IMEANDIKWA NA : RAYMOND MWALONGO
*********************************************************************************
Simulizi : Mimi Kabla Yako
Sehemu Ya Kwanza (1)
Hali ya hewa haikuwa shwari katika jiji la Entebbe nchini Uganda, nyakati hizo za saa saba usiku kulikuwa na mvua kubwa ya mawe iliyonyesha. Karaha hiyo iliongezeka katika mitaa ya matajiri wa jiji hilo kwani katika nyumba moja kulikuwa na moto mkubwa uliokuwa ukiwaka. Kulikuwa na harakati za watu tofauti ambazo hazikuwa na mafanikio dhidi ya moto huo ulioshika nyumba hiyo huku ikiaminika kuwa ulisababishwa na hitilafu ya umeme. Watu waliokuwapo nje ya nyumba hiyo walikuwa wakihofia uhai wao kujitosa katika moto huo kuokoa maisha ya wanafamilia hao waliokuwa wakipiga kelele za kuomba msaada.
Wakati huo moto ulikuwa umeshika kwa kiasi kikubwa eneo la vyumba vya kulala vya nyumba hiyo. Raia waliokuwa eneo hilo la tukio tayari walikuwa wamewasiliana na kikosi cha zima moto cha jiji hilo lakini wahusika wa kikosi hicho walikuwa hawajafika. Kelele za wahanga wa tukio hilo ziliendelea kupungua kadri dakika zilivyozidi kusogea. Ghafla alitokea mtu mmoja eneo hilo huku akipiga kelele za yowe zaidi ya watu waliokuwapo eneo hilo.Mtu huyo alipiga kelele huku akikimbia kuelekea eneo la nyumba hiyo iliyokuwa imeshika moto. Watu kadhaa walijaribu kumkamata lakini walishidwa kutokana na nguvu alizokuwa nazo mtu huyo. Alikuwa akilitaja jina la Johnson aliyekuwa mmiliki wa nyumba hiyo iliyokuwa ikiwaka moto. Alikimbia kwa kasi kabla kwenda kuurukia na kuuvunja mlango wa mbele wa nyumba hiyo ambao ulikuwa umeshika moto tayari. Wakati huo moto ulikuwa ukielekea eneo hilo la sebule alilokuwa ameingia kwa kasi ya ajabu.
Watu waliokuwapo eneo hilo waliongeza vilio wakiamini mtu huyo aliyeingia ambaye alikuwa kijana wa wastani wa miaka ishirini na nane ndiyo ulikuwa mwisho wa maisha yake. Hawakusikia tena kelele za aina yeyote hata za kijana huyo aliyeingia, baada ya dakika kadhaa kikosi cha zima moto kilifika eneo hilo la tukio na kuanza kuzima moto uliokuwa umeshika katika nyumba hiyo. Watu walikuwa wakilalamika huku wakilaumu kuchelewa kwa kikosi hicho kufika eneo hilo la tukio. Hata hivyo hakuna kitu walichokuwa wakiokoa kwani jitihada hizo zilionekana kama zilikuwa za kuzuia moto huo usishike nyumba za karibu na eneo hilo.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya nusu saa moto huo ulikuwa umepungua kwa kiasi kikubwa, wakati kikosi hicho kikiendelea na zoezi lake hilo, watu kadhaa walianza kusogea eneo hilo la nyumba hiyo kwa uangalifu. Walikuwa wakihisi uwezekano wa kuwa hai kwa kijana aliyeingia mara ya mwisho katika nyumba hiyo. Mara baada ya kuingia ndani ya nyumba hiyo walishuhudia vitu vingi vya thamani vilivyokuwa vimeungua huku sehemu kadhaa zikiwa bado zimeshika moto. Walianza kuzunguka sehemu tofauti za eneo hilo lililokuwa la sebule huku wakiamini wangempata kijana aliyeingia katika nyumba hiyo kwa lengo la kuwaokoa wahanga. Baada ya dakika kadhaa wakiwa wanaendelea na zoezi lao kwa kubadilishana kutokana na joto kali lililokuwapo walifanikiwa kumwona kijana huyo.
Alikuwa ameangukiwa na mbao za dali ambazo bado zilikuwa zikiendelea kuwaka huku akiwa hana fahamu, bila kupoteza muda walianza kuzitoa mbao hizo zilizomwangukia. Baada ya zoezi hilo walikata tamaa baada ya kuona eneo la mgongoni la kijana huyo likiwa limeungua kwa kiasi kikubwa huku kukiwa na jeraha kubwa. Alikuwa amedhurika na moto kwa kiasi kikubwa mwilini lakini zaidi mgongoni kwake. Walianza kushauriana huku wengine wakidai mtu huyo alikuwa ameshafariki, mmoja wao alionyesha mwamko wa ghafla akidai huenda mtu huyo alikuwa hai. Bila kupoteza muda alianza kumnyanyua na hatimaye alisaidiwa na wenzake. Mara baada ya kumyanyua kijana huyo walishtushwa na mtoto wa miaka kama kumi aliyekuwa amelaliwa na kijana huyo. Alikuwa kama amemkumbatia katika hali ya kumzuia mtoto huyo na karaha hiyo ya moto katika eneo hilo lilokuwa na mabaki ya vitu tofauti vilivyoungua. Mtoto huyo aliyekuwa na majera kadhaa huku akiwa hana fahamu alibebwa pamoja na kijana huyo na walianza kuondolea eneo hilo walilokuwapo kabla ya kutolewa nje na kufuatiwa na safari ya kuwawahisha hospitali kwa vile walikuwa hai.
Kikosi cha zima moto kiliendelea zoezi lake kikishirikiana na watu waliokuwapo eneo hilo la tukio. Hatimaye zoezi la kuzima moto huo lilipokamilika sawasawa walifanikiwa kuitoa miili ya watu watano waliofariki katika ajali hiyo. Alikuwapo Johnson, mkewe na mwanao mdogo wa kike pamoja na wafanyakazi wawili waliokuwa wakifanya kazi nyumbani kwao hapo. Miili yao ilichukuliwa eneo hilo la ajali na safari ilianza kuelekea katika Mochuari ya hospitali kuu ya jimbo hilo la Entebbe. Vilio vya watu ndivyo vilitawala huku watu wakiwa na hisia tofauti juu ya ajali hiyo.
* * * *
Kijana aliyeokolewa kutoka eneo la ajali ya moto walimgundua kuwa aliitwa James akiwa mdogo wake Johnson, mhanga wa ajali hiyo aliyekuwa ameshafariki. Kijana huyo aliyefanikiwa kumwokoa mtoto mdogo wa kiume alikuwa katika hali mbaya iliyotishia uwezekano wa kupona kwake. Jiji la Entebbe lilikuwa limetawaliwa na kifo cha familia ya bwanaJohnson kilichotokana na ajali hiyo ya moto. Habari za kuaminika zilikuwa zimetolewa, ilielezwa moto huo ulikuwa umesababishwa na hitilafu ya umeme.
Maeneo ya hospitali kuu ya jimbo hilo alikuwapo bwanaAbraham akiwa kaka wa Johnson, alikuwa akisimamia matibabu ya mdogo wake James pamoja na ya mtoto wa Johnson aliyeokolewa ambaye aliyeitwa David.
Tayari taratibu zote za mazishi ya Johnson na familia yake zilikuwa zimeshaandaliwa ili watu hao wazikwe katika jiji hilo. Hatimaye siku husika ya mazishi ilipofika watu hao walizikwa. Ni siku iliyokuwa ya majonzi katika familia hiyo hata ndugu wa karibu kutokana na mchango mkubwa walioupoteza ambao walikuwa wakiupata toka kwa bwana Johnson. Siku hii ilijaa majonzi zaidi kwani James akiwa mdogo wake pekeewa bwana Abraham alibakia, alifariki katika hospitali aliyokuwa akipata matibabu. Hiyo ilifuata baada ya kijana huyo kudhulika sana na majeraha yaliyochimbika ambayo yalisababishwa na ajali hiyo ya moto.
Kijana huyo naye alizikwa katika jimbo hilo siku moja baadaye huku familia hiyo ikionekana kuwa katika majonzi makubwa. Watu ambao walionekana katika majonzi hayo mmoja wao alikuwa bwana Abraham huku muda wote wa mazishi akionekana mnyonge. Bwana Abraham moyoni alikuwa akifurahia kila tukio lilokuwa likiendelea na hakujulikana katika ukweli wake huo kutokana na vile alivyokuwa mnyonge muda wote. Alikuwa amefanikisha tukio kubwa katika ajali hiyo ya moto na hakuna mtu aliyekuwa akijua. Mara baada ya kifo cha mdogo wake Johnson wazo lililomkaa kichwani lilihusiana na kurithi mali hizo za mdogo wake. Wakati huo alifurahi zaidi baada ya mdogo wake wa mwisho James kufariki kutokana na majeraha makubwa yaliyosababishwa na ajali hiyo ya moto. Wakati huo alikuwa akitamani kwa kiasi kikubwa David aliyekuwa mtoto pekee ya Johnson ambaye alikuwa katika hali mbaya afariki pia. Aliamini kama mtoto huyo angefariki ingekuwa rahisi kila kitu cha Johnson kuwa chake.
Siku zote alifika hospitalini kumwangalia mtoto huyo aliyekuwa katika hali mbaya na moyoni alikuwa akiomba mtoto huyo afariki ili yeye aendeleze na utajiri wa mdogo wake. Tayari alishaanza kuingiwa na hisia za kumuua mtoto huyo akiwa hospitali hapo kwa vile aliona mtoto huyo alikuwa akichelewa kufariki. Akionekana ni mtu mcheshi na mwenye huruma, hakuendana na mwonekano wake huo kwani hakuwa na huruma hata kidogo. Jijini Entebbe alifahamika zaidi kwa shughuli yake ya ufundi wa umeme na wakati wote akifanya kazi hiyo alikuwa akiwaza utajiri wa mdogo wake. Mbali na msaada mkubwa alioupata kutoka kwa Johnson akiwa hai ikiwa ni pamoja na kumsaidia kujenga nyumba yake, bwana Abraham hakuridhika. Yeye na mkewe ndio watu pekee waliojua mkasa wa kifo hicho cha Johnson na familia yake kwa vile walihusika, siku ya tukio bwana Abraham alikuwa amemtembelea mdogo wake huyo ikiwa ni kawaida yake.
Siku hiyo alifanikiwa kutega bomu dogo katika chanzo kimoja cha umeme kilichokuwa chooni mwa nyumba hiyo. Alifanikisha zoezi hilo wakati alipoingia katika choo hicho kama vile alienda kukamilisha shida zake. Bomu hilo lilitegwa majira ya saa kumi jioni na alitarajia lingelipuka baada ya saa tisa kama ilivyokuwa imetokea siku ya tukio. Alifurahia ushindi huo na mkewe aliyehusika kwa kiasi kikubwa na zaidi akiwa mwanamke aliyekuwa hana huruma hata kidogo.Tayari ndugu wa familia yake walikuwa wamemkabidhi mamlaka ya kusimamia utajiri wa mdogo wake na wakati huo alianza kuwaza ni jinsi gani angefanikisha zoezi la kumuua David akiwa hospitali baada ya kuona alichelewa kufariki.
Baada ya wiki mbili, tayari David alikuwa amerudiwa na fahamu vizuri na alikuwa akiendelea na matibabu katika hospitali hiyo kuu ya jiji la Entebbe. Muda wote alikuwa akilia hospitalini hapo kutokana na taarifa aliyokuwa ameipata kuwa wazazi wake pamoja na mdogo wake wa kike walikuwa wamefariki. Zaidi uchungu uliongezeka kutokana na maelezo aliyopewa kuwa baba yake mdogo alikufa katika harakati za kumwokoa yeye. Alikuwa akiwaza mambo mengi pasipo kupata majibu katika umri wake huo wa utoto. Alielezwa uchunguzi dhidi ya ajali ya moto iliyoipata familia yao ulikuwa umetoa maelezo kuwa ajali hiyo ilisababishwa na hitilafu ya umeme.Alikuwa akiingiwa na hisia mara kadhaa akiamini huenda ajali hiyo haikusababishwa na hitilafu ya umeme lakini alikuwa akishindwa kuthibitisha hisia zake.
Akiwa hospitali hapo alikuwa na faraja juu ya ujio wa baba yake mkubwa bwana Abraham akiwa na mkewe. Furaha hiyo iliongezeka zaidi kutokana na uwepo wa Sabinus, mtoto wa baba yake mkubwa huyo aliyekuwa na umri wa miaka kumi kama yeye. Hiyo yote ilitokana na kukua kwao pamoja tangu wakiwa wadogo kabisa.Hata wakati huo walikuwa wakisoma shule moja ya ghali iliyoitwa Entebbe International Schools, shule iliyokuwa inachukua wanafunzi wengi wa rika tofauti. Gharama zote zilizotolewa katika shule hiyo zilikuwa zikitolewa na baba yake marehemu Johnson. Upendo uliokuwa umejengeka baina yao ndio uliomfanya Sabinus mara nyingine aamue kulala hospitalini hapo na David ingawaje haikuhurusiwa.
Mbali na uchungu aliokuwa nao juu kifo cha wazazi wake alikuwa akiamini angetimiziwa mahitaji yake na bwana Abraham kupitia utajiri uliokuwa umeachwa na baba yake. Hakuwa na hofu juu ya hilo hasa kutokana na hali ya wazi aliyoamini ilikuwa ya upendo kutoka kwa baba yake huyo mkubwa. Siku moja wakati akiwa anaendelea na matibabu katika hospitali hiyo huku hali yake ikiwa inaendelea vizuri alishtushwa na ujio wa baba yake mkubwa nyakati za saa saba usiku. Jambo hilo ambalo halikuwa kawaida lilimfanya amuulize sababu iliyomfanya afike wakati huo,alimjibu alifika hospitali hapo kwa vile alimjali. David hakuwa na shaka alibakia akiwa kajilaza katika kitanda chake husika akimsubiri baba yake mkubwa arudi tena baada ya kuondoka. Aliingiwa na furaha akihisi kuwa huenda usiku huo angeondoka na baba yake huyo mkubwa, hiyo ilitokana na vile alivyokuwa akiendelea vizuri kiafya.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya dakika kadhaa alishtushwa na tukio la kukatika kwa umeme ghafla katika maeneo yaliyokuwapo mawodi ya wagonjwa. Alishangazwa na jambo hilo kwa vile alikuwapo katika hospitali hiyo kwa muda mrefu pasipo kutokea kwa tatizo hilo. Alitulia akihisi eneo hilo lilikuwa na matatizo. Alibaki kimya katika wodi alilolazwa huku wagonjwa wengi wakiwa wamelala toka mwanzo na hawakuelewa kama umeme ulikuwa umekatika. Baada ya sekunde kadhaa aliwashuhudia madaktari wanne wakiingia katika chumba hicho. Aligundua kuwa walikuwa madaktari kutokana na makoti yao meupe waliyovaa ingawaje hakuweza kuwaona vizuri sura zao. Watu hao waliongoza mpaka eneo alilokuwa amelala na walimzunguka huku wakiwa kimya kwa muda mfupi na David alianza kuingiwa na hofu juu yao.
“This child is the one I was talking about…”(“mtoto huyu ndiyo yule niliyekuwa namwongelea”) Alisikika mmoja wao baada ya ukimya wa sekunde kadhaa huku akionekana kama alikuwa akimwambia mkubwa wao. “Ooh! Ok…mmh let’s do our work then because he has a lot of problems.” (“sawa..tufanye kazi yetu kwa sababu ana matatizo mengi”). David alishtushwa na maongezi ya madaktari hao na hakuelewa matatizo waliyoyaongelea kwa vile alikuwa amepona kwa kiasi kikubwa. Watu hao walimkamata wakati akijaribu kuongea jambo, mmoja wao alimkaba shingoni jambo lililomfanya ashindwe hata kupiga kelele.
Kwa jinsi alivyokuwa amekamatwa sawasawa aliamini kuwa watu hao walikuwa wauaji na siyo madaktari. Wakati akiwa bado amekamatwa alihisi bomba la sindano likipenya maeneo ya begani kwake kabla ya dawa yake kusukumwa kisha bomba hilo lilitolewa. Watu hao waliendelea kumshika kwa nguvu pasipo kumwachia, baada ya sekunde kadhaa alianza kuhisi macho yake yalikuwa mazito na alipojaribu kujitahidi asiingie usingizini alishindwa, mwishoe alilala. Mara baada ya David kulala mmoja wao alitoa gunia katika moja ya begi walilokuwa wamefika nalo na kisha walimweka mtoto huyo ndani. Walisaidiana kumbeba na kuongoza mpaka eneo la nje ambako alikuwapo bwana Abraham, walilitupa gunia hilo kando ya eneo alilokuwa amesimama.
“ Well done!…We are going to kill this child withiin three hours, we have to get away” (“vizuri…. Tutamuua mtoto huyu ndani ya masaa matatu, inadidi tuondoke”) Alisikika bwanaAbraham aliyekuwa anavuta sigara. Bila kupoteza muda watu hao wakishirikiana na wengine waliokuwapo eneo hilo lililokuwa na giza walimpakia David katika gari moja kati ya mawiliyaliyokuwapo eneo hilo na safari ilianza, waliyaondoa magari hayo kwa kasi eneo hilo.
Bwana Abaraham alikuwa na furaha huku akiamini alikaribiakutimiza lengo lake la muda mrefu. Alikuwa amefanikisha kutekwa kwa David katika hospitali kuu ya jiji la Entebbe iliyokuwapo karibu na sehemu iliyojulikana kama Mpingi. Lengo lake lilikuwa ni kwenda kumuua David katika ufukwe wa ziwa Victoria na alipanga kumtupa mtoto huyo ziwani ili usipatikane ushahidi wowote wa kifo chake. Aliamini jambo hilo lingekamilisha furaha ya maisha yake kwani hakuna mtu ambaye angedhaniwa au kuwa na uwezo wa kurithi utajiri wa marehemu Johnson aliyekuwa mdogo wake. Hakuwa tayari kutimiza jukumu la kusimamia mali hizo na mwishoe kuzikabidhi kwa David aliyekuwa mrithi halali. Wakati huo wa saa nane kasoro usiku magari yao yaliendeshwa kwa kasi barabarani wakiwa wanaelekea eneo la Kalangala kulikokuwa na ufukwe wa ziwa Victoria kwa upande wa Uganda na huko aliamini lengo lake lingeenda kutimia.
Baada ya saa tatu walikuwa kando ya ziwa Victoria lililokuwa na utulivu mkubwa huku kukiwa na mitumbwi kadhaa iliyokuwa imeegeshwa. Walikuwa wameegesha pia magari yao kando ya ziwa hilo katika maeneo yaliyotumiwa zaidi na wavuvi. Nyakati hizo za saa kumi usiku eneo hilo lilikuwa tulivu na hapakuwa na mtu yeyote, kulikuwa na mtumbwi mdogo pia ambao uliandaliwa na vijana hao wa bwana Abraham. Mara baada ya kushuka kwao, David naye alishushwa huku akiwa bado hana fahamu alitolewa katika gunia alilokuwapo na kulazwa katika mchanga uliokuwapo ufukweni hapo. Bwana Abraham alimsogelea kwa karibu David na kumwangalia akiwa amechuchumaa wakati huo tayari alikuwa ameshika bastola mkononi aliyokuwa tayari kaikoki kwa kuua.
Baada ya sekunde kadhaa alisimama na kuonesha ishara fulani kwa vijana wake ambao alimpelekea pakiti moja iliyoonekana ilikuwa na kitu kama unga. Bila kupoteza muda alianza kutoa unga wa pakiti hiyo iliyokuwa ya dawa za kulevya, aliitumia pakiti hiyo akivuta unga huo kwa pua yakei. Baada ya zoezi hilo la dakika mbili, alitulia kidogo kisha aligeuza sura yake kwa David huku ikiwa yenye hasira kupindukia. Akiwa bado kasimama alimumiminia risasi mbili mtoto huyo maeneo ya kifuani zilizomfanya ahangaike akijizungusha eneo hilo kwa sekunde kadhaa kabla ya kutulia kwake. BwanaAbraham aliwaonyeshea vijana wake ishara waliyoielewa kabla ya kumchukua David ambaye damu nyingi ilikuwa ikimtoka na walimpakia kwenye mtumbwi uliokuwapo eneo hilo.
Bwana Abraham akiwa na vijana wake wanne walipanda katika mtumbi huo kabla ya kusukumwa na vijana wake waliobakia eneo hilo lililoegeshwa magari. Walisukumwa mpaka walipoyafikia maji sawasawa. Vijana wake aliokuwa nao kwenye mtumbi walianza kupiga makasia wakielekea eneo la mbele zaidi la ziwa hilo walikopanga kwenda kuutupa mwili wa David waliyeamini tayari alikuwa amefariki. Bwana Abraham kifua chake kilikuwa kimembana kwa furaha aliyokuwa nayo kupindukia huku akiamini tayari alikuwa mmiliki halali wa kila kitu kilichoachwa na mdogo wake marehemu Johnson. Waliuongoza mtumbwi wao kwa umbali wa kilometa moja toka ufukweni ambako walikuwa wameyaacha magari yao. Katika mtumbi waliopanda walikuwa wamebeba tochi kadhaa zilizowafanya waonekane vizuri kila sehemu walioyoenda. Eneo hilo la ziwa lilikuwa tulivu na hawakuona dalili yeyote ya kuwapo kwa wavuvi wakati huo.
Baada ya kuridhika na umbali huo toka eneo la ufukweni mwa ziwa hilo waliamua kumtumpa David majini huku damu ikiwa inaendelea kumtoka kwa kiasi kidogo. Waliondoka eneo hilo walilomtupa kwa kupiga makasia wakirudi kwa kasi eneo la ufukweni walilokuwa wameacha magari yao. Kulikuwa na mingurumo ya radi iliyoashiria mvua ingeanza kunyesha muda wowote toka wakati huo.Baada ya dakika kadhaa walilifikia eneo hilo la ufukweni kabla ya kuuvuta mtubwi huo kando kidogo na mwishoe waliingia kwenye magari yao kabla ya magari hayo kuondolewa kwa kasi eneo hilo ambalo mvua ilikuwa imeanza kunyesha. Bwana Abraham alifurahishwa na zoezi hilo lililokuwa limetokea kwa kiasi kikubwa, ni wakati ambao aliamini kila kitu kilikuwa chake. Ilikuwa yapata saa kumi na moja kasoro robo asubuhi, alikuwa akiongozwa na magari yake hayo kwenda nyumbani kwake, alipanga kupumzika kabla ya sherehe ya kufurahia ushindi huo aliyotarajia kuifanya na mkewe.
Majira ya saa moja asubuhi magari waliyokuwa nayo yalikuwa yakiegeshwa katika nyumba moja ya kifahari ambayo bwanaAbaraham alikuwa akiishi wakati huo. Nyumba hiyo ilikuwa ya marahemu Johnson mabayo aliijenga kabla ya kufarikia kwake. Alishuka katika gari moja kati ya mawili waliyokuwa nayo na kuwahurusu vijana wake waondoke baada ya kupeana ahadi ya kukamilisha malipo ya kazi waliyokuwa wameiifanya. Alianza kutembea akielekea ndani ya nyumba hiyo kabla ya kulakiwa na mkewe ambaye kwa sauti ya chini alimuuliza kama alikuwa amefanikiwa kumuua David.
Alimjibu kwa kutikisa kichwa akiashiria zoezi hilo lilikuwa limekamilika, mkewe akiwa na furaha alimkumbatia na wote walianza kutembea wakielekea ndani ya nyumba hiyo kabla ya kuongoza chumbani kwao. Ni wakati ambao bwanaAbraham aliwasha simu yake aliyokuwa ameizima kwa muda mrefu huku akiamini muda wowote angepigiwa simu na madaktari wakielezwa kwamba David alikuwa ametekwa hospitali. Alikuwa kitandani na mkewe wakiongea kwa sauti ya chini wakifurahia ushindi waliokuwa wameupata kwani waliamini wakati huo walikuwa wamiliki wa utajiri tofauti wa marehemu Johnson. Kulikuwa na viwanda vitatu tofauti pamoja na maduka ya biashara yaliyokuwa sehemu tofauti nchini humo Uganda. Utajiri walioamini ungekuwa wa mafanikio katika maisha yao.
Majira ya saa mbili asubuhi simu yake bwanaAbraham iliita alipoiangalia aligundua ilikuwa imepigwa na mmoja wa madaktari wa hospitali kuu ya Entebbe. Bila kupoteza muda aliipokea kabla ya kupewa taarifa aliyoitarajia kuwa David alikuwa ametekwa usiku wa kuamkia siku hiyo. Alielezwa kuwa mtoto huyo alitekwa wakati umeme wa hospitali hiyo ulipopata hitilafu ya ghafla. BwanaAbraham akiipokea taarifa hiyo alionesha jazba kupindukia na aliahidi kufika hospitali kupata maelezo zaidi. Aliondoka nyumbani kwake na mkewe wakiwa na lengo la kwenda kujifanya wakitoa ushirikiano katika jambo hilo. Baada ya nusu saa walikuwa katika hospitali hiyo huku bwanaAbraham akionekana kama mtu aliyechanganyikiwa juu ya taarifa alizopewa za kutekwa kwa David.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Taarifa hizo zilipelekwa kituo cha polisi na bwanaAbraham alionyesha ushirikiano kwa kila jambo lililoendelea. Alionekana alihitaji uchunguzi zaidi juu ya tukio hilo, askari walimweleza kuwa jibu lingepatikana baada ya siku kadhaa. Sabinus akiwa mtoto pekee wa bwanaAbraham ndiye aliyechanganyikiwa kwa kiasi kikubwa juu ya kutekwa kwa David na alionekana kuhofia uhai wa binamu yake huyo. Muda wote alikuwa akilia huku akiwa na maswali kadhaa kwa baba yake juu ya taarifa zozote ambazo zilitolewa na jeshi la polisi. Wiki mbili ziliisha pasipo taarifa zozote juu ya mafanikio ya upelelezi wa kupotea kwa David, hatimaye hata askari walianza kuliweka kando suala hilo. BwanaAbraham aliona wakati huo ndiyo ulikuwa pekee kwa yeye kusherekea na mkewe juu ya ushindi waliokuwa wameupata.
Waliandaa safari yao ya ghafla ambayo hawakumshirikisha hata mwanao Sabinus ambaye bado siku zote alikuwa akimlilia David. Walielekea nchini Kenya katika jiji la Mombasa ambako walifikia katika hoteli ya kifahari ya Baobab Holiday Resort iliyokuwapo pembezoni mwa bahari ya Hindi. Walifurahia ushindi wa kila jambo walilokuwa wamefanikiwa na waliona huo ulikuwa mwanzo mpya wa maisha yao mazuri. Baada ya siku tatu walirudi tena nchini Uganda kuendelea na shughuli zao za kibiashara.
* * * *
Otieno Ndakufurila alikuwa mvuvi maarufu katika eneo la Kalangala lililokuwapo kando ya ziwa Victoria nchini Uganda. Alikuwa mvuvi aliyeishi katika daraja la hali ya chini kimaisha kwani kazi hiyo haikuweza kumsaidia lolote mbali na jambo hilo mwili wake ulikuwa umehalibika kwa kiwango kikubwa. Mtu ambaye angemwona angeweza kudhania aliwahi kuungua na moto siku za nyuma lakini alikuwa na historia ndefu iliyomfanya awe hivyo. Akiwa na umri wa miaka arobaini hakuwa na mke wala watoto na alikuwa akiangalia maisha yake zaidi. Kikubwa alichokijali kilikuwa chakula kwa vile aliamini akikipata hakuna jambo ambalo lingekuwa gumu kwake.
Siku moja majira ya jioni alikuwa katika nyumba yake ndogo iliyojengwa kwa udongo katika eneo lililokaliwa na wavuvi walioishi maisha ya daraja la chini katika eneo hilo la Kalangala. Siku hiyo alikuwa akiwaza aende kufanya shughuli zake za uvuvi au asiende, hiyo yote ilitokana na karaha ya mvua kubwa iliyokuwa ikiendelea kunyesha. Ilikuwa vigumu sana kuendesha shughuli hiyo ya uvuvi katika ziwa Victoria kutokana na mvua hiyo iliyonyesha kila siku. Tatizo lililompata katika maamuzi yake hayo lilihusiana na ugumu wa maisha aliokuwa nao, hakuwa na fedha hata kidogo kwa ajili ya siku iliyofuata ili kujikimu kwa chakula. Jambo hilo ndilo lilimfanya apuuze karaha za mvua na kuona alihitajika kwenda kuendeleza shughuli yake hiyo ya uvuvi ili kuifanya siku iliyofuata isonge mbele.
Alikuwa na mazoea ya kufanya shughuli hiyo ya uvuvi nyakati za usiku, wakati wa mchana aliutumia kwa kiasi kikubwa kwa kulala na kupumzika. Majira ya saa sita usiku aliondoka na taa yake ya mafuta aliyokuwa akiitumia katika shughuli hiyo ya uvuvi lakini pia alikuwa na nyavu ambazo pia alizitumia. Alikuwa amebeba vifaa tofauti vilivyokuwa vikikamilisha shughuli yake hiyo ya uvuvi. Katika maisha yake hakupenda kuwa karibu na mtu na hiyo yote ilitokana na kisa kilichowahi kumpata na kumfanya awe kama mtu aliyeungua kwa moto. Alikuwa hamuamini mtu baada ya kisa hicho jambo lililomfanya aishi peke yake na kujitegemea mwenyewe kwa kila jambo alilokuwa akilifanya.
Hatimaye alifika katika eneo husika alilokuwa ameegesha mtumbwi wake mdogo kabla ya kuweka vitu hivyo husika na kuanza kupiga makasia kuelekea maeneo ya ndani ya ziwa hilo. Halikuwa jambo gumu sana kwa vile mtubwi wake huo pia ulikuwa ukisaidiwa kwa kiasi kikubwa na na upepo kwani ulitengenezwa kama Mashua. Alisogea kwenda mbele sana na eneo hilo la ziwa na huko aliendelea na shughuli yake hiyo ya uvuvi. Alikaa sana katika eneo hilo alilokuwa akifanya uvuvi kwa vile pia msimu huo haukuwa wa samaki kwa kiasi kikubwa. Majira ya saa kumi alikuwa ameridhishwa na kiasi cha samaki aliokuwa amewapata, alianza kuongoza mtumbwi wake kurudi eneo la fukwe la ziwa hilo.
Alifanya hivyo kwani aliona dalili za mvua kunyesha zaidi taa yake ya mafuta aliyokuwa akiitumia ilikuwa ikipungua mwanga kadri dakika zilivyozidi kwenda jambo lililomfanya ahisi mafuta yalikuwa yameisha. Aliongoza mtubwi wake mpaka kando ya ziwa hilo wakati ambao hata taa yake ilikuwa imezima. Alianza kushusha samaki wake katika vikapu vitatu alivyokuwa amebebea, akiwa katika eneo hilo la giza hakuhofia jambo lolote kwani aliamini haikuwa tabu kufika nyumbani kwake. Wakati akiendelea na zoezi lake hilo alishtushwa na mwanga wa magari yaliyokuwa yakiendeshwa kwa kasi kuelekea eneo alilokuwapo. Aliamua kulala pembeni ya mtumbwi wake huku akiwa na hofu tele kwani jambo hilo hakuwahi kukutana nalo eneo hilo katika maisha yake yote ya uvuvi. Magari hayo yaliegeshwa umbali wa mita kama kumi toka eneo alilokuwa amelala huku kukiwa na mitumbwi kadhaa iliyoegeshwa.
Alibaki kimya akiwa na hofu lakini ghafla alipata ujasiri na kuamua kujivuta kidogo kabla ya kuanza kushuhudia jambo lililotaka kutokea eneo hilo. Alimwona mtoto akitolewa kutoka kwenye gunia na watu ambao hakuwafahamu. Eneo hilo lilikuwa na mwanga kupindukia kutokana na taa za magari yao. Alitulia kidogo kabla ya kushtushwa na mtu aliyemfahamu na kumchukia katika maisha yake. Alikuwa bwanaAbraham ambaye aliharibu ndoto za maisha yake kwa kiasi kikubwa, lakini pia ndiye aliyesababisha aonekane kama mtu aliyekuwa ameungua na moto. Hakupiga kelele zozote kutokana na mshtuko huo alibaki mtulivu huku akiwa na hamu ya kutaka kujua jambo ambalo lingetokea. Alimwona bwanaAbraham akitumia pakiti moja ambayo aliamini ilikuwa na dawa za kulevya, baada ya zoezi hilo alitulia kidogo kabla ya kumpiga na risasi mbili mtoto aliyetolewa kwenye gunia.
Alijikaza pia pasipo kutoa kelele zozote juu ya kitendo hicho cha kinyama baada ya sekunde kadhaa aliwashuhudia watu hao wakiongozwa na bwanaAbraham walimpakia yule mtoto kwenye mtubwi. Kwa uangalifu wa hali ya juu aligeuka katika eneo alilokuwa amelala na kuelekeza kichwa chake upande wa ziwa hilo. Lengo lake lilikuwa kuangalia eneo ambalo wangempeleka mtoto huo. Alikuwa akitetemeka kupindukia kwani kulikuwa na watu kadhaa waliobaki na magari hayo ambao walikuwa wakiongea eneo hilo waliloachwa. Alikuwa akihofia kuuawa kama watu hao wangegundua alikuwapo eneo hilo. Alishuhudia bwanaAbraham akiwa na vijana wake wakiongoza mtumbwi kwa umbali wa mita kama mia tisa au kilometa moja kabla ya kuwaona wakirudi eneo hilo. Akili yake ilimtuma na kuamini watu hao walikuwa wamemtupa mtoto huyo katika maji ya ziwa hilo.
Mara baada ya kurudi waliingia kwenye magari yao yaliyowashwa kabla ya kuondolewa kwa kasi eneo hilo, yeye pia hakupoteza muda kwani alihisi mtoto huyo huenda alikuwa hai. Aliusukuma kwa haraka mtumbwi wake na kuanza kupiga makasia kwa kasi ya ajabu akiamini angeweza kujaribu kuokoa maisha ya mtoto huyo aliyekuwa ametupwa majini.Baada ya dakika kadhaa alikuwa eneo lenye giza ambalo kwa mbali alimwona bwana Abraham na watu wake wakimtupa mtoto huyo. Tayari mvua ilikuwa imeanza kunyesha jambo lililoanza kumpa hofu Otieno juu ya kila dakika iliyoendelea. Alikuwa akizunguka eneo hilo na mtumbwi wake akiamini angeweza kubahatika kumwona mtoto huyo. Mwanga ambao ulimsaidia kwa kiasi kidogo ulitoka kwenye usawa wa juu wa maji ya ziwa hilo. Alizunguka kila upande wa eneo hilo na mtumbwi huku akijitahidi kuangalia kwenye maji hayo kama angeweza kumwona mtoto aliyetupwa lakini haikuwa hivyo.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Jambo hilo ndilo lilianza kumpa hofu kwani mvua iliyonyesha pia ilikuwa ikihatarisha uhai wake kwa vile maji yalikuwa yakiingia katika mtumbwi huo na mwishoe aliamini angeishia kuzama nao. Alikuwa tayari amenyeshewa na mvua hiyo ambayo pia kulikuwa na maji yake yaliyozidi kuongezeka katika mtumbwi aliokuwapo. Mwishoe aliamua kuondoka eneo hilo baada ya kuhofia uhai wake kutokana na mvua iliyokuwa ikiendelea kunyesha. Aliugeza mtumbwi wake na kuuelekeza eneo la ufukwe wa ziwa hilo ambalo alikuwa ametokea awali. Wakati mvua hiyo ikiendelea kunyeyesha huku akipiga makasia kuondoka eneo hilo, hasira zilimpanda na kumfanya aanze kutokwa na machozi pasipo kujitambua. Alikuwa akikumbuka juu ya unyama aliowahi kufanyiwa na bwanaAbraham na zaidi mwendelezo wa tabia ya mtu huyo kwani alikuwa amemshuhudia akimuua mtoto huyo aliyehitaji kumwona.
Akili yake ya kufanya malipizi juu ya unyama wa bwanaAbraham ilianza kumrudia baada ya kuwa kimya kwa muda mrefu. Aliwaza kumuua mtu huyo aliyehalibu ndoto za maisha yake miaka kadhaa iliyokuwa imepita. Wakati huo akiwa mita kadhaa toka eneo alilokuwa akimtafuta mtoto huyo aliyetupwa majini, alishtushwa na sauti ya kitu kilichogonga kwa nguvu mtumbwi wake. Jambo hilo lilimfanya aache kupiga makasia na kusogea eneo alilosikika sauti ya kitu hicho ambacho hakukitambua. Aliposogelea eneo hilo aliushuhudia mkono wa binadamu ukizamia katika maji, Otieno alishtuka akiwa haamini alichokiona. Hatimaye mkono huo ulizamia katika maji hayo, alipatwa na akili ya haraka na kuamua kujitosa katika maji wakati mvua hiyo kubwa ikiendelea kunyesha. Aliogelea akishuka eneo la chini la sehemu hiyo aliyokuwapo akimfuata mtu huyo aliyeamini alikuwa mtoto ambaye alitupwa na bwanaAbraham na vijana wake.
Wakati akiendelea kuogelea alimshuhudia kwa mbali mtu huyo akienda kugota eneo la chini kabisa la ziwa hilo. Aliendelea kuogelea akitumia uzoefu wake wa miaka mingi huku akiwa na imani kuwa huenda mtu huyo alikuwa hai. Aliogeelea mpaka alipofika eneo alilokuwapo mtu huyo ambaye alibaini kuwa ni mtoto ambaye awali alimshuhudia akipigwa risasi na bwanaAbraham. Kulikuwa na damu ambayo bado ilikuwa ikiendelea kumtoka maeneo ya kifuani. Bila kupoteza muda Otieno alianza kumvuta lakini alikuwa hatoki eneo hilo alilokuwapo. Alifanya jambo hilo kwa kasi ya ajabu na mwishoe baada ya kuona mtoto huyo hatoki eneo hilo alilokuwa amenasa aliamua kurudi tena juu ili kupata pumzi mpya. Alikuwa ametumia dakika moja akiwa ndani ya maji hayo, baada ya sekunde kadhaa alikuwa eneo la juu ya ziwa hilo ambapo alivuta pumzi kwa mara ya pili kabla ya kuzama tena majini. Alishuka kwa kasi eneo alilokuwapo mtoto huyo kabla ya kumfikia na kuanza kumvuta, alifanya zoezi hilo kwa sekunde kadhaa pasipo mafanikio, mwishoe alikata tamaa na kuanza kuogelea akitoka eneo hilo.
Kabla hajafika juu kabisa alikokuwa ameacha mtumbwi wake kuna jambo lilimsukuma moyoni na kumpa imani kuwa iliwezekana kumwokoa mtoto huyo, aliamua kurudi kwa kasi tena eneo alilokuwapo mtoto huyo. Mara baada ya kumfikia na kumvuta mtoto huyo alitoka eneo alilonasa, hakupoteza muda kwani alianza kuogelea naye akitoka nje. Mtoto huyo alikuwa na tumbo kubwa kupindukia na yeye alitambua jambo hilo kuwa lilitokana na kunywa kwa maji mengi. Akiwa amembeba kwa mkono wake wa kushoto huku wa kulia akiutumia kwa kuogelea sambamba na miguu aligundua kitu kwa mtoto huyo. Alihisi mapigo yake ya moyo yalikuwa yakifanya kazi kwa taabu sana. Jambo hilo ndilo lililomfanya aongeze bidii ya kuogelea akielekea nje akiamini angeweza kumwokoa mtoto huyo. Mara baada ya kufika eneo la nje aliloacha mtumbwi, Otieno alihisi kuchanganyikiwa kwani mtumbwi huo haukuwepo eneo hilo.
Alikuwa amechoka kwa kiasi kikubwa huku akiwa amembeba mtoto huyo aliyemwokoa.Aliangalia huku na huko pasipo kuuona mtumbwi huo jambo lililomfanya aone njia pekee ya kupona ilikuwa ni kuogolea kuelekea eneo la ufukweni mwa ziwa hilo. Alianza kuogelea huku mvua kubwa ambayo wakati huo ilikuwa ya mawe ikiendelea kunyesha. Akilini aliwaza mambo mengi ambayo hakupata majibu yake, alikuwa akihisi kushindwa kupona katika hatari hiyo kutokana na umbali uliokuwapo. Aliendelea kuogelea huku akipiga kelele za kuomba msaada eneo hilo ambalo hakuna hata mvuvi mmoja aliyekuwepo. Jambo hilo ndilo lililomfanya azidi kuchanganyikiwa zaidi kwa vile alikuwa amechoka kwa kiasi kikubwa. Aliogelea kwa umbali wa mita kadhaa kabla ya kutulia na kuamini huo ulikuwa mwisho wa maisha yake na mtoto huyo aliyemwokoa.
Akiwa ametulia alianza kuzama taratibu akiwa amemshikilia mtoto huyo aliyemwokoa, akiwa amezama na kuanza kushuka chini majini huku akiamini mwisho wake ulifika. Alishuka chini kwa mita kadhaa akiwa amemshika mtoto huyo kabla ya kujihisi kuwa alikuwa na uwezo wa kupona katika janga hilo. Alijitahidi kujituma akiamini alikuwa mwanaume na alihitaji kuokoa maisha yake na ya mtoto huyo aliyeamini hakuwa na hatia. Alianza kuogelea tena huku akijitahidi kadri awezavyo ili kuendeleza zoezi hilo la kujiokoa na mtoto huyo. Wakati akikaribia kurudi tena eneo la juu la ziwa hilo alishtushwa na kitu kilichomgonga kichwani, alipoangalia vizuri aligundua ulikuwa mtumbwi. Hapo ndipo alipopata nguvu za ghafla na kuona iliwezekana kupona na mtoto huyo, alijitahidi kuogelea na mwishoe alitoka juu na kuushuhudia mtumbwi wake aliouacha awali wakati akijaribu kwenda kumwokoa mtoto huyo. Ulikuwa ukielea majini jambo lililopelekea uwe unazunguka eneo hilo. Bila kupoteza muda alimpakia mtoto huyo kwenye mtumbwi ambao ulikuwa na maji ndani yake. Alitulia kidogo akiwa ameshika kingo za pembeni za mtumbwi huo ilhali akiwa anapumzika baada ya zoezi hilo.
Baada ya sekunde kadhaa alihisi alikuwa sawa na aliamua kupanda katika mtumbwi huo ambao ulikuwa na maji ambayo uzito wake na ule wao bado haukuweza kuzamisha mtumbwi huo. Alianza kupiga makasia akielekea eneo la ufukweni la ziwa hilo ambalo halikuwa mbali na eneo hilo. Hatimaye alifika eneo hilo na bila kupoteza muda alimshusha mtoto huyo kutoka kwenye mtumbwi huo kabla kumweka kando yake na kuanza kumkanda tumbo lake. Alifanya zoezi hilo lililomfanya mtoto huyo aanze kutapika maji aliyokuwa amekunywa, alikuwa akitumia pia mchanga kumpiga eneo hilo la tumboni lengo haswa likiwa kumweka sawa.
Mwishoe alifanikiwa zoezi lake baada ya kuona mtoto huyo akikohoa huku tumbo lake likiwa limepungua tofauti na lilivyokuwa awali. Aliichukua taa ya mafuta aliyoiacha awali eneo hilo na kuiwasha ingawaje ilikuwa ikiwaka kwa mwanga hafifu kutokana na kuisha mafuta. Baada ya zoezi hilo aliamua kumalizia kulichana shati la mtoto huyo alilokuwa amelivaa ambalo lilikuwa limechanika chanika lengo haswa likiwa kuona eneo alilokuwa amepigwa risasi. Alishtushwa na hisia alizokuwa nazo awali kuwa mtoto huyo alipigwa risasi kifuani,alikuwa amepigwa risasi moja katika bega lake la kushoto wakati nyingine ilionekana ikiwa imekaruza kwa kiasi kikubwa mkono huo huo wa kushoto lakini haikumpata kabisa.
Hapo ndipo alipopata imani kubwa ya kuweza kufanikisha kumwokoa mtoto huyo, alimchukua na kuelekea nyumbani kwake akikimbia kwa kasi. Alikuwa na imani ya kuweza kuokoa maisha ya mtoto huyo, baada ya dakika kadhaa alikuwa katika eneo la jikoni la nyumba yake iliyokuwa ya udogo ambayo pia ilikuwa na jiko hilo na chumba cha kulala. Aliwasha moto katika chanzo chake na kuanza jitihada za kujaribu kuitoa risasi iliyokuwa imepenya katika mkono wa mtoto huyo aliyoamini angeweza kuitoa. Wakati zoezi hilo likiendelea mtoto huyo alikuwa amepoteza fahamu muda mfupi toka awasili naye nyumbani kwake hapo.
Otieno alijitahidi kwa muda mrefu na hatimaye alifanikiwa kuitoa risasi hiyo kabla ya kuufunga mkono wa mtoto huyo. Alikuwa ametumia majani ya porini kumtibu huku akiamini majani hayo yalikuwa na uwezo wa kumsaidia mtoto huyo. Alimlaza katika kitanda chake cha kamba alichokitumia nyumbani kwake hapo wakati akiendelea kufikiria mambo mengine. Alikuwa akimuwazia sana bwanaAbraham na hakujua jambo lililotokea mpaka mtoto huyo akapewa adhabu hyo kali na mtu huyo. Wazo lililokuwa kichwani lilikuwa ni kumsubiri mtoto huyo azinduke ili aujue ukweli wote wa kila kitu kilichokuwa kimemtokea. Akiwa na hasira juu ya bwanaAbraham alikuwa tayari kumsaidia mtoto huyo kadri ya uwezo wake na aliwaza kuhama eneo hilo la Kalangala kwani alihisi kuna mtu alikuwa na mawasiliano ya karibu na bwanaAbraham.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Siku iliyofuata mtoto huyo alizinduka kabla ya kushtuka baada ya kumwona Otieno katika mwonekano wa kutisha kama vile aliungua na moto. Alimtuliza na kumwondoa shaka kabla ya kumpa pole na kuhitaji kujua juu ya kila jambo lililokuwa limetokea. Mtoto huyo aliyejitambulisha kwa jina la David alianza kumsimulia kila jambo lililokuwa limejiri toka mwanzo wa kifo cha familia yake mpaka wakati huo. David alimaliza kwa kushukuru kwa msaada aliokuwa ameupata wa kumwokoa kutoka kwenye kifo. Otieno Ndakufurila alipiga kelele kwa hasira akimtaja bwanaAbraham kuwa ndiye aliyehusika katika kila jambo lililokuwa limemtokea kwa mtoto huyo. Alimpa ushauri David asirudi tena kwa baba yake mkubwa huyo kwa vile alimtaja kama muuaji. Jambo hilo lilimwingia David na alikubali kuishi na Otieno, alikuwa ameingiwa na hisia juu ya ukatili ambao alikuwa ameelezwa na hakutaka kurudi tena katika familia hiyo. Hisia zake juu ya fitina katika kifo cha wazazi wake ziliongezeka kwa kiasi kikubwa baada ya kuutambua unyama wa bwana Abraham.
David alianza kuishi na Otieno aliyemweleza kuwa ipo siku angemwambia kuhusu unyama aliofanyiwa na bwanaAbraham uliomfanya aonekane hivyo kama ameungua na moto na zaidi kuhalibu ndoto za maisha yake. Maisha aliyoishi na Otieno yalikuwa magumu ambayo hakuwahi kuishi kabla, walikuwa wakiilala katika kitanda cha kamba lakini pia mashuka na mablanketi waliyotumia yalijaa chawa. Maisha hayo yalikuwa magumu kwake na hakuwahi kuyafikiria hata kidogo. Otieno alimweleza kuwa alikuwa akifanya utaratibu ili waondoke eneo hilo na kwenda sehemu nyingine. Jambo lililompa taabu lilihusiana na kushinda ndani kwao muda wote kama Otieno alivyomweleza akihofia usalama wake. Alitii maagizo hayo katika wakati huo mgumu ambao chakula alichotumia kilikuwa samaki pekee.
Hakuna mtu aliyekuwa akifika nyumbani hapo kutokana na jinsi Otieno alivyoishi kipweke katika kijiji hicho. Hatimaye baada ya wiki mbili Otieno alikuwa amepata fedha za kutosha na alihitaji waondoke eneo hilo aliloamini lilikuwa na mfuasi wa bwanaAbraham. Alihitaji waelekee eneo la Bushenyi lililokuwa magharibi mwa eneo hilo la Kalangala walilokuwapo. Huko aliamini angeweza kuendeleza shughuli zake za uvuvi katika ziwa Edward linalotenganisha nchi hiyo ya Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Nyakati za saa tano usiku wa siku hiyo alimtoa David katika nyumba hiyo na kumpeleka katika kichaka kidogo kilichokuwa kando na eneo hilo. Lengo haswa lilikuwa ni kuuza nyumba aliyokuwa akiishi, aliongea na mwanakijiji mmoja ambaye alikubali kuinunua nyumba hiyo ingawaje kwa bei ndogo na hatimaye alifanikisha zoezi hilo. Alikuwa na fedha nyingine ambazo pia aliuza mitubwi yake miwili aliyofanyia kazi kijijini hapo.
Baada ya kumaliza zoezi hilo hakupoteza muda zaidi ya kuondoka na kuungana na David na kuanza safari usiku huo wakiondoka eneo hilo. Alikuwa hajabeba vitu zaidi ya vifaa kadhaa alivyotumia katika shughuli ya uvuvi alivyoamini vingewasaidia. Walikuwa wakitembea haraka ili kuifikia barabara kuu na mwishoe waliamini wangepata usafiri katika barabara hiyo. Wakati wakiendelea kutembea walishtusha na sauti ya mtu ikiwaita wakati huo ambao kulikuwa na giza nene. “Hey! You guys where to this time?” (“nyinyi mnaelekea wapi wakati huu/”). Waliisikia kauli hiyo ila Otieno aliyemshika mkono David aliukaza akiashiria waendelee na safari yao. “Otieno, Otieno! You cant escape with that child…. Iam going to kill him right now” ( “Otieno,Otieno! Huwezi kutoroka na huyo mtoto….namuua sasa hivi”) Alisikika mtu huyo kwa mara ya pili kauli iliyompa hofu Otieno na kuamua kusimama akiwa na David aliyekuwa akitetemeka.
Alimshika David na kumsukumia mgongoni kwake huku akiamini kijana huyo alikuwa wa bwanaAbraham ambaye pia aliongea kwa sauti iliyoonesha alikuwa amelewa. Alitupa begi lake chini na kutoa kisu kirefu alichokitumia katika shughuli zake za uvuvi. Wakati huo David ambaye mkono wake wa kushoto ulikuwa na kamba iliyoushikilia na kupita shingoni, alikuwa ameshika suruali ya Otieno akiwa na hofu. “We don’t afraid you and…”( “hatukuogopi na…” ). Kabla Otieno hajaendelea na kauli yake hiyo akimweleza mtu huyo. Alishtushwa na kasi aliyoanza kuja nayo mtu huyo eneo walilokuwapo huku kwa mwanga hafifu alimshuhudia akiwa na panga mkononi. Otieno alijiweka sawa na kisu alichokuwa amekishika huku akiwa na hofu pia. Mtu huyo aliyekuwa akikimbia huku akiyumbayumba alielekeza panga lake kwenye paji la uso wa Otieno ambaye alilikwepa ingawaje lilimkata kidogo upande wa shavu lake la kushoto. Hatimaye mtu huyo aliishia kuanguka kando yao kidogo, Otieno akiwa na hasira baada ya kukatwa alimvamia mtu huyo na kumshindilia na kisu kilichopenya sawasawa mgongoni mwake.
Otieno alishtuka na hakuchomoa kisu hicho kwani aliamini alikuwa ameua, alibeba begi lake lililokuwa chini kabla ya kumshika David mkono na walianza kukimbia wakiondoka eneo hilo. Walikuwa wamemwacha mtu huyo ambaye hata Otieno hakumtambua akiwa anahangaika eneo hilo, waliongoza mpaka barabara kuu. Walianza kutembea wakifuata barabara hiyo iliyoelekea maeneo ya Masaka huku wakiwa na imani ya kupata gari lililokuwa likipita eneo hilo. Wote walikua kimya huku Otieno moyoni akiumia juu ya tukio la kuua kama alivyokuwa akiamini kwa vile hakupanga kufanya jambo hilo hata siku moja katika maisha yake. Ingawaje mara kadhaa aliwaza kumfanyia tukio hilo bwana Abraham.
Alikuwa ameshika shavu lake lililodhuriwa huku akiwa ameshikiza kitambaa ambacho kilikuwa kimeloa damu. Baada ya dakika kadhaa waliliona lori moja la mizigo ambalo walili simamisha na watu hao walikubali kuwachukua kabla ya kupanda nyuma ya lori hilo lililokuwa tupu. Safari ikaendelea wakielekea Masaka ambako waliamini wangefanikisha safari yao ya kuelekea Bushenyi. David alikuwa amemkumbatia Otieno huku akiwa bado na hofu juu ya kila kitu kilichokuwa kimetokea. Jambo lililompa hofu zaidi lilihusiana mtandao wa baba yake mkubwa na hivyo alihisi kukamatwa kwake muda wowote.
Baada ya siku tano walikuwapo Bushenyi eneo lililokuwa kando ya ziwa Edward na walianza maisha mapya ya uvuvi ingawaje yalikuwa duni kama walivyokuwa Kalangala.David alijisikia furaha kidogo kwani alikuwa huru tofauti na ilivyokuwa awali, ndani ya siku kadhaa walizokuwapo eneo hilo aliyazoea mazingira ingawaje mara kadhaa aliikumbuka familia yake. Alikuwa akiamini bwanaAbraham alihusika na kila kitu, aliwaza kulipa kisasi juu ya unyama huo. Alielewa kila jambo lililoendelea lilitokana na sababu kubwa ya mali ambazo baba yake aliziacha. Akiwa anafikiria mengi aliendelea kuishi na Otieno aliyemchukulia kama mzazi wake. Eneo hilo la Bushenyi lilikuwa pia karibu na hifadhi ya taifa ya nchi hiyo ya Queen Elizabeth ambako watalii walikuwa wakitembelea maeneo hayo. Kulikuwa na magari yaliyokuwa yakipita katika kijiji hicho cha Bushenyi kuelekea katika hifadhi hiyo kila siku.
Otieno Ndakufurila siku zote alikuwa akimwambia David kwamba alikuwa na siri kubwa ya uovu wa bwanaAbraham. Siri hiyo alidai ilihusiana pia na mwonekano wake kama vile ameungua na moto ikiwa baada ya kumwagiwa tindikali. Alimwahidi David kumsimulia kila kitu juu ya mkasa huo baada ya kukua kwake. Akiwa na hasira alikubali maelezo hayo lakini alichukia kila kitu juu ya baba yake mkubwa bwanaAbraham. Muda wote alikuwa akimshukuru Otieno kwa kuokoa maisha yake na zaidi alimchukulia kama baba yake kwa upendo alikuwa nao.
Hasira zake ziliendelea kujengeka kadri siku zilivyoenda akimchukia bwanaAbraham ambaye pia alifanya mipango ya jaribio la kuuawa kwake katika ziwa Victoria. Baada ya miezi mitatu David alikuwa ni msaada mkubwa kwa Otieno katika suala la uvuvi huku muda wote wakionekana pamoja katika kijiji hicho. Tayari mkono wake aliokuwa ameumia ulikuwa umepona na zaidi hakuwa na maumivu tena. Suala la elimu lilikuwa limeisha kabisa na hakuwaza kusoma tena kwa wakati huo. Hiyo yote ilitokana na mazingira yaliyokuwapo katika kijiji hicho ambacho hakikuwa na shule na watoto wenzie kama yeye walikuwa wakiji shughulisha na uvuvi na familia zao. Alikuwa anapenda sana kusoma lakini aliwaza uweza wa Mungu pekee utokee ili arudi shule kama ilivyokuwa wakati wa uhai wa baba yake.
* * * *
BwanaAbraham alifurahia kila jambo lililoendelea kwenye maisha yake baada ya kutekwa kwa David kama ilivyoelezwa, watu wa familia hiyo waliamini mtoto huyo aliuawa. Hayo waliyabainisha baada ya kuhisi hata kifo cha Johnson na familia yake kilifanywa na hila ya mtu. Hivyo hawakuwa na budi zaidi ya kumkabidhi bwanaAbraham kila kitu kama mrithi wa mali za mdogo wake. Walikuwa wakiendelea kusubiria maelezo ya askari juu ya kupatikana kwa David akiwa hai au amefariki zoezi ambalo halikuwa na mafanikio. Siku zilizidi kwenda pasipo kupatikana kwa taarifa zozote kutoka jeshi la polisi na mwishoe walikata tamaa juu ya uwezekano wa kupatikana kwa mtoto huyo.
Wakati hayo yakiendelea ni muda ambao bwanaAbraham alikuwa mlevi kupindukia tofauti na ilivyokuwa awali akifurahia kila hatua ya mafanikio yake. Mbali na siri nzito ambazo mkewe alikuwa nazo juu ya kila kitu kilichokuwa kimetokea bado hakujali kwani alianza kumsaliti mkewe huyo. Alikuwa akitembea na wanawake tofauti ambao alivutiwa nao kwa sababu alikuwa akiamini ilipo fedha hakuna jambo lililoshindikana. Moyoni alikuwa na ukatili uliokuwa umejijenga kwa kiasi kikubwa na suala la kuua lilikuwa dogo sana kwake. Alikuwa akijitahidi kumtimizia mwanaye Sabinus kila alichokihitaji kwa vile alimpenda sana mtoto wake huyo. Jambo lililokuwa likimuudhi ni ni tabia ya mtoto huyo aliyependa kumuulizia sana David ambaye aliamini alikuwa ameshakufa siku nyingi zilizokuwa zimepita.
Suala hilo ndilo lililomfanya ampeleke mwanaye huyo kusoma nchini Afrika Kusini ili asahau kila kitu kilichomhusu binamu yake huyo David. Alitarajia mwanaye huyo awe anarudi nchini Uganda wakati wa likizo, jambo hilo alifanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani taratibu Sabinus alianza kumsahau David. BwanaAbraham alibakia nyumbani kwake na mkewe huku akiendeleza tabia yake ya uasherati ambayo mkewe hakuitambua na zaidi alikuwa mlevi kupindukia. Kutokana na tabia hiyo aliyokuwa nayo bwanaAbraham ilipelekea asababishe ujauzito kwa mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Aminata aliyekuwa mkazi wa jiji hilo la Entebbe. Tukio hilo lilimshtua kidogo na aligundua mwanamke huyo alifanya makusudi ili aweze kupata nafasi zaidi kwa bwanaAbraham.
Aliingiwa na hofu juu ya ujauzito huo huku akihofia mkewe kugundua jambo hilo hivyo aliamua kumlaghai mwanamke huyo, Aminata kwa kumpa kiasi kikubwa cha fedha ili atoe mimba hiyo. Mwanamke huyo alipokea fedha hizo huku akiwa amemwahidi bwanaAbraham kuwa angeitoa lakini hakufanya hivyo zaidi ya kuacha usumbufu kwa bwana Abraham. Baada ya miezi kadhaa mwanamke huyo alijifungua mtoto ambaye alifanana kwa kiasi kikubwa na Sabinus aliyekuwa mtoto pekee wa ndoa ya bwanaAbraham. Mwanamke huyo alihisi jambo hilo lingepokelewa vizuri na bwanaAbraham lakini alipojaribu kumweleza akimkataa mtoto huyo ambaye hakuthubutu hata kwenda kumwangalia. Aminata alianza maisha huku akiogopa kumfuata baba wa mtoto huyo ambaye alitishia kumuua.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
BwanaAbraham hakutaka kumsikia kabisa mtoto huyo huku akiamini angeweza kuhalibu ndoa yake iliyokuwa imedumu kwa miaka kadhaa. Akiwa anaendelea zaidi na tabia yake ya ulevi hakuwa na shaka juu ya maisha kwani biashara zake ziliendelea kukua kadri siku zilivyoenda. Baada ya miezi kadhaa Sabinus alirudi akitokea Afrika kusini alikoenda kusoma, alionekana akiwa amekua na zaidi alikuwa amejifunza mambo mengi. Furaha ya wazazi wake iliongezeka zaidi baada ya mtoto wao huyo kurudi nyumbani hapo akiwa na matokeo mazuri kitaaluma kwani alikuwa ameongoza katika darasa lake. Sabinus hakuwa na furaha na muda wote alionekana akiwa na mawazo, jambo hilo ndilo lililomfanya baba yake ahitaji kufahamu ukweli juu ya huzuni yake. Hasira zilimpanda bwanaAbraham aliyemkemea mwanaye huyo baada ya kugundua alikuwa na huzuni juu ya David, aliyekuwa binamu yake. Hakuonyesha dhahiri hasira zake, lengo likiwa kuhalibu akili ya Sabinus katika kumfikiria David.
Alimweleza kuwa ndugu yake huyo alipatikana amekufa miezi miwili iliyokuwa imepita kando ya ziwa Victoria na tayari alikuwa ameshazikwa. Taarifa hizo zilimuumiza sana Sabinus ambaye alilia kwa uchungu. Siku zote alikuwa akiamini David alikuwa hai ila taarifa hiyo ya kwamba alikuwa ameshazikwa ilimkatisha tamaa na alijikuta nafsi yake ikianza kukubali taratibu kuwa David alikuwa amefariki. Baada ya wiki mbili familia yao ilianza kuonekana na furaha ikiwa ni baada ya Sabinus kuamini taarifa alizopewa. Akiwa mtoto pekee na kiunganishi katika familia hiyo, alipunguza kasi ya ulevi ya baba yake ambaye aliwahi kurudi nyumbani kwao na muda wote walikuwa katika furaha. Walikuwa wakitembelea sehemu tofauti za vivutio vya watalii kila ilipofika mwisho wa wiki wakiwa pamoja na Sabinus aliyekuwa na miezi miwili ya likizo.
Maisha yenye furaha katika familia yao yaliendelea, hatimaye ulifika wakati ambao Sabinus alikuwa amebakiwa na wiki moja tu ili arudi shule, Afrika Kusini. Ni wakati ambao bwanaAbraham aliandaa ziara ya kifamilia kwa ajili ya kutalii hifadhi ya taifa ya Queen Elizabeth. Ziara hiyo ilitarajiwa kufanyika mwishoni mwa wiki ikiwa imebakiwa na siku tatu. Ilikuwa ikisubiriwa kwa hamu hasa kutokana na vivutio vingi vilivyokuwa katika hifadhi hiyo. Hatimaye siku ya Jumamosi ambayo ilipangwa kwa ziara hiyo ilifika, nyakati za asubuhi bwanaAbraham alionekana akiwa na mkewe pamoja na Sabinus wakipanda katika gari lililopaswa kutumiwa katika safari hiyo kati ya magari mawili waliyopanga yatumike. Mbali na gari hilo, lilikuwapo jingine la vijana wa bwanaAbraham ambao kazi yao kubwa ilikuwa ni kumlinda bosi wao huyo na familia yake. Safari ilianza wakitumia magari hayo ya kifahari aina ya Range Rover ikiwa yapata saa moja kamili asubuhi.Walikuwa wakitarajia kutumia kutwa nzima ya siku hiyo kwa safari kutokana na umbali mrefu uliokuwapo kuifikia hifadhi hiyo ya Queen Elizabeth iliyokuwa magharibi mwa jiji hilo la Entebbe.
Muda wote wa safari wakiwa wanaendeshwa na dereva wao, bwana Abraham alikuwa akiutumia kuongea mambo tofauti na mkewe. Majira ya saa mbili usiku walikuwa wakishusha mizigo yao mbele ya hoteli ya kitalii iliyokuwapo katika eneo la hifadhi hiyo. Walikuwa wamechoka sana baada ya safari hiyo ndefu wakiwa wamepita Masaka, Mbarara na Bushenyi eneo lililokuwa karibu sana na hifadhi hiyo lakini likiwa karibu pia na ziwa Edward. Siku iliyofuata walikuwa wamepanga kwenda kuripoti katika ofisi za hifadhi hiyo ili lengo lao kuu ya kuitembelea hifadhi hiyo lianze kukamilika sawasawa. Walitarajia siku hiyo iwe ya kwanza kati ya mbili za kuzunguka sehemu tofauti za hifadhi hiyo.
Siku iliyofuata walifika mapema katika ofisi za hifadhi hiyo ya Queen Elizabeth na mara baada ya kukamilisha taratibu zote za kutalii hifadhi hiyo zoezi hilo lilianza. Walikuwa wamepewa magari mawili yakiwa na waongozaji wa watalii, walianza kuzunguka katika hifadhi hiyo huku wakionekana wakiwa na furaha. Hiyo yote ilitokana na vivutio vilivyokuwa katika hifadhi hiyo. Siku hiyo iliisha wakiwa wametembelea maeneo mengi na zaidi wakiwa na furaha juu ya ziara hiyo. Siku iliyofuata kama ilivyokuwa imepangwa walimalizia ziara yao na jioni ya siku hiyo huku wakionekana wameridhika walikuwa wakipanga vitu vyao tayari kwa safari ya kurudi jijini Entebbe. Sabinus muda wote wakiwa katika hifadhi hiyo alikuwa na furaha na alionekana kama alikuwa amesahau mambo kadhaa yaliyokuwa kikwazo kwake hususani kifo cha David kama alivyoelezwa.
Siku iliyofuata majira ya saa moja asubuhi, safari ilianza wakiwa wanatarajia kupita eneo la Bushenyi na hatimaye kuendelea na maeneo mengine kabla ya matarajio yao ya kufika jijini Entebbe. Nyakati hizo za asubuhi muda wote wakati safari ikiendelea walikuwa kimya kutokana na uchovu waliokuwa nao. Baada ya kuendeshwa kwa magari yao kwa zaidi ya kilometa arobaini toka katika hifadhi ya Queen Ellizabeth, tayari walikuwa katika kijiji cha Bushenyi. Wakati huo ndio ambao gari alilokuwapo bwanaAbraham na familia yake lilipata hitilafu katika injini yake. Hivyo magari hayo yote yaliegeshwa kando ya barabara na fundi husika wa kazi hiyo waliyetembea naye alianza kulichunguza gari hilo. BwanaAbraham alikuwa akilalamika juu tukio hilo la kuhalibika kwa gari lake huku wakiwa nje ya magari hayo. Matengenezo ya gari hilo yalionekana kuhitaji muda kidogo jambo lililomfanya Sabinus amwombe baba yake aende kuzunguka sehemu ya karibu na eneo hilo iliyokuwa na makazi ya watu ambayo pia ilikuwa kando ya ziwa Edward. BwanaAbraham alimhurusu mwanaye ikiwa ni baada ya kumwamuru kijana wake mmoja aongozane naye ili kumhakikishia usalama.
Sabinus aliondoka na kijana huyo aliyekuwa na kifua kipana na kuanza kutembea wakielekeakatika makazi ya kijiji hicho cha Bushenyi. Baada ya kutembea kwa muda wa dakika kadhaa, tayari walikuwa wakizunguka katika makazi ya watu wa kijiji hicho. Sabinus alikuwa akishangaa jinsi makazi hayo duni ya wavuvi wa samaki yalivyokuwa. Kwake aliona kama alikuwa akiendeleza utalii waliokuwa wameufanya katika hifadhi ya Queen Elizabeth. Hiyo yote ilitokana na nyumba hizo ndogo zilizoezekwa kwa majani na zaidi zikiwa zimejengwa kwa udongo, lakini jambo lililomshangaza zaidi ni umati wa watu waliokuwapo katika eneo hilo. Wakati wakiendelea na mizunguko hiyo na kijana aliyeongozana naye kama alivyomweleza baba yake kuna jambo lilimshtua na kumfanya asimame na kuanza kuangalia kwa makini. Kijana aliyekuwa naye hakuelewa jambo lililoendelea na yeye alisimama huku akiendelea kushangaa pia mazingira ya eneo hilo zaidi uwingi wa watu waliokuwapo.
Sabinus alimwona mtu aliyeamini alikuwa ni David kwa mbali akiwa anaelekea eneo walilokuwapo huku akiwa amejitwisha kikapu kikubwa ambacho kilionekana kikichuruzika maji. Jambo hilo ndilo lililomfanya asimame huku akihisi mtu huyo aliyekuwa amekonda pia alikuwa ni binamu yake. Akiwa miongoni mwa watu hao wengi, mtu huyo aliyehisi ni David alikuwa akisogea eneo walilokuwapo kadri sekunde zilivyozidi kusogea. Imani yake kuwa mtu huyo alikuwa ni David iliongezeka zaidi kwani hatimaye alikuwa karibu yao na alionekana vizuri. Sabinus alijihisi kurukwa na akili kwani tayari aliambiwa na wazazi wake kuwa binamu yake huyo alikutwa akiwa amefariki kando ya ziwa Victoria na tayari alikuwa ameshazikwa.
Ghafla macho ya Sabinus na mtu huyo aliyeamini alikuwa ni David yaligongana kabla ya mtoto mwenzie huyo kushtuka kumwaona Sabinus ilhali akiwa katika mavazi duni. Alimwangalia kidogo kabla ya kutupa kikapu hicho kikubwa alichokuwa amejitwisha na kuanza kukimbia akijichanganywa kwa watu waliokuwapo eneo hilo. Kikapu hicho kilikuwa na samaki na watu waliokuwa wakipita eneo hilo walikikimbilia kikapu hicho kabla ya kuanza kuchukua samaki hizo zilizokuwa zimetupwa.
“David! David! Please Davie don’t run….I need you David” (“David! David! Tafadhari Davie usikimbie…. Nakuhitaji David”) Alilalamika Sabinus huku akimshuhudia mtu aliyeamini alikuwa ni David akikimbia na kutoweka eneo hilo. Wakati huo alikuwa akijaribu kupita katika njia ndogo iliyokuwapo ili kumfuata mtu aliyeamini alikuwa ni David lakini watu kadhaa walikuwa wakigombaniana samaki alizokuwa amezitupa walimzuia.
Hatimaye alifanikiwa kupita eneo hilo kabla ya kuanza kukimbia akielekea upande ambao mtu huyo alikuwa ameelekea huku akiwa analitaja jina la David. Kijana aliyekuwa ameongozana na Sabinus alishtushwa na jambo hilo alilokuwa analifanya mtoto huyo huku akiwa hajamwona David aliyefika kabisa mita kadhaa toka eneo walilokuwa wamesimama na Sabinus. Bila kupoteza muda alianza kukimbia akimfuata Sabinus alihisi alikuwa amechanganyikiwa. Baada ya dakika kadhaa alifanikiwa kumkamata na zaidi alihitaji kujua tatizo la mtoto huyo. “Whats the problem with you….aah! just tell me…”( “tatizo lako nini….aah! niambie…”) Alisikika kijana huyo wa bwana Abraham akiwa amemkazia macho Sabinus akihitaji kujua tatizo lililomfanya akimbie ovyo huku akilitaja jina la David
“David is alive…. My cousin is alive….” (“David ni mzima…. Binamu yangu ni mzima”) Alisikika Sabinus huku akiangalia huku na huku akiamini angeweza kumwona David. Wakati huo alikuwa ameshikwa sawasawa mkono wake na kijana huyo na alishindwa kabisa kujitoa. Kijana huyo wa bwana Abraham kwanza alicheka kwa sekunde kadhaa baada ya Sabinus kumweleza kuwa David bado ni mzima. Baada ya kucheka alisikika akisema kuwa David alikufa katika ziwa Victoria, hakuongeza jambo lolote zaidi kabla ya kuanza kumvuta Sabinus ili waondoke eneo hilo.
Alifanya zoezi hilo huku mtoto huyo akiwa analia kwa nguvu akilitaja jina la David na kusisitiza kuwa alikuwa hai. Kijana huyo wakati huu alianza kuamini kuwa Sabinus alikuwa amechanganyikiwa kwani alikuwa ni mmoja wa watu waliokuwapo katika tukio ambalo siku zote aliamini David alikufa. Alishuhudia kwa macho yake miezi kadhaa iliyokuwa imepita wakati ambao David alipigwa risasi mbili kifuani kabla ya kuwa mmoja wa watu walioenda kumtupa mtoto huyo umbali wa kilometa moja kutoka katika ufukwe wa ziwa Victoria. Siku zote alikuwa akiamini mtoto huyo alikufa katika maji ya ziwa hilo na kuwa chakula kwa samaki. Hakumsikiliza David alivyolia hata kidogo zaidi ya kuendelea kumvuta kwa nguvu huku wakiondoka eneo hilo na zaidi watu walikuwa wakiwashangaa.
Baada ya dakika kadhaa walikuwa wametoka katika eneo la makazi hayo ya wavuvi na walikuwa wakielekea eneo ambalo magari ya bwana Abraham yalikuwapo. Walikuwa katika barabara kuu huku sauti ya kulia ya Sabinus ikiwa imeongezeka kwa kiasi kikubwa.Wakiwa wanaendelea kuelekea katika eneo ambalo walikuwa wameyaacha magari hayo, waliyashuhudia yakiwa barabarani yakielekea eneo walilokuwapo ambalo ndiko njia ya kuelekea Entebbe ilikuwapo baada ya kupita sehemu za Mbarara, Masaka na Mpingi. Magari hayo yalisimamishwa na bwana Abraham na mkewe walionekana wakishangaa jinsi mwanao alivyokuwa analia huku akilitaja jina la David. Kijana aliyekuwa naye alikanusha maelezo hayo akieleza hakumwona David kama Sabinus alivyoeleza. Alieleza hisia zake kuwa huenda mtoto huyo alikuwa amechanganyikiwa. Bwana Abraham na mkewe walionekana wamemwelewa kijana huyo kwani hata wao hawakuamini hata kidogo kwamba David alikuwa hai. Walimpakiza kwa nguvu Sabinus kwenye gari kabla ya safari kuanza wakirudi jijini la Entebbe. Muda wote wa safari Sabinus alikuwa analia huku akiangalia katika kioo cha nyuma ya gari hilo maeneo hayo waliyokuwa wanayaacha. Majira ya saa tano usiku magari yao yalikuwa yanaegeshwa katika nyumba ya bwana Abraham baada ya safari ndefu.
* * * *CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
David akiwa anaendeleza shughuli za uvuvi kwa kushirikiana na Otieno alikuwa amechanganyikiwa baada ya kumwona mtu aliyeamini alikuwa ni binamu yake, Sabinus. Mara baada ya kumwona binamu yake huyo hakuona umuhimu wa samaki alizokuwa amezibeba ambazo alikuwa akizipeleka kuziuza katika kituo ambacho samaki hizo ziliuzwa kijijini hapo. Huku akikimbia akili yake ilikuwa imetawaliwa na kifo kwa vile alimchukulia Sabinus kama baba yake na kuhisi angeweza kuuawa. Alisikia sauti ya binamu yake huyo ikimwita lakini hakuthubutu kurudi kumfuata kabla ya kwenda kujificha mahali na kumshuhudia Sabinus akikamatwa na kijana mmoja aliyekuwa amejaa kifua chake. Kijana huyo aliondoka na binamu yake huyo huku akiendelea kulia na kulitaja jina lake, David alianza kuwafuatilia nyuma ili kushuhudia eneo ambalo wangeelekea. Mwishoe aliwaona wakipanda katika moja ya gari kati ya magari mawili ya kifahari huku Sabinus akiendelea kulia kwa uchungu.
Moyo wake ulishtuka kwa hofu baada ya kumwona bwana Abraham akiwa na mkewe katika gari hilo jambo lililomfanya David afichame tena katika eneo hilo alilokuwapo. Hofu ilimwingia kwa kiasi kikubwa na kuanza kuhisi kuwa angeweza kuuawa muda wowote na baba yake mkubwa huyo. Akiwa katika kichaka alichojificha aliyashuhudia magari hayo yakiondoshwa eneo hilo huku sauti ya kulia ya Sabinus ikiendelea kusikika. Kwa umbali alimwona Sabinus kupitia kioo akiwa katika eneo la nyuma la gari hilo huku akilia na zaidi akionesha nia yake ya kukutana na David. Mara baada ya magari hayo kuzamia kabisa eneo hilo, alijikuta machozi yakianza kumtoka. Hiyo yote ilitokana na ugumu wa maisha aliokuwa akiishi wakati huo huku akishuhudia baba yake mkubwa akimiliki mali za baba yake kama zake. Akiwa amekaa chini katika kichaka hicho alikuwa amevaa shati lililokuwa chafu kupindukia huku likiwa siyo la umbile lake kwani lilikuwa la mtu mzima. Shati hilo wakati akitembea lilikuwa likionekana kama gauni kutokana na ukubwa wake. Zaidi ya hapo suruali yake aliyoivaa ilikuwa imejaa viraka hususani maeneo ya makalio na sehemu za magoti huku akiwa hana viatu.
Nywele zake zilikuwa ndefu na chafu kama vile alikuwa mtu asiyeyafahamu maji lakini pia akiwa na ngozi kavu kwa vile hakutumia mafuta kabisa. Alisimama alipokuwa amekaa na kuanza kutembea akielekea katika eneo la makazi la kijiji hicho na lengo haswa lilikuwa kwenda kuonana na mlezi wake na mtu aliyeamini alikuwa ni kama mzazi kwake, bwana Otieno Ndakufurila. Wakati akiendelea kutembea alikuwa akikumbuka upendo ambao baba yake alikuwa akimpa miezi kadhaa iliyokuwa imepita ikiwa ni pamoja na kumhakikishia kila kitu kilichohusu shule. Alikumbuka pia fadhila hizo ambazo baba yake alimfanyia Sabinus sawa na yeye. Mbali na upendo aliokuwa nao kwa binamu yake Sabinus, hakuwa na imani na mtu huyo tena alikuwa akihisi angeungana na baba yake ili kumwangamiza.
Baada ya dakika kadhaa alifika katika nyumba yao ndogo ambako alimwona Otieno akiwa amejipumzisha nje. Alikuwa amemtuma akauze samaki alizozibeba lakini kwa jinsi alivyomwona David alihisi kuna jambo. Alimfuata mtoto huyo ambaye alimsimuliwa kila kitu kilichokuwa kimetokea. Otieno aliumia sana juu ya taarifa hizo za uwepo wa bwana Abraham katika kijiji hicho muda mfupi uliokuwa umepita. Kwa wakati huo Otieno hakuwa tayari waondoke katika eneo hilo walilokuwa wakiishi hivyo alimsihi David waendelee kukaa huku akimini bwana Abraham hakugundua uwepo wao. Waliendelea na shughuli yao ya uvuvi huku David akiwa amepoteza amani aliyokuwa nayo ghafla.
* * * *
* * * *
Sabinus muda wote alikuwa na huzuni akiwa chumbani kwake lakini zaidi mawazo yake yakiwa yametawaliwa na David aliyeamini alikuwa hai. Ikiwa siku ya Jumatano alikuwa amebakiwa na siku mbili ili aondoke nchini Uganda kurudi nchini Afrika Kusini kuendelea na masomo yake. Akili yake ilikuwa imetekwa na mawazo mapya ghafla, alipanga kutoenda tena shule. Alikuwa akiwaza kurudi tena katika eneo la Bushenyi ambako bado aliamini alimwona David akiwa hai. Hakutaka kumweleza jambo hilo baba yake wala mama yake kwani aliona walikuwa hawampi mchango wowote. Hiyo yote ilitokana na vile walivyokuwa wanaamini kuwa alikuwa amechanganyikiwa wakati akiwaeleza kuwa David alikuwa hai. Alipanga kuutafuta ukweli juu ya mtu aliyeamini alikuwa ni David yeye peke yake.
Akiwa na miaka kumi na moja wakati huo, alikuwa na upeo mkubwa na mawazo ya kutosha katika jambo hilo alilokuwa akiliwaza. Bado alikuwa katika mtihani mgumu akiwaza jinsi ambavyo angetoroka hasa kutokana na ulinzi uliokuwapo katika nyumba yao hiyo . Muda wote wakati akiondoka nyumbani kwao hapo alikuwa akipewa mtu wa kumlinda kila sehemu aliyokuwa anaenda jambo lililoanza kumpa shaka. Hakuwa na wasiwasi juu ya fedha kwani akiwa katika umri huo mdogo wazazi wake walikuwa na mazoea ya kumpa fedha za kutosha hususani kipindi anachoelekea shuleni. Hivyo hakuwa na shaka juu ya nauli ya kuweza kumfikisha Bushenyi.
Siku ya Ijumaa jioni kulikuwa na sherere ndogo ya kumwaga Sabinus kabla ya safari yake ya kurudi shuleni nchini Afrika Kusini. Siku hii ndio ambayo pia alipewa kiasi cha shilingi milioni moja za Uganda kwa ajili ya matumizi ya awali akiwa shule. Muda wote wakati hafla hiyo ikiendelea hakuwa na furaha kwani alikuwa akiwaza ni jinsi gani angeweza kuwatoroka wazazi wake siku iliyofuata ili aelekee Bushenyi. Hatimaye hafla hiyo iliisha huku ikieleweka siku iliyofuata angekuwa safarini kuelekea nchini Afrika Kusini.
Siku iliyofuata majira ya asubuhi na mapema alikuwa amesjiandaa huku akiwa ameshapanda kwenye gari la baba yake tayari kwa kuelekea katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa jimbo hilo la Entebbe. Tayari alikuwa ameelezwa kuwa angetumia usafiri wa ndege wa shirika la Uganda Airlines. Wakati akiendelea kuwasubiri wazazi wake hao aliwaona wakitoka ndani ya nyumba yao huku wakibishana juu ya jambo fulani. Hatimaye walijongea kwenye gari hilo na kumweleza Sabinus kuwa hawangemsindikiza uwanja wa ndege kama ilivyokuwa imepangwa. Wakionesha upendo juu yake walimweleza kuwa kulikuwa na tatizo katika mzigo wao wa kontena ishirini zilizokuwa zimewasili katika bandari ya Mombasa nchini Kenya. Hivyo walikuwa wakihitajika haraka sana na mamlaka ya kodi na mapato ya nchi hiyo. Baada ya maelezo hayo ambayo Sabinus aliyapokea kwa furaha ambayo hakuionesha, waliondoka na gari lao jingine huku wakiwa wamempa kazi dereva wao mmoja kuhakikisha anampeleka Sabinus uwanja wa ndege.
Mpaka wakati huo alikuwa akiamini ndoto zake za kwenda kumtafuta David zilikuwa zikizidi kutimia, alikuwa tayari na njia aliyoamini angeitumia kumtoroka dereva huyo. Hatimaye safari ya kuelekea uwanja wa ndege ilianza huku akiwa amekaa kwenye siti ya nyuma ya gari hilo. Eneo hilo pia kulikuwa na mabegi matatu, moja likiwa na nguo jingine likiwa na vitu vingi tofauti vya thamani alivyonunuliwa na wazazi wake kama zawadi. Begi jingine la tatu lilikuwa na vifaa vyake vya shule yakiwamo madaftari aliyoyatumia. Alikuwa akiwaza kutoroka na begi la nguo tu ambalo tayari alikuwa ameweka fedha zote alizokuwa nazo na zile alizokuwa amepewa. Baada nusu saa walikuwa tayari ndani ya eneo la uwanja wa ndege huku dereva huyo akiwa haelewi taratibu zilizokuwa zikitumika. Sabinus alishuka na begi lake lenye nguo kabla ya kumweleza dereva huyo amsubiri.
Alidai kuwa ilimpasa ajiandikishe kama mwanafunzi aliyeenda nje ya nchi huku akimweleza dereva huyo kuwa taarifa zote muhimu za kujiandikisha zilikuwa kwenye begi lake. Akionesha kujiaminia alidai pia ilimpasa akutane na wanafunzi wenzie waliokuwa wanasafiri wote siku hiyo. Dereva huyo aliyekuwa mgeni katika makampuni ya bwana Abraham alimkubalia huku akiona mabegi mengine yakiwa yameachwa, aliamini Sabinus angerudi. Mara baada ya kuondoka Sabinus akiwa na muoga kidogo aliongoza mpaka katika ofisi moja ambayo alizamia kabla ya kupita upande wa pili na kwenda kulifuata eneo lililokuwa na teksi za kukodishwa. Alichukua teksi mojawapo na safari ilianza akielekea kituo kikuu cha mabasi cha jiji hilo la Entebbe. Hakuwa na hofu juu ya wazazi wake lakini aliamini kuutambua ukweli juu ya uhai wa binamu yake ndiyo lilikuwa jambo la msingi zaidi kwa wakati huo.
Dereva aliyekuwa na Sabinus alihisi mtoto huyo alikuwa ametoka safarini na zaidi alijari masilahi yake zaidi. Baada ya dakika ishirini teksi hiyo iliegeshwa katika kituo cha mabasi cha jimbo hilo la Entebbe, Sabinus alimlipa fedha dereva huyo kabla ya kushuka na begi lake. Alikuwa na haraka ya kuondoka huku hofu yake kubwa ikiwa ni uwezekano wa kukamatwa na watu waliokuwa wakimfahamu. Jambo hilo ndilo lilimfanya awaze kupanda gari lolote lililokuwa likielekea magharibi mwa jimbo hilo alilokuwapo. Kwani huko ndiko ilikokuwa rahisi kupata gari ambalo lingempeleka maeneo ya Bushenyi kando ya ziwa Edward ambako ndiko alikuwa akikuwazia. Baada ya dakika kadhaa alipata gari lililokuwa likielekea jimbo la Masaka likiwa linapita maeneo ya Mpingi. Bila kupoteza muda alilipia gari hilo na kwenda kukaa kwenye siti yake. Awali wahudumu wa gari hilo walimtilia shaka ila baada ya maelezo yake kuwa alikuwa anaelekea shuleni walimwelewa. Wakati huo alikuwa amevaa kofia yake ndogo ambayo ilikuwa imepoteza kidogo mwonekano wa sura yake. Gari hilo lilikuwa limebakiwa na dakika kadhaa za kuondoka hivyo muda mfupi baada ya kukaa kwake liliwashwa tayari kwa safari.
Hatimaye gari hilo lilianza safari huku yeye akianza kuamini kuwa siku iliyofuata ni lazima angekutana na David. Alikuwa akiwaza kutafuta gari jingine akifika Masaka kwani sehemu hiyo ilikuwa kama katikati ya safari yake. Gari hilo lilikuwa likiendeshwa kwa kasi jambo lililompa faraja Sabinus ya kufika ndani ya muda mfupi katika safari yake hiyo. Alikuwa amekaa kando ya mama mmoja wa makamo aliyekuwa amejifunika khanga kadhaa. Alikuwa amemsalimia tu mama huyo na muda wote wa safari kila mtu alikuwa ametulia katika siti yake. Wakiwa njiani mama huyo alimnunulia Sabinus vitu tofauti jambo lilofanya waanze kuongea. Hiyo ilifuata baada ya kumwamini mama huyo kuwa alikuwa mtu mwema. Alimweleza mama huyo kuwa alikuwa akielekea shuleni na hakuhitaji maswali zaidi juu ya familia yake kwani hata jina lake alimdanganya. Baada ya kuendeshwa kwa gari hilo kwa umbali wa kilometa kadhaa, hatimaye lilisimamishwa na askari wa barabarani ikiwa ni kilometa chache kabla ya kulifikia jimbo la Masaka.
Jambo hilo lilianza kumpa hofu Sabinus ambaye alikuwa karibu na mama huyo. Askari wawili waliingia kwenye gari, aligeuka haraka na kumshuhudia askari mmoja akiwa na picha mkononi aliyokuwa akiwaonyesha watu. Akili ya haraka ilimtuma na kuamini jambo hilo lilikuwa hatari kwake, pasipo kumwambia kitu mama huyo aliyekuwa amekaa naye. Aliivuta haraka khanga ya mama huyo kabla ya kujifunika kichwani na kujiegesha begani kwa mama huyo akiwa kama amelala. Jambo hilo lilimshangaza sana mama huyo ambaye akiwa bado hajamuuliza Sabinus juu ya kitendo hicho, tayari askari hao walikuwa wamefika katika siti zao.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Do you know this child?..” (“unamfahamu mtoto huyu?”) Lilikuwa swali la kwanza la askari aliyefika katika eneo walilokuwapo huku akimwonesha picha ya Sabinus, mtu ambaye aliamini alikuwa amekaa kando yake. Mama huyo alishtuka kidogo kabla ya kusikika akikana kumfahamu Sabinus huku akiwa hajiamini “Mh! Noo! I don’t know him….” (“Hapana simfahamu) “…and who’s that little child” (“… na huyo mtoto ni nani?) alisikika askari huyo. Mama huyo aligeuka na kumwangalia Sabinus aliyekuwa anajifanya amelala huku akiwa anatetemeka kama alivyomgundua kwa vile alikuwa amemkumbatia.Hakupoteza muda aliwajibu askari hao kuwa Sabinus alikuwa mtoto wake na alikuwa alijisikia vibaya wakati huo. Askari hao walitikisa vichwa wakiashiria kuelewa kabla ya kumalizia zoezi hilo kwa kuwauliza abiria wengine. Baada ya dakika kadhaa walimaliza kabla ya kushuka kwenye basi hilo na kulihurusu liondoke.
Sabinus bado aliendelea kutetemeka huku mama huyo wa makamo aliyekuwa amekaa naye akionesha hasira juu yake akiamini huenda alikuwa mtoto mkorofi. Hakutaka abiria wengine waliokuwa kwenye gari hilo watambue kuwa mtoto aliyetafutwa alikuwamo humo jambo lililomfanya aanze kumuhoji Sabinus kwa sauti ya chini. Mama huyo aliendelea kuutambua ukweli juu ya mtoto huyo aliyekuwa bado amejifunika khanga yake huku akiwa amemfahamu kama alikuwa mtoto wa tajiri mkubwa aliyetambulika nchini Uganda, bwanaAbraham. Baada ya nusu saa alikuwa ameupata ukweli wote wa mtoto huyo na hakuona haja ya kumzuia kufanikisha ndoto yake ya kukutana na binamu yake. Majira ya saa tisa alasiri walifika eneo la Masaka kabla ya mama huyo kumsaidia Sabinus kupanda gari lililoelekea Bushenyi likipita Mbarara.
Sabinus aliendelea na safari huku akiwa na hofu juu ya kufika kwake salama eneo husika. Hofu yake kubwa ilikuwa kwa baba yake ambaye uwezo wake wa fedha ulimwezesha kufanya lolote. Tayari alikuwa anaelewa kuwa askari aliofanikiwa kuwakwepa walikuwa wameshatumiwa picha yake kwa njia ya mtandao. Zaidi aliamini vyombo vya habari jijini Entebbe hususani magazeti yangeandika habari juu yake, jioni ya siku hiyo na siku iliyofuata. Majira ya saa tano usiku gari alilosafiri nalo lilifika eneo la Bushenyi, akiwa amechoka aliongozana na watu kadhaa walilokuwa wakielekea katika eneo waliloishi wavuvi. Baada ya dakika kadhaa alifika eneo hilo lililokuwa tulivu huku akiamini watu walikuwa wamelala lakini kuna mwanga wa taa za mafuta ulikuwa ukiangaza kwa mbali ndani ya ziwa Edward ambako wavuvi kadhaa waliendelea na kazi yao.
Hakuelewa jambo la kufanya lakini aliamini siku iliyofuata ingekuwa na utatuzi wa swali lililokuwa kichwani mwake juu ya uhai wa Davidi. Alielekea kando ya ziwa hilo, wakati huo ulikuwa ni msimu wa joto kiasi na aliwaona watu kadhaa wakiwa wamelala kando ya ziwa hilo, walionekana kama walikuwa hawana makazi katika eneo hilo. Yeye pia alienda kujiegesha pembeni ya mtumbwi mmoja na kulala huku akiwa amelikumbatia begi lake lililokuwa na fedha alizoamini zingemsaidia akiwa kijijini hapo. Kulikuwa na Mbu waliomn`gata lakini alijikaza akihitaji kukutana na David siku iliyofuata. Alitamani kumtafuta ndugu yake huyo usiku huo ila uwingi wa makazi ya watu ndio uliomfanya akate tamaa ya kumtafuta. Usiku huo ulikuwa mgumu kwake akiwa katika mazingira ambayo siku zote watu walikuwa wakimsimulia. Mazingira aliyokuwapo hakudhania kama angewahi kuishi kutokana na uwezo wa kifedha aliokuwa nao baba yake. Muda wote alikuwa akihangaika kutokana na kung`atwa na Mbu jambo lililomfanya akose usingizi. Aliamua kuamka majira ya saa kumi na mbili asubuhi baada ya kuona mateso yalikuwa yamezidi eneo alilokuwapo. Tayari alikuwa na vipele vingi usoni mwake na sehemu nyingine tofauti ikiwa ni baada ya kun`gatwa na Mbu. Alianza kutembea eneo la kando kando ya ziwa hilo akiwa na begi lake, alikuwa akisubiria saa moja asubuhi ifike ili aanze kumtafuta David. Wavuvi kadhaa walionekana wakiandaa nyavu zao tayari kwa shughuli ya siku hiyo.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment