Simulizi : Mwangaza
Sehemu Ya Nne (4)
Wiki yangu ya mwisho kabla sijaenda Uingereza kusoma ilikuwa ni wiki ya raha sana japo pia nilikuwa na mawazo kuwa nakwenda kukaa mbali na mwanamke ninayempenda sana, kwa muda mrefu kiasi. Tangu usiku ule Angel aliponipa jibu, nilipata ujasiri wa kumwambia Mariana kuwa lazima tuamue juu ya hatima yetu ya mapenzi kabla sijaondoka. Nakumbuka siku nilipokaa naye kuongelea juu ya hili suala, alikuwa nayeye ni kama mtu ambaye tayari amekwisha fanya maamuzi. Ni dhahiri kuwa mapenzi yetu yalikuwa tayari yamemtesa vya kutosha. Wivu, wasiwasi, hofu na kutokujielewa vilikuwa ni vitu ambavyo vinamkosesha raha kila kukicha. Sasa ilikuwa ni lazima afanye maamuzi kama aidha ataendelea na mimi kwa gharama yoyote, au ataachana na mimi kwa ajili ya baba yake.
Nilipokaa naye kuongea, tofauti na nilivyotegemea, Mariana alinishukuru kwa kuwa mpenzi mwaminifu kwake. “Tangu umeanza kuwa rafiki yangu Nathan, hujawahi kunisaliti. Umenifanya kuwa rafiki maalumu kwako mbali na kuwa mpenzi wako. Umeonesha utayari wa kuwa na mimi kwa gharama yoyote, na hata nilipokuudhi sana bado hukuwahi kunikatia tamaa. Ulinipenda kama nilivyo, na uliniamini sana. Naumia sana kwamba tunashindwa kuendelea, na nadhani sina namna ya kufanya. Kiukweli nilikupenda sana, lakini maisha yangu yote sijawahi kufanya jambo lolote kinyume na wazazi wangu, hasa baba. Na nimekuwa ni mtoto ambaye baba anajivunia sana. Kila nikijaribu kupuuza matakwa yake, najikuta nakosa raha kupita kiasi. Nimevutwa katika njia mbili muda mrefu sana, lakini sasa nimeona nikuachie uende kwa amani. Nakupenda Nathani”.
Maneno ya Mariana yalinikumbusha siku tunaanza kuingia kwenye mahusiano na huyu binti. Siwezi kupuuza huyu ndiye msichana wa kwanza kunifundisha namna ya kuwa mpenzi wa mtu. Mariana alikuwa mchangamfu sana, na alinivutia kwa uchangamfu wake. Nikakumbuka wakati nikiwa mwaka wa nne, kuna nyakati shule ilikuwa ngumu kwangu, na mara zote nilipojihisi mzigo mkubwa, nilimtafuta Mariana. Haikujalisha tulikaa eneo la chuo, hosteli, mgahawa wa hali ya chini au uwanjani, lakini uwepo wake kwangu ulikuwa faraja na nguvu. Hakuwahi kukosa maneno sahihi ya kuongea na mimi, hata wakati hali ya uchumi ya familia yangu iliponichanganya. Nakumbuka kuna siku mama alinitumia ujumbe kunambia kuwa kulikuwa na msimu wa njaa kijijini kiasi kwamba maisha yalikuwa magumu hasa kwa watoto waliokuwa shuleni, nikaumia sana. Kwangu mimi, nilijihisi kushindwa sana kama nisingetimiliza hitaji hata moja la Neema. Sikutaka ahisi kukosa uwepo wa baba yake maishani, hivyo daima nilihakikisha hakosi chochote muhimu hivyo mama kunambia hali ya uchumi inawapa shida wale wadogo zangu wawili wa mwisho wanaosoma, iliniumiza sana, na kwa bahati mbaya sikuwa na pesa ya kutosha kwa wakati huo. Nilipokaa jioni na Mariana, si tu kuwa alinitia moyo, bali pia alinikumbusha kuwa hata Mungu kuna wakati anatuangalia tukilia kwa kukosa mahitaji yetu, japo anatupenda sana. Akanikumbusha kuwa, pengine Neema anatakiwa aelewe kuwa kwenye maisha kuna wakati kuna kukosa kile unachokihitaji.
Kuna mengi mno niliyakumbuka usiku huo, lakini mwisho wa mapenzi yetu ulikuwa umefika. Sikuwa na cha kujilaumu, kwani nilishajaribu kadiri niwezavyo, niwe na Mariana daima. Mimi na yeye tulifika muafaka kuwa hatuwezi tena kuwa pamoja. Usiku huo ni kama sasa mapenzi yalitaka kuanza upya kati yetu, kwani katika kuagana, tulijikuta tukikumbuka vitu vingi vya nyuma. Nilijua hili lingetutesa, hasa kwa yeye zaidi maana ilikuwa baada ya siku kadhaa namuacha na sitamtafuta isipokuwa labda mara moja moja kumsalimia. Lakini pia kwa upande wangu tayari nilikuwa nimeshapata mpenzi. Hataivyo hakukuwa na namna nyingine yoyote zaidi ya kukubali hatima hiyo ya mapenzi yetu. Nilimwambia kuwa nampenda, na ningetamani awe mke wangu kulingana na uzuri wa moyo, hekima na uchangamfu wake. Pia nilimshukuru sana kwa kuwa rafiki wa dhati na wa karibu sana mbali na kuwa mpenzi mwaminifu.
Sikuwa na namna zaidi ya kumshukuru Mariana, lakini siku moja kabla ya kusafiri, nilikuwa nimefikiria zawadi sahihi ambayo labda ingemfanya anikumbuke na akumbuke uhusiano wetu. Nilichukua picha yake, nikaenda studio maalumu ya picha ambapo hutengeneza picha katika vitu mbalimbali kama kikombe, nguo, mto, na mapambo ya aina tofauti. Niliomba wanitegenezee picha yake kwenye pambo la kioo fulani, dogo ambalo angeweza kukiweka kama pambo zuri chumbani kwake. Na chini ya picha yake niliomba waandike “Your true beauty, your wonderful heart”, nikimaanisha, “Urembo wako halisi, moyo wako wa ajabu”. Daima Mariana alijua jinsi nilivyokuwa nikiusifia moyo wake mzuri, na siku zote nilimwambia kuwa, waweza kuwa si mrembo kuliko wasichana wote duniani, na pengine wako wengi wamekuzidi, lakini uzuri na ukarimu wa moyo wako, ni uzuri halisi na wa kweli. Nilijua maneno ya kwenye lile pambo, yangemfanya ayakumbuke maneno yangu tukiwa wapenzi, na aelewe jinsi gani nilikuwa namaanisha.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilipompa zawadi hiyo, kama kawaida yake aliifungua dakika hiyo hiyo tukiwa sote. Alitoka na machozi kuona kuwa nimemfikiria sana, na hasa kwa hayo maneno niliyomuandikia. Namshukuru Mungu kuwa tuliachana na Mariana kwa amani kabisa, na ni maombi yangu kuwa Mariana angepata mwanaume bora kwake ambaye angetambua thamani yake. Nilikuja kumpigia simu kama miezi minne baada ya kufika Uingereza, lakini hatukuweza kuendelea kuwasiliana tena kwani kila mtu alikuwa tayari bize na maisha yake.
Wakati huo, penzi zito lilikuwa limeanza kuchanua kwa kasi kati yangu na Angel. Ni kama kila mmoja wetu alikuwa akiisubiria kwa hamu hii fursa. Sasa haikuwa tena inapita siku bila kuonana na malaika wangu. Kila mara nilitamani nimuone, walau kwa dakika chache. Sikuchoka kumuangalia machoni kila tulipokuwa pamoja. Sikuwahi kuona uzuri huo wa macho kwa mwanamke mwingine yeyote, na mpaka saivi ninapoongea, sijawahi kuvutiwa na msichana yeyote zaidi ya Angel. Baada ya kumwambia nimeachana kabisa na Mariana, nilimuhisi Angel akinifurahia zaidi. Siku zetu za mwisho kabla sijasafiri zilikuwa nzuri mno.
Angel alichukua likizo kazini ili tuwe sote muda mwingi, na ama kwa hakika aliutumia ipasavyo. Hata siku naenda kumpa zawadi Mariana, tulieenda pamoja kuichukua zawadi hiyo, na tulikuwa sote dakika chache kabla sijaonana na Mariana. Ilibidi nisikae muda mrefu na Mariana kwani alikuwa akinisubiri nikimalizana naye tu, tuende kula pamoja. Nilijisikia vizuri sana, akili yangu sikuipa nafasi ya kuwaza itakuaje siku tunaagana, bali kwa sasa nilikuwa nimeamua nifurahie kila dakika na Angel. Nilimpenda kupita kiasi, na ni kama vile alijua kunifanya nimpende zaidi kila dakika. Angel alikuwa na mambo mengi mno ya kuongea na mimi. Yani hata tungeachana sasa hivi, baada ya dakika mbili akaona kuna mtu amevaa kitu cha ajabu kikamchekesha, angenipigia simu muda huohuo acheke na mimi. Sikuwahi kuwa na rafiki wa karibu kiasi hiki. Ukiacha Mawazo ambaye urafiki wetu ulikuwa maalumu sana, Angel alinifanya kuwa rafiki yake mkubwa mno. Hakukaa na jambo dakika bila kunambia, hakunificha kitu, hakutaka niwe na mawazo au nionekane nasumbuliwa na chochote, na hata kama ningejaribu kumficha jambo linalonisumbua, alikuwa mjanja mno kunifanya nijikute nimesema tayari na kisha baada tu ya muda, tunakuwa tunacheka tena.
Nilianza kumfahamu Angel sasa kama mtu asiyependa msongo wa mawazo (stress). Ye alikuwa na msemo wake kwamba eti mwili wake mdogo sana, akiutwisha mawazo (stress) ataumaliza kabisa. Tangu tulipoanza mahusiano, alisema kuwa ameamua kutupa kando mambo ambayo yangemuumiza maishani, na uamuzi wake wa kuwa na mimi, ni uamuzi alioamini ungempa raha siku zote. Yeye aliamini, hata kama tutakuwa mbali ki jiogorafia, ikiwa mioyo yetu imeshikamana pamoja, basi hakuna cha kututenganisha. Kilichonivutia zaidi kwa mrembo huyu ni kuwa mpaka sasa bado alikuwa anaendelea na ratiba yake ya kuona wagonjwa, na mara moja kila wiki lazima angetembelea hospitali hasa za serikali kusalimia wagonjwa.
Nilitamani kujua wanaendelea vipi na Damian lakini mara zote niliona hilo si jambo la msingi kuliruhusu lichukue muda wetu mchache tulokua tumebaki nao. Siku nilipompa zawadi Mariana, mimi na Angel tulienda kula chakula cha jioni mgahawa fulani ulio ufukweni mwa bahari. Baada ya chakula tulienda kutembea tembea ufukweni na kujilaza kwenye mchanga. Sasa ilikuwa wakati sahihi kupanga juu ya uhusiano wetu baada ya mimi kuondoka. Nilimwambia ukweli juu ya wasiwasi nilionao kuwa ninaondoka na kumuacha peke yake huku. Sikutaka kuzungumza suala la Damian lakini nadhani alijua tu kuwa nayeye ni kati ya vitu vinavyonipa hofu kubwa. Pia sikuwa na namna sahihi ya kumwambia kuhusu kunifuata Uingereza kwani nilimfahamu kama binti anayependa na kuithamini sana kazi yake. Kwa bahati Angel aligundua hofu yangu na pia tayari alikuwa na mipango yakinifu kichwani
“Nenda kasome Nathani. Nilifanya maamuzi magumu siku ile tulipoonana nikakwambia nakupenda pia. Siku iyo hiyo asubuhi kabla sikutumia ujumbe, nilikuwa tayari nimeongea na Damian kumwambia kwamba hatuwezi tena kuendelea na nimeamua tuachane. Ukweli ni kwamba maneno yako ya jana yake yalinifanya nijione kwamba ni lazima niamue kile ninachohisi ni sahihi kwa maisha yangu. Tumevutana sana sana na Damian, yaani hadi kaenda nyumbani kuongea na dada na kaka zangu, na amefanya yote ilinturudiane, lakini simtaki tena. Alikuwa analazimisha kuja nikamwambia haina haja ya kuja kwani saivi nimebanwa sana na hivyo hatutakuwa na muda wa kuonana. Bahati nzuri ananijua kuwa huwa namaanisha, hivyo alijua kabisa ni kweli angekuja bila mimi kuruhusu, tusingeonana.” Alinielezea Angel kwa umakini, kisha akaendelea,”Nakupenda, tena sana. Najua uhusiano wetu ni mchanga lakini nimedhamiria kuwa tutakuwa pamoja. Yaani tuwe kama yale mapenzi yanaoandikwa kwenye vitabu au ya tamthilia. Mimi ninapenda kusoma, na najua elimu ni kati ya vitu vinavyonipa nafasi kubwa hata katika kazi za watu. Nimefikiria kuwa nianze kutafuta chuo Uingereza pia. Ofisini kwetu wanakubali masuala ya shule sana, lakini kwa kuwa ni nje ya nchi, na ndio kwanza nimemaliza shahada ya pili, ambayo nilikuwa nikipewa ruhusa kufanya kazi nusu siku, itanibidi nisubiri walau mwaka mmoja kabla sijaenda kusoma tena. Ninachokuhakikishia tu, hatutachukua muda mrefu kabla ya kuwa pamoja tena, na pia sikuizi simu na mitandao imerahisisha mawasiliano sana hivyo hatutakosana sana.” Hicho ndicho nilichotamani sana kusikia kutoka kwa malaika wangu. Japo tulikuwa sasa tunahesabu masaa tu ya kuwa pamoja, lakini maneno yake yalinipa faraja kubwa mno juu ya kuondoka kwangu Tanzania
PART 9, A: 22, Feb. 2016
Siku ilikuwa imewadia ya kusafiri kwangu. Saa tisa kasoro dakika kumi alfajiri simu iliniamsha. Jana yake nilikuwa nimelala karibu saa sita hivyo nililala kwa masaa matatu tu. Nilipokea simu nikiwa na usingizi mzito, nikasikia sauti ya malaika wangu kwa simu ikiniamsha. “Mbona bado usiku mpenzi?” nilimuuliza nikitamani anambie lala tena kidogo, lakini ilikuwa inatakiwa niamke muda huo. Ndege ilikuwa inaondoka saa 12.15 asubuhi, muda wa kufika ilikuwa ni masaa matatu kabla, au kama ningechelewa walau mawili na nusu. Nililala nimeweka kila kitu tayari kiasi kwamba haikunichukua dakika kumi kumaliza kujiandaa. Angel alifika saa tisa kamili kunichukua. Tukaondoka kwenda uwanja wa ndege wa Mwl. Julius Nyerere, ambako haikutuchukua muda mrefu kufika. Kwa usiku kama huo, hakukuwa na foleni wala magari mengi ya kutuchelewesha. Angel aliendesha gari kwa mwendokasi wa 80 hadi 110 kilomita kwa saa. Saa tisa na dakika ishirini tuliingia airport, tukakaa sehemu ya kusubiria kwa nje huku tukisubiri kuitwa.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nikiwa nje huku tunaagana na Angel, alinipa maelekezo namna ya kufanya nikiingia ndani kwani alijua ni mara yangu ya kwanza kabisa kupanda ndege. Muda ulipowadia, nilimkumbatia kwa muda wa kama dakika au zaidi, nikambusu na kumuaga. Huo haukuwa wakati mzuri kwangu. Ni mara ya kwanza niliona kuwa ‘kwaheri’ si neno zuri sana. Niliingia ndani, sehemu ya kukaguliwa, nikavua viatu na mkanda, nikatoa vitu vyote mfukoni, nikapita sehemu maalumu kukaguliwa kwa umeme. Baada ya hapo tuliingia sehemu maalumu kwa ajili ya kusubiria muda wa ndege yetu. Baadaye nilisikia abiria wa ndege ya Swiss air kuelekea Heathrow airport ya London Uingereza tukiitwa, nikaelekea mlangoni, tukakaguliwa tiketi, nikaingia uwanjani na kwa mara ya kwanza nikaona ndege karibu kabisa kiasi cha kuona mpaka watu wa ndani. Kisha nilifika kwenye ndege yetu, nikapanda ndege kubwa yenye abiria kama mia mbili au zaidi, nikakaa siti kulingana na tiketi yangu ambayo ilikuwa upande wa dirishani, nikafunga mkanda wangu, nikachukua kijitabu kilichokuwa mbele yangu chenye maelezo Fulani nikaanza kusoma. Dakika chache baadaye alisimama mbele yetu muhudumu wa ndege, binti mwembamba mrembo aliyevaa nguo za sare (uniform) zenye kuvutia. Alikuwa akitoa matangazo kadhaa ambayo niliyasikiliza kwa makini, aliongea kwa lugha ya kiingereza na kisha ya Kiswahili. Alielekeza jinsi ya kufunga mkanda, jinsi ya kujiokoa ikitokea dharura, vifaa vya usalama wa abiria na mambo kadha wa kadha. Baada ya maelekezo, tulisisitizwa kutosimama wakati ndiyo ndege inataka kupaa, na kila abiria alitakiwa awe amefunga mkanda.
Sekunde chache baadaye ndege ilianza kukimbia kama gari lenye kasi, kwa muda mfupi kiasi kisha nilisikia tumbo kama linavutwa kwa juu, nikastuka kidogo. Wakati huo macho yangu yalikuwa yakichungulia kwenye dirisha ambalo halikuwa limefunguliwa, japo liliweza kunionesha nje palivyo. Ndege ilipoanza kupaa, sikuweza tena kuendelea kuchungulia nje, niliangalia mbele kuona labda kunaweza kukawa na hatari yoyote. Kumbe ilikuwa ni kawaida ndege ikiwa inaacha uwanja. Nilipoona wenzangu wote wametulia, hasa jirani yangu, nami nikatulia. Ulikuwa ni mwanzo wa safari ndefu ya kwenda Uingereza. Nilikua sijui mtu mule ndani wala huko niendako. Jirani yangu alikuwa mzungu, mtu mzima kidogo, kama wa miaka 42 hivi, ambaye baada ya kusalimiana alipoingia, hatukuwa tumeongea chochote.
Kichwani niliwaza mambo mengi mchanganyiko. Nilimuwaza mama yangu na wadogo zangu ninaowaacha, japo niliamini ule mradi wa kilimo ungefanya vizuri lakini nilikua na hofu kuwa endapo ungekwama sijui wangepata wapi pesa za kuwatunza. Sikutaka mama apate shida maana nilimjua jinsi alivyokuwa anajali watoto wake. Nilijipa moyo kuwa mambo yatakuwa sawa, na niliamini Mungu atawasaidia. Pia nilimuwaza malaika wangu Angel, aliyekuwa amenisindikiza airport siku hiyo. Bado akili yangu ilirudia baadhi ya maneno ya kuagana kwetu aliyonambia, na yalinipa faraja. Nilifumba macho na kuhisi uwepo wake kama mtu aliye pembeni yangu kwenye siti niliyokaa. Nilijiona kana kwamba ninasafiri pamoja naye kwenda Ughaibuni, na hii ilinifanya nijisikie vizuri sana. Nilipofumbua macho na kuangalia kulia kwangu, niliona sura ya mwanaume mzungu badala ya binti mrembo Angel.
Jambo jingine lililoendelea kichwani mwangu ni suala la shule yangu ninayoiendea. Niliwaza jinsi gani Mungu amenipa nafasi ya kutimiza ndoto zangu hatua kwa hatua, na sasa nilikuwa nakamilisha hatua kubwa mno. Moyo wangu ulifurahi kila nilipojihisi kuwa hatimaye mimi ni daktari, na sasa ninakwenda kuwa daktari mwenye ujuzi maalumu (specialized doctor). Nikawa pia na hofu kidogo juu ya maisha mapya kwenye jiji kubwa ninaloliendea, katikati ya watu weupe tena nisiowajua kabisa, lakini nilikuwa tayari mtu mzima na pia nilikuwa nina elimu hivyo kunifanya nijiamini zaidi. Ufaulu wangu wa shahada ya kwanza ulikuwa mzuri na hata kama nisingepata nafasi ya kwenda nje, hospitali ya muhimbili walikuwa tayari kuniajiri baada ya ule mwaka wa mafunzo (internship).
Nilikuwa na matumaini nitaonana na rafiki yangu Luzoki nikifika lakini hiyo ilikuwa kama ndoto tu kwani sikuwa na anuani yake wala taarifa za kunisaidia kumpata. Nilipokwenda mara ya mwisho nyumbani, baba yake alinambia kijana wake amekuwa akihama kutoka mji mmoja kwenda mwingine, hivyo kushindwa kuwa na anuani maalumu. Aliwanunulia simu wazazi wake, lakini pia namba walizokuwa nazo hazikuwa zinapatikana tena, walisubiria awatafute wapate namba mpya. Kazi yake ilimtaka kusafiri mara kwa mara, na pia ilimfanya asitulie sehemu moja.
Huku mawazo hayo mengi yakiendelea kichwani mwangu, nilistuliwa na sauti ya binti mrembo,’Samahani, utahitaji kinywaji gani?’. Alikuwa na kijimeza kinachotembea chenye chai, juice, maji, na vinywaji tofauti. Pia alinikabidhi kikontena chenye vitafunwa, basi nikamuomba chai ya maziwa. Ilikuwa tayari ni saa mbili asubuhi. Nikanywa chai na vitafunwa, sasa nikaona safari bado ndefu sana hivyo inabidi nianze kuongea na huyu jirani yangu mzungu. “What is your destination?” nikimaanisha hatima ya safari yake ni wapi. “ It is USA but I will spend some hours or a day in London, before taking another flight there. I have a friend to meet in London, but my family stays in Virginia, USA.” (Ninakwenda USA-Marekani lakini nitakaa masaa kadhaa au siku moja London-Uingereza kabla ya kuchukua ndege nyingine hapo. Nina rafiki nakutana naye London, lakini familia yangu iko mji wa Virginia-Marekani).
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya hapo tulianza kuongea stori nyingi sana. Aliniuliza ninapoelekea, alianza kuongea vitu vingi na mimi kiasi cha kunishangaza sababu mwanzoni sikujua kama ni mtu msemaji namna ile. Alinihadithia kilichokompeleka Tanzania, na kuna mambo yalinishangaza kidogo kwenye hiyo stori.
“Nilikuwa na rafiki mtanzania, huwa nina kawaida ya kujenga urafiki kwa urahisi. Huyu jamaa tulikutana tu kwenye sehemu ya mkutaniko (mall) fulani huko Virginia, tulikuwa kwenye sinema, nilikaa naye karibu. Ikatokea tukaanza kuongea vitu mbalimbali nikagundua tumefanya fani moja ya elimu, yaani sayansi ya utafiti. Nilivutiwa na hilo suala, kwenye kuulizana nikagundua anaishi Tanzania na huko Marekani alikuja kwajili ya mambo ya utafiti. Mimi nilikuwa nimeisikia Tanzania miaka kadhaa kabla, na nilitamani kwenda siku nyingi lakini nilikuwa bado natafuta sababu sahihi ya kwenda hasa nitakayoingiza pesa. Hapo ilibidi nitafute habari zaidi kuhusu nchi yake, na alinisaidia kujibu maswali yote niliyotaka kuuliza. Alinambia juu ya mambo mbalimbali ambayo yalinivutia zaidi kuja Tanzania. Kikawaida mimi ni mtu ninayejali watu wa hali tofauti, na alinambia hali za maisha za watu wengi wa nchi yake, hasa wanaoishi vijijini. Nilishangaa pia kujua kwamba kuna watu wako mjini ila wanaishi wa thamani ya chini ya shilingi dola moja kwa siku, nikaona nahitaji kuja walau nitafute namna ya kusaidia baadhi ya watu.
Hiyo ilikuwa miaka nane iliyopita, na ndani ya mwaka mmoja tu tangu nilipoongea na huyo jamaa, Hemed, alinisaidia kufanikiwa kuja. Nilikuwa nina mashirika ambayo niliingia nayo mikataba mbalimbali ya utafiti, hivyo nilipokuja mara ya kwanza, nilifanikiwa kupata taarifa sahihi ya kupeleka, nikapata ufadhili wa kufanya miradi. Nimefanya miradi miwili tayari, na mmoja nimeacha unaendelea. Kuna mradi nilifanya wa kuwezesha kina mama wa hali za chini, kwa kuwagawia mitaji, huu ulikuwa wa kwanza na ulinipa kuona matatizo mengi ya watanzania. Lakini pia kulikuwa na changamoto kidogo ya utendaji kwani kuna watu walikuwa wamelenga zaidi kula rushwa na tena kwa kiwango kikubwa. Kwa bahati, nikiwa nafanya mradi wa kwanza, nilikutana na jamaa mmoja anaitwa Nathan Martin, yeye ni mkanada (m-Canada), lakini ni mtafiti wa zamani na tayari ana shirika kalianzisha Tanzania. Huyu ni daktari, lakini alijikita siku nyingi kwenye mambo ya lishe za kina mama na watoto wadogo. Shirika lake lilikuwa na taarifa nyingi kuhusu wakina mama wa vijijini. Alinisaidia watu sahihi wa kufanya nao kazi na pia kupanua mradi wangu baadhi ya mikoa”.
Akiwa bado anaendelea na hadithi zake nyingi, akili yangu ilihama kidogo. Niliposikia jina la Nathan, nilistuka, hasa aliposema kuwa ni daktari lakini aliyejikita kwenye mambo ya lishe za kina mama na watoto. Nilihisi kabisa anamzungumzia yule Nathan ambaye mama alinambia habari yake, kuwa ndiye daktari aliyenimzalisha mimba yangu, na kuyaokoa maisha yangu na ya mama. Niliendelea kumsikiliza huyu mzungu lakini nilitamani kumfahamu huyo Nathan anayemzungumzia.
Safari ya Dar kwenda Uingereza ni safari ndefu kidogo. Kwa ndege yetu, ilikuwa ni safari ya masaa kama 11 hivi. Kwa bahati jirani yangu alikuwa ni mtu ambaye tulikuwa na vitu vingi vya kuongea hivyo kupunguza urefu wa safari. Stori zake zilinivutia na kunifundisha vitu vingi, ila pia kuna wakati zilinichekesha. Nilimwambia juu ya huyo Nathan ambaye nahisi ndiye daktari aliyemsaidia mama yangu kujifungua, na aliponitajia makadirio ya umri wake kuwa ni kama miaka kati ya 54-60, nilihisi lazima atakuwa ndiye. Alinipa namba yake na kunishauri nimtafute akanambia, ni mtu rafiki sana kwa watu, na atafurahi kama ni yeye kweli unayemdhania endapo utamtafuta.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Tukiendelea na safari yetu, jirani yangu alifanya safari yangu kuwa si yenye kuchosha. Tulikuwa bize tukiongea stori za hapa na pale. Alinieleza kuhusu familia yake iliyokuwa Marekani, alinieleza kuhusu kazi alizozifanya, changamoto mbalimbali alizopitia nchini Tanzania na nilijiona kama tayari nimepata mwenyeji walau kwa muda ule nitakaposhuka Uingereza sitapata tabu sana.
Hatimaye baada ya safari ndefu tulifika Heathrow International Airport ya nchini Uingereza jiji la London. Nilikuwa nina maelekezo yote kwa njia ya ramani na wafadhili wangu walikuwa wamenipatia pesa tayari za gharama za kuanzia nitakapofika nchini Uingereza, nilikuwa nimemwambia Mr. Johannes, yule jirani yangu juu na yale maelekezo ili ikiwezekana anisaidie nisihangaike nikishuka. Jiji la London ni kubwa mno. Maisha yangu yote sikuwahi kuhisi kuna siku nitafika kwenye jiji kubwa na zuri namna ile. Kuna muda Fulani nilipitiwa na usingizi nikalala kidogo, nilipoamka na kuangalia dirishani niliona taa za ajabu kana kwamba ni maua yaliyopangiliwa. Kulikuwa na taa zinazomulika vizuri mno eneo lote. Tulikuwa tumeshaingia ardhi ya Uingereza. Tofauti kati ya nchi ile na Tanzania ilikuwa ni ya masaa mawili hadi matatu kutegemea na eneo, sisi tukiwa tumewatangulia. Hivyo baada ya mwendo wa masaa kumi na moja, tulifika jijini London mida ya kama saa tisa mchana. Lakini msimu huo ulikuwa ni wa winta, yaani jua huwahi sana kuzama. Nchi za ughaibuni kuna misimu ya ajabu sana, kuna wakati jua linaweza kuwepo mpaka saa tatu usiku na ikawa kama mchana kweupe na asubuhi sana alfajiri likawahi kuchomoza. Lakini kuna vipindi jua huwahi sana kuzama kiasi kwamba saa kumi jioni ni giza kabisa. Hivyo mida hiyo kulikuwa giza kwa mbali limeanza lakini tofauti na nchini kwangu Tanzania, kule hata usiku mwanga ni kitu cha kawaida. Maeneo ya uwanja wa ndege kuna sehemu kuna taa zenye mwanga zaidi ya jua. Yaani ni taa nyeupe mno kiasi kwamba zinaweza kufanya usahau kama ni usiku.
Wakati tunashuka kwenye ndege ilibidi niwe karibu na bwana Johannes ili nisikosee maelekezo ya vitu vidogo kama kuchukua mizigo yangu na kadhalika. Jinsi uwanja wa ndege ulivyokuwa, yani nilihisi nikiachana naye kwa dakika tuu, nitapotea. Ni uwanja mkubwa kama mji, kuna sehemu kuna ngazi za kutembea, kwingine ni kama sakafu ya kawaida laini lakini nayo inatembea, kuna sehemu ni kama mko mjini humo humo ndani, yaani kuna maduka makubwa na kila kitu. Yaani kila nilichoangalia kilinishangaza. Sehemu ya kuchukulia mizigo ilikuwa ni nyingine kabisa. Nilimfuatisha mwenyeji wangu kwa wakati huo na tukiwa bado tunaenda ilibidi nimuulize mizigo yetu inakuaje. Niliwaza kuwa tumeshuka tayari lakini sioni dalili za kupata mzigo wangu. Alisema tunaelekea sehemu ya kuichukua. Tulisimama eneo moja nikaona mashine inatembea huku imebeba mizigo. Zilikuwepo mashine nyingi sana za namna hiyo ila mimi nilifuata ile aliyoifata bwana Johannes. Tulisimama na kila mtu alipoona mzigo wake wakati mashine inazunguka aliuchukua.
Chuo ambacho nilikuwa nikienda kusoma ni chuo kikuu cha Liverpool. Mimi si mfuatiliaji wa mpira lakini niliifahamu timu ya mpira ya Liverpool. Nilihisi kusomea chuo hicho kutanifanya kwa sehemu niwe mshabiki wa timu hiyo. Bwana Johannes alinionesha sehemu ambapo nilipata usafiri wa treni itakayonifikisha chuoni hapo. Tuliagana na rafiki yangu mpya huyo, akanipa namba yake, na kisha nikapanda treni kwa mara ya kwanza kwenye maisha yangu. Na kwa hakika ilikuwa nzuri mno. Nadhani kila nilichokiona nchini Uingereza kilikuwa kizuri hata mara kumi zaidi ya mazingira ya nchini kwangu. Sikuamini macho yangu, kwani katika kuota kwangu nikiwa mdogo sikuwahi kudhani kuwa ningepata fursa ya kuishi jiji zuri namna hiyo. Nilipofika Liverpool, nilishuka, nikachukua taxi iliyonipeleka mpaka sehemu ambayo ndiyo ningeishi. Yalikuwa ni makazi ya wanafunzi yaliyokuwa kidogo nje ya chuo. Jioni hiyoiyo nilionana na uongozi wa hapo, nikaonesha vitambulisho na kutoa maelezo kidogo, baada ya taratibu fupi nilipatiwa funguo ya chumba na kuoneshwa chumba changu. Baadaye niligundua ni kati ya vyumba vya wastani lakini kiukweli kwangu kilikuwa chumba kizuri mno. Kilikuwa na kama jiko ndani, pamoja na choo na bafu. Ilikuwa ni kama chumba cha hoteli nzuri, na nilifurahia.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hali ya hewa ilikuwa tofauti kabisa na Tanzania. Mavazi ya watu wengi yalikuwa ya kujikinga na baridi. Kwa kweli nilihisi baridi pia lakini nilikuwa nimejidhatiti kwa jaketi kubwa na kofia na gloves mikononi. Chumba changu kilikuwa na kiyoyosi (AC). Nilijua baridi haingeweza kunizidia hata msimu wa baridi kali kwani nina uwezo wa kupandisha joto la kiyoyosi kitoe hewa ya joto badala ya baridi. Nililala, asubuhi nikaamka, na hivyo ndivyo maisha yalivyoanza nchini Uingereza. Nilijua nina miaka zaidi ya mitano ya kuishi huko kwani kwa mfumo ya nchini humo, daktari yeyote kutoka nje ya nchi anayetaka kuongeza ujuzi (specialization) ilimbidi asome kwanza miaka miwili ya msingi (Foundation course), mwaka mmoja wa uzoefu (Intership) na kisha ndipo asome miaka mitatu ya kujikita kwenye fani yake (specialization)
Asubuhi mapema niliamka na kuanza taratibu ili nijue ratiba za shule yangu na maisha ambayo ningeishi nchini kule. Nilienda ofisi husika, nikapata maelekezo muhimu. Ilikuwa natakiwa kuanza chuo siku mbili tu baada ya siku hiyo. Nilitumia siku hizo mbili kujua maisha ambayo wanafunzi wenzangu wa nje waliishi hapo chuoni. Niligundua natakiwa kutafuta kazi haraka sana, na kwa bahati uongozi wa chuo ulinisaidia namna rahisi ya kupata kazi za kufanya muda wa ziada. Hazikuwa kazi za mtu msomi, lakini sikujali. Zilikuwa kazi ambazo kwa Tanzania zingeonekana zisizofaa, kazi za vijana ambao hawajakwenda shule kabisa, lakini kiukweli kila saa moja niliyofanya kazi niliingiza kiasi cha paundi hamsini hadi mia, ambayo ni kama shilingi laki moja hadi mbili au zaidi za kitanzania. Hii ilikuwa pesa nyingi sana kwangu Nathan. Japokua gharama za maisha zilikuwa juu pia kulinganisha na nchinii kwangu, lakini nilikuwa na hakika sasa ningepata kiasi cha kutosha kujenga nyumba ya familia nchini Tanzania na pia ningeweza kuweka pesa kwaajili ya mipango yangu na Angel.
Kweli baada ya siku mbili nilianza shule, ambayo haikuwa ngumu sana na kidogo ilinipa muda wa kufanya kazi. Ilikuwa shule inayonipa nafasi kubwa ya kufanyia kazi ujuzi wangu kwa matendo, na pale pale chuoni kulikuwa na hospitali kubwa ambayo ndiyo ilikuwa sehemu kubwa ya mafunzo yetu. Darasani nilikutana na watanzania wenzangu wawili, jambo ambalo lilinipa faraja. Mmoja alikuwa amezaliwa na kukulia huko lakini wazazi wake wote walikuwa watanzania. Alijua Kiswahili kidogo japo hakukizoea, lakini pia alipenda kuongea nami Kiswahili. Mwingine alikuwa ni mtanzania anayeishi Kenya, mama yake alikuwa mkenya babaye mtanzania. Huyu alikuwa ni kijana mtanashati na mdogo sana pale darasani. Alionekana ni mtu anayejielewa na kiukweli alikuwa na akili hata za darasani.
Jambo lililonisikitisha sana kuhusu kijana huyu mtanashati ni kile nilichokuja kugundua juu ya maisha yake. Kijana huyu ambaye nisingependa kumtaja jina lake, alitumia muda wake mwingi kuwa na marafiki wa kike, kitu ambacho si cha ajabu. Lakini cha kushangaza hakuwa na mpenzi licha ya uzuri wake na kuvutia kwake mno. Alijipenda sana na naweza sema ni kijana wa kiume wa kwanza niliwahi kutana naye anayejipenda kiasi hicho. Siku moja jioni, kwa sababu nilikuwa nimezoeana naye, aliniambia nipitie alipokuwa anaishi nipafahamu sababu sote ni watanzania hivyo ni kama ndugu. Ilikuwa ni makazi ya wanafunzi yaliyokuwa nje kidogo na chuo, na japo ni mbali zaidi ya pale nilipokuwa naishi mimi lakini umbali haukuwa mkubwa.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kufika hosteli zao, tulipanda kwenye lifti mpaka floo ya tano. Tulishuka na kuelekea chumba kimoja kilichokuwa kwenye korido ndefu, akafungua mlango na kunikaribisha ndani. Nilishangaa kuona chumba kizuri mno ajabu. Yaani ilikuwa kama mara tano au zaidi ya chumba changu, nikajisemea moyoni, ni chake kweli?? Jambo lililonishangaza zaidi ni rangi za chumba kile. Kilipambwa kwa rangi ambazo katika uelewa wangu nilifahamu kuwa ni rangi za kile. Rangi nzuri za pinki na kijani Fulani ya kuwaka, pamoja na nyeupe. Mashuka aliyotandika yalikuwa na maua sawa na mapazia, na rangi ya zuria alilotandika chini halikuwa tofauti sana na rangi ya pazia. Sehemu tulizokuwa tunaishi zilikuwa ni vyumba vyenye sehemu ya kupikia kwa ndani, choo na bafu. Mlango wa jiko lake ulikuwa wazi na niliona napo pamepambwa kama jiko la binti msafi anayejipenda sana. Mengine siwezi elezea, ila nilipatwa mshangao kuona mahali alipoishi kijana huyu.
Kwa kuwa tulikuwa tumezoeana kidogo, nilimuuliza, “Mbona chumba chako kama cha msichana?” alitabasamu tu na kunipiga kidogo begani kisha akajibu, usijali. Nilianza kujiuliza maswali mengi ambayo niliyapatia majibu muda mfupi baadaye. Kabla hatujakaa sana alienda kuleta chakula Fulani ambacho alitoa kwenye friji na kupasha, tukala. Kisha nikaanza kuona mwenzangu akiniangalia sana machoni, jambo lililonifanya kidogo nikose pozi. Nikamwambia kuwa nadhani naweza kuondoka sasa na ni vizuri nimepaona kwako, lakini alinizuia na kunambia nisubiri kidogo. Nikashangaa kuona ananisogelea na anaanza kunishika utadhani ni mtu wa jinsia tofauti na mimi. Sasa ndipo nikaelewa kuwa huyu kijana alikuwa ni shoga. Roho iliniuma sana, halafu nikamuhurumia. Kiasi nilishikwa na hasira lakini huruma yangu kwake ilizidi hasira. Nilimuita jina lake, nikamwambia, samahani, mimi si mtu ninayeweza kufanya hayo mambo. Nikamwambia naomba uniruhusu niondoke. Alinitazama, machozi yakamlenga, akaniomba nimsamehe kisha akanifungulia mlango na kunisindikiza. Usiku huo niliwaza sana juu ya huyu kijana daktari mdogo na mtanashati sana. Nilitamani kujua ilikuwaje mpaka akafikia hatua hiyo, lakini sikuona namna sahihi ya kumuuliza. Jinsi alivyoonekana pale nilipomkatalia ni kama alijutia kwanini alinionesha kuwa yeye ni shoga. Ni kama mtu ambaye hakufurahia sana kuwa vile, na ni kama mtu ambaye alikuwa na hali ambayo hana mamlaka nayo tena. Nilimuwaza kwa muda baadaye nikaiambia nafsi yangu iachane naye, japo kama hayo niliyokuwa nafikiria yalikuwa kweli, ningetamani sana kumsaidia.
Siku chache tu baada ya kufika chuo nilifanya haraka kutafuta laini ya simu ambayo nitaweza kuwasilina Tanzania, nikaipata. Mtu wa kwanza kumpigia alikuwa mpenzi wangu Angel, ambaye alifurahi mno kupata simu yangu. Nilikuwa nina siku tatu sijawasiliana naye lakini ilikuwa kama mwezi tayari. Baada ya hapo nilijiunga na mitandao ya kijamii na sasa ikawa haipiti masaa tunawasiliana kama watu walio karibu kabisa. Nilimpigia pia mama yangu na kuongea na wadogo zangu wote waliokuwa nyumbani. Tangu baba alipofariki, nilijitahidi sana kuwa karibu na Neema walau kwa kiasi Fulani kuchukua nafasi ya baba yake, hivyo nilipoongea naye siku hiyo ilikuwa faraja kubwa sana kwake.
Maisha yangu mapya jijini Liverpool yaliendelea na hayakuwa magumu. Ratiba zangu zilikuwa za kupokezana kati ya kazi na shule. Nilifanya kazi kwa masaa walau manne kwa siku, kadiri nilivyopata nafasi. Nilipoongea na Angel kuhusu aina ya kazi nilizokuwa nafanya, alinitia sana moyo. Katika maisha yake, pamoja na kuwa alizaliwa kwenye familia tajiri lakini hakuwa mtu mwenye dharau juu ya watu wa chini. Pia nadhani kwa kuwa kipindi yuko mdogo waliishi Marekani, na mama yake alikuwa akifanya kazi zisizo na hadhi ya kisomi nchini huko, ili kuwaongezea kipato, yeye ndiye alikuwa wa kwanza kunishauri nikifika nitafute kazi yoyote. Nilihakikisha natumia kila muda nilioupata kutengeneza pesa, mbali na masomo yangu. Nikawa kijana bize sana. Sikuwa na muda wa kuwaza mambo mengine. Kujua kuwa nina mwanamke Tanzania anayenipenda sana, kujua kuwa nina mzazi anayeniamini sana, na kujua kuwa nina shahada ya kazi niliyoiota tangu utoto, vilinipa nguvu katika kila nilichokifanya.
Wakati huo nilikuwa nikifanya juhudi kumtafuta Mawazo ambaye ilikuwa tayari imepita miaka mingi bila kuonana. Wazazi wake hawakuwa kijijini tena, walihama kwenda mjini ambapo kijana wao alikuwa amewanunulia nyumba. Niliambiwa na mama, nikawatafuta kwa simu lakini sikuwapata tena. Nilitamani wanipe mawasiliano ya kijana wao, lakini haikuwezekana. Niliamini kuna siku japo kwa bahati tungeonana tena na Luzoki, jambo ambalo kwa wakati huo lilikuwa kama ndoto. Miezi ikaendelea kukatika, na ratiba zangu zikazidi kuwa bize. Lakini nilihakikisha sikosi muda wa kuwasiliana na malaika wangu Angel. Huyu binti alikuwa nguvu yangu kubwa, alinipa sababu ya kuendelea kufanya kwa ujasiri kila nilichotakiwa kufanya.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
NCHINI TANZANIA
Baada ya Angel kuanza mahusiano na mimi, Damian yule mchumba wake aliendelea kumtafuta na kumbembeleza warudiane. Wanasema mwanamke akikutoa moyoni, basi ni jambo zito sana kukurudisha. Kwa jinsi Angel alivyokuwa amempenda Damian kabla, na jinsi alivyokuwa naye miaka mingi akimvumilia kwa mambo mengi, ilikuwa ni ngumu sana kuamini kama angeweza kumuacha kwa siku moja tu. Hakujua kuwa tayari moyo wa Angel ulianza kumuacha miezi kadhaa kabla ya kumtamkia kuwa ndiyo mwisho wao. Ilimchukua muda Damian kukubali hivyo mwanzoni hakutumia nguvu sana kumtaka warudiane, lakini baada ya mwezi hivi, mimi nikiwa tayari nimeondoka, alianza sana kumsumbua Angel.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment