IMEANDIKWA NA : GLOBAL PUBLISHERS
*********************************************************************************
Simulizi : Mapenzi Yamenifanya Niwe Muuaji
Sehemu Ya Kwanza (1)
Katika maisha yangu sikuwahi kuwaza kuua hata nzi kutokana na huruma niliyokuwa nayo.
Watu wengi walipenda kuniita mlokole japo historia yangu yote niliishi maisha ya kutokuwa na dini nikiamini Mungu wa Wakristo ndiye Mungu wa Waislamu kutokana na mafundisho ya dini zote niliyoyafuatilia.
Utashangaa kwa nini niliishi bila kuwa na dini ikiwa wazazi wangu wana dini, tena dini tofauti, baba Muislamu na mama Mkristo. Katika maisha yao hakuna aliyekubali kumfuata mwenzake na kukubaliana, kila mmoja aishi katika imani yake. Hivyo basi, nikawa mtoto wa wazazi wa dini mbili, pamoja na wazazi wangu kuishi kila mmoja na dini yake, waliishi katika upendo wa hali ya juu kwa kila mmoja kuheshimu imani ya mwenzake.
Nilipopata ufahamu nilijikuta nipo njia panda kwa vile sikutaka kumuudhi mmoja wa wazazi wangu kwa kumpendelea mmoja. Halafu kitu cha ajabu nilikuwa mtoto mmoja kama roho, hivyo niliamua kusimama katikati ya wazazi wangu kwa kutochagua dini yoyote. Lakini nilikuwa nafahamu kipi mwanadamu anatakiwa kukifanya ili usimuudhi Mungu.
Katika maisha yangu yote niliamini tofauti ya dini mbili ni ndogo sana lakini anayetakiwa kuabudiwa ni Mungu mmoja. Tokea hapo niliishi nikiwa sina dini na kuishi kama mpagani, tofauti yangu nilikuwa najua Mungu ni mmoja na ndiye anayetakiwa kuabudiwa, lakini sikwenda msikitini wala kanisani na malumbano ya dini hizi mbili mimi yalikuwa hayanihusu.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wazazi wangu nao walikubaliana na mimi baada ya ushawishi wa kila mmoja kugonga mwamba. Huu ulikuwa muktasari wa maisha yangu ya awali ya kunifanya nisiwe na dini kwa ajili ya mapenzi ya wazazi wangu.
Kutokana na malezi mazuri ya wazazi wangu, niliweza kuishi sehemu yoyote na mtu wa aina yeyote, siku zote heshima na ucheshi ndivyo vilinifanya watu wanipende.
Kama nilivyosema awali, nilikuwa mtu wa huruma na heshima kwa wakubwa na wadogo, lakini mateso ya mapenzi yalinifanya nigeuke niwe na roho mbaya kukiko shetani.
Kuna maelezo niliwahi kusikia wakati nakua kwamba kuna matendo mengine shetani anakimbia akimuona mwanadamu anatenda. Baada ya kuteswa sana na mapenzi ilifikia hatua kutoa roho ya mtu kwangu ilikuwa kitu cha kawaida hata kwa kosa dogo la kuombana msamaha kwa kuamini hakuna kiumbe kibaya duniani kama mwanadamu ambaye hatakiwi kupewa nafasi kwa vile kama ukimchekea basi atakuumiza wewe.
Mkasa wangu unaanzia pale nilipotimiza miaka 21, nilitoka kwa wazazi wangu na kusafiri nje ya mkoa kwenda kufanya kazi baada ya rafiki yangu kupata kazi ya ujenzi.
Hivyo, hakutaka kuondoka peke yake, alinichukua na mimi huku wazazi wangu wakiniasa niishi na watu kwa heshima na taadhima. Nami niliwaahidi wazazi wangu kuwa nitaishi kama walivyonielekeza.
Nilitengana na wazazi wangu kwa mara ya kwanza toka nitoke tumboni kwa mama wangu. Nilifika mkoani na kufikia kwa ndugu wa rafiki yangu. Kwa vile tulifika Jumamosi jioni sana, tulilala na kesho yake tulipumzika na kupata nafasi ya kupelekwa sehemu ya kazi.
Ulikuwa mradi mkubwa sana ambao tuliambiwa utachukua miaka mitano kwisha, siku ile tulipumzika na kesho yake tulikwenda kuanza kazi. Siku ya pili tuliamka asubuhi na mapema na kwenda eneo la ofisi ambapo ndipo mnapangiwa kazi. Ilikuwa kuna tofauti kubwa na vijana wengi tuliowakuta nje ya geti wakisubiri kuitwa, lakini sisi tulikuwa na mwenyeji, mjomba wa rafiki yangu ambaye alikuwa ndiye msimamizi mkuu wa mradi ule ambao ulikuwa chini ya Wataliano, tuliingia bila kuitwa.
Basi huo ndiyo ukawa mwanzo wa kuanza maisha ya kujitegemea, tulianza kwa kulipwa kwa kutwa kama wenzetu kwa wiki mbili, baada ya hapo tulichaguliwa vijana kama ishirini tuliopewa mkataba na kulipwa kwa mwezi na posho yetu kuongezeka tofauti na wenzetu waliokuwa wakilipatwa kwa kutwa.
Maisha yalikwenda vizuri huku mimi na mwenzangu tukihama kwa ndugu zake na kupanga chumba kimoja na kukaa wawili. Wazazi wangu nao walikula jasho langu kila mwezi kwani niliwatumia robo ya mshahara wangu nao walizidi kuniombea kwa Mungu ili niendelee kupata zaidi.
Siku zilikatika huku nami nikipevuka kiakili na mawazo kufikia hatua ya kuhitaji mwenza. Nyumba tuliyokuwa tumepanga kulikuwa na binti mmoja ambaye Mwenyezi Mungu alimjalia umbile dogo lakini nzuri na sura jamili (nzuri). Binti yule alitokea kunipenda sana kiasi cha kumueleza mama yake angependa aolewe na mimi.
Moja ya njia ya kuonesha ananipenda aliniomba mambo yote ya kike ayafanye yeye kama vile kunipikia chakula cha jioni baada ya kazi, kufua nguo na kusafisha chumba lakini sikumpa nafasi ile kwa kuhofia wazazi wake.
Pamoja na mimi kumpenda sana bado sikumkubalia kutokana na kuwaheshimu sana wazazi wake ambao siku zote walinilea kama mtoto wao.
Siku moja usiku baada ya kutoka kazini, mama mwenye nyumba ambaye ni mama mzazi wa yule binti aliniita kwa kumtumia yule binti. Nami niliitikia wito ule, baada ya kuingia sebuleni kwao, nilikaribisha kwenye kochi lililokuwa karibu na alipokaa mama mwenye nyumba.
“Kazala,” mama aliita kwa sauti ya chini.
“Naam mama,” niliitikia kwa unyenyekevu mkubwa.
“Nimekuita mwanangu nikueleze jambo moja la muhimu sana.”
“Sawa mama.”
“Kwanza wewe dini gani?”
“Sina dini,” nilimjibu kwa mkato.
“Muongo, hebu niambie ukweli wewe ni dini gani?”
“Kweli mama sina dini.”
“Sasa kama ukipata mwanamke mwenye dini utafanya nini?”
“Sitafanya chochote nitaiheshimu dini yake, lakini mi nitabakia sina dini?”
“Kwa nini?”
Sikumficha nilimuelezea maisha ya wazazi wangu na kitu gani kilichonifanya nisiwe na dini.
“Lakini hata kiserikali mtu anapotimiza miaka kumi na nane ana haki ya kuamua chochote bila kuingiliwa, hivyo ulikuwa na nafasi ya kuchagua dini yoyote ya baba au ya mama.”
“Ni kweli, lakini bado kwa mimi sikutakiwa kufanya hivyo.”
“Kwa nini?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nimesimama kati ya baba na mama yangu wote nawapenda na sitaki kumuudhi mmoja kati yao.”
“Sasa mwanangu kuna kitu nimekuitia, mdogo wako Suzana anakupenda sana tena sana kapitiliza kukupenda. Siku zote amekuwa akikuonesha kwa vitendo imeonekana kama umuelewi. Mpaka kuja kunieleza mimi mama yake basi ujue yamemfika shingoni. Kutokana na tabia yako ambayo imekuwa tofauti na wavulana wengi nimeamini unafaa kuwa mkwe wangu.
“Nakuomba uwe mkwe wangu muoe Suzy kwa kweli ni mwanamke mzuri ambaye atajivunia katika maisha yako. Najua utashtuka mama kumpigia debe mwanaye lakini kwa hili sikuwa na jinsi.”
“Nimekusikia mzazi wangu naomba unipe muda ili nami niwasiliane na wazazi wangu.”
“Kuwasiliana na wazazi wako si vibaya, lakini kwanza ni wewe kukubaliana na mwenzako.”
“Mimi nimekubali.”
“Nashukuru kwa majibu yako mazuri, basi nakuruhusu, uwasiliane na wazazi wako, usihofu gharama nitakusimamiane mpaka mwisho wa harusi yenu.”
“Nashukuru mzazi wangu.”
Baada ya kutoka kwa mama mwenye nyumba nilirudi chumbani kujipumzisha, haikupita muda mlango iligongwa alikuwa Suzy.
“Karibu,” nilikabiribisha bila kunyanyuka kitandani.
Alisukuma mlango na kuingia ndani akiwa na sinia lililofunikwa kawa.
“Karibu chakula Kazala.”
Sikutaka kubisha lakini nilitaka tule pamoja Suzy hakukataa tulikuwa pamoja. Tokea siku ule Suzy akawa na uhuru wa kuja kwangu lakini sikuwa na tamaa ya mwili kwa kujiapia mpaka nimuoe kabisa. Mipango ilienda vizuri na Suzy akawa mke wangu ndoa ilifungwa kwa mkuu wa wilaya kila mtu akiwa na imani yake.
Namshukuru Mungu maisha yalikuwa mazuri kwa mke wangu kuonesha mapenzi ya kweli nami pia nilimpenda mapenzi ya dhati. Miezi sita baada ya kuoana tulihama nyumba ya wazazi wa mke wangu na kwenda kukaa kwenye nyumba nyingine ya familia yao iliyokuwepo umbali kidogo toka kwetu, wakati huo mke wangu alikuwa na ujauzito wa miezi minne.
Nyumba tuliyohamia ilikuwa na wapangaji wawili na sisi tulikuwa sehemu ya nyumba mbele iliyokuwa ya kifamilia. Kazi nayo iliendelea vizuri kila siku kuondoka asubuhi na kurudi usiku. Maisha yalisoga muda ulipofika mke wangu alijifungua mtoto wa kike.
Mwenetu alikuwa vizuri mpaka alipofikisha mwaka mmoja na miezi saba nilipatwa na mshtuko kushindwa kutembeza zaidi ya kukaa na kujibuta kwa matako. Katika maisha yangu pamoja ya kutokuwa na dini bado sikuuamini uchawi hata kidogo japo niliusikia kuwa upo. Hali ya mwanangu ya kutotembea ilinishtua sana. Katika kuulizia kwa watu waliomuona mtoto wangu walisema mtoto wangu inawezekana amebemendwa.
Kauli ile ilinishtua sana baada ya kuelezwa maana ya kubemenda ni mtu kutoka nje ya ndoa, kwa upande wangu sikuwa na shaka kwa vile sikuwa na mpenzi mwingine zaidi ya mke wangu mama Zawadi. Pia kwa upande wa mke wangu hata kwa mtutu nisingekubali kutoka nje ya ndoa kwani nilimuamini sana.
Nikawa njia panda kuelewa hali iliyomkuta mwanangu kama inatokana na mtu kutoka nje ya ndoa basi walikuwa wamekosea nikiamini huenda tatizo alilonalo mwanangu huenda linafanana na hilo.
Jumapili moja niliyokuwa nyumbani, nilitoka na mwanangu ambaye nilimpenda sana pamoja na kuchelewa kutembea. Nikiwa natoka dukani nilikutana na mama mmoja wa makamo na kusalimiana naye. Nilipishana naye lakini sikupiga hatua mbili aliniita.
“Baba Zawadi.”
“Naam mama,” niliitika huku nikigeuka kumsikiliza.
“Samahani mwanangu.”
“Bila samahani mama.”
“Basi naomba tusogee pembeni tuzungumze.”
“Hakuna tatizo mama yangu.”
Nilisogea pembeni kidogo ya barabara na kusimama kwenye uchochoro wa kutokea mtaa wa pili.
“Naam mama,” nilianzisha mazungumzo.
“Mwanangu nimekuita ili tuzungumze kitu kimoja, nina imani hukijui kinachofanyika nyuma kwa vile unatoka asubuhi na kurudi usiku kinachotendeka mchana hukijui.”
“Ni kweli mama.”
“Unamuonaje mjukuu wangu Zawadi?”
“Kwa kweli mama hata mimi nashindwa kuelewa.”
“Unashindwa kuelewa nini ikiwa mwanao mnamtesa bila kosa.”
“Mama tunamtesa kivipi?”
“Unaona hii miguu ya mwanao ipo sawa?” aliniuliza huku akiishika miguu ya mwanangu iliyokuwa haina nguvu.
“Haipo sawa, kwa kweli nachanganyikiwa hata sijui sababu ni nini japo watu wananiambia kitu ambacho naamini si kweli.”
“Kitu gani hicho?”
“Achana nacho hakina umuhimu,” sikutaka kumuambia habari ambazo mimi niliona ni za kizushi.
“Kitu gani?”
“Utayaweza maneno ya watu mama, kila kukicha hawakosi ya kusema.”
“Maneno gani?” yule mama alikazania swali lake.
“Achana nayo hayana umuhimu.”
“Inawezekana uliyoambiwa ndiyo nitakayokueleza leo.”
“Nina imani si hayo.”
“Haya, tuachane na hayo, unajua matatizo ya mtoto kuchelewa kutembea yanatokana na nini?”
“Kwa kweli sijui.”
“Yapo mambo mengi, moja kuchezewa na walimwengu na lingine ni kubemendwa.”
“Kwa hiyo tatizo la mwanangu linatokana na nini?”
“Mkeo atamuua mtoto huyu, kwa nini unakuwa na moyo wa kikatili kiasi hiki, kama hawezi kumlea basi mumpeleke kwa bibi yake kuliko kumtesa bila sababu.”
“Mama sijakuelewa, mke wangu amemfanya nini mtoto?”
“Anambemenda.”
“Eti?”
“Anambembenda na mwisho wake atamuua.”
“Mmh! Una maana gani?”
“Mkeo si muaminifu, wote mtaani wanajua, ukitoka na yeye nyuma anatoka anarudi muda umekaribia kurudi.”
“Sasa mama kutoka kwa mke wangu inaingiliana vipi na mwanangu kuchelewa kutembea?”
“Baba jasho la janaba ni baya kwa mtoto hasa ikiwa mliyekutana si wazazi wa mtoto, mmoja wenu akikosa uaminifu na akamshika na uchafu wake lazima mtoto atadhurika.”
“Sasa mama mke wangu mbona muaminifu?” kauli ile ilinishtua.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Baba acha kusema hivyo, sisi ndiyo tunayejua, isingekuwa huyu mtoto wala nisingenyanyua mdomo wangu, ningekuacha ili siku moja ujionee mwenyewe uchafu wa mkeo.”
“Kwa hiyo chanzo cha matatizo ya mtoto ni mke wangu?” nilijikuta nikikosa amani moyoni.
“Baba usiandikie mate, kwa vile mkeo hata aibu hana, siku moja rudi nyumbani mchana utajionea mwenyewe. Kabla ya kufanya lolote fanyia kazi haya niliyokueleza. Ukipata majibu ndiyo utajua mkeo muaminifu au siyo, utapata kiini cha matatizo ya mkeo.
“Ila nakuomba kabla ya yote mtoto wako mpeleke kwa bibi yake kisha fanya uchunguzi wako.”
“Asante mama kwa maelezo yako.”
“Ila nakuomba ukienda kwako usioneshe mabadiliko yoyote, kuanzia Jumatatu siku yoyote rudi nyumbani ghafla mchana utaniambia niliyokueleza ni kweli na maendeleo ya mwanao utayaona kwa muda mfupi akiwa mbali na mama yake.”
“Asante mama.”
Niliagana na yule mama ambaye alikuwa mtu wa heshima na nilimuheshimu sana pale mtaani. Nikiwa narudi, njia nzima nilikuwa na mawazo mazito juu ya maneno niliyoelezwa na sababu ya matatizo yanayomfanya mwanangu ashindwe kutembea.
Kingine ambacho sikutaka kukikubali mara moja ni kuhusu kutoka kwa mke wangu nje ya ndoa. Kwa kweli sikuamini mke wangu kama angeweza kutoka nje ya ndoa hasa kutokana na ukimya pia kuonesha mapenzi mazito kwangu.
Nilifikiria kama ni kweli mke wangu ndiye chanzo cha matatizo ya mtoto, ina maana hajui au anafanya makusudi. Nilipofika nyumbani nilijitahidi kuficha mabadiliko mke wangu alinichangamkia huku akimchukua mtoto ambaye siku zote alimuonesha mapenzi makubwa.
Siku hiyo nilikuwa nyumbani kimwili lakini kiakili nilikuwa mbali sana, kwa kuwa nilikuwa nikiwaza yote niliyoelezwa na wote walioguswa na hali ya mwanangu kuchelewa kutembea kiasi cha watu kumtania kwa kumwita fundi majiko.
Japokuwa mwanangu alikuwa hatembei lakini alikuwa akiongea maneno yote akiwa amekaa kama fundi anayetengeneza majiko.
Kila nilipomuangalia mke wangu sikummaliza, nilivyomuamini na maneno yale nilichanganyikiwa huku upande mwingine nikiona kama maneno yale yalikuwa ni njama za kutaka kuivunja ndoa yangu.
Mke wangu alikuwa mpole na wala hakuwa muongeaji kabisa, muda wote alikuwa kimya mpaka miye nianze kumsemesha.
Niliificha siri ile moyoni mwangu japokuwa kuna wakati moyo ulikubali na wakati mwingine ulikataa kuamini kile kilichokuwa kikisemwa.
Siku ya pili ilikuwani ni Jumatatu nilitakiwa kwenda kazini nilipanga kurudi mchana ili nishuhudie kile kinachosemwa kama ni kweli au la.
Siku ya siku nilipofika kazini, nilisingizia kuumwa kwa vile sikuwahi kuomba ruhusa kutokana matatizo yoyote nilikubaliwa na kurudi nyumbani saa sita kasorobo mchana.
Nilipofika nilikuta mlango ukiwa umefungwa, nilipiga simu ya mke wangu lakini haikuwa hewani. Nilizunguka upande wa pili nilimkuta mtoto wangu Zawadi akichezea matope bila kuwa na mtu yeyote wa kumwangalia.
Nilibisha hodi chumba cha jirani, alitoka jirani yangu ilhali akiwa amepatwa na mshtuko mkubwa sana kwa kuniona muda ule.
“Ha! Shemeji leo umerudi mchana?” alisema huku akimtoa Zawadi kwenye matope na dalili zote zikionesha kwamba kwa kipindi cha mchana, mtoto yule huwa anaachwa peke yake na tayari alikwisha kula kiasi kikubwa cha matope kutokana na mdomo ulivyoonesha.
“Sijisikii vizuri,” nilimjibu kwa sauti ya chini huku roho ikiniuma kwa malezi mabaya aliyokuwa akipewa mwanangu.
Hali ile ilianza kunipa picha ya maneno niliyoelezwa, jirani yangu mama Sonono alianza kumsafisha matope kisha aliingia ndani kwake na kutoka na ufunguo na kunipa huku akisema:
“Shem naomba unitolee na nguo za Zawadi.”
“Hakuna tatizo.”
Niliingia ndani huku nikijiuliza mke wangu atakuwa amekwenda wapi, pia kama nisingekuja mwanangu angekula matope na kuwa mchafu mpaka saa ngapi. Baada ya kumtolea nguo nilimuuliza:
“Mama Zawadi ameenda wapi?”
“Amesema ameitwa na mama yake.”
“Kila siku huwa anaitwa na mama yake?” Nilimshtukiza kwa swali ambalo nilijua hakulitegemea.
“Siku nyingine huwa sijui anaenda wapi.”
“Kwa hiyo akiondoka wewe ndiye unakuwa mlezi wake au siyo?”
“Kwani vipi shem?”
“Nakuuliza wewe ndiye mlezi wake, hebu angalia nimemkuta mtoto anakula matope, kwa siku zote anazoondoka kazi yako ni kumlisha mwanangu matope?” Nilimuuliza kwa hasira.
“Ha...ha...pana shem.”
“Niambie ukweli mke wangu amekwenda wapi maana nimetoka kwao?”
“Si...si...jui akiondoka huniachia mtoto.”
“Huwa anarudi saa ngapi?”
“Jioni kabla hujarudi.”
“Asante.”
Nilimchukua mwanangu na kumpeleka kwa mama mzazi wa mke wangu na kumuuliza kama mke wangu alifika pale nyumbani kwake.
Majibu yalikuwa ni tofauti na nilivyoelezwa, nilimuomba nimuachie mtoto. Alikubali kitu cha ajabu hakuniuliza swali lolote zaidi ya kumchukua mtoto.
Nilirudi nyumbani kumsubiri mke wangu aniambie alikokuwa amekwenda.
Majira ya saa kumi na mbili na nusu mke wangu alirudishwa na gari, kwa vile nilishaelezwa muda wake wa kurudi, nilitoka na kukaa nje, ufunguo nilimpatia mama Sonono na kumwambia akija amwambie kuwa mtoto amechukuliwa na mama yake mzazi.
Alipofika aliteremka na kukimbilia kwa mama Sonono kuulizia ufunguo.
Baada ya muda nilimuona akitoka barabarani akiwa kama anayetafuta kitu, huku akiwa anapiga simu, baada ya muda gari lililomleta lilirudi.
Kabla hajapanda kwenye gari nilijitokeza na kumwita.
“Mke wangu.”
Alishtuka kuniona mpaka simu ikamponyoka chini huku akisema kwa sauti kubwa:
“Ha! Mume wangu!”
“Vipi mpenzi ingia twende nina safari nyingine,” sauti kutoka ndani ya gari ilimhimiza aingie kwenye gari.
“John nenda tu, mume wangu.”
“Mumeo kafanya nini tena mpenzi?”
“John ondoka mume wangu huyu hapa.”
“He!” Sauti ilitoka kwenye gari na gari kuondoka kwa kasi bila kufunga mlango mmoja. Sikutaka kutaharuki nilimuuliza:
“Unatoka wapi?”
“Kwa mama.”
“Yule nani?”
“Bwana wa shoga yangu alinipa lifti.”
“Mmh! Sawa.”
“Vipi mbona mapema?”
“Kawaida tu kwani kuna ubaya?”
“Hakuna, Samahani mume wangu, nilikwenda kwa mama na kupishana naye huku nyuma alikuja na kumchukua Zawadi, nilikuwa naomba nimfuate.”
“Sawa, hakuna tatizo, utanikuta.”
Alisogea mbele na kukodi teksi iliyompeleka kwao, niliingia ndani nikiwa nimefura kwa hasira nikiwa siamini nilichokiona na kuanza kuamini yote niliyoelezwa juu ya uchafu wa mke wangu.
Nilimsubiri kwa hamu kubwa arudi anieleze sababu ya kujifanya kondoo mwenye ngozi ya chui.
Kitu cha ajabu mezani kulikuwa kumeandaliwa kila kitu kuonesha kwamba mke wangu kabla ya kuondoka hufanya kila kitu kwa ajili ya chakula cha jioni ili akirudi hata kama amechelewa chakula kionekane kuwa ni tayari.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Miye nilipokuwa narudi niliamini kuwa mke wangu hakutoka kwa vile chakula kilikuwa kimeshatayarishwa.
Nilikwenda hadi chumbani na kujilaza kitandani miguu ikiwa chini bila ya kuvua viatu, niliweka mikono kichwani huku macho yangu yakitazama juu nisiamini nilichokisikia, hata nilichokiona kwa macho yangu.
Nilipatwa na mtikisiko wa moyo kwa mara ya kwanza tangu niwe na akili timamu japokuwa niliishawahi kuona na kusikia usaliti ndani ya ndoa za watu.
Nikiwa katikati ya mawazo mke wangu alirudi akiwa na mtoto na moja kwa moja alikuja kukaa pembeni yangu huku akijichekesha.
Nilijiuliza mama yake amemwambia nini kutokana na kuwa katika hali ya kawaida tu.
“Vipi mume wangu?”
“Poa.”
“Mbona kama haupo sawa?”
“Nipo sawa,” nilimjibu kwa sauti ya chini.
“Hapana mume wangu lazima utakuwa na tatizo.”
“Nipo sawa.”
“Nakuja,” mke wangu alisema huku akinyanyuka na kwenda nje akimuacha mtoto pembeni.
“Baba,” mwanangu Zawadi aliniita.
“Mama,” nilipenda kumwita hivyo kwa kuwa alikuwa akitumia jina la mama yangu mzazi.
“Pipi api?”
“Nitakwenda kukununulia.”
“Tende dukani baba kanunue pipi,” mwanangu alisema huku akijivuta kwangu na kunishika mkono, niliamua kumpelekea dukani.
Nilimuangalia mwanangu na kujikuta nikitokwa na machozi ya uchungu, alizidi kunilazimisha ninyanyuke. Nilinyanyuka kitandani na kumbeba mpaka dukani ambako nilimnunulia pipi na biskuti.
Wakati napita kurudi ndani nilimsikia mke wangu akizungumza na mama Sonono. Kwa jinsi walivyokuwa wakizunguza niliamini kabisa alijua bado nilikuwa chumbani.
“Dada umeniangushia jumba bovu,” nilisikia sauti ya mama Sonono ikilalamika.
“Jumba bovu vipi, kwani anajua nilikwenda wapi?”
“Kurudi kwa mumeo kuna sababu, hata maswali yake yalionesha anajua mengi juu yako, hata mtoto kwa mama yako alimpeleka yeye.”
“Wewee usiniambie!” sauti ya mke wangu ilionesha kushtuka.
“Kweli, kabisa ila alinikataza nisikuambie.”
“Jamani kwa nini umenigeuka?”
“Sikuwa na jinsi nilihofia kupigwa na mumeo kwa jinsi alivyokuwa angeweza kumtafuna hata mtu.”
“Akupige kwani wewe ndiye uliyetoka nje ya ndoa, wa kupigwa ni miye, kwanza jeuri hiyo ataitoa wapi?” mke wangu alizungumza kwa sauti ya kujiamini.
Maneno yale yalionesha dhahiri kwamba mke wangu alifanya yote yale kwa vile alikuwa na kitu alichokuwa akikitegemea.
“Dada ukitoka tena uondoke na mwanao sitaki ugomvi na mumeo, kwani ataona labda mimi ndiye ninayekufanyia mipango.”
“Mi mtoto mdogo? Nitaondoka naye kwani kazi anafanya yeye? nitamuweka kwenye kochi kisha namaliza haja zangu, hilo shoga lisikupe shaka, basi baadaye.”
Kwa vile ilikuwa giza mke wangu alitupita mimi na mwanangu bila ya kutuona na kuingia ndani.
Nami niliingia ndani na kukutana naye mlangoni, aliponiona aliniuliza:
“Vipi umetoka wapi?”
“Dukani.”
“Eti, kwani mume wangu leo umerudi saa ngapi?”
“Kwani vipi?”
“Nasikia umerudi mapema?”
“Tatizo ni nini?”
“Sasa umerudi mapema ili iweje?”
“Sina ruhusa ya kurudi nyumbani kwangu mapema?”
“Siyo hivyo.”
“Sasa tatizo nini?”
“Ujaji wako umeonekana umekuja kwa sababu.”
“Ndiyo umekuja kwa sababu maalum.”
“Sababu gani?”
Nilijikuta nikipata nafasi ya kufungua yaliyo moyoni mwangu.
“Niambie ulikwenda wapi?”
“Kutembea.”
“Kwa ruhusa ya nani?”
“Nilisahau kukuaga naomba unisamehe kwa hilo.”
“Aliyekurudisha ni nani?”
“Ni rafiki wa shoga yangu.”
“Naomba uniambie ukweli la sivyo leo nitakufanyia kitu kibaya sana,” nilimtisha.
“Unataka kunifanyia kitu gani?” alishtuka.
“Usiponieleza ukweli nitakufanyia kitu kibaya ambacho hutakisahau maisha mwako.”
“Unataka ukweli gani mume wangu?” mke wangu aliingia woga.
“Ninajua kila siku nitokapo nawe huku nyuma unatoka, huwa unakwenda wapi?”
“Nani kakuambia?”
“Si kujua aliyeniambia, bali ni wewe kunieleza ninapotoka nawe unatoka, unakwenda wapi?”
“Waongo hao mi sijawahi kutoka, ni leo tu.”
“Mama Zawadi naomba uniambie ukweli,” nilipandisha sauti.
“Nilikwenda kwa shoga yangu na wakati wa kurudi mpenzi wake alinipa lifti kwenye gari lake.”
“Huyu mtoto kakukosea nini?”
“Kwa vipi?”
“Mbona unamfanya kama yatima, kama unafanya uchafu wako basi mhurumie mtoto, unaridhika na hali ya mtoto ya kuteseka hivi?”
“Nimemtesa kivipi?” majibu ya mke wangu hayakuonesha kushtushwa na hali ya mtoto wetu.
“Kila ukiondoka unamwacha kwa mama Sonono mtoto hana matunzo, leo tu nimemkuta akila matope, kwani nini umekuwa mkatili kiasi hiki mke wangu?”
“Mume wangu mtoto kuchezea matope ni kitu cha kawaida tu.”
“Uchafu unaoufanya umesababisha mtoto aendelee kuteseka chini kama fundi majiko, au unataka azeeke akiwa amekaa?”
“Mwanao mvivu tu wala si mimi.”
“Taarifa zako za kumharibu mtoto kila mtu mtaani anazijua, wanamuonea huruma mtoto, ona miguu ilivyolegea kwa umalaya wako.”
“Sawa mimi malaya, basi nipe talaka yangu.”
“Tatizo si talaka bali kumuonea huruma mtoto.”
“Mi si malaya naomba talaka yangu.”
“Hapa talaka haitoki kuanzia leo mtoto atakaa kwa mama na siku nirudi halafu nisikukute utanitambua.”
Kwa kweli mke wangu nilikuwa nampenda sana, sikumfanya lolote tulilimaliza kwa kuniomba msamaha kwa kuondoka bila kuaga lakini suala ya kutoka nje ya ndoa alilipinga kwa nguvu zote huku akiniuliza:
“Lini tulipokutana kimwili ulikuta nimetumika? Mara nyingi mimi ndiye ninayekulazimisha kufanya mapenzi kama ningekuwa si mwaminifu kulikuwa na haja gani ya kulazimisha mapenzi kwako?”
Kwa kweli sikuwa na jibu, kwa upande mwingine nilimuona kama mke wangu yupo sawa kutokana na tangu nimuoe hakuwahi kutoa udhuru kitandani. Tena kwa upande mwingine nilikuwa namuonea huruma kutokana na kazi zangu ambazo hunilazimu kurudi nikiwa nimechoka. Suala la mtoto kumpeleka kwa bibi yake alikubaliana nalo.
***
Maisha yaliendelea huku nikiamini kabisa kuwa mke wangu amejirekebisha, alipokuwa akitaka kutoka nyumbani alikuwa lazima aage ndipo atoke.
Na safari zake nyingi zilikuwa kwenda kumuona mtoto kwa bibi yake. Hilo halikunipa shida, nilijua ni sehemu ya upendo kwa mwanaye.
Miezi minne baada ya tukio lile, hali ya mtoto ilibadilika, akawa anaweza hata kusimama na kunyanyua mguu mmoja. Hali ile ilinifanya niamini kabisa mke wangu hakuwa mwaminifu katika ndoa yetu licha ya kujitetea kwa kuapa kwa miungu yote.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kama kawaida, siku moja nikiwa kazini majira ya saa nane mchana, mke wangu alinipigia simu na kunieleza kuwa ameitwa na mama yake mara moja, nilimkubalia. Jioni niliporudi sikumkuta, sikuwa na wasi, nikaingia ndani na kuoga, baada ya hapo nilijipumzisha sebuleni kwenye kochi kumsubiri mke wangu arudi.
Kwa vile nilikuwa nimechoka, nilipojilaza kidogo usingizi mzito ulinipitia. Nilishtuka usiku na kujiona nimelala muda mrefu, saa ya kwenye simu ilionesha ni tayari saa tatu za usiku. Nilishtuka na kwenda nje kulipokuwa na kiza kinene, nilijaribu kupiga simu ya mke wangu, iliita kwa muda bila kupokelewa na niliporudia, simu haikupatikana tena.
Nilirudia zaidi ya mara tano, nikaamini huenda chaji imekwisha, niliendelea kumsubiri nikiamini yupo njiani na angerudi muda wowote. Mpaka saa tano inaingia, bado alikuwa hajarudi. Wasiwasi ulikuwa mwingi, nikaamua kwenda nyumbani kwao kujua kuna kitu gani kilichomfanya mke wangu mpaka muda ule awe hajarudi.
Kabla ya kwenda, nilijaribu kupiga simu yake lakini bado haikuwa hewani. Niliondoka na kwenda ukweni kwa kukodi gari lililonipeleka mpaka nyumbani kwao. baada ya kuteremka, nilielekea nyumbani kwa wazazi wa mke wangu, sehemu niliyokuwa nimepanga wakati naanza maisha.
Nyumba ilikuwa kimya na taa zote zilikuwa zimezimwa kuonesha walikuwa wamelala, akili ya haraka ilinifanya nifikiri kuwa huenda nimepishana na mke wangu- ambaye ameondoka muda si mrefu na kufanya wazazi wake walale. Nilitaka kugeuza kurudi lakini niliona ni vizuri niulize ikiwezekana nijue kilichomchelewesha mke wangu.
Nilisogea kwenye nyumba na kugonga mlango, baada ya kugonga kwa muda sauti kutoka ndani iliuliza:
“Nani?” ilikuwa sauti ya mama mkwe.
“Mimi mama.”
“Nani... baba Zawadi?” aliifahamu sauti yangu.
“Ndiyo mama.”
Baada ya muda mlango ulifunguliwa na kutoka huku akionesha alikuwa ameshapitiwa na usingizi.
“Karibu baba.”
“Asante mama.”
“Vipi mbona usiku?”
“Nimekuja kumuulizia mwenzangu.”
“Nani, mama Zawadi?”
”Ndiyo mama.”
“Alikuaga anakuja huku?”
“Ndiyo, alinipigia simu akisema umemwita, niliporudi nyumbani sikumkuta, nimemsubiri tangu nimerudi mpaka muda huu sijamuona na kunifanya niingiwe na wasiwasi.”
“Amekuomba ruhusa saa ngapi?”
“Saa nane mchana.”
“Mmh! Sasa atakuwa wapi, simu yake umempigia?”
“Iliita mara moja bila kupokelewa, niliporudia haikupatikana tena.”
“Ulipiga saa ngapi?”
“Majira ya saa tatu usiku.”
“Mmh! Mbona mtoto huyu ana matatizo!”
“Mama hukumwita?” nilimuuliza bibi Zawadi baada ya kuona hakukuwa na mawasiliano na mwanaye.
“Sijamwita,” alinijibu kwa mkato.
“Sasa atakuwa amekwenda wapi?”
“Kwa kweli sijui.”
“Bora simu yake ingekuwa hewani ingekuwa afadhali lakini ndiyo hivyo haipatikani.”
“Mtoto huyu kawaje jamani, hebu baba rudi nyumbani kamuangalie huenda amerudi.”
“Sawa mama.”
“Basi lolote litakalotokea nijulishe.”
“Sawa mama.”
Niliagana na mama mkwe na kurudi nyumbani, njia nzima nilikuwa na maswali mengi juu ya ombi la ruhusa ya mke wangu kuwa ameitwa na mama mkwe. Ilionesha wazi msamaha alioomba mke wangu ulikuwa ni danganya toto. Nilijiuliza tabia ile mke wangu kaitoa wapi? Tangu nilipomfahamu alikuwa msichana mpole, mkimya tena mwenye heshima.
Nilipofika nyumbani sikumkuta mke wangu, niliingia ndani na kukaa kwenye kochi kwa kuhofia kama nitakwenda kulala na kupitiwa na usingizi mzito, labda mke wangu anaweza kurudi muda wowote na mimi kushindwa kumfungulia na kupata sababu ya kulala nje.
Nilirudisha mlango na kuzima taa ya sebuleni, nikakaa kwenye kochi ili kumsubiri mke wangu ambaye sikujua atarudi muda gani. Mpaka muda ule ilikuwa ni saa saba na nusu usiku usiku.
Nilijitahidi kukaa macho ili mke wangu akirudi na kugonga, niweze kumuona. Kuna kipindi nilipitiwa na usingizi niliposhtuka nilitoka mpaka nje kuangalia kama labda nitamuona mke wangu akiwa amerudi na kuniita na kushindwa kumsikia.
Nilizunguka nyumba nzima bila kumuona mke wangu na kurudi tena sebuleni kumsubiri.
Siku ya pili ilinikuta nikiwa bado nipo sebuleni nikimsubiri mke wangu, nikiwa najiandaa kwenda chumbani, mke wangu aliingia akionesha amekunywa pombe kitu ambacho hakuwahi kukifanya katika maisha yake yote niliyomjua na nywele zake zilikuwa timtim.
“Ooh! Mume wangu, habari za asubuhi?”
“Nzuri, habari za wapi?”
“Nilikwenda kwa mama wakati narudi shoga yangu alinipigia simu kuwa kuna harusi ya ndugu yake. Nilijua nitawahi kurudi kumbe sherehe ni sherehe kuja kushtuka muda umekwenda na usafiri ulikuwa wa tabu nikaamua kulala huko huko.”
“Kwa nini hukunipigia simu?”
“Wakati unanipigia simu ilizimika hata kabla sijakujulisha.”
“Na mbona umekunywa pombe, umeanza lini?”
“Mume wangu sherehe ina vishawishi vingi, lakini sikunywa sana.”
Nilijikuta kwa mara nyingine nikishindwa kumhukumu mke wangu, niliamua kumsamehe kwa vile nilikuwa nampenda sana. Ila nilimuomba asiondoke nyumbani bila kuaga pia asiwe anakunywa pombe.
Mke wangu kama kawaida yake aliniomba msamaha na kuniahidi kuwa hataweza kuondoka bila ya kuaga, pia hatarudia tena kunywa pombe.
Nilimsamehe mke wangu kwa vile nilikuwa nampenda sana na sikutaka kumpoteza maishani mwangu kwa kuamini kuwa yeye ni kila kitu kwangu.
Baada ya tukio lile mke wangu alitulia na heshima ya ndoa ikarudi ndani kama kawaida.
Wakati huo mtoto wetu alikuwa amekazana kutembea, kwa kitendo cha mwanangu kutembea niliwashukuru sana majirani. Wiki moja baada ya tukio la mke wangu kulala nje aliniomba tuhame mtaa ule.
“Mume wangu naomba tuhame hapa.”
“Tuhame hapa twende wapi?”
“Sehemu yoyote lakini mbali na hapa.”
“Kodi si itatusumbua?” Nilimwambia kwa kuwa hali yangu ya kiuchumi aliijua.
“Mume wangu unafanya kazi, acha kujilegeza, inatakiwa sasa hivi tuishi maisha ya kwetu wenyewe bila kuwategemea watu,” yalikuwa maneno ya kweli lakini yalitakiwa maandalizi ya muda mrefu hasa nikizingatia kulipa kodi ya miezi sita kwa haraka ulikuwa mtihani mkubwa kwangu.
“Lakini mbona mama alisema hii ni nyumba yako amekupa baada ya kuoana?” Ilibidi nihoji baada ya mke wangu kulazimisha kuhama.
“Kazala, husikii tunavyosimangwa kuhusu hii nyumba, hasa wewe mume wangu maneno yao kwa kweli huwa yananiumiza sana pale wanapokusema vibaya eti nimekuoa badala ya kunioa, hayo ni maneno gani mume wangu?”
“Mmh! Sina jinsi kwa vile ni haraka sana, nipe wiki nijaribu kukopa kazini ili tutafute nyumba.”
“Kuhusu kodi ya kuanzia nitalipa mimi itakayofuata utalipa wewe.”
“Hakuna tatizo,” nilikubaliana naye bila kuhoji fedha ataitoa wapi kwa kuhofia kubadili uamuzi wake.
Siku ya pili nilipokwenda kazini mke wangu alinipigia simu na kunijulisha kuwa amekwisha hamisha kila kitu na kunielekeza nikitoka kazini niende sehemu alipo na siyo pale tena.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilipotoka kazini nilikwenda sehemu aliyonielekeza na kushtuka kukuta amepanga kwenye nyumba ya gharama iliyokuwa ndani ya fensi, kitu kilichonipa wasiwasi na kujiuliza kama kodi aliyolipa mke wangu ikiisha nitaweza kuilipa. Mke wangu alinipokea kwa furaha.
“Karibu mume wangu kwenye makazi mapya.”
“Asante.”
“Mbona kama unashangaa?”
“Nashangaa kwa mambo mawili, kwanza nyumba nzuri sana na pili na wasiwasi kodi yake ni kubwa.”
“Ni kweli kodi ni kubwa lakini ni sehemu nzuri tutakayoishi bila bughuza za watu.”
“Nyumba yote kwa mwezi shilingi ngapi?”
“Laki moja na nusu.”
“Mke wangu laki moja na nusu kwa mwezi umelipa kwa muda gani?”
“Mwaka mzima.”
“Ndiyo shilingi ngapi?”
“Hesabu unajua, zidisha laki na nusu mara kumi na mbili.”
“Sasa mimi nitaweza kulipa fedha zote hizo?”
“Nitakusaidia, kuwa na amani moyoni mwako.”
Sikutaka kuhoji sana fedha zote hizo kazipata wapi, kwani Waswahili wana msemo wao kuwa ukimchunguza sana bata huwezi kumla na ukimchunguza sana mkeo hutaweza kuishi naye. Tuliyaanza maisha ya Uzunguni, sehemu waliyokuwa wakiishi watu wenye uwezo. Kwa kweli maisha ya makazi mapya yalikuwa mazuri sana yenye furaha na amani.
Kwa muda mfupi, afya yangu ilirudi katika hali ya kawaida baada ya kuteseka kwa muda mrefu kutokana na vituko vya mke wangu. Kutokana na kuonesha mke wangu amejirekebisha tulimchukua mtoto wetu na kuishi naye. Heshima aliyoonesha ilimshtua hata mama yake mzazi.
Maisha yalisonga mbele, mke wangu akashika ujauzito wa pili, kitu kilichozidi kunipa faraja moyoni mwangu. Lakini ilikuwa tofauti kwa upande wa pili, mke wangu hakupenda kubeba ujauzito kwa vile mtoto wetu alikuwa bado mdogo.
“Mke wangu tatizo nini?”
“Huoni Zawadi bado mdogo.”
“Miaka mitatu si michache na mpaka unajifungua atakuwa amesogea sana.”
“Kwa upande wangu nilipanga kuzaa baada ya Zawadi kufikisha miaka mitano.”
“Basi bahati mbaya, itabidi uzae hivyohivyo.”
“Siwezi, lazima niitoe hii mimba.”
“Usiitoe mke wangu, Zawadi tutampeleka kwa bibi yake ili asipate shida.”
“Bado nina hamu ya kumlea mwanangu, kama mtoto utapata tu muda ukifika,” mke wangu bado alishikilia msimamo wake.
“Nakuomba usiitoe hiyo mimba, nipo chini ya miguu yako mke wangu,” nilimbembeleza mke wangu mpaka nikampigia magoti.
“Kwa hilo siwezi kukusikiliza, sihitaji senti tano yako, nitatoa kwa fedha zangu.”
Kwa mara nyingine mke wangu alinizidi nguvu, nikamkubalia kwa shingo upande. Siku ya pili nikiwa kazini, majira ya saa tisa alasiri, mke wangu alinipigia simu kunijulisha kuwa amefanikiwa kuitoa mimba salama. Nilimkubalia lakini upande wa pili moyo uliniuma sana, hata kazi ilinishinda na kwenda sehemu ya peke yangu ambapo nililia sana kumpoteza mwanangu mtarajiwa.
Jioni niliporudi, nilimkuta mke wangu nyumbani, hali yangu ya unyonge ilimshtua mke wangu na kunifuata nilipokuwa nimekaa, akawa ananibembeleza.
“Mume wangu, najua kiasi gani nilivyokuumiza lakini sikuwa na jinsi, nilifanya vile kwa maana kubwa. Kwa sasa ni vigumu kunielewa lakini amini nilichokifanya si kukukomoa bali kumpa nafasi Zawadi. Kumbuka makosa yangu ya awali yalimtesa mwanangu hivyo sasa hivi nina deni la kumlea.”
Kutokana na kumpenda sana mke wangu, nilikubaliana naye. Maisha yalisonga huku akionesha mapenzi mazito kwangu, kitu kilichofuta mawazo ya kutoa ujauzito.
Siku zote kimya kingi kina mshindo mkuu. Mwezi mmoja baada ya kutoa ujauzito, asubuhi moja nilidamka kwenda kazini huku hali yangu kiafya ikiwa si nzuri.
Nilijitahidi kwa kuamini mwanaume si mtu wa kujilegeza. Nilipofika kazini, nilijitahidi kufanya kazi lakini kutokana na kufanya kazi juani, hali yangu ilibadilika na kuwa mbaya hivyo niliruhusiwa kwenda hospitali kupata matibabu.
Nilikwenda hadi hospitali ya wilaya na kupata huduma japo dawa nilikwenda kununua duka la kuuza dawa. Nilibeba dawa zangu na kurudi nyumbani kupumzika. Nilipofika nyumbani, ndani ya geti nilikuta kuna gari ambalo kwangu halikuwa geni sana japo sikukumbuka nililiona wapi.
Baada ya kutafakari, niligundua lile gari ndilo lililomshusha mke wangu, nikashtuka kulikuta nyumbani kwangu na kujiuliza limefuata nini pale. Niliingia ndani na kukuta sebuleni kuna pombe kali juu ya meza na glasi mbili.
Sikujishughulisha navyo, nilielekea chumbani, nilipofika kwenye mlango wa chumbani, nilikuta umefungwa kwa ndani, nikasikia sauti mbili ya mwanamke na mwanaume. Sauti ya mwanamke ilikuwa ya mke wangu ya kiume sikujua ni ya nani. Kwa haraka nilitoka mpaka nje na kuzunguka dirishani na kuchungulia ndani
Nilioyaona ndani nusra mapigo ya moyo yasimame ghafla, kitandani kwangu alikuwepo mke wangu na mwanaume mmoja ambaye hakuwa mgeni sana machoni mwangu japo sikukumbuka niliwahi kumuona wapi wote wakiwa watupu kama walivyozaliwa.
Ilionesha walikuwa wamemaliza kufanya uchafu wao muda si mrefu kwa jinsi walivyokuwa wamejilaza. Nilihisi miguu haina nguvu na kurudi chini bila kujieleza na kukaa kama mzigo. Nikiwa nimekaa chini huku nimeegemea ukutani nikisikia homa ikipanda mara mbili na jasho lilinitoka kama maji na kujiona kama nakufa muda si mrefu.
Nikiwa nimekaa chini niliyasikia mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea ndani.
“Sasa kwa nini uliitoa ile mimba, si uliniahidi utanizalia mtoto,” sauti ya kiume ilisema.
“Ni kweli, lakini damu yako ni kali sana ningeiacha ingeniletea matatizo katika ndoa yangu.”
“Matatizo gani?”
“Nilikuwa na wazo hilo, lakini siku niliyowaona watoto wako wanafanana kama mayai niliogopa. Nilikueleza niwe mke wako wa pili hutaki unafikiri ningejifungua humu ndani japo mume wangu asingejua kitu lakini walimwengu wangemweleza. Hata kutoka kwangu kuna watu wenye roho mbaya walimueleza.
“Bila kuhama kule mambo bado yangekuwa mabaya, japo inabidi kutokana na kukupenda lakini wakati mwingine namuonea huruma mume wangu. Toka tuhamia huku pamekuwa kama kwako unakuja muda wowote unakula na kuvaa tofauti na kwako.
“Ukitaka nikuzalie mtoto nitoe kwa bwana huyu haichukui hata mwezi nitakubebea mtoto.”
“Nimekuelewa mpenzi wangu, lakini japo tunamfanya yule jamaa fala huwa sijiamini sana kuja hapa unafikiri akitufumania tutafanyaje?”
“Hawezi kutufumania.”
“Kwa nini unasema hivyo?”
“Nimekueleza haruhusiwi kurudi nyumbani bila kunijulisha.”
“Kwa nini nisikupangie nyumba nyingine au uwe unatoka na kuwahi kurudi huku nani anakufahamu?”
“John hebu acha kuniudhi, nilikulazimisha tuhamie huku ili tujitawale sasa unataka twende wapi?”
“Si unajua wewe mke wa mtu.”
“Hili umelijua leo, tuna muda gani toka tuhamie hapa?”
“Muda mrefu.”
“Basi naomba wazo la kufumaniwa ondoa.”
“Sasa mpenzi wacha nikukimbie.”
“Mbona haraka.”
“Nilipokuja nilikueleza nini?”
“Ooh! Nilisahau kwa hiyo mpaka kesho kutwa?”
“Ndiyo maana yake.”
“Basi twende tukaoge uwahi.”
Niliwasikia watu wakinyanyuka kwa sauti ya kitanda kupiga kelele. Nikiwa nimekaa chini. Niliamini kama mke wangu akigundua nimemfumania angeomba taraka kutokana na kauli aliyokuwa akiitoa ndani. Nilinyanyua pale chini huku miguu ikiwa haina nguvu na kutoka nje ya geti kwa shida huku nikitetemeka mpaka nje. Nilisogea mbali ya nyumbani ili kusubiri jamaa aondoke ili nipige simu kuwa nipo njiani.
Kutokana na hali yangu kuwa mbaya sikufika mbali sana kizunguzungu na kichefuchefu kilikuwa kikali. Nilisogea kwenye mti wa jirani na nyumbani na kutapika sana na kulala kwenye matapishi kwa vile sikuwa na nguvu ya kujinyanyua. Huwezi kuamini usingizi ulinipitia palepale kwenye matapishi mpaka niliposhtuliwa na wasamalia wema mmoja aliyekuwa akipita njia na kunikuta kwenye hali ile.
“Vipi kaka?” aliniuliza akiwa amesimama pembeni yangu.
“Naumwa,” nilimjibu kwa mkato huku nikijinyanyua kwenye matapishi.
“Unakaa wapi?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Pale,” nilisema huku nikionesha ninapokaa ambako hapakuwa mbali.
“Unaweza kusimama?”
Nilijaribu kunyanyuka kidogo nilikuwa na nguvu, yule msamalia mwema alinisaidia mpaka nyumbani. Bahati nzuri mke wangu alikuwa nje aliponiona alishtuka na kuja mbio.
“Jamani mume wangu, umekuwaje?”
“Naumwa,” nilimjibu kwa sauti ya chini.
Walisaidiana kuniingiza ndani na kunilaza sebuleni, baada ya kunifikisha msamalia mwema aliaga.
“Jamani mi niwakimbie.”
“Asante ndugu yangu,” nilimshukuru.
“Hakuna tatizo Mungu atakusaidia.”
“Asante kaka yangu.”
“Hakuta tatizo.”
Yule mtu aliondoka na kuniacha na mke wangu ambaye alionesha kushtushwa na hali yangu.
“Mume wangu vipi?” aliuliza huku akitokwa na machozi.
“Naumwa?” nilimjibu huku moyo wangu ukiniuma mpaka machozi yalinitoka kitu kilichomshtua mke wangu na kuzidisha kilio.
“Maskini mume wangu, unaumwa nini baba Zawadi?”
“Malaria.”
Alinichukua hadi bafuni na kunivua nguo zote kisha alinimwagia maji na kunisaidia kurudi ndani. Alinitengenezea uji haraka na kuninywesha, kila kitendo cha upendo alichonifanyia mke wangu kiliuumiza moyo wangu baada ya kubaini unafiki.
Lakini mke wangu ugonjwa wangu ulimgusa sana, muda wote alikuwa karibu yangu mpaka nilipopitiwa na usingizi. Nilipoamka nilimkuta pembeni yangu mkono shavuni.
“Mume wangu,” aliniita kwa sauti ya upole.
“Naam.”
“Poleee.”
“Asante.”
“Inaendeleaje kwa sasa?”
“Sijambo kidogo.”
“Nikutayarishie chakula gani?”
“Sijisikii kula,” pamoja na huruma yake ya mamba sikuipenda zaidi ya kuona unafiki.
“Mume wangu kumbuka umemeza dawa kali, unatakiwa kula ili dawa zifanye kazi.”
“Nitakula baadaye.”
“Hapana kuna ndizi za nyama nimekuandalia, naomba ule kidogo.”
“Hapana sijisikii kula.”
“Mume wangu.”
“Naam.”
“Mimi nani wako?”
“Mke wangu.”
“Unataka nani akubembeleze ili umsikie?”
“Wewe.”
“Kwa nini hutaki kunisikia?”
“Si nimekueleza nitakula baadaye.”
“Ni wazi huna mapenzi na mimi hata kunisamehe kwako kulikuwa kwa uongo.”
“Jamani mi si naumwa?”
“Kuumwa gani, ni wazi najilazimisha kwako huna mapenzi nami.”
Nilishangaa aliyokuwa akizungumza mke wangu kitu ambacho hakikuwepo zaidi ya mimi kutojisikia kula.
Niliamini kama nitaendelea kukataa naweza kuzalisha mapya, nilikubali kula kitu kilichomfurahisha mke wangu.
Baada ya kula nilijitahidi kulala lakini usingizi uligoma kunichukua, kila nilipofumba macho niliyaona matukio yote yakijirudia toka la mwanangu kuchelewa kutembea na siku niliporudi ghafla na kumkuta mwanangu akiwa katika mazingira mabaya.
Pia nilipomshuhudia mke wangu akiteremka kwenye gari na pia siku aliyorudi siku ya pili na kunidanganya kuwa alikuwa kwenye sherehe ya harusi kumbe alikwenda kulala na mwanaume.
Na la siku ile nililoshuhudia kwa macho yangu akiwa na mwanaume kama walivyozaliwa katika kitanda changu na kuonesha walikuwa wameshafanya uchafu wao.
Pia kusikia katoa mimba kwa kusingizio cha kumlea mtoto wetu Zawadi kumbe haikuwa mimba yangu, ilikuwa ya yule mwanaume aliyempangia nyumba.
Kila yalivyojirudia akilini mwangu, moyo uliniuma sana na kujikuta nalia peke yangu kitandani nikiwa nimejifunika shuka ili mke wangu asijue. Niliwaza kuachana naye lakini moyo ulikataa kwa kuamini sitampata mwanamke mzuri kama yule.
Niliamua kufa kizungu na tai shingoni, niliificha siri ile moyoni mwangu kwa kuamini kama ningeisema basi ningeachana naye kwa mazingira niliyoyaona na mazungumzo niliyosikia. Kufuatia kutopenda kuwepo nyumbani kutokana na kuumia kila nilipomuona mke wangu, niliamua kwenda kazini siku ya tatu japo sikuwa nimepona vizuri.
Baada ya tukio lile, lilizidi kunitesa kila alipokuwa kazini, siku ambayo nilijua mume mwenzangu atakuja nyumbani moyo ulinilipuka kwa kujua muda ule nilikuwa nasalitiwa. Kila nilipokuwa peke yangu nilijikuta nashindwa kufanya kazi na kuhama kimawazo na kuiona dunia nzima nimeibeba kichwani mwangu.
Kutokana na kuwa na wasiwasi wa moyo juu ya vitendo vya mke wangu, hali yangu ilianza kubadilika nilikuwa nikipungua mwili kila kukicha, suruali zangu zote niliongeza matundu ya mkanda matatu kurudi nyuma ili suruali ikae kiunoni. Wa kwanza kunigundua hali ile alikuwa mke wangu ambaye alitaka kujua nina tatizo gani.
“Mume wangu mbona upo hivi, una tatizo gani?”
“Nipo sawa,” nilijibu kwa mkato.
“Hapana mume wangu, kuna kitu kinakusumbua.”
“Mbona mimi nipo sawa.”
“Si kweli, toka ulipougua hujarudi katika hali yako ya kawaida, pia hata ule uchangamfu wa ndani umepotea. Kama bado unaumwa turudi hospitali tujue una tatizo gani?”
“Hapana nipo sawa,” niliendelea kumkatalia mke wangu.
Nilimkatalia kwa kuamini chanzo ni yeye, hata kama ningemwambia ningeongeza msumari wa moto kwenye kidonda kuwa nimemuona akifanya mapenzi na mwanaume mwingine kwenye kitanda changu, lazima angeomba talaka kutokana na kunipa masharti kuwa nikirudi nyumbani nimpigie simu, japo nilimpigia zaidi ya mara kumi bila kupokelewa.
Pia niliyafuatilia maneno yake aliyomhakikishia yule mwanaume kuwa siwezi kurudi nyumbani kwa vile alinieleza nirudi kwangu kwa taarifa. Niliamini kama ningemueleza ningekuwa nimevunja masharti ya kurudi nyumbani bila taarifa japo simu haikupokelewa.
KAMA angeamua kuniacha, kwangu lingekuwa pigo kubwa kutengana na mke wangu ambaye pamoja na matatizo yote bado alikuwa mtu muhimu sana katika maisha yangu.
“Au bado una yaleyale?” mke wangu aliniuliza kwa sauti ya unyonge.
“Yapi hayo?” Nilimuuliza kwa kuhofia labda ameshtukia.
“Si kuhusu mgogoro wetu kuwa miye natembea nje ya ndoa?”
“Walaa yote mbona yalishaisha.”
“Ndiyo maana nikaja kupanga huku tuishi kwa raha mustarehe, mume wangu tangu tuhamie huku nimewahi kuondoka bila ruhusa yako?”
“Hapana.”
“Au nimeishafanya jambo lolote baya?”
“Hapana.”
“Au lile la kutoa mimba bado linakutesa?
“Walaa.”
“Sasa nini mume wangu?”
“Nina wasiwasi malaria bado haijaisha,” ilibidi nidanganye ili kumfanya mke wangu aachane na mimi kwa vile alikuwa kero mbele yangu.
“Basi mpenzi naomba ukaangalie afya yako kwa kweli hali yako ilivyo hata mimi sina raha,” mke wangu alisema kwa sauti ya huruma.
“Nina imani nitakuwa katika hali ya kawaida muda si mrefu.”
“Fanya hivyo mume wangu.”
Maneno ya mke wangu bila kumfumania nisingekubali kama anaihujumu ndoa yetu, alikuwa na maneno matamu yenye kumfanya maskini kujiona tajiri na asiye na nguvu kujiona anaweza kuibeba dunia nzima peke yake.
Nilikubaliana naye ili aondoke karibu yangu lakini nilipokuwa kazini moyo wangu ulikosa raha na kujuta siku niliyokuwa nikiumwa na kurudi nyumbani na kuyakuta yale niliyoyakuta.
Heri ningeendelea kuamini kuwa naibiwa bila kuwa na uhakika kama siku ile nilivyoshuhudia kwa macho yangu.
Kila nilipokuwa peke yangu tukio la kumfumania mke wangu lilijirudia na kuwa mateso mazito moyoni mwangu.
Kila kukicha mwili wangu ulikuwa ukipoteza ubora wake na kila aliyekuwa akinijua aliniuliza nimekumbwa na kitu gani, hata bosi wangu ambaye alifikia hatua ya kunibembeleza ili nimweleze ninasumbuliwa na nini ili aweze kunisaidia hata kwa uwezo wa kifedha lakini sikumwambia.
Moyoni niliapa kufa na siri yangu kwa kutomwambia mtu yeyote tukio lile la aibu.
Hali yangu ya kiafya ilibadilika na mwili kupungua uzito kutokana na mawazo, chakula nilikula lakini sikusikia ladha yake, kuna kipindi nililaani kuwa maskini kwa kuamini kama ningekuwa na uwezo mke wangu asingechukuliwa na mwenye fedha.
Siku moja rafiki yangu wa karibu Simon alinifuata baada ya kunikuta nikiwa nimejisahau huku machozi yakinitoka.
“Kazala,” aliita kwa sauti.
“Ee..eeh?” Nilishtuka kama niliyekuwa usingizini.
“Kazala una tatizo gani rafiki yangu?” Aliniuliza akiwa amenikazia macho.
“Sina tatizo,” nilimjibu huku nikifuta machozi kwa kiganja.
“Hapana Kazala, una tatizo zito lakini hutaki kulisema.”
“Nipo sawa rafiki yangu,” nilikataa kwa kuamini kusema linalonisumbua nitakuwa nimejivua nguo hadharani.
“Kalaza unajiona ulivyo?”
“Kwani vipi?” nilijifanya kushtuka japokuwa ukweli niliujua.
“Haupo sawa, usiponieleza mimi swahiba wako utamueleza nani? Kumbuka mimi huku ndiye ndugu yako wa karibu.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/-
Ingawa tangu mlipohamia Uzunguni hutaki nifike kwako kwa kusingizio cha mkeo na kusahau ukifa sisi ndiyo tutakaokuzika.”
Kauli ya Simon ilikuwa na ukweli kwani ndiye aliyekuwa mtu wangu wa karibu kwa kuelezana siri zetu za ndani.
Lakini siri ya mke wangu sikuwahi kumweleza hata siku moja ingawaje ilikuwa ikifahamika mtaani lakini hakukuwa na mfanyakazi mwenzangu aliyekuwa akijua kilichokuwa kikiendelea ndani ya nyumba yangu.
Pia, mke wangu baada ya kuhamia makao mapya alipiga marufuku marafiki zangu wote akiwemo Simon asifike kwetu, nami kutokana na mapenzi mazito nilimkubalia.
“Simon nipo sawa,” bado niliendelea kufa na siri yangu moyoni.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment