Simulizi : Kwa Udi Na Uvumba
Sehemu Ya Pili (2)
“AMINI hivyo,” Panja alisema kwa sauti ya chini lakini yenye msisitizo mkali. “Kwa kweli lilikuwa ni fungu kubwa la kutosha kutufanya tuachane na maisha ya aina hiyo. Zilikuwa ni milioni hamsini au zaidi kwa jinsi lile begi lilivyoshona, na kwa kuwa noti zenyewe zilikuwa ni ‘wekundu wa msimbazi’ na dola za Marekani. Tulizipata, tukaondoka huku tukiiacha mizoga mitatu ya Waarabu. Lakini mimi nimerudi mikono mitupu! Huo nd’o ukweli wenyewe, Hilda wangu!”
“Kwa nini?”
“Kipanga,” Panja alijibu. “Kipanga kanizidi kete. Ni vigumu kuamini lakini hivyo ndivyo ilivyo.”
“Kipanga huyu rafiki yako?!”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kuna Kipanga gani mwingine unayemfahamu?”
Hilda akaguna na kushusha pumzi ndefu. Kisha kwa sauti ya unyonge, aliuliza, “Ilikuwaje?”
Panja alikunja uso kidogo, akakohoa kisha akashusha pumzi ndefu. “Ni hadithi ndefu, lakini nitakuhadithia,” hatimaye alisema.
Kipindi kilichofuata kilikuwa cha Hilda kusikiliza kwa makini yaliyomsibu Panja katika safari yake ya asubuhi ya siku hiyo, safari ambayo Panja alimwongopea kuwa ni ya Morogoro.
************
HAKUKUWA na safari ya Morogoro. Marafiki hao wawili waliondoka nyumbani kwa Kipanga saa tatu asubuhi kwa teksi. Robo saa baadaye, dereva wa teksi hiyo alizamishiwa kisu shingoni na kutupwa kando ya barabara eneo la Kibamba. Gari likawa chini ya milki yao.
Saa moja baadaye walikuwa Kibaha ambako waliliegesha gari hilo nje ya jumba zuri la Nassor Khalfan, mwarabu aliyekuwa na pesa lukuki.
“Safari yetu imekomea hapa,” Kipanga alimwambia Panja kwa sauti nzito bila ya kumtazama. Kisha aliingiza mkono ndani ya jaketi lake na kuchomoa bastola mbili. “Ficha hii,” alimkabidhi Panja. Akaongeza, “Kuna gololi moja tu. Jifunze kuitumia kuanzia leo.”
Panja aliipokea bastola hiyo huku akisitasita. Hii ilikuwa ni mara yake ya kwanza kuishika silaha hiyo. Hata hivyo alikaza moyo na kuipachika kwenye mfuko wa jaketi lake.
Muda mfupi baadaye walikuwa kwenye mlango wa nyumba ya Nassor Khalfan. Kipanga alibonyeza kengele na kusubiri. Punde mtoto mdogo wa kiume alifungua mlango huo na kuwatazama wageni hao kwa mshangao.
“Mnataka nini?”
Lilikuwa ni swali baya sana masikioni na akilini mwa Kipanga. Alimtazama mtoto huyo wa Kiarabu kwa hasira iliyofichika moyoni, kisha kwa sauti ya upole, alimwambia, “Kamwite baba yako.”
“Baba ana wageni.”
“Ana wageni? Hata sisi ni wageni,” Kipanga alifoka. “Kamwite! Kamwambie kuna wageni toka Dar.”
Mikunjo iliyojitokeza usoni mwa Kipanga sanjari na wekundu wa macho yake ilikuwa ni taswira ya kutosha kumlainisha mtoto yule wa Kiarabu. Akatii amri.
Dakika chache baadaye mzee Nassor Khalfan alitokea. “Oooh, karibuni,” alisema huku tabasamu likichanua usoni pake.
Akaongeza, “Ingieni. Niko na wageni wa kawaida kwa maongezi ya kawaida. Piteni ndani.”
Huko ndani haikuhitajika faragha kwa maongezi kati ya mzee Nassor Khalfan na hawa wageni wake toka Dar. “Tunaweza kuzungumza tu,” alimwambia Kipanga. “Hawa ni wenzangu, hawana matatizo kabisa.”
Waliongea.
Yalikuwa ni maongezi ya kibiashara. Kipanga alikwishawasiliana na mzee huyo siku chache zilizopita, na wakakubaliana Kipanga amtafutie gari la wizi. Na gari walilotaka kumuuzia ni hilo walilompora dereva muda mfupi baada ya kumkodi. Wakataka awape shilingi milioni kumi, kiwango ambacho Mwarabu huyo hakukiafiki, akiungwa mkono na wale wenzake.
“Kama ni milioni tano, natoa sasa hivi,” Mzee Nassor alisema. “Vinginevyo ni bora ninunue Corolla mpya, model ya nyuma kidogo.”
‘Milioni tano!’ Kipanga aliwaza. Aliona kiwango hicho ni kidogo sana. Zikamjia hisia kuwa biashara yao inanyemelewa na mdudu mbaya. Akawaza, hilo gari wamepora na kumuua dereva hukohuko njiani. Kama watazubaa nalo, suala la kukamatwa lilikuwa dhahiri.
Lakini biashara ya milioni tano katu haikumwingia akilini. Alitaka Mwarabu huyo atoe milioni kumi ili agawane vizuri na Panja, mgawo ambao alipanga kumpa Panja asilimia kumi tu ya pato zima.
Ukimya wa muda mfupi ulitawala kisha Kipanga akasema, “Ni afadhali ungeniambia hivyo tangu siku tulipowasiliana.”
“Ndiyo, lakini usijali,” Nassor Khalfan alisema huku akikunja uso.. “Kumbuka kuwa tulikubaliana juu ya gari aina ya Benz au Volvo au BMW. Wala si Toyota. Hii Mark 11 inaonekana bado inadai lakini ndani nina Chaser ambayo haijamaliza hata miezi miwili, na nimeipata kihalali tofauti na hii yako ambayo huenda ikanitokea puani.”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Sawa, sikuja na Volvo, BMW au Benz, nd’o maana tunakupa hii kwa bei ya kutupa,” Kipanga alisema kwa sauti kavu, macho yake makali yakiwaangalia kwa zamu Nasssor na Waarabu wenzake. Kisha akaongeza, “Kwani ulitegemea nikutajie milioni kumi kwa magari ya aina hiyo?”
“Hapana, Toyota haiwezi kuifikia Benz na hayo mengine,” mzee Nassor alisema kwa majivuno huku akijiwashia sigara.
“Ulitayarisha kiasi gani kama ningekuegeshea Benz hapo nje?”
“Benz,” mzee Nassor alitamka kwa sauti ya chini huku macho yameanguka sakafuni. Kisha ghafla akaunyanyua uso na kumtazama Kipanga usoni sawia. Akaongeza, “Kama ni Benz original ya Mjerumani, na ambayo haijala kilometa zaidi ya mia moja, nilikuwa nimekutengea milioni hamsini ndani, sio za kufuata benki.”
Ilikuwa ni kauli ya kusisimua akilini mwa Kipanga. Tayari uchu wa kujitwalia pesa hizo ukamjaa. Alimtazama Panja kwa sekunde chache kisha akayahamishia macho kwa wale Waarabu wageni kabla hajayatua kwa mwenyeji wake, Nassor Khalfan. Picha ya bulungutu la noti nyingi zikiwa katika himaya yake ikamjia akilini mara mia moja kwa sekunde tano tu.
“…nilikuwa nimekutengea milioni hamsini ndani, sio za kufuata benki” yalikuwa ni maneno yaliyojirudiarudia kichwani mwake mara kwa mara na kumtia hamasa ya kujipatia pesa hizo siku hiyohiyo, iwe, isiwe. Kama ziko humo ndani kwanini asijitwalie?
Ni kazi ndogo tu, kuwaonyesha mdomo wa bastola yake au ya Panja, itatosha kuwatia jakamoyo.
Kitakachofuata baada ya hapo ni kazi moja tu; upekuzi mkali kila mahali hadi pesa zipatikane. Kwamba, ni hatua ipi itakayofuata baada ya kufanikiwa kuzitia fedha katika milki yake halikuwa jambo lililotwaa nafasi akilini mwake wakati huo. Alijua kuwa mambo yote yatajiweka sawa kadri jambo moja baada ya jingine litakapotekelezwa. Na alitambua fika kuwa Panja alikuwa akisubiri maagizo ya utekelezaji toka kwake. Hivyo aliamua kuutumia muda huo kuanza utekelezaji wa hatua mojawapo.
Aliichomoa bastola yake haraka, akaielekeza usoni pa Nassor Khalfan na kwa sauti nzito lakini yenye kuashiria kifo, alisema: “Usidhani kuwa tunafanya mchezo wa kuigiza. Sema, utatoa milioni kumi au hutoi, biashara imalizikie kichwani mwako.”
Lilikuwa ni tukio ambalo Nassor Khalfan na wenzake hawakulitarajia. Kwa muda waliduwaa wakitazamana na domo la bastola hiyo.
“Nakupa sekunde kumi tu za kutoa tamko,” Kipanga aliendelea. “Zaidi ya hapo tuna hiari ya kufanya chochote kile tupendacho. Upo hapo?”
Nassor Khalfan alifikiri harakaharaka. Mbele yake alitazamana na ‘kifo.’ Kwa jinsi alivyomfahamu Kipanga, kosa lolote dogo lingeharakisha kifo chake. Lakini aliamini kuwa uamuzi wowote unaotokana na woga husababisha majuto baadaye.
Kwamba, kama angekubali kuchukua gari hilo kwa shilingi milioni kumi ilhali amekwishamtamkia kuwa amemtayarishia milioni hamsini kwa ajili ya Benz, isingemwia vigumu Kipanga kumtia risasi kisha kuvivamia vyumba na kuvipekua akizisaka hizo milioni hamsini.
Huenda angeendelea kuifikiria mbinu ya kulitatua tatizo hilo lililozuka ghafla kama asingetupia macho kwa Panja na kukumbana na yaleyale! Domo la bastola!
Kwa fadhaa alijikuta akiropoka: “Msiniue! Nitawapa pesa hiyo…! Tafadhali…!”
Hakumalizia lolote alilotarajia kuongeza. Mlipuko mkubwa ulitokea. Sekunde mbili baadaye milipuko mingine miwili ikatanda. Kipanga alimzamishia Nassor Khalfan risasi ya kichwani kisha akamlisha mmoja wa wale wageni risasi ya kifuani, wakati kwa mara ya kwanza Panja alijaribu kuitumia bastola kwa kumfyatulia risasi Mwarabu mwingine, risasi iliyozaa matunda kwa kuzama kifuani na kuyakatisha maisha yake papohapo.
Kilichofuata baada ya hapo kilichukua muda mfupi zaidi, kitu kama dakika tatu tu. Kipanga alimhimiza Panja aweke ulinzi mlangoni na yeye akatokomea katika chumba kimoja ambako alichakurachakura na kufanikiwa kuliona begi dogo ambalo alilifungua na kushuhudia mafurushi ya noti.
Hakuchelewa, alilibeba begi hilo na kutoka kwa kasi ileile.
“Twende,” alimwamuru Panja.
Wakatoka.
“Tunakwenda wapi?” Panja alimuuliza wakati Kipanga akiling’oa gari kwa makeke.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kipanga hakujibu. Mawazo yake hayakuwa hapo tena. Kuna lililokwishajipenyeza kichwani wakati huo na akawa katika fikra za kulipatia ufumbuzi wa haraka. Gari lilizidi kusaga lami ya Barabara ya Morogoro kwa kasi iliyowashangaza waliokuwa kando ya barabara hiyo.
“Vipi, inakuwaje?” Panja alihoji kwa mshangao. “Yaani tunarudi town? Ni noma msh’kaji wangu!”
Kipanga hakutamka lolote, na kuhusu hilo, hakuwa mtu wa kuambiwa chochote. Alitambua fika kuwa kupora gari hilo, kumuua dereva na kuitupa maiti yake kando ya barabara, kisha wakawaua wale Waarabu kule Kibaha, ni matukio ambayo yangelifikia Jeshi la Polisi baada ya muda mfupi sana.
Na hapo ndipo msako mkali utakapoanza, msako ambao aliamini kuwa ungechukua siku chini ya tatu kutoa matokeo. Kwamba matokeo hayo yatakuwa mazuri kwake, hilo halikuwa ni jambo lililopata nafasi yoyote akilini mwake. Alijua kuwa Jeshi la Polisi lingeingia kazini kwa nguvu za kifaru, na lingepata kile linachokihitaji; kuwatia mbaroni na kuwafungulia mashtaka ya mauaji na wizi wa kutumia nguvu.
Lakini alikuwa na sababu iliyomfanya aamue kurudi Dar es Salaam, sababu ambayo hakuwa tayari kuiweka bayana kwa Panja hadi hapo muda mwafaka utakapotimu. Akakaza macho mbele, mikono ikiwa imeushika usukani kwa makini huku mguu wa kulia ukiwa umeganda kwenye kibati cha mwendo, gari likiwa katika kasi ya kutisha.
Sasa walikuwa katika sehemu isiyokuwa na nyumba yoyote, picha iliyomtia matumaini Kipanga katika kutekeleza lile alilodhamiria.
Alianza kupangua gia moja baada ya nyingine, gari likapunguza mwendo taratibu, hatimaye akaliegesha pembezoni mwa barabara. Hatua iliyofuata ilikuwa mithili ya mchezo wa kuigiza au ndoto isiyopendeza kichwani mwa Panja. Kipanga aliichomoa bastola yake na kumwelekezea Panja usoni.
“Hilo kopo nililokukabidhi halina kitu tena,” alimwambia. “Lakini huenda likakusaidia huko mbele ya safari. Pambana na makali ya maisha kwa kutumia kopo hilo. Ukiwa na gololi mbili, tatu hutakosa kupata pesa kutoka kwa mtu yeyote. Kwa sasa teremka, uhusiano wetu umekomea hapa.”
Yalikuwa ni maneno yaliyopenya masikioni mwa Panja kwa usahihi mkubwa. Alisikia, akaelewa lakini hakuamini.
“Teremka! Toka!” Kipanga alifoka. “Nina muda mfupi sana wa kuendelea kukuhurumia. Ukizidi kuchelewa utanipa kazi nyingine ngumu ya kuutoa mzoga wako…”
Panja alimfahamu vizuri Kipanga. Alitambua jinsi asivyojua kuwa mzaha au utani ni mdudu wa aina gani. Kwa maneno haya aliyoambiwa na Kipanga, hakuhitaji tena kukipa kichwa kazi ya kupambanua kama huo ni mchezo wa kuigiza au ndoto isiyopendeza. Ni dhahiri Kipanga alikuwa hana masikhara.
Taratibu alifungua mlango na kutoka huku akilikodolea macho lile begi aliloamini kuwa lilisheheni pesa, tena pesa nyingi. Ni kwa kutambua kuwa pesa ziko hapo, ujasiri ukamjia kwa nguvu kubwa kiasi cha kufumbua kinywa na kwa sauti ya chini, sauti nzito na yenye msisitizo mkali akasema, “Utakuwa mstaarabu sana kama utanipa mgawo wangu…”
“Nini?!” Kipanga alimtazama kwa macho makali na kufuatisha kicheko cha dhihaka. “Hakuna cha mgawo tena hapa! Nimekuachia hiyo bastola ambayo thamani yake ni kubwa sana. Itumie kwa kupata pesa. Sidhani kama utakosa kunishukuru kwa wema huo niliokutendea. Sidhani.”
“Lakini…”
“Hakuna cha ‘lakini’ tena. Toka!”
Panja hakuwa na la kufanya, zaidi ya kujiengua taratibu na kushuhudia gari likiyoyoma machoni pake kwa kasi ya kutisha. Akaachwa kaduwaa. Ikamlazimu kusota akivizia gari hili na lile kwa machale kwani tayari alijua kuwa Polisi watakuwa wakiwasaka, hivyo alipaswa kuwa makini.
Baada ya dakika kumi hivi, basi moja liliutii mkono wake, dereva akaegesha pembezoni mwa barabara. Akaingia kwa unyonge, mfukoni akiwa na shilingi 5,000 tu alizotoka nazo nyumbani.
************
HILDA alibaki kinywa wazi baada ya kuisikia simulizi hiyo ya kutisha. Akamtazama Panja kwa makini na kuigundua hasira iliyojikita moyoni mwake na kutoa taswira halisi usoni pake. Huruma ikamwingia na kwa mnong’ono akajikuta akisema, “Basi, usijali baby…”
“Hapana, lazima nijali,” Panja alimkata kauli. “Huenda saa hizi tunasakwa na Polisi kama wahaini au magaidi. Na kama ndivyo ilivyo, basi mshenzi yule ana ahueni.”
“Ahueni ki-vipi?”
“Ana pesa,” Panja alisisitiza. “Kwa Tanzania ya leo hakuna kinachoshindikana mbele ya pesa. Kelele za serikali kuhusu eti kupiga vita rushwa na ufisadi ni kelele ambazo hazitofautiani na kumpigia mbuzi gitaa. Unadhani askari gani atakataa milioni moja au mbili kama atakutana na Kipanga na kuonyeshwa kiasi hicho cha pesa? Na kwa Kipanga, milioni moja, mbili ni kitu gani kama tayari ana zaidi ya milioni hamsini? Kwa kifupi, yeye akikamatwa ni rahisi kusevu ngoma, tofauti na mimi ambaye sina mbele wala nyuma. Mimi nikikamatwa nitaozea jela.”
Ukimya mfupi ukatawala. Kisha, kwa unyonge Hilda akauliza, “ Sasa utafanya nini?”
“Nitamsaka!” Panja alitamka kwa msisitizo. “Nakuapia, nitakula nae sahani moja. Na lazima nitampata. Naapa, nitamsaka kwa udi na uvumba mpaka nimpate. Liwalo na liwe. Najua ana ‘cha moto’ na lolote linaweza kutokea nitakapokutana naye. Lakini sijali, ni afadhali aniue kuliko kumwachia hivi-hivi tu atanue na pesa yangu.”
Kilikuwa ni kiapo rasmi toka kinywani mwa Panja, kiapo ambacho hakuwa tayari kukitengua hata kwa mtutu wa bunduki, japo pia hakujua kama atafanikisha azma yake hiyo kabla ya vyombo vya dola havijamtia mbaroni. Lakini ndivyo alivyoamua; ni kwenda mbele daima, kurudi nyuma, mwiko!
************
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
KIPANGA hakuwa mjinga. Aliijua hatari ambayo ingemkuta kama angeendelea kuling’ang’ania gari hilo. Hivyo, alichofanya baada ya kumwacha Panja ni kwenda umbali wa kilometa tatu hivi, kisha akaliegesha pembezoni mwa barabara na kutoka na lile begi lenye pesa.
Hakuendelea kushangaashangaa katika eneo hilo, alizunguka nyuma ya nyumba moja kisha akaufuata uchochoro akiwa katika uelekeo uleule wa Dar. Baada ya kutembea umbali mrefu kidogo hatimaye alijitokeza tena barabarani, hiyo ikiwa ni sehemu ambayo kulikuwa na kituo cha mabasi ya abiria.
Kupanda basi la abiria lilikuwa ni jambo ambalo halikumwingia akilini. Alihofia kukutana na mtu ambaye hatakuwa ‘mzuri’ kwake. Angeweza kupanda lori, lakini pia aliona kuwa usafiri wa aina hiyo ungemchelewesha kufika Dar.
‘Acha woga, una silaha, hakuna cha kukubabaisha,’ alihisi sauti ikimwambia. Ujasiri ukamrudia. Akavuka barabara na kupanda basi moja lililotoka mikoa ya Kaskazini mwa nchi. Kitu cha kwanza alichofanya baada ya kupanda ni kuangaza macho kwa kila aliyekuwemo.
Alijivunia kuwa na uwezo wa kuyasoma macho ya mtu yeyote mwenye harufu ya uaskari, watu ambao hakuwa na fikra za kuja kuwa na uhusiano nao katika maisha yake. Hivyo, macho yake makali yaliyokuwa nyuma ya miwani myeusi yalikuwa na kazi ya kuwatafuta askari ndani ya basi hilo. Dakika mbili za zoezi hilo zilitosha kumpa picha halisi ya abiria wenzake.
Hakukuwa na mtu wa kumtilia shaka. Ndipo akachagua siti ya nyuma kabisa na kutulia. Punde gari likaanza safari. Nusu saa baadaye akateremka Ubungo na kuuvaa uchochoro mmoja baada ya mwingine hadi akaifikia gesti bubu ambayo alikodi chumba na kujifungia kwa minajili ya kuzihesabu zile pesa.
Ni baada ya takriban nusu saa nyingine ndipo alipohitimisha zoezi hilo. Akatabasamu kwa furaha. Alikuwa na sababu ya kuwa katika hali hiyo. Lile begi lilikuwa na shilingi milioni 60! Hazikuwa pesa kidogo kwakeq! Maishani mwake, tangu aanze kushika pesa na kuitambua thamani yake, hakuwahi kukamata kiwango hicho cha pesa! Hata nusu yake!
Kwa wiki nzima alijihifadhi katika gesti hiyo, akila kila alichotaka na kunywa kila alichopenda bila ya wasiwasi wowote. Awe na wasiwasi wa nini? Wasiwasi utoke wapi? Aliyafananisha makazi yake hayo na pango lililochimbwa katika mmoja wa milima ya Himalaya, hivyo kumpata ingehitajika teknolojia ya hali ya juu na ujuzi wa kiwango cha juu kwa Jeshi la Polisi, nyenzo ambazo aliamini kuwa Jeshi la Polisi la Tanzania haliwezi kuwa nazo.
Kwa hali hiyo, hata hisia kuwa huenda ipo siku Panja atamwibukia hapo hazikupata uzito wowote kichwani mwake. Alimhofia Panja kwa kuwa ndiye mwenye uchungu zaidi, siyo Jeshi la Polisi. Na kwa kuwa alimwacha Panja akiwa hoi bin taaban kisaikolojia na kiuchumi, hakuwa na cha kuhofia tena.
Hakutishwa na kauli za Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani na mwenzake wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, kuwa msako mkali dhidi ya majambazi wanaosadikiwa kumuua dereva teksi na Waarabu watatu, unaendelea.
Hakubabaishwa na kauli hiyo!
Huo ndio utaratibu wa Polisi; uchunguzi na msako. Lakini siyo lazima uchunguzi ukatoa matokeo mazuri au msako ukazaa matunda. Akilini mwa Kipanga, msako na uchunguzi wa Polisi ni sehemu ya ajira yao. Kuonekana wakihangaika hapa na pale mitaani, silaha mikononi, wakimhoji mara huyu mara yule, kumtia makofi huyu na kumpiga teke yule huwafanya waonekane wakilipwa mshahara halali.
Na kitafikia kipindi ambacho litazuka tukio jingine, tukio zito zaidi, na hapo ndipo jalada hili litawekwa kando na kuchukuliwa jalada jingine. Huo, huenda ukawa ndio mwisho wa uchunguzi au msako wa tukio la jana. Kazi itaanza upya. Kazi mpya kuhusu tukio la leo.
Imani hiyo ilimfanya Kipanga asiwe na wasiwasi wowote. Ilipita wiki moja, zikakatika wiki mbili, hatimaye mwezi ukaisha akiwa hapohapo gesti akila raha. Hakukuwa na chochote cha kumtia jakamoyo. Pesa anazo, kwa nini asifurahie maisha?
Ni kiburi cha pesa hizo kilichomfanya kila siku abadili mwanamke wa kustarehe naye usiku baada ya kugida bia. Akawa akifanya hivyo huku akihakikisha kuwa mwanamke anayechukuliwa ni yule mwenye sifa za uzuri wa hadharani, mwanamke ambaye macho ya rijali yeyote lazima yamtazame kwa uchu mkubwa.
************
TAARIFA za vifo vya Nasssor Khalfan na wenzake wawili zililifikia Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani muda mfupi tu baada ya Panja na Kipanga kutoweka. Msako mkali ukaanza. Habari juu ya wageni wawili waliofika katika nyumba ya Nassor Khalfan wakiwa na gari dogo aina ya Toyota Corolla Mark 11 zikawa chachu kwa askari katika kuboresha upelelezi wao.
Hata hivyo, licha ya operesheni hiyo kufanyika kwa nguvu kubwa siku hiyo ya mauaji, ikiwa ni operesheni iliyoihusisha pia mikoa ya Morogoro na Dar es Salaam, bado hakukuwa na matokeo yoyote ya kuridhisha.
Jijini Dar es Salaam zilipatikana habari kuhusu maiti iliyokutwa kando ya Barabara ya Morogoro, eneo la Kibamba ikiwa na kisu kilichozama shingoni. Taarifa kutoka Kibamba na Kibaha zilimfikia Inspekta Materu kwa kipindi kisichozidi robo saa. Na alipozitafakari kwa kina akajiwa na hisia kuwa mauaji hayo ama yamefanywa na mtu mmoja au yametekelezwa na kundi moja.
Kama alivyozoea, kwenye matukio ya aina hiyo hakumweka mbali Sajini Kitowela. Mchana huu, saa saba, alimwita na kumpa picha halisi sanjari na hisia zake baada ya kupokea taarifa hizo.
“Nadhani matukio haya yamefanywa na mtu mmoja au kundi moja,” hatimaye Inspekta alisema.
“Kwa vipi, afande?”
“Ni kulingana na taarifa hii niliyokupa,” Inspekta alijibu. “Taarifa kutoka Kibaha zinasema kuwa, inaaminika wauaji wa Waarabu wale ni watu wawili waliofika katika nyumba yalikotokea mauaji wakiwa na gari dogo, jeupe aina ya Toyota Mark 11. Na huyu kijana aliyeripoti juu ya maiti iliyotupwa Kibamba, kando ya barabara amethibitisha kuwa alishuhudia kwa macho tukio la kuuawa dereva teksi.”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kasemaje?”
“Kwamba marehemu alitolewa ndani ya gari na wanaume wawili, wakamburuza na kumtupa nyasini kando ya barabara.”
“Na alilikariri gari lenyewe?”
“Anachojilaumu ni kutochukua namba za gari hilo, lakini anasema ni gari jeupe aina ya Toyota kati ya Mark 11 au Chaser.”
Sajini Kitowela alikunja uso kidogo kisha akahoji, “ Gari hilo lilikuwa likielekea wapi?”
“Anasema lilikuwa likielekea nje ya jiji, kama ni Morogoro, Kibaha au wapi, haijulikani. Lakini halikuwa likielekea huku Dar.”
“Yawezekana hisia zako ni sahihi,” Kitowela alisema. “Tatizo hapa ni moja. Kama hawa waliomuua huyu mtu walikwenda Kibaha ambako pia ndiko walikowaua wale Waarabu, basi sio rahisi kurudi huku.”
“Kwa nini?”
“Wanajua kuwa wanasakwa. Huenda saa hizi wako Morogoro au wameshika njia ya Tanga.”
Inspekta Materu alikunja uso kidogo na kuguna. “Haiwezekani,” hatimaye alisema. “Taarifa nyingine toka Kibaha ndiyo inayonipa picha kuwa watu hao hawakuelekea mbele ya Kibaha; wamerudi huku.”
“Taarifa gani?”
“Kuwa gari lililotumiwa na majambazi hao limetelekezwa kiasi cha kama kilometa kumi hivi toka Maili Moja kama unakuja huku.”
Kitowela alitikisa kichwa akiashiria kutoyaafiki maneno ya Materu. Kisha: “ Kutelekezwa kwa gari hilo siyo sababu ya kutufanya tuamini kuwa wamekuja huku. Kwani hawawezi wakafanya kama wanakuja huku halafu wakalitelekeza gari hapo kisha wakadandia gari jingine, wakapita Kibaha palepale na kutokomea kusikojulikana?”
“Wanaweza. Lakini jambo hilo litafanikiwa kama askari wa Kibaha watakuwa wamelewa chakari!”
*****KIPANGA KAAMUA KUJICHIMBIA UBUNGO AKITANUA NA WANAWAKE WAZURI. WAKATI HUOHUO, JESHI LA POLISI LIMEINGIA KATIKA HARAKATI ZA KUWASAKA WAUAJI WA WAARABU KULE KIBAHA NA DEREVA TEKSI PALE KIBAMBA. MAMBO BADO NI KIZUNGUMKUTI. NI KIPI KITAFUATA?
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment