Simulizi : Makala Yangu Kutoka Darfur
Sehemu Ya Nne (4)
Kamera yangu ya picha za kawaida ilikuwa imetumika kwa kupiga picha zaidi ya kumi huku zikiwa zimebakia picha sitini hata kabla ya mkanda kuisha. Kwa wakati huo, kichwa changu kilikuwa na mawazo mengi sana, nilikuwa nikijifikiria juu ya mambo ambayo ningeweza kukutana nayo katikati ya jiji hilo la Darfur. Kwa mara ya kwanza toka nianze safari ya kuja hapo Sudan, moyo wangu ukaanza kuwa na hofu.
Kumbukumbu za mafuvu yale ambayo ulikutana nayo ziionekana kuniogopesha kupita kawaida, amani ikaanza kupotea moyoni mwangu huku ujasiri ambao nilikuwa nao ukianza kuyeyuka moyoni mwangu. Tuliendelea kwenda na wale farasi, sehemu ambayo tulikuwa tukipita ilikuwa jangwa moja kubwa, hakukuwa na nyumba nyingi sana.
Hapa labda ningependa kuzungumza kitu kimoja. Kwa sababu asilimia tisisni na nane ya nchi ya Sudan ilikuwa ni jangwa basi lilikuwa ni jambo la kawaida sana kukutana na wakinamama njiani wakiwa wamebeba mitungi ya maji huku wakionekana kutembea kwa mwendo mrefu sana kutokana na maji kuwa ya shida sana katika nchi nyingi zilizokuwa na majangwa. Bado tulikuwa tukiendelea na safari, kwa kipindi hiki, farasi hawakuwa wakikimbia, walikuwa wakitembea kwa mwendo wa kawaida tu.
Tukafika katika sehemu moja ambayo kulikuwa na miti zaidi ya ishirini ikiwa imesimamishwa kwa kuchomekwa mchangani. Nilibaki nikiwa nimeduwaa huku nikiwa nimeikodolea macho miti ile. Sikutaka kuendelea na safari, nilichokifanya ni kuwaambia watu ambao nilikuwa nao kwamba nilitaka kuona ni kitu gani ambacho kilikuwa kimetokea mahali pale mpaka miti ile kuchomekwa mchangani.
Kama kawaida yao, wote wakaonekana kuwa wabishi, hawakutaka kukubaliana nami kwamba twende kule na kuiona miti ile. Nilichokifanya mara baada ya kuwaona wanakataa, nikawakumbusha kwamba mimi nilikuwa ni mwandishi wa habari ambaye nilikuwa na wajibu wa kufahamu vitu vingi kuhusianana kitu chochote ambacho nilitakiwa kukifahamu.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kuwa mwandishi wa habari katika nchi kama ya Sudan kulikuwa na uzuri wake, watu walikuwa wakikusikiliza sana, hii ilitokana na sababu kwamba waliamini kama wewe mwandishi ungekuwa unaelezea mambo mengi ambayo yalikuwa yakitokea katika nchi hiyo basi ingekuwa rahisi kwako kwenda kwenye vyombo vya habari na kutangaza na hatimae kupata msaada kutoka katika nchi za Magharibi.
Nikaruka kutoka katika farasi ambaye nilikuwa nimempanda na moja kwa moja kuanza kuelekea katika sehemu ile ambayo ilikuwa na miti ile huku nikiongozana na Majeed huku wale watu wengine wakiwa wanatusubiria. Nilichokifanya ni kuchukua kamera yangu na kuanza kupiga picha huku tukizidi kuisogelea miti ile.
Hatua ishirini hata kabla hatujaifikia miti ile, macho yetu yakatua katika maganda mbalimbali ya risasi ambazo zilikuwa zimekwishatumika. Mwili wangu niliuhisi kusisimka kupita kawaida. Maganda yale yalikuwa mengi sana pale chini. Sikuacha kitu chochote kile, nikaanza kupiga picha maganda yale ya risasi na kisha kuanza kusogea kule kulipokuwa na miti ile.
Kama ilivyokuwa njiani na ndivyo ilivyokuwa pale, mafuvu ya watu yalikuwa yakionekana katika miti ile mchangani jambo ambalo lilizidi kuniongezea hofu zaidi. Sudan kwangu ikaonekana kuwa kama jehanamu, nilikuwa nikihofia kupita kawaida kiasi ambacho wakati mwingine nilikuwa nikitetemeka waziwazi.
“Haya ni mafuvu ya watu ambao walikuwa wamefungwa katika miti hii, pale tulipoyaona maganda ya risasi ndipo ambapo wapigaji risasi walipokuwa wamesimama na kuwalenga huku wakiwa wamewafunga katika miti hii” Majeed aliniambia.
Sidhani kama kuna siku ambayo niliumia kama kipindi kile, nilimwangalia Majeed na bila kutegemea, machozi yakaanza kunitoka. Moyoni niliumia kupita kawaida kiasi ambacho kichwa changu kikaanza kutengeneza picha ya watu ambao walikuwa wamefungwa katika miti ile na kisha kumiminiwa risasi.
Kitu ambacho kilikuwa kimeniumiza zaidi ni kwamba katika mafuvu yale pia kulikuwa na mafuvu ya watoto, hali ilionyesha kwamba hata watoto nao walikuwa wamefungwa katika miti ile na kisha kumiminiwa risasi. Hiyo ndio hali ambayo nilikutana nayo, sikutaka kuendelea kujiuliza, hapo hapo Majeed akaanza kunichukua na kamera ile kubwa huku nikielezea kile ambacho kilikuwa kimetokea mahali pale huku akijaribu pia kuipiga video kamera mafuvu yale.
Hatukukaa sana mahali pale, bado tulikuwa na safari ndefu ya kuingia katikati ya jiji hilo la Darfur. Moyo wangu uliendelea kuwa katika maumivu makali sana, macho yangu yalikuwa makavu lakini niliusikia moyo wangu ukiwa unalia kabisa. Sikutarajia kukutana na mambo kama yale, kwangu nilitarajia kukutana na miili au mafuvu lakini sikujua kama ningehisi kitu kama kile.
Safari iliendelea zaidi mpaka kufika kaika sehemu ambayo ilionekana kuwa na kijiji, nikamshukuru Mungu wangu, wote tukaanza kuelekea kaika kijiji kile. Wenyeji wa kijiji kile walionekana kutushukuru, kitu ambacho walikuwa wakikijua ni kwamba tulikuwa tumekwenda na chakula kwa ajili ya kuwasaidia kutokana na njaa kubwa ambayo walikuwa nayo, ila hatukuwa na kitu chochote kile zaidi ya vidumu vyetu vidogo vya maji na chakula cha kututosha kwa muda wa siku nne ambazo tungekuwa kule.
“Hapa ni wapi?” Nilimuuliza Majeed.
“Hapa ni Zahor. Hii ni sehemu ambayo nayo ilikumbwa sana na maafa haya ya vita” Majeed aliniambia.
Nikaendelea kuyapitisha macho yangu kwa wakazi wa kijiji kile, moyoni niliumia zaidi, sikuamini kama kuna watu ambao walikuwa katika mateso makali namna ile. Watoto walikuwa wembamba sana hali iliyonionyeshea dhahiri kwamba walikuwa wakiumwa mtapia mlo. Miili ilikuwa membamba sana ila matumbo yao yalikuwa makubwa.
Vichwa vyao vilionekana kuvimba, macho yao yalikuwa makubwa, mbaya zaidi hata mavazi hawakuwa nayo ya kutosha zaidi ya kaptura ambazo walikuwa wamezivaa. Wanawake wa kijiji kile ambao walikuwa wamejifungua, matiti yao hayakuwa yakitoa maziwa na kwa wale ambao walikuwa wakitoa maziwa katika matiti yao, maziwa hayakuwa meupe kama ya wanawake wenye afya, maziwa yale yalikuwa na unjano mwingi.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilishindwa kuvumilia kabisa, kama kuumia nadhani siku hiyo niliumia zaidi na zaidi, machozi yakaanza kunitiririka mashavuni mwangu. Nilipiga picha maeneo mbalimbali pamoja na kuwapiga picha watu ambao walikuwa katika kijiji kile cha Zahor. Nilipoona kwamba nimeridhika na upigaji wa picha, nikataka pia kurekodiwa na kamera kubwa na hivyo Majeed kuchukua kamera ile na kisha kuanza kunirekodi.
Sikupata tabu sana kutoka na kuwepo kwa wazee kadhaa ambao walikuwa wakiifahamu lugha ya Kingereza, nikaanza kuwahoji. Niliongea nao sana, katika kila neno ambalo walikuwa wakiniambia lilikuwa likiniumiza sana, nilikuwa nikijikaza kulia kwa sababu nilikuwa mbele ya kamera.
“We don’t have food anymore. We always eat doka with our family (Hatuna chakula kabisa. Mara kwa mara tunakula doka pamoja na familia zetu)” Mzee mmoja ambaye alijitambulisha kwa jina la Yakeen aliniambia.
“What is doka? (Doka ni nini?)” Nilimuuliza.
“Let me show you (Ngoja nikuonyeshee)” Mzee Yakeen aliniambia.
Hapo hapo akaondoka na kuelekea ndani ya nyumba ile, alipotoka, alitoka huku akiwa na majani fulani ambayo akanikabidhi na kisha kunitaka nile jani moja. Nikaliingiza mdomoni, jani lile lilikuwa chungu sana, halikuwa na utamu hata mara moja. Kwa wale watu wa Tanga ambao wanapenda sana kula mboga ya Mchunga watakuwa wanafahamu zaidi.
Majani yale yalikuwa ni machungu sana hata zaidi ya mboga ya mchunga, sikuweza kulitafuna jani lile, nikalitoa kutoka mdomoni. Ulimi wote nikauhisi ukiwaka moto, uchungu wote ukawa umehamia katika mdomo mzima Katika maisha yangu niliwahi kula kitu cha uchungu namna ile si kama ilivyo doka.
Kadri muda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo mdomo wangu ulivyozidi kuwa mchungu mpaka kufikia hatua ya kuwaomba maji. Baada ya sekunde ishirini nikaletewa maji yakiwa katika kikombe kilichoonekana kuwa kichafu, nilipoyaangalia maji yale, sidhani kama kulikuwa na watu ambao walikuwa wakinywa maji yale katika dunia hii.
Maji hayakuwa masafi hata kidogo, maji yalikuwa machafu kupita kawaida. Nikabaki nikiyaangalia maji yale. Mdomo ulikuwa mchungu na nilikuwa nikihitaji sana kunywa maji, ila maji ambayo nilikuwa nimeletewa mahali pale, yalikuwa ni maji machafu sana, sikujiuliza zaidi, nikayanywa maji yale huku nikifumba macho yangu.
Hayo ndio maisha ambayo walikuwa wakiishi watu wa hapo Zahor, walikuwa wakiishi maisha ya tabu sana. Yale majani ambayo kwangu nilikuwa nikiyaona kuwa machugu, kwao yalionekana kuwa matamu, maji yale ambayo nilikuwa nikiyaona kuwa machafu, kwao yalionekana kuwa masafi sana.
Hatukuendelea zaidi na safari, tulichokitaka ni kuendelea kukaa mahali pale japo kwa siku moja zaidi. Vichwani mwetu hatukujua kile ambacho kingeweza kutokea mahali pale, kama tungelewa kile ambacho kingetutokea kesho yake asubuhi, nadhani tungeondoka kijijini hapo jioni hiyo hiyo.
Bado kuna mambo mengi ambayo ningependa uyafahamu kuhusiana na hii Darfur ambayo huwa unaisikia tu katika vyombo mbalimbali vya habari. Nchi hii ilifanana na Iran au nchi yoyote ambayo ilikuwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa kipindi kirefu sana. Siku hiyo akili yangu ikawa kama imeonyeshwa kitu kingine, picha ambayo inaonekana katika upande wa pili katika maisha ya binadamu.
Maishani mwangu sijawahi kuishi kwa wasiwasi hata kidogo lakini ndani ya nchi ya Sudan, nilikuwa nikiishi kwa wasiwasi sana kwani muda mwingi nilikuwa kama mtu ambaye alikuwa ameshika roho yake mkononi mwake na muda wowote ule ingeweza kumtoka. Maisha ya watu waliokuwa wakiishi hapo Zahor yalikuwa ni ya kuhuzunisha sana, moyoni niliumia kupita kawaida.
Japokuwa nchini Tanzania kuna sehemu ambazo watu wanasema zina njaa kali lakini nadhani kwa hapo Zahor mambo yalikuwa ni zaidi ya njaa kali. Kama kuna wengine mmesahau subiri niwakumbushe kitu kimoja kwamba hapo nilipokuwa tayari nilikuwa nimeingia Darfur. Yaani ilikuwa ni kama unataka kwenda Dar es Salaam halafu umefika Kimara na mapigano makubwa zaidi yalikuwa posta (mjini), hiyo ndivyo ilivyokuwa hapo Zahor.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Zahor ilikuwa ni sehemu ya Darfur ila haikuwa sehemu ambayo mapigano yalikuwa makubwa sana kama ilivyokuwa Al Junaynah. Mimi kama mimi nilikuwa nikitaka sana kwenda huko Al Junaynah, sehemu ambayo mapigano yalikuwa makali kabisa. Kwa waandishi wengi wa habari kutoka katika vyombo mbalimbali vya habari kutoka katika mashirika makubwa ya habari duniani walikuwa wakikataa kwenda Al Junaynah kutokana na waandishi wengi wa habari kuuawa huko.
Maisha ya huko yalionekana kutisha kupita kawaida lakini mwisho wa siku nami nikatamani kuelekea huko bila kuogopa kitu chochote kile. Kama utakuwa unakumbuka vizuri ni kwamba niliondoka nyumbani huku kichwani mwangu nikifikiria kitu kimoja tu, kuwa na ndoto ya kuwa mwanadishi mkubwa wa habari kutoka katika vyombo vya habari mbalimbali duniani.
Watu walikuwa wakitaka kufahamu hali halisi ambayo ilikuwa ikiendelea Darfur, dunia haikutaka kufichwa tena juu ya hali halisi ambayo ilikuwa ikiendelea huko na ndio maana mimi leo hii nilikuwa huko. Sikutaka kuishia hapo Zahor, nilitaka kusonga mbele huku nikitaka kuona kila kitu kama ambavyo nilitaka kurekodi makala yangu na kisha kuirusha hewani.
Hapo Zahor siku hiyo ilikuwa ni balaa, joto lilikuwa kali sana kitu ambacho kilitufanya kulala nje. Usiku sikupata usingizi, moyo wangu ulikuwa na shauku kubwa ya kutaka kufika huko Al Junaynah na kutaka kuona kile ambacho kilikuwa kikiendelea. Kwa sababu nilikuwa nimefanya kazi ya kujitolea, katika kipindi hicho sikutakiwa kuhofia milio ya bunduki, sikutakiwa kuogopa kitu chochote kile, yaani hata kama kungekuwa na mtu ambaye angenifuata na kuniwekea mdomo wa bunduki mbele ya uso wangu, sikutakiwa kuogopa kitu chochote kile.
Naweza kusema kwamba usiku huo wala haukuonekana kuwa usiku wa amani hata mara moja. Nakumbuka vizuri ilipofika saa nne kama na robo hivi kwa mbali tukaanza kusikia sauti za watu. Kulikuwa na giza sana mahali pale hivyo hatukujua ni watu gani ambao walikuwa wakija kule tulipokuwa.
Sauti za farasi zikaanza kusikika, tayari wenyeji wakaonekana kufahamu ni watu gani ambao walikuwa wakija mahali hapo. Nikaanza kuwaona wenyeji wakiinuka na kisha kuanza kuelekea ndani. Ni kweli nilijipa ujasiri mkubwa sana lakini katika kipindi hicho mambo nikayaona yakianza kubadilika. Tayari nilijua fika kwamba hatari ilikuwa imeingia na ndio maana wenyeji walikuwa wamekimbia mahali hapo.
Ndani ya sekunde thelathini, pale nje nilikuwa nimebaki na Majeed tu ambaye muda wote toka tulipokuwa hapo Zahor alikuwa akitetemeka kana kwamba alijua kwamba angekufa muda wowote ule.
“Tuondoke” Majeed aliniambia.
Sikutaka kubaki, tayari niliona kwamba kulikuwa na hatari ambayo ingeweza kutokea, nikasimama na kisha kuanza kuondoka nae kuelekea katika moja ya nyumba ambayo ilikuwa mahali hapo. Tulipoifikia nyumba ile tukaanza kuusukuma mlango lakini wala haukufunguka hali iliyoonyesha kwamba ulikuwa umefungwa kwa ndani. Tukatoka na kuelekea katika mlango wa nyumba nyingine lakini napo kulikuwa vile vile.
Kwanza tukaonekana kuchanganyikiwa kupita kawaida, tayari tukaona kwamba kulikuwa na hatari ambayo ingeweza kutokea mahali hapo. Kwenye kuangalia huku na kule tukauona mlango wa nyumba moja ukiwa wazi kwani ulikuwa ukijibamiza bamiza sana, tukaanza kuufuata mlango wa nyumba ile. Tulipoufikia, tukaingia ndani, kwa nje tulifikiri ni nyumba ambayo walikuwa wakiishi ndani ila tulipoingia tu, tukakutana na wanyama mbalimbali kama ng’ombe, mbuzi na ngamia wanne.
Tulikaa katika nyumba ile ambayo kwa hapa ningependa kuiita zizi ingawa ilikuwa kama nyumba ya kawaida. Tulikaa mule kwa dakika kadhaa na ndipo tukaanza kusikia vishindo vya watu na farasi ambao walikuwa wakipita nje, tukabaki kimya kabisa. Sijajua ni kwa nini watu wa pale Zahor walikuwa wakiwaogopa watu hao. Kichwani mwangu kulikuwa na maswali mawili ambayo niliona kwamba ni lazima niwaulize watu wa hapo Zahor kuhusiana na watu hao ambao walikuwa wamewakimbia.
Swali la kwanza lilikuwa ni kuhusiana na sababu ambazo ziliwafanya kuwakimbia watu hao na la pili lilikuwa ni kutaka kufahamu watu hao walikuwa wakina nani. Hayo ndio maswali mawili ambayo niliyapanga kuyauliza mara itakapofika asubuhi kwani niliamini kwamba nayo yangekuwa katika mchakato wa kukamilisha makala yangu ambayo nilipanga kuiandika katika kipindi hicho.
Hatukulala kabisa, usiku mzima tulikuwa macho na wala hatukuwa tukiongea kwa kudhania kwamba watu wale bado walikuwa nje ya eneo la nyumba zile. Ilipofika saa kumi na moja alfajiri, mwanga ukaanza kuonekana na kisha kutoka nje. Kwanza njaa ilikuwa imenishika sana kwa sababu jana yake sikuwa nimekula chochote kile. Nilikuwa nikifikiria namna ya kupata chakula lakini wala sikuona njia yoyote ya kuweza kupata chakula asubuhi hiyo.
“Nitakufa” Nilimwambia Majeed.
“Kwa nini?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nasikia njaa sana. Yaani njaa imenikamata mpaka naona tumbo linauma” Nilimwambia Majeed ambaye alikuwa akiniangalia kwa macho ya kunionea huruma.
Tulikuwa tumekaa huku tukiwa hatufahamu ni kwa namna gani tungeweza kupata chakula mahali hapo. Baada ya dakika kama thelathini hivi, wenyeji wakatoka. Kwanza kila mtu akaonekana kutushangaa, walichokuwa wakikifikiria ni kwamba tulikuwa tumeuawa na watu ambao walikuwa wamekuja usiku uliopita mara baada ya kutuacha mahali pale.
“Hawakutuona. Tuliondoka na kuelekea katika nyumba ile” Niliwaambia huku nikinyooshea kidole ile nyumba ambayo kwangu ilionekana kuwa kama zizi.
“Siku nyingine mnapowasikia naomba msikae nje” Mzee yule ambaye alikuwa akifahamu lugha ya Kingereza aliniambia.
“Kwa nini? Kwani wale ni nani?” Nilimuuliza maswali mawili mfululizo.
“Wale ni wafuasi wa waasi wa Darfur Liberation Front” Mzee yule alituambia.
“Na wamekuja kufanya nini hapa?” Nilimuuliza.
“Huwa wanakuja huku kwa ajili ya kuhakikisha usalama” Mzee yule alituambia.
“Kuhakikisha usalama kivipi na wakati wao ni waasi?”
“Hawa huwa wanapigana na wanajeshi wa serikali pamoja na wale wa Umoja wa Afrika. Hawataki wanajeshi hao waingie ndani ya Darfur na ndio maana huwa wanazunguka zunguka” Mzee yule alituambia.
“Sasa kwa nini mlikimbia?”
“Huwa hawataki watu walale nje, wanataka watu wote wawe wanalala ndani kwa kuhofia kuchangamana na maadui zao”
“Na kama wangetukuta nje ingekuwaje?”
“Wangewaua”
“Kwa nini?”
“Sijui ila hiyo ndio sheria yao” Mzee yule alinijibu.
Hapo nikajihesabia kuwa kama mfu aliyekuwa akitembea, nikapata uhakika kwamba nilikuwa natembea huku roho yangu ikiwa mkononi mwangu kwa kuona kwamba kama ningejifanya kupuuzia mambo mengine basi ni mwili wangu tu ndio ungeweza kurudi nchini Tanzania au kuzikwa huko huko jangwani.
Maswali yaliyofuata mahali hapo ni kuulizia chakula. Hakukuwa na chakula cha kueleweka hapo Zahor, walituletea tende tu ambazo tukaanza kuzila mpaka pale ambapo nilijiona kuwa na unafuu kidogo tumboni mwangu.
Siku hiyo tulipanga kuondoka mahali hapo saa nne asubuhi kuendelea na safari yetu ya kuelekea Al Junaynah. Kila mtu alikuwa akitushangaa kwamba tulikuwa na moyo kiasi gani mpaka kudiriki kutaka kwenda Al Junaynah na wakati sehemu hiyo ilikuwa na vita vikali ambavyo vilikuwa vikiendelea?
Sikuonekana kujali, dhumuni langu katika kipindi hicho lilikuwa ni kuelekea huko kwa ajili ya kuandika makala yangu kwa kina zaidi. Huku likiwa limebakia saa moja kabla ya kuanza safari yetu, kwa mbali tukaanza kuwaona watu ambao walikuwa wakija kule tulipokuwa huku wakiwa na farasi zaidi ya kumi.
Kwanza kila mtu akaonekana kuogopa. Kwa hapa ngoja nikwambie kitu kimoja. Hapo Zahor hakukuwa na maisha ya amani hata kidogo, muda wote watu walikuwa wakiishi na mashaka kutokana na wanajeshi wa waasi ambao walikuwa wakifika mahali pale kila siku. Hatukuwa na cha kufanya, tulichokifanya ni kuanza kuwasubiri ili kujua walikuwa wakihitaji kitu gani mahali pale.
“Tukimbie” Majeed aliniambia huku akionekana kuwa na hofu.
“Tuelekee wapi?” Nilimuuliza.
“Popote pale” Majeed aliniambia.
Hilo likaonekana kuwa suala gumu sana kukubalika moyoni mwangu. Ilikuwaje tukimbie na wakati watu wale walikuwa wamekaribia kabisa na mahali pale. Nilichomwambia ni kwamba tulitakiwa tuendelee kubaki mahali pale huku tukitaka kuona ni kitu gani ambacho kingeendelea.
Watu wale wakafika, kitu cha kwanza wakaanza kuangalia huku na kule, sisi tukabaki kimya huku tukionekana kuwa na hofu kupita kawaida. Wakateremka kutoka migongoni mwa farasi wao na kisha kuanza kutuangalia. Hofu…hofu…hofu ilikuwa imenishika sana, sikuamini kama siku hiyo ndio ambayo ningeweza kuonana na baadhi ya watu ambao waliifanya Darfur kuchafuka namna ile.
Machoni mwao, watu wale hawakuonekana kuwa chembe ya huruma, walionekana kuwa watu ambao walikuwa makini sana katika kazi zao hasa za umwagaji wa damu. Mavazi yao yalikuwa yakiniogopesha zaidi, kwani yalikuwa na chembechembe za damu ambazo zilionekana kuganda.
“Wewe ni nani?” Mwanaume ambaye alionekana kuwa kiongozi aliniuliza.
“Iqram Ibrahim, mwandishi wa habari kutoka Al Jazeera” Nilimjibu mwanaume yule.
“Lete kitambulisho chako” Mwanaume yule aliniambia na kwa haraka sana kufanya hivyo, nikamgawia kitambulisho changu.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Watu wote walikuwa kimya, bunduki ambazo nilikuwa nikiziangalia zilikuwa zikinitetemesha kupita kawaida. Moyo wangu ulikuwa na woga mkubwa sana, sikuamini kama mtu yule angeweza kuniacha hai katika kipindi hicho. Macho yake yalikuwa yakikiangalia kitambulisho kile kwa makini zaidi. Hofu ikanizidi zaidi kwa kuona kwamba endapo angejua kwamba kile kitambulisho kilikuwa ni cha bandia basi angeweza kunipiga risasi pale pale.
“Una bahati” Mwanaume yule aliniambia huku akinirudishia kitambulisho kile.
“Ungekuwa mwandishi kutoka mashirika ya Ulaya au Marekani, ningekuu hapa hapa” Mwanaume yule aliniambia.
Kwa jinsi nilivyokuwa nikijisikia katika kipindi hicho ilikuwa ni balaa, mapigo yangu ya moyo yalikuwa yakidunda kwa kasi sana, kasi ambayo sikuwahi kuyahisi yakidunda namba hiyo toka nizaliwe. Muda wote nilikuwa kimya tu, jasho lilikuwa likinichirizika kupita kawaida. Baada ya kutulia kwa kipindi cha dakika kadhaa, nikajipa nguvu upya, nikajiona kama nilikuwa ninatakiwa kufanya kitu kimoja.
“Samahani mkuu” Nilimwambia mwanaume yule huku kila mwanajeshi akiwa amenielekezea bunduki kwa kuona kwamba inawezekana ningemdhuru kwa jinsi nilivyokuwa nimefuata.
“Kuna nini?” Aliniuliza huku akionekana kukasirika japokuwa sikuwa nimemkasirisha.
“Nataka kwenda Junaynah” Nilimwambia kwa sauti ya ukakamavu iliyokuwa na woga kwa mbali.
“Kufanya nini?”
“Kukamilisha kazi yangu”
“Kazi gani?”
“Ya uandishi wa habari” Nilimjibu.
Nahisi Mungu alikuwa upande wangu na alikuwa akinitetea sana. Kabla ya kuongea kitu chochote kile, mwanaume yule akawageukia wenzake na kisha kuanza kuwaaangalia. Akaamuru mwanaume mmoja anifuate na kisha kuniamuru nipande juu ya farasi wa mtu huyo aliyemuita huku akimanza kuongea nae kwa Kisudan, lugha ambayo wala sikuielewa kabisa.
“Huyu mtu atakupeleka mpaka Junaynah” Mwanaume yule aliniambia.
“Ila tupo wawili” Nilimwambia.
“Wawili?”
“Ndio”
“Na nani?”
“Mtu wa kunishikia kamera” Nilimwambia mwanaume yule ambaye akaamuru mwanaume mwingine aje na farasi na kututaka tuondoke mahali hapo kwani kulikuwa na kazi ambayo alitaka kuifanya.
Mimi na Majeed tukapanda katika farasi wale na wale jamaa na kisha kuondoka mahali hapo. Sikuwa nikiyaamini macho yangu kwamba nilikuwa nimekutana na waasi na mwisho wa siku nilikuwa nimeachwa huru. Sikujua ni kitu gani ambacho kilitokea nyuma kwani nikaanza kusikia milio ya risasi, wanawake wakaanza kulia kitu ambacho kiliniuma kupita kawaida kwa kuona kwamba watu wale walikuwa wamefanya mauaji ya kuwamiminia risasi baadhi ya watu waliokuwa mahali pale.
Safari ilikuwa inaendelea, safari ilikuwa ndefu sana, tulitumia siku mbili huku tukila mikate ya wanajeshi wale na kisha kuanza kuingia hapo Al Junaynah, sehemu ambayo nilikuwa nikitaka kufika na kisha kufanya kazi yangu rasmi. Hapa sijui nieseme nini, nadhani kweli hii sehemu ilistahili kukimbiwa na waandishi wa habari, nadhani mji wa Al Junaynah haukuwa mji wa amani hata kidogo, kwa muonekano wake tu ukanifanya nijute safari yangu ya kwenda Darfur….Oooh! My God! Kwa nini niliamua kwenda Darfur na kuingia ndani ya mji wa Al Junaynah? Nilitamani nipate mabawa na kuruka kurudi nchini Tanzania au kama haiwezekani basi nipotee kama mchawi na kuibukia Tanzania, picha ambazo zilikuwa zikionekana huko, kulikuwa na uhalali wa watu kukataa kwenda huko, nikajisikitikia mimi, nikamsikitia na Majeed pia, nilitamani kumuomba msamaha kwa ushawishi wangu uliomfanya kuelekea Al Junaynah, sehemu ile haikuonekana kuwa na amani kabisa, kama ni filamu, nadhani ilikuwa ni bora ya kuangalia filamu zile za SAW kuliko yale ambayo nilianza kuyaona hapo A Junaynah, mwili ulinisisimka kupita kawaida.
“Mungu nipe nguvu na uniondolee hofu moyoni mwangu” Nilisali kimoyo moyo, sala ambayo ilionyesha kwamba nilikata tamaa ya kuendelea kuishi kwani hali ilikuwa inatisha sana.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Je ni mambo gani nimeanza kuyaona mahali hapo?
Je nilikufa?
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment