakapoimarika.”

    “Na yule mwanamke alielekea wapi baada ya hapo?”

    “Hata sikumfuatilia.” Alinijibu na kuonekana tena kuzama kwenye lindi la mawazo.

    “ Sasa subiri nikaandae hoja za kisheria za kuja kumkabili siku ya kusikilizwa tena kesi yako, labda asije.”

    “Yule ni mchawi kaka sidhani kama utamuweza.”

    “Pamoja na uchawi wake hapa kagonga mwamba.” Aliongea Mlyanyama huku akijipigapiga kifuani kuonyesha kujigamba fulani hivi.

                “Yangu macho na masikio siku hiyo, lakini mimi nimeshamnyanyulia mikono huyo ibilisi. Nashangaa sijui kwa nini kaniandama sana na kunisababishia ndege mbaya katia maisha yangu, kanipotezea dira ya maisha kabisa, isitoshe hata hatima yangu haijulikani.” Nilijikuta nikiongea kwa uchungu huku nikionyesha kukata tamaa kwa hali zote.



     “Tatizo lako wewe ni mwepesi mno wa kukata tamaa. Hebu hakikisha unapambana mpaka dakika ya mwisho.”

    “Nitapambana vipi kaka wakati hali ninavyoiona inazidi kuelekea kubaya tu. Hebu jiulize hizo alama za vidole vyangu zimeonekanaje kwenye mwili wa marehemu na kwenye kisu wakati sikuwahi hata kugusa?”

    “Huenda ulishika bila kijielewa kutokana na kuchanganyikiwa na tukio.”

    “Hakuna kitu kama hicho kaka, mimi hata nichanganyikiwe vipi lakini huwa najielewa.”

    “Basi yote hayo tumwachie Mungu, yeye ndiye atakayeamua kuwa tushindwe au tushinde hii kesi.”

    “Mimi nahisi hata Mungu kashanipa kisogo, haya siyo matatizo ya kwanza kwangu, walianza wazazi wangu wakafariki, kipenzi changu Ana naye akanitoka kimzahamzaha. Haikuishia hapo tu, kaka James ambaye alikuwa ndiyo nguzo yangu ya pekee iliyokuwa imebakia, naye akafariki dunia, tena kifo cha ghafla ghafla tu.” Nilijikuta nikimshtakia Mungu kwa wakili huku machozi yakianza kunibubujika kwenye mifereji ya mashavu yangu.

                Ndipo mlango ulipofunguliwa kisha askari magereza akaingia na kumtaka wakili aondoke kwani muda wa kuendelea kuongea na mimi ulikuwa umefikia kikomo.

                Wakili aliniaga na kuniambia atakuja kunipa taarifa pale tarehe ya kesi yangu itakapopangwa. Aliondoka na kuniacha nikifutafuta machozi ambayo yalikuwa yameshaanza kukolea kutokana na kuyaamsha machungu yaliyokuwa yamejilaza moyoni; machungu ya kuondokewa na watu wangu muhimu katika hii dunia ambao ni wazazi wangu, kaka James na kipenzi changu Anna.

                Mawazo juu ya msichana huyo ambaye nilikuwa nimembatiza jina la Ibilisi yalianza kuzunguka kunako kichwa changu. Hata hivyo sikuweza kupata jibu ni kwa nini msichana huyo alikuwa ameniandama kiasi kile.

                Niliendelea na maisha ya gerezani ingawa nilikuwa ni mahabusu. Mpaka muda huo nilikuwa bado sijayazoea kabisa maisha ya huko, ilikuwa ni ngumu sana kwangu kuyazoea maisha ya huko.

    Siku moja kabla ya kesi yangu kuendelea wakili alikuja kunipa taarifa. Hata hivyo alipokuja aliniambia habari nyingine ambayo ilizidi kunichanganya zaidi.

    Alisema kuwa siku aliyotoka kuongea na mimi kwenye hospitali ya magereza alikutana na msichana aliyekuwa akitusumbua katika kesi hiyo. Msichana aliyekuwa amenisingizika kuwa nimeua wakati sijaua.



    “Nilikutana naye sokoni niliposimama kununua matunda, ndipo akaniita wakati naingia kwenye gari niondoke zangu sokoni hapo. Kusema kweli nilikuwa sijamfahamu ila alipofika kwangu alijitambulisha.” Alieleza wakili Mlyanyama.

    “Akakuambia vipi?” Nikamuuliza huku nikikaa makini kusikia alichomwambia wakili wangu.

    “Eti kanionya niachane na kesi yako kwa sababu hainihusu, akadai vinginevyo nitapata matatizo makubwa.”

                Taarifa hiyo ilininyong’onyeza na kunifanya niishiwe nguvu.

    “Hivyi huyu mwanamke ananitafuta nini mimi?” Nilimaka kwa machungu.

    “Hata hivyo nilimwambia sitishiki na nikamtaka ajipange kujibu maswali yangu yangu siku atakayosimama kutoa ushahidi.”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Lakini yule ni mtu hatari sana kaka, bora uachane tu na kesi yangu nisije nikakusababishia matatizo.” Nilimwambia wakili Mlyanyama.

    “Hapana, hayo ni maneno ya vitisho tu, ameona hana hoja za kunikabili na huenda kashaambiwa jinsi ninavyowakaba maswali mashahidi wengini au huwa anakuja kinyemela na kashashuhudia.”

    “Kaka mimi nimekuambia, yule msichana ni mchawi, hii kesi achana nayo tu wanihukumu yaishe.” Nilimwambia wakili huyo.

                Hata hivyo wakili huyo alikataa katakata kuiachia njiani kesi yangu. Aliapa kuwa na mimi bege kwa bega mpaka pale ambapo kingeeleweka. Alikuwa na kiu ya haki kwangu mithili ya mzee Toboa katika Kiu ya Haki.

                Tuliagana na kuachana huku tukisubiri kesho yake ifike ili nipande tena kizimbani kuendelea na kesi yangu. Nilizidi kupata wasiwasi juu ya hiyo kesi yangu. Kama mpaka yule wakili alikuwa kapewa vitisho na yule msichana, niliwaza bila kupata jibu ni kipi hasa alichokuwa akikitafuta msichana yule kutoka kwangu.

                Kwa kweli nilikuwa na mtihani, tena mzito. Nilitamani nikutane naye uso kwa macho  kisha nimuulize kinagaubaga ni nini hasa nilichokuwa nimemkosea ama ni kipi alichokuwa anahitaji kutoka kwangu.

                Kesho yake asubuhi tulisombwa tena na karandinga la magereza kuelekea mahakamani. Tulipofika mahakamani mimi nilipelekwa moja kwa moja mpaka ndani kwani kesi yangu ndiyo ilikuwa inaanzia kusikilizwa.

                Jaji alipoingia watu wote walisimama wakati sauti ya “kooort” iliposikika. Baada ya kutoa heshima ya mahakama watu wote waliketi, kesi yangu ikaendelea.

                Upande wa mashtaka uliendelea kuleta mashahidi wake ambapo baadhi ya polisi waliokuwa wamekuja kunikamata nyumbani siku ya tukio walisimama mmoja baada ya mwingine kutoa ushahidi.

                Wakili wangu hakuwa na maswali mengi sana ya kuwahoji. Yeye alichodai ni kwamba anamsubiri kwa hamu shahidi ambaye alitoa taarifa za tukio hilo kwenye kituo cha polisi. Shahidi huyo hakuwa mwingine bali ni yuleyule msichana mwenye kiinimacho.

                Baada ya polisi hao kuisha wote kutoa ushahidi, msichana huyo ambaye nilikuwa simjui hata jina aliinuka na kwenda kwenye kizimba cha upande wa pili kutoa ushahidi wake.

                Kama ilivyo ada, mwendesha mashtaka alimuongoza kutoa maelezo hatua kwa hatua.

    “Mimi naitwa Sharifa Abdul.” Alitaja jina lake baada ya kuulizwa na mwendesha mashtaka.

    “Sharifa, hebu ieleze mahakama ulikuwa wapi mnamo tarehe ishirini na moja mwezi wa kumi na moja mwaka jana muda wa jioni?” Ilikuwa ni sauti ya mwendesha mashtaka bwana Charles Ngonyani.

    “Nakumbuka siku hiyo nilikuwa nyumbani kwangu Majengo mapya, ndipo nilipoamua kwenda kumtembelea kaka yangu ambaye ni marehemu Kishoka.”

    “Endelea..,”

    “Nilipofika alipokuwa akiishi kaka yangu huyo nilikuta milango ipo wazi.”

    “Huyo kaka yako alikuwa akiishi wapi?” Mwendesha mashtaka aliuliza.

    “Alikuwa akiishi mtaa wa Tumaini.”

    “Alikuwa akiishi na nani?”

    “Alikuwa amepanga na alikuwa akiishi na mmiliki wa nyumba hiyo.”

    “Ehe, ulipokuta mlango upo wazi ulichukua uamuzi gani?”

    “Kabla sijagonga nilisikia sauti ya kilio na makelele mle ndani ambapo sauti ya mtu aliyekuwa akitoa kilio niliitambua.”

    “Ilikuwa ni sauti ya nani?”

    “Ilikuwa ni sauti ya kaka yangu Kishoka.”

    “Uliposikia hivyo ulifanyaje?”

    “Niliamua kuingia mpaka sebuleni, hata hivyo makelele hayo yalikuwa yakitokea chumbani.”

    “Chumba hicho kilikuwa ni cha nani?”

    “Kilikuwa ni cha mmiliki wa nyumba hiyo.”

    “Baada ya hapo ulifanyaje?”

    “Baada ya kuuona hata mlango wa chumbani haujafungwa, nilianza kwenda kwa tahadhari kubwa kuchungulia kilichokuwa kinaendelea ndani ya chumba hicho.”

                “Uliweza kuchungulia humo ndani?”

    “Ndiyo!”

    “Ulipochungulia uliona nini?”

    “Nilichokiona sikuamini kwa macho yangu. Nilimuona kijana mwenye nyumba akimchinja Kishoka kama mbuzi wa sherehe achinjwavyo huku kamfunga kamba miguuni na mikononi.”

    “Ulipoona hivyo uliamua nini?”

    “Kwanza niliongopa kuongea chochote kwa kuhofia usalama wangu. Kwa bahati nzuri nilikuwa na kamera kwenye mkoba wangu, nikaitoa na kuanza kupiga picha.”

    “Baada ya hapo afanyaje?”

    “Nilitoka na kuondoka mbio kurudi nyumbani, wakati nikiwa njiani nilipiga simu kituoni na kutoa taarifa hizo.”

    “Hizo picha ulizozipiga siku ya tukio unazo?”

    “Ndiyo zimo kwenye kamera yangu hii.” Aliongea Sharifa huku akiionyesha mahakama kamera ndogo ya digitali.

    “Huyo mtu aliyefanya hayo mauaji ukimuona unaweza ukamfahamu?”

    “Bila shaka!”

    “Hebu tuonyeshe kama mtu huyo yumo humu ndani ya mahakama!”

    “Ni yule pale kwenye kizimba.” Aliongea msichana huyo huku akinisonta.



    Mwendesha mashtaka aliichukua kamera na kuipeleka kwa jaji kisha akasema amemaliza muongozo wake kwa shahidi.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

                Akili yangu ilizidi kuchanganyikiwa. Ushahidi wa picha uliokuwa umetolewa na msichana huyo ulizidi kuivuruga akili yangu. Japokuwa nilikuwa bado sijaziona hizo picha lakini niliamini kabisa kuwa msichana huyo hawezi kupeleka kitu ambacho siyo cha kweli mbele ya mahakama.

    “Lazima kweli kuna picha zangu kwenye kamera hiyo, lakini sasa hizo picha kazitoa wapi wakati mimi sikumuua Kishoka?” Niliwaza na kuwazua bila kupata jibu.

    Wakati nikiwaza hivyo wakili wangu aliinuka na kuomba auone ushahidi wa vielelezo vya picha uliokuwa umetolewa na shahidi huyo. Alipoletewa kamera hiyo alibaini kuwa picha hizo zilikuwa ni zangu kweli.

    Naye alizidi kuchanganyikiwa. Akaomba nionyeshwe na mimi kisha akaruhusiwa. Nilipoonyeshwa nilizidi kupigwa na butwaa baada ya kuona picha zikionyesha namchinja Kishoka. Sikuamini kwa macho yangu.

    Zilikuwa ni picha kama saba hivi ambazo zilikuwa katika mapozi tofauti, yote yakiwa yanaonyesha nikiwa katika hekaheka ya kumchinja Kishoka kama kuku. Nilizidi kuchanganyikiwa.

    Wakili wangu aliniangalia huku akiwa amenywea kisha akatikisa kichwa. Aliondoka na kwenda karibu kabisa na kizimba cha shahidi kisha akakaa mkao wa kuanza kumhoji maswali shahidi aliyekuwa kizimbani ambaye ni Sharifa.

    Hata hivyo alishikwa na kigugumizi ghafla na kushindwa kabisa kuongea. Kila alipojaribu kuongea alijikuta akigugumia na kushindwa kuyatamka maneno waziwazi.

    Hali hiyo ilileta taflani kubwa ndani ya mahakama hiyo. Kila mtu akaanza kushangaa ni kwa nini wakili huyo amekuwa namna ile. Hali hiyo ilimfanya jaji aiahirishe tena kesi na kuipangia singu nyingine.

    Kwa upande wangu sikushangaa sana kuona vioja hivyo kwani nilikuwa najua fika kuwa mwanamke yule ambaye alikuwa amejitambulisha kwa jina la Sharifa alikuwa anatumia nguvu za giza.

    Nilirudishwa mahabusu kama kawaida, rumande sasa ikawa ni makazi yangu ya siku nyingi. Mahabusu wengine walikuwa wananikuta na kuniacha kutokana na kesi zao kufikia muafaka, wengine walikuwa wanahukumiwa vifungo na wengine waliokuwa wakishinda waliachiwa huru.

    Kwangu mimi ilikuwa kila siku danadana, limeisha hili linaingia lile. Ilifikia kipindi nikachoka kabisa na maisha ya huko rumande, nikawa natamani hata kujiua lakini niliyakumbuka maneno mazito ya marehemu Anna aliyoniambia nikiwa ndotoni ya kuwa adhabu ya mtu anayejiua ni babu kubwa.

    Kabla siku ya kusikilizwa kesi yangu haijafika nililetewa taarifa kuwa wakili wangu kafariki dunia. Tangu alipotoka mahakamani siku ile hakuweza tena kuongea, hata kile kigugumizi alichokuwa akipapatua siku hiyo kilibadilika akawa haongei kabisa. alikuwa ni zaidi ya bubu.

    Taarifa hizo ziliendelea kueleza kwamba zilipopita siku mbili alianza kuumwa sana hatimaye akawa ameaga dunia. Habari hizo za tanzia ziliniuma sana; kumpoteza wakili Jonas Mlyanyama, mtu ambaye alikuwa makini katika kazi yake.

    ‘Nilimwambia aiache kesi yangu naye akang’ang’ania kuendelea kuisimamia, ona sasa yaliyomfika. Laita kama angenisikia na kuachana na hii kesi asingekufa, huyu mwanamke ni hatari sana.’ Nilijiwazia huku moyo wangu ukiwa na simanzi kubwa kutokana na kifo cha wakili Mlyanyama.

    Taarifa hizo ambazo zilitoka serikalini ziliendelea kunijuza kuwa kwa wakati huo nilikuwa natafutiwa wakili mwingine tena ambaye angeendelea kunitetea katika kesi yangu hiyo. Hata hivyo niliwaambia wasihangaike kunitafutia wakili mwingine kwani yangeweza kumtokea kama yaliyomtokea Jonas Mlyanyama.

    “Hii kesi ina utata mkubwa mno kwani tangu mwanzo wake ni mauzauza matupu. Mimi nawaomba msinitafutie wakili yeyote, nitaimalizia mwenyewe.” Nilimwambia mtu aliyekuwa kaniletea taarifa hizo.

    “Lakini una haki kisheria kutafutiwa wakili wa kukutetea?”

    “Ndiyo nina haki, lakini kwa hali ilivyo katika kesi hii sioni maana yoyote ya kusababisha watu kupoteza maisha yao kwa ajili yangu, kesi yenyewe haina hata mwelekeo mzuri.”

    “Haya bwana wewe wasema, mimi nitapeleka taarifa kama ulivyotaka.” Alimalizia mjumbe huyo na kuondoka zake.



    Siku ayami zilipita, ukakaribia kuisha mwezi bila kupata taarifa zozote za kuendelea kwa kesi yangu kutoka mahakamani. Kadri siku zilivyozidi kwenda nilizidi kuingiwa na ujasiri wa kuja kukabiliana na mwanamke huyo siku tutakayokuwa kizimbani. Tena nikawa na shauku kubwa ya kumbana na kumhoji maswali, ukizingatia kauzoefu kakuhoji maswali nilikuwa nimeshaanza kukapatapata.

                Nilijikuta napania kumkaba maswali ya kufa mtu mwanadada yule. Japokuwa nilijua fika kuwa uwezekano wa kuwa bubu kama ilivyokuwa kwa wakili Mlyanyama ulikuwepo. Lakini sikujali kutokana na kuchoka na vimbwanga vya mwanamke huyo.

                Nikiwa mahabusu nilizidi kujipanga kwa maswali ya kwenda kumkabili huku pointi zangu nikizipangilia kiuanasheria. Nikawa nimeandaa maswali mithili ya gwiji la mawakili.

                Siku moja nikiwa sina hili wala lile nilipewa taarifa kuwa kesi yangu ingesikilizwa tena wiki moja mbele. Niliingojea kwa hamu siku hiyo huku nikiamini kuja kuushangaza umati wa watu wote watakaohudhuria siku hiyo mahakamani kwa kuuliza maswali yenye mantiki na yaliyosimama kisheria.

                Wiki moja haikukawia, nilitinga ndani ya kizimba cha mshtakiwa huku upande wa mashtaka ukimpandisha mwanadada Sharifa kuendelea kutoa ushahidi.

    “Kwa vile shahidi alitoa maelezo siku tuliyomalizia kusikiliza kesi hii, sasa upande wa utetezi utaendelea kumuuliza maswali.” Ilikuwa ni sauti ya jaji.

                Bila kuchelewa wala kuzubaa nikakohoa kidogo kuisafisha sauti yangu, na baada ya hapo nikamfakamia kwa maswali shahidi huyo.

    “Ulisema jina lako unaitwa nani vile?”

    “Sharifa.”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Sharifa unaweza ukaeleza mbele ya mahakama ulikuwa na uhusiano gani na Kishoka?”

    “Ni ndugu yangu.”

    “Ndugu yako kivipi?”

    “Kaka yangu!”

    “Kabla ya hii kesi mimi ulikuwa unanifahamu?”

    “Ndiyo!”

    “Ulikuwa unanifahamu ki vipi?”

    “Nilikuwa nakufahamu kama mmiliki wa nyumba alipokuwa amepanga kaka yangu.”

    “Siku ya tukio ilikuwa ni mara yako ya ngapi kufika hapo kwangu?”

    “Ilikuwa ni mara ya kwanza?”

    “Sasa mimi ulinijulia wapi wakati ilikuwa ni mara yako ya kwanza kuja kwangu?”

    “Nilikujulia mitaani.”

    “Wakati unaniona mitaani nilikuwa na nani?”

    “Ulikuwa peke yako?”

    “Sasa ukajuaje kuwa mimi ni mwenye nyumba wa pale anapoishi kaka yako?”

    “Nilijua tu!”

    “Sharifa, nikikuambia kuwa wewe unajaribu kutunga uongo uwe ukweli nitakuwa nadanganya?”

    “Ndiyo utakuwa unadanganya.”

    “Ngoja nikwambie kitu, mimi Kishoka nilikuwa namjua kuliko mtu mwingie hapa, siri zake zote alikuwa akiniambia, na kati ya siri alizoniambia ni kwamba hana ndugu hata mmoja katika nchi, sasa wewe unadai kuwa ni ndugu yake kutoka wapi?”

    “Labda alikudanganya, lakini mimi ni ndugu yake.” Alijibu Sharifa.

    “Wewe unajishughulisha na nini?”

    “Mimi ni fundi cherehani!”

    “Siyo mpiga picha?”

    “Siyo!”

    “Siyo mwandishi wa habari?”

    “Siyo!”

    “Na wala siyo mtalii?”

    “Nimekwambia mimi ni fundi cherehani?” Alitamka Sharifa kwa ukali.

    “Usiwe mkali Sharifa. Sasa ilikuwaje siku hiyo utembee na kamera? Au ulikuwa unajua kwamba ukifika kwa Kishoka utakuta tukio kama hilo upige picha za ushahidi?”

    “Mimi huwa na kawaida ya kutembea na kamera ili kuchukua matukio muhimu pale inapobidi.”

                “Tulipoonana na wewe kule ufukweni siku moja kabla ya tukio la kuuawa kwa Kishoka ulikuwa na kamera?”

    “Sijawahi kuonana na wewe ufukweni?”

    “Kwa nini kesho yake asubuhi ulikuwa unatusumbua na Kishoka ukigonga geti na kupotea kimiujiza?”

    “Sikuwa mimi?”

    “Alikuwa nani?”

    “Mimi sijui.”



    Baada ya kuona msichana huyo anakikataa kila nilichomuuliza hasira zilianza kuniingia. Ghafla likaniijia swali ambalo nilijikuta namuuliza kwa mtindo wa kuropoka vile.

                “Wewe ni mchawi?”

    “Hapana mimi siyo mchawi.”

    “Wewe ni jini?”

    “Hapana mimi siyo jini.”

    “Kama kweli wewe siyo jini hebu apa kwa Mungu ukisema kuwa wewe siyo jini?”

    “Sasa niape ili iweje?” Aliongea Sharifa huku naye akionekana kuanza kuhamaki.

    “A-aaah! Wewe hebu apa na kama siyo jini kweli hautadhurika na chochote.”

                Huku nikiwa nimechachamaa kumlazimisha Sharifa akiri kwa ulimi wake kuwa yeye siyo jini, nilisikia sauti ya jaji akiingilia kati mahojiano yetu.

    “Naona mshtakiwa umekosa maswali ya msingi ya kumuuliza shahidi. Kama huna swali jingine sema ili nimruhusu shahidi atoke kizimbani.”

    “Mheshimiwa jaji huyu mwanamke siyo mtu wa kawaida kabisa, na sielewi ni kwa nini kaniandama mimi tu katika dunia hii. Amini nakwambia alianza kunifanyia mauzauza siku moja kabla ya kifo cha Kishoka kutokea, hata wakili aliyekuwa akinitetea kayaona mauzauza na ndiyo maana alishindwa kabisa kuongea siku ile. Alianza kwa kumuonya aachane na kesi hii na kumuonya kuwa atamfanya kitu kibaya lakini wakili huyo hakutishika. Alipoona vile akaamua kumuua kabisa kwa kuona kwamba kakaidi, hebu muache aape kama kweli ni binadamu wa kaida, na endapo atakuwa siyo binadamu wa kawaida Mungu anaenda kumuumbua hapahapa!” Nilijaribu kujitetea kwa jaji.

    “Unaswali jingine zaidi ya hilo?”

    “Endapo ataapa maswali yatapatikana.”

    “Shahidi, unaweza ukashuka kizimbani maana mshtakiwa hana jipya.” Alitamka jaji na kunifanya niishiwe nguvu.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

                Nilipotupia jicho kwenye kizimba cha mashahidi nilimuona Sharifa akiondoka kizimbani hapo na kwenda kuketi. Kitendo cha kuondoka msichana huyo bila kufanya nilichokuwa nimemtaka akifanye kiliniumiza sana moyoni.

                Baada ya Sharifa kushuka kizimbani upande wa mashtaka ulimpandisa shahidi mwingine ambaye alikuwa ni miongoni mwa askari waliokuwa wamekuja kunikamata siku ya tukio.

                Mpaka anapanda kizimbani na kuapishwa kisha kutoa ushahidi wake, akili yangu haikuwa katika ushahidi wake bali ilikuwa ikimfikiria Sharifa tu. Tena kichwa changu kilikuwa kimevurugika vibaya vibaya kutokana na jaji kunikatalia ombi langu kwani niliamini kuwa endapo angekuwa ni jini kweli basi angeumbuka.

    Alipomaliza kutoa ushahidi wake ambao haukuwa na tofauti kubwa sana na ule uliotolewa na askari wenzake aliokuja nao kwangu siku ya tukio, jaji aliniuliza kama nina swali kwa shahidi.

    Kusema kweli nilikuwa sijasikia hata neno moja alilokuwa ameongea shahidi huyo wakati anatoa ushahidi wake kwa vile nilikuwa nimezama katika lindi la mawazo juu ya Sharifa. Sasa ningeuliza nini ilhali nilikuwa sijayanyaka maelezo yake hata kidogo!

    Ili kukata mzizi wa fitina nilifumbua kinywa changu na kusema kwa mkato kwamba sina swali lolote kwa shahidi huyo. Ndipo jaji alipomruhusu aende kuketi.   

    Baada ya hapo mwendesha mashtaka aliinuka na kumwambia jaji kuwa upande wa mashtaka ulikuwa umekamilisha mashahidi wake. Baada ya jaji kuambiwa hivyo aliniuliza kama nina mashahidi ili baraza lijalo nianze kuwaleta.

    Nilichomjibu ni kwamba sina mashahidi kwani kesi yenyewe ilikuwa imeghubikwa na utata mkubwa, pia kutokana na mazingira yake jinsi yalivyokuwa.

     Baada ya kumwambia hivyo jaji aliutaka upande wa mashtaka kuandaa maelezo ya mashtaka kuonyesha ni kwanini unamuona mshtakiwa anahatia kwa mujbu wa ushahidi uliotolewa. Shauri hilo liliahirishwa tena kwa mwezi mmoja.



                            *************************



    Siku zilipita. Tarehe ya kesi iliwadia. Siku hiyo ilikuwa ni siku ambayo upande wa mashtaka ulitakiwa kutoa maelezo ya uchambuzi wa kisheria ya kueleza ni kwa jinsi gani inaniona mshtakiwa nina hatia kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa.

    Tayari nilikuwa nimeshapandishwa kizimbani. Ndipo nilipomuona mwendesha mashtaka amesimama kisha akaanza kutoa maelezo mbele ya mahakama ya kuwa upande wa mashtaka umeleta mashahidi walioweza kuthibitisha ya kwamba nilikuwa nimetenda kosa la kumuua Kishoka Mpoto kwa kukusudia, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.

    Akaendelea kueleza kwamba ushahidi uliotolewa umeonyesha dhahiri kuwa nilimchinja Kishoka kwa mikono yangu nikitumia kisu kilichokutwa karibu na mlango kama ushahidi ulivyokuwa umeeleza.

    Akaendelea kusema kuwa licha ya mshtakiwa kudai kuwa aliyetoa taarifa za awali hakutaka kujitokeza kituoni mara baada ya kutoa taarifa hizo, shahidi huyo ambaye alikuwa ni mwanadada huenda aliogopa kwenda kituo cha polisi kutokana na kuchanganyikiwa baada ya kushuhudia ndugu yake akiuawa kikatili ama kutokana na desturi iliyojengeka miongoni mwa waafrika wengi ya kukiogopa kituo cha polisi hata kama hawana hatia.

    “Hata hivyo shahidi huyo alifanya jambo kubwa na la maana kwa kutoa taarifa kituo cha polisi.” Alizidi kueleza mwendesha mashtaka huyo ambaye ni bwana Charles Ngonyani.

    Halikadhalika kuhusu madai yangu ya kudai kuwa msichana huyo alikuwa ni mshirikina au jini, mwendesha mashtaka huyo alisema kwamba hayo yalikuwa ni madai yasiyokuwa ya msingi na mantiki hivyo shahidi huyo alikuwa na haki ya kunifungulia kesi nyingine kwa kumzushia ya kwamba ni mchawi na ni jini. Pia aliongeza kwa kusema kuwa mahakama huwa haiamini imani potofu za kichawi kama mimi nilivyokuwa nikidai.

    Hata kuhusu wakili wangu mwendesha mashtaka alidai kuwa wakili huyo alijaribu kufanya usanii mbele ya mahakama kwa kujifanya kashindwa kuongea  kutokana na uchawi aliokuwa akisingiziwa Sharifa ili kujenga hoja yetu, lakini ukweli ni kwamba shahidi huyo alikuwa ameishiwa hoja za kisheria kutokana na ukweli uliokuwa umetolewa na mashahidi wa upande wa mashtaka.

    Suala la wakili wangu kufariki dunia mwendesha mashtaka alisema kuwa hiyo ni mipango ya Mungu hivyo asisingiziwe Sharifa.

    “Hivyo kulingana na mashahidi waliotoa ushahidi mbele ya mahakama hii tukufu, ni juu ya mahakama kumuona mshtakiwa ana hatia ya kuua kwa kukusudia na hivyo tunaitaka imuhukumu kifo kwa mujibu wa sheria.” Alimalizia mwendesha mashtaka na kuketi.

    Niliumia sana kumsikia mwendesha mashtaka huyo akaniona mharifu na kuiomba mahakama inihukumu kifo wakati maskini wa Mungu nilikuwa sijatenda hiyo dhambi ya mauaji. Hata hivyo sikuweza kumlaumu sana kwa vile wajibu wa waendesha mashtaka ni kuwaona washtakiwa wana hatia hata kama hawajafanya makosa.

    Baada ya mwendesha mashtaka kumaliza kutoa maelezo yake, jaji Aneth Mwalukwa alinitazama na kuniuliza,

    “Na upande wako mshtakiwa unajibu nini?”

                Nilighutuka na kujikuta mapigo yangu ya moyo yakiongeza kasi. Hata hivyo sikuwa na lolote la kuongea bali nilisema kuwa upande wa mashtaka umeniona na hatia kwa vile mauzauza hayakuwatokea wao. Laiti kama yangewatokea hata mara moja basi wangeamini yote niliyoyasema.

                Pia niliongeza kwa kusema kuwa mimi sijabobea sana katika mambo ya sheria hivyo nisingeweza kutoa mapingamizi ya kishera juu ya maelezo ya upande wa mashtaka. Nilimalizia kwa kusema kuwa ni juu ya jaji kuyapima maelezo yangu na ya upande wa mashtaka.

                Wakati wote huo jaji alikuwa ‘busy’ kuandika maelezo niliyokuwa nikiyatoa. Baada ya kumaliza aliniambia kuwa ninawajika kujitetea kwa kosa lililokuwa linanikabili kwani ushahidi uliokuwa umetolewa ulikuwa unaonyesha ya kwamba nimetenda kosa.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

                Nilianza kujitetea palepale. Niliiambia mahakama ya kuwa sikuwa na chuki na Kishoka wala hatukuwa katika mgogoro. Niliendelea kueleza kuwa tukio la kuuawa kwa kifo hicho lilinisikitisha sana kwani siku hiyo asubuhi niliagana naye na nikaenda katika mizunguko yangu.

                “Ndipo aliponipigia simu muda wa jioni akiniambia kuwa kuna mgeni wangu hapo nyumbani, mgeni mwenyewe alikuwa ni yule aliyekuwa anatusumbua toka asubuhi akiwa anagonga geti wakati mimi napata kifungua kinywa.”

                  Nilizidi kueleza jinsi mgeni huyo ambaye kwa pale mahakamani nilikuja nikamjua jina lake kuwa ni Sharifa. Nilieleza jinsi nilivyopokea taarifa kutoka kwa Kishoka ya kuwa mgeni huyo alikuwa amekataa kuingia ndani na kunitaka niende hukohuko getini nikaonane naye.

                Niliendelea kuieleza mahakama kuwa baada ya kwenda hapo getini sikukuta mtu. Kwa kirefu kabisa nilieleza mauzauza yote aliyokuwa akinifanyia msichana huyo mpaka ile jioni niliporudi kwangu na kumkuta Kishoka kashauawa chumbani mwangu.

                “Mambo ya ushirikina yapo na yanatokea sana katika jamii zetu hivyo mahakama isinione kama naongea uongo.” Nilizidi kujitetea.

                Mwisho wa utetezi wangu niliitaka mahakama inione sina hatia na iniachie huru kisha nikafunga kinywa changu.

                Baada ya kutoa utetezi huo, jaji Aneth Mwalukwa ambaye alikuwa ni mwanamama alipanga siku ya hukumu yangu baada ya mwezi mmoja.



    Kwa namna moja au nyingine nilifurahi kusikia hivyo kwani nilikuwa na shauku kubwa ya kujua hatma ya hiyo kesi yangu. Japokuwa nilikuwa najua fika ya kwamba kuokoka kwangu ilikuwa ni bahati nasibu, kitendo cha kupelekwa mahakamani na kupandishwa kizimbani mara kwa mara kilikuwa kimeshanikifu.

    Niliona ni heri hukumu yangu ikitoka, hata kama nitahukumiwa kunyongwa basi nitakaa gerezani bila bughudha siku zote za kungojea kunyongwa kwangu.

    Niliteremka kizimbani na kuchukuliwa na askari magereza kwa ulinzi mkali mpaka kwenye karandinga lao kama ilivyo ada. Tulikaa kidogo kuwasubiri baadhi ya mahabusu ambao kesi zao zilikuwa zinaendelea kusikilizwa. Baada ya kukamilika wote, tuliondoka mahakamani na kuelekea magereza.



                            *****************************



    Mwezi mmoja ulitimia tangu siku ambayo kesi yangu ilisikiliza. Hayawi hayawi hatimaye sasa yakawa, siku ya hukumu yangu iliwadia.

    Mapigo ya moyo wangu yalikuwa yakinidunda kasi kuliko kawaida. Pamoja na kwamba nilikuwa naiombea siku ya hukumu ifike, siku hiyo nilikuwa nimenyong’onyea na kuwa mpole kama shilingi mia.

    Usiombe kuwekwa kizimbani kwa mara ya mwisho ukisubiri hukumu, tena hukumu yenyewe ya kesi ya mauaji! Hakika nilikuwa nipo maji siku hiyo.

    Nilipandishwa kizimbani huku nikiwa nimenywea pasipo mfano. Yaani ilikuwa ni tofauti kabisa na siku zingine zote nilizofika mahakamani hapo.

    Jaji alianza kusoma hukumu yangu kwa kutaja kosa lililokuwa linanikabili na kutangulia kusema kuwa adhabu ya kosa hilo ni kifo endapo mtuhumia atapatikana na hatia.

    Niliposikia hivyo moyo wangu ulilipuka pu kana kwamba ilikuwa ndiyo mara ya kwanza kusikia hiyo adhabu ya mtu mwenye hatia ya kuua.

    Jaji huyo aliendelea kwa kusema kuwa hakuna shaka yoyote kwa ushahidi ambao ulitolewa ya kuwa nilimuua Kishoka Mpoto siku ya tukio hilo.

    “Hata katika utetezi wake mshtakiwa kashindwa kutoa maelezo sawasawa ambayo yanaweza yakailinda hoja yake kuwa hajaua. Suala la kudai kuwa shahidi aliyetoa taarifa za tukio kituoni ni mchawi au ni jini haliwezi likaaminiwa na mahakama hata siku moja kwani hakuna uchawi juu ya sheria.” Aliendelea kutema maneno jaji Aneth Mwalukwa.

    Aliendelea kusema kuwa ushahidi wa picha, alama za vidole kwenye mwili wa marehemu na kwenye kisu kilichokuwa kimetumika kumuulia Kishoka vilikuwa ni vielelezo tosha kabisa kunitia hatiani.

    “Japokuwa sababu au chanzo cha mtuhumiwa kumuua marehemu hakijafahamika mpaka sasa kutokana na mshtakiwa kuendelea kushikilia msimamo wa kwamba hajaua, bado haiondoi dhana ya mtuhumia kupatikana na hatia ya kuua kwa kukusudia.” Alizidi kusema jaji huyo.

    “Kazi yangu ilikuwa ni kuchambua madai ya pande zote mbili, lakini upande wa utetezi umeonekana kuwa na hoja ambazo hazina mantiki kabisa, hoja za kusingizia ushirikia. Katika kusoma madai ya upande wa mshtakiwa sikuona shahidi yeyote ama ushahidi wowote ulioonyesha kuwa ni kweli mtuhumiwa hajaua zaidi ya maneno matupu ya kudai kuwa tukio liliambatana na ushirikina.” Aliunguruma mwanamama huyo.

    Mpaka hapo matumaini yalikuwa yameshaniishia kabisa. Nilijua fika kuwa mwisho wa hukumu yangu ni adhabu ya kifo. Huku maelezo ya hakimu hayajafika mwisho nilianza kuhisi machozi yakinilengalenga huku pua zangu zikionekana kuloa.

    Jaji aliendelea kusema kuwa jambo la shahidi aliyetoa taarifa polisi kutotokea kituoni haliwezi likaleta shaka yoyote juu yake kwani jambo muhimu ambalo ni kutoa taarifa alikuwa kashalifanya. Tena kwa kuongeza ushahidi aliamua kujitokeza mahakamani na kutoa ushahidi wa picha ambao ulionyesha hali halisi ya tukio lilivyokuwa.

    “Kutofika kituoni huenda kulichangiwa na woga pamoja na kuchanganyikiwa kutokana na uzito wa tukio jenyewe ulivyokuwa.” Aliendelea kufafanua jaji huyo.

    Ulikuwa ni uchambuzi ambao ulichukua karibu saa moja. Jaji Aneth Mwalukwa alihitimisha hukumu yake iliyokuwa na kurasa kadhaa kwa kueleza kuwa anakubaliana na upande wa mashtaka kuwa nilikuwa nimetenda kosa la mauaji ya kukusudia dhidi ya marehemu Kishoka Mpoto.

    “Kwa mujibu wa sheria za nchi yetu mtu anayepatikana na kosa hilo, adhabu yake ni kifo. Kwa hiyo natamka kwamba mahakama hii imemtia hatiani mshtakiwa Brighton David kwa kosa la kumuua Kishoka Mpoto kwa kukusudi.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Jaji alinyamaza kidogo kisha akanitazama na akuniambia,

    “Mshtakiwa Brighton David nakuhukumu adhabu ya kifo, utanyongwa kwa kitanza mpaka ufe.”

                Jaji alipomaliza kusoma hukumu yangu aligonga nyundo mezani kisha akainuka na kuondoka.

                Kwa kweli sikuweza kujizuia. Nilijikuta nikiangua kilio cha haja huku simanzi na huzuni zikitawala kwa watu wengi waliokuwa wamefika mahakamani hapo, wale waliokuwa wananijua na hata wale ambao walikuwa hawanijui.

                Wakati jaji anaondoka mahakamani askari magereza walinishusha kizimbani na kuanza kunipeleka kwenye karandinga la magereza bila hata kunipa nafasi ya kuagana na baadhi ya watu niliokuwa najuana nao.

                Kijana niliyekuwa nimemuachia kuisimamia miradi yangu alikuja mbio akitaka kuongea nami kwa mara ya mwisho, lakini bila huruma askari alinisukuma na kunitaka niingie kwenye karandinga haraka.

                Gari lililokuwa limenichukua liliondoka kwa kasi ya ajabu kuelekea gerezani

     

                              **************************



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog