Simulizi : Love Bite
Sehemu Ya Pili (2)
ILIPOISHIA………..
Jothan ilibaki kidogo tu agonge wakate anaendesha kutokana na mawazo yaliyochanganyikana na hasira kwa kile alichofanyiwa na Bahati.. Alijilaumu sana kwenda kula chakula pale na kuambulia maumivu. Alijuta kukutana tena na Bahati ingawaje mwanzoni alikuwa na hamu ya kuonana nae. Alifika nyumbani na kujilaza.
”who a Jonathan by the way??”
Aliirudia ile kauli ya Bahati na kujikuta anashindwa kuamini kuwa yule ndie bahati halisi aliyemtamkia maneno yale.
SONGA NAYO…..
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/Mawazo yalimuandama Jothan kwa kile alichotendewa na Bahati. Lakini alikubali moyoni kuwa msemo wa wahenga kuwa tenda wema nenda zako hawakukosea kusema hivyo.
Aliamua kusahau yote ya nyuma ingawaje ubongoni alikosa tafsiri. Alijua kuwa msaada wowote utakaompa mtu basi hujawekeza chochote zaidi ya maumivu pindi utakapo fadhila kutoka kwake.
Likizo yake ilipoisha alienda kazini kama kawaida. Alishangaa mabadiliko Fulani aliyoyaona pale ofisini. Meza yake alikuwa amekaa mtu mwingine kabisa.
“salama kaka.” Alisalimia Jothan baada ya kumsogelea yule mtu aliyekaa nafasi yake.
“safi tu.” Aliitikia yule mtu ambaye alionekana kuendelea na kazi yake kama kawaida.
“samahani, nadhani wewe ni mgeni hapa. Hicho kiti ulichokalia ni changu.” Aliongea Jothan na kumuangalia yule mtu ambaye alikua anamshangaa tu na kujifanya hajasikia na kuendelea na mahesabu yake.
“sina taarifa zozote hapa juu yako wewe, kwa hiyo hiki kiti nimepangiwa na bosi mkuu na hakuniambia kama nitahitajika kutoka ukija wewe.” Aliongea yule mtu kwa kujiamini.
Jothan aliona kuwa alikuwa anapoteza muda kuongea na yule mtu. Maamuzi ya kuingia ofisini kwa bosi wake yalimjia na kuamua kwenda huko.
“Mr.Jothan, hukupata barua yako mapokezi pale nje?” aliongea basi wake hata kabla ya salamu.
“barua?...barua gani?” aliuliza Jothan kwa mshangao mkuu.
“we nenda ukaichukue… utakachokikuta ndio utajua hiyo barua inahusu nini.” Aliongea bosi wake na kumfanya Jothan kuzidi kushangaa mambo yanavyoenda.
Muonekana wa bosi wake ulikuwa tofauti kabisa na muonekano wa kila siku aliokuwa nao. Alionekana kama mtu aliyemkasirikia Jothan wakati alitakiwa kuonyesha hali ya kumlaki ikiwezekana kumpandisha cheo Jothan kwa kufanya kazi kubwa ya kuirudisha kampuni katika hali yake ya kawaida.
Jothan alitoka mpaka mapokezi na kumuangalia yule dada wa mapokezi.
“doh.. nilishasahau. Kuna barua yako Mr. Jothan.” Aliongea yule dada wa mapokezi huku akishika kichwa chake baada ya kumuona Jothan kuonyesha ishara kuwa alipitiwa kumpa ile barua kabla hajaingia ndani.
“ndio nimeifuata.” Aliongea Jothan na kumuangalia yule dada aliyeinama na kuanza kupekua barua kadhaa alizokuwa nazo na kutoa moja yenye jina la Jothan na kumkabidhi.
Jothan aliichukua ile barua na kuifungua. Hakuamini kitu kilichandikwa kwenye ile barua. Hakuamini kuwa anaweza kufukuzwa kazi kwa kosa ambalo hajawahi kulifanya. Kampuni ilikuwa inamtuhumu kwa kuisababishia hasara kampuni yake huko Morogoro jambo ambalo halikuwa na ukweli ndani yake. Hasara ilitokea kabla hajaenda na yeye ndio aliyesababisha mpaka baadhi ya wahujumu wa kampuni yake kugunduliwa na kuiweka kampuni hiyo katika hali inayoridhisha kwa sasa.
Taarifa hizo zilimchanganya na kumfanya arudi tena kwa bosi wake.
“kilichoandikwa humo ndio uamuzi wangu,.. bila shuruti naomba utoke ofisini kwangu.”
Aliongea bosi wake na kukataa katukatu kumsikiliza hoja zake.
Jothan aliona kama mikosi mfululizo inazidi kumuandama. Hakubishana na mtu. Aliamua kusaini alipotakiwa kusaini na kwenda NSSF kwa ajili ya kufuatilia mafao yake.
Kwakua vyeti vyake vilikua vimependeza, hakuchukua muda mrefu kupata kazi kwenye kampuni nyingine. Huko alipewa cheo kikubwa zaidi ya alichokuwa nacho kwenye kampuni yake ya zamani. Hapo aliamini kuwa mungu hakuumba ugonjwa bali ulikuwa na dawa yake. Alimshukuru mungu kwa kupata sehemu iliyokuwa inathamini uwezo wake wa utendaji wa kazi tena kwa muda mfupi.
Saikolojia na mahusiano ndilo jambo pekee lililompa chati kwa haraka hapo ofisi kwao kutokana na wateja wengi waliokuwa wakiwasiliana na yeye alipokuwa ofisi yake aliyokwa anafanya kazi zamani wote walihamia kwenye ofisi hiyo mpya.
Miezi nane baada kampuni ilimuandalia tafrija kutokana na kuipa jina na mafanikio makubwa kampuni hiyo ambayo ilikuwa haijulikani japo kuwa ilikuwa na miaka mitatu toka ianzishwe.
Zawadi alizopewa hata yeye hakuzitegemea. Alipewa na gari aina ya prado mpya kabisa kutokana na mchango wake mkubwa ndani ya kampuni hiyo.
Baada ya sherehe hiyo kuisha, watu walitawanyika kwenda makwao. Jothan akiwa kwenye gari yake akirudi nyumbani kwake, kwa mbali alimuona msichana mrembo akimpa ishara ya kuomba lifti kwake. Bila hiyana alipunguza mwendo na kupaki pembeni kidogo.
Alipigwa na butwaa baada ya kumuona mtu mwenyewe anayeomba lifti. Hata baada ya yule msichana kumuona Jothan alishtuka kidogo na kuonyesha ishara ya kutoamini kwamba angekutana na Jothan maeneo yale.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“wewe, za miaka?” aliongea Jothan na kufungua mlango wa prado yake ambayo ndio kwa mara ya kwanza inatembea kwenye lami ya Tanzania toka ilipoagiziwa huko nchi za ng`ambo.
Yule dada alipanda na kukaa nae siti ya mbele.
“sikutarajia kama ipo siku nitaonana na wewe” aliongea yule dada na kuvua miwani yake na kuiweka kwenye pochi yake.
Jothan alimuangalia yule msichana aliyevaa gauni fupi lililomuonyesha mapaja. Juu alivalia kikoti cheusi na kofia aina ya Cow boy.
Muonekana wa yule binti ulizidi kuvutia japo kuwa ni muda mrefu Jothan hakumuona yule msichana. Weupe asilia na wa kujiongezea pia ulizidi kumfanya yule dada asijulikane kama ni Mtanzania au kachanganya na watu kutoka nchi za ughaibuni. Nywele za bandia alizobandika zililingana na muonekano wa Marichui. Tabasamu lilipasua midomo minene iliyopendezeshwa na kimsitari chembamba kilichokuwa katikati ya meno yake ndio kilikuwa kivutio kingine kwenye sura ya yule dada.
Hakua mwembamba, pia hakua na unene uliomfanya kuchukiza. Alijua kuutumia mwili wake kwa kukataa tumbo kubwa na kuyafanya maziwa yake kujitegemea yenyewe bila kutumia sidiria.
Hayo yote yalibainika haraka kutokana na mtoko alionyuka siku hiyo.
“hata mimi, yaani nikikumbuka siku ile sijui ilikuaje mpeka nikapitiwa na usingizi.” Aliongea Jothan na kuonyesha kuwa kichwa chake kilikua kimehifadhi kumbumbu kubwa toka mara ya mwisho kuonana na binti yule aliyeushitua moyo wake kabla ya kukutana na Bahati.
“una kumbukumbu wewe.. kwani wewe unaishi wapi?” aliuliza yule dada.
“naishi kinondoni kwa manyanya.” Aliongea Jonathan na kumfanya yule dada kupigwa na butwaa.
“sasa mbona mimi nakaa kinondoni kanisani baada ya kituo cha Biafra?... na mpaka nashuka nilikuacha ndani gari!” aliongea yule dada na kumfanya Jonathan kutabasamu.
“unafikiri niliamka tena?.. yaani nilipitiliza kituo na kwenda kuamshwa na konda gari ilipofika mwenge.” Aliongea Jonathan huku akiendesha gari yake hiyo mpya kwa umakini mkubwa.
Waliongea mengi ikiwemo kujuana majina na kupeana namba za simu. Jothan alimfikisha yule dada mpaka kanisani kituo anachoshukia na yeye akageuza gari na kurudi kwake.
Kwakua saa ilisoma ni saa mbili usiku, aliamua kwenda kuoga na kulala moja kwa moja kutokana na uchovu wa shughuli yao.
Macho hayakufumba haraka japokuwa alikuwa kitandani kwa takribani masaa matatu. Alikizunguka kitanda chote na kukumbatia mito huku akijenga taswira ya kuwa na msichana yule waliokuwa wameonana kitambo lakini hawakupata nafasi ya kuongea kama siku hiyo. Alitabasamu peke yake kila wakati huku ubongo wake ukijaribu kumpa data muhimu za uzuri wa msichana huyo kila nukta aliyokuwa akifanya jambo lolote lililoukosha moyo wake.
Hakujua alilala saa ngapi, ila alishtushwa na alarm yake iliyokua inamuamsha kila siku saa moja kamili asubuhi.
Aliichukua simu yake na kukuta sms tatu zilizomtakia asubuhi njema kutoka kwenye namba aliyoi save kwenye simu yake jina la SHANI.
Alitabasamu na kuzijibu zile sms na kuondoka kwenda kazini baada ya kumaliza kunywa chai aliyoiandaa mwenyewe.
Walipiga story kwenye simu alipokuwa njiani na msichana huyo na kukubaliana kukutana kwenye chakula cha mchana Bondeni hotel iliyokuwa magomeni.
Kwakua alikua hana kazi nyingi ofisini kulingana na siku yenyewe ilikua nusu siku kwao. Siku ya ijumaa waliitumia kumalizia viporo tu na kazi za siku hiyo walizihesabu kuanza nazo wiki ijayo.
Japokuwa alikua si mfuatiliaji, Jonathan aliingia facebook na kutafuta jina analo litumia Shani kwenye mtandao huo wa jamii. Baada ya kulitafuta alilipata na kuanza kuperuzi picha za binti huyo. Hakika muonekano wake ulizidi kumfanya Jothan azidi kuwa na hamu ya kuwa naye. Alikua ni binti ambaye hayuko nyuma wala kupitwa na wakati. Alijua jinsi ya kupangilia nguo na pozi zilizowaacha hoi watu wengi waliomuona. Kila picha aliyopiga ilikuwa na comments zisizopungua mia mbili kutoka kwa marafiki zake waliokuwa wanazikubali pigo zake.
Akiwa amezama mtandaoni huku akizifurahia picha za Shani, muda wa kwenda kupata chakula cha mchana uliwadia na Jothan akazima computer yake aina ya apple iliyokuwa mezani kwake na kwenda kwenye gari yake kuitafuta Bondeni hotel ilipo.
Baada ya dakika chache alishawasili maeneo hayo na kuchukua simu yake ili ampigie Shani na kumpa taarifa kuwa ameshafika walipo ahidiana kukutana.
Kabla hajabonyeza kitufe cha kupigia, moyo wake ulipatwa na mshituko wa ajabu baada ya kuangalia mbele ya meza kadhaa za kwenye hotel hiyo na kumuona Bahati akiwa na bosi wake wa zamani wakilishana huku wakiwa hawana habari.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
LAliamua kuheshimu hisia za ke na kupiga simu kwa Shani.
“umefika wapi babie” aliongea Jothan baada ya salamu.
“nimeshafika wangu, wewe upo upande gani?” aliuliza Shani kwenye simu.
“nipo upande wa mlango wa kuingilia hotelini kabisa…. Upande wa chakula huku.” Aliongea Jothan na Shani akakata simu baada ya kumuona.
Mavazi aliyovaa Shani yalizi kumpagawisha Jothan, kila mtu aliyemuona hakusita kuyagandisha macho yake kwa mdada huyo mwenye uzuri wa ajabu.
Hatua za Shani zilimfikisha kwa Jothan na kusalimiana kisha wakaingia ndani pamoja.
Macho ya Bahati yaligongana na Jothan ambaye alikuwa na msichana mzuri Shani pembeni yake. Bahati aliangalia pembeni na kujifanya hajamuona Jothan na kuendelea kulishana na mpenzi wake. Jothan naye hakujishughulisha nao, aliwaangalia tu na kuwapita. Akaenda kutafuta sehemu nzuri yenye upepo na kukaa.
“uliniambia unaisha peke yako, kwa nini sasa?” aliuliza Shani baada ya kukaa na kuletewa vitu walivyoagizwa.
“si unajua kuwa bado sijampata mwanamke wa kuishi nae, ndio maana nimekuwa mpweke pale nyumbani.” Aliongea Jothan na kutabasamu.
“jamani, wanawake wote waliojaa hapa mjini, ukizingatia your so handsome. Unanitania wewe?” aliomgea Shani na kucheka.
“sikutanii, huo ndio ukweli wenyewe. Nipo single mwenzio.” Aliongea Jothan na kucheka.
“ila kaka una moyo wa ajabu sana.” Aliomgea Shani na kumuacha Jothan njia panda.
“kwanini unasema hivyo?” aliuliza Jothan.
“unajua toka siku ya kwanza tuliyoonana mimi na wewe kule coco beach, sijui kwanini ila niseme ukweli nilitokea kuvutiwa na tabia yako. Maana angekuwa mtu mwengine baada ya kutoa ofa tu basi angeanza kutusumbua mara unaitwa nani mara nipeni namba zenu za simu. Lakini wewe ulikuwa bize na mambo yako na ulipochoka ulituaga na kuondoka zako…. Kusema ukweli nilivutiwa sana na tabia yako.” Alionge Shani na kumfanya Jothan atabasamu.
“mi naamini kama unampenda mtu si lazima mpaka umpe ofa ndio uanze kumuelezea… hata mimi nilivutiwa na wewe sema nilishindwa kukueleza kwakua ulikua na marafiki zako na nilihofia pia kuniona msumbufu kwakua niliwapa ofa.” Aliongea Jothan na kumfanya Shani atabasamu.
Walimaliza kula na na kutoka mule hotelini, Jothan hakuwaona tena wakina Bahati na hapo ndipo aipogundua sababu ya kuachishwa kazi.
Alitikisa kicwa kama ishara ya kusikitika na kuelekea kwenye gari yake na kumpakiza Shani ambaye kwa muonekana hawakuwa na tofauti na wapenzi wawapo out.
Kama kawaida yake,. Alimfikisha Shani kituo cha kanisani na yeye akarudi kwake.
Usiku wa siku ya jumamosi ilikuwa ni siku Spacial ya mtoko kati ya Shani na Jothan kwenda club. Walifika club na kucheza mziki vya kutosha na kila mmoja aliifurahia ile siku.
Walirudi nyumbani pamoja, na Shani kwa mara ya kwanza akaingia nyumbani kwa Jothan. Kwakua walikuwa wamelewa, walilala wote mpaka asubuhi bila kufanya lolote na kuamka asumbuhi. Waliangaliana na kucheka huku kila mmoja akiwa hana kumbukumbu sawa sawa kuwa ilikuwaje mpaka wakalala wote chumba kimoja tena kila mtu akiwa amelala kivyake.
Mazoea yalizidi mpaka ikafikia wakati Shani akawa anapewa ufunguo wa nyumba na Jothan ambaye akirudi kazini alikuta nyumba safi na amepikiwa chakula kizuri. Upishi wa Shani haukufanana na muonekano wa ke. Wasichana wengi wazuri jikoni huwa hamna kitu. Lakini yeye alikua anatoa vitu ambavyo akati mwengine Jothan alishindwa kuvumilia na kumwambia kuwa alikua anataka kumuoa kabisa ili awe anampkia daima.
Uakaribu ukajenga penzi moto moto lililowashinda mpaka wenyewe na kujikuta Shani amehamia kabisa nyumbani kwa Jothan.
Maisha ya furaha na yenye raha tele yalizidi kujijenga kwa Jothan. Hakuwa na mawazo tena zaidi ya kumshukuru mungu kwa kumpamsichana ambaye hata yeye alikuwa na mapenzi a kweli kwake.
Kuna siku ambazo Shani alikua analala na Jothan na siku nyingine alikuwa analala kwao kutokana na kuwa bado hajawa mke wake halali. Jothan alivizia siku ambayo Shani hayupo mule ndani na kuamua kufungua kabati yake ambayo ilijaa siri zake nyingi za maisha yake na kumbukumbu mbali mbali zinazomuhusu yeye. Vitu vilivyofaa alivirudisha kwenye kabati na vingine ambavyo vilikuwa havifai kwa usalama wa penzi lake alivichukua kwa lengo la kuvitia moto.
Baada ya kupekua muda mrefu, aliibamba alburm moja iliyokuwa na picha kadhaa za zamani toka yupo shule. Baada ya kufungua kurasa kadhaa, alishtuka baada ya kuona picha ya msichana mzuri aliyekuwa amemkumbatia huku wanatabasamu. Mawazo yalimpeleka mbali sana.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
***************************
Ilikua siku ya aina yake baada ya Jothan kupelekwa katika mashinadano na Shule aliyokuwa anasoma. Mashindano hayo yalikuwa yanatafuta mshindi wa mdahalo kwa lugha ya kiingereza. Kila shule ilitakiwa itoe wanafunzi wawili. Wakiume na wakike.
Mwanafunzi wa kiume alichaguliwa yeye kutokana na kuwa na lafudhi nzuri na ya kuvutia kwenye lugha hiyo. Ingawaje alikua kidato cha pili, lakini shule ilimuamini na kuona kuwa ni yeye pekee ndio anafaa kutokana na uwezo wake kwenye somo hilo na vile anavyojiamini.
Mashindano hayo yalifanyika kwenye ukumbi wa shule ya sekondari Jitegemee.
Kwanza ufunguzi ulifanyika na Bendi ya shule hiyo kwa kupiga ala za muziki zilizokuwa zikifuatishwa na watu wate waliohudhuria pale. Kulikua na shule zisizopungua Arobaini.
Kila shule iliwakilishwa kwenye sekta mbali mbali, wapo walioigiza kiingereza na wengine waruka sarakasi. Shule za international zenyewe zilishindana kwenye mdahalo uliokuwa wakibishana kati ya watoto wa mitaani na walio shueni, wapi wanaoharibiwa zaidi na utandawazi?.
Mada hiyo ilibeba ubishani mkubwa lakini Jothan aliweza kuifanya shule yake kuibuka kidedea kutokakana na hoja kali na zenye uzito alizokuwa akizitoa kwenye utetezi na kuwashindwa wapinzani wake.
Walipowa wakipata chakula baada ya shindano, dada mmoja aliyekuwa shule pinzani alimfuata na kumuomba akae nae kwenye meza moja.
“hamna shida, karibu” aliongea Jothan na yule dada akaweka chakula chake na kuanza kumuuliza Jothan maswali.
“nifaye nini ili niweze kuongea kingereza kizuri kama wewe?” aliuliza yule dada na kumuangalia Jothan
“ni kazi rahisi, kwanza kipende na kuwa na juhudi nacho, ni lazima utakuwa na uwezo wa kukitumia utakavyo.” Aliongea Jothan na kumfanya yule dada atabasamu.
“hivi unaitwa nani?” aliuliza yule dada baada ya kimya kifupi kupita.
“Jothan” alijibu Jothan kifupi.
“wooh.. nice name,… mimi naitwa Prisca.” Alijitambulisha yule msichana,
“Prisca, jina la mama yangu hilo.” Aliongea Jothan na kumfanya yule dada atabasamu.
“una simu?” aliuliza Prissca.
“ndio.” Alijibu Jothan huku akijua ni kitu gani kilifuata baada ya Prisca kumuuliza swali lile.
“unaonaje tukipeana contact sababu nahitaji sana ushauri wako na ukaribu pia kati yangu mimi na wewe kama hautajali.” Aliongea yule dada na Jothan alianza kumtajia namba zake na yule dada alitoa simu yake na kuandika zile namba alizokuwa anatajiwa. Baada ya kuihifadhi kwenye kitabu cha simu yake, alimbipu Jothan nay eye akai hifadi pia.
Waliagana na kila mmoja akarudi kwao baada ya kuruhusiwa. Kesho yake Jothan alienda shuleni kwao na kupongezwa na mwalimu mkuu baada ya kupigwa kengele ya dharula na wanafunzi wote kukusanyika msitarini. Alimpongeza. pia mwalimu wa Jothan kwa kumpa muongozo mzuri.
Aliporudi nyumbani, aliiwasha simu yake na baada ya sekunde kadhaa message tatu ziliingia mfululizo. Alipofungua zote zilikua za Prisca. Na zote zilimtaka akutane naye kama atakuwa na muda.
Kwakua kwenye simu yake kulikuwa na vocha za kutosha. Aliamua kumuendea hewani.
“niambie” aliongea Jothan baada ya simu yake kupokelewa upande wa pili.
“safi tu, nilikuwa nahitaji kuonana na wewe leo kama utakuwa na muda.” Aliongea Prisca na kumfanya Jothan kutabasamu.
“tutaonana wapi sasa?” aliuliza jothan huku akionyesha wazi kuafiki swala la kuonana na binti huyo.
“popote tu utakapoamua wewe.” Aliongea Prisca na kumpa mwanya Jothan wa kuchagua.
“sio mbaya kama tukikutana namanga, au wewe una semaje?” aliongea Jothan.
“poa, saa ngapi?.” Aliuliza Prisca.”
“mida hii mi najiandaa, nafikiri tukutane baada ya saa limoja kutoka sasa.” Aliongea Jothan.
“poa” alijibu yule msichana na Jothan akakata simu. Jothan alienda kuoga haraka na kuvaa nguo zake nzuri mpaka mama yake akamshangaa.
“wapi tena hiyo mwanangu?” aliuliza mama yake Jothan baada ya kumuona mwanaye amependeza kupita kiasi.
“naenda maktaba kujisomea.” Aliongopa Jothan ili kukwepa maswali mengi kutoka kwa mama yake ambaye alikuwa anampiga vita juu ya kujihusisha na mahusiano na watoto wa kike
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Jothan alishuka namanga walipopanga kukutana na yule msichana. Dakika tano baade, Prisca naye alishuka na kukutana na Jothan.
Mavazi aliyovaa Prisca yalimpendeza sana na kumfnaya Jothan kidogo moyo umshtuke kumuona msichana huyo ambaye ndio mara ya kwanza kukatana nae akiwa nje ya sare za shule.
Aliduwaa kwa muda akiutathmini uzuri wa msichana huyo mgeni kwake mwenye kasi ya ajabu.
“wooo.. umependeza sana.” Alisifia Jothan baada ya kukutana na yule msichana.
“sikushindi wewe.” Alijibu yule msichana na kutabasamu.
“kwakua muda bado unaruhusu, unaonaje tukichukua bajaji twende coco beach tukapate kipupwe na kufurahisha nafsi zetu.”
Alishauri jothan na kumuangalia msichana huyo aliyemvutia kila akimtazama.
“ok, nadhani itakuwa poa zaidi.”
Aliongea Prisca na safari ya kuelekea coco beach ilianza mara moja baada ya kupata bajaji ya kukodi iliyowafikisha salama maeneo hayo.
Walitembea huku ha huko huko wakila cone na crips. Watu walikuwa wengi na kuchangamsha eneo hilo. Tamasha pia lilikuwepo na baadhi ya wasanii wa bongo flavour walifika na kutumbuiza kwenye ufukwe huo uliomiminika watu kila dakika.
Kutokana na kutopenda makelele, Jothan na Prisca walienda kwenye mapango ambapo kulikuwa na watu wachache wakiwa wametulia na wapenzi wao. Na wao waliafuta sehemu tulivu na kukaa na kuongea yao.
Wakiwa wamejisahau baada ya kuzama kwenye stori na vicheko vya hapa na pale, ghafla wakajikuta wamezungukwa na watu watatu na mmoja wao akiwa amevalia mavazi ya kiaskari.
“aroo, mna fanya nini hapa?” aliuliza yule askari aliyevalia sare kwa ukali.
“sisi…sisi tumekaa tu.” Alijibu Jothan huku akitetemeka.
“mmekaa tu, mbona mmejitenga?” aliuliza askari huyo na kudakiwa na mwenzake aliyekuwa amevaa nguo za kiraia lakini akiwa na pingu kama nne kiunoni mwake.
“walikuwa wanafanya ufuska hawa.” Aliongea yule askari na kumfanya Jothan kukataa kwa kutikisa kichwa. Uoga uliwa jaa kupita kiasi. Huyo Prisca ndio kabisaa, hakuweza kufanya lolote zaidi ya kuanza kulia.
“wewe si mwanafunzi?” aliuliza yule askari huku akiendelea kumkazia macha Jothan
“hapana.” Alikanusha Jothan
“na wewe msichana si bado mwanafunzi wewe?”
Yule askari alimgeukia Prisca na kumuuliza kiukali na kumfanya azidi kuogopa na kijasho cha uoga kiliamza kumtiririka.
“ndio..bado mwanafunzi afande.” Alijibu kiuoga Prisca.
“sasa wewe unaenda kufungwa miaka thelethini jela, unamrubuni mwanafunzi?,,,mfunge pingu mara moja.”
Aliongea yule askari na kumfanya Jothan kushangaa. Hakuamini kuwa wale maaskari walikuwa na nia ya kuwakamata. Alizunguka askari yule mwenye pingu na kumfunga Jothan mikononi.
Walichukuliwa wote wawili na kwenda nao pembeni ambapo waliwakuta wavulana wengi rika mbali mbali waliokuwa wamekamatwa na wapenzi wao waliokuwa kule mapangoni.
Wavulana waliitwa mmoja mmoja na kuhojiwa na baadae waliruhusiwa baada ya kutoa faini kutokana na kosa hilo la kukaa faragha mapangoni kitu ambacho maaskari wanaolinda eneo hilo wamekataza.
Waliwaacha Jothan na Prisca wa mwisho kama walivyo wakamata.
“unajua kuwa kutembea na mwanafunzi ni kosa kisheria na adhabu yake ni kubwa sana. Sasa usipoteze muda. Una shilingi ngapi tuwaachie?” aliongea askari aliyekuwa anawahoji wale watu waliowakamata.
“hapa nimebakiwa na shilingi elfu nane tu.” Aliongea Jothan kiunyonge.
“sasa hiyo elfu nane tutagawanaje?.. acha utani dogo utaenda kuozea segerea.” Aliongea yule askari na kuanza kumsachi Jothan. Aligundua kuwa ni kweli salio lake lilikuwa elfu nane. Alimuita Prisca na kumuuliza.
“una shilingi ngapi ili tuwaachie?” aliuliza yule askari na kumuangalia Prisca ambaye bado alikuwa analia.
“elfu ishirini.” Alijibu Prisca.
“zilete hapa, haya na wewe zilete hizo elfu nane zako.” Aliongea yule afande na wote wakatii haraka na kutoa hela walizokuwa nazo.
“mna nauli?” aliuliza yule afande na baada ya kupokea zile hela zote.
“hatuna, hela zote ndio hizo.” Alijibu Jothan.
Yule afande alichomoa elfu tatu na kuwapa kama nauli.
“haya poteeni haraka, msirudie tena kujiingiza kwenye vitendo vinavyoshawishi ngono sawa..haya potea kabla sijabadili maamuzi.”
Alipiga mkwara yule askari na wao wakaondoka haraka. Hawakuwa na hamu ya kuendelea kukaa pale coco beach, waliamua kuondoka. Walipofika kituoni waliagana na kila mmoja akapanda magari yaendayo kwao.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Walipigiana simu na kila mmoja alimtaarifu mwenzake juu ya kufika salama nyumbani kwao. Kisanga kilichowakuta ilibaki kuwa siri yao. Hakuna aliyediriki kumuhadithia mtu yeyote.
Mapenzi ya kishule shule yalianza taratibu na mwosho wakajikuta wanapendana kiukweli na hakuna aliyeridhika kupita siku bila tukio la kuonana. Walimaliza elimu yao ya kidato cha nne huku mapenzi yakiendelea kati yao.
Waliridhika kuonana na kuchat kupitia simu na mitandao ya kijamii.
Jothan alipomaliza kidato cha nne alichaguliwa kwenda kibaha kumalizia elimu yake ya kidato cha tano na sita. Alifaulu vizuri na kwenda chuo kikuu morogoro.
Huo ndio ulikuwa mwanzo wa kupotezana na Prisca. Kwani alipoteza simu na akaamua kubadisha line wakati namba ya Prisca haikuwa kichwani mwake kutokana na tabia ya Prisca kutodumu na namba mmoja muda mrefu.
Alimuwaza sana mpenzi wake huyo waliyekutana enzi za shule na kukua pamoja. Hakua na jinsi zaidi ya kupiga kitabu baada ya kuona anapoteza muda kumuwaza mtu ambaye hata kwao walipo hivi sasa hapafahamu. Hii ni baada ya kupewa taarifa za kuhama Prisca pale walipokuwa wana kaa mwanzo baada ya kuuza nyumba yao.
*****************
Mawazo yalirudi tena kwenye ile picha na kuamua kuificha bila kuichoma moto kama alivyotaka mwanzo kufanya. Badala yake alienda sehemu ambayo kulikuwa na hati ya nyumba yake na kuiweka ile picha katikati. Ni kweli Prisza alikuwa anampenda na hawakuwahi kuachana. Ni muingiliano tu wa maisha ndi uliowatenganisha. Moyo wake aliona kama si haki kuichoma ile picha kwakua bado alikua na nafasi ndani ya moyo wake japokuwa kuonana na msichana huyo ni ngumu sana. Hata alipomaliza chuo alijitahidi kumtafuta bila mafanikio. Mpaka muda huu anajitegemea ni kipindi kirefu cha miaka sita tuko walipokutana na Prisca kwa mara ya mwisho.
Mawazo ya msichana huyo wa kwanza katika maisha yake yalimchanganya kichwa na hakuwa na jinsi zaidi ya kukubali matokea na kuanzisha ukurasa mwengine wa maisha yake kwenye mapenzi na shani
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya usafi huo wa kabati lake, aliamua kujilaza kitandani na usingizi ukamchukua.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment