Simulizi : Mwangaza
Sehemu Ya Tatu (3)
Nikiwa namalizia mwaka wangu wa tano muhimbili, kabla ya ule mmoja wa majaribio, nilianza kufikiria juu ya maisha yangu baada ya chuo. Kuna ushindani wa ajira nchini Tanzania. Na japo madaktari wengi wanaomaliza hasa wa Muhimbili, hupata kazi serikalini, lakini mishahara ya madaktari wa shahada ya kwanza si mikubwa, na endapo ingenibidi niajiriwe tu baada ya shahada ya kwanza, ingenilazimu kukubaliana na mshahara mdogo. Nilianza kuwaza kwa mapana kuwa sasa nakaribia kumaliza chuo na hivyo nitahitaji kuwa na mwenzi na familia, mbali na familia ya mama na wadogo zangu inayonitegemea. Wazo lililonijia ni kutafuta udhamini wa kusoma shahada ya pili ya udaktari ili kutengeneza uzoefu wa juu zaidi (specialization). Lakini sikutaka tena kusomea Tanzania kwani kwa masomo ya juu sana niliamini nchi za wenzetu zinafanya vizuri zaidi.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilianza jitihada za kutafuta nafasi za kusoma nje zenye udhamini nikiwa mwaka wa tano, mwaka 2013. Nilifatilia kwenye mitandao, vyuoni na kila sehemu ambapo nilihisi ingekua chanzo kizuri cha taarifa hiyo. Niliongea na madaktari wa hapo Muhimbili wenye elimu za juu, na maprofesa kwa jitihada zote. Kuna daktari mmoja wa shahada ya tatu (PhD) ambaye pia ni mtaalam wa magonjwa ya wanawake alikuwa akinisaidia kwa karibu kufuatilia nafasi za kusoma nje. Kwa nafasi yake yeye alikuwa na mawasiliano na baadhi ya vyuo vya nchini Wingereza alikochukua shahada yake ya pili, na pia vya nchi ya Ujerumani alikosoma shahada ya tatu. Alinishauri nitume maombi kwa vyuo viwili nchini Wingereza na kimoja cha Ujerumani, ili nikishapata nafasi hatua inayofuata ndo iwe kutafuta udhamini. Nilituma maombi na kila kilichohitajika kwa vyuo hivyo vitatu mwaka huo huo 2013. Daktari Mkinga (mshauri wangu) alikuwa amependekeza zaidi vyuo vya Wingereza kwani alisema kwa nchi hiyo kuna nafasi nzuri za kufanya kazi ndogo ndogo ukiwa unasoma, na hivyo kujiongezea kipato.
Nilijibiwa na chuo kimoja cha Wingereza miezi kadhaa baada ya kuomba, na namshukuru Mungu nilikuwa nimepata nafasi ya kusoma (admission). Nikiwa mwaka wa mafunzo ya uzoefu (internship), yaani mwaka wa sita wa udaktari, mwanzoni, nilianza kazi kubwa ya kutafuta udhamini baada ya kuwa tayari nina barua ya kupokelewa chuo. Hii ni moja ya kazi yenye kunikatisha tamaa sana niliyowahi kukutana nayo. Kwa msaada wa Dk. Mkinga nilikuwa nikituma maombi kwa wadhamini/wafadhili wengi sana lakini tumaini lilikuwa dogo kwani sikuwa Napata majibu yoyote. Mwanzoni niliamini ushindani ni mkubwa ila nitafanikiwa, lakini baada ya majaribio mengi nilianza kukata tamaa. Japo nilipoteza tumaini, sikukubali kupoteza nguvu ya kuendelea kutuma maombi. Kulingana na maisha yangu, nimejifunza kupambana kwa kila kitu ninachokihitaji maishani, hivyo hata wakati ambapo akili yangu ingenishawishi kukata tamaa na kuachilia, bado niliamini natakiwa kupambana mpaka nipate ninachokitaka.
Hatimaye nikiwa mbioni kumaliza mwaka wa mafunzo (intership) pale muhimbili, nilipata majibu kutoka kwa moja kati ya wadhamini wengi niliowaomba kunifadhili. Hii siku ilikuwa kama ndoto kwangu kwani mawazo ya kwenda nje kusoma yalikuwa tayari yameanza kufutika. Ufadhili huo ulikua ni wa asilimia 100, yaani ada, nauli pamoja na makazi, na pesa kidogo ya matumizi. Kilichokuwa kimebaki sasa ni kusubiri miezi kadhaa kuhu nikikamilisha yanayohitajika kwa ajili ya safari.
Katika kila hatua, mama alikuwa ni mtu wa karibu sana ambaye nilimshirikisha. Wakati huo nilikuwa nimemnunulia simu ndogo ya kawaida kuturahisishia mawasiliano. Daima mama alinipa nguvu na sababu ya kupigania kila hatua ya muhimu maishani mwangu. Mafanikio yangu aliyapokea kwa furaha kubwa siku zote nadhani kuliko hata mi mwenyewe. Bila kujali kuwa shule hiyo ingetuweka mbali kwa muda mrefu, pia bila kujali kwamba huenda ningeoa hukouko na kujenga familia yangu nje ya Tanzania, mama alifurahi mno kuona nimepata wafadhili kunisomesha nje ya nchi. Mama aliniamini, alinihakikishia kuwa ninaweza kufika popote ninapotaka, na pia alinitia moyo sana mara zote alizoona naelekea kukata tamaa. Kwake ndoto zangu zilikuwa muhimu kuliko hata zake. Naweza sema ni mmoja kati ya wanawake wenye moyo shujaa, ulio na upendo na huruma ya kweli.
Mwaka wangu wa mwisho chuo kikuu muhimbili, katika suala la mahusiano ulikuwa na mambo mengi. Naweza sema ulikuwa wakati wa changamoto kubwa kwangu. Mpenzi niliyekuwa naye, Mariana, alikuwa akinisumbua kichwa changu. Ulalamishi wake na kutokujiamini vilizidi kuwa kikwazo kwetu, lakini pia hakuwa ameridhia safari yangu ya kwenda kusoma. Kama tungekubaliana, nilipanga baada tu ya mwaka mmoja wa masomo nifanye mpango naye anifuate, lakini kwake lilikuwa jambo gumu. Najua hakutamani tuachane, lakini kulingana na hali ya kwao, hakutamani pia tupige hatua moja zaidi ya mahusiano yetu, kama kutambulishana, mahari ama ndoa. Alinipa wakati mgumu kufikiria nini hatima ya mahusiano yetu. Nakumbuka kuna siku nilijaribu kumwambia kuwa kama inakua ngumu sana sisi kuwa pamoja basi tuachane. Nilijutia kusema hiyo kauli, kwani Mariana alihamaki sana. Aliona kana kwamba ndio nimemwambia namuacha, alilia na kuniongelea mambo mengi ya ajabu. Labda alidhani ningeamua sote tubadili dini kwa ajili ya baba yake. Kwangu hilo jambo lilikua haliwezekani, kwani kwa jinsi nilivyolelewa, mzazi nilimuona kama mshauri mkubwa lakini si mwamuzi wa mwisho katika maisha yangu. Kwangu, mimi na Mariana tungetakiwa kufanya maamuzi yetu, huku tukiangalia kama ushauri wa wazazi unafaa kufuata au la.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baadaye niliamua nitamuacha kimya kimya, hasa nitakapo kwenda Ulaya. Hofu na wasiwasi wa Mariana vilizidi baada ya kuona nimedhamiria kwenda kusoma nje ya nchi, na hasa baada ya kupata ufadhili. Hata hivyo nilijitahidi kutomjali sana japo niliumia. Ukiachilia mbali uchangamfu wake wa asili, binti huyu alikuwa na hekima katika ushauri wake. Ni yeye aliyenishauri kumnunulia mama yangu simu lakini pia alikuwa amenisisitiza sana kujenga nyumba kijijini kwetu haraka sana nikianza kupata pesa. Stori ya maisha yangu ilimfanya aelewe ni jinsi gani ninategemewa na nina majukumu mengi, na ilinipa amani kuwa nitaoa mwanamke mwenye upendo wa kweli na mimi, ambaye ananielewa na kujali familia yangu. Haikuwa rahisi kuachana na binti wa namna hii, na hii ndiyo sababu nilijitahidi kadiri niwezavyo kutompoteza, lakini kwa sasa nilianza kuona jitihada zangu zikigonga mwamba.
Wakati huo, rafiki yangu Angel alikuwa tayari amemaliza shahada yake ya pili, lakini alikuwa akiishi jijini Dar. Alifanya kazi kwenye shirika moja maarufu, la binafsi, kama mhasibu. Tuliendelea kuwasiliana kama marafiki, na mara kadhaa tulionana kwa chakula cha mchana au cha jioni, na maongezi. Nilichogundua ni kuwa, mara zote nilipokuwa na Angel, nilijihisi kama niko na mtu ninayejuana naye siku nyingi, rafiki na mtu ambaye namuamini sana. Lakini pia nadhani namna ambavyo binti huyu alinichukulia ni kama mtu aliyemuamini sana. Hatukuwa tumepata fursa ya kujenga urafiki wetu kabla, lakini tulivyokutana mara ya pili baada ya kupotezana miaka kadhaa iliyopita, ilikuwa ni kama watu waliozoeana sana kabla. Nilijikuta tukiongea na Angel mipango mingi ya maisha na malengo, tukishirikishana na kushauriana. Angel alianza kuwa ananieleza kuhusu mahusiano yake japo si sana. Niligundua kuwa hakuonekana kuwa mtu anayefurahia sana mahusiano yake kwani kuna mara kadhaa alipigiwa simu na mpenzi wake tukiwa tumekaa naye, aliinuka kwenda kuongea pembeni, lakini aliporudi hakuwa na raha tena.
Siku zote sikutaka kumuuliza kuhusu undani wa mahusiano yake, lakini mara chache aliniambia kuwa mchumba wake anamtaka aache kazi arudi Arusha. Nilijaribu kumshauri labda inabidi atafute kazi Arusha, lakini inaonesha alikuwa na nafasi nzuri pale ofisini kwake na pia alikuwa akifanya kazi kwenye shirika linalompa nafasi ya kukua kitaaluma. Mchumba wake alitaka waoane mapema iwezekanavyo, lakini inaonesha Angel hakuwa bado tayari kwa ndoa. Labda ni kwa sababu ya baadhi ya kasoro alizokuwa akiziona kwa mchumba wake, au kwa ajili ya mipango yake binafsi ya kimaisha, sijui, lakini mimi nilifarijika kuona bado tuna muda walau zaidi wa kuwa marafiki
Katika kipindi hiki nilihisi namuhitaji Angel sana. Mara nyingi alinisaidia kupunguza msongo wa mawazo kulingana na changamoto nilizokuwa nikipitia kwenye mahusiano yangu, japokuwa hakuwa anajua lolote. Kila mara nilipoonana na Angel, nilijihisi kusahau shida zangu zote. Hivyo hii ilinifanya nitamani kutenga muda zaidi na yeye. Siku niliyomwambia kuhusu safari yangu, alijitahidi kuonesha amefurahi pamoja nami ila alishindwa kuzuia hisia halisi za huzuni ndani yake. Nilipomtazama machoni, ni kama mtu aliyeniambia, sitamani uondoke. Lakini hakuwa na namna ya kusema hilo neno. Baadaye, tukiwa katika maongezi, alinishika mkono na kunambia, “Ukiondoka nitakumisi sana”. Kwajinsi alivyosema, nilijua ukweli wa kile nilichokihisi, kuwa hakutamani niondoke. Nilitabasamu na kumwambia kuwa tutaendelea kuwasiliana bila shaka, japo sidhani kama urafiki wetu utaendelea ukiwa kwenye ndoa.
Kuna siku ilitokea tumetoka kwa chakula cha jioni na Angel. Siku hiyo mchana niligombana sana na Mariana kiasi kwamba nilitamani kumwambia ni bora tu tuachane, lakini sikuweza. Nadhani pia nilimuhurumia mpenzi wangu kwani kuna wakati niliona anajiadhibu kwa utii na heshima yake kwa mzazi wake. Lakini kusema kweli nilimtafuta Angel jioni yake kupunguza hasira na mawazo niliyokuwa nayo. Tulikaa sana na Angel siku hiyo. Nilijikuta naanza kumwambia kuhusu mahusiano yangu, vitu vingi sana. Nilimwambia sitamani kumpoteza mpenzi wangu lakini naona sasa nafika mwisho. Hakuwa na cha kunishauri zaidii ya kunambia niendelee kumvumilia na kujaribu kumuelewesha kwa upendo. Tuliendelea kukaa hapo kwenye mgahawa tukiongea vitu vingi na kucheka. Huo wakati ulikuwa mzuri kwangu na nilijiona kama niko na rafiki wa karibu mno.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mida ya saa tano usiku Angel alipigiwa simu na mchumba wake, na tofauti na siku zote, siku hiyo hakuinuka kwenda kuongelea pembeni. Kwa jinsi walivyoongea, nilihisi kati yao kuna shida pia. “Siwezi kuacha kazi kwa ajili yako Damian, nimeshafanya vitu vingi kwajili yako lakini sasa unakoelekea utanambia mpaka niache wazazi wangu kwajili yako”. Hiyo ilikuwa sentensi ya mwisho kabla hajamkatia simu. Baada ya hapo simu iliita mara mbili na meseji kama tatu hivi kuingia lakini Angel aliipuuza simu yake. Alionekana mtu aliyevurugwa sana na ile simu na nadhani kama angekuwa mlevi angelewa sana siku hiyo. Baada ya dakika, aliagiza glasi ya mvinyo (wine) na kuinywa kwa haraka. Muda wote huo nilikua kimya sana na hata baada ya kumaliza kuongea tulikaa dakika chache bila kuzungumza chochote.
Baadaye Angel alianza mwenyewe kunambia, na hapo ndipo nikagundua kwanini hayuko tayari bado kuolewa na huyo jamaa.”Tulianza mahusiano na Damian nikiwa kidato cha sita, na ndiye mwanaume pekee nimewahi kuwa naye. Mwanzoni nilikuwa na mapenzi ya kitoto naweza sema, Damian amenizidi sana hivyo wakati huo yeye tayari alikuwa anafanya kazi. Nyumbani hawakujua mapema lakini mama aligundua jinsi ambavyo sikuwa tena mtulivu. Damian alinifanya mapenzi yachukue nafasi kubwa sana kwangu kiasi kwamba kuna wakati nilikuwa nadanganya kuwa niko kwa rafiki zangu kumbe nimelala kwake. Kwa jinsi nilivyomuamini na kumpenda, sikuwahi kutegemea kama angekuwa na mpenzi mwingine zaidi yangu, lakini baada ya miaka mitatu ya uhusiano wetu nilianza kugundua kuwa Damian hakuwa mwaminifu. Nilikuta jumbe za mapenzi mara kadhaa na kuna siku mwanamke mwenzangu alinipigia simu kunitukana. Nilishindwa kumuacha Damian kwa kuwa nilimpenda sana na labda pia kwa kuwa ndiye alikuwa mwanaume wa kwanza kumpenda. Lakini baada ya kumaliza shahada ya kwanza nilianza kujiona kuwa nimekuwa mtu mzima na mwanaume hatakiwi kuniliza na kuniumiza kiasi hicho. Nilianza kumuonesha misimamo yangu kuwa kama anataka kuwa na mimi lazima niwe pekeangu. Kiukweli Damian alibadilika na naweza sema ameachana na wanawake wengine, hasa baada ya wakati Fulani kufanya jaribio la kumuacha. Alipofanikiwa kunishawishi turudiane, aliniomba kwenda kujitambulisha nyumbani, na alitaka kutoa mahari kabisa lakini mimi nilimwambia asubiri kwanza.
Damian alifanya nigombane na baadhi ya ndugu zangu, hasa dada zangu kwani jinsi alivyonitesa na nikamkubalia kuja nyumbani kwa utambulisho, dada zangu waliniona kama nimechanganyikiwa kukubali kuolewa na huyu mwanaume. Pia kuna marafiki zangu ambao walikuwa wakimstukia kuwa ni muhuni basi atapingana nao mpaka ahakikishe nimeachana nao. Mama yangu aliwahi kukaa na mimi kunishauri kuwa mwanaume yeyote anayenipenda atajitahidi kuwa mwaminifu kwangu, japo mama hajawahi kuonesha kumpinga Damian. Sasa kwa saivi nadhani ameona ni kama nimepunguza mapenzi na wivu kwake, hivyo anajaribu kusukuma ndoa kwa haraka. Ukweli ni kuwa akili yangu inaogopa kuolewa naye, nahisi kama atakuja kurudi vile alivyokuwa hasa akishaona ameniweka ndani. Naogopa kuwa mtumwa wa ndoa yangu mwenyewe.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Damian ana hali nzuri sana ki maisha, anafanya kazi nzuri na ni mtu mkubwa kazini kwake. Yeye anaona haina haja ya mimi kuhangaika maana kazi yake inauwezo wa kututunza hata nikikaa nyumbani. Ameniahidi kunifungulia biashara yoyote kubwa ninayotaka nikiacha kazi, na ukweli huwa ananipa pesa sana tu. Lakini hata kama naolewa naye, kazi yangu ni muhimu kwangu. Mimi si mzoefu wa biashara na pia simuamini kiasi kikubwa cha kumtegemea kwa asilimia 100. Pia hakuna atakayenielewa nikiacha kazi kwajili yake, hasa ukizingatia tabia alizokuwa nazo kabla. Yaani Nathan, huyu mwanaume anaipa wakati mgumu sana, na kadiri siku zinavyozidi nahisi pia na upendo wangu kwake unapungua”. Angel alimaliza kuongea, akionekana kama mtu aliyetua mzigo mkubwa.
Nilikuwa nikimtazama machoni muda wote anaongea, huku nikimsikiliza kwa makini. Sikuwa na cha kumshauri, japo pia nilijua alinambia tu kama rafiki na si kwa kutaka ushauri. Nilimwambia kuwa pengine hatakiwi kupiga hatua kubwa kama hiyo ya ndoa kama anahisi hamuamini au hampendi mume wake mtarajiwa. Hatukuongea sana tena kuhusu Damian, japo nilimshukuru kwa kuniamini na kunambia mambo yake ya ndani.
Usiku huo tulikaa sana, Mariana alipopiga simu niliongea naye kwa upole kana kwamba hakuna ugomvi ulotokea mchana, ili kumfanya asistukie kuwa niko na binti mwingine. Mida ya saa sita na nusu hivi ndipo tuliachana. Maeneo hayo hayakuwa mbali na mahali alipokuwa anaishi Angel hivyo nilimsindikiza kwa gari yake, nikachukua taxi kunipeleka. Nilipomfikisha kwake, wakati namuaga, nilijikuta nikimkumbatia, nayeye akanipa ushirikiano. Hii ilikuwa mara ya kwanza tangu tuwe marafiki kukumbatiana. Lilikuwa ni tukio la sekunde kadhaa tu, lakini nilitamani niendelee. Usiku mzima siku hiyo akili yangu ilirudia lile tukio na nilijisikia vizuri. Hapa sasa nilianza kuhisi labda nampenda Angel, lakini sikutaka kuzipa nafasi hisia zangu. Bado nilikuwa nampenda sana Mariana, bado Angel alikuwa na mchumba ambaye alisisitiza kumuoa.
Nikiwa nafanya mafunzo (intership), nilimudu kuanza kumtumia mama pesa ya ujenzi. Nilitamani walau tuanze kujenga msingi kisha tutamalizia nikiwa Ulaya. Lakini kwa bahati mbaya mzigo wa familia ulikuwa mkubwa hivyo hiyo pesa haikuweza kufanya nilichokusudia. Niliporudi nyumbani mara ya mwisho kabla sijaenda nje, nikagundua kuwa kweli ingekuwa ngumu kuanza ujenzi wakati bado kuna uhitaji mkubwa nyumbani. Mama hakuwa na nguvu sana za kulima, wadogo zangu walimsaidia, na pesa nyingi ilitumika shambani. Baadaye nikagundua kuwa tunaweza tukawekeza zaidi shambani, tukaanza kupata pesa zaidi. Kwa bahati kulikuwa na maeneo ya kutosha ambayo yangelimwa mahindi na kuleta faida. Pesa niliyokuwa nimeenda nayo wakati huo, tulishauriana na mama, tuweke vijana wa kulima, wakisaidiana na wadogo zangu, tulime walau heka tatu za kuanzia. Pia nilimtafuta bwana shamba wa pale kijijini na kumuomba atusaidie ushauri, nikamlipa kwa hiyo kazi. Lengo langu ilikuwa ninapoondoka, nimuache mama na mradi wa kumpa pesa, kabla sijaanza kupata pesa za kumtumia. Nilihakikisha naweka mikakati sahihi ya masoko na namna ya kuuza ili watakapovuna iwe rahisi. Bahati nzuri, mdogo wangu wa tatu kuzaliwa alikuwa ana akili za kuzaliwa na alikuwa msaada mkubwa sana kwa mama, hivyo nilihakikisha namfundisha namna ya kuhudumia majukumu makubwa kama hayo. Nilienda naye kila sehemu wakati naendelea na mchakato wa kilimo na nilimsaidia kujitambua zaidi, na nafasi yake katika familia, hasa mimi nikiwa mbali.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya miezi miwili kasoro ya kukaa nyumbani, muda wangu wa kuondoka ulikuwa umewadia. Nilijua mama angependa kuwa na namna maalumu ya kuniaga, hivyo nilihakikisha ana pesa za kufanya anachotaka. Siku mbili kabla ya kuondoka mama alikuwa ameandaa sherehe, amealika rafiki zake na ndugu. Bibi na babu walikuwepo, na kwangu ilikuwa siku nzuri ya kuaga familia yote kwa pamoja. Kwenye hizo sherehe, mama aliongea maneno ambayo sitayasahau.”Mwanangu Nathani, kuzaliwa kwako ilikuwa ni kama bahati kwani Mungu alileta watu kuokoa maisha yako. Pengine wasingekuwepo labda usingekuwepo leo. Lakini najiona kama mwanamke niliyependelewa sana kuwa na kijana kama wewe, hasa kwa kukuzaa wa kwanza. Siku zote umekuwa mfano kwa wadogo zako, umepambana kwa kila hatua ya maisha yako kuhakikisha unafikia ndoto zako, umenipenda na kunijali kuliko unavyojijali mwenyewe, umekuwa baba kwa kipindi chote tangu tumpoteze baba yako na umekuwa nguzo ya familia. Leo nakuaga, najua nitakukosa sana. Pengine utapata mke Ulaya na kuanzisha familia huko, na ukaishi huko siku zote, lakini maadamu najua utakuwa mwenye furaha na mafanikio, nafsi yangu imeridhika. Kama mama, naumia lakini pia nina furaha isiyo na kifani. Kwani namuona Nathani aliyekuwa akichunga ng’ombe, aliyekuwa akizuiwa kusoma, aliyekuwa akitengwa na wenzake darasani, sasa ni Nathani daktari aliyefanikiwa sana. Sina mashaka na maisha yako ya baadaye, hata kama sitakuwepo kukushauri. Ninachokuomba ni kuwa na Mungu siku zote za maisha yako. Mfanye mshauri wako mkuu”.
Nilikuwa namsikiliza mama muda anaongea na kiukweli nilishindwa kuzuia machozi. Huyu mwanamke alinionesha upendo mkubwa sana, niliusoma moyo wake jinsi ambavyo alikuwa tayari hata kama hataniona tena lakini ana furahi sababu anaona mafanikio yangu. Nilimsogelea mama yangu na kumkumbatia, na kisha nikampa zawadi ya simu nzuri niliyokuwa nimemnunulia. Kwa ulimwengu tuliokuwa tunauendea, nilijua mama angehitaji simu ya kisasa zaidi ili kuwasiliana na mimi.
Siku naagana na Angel haikuwa siku rahisi kwangu na kwake. Tangu siku ile tulipokaa mpaka saa sita na nusu, ni kama urafiki wetu ulienda kwenye hatua nyingine. Tulionana mara chache tena baada ya hapo lakini mida ya mchana na maeneo ya kawaida. Binafsi nilijitahidi tusikae tena mazingira kama yale na muda wa usiku sana, kwani sikutaka kusababisha hisia za mapenzi kati yetu, lakini mara zote nilizokutana naye nilijiona kumzoea zaidi. Tulikuwa tayari na ukaribu, na ni kama hakukuwa na siri tena kati yetu.
Nilipotoka nyumbani, nikiwa na siku kama kumi kabla ya kuondoka, nilikaa na Angel tena mida ya saa 12 jioni mgahawa Fulani tulivu maeneo ya masaki. Tulianza kuongea mambo mengi, kutaniana, stori za kazini nk.
Baadaye nikamwambia sasa nakaribia kuondoka, na sijui kama tutaonana tena hivi karibuni. Angel alijaribu kutoonesha huzuni lakini nilijua nampa habari ya kumuumiza. Baadaye alijikuta akianza kunambia jinsi gani nimekuwa mtu wa karibu kwenye maisha yake. Hapa ndipo nikajua kuwa yeye pia alijihisi vilevile nilivyojihisi. Alisema kuwa ananiona kama mtu aliyemzoea sana, anayemuamini sana na mara zote anakuwa huru kwangu kuliko hata kwa mchumba wake. Alisema kuwa urafiki wetu umempa faraja kubwa sana na mara zote amejisikia salama kuongea na mimi juu ya mambo yake. Sikuwahi kumuona Angel akiongea kwa kumaanisha namna hii, na sikuamini kuwa nina nafasi muhimu kiasi hicho maishani mwake. Nilijisikia vibaya kuwa inanilazimu kwenda mbali na sitakuwa karibu naye mara atakapo kuwa ananihitaji.
Baada ya kuongea kwa muda mrefu usiku huo, niligundua kuwa sitaki kumpoteza huyu binti. Nilimshika mkono wake na kumwambia ‘Nakupenda’. Akiwa ananishangaa na kama hanielewi, niliamua kuwa nitamwambia kile ninachojisikia.”Tangu siku ya kwanza nakufahamu nilikuona kama msichana analiyenivutia zaidi kuliko wasichana wote nimewahi kuwaona. Siku ya mwisho pale hospitali ya mlima Meru, kabla hujaja nilikuwa nikifanya maombi uwahi kabla sijaondoka. Siku zote, hata baada ya kumaliza shule nilikuwa nafatilia kama kwa bahati ningepata barua yako.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Tulipoonana hosteli nilijiona kama naonana na rafiki wa siku nyingi tuliyezoeana sana. Ukweli ni kuwa sijawahi kujisikia hivi kwa msichana mwingine yeyote, na nahisi huu ni zaidi ya upendo wa kirafiki. Nahisi kama sitakiwi kuwa mbali na wewe tena. Nahisi kama tunahitaji kuwa marafiki daima, na pia nadhani hisia ninazosikia ndani yangu zinazidi kukua kila tunapoongea. Najua nina mpenzi, lakini nimegundua kuwa hatuwezi tena kuendelea. Lakini pia kila ninavyojaribu kuiambia nafsi yangu kuwa wewe si wangu, moyo unakataa. Nakupenda, na nimehakikisha hilo mara kadhaa japo sikuwa nakubaliana. Nakuhitaji, kwenye maisha yangu nahitaji kuwa na mtu ambaye nina hakika moyo wangu unamuhitaji. Najua ni ngumu kuamua chochote kwa sasa ila naomba ujue kuwa nakupenda na nataka tuwe sote”.
Usiku wake ndipo nilitambua kuwa hakuna msichana maishani niliyempenda kama Angel. Nilikuwa nimeufungua moyo wangu, na hisia kali za mapenzi zilianza kunitawala. Akili yangu usiku kucha ilimuwaza Angel. Ilikuwa kama ndiyo nimeanza kupenda, japo tayari nilikuwa kijana mkubwa. Kila nilipojaribu kulala, sikupata usingizi. Nilipofumba macho, maneno aliyonambia kuhusu urafiki wetu yalijirudia akilini mwangu. Nilisahau kabisa kama nina mpenzi mwingine, na sasa sikujali tena kama nitamuumiza Mariana nikimuacha. Niliwaza juu ya safari yangu na kujikuta napanga ni namna gani tutakuwa na Angel pamoja hata nikiondoka nchini. Nikaanza kupanga jinsi nitakavyokuwa nawasiliana naye. Nilijipongeza kumwambia ukweli, na japokuwa alikuwa hajajibu, niliona nimepiga hatua moja kubwa katika kumfanya awe mpenzi wangu.
Kesho yake asubuhi sana nilimtumia ujumbe wa simu malaika wangu kumjulia hali. Kiukweli, penzi kubwa lilikuwa limeshamiri ndani yangu nadhani kwa usiku ule mmoja. Kitendo cha kumwambia Angel ukweli ilikuwa ni kama kufungulia maji yenye kasi kubwa kutoka moyoni mwangu, kwani nguvu ya pendo ilinifanya nishindwe tena kujizuia. Aliponijibu ujumbe wangu wa asubuhi, ilinistua kidogo. “Tunaweza kuonana leo?,” Alijibu Angel bila hata salamu. Nilimpigia haraka na kumuuliza kama kuna usalama. Nilijitahidi kutomuonesha nilivyohamaki kwenye simu. Tuliongea kwa kifupi na kisha kupanga miadi nyingine siku hiyo jioni tena. Kichwani nilijiuliza vitu vingi mno ambavyo sikuvipatia majibu. Labda jana nilimkera sana, au ndiyo mwisho wa urafiki wetu, au mchumba wake kamtibua, au pengine anataka kunambia ananipenda pia, ni baadhi ya maswali yaliyokuwa yakiendelea. Haikuwahi kutokea Angel kuomba kuonana na mimi kwa namna hiyo. Japo mimi ndiye niliyeanza kumtafuta, lakini namna alivyojibu ilikuwa kama dharura. Ni kama mtu aliyekuwa ameshika simu tayari kwa kutuma ujumbe sekunde chache kabla ya wangu kuingia.
Asubuhi hiyo pia Mariana aliniomba tuonane, lakini nilitafuta sababu ya kukwepa kuonana naye. Najua ningeweza kupata muda naye mchana, lakini kwa jinsi nilivyokuwa na hisia za mchanganyiko ndani yangu, najua lazima angenishtukia. Mariana alikuwa ananifahamu kwa undani sana kiasi kwamba haingekuwa rahisi kumficha kuwa kuna jambo linasumbua akili yangu, hasa kwa jinsi nilivyokuwa na wasiwasi juu ya kile Angel anataka kuongea na mimi. Mariana alikasirika kiasi lakini sikujali, nilichohitaji kwa sasa ni kujua maongezi yangu na Angel ya jioni yangenipa muelekeo gani wa mahusiano yangu. Nilitamani angenambia tuonane mchana huo. Nilitamani kuwasiliana naye kutwa nzima lakini niliogopa pia. Ujumbe alionijibu asubuhi haukuniwekea mazingira ya kuwasiliana naye zaidi kwa siku hiyo, hasa kwa kuwa nilikuwa nimemwambia ukweli jana yake tu, kuwa nampenda. Kwa upande mwingine nikaanza kujuta kwanini nilimwambia ukweli. Labda tungeendelea kuwa marafiki wazuri, kama nisingemwambia. Nilikuwa na siku mbaya kwa kweli, na ilikuwa ndefu sana. Wakati fulani mida ya mchana nilishindwa kujizuia nikampigia simu, walau nione kama atapokea na ataongeaje na mimi. Alipokea simu na kuongea kama mtu aliye katikati ya mambo mengi. Kwa asili ya kazi zake, alikuwa ni mtu bize kidogo, hasa kwa baadhi ya siku kama mwisho wa mwezi, hivyo sikustuka sana aliponambia naomba nikupigie badae, nimebanwa.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hatimaye jioni ilifika, tukakutana. Saa 12 kasoro dakika kumi, yaani dakika kumi kabla ya muda tuliopanga kukutana, nilikuwa tayari nimefika eneo la miadi. Siku hiyo nilijitahidi kuvaa vizuri na kupulizia manukato yale niliyodhani ni maalumu. Nilitoka kama kijana mtanashati na anayejipenda, na japokuwa watu wengi husema sisi madaktari huwa hatuna asili ya kujipenda lakini siku hiyo nilihakikisha mtu yeyote ambaye angeniona, angesema huyu kijana ni mtanashati. Sikutana kupoteza fursa ya kuonekana mwenye kuvutia machoni pa Angel. Labda angebadili mawazo yake hata kama alitaka iwe mwisho wa urafiki wetu. Pia sikutaka kupoteza fursa ya kuonekana ni kijana ninayejali muda. Kwangu ilikuwa ni kama nimepewa nafasi moja tu kumuhakikishia Angel kuwa mimi ni mwanaume ninayefaa. Kiuchumi, nisingejilinganisha na Damian, na hata Angel mwenyewe, lakini nilijiamini kuwa nina nafasi nzuri ya kuwa mwanaume ambaye atamjali na kumpenda huyu malaika, na kumtunza kwa namna zote. Moyoni niliomba Angel anipe nafasi tena ya kumueleza kwanini nahisi nafaa kuwa mume wake. Yaani ilikuwa ni kama mtu anayeenda kwenye interview ya kazi aliyoitafuta kwa muda mrefu, na ambayo hataki kuipoteza kwa gharama yoyote. Nilihakikisha mpaka kucha zangu za mikono ziko kwenye hali ya usafi, viatu na kila kitu. Hii haikuwahi kunitokea kabla.
Mida ya saa 12 na dakika kama saba hivi Angel alifika. Alikuwa hana kawaida ya kuchelewa pia hivyo nilimtegemea mapema tu. Nilimtazama akishuka kwenye gari yake ambayo hakupaki mbali, hofu na wasiwasi nilivyokuwa navyo vilipotea kwa muda. Akiwa bado umbali wa mita kadhaa, nilimtazama machoni, macho yetu yakagongana. Niliona tena kama naona malaika, akili yangu iliniambia, “Nathani, huhitaji kumpoteza huyu mwanamke”. Nilikuwa naingia kwenye ulimwengu halisi wa mapenzi. Jicho langu halikumuacha mpaka anafika mezani. Niliangalia alivyovaa, anavyotembea, na kwa mbali alinionesha tabasamu lake ambalo mara zote alikuwa akilitoa tulipoonana, japo leo ilikuwa kama tabasamu lenye wasiwasi kidogo, ambalo liliifanya akili yangu irudi tena kulekule kwenye hofu ya ‘ninini anataka kunambia?’.
Kitu cha kwanza kumwambia ilikuwa ni jinsi alivyopendeza. Kikawaida, nilikuwa huru sana kwake na hata siku ambazo hakupendeza nilimwambia ukweli kwani tulikuwa marafiki huru, hivyo aliniamini kila nilipomwambia amependeza. Siku hiyo sijui ni macho yangu au ni kweli, lakini niliona kama alipendeza sasa zaidi. Alivaa blauzi fulani nyepesi ya njano na sketi fupi nyeusi yenye duara nyeupe. Alivaa na viatu vya kima cha kati, vyenye uwazi kwa mbele vilivyoonesha rangi nyekundu ya kucha zake za miguu. Blauzi iliishia sketi ilipoanzia hivyo kumuonesha umbo lake kwa uzuri. Angel alikuwa ni binti mwembamba mwenye tumbo flati yaani dogo kabisa, lakini alikuwa na hipsi lililochomoza vizuri, na lilionekana kwa uzuri zaidi alipovaa sketi zenye kumshika kidogo. Rangi yake haikuwa nyeupe sana ila kwa wastani alikuwa mweupe, si mweusi wala si maji ya kunde. Nadhani alijua miguu yake ilivyofaa kuvaliwa sketi zenye kuionesha kwani sketi fupi zilikuwa ni kati ya mavazi aliyopendelea sana. Alikuwa na miguu laini, yenye ukubwa zaidi kidogo ya mwili wake na mizuri mno. Kucha zake ndefu za mikono zilikuwa na rangi nyekundu pia, ambazo alioanisha na rangi ya kidani cha cheni yake ya dhahabu aliyokuwa amevaa, rangi ya mawe (stones) ya hereni zake na rangi ya moja ya vitu alivyovaa mkononi mbali na saa ya mithili ya dhahabu.
Mara zote nilikuwa nikimsifia Angel ana macho mazuri, na alijua nilipenda kumuangalia machoni, lakini siku hiyo macho yake yalikuwa kama yenye sumaku. Alipokaa nilimtazama machoni na kuona uzuri zaidi ya ule niliokuwa nikiuona siku zote. Sasa nikawa sijielewi tena kama nina hofu au hisia za juu sana za mapenzi, zilizonipa kujiamini. Nilijiambia kuwa hata kama angenikataa, ningemng’ang’ania hata kwa magoti au machozi. Nilivutiwa mno na huyu binti siku hiyo kiasi kwamba nilijiona kana kwamba siwezi kuishi bila yeye. Siku hiyo Angel hakuwa mchangamfu kama nilivyozoea. Nilimsifia kwa dhati lakini alinipa tabasabu laini tu na kunambia asante. Sikuweza kuwa mvumilivu kusubiria aamue kuanza kusema. Tukiwa tunasubiri oda ya vinywaji, nilimuuliza anambie alichotaka tuongee. Nilikuwa muwazi kidogo kuwa ujumbe wake wa asubuhi umenistua kidogo. Ni kama alijua, aliniangalia tu na kutabasamu. Macho yake yalipotazamana na yangu nilihisi kuvutiwa zaidi.
“Nathan, jana tumeongea vitu vingi sana ambavyo hatukuwahi kuongea kabla. Ukweli ni kwamba usiku wangu wa jana ulikuwa mrefu sana. Niliwaza juu ya uhusiano wangu na Damian, nikawaza jinsi ambavyo Damian ana wivu na mimi na namna anavyonipa presha kuhusu ndoa. Pia niliwaza jinsi gani ni mwanaume pekee nimewahi kuwa naye kwenye mahusiano, na nimewahi kumtambulisha nyumbani kama mchumba. Lakini pia nimewaza kwa kiasi gani siku nyingi nimekuwa nikipingana na hisia za mapenzi ndani yangu. Tulipoonana mara ya pili, pale hosteli, ni kweli nilijihisi kama ninakutana na rafiki wa karibu. Kwa siku zote ambazo tumekuwa karibu, nimejihisi salama sana nikiwa na wewe. Nimekuwa nikijisikia kukuamini kuliko nilivyowahi kumuamini Damian, nimekuwa pia nikijisikia huru kwako na nafurahia kila dakika tunayokuwa pamoja. Siku zote nilijiambia kuwa ni kwa sababu wewe ni mtu mzuri na imetokea urafiki wetu ukawa maalumu, lakini jana uliponambia unanipenda, ndipo ulinifanya nigundue kuwa nakupenda pia”. Alipumzika kidogo na kushusha pumzi. Maneno yake yalinifanya nijifinye kidogo kwenye paja kujiona kama naota au la. Nilikuwa kama mtu anayetunukiwa tuzo ya ushindi ambao hajaufanyia kazi jinsi nilivyopata mshangao. Baada ya sekunde kadhaa, aliendelea
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nimelala nawaza nini cha kuamua. Mbele yangu nina wewe na Damian. Usiku wa jana nimegundua nahitaji kuwa na wewe walau kama rafiki mara kumi zaidi ya ninavyomuhitaji Damian. Nahisi hata kama mi na wewe hatutakuwa wapenzi, ni bora niwe na mwanaume mwingine lakini si huyu. Nimeamua kuwa sitakubali Damian, familia yangu au safari yako, ituzuie kuwa pamoja. Siku ya leo nimekuwa na wasiwasi sana juu ya maamuzi yangu, na nini hasa nilichoamua, lakini nilipokuona tena jioni hii, nimejihakikisha kuwa wewe ndiye mwanaume ninayetaka kuwa naye bila kujali mazingira, ugumu wala changamoto.” Hapo nilivuta pumzi ndefu sana. Tulikuwa tumetazamana machoni wakati anaongea, na nilihakikisha sipepesi jicho ili niwe nna hakika kweli anamaanisha anachokisema au la. Ni kweli alikuwa akimaanisha. Katika maisha yangu nadhani sikuwahi kuwa na furaha kiasi hicho. Hapo ndipo nilipogundua kuwa mapenzi yana nafasi kubwa mno kwenye maisha ya mwanadamu. Akilini nikajikuta nimeanza kuwaza juu ya mama yangu, aliyeingia kwenye mapenzi katika umri mdogo, kabla hata hajaelewa mapenzi ni nini. Lakini pia nikakumbuka jinsi mpenzi wake, ambaye ni baba yangu, alivyoutesa moyo wake, na kisha nikakumbuka kuwa wakati wa mwisho wa safari ya mapenzi yao ndipo penzi lilikuwa limeanza kushamiri. Nilijikuta nafuta chozi jicho langu la kulia huku nimemtazama Angel kama mtu niliyepigwa na butwaa na kumfanya ashindwe kuelewa kama ni chozi la furaha au vipi.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment