Search This Blog

Thursday, 2 June 2022

MWANGAZA - 5

 







    Simulizi : Mwangaza

    Sehemu Ya Tano (5)





    Japokuwa Angel alijua angenitia wasiwasi kunambia jinsi gani Damian alikuwa akimsumbua lakini jinsi mbavyo tulikuwa marafiki, hangeweza kunificha. Mwezi na nusu baada ya mimi kuondoka Damian alienda jijini Dar es Salaam kwa lazima. Alimlazimisha waonane, na alipokataa alimfata ofisini mida ya kazi. Kwajili ya wivu wake, ofisini walimfahamu kama mchumba wa Angel, na alipofika mara hii, alijitahidi kuonesha kwa kila mtu kuwa yeye ndiye mume mtarajiwa wa Angel. Mawazo yake yalimwambia kwamba kilichompa jeuri Angel kumuacha kilikuwa ni mwanaume mwingine, na alihisi wanafanya wote kazi. Miaka yote waliyokuwa pamoja, hakuwahi hata kuhisi siku moja Angel angemucha au angewahi penda mwanaume mwingine.

    Baada ya kumsumbua kumfata ofisini mara kadhaa, aliamua akubali wakae chini waongee ili wamalizane. Wakiwa kwenye mgahawa mmoja maarufu jijini, siku moja baada ya Angel kutoka ofisini, walikuwa na maongezi marefu ambayo Angel alidhani ndiyo yalikuwa yanahitimisha uhusiano wao, lakini haikuwa hivyo. “Najua tu kuna mwanaume umempata mke wangu. Sijui amekudanganya kwa lipi mpaka ukaamua kuniacha. Yani siamini kama umesahau mimi ndiye mwanaume wa kwanza kabisa maishani mwako. Umesahau mapenzi tuliyokuwa nayo kabla. Angel, mimi ndiye niliyekufundisha mapenzi na ndiye ninayekupenda kwa dhati. Nina uwezo wa kukupa chochote au kukufanyia chochote unachohitaji mke wangu, niambie unataka nini uachane na huyo ng’ombe aliyekudanganya”. Bwana Damian alijigamba kwa maneno mengi huku akiamini kabisa kuna mwanaume amemdanganya mchumba wake ili waachane. Alitamani sana kumjua huyo mwanaume na mara kadhaa alijaribu kufanya upelelezi pale ofisini kwa Angel kujua ni nani, japo hakupata habari yoyote ya kumsaidia. Wakati huo Angel alimsikiliza huku akiwa kimya, alikerwa na jinsi ambavyo alijisifu kwa kuwa mwanaume wa kwanza na wa pekee kwake. Aliwaza amwambie nini akubaliane kuwa hana nafasi tena moyoni mwake.

    “Sikiza Damian, ni kweli wewe ndiye mwanaume wangu wa kwanza kabisa kuwa naye, na pia ni wewe uliyenifundisha mapenzi nakubali, lakini si sheria kuwa mpenzi wa kwanza ndiye mume wako. Nilikupenda mno wewe unajua, lakini ulipojua hilo, ulitumia udhaifu wangu kuniumiza. Usidhani nimesahau jinsi nilivyolizwa na kutukanwa na wanawake wenzangu. Mbali na hayo ambayo sikuizi yameisha, una jeuri sana ya pesa. Unadhani pesa ni kila kitu. Ugomvi wetu mkubwa umekuwa kuniachisha kazi na unadai mwanamke wa mtu tajiri kama wewe hapaswi kufanya kazi. Kwa kuwa mshahara ninaopokea unaweza kunilipa hata mara tano yake basi huoni sababu ya mimi kuajiriwa hata kama naipenda kazi yangu. Hujui kuwa najiendeleza kitaaluma na hii kazi inaniongezea ujuzi na soko la nafasi kubwa zaidi. Pia kujua kuwa u mwanaume wangu wa kwanza basi ulihisi sitakuwa na jeuri ya kupenda tena, lakini nikwambie tu, unachowaza ni kweli, nimepata mpenzi mwingine. Huyu anajijua kuwa si wa kwanza, lakini ananipenda na kunithamini. Anajua nafasi ya maamuzi yangu binafsi katika maisha na anathamini ndoto na malengo yangu. Kwa bahati, hutamjua ni nani maana najua jinsi ambavyo unaweza kutumia nguvu ya pesa zako kumfanyia chochote. Na nadhani sasa sihitaji tena mahusiano wala mawasiliano kati yetu yaendelee, huwezi kunibadilisha Damian, sikutaki tena”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kulingana na Angel, wakati anamwambia maneno hayo, macho yake yalibadilika yakawa mekundu kabisa. Akakumbuka kipindi cha nyuma ambapo alikuwa akikasirika namna hiyo kinachofuata ni kipigo, na kidogo akaogopa, lakini alijua hana jeuri ya kunyoosha mkono wake tena. Aliishia tu kusema kwa ukali, ‘Angel stop’. Moyo wake haukuweza kuchukua tena yale maneno yenye ukali wa msumeno aliyoambiwa na mwanamke aliyempenda. Alianza kumwambia mambo ambayo alihisi yatamfanya ajilaumu kumpoteza. “Angel, wanawake wengi sana wananitaka mimi, lakini nakutunzia heshima. Kuna wasichana warembo sana, wenye pesa nyingi, wananisumbua lakini sina habari nao kwa kuwa nakupenda. Nyumbani kwenu mimi ndo mwanaume pekee wananijua, nina uwezo wa kukufanya uishi kama malkia hapa duniani, hapa saivi nimekuja na cheki nikuandikie pesa yoyote, hata milioni mia mbili, au mia tano uitumie kama mtaji, uache kazi turudi Arusha. Najua huku Dar wanakuharibu washenzi hawa”. Alisema hayo huku anatoa cheki na kuandika kisha akampa Angel. Ni kweli alijua Damian ana pesa lakini hakuwahi kumpa pesa nyingi kiasi hicho. Mbali na ajira yake, kuna biashara alizifanya zilizomuingizia pesa nyingi. Akimpa hiyo cheki iliyosainiwa kiasi cha shilingi za kitanzania milioni mia tano, aliendelea kujigamba kuwa ana nafasi nzuri ya kumfanya awe mwanamke mwenye furaha zaidi maishani.

    Wakati mpenzi wangu ananihadithia hiyo stori, nilikuwa natetemeka kwa wivu na hasira. Niliona jinsi gani jamaa anataka kutumia nguvu yake ya pesa kummiliki mwanamke. Japo nilimuamini sana Angel, lakini nilihisi hiyo pesa ni nyingi mno kiasi cha kuweza kumshawishi. Sikutaka kumuharikisha kujua alifanya nini lakini nilitamani amalize hiyo stori kwa haraka sana nijue mwisho ilikuaje. “Niliishika hiyo cheki na kuichana mbele yake. Kikawaida mimi si mtu ninayethaminisha penzi na kitu chochote. Hata nisingekuwa na wewe Nathan, nisingerudiana na Damian, hasa kwa kunipa cheki ya pesa nyingi. Hii ingemuonesha kama ananunua penzi langu, jambo ambalo si sahihi hata kidogo”. Hapo nilivuta pumzi ndefu sana mpaka na yeye akasikia, akacheka sana na kuanza kunitania kuwa macho yalishanitoka nikahisi nanyang’anywa.

    Nilijisikia fahari sana kuwa na mwanamke anayejiamini kiasi hicho. Kwa dunia ya sasaivi, nguvu ya pesa imetawala penzi la dhati kwa kiasi kikubwa mno kiasi kwamba si rahisi msichana mrembo kama Angel kukubali kuwa na mwanaume wa hali ya chini kama mimi ukilinganisha na tajiri mkubwa kama Damian

    Siku hiyo walimalizana na kuagana na Damian ambaye aliondoka akiwa amekasirika na kuumia sana baada ya kuchaniwa cheki, akamuahidi kuwa watarudiana kwa gharama yoyote ile. Ati yeye ni mwanaume mwenye mkono wenye nguvu, usioshindwa. Alirudia tena kusema kuwa hakuna mwanaume anayeweza kumnyang’anya mwanamke wake. Atapambana mpaka Angel mwenyewe akubali kurudi iwe nataka au hataki.



    Baada ya siku kadhaa Angel alipigiwa simu na dada yake waliofatana. Katika familia yao wamezaliwa wasichana wanne na mvulana mmoja. Angel ni wa pili kutoka mwisho. Huyu dada yake alikuwa ndiye pekee aliyekuwa upande wa Angel wakati familia yote inampinga Damian, na hivyo kuwafanya yeye na Angel wawe marafiki. Alikuwa mtu wa kwanza kabisa kufahamu uhusiano wa Angel na Damian, na mara nyingi Angel alimwambia kuhusu chochote kilichotokea kati yao. Japokuwa alijua kipindi ambacho Damian alimuumiza mdogo wake, lakini kwa jinsi ambavyo walikuwa wamejenga ukaribu hata na Damian mwenyewe, mara zote ndiye alikuwa akimshauri Angel amsamehe. Baadaye Angel alikuja kugundua kuwa Damian alikuwa akimuhonga dada yake ili amuombee msamaha, jambo ambalo liliwasababisha kukosana na dada yake.

    Kwa kipindi cha mwisho Angel alikuwa ameacha kumwambia dadayake huyo kuhusu Damian, lakini sasa Damian alikuwa akiongea naye sana kuhusu Angel. Alimuomba amshawishi akubali kuacha kazi akafanye biashara, na huo mara nyingi ulikuwa ugomvi kati ya Angel na dadake pia. Walipoachana na Damian, Angel hakuwa amemwambia mtu yeyote nyumbani, nadhani na Damian pia alikuwa bado hajasema kwa dadake Angel kwani alikuwa bado na matumaini. Baadaye, aliporudi Arusha, ndipo Angel alipopigiwa simu na dadake ikimuomba arudi Arusha haraka sana. “Kwani tatizo ni nini? Mie niko bize kazini sister, nambie nini hasa cha kunileta huko kwa haraka”, aliuliza Angel wakiongea na dadake. “Fanya uje we mtoto, unatakiwa huku haraka. Hiyo kazi wanakulipa bilioni? Mbona umeng’ang’ana utadhani we ndo wa kwanza kuajiriwa msichana?”

    Kwa jinsi alivyokuwa akiongea, Angel alijua kabisa anamuita ili kumsuluhisha na Damian. “Najua keshakuhonga hapo ili unirudishe kwake. Mie simtaki tena sister, na wala saivi hata nani aje kusuluhisha nimeshaamua kuachana naye. Nimegundua kuna mwanaume ananipa furaha sana kuliko Damian, na saivi ndo akili yangu inaelewa kuwa kuna mapenzi ya dhati duniani, yanayoweza kunifanya nijione thamani yangu”. Siku hiyo kwenye simu waligombana sana na dadake. Aliendelea kumlazimisha aende Arusha wakaongee. Alisisitiza kuwa hakuna mwanaume anayempenda kuliko Damian, na kuwa ulimwengu huu wa sasa mwanaume anayeweza kutoa mamia ya milioni kwaajili ya mwanamke huyo ana mapenzi ya dhati.

    LIVERPOOLCHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kila nilipoongea na Angel, nilimuhakikishia kuwa nampenda sana na kuwa yeye ndiye mwanamke pekee anayeyapa thamani maisha yangu. Angel alikuwa furaha yangu kubwa mno. Alinipa ujasiri kufanya kazi na shule yangu kwa jitihada kwani ye ndo alikuwa mshauri wangu mkubwa. Licha ya kuwa mpenzi wangu, urafiki kati yetu uliendelea kukomaa kila siku. Umbali haukuwa tatizo kati yetu kwani tulitumia kila namna rahisi ya kuwasiliana. Nchini Uingereza kuna wanawake warembo, wengi weupe lakini kuna weusi pia. Baadae nilikuja kufahamiana na watanzania wenzangu wa chuo nilichokuwa nasoma, baadhi yao ni wasichana warembo. Lakini akili yangu ilikuwa na mtu mmoja tu siku zote.

    Nakumbuka kuna dada mmoja wa kitanzania ambaye familia yake yote wanaishi Uingereza wakati huo ikiwa ni miaka kumi tangu wahamie, alionesha sana kuvutiwa na mimi. Kwa tamaduni za wenzetu, ni jambo la kawaida kwa msichana kumuonesha mwanaume kuwa anampenda endapo atamuhitaji. Binti huyo, Nirvana Laiser alikuwa mrembo na mwenye muonekano wa upole. Kwa jinsi alivyokuwa anavutia, sikuwahi kuhisi kama angekuwa hana rafiki wa kiume. Na hata kama hakuwa na rafiki wa kiume au mpenzi, sikutegemea kama anaweza kumfuata mwanaume kumwambia anampenda. Niliamini ana changamoto kubwa ya kuwakataa vijana wengi wanaomsumbua. Mimi na yeye tulifahaiana miezi ya mwanzoni pale chuo. Alikuwa anasoma kozi tofauti na mimi lakini siku moja nikiwa maktaba ya pale chuo, alikuja na kukaa karibu na mimi. Hatukuongea chochote mpaka wakati natoka ambapo alitoka nyuma yangu na kuanza kuniita nimsubiri. Tulisalimiana nje kisha akaniomba namba yangu. Nilihisi kanifuata kwa kuwa ni mweusi mwenzie. Ukiwa nchi za wenzetu, hasa Uingereza, kuona mtu wa rangi nyeusi unahisi ni kama ndugu yako. Tulipobadilishana namba, Nirvana alianza kuwasiliana na mimi kwa kasi sana mara akiniomba tuonane kwa chakula cha jioni, mara twende sinema, lakini kwa jinsi maisha yangu yalivyokuwa na mambo mengi kila mara nilitoa sababu.

    Baada ya kuona kila anapojaribu kuwa na muda maalumu na mimi namnyima, siku moja aliniomba tutoke na kunambia kuwa kuna jambo la muhimu anataka kunambia. Tulikaa kwenye mgahawa mmoja jioni, nimsikilize. Kwenye maisha yangu sikuwahi kutamkiwa na binti maneno ya mapenzi kabla ya mimi kumuanza, huyu alikuwa wa kwanza.”Nathan, tangu nilipokuona mara ya kwanza pale maktaba nilitokea kukupenda sana. Huwezi amini, nilikuwa na rafiki wa kiume lakini ile ndiyo siku niliyomwambia tuachane. Nilipokuona wewe nilihisi nimekutana na mwanaume wa maisha yangu. Tangu siku hiyo, nadhani mwezi umepita sasa, sijielewi nina nini. Muda wote nakuwaza wewe, tayari nimemwambia mama yangu kuhusu wewe na kila mara ninapojaribu kukutaka uwe karibu yangu zaidi lengo ni kufanya tuwe wapenzi. Sijui nitafanya nini ukinambia huwezi kuwa na mimi. Najua labda kwa mwanzoni nitahitaji kushea moyo wako na mpenzi uliye naye, lakini najua badaye nitachukua nafasi yote kwani ukinipa hiyo nafasi, nitakufanya uwe mwanaume mwenye furaha zaidi duniani”

    Muda wote huo Nirvana akiongea, nilimuangalia machoni. Aliongea kwa hisia kali. Mara zote mimi huangalia mtu ninayeongea naye machoni ili kujua ni kiasi gani anamaanisha. Maneno aliyoyasema ilikuwa kana kwamba ni msichana ambaye hajatulia na hana msimamo kwenye mapenzi, lakini baadaye nilikuja kuelewa kuwa kwa wenzetu wa nje haikuwa kitu cha ajabu. Pia kama miezi mitatu baadaye alinifuata huyo aliyekuwa rafiki yake wa kiume na kuongea na mimi juu ya huyu msichana, nikashangaa sana. Aliniambia kuwa wamekuwa kwenye mahusiano kwa miaka miwili sasa, na mbali na hapo walikuwa marafiki kabla, na mpenzi wake hakuwahi kuonesha dalili yoyote ya kupoteza uaminifu, lakini siku anayodai alikutana na mimi, alimuomba mpenzi wake waonane akamwambia kuwa kwa siku zote wamekuwa pamoja alidhani anampenda na alikuwa mwaminifu sana kwake, lakini siku hiyo alihisi amekutana na mwanaume wa maisha yake.





    Kijana huyo alinitafuta baada ya kuona amebembeleza sana kwa mpenzi wake warudiane lakini amegoma, na vile alivyoona ameachwa bila sababu. Ila pia alikuja kunambia kuwa anajua simpendi msichana wake, jambo ambalo linamsumbua sana Nirvana. Akaniomba nifanye namna yoyote akubali warudiane naye. Hapo ndipo nilielewa mapenzi ni kitu cha ajabu sana. Wakati akili, mawazo na mapenzi yangu yote yapo kwa mwanamke mmoja tu, Angel, kuna msichana mrembo alitamani niufungue moyo wangu kwake. Wakati yeye akilizwa kila siku na penzi hewa kwa kijana ambaye hana habari naye, kuna mwanaume mmoja alitamani arejeshewe nafasi ndani ya moyo wake. Yaani unayempenda hakupendi, na anayekupenda humpendi. Nikaona kuna sababu kubwa ya kumshukuru Mungu kwa ajili ya penzi letu na Angel linaloendelea kukua kila siku



    Maisha yangu nililelewa kwenye misingi ya dini, na daima nimekuwa nikimtanguliza Mungu katika mambo yote. Nchini Uingereza nilitafuta kanisa ambalo nitakuwa nikienda kila Jumapili. Ibada za kule ni fupi, masaa mawili tu, hivyo muda wa ibada daima haukuvuruga ratiba zangu nyingine. Kila Jumapili nilienda kanisani mapema sana, nilitumia masaa mengine ya siku hiyo kufanya usafi, kupumzika na kuongea na watu wa nyumbani Tanzania. Sikutaka kushughulika na kazi wala shule siku ya Jumapili japokuwa kuna wakati nilihitajika hospitali-chuoni, mara chache. Kanisa nililosali lilikuwa na watanzania wengi hivyo kwa kiasi ilinisaidia kupunguza upweke, hasa tulipoimba nyimbo za Kiswahili kanisani. Mara zote nilipoongea na Angel, pamoja na mambo mengi, tuliambiana mambo kadhaa kuhusu yale tuliyokuwa tukipitia.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Siku moja Jumapili, ikiwa ni mwaka na mwezi mmoja sasa tangu nifike nchini Uingereza, Angel alinipigia simu nikiwa kanisani. Haikuwa kawaida yake kabisa kunipigia simu muda wa kanisani kwani si tu kuwa alijua nakuwa kwenye ibada, ila pia mara nyingi na yeye unakuwa ni muda yuko kanisani. Nikastuka kidogo, lakini sikuipokea simu. Nikiwa ibadani mara zote hutoa sauti kwenye simu ili isinisumbue, lakini pia siizimi ili mtu akinitafuta baadaye nimpigie. Kabla hata ya kuondoka eneo la kanisani baada ya ibada, nilimpigia Angel. Siku hiyo sikusalimiana na mtu hata mmoja baada ya ibada. Akili yangu ilimuwaza tu Angel. Alipopokea simu hakikuwa kitu cha kawaida ule ukimya niliousikia. Niliita haloo kama mara tatu hivi, huku nasikia kabisa yuko hewani, lakini haongei. Nilipoita mara ya kwanza nilisema,’nambie mpenzi wangu’, hakujibu, kisha nikasema tena,’haloo’, hakujibu, mara ya tatu nikasema vipi Angel wangu? Pia hakujibu, nikakata simu tena, nikapiga muda huohuo, nikaita tena ‘haloo’, alipoitika ndipo niligundua alikuwa analia. Nafsi yangu ikastuka sana. Tangu baba yangu alipofariki, nimekuwa nikiumizwa sana na machozi, hasa ya mwanamke. Ile picha ya mama alivyokuwa akilia, pamoja na mdogo wangu Neema, siku ya msiba wa baba, haijawahi kuondoka akilini mwangu tangu wakati ule. Nadhani ni mambo ambayo yamewahi kuniumiza zaidi maishani mwangu kuliko kitu chochote.



    Nilisikiliza kwa shauku huku nikiuliza nini tatizo kujua Angel analia nini lakini mpaka simu inakata alikuwa hajanambia chochote zaidi ya kuendelea kulia. Alipokata simu sikusubiri hata sekunde nikapiga tena. Moyo wangu ulienda mbio mno, nikahisi pengine kuna msiba umetokea. Lakini nilipojaribu tena kupiga simu yake ilikuwa bize, kisha baada ya muda mfupi yeye akanipigia. Nilihamaki zaidi kusikia bado analia. Akanambia ‘Nathan, nakupenda’. Nilimuuliza kuna nini, mbona unanichanganya? Hakujibu kitu ila nilisikia kama mlio wa kofi/ kibao. Nikajiuliza maswali mengi mno ambayo sikuyapatia majibu. Hapo simu yake ilikata tena na haikupatikana tena siku hiyo nzima. Nikajaribu kumtafuta rafiki yake mmoja waliyekuwa wanafanya naye kazi, lakini hakuwa ameonana naye siku hiyo. Nikajaribu kumpigia dada yake mdogo ambaye kidogo tulizoeana, ili nijue endapo kuna tatizo lolote nyumbani. Ila nilipoongea naye alikuwa amechangamka na alikuwa nyumbani, hivyo hata sikumuuliza habari za Angel. Nikashukuru kuwa nyumbani kwao wote walikuwa salama.



    Jioni ya siku hiyo nilipigiwa simu kwa namba ya Tanzania nisiyoifahamu. Nilipoiona, nilijifariji kuwa atakuwa mpenzi wangu. Kiukweli siku hiyo nzima nilishinda kama mgonjwa, sikuweza kufanya usafi wala chochote. Niliondoka kwenda mjini kutembea tembea na kupoteza mawazo. Wakati simu inaingia nilikuwa ndiyo nimerudi tena nyumbani kama mtu asiye na matumaini hata kidogo. Kichwani mawazo mengi na maswali yaliendelea, lakini sikuwa na majibu juu ya nini kilikuwa kinamliza mpenzi wangu na amepatwa na nini haswa. Haikuwahi kutokea hata siku moja Angel kunipigia simu akilia, na pia haikuwahi kutokea kukosekana hewani kwa muda wote huo tena bila kunipa taarifa. Nilijua lazima kutakuwa na shida kwani hata kama angekuwa ameibiwa simu, lazima angenitafuta kwa namba nyingine. Katika siku zote nilizokuwa nimeishi nchini Uingereza, hii ilikuwa siku mbaya zaidi kwangu. Nilijihisi mpweke na mnyonge sana. Nikampigia mama yangu lakini sikutaka kuongea naye sana kwani lazima angejua nina tatizo. Nilikuwa tayari nimemwambia kuhusu Angel kama miezi miwili hivi baada ya kufika Uingereza. Sikutaka apate mawazo kuwa huenda nitaoa mzungu hivyo nilimwambia tayari kuna mwanamke wa kitanzania niko kwenye mahusiano naye na ninampenda sana, na mara nyingi pesa nilizomtumia mama nilituma kupitia kwake hivyo walifahamiana japo si kwa kuonana.

    Baada ya kupokea ile simu, nilisikia sauti ya mwanaume ikiuliza kwa kujiamini,”Wewe ndiyo Nathan?” Nikataka kusema ndiyo mimi, lakini akili nyingine ikanambia niseme hapana. Kwanza nikajifanya sijui Kiswahili hivyo akabadili lugha akaniuliza kwa kiingereza. Nilivyomjibu hapana akauliza tena kwa mshangao,” wewe si Nathan Ndazi?” nikamjibu tena, siyo mimi kwani vipi? Ilikuwa ni kama mtu aliyekuwa na maneno ya kusema na alitaka tu kuthibitisha kuwa anaongea na mtu sahihi, ila pamoja na kunitaja jina langu kamili nilimkatalia kuwa si mimi. Hakusema chochote, alikata simu. Nadhani alihisi kweli amekosea namba kwani sikumfanya ahisi kuwa anaongea na mswahili mwenzie. Nikazidi kuchanganyikiwa na kujiuliza maswali. Nikahisi labda alikuwa na taarifa juu ya Angel, nikaanza kujilaumu kwanini sikumwambia ukweli. Lakini nafsi yangu ikanambia kuwa nilifanya jambo sahihi.

    Usiku huo ukapita, sikulala kabisa. Mawazo yaliujaza moyo wangu, huzuni na wasiwasi, sikujua nini cha kufanya. Kila dakika nilimuwaza Angel. Usiku ukawa mrefu mno, nikasubiri asubuhi ifike nimtafute kwa rafiki yake wanayefanya naye kazi. Nikatuma jumbe kadhaa huku kila mara nikijaribu kama ningempata kwa simu, bila mafanikio. Ilipofika saa 12 asubuhi nikamtumia ujumbe rafiki yake kumuuliza kama Angel alifika kazini siku hiyo. Kwa majira ya saa za Tanzania, muda wa kazi ulikuwa tayari umefika. Ujumbe ukajibiwa haraka kuwa hajafika na hampati kwenye simu. Wasiwasi ukanizidi, nikatamani nimwambie aende kwake. Baada ya muda nikampigia, nashukuru kabla sijamwambia yeye mwenyewe alisema kuwa ikifika lunch time bado hapatikani atamfata nyumbani. Nikamshukuru sana, sasa nikawa nasubiria masaa yapite nijue nini kimetokea.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Wakati huo ilikuwa ni kipindi cha likizo hivyo ratiba zangu zilikuwa ni kufanya kazi tu. Siku hiyo nilifika kazini mapema zaidi kwani usiku sikupata usingizi hivyo ilibidi mapema tu nijiande niende kazini. Nilihisi nikibadili mazingira ingenipa unafuu kidogo. Nashukuru kuwa kazi zangu zilikuwa zinaniweka bize kiasi cha kutonipa muda wa kuwaza sana. Nikafanya kazi mpaka muda wa mchana, nilipopokea simu kutoka kwa rafiki yake Angel, akanambia amefika kwa Angel. Amemkuta hayuko kwenye hali nzuri sana ila akanipa niongee naye



    “Angel, una nini mama? Unataka kuniua? Niambie nini kimetokea?” Nilihisi kama kuchelewa nikisubiri aanze kujieleza. Nilijiona kama nina mwezi mzima sijasikia habari za huyu binti. Nilichohitaji kujua kwa wakati huo ni nini kilitokea. “Nathan, kuna kitu kikubwa kimetokea. Tunahitaji kuongea nikuelezee lakini saivi sina nguvu. Nashukuru Rehema yuko hapa atanisaidia kisha badae kidogo tunaweza kuongea.” Aliongea mpenzi wangu kwa sauti dhaifu sana na ya unyonge pia. Nikampa pole, nikamwambia nampenda sana, nikajaribu kumtia moyo japo sikujua yaliyomsibu. Nikamkumbusha kuwa penzi lake kwangu ndilo linanipa nguvu ya kila ninachokifanya. Nikamwambia kuwa naweza nikawa mbali kijiografia, lakini niko karibu yake kuliko mtu yeyote. Namuwaza muda wote, nampenda kuliko mtu yeyote, na siko tayari kumpoteza kwa gharama yoyote. Nilimuomba niongee na Rehema tena kwanza, nikamuomba Rehema akamtafutie glucose na kinywaji kingine kinaitwa Lucozade kwa ajili ya nguvu ampe, pia ampikie uji wenye maziwa ya kutosha, auweke na glucose amlazimishe anywe, akiona bado yuko dhaifu ampeleke hospitali. Nikamuomba asimlazimishe sana kusema nini kimetokea kama hatokuwa tayari. Tulipomalizana na Rehema nikaongea tena na Angel, nilichotaka kumwambia ni vile tu ninavyompenda sana. Kumkosa kwa siku moja kulinifanya nigundue kiasi gani nampenda kupita kawaida. Nilijiona kuwa maisha yangu hayana tena maana bila kuwa na huyu binti maishani.

    Licha ya penzi kubwa lililokuwepo kati yetu, tayari tulikuwa na mipango na malengo makubwa maishani. Mimi na Angel tulifungua akaunti ya pamoja ya malengo, na kila mmoja wetu aliweka kiasi kadhaa cha pesa kila mwezi. Wakati huo Angel alikuwa ameanza kufatilia chuo cha kuchukua shahada ya tatu nchini Uingereza ili baada ya muda mfupi na yeye aje. Tulipanga kujenga Tanzania kwani hata kama tungeishi Uingereza kwa miaka kadhaa bado tusingependa yawe makazi yetu ya kudumu. Sikuona mwanamke mwingine anayeweza kunifanya nijisikie vizuri kama Angel wangu, na siku hiyo niliwaza sana nini kitakuwa kimemtokea, lakini nikawa mvumilivu, nikampa muda, na kwa vile nilijua sasa hana simu nilimuomba rafiki yake amtafutie simu hata ya kuazima kwa muda kabla hajaondoka ikiwa atalazimika kumuacha peke yake. Rehema alipiga simu kazini, akaomba ruhusa, akawambia amemkuta Angel anaumwa na yuko pekeake hivyo itambidi kukaa naye kwa muda amhudumie.



    Niliporudi nyumbani jioni hiyo nilikuwa nikiwaza na kujiuliza nini kilimtokea Angel, lakini walau nilikuwa na amani kuwa nimempata kwenye simu. Hiyo ilinitosha kunirudishia utulivu wa nafsi, nikajitahidi nisimlazimishe kusema mpaka atakapo kuwa tayari. Nikampigia baada ya muda mfupi, kumuuliza hali yake. Nikashukuru anaendelea vizuri na kidogo amepata nguvu. Nikamshukuru sana Rehema kwa kumuhudumia na kuwa karibu naye wakati alipohitaji rafiki na mtu wa kumjali. Mida ya saa nne usiku tena nikapiga simu ili nimuage apumzike mapema, lakini nilipoanza kuongea naye alikuwa kidogo amechangamka na yeye mwenyewe akaanza kunieleza kisa kilichomtokea Jumapili. Akaanza kwanza kwa kuniuliza kama kuna namba ilinipigia ya Tanzania ambayo siijui, nikamwambia ndiyo lakini aliniuliza kama mimi ni Nathan Ndazi nikamwambia si mimi na nikajifanya sijui Kiswahili. Akasema afadhali sikumjulisha kama ni mimi.



    “Siku ya Jumapili niliamka asubuhi nikajiandaa kwenda kanisani, nilitaka kwenda mjini siku hiyo ibada ya kwanza hivyo niliondoka mapema kidogo. Jana yake usiku Damian alinipigia kama mara nne nikawa sijapokea, akatuma ujumbe kunambia nipokee simu ni muhimu sana, nikapokea. Akaongea na mimi kwa upole sana akiniambia ananipenda sana na anahitaji kuwa na mimi. Akasema nikimpa sharti lolote atalifuata lakini ni lazima awe nami tena, na kuwa amegundua hawezi kuishi bila mimi. Nilimsikiliza kisha nikamjibu kuwa nilisha fanya uamuzi wa kuachana naye na siwezi tena kurudiana naye. Aliendelea kunibembeleza mpaka nikamkatia simu. Akapiga tena sikupokea, nikazima simu nilalala. Asubuhi nilipokuwa nikitoka kwenda kanisani, kama unavyojua hapa kwangu mpaka ninapopaki ni mwendo kama wa dakika tatu hivi, nikakutana na kijana mmoja akanisalimia. Nilipomjibu akanisogelea, na kwa bahati mbaya hakukuwa na mtu yeyote karibu. Nikastuka kidogo, nikaangalia nyuma maana nilihisi si mtu mzuri. Nikajaribu kumpuuza na kuendelea kutembea lakini akanizuia kuendelea mbele, kumbe pembeni kulikuwa na gari ambalo sikuwa nimeliona mwanzo, gari nyeusi yenye vioo vyeusi pia yaani tinted. Nilivyoliona nikazidi kustuka, nikataka kupiga kelele, yule kijana akanisogelea n kuniziba mdomo na nikiwa bado nashangaa akaniwekea kitambaa puani na hapo sikujua nini kiliendelea” Alinielezea Angel kama mtu anayehadithia muvi Fulani aliyoiona. Sikuamini ninachokisikia, na nilikuwa na shauku kubwa ya kutaka kusikia mwisho wa hilo tukio. Akavuta pumzi kisha akaendelea

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nilikuja kustuka niko kwenye chumba kibaya tu mahala nisipopajua. Kulikuwa na wakaka wawili walioonekana hawana huruma. Nilianza kulia na kuwauliza niko wapi na wanataka nini wakawa tu wakinigombeza na kunambia ninyamaze. Mmoja alinambia kuwa wanachotaka ni kumjua mwanaume anayenipa jeuri mjini hapa, niwaoneshe wamshughulikie na kisha hawatakuwa na habari na mimi. Ndipo nikaelewa ni Damian yuko nyuma ya huu mchezo. Nikashikwa na hasira sana, nikawaambia najua Damian amewatuma lakini nakuhakikishia, atajutia. Wakachukua simu yangu, wakanilazimisha niwaoneshe namba ya mpenzi wangu, nikakataa hata kuifungua. Wakanipiga makofi kadhaa na kunilazimisha niifungue, nikaifungua, wakachunguza kidogo wakaona namba yako, wakaipigia hukupokea. Baadaye ulipopiga wakanipa niongee na wewe, nikwambie kuwa huu ndiyo mwisho wetu, siwezi tena kuendelea na wewe. Pale nilikwambia nakupenda, walikuwa wanataka nikwambie tunaachana na walinipangia maneno kadhaa kukwambia, nilipokwambia nakupenda wakanipiga kofi la nguvu. Baadaye wakachukua simu yangu na kuizima, akamwambia mwenzake, mtumie hiyo namba bosi. Akaanza kunambia maneno ya kunitisha kuhusu kitu wanachoweza kukufanyia. Akasema hata kama uko mbali, watakupata kwa simu na kufanya chochote wanachoweza kufanya. Baadaye nililetewa simu niongee, alikuwa amepiga Damian, akaanza kunambia kuwa ananipenda sana na hangependa kuniumiza kwa namna yoyote, ila ninapokataa kuwa naye, atatumia nguvu kunilazimisha tuwe sote. Alisema hakuna polisi wala mtu yeyote anayeweza kumzuia au kumkamata, kwani anafahamiana na wenye nchi na mkono wake una nguvu. Alisema maadamu amepata namba ya huyo anayenipagawisha, atahakikisha anashughulika naye na kama nisipokubali mimi mwenyewe kukuacha basi nitakuwa ninakuweka kwenye matatizo” Angel aaliendelea kuzungumza huku nasikiliza mwili wote ukinisisimka. Nilikuwa na hasira kali mno wakati huo, nilitamani kupaa kuamkia Tanzania dakika iyohiyo, tena Arusha kwa Damian



    “Nathan, siku ya jana ilikuwa mbaya mno kwangu. Damian ameniahidi kuwa hii ni tlera tuu, lakini picha yenyewe itaanza hivi karibuni. Amesema yuko tayari kusafiri kukufata popote ulipo akumalize maana umemuibia mke wake. Amesema atajitahidi asinifanyie hivi tena maana hataki kuniumiza, ananipenda, lakini wewe atahakikisha ameyamaliza maisha yako. Wale vijana walinipiga japo si sana, na pia siku nzima sikuweza kula chochote zaidi ya maji. Walileta chakula nikakataa. Muda wote nilikuwa nikilia sana yani, hata sikuwa najua nini cha kuwaza. Pia nilihofia sana kuwa huenda hata wangenibaka lakini namshukuru Mungu hakuna aliyefanya hivyo. Walinirudisha nyumbani mida ya saa tatu asubuhi nikiwa nimefungwa kitambaa usoni, mpaka nafika ndo nafunguliwa ili niingie ndani kwangu. Sikulala usiku kucha nawaza nafanya nini na huyu shetani Damian. Yani sijawahi kumchukia mwanaume kiasi hiki. Simpendi hata kidogo, najuta hata kwanini niliwahi kuwa na mahusiano na mtu katili na mshenzi namna hii”



    Alimaliza kunihadithia Angel huku akiwa na jazba sana. Nikamtuliza, nikampa pole za kutosha na kuhakikisha hasira zimeshuka.

    Tulipomaliza kuongea nilikaa nawaza itakuaje. Niliwaza huyu mwanaume anapanga kufanya nini, na atatufatilia kwa muda gani. Kwakuwa jana yake pia sikulala kabisa, na siku hiyo sikupata hata nafasi ya kupumzika, ilipofika mida ya saa sita nilipitiwa usingizi. Asubuhi sana, au wanasema alfajiri, majira ya saa 10, usingizi ulikata licha ya kuwa nililala saa sita usiku. Nilikaa kitandani nikiwaza itakuaje, na nilijikuta nikitumia muda mwingi sana kuwaza kiasi kwamba japo ilikuwa msimu wa ‘winta’ ambao jua huchelewa sana kuchomoza kwa nchi za ughaibuni, jua ndilo lilinifanya nijue nimechelewa kazini.

    Niligundua kuwa siku hiyo tayari nilipoteza masaa kadhaa ya kazi yangu. Niliamka haraka na kuanza kujiandaa. Haikunichukua nusu saa kabla sijamaliza kujiandaa na haraka sana nilielekea kituo cha usafiri (treni), kusubiri ili niende kazini.

    Ghafula, nikiwa natembea, huku akili inashindwa kujizuia kuwaza na kutafakari juu ya kile kilichotokea kwa mpenzi wangu, nilikutana na yule niliyekuwa nikimtafuta kwa muda wa zaidi ya mwaka sasa. Sikuamini macho yangu kumuona rafiki yangu Mawazo. Inaonekana alikuwa anatoka supermarket (supamaketi). Hakuonekana kama mawazo niliyemfahamu. Nilimtazama kwa muda na kumuita lile jina la kijijini kwetu tulilolizoea ‘Luzoki’



    Ni dhahiri na mimi nilikuwa nimebadilika kidogo hivyo sikushangazwa na yeye kutonikumbuka kwa haraka. Ila niliona mshangao machoni na akilini mwake kusikia jina la kijijini Tanzania katikati ya wazungu. Ilimpa tabu kidogo; nguo nyingi za baridi nilizovaa, ikiwemo kofia; pamoja na hali ya hewa ya Ughaibuni, vilinifanya nibadilike. Sikuwa Nathani yule wa miaka nane iliyopita tulipomuaga Mawazo. Tuliposogeleana, alishangaa sana sana. Hakutegemea kuwa tunakutana kwa mara nyingine. Aliponifahamu, alinikumbatia huku machozi yakimtoka. Nilielewa sasa kuwa japo hali ya hewa, marafiki, na hali ya uchumi aliyonayo sasa ni tofauti kabisa, ukiachilia mbali mwonekano ambao pia umebadilika, bado moyo wa huruma na upendo wa Mawazo haukuweza kubadilishwa na hayo yote. Macho yake yalifanya nimuone Mawazo yule niliyekuwa tayari hata kugombana na wazazi wangu kwa ajili yake

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nilijiona kama naota, nikaamini kwa hakika milima haikutani lakini si binadamu. Nikamshukuru Mungu ametupa tena nafasi ya kukutana, tukiwa watu wazima. Kwa kuwa nilikuwa na haraka kuwahi kazini, na yeye pia sikujua ratiba yake ilikuaje, tulibadilishana namba za simu na anuani za mahali tunapoishi. Mkononi nilimuona na pete ya ndoa, nikajua tayari alishaoa. Nikampongea, akasema siku nyingi sasa, tayari nina watoto wawili. Nikamuuliza kama ni mzungu au mwafrika, akasema ni Mtanzania lakini mama yake mzungu na amezaliwa Uingereza. Tulipoagana, kidogo mawazo niliyokuwa nayo yalikuwa yamepungua au naweza sema yamepumzishwa na habari ya Luzoki. Kwa dakika kadhaa, furaha niliyokuwa nayo ilinifanya nisitishe kuwaza juu ya Angel. Nikajikuta nikiwaza maisha ya kijijini kwetu hasa wakati nasoma shule ya msingi. Nikakumbuka jinsi ambavyo tulipanga mipango pamoja, na sasa maisha yametupa nafasi ya kukutana tena huku kila mmoja akiishi ndoto ya maisha yake.



    Kwa jinsi Mawazo alivyoonekana, nilijua ametoka kwenye ndege iliyowasili muda si mrefu. Na kwajinsi alivyokuwa amevaa, nilijua alikuwa rubani wa ndege hiyo. Hiyo ilikuwa ni furaha yangu kubwa mno. Nikamuuliza tu, ni ndege gani? Akajibu shirika la KLM. hatimaye kijana wa kitanzania, mnyenyekevu, mpole na mwenye upendo wa kweli, aliyekulia maisha ya kijijini, aliyepata nafasi ya kusomeshwa kwa akili na jitihada zake, sasa alikuwa rubani wa watu weupe na wenye pesa nyingi. Nikaamini kwa hakika hakuna jitihada inayoanguka chini, hasa Mungu akinyoosha mkono wake.



    Tulipoachana na Luzoki, nilielekea kwenye usafiri na kwenda kazidi. Nikampigia Angel wangu kumjulia hali na kumpa habari hiyo njema. Siku hiyo sikutaka kumpigia mapema kwani nilihisi angekuwa bado amelala. Nilipiga kwa simu ya rafiki yake ambaye alikuwa bado hajatoka nyumbani kwa Angel. Alifurahi sana pia kusikia nimempata Luzoki kwani siku zote alijua nilivyokuwa natafuta sana kuonana naye tena, na japokuwa hakumjua kwa sura, ila alijua sifa zake kwa undani sana kulingana na stori nilizompa hapo nyuma. Ninashukuru hali ya Angel ilikuwa imeimarika zaidi asubuhi hiyo na baadaye mchana hata uchangamfu wake ulikuwa umerudi. Ilibidi akatafute simu nyingine na pia alisajili namba nyingine kabisa kwani hakutaka tena kuwa na ile namba ya awali. Nilihisi na mimi nahitaji kufanya hivyo ili hata kama Damian atajaribu kunitafuta tena kwa namba yangu, asinipate. Hivyo baada ya siku mbili name pia nilikuwa nimebadili namba ya simu.



    Niliwaza mbali zaidi na kumuomba Angel aanze kutafuta nyumba nyingine ya kuishi, lakini pia afanye mpango haraka kazini wamruhusu aje kusoma Uingereza. Tayari alikuwa ameshaanza kuomba lakini safari hii bosi wake alikuwa mgumu kidogo. Alitakiwa kwenda kusomea stashahada ya juu ya uchumi yaani PhD, ili awe daktari wa mambo ya uchumi, lakini masomo hayo yangemchukua miaka mitatu hadi minne, suala ambalo liliwapa hofu ofisini kumkosa muda mrefu. Lakini akiwa bado anafuatilia, aliongea na bosi wake mwingine ambaye alikuwa mkurugenzi msaidizi kwa Tanzania, alikuwa ni mama mtu mzima na walikuwa wanaelewana kwa kiasi kikubwa. Ilibidi aongee naye kwa undani kidogo kuhusu kwanini anahisi anahitaji sana safari ya masomo nje ya nchi. Alimueleza kuhusu Damian na kitendo alichokifanya, wakati huo ni wiki kadhaa zimepita. Yule mama alishangaa sana, akamuuliza kwanini hakumshitaki, lakini kwa jinsi Damian alivyokuwa na uwezo wa kifedha, na jinsi alivyokuwa mjanja, hata Angel angeamua kumshitaki, ushahidi usingepatokana na hiyo kesi angeikwepa.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Yule mama alimshauri Angel aongee na mkugenzi tena ampe wazo la kuwaandikia ofisi ya shirika lao iliyopo Uingereza, ili wamruhusu ahamie huko kikazi na hiyo ndiyo itakuwa nafasi nzuri kusoma akiwa bado yuko kazini. Hili lilikua wazo zuri sana kwetu, na nilihisi sasa urahisi umepatikana. Kwa mkurugenzi mkuu pia halikuwa wazo baya, na yeye mwenyewe aliandika barua kwa ofisi za Uingereza kuomba wamkubali na pia kumruhusu asome akiwa anafanya kazi.





    Ndani ya miezi minne kila kitu kilikuwa kimekamilika. Angel alimwambia mama yake kila kitu lakini hakutaka dada yake waliyefatana ajue hivyo ilimbidi kuwaficha baadhi ya ndugu zake mpaka majuma kadhaa kabla ya kuondoka. Kwa kipindi chote hicho Damian alikuwa amemtafuta kwa njia mbalimbali bila mafanikio, kwani alikuwa na simu ambayo aliitoa kwa watu wa ofisini tu, na hao aliwaomba wasimpe mtu namba yake. Ile namba nyingine ilikuwa ni kwa ajili yangu na familia tu na alimuonya dada yake kuwa endapo Damian angepata hiyo namba basi ugomvi wao usingesuluhishwa. Watu wachache aliowapa namba zake mpya walikuwa ni wale aliowaamini na ni wa muhimu tu. Ofisini pia aliwajulisha kuwa wameachana na Damian na hivyo hana haki ya kwenda kumtafuta tena. Baadhi yao aliwambia ukweli juu ya kile alichofanya hivyo kumfanya asikubalike tena pale ofisini.



    Kabla safari ya Angel haijawadia, nilihakikisha wanakutana na mama. Kwa kuwa mimi mwenyewe sikuwepo, kuna kipindi mama alikwenda Dar kama kumsalimia yule shangazi yangu, nikahakikisha wamepanga kukutana. Mimi ndiye niliyeipangahiyo safari ya mama ya kwenda kwa shangazi, ili akifika, wawasiliane na Angel waonane. Mama yangu hana makuu, na kwake yeye mwanamke yeyote ambaye ningempelekea, angemkubali kwa moyo mmoja, lakini kwa Angel si tu kuwa alimkubali kwa kuwa ni chaguo langu, bali pia alimpenda sana. Angel alikuwa mwenye moyo wa huruma sana na mkarimu, na hilo kila mtu aliyewahi kuwa karibu naye alilijua. Siku walipoonana na mama, alimpa zawadi nyingi lakini siku mama alipomwambia anataka kuondoka, alimuomba tena waonane naye na kumpa zawadi kibao kwajili yake na Neema na wadogo zangu wengine. Mama alijaribu kukataa kwani ni mtu mwenye aibu kwa asili na hakutaka kumlemea mtoto wa watu, lakini Angel alimdanganya kuwa hizo zawadi ameagizwa na mimi ampe. Tulipoongea na mama akinishikuru ndipo nikamwambia ukweli kuwa ni Angel mwenyewe wala hata mimi sina taarifa kama alimpa zawadi zote hizo.



    Pia kwa kuwa alikuwa amekaribia kuondoka, alifanya kitu ambacho hata mimi kilinishangaza sana. Angel alipakia vitu karibu vyote vya ndani kwake kwenye gari ya mizigo aliyokodi, na kumtumia mama kijijini. Haya yote Angel hakuwa ananambia, yaani taarifa nilipata kwa mama. Nikaelewa kuwa binti huyu hakuwa anafanya hivi kunifurahisha, bali kwa moyo wake wa ukarimu. Nikakumbuka mara ya kwanza namfahamu akiwa anatembelea wagonjwa hospitali, mmoja mmoja, tena asiowafahamu, na kumfanya kila mmoja ajihisi ni maalumu sana. Kusema kweli nilijiona ni mwanaume mwenye bahati mno kwenye hii dunia, nikaiambia nafsi yangu, hata ikinilazimu kupambana na Damian hata kufa kwa ajili ya Angel, sitaweza kumuacha kwa gharama yoyote. Hakukuwa na mwanamke yeyote aliyewahi kunifanya nijisikie mwenye thamani kama huyu binti. Ukiacha mama yangu, ambaye siku zote amekuwa na nafasi ya pekee na maalumu kwenye maisha yangu, Angel alinifanya nione ninamiliki kila kitu duniani. Leo hii ninaandika hadithi hii ya maisha yangu, nina hakika huyu malaika, japokuwa amekuja kwenye maisha yangu nikiwa tayari mtu mzima, lakini ni sehemu kubwa mno ya mafanikio yangu.



    Kuonana kwangu na Mawazo ilikuwa kati ya vitu vilivyoyapa faraja sana maisha yangu ya Uingereza. Nilimpigia simu siku hiyo hiyo niliporudi kutoka kazini jioni. Baada ya kuongea kwa muda mrefu, tulikubaliana kuwa siku ya Jumapili nitakwenda kwake, hasa niione familia yake. Japokuwa kazi yake ilimfanya asiwepo nyumbani kwake muda mwingi lakini kwa bahati wiki hiyo alikuwepo. Jumapili ilipofika nilikwenda kanisani na kwenda moja kwa moja nyumbani kwake baada ya ibada. Hapakuwa karibu sana na nilipokuwa naishi, ilikuwa ni kama mwendo wa saa nzima kwa usafiri wa treni. Nilikuwa na wakati mzuri mno na rafiki yangu siku hiyo kiasi kwamba muda haukututosha. Nilifurahi kumuona mke wake ambaye alishaambiwa habari zangu siku nyingi kabla ya kuniona. Nilifurahi kuwaona pia watoto wake wake, mabinti wawili warembo sana. Nikamuuliza kuhusu wazazi akasema hata kwenye harusi yake walikuja, aliwatumia mualiko. Hatimaye zile ndoto tulizoota tukiwa vijana wadogo wa shule ya msingi zilikuwa zinatimia. Siku hiyo tulikumbushana na kuhadithiana mambo mengi mno. Kwa hakika urafiki wangu na Mawazo ulikuwa zaidi ya ndugu. Niliondoka usiku sana kurudi nyumbani kwangu lakini huo ulikuwa ni mwanzo wa mawasiliano tena na Luzoki, na ulikuwa pia urejesho wa urafiki wetu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hatimaye siku iliwadia, Angel alikamilisha mipango yote na kuja Uingereza. Ofisi yao na chuo alichopata vyote vilikuwa mbali na Liverpool, lakini kitendo cha kuwa nchi moja nami, tena mbali na Damian, ilikuwa ni habari njema mno kwangu. Tulikuwa tunaanza maisha mapya, na sasa hakukuwa na wa kusimama kati yetu. Kwetu Uingereza ilikuwa ni nchi salama na amani ilikuwa kubwa. Mwendo wa nusu saa au dakika 45 hivi kwa treni kwangu ilikuwa ni kama dakika tano, na haikunizuia karibu kila siku kuonana na Angel. Furaha yangu ilikuwa ni kuuona uso wa malaika wangu tu, kuwa karibu naye, kumuhakikishia nampenda na kupanga naye mipango



    MIAKA MITANO ILIYOFUATA:

    Tukiwa Uingereza, tulianza kufanya mipango ya mahari na ndoa kwa familia ya kina Angel, na kwa msaada wa shangazi na mjomba wangu wa vingunguti, mama na baba yangu mdogo, tulifanikisha, mahari ikalipwa na sasa ilibaki harusi. Wakati huo Damian aliendelea kumsumbua dada yake Angel lakini wazazi na ndugu wengine wa Angel walikuwa wamemuonya asimpatie mawasiliano hasa baada ya Angel kuwahadithia juu ya kutekwa kwake. Wazazi na ndugu wa Angel walikuwa na uwezo kiuchumi hivyo wakati tunapanga sherehe za harusi walikuwa tayari kuja Uingereza kwa gharama zao. Tulifanya mpango mama na wadogo zangu wawili, akiwemo Neema, pamoja na mdogo wa Angel wa mwisho wahudhurie kwenye harusi yetu kwa gharama zetu. Wakati huo tulikuwa na kiasi cha fedha za kutosha, kwa nchi za ughaibuni hakuna kuchangisha watu kwa ajili ya harusi lakini pia sherehe hufanyika za kiwango cha kawaida. Mimi na Angel tulijipanga kwa yote yaliyokuwa mbele yetu pamoja hivyo mzigo haukuwa mkubwa na kila kitu kilienda sawa.



    Hatimaye siku ilifika, katika kanisa moja kubwa la Lutheran nililokuwa ninasali nchini Uingereza, tulifungishwa ndoa na mchungaji Leonard Stanley. Rafiki yangu Mawazo na mke wake Yvonne walikuwa ndio wasimamizi wetu. Hakukuwa na siku kubwa, maalumu, na ya furaha maishani mwangu kuwahi kutokea kiasi hiki. Hakukuwa na kitu zaidi nilichokuwa nahitaji kwenye maisha kama kuwa na mpenzi wangu milele. Binti huyu alinitunzia heshima, alinipenda kama nilivyo, aliutoa moyo wake kwangu, aliipenda familia yangu, alinithamini kuliko mali nyingi na alikuwa na moyo wa kipekee hata kwa watu wengine. Zawadi pekee ambayo ningempa ni kuwa mwaminifu kwake siku zote za maisha yangu, na hicho ndicho nilichomuahidi. Daima malaika wangu atabaki kuwa malkia pekee wa maisha yangu, na kama kuna njia nzuri zaidi ya kumuonesha nampenda basi daima nitaifuata.



    Mungu alitujalia mtoto wa kwanza wa kiume mwaka mmoja na miezi nane baada ya ndoa yetu. Tukampa jina la Jothan, linalomaanisha Mungu ni mkamilifu. Hii ilikuwa zawadi kubwa ya matunda ya penzi letu. Pia ilikuwa ishara kubwa kwamba Mungu ndiye aliyekamilisha mipango, ndoto na maono ya kila mmoja wetu, kabla hatujakutana na baada ya kuwa wapenzi mpaka sasa tuko kwenye ndoa.



    Kipindi mke wangu anajifungua, tulimuomba mama aje amuhudumie, na ilikuwa ni furaha kubwa mno kwake kuitwa bibi kwa mara ya kwanza. Mama na Angel wamekuwa marafiki wakubwa kiasi kwamba hata mimi kuna wakati naona wivu. Jotham amekuwa furaha kubwa mno kwenye maisha yetu na nauona moyo wa upendo ndani yake kama mama yake.

    Kipindi fulani nilimtafuta na kufanikiwa kumpata yule daktari niliyepewa namba yake na rafiki yangu niliyesafiri naye wakati naenda masomoni, na kweli alikuwa ndiye dokta Nathan aliyemzalisha mama yangu mimba yangu. Baada ya kujieleza kwa kina, alikumbuka kila kitu na akafurahi mno. Kwa bahati kubwa kipindi nafunga ndoa alikuwa amekuja Uingereza na alifurahi sana kuhudhuria ndoa yangu, nikamkutanisha na mama yangu. Hii ilikamilisha furaha yangu kuu ya siku ya harusi.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kuna mengi mno ningependa kuelezea ikiwa ni pamoja na mafanikio ya kiuchumii ya mama na wadogo zangu ambayo tuliyafikia nchini Tanzania, lakini natumai hadithi hii ndefu ya maisha yangu imekufundisha, imekuelimisha na kukupa MWANGAZA wa maisha, hasa katika changamoto mbalimbali unazopitia. Natumai pia itakusaidia kujua kutilia mkazo mambo ya muhimu, na kutoa nafasi sahihi kwa watu wa muhimu katika maisha. Kama ni kijana bado, naamini umejifunza jinsi ambavyo jitihada sahihi huleta mafanikio hata kama kuna vipingamizi. Zaidi ya yote, natumai kwa nafasi na imani uliyonayo, siku zote utampa Mungu nafasi inayostahili kwenye maisha yako.



    **MWISHO

0 comments:

Post a Comment

Blog