Search This Blog

Thursday, 2 June 2022

MIRATHI YA KAKA - 4

 







    Simulizi : Mirathi Ya Kaka

    Sehemu Ya Nne (4)



    Gari lililokuwa limenichukua liliondoka kwa kasi ya ajabu kuelekea gerezani

        CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

                              **************************

    SASA ENDELEA.......

    Maisha ya jela ndiyo niliyoanza kuishi kwa wakati huo. Niligundua tofauti kubwa sana kati ya jela na mahabusu. Ukiwa mahabusu husumbuliwi kufanya kazi ama adhabu yoyote kwani unakuwa bado ni mtuhumiwa tu.

    Lakini ukiwa jela unatakiwa kufanya kazi za hapa na pale zikiwa ni adhabu kwani tayari utakuwa umeshahukumiwa. Na ndiyo maana watu wengine husema jela kuna mateso.

    Yote hayo ni tisa, kumi mkienda kulala, heheeeh! Kama utalemaa mithili ya kalio la kushoto basi unaweza ukawa mke wa wanaume wenzio. Huko ndiyo kuna watu waliopinda, watu wasiokuwa na dira na maisha.

    Jela ni ubabe ubabe tu, unyama na mikwara ndiyo hutawala hasa kwa mtu mgeni gerezani humo. Hata hivyo kwa upande wangu hayo yote hayakutokea licha ya kuwa na muonekano wa upole.

    Kilichonisaidia kutoionja adha ya ugeni wa jela ni kitu kimoja. Kuna jamaa mmoja nilimkuta humo gerezani ambaye tulikuwa tukifahamiana na kuheshimiana sana. Huyo mtu ndiyo alionekana kuwa msaada mkubwa sana kwangu kwani alikuwa kakaa humo kwa muda wa miaka miwili hivyo mikikimikiki ya huko alikuwa kashaizoiea.

    Mbali na kuizoea mikiki mikiki ya humo; jamaa huyo alikuwa kashateuliwa kuwa mnyapara wa gereza. Mnyapara wa gerezani ni yule mfungwa anayewaongoza wafungwa wezake gerezani humo.

    Jamaa huyo hakuwa mwingine bali ni Mack. Uhusiano wetu haukuanza siku hiyo ama siku za karibuni, ulianza miaka mingi iliyokuwa imepita. Tulikuwa tunafahamiana toka kitambo na tulikuwa tumeshafanya mambo mengi.

    Baada ya kifo cha marehemu kaka James; mali zake zote nilizirithi mimi kwani ndiyo nilikuwa ndugu yake wa pekee. Ikumbukwe kuwa mimi na marehemu James tulizaliwa tumbo moja ila baba zetu ni tofauti.

    Yeye ndiye alikuwa kifungua mimba katika tumbo la mama yetu. Mama yetu alipata ujauzito kwa bahati mbaya wakati anasoma elimu ya sekondari.

    Baada ya kupewa ujauzito alilazimika kukatisha masomo ili aulee huo ujauzito hivyo akashindwa kuendelea na elimu na kujikuta akiishia kidato cha tatu.

    Jamaa aliyekuwa amempa ujauzito alikimbia na kupotelea pasipojulikana kwa kuogopa kushtakiwa na wazazi wa mama yetu kwa kumrubuni na kumkatisha masomo mtoto wao.

    Si wazazi peke yao waliokuwa wakila sahani moja na wanaume waliobainika kuwapa mimba watoto wao, hata serikali ilikuwa ipo mstari wa mbele kuhakikisha wanafikishwa mbele ya sheria.

    Tangu siku hiyo jamaa huyo alipotea kabisa na hakuonekana tena kama walivyopotea wadudu aina ya nzige. Nadhani waliozaliwa siku za nyuma kidogo wanakumbuka miaka ile ya uvamizi wa nzige katika mashamba ya wakulima.

    Nzige ni wadudu hatari sana ambao hutembea katika kundi kubwa na wakivamia shambani mwako basi wanakula mimea yote iliyomo shambani humo. Usiombe shamba lako livamiwe na wadudu kama hao kwani wanakula hadi mashina ya mimea ya shamba wanalolivamia.

    Sasa mwanaume aliyekuwa amempa ujauzito mama yetu na kumsababisha kukatisha masomo alipotea mithili ya wadudu hao.

    Hakuonekana kabisa wala hazikusikika fununu zake hata kidogo. Kutokana na hiyo hali; mpaka wa leo haijulikani kama jamaa huyo bado yungali hai ama kashakumbwa na mauti.

    Mama aliiingia katika wakati mgumu sana baada ya kubebeshwa huo ujauzito. Kilichokuwa kinamfanya apate tumbo joto ni jinsi baba yake alivyokuwa mkali na katili kupindukia, yaani marehemu babu.

    Babu yangu huyo alikuwa ni mkali kama simba. Sijui kutokana na ujeshi wake aliokuwa nao, maana alikuwa mbogo kupita maelezo. Alikuwa hataki kabisa ‘Ujinga jazz bend’ katika familia yake.

    Sasa ujauzito huo ulimfanya mama yangu azidi kuchanganyikiwa, kibaya zaidi hata aliyekuwa amempa huo ujauzito alikuwa kashakimbia na kutokusikika hata zile fununu zake.

    Alichoamua ni kutoroka na kuenda asikokujua kwani aliona hata akienda kwa ndugu wengine baba yake angempata, na hapo ndiyo angelionja joto la jiwe.

    Hakutaka kujiua wala kuitoa hiyo mimba kwani alikuwa akiijua vyema dhambi iliyopo kwa binadamu anayejiua ama anayeua. Hayo yote alikuwa ameyaweka akilini tangu utotoni alipokuwa akipewa mafundisho ya dini.

    Mama yangu alilelewa katika maadili ya kidini sana japokuwa alikuja kuanguka dhambini na kurubuniwa na kamjamaa kalikokuja kumpa ujauzito.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Huku ujauzito aliokuwa nao ukiwa na miezi mitatu, mama aliamua kutorokea katika mji jirani ili kujiepusha na hasira za baba yake. Kwa mtazamo wake alihisi suluhu ya hiyo kashfa ni kulala mbele.

    Alfajiri na mapema alitoka nyumbani kama anaenda shule akiwa na sare zake za shule huku nguo zingine akiwa ameziweka kwenye mfuko wake wa kubebea vitabu vya shule.

    Kwa vile ilikuwa bado asubuhi sana, hakuna mtu yeyote  aliyemuona kwa pale nyumbani wakati anatoka. Alitembea mpaka kwenye stendi ya mabasi, akakata tiketi ya basi lililokuwa linaondoka muda si mrefu.

    Wakati huo alikuwa tayari kashazivua sare za shule na kuvaa nguo zake za nyumbani alizokuwa ameziweka kwenye mfuko wa kubebea vitabu vyake vya shule.

    Baada ya robo saa alikuwa tayari kajikausha kunako viti vya basi hilo huku likichanja mbuga kwa mwendo wa kasi.

    Mambo yaligeuka kuwa si mambo mara baada ya basi hilo kuupa mgongo mji huo. Liligongana uso kwa uso na lori la mafuta na kusababisha ajari mbaya sana.

    Basi hilo lilipiga mweleka na kubingirika mpaka mara tatu, likawa nyang’anyang’a kutokana na ajari hiyo.

    Ilikuwa ni ajari mbaya sana na ya kutisha ambapo watu kumi na sita walipoteza maisha papo hapo, watu ishirini walikuwa ni mahututi na watu kumi na tano wakijeruhiwa ila siyo sana. Kati ya wale mahututi na mama yangu naye alikuwa ni mmoja wao.

    Haukupita muda sana magari ya kubeba wangonjwa (ambulance) yakawa pale kubeba wahanga wa ajari hiyo pamoja na maiti na kuwapeleka katika hospitali ya jeshi iliyokuwa karibu kabisa na sehemu ilipokuwa imetokea ajari hiyo.

    Mpaka anafikishwa hospitali mama yangu alikuwa hajielewi hata kidogo. Alikuwa kaumia vibaya sana



    Taarifa za ajali ziliwafikia wazazi wa mama majira ya mchana, walipigiwa simu na mwalimu mkuu wa shule aliyokuwa akisoma mama na kuambiwa kuwa mtoto wao kapata ajali katika moja ya basi lililokuwa likienda mji jirani muda mchache baada ya kutoka mjini hapo.

    Walishangaa sana kusikia habari hiyo, wakaanza kujiuliza mtoto wao alikuwa kapanda gari hilo kuelekea wapi! Walipojaribu kumuuliza mwalimu kuwa labda alikuwa na taarifa na hiyo safari naye aliruka kimanga na kudai hana ajualo.

    Hapo ndiyo wazazi walizidi kuchekecha akili wakijiuliza kuwa mtoto wao alikuwa anasafiri kuenda wapi na ni kwa nini aondoke bila ya kuaga ama kutoa taarifa?

    Hata hivyo hilo halikuwa la kujadili sana kwa wakati huo, kilichokuwa cha msingi kwa wakati huo ni kwenda hospitali kumuona mtoto wao, hata hayo maswali yao yote yangeweza kupata majibu hukohuko kwa kumuuliza mwenyewe.

    “Au labda alikuaga wewe lakini unanificha tu?” Ilikuwa ni sauti ya babu yangu akimuuliza mkewe wakati gari yao inachoma mafuta kuelekea hospitali aliyokuwa kalazwa mama. 

    “Aka! Mimi sijui chochote kuhusu safari hiyo, atakuwa kajiamulia mwenyewe.”

    “Maana nyie wanawake wakati mwingine huwa mnakula njama na watoto wenu hasa hasa watoto wa kike.”

    “Mimi siwezi nikafanya ujinga kama huo.”

                Mara baada ya maongezi hayo ukimwa ulitawala katika safari hiyo. Hawakuchukua muda wakawa wamefika kwenye hospitali ambayo majeruhi na maiti waliopatikana katika ajali ya asubuhi walikuwa wamehifadhiwa.

                Wakaanza kumtafuta mtoto wao kwenye wodi walizokuwa wameweka majeruhi. Kwa bahati nzuri hawakuhangaika sana wakawa wamemuona, ila alikuwa bado hajazinduka.

                Fahamu zilimrudia muda wa usiku, akashangaa kujiona yupo hospitali huku akiwa na majeraha mwili mzima. Hata hivyo tukio zima alilikumbuka mara baada ya kuvuta kumbukumbu. Ndipo akakumbuka kuwa  alikuwa akitoroka kwa kuogopa kugundulika nyumbani ya kuwa ni mjamzito.

                Akili yake ikamtuma kuwa huo ndiyo ulikuwa ni muda muafaka wa kuomba radhi kwa wazazi wake kwani hata zile hasira za baba yake zisingewaka sana juu yake kwa vile alikuwa anaumwa na yupo hospitali. Alijua fika mpaka kuja kupata nafuu baba yake atakuwa kashapunguza hasira kama siyo kuisha kabisa na hapo asingekipata kichapo cha paka mwizi.

    Kesho yake asubuhi baba na mama yake walikuwa wameshafika hospitali hapo kumjulia hali. Kwa wakati huo hali yake ilikuwa inaendelea vizuri ingawaje alikuwa bado ana maumivu makali.

    Ndipo alipopata fursa ya kuwaeleza wazazi wake kinaga ubaga juu ya tatizo lililokuwa likimsumbua kiasi kwamba mpaka akachukua uamuzi wa kutoroka nyumbani.

    “Huyo bwege aliyekupa ujauzito huo ni nani na yuko wapi?” Lilikuwa ni swali la baba yake baada ya kusikia hivyo.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kashakimbia, hicho nacho ndicho kimechangia kunifanya nichukue uamuzi huo kwani ana wiki mbili sasa hayupo.” Alijibu mama yangu kwa shida.

    “Jamani, mimi sioni sababu yoyote ya kuanza kuyajadili mambo haya huku hospitali, haya mambo ni ya kuyajadili tukiwa nyumbani.” Aliingilia kati bibi yangu.

                Hata hivyo mama alikuwa na hofu kwamba maelezo hayo akiyatoa wakiwa nyumbani yanaweza yakaupandisha ‘mzuka’ wa baba yake na kuanza kumshushia kichapo. Lakini alipiga moyo konde na kusema litakalokuwa na liwe. Kizuri zaidi alikuwa tayari kashatoa utangulizi wa jambo hivyo hasira za baba yake zisingekuwa nyingi sana.

                Baada ya wiki moja mama yangu aliruhusiwa kutoka hospitali, afya yake ilikuwa inaimarika vizuri ingawaje majeraha mengine yalikuwa hayajapona ikiwemo mkono wake ambao ulikuwa umevunjika hivyo alikuwa kawekewa ‘p.o.p’

                Siku hiyo hiyo alipofika nyumbani hakutaka kulaza damu, aliianzisha tena mada kwa kuwaomba msamaha wazazi wake kwa kile kilichokuwa kimejitokeza.

                Suala hilo liliongelewa na kufikia muafaka, akawa ameambiwa asiwe na wasiwasi kwani kuteleza si kuanguka.

    “Usiwe na wasiwasi mwanangu mimi na mama yako tumeshakusamehe, ila ole wake huyo mpumbavu aliyejifanya rijali apatikane, hapo ndiyo atajua kuwa kumbe koti huwa halichomekewi, atajuta kuzaliwa.” Mzee wa kazi alimalizia kuongea kisha akaondoka zake.

                Mama aliendelea kuilea mimba yake akiwa nyumbani. Mpaka miezi tisa ilipoada ndipo alipojifungua mtoto wa kiume ambaye ndiyo alikuwa kifungua mimba wake, huyo hakuwa mwingine bali ni kaka James.

                Kuzaliwa kwa kaka James ndiyo kulikuwa hivyo. Wakati huo mimi nilikuwa bado sijafikiriwa hata kuiona hii dunia. Nilikuwa bado nipo mbinguni nikicheza na kufurahia tu na malaika.



    Baada ya kujifungua mama yangu hakupata tena nafasi ya kuendelea na masomo ya sekondari kwani huo mfumo umekuja miaka ya hivi karibuni. Zamani ukinasa huku bado unasoma basi hiyo ndiyo nitolee tena.

    Haikuwa kama siku hizi ambapo msichana akipata mimba yungali anasoma anaruhusiwa kwenda kuilea mimba kisha akishajifungua anaendelea na masomo. Miaka ile haikuwa hivyo.

    Hata hivyo mama yangu alikuja kujiunga na ualimu wa UPE enzi zile rais wa kwanza wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania hayati Mwl. Julias Kambarage Nyerere alipotangaza elimu ya UPE.

    Kwa wale wenzangu na mimi ambao wamezaliwa juzijuzi  kuelekea kwenye mfumo wa digitali, maana ya UPE ni mpango ulioanzishwa na aliyekuwa rais wa kipindi hicho hayati Baba wa taifa Mwl. Nyerere ambao ulitaka kila mtoto wa kitanzania asome elimu ya shule ya msingi.

    Hapo ndipo ulipotokea upungufu mkubwa wa walimu wa shule za msingi kiasi kwamba walimu waliokuwa wametoka vyuoni wakawa hawakidhi mahitaji.

    Ndipo serikali ilipotangaza nafasi za ualimu hata kwa wale waliokuwa wameishia njiani na kushindwa kumaliza kidato cha nne pamoja na wale waliokuwa wamemaliza darasa ya saba nao walichukuliwa na kupewa jukumu ya kuwa walimu.

    Kati ya hao walimu wa UPE na mama yangu naye alibahatika kuwamo. Akawa amepangiwa shule ya kufundisha.

    Ilipita miaka kadhaa. Huku akiwa mwalimu alipata mume na kumuoa. Ndipo nilipozaliwa mimi.

    Wakati huo kaka James alikuwa akiishi na wazazi wake na mama, yaani namaanisha kwa bibi na babu. Mpaka walipokuja kufariki ndipo alipochukuliwa na mama na kukaa pamoja katika familia moja.

    Baba yangu alimchukulia kaka James kama alivyokuwa akinichukulia mimi, yaani alimlea kama mwanae wa kumzaa wakati alikuwa ni baba yake wa kufikia.

    Hapakuwa na ukambo ukambo hapo, baba yangu alikuwa kapenda boga pamoja na maua yake. Alikuwa tofauti kabisa na baadhi ya wanaume ama wanawake wengine wanaowachukia watoto wa kambo.

    Kama zawadi alituletea wote bila ya upendeleo, kama adhabu alitoa bila ya kupendelea, kama ni mapenzi basi alitupatia mapenzi mema wote wawili.

    Kaka James hakuwahi kuwa na upweke kwa kulelewa na baba wa kambo. Alikuwa akithaminiwa kama kawaida, hakika maisha yake yalikuwa ni ya furaha siku zote.

    Nadhani upendo tuliokuwa tukiupata kutoka kwa baba na mama ndiyo ulioimarisha uhusiano wetu na udugu wetu uliokuwa wa kushibana kama vile mapacha.

    Hata hivyo furaha yetu ilikuja kubadilika na kuwa majonzi pale wazazi wetu walipokuja kupata ajari mbaya ya gari na kupoteza maisha papo hapo. Vifo vya wazazi wetu kwa mkupuo vilichimba donda kumbwa mno moyoni mwangu.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Usiombe ndugu msomaji kuwapoteza wazazi wako kwa wakati mmoja, maumivu yake ni zaidi ya msumari wa moto ukandamizwapo kwenye kidonda kinachoelekea kupona.

    Tukio hilo huwa sipendi hata kulielezea kwani huwa linaibua machungu makubwa mno ndani ya moyo wangu. Yaani wee acha tu. Kama ukitaka nianze kububujikwa na machozi basi nikumbushie tukio hilo tu, aisee! Bora niachane na hizo habari kwani zitanifanya nishindwe hata kuendelea kukuhadithia yanayohusu mirathi ya kaka.

    Wakati wazazi wetu wanatutoka mimi nilikuwa nipo darasa la tatu na kaka James alikuwa ndiyo kahitimu kidato cha nne.

    Mara baada tu ya wazazi wetu kufariki kaka James alitaka tugawane mali tulizokuwa tumeachiwa. Kwa kuwa mimi nilikuwa mdogo sana, sikuwa na la kuamua wala kushauri zaidi ya kuwa kama bendera nikifata maamuzi ya kaka yangu.

    Tuligawana mali zote huku nyumba akiniachia mimi. Hata hivyo tuliendelea kuishi hapo wote licha ya nyumba kuwa mikononi mwangu. Baadhi ya mali  nilizokuwa nimegawiwa kutoka kwenye mirathi hiyo tuliziuza ili zinisaidie katika masomo.

    Kaka James yeye aliuza kila kitu, lakini hakutaka tena kuendelea na shule badala yake alianza kufanya biashara huku akiwa na mtaji wa kutosha kutokana na kuuza mirathi yake yote.

     Nilifanikiwa kusoma mpaka kidato cha sita huku kaka yangu yeye akiishia kidato cha nne tu. Lakini mpaka namaliza shule mwenzangu alikuwa kashakuwa tajiri huku biashara zake zikishamiri vizuri.

    Kasi ya kupata utajiri kwa kaka James ilikuwa kubwa sana mpaka nikaanza kushangaa. Nilipojaribu kumuuliza kaka James kulikoni naye aliniiambia ni baraka kutoka kwa Mungu. Hilo ndilo lilikuwa jibu lake pindi nilipomuuliza kuhusu utajiri huo aliokuwa akiupata kwa kasi.

    Mpaka namaliza kidato cha sita alikuwa ni tajiri wa kuogopeka mji mzima. Alikuwa na magari mawili ya kifahari na nyumba mbili za kifahari.



    Tulihamia kwenye nyumba moja na kuanza kuishi pale. Mambo yalizidi kuwa safi kwa kaka James. Nilizidi kupata wasiwasi kwa jinsi utajiri wake ulivyokuwa ukiongezeka kila kukicha.

    Kati ya miradi mikubwa aliyokuwa nayo ni pamoja na kampuni ya usafirishaji ambayo ilikuwa na malori ya kusafirisha mizigo ndani na nje ya nchi. Ilikuwa ni kampuni kubwa iliyokuwa imeajiri wafanyakazi wengi mno.

                         

    ************************

             

                Mahusiano ya kimapenzi kati ya kaka James na mwanadada Neila yalizidi kupamba moto. Hapo awali mimi nilikuwa sijui chochote kuhusu uhusiano huo kwani alikuwa hajanitambulisha.

                Ilifikia kipindi akanitambulisha rasmi na kuniambia Neila ndiye alikuwa tashtiti wake, nyonga mkalia ini kama wasemavyo watu waliobobea kwenye mahaba.

                Sikuwa na pingamizi juu ya uhusiano wao ila niliwasisitiza tu watangulize uaminifu mbele pamoja na upendo wa dhati kwa ujumla.

                Mapenzi yao yaliendelea kukolea kila siku iliyoenda kwa Mungu. Hapo ndipo Naila alianza katabia ka kudai makuu ikiwemo kukabidhiwa nyumba kununuliwa gari zuri la kifahari pamoja na kufunguliwa akaunti yenye hale nyingi.

    Hayo yote hayakuwa tatizo kwa kaka James maana pesa ilikuwa chekwa. Kila alichotaka mtoto wa watu alitimiziwa, mpaka nikaanza kumuonea wivu kwani alizidi mno kumpiga ‘kibomu’ kaka yangu. Naye James kwa kutaka kumkoleza mwanadada huyo hakuona ajabu kuvitoa vimilioni kwa ajili yake.

                Siku chache baada ya kaka James kumkamilishia mambo hayo; mwanamke huyo alibadilika ghafla na kuanza kufanya vimbwanga vilivyokuwa vikileta kichefuchefu mbele ya James.

                Tabia ya mwanamke huyo ilizidi kuwa mbaya, akawa anamletea kiburi kaka yangu huku akimpa masharti mengimengi ikiwa ni pamoja na kuwa anatoa taarifa akitaka kwenda kwake.

                Siku moja kaka James alienda kwa mwanamke huyo bila taarifa. Alichokikuta huko hakuamini kwa macho yake kwani alikikuta kidume kimejilaza kitandani kikiwa na mwanamke huyo huku wakiwa kwenye pozi la kimahaba.

                Ghadhabu zilimjaa sana kaka James baada ya kuyashuhudia yale mambo.

    “Nini hicho unafanya mpenzi wangu?” Alisikika James kwa sauti ya kitetemeshi akionyesha ni jinsi gani hasira ilivyokuwa imepanda.

    “Nani mpenzi wako?” Aliuliza mwanamke huyo kwa jeuri na nyodo za kila aina.

    Kauli hiyo ilizidi kuipandisha hasira ya James. Hapo ndiyo alipojua ya kwamba mwanamke huyo ni nyoka ndumilakuwili mwenye sumu kali.

    “Sikia nikwambie James; kama kusoma hujui basi jaribu hata kuangalia picha! Wewe ni zilipendwa ndugu yangu, tangu lini mavi ya kale yakanuka?. Mwanaume mwenyewe upo kianalojia utarandana vipi na mimi nipo kidigitali zaidi? Sasa nakutangazia rasmi leo kuwa sikupendi na sikuhitaji, na huyu unayemuona hapa ndiye mwanaume ninayempenda kwa dhati ambaye anastahili kuniona. Upo hapo? Hii ndiyo habari ya mjini babu wee!” Alizidi kutamba mwanamke huyo kisha akamalizia kicheko cha kishambenga,

    “Heheheeeyah!”

    “Kefle! Unajifanya mjanja na kuniona bwege mimi, sasa anza kusali sala zako za mwisho kwani uhai wako naukatisha sasa hivi?” Alidakia James kwa sauti ya juu iliyowashitua Neila na jamaa yake aliyekuwemo humo ndani.

    Siyo sauti ya juu pekee iliyowafanya waduwae bali ni pamoja kitu alichokuwa amekishika mkononi. Kitu hicho hakikuwa kingine bali ni kidubwasha mithili ya kipaja cha kuku kilichoundwa kwa madini shaba. Alikuwa ameshika bastola.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mwanamke yule alianza kutetemeka na kuanza kuomba msamaha kwa James, kwa bahati mbaya alikuwa amechelewa! Bila ya huruma James alikitekenya kitufe cha kufyatulia risasi kisha akamtwanga mwanamke huyo ya kichwa.

    Huku akiwa anatweta kwa hasira aliisukuma risasi nyingine ambayo ilimpata yule jamaa aliyekuwa akijaribu kulamba asali kwenye mzinga wa James.

    Risasi hiyo nayo ilimpata barabara kijana huyo, ikapenya kupitia kwenye paji lake la uso na kumfanya naye aanguke chini. Hakuchukua muda akawa amerudisha jezi ya kuendelea kuishi kwa mwenyezi Mungu, ikawa ni kwa heri mwalimu!

    Mpaka hapo dhambi ya mauaji ya watu wawili kwa mpigo ilianza kumtafuna kaka James. Hofu na woga vilitanda katika moyo wake, akaanza kuona kesi ya mauaji ya watu wawili ilikuwa inamkabili.

    Baada ya kuwaza kidogo alikumbuka kuwa bastola yake ilikuwa imebakiza risasi moja ndani. Ndipo alipoamua kujimaliza na yeye kwa kujipiga risasi.



    Wakati huo nilikuwa namfuatilia kwani machale yangu yalikuwa yamenicheza. Wakati anaondoka nyumbani alikuwa kashaniambia kuwa anaenda kwa mpenzi wake ila alikuwa akienda bila ya taarifa huku akiyavunja masharti aliyokuwa amepewa na mpenzi wake huyo.

    Niliamua kumfuatilia ili nikashuhudie ‘timbwilitimbwili’ nililokuwa nikilitegemea kuibuka baada ya kaka James kufika kwa mpenzi wake huyo. Hata kama yangetokea mapigano kisha kaka yangu akazidiwa basi mimi ningekuwepo nyuma yake kuokoa jahazi.

    Hata hivyo aliniacha njiani kwani alikuwa akiendesha gari lake kwa kasi mno. Mimi nilikuwa naogopa ajali hivyo nikawa naendesha mwendo wa kistaarabu.

    Kwenda kwangu polepole ndiyo kulinifanya nimkose kaka James katika dunia hii kwani nilichelewa kiduchu mno. Wakati naufikia mlango wa chumba walichokuwamo kina Neila, tayari kaka James alikuwa kashakitekenya kitufe cha kufyatulia risasi huku akiwa amejilenga kwenye kichwa chake.

    Nilimshuhudia kaka James akianguka mzima mzima kisha akakata roho. Ndipo nilipopoteza fahamu na kushindwa kuelewa kilichokuwa kikiendelea.

    Fahamu zilinijia masaa matano mara baada ya tukio hilo kutokea. Nilijikuta nipo wodini huku nikiwa nimetundikiwa drip ya maji. Nilishangaa sana kujikuta nipo hospitali.

    Katika kuvuta kumbukumbu nilikumbuka jinsi mambo yalivyokuwa masaa matano yaliyokuwa yamepita. Nilikumbuka kuwa kaka James hakuwepo tena duniani.

    Nilizidi kuchanganyikiwa, akili yangu ikazidi kuvurugika baada ya kukumbuka hilo tukio lililokuwa na tanzia kubwa katika moyo wangu na akili yangu kwa ujumla.

    Sikuona kabisa mantiki ya kuendelea kubaki hospitali wakati nyumbani kulikuwa na msiba wa marehemu kaka yangu. Sikujua ni vipi mipango ya mazishi ilikuwa inapangwa huko kwani mimi ndiyo nilikuwa ndugu wa pekee wa marehemu. Kwa kifupi mhusika mkuu wa msiba huo nilkuwa ni mimi.

    Nilipojaribu kuangaza angaza niliona karibu wagonjwa wote wamelala kwenye vitanda vyao kila mmoja. Sikuona muuguzi wala dakitari yeyote aliyekuwemo kwenye wodi hiyo.

    Bila kuchelewa wala kuduwaa niliichomoa sindano ya drip na kutoka mbio kuelekea nyumbani kuungana na majirani kuomboleza kifo cha kaka James.

    Kwa vile James alikuwa mtu mashuhuri sana katika mji huo, tayari taarifa za kifo chake zilikuwa zimeshazagaa mtaani na katika mji wote kwa ujumla.

    Nilipofika nyumbani niliwakuta watu wengi wameshakusanyika. Hata hivyo mwili wa marehemu ulikuwa upo hospitali umehifadhiwa kwa uchunguzi zaidi. Nilijumuika na watu waliokuwa wameshafika, maombolezo yakaendelea.

    Watu walizidi kumiminika kuja kunipa faraja kwenye msiba huo. James alikuwa ni mtu wa watu, alijua kukaa vizuri na majirani pamoja na watu wengine aliokuwa akifahamiana nao. Hali ya watu kujaa ilinifariji kwa kiasi fulani ingawaje moyo wangu ulikuwa umeghubikwa na majonzi yasiyokuwa kifani.



    Pamoja na kwamba ni miezi kadhaa ilikuwa imepita tangu kifo cha kaka James kutokea, akili yangu ilikuwa haijachanganya kabisa. Kila nilichokuwa najaribu kukifanya nilikiona hakifai.

    Kifo hicho kilikuwa kimetonesha donda jingine kwenye mtima wangu ambalo lilikuwa bado halijapona. Donda hilo nilikuwa nalifananisha na donda ndugu kwani lilikuwa limechukua muda mrefu sana bila kupona ndani ya moyo wangu.

    Usiombe kupata majeraha palipo na donda ndugu mpenzi msomaji. Hebu fikiria maumivu yake yatakavyokuwa. Ni zaidi ya uchungu!

    Donda lililotoneshwa na kifo cha kaka James ni lile lililokuwa limeachwa na kipenzi cha roho yangu marehemu Anna pamoja na wazazi wangu, hasa hasa kile cha Anna.

    Kuondoka kwa Anna katika dunia hii kuliniathili pakubwa sana kisaikolojia na athari yake hiyo ilikuwa bado haijaisha moyoni mwangu.

    Mpaka leo huwa sipati jibu ukiwa wanaoupata wale wanaoondokewa na wenzi wao wa ndoa wanaowapenda kwa dhati. Ikiwa mimi niliipata freshi kwa mpenzi tu ambaye tulikuwa hata bado hatujaoana, wao sasa inakuwaje ukizingatia tayari wameshaonja tamu ya ndoa?

    Marehemu Anna alikuwa ni msichana wa pekee ambaye nilitokea kumpenda kipindi nasoma. Mimi nilikuwa nasoma elimu ya sekondari yeye alikuwa bado yupo shule ya msingi.

    Uzuri wa sura yake, umbo pamoja na tabia ndivyo vilikuwa vimenichengua mtoto wa kiumi mpaka nikawa sijiwezi, nikafa na kuoza kwake kama vijana wa kileo wasemavyo. Mtoto alikuwa yupo kamili gado, kamili kila idara.

    Mpaka wa leo huwa natafutia msichana mwenye sifa kama zake lakini naambulia hola! Wasichana wa namna hiyo ni adimu sana kuwapata, yaani ni sawa na kumsaka bikira uswahilini kwani unaweza ukakesha bila hata ya kumpata.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mapenzi yetu hayakuwa kama mapenzi yale yanayofanywa na vijana wa siku hizi, mapenzi ya kuanza kuzini kabla hata hamjafunga ndoa. Eti wao husema huwezi ukauziwa mbuzi kwenye gunia; wapi ndugu zangu hizo ni roho za pepo wachafu tu, pepo wa uzinzi.

    Ndiyo zao vijana wa siku hizi, hasa wavulana. Utakuta wanakwambia kumuoa mwanamke huku hujafanya naye mapenzi ni kosa la jinai kwani unaweza ukakuta hayawezi ‘mahabati’,mwenye kutulia kama gogo kwenye mambo fulani. Wanasema yote hayo ni tisa, kumi ukute bwawa na siyo kisima, au ukutane na ile timu ya Songea; unaweza ukatangaza taraka. Hiyo ndiyo mitazamo yao.

    Mimi hayo sikujali kwani niliona ni upuuzi na ulimbukeni mkubwa unaotokana na utumwa wa mapepo ya uzinzi. Kutokana na misingi mizuri ya kidini niliyokuwa nimefundishwa tangu utotoni niliamini kuwa hakuna linaloshindikana mbele ya Mwenyezi Mungu.

    Kama yeye huwatakasa mpaka wenye ukoma, kwa nini asikibadilishe kitu chochote kinacholeta kikwazo kwako kilichopo kwenye mwili wa mwenzi wako wa ndoa uliyemuoa kwa ndoa halali kabisa? Yote yanawazekana.

    Hivyo ndivyo mitazamo wetu ilivyokuwa. Bahati nzuri ni kwamba Anna alikuwa bado hajaupoteza usichana wake na mimi nilikuwa sijaupoteza uvulana wangu. Wote tulikuwa safi kabisa.

    Pamoja na kupendana kwetu lakini tulikubaliana kutofanya mapenzi mpaka tuje kufunge ndoa kwani kinyume na hapo ni dhambi kwa Mungu, dhambi ya kuzini ambayo inawatafuna vijana wengi wa siku hizi.

    Huo ndiyo huitwa upendo wa kweli, mapenzi yasiochuja mpaka uzeeni. Siyo mapenzi feki ambayo leo mko pamoja halafu kesho mnazinguana na kushika hamsini zake kila mmoja.

    Kifo cha Anna ndiyo kilizima taa za upendo moyoni mwangu na kuacha giza totoro ambalo mpaka leo ni athari kubwa kwangu.

    Alikuwa anajipenda, alikuwa anajiheshimu, wala hakuwa mapepe na ndio maana vijana wengi wa mtaani walitamani sana awe wao matokeo yake waliishia kula ‘vibuti’ vya uso.

    Amini usiamini siku zote mti wenye matunda ndiyo hupigwa mawe. Kutokana na usemi huo, kipenzi Anna nilimfananisha na mti wa mnazi ambao hata ukiupopoa kwa mawe huwezi kuangusha nazi wala dafu. Kumbe nilikuwa najidanganya kwani kuna wakwezi ambao hupanda mpaka matunda yaliko kisha huanza kuyasanifu kwa vyovyote vile wanavyotaka.

    Hicho ndicho kilichotokea kwa marehemu Anna. Pamoja na kuwa na msimamo zaidi ya binti wa kilokole, ilifika siku maagano yetu yakavunjika japokuwa siyo kwa ridhaa na utashi wake.

    Ilikuwa ni siku ngumu sana kwake; siku aliyorubuniwa na dada yake kisha wakaenda kwenye sherehe ya kuzaliwa ya mpenzi wa huyo dada yake. Kumbe kulikuwa na mipango kabambe ya kumwingiza kipenzi changu kwenye jaribu zito lililokuja kupelekea kifo chake.



    Kuna kijana mmoja ambaye alikuwa akimtaka Anna kimapenzi siku nyingi lakini ikashindikana. Kwenye hicho kisherehe naye alikuwepo.

    Baada ya kumuona Anna kijana kijana huyo akasema kuwa lazima lengo lake litimie, ndipo alipomchanganyia dawa za kulewesha kwenye soda na hatimaye akalewa na akawa hajielewi.

    Baada ya kufanya hivyo kijana huyo alijichukulia mzigo kiulaini na kwenda kuutumia jinsi alivyotaka. Lengo lake lilikuwa ni kufanya mapenzi na Anna, kweli alifanikiwa japokuwa Anna alikuwa hajitambui.

    Tukio hilo lilimuumiza sana kipenzi changu. Hata hivyo wakati huo mimi nilikuwa masomoni hivyo hakuweza hata kupata faraja kutoka kwangu. Miezi miwili baadaye tulifunga shule. Ndipo niliporudi nyumbani na kukuta habari za kubakwa kwa Anna ambazo ziliurarua moyo wangu.

    Tunu ya usichana wa Anna ambayo alikuwa ameitunza kwa ajali yangu ilikuwa tayari imeshahujumiwa. Hakuwa bikira tena. Iliniuma sana kusikia hivyo. Hata hivyo sikutaka kuukatisha uhusiano wetu kwa sababu ya hilo, nilimwambia kuwa tutakuwa pamoja licha ya kwamba tunu yangu ilikuwa imeshahujumiwa.

    Ndipo nilipomshauri aende kuangalia afya yake huenda siku hiyo alipata maambukizi ya virusi vya UKIMWI. Naye bila ubishi alienda, hata hivyo majibu yalikuwa safi.

    Siku kadhaa zilipita. Nikiwa sijui hili wala lile nilipokea taarifa za kifo cha Anna, taarifa ambazo zilizidi kuuchoma moyo wangu.

    Taarifa hizo zilisema kwamba Anna alikuwa amekufa baada ya kufanya jaribio la kutoa mimba. Niliposikia hivyo nilijua moja kwa moja mimba hiyo iliingia siku ile alipobakwa na yule kijana.

    Ndipo nilipozidi kuumia na kujihisi mpweke zaidi ya kinda lililoachwa na mama likabaki peke yake kwenye kiota. Huo ndiyo ulikuwa mwisho wa maisha ya Anna kwa hapa duniani ingawa mpaka leo moyoni mwangu yu hai.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Tukio hilo liliniacha na kidonda kikubwa sana ndani ya moyo wangu. Mpaka nakuja kuondokewa na kaka yangu kidonda hicho kilikuwa hakijapata hata dalili za kupona, kikawa kimegongomewa msumari mwingine tena mkubwa zaidi.

    Aliyekuwa mstari wa mbele kunifariji juu ya machungu ya kuondokewa na Anna naye alinitoka, tena kwa kifo cha ghafla ghafla huku nikimshuhudia wakati roho inaachana na mwili wake. Hakika lilikuwa ni pigo mjaarabu.

    Huku nikiwa na majonzi yangu tele moyoni niliendelea kulisongesha huku nikipata faraja kutoka kwa majirani na rafiki zangu wa karibu, faraja ambayo hata haikukidhi mahitaji ya upweke uliokuwepo ndani ya moyo wangu.

    Kitu kingine ambacho kilianza kuniacha hoi ni hizo mali zilizokuwa zimeachwa na kaka James. Nilizidi kuchanganyikiwa kwa jinsi zilivyokuwa zikipukutika na kuisha bila kuelewa zinaishaje.

    Biashara zote zikawa haziendi. Nikienda kwenye maduka mauzo yalikuwa mabovu, kampuni ya usafirishaji nayo ikazidi kufilisika siku hadi siku. Ajali za mara kwa mara zikawa zinatokea kwenye malori ya kusafirisha mizigo kwanye kampuni hiyo. Nilizidi kuchoka.   

    Baada ya kuona mambo yanazidi kwenda kombo niliamua kuanza kupiga bei mali moja baada ya nyingine. Nilianzia kuuza nyumba aliyokuwa kahongwa Neila, mwanamke aliyepigwa risasi na kaka James.

    Mara baada ya kuiuza nyumba hiyo, niliyatangazia dau magari mawili ya kifahari yaliyokuwa yameachwa na kaka James. Gari moja ni lile alilohongwa Neila; mwanamke aliyekuwa akijidai ana mapenzi ya kweli kwa kaka James kumbe hamna chochote. Mwanamke ambaye alisababisha kifo cha kaka yangu huyo.

    Gari la pili ni lile alilokuwa akitumia kaka James. Yote yalikuwa ni magari ya kifahari. Nilibakiza gari moja ambalo nilikuwa nalitumia mimi. Hilo sikutaka kuliuza.

    Ndani ya miezi sita nilikuwa nimeshauza kila kitu; maduka, nyumba pamoja na kampuni ya usafirishaji. Lengo langu lilikuwa ni kuhama kabisa mji huo.

      Nilipomaliza michakato yote nilihama mji huo na kuhamia mji mwingine ambako nilienda kununua nyumba na kuendelea na maisha kama kawaida. Nilianza kufanya biashara zangu huko.

    Nyumba hiyo ilikuwa kubwa mno kukaa peke yangu kwani nilikuwa bado nahisi upweke kutokana na kuondokewa na nguzo yangu muhimu katika dunia hii.

    Ndipo nilipoamua kukipangisha chumba kimoja na mpangaji aliyekuja kupanga alikuwa ni marehemu Kishoka. Alikuwa ni kijana mstaarabu sana ambaye hakuwa na makuu.

    Maisha yetu yalizidi kuwa ya furaha kadri siku zilivyozidi kusonga. Tukawa tunaishi kama ndugu wa damu ilhali tulikuwa tumekutana ukubwani tu kila mmoja akiwa na meno thelethini na mbili.

    Kiumri tulikuwa hatupishani sana japokuwa alikuwa ananizidi miaka mitatu. Nilipomuita kaka naye aliniita kaka. Pamoja na kunizidi umri lakini na mimi nilikuwa mwenye nyumba wake.

    Ilifikia wakati nikamwambia asiwe ananilipa kodi ya nyumba kwani urafiki wetu ulikuwa umefikia hatua nyingine. Akawa anaishi bila kulipa kodi ya pango siku zote.

    Mpaka matatizo ya kifo chake yanatokea tulikuwa tunaishi naye kama ndugu, kifo ambacho kilikuja kikanigharimu hukumu ya kunyongwa nikisingiziwa kuwa mimi ndiye niliyemchinja.

    Nilizidi kuchanganyikiwa kwa kuona maisha yangu yakiandamwa na mikasa, mikosi na ndege mbaya kila wakati. Kichwa kilizidi kuuma.



    Maisha ya gerezani yalizidi kusonga huku nikiwa nasubiri siku yangu ya kutundikwa kwenye kitanzi ifike, siku ambayo nilikuwa sijui tarehe yake, mwezi wala mwaka wake.

    Huko gerezani nilishangaa sana kumkuta jamaa mmoja ambaye nilikuwa namfahamu. Jamaa huyo ni yule niliyekuwa nimemuuzia nyumba aliyokuwa kahongwa Neila, mwanamke aliyeuliwa na James baada ya kumuonyeshea utapeli wa mapenzi na nyodo za kila aina.

    Nilishangaa sana kumkuta jamaa huyo aliyekuwa anajulikana kwa jina la Mack. Alikuwa kakaa gerezani kwa muda mrefu kiasi kwani alikuwa kashapewa mpaka unyapara wa humo gerezani.

    “Kulikoni tena ndugu yangu na wewe umeletwa huku?” Lilikuwa ni swali la Mack siku ya kwanza kabisa kuingia jela mara baada ya kuniona.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Matatizo makubwa ndugu yangu, hapa nilipo sina hata hamu! Na wewe lini tena humu na kipi kilichopelekea kuletwa sehemu hii isiyofaa?” nilimuuliza nikiwa na shauku kubwa ya kujua kilichokuwa kimemsibu.

    Kabla ya kunijibu aliguna kisha akavuta pumzi ndefu na kisha  kuzishusha.

    “Ni stori ndefu mdogo wangu, hebu anza kwanza wewe kunieleza mkasa uliokusibu mpaka ukaletwa humu.”

    Niliamua kuanza kumsimulia jinsi mambo yalivyokuwa. Nikamweleza kinaga ubaga, hatua kwa hatua tangu kipindi nahama mji tuliokuwa tunaishi na kaka James.

    Wakati namsimulia alikuwa katulia tulii huku akinisikiliza kwa umakini mkubwa. Nilipomaliza nikamuachia naye aweze kufunguka. Alianza kwa kusema,

    “Kisanga chako hakina tofauti sana na kile kilichonitokea mimi.” Alitulia kidogo kumeza mate.

                Nilishtuka sana baada ya kusikia hivyo. Nikawa na hamu ya kusikia mambo yalivyokuwa huko. Aliendelea kuniambia kuwa mara baada ya kumuuzia nyumba ile alihamia. Akawa anaishi pale yeye na familia yake ambayo ilikuwa na jumla ya watu watatu, yaani yeye mwenyewe, mke wake na mtoto wake mmoja.

                Kabla hajamaliza hata mwezi kuna msichana alijitokeza na kumtaka ahame pale akidai kuwa nyumba ile ni yake. Baada ya kuambiwa hivyo hakutishika kwani ushahidi wote wa kuonyesha kuwa nyumba ile ni mali yake ya halali alikuwa nao.

                Mwanadada huyo alizidi kumwandama kwa kumtisha na vitisho kedekede. Pamoja na vitisho hivyo Mack aliendelea kukaidi madai ya mwanadada huyo.

                “Huyo msichana ulikuwa unamfahamu kabla?” Nilimtwanga swali hilo nikiwa najaribu kudadisi juu ya msichana huyo.

    “Hapana! Nilikuwa sijawahi hata kumuona kabla ya hapo.” Mack alinijibu kama hivyo.

    “Alisema yeye ni mwenyeji wa wapi?” Niliuliza tena.

    “Alidai kuwa ni mwenyeji wa palepale mjini mtaa wa Matopeni. Lakini mimi niliona ni muongo kwani Matopeni nilikuwa mwenyeji kidogo na nilikuwa sijawahi kuona sura kama yake.”

                Niliona niachane na kuuliza uliza maswali kwani yalikuwa yanakatisha uhondo wa stori yenyewe. Nikamuacha Mack aendelee kunipa michapo hatua kwa hatua.

    Aliendelea kueleza kuwa baada ya kukaidi mwanamke huyo hakuchoka kumghasi akimwambia ahame katika nyumba ile.

    Baada ya Mack kuona kero imezidi aliamua kulipeleka shauri hilo kwenye uongozi wa serikali za mtaa ili wamsaidie kuipata suluhu. Alipowaeleza viongozi hao walimwambia aende na mlalamikaji huyo ili wakapate kuyasikiliza malalamiko yake.

    “Nikaenda kumtafuta mtaa wa Matopeni lakini sikufanikiwa kumuona. Kila niliyemuuliza alisema hamfahamu.” Alisikika Mack akiniambia.

    Sikutaka kutia swali katika maelezo yake, nikachombeza tu kwa kumwambia aendelee, naye akaendelea.

    “Baada ya kumkosa nilirudi nyumbani. Nikaamua kumsubiri atakapokuja nimkamatishe na kumpeleka kwenye ofisi za serikani za mtaa.”

                Huku nikimsikiliza lakini kwenye ubongo wangu kulikuwa na mjadala mzito uliokuwa ukiendelea. Suala la kulifahamu jina la msichana huyo ndiyo lilikuwa nimetawala kwenye akili yangu. Mawazo yangu yote yalikuwa yananituma kuwa piga ua galagaza yule msichana alikuwa ni Sharifa, msichana aliyenisababishia matatizo ya kupatikana na hatia ya kuua wakati sijaua.





    Pale pale nikajishauri kuwa nimkatishe Mack kwa kumuuliza swali tena kwani kuuliza ilikuwa siyo dhambi na nilikuwa sijakatazwa. Ndipo nilipomuuliza kuwa msichana huyo alijitambulisha kwa jina gani.

                “Alisema kuwa anaitwa Sada, mwenyeji na mzaliwa wa Matopeni ila wazazi wake walikuwa wameshafariki kwa kipindi hicho.” Hilo ndilo lilikuwa jibu la Mack kwa swali nililokuwa nimemuuliza, jibu ambalo lilianza kunitoa katika hisia zangu juu ya msichana huyo.

                “Alikuwa yukoje yukoje kimuonekano?” Nilizidi kudodosa nikidhani ya kuwa huenda alikuwa kabadilisha tu majina.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Alikuwa ni mwembamba halafu kaenda hewani kimtindo, mweupe na mwenye mwanya. Akiwa anaongea sauti yake ilikuwa nzito kiana.” Alidadavua Mack.

    Jibu hilo pekee lilitosha kuitengua hoja iliyokuwa imejengeka akilini mwangu ya kwamba mwanamke huyo alikuwa ndiyo Sharifa. Nilimuacha Mack aendelee kunipa michapo labda kwa baadaye ningeweza kung’amua kitu kuhusu mwanadada huyo.

    Aliendelea kunielezea. Akasema kuwa baada ya siku mbili kupita mwanamke huyo alijileta mwenyewe kwa Mack akija kumwambia anampa onyo la mwisho, kama hatahama vitendo vingefuata.

    Mack alitaka sana kuumaliza mgogoro huo kwa njia ya amani akiamini kabisa kuwa yote yanawezekana kwa nguvu ya hoja. Alimsihi mwanadada huyo waende kwenye ofisi za serikali ya mtaa ili wakaliongelee shauri hilo.

    Hata hivyo mwanamke huyo alimjibu kwa nyodo nyingi akisema kuwa hana muda mchafu wa kwenda kuonana na hao viongozi wa serikali za mtaa. Siyo muda peke yake, hata hadhi yake ilikuwa siyo ya kwenda kuvimbisha tumbo lake mbele ya watu kama hao aliowaita majuha.

    Mack aliyapeleka majibu hayo kwa hao viongozi, nao wakamwambia ya kuwa asubiri hatua atakayochukua mwanamke huyo huku wakiahidi kuwa mstari wa mbele kumtetea.

    Wiki moja baada ya hapo kioja kilitokea nyumbani kwa Mack. Wakati anatoka kwenye mihangaiko yake ya kila siku, alikutana na askari polisi waliokuwa wakimsaka kwa udi na uvumba. Walipompata walimweka chini ya ulinzi wakimwambia ametoka kuua mtaa wa Matopeni.

    Alishangaa sana kusikia hivyo, akawaambia kuwa yeye hajaua. Wakamwambia kuwa ameua kwani nyumba aliyokuwa ameenda kufanya tukio hilo ilikuwa na kamera maalum za kunasa wezi na wahalifu mbalimbali.

    Alipouliza kamuua nani akaambiwa kuwa kamuua mwanadada mmoja aliyekuwa akijulikana kwa jina la Sada, mwanamke aliyekuwa akiishi katika mtaa wa Matopeni.

    Mack aliendelea kubisha. Askari hao wakaanza kupekua kwenye gari lake. Katika pekua pekua waliona bastola ndani ya gari la lake, kitu ambacho kilikuwa ni kigeni kabisa kwake.

    Kiukweli alikuwa hana bastola na alikuwa hajawahi kumiliki siraha kama hiyo katika maisha yake, hata kule kuishika masikini wa Mungu alikuwa hajawahi. Cha ajabu sasa ilipatikana, tena ndani ya gari lake. Alizidi kuchanganyikiwa.

    Askari waliendelea kueleza kuwa kwenye kamera hizo Mack alianza kuonekana tangu anafika kwenye nyumba ya Sada na zilikuwa zimerekodi tukio zima.

    Kati ya askari waliokuwa wamemkamata mmoja alikuwa akimfahamu, hivyo baada ya kuiona picha yake kwenye kamera hizo akawa amemtambua.

    Habari hiyo ilikuwa ni ngeni kabisa kwa Mack. Aliwaeleza askari hao kuwa yeye hakuua ingawaje kweli alikuwa katika mgogoro wa nyumba na huyo Sada. Alizidi kujitetea kuwa hata nyumbani kwake (yaani kwa Sada) alikuwa hapafahamu kwani siku moja alienda kumtafuta ili waende kwenye ofisi za serikali ya mtaa kuuongelea mgogoro wao lakini hakufanikiwa kumpata msichana huyo.

    Pamoja na kujitetea kote huko, Mack aliambulia kuwekwa chini ya ulinzi na kupelekwa kwenye kituo cha polisi cha kati. Alikaa hapo kwa siku moja na nusu kisha jalada la kesi yake likapelekwa kwenye mahakama ya hakimu mkazi



    Alipopandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza alisomewa mashtaka kisha akatakiwa kutojibu chochote kwani mahakama hiyo ilikuwa haina uwezo wa kusikiliza kesi kama hiyo, yaani kesi ya mauaji.

    Aliendelea kukaa rumande wakati taratibu za upelelezi wa kesi yake zikiwa bado hazijakamilika. Jalada lake lilipokamilika kesi yake ilihamishiwa kwenye mahaka kuu.

    Kesi iliendelea kurindima. Kitu kilichomuacha hoi Mack ni yule shahidi namba moja wa kesi hiyo ambaye alijitambulisha kuwa ni mume  wake na Sada, yaani mwanadada aliyekuwa ameuawa.

    Mack alishangaa kumuona shahidi huyo ndiye jamaa aliyekuwa ameuliwa na kaka James kwa kupigwa risasi baada ya kumkuta na Neila ambaye alikuwa ni mpenzi wake (yaani kaka James). Kijasho chembamba kilianza kumtoka.

    Jamaa alitoa ushahidi wake akidai kuwa siku ya tukio alikuwepo na alimshuhudia Mack wakati anafanya mauaji.

    Kilichozidi kumchanganya Mack na ndiyo hicho hicho kilichokuwa kinazifanya kesi zetu ziwe mapacha ni ushahidi wa ule mkanda uliorekodiwa na kamera maalum za nyumba hiyo ukionyesha mwanzo mpaka mwisho wa tukio.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mack hakuua. Tena maskini wa Mungu alikuwa haijui hata hiyo nyumba aliyokuwa akiishi mwanamke huyo. Ni sawa kweli alikuwa na wenyeji kidogo kwenye mtaa wa Matopeni, lakini alipokuwa akikaa Sada alikuwa hapajui na ndiyo maana alichemsha kumpata siku alipoenda kumtafuta.

    Yale yale kama yaliyotokea kwangu, kuonekana alama za vidole vyangu kwenye mwili wa Kishoka na kwenye kisu wakati sikuwahi hata kuvigusa. Tena hiyo ni tisa, kumi kuonekana picha zangu kwenye kamera nikimchinja Kishoka wakati sikuhusika abadani!

    Mwisho wa siku Mack alihukumiwa kunyongwa mpaka afe kwa kosa la kumuua Sada kwa kukusudia. Hivyo ndivyo stori ilivyoenda kwa mujibu wa maelezo yake.

    Nilivuta pumzi ndeefu kisha nikaishusha baada ya kumaliza kusimuliwa simulizi hiyo na Mack mwenyewe.

    “Mbona kama kuna zengwe fulani hivi kwenye mirathi ya kaka James? Maana mambo yanayotokea siyaelewielewi!” Nilitamka maneno hayo nikimwambia Mack.

    “Na hayo matatizo siyo kwetu sisi peke yetu tu, takribani watu wote uliowauzia mali za huyo marehemu kaka yako wamepatwa na matatizo!” Alisikika Mack na kuzidi kunipa mpasuko wa moyo.

                Sasa moyo wangu haukuwa na amani tena. Niliishiwa nguvu mithili ya mtu anapoletewa msiba wa mtu ampendaye kwa dhati. Hata hivyo hamu ya kutaka kujua kilichojiri kwa wateja wangu hao ilizidi kunifukuta.

                “Mungu wangu! Ni matatizo gani yaliyowapata?” Nilijikuta nikiuliza kwa mshangao mkubwa.

    “Yule jamaa uliyemuuzia ile kampuni ya usafirishaji hayupo tena duniani.”

    “Wewe! Kunesa alishafariki? Ilikuwaje?” Nilijikuta nikizidi kuchanganyikiwa huku nikiuliza maswali dabodabo.

                Mack alianza kunieleza yaliyojiri huko moja baada ya jingine. Alianza na habari za huyo Kunesa, jamaa niliyekuwa nimemuuzia kampuni ya usafirishaji niliyokuwa nimerithi kutoka kwa kaka yangu.

                Alinieleza jinsi kifo cha Kunesa kilivyokuwa. Japokuwa hata yeye hakuwepo huko wakati kifo hicho kinatokea ila alisimuliwa na baadhi ya ndugu na jamaa zake waliokuwa wakienda kumuona pale gerezani.

                Alieleza kuwa Kunesa alikutwa kafa kwenye ofisi yake. Alikuwa kachinjwa huku kichwa kikiwa mbali na kiwiliwili chake. Aliyefanya tukio hilo hajajulikana mpaka wa leo.

                Nilipouliza watu wengine waliokumbwa na matatizo nikaambiwa ni wale jamaa waliokuwa wameyanunua yale magari. Waliyakuta magari yanawaka moto yenyewe kwa nyakati tofauti na chanzo cha moto huo wala hakikujulikana. Habari hizo zilizidi kunipa wasiwasi mkubwa juu ya mali za kaka James. Nikazida kujiuliza kulikoni kuhusu hizo mali.

                Walionunua maduka walifilisika wote, maduka yaliisha na kubakia matupu kabisa. Nilianza kuwaza endapo watu hao wangeamua kunitafuta sijui wangenifanya nini!

                “Na wewe umefikaje kwenye gereza hili wakati hata huko mahakama kuu ipo pamoja na magereza ya kutosha kabisa.” Niliona nimuulize Mack swali hilo lililokuwa linanitatiza tangu nilipomuona tu.

    “Afya yangu ilianza kuwa mgogoro mara baada ya kufungwa. Ndipo daktari wa hospitali ya gereza hilo akashauri kwamba nihamishiwe gereza jingine akidai kuwa hali ya hewa ya pale ilikuwa imenikataa. Ndipo nilipoletwa huku.”

                Kwa kweli zilikuwa ni habari nzito za kutisha na kusikitisha. Nilianza kujiona kuwa ni muuaji kwani mtu kama Kunesa nilihisi kuwa nina mchango mkubwa mno juu ya kifo chake, ukizingatia nilimbembeleza kuinunua hiyo kampuni baada ya kukosa mtu wa kuinunua.

                Hiyo ilikuwa ni siku ya kwanza kukutana na Mack, siku ambayo ndiyo kwanza nilikuwa nimetoka mahakamani kuhukumiwa.



    Suala la kuandika barua kwa rais ndiyo lilikuwa limetawala katika kichwa changu. Hiyo ndiyo fursa pekeee iliyokuwa imebakia ya kujaribu kujitetea, si unajua tena mfa maji haishi kutapatapa.

                Rais anao uwezo wa kumsamehe mfungwa wa mauaji endapo ataandika barua kuelezea ambavyo haki haikutendeka katika hukumu yake kwa mujibu wa sheria za nchi yetu naye akajiridhisha na sababu hizo.

                Wazo hilo alinipa Mack, akaniambia unaweza ukamwandikia barua rais na kumweleza jinsi mazingira ya kesi yako yalivyokuwa. Kama akiridhika na maelezo yako anaweza akakuachia ukawa huru.

                Wazo hilo nililiafiki na kulipokea kwa mikono miwili. Nikaandika barua na kuikabidhi kwa mhusika gerezani hapo ambaye alifanya harakati za kuipeleka kwa mheshimiwa rais. Nilijipa matumaini kuwa huenda mheshimiwa ataridhika na malalamiko yangu na kuniachia huru.

                Siku zilizidi kukatika bila kupata majibu yoyote. Miaka kadhaa ilipita nikiwa gerezani kusubiri siku za adhabu yangu ya kunyongwa. Ilibidi nikubaliane na hali halisi ya kwamba kifo changu kitakuwa cha kupigwa kitanzi.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

                Hayawi hayawi hatimaye yalikuwa. Siku moja nikiwa sina hili wala lile niliitwa na kuambiwa masaa yangu yalikuwa yanahesabika. Yaani namaanisha siku yangu ya kupigwa kitanzi ilikuwa ndiyo hiyo.

                Nilipelekwa kwenye chumba kimoja ambako niliambiwa nitakutana na mtumishi wa Mungu ili anihubiri na kuniombea pia. Kama ningetaka kutubu dhambi zangu huo ndiyo ulikuwa ni muda muafaka.

    Nilijikuta mwili ukinyong’onyea ghafla kwa hofu ya kifo. Usiombe kuijua siku na saa unayokufa.

                Wakati naukanyaga mlango wa chumba hicho nilimuona mwanamke aliyekuwa kainama chini akisomasoma kitabu. Niliambiwa huyo ndiye mtumishi wa Mungu na nilipewa masaa kadhaa ya kuongea naye kabla sijapelekwa kwenye chumba cha kunyongea.

                Mwanamke huyo alionekana kuwa bado yungali msichana. Hata hivyo mpaka nakaa nilikuwa bado sijaiona sura yake kutokana na sababu kuu mbili; sababu ya kwanza ni kutokana na yeye kuwa ‘busy’ na kusoma kitabu na sababu ya pili ni kutokana na machozi kunifumba macho kwani nilikuwa nikilia kilio cha kimya kimya. Hicho huitwa kilio cha ng’ombe; kilio cha kutoa machozi bila ya kutoa sauti.





    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog