IMEANDIKWA NA : NYEMO CHILONGANI
*********************************************************************************
Simulizi: Let's Call It A Night
Sehemu Ya Kwanza (1)
Leo ninaianza hadithi hii mpya ambayo nina uhakika itakwenda kukuhuzunisha, kukufurahisha, waliokata tamaa, watajazwa nguvu na hata wale wasiokuwa na matumaini, watapata matumaini mapya.
Ni hadithi ndefu mno ila kamwe haitoweza kukuchosha, kila utakaposoma, utatamani kujua kile kinachofuata siku ijayo. Kuwa nami, kwani pamoja na kukuhuzunisha huko, mwisho wa siku, kuna vingi utavifurahia na kufarijika.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ANZA NAYO....!!!
Dar es Salaam, 2013
Saa 12.30 asubuhi, alamu ya simu ilikuwa ikilia kwa sauti kubwa, Henry akaamka kutoka usingizini, mwili wake ulikuwa na uchovu mwingi huku macho yake yakiwa mazito. Akainuka kitandani pale na kujinyoosha kiuchovu na kisha kuteremka kitandani pale.
Huku akionekana kuwa na uchovu mwingi, Henry akaanza kupiga hatua kuelekea bafuni kuoga. Kwa wakati huo, kichwa chake kilikuwa na mawazo mengi juu ya kazi aliyokuwa akiifanya, kazi ya uandishi wa habari ambayo ilimpa heshima kubwa nchini Tanzania.
Alikuwa mwandishi wa magazeti yanayotolewa na Kampuni ya Amazon Newspapers iliyokuwa Kinondoni Jijini Dar es Salaam. Henry alikuwa amejiwekea heshima kubwa kutokana na kazi hiyo aliyokuwa akiifanya.
Kila siku jina lake lilikuwa likisikika midomoni mwa watu kwamba alikuwa mwandishi bora asiyekuwa na mpinzani nchini Tanzania. Kazi zake, alikuwa akiziandika kwa ufasaha katika mtiririko ambao ulipendwa na kila mtu.
Mbali na uandishi wa magazetini, Henry alikuwa mwandishi wa vitabu vya Riwaya. Katika maisha yake, aliwahi kutoa vitabu vingi vya Riwaya vilivyotikisa sana Afrika Mashariki.
Uandishi wake wa vitabu ukampa fedha nyingi, akafungua biashara lakini kila siku, hakutaka kuacha kazi katika kampuni hiyo iliyokuwa imempa heshima kubwa, Kampuni ya Amazon Newspapers.
Mbali na mafanikio makubwa aliyokuwa nayo, Henry hakuwa ameoa. Mpaka kipindi hiki alikuwa amefikisha miaka ishirini na tano lakini kichwani mwake hakuwa na ndoto za kuoa kabisa.
Alipenda kuishi peke yake kwani alijua kwamba endapo angekuwa na mke, basi kazi zake za kuandika simulizi na kufanya kazi za kampuni zingeshuka na hivyo jina lake kupotea.
Mpaka muda huo, Henry alikuwa ameandika vitabu vya maisha ya watu wengi maarufu wakiwepo wanasiasa, wanamuziki, wanamichezo, wachungaji na watu wengine wengi maarufu.
Vitabu vyote ambavyo alikuwa ameviandika, vilinunuliwa mno kitu kilichoendelea kumpa fedha na heshima kubwa. Waandishi wadogo ambao walikuwa wakichipukia, walikuwa wakimtafuta kwa ajili ya kuwashauri juu ya kipi kilichotakiwa kufanyika ili nao wawe waandishi wazuri kama alivyokuwa.
“Soma sana vitabu, pia jitoe katika kila kitu kuhusiana na uandishi. Mbali na hivyo, jitahidi uwe mtafiti ili ujue mengi katika dunia hii,” alisema Henry mbele ya wanachuo wa Chuo cha Uandishi wa Habari cha DSJ ambao wengi wao walikuwa wakitamani kuwa mwandishi kama alivyokuwa yeye.
“Mbali na mafanikio yako, kuna changamoto gani ambazo uliwahi kukutana nazo kabla?” aliuliza mwanachuo mmoja.
“Kuna mengi ambayo unakutana nayo kama mwandishi, wakati mwingine unachukiwa kwa kile unachokiandika, waandishi wenzako wa vitabu wataanzisha manenomaneno kwamba simulizi zako si nzuri, zote hizo tunaziita changamoto ambapo mara baada ya kuzisikia, hautakiwi kurudi nyuma, songa mbele zaidi,” alisema Henry.
Siku hiyo alikuwa akiongea maneno mengi kwa waandishi hao, alionekana kuwa mtu wa busara kwani kila swali ambalo alikuwa akiulizwa, majibu yake yalikuwa ni ya kujitosheleza sana.
Henry akaonekana kuwa ‘genius’ japokuwa katika historia ya maisha yake hakuwa na akili nyingi darasani. Wanachuo wengi wakatamani kuwa kama yeye, mafanikio yake yakawafanya waandishi wengi kuona kwamba inawezekana endapo tu utaamua kujituma kwa nguvu zote.
Siku hiyo, Henry alionekana kuwa mhamasishaji mkubwa ambaye aliwatia moyo waandishi wale, mpaka anaaga, bado wanachuo walitamani kuendelea kumsikiliza kwani kila neno alilokuwa akiliongea lilionekana kuwa msaada mkubwa kwao.
Henry akaingia ndani ya gari lake la kifahari aina ya V8 na kuondoka mahali hapo kurudi ofisini. Njiani, mawazo yake yalikuwa juu ya maisha yake ya nyuma, alikuwa kwenye maisha ya kimasikini mno kiasi kwamba wakati mwingine hakuwa akiamini kama kweli yeye ndiye aliyekuwa na mafanikio hayo aliyokuwa nayo.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nimetoka mbali sana.” alisema Henry huku akionekana kuwa kwenye hali ya mawazo.
Huku akiwa amefika Magomeni Mikumi, kwenye foleni kuelekea nyumbani kwake Mikocheni B, simu yake ikaanza kuita, alipokiangalia kioo, alikuwa msichana Husna, mfanyakazi wake wa ndani ambaye alikuwa akimthamini kama ndugu yake. Akaichukua simu ile na kuipokea.
“Kuna mgeni anakusubiri,” alisikika Husna.
“Ni nani?” aliuliza Henry.
“Maimartha Paul,” alijibu Husna.
“Kwa nini asingenipigia simu?”
“Anasema alikupigia lakini hakukupata.”
“Sawa, mwambie nakuja, nilikuwa naongea na wanachuo, nipo Magomeni,” alisema Henry na kukata simu.
Maimartha Paul alikuwa mwimbaji wa nyimbo za Injili aliyekuwa akivuma sana kipindi hicho. Kupitia nyimbo zake za Injili, alikuwa amejijengea jina kubwa lililompa heshima kila sehemu aliyokuwa akienda.
Watu walimfahamu kama mwimbaji ambaye kila alipokuwa akiimba uwepo wa Mungu ulikuwa ukionekana mahali hapo. Nyimbo zake zilionekana kuwa na upako kwani kila alipokuwa akiimba, mapepo yalikuwa yakiwatoka watu, wagonjwa walikuwa wakipona magonjwa yao.
Kupitia nyimbo zake, Maimartha alikuwa amejijengea jina kubwa, kila siku aliendelea kujitengenezea fedha kupitia albamu alizokuwa akizitoa ambazo zilinunuliwa kwa kugombaniwa sana.
Japokuwa Maimartha alikuwa akisali katika Kanisa la Praise And Worship lililopo Bamaga, Mwenge jijini Dar es Salaam lakini ulikuwa umepita mwezi wa nne hakuwa amesali katika kanisa hilo, kila Jumapili alikuwa akialikwa katika makanisa mengine kwa ajili ya kumuimbia Mungu tu.
Baada ya kuishi katika maisha ya mafanikio kwa muda mrefu, Maimartha alifuatwa na Henry na kuambiwa kwamba alitakiwa kuyaweka maisha yake wazi, mbele ya watu ili wapate kuyafahamu kwani kuna wengi kupitia maisha hayo wangeweza kubadilika na kufanikiwa.
Kwa mara ya kwanza, Maimartha alikuwa mgumu kukubali lakini kutokana na kusisitiziwa umuhimu wa kuyaweka maisha yake wazi kupitia vitabu, mwisho wa siku akakubaliana na Henry hivyo kupanga siku ya kuonana.
Siku hiyo alikuwa amekwenda nyumbani kwa Henry, alijaribu kumtafuta simuni lakini hakuwa akipatikana. Hakutaka kubaki nyumbani, alitaka kuonana na Henry uso kwa uso ili aweze kumhadithia maisha yake yaliyopita na hatimae ayaweke kwenye kitabu chake na watu waweze kuyasoma.
“Samahani kwa kuchelewa,” alisema Henry mara baada ya kuingia ndani ya nyumba yake, Maimartha alikuwa kochini.
“Usijali. Sikukupa taarifa ndiyo maana imekuwa hivi,” alisema Maimartha.
Baada ya maongezi machache, Henry akaelekea chumbani, akaoga na kisha kurudi sebuleni hapo kwa ajili ya kuongea na msichana huyo, muimbaji wa nyimbo za Injili.
Mara baada ya kufika sebuleni, Henry akatulia kochini na kuanza kumwangalia Maimartha. Alionekana kuwa msichana mrembo mno ambaye kwa kumwangalia tu, lisingekuwa jambo gumu kugundua kwamba msichana huyo alikuwa amepitia mambo mengi maishani mwake.
Mavazi aliyokuwa amevaa, yalikuwa ni ya heshima kubwa, nywele zake hakuwa amezisuka, aliziweka katika mtindo wa ‘afro’ huku uso wake ukiwa umependezeshwa na miwani yenye rangi nyeusi.
Mbali na hayo yote, msichana huyo alikuwa na mvuto mkubwa, kila wakati alionekana kuwa mtu mwenye furaha japokuwa katika maisha yake alipitia shida nyingi zilizomkatisha tamaa hata wakati mwingine kutamani kujiua.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kila alipokuwa akicheka au kutabasamu, vishimo viwili vilikuwa vikionekana mashavuni mwake huku kidoti cheusi kikiwa karibu kabisa na mdomo wake. Kwa kifupi, Maimartha alivutia kupita kawaida.
“Nahisi umekuja tuzungumze zaidi kuhusu kitabu chako,” alisema Henry.
“Ningependa kiandikwe, ila naona kama kitanichafua,” alisema Maimartha, hata sura yake tu ilionekana kuhofia kile alichokuwa akitaka kukifanya Henry.
“Kitakuchafua vipi sasa?”
“Unajua mimi ni mwanamuziki wa Injili, sasa mtu asome kwamba ulikuwa na mahusiano na fulani kipindi cha nyuma, huoni kama kitanichafua?” alisema Maimartha na kuuliza.
“Hapana, hakuna kitu kama hicho, kupitia maisha yako nadhani kuna wengi watakwenda kujifunza, wengi watafarijika na wengi watapata nguvu ya kusonga mbele, cha msingi, yaweke wazi kwa ajili ya kuwasaidia wengine,” alisema Henry kwa sauti ya upole kama kawaida yake.
Maimartha akashusha pumzi ndefu na nzito, aliyokuwa ameyaongea Henry yalikuwa maneno ya kweli lakini bado moyo wake ulikuwa ukiogopa. Aliyajua maisha yake ya nyuma, yalikuwa maisha mabovu mno ambayo hakupenda mtu yeyote ayafahamu kwani aliamini kwamba yangemchafua sana.
“Ninaogopa,” alisema Maimartha.
“Nchi yetu ina masikini wengi, kuna watu wengi waliokata tamaa na pia kuna watu wengi sana ambao hawajamjua Mungu, je hautaki kuwaona watu masikini wakifarijika kwa kuamini kwamba kuna siku nao watakuja kuwa matajiri? Je hautaki kuwaona watu waliokata tamaa wakitiwa nguvu na kusonga mbele? Je hautakiwa kuona wale watu ambao maisha yao hayamjui Mungu waje kumjua? Hebu jifikirie ni kwa kiasi gani utakwenda kuwabadilisha wengi,” alisema Henry, katika kuongea, mara nyingi alionekana kuwa mtu mwenye busara kubwa.
“Maneno yako yananipa nguvu ya kukubaliana nawe, ila naomba nijifikirie juu ya hilo,” alisema Maimartha.
“Maimartha, yaani kipindi chote hicho bado tu haukujifikiria? Umetoka nyumbani kwako mpaka hapa kwangu kwa ajili ya kuanza kazi, bado tu unahitaji muda zaidi wa kujifikiria?” aliuliza Henry kwa sauti ya chini.
“Usijali Henry, nitakwambia tu,” alisema Miamatha.
Henry akashusha pumzi ndefu, maneno aliyoyaongea Maimartha yalimkasirisha lakini hakuwa na jinsi, kwa sababu yeye ndiye alikuwa na uhitaji wa kufanya kazi na mwanamuziki huyo, akakubaliana naye.
Kila siku Henry alikuwa akimsumbua mwanamuziki huyo kwamba ilikuwa ni lazima akiandike kitabu hicho kwa ajili ya kuwafundisha Watanzania mambo mengi, bado Maimartha alikuwa akikataa huku akisisitiza kwamba alikuwa akiogopa kuchafuliwa.
Henry hakutaka kukata tamaa, katika kipindi hicho, mtu pekee ambaye alikuwa akihitaji kuandika historia ya maisha yake alikuwa ni mwanamuziki huyo wa Injili ambaye alikuwa akivuma sana, Maimartha Paul.
Mara kwa mara alikuwa akielekea katika kila kanisa ambalo Maimartha alipokuwa akiabudu na kuanza kuongea naye, huko, aliendelea kumsisitizia kwamba alikuwa akitaka kuandika kitabu cha maisha yake lakini bado Maimartha alikuwa akikataa, sababu kubwa ilikuwa ni kuogopa kujichafua.
“Nina uhakika jina lako halitochafuka bali maisha yako yatakwenda kuwafundisha watu mambo mengi mno,” alisema Henry lakini Maimartha hakutaka kukubaliana naye.
Henry hakujua afanye nini, alijitahidi sana kumwambia msichana huyo juu ya kumwandikia kitabu hicho lakini bado aliendelea kukataa. Kila siku akawa mtu wa mawazo tu, kila alipokuwa akimuona Maimartha katika magazeti, televisheni, alikuwa akijisemea kwamba kuna siku angeweza kuandika kitabu cha maisha ya msichana huyo.
Kila siku ilikuwa ni lazima Henry ampigie simu Maimartha na kuendelea kumuomba kumpa nafasi ya kukiandika kitabu hicho ambacho kilionekana kusubiriwa sana na Watanzania.
Maimartha hakuwa mwepesi kukubaliana naye, bado alikuwa akiendelea kusisitiza kwamba hakutaka jina lake lichafuliwe kwani alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakijiheshimu sana.
“Maimartha....” Henry aliita simuni kwa sauti ya kubembeleza.
“Nakusikiliza.”
“Naomba unikubalie niandae kitabu chako, Watanzania wanatamani kusikia mengi kuhusu wewe, mbali na hiyo, utakwenda kuvuna fedha nyingi mno, zaidi ya milioni mia tano, hauoni hiyo kama ni faida kwako?” alisema Henry na kuuliza.
“Milioni mia tano kuingia zinaweza kuingia, ila kuchafuliwa kwa jina ni vibaya zaidi ya kupokea kiasi hicho cha fedha,” alisema Maimartha.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hapana. Nakuhakikishia kwamba jina lako halitoweza kuchafuka,” alisema Henry.
“Haiwezekani Henry, siwezi,” alisema Maimartha na kukata simu.
Henry akabaki na mawazo mengi, ni kweli alikuwa ameandika vitabu vya watu wengi katika maisha yake, watu walimheshimu kwa kazi kubwa aliyokuwa ameifanya, kufanya kazi ya kuandika kitabu cha maisha ya Maimartha, ilionekana kuwa nafasi kubwa zaidi ya kujitangaza na kujizolea sifa.
Maisha ya Maimartha yaliendelea kila siku, kitu ambacho kilikuwa kikimuumiza kichwa kila siku kilikuwa ni kuhusu kuandikiwa kitabu cha maisha yake na Henry. Aliyajua maisha yake yaliyopita, hayakuwa na ushuhuda mzuri, alihofia kwamba inawezekana katika kipindi ambacho angeamua kuyaweka wazi maisha yake ya nyuma basi angeweza kuchafuka na hatimae kuonekana kama Shetani.
Bado aliendelea kusisitiza kwamba kuyaweka wazi maisha yake kitabuni lilikuwa suala gumu kufanyika, kitu alichokuwa akikitaka ni kuona maisha yake ya nyuma kuwa katika ulimwengu wa giza tu.
“Nilimkosea sana Mungu, haiwezekani kuyaweka maisha yangu kitabuni,” alijisemea Maimartha.
Siku ziliendelea kukatika, kwa takribani miezi sita, bado Henry alikuwa akiendelea kumsisitizia Maimartha kwamba alitaka kuandika kitabu cha maisha yake lakini msichana huyo alikuwa akikataa. Hilo lilimuumiza sana Henry, hakutegemea kupata ugumu kama aliokuwa akiupata kipindi hicho.
“Sasa nifanye nini? Mungu, zungumza na Maimartha ili akubali niandike kitabu cha maisha yake,” alisema Henry huku akiangalia juu, kwake, kitendo kile kilikuwa kama kumtazama Mungu kule alipokuwa.
Mara baada ya kuona tangazo kwamba kitabu cha Maimartha kingekuwa mitaani mwaka huo, Watanzania wakajiandaa kwa ajili ya kukisoma kitabu hicho. Japokuwa Maimartha hakuwa amekubaliana na Henry kuandika kitabu cha maisha yake lakini Henry aliamua kuliweka tangazo hilo gazetini ili mradi amuoneshea Maimartha ni kwa kiasi gani maisha yake ya nyuma yangeweza kuwabadilisha watu wengi.
Kila siku ilikuwa ni lazima aendelee kumwambia Maimartha kwamba alitaka kuandika kitabu cha maisha yake lakini msichana huyo alikuwa akikataa.
Alichokifanya Henry, akaanza kuwatumia wachungaji mbalimbali waweze kumuombea apate ruhusa ya kuandika kitabu hicho lakini hiyo wala haikusaidia, bado Maimartha alikuwa akikataa tu.
“Amekataa,” alisema mchungaji Michael Kipute.
“Daah! Nina hamu sana ya kuandika kitabu chake, sasa nitafanyaje?” aliuliza Henry.
“Cha msingi mtafute askofu mkuu, Lutengano, anaweza kukusaidia,” alisema mchungaji Kipute.
Henry akapata kazi nyingine tena ya kumtafuta askofu Lutengano. Katika kipindi hicho, askofu huyo hakuwa nchini Tanzania, alikuwa safarini nchini Uholanzi hivyo Henry alitakiwa kusubiri.
Hiyo wala haikuwa tatizo, wakati akiwa anamsubiri Askofu huyo, huku alikuwa akiendelea kumuomba Maimartha kumwandikia kitabu cha maisha yake, bado muimbaji huyo wa Injili alikuwa akikataa.
Henry akaonekana kuchoka kwani alitumia kila njia ili afanikishe lengo lake alilokuwa ameliweka, kitu alichokiona kwamba kingekuwa na busara ni kumsubiria Askofu Lutengano ili aongee na Maimartha na hatimae amruhusu kuandika kitabu kile.
Baada ya wiki mbili, Askofu Lutengano akarudi nchini Tanzania. Henry hakutaka kuchelewa, alichokifanya ni kumfuata ofisini kwake ambapo huko akakaa na kuanza kuzungumza naye.
“Ninatamani niandike kitabu chake, ila anakataa kunipa ushirikiano,” alisema Henry.
“Unataka nikusaidie nini Henry?” aliuliza Askofu Lutengano.
“Naomba uongee naye, nahisi anaweza kukubali,” alisema Henry.
“Hakuna tatizo, nitaongea naye, ila naomba usimchafue,” alisema askofu.
“Hakuna tatizo, sitoongeza kitu, nitaandika kile atakachoniambia tu,” alisema Henry.
“Basi hakuna tatizo.”
Kidogo, Henry akapata ahueni kwa kuona kwamba askofu angefanikisha kile alichokuwa amemwambia, alichotakiwa kukifanya wakati huo ni kusubiria tu. Kila siku alikuwa akimsikilizia askofu Lutengano ili ampa taarifa juu ya kilichokuwa kikiendelea, naye alikuwa kimya.
Wiki ya kwanza ikakatika, wiki ya pili ikaingia na mwisho wa siku mwezi kukatika, hakupokea simu yoyote kutoka kwa askofu kitu kilichomfanya kumpigia simu ili ajue kipi kiliendelea.
“Nilisahau kumwambia,” alisema askofu Lutengano.
“Ulisahau kumwambia?, Daah! Mbona hili suala linakuwa gumu sana?”
“Usijali, nitaongea naye kesho, nimemualika kanisani kwangu,” alisema askofu Lutengano.
Siku iliyofuata ambayo ilikuwa ni Jumapili, Maimartha akaenda kusali katika Kanisa la Praise And Worship la askofu Lutengano lililokuwa Mikocheni A kwa ajili ya kumsifu Mungu kanisa hapo.
Askofu hakutaka kusahau, alipomuona Maimartha tu, akakumbuka kile alichokuwa ameambiwa na Henry, hivyo alitakiwa kuongea na msichana huyo siku hiyo.
“Kiukweli haitowezekana,” alisema Maimartha.
“Kwa nini?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Baba askofu, ninaogopa kuchafuliwa, maisha yangu ya nyuma yanatisha sana,” alisema Maimartha.
“Yaliyopita yamepita Maimartha, hata kama uliua, baada ya kumpa Yesu maisha yako, kila kitu kimepita na tazama yamekuwa mapya,” alisema askofu Lutengano.
“Najua baba askofu, ningependa kila kitu katika maisha yangu kiwe kwenye usiku wa giza, huwa sipendi kukumbuka kuhusu maisha yangu yaliyopita,” alisema Maimartha.
“Yesu atakutia nguvu, naomba ufanye kile Watanzania wanachotaka ukifanye, naamini utakwenda kubaddilisha maisha ya watu wengi,” alisema askofu Lutengano.
Maimartha akawa mtu mwenye mawazo, kichwa chake kilikuwa kikifikiria kuhusu kitabu cha historia ya maisha yake ambacho alitakiwa kumuhadithia Henry ili akiandike na kuanza kukiuza nchini Tanzania.
Kwake lilionekana kuwa jambo gumu lakini kwa sababu askofu Lutengano alikuwa ameingiza mkono wake, Maimartha akajikuta akianza kulegeza msimamo wake na hivyo kumpigia simu henry kumwambia kwamba alikuwa amekubali.
“Asante Yesu, hatimae umekubali baada ya mwaka kupita,” alissema Henry huku akionekana kuwa mwenye furaha tele.
“Kwa hiyo unataka nije kwako lini?”
“Hata sasa hivi.”
“Una muda?”
“Wa kumwaga tu,” alisema Henry.
“Ndani ya nusu saa nitakuwa hapo,” alisema Maimartha na kukata simu.
Henry akaruka juu kwa furaha, hakuamini kile alichokuwa amekisikia, alisota kwa takribani mwaka mmoja akimtaka Maimartha akubali kumwandikia kitabu cha maisha yake, alikuwa amekataa kwa kipindi kirefu lakini mwisho wa siku, alikuwa amekubali.
Shukrani zake zote zikaenda kwa askofu Lutengano kwani aliamini kwamba huyo ndiye alikuwa mtu pekee aliyekuwa amefanikisha jambo hilo, alichokifanya ni kumpigia simu na kuanza kumshukuru.
“Nashukuru sana baba askofu, Mungu akubariki,” alisema Henry.
“Usijali, amani ya Bwana ikutawale.”
“Amen,” alisema Henry na kukata simu.
Muda mwingi macho yake yalikuwa kwenye simu yake ya mkononi, mtu ambaye alikuwa akimsubiria kwa wakati huo alikuwa Maimartha tu. Muda wote moyo wake ulikuwa na kimuemue cha kuwapigia simu waandishi wenzake na kuwapa taarifa kwamba hatimae Maimartha alikuwa amekubali kuandikiwa kitabu cha maisha yake.
Alipotaka kufanya hivyo, akasita, akataka mpaka kuona kipindi atakapoanza kuandika kitabu cha maisha ya msichana huyo ndipo hapo ambapo angewapigia simu waandishi wenzake na kuwaambia.
Simu ilikatwa saa 10:36 jioni, mpaka inafika saa 12:23 jioni, Maimartha hakuwa amefika mahali hapo.
“Mmh!” mbona kachelewa hivyo?” alijiuliza Henry lakini hakupata jibu. Bado alikuwa na presha kubwa ya kumuhoji mwanamuziki huyo wa Injili.
Maimartha alikuwa akiendesha gari kwa mwendo wa kawaida, kichwa chake kilikuwa na mawazo mengi kuhusiana na kitabu cha maisha yake alichokuwa akitaka kukiandika Henry. Moyo wake ulikuwa umegawanyika mara mbili, upande mmoja ulimwambia kwamba alikuwa akienda kujichafua lakini upande mwingine ulimwambia kwamba alikuwa akienda kuwasaidia watu wengine.
Kitu alichokuwa amekiamua ni kuyaweka maisha yake hadharani tu. Ushawishi mkubwa alioupata kutoka kwa askofu Lutengano ulimfanya kuamini kwamba asingeweza kujichafua zaidi ya kuwasaidia wengine.
Hakufikiria fedha, alijua kwamba endapo angeuza kitabu hicho angepata sana fedha nyingi lakini suala hilo hakutaka kulifikiria kichwani mwake, Kile alichokuwa akikifikiria ni maisha yake na maisha ya Watanzania ambao wengi wanaishi katika maisha ya kimasikini.
Barabarani hakukuwa na foleni hivyo ilimuwia urahisi kutoka Tabata kwenda Mikocheni B ila alipofika Ubungo, foleni kubwa ilikuwa mahali hapo.
Hapo ndipo alipopatumia kuendelea kufikiria zaidi. Kichwa chake kilifikiria kila kitu alichokuwa akitakiwa kukifanya. Alipitia katika maisha ya tabu, yaliyojaa msisimko ambayo hakuamini kama yangekwenda kuwafundisha watu zaidi ya kujichafua yeye mwenyewe.
Moyo wake ulikuwa mgumu kukubaliana na suala hilo lakini mwisho wa siku alijikuta akikubaliana na Henry. Alimfahamu kama mwandishi bora ambaye kila siku kazi zake zilikuwa zikisifiwa kila kona. Vitabu vyote ambavyo alikuwa ameviandika mwandishi huyo, vilikuwa katika kabati lake la vitabu, alipenda kila kitu, uandishi wa Henry ulimfurahisha mno.
Leo hii ilikuwa zamu yake, ukiachana na wale wasanii na wanasiasa, zamu yake ilikuwa imefika. Alichokifanya, hata kabla magari hayajaruhusiwa, akachukua simu yake na kumtumia meseji Henry.
“Unajua kwamba sina mtoto?” aliuliza Maimartha katika meseji hiyo, wala hazikupita sekunde nyingi, ikajibiwa.
“Ninajua, kuna nini?” meseji ya Henry ilisomeka.
“Nitakuhadithia mengi tu, nipo hapa Ubungo, foleni kubwa ila baada ya dakika kadhaa nitafika hapo,” aliandika Maimartha.
Wala hazikupita dakika nyingi, magari yakaruhusiwa na foleni ile kuanza kusogea tena. Gari lake ndilo lilikuwa ka mwisha kabisa katika msururu wa foleni ile.
Huku akiwa na mawazo mengi, ghafla kwa mbali akaanza kusikia honi nyuma yake, wala hakutaka kujali sana kwani ni mara nyingi magari hasa ya madereva waliokuwa na haraka walikuwa wakipiga sana honi hata kama kulikuwa na foleni.
Maimartha akapuuzia, alipoona honi zikizidi kusikika tena kadri muda ulivyokwenda zikiwa kwa ukaribu zaidi, akageuka nyuma kuangalia kuna nini, macho yake yakatua katika gari kubwa, gari la mafuta kutoka Ecom ambalo lilikuwa likija kwa kasi hali iliyoonesha kwamba lilikuwa limekatika breki.
Hata kabla hajajua afanye nini, gari lile likalifikia gari lake, likaligonga kwa nyuma, kwa sababu hakuwa amefunga mkanda, akajikuta akikipigiza kichwa chake katika kioo cha mbele cha gari lile, kioo kikapasuka, mwili wake, kuanzia miguuni hadi kiunoni ulikuwa ndani ya gari na kuanzia kiunoni kwenda juu ulikuwa nje, juu ya boneti la mbele la gari yake.
Ilikuwa ni ajali mbaya mno, watu waliokuwa pembeni wakashika vichwa vya, damu zilikuwa zimetapakaa kila sehemu hasa juu ya gari lile. Kichwa cha Maimartha kilikuwa kimepasuka na kufanya damu kutoka kwa kiasi kikubwa.
Watu waliokuwa pembeni mwa barabara ile, kwa haraka wakasogea na kuanza kumtoa pale kwenye boneti, wakamuingiza ndani ya gari la msamaria mwema, canter na kuanza kuondoka ahali hapo.
Mwili wake ulitisha, japokuwa alikuwa supastaa, lakini kwa jinsi alivyokuwa hakukuwa na mtu yeyote yule aliyeweza kumtambua kwani kichwa chake kilijaa damu zilizotapakaa mpaka usoni mwake.
Maimartha alikuwa akitetemeka tu mule garini kama mtu ambaye angekata roho muda wowote ule. Ukiachana na damu zilizokuwa zikitoka kichwani mwake kutokana na kupasuka kwa kiasi kikubwa, mdomoni mwake alikuwa akitokwa na machozi.
Garini, damu zilikuwa zimetapakaa kila sehemu huku nyingine zikiendelea kutoka. Kutetemeka mwili hakukuacha, bado aliendelea kuwa kwenye hali ileile, alionekana kubakiwa na sekunde chache za kuvuta pumzi ya dunia hii.
“Mmmh! Hii noma,” alisema jamaa mmoja aliyekuwa ndani ya hiyo gari hilo lililoanza kuendeshwa kwa mwendo wa kasi kama ambulance kuwahi hospitali.
“Kama atapona, yampasa kumshukuru Mungu maisha yake yote,” alisema jamaa mwingine huku akiuweka mwili wa Maimartha vizuri garini mule. Hakukuwa na mtu aliyejua kwamba msichana yule aliyekuwa amepata ajali alikuwa Maimartha, muimba nyimbo za Injili ambaye alikuwa akitamba na albamu yake iitwayo Hapana Rafiki Kama Yesu.
***CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Henry bado alikuwa akiisubiria simu kutoka kwa Maimartha, moyoni alikuwa na presha kubwa ya kutaka kufanya kazi na muimbaji huyo wa Injili kwa kuamini kwamba angelifanya jina lake kuwa kubwa zaidi.
Kila wakati alikuwa akiiangalia simu yake, alikuwa akitaka kuona Maimartha akipiga simu na kumwambia kwamba amekaribia kufika hivyo aache geti wazi. Sekunde zikasogea, dakika zikasonga lakini hakukuwa na simu yoyote ile iliyoingia kutoka kwa Maimartha.
Haikuwa kawaida, alimfahamu vizuri msichana huyo, kila alipokuwa na miadi ya kuonana naye, alikuwa akimuahidi huku kila wakati akimtumia meseji kumpa taarifa kwamba alikuwa amefikia wapi, siku hiyo hali ilionekana kuwa tofauti.
“Amepatwa na nini? Hii si kawaida yake,” alisema Henry.
Hakutaka kuvumilia zaidi, alichokifanya ni kuanza kumpigia simu msichana huyo. Simu ikaanza kuita, kadiri ilivyokuwa ikiita ndivyo alivyokuwa akijipa uhakika kwamba ingepokelewa, iliita zaidi na zaidi, haikupokelewa mpaka ikakatika.
Hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza, akajaribu kupiga tena mara ya pili, kama ilivyokuwa mwanzo ndivyo ilivyokuwa tena, simu ilianza kuita, iliita zaidi na zaidi lakini matokeo yalikuwa ni yaleyale, simu haikupokelewa.
Masaa yalizidi kwenda mbele, mpaka inaingia saa mbili usiku, simu haikuwa ikipokelewa, mwisho wa siku, haikupatikana kabisa. Henry akachukia, kwake ulionekana kama usumbufu, mtu kumwambia kwamba aje, akubaliane naye na mwisho wa siku kutokupatikana simuni, kumlimkasirisha.
“Hawa watu wengine mpaka wanakera, yaani tumekubaliana aje, akasema anakuja, amechelewa, nampigia simu, hapokei, mwisho wa siku kaizima kabisa hiyo simu, huu ni ujinga, kuanzia leo, simtafuti tena, asijifanye yeye ni supastaa zaidi ya raisi,” alisema Henry kwa hasira.
Mpaka usiku mwingi unaingia, bado Henry aliendelea kuwa na hasira, akajikuta akianza kumchukia Maimartha kwa kile alichomfanyia, hakutaka tena kusikia kitu chochote kutoka kwa msichana yule, kitendo kile alichokifanya siku ile kilimkera kupita kawaida.
Kutokupokea simu kwa msichana huyo kulimuoneshea kwamba alikuwa na maringo mengi, akaachana naye, akajilaza kitandani, moyo wake bado ulikuwa na hasira mno, kila wakati alikuwa akiyauma meno yake, hakuamini kama Maimartha alikuwa amemfanyia kile alichomfanyia.
“Yaani ananichomesha mahindi, huu ni ujinga, ngoja kesho akinipigia simu, atajuta kuzaliwa, nitampa makavu live,” alisema Henry kwa hasira na kulala huku bado moyo wake ukiendelea kuwa na hasira tele.
Habari za mitandaoni ndizo zilizomshtua, hakuamini kile alichokuwa akikisoma kwamba muimbaji wa Injili, Maimartha Paul alikuwa amepata ajali mbaya alipokuwa Ubungo. Kwanza akashtuka, usingizi na uchovu wote aliokuwa nao ukapaa, hakuamini kile alichokuwa amekisoma.
Picha ambazo zilionekana katika mtandao ule zilimsikitisha, ghafla, hasira zote alizokuwa nazo juu ya Maimartha zikapotea na huruma kuanza kumuingia.
Alichokifanya ni kuinuka kutoka kitandani, akaelekea bafuni kuoga na kwa harakaharaka akaanza kuvaa nguo zake, kitu alichokitaka kwa wakati huo ni kuelekea katika Hospitali ya Muhimbili kwa ajili ya kumuona Maimartha tu.
“Mimi ndiye nimeyataka,” alisema Henry, aliona kwamba yeye ndiye aliyesababisha hayo yote, pasipo kumuita nyumbani kwake kwa ajili ya kufanya naye mahojiano kuhusu kitabu chake basi asingepata ajali aliyokuwa ameipata.
Mara baada ya kumaliza kujiandaa, Henry akatoka nje ambako akachukua gari lake na kuanza safari ya kuelekea hospitali. Njiani, Henry alikuwa na mawazo mengi, kichwa chake kilikuwa kikimfikiria Maimartha tu, alijiona kuwa yeye ndiye chanzo cha ajali hiyo kitu ambacho kilimuumiza mno.
Kwa sababu hakukuwa na foleni kubwa, wala kufika hospitalini hapo hakuchukua muda mrefu. Kwa sababu haukuwa muda wa kuona wagonjwa, Henry akaonesha kitambulisho chake cha kazi, akaruhusiwa kuingia.
Akaelekea sehemu ya maegesho na kuliegesha gari lake. Kwa sababu hakuwa akifahamu ni sehemu gani alipokuwa amelazwa Maimartha, akamfuata nesi mmoja aliyekuwa akipita karibu yake na kuanza kumuuliza.
“Samahani dada yangu, jana usiku kulitokea ajali maeneo ya Ubungo, msanii wa Injili aligongwa na gari na kuletwa hapa, yupo wodi gani?” aliuliza Henry huku machozi yakianza kumlenga.
“Sina uhakika, ila nenda kule katika Wodi ya Mwaisela,” alisema nesi yule.
“Nashukuru.”
Henry akaondoka mahali hapo na kuanza kuelekea katika Wodi ya Mwaisela. Mwendo wake ulikuwa ni wa harakaharaka, bado kichwa chake kilikuwa kikimfikiria Maimartha, kwake, kila hatua aliyokuwa akipiga alijiona kwamba yeye ndiye aliyesababisha Maimartha kupata ajali ile mbaya.
“Dada samahani,” alisema Henry, alikuwa amemsimamisha nesi.
“Bila samahani.”
“Ninamuulizia Maimartha, alipata ajali jana.”
“Umeambiwa uje huku Mwaisela?”
“Ndiyo.”
“Hapana, hayupo huku, nenda kitengo cha mifupa, MOI,” alisema nesi huyo.
“Nashukuru.”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Henry hakutaka kubaki mahali hapo, akaanza kutembea kwa mwendo uleule wa harakaharaka, kitu pekee alichokuwa akikitaka kwa wakati huo ni kumuona Maimartha tu.
Alipofika huko, waandishi wa habari wengine zaidi ya kumi walikuwa wamekusanyika katika mlango wa kuingilia katika jengo la kitengo cha mifupa, MOI. Kila mmoja alikuwa na kamera mkononi tayari kwa kumpiga picha Maimartha endapo tu angepitishwa nje kuelekea Mwaisela.
“Vipi?” aliuliza Henry.
“Bado anaendelea na matibabu, hali yake mbaya sana,” alisema mwandishi wa Gazeti la Uwazi, Haroun Sanchawa.
“Kwani ilikuwaje?” aliuliza Henry.
“Sijui chochote kile, chanzo kilinipigia simu na kuniambia kwamba Maimartha kaletwa mahali hapa baada ya kupata ajali, zaidi ya hapo, sijui chochote kile,” alisema Sanchawa.
Hakuwa na jinsi, kwa sababu alifika mahali hapo kwa ajili ya kumuona Maimartha na waandishi wengine walikuwa nje, naye ilimpasa kusubiria kama wengine. Muda wote Henry alikuwa akimuomba Mungu kwamba amponye Maimartha lakini zaidi ya hilo, alikuwa akiomba msamaha kwa kuongea maneno mabaya dhidi ya Maimartha katika kipindi ambacho hakutokea nyumbani na alipokuwa akimpigia simu bila kupokelewa.
Muda wote Henry alikuwa akijihukumu, bado alijiona kuwa chanzo cha mambo hayo yote kwani endapo asingempigia simu Maimartha ilimaanisha kwamba asingepata ajali ile aliyokuwa ameipata.
“Nisamehe Mungu,” alisema Henry huku machozi yaliyokuwa yakimlenga yakianza kububujika mashavuni mwake.
Hakufikiria tena kuandika kitabu cha maisha ya Maimartha, kitu alichokuwa akikifikiria mahali hapo kilikuwa ni kumuombea uzima msichana huyo ambaye bado alionekana kuwa na muda mwingi wa kumsifu Mungu.
****
Watanzania hasa wakristo walionekana kama kuchanganyikiwa, taarifa za kupata ajali kwa Maimartha kuliwashtua. Wengi hawakuziamini taarifa hizo kitu kilichowafanya kuelekea hospitalini ili kupata uhakika juu ya kile kilichokuwa kimetokea.
Huko, wakapata uhakika kwamba taarifa ambazo zilikuwa zikiendelea kuvuma hazikuwa tetesi bali zilikuwa taarifa kamili. Hilo likaonekana kuwa kama pigo kwa waimbaji wa nyimbo za Injili na makanisa mengi ya kilokole Tanzania.
Maombezi yakaanza rasmi, katika kila ibada ya Jumapili, washirika wa makanisa mbalimbali wa
likuwa wakikusanyana katika Kanisa la Kilokole la Praise And Worship lililokuwa Kinondoni na kuanza kumuombea Maimartha.
Huyo ndiye alikuwa muimbaji mkubwa na maarufu aliyekuwa amebaki, nyimbo zake zilizojaa uwepo wa Mungu ndizo zilizokuwa zikisikika kila sehemu. Kitu cha ajabu, mara baada ya kupata ajali hiyo, albamu zake zilizokuwa sokoni zikanunuliwa zote.
“Mungu, tunakuomba umponye Maimartha, tunampenda sana,” alisema msichana mmoja huku mkononi mwake akiwa ameshika Biblia.
Kila siku wachungaji walikuwa wakielekea hospitalini hapo kwa ajili ya kumuona muimbaji huyo. Hawakuwa wakiruhusiwa kwani mgonjwa alikuwa akihitajika kupata muda mwingi wa kuwa peke yake kitandani.
Hakuwa amepata fahamu, kwa muda wa wiki nzima, alikuwa kimya kitandani hali ambayo iliwapa wasiwasi mkubwa washirika wa makanisa kwa kudhani kwamba Maimartha alikuwa amefariki japokuwa madaktari hawakutaka kuzungumza ukweli.
Baadhi ya ndugu zake waliokuwa Iringa wakiwepo wazazi wake wakaingia jijini Dar es Salaam, taarifa walizokuwa wamezipata ziliwashtua. Maimartha alikuwa miongoni mwa watoto wao saba, kutokana na kuingiza kiasi kikubwa cha fedha, wao wenyewe walikuwa wamebadilika kwa kujengewa nyumba ya kifahari na shamba kubwa ambalo liliwaingizia fedha kila walipokuwa wakilima na kuvuna.
Mama yake, bi Estelina alikuwa akilia tu, muda wote alionekana kuwa mwenye majonzi. Alimpenda sana Maimartha, kwake alionekana kuwa mtoto wa tofauti aliyekuwa na kiu ya kubadilisha maisha ya watu wengi, wale wasiokuwa wakimjua Mungu, kupitia nyimbo zake wamjue.
Ndoto zake zote alizokuwa nazo zilionekana kufikia tamati, ajali ile aliyokuwa ameipata ilionekana kuwa mwisho wa kila kitu. Hakukuwa na matumaini ya kupona, kitu walichotakiwa ni kumuomba Mungu kwani japokuwa madaktari walikuwa wataalamu wa kuujua mwili wa binadamu, Mungu alikuwa zaidi kwani Yeye ndiye aliyeuumba mwili huo.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Jopo la madaktari kumi walikuwa wamekutana ndani ya chumba cha mkutano kwa ajili ya kuzungumzia hali aliyokuwa nayo Maimartha. Wiki ya kwanza ilikuwa imekwishakatika na hali ya Maimartha ilikuwa vilevile, hakuwa amerudiwa na fahamu zake.
Kila mmoja alikuwa na karatasi juu ya majibu ya vipimo ambavyo vilichukuliwa toka siku ya kwanza msichana huyo alipoletwa hospitalini hapo.
Katika karatasi hizo, pia kulikuwa na majibu ya vipimo vya CT (Computed Tomography) ambacho hutumika kupiga picha kwa watu waliopata mivunjiko kadhaa miilini mwao, hasa uti wa mgongo.
Mbali na hayo, kulikuwa na karatasi nyingine ambayo ilikuwa na majibu ya mwili wa Maimartha. Katika vipimo vyote ambavyo vilifanyika kama x-ray, CT, kipimo cha mwisho kabisa ambacho kilifanyika kilikuwa ni Magnetic Resonance Imaging (MRI).
Hiki kilikuwa kipimo kikubwa na cha mwisho kabisa kufanyika ambacho kilikuwa na uwezo wa kuchunguza kila kitu kuhusiana na mvunjiko kisha kutoa majibu kwa ufasaha zaidi.
Vipimo vyote hivyo, vilitumika katika kipindi ambacho Maimartha alikuwa ndani ya chumba cha wagonjwa mahututi. Hakuwa akijitambua, alikuwa kimya kitandani huku akionekana kama mtu ambaye tayari alikwishakufa.
Madaktari hao waliokuwa ndani ya chumba hicho walikuwa kimya, vichwa vyao vilikuwa vikiuma sana kwani mgonjwa aliyekuwa ameletwa alionekana kuwa tofauti kabisa na wagonjwa wengine, huyu alionekana kuwa kwenye hali ya hatari zaidi.
Kila mtu hakuwa akiamini kile alichokuwa akikiona katika karatasi zile za majibu. Hawakuamini kama kungekuwa na mtu ambaye angepatwa na tatizo kubwa kama alilokuwa nalo Maimartha. Kila mmoja alijua kwamba huo ungekuwa mwisho wake.
“Hali imekuwa ni ngumu mno, mpaka sasa hivi sidhani kama huyu mgonjwa tutamuweza,” alisema Dk. Mshana, huyu alikuwa mtaalamu wa mifupa hospitalini hapo.
“Vipimo vinaonesha nini?” aliuliza Dk. Kimosa.
“Uti wake wa mgongo umevunjika, sidhani kama tutaweza, cha msingi, ni bora asafirishwe tu,” alisema Dk. Mshana.
Uti wa mgongo wa Maimartha ulikuwa umevunjika. Hali ilionekana kuwa mbaya kwake kwani watu wote waliokuwa wakivunjika uti wa mgongo ilikuwa ni lazima wapooze huku watu hao wakihitajika kufanyiwa oparesheni ndani ya miezi sita tu, kama ikipita miezi hiyo na bado hali inaendelea basi kupooza huko kutakuwa kwa maisha yake yote.
“Ni lazima tutafute msaada,” alisema Dk. Mshana huku akishusha pumzi ndefu.
“Msaada gani?”
“Asafirishwe kuelekea India kwa matibabu zaidi, vinginevyo, anaweza kufariki dunia,” alisema Dk. Mshana.
Kikao hicho cha kuijadili hali ya Maimartha kilichukuwa masaa matatu, makubaliano ambayo waliafikiana yalikuwa ni Maimartha kusafirishwa na kupelekwa nchini India. Walichokifanya madaktari hao ni kuwasiliana na uongozi wa Hospitali ya Ganga kwa ajili ya kumpeleka Maimartha huko ili aweze kupata matibabu mahali hapo.
“Anatakiwa kusafirishwa na kupelekwa nchini India,” alisema Dk. Kipwate, alikuwa akiwaambia wazazi wake.
“Hilo si tatizo, tunachokitaka ni kuona akipona tena,” alisema mzee Paul.
“Na mimi nataka kwenda huko, nitajigharamia kila kitu,” alisema Henry, mzee Paul na bi Estelina wakapigwa na mshangao kwani hawakuwa wakimfahamu kijana huyo.
“Utaongea na wazazi wake, hilo ni nje ya uwezo wetu,” alisema Dk. Kipwate na kuondoka mahali hapo.
Hapo ndipo Henry alipoanza kuwaambia wazazi hao juu ya mchakato ambao alikuwa nao kwa Maimartha. Hakutaka kuficha kitu chochote kile, aliendelea kuwaambia kwamba hata ajali ile aliyokuwa ameipata, yeye ndiye aliyesababisha hilo kwani Maimartha alikuwa njiani akielekea nyumbani kwake.
Bi Estelina alijikuta akianza kulia tena, maneno aliyokuwa ameyaongea Henry yalimuumiza kupita kawaida. Alimkumbuka mtoto wake, katika kipindi alichokuwa mzima, moyo wake ulikuwa na furaha tele, kila wakati alikuwa mtu wa kufurahi tu lakini ghafla, maisha yake hayo yakawa yamebadilika, furaha aliyokuwa nayo ikapotea maishani mwake.
Maneno ya faraja na pole walizokuwa wakipewa na washirika wa makanisa mbalimbali waliofika hospitalini hapo ziliwaumiza mno, washirika hao walionekana kama watu waliowakumbusha maisha ya furaha ya nyuma waliyokuwa wakiishi na mtoto wao.
“Mungu ni mponyaji, atamponya tu,” alisema kijana mmoja, naye alikuwa muimbaji wa nyimbo za Injili kama alivyokuwa Maimartha.
“Tunaamini hilo, cha msingi ni kuendelea kumuomba Mungu,” alisema mzee Paul.
“Kwani anasumbuliwa na nini?” aliuliza mwandishi wa habari wa Gazeti la Uwazi, Sanchawa.
“Uti wa mgongo wake umevunjika, madaktari wanasema kwamba ataweza kupooza,” alimjibu mzee Paul.
“Poleni sana. Kwa hiyo ndiyo anataka kusafirishwa kuelekea India?” aliendelea kuuliza mwandishi huyo.
“Ndiyo.”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Mtasafiri lini?”
“Tutasafiri siku ya Jumatano, tuna siku tatu za kujiandaa,” alijibu mzee Paul.
Henry alitakiwa kujiandaa kwa ajili ya safari ya kuelekea nchini India. Kwa sababu alikuwa na vibali vyote, akahangaikia viza, alipopata, kitu alichokuwa akikisubiria kilikuwa ni safari tu.
Kila siku alionekana kuwa mtu wa mawazo, bado kichwa chake kilikuwa kikimuuma kwani kila alipokuwa akiliona jina la Maimartha na picha yake katika vyombo mbalimbali vya habari, moyo wake ulikuwa ukimuuma sana.
Japokuwa hakuwa amesababisha ajali ile barabarani lakini Henry alijiona kwamba yeye ndiye mtu pekee ambaye alitakiwa kubebeshwa mzigo wa lawama kwa kila kitu kilichokuwa kimetokea.
“Mungu, naomba umponye, mzigo huu wa lawama ni mzito mno kuubeba,” alisema Henry huku machozi yakimbubujika mashavuni mwake.
Moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali, kwa kila kitu kilichokuwa kikiendelea kilimuumiza zaidi. Hakuacha kwenda hospitalini, kila siku ilikuwa ni lazima kuelekea huko, mpaka kipindi hicho, bado hakukuwa na mtu aliyeruhusiwa kuingia ndani.
“Lakini tunataka japo kumuona,” alisema Henry, alikuwa akimwambia Dk. Mshana.
“Hakuna mtu anayeruhusiwa kuingia humo.”
“Dokta, hawa ni wazazi wake, mimi ni mwandishi ninataka kumwandikia historia ya maisha yake, kweli hatuwezi kuingia na kumuona? Mimi ni Henry, mwandishi wa habari, nadhani unanifahamu, tafadhali dokta, tunaomba kumuona,” alisema Henry huku akijitahidi kumbembeleza Dk. Mshana.
“Mtamuona tu, si kesho ndiyo mnaelekea India, hakuna tatizo, mtamuona tu,” alisema Dk. Mshana.
Siku iliyofuata baada ya kila kuandaliwa, safari ya kuelekea nchini India ikaanza. Wote walikuwa ndani ya ndege ya Shirika la Indians Airlines huku kukiwa na kitanda maalumu ambacho Maimartha alikuwa amelala kimya. Hawakuwa peke yao ndani ya safari hiyo bali Dk. Mshana alikuwa pamoja nao.
Japokuwa alikuwa na kiti chake, muda mwingi Henry alikuwa akielekea karibu na kitanda hicho na kukaa karibu na Maimartha. Kila alipokuwa akimwangalia, uso wake ulitawaliwa na majonzi, hakuamini kama msichana huyo aliyekuwa kitandani alikuwa Maimartha, muimbaji wa nyimbo za Injili ambaye alikuwa akitaka kuandika kitabu cha historia ya maisha yake.
“Mungu, naomba usimchukue Maimartha, mpe nafasi nyingine ya kuishi, japo nafasi moja tu, nadhani ataitumia awezavyo ili kukiandika kitabu cha maisha yake,” alisema Henry.
Machozi hayakukoma kumbubujika mashavuni mwake, kila alipokuwa akimwangalia Maimartha kitandani pale, aliumia kila alipokumbuka kwamba pamoja na uzima tuliokuwa nayo, pia Mungu aliumba kifo, kitu ambacho Maimartha alikuwa akielekea kukutana nacho.
“Usiniache Maimartha,” alisema Henry, shati alilokuwa amevaa lililoanishwa na machozi yake kifuani mwake.
Baada ya masaa kumi, ndege ya Shirika la Indians Airlines ilikuwa ikitua katika
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Indira Gandhi uliokuwa New Delhi, hali ya
hewa haikuwa tofauti na jiji la Dar es Salaam, joto lilikuwa imetawala jijini
hapo.
Gari la Hospitali ya Ganga lilikuwa mahali hapo kwa ajili ya kumchukua
Maimartha ambaye mpaka katika kipindi hicho hakuwa amepata fahamu. Abiria
wakaanza kuteremka kutoka ndani ya ndege na kuelekea katika sehemu
iliyokuwa na mlango wa kuingilia ndani ya jengo la uwanja huo.
Baada ya abiria wote kumalizika, kitanda alichokuwa amelalia Maimartha
kikaanza kuteremshwa huku wazazi wake, Henry wakifuata.
Japokuwa hiyo ilikuwa ni mara yake ya kwanza kufika nchini India lakini Henry
hakuonekana kuwa na furaha kabisa, muda wote uso wake ulionekana kuwa na
mawazo mengi, hakuamini kama siku yake ya kwanza kufika nchini humo
ilikuwa ni kumleta msichana Maimartha ambaye alikuwa hoi kitandani.
Baada ya Maimartha kupandishwa ndani ya gari hilo, nao wakatakiwa kupitia
katika mlango maalumu ambapo baada ya dakika chache, wakaungana na gari
hilo na safari ya kuelekea katika hospitali hiyo kuanza.
Mwili wa Maimartha haukuwa na majeraha makubwa, vidonda kadhaa
alivyokuwa navyo vilikuwa vimekwishafishwa, kitu kilichokuwa kimebakia
kilikuwa ni kurudiwa na fahamu tu.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Dripu za maji yaliyochanganywa na dawa ziitwazo alendronate (fosamax),
ibandronate (bonviva), risedronate (actonel) ziliendelea kupitisha maji katika
mwili wake, kwa kumtazama kitandani pale ungeweza kusema kwamba
Maimartha alikuwa amelala na angeamka muda wowote ule.
“I want to see her back” (Ninataka nimuone tena)” alisema Henry akimaanisha
kwamba alitaka kumuona Maimartha akirudiwa na fahamu.
“She will come back, let them do their work” (Atarudi tu, waachie wafanye kazi
yao)” alisema mmoja wa manesi waliokuwa ndani ya gari hilo.
“We trust them with their treatment, this is not the first time (Tunawaamini na
matibabu yao, hii si mara ya kwanza)” alisema Dk. Mshana ambaye
aliongozana nao.
Kutokana na idadi kubwa ya watu, foleni za magari ambazo hazikuangalia
kama hili lilikuwa gari la wagonjwa au la, walichukua dakika ishirini mpaka
kufika katika hospitali hiyo.
Lilikuwa jengo kubwa la ghorofa sita ambalo kwa juu kabisa liliandikwa Ganga
Medical Center. Gari likaingizwa ndani ya eneo la hospitali hiyo, manesi wawili
wakaanza kulisogelea, machela ikashushwa na machela kushushwa.
Katika kila hatua iliyokuwa ikiendelea mahali hapo, Henry alikuwa akihuzunika
tu, hakuamini kama msichana aliyekuwa akipenda sana kusikiliza nyimbo zake
leo hii alikuwa kitandani huku akionekana kama mfu anayepumulia mashine ya
oksijeni.
Kwa sababu walikuwa wamekwishafanikisha kumfikisha Maimartha hospitalini
hapo, kilichofuatia ni kwenda mitaani ambapo huko wakachukua vyumba katika
Hoteli ya Banjubanju ambayo haikuwa na gharama sana.
“Mungu, bado nina kazi na Maimartha, kama inawezekana, naomba hata umpe
nguvu kwa wiki moja tu, naomba uisikie sala yangu,” alisema Henry.
***
Matibabu yakaanza rasmi hospitalini hapo. Kuumia kwa Maimartha kulionekana
tofauti na wagonjwa ambao waliwahi kuletwa hospitalini hapo, yeye alionekana
kuumia zaidi.
Uti wa mgongo wake ulikuwa umefunjika mara mbili, mpaka hapo, hali ilionesha
kwamba ajali aliyokuwa ameipata haikuwa ya kawaida, ilikuwa ni ajali mbaya
ambayo ingeweza hata kukatisha maisha yake.
Dokta Bingwa wa Upasuaji, Sunil Kushey akachaguliwa kumtibia Maimartha ili
apone haraka hata kabla miezi sita haijakatika kwani kama angechelewa mpaka
miezi hiyo kukatika, inamaanisha kwamba angekuwa katika hali ya kupooza
maisha yake yote.
Kazi hakuwa ndogo, kila siku Dk. Sunil alikuwa akifika hospitalini hapo, hatua
ya kwanza ilikuwa ni kuingia katika chumba cha upasuaji ambapo huko
akakutana na wenzake na kuanza kuifanya kazi hiyo.
Japokuwa nchini Tanzania vipimo vilikuwa vimetolewa na majibu kuwekwa
wazi lakini hawakutaka kukubali, ilitakiwa vipimo zaidi vifanyike ili kuchunguza
kwa undani juu ya uti huo, jinsi ulivyovunjka na chembechembe ambazo zilitoka
katika uti wa mgongo.
“Upasuaji huu utachukua miezi mitano mpaka kukamilika,” alisema Dr. Sunil.
“Baada ya hapo, atakuwa kwenye hali yake nzuri? Namaanisha hatokuwa
amepooza?” aliuliza Dk. Malish.
“Bado sijajua, huyu mgonjwa amekuwa ni wa tofauti sana, cha msingi,
nitajitahidi kadri niwezavyo,” alisema Dk. Sunil.
Mipira kadhaa ilipitishwa katika mwili wake kwa ajili ya chakula na kujisaidia
haja zote. Hakuwa akiongea, bado ukimya wake uliendelea kitandani pale huku
akiwa kimya kabisa.
Kila kitu alikuwa akifanyiwa, manesi walikuwa na kazi kubwa ya kuhakikisha
kila wiki mipira ya chakula na haja inabadilishwa na kuwekwa mingine.
Henry, wazazi wa Maimartha na Dk. Mshana waliendelea kufika hospitalini
hapo kuangalia hali ya mgonjwa. Huko, hawakuzuiliwa, kila walipokuwa
wakienda, waliruhusiwa kuingia ndani ya chumba hicho na kumwangalia
mgonjwa wao kitandani pale alipokuwa amelala.
“Naomba unisamehe Maimartha,” alisema Henry huku akiwa akiwa pembeni
mwa kitanda alichokuwa Maimartha, alikuwa amemshika mkono.
“Najua bila mimi usingekuwa katika hali hii, nisamehe kwa kila kitu, nisamehe
kwa kukuhisi vibaya, nisamehe kwa kukulazimisha kukiandika kitabu cha
maisha yako, naomba unisamehe kwa kila nilichokifanya kwako, ninatamani
uyafumbue macho yako na uniangalie tena, uangalie ni kwa jinsi gani nimeumia
moyoni mwangu, Maimartha...Maimartha...Maimartha amka,” alisema henry
huku machozi yakimbubujika mashavuni mwake.
Maneno yake hayakubadilisha kitu chochote kile, bado Maimartha aliendelea
kubaki kitandani pale. Kadiri siku zilivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo
hali yake kitandani pale ilivyozidi kudhoofika, mwili wake ukaanza kupungua
jambo lililoonekana kuwatisha hata wazazi wake.
“Mume wangu, Maimartha atakufa,” alisema bi Estelina huku akilia.
“Hatoweza kufa, nyamaza mke wangu,” alisema mzee Paul lakini bi Estelina
hakutaka kunyamaza.
Kila alipokuwa akimwangalia mtoto wake kitandani pale alionekana kuwa
kwenye mateso makali, hakuonesha dalili zozote za kupona na kurudi katika
hali yake kama kawaida.
“Amka Maimartha, Amka unitazame tena, amka uongee na uimbe tena,
Tanzania imeikumbuka sauti yako, amka Maimartha, amka uimbe tena,”
alisema Henry kwa maumivu makali moyoni mwake huku akiamini kwamba
Maimartha angeweza kuisikia sauti ile na kuyafumbua macho yake. Bado
alikuwa kimya, kwa jinsi alivyoonekana kitandani pale, alionekana kama mfu
anayepumulia mashine ya oksjeni.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment