Simulizi : Mwangaza
Sehemu Ya (2)
Nilirudi shule wiki moja baada ya kumzika baba yangu. Nikiwa njiani nilikua nikiwaza sana maisha yatakuaje baada ya baba kufariki. Ni kweli mwanzo wa shule yangu baba alikuwa mpinzani mkubwa sana lakini kwa sasa alikua ameshakubali nisome na alikua ni yeye ananilipia ada. Bahati mbaya hakuacha mradi wowote ambao labda ungeendelea kuingiza pesa kwa familia. Mama alikua na mzigo mkubwa tayari na nisingetamani ada yangu iwe jukumu lake.
Nilizungumza na mwalimu wangu kwa kirefu, yule rafiki yangu (Mr. Olengai), kumuelezea yaliyojiri nyumbani. Kwa kiasi kikubwa Mr. Olengai alifahamu maisha yangu ya nyuma mpaka nilipofikia, na alijua uwezo wetu haukua mzuri, kwa bahati mbaya naye hakuwa na uwezo wa kunipa msaada wa kiuchumi kwani alikuwa ni mtu mwenye familia. Msaada alokua akinipa wa kuniruhusu nikae kwake tayari ulikua mkubwa sana na nisingetamani kumbebesha mzigo mwingine wa ada, japo nilifahamu jinsi alivyotamani kunisaidia.
Huku nikitafakari ni namna gani nitapata pesa ya kunisaidia kumaliza kidato cha nne bila shida, siku moja tulikaa na Mr. Olengai kuongea kwa kirefu stori mbalimbali za maisha. Baadaye nilipata wazo la kutafuta kazi nitakayoweza kufanya kwa muda wangu wa ziada. Tatizo ilikuwa ni kazi gani nitakayoweza kufanya ambayo haitakula muda wangu wa masomo, lakini pia nilikuwa sielewi kama naweza kupata hiyo nafasi huku nikiwa shule. Mwalimu alinipa wazo la kufundisha masomo ya ziada, yaani tuisheni. Ilionekana ni wazo zuri kwani halingenifanya nishindwe kuendelea vizuri na masomo yangu, lakini ningepata wapi wanafunzi, na ningewafundisha wakati gani? Hayo ndo maswali yalikuwa yakinisumbua kichwani.
Mr. Olengai aliniahidi kushughulikia kila kitu ndani ya wiki mbili. Kweli baada ya wiki mbili tulipoongea tena, alikuwa ameshughulia hilo suala kama alivyoahili. Alizungumza na mwalimu mkuu aniruhusu kuwa natoka shule baada ya muda wa darasani, pia alikuwa amenitafutia wanafunzi wa kidato cha kwanza kuwafundisha kama sita wa kuanza nao. Hii ilikua habari njema sana kwangu. Japo hawangenipa pesa nyingi lakini kufanya hivyo kila siku, lilikua ni wazo ambalo kwanza litanifanya nikusanye pesa kidogo kidogo lakini za kutosha kunisaidia, pia aliniaminisha kuwa idadi ingeendelea kuongezeka. Tulipanga kuwa na muda wa saa moja na nusu kila siku, na kwa bahati nyumba ya mwalimu haikua mbali na shule ambapo ndipo ningefundishia.
Nilimuandikia mama barua upesi kumtoa wasiwasi alokua nao juu ya ada yangu. Najua habari hii ilikua njema mno kwake. Nilimueleza mpango mzima wa kufundisha tuisheni, na kama kawaida yake, alipojibu hiyo barua aliandika na barua nyingine kwa Mr. Olengai kumshukuru. Haikua changamoto kwangu kufundisha, kwani kama ambavyo mwalimu wangu aliamini, nilikua nikiyamudu vizuri masomo ya kidato cha kwanza. Wanafunzi wangu walinipenda na pia kama ambavyo tulitegemea, hawakuchukua muda mrefu kuanza kuongezeka. Ndani ya miezi miwili nilikua na wanafunzi karibu ishirini, na sasa ilianza kuwa changamoto juu ya mahala pa kufundishia kwani sehemu tulokua tukikaa haingetosha wanafunzi wengi.
Baadaye nilianza kuwa nakodisha viti kwajili ya darasa langu, na kwakua muda haukua unaniruhusu, niliamua niweke mkazo kwa kidato cha kwanza tu japo kuna wanafunzi wa kidato cha pili pia walianza kuniomba niwafundishe. Nilifundisha masomo ya Kemia na Biolojia, na kiukweli vijana wangu walikua wakifanya vizuri shuleni jambo ambalo lilinitia moyo. Mwaka wangu wote wa kidato cha nne nilitumia muda wangu wa ziada kufundisha, nilianza kupata pesa si tu kujilipia ada, lakini baadaye nilipata hata pesa za kumtumia mama nyumbani. Hii ilikua faraja kubwa sana kwa mama yangu kwani hali ya maisha kwake haikua sawa na wakati baba akiwa hai.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilimaliza kidato cha nne mwaka 2005 mwezi wa 11, tukafanya maafali ya kawaida shuleni na kisha nilirudi nyumbani. Wakati huo tayari nilikuwa natengeneza pesa nyingi sana kutokana na tuisheni niliyokuwa nafundisha, hivyo nilifikiria kuwa nirudi nyumbani kwa muda mfupi tu na kisha nifanye taratibu za kurudi Arusha kuendelea kufundisha. Hali ya maisha nyumbani kidogo haikuwa nzuri, pia nilipanga kusomesha wadogo zangu wa mwishoni, ambao umri ulikuwa bado unaruhusu yaani Neema na kaka yake walofatana ambaye sasa alikua na kama miaka tisa.
Nilikaa wiki moja tu nyumbani na kumuachia mama pesa ya kuwaandikisha shule kisha nikarudi Arusha kuendelea na kazi niliyokua nafanya. Namshukuru sana Mr. Olengai daima kwani mimi kurudi na kuishi kwake haikua taizo hata kidogo. Nilijitahidi nisiwe mzigo kwake kwa kuchangia matumizi kwa kadiri nilivyoweza na kwa kiasi kikubwa nadhani hilo lilifanya familia yake inipende zaidi. Tuliishi kama ndugu. Matokeo yangu yalitoka nikiwa Arusha na haikuwa tofauti na mategemeo yangu sana kwani nilipata daraja la kwanza la kiwango cha pili (divisheni 1.8). nilitamani kushiriki furaha yangu na mama pamoja na wadogo zangu lakini majukumu yalikuwa yamenitenga mbali nao kwa muda. Mwalimu alifurahia sana sana matokeo yangu utadhani ni mzazi wangu.
Matokeo ya kupangiwa shule yalipotoka hayakuwa mazuri kwangu, kwani nilipangiwa shule ya mkoa wa Tabora (Tabora boys) kusoma kidato cha tano. Mwalimu alinishauri tufatilie uhamisho na aliahidi angenisaidia kufanya hivyo. Tulifatilia uhamisho kweli, na japo ilisumbua kidogo kiasi cha kunifanya nichelewe kuanza shule lakini nilifanikiwa kupata uhamisho na kurudi shule ile ile Ilboru kwa masomo ya udaktari yaani Fizikia, Kemia na Biolojia. Kabla sijaanza kidato cha tano nilikuwa tayari nina wanafunzi wengi wa kufundisha tuisheni hivyo nilikua nina akiba ya kutosha kujilipia ada mbali na pesa nilokua nikimtumia mama.
Shuleni pia haikuwa ngumu sana kuendelea na madarasa yangu kwani mkuu wa shule alikua yule yule ambaye tayari alikuwa anajua maisha yangu, na alishaniruhusu kufundisha tangu nyuma. Nilisoma na kufanya kazi kidato cha tano na cha sita, huku nikiendelea kumtumia mama pesa kila mwezi ya kusomesha wadogo zangu na ya matumizi ya nyumbani. Wakati huo pia nilifanikiwa kuweka akiba ya kutosha kila mwezi. Nilifungua akaunti ya benki kwani nilijua kadiri siku zinavyoendelea ndivyo ninavyohitaji pesa nyingi kukidhi mahitaji yangu na ya watu wanaonitegemea.
Kama kawaida pia bado shuleni nilifanya vizuri. Kikawaida masomo ya udaktari ni magumu kidogo lakini jitihada nyingi nilizoweka kwa elimu yangu, na pia malengo niliyokuwa nayo yalinifanya nisitetereke. Tangu nilipoanza kidato cha tano mwaka 2006, nilijigundua kuwa sasa naelekea utu uzima. Kila nilipofikiria nina wadogo zangu saba ambao hawana baba, nilijiona kama tayari baba mwenye familia. Mama alijitahidi kunifanya nisiwaze kama mtu mwenye majukumu, yani nibaki kwenye hali ya kujiona mtoto na si mzazi lakini kiukweli haikuwa rahisi. Pia umri tayari ulikua umesogea kwani kwa wakati huo nilikua ni kijana wa miaka zaidi ya ishirini. Kilichoniumiza zaidi ni kuwa kati ya wadogo zangu saba, watano hawajasoma kabisa, na hivyo nilijiona jinsi gani nina mzigo mkubwa mbeleni. Kwa wale wakubwa walifanya vibarua huko kijijini na hivyo kuchangia matumizi ya nyumbani.
Nikiwa kidato cha sita nilienda nyumbani kuwasalimia walau kwa siku chache, ile likizo ya mwisho wa mwaka. Tulipewa likizo fupi sana kwani tulikuwa tunajiandaa na mitihani ya mwisho. Nyumbani, kila mtu alikua mzima, anaendelea vizuri, na hii ilinifariji hasa kuona Neema amezoea maisha bila baba na amerudi kwenye hali yake ya kawaida. Baada ya baba kufariki, mtoto alipata shida sana kuwa sawa. Alikuwa mnyonge kupita kiasi, ulaji wake ulibadilika sana na alipata homa mara kadhaa. Kwa muda wa kama miezi sita hali ya Neema ilikuwa si nzuri kabisa, japo hospitali hawakuwa wakiona ugonjwa wowote. Madaktari walishauri kwa kipindi hicho mama na ndugu zake wengine wawe karibu naye sana na kuhakikisha hapatikani na vitu vya kumkwaza au kumuumiza. Hivyo kuona sasa Neema amerudi kuwa sawa, amechangamka na anasoma, ilinipa moyo sana.
Jambo lililoniumiza kichwa kiasi ni mdogo wangu tuliyefatana, kwa wakati huo alikua na miaka 24, alikua anataka kuoa. Mama alijaribu kumwambia asubiri kidogo akihofia mimi kaka yake nisingeridhia uamuzi wake. Sikutamani aoe mapema kweli, kwani majukumu ya nyumbani yalihitaji nguvu zake pia, na nilijua baada ya kuoa atakuwa na familia ya kumtegemea, watoto na mke na hivyo ingebidi ahamishie nguvu zote kwa familia yake binafsi. Lakini kwa maisha ya pale kijijini, kijana wa miaka 24 alikuwa ni mkubwa kiasi cha kutosha kuendesha familia. Vijana wengi walioa wakiwa na kati ya miaka 19 hadi 25 hivyo hata yeye alionekana amechelewa. Pia kwakua yeye hakusoma kabisa, alikuwa tayari ameshakuwa na mahusiano ya mapenzi kadhaa na sasa ilikuwa ni muhimu aoe kuepuka mahusiano zaidi kabla ya ndoa.
Mama aliponiambia, japo nilistuka kidogo, lakini sikuonesha kuwa ni suala ambalo siliafiki. Nilimuita Mazoya, mdogo wangu, na kuongea naye kwa kirefu kujua kuhusu uamuzi wake. Ilionekana ni mtu ambaye tayari amefanya maamuzi na kama ningeridhia angeoa hata wiki iyo hiyo. Sikuruhusu hilo kwa sababu muda wangu pia haukuniruhusu kusimamia taratibu za mahali na ndoa hivyo nilimuomba anisubiri nikamalizie shule, kwani ilibaki miezi kama mitatu tu.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Rafiki yangu Luzoki (Mawazo) pia alikua amerudi likizo. Urafiki wetu ulikuwa bado imara kama awali, na tulikua tukiendelea na mawasiliano siku zote, lakini safari hii ilikuwa ni kama ya mwisho kwetu kuonana. Luzoki alipata ufadhili wa kwenda kusomea nje elimu ya chuo kikuu. Ilikuwa inasubiriwa amalize kidato cha sita tu kisha aende Uingereza. Changamoto iliyokuwepo ni kuwa, ufadhili huo uliwataka wazazi wake wachangie baadhi ya gharama. Alitakiwa kujitafutia pasi ya kusafiria, viza na nauli ya kutoka Singida mpaka Dar es Salaam na pia gharama za kufikia Dar na kukaa siku chache kabla ya kuondoka, kwani pasi na viza alitakiwa kuvishughulikia akiwa Dar. Alikuwa na msaada wa wafadhili namna ya kupata viza lakini gharama ilikuwa juu yake.
Tulipoongea kwa kirefu na Mawazo, niligundua kuwa suala la gharama linamuumiza kichwa kwani kwa maisha ya pale kijijini, kukusanya pesa zaidi ya laki tano, ilikuwa ni ngumu. Wazazi wake walikua na kiasi kadhaa lakini bado pesa nyingi ilikuwa inahitajika. Aliongea na mimi kama rafiki yake lakini hakuwa anategemea msaada wowote kutoka kwangu kwani alijua japo nafanya kazi ya ualimu lakini kipato nnachopata kitakuwa ni cha kukidhi mahitaji ya familia yangu tu. Nilimtia moyo na kumwambia kuwa tumwombe Mungu, kwani yeye ndo aliyempatia hiyo nafasi kwahiyo atampatia njia sahihi ili aweze kufanikisha safari.
Usiku wake nilikaa na mama kuongea naye kuhusu suala la Luzoki na uhitaji wake wa pesa. Mama alijua kuwa ninaweka akiba, lakini hakujua ni kiasi gani. Pia alifahamu jinsi gani tulivyokuwa marafiki na Luzoki, hivyo alihisi ninatamani sana kumsaidia, lakini kiasi cha pesa kilichokuwa kinahitajika kilikua ni kikubwa sana kwa mtazamo wake. Nilimwambia mama kuwa akiba yangu inaniruhusu kumpa kiasi chote alichopungukiwa. Mama alishangaa lakini pia hakuonesha kulikubali wazo langu mwanzoni. Alijua kuwa nafanya kazi kwa bidii sana kupata pesa ya kutunza familia, lakini pia mbele yangu nilikuwa nina elimu ya chuo kikuu ambayo bado nilikuwa sijajua kama nitapata fursa ya kusomeshwa au nitajisomesha.
Nilijaribu kumshawishi mama kwa muda lakini kwa usiku huo sikufanikiwa. Kwa bahati mbaya pia sikuwa na muda zaidi wa kushauriana naye kwani siku mbili zilizofuata ilinilazimu kuondoka kurudi shule, na pia Luzoki naye alikuwa anakaribia kuondoka kumalizia shule. Niliamua kwa mara ya kwanza nipingane na mama yangu kwajili ya rafiki yangu. Siku iliyofuata asubuhi nilienda mjini mapema kuchukua pesa benki, kiasi kile kile ambacho alipungukiwa. Nilivyorudi, nilienda kwao moja kwa moja lakini sikumkuta. Alikuwa akizunguka kwa baadhi ya ndugu zake kuangalia kama wataweza kumchangia. Nilimsubiri kwa muda kiasi lakini nilipoona anachelewa, nilimuachia baba yake bahasha yenye pesa na kumuomba asiifungue, bali amkabidhi tu Luzoki akirudi.
Saa tatu usiku nilimsikia Luzoki akigonga hodi nyumbani, kwa nguvu na msisimko. Nilikaa naye nje kumsikiliza. Kama kawaida yake alishindwa kujizuia kulia. Hakutaka kuchukua ile pesa yote kutoka kwangu. Alijua nina majukumu mengi, na pengine alihisi labda hata nimekopa ili nimfadhili. Alirudi na nusu ya ile pesa na kuniomba niichukue huku akinishukuru sana kwa msaada mkubwa niliompa. Ilibidi nimueleze kuwa nimekuwa nikiweka akiba kwa muda mrefu sasa na pamoja na kumpa pesa yote hiyo, bado nimebakiza akiba kwenye akaunti yangu. Pia nilimwambia bado nitaendelea kufanya kazi na kukusanya pesa hivyo asiwe na wasiwasi kabisa kuhusu ile pesa. Nilimuhakikishia kuwa nimempa na wala sijamkopesha, lakini pia sijakopa popote. Ilikuwa vigumu kumshawishi Mawazo kuikubali ile pesa, lakini ilimbidi akubali tu, kwani nilijua pia hata angekataa, hakuwa na sehemu nyingine ya kupata pesa. Tuliagana na Mawazo na huo ndo ulikuwa mwisho wa kuonana kwetu kwa pale kijijini, mpaka tulipokuja kuonana tena miaka nane baadaye
Mama alipojua nimetoa pesa yote ile kumpa Mawazo, hakufurahia hata kidogo, lakini hakuwa na cha kunifanya. Lakini aliyenikasirikia zaidi ni mdogo wangu Mazoya ambaye alitegemea kwa kuwa anakaribia kuoa na mimi ndiyo kaka mkubwa basi ningempa msaada mkubwa wa kifedha. Alimwambia na baba yangu mdogo kuhusu hilo suala, na kwa kiasi ilizua mgogoro katika familia japokuwa siku zote, hakuna ndugu aliyekuwa anajali familia yetu kwa mahitaji ya kifedha. Kwa mara ya kwanza, siku hiyo mdogo wangu alinikaripia na kuongea vibaya na mimi. Mama yetu alijitahidi kutulea kwa adabu kweli na wadogo zangu walikuwa wakiniheshimu na kunithamini sana, ila pia tulipendana kwa dhati sote.
Nilijisikia vibaya hasa kwakua siku zote sikutamani kufanya jambo lolote kinyume na mama yangu. Sikuwa na muda zaidi kukaa nyumbani hivyo niliacha hali ya kutokuelewana, nikarudi shule. Namshukuru Mungu, barua iliyofuata kutoka kwa mama alikuwa ameridhia uamuzi wangu na kunibariki. Alituma barua mwezi mmoja na kitu baada ya mimi kurudi shule, akisema kuwa amekaa na kutafakari jinsi Luzoki alivyokuwa amenisaidia huko nyuma na pengine bila yeye nisingekuwa vile nilivyo. Nilifarijika kuona kuwa amani kati yetu imerudi. Nadhani pia mama aliniwazia kuwa kama angeendelea kunilaumu na nilikuwa nakaribia mtihani labda ingeathiri masomo yangu
Mtihani wa kidato cha sita ulikaribia lakini zikiwa zimebaki wiki tatu tu, nilianza kuumwa. Kikawaida mimi si mtu dhaifu, na pia si mtu wa kuugua. Nadhani mwili wangu una kinga kubwa kwani tangu naanza kupata akili sikuwa nimewahi kuumwa mpaka kufikia kulazwa. Siku hiyo nilianza kusikia tumbo linakata sana, na kama linajaa. Niliumwa sana tumbo kiasi cha kushindwa kufanya chochote. Nilipelekwa hospitali na uongozi wa shule, hospitali ndogo ya jirani, lakini ilionekana tatizo ni kubwa hivyo ilibidi nikimbizwe hospitali ya mlima Meru (Mount Meru Hospital). Nilipelekwa chumba cha dharura (emergency) kwani mpaka kufika pale hali yangu ilikuwa mbaya sana. Mwalimu Olengai alihakikisha napata huduma za haraka.
Baada ya vipimo, ilionekana nina ‘kidole tumbo’ (appendix). Kwa kifupi, kuna kiungo kimoja ndani ya tumbo ambacho ni kama hakina kazi kwani hata kikitolewa hakuna madhara, lakini kinapokuwepo hua kinafanya kazi ya kukusanya vitu visivyosagika kama mchanga au mchele mbichi na kuhifadhi. Tatizo linakuja hicho kiungo (kidole tumbo) kikijaa. Wasipokiwahi kikapasuka, mtu huweza kupoteza maisha. Maumivu makali niliyokua nasikia ni kwa sababu kidole tumbo kilikua kimejaa. Daktari alisema ningechelewa kidogo pengine kingepasukia na hivyo ningeweza kupoteza maisha. Ilitakiwa nifanyiwe upasuaji wa haraka sana. Mtu wa kusaini upasuaji wangu alikuwa ni mwl. Olengai na alifanya hivyo bila kusita. Shule iligharimia matibabu yangu kwa kiasi ila ilinibidi niongeze pesa binafsi kukamilisha deni kabla ya kuruhusiwa. Hiyo ilinifanya kumaliza akiba yangu yote maana matibabu yalikuwa na gharama ya juu kidogo. Kulala hospitali wiki nzima, na upasuaji uliofanyika, viligharimu pesa nyingi hasa ukizingatia nimetoka kumpa rafiki yangu kiwango kikubwa cha pesa.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nikiwa hospitalini mlima Meru, jirani kulikuwa na mwanaume amelazwa anaumwa. Huyu baba alikua ana familia kubwa inaonesha na watu wake walimjali sana. Kila mara walikuja watu wapya na muda wa kuona wagonjwa haukuwatosha siku zote. Lakini kuna sura kadhaa zilijirudia kila walipokuja kumuona huyu mzee, ikiwepo sura ya binti mmoja mweupe mwembamba. Siku za mwanzo nilikua naumwa hivyo sikufatilia chochote kilichokua kinaendelea wodini, lakini siku mbili baada ya kufanyiwa operesheni niligundua kuwa huyu binti alikuwa kila akija wodini kumuona huyo mzee, alitembelea vitanda vya wagonjwa karibu wote. Waloweza kuongea aliongea nao kidogo na kuwapa pole huku akiwatia moyo. Nilipoanza kupata nafuu alikuwa akija pia kwenye kitanda changu na kunijulia hali. Nilifarijika kuona kuwa kuna mtu zaidi ya Mr. Olengai ambaye alikuwa akinijulia hali mara kwa mara kwani kila akija lazima alifika kitandani kwangu. Kwa siku walikuja hospitali mara tatu au walau mbili, na binti yule mrembo hakuacha kutembelea wagonjwa wote. Alipokuwa akija kitandani kwangu nilijitahidi kumpa tabasamu zuri na kuwa mchangamfu kwake, japo nilikua bado mwenye maumivu kiasi na hivyo sikuweza kuchangamka sana.
Siku moja kabla sijaruhusiwa kuondoka, nilidhani sasa nina nguvu za kutosha kuongea na binti yule, nimuulize kwanini alifanya hivyo alivyofanya siku zote. Pia nilitamani kujua yule mzee ni nani kwake na anaumwa nini. Siku hiyo jioni alipokuja, kwani huo ndio muda ambao angekaa masaa mengi kiasi wodini, nilimsubiri kwa hamu aje kitandani kwangu. Alipofika nilikua mchangamfu zaidi kwake kwani sasa nilikua nimepata nafuu sana. Tuliongea dakika kadhaa na kisha nilitupia maswali yangu. Binti alinambia yule mzee ni baba yake, ana tatizo la kibofu na kuna matibabu ambayo kidogo ni ya muda mrefu, anafanyiwa kwa hiyo wanategemea ataendelea kuwepo hapo hospitali kwa muda licha ya kuwa alishakaa wiki mbili tayari
Kuhusu kuzungukia wagonjwa, binti yule alinambia kuwa yeye ni mtu anayejaribu mara zote kujiweka kwenye viatu vya watu. Alisema kuwa anapoona watu wamelala vitandani, anahisi kuna wengine hawana hata ndugu wa kuwatembelea, wakati kitanda cha baba yake muda wote kimezungukwa na watu. Hivyo alijijengea utaratibu wakutembelea wagonjwa na kuongea nao, si tu kwa wakati baba yake akiwa amelazwa, bali tangu mwaka mmoja uliopita alipomaliza kidato cha sita. Japo alikuwa ni mwanafunzi wa chuo kwa wakati huo, bado haikumzuia kufanya hilo zoezi kila wiki. Nilimuomba anikumbushe jina lake tena ambalo siku ya kwanza kabisa alijitambulisha kwangu lakini sikuwa nalikumbuka tena. “Naitwa Angel”, alisema. “Mimi nitakuwa nakuita Malaika kwani ni malaika tu ndiyo wana tabia kama zako”, nilimtania huku nikitabasamu. Alipotaka kuondoka, nilimwambia pengine kesho asubuhi nikaruhusiwa hivyo tusionane tena. Tulipotazamana usoni, niligundua sote wawili tumeonesha sura za huzuni kidogo na kukaa kimya sekunde kadhaa. Nilimshika mkono na kumwambia,”Natamani tuonane tena”. Hakunijibu chochote zaidi ya kunambia kwaheri na kuondoka.
Ilikuwa mara ya kwanza najisikia vile nilivyojisikia niliposhika mkono wa Angel. Siwezi kuelezea sana, lakini nilihisi kama kweli nilishika mkono wa malaika. Hisia za ulaini wa mikono yake hazikutoka akilini mwangu usiku wote, na ni kama ni msichana pekee niliyewahi kumuona mrembo machoni mwangu, japo nilikuwa nimeona warembo wengi kabla. Nilipuuza hisia zangu ambazo zilijirudia mara kwa mara, kisha nikapitiwa usingizi. Asubuhi daktari alipita kitandani kwangu na kunambia kuwa sasa naweza kuruhusiwa. Rohoni nilikuwa natamani Mr. Olengai achelewe kidogo ili Angel aje tena kabla sijaondoka. Nikiwa naangalia mlangoni kila mara kuona kama atafika, mida ya saa 12.30 hivi alifika pamoja na ndugu zake. Nilitamani aanzie kwenye kitanda change lakini hicho kingekua kitu cha ajabu.
Angel alipokuja kunisalimia siku hiyo, japo muda wa kuona wagonjwa ulikua umekaribia kwisha, nilihakikisha natumia muda wetu kuongea mambo ya muhimu. Baada ya kusalimiana naye nilimuangalia machoni na kumwambia tena,”Nahitaji kuonana na wewe tena”. Sikujua nitampataje ila nilimpa anuani ya shule yangu na kumuomba aniandikie barua haraka iwezekanavyo. Nilikua kama mtu anayejaribu tu bahati yake kwani sikuamini kwa msichana mrembo na mwenye maisha mazuri kama huyu angeweza kukaa na kumtafuta kijana kwa barua ambaye hata hawafahamiani kwa ukaribu. Aliniangalia tu na kutabasamu na kisha akaondoka. Sikutamani dakika zile ziishe. Nilijua sasa naanza kuingia kwenye ulimwengu mwingine wa maisha kwani kama Angel angenitafuta, basi kwa hakika ningejenga naye urafiki wa mapenzi.
Niliporudi shule nilikuwa nimepoteza siku kadhaa za kujiandaa na mtihani kwani sasa zilibaki siku chache tu tuanze mitihani ya taifa. Kwa bahati nzuri maisha yangu ya kitaaluma yalikuwa yenye mkazo siku zote hivyo niliamini japokuwa ugonjwa ungeathiri matokeo yangu, ila si kwa kiwango kikubwa sana. Tulifanya mitihani ya kumaliza kidato cha sita mwaka 2008 mwezi wa pili, na tulimaliza salama kabisa, ikabaki matokeo tu. Baada ya kumaliza, nilikuwa na changamoto ya pesa kidogo hivyo ilibidi nibaki zaidi Arusha kuendelea kufundisha kwa muda walau wa miezi mitatu kabla sijarudi nyumbani kusalimia. Wakati huo nilikuwa nikifatilia sanduku la shule kila wiki kujua kama Angel alituma barua au la, na kwa bahati mbaya mpaka muda wa likizo yangu fupi unafika alikuwa hajatuma
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilirudi nyumbani kipindi ambacho matokeo yalikua yanakaribia kutoka kwani safari hii nilitaka niwe pamoja na familia yetu nikipata matokeo ya kidato cha sita. Pia ilikuwa imenilazimu kutafuta pesa zaidi kwajili ya mdogo wangu anayetaka kuoa. Kwa kijijini haikuwa gharama sana kuoa, lakini pia nyumbani kulikuwa na ng’ombe kadhaa ambao tungeweza kutoa wawili watatu wa mahari.
Mahusiano yangu na mdogo wangu Mazoya hayakua yamekaa vizuri bado, niliporudi nyumbani, lakini haikuwa tatizo. Baada ya vikao kadhaa na kuona utayari wangu wa kumsaidia, nafsi yake ilifunguka na nadhani aliamua kuachilia juu ya ile pesa niliyompa Mawazo. Mazoya alioa binti wa pale pale kijijini ndani ya mwezi ule ule niliorudi nyumbani. Siku chache baada ya harusi, matokeo yangu yalitoka na nilikuwa nimepata daraja la kwanza tena (1.7). Kwa masomo ya udaktari na kwa jinsi nilivyougua, nilimshukuru Mungu sana kwa alama hizo. Kama kawaida, mama yangu alifurahia sana na kujivuna juu yangu. Sikua na wasiwasi kuwa ningepata sasa chuo nilichotamani kwenda kusomea udaktari, lakini sikua na hakika sana kuhusu serikali kunilipia.
Sikukaa sana nyumbani baada ya harusi ya mdogo wangu, hasa baada ya matokeo kutoka. Nilirudi Arusha upesi kuendelea na kazi yangu. Wakati huu sasa sikua na siku nyingi za kuendelea kufundisha kwani nilikua nikisubiria kwenda kufanya mtihani wa kuingia chuo (matriculation). Hataivyo wanafunzi wangu walinifahamu kama mwalimu mwenye kasi kubwa mara zote. Daima nilihakikisha tunajali sana suala la muda hivyo hata silabi (syllabus) mara zote tuliwahi kumaliza. Nilichohakikisha tu ni kuwa kila mwanafunzi wangu anafanya vizuri darasani kwahiyo nilijitahidi kuwa makini pamoja na kuwa tulienda kwa kasi sana. Kufika kipindi natakiwa kuondoka kwajili ya kwenda chuo Dar, nilikuwa nimebakiza sehemu ndogo tu ya silabi ambayo rafiki yangu mwl. Olengai aliahidi kunisaidia kumalizia.
Niliondoka kwenda Dar es Salaam baada ya kupata taarifa juu ya siku ya kufanya mtihani wa kujiunga na chuo, na kwa upande wangu, chuo nilichokuwa natarajia kupata ni chuo cha udaktari Muhimbili. Kwa bahati mbaya sana, mpaka siku naondoka Arusha, malaika wangu Angel hakuwa amewasiliana na mimi kabisa na hapo ndipo nilipoamua kukata tamaa nikajihakikishia kuwa hangeweza kunitafuta tena.
Siku ya kwanza jijini Dar es Salaam ilikuwa ni moja kati ya uzoefu wa tofauti niliowahi kuupitia tena nikiwa mtu mzima kabisa. Sikuwa nimewahi kufika Dar es Salaam kabla, japo nilikuwa na shangazi yangu mmoja ameolewa huko. Mara ya mwisho tulionana kwenye msiba wa baba, nikamwambia Mungu akijalia chuo kikuu nitasoma Dar es Salaam. Wiki mbili kabla ya kwenda Dar nilikuwa nimemwandikia barua, hivyo alikuwa tayari anajua ujio wangu.
Kwa stori ambazo niliwahi kusikia, nililihisi jiji la Dar kama jiji kubwa sana, lenye watu wengi, magari, magorofa na vitu vingi sana ambavyo kijijini havipo. Kweli fikra zangu juu ya mji huu mkubwa hazikuwa tofauti sana kwani niliona taa mpaka barabarani, watu wengi wasioogopa magari pamoja na magorofa mengi makubwa. Niliposhuka Ubungo kituoni, ilinibidi kuuliza magari ya kwenda vingunguti ambako ndiko shangazi yangu alikuwa anaishi. Shangazi alikuwa amenitahadharisha juu ya vibaka na wezi hivyo japo sikuwa na pesa nyingi, nilikuwa makini sana na mizigo yangu yote.
Kwa bahati mtaa alokuwa anaishi shangazi ni maarufu pale vingunguti hivyo haikuwa tabu kufika, na nilipofika mtaani nilielekezwa mpaka nyumbani kwake na kijana mdogo tu. Shangazi alinipokea vizuri, mtoto wake mkubwa alinisaidia kufahamu jiji la Dar kwa kiasi kwa muda niliokuwa pale, siku ya mtihani nilienda chuo na kufanya mtihani ambao haukuwa mgumu hata kidogo na kama nilivyokusudia nilichagua masomo ya udaktari kwa chuo kikuu cha Muhimbili kama kipaombele cha kwanza.
Matokeo ya chuo yalitoka baada ya siku kadhaa na kwa bahati nilipata fursa ya kusomea udaktari pale pale Muhimbili. Mwezi wa tisa, mwaka 2008 nilianza mwaka wa kwanza wa udaktari chuo kikuu Muhimbili. Hii ilikuwa ndoto yangu kubwa mno inaelekea kutimia na sikuamini kama kweli Napata hii fursa. Nilipangiwa kukaa hosteli za mabibo, jambo ambalo kidogo lilikuwa changamoto kwangu.
Pale mabibo kulikuwa na vijana waliochangamka sana. Chumba changu, bloko E, japo tulitakiwa kulala wanne lakini tulikuwa saba. Kila mwenzangu alikua na rafiki yake, yani kambeba mtu, isipokuwa mimi tu. Vijana wa chumbani kwangu wote walikuwa wajanja na wamechangamka sana kuliko mimi. Shule ya udaktari haikuwa rahisi hata kidogo. Kabla hata sijaelewa mazingira vizuri, tayari nilikuwa na mzigo mkubwa wa kusoma kana kwamba nina mwaka mzima chuoni tayari, hivyo ilinibidi kutumia maeneo ya kusoma, maarufu kama ‘vimbweta’ kila ninapokuwa mabibo. Ninachomshukuru Mungu sikuhitaji kuwaza juu ya ada ya shule kwani nililipiwa na serikali ada yote, na pia kuna pesa kiasi za matumizi ambazo hutolewa maarufu kama ‘bumu’. Sikuwa mtu wa matumizi kabisa zaidi ya mahitaji ya muhimu tu, hivyo pesa niliyopewa ilinitosha pamoja na kutuma kiasi nyumbani japo kwa sasa ilibidi pesa ya kutuma nyumbani ipungue.
Changamoto nyingine ya mabibo hosteli ilikuwa ni wenzangu kuingiza wasichana chumbani. Ilikuwa kitu cha kawaida kwa kijana wa kiume kuleta msichana wake chumbani na wakati mwingine ilinilazimu kutoka kuwaachia nafasi. Kwajinsi ambavyo shule ilinifanya kuwa bize na kukosa muda kabisa, suala la mapenzi kwangu kwa wakati wote huo lilikuwa mbali na mimi. Sikutamani kuwa na msichana, na pia mbali na malaika wangu aliyepotea ‘Angel’ sikuwahi kuvutiwa tena na msichana mwingine japo kulikuwa na wasichana warembo sana wenye kuvutia hosteli ya mabibo. Madarasa ya udaktari ni namna fulani kama ya shule ya msingi, yaani Jumatatu hadi Ijumaa mnaingia darasani asubuhi mpaka jioni.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hapa kilichotakiwa si tena ushindani wa kuwa wakwanza au kumzidi maksi mtu Fulani, badala yake ilinibidi kusoma sana kuendana na kasi kubwa ya masomo yangu. Nilitegemea niwe daktari mzuri, na ilikuwa ni lazima nifanye kila niwezalo bila kujali ugumu wa masomo au changamoto mbalimbali nilizokutana nazo. Miaka miwili ya mwanzo wa masomo yangu ilikuwa migumu na nilijiona kama sina hakika kama nitaweza kufikia malengo yangu. Presha ya masomo ilikuwa kubwa sana kiasi cha kunifanya nihisi ninaweza kushindwa, lakini kila nilipopokea barua kutoka kwa mama, ilinipa nguvu zaidi za kusoma sana. Mara zote mama aliniandikia akinambia jinsi anavyojivunia kuwa na kijana kama mimi, na alinitia moyo kuwa hata kama masomo ni magumu sana bado anaamini nitakuwa daktari mzuri mbeleni.
Baada ya miaka miwili ya mwanzo, nilikuwa sasa nimezoea shule na ile kasi kwangu haikuwa tatizo tena. Niliwapuuza wenzangu waloleta wasichana chumbani na sikujali vitu vingi kiasi kwamba sikuwa tena napata changamoto nilizoziona mwanzoni. Darasani pia nilikuwa tayari nimezoeana na wenzangu na kujenga urafiki na baadhi ya watu japo miaka yangu sita kwenye shule ya wavulana tu, ilinifanya nipate ugumu kuwa na ukaribu na wasichana.
Mwaka wa tatu pale muhimbili nilijikuta naanza kuzoeana na binti mmoja tuliyekuwa tunasoma naye. Mazoea yetu hayakuwa na urafiki hasa bali ilikuwa ni kama tu wanafunzi wanaosoma pamoja, lakini tofauti na wasichana wengine tuliosoma nao, binti huyu, Mariana alikuwa mchangamfu zaidi kwangu na hivyo kufanya nimzoee zaidi. Kadiri siku zilivyozidi kwenda, niligundua kuwa mimi na Mariana tunakuwa karibu sana kiasi kwamba nilikuwa sasa sielewi kama ni urafiki wa karibu unajengeka au kuna hisia za mapenzi zinaanza ndani yangu. Nilitamani kuwa na muda naye zaidi, nilifurahi kumuona, na kwa kiasi alianza kuyafanya maisha yangu ya chuo yawe ya furaha.
Sikuwahi kumwambia Mariana chochote kuhusu nilivyojisikia kwani si tu sikuwa na uhakika wa nnachokihisi, bali pia nilikuwa siko tayari bado kuingia kwenye mahusiano hasa ukizingatia ugumu wa shule ya udaktari. Nilihisi pia Mariana alianza kuwa na hisia na mimi, lakini nadhani kila mmoja wetu alijitahidi kuzuia hisia zake kwa muda. Baada ya miezi kadhaa ya urafiki wa karibu, tulijikuta tumeingia kwenye mahusiano mimi na Mariana, na nadhani kasi ilikuwa kubwa kidogo. Mariana yeye alishawahi kuwa na mahusiano kabla, na mpaka tukiwa mwaka wa pili alikuwa na mpenzi japo alikuwa mbali. Nadhani kwa sehemu, ugomvi wake na mpenzi wake ulisababisha Mariana kuwa karibu na mimi zaidi.
Kwangu maisha ya mapenzi yalikuwa mageni na mapya, lakini kwakua nilikuwa tayari mtu mzima, hayakunivurugia masomo yangu. Tulitumia karibu muda wetu mwingi sana pamoja, wa chakula, kusoma na kufanya vitu vingi. Mariana alikuwa binti mchangamfu ambaye mara zote nikikaa naye najisikia vizuri. Urafiki wetu uliendelea kwa muda, lakini nilikuja kugundua kuwa kuna tatizo kidogo ambalo pengine lingefanya uhusiano wetu usidumu. Baba yake Mariana, mzee Juma, alikuwa ni muislamu, japo Mariana mwenyewe alifata dini ya mama yake. Hii haingekuwa tatizo kwangu kama baba yake angeruhusu binti yake awe na mwanaume wa dini anayochagua yeye, lakini mzee Juma alikuwa hataki kabisa mtoto wake yeyote kuoa dini nyingine tofauti na dini yake.
Baba na mama wa Mariana walikuwa wameshaachana siku nyingi, na kwakua yeye alienda kuishi na mama yake, alijikuta amefata dini ya mamake. Pamoja na hilo lakini babake alisema kuwa watoto wake wote chimbuko lao ni waislamu hivyo hata kama wangechagua dini zao, katika kuolewa wale wa kike ni lazima wangeolewa na waislamu, lakini pia kwa wa kiume hakukubali kabisa wawe dini tofauti. Mwanzo sikuwahi kujua hilo, lakini baadaye nilianza kuhisi ni jambo ambalo linamsumbua Mariana, kwani mara zote nilipojaribu kuzungumza kuhusu hatima yetu na kuonesha kuwa tutakuja kuwa na familia, mpenzi wangu alionekana kama asiye na uhakika kama tutakuja kuoana.
Siku moja alinieleza kwa kirefu kuhusu maisha ya familia yake na hiyo changamoto aliyonayo kwa baba yake. Nilijua Mariana ananipenda sana hivyo nilijiambia moyoni kuwa wakati ukifika atapigania penzi letu. Nilimwomba kuwa tukubaliane kuwa daima kila mmoja wetu angepigana kuhakikisha tunafika hatima yetu, na katika hisia za mapenzi, tuliwekeana ahadi ya kuwa pamoja daima. Kuna wakati nilihisi kama huenda Mariana akashindwa kutimiza ahadi yake kwangu, hasa wakati fulani aliposafiri kurudi kwao kipindi cha likizo. Wakati huu nilikuwa nimenunua simu ndogo ya nokia tochi ambayo ingenirahisishia mawasiliano. Akiwa likizo mara nyingi tulipoongea alionekana ni kama mtu anayepata wakati mgumu sana kutoka kwa baba yake. Wakati mwingine alinambia baba yake anavyomuweka vikao vya mara kwa mara, na pia kuna kama dalili anaona za kutafutiwa mume na mengine mwengi. Kwangu bado niliona hivyo si vikwazo vya mimi na yeye kuoana lakini iliniumiza kichwa kuona mambo hayo yalimpa wakati mgumu sana Mariana.
Siku moja, kipindi cha likizo, nilienda mabibo hosteli kufatilia vitu fulani kuhusu hosteli. Kuanzia mwaka wa nne nilipata chumba muhimbili lakini kuna baadhi ya vitu nilitakiwa kufatilia kwa basa kuhakikisha napata tena chumba muhimbili mwaka wa tano, kwani miaka yangu ya mwanzo nilikuwa nikipangiwa mabibo. Likizo ilikuwa imekaribia kuisha hivyo ilinilazimu kuhakikisha nakamilisha kila kitu mapema. Siku hiyo, nikiwa mabibo, nilisimama sehemu moja kununua vocha. Akaja binti mmoja mweupe, mwembamba hapo nilipokuwa nanunua vocha. Ilikuwa ni duka la vifaa vya shule na fotokopi (stationery), na yeye alikuja kama mtu anayetaka kutolewa kazi yake kwenye kifaa (flash). Alikuja na haraka na hivyo aliomba samahani na kumwambia yule muhudumu, “naweza kuprint kazi yangu? Samahani nina haraka kidogo”. Mimi sikumuona mstaarabu kwani nilikuwa ndo nimefika pale na bado sijahudumiwa, na hakuonesha kujali kama amekuta mtu, na pia alijaribu kuonesha kama ye ndo anastahili kuhudumiwa kwanza. Niligeuka kumtazama kwa kushangaa, lakini tulijikuta tumetazamana, na kwa aibu akanambia, ‘samahani kaka’.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ghafula nilihisi ni sura niliyoshaiona mahali, sura rafiki na iliyowahi kunivutia sana. Wakati huo na yeye alikua akinitazama na kuduwaa kama mtu anayejaribu kunikumbuka. Ndani ya sekunde kadhaa, sote tuliitana majina yetu kwa pamoja na kwa mshangao, “Angel”, “Nathan”!! Nilikuwa nakutana na malaika wangu kwa mara nyingine. Sikuamini! Nilishakata tamaa kama kuna siku tena ningewahi kumuona huyu binti. “Ama kweli milima haikutani lakini si binadamu”, nilimwambia huku kama nikilenga kumlaumu kwanini hakutaka kunitafuta tena.
Alikuwa na haraka sana, alikuwa akifanya masomo ya shahada ya pili chuo kikuu cha mlimani na ndio alikuwa yupo kwenye utafiti (research dissertation). Siku hiyo alitakiwa kuwahi kukusanya makala ya pili (second draft) na inaonesha msimamizi wake alikuwa mkali kidogo, ambaye walikuwa na miadi naye masaa machache baadaye. Hatukuweza kuongea sana zaidi ya kupeana namba za simu, ila nilichoona machoni mwa Angel ni kuwa alikuwa amefurahi sana kuniona tena, nadhani kama ambavyo mimi nilifurahi. Baada ya muda tu nilimtumia meseji kumwambia jinsi gani ambavyo nimefurahi kumuona tena na kumuomba mapema iwezekanavyo tukae tuongee. Alivyojibu kwa haraka niligundua kuwa safari hii hatanipotea tena.
Mariana alivyorudi kutoka likizo hali ya uhusiano wetu haikua sawa na awali. Kila nilivyojaribu kumfanya asiwaze juu ya nyumbani na baba yake, ilionekana ngumu kidogo. Mpenzi wangu alianza kuonesha kana kwamba kuwa kwetu pamoja si jambo la kuaminika sana na hakuwa tena Mariana ambaye niliamini hatutaachana kwa gharama yoyote. Kwa kiasi iliniathiri, nilikuwa nikimpenda na nilimzoea sana. Ule muda mwingi tuliokaa pamoja sasa ulikuwa na doa kwani badala ya uchangamfu wake niliouzoea alianza kuwa mtulivu sana na mwenye mawazo. Haikuwa rahisi kwangu, na mara nyingi zaidi tulipoongea nilimwomba asiniache. Baada ya hali hiyo kuendelea kwa muda, nilijikuta kuna baadhi ya vitu naanza na mimi kubadilika. Basi hapo ndo ikaanza kuwa tatizo. Nikagundua kuwa nina mpenzi mwenye wivu na mlalamishi. Alilalamika kwa kuto mpigia simu, kwa kutomtafuta mara kwa mara na kwa vitu vingi, japo binafsi sikuona kama nilimtendea vibaya. Sikutaka kupunguza ukaribu naye na nilijitahidi nisifanye hivyo, lakini kuna wakati nilipowaza kukaa naye, niliwaza jinsi ambavyo si mchangamfu tena na hivyo tutakosa maneno ya kuongea. Sasa ilikuwa kila mara tunapoonana tuna ka ugomvi ka kusuluhisha, na hiyo hali ilinikera sana.
Wakati huo, Angel alikuwa amenitafuta siku kadhaa tu baada ya kuonana lakini kwa bahati mbaya hatukupata muda wa kuonana bado. Kazi yake ilimpa wakati mgumu kidogo kuimalizia hivyo hakuwa na muda. Hataivyo tulianza kuwasiliana kama watu wanaofahamiana. Kwangu huyu binti alikuwa mtu maalumu sana. Kwanza ni binti pekee aliyewahi kunivutia kwa mara ya kwanza niliyomuona, pili niliupenda sana moyo wake na ingenitosha sana kuwa karibu naye. Japo nilivutiwa sana na Angel, lakini kwasasa sikuwa na wazo la kuwa naye kama mpenzi. Nilikuwa nampenda Mariana, namuheshimu na nisingependa kumuumiza kabisa hasa kwa kumchanganya na msichana mwingine. Na pia nilihisi lazima tu Angel atakuwa na mtu wake na nisingependa kuingilia
Baada ya kama miezi miwili hivi tulipata nafasi ya kuonana na kukaa na Angel. Pamoja na mambo mengi tuliyoongea, alinieleza kwanini hakuweza tena kunitafuta. Mara ya mwisho tulipoonana nikampa kikaratasi cha anuani yangu, alikiweka kwenye mfuko wa suruali ya jinzi aliyokuwa amevaa na kwa bahati mbaya alisahau kukitoa, ikafuliwa. Sikuona kama ni sababu ya msingi kwani hangeshindwa kutafuta anuani ya shule ya Ilboru na kuniandikia barua, lakini hata hivyo walau niliridhika kuwa hakufanya kusudi. Jioni ile tulikaa muda mrefu sana kuongea na Angel, na ulikuwa ni wakati mzuri mno kwangu. Aliniambia pia maisha yake ya mahusiano na kuwa angetarajia kuolewa na mwanaume fulani Arusha, kama baada ya miezi sita au pungufu. Japo sikuwa na mpango wa kuanzisha mahusiano naye, lakini habari hii haikuwa nzuri kwangu hata kidogo. Nilitamani ningekuwa rafiki na huyu binti kwa muda zaidi akiwa bado hajaolewa. Nadhani aligundua kuwa hizo habari sikuzifurahia, japo sikusema. Aliuliza pia kuhusu maisha yangu ya mahusiano na nilimwambia kuhusu Mariana. Sikutaka kuongelea kwa undani changamoto za uhusiano wetu, kwani niliona angedhani natafuta namna ya kuwa karibu nayeCHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilipomalizana na Angel ilikuwa tayari saa tatu usiku. Siku hiyo nilikuwa sijamtafuta Mariana muda ambao alitegemea ningemtafuta, na pia sikuwa nimemwambia ratiba yangu ya kuonana na Angel. Nilijua nina maelezo ya kutoa, lakini miadi yangu na Angel ilikuwa muhimu sana. Pia angekuwa Mariana yule wa zamani, labda ningemwambia kabla, lakini sasa hakuwa mtu rafiki na muelewa, hivyo kama ningemwambia ingeleta shida kubwa. Kuna wakati alinipigia nikiwa na Angel nikaongea nae kifupi kisha nikamwambia nitakupigia badae kidogo. Nilipomtafuta usiku huo alikua amekasirika na ilibidi tuonane usiku huo kuongea. Nilimdanganya mambo kibao ambayo najua hayakumridhisha lakini hakuwa na namna ya kukataa ninachomwambia.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment