Search This Blog

Thursday, 2 June 2022

MWANGAZA - 1

 





    IMEANDIKWA NA : GRACE G.R



    *********************************************************************************



    Simulizi : Mwangaza

    Sehemu Ya Kwanza (1)



     Asubuhi sana, au wanasema alfajiri, majira ya saa 10, usingizi ulikata licha ya kuwa nililala saa sita usiku. Nilikaa kitandani nikiwaza itakuaje, na nilijikuta nikitumia muda mwingi sana kuwaza kiasi kwamba japo ilikuwa msimu wa ‘winta’ ambao jua huchelewa sana kuchomoza kwa nchi ya ughaibuni, jua ndilo lilinifanya nijue nimechelewa kazini.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Niligundua kuwa siku hiyo tayari nilipoteza masaa kadhaa ya kazi yangu. Niliamka haraka na kuanza kujiandaa. Haikunichukua nusu saa kabla sijamaliza kujiandaa na haraka sana nilielekea kituo cha usafiri (treni), kusubiri ili niende kazini.



    Ghafla, nikiwa natembea, huku akili inashindwa kujizuia kuwaza na kutafakari juu ya kile kilichotokea kwa mpenzi wangu aliyeko Tanzania, nilikutana na yule niliyekuwa nikimtafuta kwa muda wa zaidi ya mwaka sasa. Sikuamini macho yangu kumuona rafiki yangu Mawazo. Inaonekana alikuwa anatoka supermarket (supamaketi). Hakuonekana kama mawazo niliyemfahamu. Nilimtazama kwa muda na kumuita lile jina la kijijini kwetu tulilolizoea ‘Luzoki’



    Ni dhahiri na mimi nilikuwa nimebadilika kidogo hivyo sikushangazwa na yeye kutonikumbuka kwa haraka. Ila niliona mshangao machoni na akilini mwake kusikia jina la kijijini Tanzania katikati ya wazungu. Ilimpa tabu kidogo; nguo nyingi za baridi nilizovaa, ikiwemo kofia; pamoja na hali ya hewa ua Ughaibuni , vilinifanya nibadilike. Sikuwa Nathani yule wa miaka nane iliyopita tulipoagana na Mawazo. Tuliposogeleana, alishangaa sana sana. Hakutegemea kuwa tunakutana kwa mara nyingine.



    Aliponifahamu, alinikumbatia huku machozi yakimtoka. Nilielewa sasa kuwa japo hali ya hewa, marafiki, na hali ya uchumi aliyonayo sasa ni tofauti kabisa , ukiachilia mbali mwonekano ambao pia umebadilika, bado moyo wa huruma na upendo wa Mawazo haukuweza kubadilishwa na hayo yote. Macho yake yalifanya nimuone Mawazo yule niliyekuwa tayari hata kugombana na wazazi wangu kwa ajili yake



    Kwa mara nyingine nilijisemea moyoni ‘Sijutii uamuzi wangu’. Akiba yangu ya fedha niliyotumia kumsaidia akamilishe mipango yake ya safari ilinifanya nigombane na wazazi na ndugu zangu pia. Japo nilifanya hivyo kwa ajili ya thamani ya urafiki wetu, lakini pia nilikuwa na mategemeo makubwa kuwa kuna siku Mawazo angenisaidia kutimiza ndoto na malengo yangu ya kuagana na ufukara ambao familia zetu zilikuwa nao...



    Mwaka 1994, nikiwa ni kijana mdogo wa miaka 13, katika shule ya msingi ya Kilimahewa mkoani Singida, nilifanya uamuzi wa kuacha shule. Haukuwa uamuzi rahisi kwangu. Umasikini na hali ya maisha katika familia yetu ilinifanya nichelewe kuanza shule na hivyo nikiwa darasa la pili tayari nilikuwa naelewa nini maana na umuhimu wa elimu. Akili zangu darasani hazikuwa dhaifu japo hali ya maisha ilinifanya nishindwe kufanya vizuri darasani.



    Tumezaliwa watoto nane kwa baba na mama, na mimi ndiyo mzaliwa wa kwanza. Wakati huo nilikuwa na wadogo zangu watano wote wa kiume. Baba hakufurahishwa nasi sana. Mara zote alisema, ”Nahitaji binti atakayejaza zizi langu”. Kila alipoenda kwenye sherehe za kuozesha watoto wa rafiki zake, alirudi akiwa amelewa na tulisikia akimpiga mama na kumwambia, nataka mtoto wa kike.



    Vilevile baba hakuona kama ni kipaumbele kutusomesha. Mara nyingi alisema elimu ni gharama kubwa isiyo na faida. Nilipoona watoto wenzangu wakienda shule niliumia sana sana. Nilifatilia kujua gharama za kujiunga shule ni kiasi gani nikiwa na miaka tisa na nusu hivi. Haikuwa gharama kubwa sana japo sikuweza kumwambia baba. Wakati huo kazi yangu kubwa ilikuwa ni kuchunga mbuzi wa nyumbani. Mama alijua jinsi gani napenda kusoma na kila wakati alijaribu kumweleza baba juu ya elimu lakini mara nyingi hiyo mada ilimfanya aambulie kipigo au matusi.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nilifanya uamuzi wa kutafuta pesa mwenyewe ili nijisomeshe. Nilipoenda kuchunga niliongea na wazee wenye mifugo ambao watoto wao wanasoma ili kwamba muda wa shule niwachungie mifugo yao, wanilipe. Kwa bahati nilipata hiyo fursa na ndani ya miezi sita nilifanikiwa kupata fedha ya kutosha kununua mahitaji yote ya shule pamoja na ada. Nilimshirikisha mama nia yangu ya kusoma, Machozi yalimtoka. Pengine aliwaza jinsi baba atakavyompiga akijua nimeanza shule. Au labda aliguswa na nia yangu na shauku ya kusoma. Siku hiyo mama alinambia maneno mazito sana. “Mwanangu, najua unapenda kusoma. Naumia kwamba wazazi wako tumekuwa tukikunyima hiyo nafasi mara zote, lakini naamini unajua mimi mama yako nataka usome. Najua haitakuwa rahisi kwako. Baba yako hatafuirahishwa na uamuzi wako. Wakati mwingine shuleni utapata changamoto nyingi, lakini mara zote kumbuka nipo upande wako. Hata kama sitakutetea utakapoumizwa, nitakuombea. Lengo lako liwe kusoma kwa jitihada zote ili siku moja ulete maendeleo kwangu na kwa wadogo zako."



    Jinsi mama alivyoongea, japo nilikuwa bado mdogo, nilielewa ilikuwa ni hatari kwake na kwa ndoa yake kuniruhusu nisome. Siku hiyo usiku sikulala. Niliwaza sana na kulia. Kichwani zilinijia kumbukumbu za mama akipigwa na baba alipojaribu kuzungumza suala la shule. Mbele yangu kulikua na njia mbili, ’Nijiunge na shule na kumtesa mama, kisha baadaye nimtoe kwenye umasikini’ au ‘Niachane na shule na hizi hela ninazopata niwe nampa mama.'



    Kesho yake niliamka nimefanya maamuzi. Tabia ya baba yangu kumtesa mama na kutuchukia ilinifanya nisimpende hata kidogo. Niliwaza moyoni, “Mama hatakiwi kuishi na baba siku zote. Lazima nisome, nipate maisha mazuri ili nimtenganishe mama na baba”. Hilo tu lilinipa nguvu na ujasiri wa kwenda kuanza shule. Nilimuahidi mama kuwa nitasoma kwa ajili yake na wadogo zangu. Sikuhiyo nilienda shule na kuonana na mwalimu aliyenipeleka kwa mwalimu mkuu. Nilimueleza mwalimu mkuu vitu vingi maana haikuwa kawaida mtoto kujiandikisha shule mwenyewe. Kwa bahati mbaya nilitakiwa kusubiri miezi kadhaa kabla muda wa kuandikisha watoto haujafika.



    Nikiwa na miaka karibu kumi na mmoja nilianza chekechea. Nilikuwa mtoto mkubwa darasani lakini sikujali. Siku ambayo baba aligundua nimeanza shule, nadhani ilikuwa siku mbaya zaidi maishani mwangu kwa wakati huo. Baba alitufungia chumbani mimi na mama halafu alitumia mkanda wake maalumu wa ngozi kutuchapa. Mara zote nilisikia baba akimpiga mama wakiwa chumbani, lakini sikuwahi kujua alimpiga akiwa mtupu bila nguo yoyote. Baba alitoa nguo za mama mbele yangu na kumuacha na chupi tu, kisha akanilazimisha nami nitoe nguo. Alitupiga bila huruma. Alisema mama amepata wanaume wa kunilipia mimi ada. Aliniambia lazima niache shule. Siku hiyo mama alipigwa sana maana alionekana ni mwenye ujasiri. Alimweleza baba ukweli kuhusu namna nilivyofanya kazi mwenyewe kutafuta ada, japo baba alijifanya kutomuamini. Na pia alimwambia kuwa sitaacha shule hata kama itabidi anihamishe nyumbani.



    Kesho yake sikuweza kwenda shule. Nilikuwa na maumivu makali. Kwakua baba hakuwa mtu wa kushinda nyumbani, nilipata nafasi nzuri ya kukaa kuongea na mama. Alijitahidi kutonionesha jinsi alivyoathiriwa na tukio la jana usiku. Aliniambia, hata ikimbidi apigwe kila siku, nisiache shule. Alisema, baba yako akiendelea kukupiga na wewe, nitakutafutia sehemu nyingine ukaishi. Kwa bahati, baba hakufanya hivyo tena siku nyingine, japo mara kadhaa alimpiga mama (kama alivyozoea), na kuna wakati alinitafutia sababu na kunipiga bila makosa, lakini si kwa namna alivyofanya usiku ule.



    Nikiwa naendelea na shule, maisha yangu hayakuwa sawa na watoto wengine. Muda wangu wa kufanya kazi ya kuchunga kwa malipo ulipungua, hivyo kufanya kipato changu kipungue pia. Pesa haikunitosha tena kujilipia ada, kununua sare na mahitaji mengine ya shule. Nyumbani pia maisha yalizidi kuwa magumu kwani mama alipata ujauzito mwingine ambao ulimfanya aumwe na hivyo kushindwa kufanya shughuli zake za kuingiza kipato kama awali. Ni dhahiri baba hakuwa mtu wa kujali familia hivyo chakula chetu kilitegemea zaidi biashara za mama. Pesa kidogo niliyokuwa naipata niliigawana na mama ili kusaidia mahitaji ya nyumbani.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mwaka huo nadhani ulikuwa mgumu zaidi kwangu na kwa mara ya kwanza niliruhusu wazo la kuacha shule linishinde. Ilikuwa siku ya jumatano niliporudi nyumbani na kumkuta mama yangu anaumwa sana. Alikuwa akitapika mfululizo na damu ilimtoka. Wadogo zangu walonifuata walikuwa wamekwenda kuchunga na kuteka maji. Aliyekuwa nyumbani na mama ni mdogo wangu wa mwisho kwa wakati huo aliyekuwa na miaka miwili, ambaye hangeweza kufanya chochote kumsaidia mama. Nilijua mama anatakiwa kupelekwa hospitali, hivyo niliita majirani tukampeleka hospitali.



    Kabla hatujatoka nyumbani mama alinambia, “Mwanangu nisipopona utaenda kwa fulani (alimtaja mmoja wa rafiki zake wa karibu kijijini), utamwambia mama aliomba unisaidie niishi kwako. Lakini wadogo zako, bibi yako akija kwenye msiba utamwambia mama alisema aondoke nao.”[Bibi yangu aliishi kijiji kingine. Maisha yake na nguvu zake zingemfanya asipate shida kutunza wadogo zangu iwapo mama angefariki].“Ukikaa hapa baba yako hatakuruhusu uendelee na shule” aliongeza kusema kwa uchungu. “Pia anaweza kukuumiza kwa kukupiga”. Jinsi hali ya mama ilivyokuwa, na namna alivyoongea, nilijua fika kuwa baba ndo alisababisha kuumwa kule. Tulimuacha mama amelazwa hospitali halafu nilirudi nyumbani niliwa na hofu kubwa mno. Nilijilaumu sana kwani nilihisi kwa kung’ang’ania kwangu kusoma, ninakwenda kumpoteza mama yangu. Nilisema kuwa sitaendelea tena kusoma endapo mama atapona, au labda nitamshawishi sote tuhamie kwa bibi.



    Baba aliporudi usiku na kumuulizia mama, nilimwambia kuwa tumemwacha hospitali. Aliniuliza kwa hofu kubwa maswali kadhaa na kunitaka twende wote hospitali usiku huo. Akiongea na daktari, sikuamini kile nilichosikia, japo nilijifanya siwasikii. Daktari alimwambia baba kuwa inaonesha mgonjwa kapigwa sana kiasi cha kusababisha tatizo kwa mtoto, na kama asingewahishwa hospitali huenda asingeishi. Aliongeza kuwa inatakiwa ripoti ya polisi ili kumtibu, japo walimpa huduma ya kwanza kuokoa maisha yake. Baba alimpa daktari kiasi cha hela na kumwambia aachane na habari ya polisi, amtibu tuu. Hapo ndipo nilipohakikisha kuwa kweli baba alikuwa amerudi nyumbani mchana na kumpiga sana mama kisha kuondoka tena. Nilipomuuliza mama sababu baada ya kupona alisema siku hiyo baba alitudi na kukuta mdogo wangu tunayefatana alikuwa amerudi kutoka machungoni akilia kuwa mbuzi mmoja kapotea. Baba alikasirika sana na kusema ni kwa sababu mama aliruhusu nisome badala ya kuchunga mali zetu, hivyo kuwapa majukumu wadogo zangu ambao bado ni wadogo. Baba alimrudisha mdogo wangu machungoni na huku nyuma alianza kumpiga mama. Alimpiga kwa hasira hadi mama kufikia hali mbaya, kisha akaondoka na kumuacha.



    Siku mbili zilizofuata sikwenda shule. Ijumaa jioni alikuja rafiki yangu Mawazo. Ki-umri nilimzidi Mawazo kiasi, lakini tofauti na watoto wengi shuleni ambao walinidharau na kunichokoza kwa ajili ya utulivu wangu na umri wangu mkubwa, Mawazo alinijali sana. Mara zote huwa nasema, pengine Mungu alimleta ili kuongeza thamani ya maisha....



    Nilimueleza Mawazo juu ya uamuzi wangu wa kuacha shule. Katika umri mdogo, nilikuwa nimejifunza kuwa jasiri au pengine sugu, na mtu asiyependa kuonesha udhaifu au maumivu yake hasa kwa machozi, lakini siku hiyo nikiongea na rafiki yangu nililia sana kiasi cha kumfanya nayeye alie na kushindwa kunifariji. Nilimuelezea hali halisi ya nyumbani, japo alikuwa anafahamu kwa kiasi kikubwa tayari. Nilimuhadithia jinsi ambavyo nilikuwa hatiani kumpoteza mama yangu siku mbili zilizopita. Kisha nikamwambia juu ya uamuzi wangu wa kuacha shule. Nilijua Mawazo lazima angepinga uamuzi huo bila kujali ni kiasi gani namaanisha, ila sikujua ni kwa kiasi gani hasa Mawazo alijali elimu yangu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nilimuangalia Mawazo akiwa kama mtu aliyepigwa na butwaa akinisikiliza. Kadiri nilivyoanza kusisitiza kuwa sitaki tena kuendelea na shule ndivyo alivyozidi kubaki kama mtu aliyepoteza fahamu. Alinitolea macho huku akitokwa na machozi. Alinisikiliza na kukaa kimya kwa muda kiasi cha kunifanya nitamani kusikia kilichomo akilini mwake.

    Urafiki wetu ulianza mara tu tulipoonana, nah ii nadhani kwa sababu yeye ni mtu mwenye huruma nyingi. Japo familia zetu sote zilikua na hali duni ya kiuchumi, wazazi wake walikua wanaelewana na kupendana, baba yake hakuwa mlevi kama baba yangu, alisapoti elimu na alipenda watoto wake, na hivyo kufanya hali ya maisha na uchumi kwao kuwa bora sana kuliko ya kwetu.



    Mawazo alianza kuwa karibu na mimi baada ya kuona ni mtu niliyependelea kukaa pekeangu na vile wanafunzi wenzangu walivyonidharau. Sikuwa huru kwake mwanzoni kwani ki kawaida sikuwa mtu wa kujiamini au kuamini marafiki, lakini hiyo haikumsumbua. Alijipendekeza kwangu kana kwamba yeye ndo mwenye uhitaji sana wa urafiki wetu. Darasani Mawazo alikuwa kati ya watoto wanaofaulu sana. Na japo tulikuwa kijijini, lakini mipango yake na malengo makubwa aliyokuwa nayo yalinifanya nione kuwa kuna nafasi ya kufanikiwa kimaisha kama tungetia bidii kwenye masomo.



    Urafiki wetu uliimarika zaidi nilipokuwa nikipata changamoto mbalimbali za maisha. Mawazo alinitambulisha kwa wazazi wake na ilinishangaza sana sana kuona kuwa kuna familia zinazoishi kwa upendo na maelewano. Wazazi wake pia walionesha kunijali kana kwamba tuna undugu. Nakumbuka mara ya pili kumtembelea Mawazo nyumbani kwao, nikiwa sina viatu baada ya viatu vyangu kuisha, baba yake alimwambia anipe viatu vyake vipya (alivyomnunulia vikawa vikubwa kwake), japo alikuwa amepanga kuvirudisha dukani. Kwakweli sikuwahi kukutana na mwanadamu wa namna hiyo maishani mwangu kabla. Siku ile yule mzee alinifanya nijisemee moyoni kuwa, japo baba yangu ni mtu katili na asiyefaa, bado nikiwa mkubwa nitataka niwe baba mwema na mwenye upendo kwa familia yangu na kwa watu wengine.



    Rafiki yangu Mawazo alikuwa amenisaidia sana kufika hapo nilipokuwa. Japo bado tulikuwa madarasa ya chini lakini alikuwa amenionesha thamani kuu ya urafiki wetu. Alinifanya kujikubali tena mara zote nilipohisi kujikataa, alinifanya nimsamehe baba licha ya kuwa aliniumiza mara nyingi, alinisaidia kuwa na ndoto na malengo makuu maishani, alinifanya nijipe moyo wa kuendelea na shule licha ya vipingamizi nilivyokuwa nakutana navyo nyumbani, na mara zote alipoongea na mimi, hata kama nilikuwa nakaribia kukata tama, nilipata nguvu mpya. Kijana huyu mdogo alikuwa mwenye hekima nyingi na akili si tu za darasani, bali pia za kuishi na watu wote. Alipendwa na walimu shuleni na pia wanafunzi wengi tulimpenda kwani hakukuwa na kasoro ya kumtoa.



    Baada ya kunitazama dakika kadhaa akilia, Mawazo alifungua kinywa kusema,”Nasikitikika kuwa ni uamuzi umekwisha fanya na siwezi kuubadili. Pengine ingekuwa ni mimi ningeamua hivyo pia kwani sidhani kama nina uwezo wa kubeba mzigo ulionao moyoni. Kinachoniuma ni jinsi ambavyo ndoto na maono yetu makubwa yanaishia njiani. Tulipanga tusome, tupate maisha mazuri, familia zetu zifaidi matunda yetu. Tulipanga tukiwa wakubwa wake zetu wasiishi kijijini na watoto wetu wasisomee shule za vijijini. Tulipanga tutajenga magorofa jirani mimi na wewe, na watoto wetu watakuwa marafiki kama sisi tulivyo.



    Wewe ulipanga kuwa daktari mkubwa na mimi niwe rubani. Nilitamani siku moja nikiumwa nije hospitali kwako unitibu, lakini naona ndoto zote zinaishia hewani. Mimi nitaendelea kusoma, na nitakuwa na maisha mazuri. Nitakupa msaada wa kiuchumi kadiri nitakavyoweza, lakini sitaweza kutoa msaada wa kuitosheleza familia yako, wazazi wako, wadogo zako, mke na watoto wako na kukujengea nyumba mjini. Msaada pekee ninaoweza kukupa ni ushauri wa kukuomba usiache shule”.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Maneno ya Mawazo yalinifanya nisahau kama siku mbili zilizopita mama yangu alikaribia kuuawa kwa ajili yangu. Pia yalinifanya nisahau kama baba yangu anaweza fanya chochote ili nisiendelee kusoma. Nilifanya uamuzi mwengine tofauti siku hiyo kuwa NITASOMA, kwa gharama yoyote. Nilimuahidi Mawazo kuwa sitarudi nyuma na hakika kuna siku tutatimiza pamoja zile ndoto zetu. Japo alionekana kutoamini ninachomwambia, lakini alionekana mwenye furaha sana kujua kuwa nimeupokea tena ushauri wake na kubadili maamuzi



    Siku zilipita, mama alipona, alijifungua salama, alibeba mimba nyingine na kwa bahati mtoto wa nane alikuwa wa kike. Siku mdogo wangu wa mwisho alipozaliwa, nikiwa darasa la tano, nilirudi nyumbani na kukuta furaha ya ajabu. Wakati huo baba alikuwa ameamua kuniruhusu nisome japo alikua hajishughulishi na gharama yoyote ihusuyo elimu yangu. Pia wadogo zangu wengine hawakuweza kusoma, alikataa kabisa. Ilibidi nifanye bidii zaidi shuleni nikijua mzigo wote wa familia ni wangu. Kwa sasa akili yangu ilikuwa imekomaa zaidi. Sikusumbuliwa na mambo ambayo awali yalinifanya nishindwe kujiamini na pia kufanya vizuri darasani. Walimu walinijua kama kijana mtulivu zaidi na aliye makini kwa kazi zake.



    Wakati huo mimi na Mawazo tulikua tukichuana vizuri kwenye mitiani. Katika somo la hesabu yeye alifanya vizuri siku zote lakini katika somo la sayansi nilimzidi. Hii ilifanya mara zote yeye akiwa wa kwanza mimi ninafuata, ama mimi nikiongoza yeye anafuata. Urafiki wetu ulijulikana shuleni na nyumbani, na wanafunzi wenzetu walituonea wivu. Muda wa ziada tuliutumia kuomba walimu watufundishe na maisha yangu sasa yalikuwa yenye furaha zaidi.

    Siku hiyo baba alikuwa amerudi mapema nyumbani kwani alipata taarifa akiwa katika shughuli zake, kuwa mama anajifungua. Mkunga aliyemzalisha mama alitoka ndani na kumpa baba habari njema kuwa amepatikana mtoto wa kike. Baba alikwenda kuita marafiki zake kadhaa, alichinja mbuzi haraka mchana huo na walikaa na rafiki zake wakisherehekea mpaka usiku wa manane nyumbani.



    Kwa mara ya kwanza niliona baba yangu akimfurahia mama yangu kama mke wake. Alimpa pole, alimwambia kwa sauti ya upole, umenizalia mama yangu, na pia alimuahidi kuwa huo ni mwisho wa ugomvi wao. Japo alikuwa amelewa, lakini niliona hali ya kumaanisha katika maneno ya baba siku hiyo.



    Baba alimpa jina la Neema, na kwa hakika neema ilikuwa imeingia nyumbani kwetu. Baba alianza kuonesha kubadilika. Kwa muda wa kama wiki mbili hakwenda tena kunywa pombe na mida ya mchana alirudi nyumbani na kukaa na mama na mtoto. Upendo wake kwa Neema ulionekana na kujulikana kwa kila mtu. Tofauti na nilichokiona kwa wadogo zangu wengine, baba alijifunza kukaa na mtoto na kumlea. Japo hakufanya lolote la ajabu ila kwa jinsi nilivyomjua ilikua ni ajabu sana kukaa amemshika mtoto mikononi mwake kwa muda wa nusu saa mfulilizo, akimuacha mama apumzike na kufanya shughuli nyingine. Kwa miezi ya mwanzo baba hakutaka mama afanye kazi yoyote na kwa bahati nzuri tulikuwa tayari ni vijana wakubwa tuliofundishwa kufanya kazi zote za ndani.



    Siku moja tukiwa darasa la saba, tulichukuliwa wanafunzi wachache tuliokuwa tunafanya vizuri darasani kwa ajili ya kwenda kushindanishwa na shule nyingine za mkoa wa Singida. Hii ilikuwa ni wiki kadhaa kabla ya kufanya mtihani wa moko (mock). Mashindano hayo hayakuwa na lengo tu la kutupima akili au kutuandaa na mtihani wa mwisho, bali pia yalikuwa na lengo kubwa la kuwapatia baadhi ya watoto wenye uwezo mkubwa darasani lakini wenye hali duni za uchumi wa familia zao fursa ya kuendelea na elimu ya sekondari. Mwaka huo ilitokea bahati kuwa kulikuwa na wafadhili waliojitolea kufadhili masomo ya sekondari kwa vijana ambao kwa namna moja au nyingine walikuwa na changamoto za ki uchumi katika familia zao, huku wakitilia mkazo wale tu wanaofanya vizuri darasani.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kwa bahati shule yetu ilikuwa moja ya shule zilizopata hiyo fursa kuingia kwenye shindano, na watoto watatu tulichukuliwa kushindanishwa na watoto wengine zaidi ya 100 kutoka kwenye shule mbalimbali za vijijini mkoani Singida. Walihitajika washindi kumi tu kati ya vijana wote ambao walitakiwa kushinda kwa wastani wa juu sana ili kupata fursa hiyo. Mimi na Mawazo na mwenzetu mwingine mmoja tulichaguliwa.



    Licha ya kuwa nilikuwa nafanya vizuri sana darasani, lakini bado nilikuwa sijiamini vya kutosha kushindanishwa na watoto mahiri na wengi kutoka kwenye shule mbalimbali. Baba yake Mawazo alitafuta mwalimu maalumu kwa ajili yetu ili kutusaidia na maandalizi. Nilipewa ruhusa nyumbani kuhamia nyumbani kwa kina Mawazo kwa muda wa kama mwezi mmoja hivi kabla ya siku ya shindano. Tulisoma usiku na mchana. Mwalimu alitusaidia kufanya na kurudia maswali ambayo mara nyingi huulizwa kwenye mitihani ya mwisho.



    Siku zilienda na hatimaye siku ya shindano ilifika. Tuliondoka na mwalimu wetu mmoja shuleni, tukapanda basi kuelekea Singida mjini. Kwa mara ya kwanza kwenye maisha yangu nilifika mjini, nikaona magari mengi, nyumba kadhaa za bloko na umeme kila mahali. Pia nilishangaa kuona maji yakitoka ndani, bombani kwenye chumba tulimolala. Mimi na Mawazo tulilala chumba kimoja, na mwalimu alitafuta chumba kwajili ya mwenzetu wa kike tuliyekuwa naye.



    Asubuhi tulipelekwa sehemu ambapo tulikutanishwa na wenzetu wote ambao tungefanya nao mtihani. Ilikuwa ni shule ya bweni, na tulilala hapo siku mbili huku tukiendelea kujiandaa na mtihani na baada ya hizo siku mbili, hatimaye siku ilifika. Tulitumia siku nzima (moja) kufanya mitihani mitatu (Hisabati, Maarifa na Lugha). Baada ya siku hiyo ndefu tulilala tena hapo shuleni siku hiyo na kesho yake tukaanza safari kurejea nyumbani.



    Siku kadhaa baada ya matokeo ya mitihani ya moko kutoka, tuliitwa ofisini kwa mwalimu sote watatu. Mwalimu alianza kwa kututia moyo kuwa sote tulifanya vizuri katika lile shindano, na hasa mimi na Mawazo kwani wastani tuliopata ni zaidi ya asilimia 90 kwa kila somo. Pia alisema kwamba hii inaonesha hata kama hatujapata ile nafasi ya kuchaguliwa na kusomeshwa na wafadhili, bado tuna fursa nzuri sana ya kuchaguliwa kusoma shule za serikali baada ya mtihani wa taifa, kwani kwa ufaulu ule, ni lazima tutachaguliwa kusoma shule nzuri za serikali. Maneno ya mwalimu yalinifanya nilowe jasho. Nilijua ushindani uliokuwepo lakini nilikuwa na matumaini makubwa sana ya kuchaguliwa. Ufadhili huo kwangu ungekuwa na maana kubwa sana, kwani sasa si tu kuwa nisingehitaji tena kujilipia ada, bali pia wafadhili waliahidi kutoa msaada wa kifedha kwa familia za watoto husika. Nilikuwa tayari kichwani nina ndoto kubwa kuhusu huo ufadhili na kiukweli, japo Mawazo ni rafiki yangu niliyempenda sana sana, siku ile nilimuonea wivu mwalimu alipotuambia kuwa ni yeye pekeake kati yetu sote watatu aliyefanikiwa kuingia kwenye kumi bora.



    Tulioneshwa alama zetu, Mawazo alikuwa amenipita kwa alama moja tu. Ila kwa ushindani uliokuwepo, tofauti hata ya nusu alama ilimaanisha ushindi mkubwa. Nilimtazama Mawazo na kutoa tabasamu feki, na nilitegemea angenionesha furaha japo kidogo, lakini badala yake Mawazo alitoa machozi. Ni dhahiri hayakuwa machozi ya furaha, kwani nikiwa bado najiuliza swali hilo, alimuuliza mwalimu,’Hakuna uwezekano wa kugawa nafasi yako kwa mtu mwingine kama tukiongea nao?’ Mwalimu hakumjibu, alimtoa yule msichana akabaki na sisi wawili. Alimjua Mawazo vizuri na alijua alikuwa akimaanisha alichouliza. Hata mimi pia nilijua kuwa alikua akimaanisha.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Tulikaa na mwalimu wa taaluma karibu saa nzima akijaribu kumueleza Mawazo kuwa japo sikufanikiwa kupata ile fursa, bado nina nafasi nzuri ya kuchaguliwa tena shule nzuri sana. Mawazo aliumia sana kiasi cha kunifanya huzuni na wivu niliojisikia vitoweke na badala yake niliona aibu. Baadaye, alipokubaliana, alianza kunitia moyo. Japo nilimjua Mawazo kwa undani kabla, ila siku hiyo niligundua kuwa nina rafiki mwenye huruma sana. Kwa kiasi kikubwa alinifanya nikubaliane na matokeo. Niliporudi nyumbani mama pia alinisaidia kukubali matokeo yale, kwani yapo alijua kiasi gani nilitamani sana ile nafasi, lakini hakuonesha kuvunjwa moyo nilipomwambia sikupita. Mama alimpa pongezi za dhati Mawazo (alinisindikiza nyumbani siku hiyo), na pia alimshukuru jinsi alivyonisaidia kukubali, kwani alijua hali yangu ingekuwa tofauti kama tusingekuwa wote, (japo wakati huo nilikuwa bado sijamweleza yaliyojiri ofisini kwa mwalimu wa taaluma).



    Hatimaye mwaka 2001 tulihitimu darasa la saba. Siku ya maafali ilikuwa siku yenye hisia mchanganyiko kwangu. Kwa upande mmoja nilikuwa mwenye furaha, nilipewa zawadi ya kuwa mwanafunzi mtulivu zaidi kwa mwaka wetu, pia nilipewa zawadi ya usafi na nilipewa zawadi ya kuongoza katika somo la Maarifa kwa mtihani wa moko. Mama yangu alikuja kunipokea kila nilipotoka kupokea zawadi, na furaha aliyoionesha usoni mwake ilifanya nijione mwenye mafanikio makubwa. Hakuwa na zawadi kubwa ya kunipa, lakini alinizawadia kitabu cha wastani chenye jina KUISHI NDOTO YAKO. Yeye hakuona uthamani mkubwa wa zawadi aliyonipa, lakini mpaka leo hii ninaandika hadithi ya maisha yangu, sitaacha kamwe kukumbuka mchango mkubwa wa kile kitabu katika mafanikio na changamoto zote nilizopitia.



    Hataivyo kwa upande mwingine nilikuwa mtu mwenye huzuni. Kumaliza shule ya msingi ilimaanisha mwanzo wa safari nyingine ya elimu ambayo mpaka sasa nilikuwa sijajua itakuwaje. Kama mtoto wa kwanza, na kulingana na hali halisi ya nyumbani kwetu, sikutegemea msaada wowote wa kiuchumi kutoka kwa familia yetu. Nilijua lazima ningefaulu kwenda shule nzuri ya serikali, na katika shule nilizochagua, mbili zilikua za mikoa mingine, hivyo ilimaanisha kama ningepata kati ya hizo, ingenilazimu kwenda kuishi mbali na nyumbani kwetu.



    Niliwaza nitawezaje tena kujisomesha elimu ya Sekondari, pia niliwaza jinsi gani nitaanza maisha ya kuishi mbali na familia yetu ambayo kwa namna moja ama nyingine nilionekana kama mtu anayetegemewa. Nikiwa katikati ya mawazo mengi juu ya maisha yanayofuata, alinipiga begani Mawazo ambaye alikuwa ametoka kuchukua sahani ya chakula. Nilimuangalia na kutabasamu japo sikuonesha furaha kama aliyokuwa nayo yeye. Ghafula nilipata huzuni zaidi nilipogundua kuwa miezi michache ijayo urafiki wetu utatenganishwa na umbali wa shule tutakazokuwa tunasoma. Nilijihisi kumkosa tayari Mawazo japo nilikuwa hata sijajua ni lini tutatengana.



    Sherehe iliendelea, tulikunywa na kula chakula kilichoandaliwa kwa michango kidogo tuliyokuwa tumeichanga, wazazi walifurahi, wanafunzi tulipiga picha za pamoja, na hapo ndipo nilipogundua kuwa vijana wenzangu wengi sana tuliosoma nao walinipenda na kuniheshimu sana, kwani wengi waliomba kupiga picha na mimi, wengi walinitambulisha kwa wazazi wao wakisema ‘huyu ndio Nathani’, na pia kuna ambao hata sikuwachukulia kama marafiki, waliniaga kwa kunikumbatia na wengine kunishukuru. Mara nyingine unaweza ukawa unafanya vitu ambavyo unaona ni vya kawaida tu kwa watu, kumbe vina maana kubwa sana. Nikiwa shule, na hasa nilipoanza kufanya vizuri darasani, mara nyingi wanafunzi wenzangu waliniomba tukae pamoja na kufanya maswali ya nyuma (past papers) pamoja, hasa wakati wa mitihani. Utayari wangu wa kuwasaidia wenzangu wakati mwingine hata kuharibu ratiba zangu za kujisomea au kurudi nyumbani, sikujua kuwa ulinijengea urafiki kwa wenzangu wengi sana. Daima sikupenda kukataa kutoa msaada hasa wa masomo kwani nilitamani kila ninayeweza kumsaidia afanye vizuri kwenye masomo yake, nimsaidie afanye hivyo. Kulingana na hotuba ya mwalimu wa taaluma, mwaka huo walitegemea kupata matokeo bora zaidi kwa vijana kwani lilikuwa darasa lenye ushirikiano mkubwa na motisha ya juu ya kusoma. Mwalimu pia alitaja baadhi ya wanafunzi ambao walionesha juhudi kubwa sana za kuwasaidia wenzao, nikiwemo mimi, na nilipotajwa wanafunzi wenzangu walipiga makofi mengi mno.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wakati wa chakula tulikuwa pamoja na wazazi wa Mawazo, na hapo mama alipata fursa ya kuwashukuru tena wazazi wake kwa jinsi ambavyo kijana wao amenisaidia kwa kiasi kikubwa kufanya vizuri kwenye masomo yangu. Mama yangu alikuwa ni mtu mwenye utajiri wa shukurani. Mara zote alinifundisha kuwa mtu anaponifanyia kitu, neno la shukurani lina thamani kuliko pesa na mali. Nilitumia wakati huo kujichangamsha na kujisahaulisha shida zangu kwani nilijua hii ni siku ya mwisho ya kufurahi kwa pamoja na wanafunzi wenzangu, hivyo nilikula kwa haraka na kisha kwenda kuendelea na stori za hapa na pale, huku tukikumbushana miaka ya nyuma, tukicheka na kufurahi.



    Katika mambo ambayo shule yetu imefanikiwa sana, ni uandaaji wa mahafali. Tofauti na shule nyingi za vijijini, shule ya msingi Kilimahewa inasifika kwa kuandaa mahafali yaliyochangamka sana, na japo uandaaji wake si wa gharama kubwa, walimu walizitumia siku hizo kuwa siku nzuri za kuwakutanisha wazazi na wanafunzi, na pia kutenga muda wa kutosha kufahamiana, kuzungumza na kucheka. Siku hiyo nadhani ilikuwa na furaha zaidi kwani kulingana na mshikamano mkubwa tuliokuwa nao wanafunzi, wazazi wetu wengi walifahamiana na hivyo hawakuwa wapweke.



    Tukirudi nyumbani, mama alishindwa kujizuia kuonesha furaha yake kwa tabasamu lililokuwa halipotei usoni mwake. Kila nilipomtazama alikuwa akitabasamu. Kuna wakati alirudia maneno yake,’Mwanangu umenifurahisha’, lakini muda mwingi alitabasamu. Mama yangu ni mtu mpole sana, na nadhani hiyo ndiyo sababu japokuwa baba alimtesa sana, sikuzote aliweza kumvumilia. Kikawaida si mtu wa maneno mengi, lakini siku hiyo tuliporudi nyumbani alionesha furaha yake kwa kuongea hadithi zote za mahafali kwa kila mtu.



    Alitamani kumuhadithia baba pia, lakini hakuweza kufanya hivyo akimlenga yeye pekeake, bali alijifanya akirudia tena wakati baba akiwepo kwa kujidai anawambia wadogo zangu ambao tayari walishasikia. Japo baba hakusema chochote, lakini alionekana mwenye kuchangamka usoni. Nilikuja kugundua kuwa baba pia alienda kuwahadithia rafiki zake kwa sifa kuwa kijana wake ana akili kuliko wote aliosoma nao darasa moja, kwani siku chache baadaye nilikutana na mzee mmoja rafiki wa baba, akiwa amelewa, na alinisifia huku akipiga piga kichwa changu na kunambia wewe una akili nyingi, lazima usome sana, na kunipa maneno mengi ya kunisifia.



    Ni kweli, sawa na ambavyo walimu wangu walitazamia, matokeo yalipotoka nilichaguliwa shule ya vipaji maalumu ya Elbol mkoani Arusha. Sitasahau siku hiyo! Nilisikia kwenye redio mchana kuwa matokeo ya darasa la saba yametoka, nikamwambia mama, kisha nikaenda kufatilia shuleni. Sikufanikiwa kupata taarifa zozote shuleni kwani nadhani kwa wakati huyo yalikuwa hayajafika. Nilirudi nyumbani nikiwa mnyonge kidogo. Nilijua nitafaulu na kupata shule nzuri lakini bado nafsini nilikosa raha, nikikumbuka jinsi ambavyo nilikuwa na mategemeo juu ya ule mtihani wa shindano tuliofanya na kisha kukosa nafasi. Mama alijitahidi kunichangamsha jioni hiyo kwa kunipa hadithi ya kipindi nazaliwa.



    Kweli hadithi hiyo kwa kiasi kikubwa ilinisahaulisha, kwani ilikuwa na historia juu ya jina langu la Nathani. “Wakati nina mimba yako, kijijini kwetu kwa mara ya kwanza walitembelea watu weupe. Mimi binafsi sikuwa nimewahi kuona mtu mwenye rangi nyeupe zaidi ya binti mmoja albino aliyeishi kijijini kwetu zamani tukiwa wadogo. Japo tulimuita mzungu lakini sikujua jina hilo limetokana na nini. Nilishangaa kuona watu weupe kiasi kile pindi wazungu hao walipokuja. Walileta mradi wa lishe bora hasa kwa wanawake na watoto. Tulihamasishwa kuhudhuria mafunzo yao hasa kwa wanawake wajawazito, na wenye watoto. Siku moja tukiwa kwenye mafunzo nilianza kuumwa. Kwa kuwa ulikuwa motto wa kwanza, na pia umri wangu ulikua bado mdogo, nilikuwa nina nguvu mpaka siku ya mwisho, hivyo sikuwa najua kuwa nimekaribia kujifungua. Siku hiyo, wawezeshaji walikua vijana wawili wa kiume, na mmoja mswahili akitafsiri.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nilipoanza kuumwa, bahati mbaya nilipata kifafa cha mimba. Mmoja kati ya wawezeshaji ambaye alikuwa pia ni daktari, alinibeba na kunikimbiza kwenye gari yao na kisha kunipeleka hospitali. Kijana huyo ambaye ndiye tulikupa jina lake, alijitahidi sana kuokoa maisha yako kwani kulingana na maelezo yake, hali kama yangu ilihitaji aidha madaktari wa utaalamu wa juu sana au operesheni, ili kuokoa maisha yangu na yako. Na kwa kuwa mazingira ya hospitali hayakuwa salama kwa operesheni hasa kwa wakati huo, Dokta Nathani alijitahidi kuokoa maisha yetu bila ya operesheni. Namshukuru Mungu sana kwajili yake, na zawadi pekee kwake ilikuwa ni kukupa wewe jina lake.”



    Mama alimaliza hadithi yake tuliyoisikiliza sote kwa makini na msisimko, na dakika chache baadaye baba alirudi nyumbani ikiwa ni tayari saa tano usiku. Cha ajabu baba alikuja na matokeo yangu. Sikuwahi kujua kuwa baba alifurahia jitihada zangu shuleni mpaka siku hiyo. Nilikuja kujua badae kuwa baada ya ile hadithi ya mama ya siku ya maafali, baba aliwatangazia watu wengi sana kuwa kijana wake ana akili kuliko watoto wote shuleni kwao na hivyo atapata shule maalumu. Hivyo nadhani aliposikia matokeo yametoka alikuwa na wasiwasi mkubwa kuliko mimi niliyefanya mtihani. Baba yangu alinipa pongezi kubwa sana usiku huo, na kisha kutueleza kuwa muda wote alikuwa anahangaika apate hayo matokeo siku hiyoiyo. Sikujua alipoyapatia, ila nina hakika alihangaika sana kwani haikuwa rahisi kwa vijijini kupata matokeo siku hiyo.



    Kwa furaha kubwa baba yangu aliniahidi kunisomesha Sekondari. Mama alilia machozi, nami pia. Hata kama asingetimiza ahadi hiyo, bado ilikuwa na maana kubwa sana kwangu. Kitendo cha yeye kukubali sasa kwa moyo mweupe nikasome ilimaanisha sitawaza tena mama anateseka kiasi gani nikiwa shule. Alinipa kikaratasi cha jina la shule kwani hakuweza kilitamka vizuri yeye mwenyewe, na nilifurahi mno kuona nimepata shule niliyokua naisikia kwenye magazeti. Mungu alikuwa amejibu maombi yangu matatu kwa wakati mmoja, kwanza ni kumfanya baab akubaliane mimi kusoma, na pia yeye mwenyewe kukubali kunisomesha, lakini pia kunipatia shule nzuri sana. Sasa nilijiona nikianza kuishi ndoto zangu kwani mkono mkubwa wa mafanikio ulikuwa juu yangu.



    Baada ya miezi kadhaa nilienda kuanza elimu ya Sekondari. Baba kama alivyoahidi, alininunulia mahitaji yote ya shule na kunilipia ada. Wakati huo rafiki yangu Mawazo pia alikuwa tayari amepangiwa shule nzuri sana chini ya wale wadhamini. Tofauti na mimi, yeye hakusoma shule ya Serikali, bali ya kidini, ya kanisa katoliki. Ilikuwa ni moja kati ya shule zilizofanya vizuri sana mkoani Mbeya. Yeye alitangulia kuondoka kwani walitakiwa kuwasili shule mapema zaidi, lakini pia maandalizi ya awali yote yalifanywa mapema na wale wadhamini. Siku tunaagana, sikutaka kumwonesha huzuni kubwa niliyokuwa nayo moyoni. Kilichonifanya nisilie ni uanaume tuu, japo yeye hakuweza kujizuia. Tulimsindikiza na kumuaga, lakini tuliahidi kuwasiliana kwa barua kadiri tutakavyoweza, hasa baada ya sote kufika shule tunazoenda kusoma.



    Siku ya kwanza shuleni Elbol kila kitu kilikuwa kigeni. Sura za wanafunzi wote na walimu zilikua mpya kabisa. Kwa muda nilijihisi mpweke lakini furaha niliyokuwa nayo ilizidi huo upweke. Nilioneshwa bweni langu na tulikua wanafunzi kadhaa wa kidato cha kwanza tukilala humo. Nilipewa kitanda cha juu na chini yangu alikuwa kijana mmoja, mdogo kidogo kwangu lakini sikumzidi sana kama vijana wengi wengine wa kidato cha kwanza. Kijana huyu, Athumani aliyetokea mkoa wa Mbeya, hakuonekana kama ni mtu ninayeweza kuzoeana naye ki urahisi. Alikuwa ni mtu mwenye uso mkali na alionekana asiyependa utani kabisa kwani ndani ya juma moja tu baada ya kufika alisababisha ugomvi mkubwa bwenini na kumpiga vibaya kijana mwenzake wa kidato cha kwanza.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mara kadhaa Athumani alionywa na kupewa adhabu lakini hakuonekana kama mtu wa kubadilika. Mwanzoni aliyafanya maisha yangu ya shule kuwa magumu, kwani kuna wakati aliniibia vitu vyangu kila mara niliposahau kufunga ‘tranka’ langu, pia alikuwa kijana mbabe zaidi kwa wenzake, na hakuna aliyekuwa juu yake. Nilishangaa kuna ugumu gani walimu kumshughulikia kijana huyo hata ikibidi kumfukuza shule kwani tabia zake hazikuvumilika si kwa walimu wala kwa wanafunzi, na ndani ya miezi sita tu, Athumani alikuwa ameshafanya matukio mengi makubwa shuleni.



    Mara nyingi, kwa shule nyingi za bweni, wanafunzi wa madarasa ya juu hupenda kuwaonea kidato cha kwanza, kuwanyanyasa na kuwafanyisha kazi. Kwa mwaka wetu ilikuwa tofauti kidogo; licha ya kuwa Athumani alikuwa mtoto mwenye shida nyingi sana, lakini alijizolea umaarufu kwa kuwa mtetezi wa kidato cha kwanza. Kama wewe ni kijana wa kidato kingine, ukimuonea kidato cha kwanza (wakati huo walituita ‘njuka’, basi ujue kwa hakika Athumani akijua atashughulika na wewe na hutorudia). Yeye hakukubali kushindwa hata siku moja. Kama angekuona umemzidi umri na hasa nguvu, angekuvizia wakati wowote na kukufanyia kitu chochote kibaya. Athumani hakuwa na rafiki kabisa, bali kila mtu kwake alikuwa sawa na mwingine. Alimuibia mtu yoyote pesa, chakula au kitu chochote, alidharau walimu na hata siku moja hakukaa kwenye makundi ya watu kama wanafunzi wenzake.



    Shuleni kulikua na nafasi za kutembelea shule za jirani mara chache, lakini Athumani hakuwahi kuongozana na wenzake kwenda. Kilichonishangaza ni siku ambazo wazazi au ndugu walikuja kututembelea shuleni, mara zote kijana huyu hakuwa na mgeni isipokuwa mzee mmoja wa miaka kama themanini hivi. Tukiwa kidato cha tatu ndipo nilikuja kugundua uhusiano wa Athumani na huyu mzee ambaye ndiye pekee alikuwa ndugu kwake.



    Ukiacha usumbufu wa Athumani ambao baadaye niliuzoea na kuchukulia kawaida, maisha yangu ya Sekondari hayakuwa na shida hasa kwa miaka mitatu ya mwanzo. Ilikuwa rahisi kujenga urafiki na wenzangu wengi sana kwani lengo letu kubwa lilikuwa moja, yaani kusoma na kufaulu kwa viwango vya juu. Sikuwahi kukutana na watoto wanaopenda kusoma kama niliokutana nao katika shule hii. Kila mwanafunzi alionesha ushindani mkubwa na kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi, nilikutana na watu kadhaa waliofanya vizuri zaidi yangu darasani



    Hata hivyo haikunivunja moyo kujiona kuwa nina wapinzani kadhaa kitaaluma waliofanya vizuri kuliko mimi. Nilisoma kwa jitihada kubwa mno, masaa yangu ya kulala hayakuwa mengi. Mara kadhaa nilipata barua kutoka nyumbani kwani mama alijua kusoma na kuandika, lakini pia nilipata barua mara kwa mara kutoka kwa Mawazo. Bado urafiki wetu uliendelea kuwa imara. Alinieleza maisha yake shuleni, changamoto na uzoefu mpya alokua akipitia nami pia nilimueleza kwa upande wangu.



    Siku za kutembelea wageni sikuwa na ndugu wala rafiki wa kunitembelea, lakini kwangu hilo halikua tatizo hata kidogo. Tulikaa na wenzangu kadhaa ambao pia hawakua na ndugu na kuwa na wakati wa kuongea na kupumzisha akili mbali na mambo yahusuyo shule. Nilikuwa pia na marafiki wa vidato tofauti pale shuleni, wakiwemo waliokua juu yangu, kwani umri wangu mkubwa na utulivu wangu vilifanya waone nafaa kuwa rafiki. Nilibahatika kuwa karibu sana na walimu akiwemo mwalimu mmoja wa hesabu kidato cha pili ambaye alikuwa rafiki yangu mkubwa sana kwa kipindi chote nilipokuwa shuleni hapo.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Siku moja nikiwa kidato cha tatu, usiku tumelala, niliamshwa na sauti kali sana ya kelele ya Athumani kutoka kitandani chini. Nilishuka kwa haraka na kumuuliza, tatizo nini, aliniangalia na kunambia kwa uwoga, ‘Naota’. Sikuwahi kumuona Athumani katika hali ya uwoga na wasiwasi kama siku ile tangu tumeanza shule. Alikua akitoka jasho japo kulikua na baridi kali, lakini pia mikononi alionekana kutetemeka. Aliniomba nisipande juu kitandani kwangu bali nikae naye au hata nilale pale chini. Nilimuuliza tatizo ni nini lakini hakutaka kunambia. Nilimkubalia na nikalala kitandani kwake japo ilikua imebaki masaa machache tu asubuhi ifike.



    Asubuhi, aliniamsha yeye na kuniomba sana nisimuhadithie mtu kilichotokea usiku. Nilimkubalia lakini nikamwambia baadaye tutakaa unielezee nini hasa kilikupata usiku. Kweli siku hiyo jioni, baada ya chakula cha jioni, tulikaa na Athumani sehemu ambayo watu hawakutuona, kwani haikuwa kawaida yake kuwa na maongezi na mtu yeyote, hivyo kama watu wangeniona naye ni lazima wangetaka kujua alikuwa akiongea nini na mimi





    “Nilizaliwa pekeyangu kwa baba na mama yangu ambao nikiwa na miaka minne wote walifariki kwa ajali na hivyo nikaanza kuishi na bibi na babu yangu. Nilipofika miaka nane, siku moja babu yangu alikuja kuniamsha usiku na kwenda na mimi sehemu ambayo tuliona mambo ya ajabu sana kiasi kwamba nashindwa kuyaelezea. Hapo ndipo nilipogundua babu yangu alikuwa mchawi maana kati ya vitu nilivyoona ni watu wakiwa watupu na wengine wakila nyama mbichi. Niliogopa na kulia huku nikimuuliza babu kwanini umenileta huku. Alinambia kwa ukali kuwa sitakiwi kulia kwani hilo ni jukumu kubwa ninatakiwa kukabidhiwa na hivyo inabidi nizoee.



    Tulirudi nyumbani kulala lakini sikuweza kulala tena usiku huo. Babu pia alikuwa amenionya nisimwambie mtu yeyote kwani nikifanya hivyo nitakufa. Sikumwambia mtu yeyote kweli, hata bibi ambaye aliniona jinsi nilivyobadilika baada ya usiku huo na kuwa mtu mwenye mawazo mengi. Japo alinifatilia na kuniuliza mara nyingi lakini sikuwahi kumwambia chochote, mpaka kifo chake. Kabla ya bibi kufariki, babu alinichukua mara kadhaa na kunipeleka sehemu tofauti, nikaona ,ambo ya kutisha sana lakini nakumbuka siku ambayo kesho yake bibi alifariki nilimuona babu tukiwa katika mizunguko alisimama mbele ya mtu mmoja mkuu wao, akahojiwa sana maneno ambayo mimi sikuelewa na mwisho aliongea kwa Kiswahili NAKUBALI KUMTOA, kisha akakaa chini kama mtu aliyenyeshewa na baadaye tukaondoka. Asubuhi babu aliamka hana raha hata kidogo na bibi alipoanza kuumwa babu hakutoka pembeni yake, lakini aliumwa kwa masaa machache tu na kufariki.” Alieleza Athumani huku akionesha wasiwasi mkubwa usoni.

    “Sikuwahi kukubaliana na kile ambacho babu alitaka niwe lakini sikuwa na namna. Baada ya kifo cha bibi yangu nilianza kuwa mtu mwenye hasira kali sana na huzuni lakini babu yangu alinipa ahadi nyingi sana kunifanya nitamani kuchukua nafasi yake ya kichawi. Japo ahadi zake hazikunishawishi lakini ilinilazimu nikubali na mpaka sasa tayari nimefanya mambo mengi maovu, lakini wakati nakuja shule tuliweka makubaliano kuwa sitafanya uchawi kabisa nikiwa shuleni. Babu alikubaliana kwa sharti la kuwa nitakapomaliza shule nitamrithi nafasi yake moja kwa moja na nitakuwa tayari kurithisha watoto na wajukuu zangu. Ukweli ni kuwa hii kazi siipendi hata kidogo na natamani ningekuwa na uwezo wa kuachana nayo. Katika maisha yangu yote wewe ndio mtu wa kwanza kukuhadithia, lakini jana usiku niliota nikipigana na babu yangu ngumi. Nilimpiga sana kiasi cha kummaliza nguvu lakini alipoona anashindwa alibadilika na kuwa mwenye macho makubwa na kucha ndefu sana kisha akatumia kucha zake kunitoboa shingoni ili aniue, na hapo ndipo nilistuka kwa kelele.

    Hii ndo sababu imenifanya niwe tayari kwa lolote na kukubali kuhadithia japo nakusihi usimwambie mtu. Najua babu atajua nimesema na atakuja kunimaliza lakini nitajua cha kufanya.” Alimaliza kuongea huku jasho jembamba likimtoka.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ni kweli kama alivyotegemea, kesho yake asubuhi babu yake alikuja shuleni. Nilichogundua ni kuwa, tofauti na wazazi wengine ambao hawakuruhusiwa isipokuwa siku za wazazi, yule mzee alimtembelea Athumani siku yoyote aliyotaka na hakuzuiliwa na mtu yeyote. Alimchukua na walikaa faragha kwa muda mrefu sana. Athumani aliporudi bwenini alikua ni mtu wa tofauti siku hiyo. Alizungumza na watu na alikaa sehemu ya kusomea, na cha ajabu hakusoma isipokuwa alitafuta kila wanaoongea na kukaa nao kupiga stori. Tuliporudi bwenini aliongea sana, na aliwapa watu hadithi za vichekesho kiasi kwamba watu walishangaa lakini hakuna aliyemuuliza. Tulichelewa kulala siku hiyo, kwani tulikaa mpaka saa saba usiku.



    Asubuhi ilipofika, tuliamka mapema na kwenda kwenye ratiba yetu ya siku kwani ilikua Jumatatu. Sikuzote Athumani alikua na kawaida ya kuwahi sana kuamka lakini siku hiyo ilikua tofauti. Nilimpiga begani kidogo nilipoona haamki nikaachana naye. Saa nne, wakati wa mapumziko, akili yangu iliniambia nirudi bwenini. Sikujua ninachofata lakini nilirudi na kumkuta Athumani bado yuko kitandani. Nilianza kuogopa, nikamuita kwa nguvu huku nikimpiga mguuni, lakini hakujitikisa. Masikini, Athumani alikua ameamua kujiua. Pembeni ya mto wake aliacha barua yenye maelezo marefu zikiwemo lawama nyingi kwa babu yake. Aliandika kuwa nafsi yake haimruhusu kuishi maisha yake yote kama muuaji na adui wa watu wote. Alisema ni bora kuondoka mapema kuliko kuendelea kupoteza maisha ya watu wengine. Kiukweli niliumia sana.

    Taratibu zilifuatwa na kwa bahati mbaya yule mzee hakuweza kushtakiwa kwa lolote, kwani si tu kuwa serikali haiamini mambo ya uchawi, bali pia nguvu zake za kichawi kwa namna moja ama nyingine zilimpa ulinzi na jeuri juu ya sheria.



    Nilikua nikienda nyumbani likizo mara moja tu kwa mwaka, na kwa bahati yule rafiki yangu mwalimu wa hesabu aliniruhusu niishi kwake likizo za katikati ya mwaka. Hali ya uchumi haikuniruhusu kusafiri mara kwa mara, na kwangu hili halikuwa tatizo. Mara zote niliporudi nyumbani ilikuwa ni furaha isiyo na kifani. Wadogo zangu, akiwemo kipenzi cha baba, Neema, pamoja na mama walifurahi mno kuniona. Najua na baba pia alifurahi, hasa nilipompa ripoti za shule zilizoonesha mara zote nafanya vizuri. Japo hakujua kusoma, lakini kila nilipoleta alitembea nazo kama juma zima akiwaonesha rafiki zake kijana wake alivyo na akili.

    Likizo ya kumaliza kidato cha tatu, nilirudi nyumbani. Tofauti na siku zote, nilikuta hali si nzuri nyumbani. Baba alikuwa anaumwa sana. Kwa taarifa nilizokuta alikua ameumwa kwa muda wa wiki tatu sasa. Hospitali walisema ana tatizo kubwa la figo ambalo limetokana na sumu kali za pombe alizokuwa akinywa.

    Nakumbuka tangu tukiwa watoto baba alikuwa mtu wa kulewa sana. Baada ya Neema kuzaliwa alipunguza sana kulewa, lakini kuna mara chache alizolewa sana. Tatizo kubwa zaidi, pombe walizokuwa wakinywa wazee wengi pale kijijini ni kali mno, na ilikuwa ni kama sifa na uanaume mtu kunywa pombe kali hivyo wamama waliokuwa wanauza pombe walilazimika kutengeneza pombe kali sana ili kupata wateja.



    Likizo yangu haikuwa nzuri kabisa. Nilikuwa sijui cha kufanya kwani hali ya baba ilizidi kudorora kila siku. Hospitali walikua wamemtibu lakini mwisho walisema matibabu yake ni lazima asafirishwe kwenda Dar es Salaam, ambapo gharama zilikuwa kubwa mno. Hatukuwa na jinsi zaidi ya kumuweka nyumbani apumzike tu. Niliandika barua shuleni kuwataarifu hali halisi ya nyumbani kupitia rafiki yangu mwalimu, hivyo nipewe ruhusa ya kuchelewa kidogo. Baba alikuwa hajiwezi tena, alijisaidia haja ndogo na kubwa hapohapo na alishindwa kula. Alituita sote kuzungumza nasi na mara zote maneno aliyorudia tena na tena ni kutuomba msamaha, hasa mama yangu. Mateso makali aliyokuwa akiyapata, kwake ilikuwa ni bora kufa kuliko kuendelea kuishi. Mara kadhaa aliomba aitiwe mchungaji na aliongozwa maombi ya kutubu kila mara. Sikuwahi kumuona baba yangu akikanyaga kanisani tangu napata akili ya kujua mema na mabaya, japo siku zote mama alihakikisha tunaenda kanisani. Lakini alipoanza kuzidiwa, aliweka sheria kila siku ya Jumapili lazima aje kiongozi walau wa ngazi za chini kutoka kanisani amuombee.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Likizo ilikua ni ya mwezi mmoja na wiki moja, lakini iliisha nikiwa bado namuuguza baba. Nikiwa kama kijana mkubwa, ilinilazimu kukaa kumsaidia mama kazi kubwa ya kumuuguza baba. Mama alijitahidi kuwa na nguvu mara zote, na alikuwa akimtia moyo baba kuwa japo hali ni mbaya sana, lakini bado kuna nafasi ya kuishi. Najua zilikua siku ngumu sana kwa mama. Watoto nane tulitegemea nguvu na ujasiri wake, na kama angeonesha kukata tamaa basi ingekua adhabu kwetu sote. Mdogo wangu wa mwisho ambaye kwa wakati huo alikua na miaka karibia sita, ndiyo nadhani alimfanya mama ajitie nguvu sana. Neema ambaye alikuwa kipenzi cha baba sana alishinda chumbani kwa baba muda wote. Kila wakati alipoona baba akilalamika maumivu, alimpa pole na kujaribu kumsaidia kwa namna yoyote ile. Mara nyingine alimpa dawa yoyote aloiona, alitaka kumpa maji, alimfuta usoni kwa mkono wake mdogo, alimshika mkono, yaani ilimradi tu kumuonesha kuwa yuko tayari kumsaidia.



    Kila nilipomuangalia Neema nilitamani baba aendelee kusogeza siku. Kwake uwepo wa baba katika hali mbaya ya ugonjwa ulikuwa na maana kubwa mno kuliko angefariki. Rafiki yangu Luzoki (Mawazo) naye alikuwa likizo. Nilitamani kama ule wakati tuliokua tunautazamia baada ya kumaliza elimu ungekuwa umefika. Niliamini kama ningekuwa tayari nimemaliza shule na kupata kazi nzuri, ugonjwa wa baba yangu usingekuwa tatizo kwani ningempeleka Dar es Salaam kwajili ya matibabu bila kujali gharama.

    Tuliuanza mwaka mpya 2005 bila amani hata kidogo. Kiukweli kila siku ambayo baba alikua akiishi niliamini ni kwa neema tu. Siku za baba za mwisho zilikuwa nzuri kidogo, kwani alianza kupata nafuu kiasi hadi cha kwenda kujisaidia uwani, japo kwa kupelekwa. Tuliamini kuwa Mungu ametuhurumia na kutenda muujiza, lakini wakati sote tunaona matumaini, baba mwenyewe alikuwa akituaga kila siku. Kwa muda wa kama wiki hivi, baba alipata nafuu kwa kiasi kikubwa. Mdogo wangu Neema, japo alikuwa na furaha lakini kuna wakati aliamka asubuhi akiongea vitu vya kushangaza. Mara alisema nilimuona baba usiku anasafiri kwenda mbalii, wakati mwingine alisema kuna watu wazuri walikuja usiku kumchukua baba, na karibu kila asubuhi kwa wiki nzima aliamka mapema sana akakimbilia chumbani kwa baba kuangalia kama yupo.



    Mama aligundua hivi ni viashiria kuwa wakati wa baba kufariki umekaribia. Siku moja baada ya chakula mama alikaa nasi watoto wake wakubwa na kutuambia, “Wanangu, baba yenu anaumwa na kila siku anatuaga. Nataka mjue, tunamuamini Mungu lakini pia ikiwa ni mapenzi ya Mungu apone atapona, vinginevyo Mungu atatupa nguvu na ujasiri wa kukabiliana na lolote. Cha msingi kwa sasa ni kumuomba Mungu na kutokuwa waoga, na pia kuamini kuwa yeye ndo muweza wa yote”. Binafsi nilijua kweli kifo cha baba hakiko mbali, na japo hayo maneno aliyosema mama yalikuwa magumu sana kwake kutamka hasa kwa watoto wake, lakini ilibidi atusaidie kujiandaa endapo baba hatapona.



    Hatimaye tarehe 16 mwezi wa kwanza mwaka 2005 baba alifariki. Asubuhi mama aliamka na kumuacha kitandani na Neema kama kawaida yake alikimbilia chumbani kwa baba na kumuita kwa nguvu, bahati mbaya alikua ameshafariki. Neema aliita san asana huku akimsukuma lakini hakuamka. Alitoka mbio kwenda kwa mama kumwambia baba haamki. Mama alikimbia chumbani na kweli alihakikisha baba amefariki. Kilichofuata ni ujio wa majirani na taratibu nyingine, lakini kama kuna siku niliwahi kuumizwa na mdogo wangu Neema, ni pindi baba yangu alipofariki.

    Tukiwa msibani siku ya kwanza Neema aliuliza maswali na kuongea vitu vingi vya simanzi. “Baba mbona haamki? Wamempeleka wapi? Afu alikua wabaridii. Au ndio wale watu wazuri wamemchukua? Watamrudisha? Wamempeleka mbaliii, niliwambia wanichukue na mimi wakakataa.” Hayo ni baadhi ya maswali aliyokuwa akiuliza Neema ambayo hakuna aliyekuwa na majibu ya kumpa. Alimuuliza mama, mimi na kila aliyekaa naye karibu. Alitaka kukaa na mama muda mwingi kwani alitaka ambembeleze, japo watu walimchukua mara kadhaa kumpa nafasi mama.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Siku ya mazishi Neema alilia sana alipoona baba anawekwa kaburini na kufukiwa. Akili yake ndogo haikuweza kuelewa kwanini baba anazikwa. Alisema kama wale watu wanamchukua watampataje akiwa chini ya mchanga? Aliomba sana wasimfukie baba lakini ni kama mtu aliyekua analia bila msaada. Niliumia kuona jinsi Neema anavyolia kwa uchungu huku akibembeleza wasimfukie baba yake. Mama na kila mtu ambaye msiba ulimgusa, walilizwa sana na Neema, lakini mwisho wa maisha ya baba ulikuwa umefika na hakuna namna tungefanya kuzuia hilo



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog