IMEANDIKWA NA : NYEMO CHILONGANI
*********************************************************************************
Sehemu Ya Kwanza (1)
Nakumbuka ilikuwa mwaka 2005, mwaka ambao nilimaliza kuchukua Diploma yangu ya Uandishi wa habari katika chuo cha uandishi cha DSJ (Dar es Salaam School of Journalist) kilichokuwa mtaa wa Bungoni, Buguruni jijini Dar es Salaam. Katika kipindi hicho nilionekana kuwa na furaha sana kwa sababu ndoto zangu ambazo nilikuwa nimejiwekea katika maisha yangu niliziona kuanza kutimia katika muda mchache ujao.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Katika kipindi chote ambacho nilikuwa katika chuo hicho nikipata elimu yangu, kichwani mwangu kulikuwa na ndoto nyingi sana, ndoto za kuwa mwandishi mkubwa ambaye ningekuja kuheshimika na jamii yote, mwandishi ambaye ningeweza kuleta mabadiliko makubwa katika sekta zote za uandishi nchini Tanzania. Kila nilipokuwa nikimwangalia mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC, Charles Hilary, nikajiona nikizidi kupata nguvu zaidi za kusoma kwa sana, nilitamani sana kuwa kama yeye katika maisha yangu.
Nilikuwa na kiu sana ya kuwa mwandishi bora na kisha kutafuta nafasi ya kutangaza katika shirika lolote kubwa la Habari kama la BBC, Cnn, Aljazeera au shirika lolote ambalo lilikuwa likitambulika kimataifa. Hapo ndipo ambapo nilifikiria kitu kimoja ambacho nilitakiwa kukifanya, kitu kimoja ambacho kingekuwa cha hatari sana katika maisha yangu.
Nakumbuka siku hiyo mara baada ya kutoka katika field yangu niliyoifanyia katika kituo cha utangazaji cha ITV, nikarudi nyumbani na kisha kutulia chumbani kwangu. Siku hiyo sikuonekana kuwa na furaha kabisa, kichwa changu kilikuwa kikifikiria ni kwa namna gani ningeweza kuwaambia wazazi wangu kuhusiana na kile ambacho nilikuwa nimekifikiria kichwani mwangu.
Kiukweli nilikuwa nahitaji sana kampani ya wazazi wangu, wao ndio nilikuwa nikiwaona kuwa watu sahihi ambao kamwe wasingeweza kunishauri kitu kibaya, niliwaamini kupita kawaida. Nilitulia chumbani kwangu kitandani, hakukuwa na siku ambayo niliwaona wazazi wangu wakichelewa kufika nyumbani kama siku hiyo. Muda wote macho yangu yalikuwa yakiangalia saa yangu ya mkononi, nilitamani sana waingie nyumbani hapo na kisha kuwaambia kile ambacho nilikuwa nimepanga kuwaambia.
Saa 2:23 nikasikia muungurumo wa gari kutoka nje ya nyumba yetu, sikutaka kujiuliza zaidi, nikajua fika kwamba wazazi wangu walikuwa wakiingia ndani ya eneo la nyumba yetu. Sikutaka kutoka, sikutaka kuonyesha kwamba nina presha, nikatulia chumbani mpaka pale ambapo wakaingia ndani ya nyumba ile na kuelekea chumbani kwao.
Baadae walipotoka kwa ajili ya kula chakula cha usiku, nikaelekea mezani na kuanza kula pamoja nao. Kwa wakati huo kichwa changu kilikuwa kikifikiria mengi, sikujua kama wangeweza kunielewa juu ya kile ambacho nilikuwa nikitaka kuwaambia kwa wakati ule. Katika kipindi chote ambacho tulikuwa tukila, muonekano wagu ulionekana kuwa si wa kawaida, nilionekana kuwa na kitu moyoni mwangu.
“Nyemo….!” Niliisikia sauti ya baba ikiniita, nikashtuka kutoka katika lindi la mawazo.
“Naam…!” Niliitikia huku nikionekana kushtuka.
“Unawaza nini?” Baba aliniuliza huku akiacha kula.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Siwazi kitu baba” Nilimwambia huku macho yangu yakionyesha dhahiri kwamba nilimdanganya.
“Hapana. Hauko kawaida leo. Hebu tueleze unawaza nini” Baba aliniambia.
Nilibaki kimya kwa muda, nikaanza kufikiria ni kitu gani ambacho nilitakiwa kuwaambia kwa wakati huo. Nikaanza kujiuliza kama lilikuwa jambo sahihi kuwaambia kile ambacho nilitakiwa kuwaambia ili waweze kunishauri au nilitakiwa kukaa kimya na kuwashtukiza hapo baadae.
“Kuna nini kipenzi” Mama aliingilia kwa kuniuliza swali. Nikayapeleka macho yangu usoni mwa mama yangu.
“Nataka kuwa mwandishi mkubwa wa habari” Niliwaambia.
“Hilo tunalifahamu na umekuwa ukituambia kila siku. Nakumbuka huwa unatuambia kwamba unataka kuwa kama Charles Hilary” Baba aliniambia.
“Ndio. Natamani sana niwe nafanya kazi katika mashirika makubwa ya habari duniani” Niliwaambia.
“Kila kitu kinaanza kwa hatua Nyemo, hauweza kuwa mwandishi mkubwa wa habari na wakati haujapitia katika mashirika madogo. Unakumbuka kuwa hata Charles Hilary kabla ya kujiunga na BBC alikuwa akifanya kazi ITV?” Baba alisema na kuniuliza.
“Nakumbuka”
“Basi hautakiwi kuwa na presha. Kuna siku utakuwa mwandishi mkubwa tu” Baba aliniambia.
Nikabaki kimya kwa muda, baba alionekana kuniondoa katika kile ambacho nilikuwa nimekifikiria kabla, alijitahidi kuniambia maneno mengi mengi kwamba ningekuwa mwandishi mkubwa wa habari kama tu ningekuwa mvumilivu na kufanya kazi katika mashirika madogo, sikukubaliana na maneno yake.
“Kuna kitu nimekifikiria na ningehitaji ushauri wenu” Niliwaambia.
“Kitu gani?”
“Nataka nitengeneze makala yangu ihusuyo mambo fulani, na kama ikiwezekana basi nisafiri” Niliwaambia.
“Kuandaa makala yahitaji utulivu mkubwa sana. Wewe unataka kusafiri kuelekea wapi kuiandika hiyo makala yako?” Baba aliniuliza.
“Nataka kwenda Darfur, nchini Sudan” Niliwaambia.
Kila mmoja akaonekana kushtuka, wote wakaacha kula na kuniangalia kwa macho ambayo yalionyesha kwamba kutokuamini kile ambacho nilikuwa nimekisema mbele yao. Wakanikazia macho zaidi, nilionekana kuongea kitu kimoja ambacho kilikuwa kimewashtua sana. Nikamuona baba akiisogeza sahani yake mbele kuonyesha kwamba alikuwa ameshiba.
“Unasemaje?” Aliniuliza huku akionekana kushtuka.
“Nataka kwenda Darfur” Nilimwambia.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/-
Chakula hakikulika tena, kila mmoja alionekana kushiba kwa wakati huo Maneno ambayo niliwaambia kwamba nilikuwa nikitaka kwenda nchini Sudan tena katika mji wa Darfur yalionekana kuwashtua sana. Waliufahamu vilivyo mji wa Darfur pamoja na mauaji ambayo yalikuwa yakiendelea katika nchi hiyo.
Hapa ningependa kuwaambia wale watu ambao hawakuwa wakiijua hii Darfur ambayo nilikuwa nimeizungumzia mahali hapo. Darfur ni mji mkubwa ambao unapatikana nchini Sudan. Mji huu ndio ambao umekuwa na machafuko mengi sana ambayo yamepelekea nchi nzima kutokuwa na maelewano.
Watu wakaonekana kuogopa, wakulima wakahofia kuelekea katika mashamba yao jambo ambalo lilipelekea nchi kuingia katika njaa kali. Nchi hii ilionekana kuwa na laana kwani toka kipindi ambacho machafuko hayo yameanza nchini humo, mvua nazo zimeonekana kunyesha kwa nadra sana. Waandishi wengi wa habari wamekuwa wakielekea katika mji huo na wengi kuuawa kinyama.
Umoja wa Mataifa ulijaribu kuingilia kati lakini hakukuonekana kuwa na mabadiliko kabisa, bado vita vya wenyewe kwa wenyewe vilikuwa vikiendelea kama kawaida. Katika mji huo huo ambao milio ya risasi ilionekana kuwa kama midundo ya muziki katika kumbi za usiku, katika mji huo huo ndio ambao mabomu ya mikono yanaonekana kuwa kama mipira ya miguu, mji huo huo ndio mji ambao nilikuwa nikitamani sana kwenda kwa wakati huo.
Kiu yangu kubwa kwa wakati huo ilikuwa ni kuingia ndani ya nchi hiyo na kwenda katika mji huo ambapo ningetengeneza makala yangu nzuri ambayo ningeweza kuitangaza na hatimae mashirika makubwa ya habari kunikubali na hivyo kuwa na haja ya kuniajiri na kuanza kazi pamoja nao. Niliamini sana kama ningeweza kuelekea Darfur basi kila kitu kingekwenda kama kinavyotakiwa, kiu ya kuwa kama Charles Hilary ilikuwa imenikaba kooni.
“Haiwezekani” Baba aliniambia.
“Kwa nini?”
“Ile si sehemu salama katika maisha ya binadamu”
“Hata kama baba. Naomba mniruhusu nielekee huko, ninataka kupata kile ninachokitaka katika maisha yangu” Niliwaambia.
“Haiwezekani” Baba aliniambia kwa sauti kubwa iliyojaa ukali ambayo ilinifanya kubaki kimya.
Baba alionekana kukasirika sana, hapo hapo akanywa maji haraka haraka na kisha kuondoka mahali hapo na kueleka chumbani kwake. Japokuwa sikuwa nimemaliza kula chakula, chakula kile kikaonekana kunikinai, sikuwa na hamu ya kukila tena. Mama nae akainuka, kwa jinsi nilivyokuwa nikimwangali, nae alionekana kukasirika, hakupenda nielekee Darfur, bado alikuwa akinihitaji.
“Nitakwenda tu, hata kama nitatoroka. Nitakwenda tu” Nilijisemea.
Japokuwa katika kipindi cha nyuma nilijifanya kutaka kuomba ushauri kutoka kwa wazazi wangu lakini moyo wangu ulikuwa umeweka msimamo mmoja tu kwamba ningekwenda tu nchini Sudan hata kama wangekataa kunipa nauli. Moyo wangu ulikuwa umkwishaamua kwa wakati huo, nilichokuwa nikikitaka ni kuelekea nchini Sudan na kisha kuandika Makala ambayo niliamini ingenitangaza sana na hatimae kuajiriwa katika mashirika makubwa duniani.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilibaki pale mezani kwa muda, mara nikaichukua simu yangu na kisha kumpigia simu mpenzi wangu niliyekuwa nae katika kipindi kile, Myra na kisha kumwambia kile ambacho nilikuwa nimekifikiria kukifanya kwa wakati ule. Nilipompa taarifa Myra, nae alikuwa sawa na wazazi wangu, alikataa kata kata kunikubalia nielekee nchini Sudan.
“Hapana mpenzi” Myra aliniambia kwa sauti iliyojaa wasiwasi.
“Itanibidi nifanye hivyo Mage. Ni lazima niende Sudan. Haijalishi wewe hautaki au wazazi wangu hawataki, NI LAZIMA nilekee Sudan” Nilimwambia Myra.
Huo ndio uamuzi ambao nilikuwa nimeupanga. Nikaanza kufikiria gharama ambazo zingenigharimu mpaka kukamilisha kila kitu, kitu cha kwanza kilikuwa kamera, nilihitaji kuwa na kamera ya video na ya picha. Pia nikahitaji kuwa na begi kubwa la mgongoni pamoja na kiasi fulani cha fedha ambacho kingeniwezesha kukitumia katika kipindi ambacho ningekwenda nchini Sudan.
Vitu hivyo havikuwa na shida sana, pia nilitakiwa kuwa na kitambulisho cha uandishi wa habari ambacho ningekionyesha kwa kila mtu ambaye angetaka kukiona hasa wale wafuasi wa upande wa pili ambao walikuwa kinyume na serikali ya Sudan. Hapa ndipo nilipoamua kuwasiliana na rafiki yangu, Hamza Kimosa ambaye nilimwambia anitengenezee kitabulisho cha uandishi wa habari cha shirika la Aljazeera huku nikiwa nimemtumia picha ya itambulisho hicho ambayo niliipata kwenye mtandao.
“Ni LAZIMA niende Darfur hata kama hawataki. Hata kuwatoroka nitawatoroka tu” Nilijisemea katika kipindi ambacho nilikuwa nikielekea chumbani kwangu.
Je unajua nini kiliendelea?
Je nilifanikiwa kwenda Darfur?
Na kama nilikwenda nilikutana na mambo gani huko?
Je unavyohisi hii ni kweli au hadithi ya kutunga?
Majibu utayapata.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment