Search This Blog

Thursday, 2 June 2022

MIRATHI YA KAKA - 5

 







    Simulizi : Mirathi Ya Kaka

    Sehemu Ya Tano (5)



    Mara baada ya kuketi mwanamke huyo aliinua kichwa chake, mbona nilizidi kuchoka! Niliweza kumtambua barabara. Huwezi amini ndugu msomaji mwanamke huyo alikuwa ni Sharifa, mwanadada aliyenisingizia kuwa nimeua kisha akaonyesha ushahidi wa picha na kunifanya nihukuniwe kunyongwa.

                Baada ya kumuona hasira zilinijaa ghafla, nikasema potelea pote lolote na liwe, hakuna cha maungamo wala nini. Moyo wa kulipa kisasi ulinijaa mtoto wa kiume, nikatamani nimraruwe mle mle kwenye chumba hicho ili hata kama ninanyongwa na yeye awe ameshakufa.

                Hata hivyo nilipiga moyo konde na kujishauri nitulize munkari na kuzizuia papara zangu ili nimsikilize ananiambia nini.

                Aliniangalia kisha akaachia bonge la tabasamu. Hapo ndiyo niliweza kuuona uzuri wake ulivyokuwa wa shani, mtoto masharah alikuwa kamili kila idara.

                Hata hivyo sikutishika na tabasamu lake hilo kwani nilijua wazi kuwa tabasamu hilo lilikuwa ni la kinafiki. Nikazidi “kumlia buyu” nikisubiri aanzishe yeye mjadala.

    Alikuwa katupia suti ya kike rangi nyeusi huku macho yake yakipendezeshwa na miwani midogo iliyokuwa imemkaa kisawasawa.

    “Sharifa, leo hii wewe ndiyo mtumishi wa Mungu?” Niliamua kumuuliza bila woga baada ya ukimya mrefu kidogo kutawala.

    “Tulia Brighton na unisikilize kwa makini.” Sauti nyororo ya msichana huyo ilipenya kupitia kwenye ngoma za masikio yangu, sauti ambayo ilinikumbusha ufukweni siku niliyoanza kabisa kukutana naye.

                “Hivi unajua ni kwa nini matatizo yote hayo yamekuaandama?” Alinihoji huku nami nikiwa makini kumsikiliza.

    “Sijui labda uniambie wewe kwa maana umeonekana kuyasakama sana maisha yangu.” Nilijibu kwa mkato na kukaa kimya.

    “Chanzo cha matatizo hayo yote ni mirathi ya kaka yako James.”

    “Mirathi ya kaka yangu James! Imefanya nini?”

    “Ujio wangu siyo kuja kujadili chanzo cha matatizo yako, ila nilikuwa nakutaarifu tu ili ukae unajua.”

    “Kwa hiyo umekuja kufanya nini?” Nilizidi kumtwanga maswali bila woga wowote.

                “Lengo la mimi kuwa hapa ni kuja kukuokoa na adhadu ya kunyongwa kama utakuwa tayari kutekeleza masharti nitakayokuambia.”

    “Masharti yapi hayo?” Nilihohoji huku hisia za wokovu wa chupuchupu nikizitazamia.

                Hata hivyo kazi ilikuwa kwenye hayo masharti. Ingawa alikuwa hajaniambia ila nilihisi yangekuwa magumu mno.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Huhitaji kuyajua kwa sasa hayo masharti, kama upo tayari nikuokoe sema.” Aliongea Sharifa na kuzidi kuniweka katika wakati mgumu.

                Akili yangu ilikuwa ikizunguka kama korona kwa wakati huo huku nikiwaza na kuwazua ni uamuzi gani nichukue, lipi nishike na lipi niache.

                Kibaya zaidi nilikuwa sijaambiwa masharti nitakayopewa, hapo ndiyo nilizidi kuchanganyikiwa. Kuendelea kuishi nako nilikuwa bado nakutamani, isitoshe kufa kwa kunyongwa nako kulikuwa kukinitisha.

                ‘Hii ni bahati ya mtende nisiiachie Brighton mimi. Hayo masharti nitahangaika nayo mbele kwa mbele, kikubwa ni kwamba niwe nimeokoka na adhabu ya kunyongwa. Yakienda kunishinda si nakataa tu, atanifanya nini wakati gerezani tayari kashanitoa?’ Niliwaza kimoyomoyo huku nikionekana kuukubali msaada wa Sharifa.

                Nilitulia kidogo kama nawaza kitu fulani kwa kina, ghafla niligutushwa na sauti ya Sharifa iliyokuwa ikiniambia nifanye maamuzi yangu haraka kwani nilikuwa namchelewesha.

                “Sawa nimekubali niokoe” Nilijikuta najiropokea tu wala nilikuwa sijakamilisha sawasawa.

                Baada ya kuongea hivyo nilimuona Sharifa akitoa tena tabasamu lake la ukweli, tambasamu ambalo nilikuwa nikilifurahia kila alipolitoa. Aliinuka kwenye kiti alichokuwa amekaa kisha kitabu alichokuwa nacho mkononi akakitumbukiza kwenye mkoba wake aliokuwa nao. Akaja upande niliokuwa nimekaa, akaniambia nami niinuke. Nilipoinuka akanishika mkono na kuniambia tuondoke zetu.



      Mlango wa chumba kile ulikuwa umefungwa. Nilishangaa kuona tunapenye kwenye ukuta kama vile tunapita sehemu yenye uwazi.

                Tuliendelea kutembea kwa hatua za madaha huku akiwa amenishika mkono. Tulitokezea mpaka nje ya jengo tulilokuwemo. Tukaendelea kutembea kuelekea kwenye lango kuu la kuingilia kwenye magereza hiyo.

                Niliweza kuwashuhudia askari magereza wakizunguka zunguka na wengine wakiwasimamia wafungwa waliokuwa wanafanya kazi kwenye ngome ya gereza hilo.

                Katika fikra zangu nilijua kuwa kila mtu anatuona, nikaona nimuulize Sharifa,

    “mbona tunatoka kwa kujiamini hivi? Hao askari wakituona si tutapata tabu?”

    “Hapa hatuoni mtu yoyote hata tupite palepale aliposimama, labda ngoja nikupe mfano kwa ofisa yule tunayekutana naye.” Alinijibu huku akinionyesha ofisa mmoja tuliyekuwa tunakutana naye.

                Alipomsogelea alimwasha kibao cha haja. Ofisa huyo aliishia kujipapasa tu na hakujua alikuwa kapigwa na nani. Nilianza kucheka kwa kicheko cha chinichini baada ya kukishuhudia hicho kisanga.

                “Hata ukicheka kwa sauti hamna atakayekusikia. Usiwe na wasiwasi upo kwenye mikono salama kabisa.” Aliniambia baada ya kuniona nacheka kwa chinichini.

                Tulitembea mpaka tukafika kwenye geti kubwa. Tulipita bila ya kubughudhiwa na mtu yeyote. Tulipofika nje akaniambia niende mpaka nyumbani kwangu halafu mambo mengine tutayaongea hapo baadaye.

                Nilipojaribu kumuuliza kuwa yeye anaelekea wapi kwa wakati huo aliniambia sipaswi kujua. Nilimuaga na kumshukuru kwa kuniokoa na adhabu iliyokuwa inanikabili kisha nikaanza mdogomdogo kuchapa lapa kuelekea nyumbani kwangu.

                Wakati namuaga alikuwa kasimama barabarani. Nilitembea kidogo kisha nikageuka nyuma kumwangalia. Lahaula! Sikumuona tena.

                Akili yangu ilibaki kuwa na kazi ya ziada japo kuwa nilikuwa nimetoka jela na nimenusurika na adhabu ya kunyongwa. Kikubwa kilichokuwa kinaniumiza akili ni hayo masharti yake. Mpaka muda huo nilikuwa sijajua ni masharti gani atanipa. Kilikuwa ni kitendawili kigumu sana akilini mwangu.

                Nilifuata barabara nikitembea kwa miguu kwani mifuko yangu ilikuwa imetoboka, yaani sikuwa hata na shilingi. Njiani nilikoma na moshi wa magari. Sikuwa na cha kufanya zaidi ya kuyakenulia meno magari yote yaliyokuwa yakinipita kwa vile sikuwa na nauli.

                Safari ya kutoka lilipokuwa gereza nililokuwa nimefungwa mpaka nyumbani kwangu ni mwendo wa masaa mawili kwa miguu. Kibaya zaidi mambo ya kuombana lifti hayakuwepo kabisa katika mji huo. Niliendelea na ‘ba funika ba funua’ mpaka nikafika.

                Nilifika mpaka kwenye geti la fensi ya nyumba yangu, nikajaribu kulisukuma lakini likawa gumu. Kwa kuwa kulikuwa na swichi ya kengele wala sikuhangaika. Nilipeleka mkono wangu panapo swichi, nikabofya kistaarabu kisha nikakaa pembeni kusubiri majibu.

                Punde si punde geti lilifunguliwa. Akatokea jamaa mmoja akiwa kifua wazi.

    “Karibu!” Alisikika jamaa huyo akiniambia.

    “Asante! Habari yako kaka?”

    “Nzuri! Sijui nikusaidie nini?” Alihoji swali hilo ambalo lilinifanya nimshangae.

                ‘Hivi huyu hajui ya kuwa mimi ndiyo mwenye nyumba hii? Au anavyoniona nimekondeana namna hii basi anajua kuwa mimi ni kapuku?’ Niliwaza huku nikiwa ninamwangali jamaa huyo pasipo kummaliza. .

                “Ndugu, sema shida yako nina mambo kibao ya kufanya huko ndani, ila kama unakuja kupiga kibomu kwa mheshimiwa kasafiri, tena hayupo kabisa ndani ya nchi hii.” Alizidi kueleza jamaa huyo.

                Maelezo hayo yalinishtua na kunifanya nianze kupatwa na wasi wasi fulani. Niliyekuwa nimemkabidhi nyumba pamoja na miradi yangu yote alikuwa ni kijana tu kama mimi. Sasa nilizidi kuumiza kichwa uheshimiwa umetoka wapi kwa kijana kama huyo!



    Hata hivyo nilijishauri mwenyewe kuwa kama ningeenda kwenye nyumba hiyo basi ningeonekana kwa watu wengi, na hofu yangu ilikuwa ni kuvuja kwa siri ya kutoroka gerezani.

                Nilijua fika dunia haina siri na walimwengu hawana dogo. Kitendo cha kuniona tu basi wangeanza kuhoji kutaka kujua kulikoni. Watu wengi walikuwa wanajua fika kuwa mimi nilihukumiwa kifo, sasa kuonekana pale mtaani kungeweza kuzua gumzo na kuniletea matatizo mengine tena, huenda ningejikuta nakamatwa na vyombo vya dola.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

                Hata wakati naenda kwenye nyumba yangu hiyo nilienda kwa kujificha ficha sana ili nisionekane kwa watu wa mtaa ule. Lengo langu lilikuwa ni kwamba nifike kwa Mapara na kumwambia tufanye mipango ya kuhama mji huo kinyemera na kuenda katika mji mwingine ambao ingekuwa vigumu watu kunishtukia.

                Akili yangu ilikuwa imenituma kuuza kila kitu kisha kutimkia mji wa mbali ambako ningeweza kuishi kwa raha zangu bila kushtukiwa mpango wangu wa kutoroka jela.

                Sasa kitendo cha kuambiwa Mapara hakuwa anaishi hapo tena kiliichokesha akili yangu mara dufu. Nikawa nawaza cha kufanya bila kupata majibu.

                Jamaa baada ya kuniona nimekaa kimya kirefu nikiwaza kwa kina huku nikipiga miayo mfululizo isiyo na idadi; aliamua kuzama ndani kisha akafunga geti ‘paa!’ Nilibaki pale nje peke yangu nikiwaza na kuwazua bila kupata muafaka wa mawazo yangu.

                Hatimaye niliamua kuchukua maamuzi ya hatari kwani sikuwa na jinsi.

    ‘Potelea mbali kifo hakina breki, ngoja niende hapo hapo alipokuwa kapanga Mapara ili nikajaribu kuulizia kama bado kapanga hapo au la!’ Nilijishauri na kuanza kuondoka.

                Kwa jinsi nilivyokuwa nimekonda ilikuwa ni vigumu sana kwa mtu yeyote aliyekuwa akinifahamu kugundua kwa haraka kuwa ndiyo mimi. Ukizingatia miaka mingi sikuwepo mtaani hapo na pia watu walikuwa wameshanifuta hata katika fikra zao kutokana na hukumu niliyokuwa nimepewa, yaani hukumu ya kunyongwa; basi niliweza kupishana nao kama vile hatujuani.

                Nilienda moja kwa moja mpaka kwenye nyumba alimokuwa kapanga Mapara. Nikaingia mpaka ndani ya nyumba hiyo. Moja kwa moja nilienda mpaka kwenye chumba alichokuwa akikaa.

                Nilipogonga ilisikika sauti ya mwanamke ikiniitikia.

    ‘Huyu jamaa kashavuta jiko nini?’ yalikuwa ni mawazo yangu baada ya kuisikia sauti ya mwanadada huyo.

                Mara mwanamke mrembo alifungua mlango na kutoka kidogo kisha akasimama mlangoni kwa mtindo wa kuegemea mlango. Alikuwa ndani ya kanga tu lakini kanga hizo zilikuwa ni mbili, ya kwanza ilikuwa imeanzia kifuani kuyafunika maziwa na ya pili ilikuwa imeanzia kiunoni.

                Nilimsabahi naye akaitikia. Kilichofuata baada ya salamu ni kumuuliza habari za Mapara.

    “Mh! Mapara, mbona simfahamu?” Alijibu mwanamama huyo aliyekuwa na uzuri wa shani.

                Baada ya kujibiwa hivyo moyo wangu ulishtuka utadhani umepigwa shoti ya umeme. Tumbo likawa joto kwani dalili za mambo kuzidi kuniwia ugumu zilikuwa zinajidhihirisha waziwazi. Wahenga walisema dalili ya mvua ni mawingu, pia mwanzo wa ngoma siku zote huwa ni lele.

                “Kwani wewe siyo mpangaji wa siku nyingi hapa?” Nilimhoji  mama huyo.

    “Ndiyo sina siku nyingi hapa, nina miezi kama mitano hivi tangu kuhamia kwenye hiki chumba.”

    “Ndiyo maana, kwa maana Mapara alikuwa kapanga kwenye chumba hikihiki na  ni muda mrefu umepita tangu nifike kumsabahi.”

    “Labda muulize kaka wa kwenye chumba  kinachofuata kwani huwa nasikia yeye ndiyo mkongwe zaidi hapa.”

    “Sawa, asante kwa msaada wako.”

    “Wala usijali, karibu tena.”

    “Nimekaribia.” Nilijibu kisha nikaondoka kwa hatua za taratibu kabisa mpaka kwenye chumba kilichofuata.

                Kwa adabu zote nilianza kuugonga mlango. Sikujibiwa chochote. Mle ndani kulikuwa na mdundo wa redio uliokuwa ukikita kwa sauti utadhani ni ukumbi wa disko.

                Niliamua kugonga tena kwa kuamini kuwa labda nilipogonga kwa mara ya kwanza hawakusikia kutokana na makelele ya redio. Tena safari hii nililazimika kuukaza mkono ili kuwafanya waliokuwemo humo ndani wanisikie.



    Wakati nagonga wimbo uliokuwa unakita ulifikia mwisho, hapo hapo na mimi nikagandamizia kuendelea kugonga ili nipate kusikika. Kabla wimbo mwingine haujaanza kusikika niliweza kuona mlango ukifungulia. Ndipo alipotoka kijana ambaye nilikuwa namfahamu; alikuwa akiitwa Benja.

                Hata hivyo hakuonyesha dalili zozote za kuweza kunitambua. Nilikuwa nimebadilika si mchezo. Sikuwa kama Brighton wa kipindi kile, enzi hizo kina Mapara na hao kina Benja walikuwa wanapenda kuniita pedeshee mtoto, jina ambalo nilikuwa nalipinga vikali kwani nilikuwa sipendi majisifu.

                Nilipogundua kwamba hajanifahamu nilianza kujiuliza,

    ‘Sijui nimkumbushe, sijui nijikaushe tu ili siri yangu izidi kudumu. Lakini nikijikausha atanipa michapo yote kuhusu Mapara?” Nilizidi kuwaza na kuwazua wakati tukisalimiana.

                Suala la kujikausha ndilo lililopitishwa na halmashauri ya ubongo wangu japokuwa kama angekuwa mgumu kunieleza habari nilizokuwa nazihitaji basi ningejifunua kwake.

                Baada ya salamu mazungumzo yaliendelea,

    “Karibu bwana!”

    “Asante!”

    “Karibu pita ndani.”

    “Asante lakini nipo haste haste kidogo, namulizia Mapara.”

    “Unamuulizia Mapara?”

    “Ndiyo!”

    “Ni nani yako huyo Mapara?”

    “Ni rafiki yangu!”

    “Mara ya mwisho kuonana naye ilikuwa ni lini?”

    “Ni miaka mingi kidogo lakini sikumbuki”

                Maswali ya Benja aliyokuwa akiuliza mfululizo utadhani naye ni polisi yalianza kunikera. Hata hivyo niliona nikianza kumjibu utumbo sitafanikisha nilichokuwa nakihitaji. Nililazimika kuwa mpole kama simba jike anapozaa ili nifanikishe suala langu, suala la kupata habari za Mapara.

                Niliendelea kjitahidi kumjibu kila swali alilouliza.

    “Wewe ni mwenyeji wa wapi?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ni mwenyeji wa mji huu huu ila nilisafiri siku nyingi.”

    “Dah! Huyu Mapara ana miaka mingi sana hayupo nchi hii!”

    “Yupo nchi gani sasa?”

    “Hata mimi sijui ila ninachojua ni kwamba huwezi ukampata mji huu wala nchi hii.”

                Mpaka hapo nilikuwa nimeishiwa maji. Mambo yalizidi kuniwia ugumu baada ya kuambiwa kuwa Mapara alikuwa yupo nchi za ng’ambo.

                Hata hivyo nilijua dhahiri ya kwamba Benja alikuwa ananificha kunieleza habari kamili. Niliamini kabisa kuwa alikuwa anajua mambo mengi sana kuhusu Mapara kwani alikuwa ni mtu wake wa karibu sana.

                Baada ya kuona mambo yamenikaa vibaya sikuwa na budi kunyolewa. Nilimuomba Benja tuingie ndani kwake ili nikamuelezee matatizo yangu kwani nilikuwa na matatizo makubwa.

                Benja hakukataa. Alinikaribisha ndani nami nikaingia. Tulipofika ndani nilimweleza kinaga ubaga bila kumficha kitu chochote kuhusu kesi yangu ilivyoenda, hukumu mpaka kutoroka kwangu siku hiyo ambayo ilikuwa ndiyo siku ya kunyongwa.

                Alistaajabu sana kusikia hivyo.

    “Unajua nilikuwa nakufananisha kwa mbaali lakini nikawa najiambia mwenyewe itawezekanaje mtu aliyehukumiwa kunyongwa aonekane tena uraiani? Na ingekuwa kwa msamaha wa rais basi tungesikia kwenye vyombo vya habari.”

                Kabla hatujaanza hata maongezi yetu Benja aliniambia nimsubiri kidogo, alitoka nje na kwenda sehemu ambapo sikukujua. Huku nikiwa ndani niliendelea kusikiliza nyimbo za mziki wa kizazi kipya ambao niliuacha ndiyo kwanza unachipuka.

                Hata hivyo nilihisi mabadiliko makubwa sana kwenye mziki huo kwani nyimbo zilikuwa na ubora wa hali ya juu kushinda enzi zile bado sijafungwa. Kweli kuwa jela ni sawa na kutokuwa kwenye hii dunia kwani unakuwa hujui kinachoendelea uraiani.

                Baada ya muda usiozidi nusu saa niliona mlango ukifunguliwa, ndipo alipotokea Benja akiwa na kifuko kaning’iniza ambamo kulikuwa na chakula.

                Alinitengea nami nikaanza kula. Kusema kweli nilikuwa na njaa ya kufa mtu. Tumbo nilikuwa likisokota kwa njaa si mchezo. Nilianza kula chakula kilichokuwa kimeletwa na Benja kutoka mkahawani.

                Nilipomaliza kula mazungumzo yalianza. Shauku yangu kubwa ilikuwa ni kusikia habari za Mapara. Hata hivyo kwa wakati huo nilikuwa na uhakika wa kusikia habari zote za Mapara kutoka kwa Benja kwani ukaribu wao ulikuwa ni kama pete na chanda.



    Alianza kwa kunipa pole kwa matatizo yote yaliyokuwa yamenisibu. Baada ya hapo alianza kunieleza habari niliyokuwa naingijea kwa hamu kubwa.

                “Tangu upatwe na matatizo Mapara alikuwa akijitahidi sana kuisimamia miradi yako. Tena ilikuwa ikiendelea vizuri kila kukicha.” Alinieleza Benja.

                Wakati huo nilikuwa makini kusikiliza; hatua kwa hatua, neno kwa neno huku nikiwa na maswali tele kichwani juu ya hatima ya mali zangu baada ya kudokezwa kuwa niliyekuwa nimemwachia dhamana ya kuziangalia na kuzitunza alikuwa katimkia ughaibuni.

                Benja aliendelea kunieleza kuwa baada ya hukumu yangu Mapara alianza kujitapa kuwa mali zote hizo nilikuwa nimemkabidhi. Akawa na jeuri ya pesa kupindukia, si unajua tena baadhi ya watu wanapopata pesa kirahisi rahisi huwa hawana machungu nazo!

                Akawa ni mtu wa ahasa. Wanawake na yeye, tena akawa anawabadilisha kama nguo. Mchana yupo na huyu, asubuhi alikuwa na yule na usiku utamuona na mwingine. Pombe na yeye kila wakati.

                Baada ya kutapanya mali kwa miezi kadhaa uchumi wa miradi yangu ulianza kushuka. Ndipo alipoanza kuuza kila kitu ili atimkie Bondeni kwa mzee Madiba, yaani Afrika ya kusini.

                Alimalizia kwa kuuza nyumba yangu akamuuzia kigogo mmoja ambaye alikuwa ni mbunge. Baada ya kukamilisha uuzaji wa nyumba yangu Mapara alikwea ‘pipa’ na kuishia ‘Sauzi’. Huo ndiyo ulikuwa mwisho wa habari ya Mapara kwa mujibu wa maelezo ya Benja.

                Kichwa changu kilizidi kuwa kizito utadhani kilikuwa kimeng’atwa na manyigu. Sikutegemea kabisa kama Mapara angefanya utumbo kama ule.

                Mpaka hapo mipango yangu yote ilikuwa imechemka, kwa msemo wa vijana wa kileo ilikuwa ‘imebuma’. Niliendelea kupiga miayo mfululizo utadhani sijala siku tatu wakati ndiyo nilikuwa nimemaliza kushindilia sahani ya ubwabwa..

                “Sasa utanisaidiaje rafiki yangu, maana sitaki kabisa kuendelea kuishi kwenye mji huu kwani watu wanaweza wakasanua ishu kuwa nimetoroka jela.” Nilimuuliza Benja kwa sauti ya huruma.

    “Kwa hiyo unataka ukaishi mji upi?”

    “Mji wowote ule ilmradi uwe upo mbali na huu, nchi yetu ina miji mingi tu ambayo shughuli za kiuchumi zinapatikana. Nina imani nikifika sehemu na kutulia baada ya muda fulani mambo yangu yatakaa sawa.” Nilizidi kumweleza Benja.

                Pamoja na kuwa nilikuwa nipo mikononi mwake nikiamini kabisa kuwa shida yangu itafanikiwa, mambo yalizidi kuwa si mambo. Msaada wake ulikuwa si zaidi ya kunihifadhi kwa siku kadhaa ambazo ningekaa kwake. Kuhusu suala la pesa alikuwa ni mtupu.

                Sikushangaa kusikia hivyo kwa kijana huyo kwani tangu sijaenda jela maisha yake yalikuwa yapo vilevile. Pamoja na kukaa miaka lukuki jela bado nilimkuta hajaongeza hata stuli kwenye chumba chake hicho zaidi ya godoro la kulalia na redio kaseti aliyokuwa nayo.

                Hii yote ilitokana na kutojishughulisha katika maisha yake. Si yeye peke yake bali kulikuwa na vijana wengi tu katika mji huo waliokuwa na kasumba ya kukusanyikana kwenye masikani zao tu na kuanza kucheza kamali kutwa nzima.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

                Baada ya kukosa msaada kwa mwenyeji wangu huyo nilikaa kimya kama dakika kumi hivi nikitafakari la kufanya ili kukimbilia kujificha kwenye mji mwingine tofauti na huo. Mapara alikuwa kashaniponza kwa kuyapeleka kombo mambo yangu yote.

                Kabla hatujafikia muafaka juu ya sakata langu, mlango wa chumba cha Benja uligongwa. Moyo wangu ulilipuka ‘lipu’ huku hofu ya kukamatwa ikitanda katika mawazo yangu.

    Naye Benja aliinuka taratibu na kwenda kufungua mlango kidogo kidogo kisha akatoka kumsikiliza aliyekuwa anagonga.

    Sauti ya msichana niliisikia ikimsalimia Benja kisha kumhoji ikimuuliza kama nilikuwemo ndani. Mapigo ya moyo yalizidi kwenda kasi baada ya kusikia jina la Brighton likitajwa, yaani jina langu.

    Ilikuwa hainipi kabisa akilini kwa mtu mwingine yeyote katika mtaa huo au mji kwa ujumla kujua kuwa nilikuwa nimetoka jela. Sasa kitendo cha mtu kuja moja kwa moja na kugonga nilipokuwa nimefikia kisha kuniuliza kilikuwa kimenikosesha kabisa amani moyoni.

    Nilibaki nikiomba kimungu mungu wasije wakawa askari polisi ama wana usalama. Nilijikuta nikiogopa hata kupumua kwa kuhofia mihemo yangu kusikika huko nje ya chumba.

    Mara nilimsikia Benja akimhoji mtu aliyekuwa akiniulizia kuwa ni nani na alikuwa akinitafutia nini. Hata hivyo majibu ya msichana huyo sikuyasikia kwani alikuwa akiongea polepole sana.

    “Huyo Brighton unayemuulizia haishi hapa wala mimi simjui. Kwanza hilo jina ni geni kabisa katika mtaa wetu, kama vipi endelea kuulizia kwa wengine.” Nilimsikia Benja akijibu hivyo.

    Moyo wangu ulifurahi sana kusikia Benja akijaribu kupapatua ili kuokoa maisha ya uhai wangu uliokuwa umebaki. Hata hivyo mabishano makali yaliibuka baina ya mwanadada huyo na Benja.

    Mwanadada huyo alikuwa akidai kuwa ana uhakika wa asilimia mia moja kuwa nilikuwemo chumbani humo huku Benja yeye akikanusha vikali.

    Alirudi ndani haraka huku akiwa na hasira kisha akaufunga mlango kwa kuukomea ili kumkomoa mtu aliyekuwa akileta ubishi pale mlangoni. Sikutaka kumuuliza chochote kwani kama ningeongea basi sauti yangu ingesikika na kisha mpango wetu kubumbuluka.





    Alijitupia kitandani huku akimlaumu mwanamke huyo kwa kuwa mbishi bila sababu. Huku akiwa bado analalama, tuliuona mlango ukifunguka licha ya kukomea wakati anaufunga.

     Pamoja na ubabe aliokuwa nao Benja alijikuta akinywea baada ya kuona mlango unafunguka. Hakuendelea tena kubwabwaja badala yake alibaki mdomo wazi huku hofu na woga vikimjaa.

    Baada ya mlango kufunguka msichana aliyekuwa anabishana na Benja mlangoni aliingia mpaka chumbani. Kumbe alikuwa ni Sharifa, msichana aliyekuwa kanisababishia kufungwa kisha kuniokoa dakika chache kabla ya kunyongwa kitanzini.

    Sasa nilikuwa nimeshaanza kumzoea msichana huyo.

    “Ooh! Sharifa, kumbe ni wewe, samahani kwa yote yaliyojitokeza kwani mwenzio nalazimika kuishi kama digidigi.” Nilimwambia huku nikimlaki kwa kumkumbatia.

                Wakati huo Benja alikuwa aking’aang’aa sharubu tu, nikamtambulisha kwa Sharifa huku tukiwa bado tumekumbatiana. Alishusha pumzi kwa nguvu na kurudi katika hali yake ya kawaida.

                “Mbona unaishi kwa woga na wasiwasi hivi?” Sharifa alinitwanga swali hilo.

    “Naogopa kugundulika kuwa nimetoroka jela, maana jambo hilo tulilifanya tu kwa uwezo wako ila ni la hatari mno.” Nilijibu vile.

    “Wasiwasi wako tu. Hakuna mtu yeyote atakayekuuliza juu ya hilo hata kama uende gerezani hapo hapo.” Aliongea tena Sharifa kunitoa wasiwasi.

                Hata hivyo maneno yake sikuyasadiki hata kidogo ila nilikubali ili yaishe. Nilipomuomba tukae japo pale kwenye godoro ili anisaidie ushauri juu ya suala lililokuwa linaumiza kichwa changu  alikataa. Akasema alikuwa amekuja kunichukua ili tuende kumalizia maongezi yetu tuliyokuwa tumeyabakisha kule gerezani kabla ya kutoroka.

                Nilipomuuliza tunaenda kuongelea wapi aliniambia anajua yeye, nilichokuwa natakiwa kufanya ni kumfuata kokote ambako ataniambia tuende.

                Nilimuaga Benja kisha tukaondoka na Sharifa. Sikuwa na nijualo juu ya safari hiyo.  Tulipotoka nje ya nyumba alimokuwa kapanga Benja tuliingia kwenye gari moja la kifahari ambalo alikuwa amekuja nalo msichana huyo. Safari ya kuelekea nisikokujua ilianza huku dreva akiwa ni yeye.

                Baada kama ya nusu saa tulikuwa tupo kwenye hoteli moja mashuhuri sana mjini hapo. Hoteli hiyo ilikuwa siyo ngeni kwangu japokuwa nilikuwa sijawahi kuingia ndani zaidi ya kuliona jengo lake kwa nje nikiwa napita karibu nayo.

                Wakati tunashuka kwenye gari hiyo mara baada ya kufika hotelini hapo, Sharifa alichukua ‘brificase’ na kushuka nayo akiwa kaishikilia mkononi.

                Sikuelewa kama tayari alikuwa kashalipia chumba au vipi kwa sababu tulipapita mapokezi bila kusimama, tukaenda moja kwa moja kwenye lift. Tulipofika lift ikatupandisha mpaka ghorofa ya saba, tukatembea kwenye korido mpaka kwenye chumba namba 138.

                Tulipofika kwenye chumba hicho Sharifa alifungua mlango kwa kadi maalumu nao ukafunguka kisha tukazama ndani. Chumba kilikuwa matawi ya juu kweli kweli, kila huduma inayopatikana kwenye vyumba vya hoteli kubwa kubwa basi hata humo ilikuwepo.

                Kimawazo nilikuwa mbali sana wakati huo. Akili yangu ilikuwa inazunguka kuwaza ni masharti gani nitapewa na msichana huyo ikiwa ni malipo ya kuniokoa kutoka kwenye kunyongwa kwa kitanzi.

                Mwili wangu ulikuwa umezizima mithili ya mtu aliyetota kwa kunyeshewa mvua. Nilikuwa mdogo kama pilton.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

                Tulipoingia tulikaa kwenye sofa za nguvu, ndipo mazungumzo yetu yalipoanza.

    “Brighton mwana wa David!” Sharifa alichokoza mada kwa kuanza kuniita.

    “Naam!” Niliitikia na kukaa kimya kusikilizia kitachachoongewa.

    “Bila shaka unapenda sana kuwa tajiri, maana umekuwa ni mtu mwenye kujituma na kujishughulisha ukiwa na lengo la kuusaka utajiri! Kweli ama si kweli?”

    “Ni kweli, lakini utajiri ninaopenda mimi ni ule wa kuupata kwa njia za halali zenye kumpendeza Mungu.”

                Baada ya kujibu hivyo nilimuona Sharifa akiangua kicheko cha dharau kisha akaendelea kusema,

    “hayo ni mawazo finyu ambayo hayataleta tija katika maisha yako. Utajiri hauji kwa njia za halali hata siku moja na Mungu hawezi akakuletea utajiri. Tangu lini kitu haramu kikaja kwa njia halali?”

                Kauli hiyo iliniacha njiapanda kidogo. Ikanifanya nirejee kwenye mafundisho ya dini niliyoyapata nikiwa bado kinda wakati huo, mafundisho yaliyozungumzia matajiri wa kale ambao miongoni mwao ni kina Ibrahim na kina Ayubu, mbona wao walikuwa ni wacha Mungu wazuri tu?

                Nikakumbuka tena maneno ya Yesu kristo alipokuwa akiwaambia wanafunzi wake kuwa ni vigumu kwa tajiri kuingia kwenye ufalme wa Mungu kuliko hata kwa ngamia kupenya katika tundu la sindano.

    ‘Je, maneno haya huenda ndiyo yanaashiria anachokisema Sharifa?’ nilimalizia tafakuli yangu kisha nikatoa jibu kuwa si matajiri wote wanaoupata utajiri kwa njia za mkato.

                “Tuendelee!” niliropoka mara baada ya kugutuka kutoka kwenye kuwaza kwa kina.

    “Huo ulikuwa ni utangulizi tu, hivyo kama unataka kuwa mmoja kati ya matajiri wa dunia hii yakubali nitakayokuambia.” Aliongea Sharifa kisha akanyosha mkono wake kuichukua brificase iliyokuwa mezani.





    Aliifungua brificase na kuniambia niangalie. Naam! Ilikuwa imesheheni fedha za kigeni, fedha ambazo zilikuwa zimebanwa katika maburungutu. Nilijikuta nikimeza mate baada ya kuviona vitita hivyo.   

                “Kama utakubaliana na ninachoenda kusema basi matumizi yako kwa siku yatakuwa ya pesa kama hizi.” Mwanadada huyo alizidi kunitamanisha japokuwa nilikuwa sijajua atakachokitaka kutoka kwangu.

                Nilishusha pumzi huku nikiongeza umakini wa kumsikiliza. Nilizidi kuwa katika wakati mgumu kwa kujua kwamba kama nitamuendekeza sana msichana huyo basi pepo ya Mwenyezi Mungu nitakuwa nimeipa kisogo.

                Hata hivyo nilijiambia ngoja kwanza nimsikilize, uamuzi si ulikuwa ni wangu bwana, kama ningetaka kukubali basi ningekubali na kama ningetaka kukataa basi ningekataa.

                “Najua mwanzo ulikuwa ukinichukia sana, hasa hasa pale niliposimama mbele ya mahakama kutoa ushahidi juu ya kesi yako. Lakini sasa hivi hunichukii tena, hasa baada ya kukuokoa kutoka kwenye kunyongwa, uongo?”

    “Ni kweli.”

    “Mateso yote uliyokuwa ukiyapata tangu kifo cha marehemu kaka yako ulikuwa ukitumikia adhabu.”

                Maneno hayo yalinishtua na kunifanya nigutuke.

    “Adhabu! Adhabu kwa kosa lipi? Na kosa hilo nilikuwa nimemkosea nani?” Niliuliza.

    “Kosa hukutenda wewe bali ni kaka yako James.”

    “Alitenda kosa gani kaka yangu?”

    “Usiwe na pupa, nipo hapa kukufunulia kila kitu hivyo nitakueleza siri nzito aliyokuwa nayo kaka yako.”

                Hilo nalo lilikuwa neno; kujua kile kilichokuwa kimejificha nyuma ya pazia wakati wa uhai wa kaka James, nilizidi kuongeza umakini. Kikao chetu kilizidi kutia fora, sasa nikawa na shauku ya mambo matatu. Jambo la kwanza ni shauku ya kujua siri nzito iliyokuwepo kwa kaka James.

                Jambo la pili lilikuwa ni shauku ya kujua masharti ambayo nilikuwa nimeambiwa nitapewa wakati natoroshwa gerezani. Jambi la tatu ni shauku ya kutaka kujua madhara yatakayonipata endapo ningeshindwa kutekeleza masharti hayo.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

                Sharifa alianza kunieleza habari ya kaka James. Habari ambayo iliyaamsha machungu ya moyo wangu, nikahisi maumivu makali yakipenya barabara kunako mtima wa moyo wangu.

                Kaka James alipokuwa anamalizia masomo yake ya kidato cha nne aliambiwa na rafiki yake mmoja kuwa kuna mganga wa kikongo aliyekuwa kaingia nchini. Mganga huyo alikuwa akiwatengenezea watu dawa ya kupata utajiri.

                Kutokana na tamaa za kutaka kupata utajiri, kaka James alimtaka rafiki yake huyo ampeleke kwa mganga huyo ili akatengenezewe dawa ya kuwa tajiri. Ndipo alipopelekwa.

                Alipofika kwa mganga huyo aliambiwa kuwa masharti ya kupata utajiri ni lazima uingie maagano na majini. Maagano hayo yalikuwa ni maagano ya kafara za damu huku yakiwa katika madaraja matatu.

    Daraja la kwanza lilikuwa ni kuwatoa kafara wazazi wako wote pamoja na ndugu yako mmoja wa damu. Ndugu aliyetakiwa katika daraja hili ni mdogo wako, kaka yako ama dada yako. Kama wote hao huna basi mjomba ama shangazi hutakiwa.

    Baada ya hapo utajiri unaanza kwa kasi ya kawaida. Ukishakaa miaka mitano unatakiwa kutoa tena kafara ya mtoto wako wa kwanza pamoja na mama yake kama wewe ni mwanaume. Lakini kama ni mwanamke basi unatakiwa kumtoa mtoto wako wa kwanza pamoja na baba yake.

                Ukishakamilisha kafara za daraja la kwanza na la pili unatakiwa sasa kuhamia kwenye daraja la tatu ambalo kafara yake huendelea mwaka hadi mwaka. Kafara katika daraja hili ni ya mtu yeyote ama awe mfanyakazi wako au anayetumia vitu vyako mfano abiria katika magari yako, mpangaji katika nyumba yako na kadhalika.

                Masharti hayo ndiyo aliyopewa James naye akakubaliana nayo. Siku chake baada ya kuingia kwenye maagano yale ya kishetani wazazi wetu walikufa wote kwa mkupuo katika ajali ya kutisha.



    Habari hii ndiyo iliyonitonesha majeraha yaliyokuwa yamejengeka ndani ya moyo wangu mithili ya donda ndugu. Kuanzia hapo nilianza kumchukia James na kumuona ni shetani mkubwa ambaye alikuwa anastahili kutupwa kwenye moto wa jehanamu.

                Nilijikuta nahukumu wakati maandiko ya Mungu yanatuambia tusikuhumu ili na sisi tusije tukahukumiwa. Niliumia sana nilipoambiwa hiyo habari.

                ‘Ndiyo maana mambo ya kaka James yalianza kuwa safi mara baada ya vifo vya wazazi wetu.’ Niliwaza.

                Wakati huo huo nikakumbuka swali, nikaona nimuulize huyo huyo Sharifa kwani hata yeye alikuwa ni mdau wa kafara hizo.

    “Umesema kafara ya daraja la kwanza inahusisha wazazi wote wawili na ndugu mmoja wa damu, mbona sasa baba yangu alikufa wakati hakuwa baba wa kumzaa James?”

    “Kwa kuwa alikuwa kamuoa mama mzazi wa James na pia alikuwa na mapenzi ya baba kwake, basi kafara yake ilifana.” Alijibu Sharifa.

                Akaendelea kunieleza kosa la James lilikuja kutokea baada ya kutakiwa kutoa kafara nyingine ili kukamilisha kafara za kwenye daraja la kwanza. Hapo alitakiwa ndugu yake wa karibu; mdogo mtu, kaka mtu, shangazi ama mjomba.

    Kwa bahati mbaya sana ndugu wa damu aliyekuwa yu ngali hai nilikuwa ni mimi peke yangu. Aliamua kukaidi kunitoa kafara kutokana na mambo mawili.

    Jambo la kwanza ni upendo uliokuwepo baina yangu na yeye. Kusema kweli kaka James alikuwa ananipenda kupita kiasi, na ndiyo maana hakuwa tayari kunitoa kafara.

    Jambo lingine lililomsababisha kaka James agome kunitoa kafara ni kwamba hapakuwa na ndungu mwingine wa karibu zaidi yangu mimi. Kama angenitoa kafara basi angebaki bila ndugu wa karibu katika dunia hii. Sasa kubaki bila ndugu wa karibu lilikuwa ni jambo gumu sana kwake.

    Nadhani hata wewe mpenzi msomaji usingepata fursa ya kusimuliwa simulizi hii nzuri iliyojaa vitisho vya lejaleja na yenye kusisimua kwani ningekuwa tayari nimeshalala mauti.

    Baada ya kuona kunitoa kafara haiwezekani, James aliacha kabisa kwenda kwa mganga aliyekuwa amemfanyia dawa ya kumpa utajiri huo wakati alitakiwa awe anaenda mara moja kwa mwezi kufanya ibada. Muda wa kukamilisha kafara ya daraja la kwanza ulipita huku akiwa hajakamilisha, akaongezwa muda wa ziada nao ukawa umepita.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mganga alipoona James kapuuzia agano hilo aliamua kumripoti kwa wataalamu wake ambao ndiyo waliokuwa wanamwezesha kufanya uganga huo.

    Wataalamu hao walikasirishwa sana na kitendo  chake cha kujifanya mjanja na mwenye akili kuzidi wao waliokuwa wamempa maagizo yale. Ndipo walipoamua kumtoa duniani kwa staili ya kujiua mwenyewe ili akaonekane ana dhambi hata mbele za mwenyezi Mungu. 

    Japo kabla ya kutoa adhabu hiyo walitoa muda wa kutosha kwake wakitegemea labda angejirudi na kukamilisha agano lao, siku zilizidi kwenda bila ya mabadiliko yoyote ya kutaka kujirudi kwa James.

    Tena alipoona kakaa muda mrefu bila kupatwa na matatizo yoyote ilhali alikuwa hajakamilisha kutoa kafara alijua kuwa huenda zile zote zilikuwa ni danganya toto tu na vitisho visivyokuwa na misingi yoyote. Baada ya muda wa nyongeza kuisha uhai wa James ukawa ni halali ya wataalamu hao.

    Hayo ndiyo mambo yaliyosababisha kifo cha wazazi wangu pamoja na kaka yangu. Tamaa ya kaka yangu kupata mali nyingi kwa njia ya mkato ndiyo iliyagharimu maisha yake na ya wazazi wetu kwa ujumla. Habari hiyo yote mimi nilikuwa siijui ila Sharifa ndiye aliyekuja kuning’amua.



    Pamoja na maelezo hayo kuhusu kifo cha kaka James nilikuwa bado na maswali mengi sana kichwani mwangu. Maswali menyewe ni pamoja na yeye Sharifa anahusika vipi na kafara hiyo ama ana uhusiano upi na mganga wa kaka James?

    Pia swali jingine lililokuwa limetanda kwenye ubongo wangu ni kwamba mimi kosa langu lilikuwa ni lipi hapo wakati aliyefanya maagano na mganga ni kaka yangu tu? Sikuwa na majibu yake ila niliamini kuwa maswali hayo yangejibika kwa Sharifa.

    Sikusita kumuuliza kwani mpaka wakati huo nilikuwa nimemzoea na kumuona kama alikuwa ni mtu wa kawaida wakati alikuwa si wa kawaida.

    Nilianza na kutaka kujua hao wataalamu hasa ni kina nani na wanapatikana wapi? Swali lilijibiwa. Nikaambiwa kuwa wataalamu ni wale viumbe waliokuwa wamemuweka mganga huyo ili aweze kufanya mawasilo nao katika kumpatia mtu utajiri aombapo. Sikutaka kuendelea tena kudodosa juu ya swali hilo kwani tayari niling’amua kuwa wataalamu hao ni majini ama pepo wachafu.

    Nikahamia kwenye swali la pili ambalo ni kutaka kujua Sharifa anahusikanaje na huyo mganga. Alichonijibu wala sikukitila shaka, nikaachana na swali hilo mara baada ya kupewa jibu.

    “Na wewe una shirika gani na yule mganga?”

    “Ni mmoja kati ya wataalamu wake. Na mimi ndiye nilichaguliwa kuhakikisha James anaaga dunia pamoja na kukuandama wewe ili tukutie adabu, na ukiwa mgumu wa kuelewa utamfuata kaka yako aliko.”

                Sikutaka hata kuendelea kudodosa kwani majibu yenyewe yalikuwa yanajitosheleza. Tangu mwanzo wa kuniandama mpaka kunitoa jela nilikuwa nimeshabaini kuwa Sharifa hakuwa kiumbe wa kawaida. Alikuwa ni jini.

                Hofu ilizidi kujengeka alipotamka kauli ya kwamba hata mimi nikileta za kuleta atanitia adabu ya kumfuata kaka James alikokuwa. Tafsiri ya maneno hayo ilikuwa ni kwamba ataniua kwani James hakuwa Marekani wala Dubai bali alikuwa kuzimu.

                “Kosa langu hapo mimi ni lipi mpaka uniandame hivi?”

    “Mirathi ya kaka yako.” Alijibu kwa mkato kisha akafunga bakuli lake, yaani namanisha akanyamaza kimya.

                Bado kichwa changu kilikuwa na maswali ya kumhoji Sharifa. Mirathi ya kaka ilikuwa imefanya nini? Nilizidi kuwaza kabla sijalitupia swali hilo kwa Sharifa.

                Nilipomuuliza alinijibu kuwa mali ya aina hiyo huwa haitakiwi kurithiwa na mtu yeyote yule. Nilifanya kosa kubwa sana kurithi mali alizokuwa ameziacha kaka James wakati zilikuwa ni za maagano.

                Mpaka hapo niliweza kuelewa kiini cha matatizo yangu. Nilijikuta nikianza kujuta kurithi hizo mali pamoja na kuzaliwa pia. Niliweza kubashiri hatari iliyokuwa inaninyemelea mbele yangu huku chanzo chote kikiwa ni mirathi ya kaka James.

                “Kumbe chanzo cha misukosuko yote hii ni hicho, sasa utanisaidiaje ili nijinasue kwenye hili balaa?” Niliamua kumuuliza hivyo ili nijue hatima yangu.

    “Dawa ya hapo ni moja tu”

    “Ipi hiyo?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kufanya yale yote tunayokutaka uyafanye, zaidi ya hapo anza kujihesabu kuwa ni marehemu mtarajiwa.”

                Hakuna anayependa kufa jamani. Sikujua nifanye nini ili kujinasua kwenye urimbo niliokuwa nimenasa. Kuendelea kuishi nako nilikuwa bado nakutamani. Sasa nilizidi kuwa katika wakati mgumu.

                Maelezo ya mwanadada huyo hayakuwa na chembe ya utani ndani yake hata kidogo. Alichokuwa anakisema alikuwa anakimaanisha. Uwezo wa kufanya hivyo alikuwa nao.

                Tulibaki tukiwa tumetumbuliana macho, mimi nikiwaza yangu kutokana na uzito wa jambo ulivyokuwa. Nilikuwa najiona dhahiri ninavyodumbukia kwenye shimo lenye kina kirefu nisiloweza kutoka tena.

                Wakati nikiwa katika lindi la mawazo niligutushwa na sauti ya Sharifa. Alianza kwa kuniita jina langu.

    “Brighton!”

    “Naam!” Nami nilimwitikia.



    “Usiwaze sana kwani kazi nzito ilishafanywa na kaka yako, unachotakiwa wewe ni kuikamilisha tu na utakuwa bilionea wa kuogopeka.” Alinyamaza kidogo kisha akaendelea.

    “Daraja la kwanza utakuwa umeshalivuka kwani wazazi wa James ni wazazi wako, pia kufa kwake kutachukua nafasi ya ndugu wa karibu, kafara ambayo ilikuwa utolewe wewe. Kitakachohitajika kwako ni kuoa mke kisha mkishazaa mtoto unamtoa kafara akifuatiwa na mama yake, hapo utakuwa tayari umeshakamilisha daraja la pili.” Alipozi kidogo.

    Wakati wote huo nilikuwa nimemsikiliza kwa makini. Baada ya kupozi kidogo aliendelea kuniambia kuwa nikishaimaliza daraja la pili lile lililokuwa linafuata ni mteremko. Daraja hilo ambalo ni daraja la tatu lilikuwa ni kumtoa kafara mtu mmoja kila mwaka, mtu huyo anaweza kuwa ni mfanya kazi wako ama ni mteja wako. Hiyo hatua ndiyo ilikuwa ni nyepesi kuliko zote kwani pale unamtoa mtu ambaye siyo ndugu wa karibu.

    Hata hivyo bado ulikuwa ni mzigo mzito moyoni mwangu. Dhambi ya kuua nilikuwa naichukia na nilikuwa sitegemei kabisa kuitenda katika maisha yangu.

    Nilivuta kumbukumbu ya maneno ya marehemu kipenzi changu Anna aliyoniambia kwenye ile ndoto niliyoota, ndoto ya kutisha. Katika maneno yake alinisisitiza sana nisiue wala kujiua kwani adhabu yake huwa ni kubwa mno.

    Alinisisitiza nizidi kutenda mema huku nikiongeza upendo kwa watu wote wanaonizunguka ili siku zangu zikiisha duniani nikapumzike kwa amani na siyo kwa mateso.

    Sasa mwanamke aliyekuwa mbele yangu alikuwa ananishawishi nianze kuua kwa ajili ya kupata utajiri, tena siyo kuua mara moja bali ni kuua kila mwaka mpaka pale maisha yangu yatakapofika kikomo duniani. Niliogopa sana.

    Kibaya zaidi jambo lilikuwa limekaa kwenye njia panda, kama nisingefanya hivyo basi ningeuliwa mimi. Kweli maisha ni matamu sana mithili ya asali mwitu japokuwa ni mafupi zaidi ya watu wa Uturuki.

    Hapo ndipo nilizidi kuumiza kichwa. Lakini kumbukumbu ya maneno ya marehemu Anna ilionekana kunipa nguvu. Nikajisemea kimoyomoyo kuwa ni bora nife kuliko kubeba dhambi mbaya na nzito kama hiyo, dhambi ya kuua.

    Nikiwa katika kuwaza wazo lilinijia, nikaliona linafaa kulifanyia kazi. Nikataka kufumbua kinywa changu ili nieleze msimamo wangu juu ya jambo lililokuwa lipo mbele yangu. Kabla sijaongea chochote nilimuona Sharifa akisimama na kuniwekea mkono wake kichwani. Mwili wote ulisisimka, nikajihisi kama nimepigwa shoti ya umeme.

    Alipotoa mkono wake juu ya kichwa changu aliniambia gari tuliyokuwa tumeenda nayo hotelini hapo imekuwa yangu kuanzia wakati huo. Pia akaniambia pesa zote zilizokuwemo kwenye brificase iliyokuwa mezani zote ni zangu.

    Mara baada ya kuongea hivyo alinikabidhi funguo za gari zilizokuwa mezani. Kufumba na kufumbua alipotea ghafla, nikabaki peke yangu kwenye chumba hicho. Niliogopa sana.



                            ************************** 

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/*

    Asubuhi ilifika, ilikuwa ni asubuhi ya kwanza kuiona nikiwa uraiani baada ya kukaa rumande na hatimaye gerezani kwa miaka mingi. Niliamkia kwenye hoteli hiyo hiyo niliyokuwa nimepelekwa na Sharifa jana yake.

    Mara baada ya kuamka nilitupia jicho langu kitandani kuiangalia brificase iliyokuwa imejaa mapesa niliyokuwa nimeachiwa na Sharifa. Niliiona imetulia. Nikajiinua kisha nikaifungua na kuiona minoti imejaa tele.

    Nilipoangalia mezani niliziona funguo za gari niliyokuwa nimeachiwa. Kwa bahati nzuri chumba nilichokuwa kilikuwa kipo upande tuliokuwa tumeegesha gari. Nikaamua kuchungulia nje ili kujiridhisha kama gari hilo lilikuwepo kweli. Nikaliona limetulia.

    Wazo nililokuwa nalo usiku wakati Sharifa hajaondoka ni kukataa katakata kufuata masharti yote niliyokuwa nikishinikizwa kuyafanya; masharti ya kuoa mwanamke kisha akishanizalia mtoto nimtoe kafara pamoja na mtoto aliyemzaa, na baada ya hapo niwe natoa kafara mtu mmoja kila mwaka ambaye ni mfanyakazi wangu ama mteja wangu wa aina yoyote ile.

    Hata hivyo baada ya Sharifa kunishika kichwani muda mfupi kabla ya kuyeyuka ghafla wazo hilo nalo liliyeyuka kabisa kichwani mwangu. Nikaanza kujiona kama mtu anayechezea shilingi kwenye tundu la msala.

    Nililipima jambo hilo usiku kucha kwa mapana na marefu, nikaona hakuna sababu yoyote ya kulipiga teke debe la bahati kama hilo. Kitu kilichonipa moyo ni kwamba sikutakiwa kumtoa kafara ndugu yangu yeyote wa karibu zaidi ya mke ambaye nitamuoa kwa ajili hiyo pamoja mtoto nitakayemzaa kwa ajili hiyo.

    Nikaona ni bora nikubaliane na shinikizo la Sharifa ili nitengeneze maisha yangu, niwe mmoja kati ya matajiri wakubwa nchini na duniani pia. Moyo wangu uliridhia kabisa kutajirika kwa njia hiyo, njia ya nguvu za giza na ya kishetani huku nikiwa tayari kuendelea kuteketeza watu kila mwaka kwa kuwatoa kafara ili nizidi kuulinda utajiri wangu huo.

    Pesa nilizokuwa nimeachiwa na Sharifa zilizidi kunipa jeuri, jeuri ya kwenda kununua nyumba sehemu yoyote katika nchi hiyo. Jambo la kuendelea kuishi kwenye mji huo sikuwa nalo kabisa akilini mwangu, hivyo nikaamua kuondoka asubuhi hiyo kwenda mji mwingine uliokuwa mbali na mji huo.

    Niliinuka na kwenda maliwatoni kujimwagia maji mwilini mwangu. Nilipotoka nilivaa nguo zangu kisha nikainua simu ya mezani iliyokuwemo hotelini humo kuangiza kifungua kinywa.

    Haukupia muda sana mlango ukagongwa, nami nilifungua na kumuona dada aliyekuwa amebeba trei (chano) iliyokuwa imesheheni mazagazaga kwa ajili ya kifungua kinywa.

    Kabla hajaondoka nilichukua noti moja iliyokuwa na rangi ya kaki na kumpa ikiwa ni malipo ya kifungua kinywa hicho.

    “Haina haja ya kulipa maana kila kitu kimelipiwa.” Aliniambia mwanadada huyo.

    Hata hivyo ili kumuonyesha kuwa nilikuwa ni bilionea mtarajiwa kwa wakati huo, nilimwambia achukue tu hiyo pesa kwani nilikuwa nimeshaitoa kwenye mahesabu. Naye bila kuvunga aliipokea, si alikuwa kapewa!

    “Samahani dada yangu kama nitakukwaza, ningependa kulijua jina lako.” Nilijikuta namchombeza zikiwa ni harakati za kutaka kutangaza nia katika suala zima la mapenzi.

    Bila kinyongo wala malingo msichana huyo alinionyesha jina lake kwenye kitambulisho chake cha kazi alichokuwa amekining’iniza shingoni.

    Nililisoma jina na kujikuta naachia tabasamu.

    “Kumbe unaitwa Anna, jina lako lina historia ndefu sana katika maisha yangu.”

    “Historia gani tena kaka yangu?”

    “Kwanza mama yangu mzazi alikuwa akiitwa jina hilo, pili kuna msichana ambaye nilitokea kumpenda kupita kiasi naye alikuwa akiitwa Anna, ni jina muhimu sana katika maisha yangu.”

    “Kumbe! Basi na mimi naitwa hivyo!”

    “Natabiri na wewe utakuwa na historia ndefu sana katika maisha yangu,”

    “Yaweza kuwa!” Aliongea Anna na kuanza kunipa mgongo ili aondoke.

    Bila kufikiri wala kuwaza nilijikuta naropoka kumuomba namba ya simu ama mawasiliano yoyote. Pale pale alinitolea kadi yake ya biashara (business card) iliyokuwa na kila aina ya mawasiliano aliyokuwa akitumia.

    “Asante sana mrembo!”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Usijali!” Alimalizia maneno hayo huku akifungua mlango na kuondoka zake.

    Taratiibu kabisa nilijongea kwenye kimeza kilipokuwepo chano cha mapochopocho ya chakula cha asubuhi. Pasipo kuvunga nilikaa na kuanza kujichana kwa raha zangu. Kilikuwa ni kifungua kinywa cha haja, waswahili wa siku hizi wanakwambia ‘msosi draft’ulioenda shule.

    Muda mfupi baada ya kumaliza kushambulia kifungua kinywa niliondoka kwa mwendo wa madaha mpaka kwenye mchuma wangu huku nikiwa nimening’iniza kibrificase changu mithili ya kibosile ama fisadi aliyefutuka tumbo kwa kuchakachua fedha za umma.

    Mpaka nafika nje sikumuona Anna, nilitamani sana japo tupungiane mkono wa kuagana ili nimringishie gari langu la kifahari, lakini haikuwezekana. Nadhani alikuwa kwenye majukumu yake mengine hotelini hapo.



    MWISHO



0 comments:

Post a Comment

Blog