Simulizi : Mapenzi Yamenifanya Niwe Muuaji
Sehemu Ya Pili (2)
ILIPOISHIA
“Simon nipo sawa,” bado niliendelea kufa na siri yangu moyoni.
“Lakini sipo tayari kukuona ukipotea kwa vile unanihusu Kazala.”
Yalikuwa maneno makali yaliyonifanya mwili wangu utetemeke na jasho kunitoka.
ENDELEA...
Kauli ile ilikuwa kama mkuki moyoni mwangu, nilijikuta midomo na koo vikinikauka ghafla na kukosa la kusema, nikajiona kama mtu niliyekuwa nikitembea uchi siku zote na kujiona nimevaa kumbe watu wananiona sina nguo. Moyo uliniuma sana na kujiona kiumbe niliye na bahati mbaya.
Nikiwa nimeinama chini kama mwari machozi yakinitoka, Simon alinishika begani na kuniita jina langu.
“Kazala.”
Sikuitikia kwani midomo ilikuwa kama ina nta, kila nilipojaribu kuifungua ili niitikie iligoma kufunguka. Nilinyanyua uso na kumtazama Simon aliyekuwa akinitazama kwa jicho la huruma huku machozi yakinitoka.
“Kazala,” aliniita tena.
“Na.na..am,” niliitika.
“Pole sana, najua kiasi gani mapenzi yanavyotesa.”
“Ninyi mmejuaje?” nilijikakamua na kumuuliza swali ambalo niliamini ni siri yangu.
“Mbona siri ipo wazi, taarifa hizi zilinifikia muda mrefu toka matatizo ya mwanao kuchelewa kutembea. Pale mtaani kwenu kila nilipokuja kukutembelea nilielezwa tabia chafu za mkeo lakini nilishindwa nianzie wapi kukueleza kutokana na jinsi unavyompenda mkeo.
“Kwa kweli nilihofia kuitenganisha nyumba yako kutokana na wewe kumuamini sana mkeo. Huwezi kuamini kuna mtu mmoja wa nyumba mliyokuwa mnakaa zamani, kila nilipokuja na kuondoka alinifuata njiani na kunieleza unavyopelekwa na mkeo kwa tabia zake chafu na kuniomba nikueleze ili umdhibiti mkeo.
Lakini ningeanzia wapi kukueleza unielewe? Bado kwangu ulikuwa mtihani mkubwa. Baada ya ninyi kuhama nilikutana naye tena yule aliyekuwa akinipa taarifa za mkeo kuwa nyumba uliyohamia umepangiwa na mwanaume mwenzio, bwana wa mkeo.
“Kwa kweli habari zile ziliniumiza sana lakini vilevile sikuweza kukueleza chochote baada ya mkeo kukukataza usitembelewe na rafiki zako nikiwemo mimi mtu wako wa karibu. La kunikataza nisije kwako halikuniumiza kwa vile hata nilipoacha kuja kwako hakuna kilichopungua kwangu.
“Hali yako ya sasa iliwachanganya sana watu wengi, najua uliulizwa na kila mtu akiwemo bosi lakini hakuna hata mmoja uliyemueleza tatizo lako. Juzi kuna kitu nilisikia kwamba sijui mkeo katoa mimba ya mwanaume wa nje na watu kusema huenda imekuchanganya sana.
“Japokuwa nilikuwa najua kila kitu lakini nilitaka kauli toka kwako kwa kujitahidi kukubembeleza nijue tatizo lako kwa kauli yako mwenyewe lakini umekuwa ukificha ukweli wakati unazidi kuteketea. Lakini hali yako kila kukicha imekuwa ikizorota huku ukiwa mtu wa kuhama kimawazo kila dakika, unajisahau kama upo kazini.
Wengi wanakuonea huruma japokuwa matatizo yako wewe unajua ni siri yako, kutokana na kufanya siri wenzako waliamua kukuacha waone mwisho wako, wengi wanakuona mjinga kuendeshwa na mwanamke. Hebu naomba unieleze kila kitu usinifiche mimi rafiki yako. Kwa nini umefikia hatua hii ikiwa kila kitu cha mke wako unakijua?”
“Simon, sijui hata nikuambie nini, kwa kweli vitendo vya mke wangu vinaniumiza na kunitesa sana.
Nilimuamini sana lakini aliyonifanyia nashindwa cha kufanya. Niliona aibu kukueleza mwanzo kwa kuogopa aibu hii, lakini kumbe natembea uchi nikiamini nimevaa nguo,” niliinama kwa uchungu huku machozi na kamasi zikinitoka.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Moyo uliniuma na kujiona kwa hali ile sikuwa na faida ya kuendelea kuishi, niliona heri nife kuliko aibu ile ambayo nilijiuliza kazini pale watanielewaje. Baada ya kuwaza na kukosa jibu, nilimuuliza Simon anaweza kunisaidia nini.
“Simon ndugu yangu hapa nilipo najiona kiumbe nisiye na faida duniani.”
“Kwa nini?”
“Hebu nieleze nitaficha wapi sura yangu ikiwa kila mtu anaijua siri yangu, kupungua kwangu si kwa sababu ya yote uliyosema ni kitu kingine kabisa heri nife.”
“Ufe kwa ajili ya mwanamke?”
“Ndiyo Simon, jambo alilonifanyia kwa kweli limeniumiza sana sana.”
“Kitu gani tena rafiki yangu?”
Kwa vile kila kitu changu kilikuwa wazi niliamua kumueleza ukweli nilivyomfumania mke wangu na mwanaume ndani ndipo aliponiuliza huku ameshika mdomo kwa mshtuko.
“Ha! Halafu ukafanyaje, haki ya nani ningekuwa mimi, sasa hivi ningekuwa nasubiri hukumu ya kunyongwa. Ndani ya nyumba yangu tena kitandani kwangu dharau gani hiyo Kazala?” Simon aliniuliza macho yamemtoka pima.
NILIMUELEZA nilivyoondoka na homa yangu na niliyoyakuta nyumbani na jinsi nilivyoshindwa kuingia ndani na kuondoka na kuzidiwa na kuanguka njiani na kulala kwenye matapishi.
“Kazala...Kazala...Kazala huo ni uanaume gani? Unamuacha mgoni wako ndani chumbani kwako, tena kitandani kwako?
“Hata kama nyumba amepanga bado pale ni kwako. Kibaya umeondoka unaumwa unataka kufia njiani, rafiki yangu hayo ni mateso gani anayokutesa huyo mkeo?”
“Ningefanyaje na mke wangu alinikataza nisirudi nyumbani mpaka niwe nimemtaarifu? Kama ningerudi na kufumania lazima ningekuwa nimevunja makubaliano yetu lazima angedai talaka yake.”
“Kazala umeoa au umeolewa?”
“Nimeoa.”
“Kwa nini mkeo akupande kichwani na kukupangia atakavyo?” Simon alisema kwa uchungu.
“Siyo kunipangia ni makubaliano yetu,” nilijikuta nisema huku nikimtetea mke wangu pamoja na yote aliyonifanyia.
“Acha ujinga, mwenye amri ndani ya nyumba ni mwanaume, umeona sababu ya kupangiwa kurudi nyumbani ili ajiandae usifumanie. Umerudi mara moja na kukuta yale, hebu jiulize tangu mhamie hapo ni mara ngapi yule mwanaume amefika kama kwake na kufanya uchafu wake?”
“Nashangaa sasa hivi sijui amekuwaje, lakini siku zote mke wangu alikuwa mtu mwenye heshima, hata sijui amebadilika vipi?” bado niliendelea kumtetea mke wangu.
“Kazala mkeo si mtulivu tangu mwanzo, sema ulikuwa hujui kwa vile jambo usilolijua ni sawa na usiku wa kiza. Lakini hafai kuwa mke wa mtu. ”
“Kwa hiyo unanishauri nini kwa hili?”
“Hapa hakuna chochote cha kufanya kama umeyajua yote mabaya ya mkeo na mengine kuyashuhudia kwa macho yako unasubiri nini, unataka akuue?”
“Unanishauri nifanye nini?”
“Yule mwanamke hakufai achana naye ujipange upya, bila ya hivyo atakuua kwa kihoro. Hebu jiangalie, umeshuhudia uchafu wa mkeo mara moja tu, umekuwa hivi kama mgonjwa wa kifua kikuu.
“ Tatizo ameshakujua kwamba wewe ni nyoka wa plastiki huumi, ipo siku atakuteremsha kitandani ili alale na mwanaume wake.”
“Wee atawahi?” Nilijikakamua mwanaume.
“Utafanya nini?”
“Nitaua mtu.”
“Hukuua mtu ulipofumania watu wakiwa kitandani hawana kitu milini mwao, utaweza kusema kitu mbele ya mwanaume mwenzako aliyewapangia nyumba?”
“Lakini nilimsikia akisema hata yeye hapendi kuja pale nyumbani ila mke wangu ndiye anayemlazimisha,” najua kwa majibu yangu msomaji utacheka na kuniona miye ni zuzu, nioneeni huruma mwenzenu kweli nilikamatika, kupenda kubaya nilikuwa zuzu kwisha kazi.
“Kazala majibu gani mbona kupenda kumekugeuza zuzu, au umeinamishwa wewe?”
“Sijainamishwa,” nilikataa klatakata neno la kuinamishwa na mke wangu zaidi ya kumpenda kwa mapenzi ya dhati tu.
“Basi ndugu yangu kwa usalama wako achana na yule mwanamke kabla hajakuacha, la sivyo muda si mrefu utakufa au utakuwa nwendawazimu.”
“Kwa kweli kuachana na mke wangu siwezi labda unipe njia nyingine ya kumtuliza.”
“Nitamtuliza vipi?”
“Kwa vyovyote vile hata kwenda kumueleza yule jamaa aachane na mke wangu.”
“BOSI nilikuwa naomba mkopo wa kulipia nyumba ili nihame ninapokaa, nina imani kila kitu unajua.”
“Najua, lakini hukutaka kuniambia.”
“Tusameheane mkuu wangu si unajua kulemewa ni kubaya.”
“Najua, kwa hiyo hii itakuwa tiba ya matatizo yako?”
“Nina imani nipo katika mkakati huo kuhakikisha ninadhibiti kila sehemu.”
“Mmh! Sawa, unataka kiasi gani?”
“Laki mbili na arobaini tu.”
Baada ya kusema maneno hayo, bosi aliinama na kuandika kwenye kikaratasi na kunieleza nikipeleke idara ya uhasibu.
“Kampe mhasibu.”
“Asante bosi,” nilikipokea na kushukuru.
“Kawaida tu, chumba umeishapata?”
“Simon alinieleza nikipata mkopo kuna sehemu anaijua ina vyumba atanipeleka.”
“Unataka uhamie lini?”
“Ikiwezekana hata leo.”
“Basi una nafasi ya kuondoka kwenda kulipia kodi ikiwezekana leo hii uitumie kwa ajili ya kuhama kabisa.”
“Nashukuru sana bosi.”
Nilitoka hadi uhasibu na kumpa kikaratasi mhasibu aliyekisoma kisha alivuta droo ya fedha na kuhesabu laki mbili na arobaini na kunipa. Baada ya kuipata zile fedha niliamini kabisa kila kitu kitakwenda kama nilivyokipanga. Nilijishangaa kujiona nimekuwa na nguvu za ajabu hata hali yangu ya uchangamfu ilirudi kama zamani, kitu kilichowashangaza hata watu wengine walioniona muda ule.
Wa kwanza kunifikia alikuwa Simon na kuniuliza:
“Vipi mwenzangu?”
“Aisee mambo yamekwenda kama tulivyoyapanga jana, huwezi kuamini kila ulichokisema kimekwenda vilevile.” Nilimweleza huku nikionesha uso wa furaha.
“Mkopo umepata?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ndiyo, yaani bosi nilipomuomba hakuniuliza kitu chochote zaidi ya kuniandikia karatasi kwenda kuchukua uhasibu.”
“Na nyumbani?”
Nilimueleza yote niliyokubaliana na mke wangu kitu kilichomshtua.
“Yaani mkeo kakubali kirahisi tu.”
“Hata mimi nimeshangaa japokuwa mwanzo alitaka kupinga lakini kauli ya kiume ilimfanya akubaliane na matakwa yangu.”
“Ingawaje kazi ni nzito, lakini mwanzo unaonekana kuwa ni mzuri, vipi umemtaarifu kama mnahama?”
“Nimtaarifu ili iweje, yeye alipohamia kule alinitaarifu?” Nilimjibu Simon kwa kujiamini.
”Kwa hiyo?”
“Bosi katoa ruhusa ya kwenda kulipia na kuhamia leo.”
“Sasa mimi nitatokaje?”
“Nimekuombea ruhusa kabisa.”
Niliondoka na Simon hadi sehemu iliyokuwa na hicho chumba na sebule, kwa kweli kilikuwa katika hali nzuri sana. Nililipia miezi kumi ili nibakize na fedha ya kubebea mizigo.
Baada ya kutoka kulipia chumba, tulipita kwenye magari ya mizigo na kukodi gari hadi nyumbani. Nilipofika nilimkuta mke wangu akifua nguo, aliponiona naingia nimo ndani ya gari alishtuka sana.
“Vipi mume wangu?”
“Leo tunahama.”
“Na hapa?”
“Tunamuachia mwenyewe.”
“Mwenyewe nani?”
“Mke wangu huu si muda wa maswali, tupakie mizigo tuhamie makazi mapya.”
“Mume wangu mbona kodi yetu ndiyo ina miezi saba tu.”
“Hiyo iliyobaki atakaa mwenyewe.”
“Mume wangu mwenyewe nani, mwenyewe si sisi?”
“Mke wangu, hebu nyanyuka tuondoke.”
“Mume wangu mbona toka jana sikuelewi, kuna nini?”
“Hebu kwanza tuhame muda si mrefu utanielewa.”
Tulikubaliana kuhama japo kwa shingo upande, tulipakia mizigo nikisaidiana na Simon, baada ya kupakia tuliondoka na kuhamia sehemu nyingine kwenye nyumba yenye wapangaji watatu na sisi kuwa wa nne. Baada ya kupanga vitu huku mke wangu akionekana kulazimishwa, sikuiangalia ile hali.
