IMEANDIKWA NA : INNOCENT A. NDAYANSE (ZAGALLO)
*********************************************************************************
Simulizi : Kwa Udi Na Uvumba
Sehemu Ya Kwanza (1)
MTU MMOJA ALIWAHI KUSEMA KUWA PESA NI ZAIDI YA KILA KITU MAISHANI. UKIWA NA PESA HAKUNA LITAKALOSHINDIKANA. NI PESA HIZO ZINAZOWEZA KUZUA UHUSIANO MZURI KWA WATU KAMA AMBAVYO PIA ZINAVYOWEZA KUSABABISHA MAAFA YASIYOTARAJIWA. PESA NI SABUNI YA ROHO, NA PIA PESA HUWEZA KUWA CHACHU YA MATATIZO.
KATIKA RIWAYA HII YA AINA YAKE, PESA ZIMEDHIHIRISHA JINSI ZINAVYOWEZA KUWA CHANZO CHA FURAHA MAISHANI AU KERO NA MTAFURUKU KATIKA JAMII. NI KIPI KILICHOJIRI? FUATILIA MKASA HUU MZITO WENYE MCHANGANYIKO WA MAPENZI, VISASI NA MAUAJI YA KIKATILI…
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
*****
NI usiku wa manane. Saa saba! Kwa wapenzi hawa wawili, bado ilikuwa mapema sana. Walikuwa hawajaambua hata lepe la usingizi. Na zaidi, ni Hilda aliyekuwa akitaabika kwa kukikosa kile alichokihitaji, kile ambacho huukonga moyo wake kwa namna inayosisimua na kufariji.
Tayari alikwishaitumia mikono kugusa hapa na pale, kutomasa na kupapasa huku na kule lakini haikusaidia. Akayatumia matiti yake makubwa yenye joto la uhai, haikusaidia. Alitumia hata ulimi wake kitaalamu na kwa mbwembwe nyingi; lakini bado ni kama alikuwa akipoteza muda!
“Una nini leo?” Hilda alitokwa na swali hilo huku akiuondoa kwa taabu mkono wake ambao kwa dakika mbili, tatu ulikuwa mahala fulani mwilini mwa Panja, ukiendelea kujaribu kuyashtua mashetani.
“Kwani vipi?”
“Hii siyo kawaida yako.”
Ni kweli, hiyo haikuwa kawaida ya Panja kila arudipo jioni kutoka katika safari zake ambazo Hilda hakuzijua. Alishajenga mazoea ya kila aliporejea huvuta bangi na kunywa pombe kali kidogo. Kinachofuata baada ya hapo ni ile adhabu yenye kusisimua maungoni mwa Hilda, wakitumia muda mwingi wa usiku huo kufanya hicho walichozoea kukifanya.
Lakini usiku huu Panja alikuwa mwingine. Alionekana kutingwa na mawazo mengi kichwani, mawazo yaliyosababishwa na mkasa uliomkuta katika safari yake aliyorejea mchana uliopita.
***********
GEREZA la Segerea lilipompokea Panja na kumpa hifadhi ya miaka miwili kwa kosa la wizi wa kuaminiwa, alipata mafunzo mengi ambayo hakuyatarajia. Kati ya mafunzo hayo ni machache tu aliyoyapenda. Alitoka huko akiwa ameshajua kuvuta bangi. Zaidi ya hayo, marafiki zake aliokumbana nao huko walimpa mbinu mbalimbali za kupata fedha kwa njia za haraka na fupi.
“Wenzio tumeingia humu kwa sababu za maana,” Makata, mmoja wa wafungwa wakongwe alimwambia. “Tulikuwa wanne, tukamvaa bwege mmoja wa Kihindi, tukamlisha za kichwani na kutoka na milioni ishirini. Tatizo, mnoko mmoja aliwatonya ‘wazee,’ tukataitiwa kabla hata hatujakatiana mshiko.”
Mwingine alimwambia kuwa atakapotoka kifungoni atakuta milioni zake tatu katika akaunti yake, benki. Yeye alidai kuwa alihukumiwa miaka mitano jela baada ya kutuhumiwa kuvamia nyumba ya jirani na pale alipoishi, tuhuma alizokiri kuwa ni za kweli.
Kipanga, mfungwa aliyekuwa amebakiza wiki moja tu za kutumikia kifungo, yeye, japo aliwasikia wenzake wakitamba, hata hivyo hakutamka chochote bali baadaye alimwita Panja faragha na kumuuliza, “Hivi wewe umebakiza miezi mingapi?”
“Siyo miezi, ni siku kumi na tano tu.”
“Wiki mbili tu!” Kipanga alimtazama kwa mshangao. “Kumbe siku zimekwisha! Nilidhani bado una siku nyingi, kumbe…”
Ukimya wa sekunde kadhaa ukatawala. Kisha Kipanga akaendelea, “Kumbe hatupishani sana. Mie bado siku saba tu. Nitakutangulia wiki moja.”
Panja hakumwelewa. Kwa sauti yenye kijimkwaruzo cha mbali, alimuuliza, “Kwa hiyo nd’o nini?”
Kipanga alicheka kidogo, kisha akasema, “Kuna jambo unalopaswa kulijua msh’kaji wangu. Kwamba, umesota humu kwa ‘mvua mbili’ kwa kosa la kipuuzi. Utafanya nini utakaporudi uraiani?”
“Hilo nitalijulia hukohuko,” Panja alijibu. “Kama maisha ya Bongo yatanishinda, basi nitazamia majuu.”
Kwa mara nyingine Kipanga alicheka, safari hii kicheko chake kikionyesha kuyadharau maneno ya Panja. “Utazamia?” hatimaye alimuuliza. “Una akiba ya nguvu, benki?”
“Sina. Lakini n’tafaiti hukohuko uswazi.”
“Una hakika na unachokisema?”
“Sina. Mambo yote n’tayajulia hukohuko.”
“Siki’za, Panja,” Kipanga alisema kwa sauti ya chini. “Unaonekana uko fiti kishenzi. Umbo lako linafaa kutumika katika kukunufaisha. Siku hizi maisha ni magumu. Ili ufanikiwe usitegemee kukesha kanisani au msikitini ukisali. No. Mwanaume unapaswa kuhangaika. Fanya kila liwezekanalo, na kulazimisha uwezekano kwa lile lisilowezekana ili ufanikiwe maishani. Tangu uzaliwe u’shawahi kupiga mtu roba?”
“Bado,” Panja alijibu kwa sauti ya chini huku akimkodolea macho Kipanga. Hakutarajia kuulizwa swali hilo.
“Wewe bado, mie tayari. Na siyo kupiga mtu roba tu, mwanangu. Mi’ ni’shazimisha mtu nne, kudadek! Na sikufanya hivyo kwa kujifurahisha tu. Hapana. Nilikuwa na sababu. Pesa. Nilitaka pesa, na nilizipata. Nikajenga. Najua nikitoka humu nitafikia nyumbani kwangu siyo kuhaha tena mjini.
"Kwa kweli huo ndio mfumo wangu wa maisha. Na nikitoka humu kazi yangu ni hiyohiyo. Lakini nahitaji kampani. Mtu kama wewe nd’o anayefaa kunipa kampani, mwanangu. Chimbo langu liko Kariakoo maeneo ya Jangwani, jirani na jengo la Yanga. Siku n’takayosepa n’takumwagia vizuri jinsi ya kunicheki.”
************
SIKU Panja alipotoka gerezani, fikra zake zote zilikuwa juu ya Kipanga. Hakuchukua zaidi ya nusu saa nyumbani, Kinondoni ‘A’ jirani na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri, Usharika wa Kinondoni kabla hajarudi kituoni ambako alipanda daladala lililompeleka Kariakoo kwa Kipanga. Na alimkuta.
“Ni siku njema sana,” Kipanga alisema. Ni muda mfupi tu uliopita alikuwa akivuta bangi huku akijihisi yu huru kuliko alivyokuwa akibahatika kuvuta kwa siri wakati alipokuwa gerezani.
Papohapo akamkabidhi Panja msokoto wa bangi kutoka kabatini. Panja hakuwa mvutaji mkongwe wa bangi, tabia hii aliianza wakati yuko kifungoni.
“Vuta upate akili, tuzungumze kiutu-uzima,” Kipanga alimwambia.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Dakika chache baadaye bangi ilizimwa. Wakatazamana.
“Vipi, una pesa?” Kipanga alirusha swali.
“Pesa!” Panja alimtazama kwa mshangao wa mbali. “Una maana gani?”
“N’na maana una pesa za kuitwa PESA? Au una vijisenti vya nauli ya daladala? Kama una kilo nne, tano hivi, naweza kusema ni pesa za kutambia hata kwa wanaume wenzako.”
Kilo nne, tano zilizotajwa na Kipanga ni usemi uliomaanisha shilingi laki tano. Panja alimwelewa na papohapo akamjibu, “Sina. Nina pesa kidogo sana.”
“Kiasi gani?”
“Ni aibu. Hazifiki hata alfu kumi.”
Kipanga aliguna kidogo kisha akamponda kwa kusema, “Kwa kifupi sema huna pesa. Alfu kumi hata ishirini si’o pesa za kutosha hata kwa kuhonga demu.”
Panja alikosa hoja, akaishia kutabasamu, tabasamu ambalo halikutoa taswira yoyote kama ni la furaha au huzuni.
Kipanga akaendelea, “Muda huu ni saa saba. Saba na robo. Najua una uchovu kidogo. Lakini we’ ni mwanamume, haupaswi kulemaa. Kuna kazi. Kazi ya pesa, na inabidi ifanyike leo. Uko tayari?”
“Hata sasa hivi, mwanangu.”
“Poa,” Kipanga alisema. Akaongeza. “Ni vizuri tusilaze kazi. Wewe una vijipesa kidogo, mie nina shombo ya sarafu. Lakini kwa sasa nenda nyumbani, kapumzike, urudi hapa saa mbili usiku. Unahitaji muda kidogo wa kupumzika kabla ya kupumzika kwa starehe huku kitu kama milioni tatu au nne hivi zikiwa kibindoni.”
“Dili lenyewe linafanyikia wapi?” Panja alihoji kabla ya kunyanyuka.
“Tutaongea ukisharudi. Lakini ni hapahapa town.”
************
SAA saba usiku, Panja na Kipanga walikuwa wakitoka ndani ya chumba maalum katika nyumba ya Kipanga. Mkakati ambao Kipanga alimpa Panja tangu walipokutana saa tatu na dakika kadhaa, ulimpa ujasiri mkubwa Panja. Wakatembea wakikata mtaa huu na ule, kwa hadhari na kwa kujiamini, bangi waliyovuta usiku huo ikawaongezea hali ya kujiamini.
Walipofika Mtaa wa Libya, Kipanga akamnong’oneza Panja: “Subiri kidogo.”
Panja alisimama kando ya barabara, akamwona Kipanga akilifuata jengo moja ambako alinong’ona na mlinzi mmoja kwa takriban dakika mbili kisha akarudi. “Una silaha yoyote?”
“Sina,” Panja alijibu haraka.
“Shika hii,” alikabidhiwa kisu kisha ikafuata amri nyingine,
“Nifuate.”
Wakatoka, hatua zao zikiwa za asteaste, Kipanga akiwa na bastola mkononi, Panja akiwa na kisu. Wakafunguliwa geti na yule mlinzi na kuingia ndani, Kipanga mbele, Panja nyuma.
Dakika kumi baadaye, milipuko miwili ilisikika. Panja na Kipanga walikuwa kazini, na walipotoka humo ndani waliiacha maiti ya mzee wa Kihindi ikivuja damu shingoni.
*
Nje ya geti, Kipanga aliyekuwa na fuko kubwa la nailoni lililojaa noti alimnong’oneza yule mlinzi: “Uje home asubuhi.”
************
NYOTA ya jaha ilikuwa imemshukia Panja. Tangu azaliwe na kufikia umri wa kuweza kutambua thamani ya pesa, hakuwa na kumbukumbu ni lini aliwahi kumiliki shilingi laki moja. Usiku huu baada ya mgawo alijikuta akimiliki milioni tatu na robo.
Zilikuwa ni pesa nyingi kwake kiasi cha kujiona yu tajiri mdogo wa Dar, na kwamba ni pesa ambazo kamwe zisingekwisha. Kwa mantiki hiyo, starehe alizipa kipaumbele katika ratiba zake za kila siku. Leo aliingia baa hii, kesho baa ile na keshokutwa, ile. Kote huko hakukosa kuondoka na mwanamke mwenye mvuto mkali.
Hakuhitaji kutongoza, pesa zilizungumza. Na hakuwa na mkataba na mwanamke yeyote; leo akimchukua Zainabu, kesho atambeba Zinduna. Alichojali ni uwezo wa anayechukuliwa; uwezo wa faraghani.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ni katika bebabeba hiyo ndipo alipokumbana na Hilda, lakini huyu hawakukutana baa bali katika kituo cha daladala, Posta Mpya katikati ya Jiji la Dar es Salaam, wote wakisubiri usafiri wa Kinondoni.
Kwa kumtazama harakaharaka, Panja alivutiwa na umbo la Hilda. Ndiyo, Hilda alikuwa ni mzuri kiasi cha kumlinganisha na Sofia, mwanamke aliyeishi mtaa mmoja na Panja na akawa ni mwanamke ambaye, kichwani mwa Panja alipewa nafasi ya kwanza kwa uzuri wa sura na umbo.
Naam, Panja alihisi kamwona pacha wa Sofia. Akajaribu kuzikumbuka siku mbili ambazo walijichimbia gesti wakifanya hivi na vile katika kuzikonga nyoyo zao. Siku ya kwanza Sofia alionekana kalewa sana hali iliyomfanya Panja ajenge hisia kuwa huenda ndiyo maana hakujishughulisha inavyostahili katika starehe iliyowakutanisha. Akamsamehe.
Siku ya pili, wote hawakulewa, walikunywa bia mbilimbili tu baada ya kuyajaza matumbo yao chakula kizito. Kisha wakachukuana tena hadi gesti. Ni siku hiyo ndipo Panja alimjua vizuri Sofia, kwamba pamoja na dosari nyingine, pia alikuwa mbumbumbu wa kutupwa katika fani hiyo. Asubuhi ya siku ya tatu alimtema kama kapi la muwa.
Lakini, pamoja na hayo, Panja hakutaka azihamishie kasoro za Sofia kwa mwanamke huyu mrembo maradufu. Hapana. Aliamini kuwa kufanana sura na umbile si kufanana nguvu na maarifa katika kila nyanja. Ni hilo lililomfanya ajikute anapanda daladala ambalo Hilda alipanda japo kwa wakati huo hakujua Hilda alikuwa akielekea wapi.
Daladala la Mwananyamala lilipofika Hilda alipanda, Panja naye hakubaki nyuma, akajitoma garini. Bado alikuwa ni mwanamume wa ‘kutesa.’ Alipoingia ndani ya daladala hilo alikuwa na shilingi laki moja na vikorokoro vichache mfukoni, achilia mbali milioni moja na kidogo zilizobaki nyumbani, hizo zikiwa ni masalia ya zile milioni tatu.
Akabahatika kuketi siti moja na Hilda, roho yake ikasuuzika. Hata hivyo kwa jinsi mazingira yalivyokuwa ndani ya daladala hilo, Panja hakuweza kuiweka bayana dhamira yake kwa Hilda. Alichoambulia ni jina na kituo atakachoteremkia.
“Na mimi nateremkia hapohapo Kinondoni,” Panja alimwambia.
“Naishi Mtaa wa Sekenke.”
“Mie niko Mtaa wa Togo,” Hilda alisema.
Walifahamiana zaidi baada ya kuteremka. Na usiku wa siku hiyo ukawazalishia uhusiano wa mapenzi wakiwa pamoja nyumbani kwa Panja.
Siku ya pili walirudia.
Ya tatu wakanogewa.
Hatimaye Hilda akawa ‘mke.’ Na akilini mwa Panja, kati ya wanawake wote waliowahi kumchojolea nguo, ni huyu Hilda aliyemtoa jasho!
**********
MIEZI miwili ilipita, sasa Hilda akiiona dunia tamu kuliko kile kipindi alipokuwa akiishi peke yake. Ni kipi alichokosa? Kama ni pesa, lilikuwa ni kosa la jinai ndani mwao kukosekana shilingi laki mbili, tatu au zaidi ya hizo. Jinsi zilivyopatikana, hakujua. Kwa jumla hakujua bwana wake alikuwa akifanya kazi gani iliyomwingizia pesa. Na ilipotokea akahoji japo kwa mbali, hakupata majibu sahihi. “Napata tenda ya kuendesha daladala…” au “nafanya kazi kwenye benki moja ya nje…” au “Niko bandarini…” na kadhalika na kadhalika.
Hata hivyo, Hilda hakujali kupewa majibu tofauti, alijali kupata kile ambacho mwili wake kiliuhitaji. Ndiyo, alijali kuufaidi mwili wa Panja ambao kama si kumkanda basi ulimkaanga pindi kitanda kilipowalaki sanjari na pesa lukuki za matumizi, ambazo Panja alimpa.
Ndipo ikaja siku ambayo Panja alimwambia Hilda kuwa alitarajia kwenda Morogoro.
“Morogoro?” Hilda alihoji kwa mshangao. “Kufanya nini Morogoro?”
“Kuna kazi kidogo. Nitarudi kesho au keshokutwa. Lakini hiyo itatokea kama mipango yangu itasababisha nishindwe kurudi leo hii.”
Hilda, kama kawaida yake, hakujali. Si mara moja au mbili ameshalala peke yake hadi alfajiri arudipo Panja. Siku nyingine alijikuta akipitisha saa arobaini na nane bila ya kumwona. Taarifa hii ilikuwa haitofautiani na taarifa nyingine nyingi alizokwishampa.
Alichofanya ni kumdhibiti kitandani kwa takriban nusu saa, akimuaga kwa namna waliyoizoea, shahidi wa kuagana huko wakiwa ni mijusi wadogo wawili waliokuwa darini. Na Hilda aliamini kuwa kama ilivyokuwa katika safari zote zilizopita, Panja angerejea na pesa, tena pesa nyingi.
************
NI baada ya nusu siku ndipo Panja alirejea. Na hakurudi hata na sarafu moja, zaidi ni uso wake ndio uliobeba hasira kali iliyodhihirika hata machoni mwa Hilda ambaye alizoea kuuona uso huo ukiwa umechangamka.
Usiku mambo yalizidi kuwa mabaya kwa Hilda. Hakuipata huduma aliyozoea kupewa na Panja. Akajaribu kutumia zile mbinu zake zote, mikono ikitalii kila sehemu na ulimi ukiteleza kila palipostahili kwa namna aliyoamini kuwa ingeyaamsha ‘mashetani’ ya Panja ambayo siku hiyo yalilala usingizi mzito.
Haikusaidia!
Mtoto wa kike akashangaa, na ndipo alipoamua kumtupia lile swali: “Una nini leo?”
Alikuwa na sababu ya kumuuliza hivyo. Kwa kawaida, muda kama huo, usiku kama huo, Panja huwa akimsumbua, akihitaji kwa mara nyingine, na Hilda apende asipende, angemtimizia matakwa yake.
Lakini usiku huu hakuwa yule Panja wa siku zote, Panja ambaye hakuwahi kudai kuwa ana uchovu uliosababishwa na mahangaiko ya mchana kutwa.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Huyu alikuwa ni Panja mwingine, Panja ambaye hakuonesha kufurahishwa na chochote kati ya aliyofanyiwa na huyu mpenziwe. Na kutokana na uchungu uliomjaa moyoni, aliamua kulitoa lile lililomsonga na kumfanya aonekane kiumbe wa ajabu kwa Hilda.
“Sikia Hilda,” alitamka kwa sauti ya chini. “Kama kuna safari ambayo ilikuwa mbaya kwangu basi ni hii ya leo.”
Hilda alishtuka. “Hii ya Morogoro?” alimuuliza.
“Hiyohiyo.”
“Ilikuwa mbaya ki-vipi?”
“Sikurudi na pesa.”
“Hukurudi na pesa?” mshangao ulidhihirika katika sauti ya Hilda. “Hilo ndio limekunyong’onyesha ivo? Siku hazifanani, mpenzi. Kuna siku mtu unapata pesa na kuna siku ambazo mambo yanakuwa kama ivo tena.”
“Usemavyo si uongo, lakini hayo siyo ya kutokea kwa upande wangu.”
“Ki-vipi?”
“Uelewe maana ya kukwambia kuwa sikurudi na pesa,” Panja alisema kwa msisitizo mkali japo sauti yake ilikuwa ya chini. Akaongeza: “Siyo kwamba pesa sikupata. Nimezipata, lakini sikurudi nazo. Mpaka hapo tuko pamoja?”
Hilda hakuwa mwepesi wa kuelewa. Maneno hayo ya Panja bado yalimwacha njiapanda. Akashusha pumzi ndefu kabla hajauliza, “Una maana kipi kilichotokea hadi ukapata pesa na hukuja nazo? Umeporwa na majambazi?”
Ilimbidi Panja atumie juhudi za ziada na kufanikiwa kukizuia kicheko kilichomjia kufuatia swali hilo la Hilda. Moyoni akamsikitikia kwa kutoijua sababu ya yeye kutorudi na pesa, na zaidi, kwa kuishi na mtu asiyekubalika katika jamii iliyostaarabika.
Jambazi!
Alimtazama kwa sekunde chache kisha, kwa sauti ndogo, akasema, “Tulia. Najua, kuna jambo ambalo hulijui, na sasa ni vizuri ukilijua.”
“Ni nini? Mbona sikuelewi?” sauti ya Hilda ilikuwa ya mchanganyiko wa woga na mshangao.
“Ni vizuri ukiifahamu kazi yangu,” Panja alisema kwa unyonge.
“Kazi yako?” Hilda alimdaka.
“Tulia. Mbona una papara?”
Hilda akanywea.
Panja akakohoa kidogo kisha akamuuliza, “Hushangai kuona mara nipo, mara sipo?”
“Hata nikishangaa itanisaidia nini? Najua kawaida ya mwanaume ni kuhangaikia maisha.”
Panja aliachia tabasamu la mbali, tabasamu ambalo alilikata ghafla na kusema, “Ndiyo, ni kawaida ya mwanaume kufaitia maisha, lakini si kwa mfumo kama huu wangu.”
“Mfumo gani?”
Kwa mara nyingine Panja alimtupia macho Hilda. Nuru hafifu ya rangi ya bluu iliyotoka kwenye globu iliyoning’inia darini iliuongeza uzuri wa mwanamke huyo ambaye wakati huo, zaidi ya nguo laini ya ndani, hakuwa na vazi jingine mwilini. Kulingana na ujenzi bora wa umbo lake teketeke, macho yake malegevu yakisihi badala ya kushinikiza, na kwa jinsi alivyolala kihasara-hasara pale kitandani, isingekuwa rahisi kwa mwanamume rijali aendelee kumtazama hata kwa dakika tano kabla hajamparamia kwa uchu usiokadirika.
Ndiyo, angekuwa ni mwanamume mwingine, siyo huyu Panja ambaye kwa wakati huo, kutokana kuathirika kisaikolojia, hakuwa hata na wazo kuhusu mwili huo mzuri uliokuwa kando yake. Aliendelea kumtazama Hilda kisha akasema, “Kachukue funguo kwenye ile suruali niliyoivua.”
Hilda alijitoa kitandani na kufanya alivyoagizwa.
“Fungua droo ya chini, kabatini,” agizo jingine.
Kama awali, Hilda alitii agizo hilo la pili. Papohapo mshtuko mkubwa ukampata! Ndani ya saraka kulikuwa na kitu kimoja tu, bastola! Akilini mwa Hilda, tangu aanze kuishi na Panja, hakuwahi kubaini kuwa Panja alimiliki chombo hicho.
Taharuki ikiwa imejikita akilini na usoni pake, alikurupuka na kuiacha saraka hiyo wazi, akasimama kando na kumkazia macho Panja, utazamaji uliojitenga na masikhara kwa maelfu ya kilometa. Akawa akihemea juu, juu.
“Ni nini hiki?!” hatimaye alihoji kwa sauti yenye kitetemeshi cha mbali.
Badala ya Panja kujibu, alitabasamu kidogo, akauwasha msokoto wake wa bangi na kuvuta mkupuo mmoja wa nguvu kisha akauzima. Harufu kali ya bangi hiyo lilikuwa ni jambo lililokwishazoeleka kwa Hilda. Haikumkera. Lakini hii bastola!
“Panja ni nini hiki?” aliuliza tena.
“Sidhani kama unaweza kuwa mshamba wa kutokukitambua chombo hicho,” Panja alijibu kwa sauti ya chini, akionesha dhahiri kujiamini kwa kiwango kikubwa.
“Kimefikaje humu?”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kimeletwa na jini.”
“Panja, ni silaha hii, Panja!” Hilda alisema kwa sauti ya woga.
“Ndiyo, kwani unadhani mie naichukulia kama toyi la mwanasesere?”
Hilda alisonya, kisha akauliza, “Ni ya nani?”
“Ni ya padri mmoja amenipa nimtunzie.”
“Padri?!” Hilda alishangaa. “Panja mbona unaleta mzaha kwa jambo zito kama hili?”
Sasa badala ya kutabasamu, Panja aliachia kicheko hafifu, kisha akasema, “Rudi kitandani tuzungumze. Tatizo lako ni papara. Njoo nikupe ukweli wenyewe, baby.”
Akiwa bado amechanganyikiwa, Hilda alimfuata Panja kitandani ambako sasa alivuta shuka na kuusitiri mwili wake. Wakatazamana tena.
“Iwe ni siri yako,” Panja alisema kwa sauti ya mnong’ono, sauti nzito, yenye msisitizo mkali. “Ikivuja, ndipo utakaponitambua vizuri kuwa mimi ni nani. Sikufichi; kazi yangu ya kunipatia pesa inakitegemea kifaa hicho.”
“Mamaa!” Hilda alibwata kwa sauti ya chini. Hakuhitaji ufafanuzi zaidi wa kauli ya Panja. Sasa aliijua vizuri kazi ya mwanamume huyo. Kwa mbali mapigo ya moyo wake yaliongeza kasi. Alikumbwa na jakamoyo.
“Usishangae,” Panja aliendelea. “Usidhani kila mtu aliyetajirika au kuwa na kiwango kizuri cha maisha amefanikiwa kwa kutumia njia halali tu. Hapana. Kuna wezi wa kalamu, ambao ni wakongwe wa kughushi. Kuna walioanzia kupata pesa kwenye shughuli ndogo ndogo za halali, na Mungu akawajalia hadi wakatajirika. Na kuna waliotajirika kwa kupora mamilioni ya pesa na wasikamatwe, leo hii wanatanua.
“Mimi nimo katika kundi hilo la mwisho, kundi la kufukuzana na dola. Lakini naamini ipo siku nitaiacha kazi hii. Nitaiacha nikiwa tayari n’na pesa inayoeleweka. Kuna haja gani ya kufanya kazi ya roho mkononi kama tayari mtu una kitu kama milioni ishirini au thelathini ndani?”
Akatulia kidogo na kumtazama Hilda sawia. Akahisi kuwa kwa kiwango kikubwa maneno hayo yamemwingia.
“Unasikia mpenzi,” aliendelea. “Huenda leo nd’o ningechukua uamuzi wa kujipumzisha au kustaafu kazi hii. Ningechukua uamuzi huo kama ningerudi na pesa tulizopata na Kipanga. Na huenda kesho asubuhi ningeripoti kwenye duka la magari na jioni kitu chenye miguu minne kingekuwa kimepaki hapo nje kikilindwa na Mmasai mwaminifu.”
Baada ya ksema hivyo, Panja aliachia kicheko hafifu, kicheko cha uchungu, kicheko ambacho hata Hilda alipomtazama usoni alibaini kuwa ni kicheko kilichoficha hasira kali nyuma yake.
“Panja, mbona sikuelewi? Naona kama unaanza kujifunza kuwa mtunzi wa hadithi au mashairi. Umeingia lini katika fani hiyo?” Hilda alimuuliza huku akimpapasa kifuani.
“Huenda kwako ni mashairi, au labda unaona nakusimulia hadithi ya kubuni. Lakini naomba uniamini; huo ni ukweli mtupu, sio mashairi wala hadithi ya kubuni.”
Mkono wa Hilda ulikuwa umekiacha kifua cha Panja, na sasa ulikuwa ukiendelea kufanya ziara katika sehemu nyingine. “Sikiliza, Panja,” hatimaye alisema kwa mnong’ono. “Tuna usiku mfupi sana na tuna mengi ya kuzungumza na kufanya. Unaonaje, fupisha mazungumzo tufurahi kidogo.”
Panja alicheka kidogo, kicheko kilekile ambacho hakikuwa hata na chembechembe za furaha halisi. Kisha akasema, “Si vibaya kama leo tutaahirisha hayo mengi mengine, na tukakamilisha hili ninalokueleza.”
“Lakini…” Hilda alisema na kusita baada ya Panja kuutoa mkono wake ambao wakati huo ulikuwa mahala fulani ukipapasa kwa namna iliyomtia Panja wazimu wa mbali kiasi cha kujikuta akishusha pumzi ndefu.
Hilda alijilaza pembeni na kukodoa macho darini akikosa la kusema.
“Sikia mpenzi,” hatimaye Panja alisema. “Huko safarini tulipata pesa, kitu kama milioni hamsini hivi.”
“Wee!” Hilda alibwata kwa mshangao.
“Amini hivyo,” Panja alisema kwa sauti ya chini lakini yenye msisitizo mkali. “Kwa kweli lilikuwa ni fungu kubwa la kutosha kutufanya tuachane na maisha ya aina hiyo. Zilikuwa ni milioni hamsini au zaidi kwa jinsi lile begi lilivyoshona, na kwa kuwa noti zenyewe zilikuwa ni ‘wekundu wa msimbazi’ na dola za Marekani. Tulizipata, tukaondoka huku tukiiacha mizoga mitatu ya Waarabu. Lakini mimi nimerudi mikono mitupu! Huo nd’o ukweli wenyewe, Hilda wangu!”
“Kwa nini?”
“Kipanga,” Panja alijibu. “Kipanga kanizidi kete. Ni vigumu kuamini lakini hivyo ndivyo ilivyo.”
“Kipanga huyu rafiki yako?!”
“Kuna Kipanga gani mwingine unayemfahamu?”
Hilda akaguna na kushusha pumzi ndefu. Kisha kwa sauti ya unyonge, aliuliza, “Ilikuwaje?”
Panja alikunja uso kidogo, akakohoa kisha akashusha pumzi ndefu. “Ni hadithi ndefu, lakini nitakuhadithia,” hatimaye alisema.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
*****HAYA, KUMEKUCHA. PANJA ANATAKA KUMSIMULIA HILDA KILICHOJIRI HADI AZIDIWE KETE NA KIPANGA. TUONANE
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment