Search This Blog

Sunday, 19 June 2022

MAKALA YANGU KUTOKA DARFUR - 2

 





    Simulizi : Makala Yangu Kutoka Darfur

    Sehemu Ya Pili (2)



    Nilijisikia vibaya sana hasa mara baada ya wazazi wangu kunikatalia kile ambacho nilitaka kukifanya kwa wakati huo. Nilichukia sana na wala sikutaka kuongea nao, niliwaona kuwa kama wasaliti katika maisha yangu ambao hawakutaka kuniruhusu kufanya kitu ambacho kingenifanya kufaidika katika maisha yangu.

    Siku iliyofuata nikaanza kuondoka kuelekea nyumbani alipokuwa akiishi Hamza, rafiki yangu ambaye alikuwa mtaalamu na mambo ya Graphic. Nilimkuta Hamza na hivyo kumtaka anionyeshee kitambulisho cha mwandishi wa habari wa shirika la habari la Aljazeera na kisha kunionyeshea. Kitambulisho kile kilionekana kutengenezwa katika utaalamu wa hali ya juu, japokuwa kilikuwa kikionekana kwenye kompyuta lakini kilionekana kuvutia sana.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/-

    “Kwa hiyo jina niweke Nyemo Chilongani kama kawaida au?” Hamza aliniuliza.

    “Nope. Weka Iqram Ibrahim” Nilimwambia.

    Pale pale Hamza akabadilisha na kisha kuliweka jina lile. Kichwani mwangu nilikwishajua kwamba katika kipindi kile nilikuwa nikielekea katika nchi ambayo ilikuwa na waumini wengi wa dini ya Kiislamu, hivyo nilihakikisha kwamba nafanya kila jitihada ili nionekane kuwa mtu wao ili hata kama nitahitaji vitu fulani kutoka kwao basi niweze kuvipata kwa urahisi. Siku hiyo nilikamilisha kila kitu kilichokuwa kikihitajika na kisha kuondoka kuelekea nyumbani.

    Nilichokifanya kwa wakati huo ni kuelekea katika mashine ya ATM na kisha kuchukua kiasi cha fedha cha shilingi milioni mbili na kuanza kuelekea Posta kwa ajili ya manunuzi ya kamera. Nikapata kamera mbili ambazo zilionekana kuwa bora na kuanza kurudi nyumbani. Kwa wakati huo, nilitaka kufanya mambo yangu kwa siri sana, sikutaka mtu yeyote nyumbani afahamu kwani kwa kuwafanya wafahamu basi wangeweza kunizuia kwenda kwa kutumia maneno yao ya kunikatisha tamaa na kunitisha.

    Maandalizi yangu yaliendelea zaidi na zaidi, baada ya miezi miwili, nikawa nimekwishagongewa viza ya kukaa kule kwa muda wa miezi mitatu. Bado siri iliendelea kuwa siri tu, sikuwaambia wazazi wangu na wala sikumwambia mpenzi wangu, Myra kwani nilimuona msichana huyo kuwa kama wazazi wangu tu.

    Kiu ambayo nilikuwa nayo katika kipindi hicho ni kuwa mwandishi mkubwa wa kimataifa, mwandishi ambaye ningeweza kufanya kazi ya uandishi katika mashirika makubwa duniani, sikutaka kuonekana kujali au kuhofia kuuawa, kwangu niliamini kwamba nafsi zote zingeonja mauti, haijalishi kama ni Mchungaji au Imamu, wote wangeonja mauti.

    Ingawa nilifahamu fika kwamba nchi ya Sudan haikuwa na usalama mkubwa katika maisha yangu lakini katika kipindi hicho sikuonekana kuhofia kitu chochote kile, yaani nilijiona kwamba ningeweza kufika salama na kurudi salama nchini Tanzania ambapo ningeendelea na maisha yangu huyku nikianza kuipeleka makala yangu katika mashirika mbalimbali ya habari.

    Naikumbuka sana siku hii ya tarehe 12/11/2005 siku ambayo nilianza safari yangu ya kuelekea nchini Sudan. Moyo wangu ulikuwa na furaha kubwa sana, sikuamini kama katika kipindi hicho nilikuwa nimeweza kuondoka nchini Tanzania na kuelekea nchini Sudan kwa ajili ya kutengeneza makala moja ambayo kila mtu ambaye angeiangalia basi angeonekana kushangaa sana.

    Ndani ya ndege nilikuwa na mawazo mengi, nilikuwa nikiwafikiria wazazi wangu ambao nilikuwa nimewaambia kuhusiana na safari hiyo lakini hawakuonekana kuwa radhi kuniruhusu kuelekea katika nchi hiyo ambayo vita vya wenyewe kwa wenyewe vilikuwa vikiwasumbua sana. Ukiacha na wazazi wangu, pia nilikuwa nikimkumbuka mpenzi wangu, Myra ambaye nae wala hakutofautiana sana na wazazi wangu, kwani nae hakutaka nielekee katika nchi hiyo.

    Nilijiona nikiwa nimefanya maamuzi magumu sana, maamuzi ambayo baadae yangeweza kuleta lawama za kila aina, sikutaka kujali kuhusiana na lawama ambazo ningezipata, nilichokuwa nikikitaka ni kuwa mwandishi mkubwa sana ambaye ningeonekana kuifanya dunia kuelewa kwa undani kile ambacho kilikuwa kikiendelea ndani ya nchi ile.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ingawa nchi ambayo nilikuwa ikielekea katika kipindi hicho ilionekana kuwa nchi ya hatari, lakini moyoni mwangu wala sikuonekana kuwa na wasiwasi wowote ule, nilikuwa nikizidi kujipa matumaini kwamba kila kitu kingekwenda kama ambavyo kilitakiwa kiwe. Nilipanga kuandaa makala moja kubwa na ya maana sana katika kila chombo cha habari ambacho kingediriki kuonyesha makala hiyo ambayo ilikuwa imeandaliwa na kijana mbunifu ambaye alikuwa na uwezo wa kuelezea mambo mengi kwa undani zaidi, Nyemo Chilongani.

    Saa 11:15 jioni, ndege ikaanza kutua kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Khartoum uliokuwa katika jiji la Khartoum. Hali ya hewa haikuwa nzuri sana, joto liionekana kuwa juu kwa kiasi fulani. Mimi pamoja na abiria wenzangu tukaanza kutoka nje ya uwanja ule. Macho yangu yalikuwa yakiangalia katika kila upande, nilijitahidi kutaka kuyazoea mazingira ya jiji lile.

    Watu wengi ambao walikuwa wakionekana katika macho yangu walikuwa wamevaa kanzu pamoja na vilemba vichwani, mavazi yale ndio yalionekana kuwa makubwa sana katika nchi ile. Nilipofika nje ya uwanja ule, moja kwa moja nikamfuata dereva wa teksi na kutaka aniepeleke sehemu yoyote ambayo ingeniwezesha kubadilisha fedha zangu na kuwa paundi, fedha ambayo ilikuwa ikitumiwa nchini humo.

    Baada ya kumwambia kitu nilichotaka kukifanya, akaniambia niingie ndani ya gari lake na kisha safari kuanza. Mji wa Khatoum haukuwa mzuri sana, majengo yao yalikuwa kama ya kizamani sana, kwa jinsi ulivyokuwa ukionekana mji ule, hali ilionyesha dhahiri kwamba sehemu kubwa ya nchi ile ilikuwa ni jangwa.

    Mitaa ya jiji lile ilikuwa katika mpangilio mzuri japokuwa haukuwa ukivutia sana. Kwa kila mtu ambaye nilikuwa nikimuona alikuwa akionekana kuwa na kanzu jambo ambalo likanifanya hata mimi pia kutamani kununua kanzu ili nionekane kuwa mmoja wapo. Safari yetu ile iliishia njie ya duka moja kubwa ambalo nikaingia ndani na kisha kutoa kiasi cha shilingi milioni saba na kisha kunibadilishia katika fedha zao za paundi ya Sudan ambayo walikuwa wakiitumia.

    Kutokana na nchi ile kubwa imeanguka sana katika uchumi, fedha zangu nilizozipata zilikuwa nyingi sana. Kitu cha kwanza nilichokifanya ni kumlipa dereva fedha zake na kisha kumtaka kunipeleka katika hoteli yoyote ambayo haikuwa na gharama kubwa. Huku tukiwa njiani kuelekea katika hoteli hiyo, nikamwambia kwamba nilikuwa na uhitaji wa kununua kanzu na kiremba na yeye kuniita muuzaji na kununua, sikutaka kuchelewa, nikanunua na kisha kuvivaa pale pale.

    “How do I look? (Naonekana vipi?)” Nilimuuliza dereva yule.

    “Like a Sudanese (Kama Msudani)” Dereva alinijibu huku akionyesha tabasamu pana.

    Kutokana na nchi ile kuwa katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe ambayo yalikuwa yakiendelea, wanajeshi wa majeshi ya Umoja wa Mataifa walikuwa wametapakaa katika kila kona huku wakiwa kwenye magari yao ambayo yalionekana kutengenezwa kwa ajili ya vita tu. Si wanajeshi wa Umoja wa Mataifa tu ambao walikuwa wakirandaranda mitaani bali hata wanajeshi wa Umoja wa Afrika (A.U) nao walikuwa wametapakaa katika mitaa ile, kwa picha ambayo ilionekana, sehemu ile haikuonekana kuwa ya usalama hata kidogo.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya dakika chache dereva akasimamisha gari lile nje ya hoteli moja ndogo iliyoitwa Selima Oasis. Nikateremka, nikamlipa dereva kiasi ambacho alikuwa ameihitaji na kisha kuelekea katika sehemu ya kaunta na kukutana na msichana mrembo. Nikaanza kumuuliza kuhusu vyumba na kisha kulipia na kupelekwa katika chumba ambacho nilitakiwa kukaa katika siku ambazo ningekuwa hapo Sudan.

    Sehemu ambayo nilitamani sana kufika tayari nilikuwa nimekwishafika. Sikujali kama wazazi wangenitafuta na kunikosa, nilichokuwa nikikijali kwa wakati huo ni kutengeneza makala yangu tu. Nilibaki chumbani mule huku nikianza kuifikiria safari yangu ya kuelekea Darfur, magharibi mwa nchi hiyo ya Sudan.

    Ingawa ilionekana kuwa sehemu iliyokuwa na hatari lakini wala sikuonekana kujali kabisa, sikuwa na woga wowote moyoni mwangu, nilikuwa nimedhamiria kwa moyo mmoja kwamba ilikuwa ni lazima nifanye kazi ambayo ilikuwa imenleta mahali pale, sikujali kupigwa risasi, kuchomwa moto au kuchinjwa, kile nilichokuwa nikikihitaji kwa wakati huo ni kufanya kazi yangu ambayo niliiona kuwa bora na kuniingizia fedha na kunitambulisha kama mwandishi wa habari wa Kimataifa.

    ****

    Kwa muonekano wa haraka haraka, nchi ya Sudan haikuonekana kuwa miongoni mwa nchi ambazo zilikuwa na amani kama nchi ya Tanzania, katika kila kona, magari ya kijeshi ya Umoja wa Mataifa pamoja na yale ya Umoja wa Afrika yalikuwa yakionekana. Ukiachana na magari hayo ya jeshi, vile vile kulikuwa na magari makubwa ambayo yalikuwa yakitumika kupeleka vyakula katika nchi hiyo.

    Nchi ya Sudan ikaonekana kuwa na njaa, watu walikuwa bize kuyakimbia makazi yao hasa wale ambao waliishi sehemu za nje ya jiji la Khatoum. Mashambani, wakulima hawakufika huko kulima kabisa. Vyombo vingi vya habari vilikuwa vikitangaza mara kwa mara kuhusiana na vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vilikuwa vikiendelea kutokea sana nchini Sudan.

    Darfur ndio ilionekana kuwa sehemu moja kubwa ambayo mapigano yalikuwa yakiendelea kutokea. Japokuwa nilikuwa sijafika lakini tayari niliona kwamba sehemu hiyo haikuwa hata na amani. Watu wengi ambao walikuwa wakizungumza na vyombo vya habari walikuwa wakiendelea kuvilaani vitendo ambavyo vilikuwa vikiendelea kutokea Darfur.

    Nilikaa na kuiangalia televisheni na habari za mauaji ambazo zilikuwa zikiendelea kutokea Darfur, nilipoona kwamba nimeridhika, nikainuka na kisha kulifuata begi langu. Nikalifungua na kuanza kutoa kitu kimoja baada ya kingine. Nikaitoa kamera na kisha kuiweka juu ya meza huku nikiwa nimeiseti sawa sawa na pale nilipokaa.

    Hapo ndipo ambao nikaanza kujirekodi, makala ambayo nilikuwa nimekwenda kuifanya Darfur ikaanzia hapo. Niliongea maneno mengi kwa lugha ya Kingereza huku nikiwataka waangaliaji wawe makini katika kuangalia kila kitakachokwenda kuonekana pamoja na kukisikia kile ambacho nilikuwa ninatarajia kukiongea.

    Nilipoona kwamba inatosha, nikaifuata kamera ile na kisha kuizima. Nikatoa vitu vingine zaidi na zaidi, kazi ambayo ilikuwa mbele yangu ilikuwa kubwa tena ya kujitoa mhanga lakini kwangu sikuonekana kujali, nilichokijali ni kuajiriwa katika moja ya makampuni makubwa ya habari tu. Siku hiyo sikutaka kufanya mambo mengi, nikalala.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kelele zilikuwa zikisikika nje, hapo hapo nikashtuka kutoka katika usingizi mzito. Kwanza sikujua mahali ambapo nilikuwepo katika kipindi hicho lakini mara baada ya kumbukumbu zangu kunijia vizuri, nikasimama na kisha kuanza kuelekea dirishani na kuanza kuchungulia kwa nje ili kuona ni kitu gani kilikuwa kikiendelea.

    Watu walikuwa wakikimbia huku na huko, wanajeshi wa Serikali tawala walikuwa wameingia mitaani huku lengo lao likiwa ni kuwatafuta wanajeshi wa kikundi kilichojiita DLF (Darfur Liberation Front) ambacho kilikuwa kinyume na Serikali ambayo ilikuwa madarakani. Kwa haraka hara mara baada ya kuona watu wakikimbia huku na kule, nikaichukua kamera yangu ambayo ilikuwa mezani, nikaiwasha na kisha kuanza kurekodi kupitia katika dirisha lile.

    Kila kilichokuwa kikionekana nilikuwa nikiendelea kukirekodi. Sikuonekana kuridhika, nilichokifanya ni kuivaa suruali yangu pamoja na shati na kisha kuchukua kitambulisho changu cha bandia cha kunionyesha kwamba nilikuwa mwandishi wa habari kutoka katika kituo cha habari cha Aljazeera na kisha kutoka nje huku kamba yake nikiwa nimeining’iniza shingoni.

    Nilipofika nje, nikaanza kurekodi, nilikuwa nikiendelea kurekodi kimoja baada ya kingine. Kwa jinsi wanajeshi wa serikali walivyokuwa wakianza kuwatafuta watu hao na mambo mengine mengi tu. Hapo ndipo nilipogundua kwamba nilikuwa nikifanya kosa, kwa sababu ile ilikuwa ni makala ihusuyo mambo mbalimbali yaliyokuwa yakiendelea nchini Sudan, yalihitaji maelezo ili kila atakayeiangalia aielewe.

    Kwa haraka sana macho yangu yakaanza kuangalia huku na kule na kutua kwa kijana mmoja ambaye alikuwa ameshika madaftari, umri wake bila shaka nilikuwa nimemzidi kidogo. Nikaanza kumfuata kijana yule na kisha kujitambulisha kwamba nilikuwa mwandishi wa habari na hivyo nilihitaji msaada wake.

    Hakuonekana kufahamu lugha ya Kingereza vizuri lakini tuliweza kuelewana. Nilichokifanya ni kumpa kamera ile na kisha kuanza kunirekodi kwa malipo ya paundi mia tano za Sudan. Kazi ikawa imeanza mahali hapo, nilikuwa nikielezea kila kilichokuwa kikiendelea mahali hapo huku kijana yule aliyejitambulisha kwa jina la Majeed akiendelea kunirekodi.

    Mahali pale sikuwa mimi peke yangu, waandishi wengine wa BBC, CNN walikuwa mahali pale huku nao wakichukua habari juu ya kila kilichokuwa kikiendelea mahali pale. Kitendo cha kuwaona waandishi wale wa habari kiliniuma sana, niliwaonea wivu mkubwa kwa kuwa walikuwa wakifanya kazi katika mashirika ambayo yalinifanya kusafiri mpaka nchini Sudan kwa ajili ya kutengeneza makala yangu.

    Majeed aliendelea kunirekodi mpaka katika kipidi ambacho hali ilipoonekana kutulia. Katika kipindi ambacho Mkuu wa Majeshi alipokuwa akiongea, mimi pamoja na waandishi wengine tukaanza kumsogelea na kisha kuanza kumrekodi. Moyoni nilijisikia furaha kupita kawaida, sikuamini kwamba nilikuwa nimefanikisha kuanza kile ambacho nilikuwa nimekipanga kukifanya.

    Siku hiyo ndio ilikuwa siku ya kwanza kukutana na Majeed ambaye aliniahidi kunisaidia katika kila kitu ambacho nilitakiwa kukifanya huku yeye akiwa kama mshika kamera. Nilifurahi sana, nilichokifanya ni kuahidiana na malipo ya siku nzima, hasa wiki nzima ambayo ningekwenda kuitumia nchini humo na kisha kurudi nyumbani japokuwa viza yangu ilikuwa ikionyesha kwamba nilikuwa na uwezo wa kukaa kwa miezi mitatu.

    “Nitataka twende Darfur” Nilimwambia Majeed ambaye akaonekana kushtuka.

    “Kufanya nini?” Aliniuliza huku akionekana kuwa na hofu.

    “Kufanya kazi ambayo ilinileta mahali hapa”

    “Mmmh! Mbona kama inakuwa ngumu”

    “Ugumu wake upo wapi hapo?”

    “Mauaji. Huko kumejaa damu, watu wanauawa kila siku” Majeed aliniambia.

    “Hayo hayo mauaji ndio ambayo ninataka kuyarekodi. Vipi upo tayari twende hiyo kesho?” Nilimwambia na kumuuliza.

    “Hapana. Siku tayari” Alinijibu.

    Majeed alionekana kuwa msaada mkubwa kwangu, nilikuwa nikimhitaji sana kwa ajili ya ile kazi ambayo nilikuwa nikitaka kuifanya mahali hapo, alikuwa amekwishakataa katakata. Kwa sababu nilijitambua kwamba mimi ni Mtanzania, tena mwenye maneno mengi, nikaanza kuutumia uongeaji wangu na ushawishi mkubwa kumlaghai Majeed.

    Ni ndani ya dakika thelathini tena huku nikiwa nimeongea maneno mengi ya ushawishi, Majeed akakubali kwenda pamoja nami Darfur huku nikiwa nimemhakikishia ulinzi mkubwa katika kipindi ambacho tungekuwa huko. Tukakubaliana na kisha kumuacha kwenda kujiandaa kwa ajili ya safari hiyo ya kuelekea katika sehemu ambayo ilikuwa na mauaji ya kikatili.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mimi ndiye nilikuwa mwandishi wa habari, na mimi ndiye nilijifanya kuwa mlinzi katika maisha yake bila kujua kwamba Darfur ilikuwa ni sehemu gani, ilikuwa na hatari kwa kiasi gani. Majeed akakubaliana nami, hakuonekana kujali sana kuhusiana na fedha, kitu alichokuwa akikijua ni kwamba nilitoka katika shirika la habari la Aljazeera na ndio maana alijisikia fahari kunikubalia kutaka kufanya kazi pamoja nami, hakujua kwamba kitambulisho kile nilichokuwa nacho ambacho kilinionyesha kwamba mimi ni mwandishi wa habari kilikuwa kitambulisho bandia. Alijua anafanya kazi na mwandishi wa Aljazeera kumbe ukweli ni kwamba alikuwa akifanya kazi na Mwananchi wa kawaida tu, yaani kama yeye.



    Majeed kakubali kwenda na mimi Darfur.

    Je unajua ni mambo gani yatatokea huko Darfur?

    Je nitaweza kugundulika kama mimi sikuwa mwandishi wa habari kutoka Aljazeera?

    Kuna mengi yatatokea, tuendelee kuwa pamoja tu.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog