Simulizi : Makala Yangu Kutoka Darfur
Sehemu Ya Tatu (3)
Nchi ya Sudan ilikuwa nchi kubwa sana zaidi ya jinsi ambavyo nilifikiria kabla. Nilipomuuliza dada wa mapokezi katika hoteli ile, alionekana kunishangaa sana kwamba nilikuwa vipi na uhitaji wa kuelekea Darfur na wakati mapigano ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilikuwa vikiendelea. Nilimtoa wasiwasi dada yule na kisha kutaka kunipa maelekezo mengi kuhusiana na kwenda katika mji huo ambao ulionekana kuwa tishio sana.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Dada yule akaanza kunielezea mambo mengi na hata umbali aliniambia kwamba kulikuwa na zaidi ya kilometa elfu nane kutoka katika jiji la Khatoum. Umbali ule ukaonekana kunishtua sana, sikutegemea kama kungekuwa na umbali wa namna ile. Hapo ndipo ambapo nilifikiria kupanda ndege, ila tatizo lililokuja ni kwamba hakukuwa na uwanja wowote wa ndege huko Darfur ambao ulikuwa ukitumika katika kipindi hicho cha mapigano.
Maneno ya dada yule yalionekana kunichosha kupita kawaida, ni mabasi tu ndio ambayo yalikuwa yakifanya safari ya kwenda huko kwa kutumia barabara ya lami ambayo ilikuwa ikionganisha mpaka Kurdufan, kilometa mia tano kabla ya kuingia Darfur. Hapo ndipo niliporudi chumbani na kisha kuanza kujiandaa na safari, asubuhi ya siku iliyofuata, safari ikaanza huku nikiwa pamoja na Majeed.
Ndani ya basi hatukuwa watu wengi sana, tulikuwa tumekaa katika viti vya nyuma kabisa. Lugha ya Kiarabu ndio ambayo ilikuwa ikisikika ndani ya basi lile, sikuwa nikielewa kitu chochote kile lakini kila nilipotaka kuambiwa kile kilichokuwa kikiongelewa, Majeed alikuwa akiniambia.
Safari ilikuwa ni ya kuchossha sana, mizigo mingi ilikuwa imepakiwa ndani ya basi lile, kila basi lilipokuwa likisimama, hali ya hewa ilikuwa ikibadilika kabisa, ilikuwa ni ya joto kali sana. Kichwa changu katika kipindi hicho kilikuwa kikifikiria kitu kimoja tu, kufika Darfur na kisha kuanza kufanya kile ambacho kilikuwa kimenifanya kufika ndani ya nchi ile.
Dereva alikuwa akiendesha gari kwa kasi kubwa sana ambayo ilionekana kuwa na hatari kupita kawaida. Ndani ya gari hakukuonekana mtu yeyote ambaye alionekana kujali kutokana na mwendo ule mkali, watu walionekana kutokuwa na habari, walikuwa wakiendelea kupiga stori kama kawaida. Ndani ya masaa nane, tukawa tumefika Ad Duwaym, kusini mwa jiji la Khatoum.
Hapa ilikuwa ikinishangaza sana, mji wa Darfur ulikuwa ukipatikana Magharibi mwa nchi ya Sudan, sasa ilikuwaje katika kipindi hicho tulikuwa tukielekea Kusini. Maswali hayo wala sikutaka kuyauliza, nilibaki nayo moyoni huku nikisubiri muda muafaka wa kuuliza utakapofika.
Kama ilivyokuwa Khatoum ndivyo ilivyokuwa hapo Ad Duwaym, idadi kbwa ya watu ilikuwa ikionekana mahali hapo huku magari mengi ya Umoja wa Mataifa pamoja na Umoja wa Afrika yakiwa mahali hapo. Hapo tukaruhusiwa kushuka na kisha kuanza kununua vyakula. Hali ilikuwa ngumu sana kwangu, vyakula ambavyo vilikuwa vikipatikana mahali hapo vilionekana kutokuwa sawa kabisa kwangu.
Chakula ambacho nilionekana kukiweza ni nyama ya ngamia tu, nyama tamu ambayo mara nyingi nilikuwa nikiila nchini Tanzania hasa katika kipindi cha Iddi Al Hadji na El Fitri katika kipindi ambacho rafiki yetu, Ustadhi Maliki alipokuwa akituletea. Japokuwa Majeed alikuwa akinilazimisha kula vyakula vingine, kwangu ikaonekana kuwa ngumu sana.
Baada ya nusu saa tukaingia ndani ya basi na kisha kuendelea na safari yetu. Hakukuwa na safari ambayo ilikuwa inachosha kama ile. Muda mwingi nilikuwa nikiiangalia saa yangu ya mkononi ambayo nilikuwa nimeiseti katika majira ya Sudan. Safari iliendelea zaidi, sehemu kubwa ya nchi hiyo ilikuwa ni jangwa kubwa, tena jangwa lile ambalo lilikuwa na joto kali katika kipindi cha mchana.
Baada ya masaa mngine nane kupita, tukaingia katika mji wa Kust na kisha kuonganisha kuutafuta mji wa Rabak ambapo hapo tungechukua barabara ya kuelekea Darfur kwa kutumia barabara ambayo ilikuwa na ubora zaidi ya ile. Mchoko wa safari bado ulikuwa ukiendelea kama kawaida, saa nne na robo usiku tukaingia Rabak ambapo hapo tulitakiwa kulala.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Usingizi haukupatikana hata kidogo, tulishinda usiku mzima tukipiga stori na Majeed ambaye hakuonekana kuwa na amani katika safari ile. Bado niliendelea kumfariji na kumtoa wasiwasi wa safari ile. Tulikula na kisha kuendelea kupiga stori. Ilipofika saa kumi na mbili alfajiri, tukaanza tena safari ya kuelekea Darfur.
Hapo Rabak ndipo ambapo tulichukua abiria wengine waliokuwa wamefika na mabasi kutoka Sannar, Sanjar na Al Qadarif miji ambayo ilikuwa ikipatikana Mashariki mwa nchi ya Sudan. Majeed ndiye ambaye alionekana kunichosha zaidi hasa mara baada ya kunitaarifu kwamba hata nusu ya safari tulikuwa hatujamaliza, tulisafiri kwa masaa kumi na sita lakini hata nusu ya safari haikuwa imekwisha.
Safari ikaendelea zaidi, tayari nilionekana kukata tamaa ya kufika mapema. Safari iliendelea zaidi, jua lilipochomoza mpaka kuwa jua la utosini na ndipo tukafika Al Ubayyid. Hapo tukanunua chakula na kisha kula tena. Hali ya joto ilionekana kuwa na usumbufu sana, nilitamani kuvua shati langu lakini sikufanya hivyo kwa kutotaka kuonekana vibaya mbele za macho ya watu waliokuwa na asili ya Uarabu.
Safari ikaendelea zaidi, saa tano na robo usiku ndipo tukaingia An Nunud, kilometa mia saba kabla ya kuingia Darfur. Nikatoka garini na kisha kukaa nje ya basi. Kila abiria alionekana kuchoka katika kipindi hicho, nilibaki nikiongea na Majeed kwa kipindi kirefu zaidi huku nikitaka kufahamu mengi kuhusiana na Darfur.
“Kwa hiyo nitajua vipi kama tumeingia Darfur?” Nilimuuliza Majeed.
“Utajua tu”
“Nitajua tu. Kivipi?” Nilimuuliza.
“Swali lako litajibika kirahisi sana” Majeed aliniambia.
“Sijakuelewa”
“Kimuonekano. Utakavyouona muonekano, utajua tu kwamba tutakuwa tumeanza kuingia Darfur” Majeed aliniambia.
Sikutaka kuuliza maswali mengine zaidi, kiu yangu ilikuwa ni kuanza kuona dalili hizo ambazo niliambiwa kwamba ningejua tu kwamba tulikuwa tumeingia Darfur. Ilipofika asubuhi tukaanza safari. Katika kipindi hiki kulikuwa kumebaki vituo viwili vikubwa, cha kwanza kilikuwa Nyala na cha pili kilikuwa Al Fashir.
Hiki kituo cha Al Fashir kilikuwa ndani ya Darfur ila huku pembeni pembeni kabisa katika upande wa Kusini mwa mji wa Darfur. Hapo ndipo ungekuwa mwisho wa safari yetu, japokuwa katika kipindi hicho nilitaka kuelekea katika sehemu iliyo na mapigano zaidi ya Al Junaynah, lakini Majeed aliniambia kwamba basi lisingeweza kufika huko.
“Kwa nini?” Nilimuuliza.
“Huko ndipo kwenye mapigano yenyewe, huko hakuna amani hata kidogo” Majeed aliniambia.
“Safi sana. Uko ndipo pazuri sana, na huko ndipo nilipotaka kwenda” Nilimwambia Majeed ambaye alionekana kushtuka zaidi.
Safari iliendelea zaidi, abiria wengi waliishia hapo Al Ubayyid. Kipindi cha nyuma ndani ya basi tulikuwa zaidi ya watu sitini lakini katika kipindi hicho tulikuwa tumebakia watu kumi na sita tu, wengine walikuwa wamekwishashuka. Safari haikuishia hapo iliendelea zaidi na zaidi mpaka tukaingia Nyala, kituo cha mwisho kabla ya kuingia kituo cha Al Fashir, mwisho wa safari ya basi lile.
****CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Safari ya kuelekea Al Fashir ikaanza. Hapa ningependa kuongea kitu kimoja kwa wale ambao waliweza kuongea mengi hata kabla safari ya kufika Darfur haikukamilika. Mji wa Darfur ndio mji mkubwa sana nchini Sudan na ndio maana mapigano ambayo yalikuwa yakiendelea huko yaliweza kuiathiri sana nchi hiyo ya Sudan.
Safari ya kuelekea katika mji mdogo wa Al Fashir ilikuwa ikiendelea. Hapa pia ningependa kuongea kitu kimoja ili kwa wale ambao walionekana kushangaa wasiweze kushangaa tena. Umbali wa kutoka Khatoum mpaka Darfur ilikuwa ni umbali wa kilometa 8000 ila kilometa hizo ni mpaka pale ambapo unaingia katika mji wa Nyala ambao upo kusini mwa mji huo wa Darfur. Umbali kutoka Khatoum mpaka hapo Nyala haukuwa ukipishana sana na umbali kutoka Nyala mpaka mwisho wa basi lile, Al Fashir.
Darfur ile ilikuwa kubwa sana, upana wake ulionekana kumshangaza kila mtu kiasi ambacho kuna wakati nchi ya Chad ikang’ang’ania kwamba Darfur ilikuwa ni sehemu ya nchi yao. Umbali wa kutoka Nyala mpaka Al Junaynah ilikuwa ni mbali zaidi ya kutoka Khatoum mpaka hapo Nyala. Umbali wa kutoka Khatoum mpaka hapo Nyala ulikuwa ni umbali wa kilometa elfu tatu mia tano na umbali wa kutoka hapo Nyara mpaka Al Junaynah ilikuwa ni umbali wa kilometa zaidi ya elfu nne mia tano.
Darfur ilikuwa kubwa sana, eneo kubwa la Darfur lilionekana kuwa jangwa kubwa, jangwa ambalo lilikuwa na joto kali katika kipindi cha mchana. Umbali huo mkubwa ndio ambao ukanifanya kupata majibu ya sababu ambayo ilimfanya dereva kuendesha gari kwa kasi kubwa zaidi ya magari ambayo yalikuwa yakisafiri katika ardhi ya Tanzania.
Nakumbuka nilikwishawahi kwenda Nairobi kwa kutumia mabasi ya Akamba ambayo yalikuwa yakikimbia sana, ila kwa mabasi yale ambayo yalikuwa yakisafiri kuelekea Darfur, mwendo wake ulikuwa ni mara mbili ya mabasi ya Akamba. Dereva alikuwa akikanyaga mafuta hasa, muda mwingi nilikuwa nikionekana kuwa na wasiwasi lakini hakukuwa na mtu yeyote ambaye alionekana kuhofia chochote kile, walionekana kuzoea.
Hapo ndipo ambapo safari ilionekana kuchosha sana, tulisafiri usiku na mchana na hatimae kuingia Al Fashir, mji ambao basi lile lilikuwa limefikia mwisho. Nikateremka na kisha kumshukuru Mungu kwa kunifikisha salama katika ardhi ya mji wa Al Fashir. Nilichokifanya ni kwenda kwenye kimghahawa kidogo na kisha kupata chakula,
Kumbuka kwamba hapo ilikuwa ni tayari tumeingia katika mji wa Darfur ila hatukuwa tumefika katika sehemu ile ambayo ilikuwa na mapigano makubwa. Baada ya kukaa mahali hapo kwa muda wa masaa mawili, hapo ndipo tukaanza safari ya kuelekea sehemu iliyo na mapigano makali, Al Junaynah. Usafiri haukuwa wa basi tena, madereva wengi walikuwa wakiogopa kuelekea huko kwa hiyo tulichokifanya ni kutumia usafiri wa farasi ambao ndo ulikuwa usafiri uliokua ukitumika katika kipindi hicho sehemu hiyo.
Katika safari ya kuelekea Al Junaynah hatukuwa peke yetu, tulikuwa na watu zaidi ya kumi ambao nao walikuwa wakielekea huko. Farasi walikuwa wakikimbia kwa kasi kubwa, na kwa kutumia farasi hao huku tukipumzika katika sehemu mbalimbali hasa nyakati za usiku na pale ambapo farasi walipoonekana kuchoka, tuliweza kutumia siku sita na ndipo tukaanza kuingia katika mji wa Al Junaynah.
Mpaka hapo wala sikutaka kuuliza zaidi kama tulikuwa tumeingia katika mji huo au la, magari mengi ya Umoja wa Mataifa yalikuwa yakionekana machoni mwetu, mara kwa mara walikuwa wakitusimamisha na kutuuliza baadhi ya maswali na waliporidhika na majibu yetu, tulikuwa tukiendelea na safari kama kawaida.
Tukafika katika sehemu ambayo wala haikuwa ikieleweka kabisa, macho yangu yakatua katika vitu vyeupe ambavyo nikashikwa na shauku kubwa ya kutaka kuvijua ni vitu gani. Nilichokifanya ni kuanza kuwaambia wenzangu kwamba ilikuwa ni lazima nijue vitu vile vilikuwa ni nini. Watu wote walionekana kukataa lakini nilipowalaziamisha zaidi, wakakubaliana nami.
Nikateremka juu ya farasi pamoja na Majeed na kisha kuanza kuelekea kule ambapo kulikuwa na mchanga mwingi. Sikuamini kile ambacho nilikuwa nikikiona mahali pale, yalikuwa ni mafuvu ya watu. Kwanza nikapigwa na mshtuko sana, toka nizaliwe sikuwahi kuyaona mafuvu ya watu, wakati huo ndio ilikuwa mara ya kwanza.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kuna vitu vingine huwa tunavipuuzia sana kila tunavyoviona kwenye televisheni, ila ukweli ni kwamba vinatisha kupita kawaida. Mafuvu ya watu yanatisha sana. Nilichokifanya huku nikijivisha ujasiri, nikamwambia Majeed achukue kamera na kisha kuanza kazi mahali hapo. Nikaanza kuongea huku Majeed akinirekodi, sikuonekana kuongea nikiwa na amani, nilikuwa na hofu sana.
Kitendo changu cha kuyainamia mafuvu yale nilikiona kuwa kitendo cha ujasiri sana. Mafuvu ambayo yalikuwepo mahali pale yalikuwa ni mafuvu ya tofauti tofauti. Kulikuwa na mafuvu ya watoto wadogo na pia kulikuwa na mafuvu ya watu wakubwa. Eneo hilo lilionekana kutokuwa na amani katika kipindi cha nyuma, kuna watu ambao walikuwa wameteketezwa kwa kupigwa risasi mahali hapo.
Mafuvu ya binadamu yalikuwa mengi mahali hapo, kwa idadi ya haraka haraka ya kuhesabu huku nikiwa na hofu, yalikuwa yakifikia hata mia tatu mahali hapo. Watu wengine ambao tulikuwa tukisafiri pamoja katika farasi wale walibaki wakiniangalia katika kipindi hicho ambacho nilikuwa nikitengeneza makala yangu.
Tulikaa mahali pale kwa takribani dakika arobaini na tano na ndipo tukaendelea na safari yetu. Moyoni nilikuwa na majonzi makubwa, hofu ambayo sikuwa nayo kabisa ikaonekana kuanza kunijia moyoni mwangu, kama pale mwanzo wa kuingia Al Junaynah kulikuwa na mafuvu ya watu ambao waliuawa kipindi cha nyuma, ingekuwa vipi katikati ya mji huo ambao mapigano yalikuwa makubwa zaidi? Kila nilichokuwa nikijiuliza nilikosa jibu kabisa.
Je nini kitaendelea?
Nimekwishaanza kuingia Darfuru, macho yangu yashaanza kukutana na vitu nisivyowai kuviona.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment