Simulizi : Makala Yangu Kutoka Darfur
Sehemu Ya Tano (5)
Damu zilikuwa zimetapakaa katika maeneo mbalimbali mahali hapo. Kuta za nyumba ambazo zilikuwa zimejengwa katika eneo ambalo tulilokuwepo katika kipindi hicho zilikuwa na damu nyingi, tena damu mbichi ambazo zilionyesha kwamba si muda mrefu watu walikuwa wameuawa mahali hapo.
Hofu ikanishika moyoni, sikuamini kile ambacho nilikuwa nakiangalia, wakati mwingine nilijiona kama nipo katika usingizi mzito ambao ulisababisha niwe na ndoto moja mbaya na ya kutisha sana. Maganda ya risasi yalikuwa yametapakaa katika barabara ambayo tulikuwa tukipita na farasi, mwili wangu ulikuwa ukinitetemeka sana kiasi ambacho wakati mwingine nilikuwa nikijutia sababu ambayo ilinifanya kuelekea katika nchi ile kwa ajili ya kutengeneza makala yangu.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wanajeshi wa waasi walikuwa wametapakaa huku wakiwataka watu kuendelea na kazi zao kama kawaida. Nyuso zao zilionyesha kwamba hawakuwa na woga hata mara moja, kila kitu ambacho kilikuwa kikionekana kwao kilikuwa kitu cha kawaida sana. Tulikwenda na wale farasi mpaka tukafika katika eneo moja ambalo lilionekana kuniogopesha zaidi. Ukiachilia mbali damu ambazo zilikuwa zimetapakaa, pia kulikuwa na viungo vya watu barabarani kama mikono, miguu na wakati mwingine mpaka vichwa vya watu ambao walikuwa wamechinjwa.
Ile ikaonekana kuwa picha ya kutisha sana, nilichokifanya ni kuchukua kamera yangu na kisha kuanza kupiga picha huku nikitetemeka na wakati mwingine nikijisikia kutapika. Hapa ningependa kuongea kitu kimoja na nieleweke kwa watu wote wanaosoma haya ninayoandika.
Unaposikia sehemu fulani kuna vita, wewe acha tu vita viendelee huku ukiendelea kumuomba Mungu awaepushie na vita hivyo. Hapo ndipo nikaanza kuwaona watu wengine kuwa wapumbavu sana, baadhi ya Watanzania ambao mara zote wamekuwa wakilalamika na kusema kwamba ilikuwa ni heri vita vya kidini viingie nchini ili ijulikane nani bingwa.
Vita si mchezo, unaposikia mwenzako yupo vitani usiombee vikukute. Mambo yalikuwa yakitisha sana, ninakuhadithia haya huku nikitamani kile ambacho nilikuwa nikikiona machoni mwangu basi na wewe ukione na kuhisi kile nilichokuwa ninakihisi. Tulivyozidi kwenda mbele na ndipo tukafika katika eneo moja ambalo lilikuwa na maiti nyingi ambazo zilikuwa zimezagaa hovyo, katika eneo hili, kulikuwa na harufu mbaya na kali sana, harufu ambayo ilinishinda kuvumilia na kuanza kutapika.
Hapo ndio ulikuwa mwisho wa safari yetu. Jamaa wale wakatuambia tushuke kutoka katika farasi wale na kisha kutupeleka kwa baadhi ya wanajeshi wa waasi ambao walikuwa pembeni na kunitambulisha kwamba nilikuwa mwandishi wa habari kutoka katika kituo cha habari cha Al Jazeera, moja ya kituo kilichokuwa Uarabuni.
Wakaniomba kitambulisho changu nami nikawapa na kuanza kukiangalia. Nilichokuwa nimekigundua zaidi ni kwamba wanajeshi wa waasi hawakuwa wakiwapenda kabisa waandishi kutoka katika mashirika ya habari kutoka Uingeza, Marekani au nchi nyingine za Ulaya. Waliponiona kwamba nilikuwa mwandishi wa habari wa kituo cha Al Jazeera, wakaamua kuniacha na kunipa saa moja tu ya kufanya kazi mahali hapo.
Nikampa kamera Majeed na kisha kuanza kutangaza kile ambacho kilikuwa kimeendelea pale Darfur. Sikutangaza kwa amani kwani macho ya wanajeshi wa kundi la waasi walikuwa wakiniangalia kwa mtazamo ambao ulinitia wasiwasi sana. Majeed hakutofautiana na mimi, nae alikuwa akihofia uhai wake, mazingira ya mahali pale hayakuonekana kuwa ya amani kabisa.
Niliendelea na kipindi kile kwa muda wa saa moja, nilikuwa natangaza huku nikionekana kuumizwa na kile kilichokuwa kikionekana mahali pale. Nilitangaza pamoja na kupiga picha huku nikiwaoba wale wanajeshi wa waasi nipige nao picha, wakakubaliana nami jambo ambalo lilionekana kunifurahisha sana.
Siku hiyo hiyo hatukutaka kubaki mahali hapo, harufu kali pamoja na uwepo wa maiti zile ulionekana kutuogopesha kupita kawa, hivyo tukaondoka na kurudi kule Zahor. Mambo mengi ambayo nilikuwa nikiyataka yakawa yamekamilika na hivyo nilitakiwa kurudi nchini Tanzania huku nikiwa salama kabisa.
Sikutaka kukaa sana Zahor, tukaonganisha safari mpaka baada ya siku nne kufika Al Fashir ambapo tukaonganisha mpaka Nyara. Kwa ujumla tuliendelea na safari ile na baada ya siku sita ndipo tukaingia Khartoum. Mpaka kufikia hapo tayari nilikuwa nimeona mambo mengi sana ambayo yalikuwa yameniogopesha upita kawaida.
Nilichokifanya kwa wakati huo ni kuonana na mwandishi mmoja wa habari wa BBC na kumuelezea kila kitu kilichokuwa kimetokea. Kwanza alifurahia na pia alikuwa akitaka nimuachie makala yangu ile jambo ambalo wala sikuwa na shaka nalo. Sijui kwa sababu gani nilitokea kumwamini mwandishi yule aliyejitambulisha kwa jina la Michael Penn, mwandishi wa shirika la habari la BBC ambaye nae alikuwa amefika mahali hapo lakini aliogopa kuelekea Darfur kwa sababu ya kuhofia mauaji.
Penn akaniambia kwamba angefanya kila linalowezekana ili nikamilishe kile ambacho nilikuwa ninakitaka katika maisha yangu. Akanitoa wasiwasi sana kwa kuongea nami kuhusiana na mambo mengi sana na ndio maana hata aliponiambia kwamba anataka kwenda na makala yangu ile nchini Uingereza wala sikubisha hata kidogo kwa kujua kwamba ni lazima angekuwa ngazi ya mimi kuwa mwandishi mkubwa wa habari.
Baada ya siku moja kukaa hapo Khartoum ndipo nikaanza safari yangu ya kurudi nchini Tanzania huku nikiwa nimemuachia Majeed paundi milioni moja na huku nikimuahidi kuwa nae katika mambo mengi hasa masomo yake. Ndani ya ndege nilikuwa nikifikiria namna ya kujitetea kwa wazazi wangu kwa uamuzi ambao nilikuwa nimeuchukua wa kutoroka na kuelekea nchini Sudan.
Sikuacha kumfikiria mpenzi wangu, Myra ambaye nafikiri katika kipindi hicho alikuwa na wasiwasi sana juu ya maisha yangu nchini Sudan. Ndege ile ilichukua zaidi ya masaa sita angani na ndipo ilipotua nchini Tanzania na kisha kuanza kuelekea nyumbani.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Niliingia nyumbani saa kumi na moja jioni. Kwanza ile kukutana na mama tu, akaanza kunilalamikia kwa kile ambacho nilikuwa nimekifanya. Wala sikujuta kwani kile ambacho nilitaka kukifanya nilikuwa nimekwishakifanya. Mama hakuonekana kuridhika, akampigia simu baba na kisha kumwambia kwamba nilikuwa nimekwisharudi, baba akaacha kazi zake na kuja nyumbani.
“Wewe ni mpumbavu sana” Baba aliniambiwa kwa sauti ya ukali.
“Naomba unisamehe baba”
“Wewe ni mpumbavu mkubwa Nyemo. Kwa nini utoroke nyumbani?” Baba aliniuliza ka ukali.
Sikuwa na la kujitetea, nilijua kwamba nilifanya makosa kwa ule uamuzi ambao niliuchukua lakini katika kipindi hicho nilijiona kuwa shujaa, shujaa ambaye angeielezea dunia kwa kile kilichokuwa kimetokea. Kwanza sikutaka kuwaambia wazazi juu ya kile kilichokuwa kimetokea kwani hawakuonekana kutaka kunisikiliza.
Siku hiyo nilishinda chumbani na baada ya muda kumpigia simu Myra ambaye alikuja nyumbani na kupitiliza mpaka chumbani kwangu. Machozi yalikuwa yamejikusanya machoni mwake, hakuamini kuniona nikiwa hai kwa mara nyingine, akashindwa kuvumilia na kunikumbatia.
“Kwa nini ulitoroka?” Myra aliniuliza huku akiwa amenikumbatia.
“Sikuwa na jinsi” Nilimjibu huku nami nikimkumbatia.
Nikajiona kama mwanajeshi ambaye alikuwa amerudi kutoka vitani na ushindi mkubwa na hivyo Myra alitakiwa kunipa zawadi ya ushindi. Ndani ya dakika chache tukawa watupu.
Bado kumbukumbu zangu za Darfur ziliendelea kuwepo kichwani mwangu na hata nilipowaelezea wazazi wangu yale niliyokuwa nimeyaona kule, mama alibaki akilia huku baba aliyekuwa akijifanya mgumu machozi kuanza kumlenga.
Maisha ya Darfur yalikuwa mabaya, maisha ya Darfur yalikuwa yakitisha sana kupita kawaida. Machoni mwangu nikawa nimekwishawahi kuiona nchi ambayo ilikuwa ikiteseka kwa ajili ya vita vya wenyewe kwa wenyewe na ndio maana nakuwa na nguvu ya kusimama na kuwaambia kwamba vita ni hatari na kamwe usiombee vitokee nchini mwako.
Maiti za watoto na wanawake ambayo walikuwa wajawazito zilikuwa zikiendelea kujirudia kichwani mwangu. Sikuweza kusahau kwani mambo yale niliyaona kwa macho yangu na si kuambiwa na mtu, ila yote kwa yote, vita vinatisha sana na ndio maana sikushtuka nilipoambiwa kwamba kulikuwa na mwanamke alimbeba mbwa mgongoni kwa kudhani kwamba alikuwa mwanae na kukimbia nae kwa zaidi ya kilometa mia moja na kugundua kwamba alimbeba mbwa na si mtoto wake katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Rwanda mwaka 1994.
“Kwa nini umemuamini tu kirahisi sana Nyemo? Au kwa sababu ni mzungu?” Baba aliniuliza kuhusiana na Penn.
“Hapana. Nimemwamini kwa sababu ni mwandishi wa habari wa kimataifa” Nilimjibu.
“Hata kama. Sasa akikimbia nayo?”
“Atakuwa anajisumbua kwani ushahidi ninao”
“Ushahidi gani?”
“Majeed” Nilimjibu baba.
Kila siku macho yangu yalikuwa ni kuangalia BBC kwa kuamini kwamba ningeweza kuiona makala yangu ile kuhusiana na Darfur lakini wala sikuiona. Nilichokifanya ni kuanza kuwasiliana na Penn kwa njia ya barua pepe lakini nae alikuwa kimya kabisa. Nikaonekana kukata tamaa kwa kuona kwamba nilikuwa nimedhulumiwa ila baada ya mwezi mmoja mambo yakaonekana kujipa.
Nilikuwa nimetumiwa barua pepe kutoka nchini Uingereza. Haikuwa kutoka kwa Penn bali ilikuwa imetoka kwa mkurugenzi wa kituo cha habari cha BBC ambaye alinitaka nielekee huko huku kila kitu kikiwa kimeandaliwa. Sijui ni furaha ya aina gani ambayo nilikuwa nayo, sikuamini kama kile kilichokuwa kikiendelea kilikuwa halisi au ndoto.
Nikawaambia wazazi wangu, nikamwambia mpenzi wangu, Myra na Hamza ambaye alinitengenezea kitambulisho cha uandishi wa habari. Kila mmoja akaonekana kuwa na furaha, baada ya wiki mbili nilikuwa ndani ya ndege ya British Airways nikielekea nchini Uingereza. Ile ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuelekea katika bara la Ulaya. Nilipofika huko, Penn pamoja na mwanaume mmoja walikuwa wamekuja kunipokea na hivyo kunipeleka hotelini.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilikaa huko huku usiku nikiwasiliana na wazazi wangu pamoja na Penny. Baridi la nchini Uingereza lilikuwa kali sana ila nikavumilia na hatimae kesho kupelekwa katika jengo la BBC lililokuwa hapo London na kisha kuanza kufanyiwa mahojiano ya siri kidogo. Kila mtu hakuamini kama nilikuwa nimeingia Darfur kama mwandishi wa habari na kutoka salama.
Siku ambayo MAKALA YANGU YA DARFUR ilipoanza kuonyeshwa, watu walikuwa wakilia, mambo ambayo yalikuwa yameonekana katika video ile yalionekana kuwatisha sana. Ndani ya wiki moja niliyokaa nchini Uingereza nikaonekana kuwa maarufu, watu wakaanza kunitafuta kwa ajili ya kufanya mahojiano binafsi pamoja nami.
Mkurugenzi wa BBC, Bwana Patrick Pegg anaona dhahiri kwamba ningeweza kushawishiwa na kwenda kufanya kazi katika mashirika mengine na wakati wao wenyewe walikuwa wakinihitaji, wakanisainisha mkataba wa kufanya kazi hapo huku nikilipwa paundi elfu ishirini kwa wiki ambazo zilikuwa ni zaidi ya shilingi milioni hamsini. Mwaka huo ndio ulikuwa mwaka ambao nilipokea tuzo ya mwandishi bora duniani kutokana na makala ambayo nilikuwa nimeiandaa kitu ambacho kiliifanya nchi yangu ya Tanzania kutangazika sana.
Nililipwa kiasi kikubwa kwa sababu nilikuwa nimeandaliwa kazi nyingi sana za kufanya katika nchi ya Iraq na Iran ambapo kulikuwa na mapigano mengi yaliyokuwa yakiendelea. Sikufa, nilifanya kazi zao zote na katika kipindi chote na mpaka sasa hivi imepita miaka nane na bado naendelea kufanya kazi mahali pale huku mke wangu, Myara akiwa amenizalia watoto watatu, Prince, Furaha na Magreth.
Mpaka nimefikia hatua ya kuandika kitabu hiki kifupi cha MAKALA YANGU YA DARFUR kuna watu wengi sana wamehuzunika na kulia sana, wanajeshi wa waasi wakaonekana kusababisha vidonda vingi mioyoni mwa watu wa Sudan na Afrika kwa ujumla. Kuna wengine ambao walikamatwa na kuhukumiwa katika mahakama ya The Hague nchini Uholanzi lakini kuna wengine bado waliendelea kujificha mpaka leo hii.
Pamoja na yote, sikumsahau rafiki yangu, Majeed. Kwa kumuonyeshea kwamba tulikuwa pamoja, nikawa namlipia ada huku nikimtumia paundi elfu mbili mia tano mpaka pale alipomaliza masomo yake ila msaada wangu wa kifedha haukuisha kwani bila yeye, mabo yangekuwa magumu sana kwangu kukamilisha makala ile.
MWISHO.
Hii ni hadithi ya kutngwa japokuwa yale niliyoyaandika ndio yanayoendelea kutokea huko. Shukrani kwa walionifuatilia toka mwanzo mpaka mwisho.
0 comments:
Post a Comment