Kwa vile siku ile nilikuwa na ruhusa, nilipumzika na Simon aliondoka kwenda kwake. Tukiwa tumebaki wawili, mke wangu aliniuliza:
“Sasa ndiyo unafanya nini? Tumetoka kwenye nyumba kubwa tunakuja kwenye vyumba viwili?”
“Ndiyo uwezo wetu.”
“Sasa kwa nini tumehama kule?”
“Ile siyo nyumba yetu.”
“Si tulikuwa tumepanga?”
“Na hapa tumepanga.”
“Kama tumepanga huoni tunapoteza fedha bure, si heri tungerudi kwenye nyumba yetu kuliko kuja huku?”
“Hatujapoteza ila yeye ndiye kapoteza.”
“Mume wangu mbona sikuelewi nani kapoteza?”
“Mke wangu wewe mkubwa, si kila kitu nizungumze, unatakiwa kutumia akili.”
“Una maana ile nyumba nilipangiwa na mwanaume?” mke wangu aliuliza macho yamemtoka pima.
“Wewe ndiyo unasema,” nilijifanya sijui kitu.
“Lakini mume wangu kwa nini unapenda kusikiliza maneno ya watu?”
“Mke wangu wewe si mtoto, tumia akili, utajua sababu gani imetufanya tuhame kule na tusirudi kwenye nyumba yako.”
“Najua tu watu wameshaanza kupenyeza umbeya, nina imani nyumba hii muda si mrefu itanishinda.”
“Haiwezi kukushinda kama utanisikiliza.”
“Nikusikilize nini, kila siku unasikiliza maneno ya nje.”
“Kwani uongo?”
“Uongo nini?” mke wangu alishtuka.
“Yote yaliyotokea siku za nyuma,” nilimueleza ya nyuma sikutaka kumueleza niliyoyashuhudia mwenyewe yaliyosababisha nitake kutoka roho.
“Basi mume wangu, lakini kumbuka kusikiliza maneno ya watu tutaachana tukiwa tunapendana.”
“Unanipenda?” nilimuuliza swali ambalo naamini hata wewe utaona la kijinga. Nilimuuliza kwa makusudi pamoja na kunifanyia yote bado mke wangu niliamini ninampenda na nilikuwa nina imani hata yeye ananipenda.
“Nakupenda sana mume wangu.”
“Kweli?”
“Tena sana, hebu nieleze toka tuhame uswahilini nimekukosea kitu gani kibaya.”
“Hujawahi ila nakuomba iheshimu ndoa yetu,” niliamua kufunika kombe ili mwanaharamu apite kwa kuamini mke wangu hakuwa anajua lolote juu yake.
“Nimekuelewa mume wangu.”
Tulianza maisha mapya kwenye makazi mapya, kama ilivyokuwa kawaida ya mke wangu, muda wote alikuwa mpole bila kuonesha mabadiliko yoyote mabaya. Kila nilipokuwa kazini alipoomba ruhusa ya kwenda kwa mama yake nilimkatalia na yeye hakulalamika, japokuwa aliona kama nimemnyima uhuru. Nilimueleza yeye ndiye wa kunishawishi kumpa uhuru bila hivyo nilimhakikishia safari yake kubwa ni dukani na sokoni tu.
Mke wangu alionekana kunielewa kwa kufuata yote niliyomueleza, ili kupata uhakika kuna siku nilimjaribu kwa kutoroka kazini na kurudi nyumbani bila taarifa na kumkuta
mke wangu kapoa kama maji ya mtungi
Hali ile ilizidi kunijengea imani kuwa mke wangu amebadilika, nami kidogokidogo mwili wangu ulirudi na kuonekana mtu mbele ya watu.
Japokuwa si tabia nzuri mume kumchunguza mke lakini sikuwa na jinsi kufanya hivyo siku mojamoja, niliendelea kumdodosa Simon juu ya tabia ya shemeji yake, jibu lake lilikuwa hata yeye hajasikia lolote baya la kumhusu.
Hata mtu aliyekuwa akimpa taarifa zile za awali, alimweleza kuwa sasa hivi mke wangu ametulia, nilimshukuru rafiki yangu Simon kwa mpango wake uliofanikiwa kumrudisha mke wangu kwenye mstari.
Kweli moyo ukipata furaha hata kama huna kitu, maisha utayaona mazuri. Nilipendeza na kuanza kutokwa na kitambi kwa mbali, kila mmoja aliyeniona alinishangaa kwa jinsi nilivyokuwa na mabadiliko ya ghafla.
Niligundua kuwa kero za moyo ni mateso mazito, yanapoutikisa mwili na binadamu ukiyapata lazima utakwisha na watu watakucheka.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Siku zilikatika huku nikiyafurahia maisha mapya na mke wangu, kingine kilichonipa faraja ni kusamehewa deni langu na kampuni kutokana na ufanisi wangu mzuri wa kazini uliokuwa umelenga kurudisha uwezo wangu wa zamani wa kujituma.
Waswahili wanasema la kuvunda halina ubani, miezi sita baada ya kubadili makazi yaliyotawaliwa na utulivu na amani, siku moja baada ya kumaliza kazi, nilirudi nyumbani saa moja na nusu usiku kama kawaida. Nilipofika nilikuta mlango wa nyumba umefungwa, nilikwenda kuuliza kwa jirani wa chumba cha pili, alinieleza kuwa mke wangu ameondoka katika gari ambalo nilivyoelezwa tu lilivyo, moyo wangu ukapasuka pah!
Lilikuwa ni gari lilelile la mwanaume aliyekuwa akimzuzua mke wangu siku zote kabla mambo hayajatulia. Kwa kweli nilichanganyikiwa na kubaki nimesimama kama zuzu, kitu kilichomfanya hata jirani yangu kunishangaa.
“Kwani vipi shem mbona hivyo, kwani kuna nini?”
“Hataa,” nilikataa ilhali mikono yangu ikiwa kiunoni na kuonekana kugeuza kichwa changu kutaacha macho yaangaze huku na kule.
“Hapana shem, nilipokuelekeza kuhusu gari lililomchukua mkeo umeshtuka na kupoteza hali yako ya kawaida na kutawaliwa na hali ya kutaharuki ghafla, kwani lile gari lina nini?”
“Ameondoka saa ngapi?”
“Saa tano asubuhi.”
“Alikueleza anakwenda wapi?” Nilimuuliza huku nikiwa na shauku ya kujua.
“Hakuniambia ila iliniletea ufunguo na kuniambia ukirudi nikupe.”
“Na mtoto?”
“Ameondoka naye.”
“Alibeba nini?”
“Alikuwa na mkoba wa kawaida tu.”
“Mmh!” Niliguna huku nikiinamisha kichwa kusikitika.
“Kwani kuna nini shemeji, mligombana?”
“Jirani si ungesikia.”
“Sasa mbona umeshtuka, msubiri akirudi umuulize, hakukuaga?”
“Asante shemeji.” Niliachana na mke wa mpangaji mwenzangu na kuelekea ndani kwangu.
Nilipofika nilijitupa kwenye kochi na kutazama juu huku nikijiuliza yule bwana kampeleka wapi mke wangu.
Moyo mwingine uliniambia huenda kapewa lifti tu hakuna kitu kibaya kitakachoendelea, pia nikahisi labda atakuwa amekwenda kwa mama yake.
Nilipanga akirudi nisimuulize kitu chochote kuhusiana na kupanda kwenye gari la mwanaume ambaye ilionekana haja yake kubwa ni kuivunja nyumba yangu wakati na yeye ana familia yake.
Kupanda gari lile halikuwa tatizo, bali kuondoka bila ya kuaga kama tulivyokubaliana, kwa upande mwingine sikumlaumu sana mke wangu kutokana na msimamo wangu wa kumkatalia kutoka hata alipoomba ruhusa.
Kingine kilichonishangaza ni kuiacha nyumba bila ya kuifanyia usafi, vyombo tulivyovitumia kwa chakula jana yake vilikuwa havijaoshwa, nyumba ilikuwa haijasafishwa kabisa, chumbani kitanda kilikuwa hakijatandikwa, shuka zilikuwa zimekaa ovyo pia, hata chakula kilikuwa hakijapikwa.
Nilijiuliza kitu gani kitakuwa kimempata mke wangu hadi kumfanya atoke haraka na kushindwa kufanya majukumu muhimu ya ndani.
Nilijikuta nikiingiwa na wasiwasi na kuamua kumpigia simu mke wangu, nilizidi kuchanganyikiwa baada ya simu ya mke wangu kutokuwepo hewani.
Nilirudia zaidi ya mara kumi kuipiga simu hiyo lakini jibu lilikuwa ni lilelile, simu haikuwa hewani.
Nilijiuliza tatizo gani lililomkuta mke wangu kiasi cha kushindwa kupatikana kupitia simu yake, muda nao ulikuwa umekwenda sana, wazo la kumsubiri na kujipa imani kwamba atarudi muda si mrefu nililiafiki kwa saa moja zaidi.
Ilipotimu saa tatu usiku bila ya kumuona mke wangu, nilijaribu kumpigia tena simu yake, lakini bado haikupatikana.
Nilikata shauri kwenda kwa wazazi wake kutaka kujua kama walikuwa wakijua tatizo lililomkuta mtoto wao kufikia kuondoka nyumbani na simu yake kutokuwa hewani kwa kipindi kirefu.
Nilitoka na kuegesha mlango, sikutaka kuufunga kwa kuhofia labda tungeweza kupishana njiani, nilikodi gari mpaka kwa wakwe zangu, bahati nzuri niliwakuta bado hawajalala. Baada ya kugonga mlango, mama mkwe alinikaribisha kwa vile aliifahamu sauti yangu.
“Karibu baba Zawadi.”
“Asante mama, shikamoo,” nilimwamkia huku nikiingia ndani na kukaa kwenye kochi.
“Marhaba, kwema utokako?”
“Namshukuru Mungu, sijui mwenzangu amefika huku?”
“Mmh! Kwa leo sijamuona,” kauli yake ilinishtua sana lakini nilificha mshtuko wangu.
“Sasa atakuwa amekwenda wapi?” Bila ya kutarajia nilijikuta nikimuuliza swali lisilomhusu mama mkwe.
“Nitajuaje baba, kwani alikuaga anakwenda wapi?”
“Mamaa, yaani nimerudi nyumbani nimekuta ufunguo kwa jirani bila maelezo yoyote.”
“Zawadi yupo wapi?”
“Ameondoka naye.”
“Mmh! Sasa atakuwa amekwenda wapi?”
“Hata mimi nashangaa tena nasikia kaondoka na ile gari ya yule mwanaume wake.”
“Mmh! Unasema kweli?” mama mkwe alionesha kushtuka.
“Kutokana na maelezo ya mtu aliyemuona.”
“Kwa hiyo hukumuona?”
“Sijamuona mama, nimeambiwa.”
“Basi usifikirie moja kwa moja kuwa ameondoka na mwanaume wake wa zamani, kwani ameondoka tangu saa ngapi?”
“Saa tano.”
“Saa tano, sasa atakuwa amekwenda wapi na mtoto? Kwani hali hii imetokea mara ngapi?”
“Ni leo tu mama toka tumalize yale matatizo yetu.”
“Nakuomba rudi nyumbani ukapumzike, akirudi atakueleza alikuwa wapi kama maneno yake hayaeleweki mlete kwangu. Nimechoka na upumbavu wake, hawezi kutuchezea akili kiasi hiki,” mama mkwe naye alionekana kukerwa na kitendo cha mke wangu kuondoka bila kuaga.
“Sawa mama.”
“Nina imani hakufika mbali, angekuwa amekwenda peke yake ningekuwa na wasiwasi, lakini kwa vile ameondoka na mtoto, atawahi kurudi tu, huenda mmepishana amesharudi nyumbani.”
“Nitashukuru mama.”
“Basi baba rudi nyumbani nina imani mpaka muda huu atakuwa amerudi tu.”
“Sawa mama,” nilikubaliana na mama mkwe na kugeuza kurudi nyumbani nikiwa na matumaini ya kumkuta.
Nilikodi gari ili niwahi nyumbani huenda mke wangu amerudi na kutonikuta kumemsababisha kuwa na wasiwasi wa kutaka kujua mimi nipo wapi. Nilikwenda hadi nyumbani na kuingia ndani, nyumba ilikuwa kimya kuonesha hakukuwa na dalili za kuwepo mtu ndani.
Wazo langu lilikuwa labda amerudi na kuingia kulala, nilikwenda chumbani. Chumba kilikuwa kitupu na hali ilikuwa ileile ya chumba kuwa katika hali ya uchafu. Nilibaki nimesimama kwenye mlango wa kuingilia chumbani kwa dakika kadhaa nikiwa siamini kilichokuwa mbele yangu.
Nilijiuliza mke wangu atakuwa wapi? Nilirudi sebuleni na kukaa kwenye kochi nikiwa sijui mke wangu amekwenda wapi. Japokuwa wasiwasi wangu mama mkwe alikuwa akijua kila kitu ila alinificha. Ilikuwa ni mateso juu ya mateso kwani siku ile ilikuwa nimefanya kazi nzito kwa muda mrefu na kuamini ningerudi nyumbani ningepumzika. Lakini tangu nilipofika nilikuwa juujuu kwa ajili ya kumtafuta mke wangu tena bila kula.
Njaa iliyokuwa ikiniuma kama kidonda ilitoweka kutokana na mshikemshike wa kuzunguka kumtafuta mke wangu. Saa ya ukutani ilionesha ni saa sita na nusu usiku bila dalili za kuonekana mke wangu. Bado sikukata tamaa, nilirudia kumpigia simu, hali ilikuwa ileile, simu haikuwa hewani.
Nilijikuta nikiwa na wasiwasi kuhusu mke wangu na kujiuliza kipi kimemsibu hadi muda ule awe hajarudi. Ingekuwa ameondoka peke yake, ningejua amerudia matatizo yake. Lakini alikuwa ameondoka na mwanangu wa pekee Zawadi, nilijiuliza kama kweli ameparama tena na kurudiana na yule mwanaume na huenda ikawa hata Zawadi si mtoto wangu wa kumzaa.
Kwa upande wa Zawadi ningekuwa tayari kufa kama ningeambiwa si mtoto wangu. Zawadi nilifanana naye kila kitu kila, aliyemuona alijua ni mwanangu bila hata ya kumwambia. Nilikaa sebuleni kumsubiri huenda amekwenda kwenye sherehe na kuchelewa kurudi.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilikaa sebuleni mpaka alfajiri ilipoingia bila kumuona mke wangu wala kivuli chake. Nilijiuliza mke wangu atakuwa wapi, kutokana na kulala usingizi wa mang’amung’amu, niliamka asubuhi kichwa kikiwa kizito. Kwa vile niliacha kiporo cha kazi, niliposhtuka nilioga haraka nikitegemea huenda mke wangu akatokea kabla ya kwenda kazini kama alivyofanya siku za nyuma lakini haikuwa hivyo.
Mpaka naondoka sikumuona mke wangu na kumuachia funguo jirani nikiamini huenda jioni nikirudi naweza kumkuta. Nilikwenda hadi kazini nikiwa nimechoka sana, nilificha uchovu wangu na kufanya kazi kwa nguvu japo kila nilipokuwa peke yangu, nilisinzia na kuwafanya wafanyakazi wenzangu kunitania eti nilikesha na shemeji bila kujua msiba mzito uliokuwa moyoni mwangu, baada ya bomu lililotulia kulipuka tena.
Baada ya kazi nilirudi nyumbani nikiwa na matumaini ya kumkuta mke wangu lakini nilipofika nilikuta mlango umefungwa. Nilikwenda kwa mke wa jirani yangu kuulizia huenda alikuja na kuondoka.
“Karibu shemeji,” alinikaribisha aliponiona.
“Asante, vipi hajarudi mke wangu?”
“Sijamuona kwani alikwenda wapi?” lilikuwa swali juu ya swali.
“Hata najua! Mbona huyu mwanamke ananitesa sana, kosa langu nini kila kukicha niwe mimi tu,” nilijikuta nikibwabwaja kwa uchungu bila kujielewa.
“Kwani kuna nini shemeji?”
“Yule mwanamke kila kukicha amekuwa akinifanyia mambo yaliyokosa ubinadamu kabisa.”
“Lakini mbona tumeishi naye vizuri tena mke wako ni mpole na msikivu tatizo nini?”
Nilijikuta nikifunguka mwanaume na kuuanika ubaya wa mke wangu, mke wa jirani alinionea huruma na kusema:
“Mbona haendani na unayosema?”
“Mke wangu ni chui ndani ya ngozi ya kondoo.”
“Pole sana shemeji na mtoto kampeleka wapi?”
“Nitajuaje?”
“Kwani kwao wanasemaje?”
“Nao hawajui lolote.”
“Ungesubiri na leo huenda akarudi usiku huu.”
“Mmh! Sidhani.”
Niliagana na mke wa jirani yangu na kuingia chumbani ambako kulikuwa vululuvululu. Baada ya kuoga nilikwenda kununua soda na mkate ili nitulize njaa. Chakula kilinishinda na kulala na njaa.
Usingizi wangu ulikuwa wa kushtukashtuka kila mara kwa kuamini labda mke wangu angerudi.
Kila niliposhtuka nilitulia na kusikilizia huenda kulikuwa na sauti ya mtu kuniita.
Nilikata shauri kwenda kulala sebuleni kwa kuwa niliona chumbani kama nikilala sitaweza kumsikia mke wangu pindi akirudi.
Niliamua kuhamia sebuleni na kukaa kwenye kochi kumsubiri mke wangu, muda nao ulikuwa umekwenda, ilikuwa saa saba na nusu za usiku na bado niliamini angeweza kurudi.
Mpaka kunakucha hakukuwa na dalili za mke wangu kurudi, hata bila kunawa uso nilikwenda ukweni kuulizia taarifa za mke wangu, nilidhani labda alirudi nyumbani kwetu na kuogopa, akaamua kwenda kwa mama yake.
Nilipofika ukweni niliwakuta ndiyo kwanza wanaamka.
“Vipi baba, mbona asubuhiasubuhi?” mama mkwe aliniuliza baada ya kuniona.
“Mama, mke wangu yupo huku?”
“Ina maana alirudi na kuondoka tena?”
“Hapana, hajarudi kabisa.”
“Toka juzi?”
“Ndiyo mama.”
“Mmh! Mbona mwana huyo ana matatizo, sasa atakuwa amekwenda wapi?”
“Kwani huku hajafika?”
“Sijamuona baba yangu.”
“Basi lazima atakuwa amekwenda kwa mwanaume wake.”
“Jamani, yaani ndiyo kafikia hatua hii?” Mama mkwe alishika kiuno kuonesha naye kachoshwa na taarifa zile.
“Basi mama acha niwahi kazini.”
Niliagana na mama mkwe na kurudi nyumbani ili nijiandae kwa ajili ya kwenda kazini japokuwa nilikuwa katika wakati mgumu baada ya kumkosa mke wangu kwao.
Nilipofika nyumbani nilihisi kichwa kizito, chumba nilikiona kama dunia asiyokuwa na kitu chochote, nimebaki mpeke yangu.
Moyo ulikufa ganzi, nilishindwa kwenda kuoga ili kuwahi kazini kwani muda ulikuwa umekwenda sana.
Nilihisi kama mwili wangu umekosa nguvu, kichwa kilianza kuniuma kwa mawazo na mapigo ya moyo yalianza kwenda kasi.
Nilikaa kwenye kochi kabla sijaanguka, nilijilaza huku nikiwa na maswali mengi juu ya mke wangu kuondoka nyumbani bila ya taarifa.
Nilijiuliza tatizo nini hasa ikiwa kila kitu kilikuwa kikienda vizuri, nilikuwa bado natafuta sababu ya mke wangu kuondoka bila ya kuniaga na kutaka kujua sehemu aliyokwenda.
Nikiwa nimekaa bila ya kuwa na hili wala lile, ghafla niliiona bahasha iliyokuwa imefungwa vizuri na kuwekwa chini ya meza.
Nilijikuta nikipata shauku ya kutaka kujua ile barua ya nani. Nilipoichunguza, niligundua ilikuwa na jina langu, moyo ulinilipuka kwani ule ulikuwa mwandiko wa mke wangu. Nilijikuta nikiingiwa na wasiwasi kwa kuhisi huenda mke wangu alirudi asubuhi ile na kunikosa wakati nimekwenda kumtafuta kwao na kuamua kuondoka na kuacha ujumbe.
Niliichukua ile bahasha na kuifungua ndani, nikakuta karatasi iliyokuwa imeandikwa kwa wino mwekundu.
Nilipoanza kuisoma nilikutana na maneno ambayo almanusura yasimamishe mapigo yangu ya moyo. Barua ile ilinikatisha tamaa na kujikuta kila herufi moja niliyokuwa nikiisoma ndivyo moyo wangu ulivyokuwa ukikamuliwa bila ganzi. Maumivu yake siwezi kuyaeleza kwa maneno bali kuyasikia tu yalikuwa sawa na kung’olewa jino bila ganzi.
Mpaka namaliza kuisoma, machozi yalikuwa yamefunika macho yangu na sehemu ya karatasi ilikuwa umelowa upande kwa machozi.
Barua ilisema hivi:
Kazala, najua utashtuka kupokea ujumbe huu na kukufanya uchanganyikiwe. Najua wewe ni mwanaume na mwanaume ameumbwa kukabiliana na matatizo.
Najua unanipenda na utaendelea kunipenda, lakini kutokana na kushindwa kwenda na wakati na kunigeuza mwanamke wa kizamani wa kukaa ndani kama samani, nimeamua kuishi maisha yangu ya uhuru kama wanawake wengine.
Nimeamua kuondoka, sitaki unitafute hata mama yangu naye sitaki anitafute, nimeamua kuishi maisha niliyoamua kuishi mwenyewe. Nimekuvumilia mengi Kazala lakini huna shukurani, nyumba yetu imekuwa ikiendeshwa na watu wa pembeni kuliko sisi wanandoa.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kazala, umekuwa ukiwasikiliza watu wa pembeni kuliko mimi mkeo, nilikueleza tutaachana tukiwa tunapenda, nina imani kauli yangu imetimia. Najua utajiuliza kuhusu mtoto, Zawadi ni mtoto wako na ataendelea kuwa mtoto wako, nimeamua kuondoka naye ili aendelee kupata malezi mazuri. Akitimiza miaka saba nitamleta kwako ila mimi naomba unisahau kabisa.
Tokea leo ninapoondoka kwako, mwisho wa wiki hii nafunga ndoa ya kidini tena kanisani na kuwa mke wa mtu anayefahamika mbele ya Mungu. Nawe mpenzi wangu wa zamani fanya hivyo, tafuta mwanamke anayeendana na wewe ili ufunge naye ndoa, ukichelewa unaweza kuugua ugonjwa wa akili.
Nakutakia maisha mema wewe na huyo mwanamke utakayemuoa ila nakuonya kitu kimoja, nyumba haiendeshwi na watu wa pembeni, ukifanya hivyo kila utakayemuoa atakukimbia.
Ni mimi mzazi mwenzako, mama Zawadi.
Barua ile ilikuwa pigo mujarabu moyoni mwangu, ilikuwa sawa na kuupasua moyo wangu kwa kisu butu bila ganzi. Akili yangu haikukubaliana na kutaka kuirudia kwa mara ya pili lakini kila nilipotaka kuisoma, machozi yalitanda usoni na kushindwa kufanya hivyo.
Nilinyanyuka na kutembea taratibu hadi chumbani na kurudi sebuleni, kichwa kilikuwa kizito hata la kufanya sikulijua na kuona kazi yote niliyoifanya ilikuwa bure.
Niliyarudia maneno aliyowahi kuniambia mke wangu na kuyaandika katika barua niliyokuwa nimeishikilia kuwa maneno ya nje yatavunja nyumba yetu tukiwa tunapendana.
Nilijikuta nikianza kumlaumu Simon kumuona kuwa ndiye chanzo cha nyumba yangu kuvunjika baada ya kukubali kuufuata ushauri wake ambao mwanzo niliuona kama umenisaidia, kumbe ulikuwa ni bomu lililokuwa likisubiri kupasuka na matokeo yake kuisambaratisha nyumba yangu.
Nilijiuliza nitafanya nini ili kumrudisha mke wangu mikononi mwangu kabla ya mwisho wa wiki haujafika. Nilijiuliza hiyo ndoa itafungwa kanisa gani na itakuwa siku gani kati ya Jumamosi na Jumapili.
Kwangu ulikuwa ni mtihani mkubwa, kwa sababu nilitaka kujua mke wangu ataolewa kanisa gani ili nikaweke pingamizi.
Mawazo yalinizidi kichwani na kukiona kichwa changu kama kinataka kupasuka, ghafla niliona kiza kizito mbele yangu, kwa kifupi sikuwa ninajua kilichokuwa kinaendelea.
Niliposhtuka nilijikuta nikiwa hospitali, pembeni yangu alikuwepo rafiki yangu Simon ambaye alikuwa akizungumza na daktari. Nilimsikia akimuuliza:
“Vipi daktari siyo tatizo kubwa?”
“Si kubwa, ni wazi mgonjwa aliwaza sana hadi kufikia hatua ya mishipa yake kushindwa kufanya kazi yake vizuri.
“Lakini muda si mrefu atarudia katika hali yake ya kawaida, ila atatakiwa kuondokana na tabia ya kuwaza sana.”
“Sawa daktari.”
Simon alipogeuka alishtuka kuniona nakimtazama, hata bila ya kunisemesha nilimuona akigeuka na kumwita daktari:
“Dokta.”
“Unasemaje?”
“Naona mgonjwa ameamka.”
Daktari alikuja kitandani na kunisemesha:
“Pole Kazala.”
“Asante,” nilimjibu kwa sauti ya chini.
“Unaendeleaje?”
“Kichwa kinaniuma kwa mbali.”
“Punguza mawazo ndugu yangu, unaki – over load kichwa na kusababisha maumivu makali.”
“Nimekuelewa daktari,” nilimkubalia lakini niliamini bila ya mke wangu kurudi sitaweza kuepukana na hali hiyo.
“Huna ugonjwa mwingine zaidi ya huo, dawa yake ni kupunguza mawazo na kumeza dawa za maumivu tu.”
Nilidungwa sindano ya maumivu sambamba na ile ya usingizi na kuambiwa niendelee kupumzika mpaka siku ya pili ili nipate muda wa kukifanya kichwa kitulie.
Siku ya pili niliruhusiwa na kuchukuliwa na Simon ambaye alionesha hakwenda kazini kwa ajili ya kunishughulikia.
Tulipotoka tukapitia hotelini na kupata kifungua kinywa, kisha tukaelekea nyumbani. Tulipofika Simon alinitaka nipumzike na yeye kuanza kupanga baadhi ya vitu vilivyokuwa shaghalabaghala, baadaye alikuja kukaa karibu yangu na kuniita:
“Kazala,”
“Naam.”
“Tatizo nini?”
“Shemeji yako ataniua,” nilimjibu huku nikishika kifua kuzuia presha iliyokuwa ikitaka kupanda.
“Tatizo ni nini?”
“Ameamua kunikimbia.”
“Bado hujanieleza tatizo ni nini?”
“Hata sijui, yaani dawa uliyonipa mwenzangu imeharibu kila kitu,” nilianza kumlaumu Simon.
“Acha lawama za kijinga, pale hukuwa na mke ndugu yangu, kama mwanamke anafikia kukuletea mwanaume ndani na kulala naye kwenye kitanda chako bado unalaumu watu, huu si uzoba?”
“Kama ningemuacha afanye anavyotaka wala asingenikimbia.”
“Ningekuwa miye nisingeumia, tena ndiyo kwanza ningeshukuru.”
“Ungeshukuru nini Simon?” nilishangazwa na majibu ya Simon.
“Kuondoka kwa yule mwanamke, kwa kuwa hukuwa na mwanamke ndugu yangu. Kama angekuwa mwanamke mwenye staha zake angeandika barua kama hii? Kazala aliyekuroga amekufa si bure, pamoja na kufanyiwa mambo yote haya bado unamlilia?”
“Ndugu yangu mazoea mabaya, pamoja na yote bado nampenda sana mke wangu.”
“Unampenda! Haya ameshakukimbia kazi kwako sasa.”
“Utanisaidia vipi?” pamoja na Simon kumnanga mke wangu lakini bado nilimuomba ushauri wa kumrudisha mwanamke huyo nyumbani kwangu.
“Kazala tumekuja mjini kutafuta maisha na wala si wanawake, ujinga wako huo utasababisha ufukuzwe kazi. Hakuna mwajiri atakayevumilia matatizo yako ya kifamilia yasiyoisha.
“ Kumbuka wazazi wako wanakutegemea, matokeo yake unaacha kilichotuleta huku unakuwa bwana pendapenda.”
“Nitajitahidi lakini itanichukua muda kumsahau nilimpenda sana mke wangu.”
“Ndugu yangu mazoea mabaya, pamoja na yote bado nampenda sana mke wangu.”
“Unampenda! Haya ameshakukimbia kazi kwako.”
“Utanisaidia vipi?” pamoja na kumnanga mke wangu bado nilimuomba ushauri wa kumrudisha.
“Kazala tumekuja kutafuta maisha si wanawake, ujinga wako huo utasababisha ufukuzwe kazi. Hakuna mwajiri atayekuvumilia kwa matatizo yako ya kifamilia yasiyoisha. Kumbuka wazazi wako wanakutegemea matokeo yake unaacha kilichotuleta huku unakuwa bwana pendapenda.”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nitajitahidi lakini itanichukua muda kumsahau mke wangu, nilimpenda sana.”
Nilikubaliana na Simon niachane na mke wangu ili nifanye kilichonipeleka kule japokuwa nilijua kilikuwa kitu kigumu kwa upande wangu kumuondoa moyoni mke wangu mara moja.
Nilipanga kwa siri Jumamosi au Jumapili nizunguke katika makanisa yote kwa kutumia pikipiki ili nijue ni kanisa gani mke wangu angefunga ndoa nimuwekee pingamizi.
Kwa vile mke wangu alikuwa ni Mkristo wa dhehebu la Romani Katoliki, niliamini lazima ningejua anafunga ndoa kanisa gani.
***
Jumamosi ilipofika nilikodi pikipiki kwa ajili ya kuzunguka makanisa yote ya mjini. Kanisa kubwa lilikuwa katikati ya mji na madogo yalikuwa pembezoni kidogo mwa mji ambayo hayakupungua manne.
Niliamini hata kama ningezunguka kutwa nzima ningeweza kufika kanisa moja baada ya lingine bila ya kuchelewa.
Nilifanya kama nilivyopanga katika dhamira yangu lakini baada ya kuzunguka kwa muda mrefu bila ya kupata mafanikio yoyote, dereva wa pikipiki aliniambia .
“Sikiliza ndugu yangu, tutamaliza mafuta bure kwa nini tusiende kwenye ofisi za makanisa ili tujue kuna ndoa au hakuna na kama ipo itafungwa saa ngapi, hiyo itatusaidia kwenda kwa wakati kuliko kuzunguka na kukufanya upoteze fedha nyingi.”
Wazo lile nilikubaliana nalo na kuamua kwenda kwenye ofisi za kanisa kuulizia kama kulikuwa na ndoa siku ile. Makanisa yote manne yalinieleza kuwa, hakukuwa na ndoa yoyote ila Jumapili yaani kesho yake kulikuwa na ndoa nne ambazo zote zingefungwa kwenye kanisa kuu tu.
Niliamini katika ndoa zile nne lazima mojawapo ingekuwa ya mke wangu kipenzi Suzana au mama Zawadi.
Nilimshukuru dereva wa pikipiki ambaye nilikubaliana naye anifuate nyumbani siku inayofuata na kunipeleka katika kanisa hilo kuu ili nikaweke pingamizi la ndoa ya mke wangu.
Baada ya kurudi nyumbani nilikuwa na mawazo mengi kuhusiana na itakavyokuwa kesho yake, nijiuliza nitakapotoa pingamizi litakubaliwa au nitajiingiza kwenye aibu kwa kuwa ndoa yetu ilifungiwa bomani na ile inafungwa kanisani.
Upande mwingine niliamini nitakuwa na nguvu ya kuvunja ndoa ya mke wangu kwa vile ilikuwa ikitambulika kiserikali na vyeti nilikuwa navyo.
Nilipanga siku hiyo nikienda kuweka pingamizi niende na vyeti vya ndoa ili kutia uzito pale mke wangu atakaponikana.
Siri ile sikutaka kumshirikisha Simon kwa kuhofia kunipa ushauri mbaya ambao ungeharibu mipango yangu yote. Ushauri wa Simon mwanzo niliuamini lakini baada ya kusababisha mke wangu kukimbia, sikumuamini tena na kumuona kuwa ndiye chanzo cha matatizo yangu.
Siku ya pili baada ya kufuatwa na dereva wa pikipiki nilifika kanisani saa tatu asubuhi japokuwa ndoa ilikuwa ikifungwa saa saba mchana.
Nilikaa pale mpaka saa nne na nusu ambapo magari ya maharusi yaliobeba ndugu, jamaa na marafiki yalipoanza kuwasili.
Ndani ya muda mfupi tu, kanisani pakawa na watu wengi na magari kutokana na harusi nne kufungwa, nilisubiri kwa hamu nimuone mke wangu akitaka kufunga ndoa na kuweka pingamizi.
Baada ya muda nilikuwa mmoja kati ya watu waliowahi kuingia ndani na kuketi siti za mbele ya kanisa kusubiri ibada ya ndoa.
Kanisa lilijaa watu wengi sana pamoja na maharusi wote. Kwa vile mabibi harusi walikuwa wamezibwa nyuso zao iliniwia vigumu kumtambua mke wangu ni nani kati ya wale wanne.
Baada ya taratibu zote kufanyika ndoa zilianza kufungwa moja baada ya nyingine huku nikisubiri kwa hamu kuiona sura ya mke wangu.
Ajabu ndoa zote zilifungwa bila kuiona sura ya mke wangu. Nilijikuta nikipagawa na kujiuliza nilielezwa ndoa nne au tano?
Baada ya ndoa zote kufungwa bila kushuhudia sura ya mke wangu, watu wote walitoka kanisani na kunifanya nibaki peke yangu.
Nilijiuliza mke wangu atakuwa amekwenda kufunga ndoa kanisa gani, nikiwa bado nimesimama kama sanamu na kuamini kuwa huenda kuna ndoa nyingine ingekuja kufungwa, nilishtuliwa na mhudumu wa kanisa.
“Ndugu vipi mbona huondoki na wenzako?”
“Samahani kaka kuna ndoa nyingine zaidi ya hizi?”
“Hakuna, leo kulikuwa na ndoa nne tu hakuna zaidi ya hizi.”
“Mmh! sijui atakuwa amekwenda kufunga ndoa wapi?” nilijikuta nikizungumza peke yangu kwa sauti.
“Kuna nini?” mhudumu wa kanisa aliniuliza.
“Ooh! samahani,” nilijikuta nikijibu na kuondoka bila kuaga mpaka nje ya kanisa.
Nje watu walikuwa ndiyo wanamalizikia kuondoka, nilijikuta nimerudi nyumbani kwa miguu na kumsahau yule dereva wa pikipiki.
Kwa kweli nilikuwa nimechanganyikiwa na kuamini kama maneno aliyonieleza mke wangu yalikuwa na ukweli basi atakuwa amefunga ndoa siku za nyuma.
Usiku ulikuwa mrefu kwangu, usingizi ulinikimbia kabisa, mawazo yangu yote yalikuwa kwa mke wangu na kuona kama kweli ameolewa, basi atakuwa amenifanyia ukatili mkubwa sana.
Jumatatu sikuweza kwenda kazini nilikuwa kama mtu niliyefiwa, hata chakula kilinishinda.
Jioni Simon alikuja kunitazama alikuja na mmoja wa wafanyakazi wenzangu na kunikuta nimejilaza sebuleni mikono kichwani huku macho yangu yakiweka michirizi na kulowesha kwenye mito ya kochi.
Simon alinishangaa sana na kuniuliza:
“Kazala una matatizo gani?”
“Simon wewe si wakuniuliza swali kama hilo, unajua vizuri matatizo yangu,” nilimjibu bila kumuangalia.
“Kazala umetoka nyumbani kufuata mapenzi au kazi?”
“Nimefuata kazi.”
“Unaacha kwenda kazini kwa ajili ya mwanamke, nilikueleza tangu mapema kuwa huyu mwanamke si chaguo sahihi kwako, lakini ukaona labda nakuchokonoa majibu sasa umeyaona.”
“Simon usiseme hivyo, wewe ndiye sababu ya mke wangu kukimbia.”
“Mimi?” Kauli yangu ilimshtua Simon.
“Ndiyo.”
“Mimi nimefanya nini?”
“Ushauri wako ndiyo uliosababisha mke wangu kunikimbia.”
“Kweli aliyekuroga amekufa, kitendo cha kumfumania mkeo ni mimi? si ulitaka kufa kwa mawazo, nimekusaidia bado huoni msaada wangu?”
“Msaada gani wakati mke wangu kanikimbia?”
“Mkeo yule sawa na kuku aliyelala nje si kuku tena ni kwale.”
“Lakini umeona lawama zote zinatokana na ninyi watu wa pembeni kuingilia ndoa yangu.”
“Hao watu wa pembeni unaowalaumu ndiyo waliyomponya mwanao aliyekuwa fundi majiko.”
“Pamoja na hayo, lakini ninyi ndiyo chanzo cha mke wangu kukimbia.”
“Kwani shemeji kaenda wapi?” Shedu mfanyakazi mwenzangu aliyeongozana na Simon aliniuliza.
“Hata najua yule mwanamke kaamua kuniua ningali hai,” nilizungumza sauti ya kukata tamaa.
“Kazala wanawake wamekwisha mpaka uchanganyikiwe kiasi hiki?” Shedu aliniuliza.
“Kwani huyo aliyemchukua mke wangu hakuona wanawake wengine mpaka kamchukua mke wangu. Kibaya zaidi jana kamuoa kabisa.”
“Utani huo! Atamuoaje mke wa mtu?” Shedu alishtuka.
“Mpaka kamtoa kwangu atashindwa vipi kumuoa kabisa?”
“Kwa hiyo Kazala bado unampenda mkeo?” Shedu aliniuliza kanikazia macho.
“Tena sana.”
“Na akirudi utakuwa tayari kumsamehe?”
“Ndiyo, najua si akili yake ni ushawishi wa watu wenye fedha wanaoona maskini kama sisi hatuna haki ya kuwa na wanawake wazuri.”
“Mtu mwenyewe unamjua?”
“Kwa sura namjua ila sijui anakaa wapi?”
“Upo tayari kumeza mfupa?”
“Una maana gani?”
“Najua huna uwezo wa kushindana na yule bwana kwa nguvu na fedha, lakini lipo kimbilio la wanyonge nakwambia mkeo atarudi mwenyewe.”
“Kimbilio la wanyonge! Kimbilio gani?” nilishtuka kusikia vile na kuraka kulijua hilo kimbilio la wanyonge.
“Kwa babu.”
“Kwa babu una maana gani?”
“Kwa mganga wa kienyeji.”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/-
“Kweli ataweza?” nilimuuliza kutaka uhakika.
“Bwana wee tena hawa wanaopenda wake za watu kazi yake ndogo sana nakwambia ndani ya siku mbili mkeo anarudi, ikivuka haifiki wiki.”
“Kweli?”
“Kweli kabisa, unajua taarifa zako nimezisikia toka kwa swahibu wangu hapa, roho iliniuma na kuona umefanyiwa ukatiri kibaya, nasikia jamaa ana mke yaani asiridhike na mkewe aje amchukue wako. Tena nitakupeleka mguu kwa mguu hadi kwa mzee wangu nakuapia mkeo atarudi.” Shedu alinihakikishia kunirejeshea furaha.
“Kama kamuoa?” niliuliza swali ambalo kwangu lilikuwa tata.
“Nimekueleza mkeo atarudi, si mkeo wa ndoa?”
“Ndiyo.”
“Basi atarudi huyo lina madogo tukifika kwa babu kazi imekwisha.”
“Gharama zake?”
“Si kubwa sana utaimudu tu.”
“Huyo babu yako yupo wapi?”
“Tanga katika wilaya ya Lushoto kijiji cha Mlalo kisha unaingia ndani zaidi kuna sehemu inaitwa Tewe hapo temea chini kuna kufuru za ajabu wa kumfufua maiti akatembea.”
“Nauli yake si kubwa?”
“Ya kawaida utaimudu.”
“Mmh! Nipo tayari hata kesho.”
“Itabidi muombe ruhusa ya siku mbili ili mwende na kurudi,” Simon aliyekuwa kimya muda wote alichangia.
“Lakini Shebu usemacho ni kweli?” pamoja na Simon kuchangia bado sikumuamini Shedu.
“Kwa nini tuandikie mate na wino upo, we twende halafu uniulize swali hilo baada ya kutoka kwa babu.”
Tulikubaliana kesho nikaombe ruhusa kazini ili twende mkoa wa Tanga kwa mtaalam.
***
Siku ya pili nilikwenda kazini kuomba ruhusa. Bosi alinikubalia bila kuniuliza swali lolote. Kwa muda mfupinilikuwa nimekonda kwa mawazo usiombe kumpenda mtu asiyejua thamani ya upendo wako kwake. Sikutaka kuomba mkopo kwa vile zilikuwa tarehe ya mshahara wafanyakazi wengi mifuko ilikuwa imenona.
Kwa vile muda ulikuwa bado Baada ya ruhusa tuliondoka siku ileile saa tano na kufika Chalinze saa kumi na mbili jioni. Mwenyeji wangu alinieleza itatubidi tualale pale ili tundoke siku ya pili kutokana na umbali wa kufika Lushoto. Tulilala Chalinze mpaka siku ya pili majira ya saa moja tupande basi linalotoka Dar es salaam kwenda Lishoto.
Siku ya pili tulipanda basi lililotoka Dar na kufika Lushoto kwenye kijiji cha Mlalo saa kumi jioni. Hatukukaa tulichukua usafiri mwingine wa baiskeli kuliingia vijiji vya ndani zaidi mpaka katika kijiji cha Tewe kijiji maarufu kwa waganga wenye uwezo wa juu.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment