Search This Blog

Thursday, 2 June 2022

KWA UDI NA UVUMBA - 5

 





    Simulizi : Kwa Udi Na Uvumba

    Sehemu Ya Tano (5)



    ALIPOUFIKIA mlango wenye maandishi: No.10 akasimama bila ya kubisha hodi. Akaangaza pande zote za korido hiyo na kutomwona mtu yeyote, hali iliyompa matumaini ya kutoshindwa kuitekeleza azma yake. Akaunyanyua mkono ili agonge mlango, lakini akasita. Na alikuwa na sababu ya kusita.



    Masikio yake yalinasa miguno tofauti, miguno ambayo haikuhitaji mtu mzima, mwenye akili timamu ashindwe kujua ni kipi kilichoendelea.



    Hasira zikampanda, hasira zilizotokana na kumbukumbu ya tukio la kiasi cha mwezi mzima huko Maili Moja, Kibaha, tukio lililompa Kipanga utajiri wa wastani kiasi cha kuja kutanua huku Ubungo, akitumia pesa kama ‘mwendawazimu.’



    Hakuendelea kuvuta subira, alikurupuka kugonga mlango. Aligonga mara mbili. Kimya. Sasa hata ile miguno iliyotoa taswira ya starehe ya mapenzi na maneno ya kimahaba-mahaba ilikatika ghafla. Akatulia kama sekunde kumi hivi na kurudia kugonga, safari hii ikiwa ni mara tatu na kwa nguvu zaidi.



    ***************



    “NAJISIKIA kuamini kuwa tunayemfuata ni Kipanga, wala hatubahatishi,” Inspekta Materu alimwambia Kitowela.



    “Kwa nini?”



    “Sijui, lakini nina imani ni yeye. Mara nyingi ndoto zangu huwa ni za kweli.”



    Sajini Kitowela alicheka. Akataka kupachika neno la masikhara lakini akasita kufanya hivyo. Akilini mwake aliona wakati huo haukuwa mwafaka kwa mzaha wa aina yoyote.



    Walitembea kwa hatua ndefu, za kikakamavu, wakiifuata ile gesti bubu.



    “Huko tunakokwenda ni mawili,” Materu alisema huku akimkazia macho Kitowela. “Tukimkuta, na akaleta kujua, tunaharibu tu! Au vipi?”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Yap! Nd’o maana’ake!”Kitowela aliafiki kwa msisitizo. “Kifo cha jambazi mmoja ni faraja kwa mamilioni ya Watanzania.”



    Wakaendelea kutembea kwa kasi ileile. Dakika chache baadaye walikuwa mbele ya mhudumu wa gesti hiyo.



    “Karibuni,” mhudumu huyo aliwatazama kwa zamu huku akionesha dhahiri kuwashangaa. Walikuwa ni watu ambao ndiyo kwanza alikuwa anawatia machoni. Akaongeza, “Niwasaidie nini?”



    Inspekta Materu hakujibu. Na wala hakuwa na muda wa kupoteza. Alitoa kitambulisho mfukoni na kumwonesha kijana huyo. Kisha, kwa sauti nzito akasema, “Tuko kazini. Fuata maelekezo yetu tangu sasa, na ujibu maswali tutakayokuuliza bila kuficha kitu wala kusema uongo. Umenielewa?”



    “Ndiyo, afande,” mhudumu huyo alijibu kwa sauti iliyojaa woga huku macho yakiwa yamemtoka pima.



    “Wewe si ndiye mpokeaji wa wageni wote katika gesti hii?”



    “Ndiyo.”



    “Leta leja ya wageni wako.”



    Kijana yule alishusha pumzi ndefu na kufungua saraka ya meza ambako alitoa leja na kuiweka juu ya meza. Inspekta Materu aliifunua ukurasa wa kwanza na kutupa macho kwenye tarehe. Akaguna. Tarehe ya kwanza ilikuwa ni ya miezi mitano iliyopita. Akafunua kurasa nyingi kwa mkupuo hadi katikati ya leja hiyo. Hapo akatulia kidogo na kutupa macho tena. Akawa makini zaidi katika zoezi la kuyafuatilia majina yaliyoandikwa katika kurasa hizo.



    Akilini mwake alikuwa akilitafuta jina la KIPANGA. Akafunua kurasa hadi kurasa. Hatimaye akajikuta akigota mwisho. Jina la Kipanga halikuwemo. Halikuwa jambo la kumshangaza mtu kama yeye.



    Alizijua mbinu nyingi za majambazi katika kuuepuka mkono wa sheria. Moja ya mbinu hizo ni kutoyatumia majina yao halisi wakati wanapochukua chumba katika gesti yoyote.



    Hivyo, badala ya kuhoji swali jingine lolote, kwanza aliichomoa picha ya ukubwa wa ‘postcard’ na kumwonyesha kijana huyo. “Unamfahamu huyu?” alimuuliza huku akimkodolea macho.



    Kijana huyo aliishika picha hiyo na kuitazama kwa makini. Akakunja na kuukunjua uso wake. Kisha akasema, “Sina hakika. Lakini siyo sura ngeni machoni pangu.”



    “Siyo sura ngeni?” Materu alimkazia macho. “Unadhani ulishamwona wapi?”



    Kijana alisita na kuendelea kuikazia macho picha hiyo. “Hapana, labda nimemfananisha,” hatimaye alisema.



    “Umemfananisha?” Materu aliwaka. “Mbona hueleweki? Zungumza kitu kinachoeleweka. Acha kusitasita, lakini nakukumbusha, zungumza kweli tupu! Uongo wa aina yoyote utakuponza! Inabidi uelewe hivyo. Ok, sema, unamfananisha na nani?”



    Kijana yule alijibu, “Na mpangaji wetu.”



    “Mpangaji wenu?” Materu alishusha sauti huku uthabiti wa kauli yake ukiwa palepale. Akamsogezea kijana huyo leja na kuongeza, “Leja yako hiyo. Hebu nionyeshe jina la huyo mpangaji unayemfananisha na huyu mwenye picha hii.”



    Kijana alikumbwa na kigugumizi. Alitambua wazi kuwa huyo mpangaji aliyesema kuwa anafanana na sura ya mwenye picha aliyoonyeshwa hakuwa akiandikisha jina lake kwenye leja tangu siku ya kwanza. Alikumbuka kuwa wakati alipomuuliza jina ili alijaze kwenye leja, mpangaji huyo alicheka na kumtupia noti ya shilingi 10,000 huku akimwambia, “Achana na mambo hayo. Ukijaza kila jina kwenye leja, wewe utakula wapi?”



    Na tangu siku hiyo hadi leo hii anapojiwa na askari hawa, hakuwahi kuliandika jina la mteja huyo hata siku moja! Takriban mwezi ulishakatika!



    Hivyo ndivyo ilivyokuwa, na sasa yuko mbele ya askari ambao tayari wameshamtisha kuwa kama atawalaghai kwa njia yoyote, basi atajikuta katika wakati mgumu. Kuswekwa mahabusu ambako ataambulia vipigo na mateso mengine yasiyovumilika, ni jambo ambalo hakuwa radhi limkute.



    Kwa hali hiyo alisema, “Afande kwa kweli jina lake halimo humu.”



    “Kwa nini?” Materu alimuuliza huku akimtazama kwa mshangao. Akamtupia macho Kitowela na kumkuta naye akimtazama kijana huyo kwa mshangao.



    Kijana alikosa jibu.



    Inspekta Materu hakuhitaji kudadisi zaidi kuhusu hilo. Badala yake aliendelea kumbana: “Huyo mpangaji wako ana muda gani hapa?”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kama mwezi mmoja hivi.”



    “Mwezi mmoja,” Inspekta Materu alisema kwa sauti ya chini zaidi huku akimtazama Kitowela. Kisha akamgeukia tena yule kijana. “Na hana matatizo yoyote katika ulipaji?”



    “Kwa kweli hana matatizo yoyote.”



    “Umesema ana takriban mwezi mmoja tangu awe mpangaji wako, japo humjazi kwenye leja yako. Lakini kutomjaza kwenye leja siyo kigezo cha kutomfahamu mpangaji wako wa muda mrefu kiasi hicho. Kila siku mnaonana, utaniambia kuwa hata jina lake hulijui?”





    Ukimya wa sekunde kadhaa ukatawala. Kijana akabaki ameyatupa macho juu ya meza.



    “Ok, tusipoteze muda. Tupe jina lake,” Materu alisema kwa sauti ya ukali kidogo.



    Kijana alishusha pumzi ndefu na kusema, “Mwanzoni alikuwa akijitaja kwa jina la Kakinga.”



    “Kakinga?!” Inspekta Materu na Sajini Kitowela walilirudia jina hilo kwa mkazo, macho yao makali yakiwa yameganda usoni pa kijana huyo.



    “Ndiyo, Kakinga. Lakini…”



    “Enhe, lakini nini tena?”Kitowela alimdaka.



    “Lakini siku hizi nasikia watu wengine wakimwita, Kipanga.”



    “Kipanga?” Materu na Kitowela walilirudia jina hilo kwa sauti ya chini zaidi, macho yao makali yakiwa yameganda usoni pa kijana huyo.



    “Ndiyo.”



    “Na unasema eti unasikia- ‘watu wengine wakimwita’- ni watu gani hao?”



    “Wanawake.”



    “Wanawake gani?”



    “Hawara zake.”



    Inspekta Materu alimtazama Kitowela huku kwa mara ya kwanza tabasamu jepesi likichanua usoni pake. “Ni mwenyewe,” hatimaye alisema kwa sauti ya chini.



    Kitowela aliafiki kwa kutikisa kichwa.



    Mara Inspekta Materu akayarejesha macho kwa kijana yule na papohapo akamtupia swali fupi: “Yupo?”



    “Ndiyo. Yupo.”



    “Yuko chumbani mwake saa’izi?”



    “Ndiyo.”



    “Ok, tuonyeshe chumba chake. We’ tuelekeze tu, tutaenda wenyewe.”



    Aliwaelekeza.



    ***************



    “MPUUZI gani tena huyo?” Kipanga alijiuliza kwa mnong’ono ambao hakuyafikia hata masikio yake mwenyewe. Alijihisi kukerwa na ugongaji mlango katika kipindi hicho ambacho hata mhudumu wa gesti hiyo alitambua fika kuwa yuko na wageni maalum.



    Tangu wanawake hawa walipojitoma chumbani humo wamekuwa wakimfanyia yale aliyoyapenda na yale aliyoyahitaji, aibu zikiwa umbali wa kilometa elfu nyingi toka nafsini mwao na wakati huohuo utaalamu ukijidhihirisha maungoni mwao.







    Wakati mlango huo wa chumba ulipogongwa mara mbili mfululizo, mmoja wa wanawake hao alikuwa amekilaza kichwa kwenye maungio ya mapaja na kiuno cha Kipanga, akikitumia kinywa chake kuendelea kumstarehesha kwa kiwango cha hali ya juu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wakati huo, mwenzake alikuwa akimpapasa Kipanga kifuani taratibu na mara chache akimminyaminya chuchu. Kilikuwa ni kipindi ambacho Kipanga hakuhitaji bughudha ya aina yoyote.



    Alihitaji starehe. Mlango ulikuwa umefungwa kwa ndani. Hivyo isingewezekana kwa mtu yeyote kuingia na kuikatisha starehe yao. Kwa hali hiyo, Kipanga hakujali, alizirejesha hisia zake kwa wanawake hawa warembo walioendelea kumpa burudani ya kipekee.



    Labda wangeendelea kuburudika kwa namna yoyote watakavyo, kama mlango huo usingegongwa tena, safari hii ikiwa ni mara tatu, tena kwa nguvu zaidi. Wote wakashtuka, wakasitisha zoezi lao. Mwanamke mmoja akanyanyuka na kutaka kwenda kuufungua lakini Kipanga akamvuta na kumketisha kitandani haraka huku akimtazama kwa jicho kali.



    Kwa ujumla Kipanga alishahisi hatari fulani, hisia ambazo kwa takriban wiki tatu zilizopita hazikuwa zikimjia. Ni hisia hizo zilizomfanya amzuie mwanamke huyo aliyetaka kwenda kufungua mlango huku wakati huohuo akimng’atua huyu aliyemng’ang’ania kwenye maungio ya kiuno na mapaja.



    Akakurupuka na kuitwaa bukta. Akaivaa harakaharaka kisha akalivuta begi lililokuwa uvunguni mwa kitanda na kuitoa bastola yake.



    “Vaeni!” aliwaamuru wanawake hao.



    Wakiwa tupu kama walivyotoka matumboni mwa mama zao, kwanza waliduwaa, wakaonekana kushangazwa na hali hiyo, wakitaka kuhoji, kulikoni, lakini macho makali ya Kipanga yaliwafanya wafyate mkia. Wakakurupuka na kusimama kando huku wakigwaya.



    Mlango uligongwa tena.



    Kipanga akawatazama mara moja wanawake hao na kuwaona wamejikunyata ukutani bila ya kuvaa nguo zao. Hakuwa na muda wa kuwashangaa wala kuzungumza nao chochote kile kwa wakati huo.



    Sasa alikabiliwa na jukumu zito mbele yake, jukunu alilopaswa kulitekeleza kwa umakini wa hali ya juu. Akiwa kifua wazi na bukta ikiwa ndilo vazi pekee mwilini mwake, Kipanga aliikamata vizuri bastola yake kisha akaufuata mlango taratibu na kuushika ufunguo.



    Wazo moja likamjia, kwamba amuulize jinale mgongaji kabla ya kufungua, lakini wazo hilo akaliona la kipuuzi. Kwa vyovyote vile mgongaji anaweza kujitambulisha vyovyote mradi ajue kuwa utambulisho atakaoutumia hautamtia shaka mgongewa. Akaamua, liwalo na liwe, akauzungusha ufunguo mara mbili, kitasa kikaitika. Akakikamata kitasa na kuufungua mlango.



    Kilichotokea mara tu alipoufungua mlango, hakutarajia kama kingekuwa kitendo cha haraka kiasi kile. Teke moja kali la guu la kulia liligota kwenye bastola aliyoishika na kuirusha juu, ikaenda kuanguka kitandani, zaidi ya hatua tatu toka hapo mlangoni. Tandabelua haikuishia hapo, makonde mawili yenye uzito wa kilo nyingi nyuma yake yalitua usoni pake na kuivuruga programu yake yote!



    Kwa kiasi kikubwa alichanganyikiwa, akapepesuka na kurudi nyuma hatua mbili. Hata hivyo, akiwa ni mtu wa mazoezi, na ambaye kashkash za aina hiyo hazikuwa ngeni kwake, hazikumchukua sekunde tano kurudiwa na hali ya kawaida. Na tayari alijua kuwa hisia zake zilikuwa sahihi.



    Akatumia wepesi wake kujibu mapigo kwa kumvurumishia mateke matatu ya mfululizo mvamizi wake, mateke yaliyokumbana na kizuizi kikubwa cha mikono iliyokakamaa toka upande wa pili.



    “Panja!” hatimaye Kipanga alifoka kwa sauti kali, macho kayatoa pima akimtazama Panja.



    Kitambo kifupi kikapita huku mafahali hao wakitazamana huku wakihema kama majogoo ya kuku mtetea mke.



    “Panja… Panja… nitakuua…!” Kipanga alifoka tena, safari hii akivuta hatua moja kumsogelea Panja.



    “Ni bora iwe hivyo,” Panja alijibu kijasiri, naye macho yakiwa yametua usoni pa Kipanga bila ya kupepesa. “Nimefuata kifo changu, pesa zangu au kifo chako. Uelewe hivyo!”



    Kitambo kingine kifupi kikapita bila ya yeyote kati yao kuzungumza chochote. Wakaendelea kutazamana kwa hadhari kubwa, kila mmoja akiwa na mpango wake wa kujihami. Ghafla Panja akamsogelea Kipanga huku akiwa amejiweka sawa tayari kwa mashambulizi. Kipanga akarudi nyuma, si kwa kuhofia chochote bali kwa dhamira ya kujipanga upya.



    Wakati huo pia, Kipanga alishajiwa na wazo la kuipata bastola yake iliyokuwa kitandani, hivyo rudi yake nyuma ilikuwa ya dhamira hiyo. Kwa upande mmoja alikuwa na bahati, kwani hatimaye alikikaribia kitanda, na papohapo akageuka kwa kasi ya ajabu na kuitwaa bastola.



    Lakini kama alifikiria kuwa Panja alikuwa hana silaha yoyote ya kujihami, basi alikuwa amekosea sana. Ndani ya mmoja wa mifuko mingi ya suruali yake kulikuwa na ile bastola yenye risasi tatu, ambayo ilikuwa tayari kwa matumizi.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Panja alipomwona Kipanga akiishika bastola, naye alikuwa mwepesi wa kuichomoa yake. Punde kila mmoja akajikuta akitazamana na bastola ya mwingine.



    Sekunde chache baadaye mshindo mkubwa ukasikika! Panja alianguka chali, risasi moja ikiwa imezama kifuani huku Kipanga akiruka juu na kuangukia kitanda, kichwa chake kikiwa kimefumuliwa na risasi moja kutoka katika bastola ya Kipanga.



    ***************



    INSPEKTA Materu na mwenzake, Sajini Kitowela walishtushwa na mlipuko mkubwa uliotokea ndani ya jengo hilo muda mfupi baada ya kuanza kuelekea katika chumba walichokihitaji. Wakaongeza mwendo, kila mmoja wao akiwa ameishika bastola yake mkononi tayari kwa matumizi.



    Waliimaliza varanda ya kwanza, wakaingia ya pili ambako kulikuwa na chumba walichokifuata. Wakavuta zaidi hatua huku wakichukua hadhari zaidi, macho yao yakisoma namba ya kila chumba mlangoni. Muda mfupi baadaye wakafika kwenye chumba namba 10.



    “Ni hapa,” Kitowela alisema huku wakiwa wamesimama kando ya mlango huo ambao ulikuwa umefunguliwa nusu.

    Wakatazamana kidogo kisha wakakivamia chumba hicho kwa kishindo, bastola zikiwa zimewatangulia.



    “Hee!” Inspekta Materu alibwata kwa mshangao.



    Alikuwa na sababu ya kushangaa. Mbele yao, ndani ya chumba hicho kulikuwa na picha ya kutisha! Picha iliyochefua. Ndiyo, kulikuwa na maiti mbili za wanaume zikivuja damu kwa wingi, moja ikivuja katika tundu kubwa la risasi mgongoni na maiti nyingine ikiwa na sura ya kuogofya zaidi kutokana na kichwa kufumuliwa na ubongo kumwagika kitandani kama uji wa moto.



    Katika pembe moja ya chumba hicho kulikuwa na wanawake wawili waliokuwa tupu kama walivyozaliwa, wakiwa wameikusanya mikono katikati ya miguu na kuwatazama askari hao kwa woga. Chini yao, sakafu ilikuwa imelowa chepechepe na haukuhitajika uchunguzi wa kina kubaini kuwa haja ndogo ziliwatoka kutokana na jakamoyo lililowakumba.



    Inspekta Materu na Sajini Kitowela walitazamana kidogo kisha Materu akasema, “Wamemalizana!”



    “Nd’o maana’ake,” Kitowela aliafiki. Akaongeza, “Huyu si Kipanga, huyu?” Wakati huo macho yake yalikuwa yameikodolea maiti iliyokuwa kitandani.



    “Ni mwenyewe,” Materu alijibu



    “Na huyu?”



    Materu akaigeukia maiti nyingine na kuitazama kwa makini kisha akajibu kwa upole, “Atakuwa ni jambazi mwenzie. Huenda walidhulumiana ndiyo wakaamua kufanyiziana.”



    “Na huenda wote ndiyo waliohusika na tukio la kule Kibaha,” Kitowela aliongeza.



    “Inawezekana,” Inspekta Materu aliafiki. Akaongeza, “Nadhani sasa piga simu kituoni, askari waje wakazichukue maiti hizi.”



    Mara Sajini Kitowela aliwageukia wale wanawake. “Na hawa wanawake vipi?”



    “Hawa si unajua tena, walikuwa kiofisi zaidi,” Inspekta Materu alisema huku akitabasamu kwa mbali. “Hawana chochote. Tuwape nafasi wavae, waende zao. Lakini…” akasita kidogo.



    “Vipi?” Kitowela akauliza.



    “Hebu leta begi lile,” Materu alisema huku akiliangalia begi lililokuwa kando ya kitanda.



    Kitowela alilitwaa na kulifungua. Mafungu ya pesa yakajidhihirisha pamoja na nguo chache, dawa ya meno na mswaki.



    “Twende nalo kituoni,” Materu alimwambia. Kisha akawageukia wale wanawake na kuwaambia, “Dakika mbili zitawatosha kwa kuvaa na kupotea malaya wakubwa.”



    Wakati Inspekta Materu na Sajini Kitowela wakiondoka, Inspekta Materu alikuwa akizungumza kwa simu, akitoa agizo kwa askari wa vitengo vingine waje kutekeleza majukumu yao.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    *****MWISHO*****MWISHO*****MWISHO*****



0 comments:

Post a Comment

Blog