Search This Blog

Thursday, 2 June 2022

MAPENZI YAMENIFANYA NIWE MUUAJI - 4

 







    Simulizi : Mapenzi Yamenifanya Niwe Muuaji

    Sehemu Ya Nne (4)





    NILIJUA KILE kilikuwa ni kilio cha majuto lakini mke wangu alikuwa na akili za mbuzi, alikuwa hakawii kujisahau na baada ya tukio alikuwa akitulia na kujutia.

    Kwa upande mwingine kiapo cha mke wangu nilikiona kizito sana, kwa kuwa alijichagulia adhabu na kama atarudia utakuwa ni upumbavu wake.

    Wazo la kusitisha safari yangu lilinijia na kuona hakukuwa na haja ya kwenda kwa mzee Kidereko, kwani niliona ni heri nitulie tu na kufanya mambo mengine.

    SASA ENDELEA...

    KWA kweli nilitaka kulipa nafasi suala hilo la kuahirisha safari yangu lakini aibu ya mke wangu kutembea na jirani yangu ilikuwa kubwa kwangu.

    Niliamini kila nitakapokuwa nikikutana na mgoni wangu moyo wangu utakuwa ukikosa amani. Baada ya kusimama kwa muda nikishauriana na nafsi yangu, nilishtuliwa na mke wangu aliyeonekana kunifuatilia kwa karibu.

    “Mume wangu najua huniamini lakini namuomba Mungu tena na tena aniepushe na tabia hii ambayo imekuwa ikikuchukiza, naomba unisamehe japokuwa sijui unawaza kunipa adhabu gani, lakini narudia tena kuapa mbele yako na Muumba wangu kama nitarudia tena nitakuwa sifai kuishi, Mungu ayachukue maisha yangu.”

    “Mke wangu nimekusamehe kutoka moyoni wala sina nilichokipanga kukufanyia, ila huyu mshenzi atakiona.”

    “Mshenzi gani tena mume wangu?”

    “God lazima awe mfano kwa mtu yeyote atakayekugusa kwani nimechoka, kila siku nafanyiwa mimi tu,” nilisema maneno hayo kwa uchungu japokuwa sikupenda mke wangu ajue dhamira yangu.

    “Mume wangu nimekuahidi haitatokea tena madhara yake nimeyaona, nikifanya tena ni heri Mungu anigeuze kuwa mnyama maana nitakuwa sifai kuwa binadamu.”

    “Nimekuelewa mke wangu, acha niwahi usafiri japo sina uhakika nitaondoka na gari gani maana muda umekwenda sana.”

    “Nakutakia safari njema mume wangu, wasalimie baba,mama na mashemeji pamoja na wifi zangu.”

    “Salamu zimefika.”

    Niliwaaga wanangu kisha niliondoka na nguo chache za kubadili kwa siku mbili nitakazokuwa kwa mzee Kidereko huku nikimuomba Mungu nirudi Jumapili usiku ili Jumatatu niamkie kazini.

    Niliondoka nyumbani saa kumi na moja jioni hadi sokoni na kununua vitu vya kumpelekea mzee Kidereko.

    Baada ya kununua mahitaji muhimu nilikwenda njia panda ambako nilibahatika kupata basi la kutoka Mwanza lililokuwa limechelewa kidogo kutokana na kuharibika njiani, dereva alikuwa akiendesha kwa mwendo wa kasi, tuliingia Chalinze saa nne na nusu za usiku. Niliteremka na kwenda kutafuta nyumba ya kulala wageni.

    Nililala mpaka siku ya pili saa mbili asubuhi ndipo nilipanda basi la Shambalai la kutoka Dar kwenda Lushoto, Niliwasili Mlalo majira ya saa kumi na moja jioni.

    Kwa vile nilishakuwa mwenyeji nilikodi baiskeli mbili, moja ilinibeba mimi na nyingine ilibeba bidhaa nilizonunua kwa ajili ya matumizi ya kijijini ambazo zilikuwa maalum kwa ajili ya mzee Kidereko.

    Nilipofika nilipokelewa kwa furaha na yule msichana aliyetupokea siku ya kwanza, kutokana na muda mrefu kupita bila kufika pale kijijini, nilimkuta akiwa na mtoto mdogo mwenye umri wa kama mwaka mmoja na nusu.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya kupokelewa nilikaribishwa chini ya mti na kupewa mkeka kwa ajili ya kujipumzisha.

    Mzee Kidereko sikumuona nilijiuliza na kuamini labda alikuwa amekwenda kwenye kazi zake za porini au sehemu nyingine.

    Baada ya muda nilimuuliza mtoto wa mzee Kidereko ambaye nilikuwa nikizungumza naye habari za safari.

    “Vipi mzee yuko wapi?”

    “Yuko ndani amelala siku hizi amekuwa mgonjwamgonjwa sababu ya uzee na kazi za mikiki mikiki. Kuna kazi moja ilikuwa nzito sana kwake na akaifanya na kumfanya kuwa katika wakati mgumu, sote tulijua kuwa mzee amekufa.

    “Alizimia kwa muda wa wiki nzima akiwa amelala kitandani, tangu alipozinduka amekuwa akiumwa mara kwa mara, hivyo muda mwingi anapumzika na kazi zake nyingine huwa zinafanywa na kaka.”

    Habari zile zilinishtua baada ya kusikia mganga anaumwa kiasi cha kufikia hatua ya kushindwa kufanya kazi zake na kumpa mtu mwingine.

    Niliamini uwezo wa mzee Kidereko ulikuwa ni karama kutoka kwa Mungu lakini mwanaye ni uganga wa kujifunza ambao hauna nguvu sana.

    Nilimuhoji yule mtoto wa mzee Kidereko uwezo wa kaka yake kwa wateja waliokuja.

    “Umesema kaka yako anashika mikoba ya baba yenu, kweli ana uwezo kama mzee?”

    “Kwa kweli sijasikia malalamiko yoyote kutoka kwa wateja ila kazi ikiwa kubwa sana anaifanya mwenyewe.”

    “Kwa hiyo kazi zingine anazifanya mwenyewe?”

    “Ndiyo, bado hajaacha rasmi kwa vile bado anamkomaza kaka ila akikomaa kazi zote atazifanya yeye.”

    “Nikitaka kazi yangu aifanye yeye itakuwaje?”

    “Atakusikiliza kama itakuwa nyepesi ataifanya kaka, sema tu hujafanya naye kazi lakini kila kukicha amekuwa akiivaa sawasawa kofia ya baba.”

    “Na mzee huamka saa ngapi?”

    “Muda wake umekaribia.”

    “Kwa hiyo mgeni akifika anaonana na kaka yako?”

    “Hapana, mgeni yeyote aliyetoka mbali lazima kwanza aonane na mzee ili kumpa faraja ya safari yake ndefu ya kuja kijijini.”

    “Mmh! Kama hivyo sawa.”

    Tukiwa katikati ya mazungumzo alitumwa mtu kuniambia kuwa nilikuwa nikiitwa na mzee ndani. Nilinyanyuka hadi sebuleni kwake, mzee Kidereko aliponiona alisimama katika kiti chake cha uvivu na kunikaribisha.

    “Kazala karibu baba.”

    “Asante baba, shikamoo.”

    “Marahaba, karibu sana.”

    “Asante, pole na matatizo.”

    “Asante, lakini ndiyo maisha tuliyoyachagua hatuna budi kukubaliana nayo.”

    “Vipi unaendeleaje?”

    “Ndiyo nimeishakuwa mgonjwa, hivyo sina zaidi ya kusubiri mauti yanichukue.”

    “Hapana baba, nina imani ukitumia dawa utakuwa sawa tu,” nilimpa moyo.

    “Hapana, pigo nililokutana nalo ni Mungu tu ndiye analijua, lakini namshukuru hata nikifa leo kuna mrithi nimemuacha japokuwa si kwa kiwango changu lakini atawasaidieni sana. Ningekufa na kinyongo kama dhoruba lile lingeniua bila ya kuacha mrithi, lakini kwa sasa wala sina wasiwasi mauti na yanichukue tu.”

    “Baba maneno gani hayo ya kuchoma moyo?” maneno ya mzee Kidereko yalinikatisha tamaa.

    “Kukuchoma moyo kivipi Kazala? Wakati kila mwanadamu lazima atakufa hakuna atakayeishi milele.”

    “Ni kweli baba,lakini basi tupe maneno ya kutupa faraja si unajua tunakutegemea?”

    “Kazala usiogope kufa kwa vile kifo kipo hata usipotaka kukisikia lakini kifo kipo tu.”

    “Kwani mzee wangu hiyo kazi ilikuwa nzito kuliko ile ya kwangu?” Nilimuuliza.

    “Hiyo mwanangu temea mate chini, unajua tunafanya kazi na watu wengi wenye nyadhifa serikalini na watu wa kawaida. Kuna kigogo mmoja wa serikalini ambaye nilimsaidia kupata ubunge na kumweleza kuwa ipo siku atakuwa mtu mkubwa serikalini.

    “Kwake aliona kama ndoto ya mchana, basi baada ya kupata ubunge tu akatajwa kwenye baraza la mawaziri.

    “Alikuja hapa akiwa haamini kilichomtokea, kwa kweli alichanganyikiwa. Nilimwambia bado namtengenezea mazingira ya kuwa rais.

    “Kwa kweli nyota yake ikawa inang’aa kila kukicha, hata vyombo vya habari vikawa vikimtaja sana kama mrithi wa rais anayemaliza muda wake.

    “Kumbe kuna watu wakawa wanamtafuta ili kumzima kama kibatari. Kuna siku asubuhi aliingia ofisini kwake bila ya kujua kama alikuwa ametegewa bomu. Alipokaa kwenye kiti alikutana na hilo bomu, alikuwa afie palepale kwenye kiti.

    “Lakini kinga niliyompa ndiyo iliyomsaidia. Kwa vile watu wa familia yake walikuwa wakijua kila kitu, wakamchukua na kumleta huku akiwa nusu mfu.

    “Baada ya kuletwa, nilifanya kosa kubwa la kufanya kazi kimazoea bila kuangalia uzito wa tatizo lile.

    “Nilidhani tatizo halikuwa kubwa kutokana na nilivyomkinga, kumbe watu walikuwa wamehangaika na kuufuata uchawi mpaka Nigeria ili wammalize baada ya waganga wa hapa kuchemsha.

    “Kosa nililolifanya nilimhudumia bila ya kujikinga, nilifanikiwa kulitegua lile bomu alilotupiwa. Wakati lilipokuwa likitoka likanipamia kwa vile sikuwa sawa lilinitingisha si kitoto.

    “Kutokana na uzito wa bomu lile na mimi nilivyokuwa nimelidharau lilitaka liniondoe lakini nilijiweka sawa, ndipo liliponilaza wiki nzima nikiwa sijitambui nilikuwa kama nusu mfu.

    “Vijana wangu walishindwa, ilibidi afuatwe mganga mwingine kuja kunizindua. Tangu nilipozinduka hali yangu imekuwa si nzuri, mwili umekuwa dhaifu mno lakini namshukuru Mungu hali yangu inaendelea vizuri.”

    “Una muda gani tangu upatwe na matatizo haya?”

    “Mwaka sasa.”

    “Mbona muda mrefu huna mabadiliko yoyote?”

    “Ninayo makubwa sana, enhe za siku?”

    “Nzuri mzee wangu, za miaka na wewe?”

    “Kama ulivyozikuta, ila nashukuru sana kwa kutukumbuka kila mara, vitu vyako unavyotutumia tunavipata, kwa kweli umekuwa kijana wa ajabu sana, kukufanyia kazi moja tu lakini umekuwa ukitukumbuka tofauti na watu niliowawezesha kimaisha, wengi wao hawatukumbuki mpaka wawe na shida.”

    “Kila mtu ana roho yake, wapo wasiojua kushukuru hata wakipewa.”

    “Ni kweli mwanangu, haya leo umekuja kwetu una tatizo gani tena?”

    “Kama la awali.”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mkeo katoka tena nje ya nyumba?” Mzee Kidereko alishtuka.

    “Ndiyo mzee wangu.”

    “Kwa hiyo unatakaje?”

    “Kwa vile yule jamaa amenfanyia kitendo cha dharau kwa kutembea na mke wangu, nataka afe kifo cha mateso na aibu.”

    “Hakuna tatizo, japo kazi hii ni kubwa lakini nitaifanya mwenyewe.”

    “Nitashukuru mzee wangu.”

    “Unataka kifo cha aina gani?”

    “Chochote ilimradi wadoezi wa wake za watu wakome.”

    “Kwa vile mkeo haaminiki nitakufundisha baadhi ya adhabu utakazokuwa ukiwapa wagoni wako ili usisumbuke kuja huku kila mara. Nitakupa zawadi moja kubwa sana, nina imani utakaporudi unaweza usinikute.”

    “Unataka kwenda wapi?”

    “Na uzee huu si kifo tu kitakachoniondoa? Nataka nikifa nikuachie zawadi ya kukusaidia katika maisha yako.”

    “Zawadi gani?”

    “Tego la mtu atayetembea na mke wa mtu na vitu vingine, nitakupatia ili uweze kujilinda na kuwasaidia waliokuzunguka.”

    “Nitaweza kweli?” Kazi ile niliona nzito kwangu.

    “Utaweza tu wala si kazi ni vitu vyepesi kama utakuwa tayari.”

    “Haya baba hakuna tatizo.”



    TULIKUBALIANA siku ya pili anipeleke porini kunionesha baadhi ya dawa za kuwakomesha wadoezi wa wake za watu.

    Siku hiyo ilipofika, alfajiri na mapema tuliondoka nyumbani na kuelekea porini, ajabu siku ile tulikuwa wawili tu, mimi na mzee Kidereko ambaye pamoja na maradhi na umri wake mkubwa tulikwenda kwa mwendo wa kasi kiasi.

    Saa nne tulifika kwenye pori kubwa ambalo lilikuwa na miti mingi.



    Mzee Kidereko alinionesha miti mingi na kuniambia kazi zake na jinsi inavyotibu maradhi, pia alinionesha miti mingine ambayo kama mtu akiitumia anaweza kugeuka kuwa uchawi na kuanza kudhuru watu.

    Nilijiuliza miti ile nitaijuaje kwa mara moja kiasi kile kwa kuwa, sikuwahi kuwa mganga wala sikuwa na mzoefu wa kazi ile. Kwa upande wangu niliona kama vile mzee Kidereko alikuwa akipoteza muda wake kunionesha vitu ambavyo nisingeweza kuvikumbuka.

    Alinitembeza hadi kwenye miti mingine yenye ukuwa mfano wa mibuyu, tulipofika pale tulisimama na akanitaka niweke mkoba chini na kuniomba nivue shati.

    Nifanya kama alivyoniambia na kubakia na suruali, kisha akinipa kaniki ya kujifunga kwa chini na kunielekeza kuwa nibakie kifua wazi.

    Alichukua maji yaliyokuwa kwenye chupa na kuyaweka mdomoni mwake, kisha aliyapuliza kuelekea kwenye ule mti mkubwa.

    Baada ya kumaliza zoezi lile alichukua unga wa dawa na kuurusha pande nne za dunia na kusema kwa sauti...

    “Hodi mizimu.. hodi majini yote kuanzia Kibwengo na majini wengine wote..hodi tumekuja kutaka msaada wenu.. tunajua ninyi mna nguvu, mizimu yote na majini tupokeeni tufanye kazi yetu,” baada ya kusema maneno yale nilisikia kitu kama muungurumo ambao haukudumu kwa muda mrefu na hatimaye ukanyamaza.

    Baada ya hali ile kutulia nilimsikia mzee Kidereko akisema:

    “Asante mkuu wa mti huu, asante mizimu yote, asanteni majini wote.”

    Baada ya kumaliza kutoa shukrani, akanitaka nikae chini sehemu yenye mwinuko na kunyoosha miguu kuuelekea ule mti mkubwa.

    Nilikaa na kutulia kusubiri maelekezo mengine.

    Mzee Kidereko alichukua shanga zilizokuwa zimetengenezwa kama mikufu, hirizi mbili za rangi yekundu ambayo ilikuwa kubwa na nyingine nyeusi iliyokuwa saizi ya kati, akanivisha shingoni na vitu vile kunilalia kifuani.

    Baada ya kunivishwa vitu vile nilitulia kusubiri kinachoendelea, alitoa kibuyu kidogo chenye shanga shingoni kwenye mkoba na kukiwekea kwenye mikono yangu.

    Mzee Kidereko alikichukua kile kibuyu kidogo na kuniwekea kichwani, akaanza kuzungumza kwa sauti kama anazungumza na mtu.

    “Mizimu nimekuja na mgeni, huyu ni mtu muhimu sana kwangu, naomba mumpe nguvu za kuweza kujilinda hata kufanya mambo yake mwenyewe kwa msaada wenu. Nimemleta huku ili muwe naye karibu kwa vile maisha ya mwanadamu si ya kudumu.”

    Baada ya kusema maneno yale ulizuka upepo mkali ulionitisha, ulivuma kwa muda kidogo kitu kilichoongeza hofu moyoni mwangu na baada ya muda ukatulia na hali kuwa ya kawaida.

    Baada upepo ule kutulia mzee Kidereko alikitoa kibuyu kichwani kwangu na kunirudishia mkononi na kunieleza:

    “Nuia mambo yako yote kwenye kibuyu hicho.”

    “Ninuize nini?” Nilimuliza kwa vile nilikuwa sijui cha kunuiza.

    “Chochote kuhusiana na maisha yako pia na kilichokuleta. Huku ndiyo kila kitu, wote tunategemea huku, mpaka kukuleta ujue umekuwa mtu wa muhimu sana, hata nikifa uwe na kinga ya mizimu na majini.”

    Nilitulia na kunuiza kupata fedha ili maisha yangu yawe juu, pia mtu yeyote atakayemgusa mke wangu basi afe kifo cha aibu. Baada ya kunuiza nilimweleza mzee Kidereko kwamba nimemaliza.

    Alikichukua kile kibuyu na kukizungusha kichwani kwangu mara kadhaa huku akinuia maneno yake kwa sauti ya chini yenye kusikika lakini bila ya kuelewa kile alichokuwa akikizungumza.

    Baada ya kuzungumza vile aliweka kibuyu chini na kunishika mikono yote na kuninyanyua.

    Alipofanya vile tu, upepo ulivuma tena na kufanya baadhi ya vitu kupeperuka.

    Haikuchukua muda mrefu upepo ulitulia, mzee Kidereko aliniambia nizunguke ule mtu mkubwa mara saba huku nikinuia tena.

    Nilifanya kama alivyoniagiza kisha nikarudi alipokuwa amesimama. Baada ya muda palitokea mtikisiko wa ajabu, ilikuwa kama mti ule ulikuwa unataka kung’oka.

    Niliingiwa na hofu ya kuangukiwa na mti na kuamini tusingeweza kupona kama ungetuangukia. Kama ningekuwa peke yangu ningetoka mbio lakini nilipomuona mzee Kidereko akiwa katika hali ya kawaida huku uso wake hauoneshi wasiwasi wowote, nami nikatulia.

    Hatimaye mtikisiko ule ulitulia. Mzee Kidereko alinipa kipande cha mti na hirizi ndogo nyekundu.

    “Hivi vitu vitakusaidia katika mambo yako, hakikisha unakuwa na vitu hivi muda wote. Hivi ndivyo vitakavyokuwa kinga yako popote utakapoenda, kila ukitaka kufanya jambo lolote gumu tafuna kidogo kipande hiki cha mti na nuiza halafu fanya ulichopanga kukifanya kitakwenda kama utakavyopanga.”

    Baada ya kutoka pale tuliingia katikati ya pori ambalo lilikuwa linatisha sana, mzee Kidereko aliendelea kunielekeza baadhi ya miti.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Aliniambia jinsi miti hiyo inavyoweza kuchanganywa na kutoa matokeo mengine, kwa kweli ilihitaji uvumilivu wa hali ya juu kuyapokea mafunzo yale, mengine yalikuwa yanatisha sana kiasi cha kuhitaji moyo wa chuma, niliamini ule ndiyo ulikuwa uchawi niliowahi kuusikia.

    Tulipofika kwenye mti mmoja alinieleza mti ule ukiuchanganya na mafuta ya mnyama na maji ya maiti basi, unamlaza mtu kitandani bila kuamka hata kwa miaka kumi kama bado muda wake wa kufa haujafika.

    Mti mwingine alinielezwa kuwa ukichanganywa na dawa fulani unaweza kuumaliza ukoo mzima kwa kutumia mkungu wa ndizi.

    Aliniambia mti huo ukiuchanganya na dawa nyingine huku ukiwa na mkungu wa ndizi, kila ndizi moja ikiiva mtu mmoja katika ukoo unaoukusudia anakufa, aliniambia mti ule ulikuwa ukitumika kwa ajili ya kulipa kisasi.

    Miti na vitu vya kuchanganyia nilivyoelekezwa kwa kweli sitaweza kuviweka hadharani kwa kuhofia watu wenye roho mbaya wanaweza kuvifanyia kazi na kuwaumiza wenzao.

    Mzee Kidereko aliendelea kunifundisha vitu vingi vya kiganga na kichawi. Siku zote mtu akitibu huwa mganga lakini akidhuru au kuua huwa mchawi.

    Alinifundisha njia za kumtega mwanamke anayetoka nje ya ndoa. Alinionesha tego la kung’ang’aniana, mwanaume anaweza kufariki baada ya kufika kileleni au kutokwa na damu na usaha mpaka kifo chake kinamkuta hapohapo.

    Alinionesha na matego mengine ambayo utengenezaji wake haukuwa mgumu, baada ya kumaliza ilikuwa yapata saa kumi na moja jioni tukaanza kurudi.

    Njiani wakati tunarudi nilimuuliza vitu nilivyoviona kule porini.

    “Babu,” nilimwita.

    “Naam,” aliitikia huku akinitazama.



    “Naweza kukuuliza baadhi ya vitu vilivyonitatiza?”



    “Uliza chochote wala usihofu mwanangu,” mzee Kidereko alinitoa wasiwasi.



    “Ule upepo ulikuwa ukiashiria nini?”



    “Ile ni ishara ya kukubaliwa.”



    “Na ule mtikisiko?”



    “Ule ni kukaribishwa kwenye mizimu, huwezi kufanya kazi yako yoyote bila kukaribishwa na wenyeji wa mti ule. Pale ndipo penye mizimu na majini yote ambayo yapo kwa ajili ya kutulinda na kutuelekeza dawa.”



    “Ina maana kila ukiwa na tatizo lazima uje huku?”



    “Hapana, ukishakuwa chini yao hukulinda muda wote.”



    “Kwa hiyo na mimi nitakuwa chini yao?”



    “Utapata ulinzi si mkubwa sana kwa vile kuna vitu unatakiwa kutoa pia kuwa tayari kuwa mganga.”



    “Kama sitaki kuwa mganga?”



    “Utapata ulinzi wa muda mfupi hasa katika vita yako inayoendelea.”



    Safari ya kurudi nyumbani ilikuwa ndefu kuliko tulivyo kwenda, kwani upande wangu nilikuwa nimechoka sana. Tukiwa njiani akanionesha baadhi ya majani ya miti miwili nichume ambayo alinieleza kuwa, nikichanganya na kitu kingine nikiwa nyumbani nitamfanya mbaya wangu ninavyotaka.



    Kwa vile nilikuwa sijiamini, nilimweleza kazi ile aifanye yeye lakini mengine nitafanya mimi.



    Tulifika nyumbani saa tatu na nusu usiku tukiwa hoi, kwa vile ilitakiwa niondoke kesho yake, mzee Kidereko hakutaka kupumzika, alianza mara moja kazi iliyonipeleka na kuniuliza mbaya wangu nataka afe kwa mtindo gani.



    “Mzee wangu nataka kila mtu ajue mimi ndiye niliyefanya vile baada ya kutembea na mke wangu,” nilijibu bila hofu.



    “Sawa, basi kitakachomtokea nina imani itakuwa fundisho kwa wote wenye tabia kama hizo.”



    Kama kawaida alichukua beseni la maji, alinipa dawa ya unga na kuniambia ninyunyize ndani wakati nalitaja jina la mbaya wangu huku nikiendelea kunyunyizia ule unga kwenye beseni. Baada ya muda, maji yaligeuka rangi na kuwa meusi.



    “Basi,” mzee Kidereko alinieleza niache kunyunyizia dawa baada ya maji kubadilika rangi.



    Alichukua dawa nyingine kwenye chupa na kuiweka kwenye beseni, baada ya muda maji yale yalikuwa meupe huku God, mbaya wangu akionekana amekaa kwenye kochi.



    “Ni yeye?” mzee Kiredeko aliniuliza.



    “Ndiyo.”



    “Muangalie vizuri.”



    “Ni yeye,” nilimhakikishia mzee Kidereko.



    Baada ya kumweleza aliniletea vitu viwili na kuniambia:



    “Hapa kuna vitu viwili, chagua kimoja, kisu kwa ajili ya kumuua ukiwa hukuhuku na ukifika utamkuta mbaya wako amekufa. Hii chupa ina uchawi wa kumuua taratibu kwa mateso mazito.”



    Nilichagua ya kifo cha taratibu cha mateso mazito. Baada ya kushika chupa yenye uchawi wa kuua taratibu, alichukua chupa nyingine na kutoa dawa ya unga na kuiweka kwenye maji kisha alisema niiweke ile dawa kuhakikisha inampata mgoni wangu mwili mzima.



    Nilifanya zoezi lile kwa umakini mkubwa. Baada ya kuhakikisha dawa imemfikia kila kona ya mwili, mzee Kidereko alitoa chupa ambayo ilionesha ina damu na kumimina kidogo kwenye maji na kuniambia nikiweke kile kisu ndani ya maji yale. Nilifanya kama alivyonielekeza kwa kukiweka kisu ndani ya maji bila vikwazo kama vya mwanzo na kiliingia moja kwa moja.



    Baada ya kumaliza zoezi lile alichukua lile beseni na kutoka nalo nje, baada ya muda alirudi na kunitaka nikapumzike kujiandaa na safari.



    “Haya kijana wangu kazi imeenda vizuri, mtu wako ni mwepesi hakutupa kazi yoyote, hivyo kalale kwa amani ili kesho uwahi kazini.”



    Baada ya zoezi lile kukamilika, niliagana na mzee Kidereko na kwenda zangu kulala nikiwa nimechoka sana kwa kazi na safari ya kutwa nzima. Siku ya pili kama nisingeamshwa niwahi usafiri, lazima ningechelewa. Pamoja na kuamshwa bado mwili ulikuwa mzito kutokana na mwili kuwa umechoka.



    Niliamka na kujiandaa na safari, ajabu siku ile sikuonana na mzee Kidereko kutokana na kuwa amechoka sana ila nilipewa mzigo wa dawa na vitu tulivyochuma porini. Kabla ya kuondoka nilioneshwa kazi ya jana tuliyofanya na mzee Kidereko. Mh! Inatisha, beseni lilikuwa na damu tupu, maji yote yaligeuka damu kitu kilichofanya niulize hali ile inamaanisha nini.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ile ni kuonesha kwamba mambo yamekwenda vizuri kwa asilimia mia moja.”



    “Kwa hiyo jamaa haponi?”



    “Yaani sasa hivi ni marehemu mtarajiwa.”





    Baada ya maelezo yale vijana wa mzee Kidereko walinisindikiza hadi kituo cha basi cha Mlalo ambako nilipanda basi la Shambalai.

    Kwa vile niliwahi, nilipata siti nzuri sehemu ya mbele upande wa dirishani.

    Muda ulipofika basi liliondoka Mlalo na kunifanya niwaze ya nyumbani na kutaka kujua mbaya wangu kitampata kitu gani.

    Kwa vile nilikuwa nimechoka, baada ya gari kuondoka kituoni sikuchukua muda mrefu nilipitiwa na usingizi mzito.

    Nilishtuliwa na abiria mwenzangu ambaye nilizungumza naye wakati nilipokuwa nikikaa kwenye siti na kumwambia kuwa nilikuwa nikiteremkia Chalinze.

    “Kaka..kaka,” aliniita.

    “Naam,” nilifumbua macho na kumwangalia.

    “Ulisema unashukika wapi vile?”

    “Chalinze.”

    “Tumefika watakupitisha mpaka Dar.”

    “Ooh! Asante,” nilimshukuru huku nikiufuta uso wangu.

    Niliteremka kwenye gari macho yangu yakiwa mekundu kutokana na kuuchapa usingizi kwa muda mrefu.

    Nilipoulizia muda niliambiwa ni saa nane mchana kuonesha kuwa basi lilikuwa limewahi kidogo. Kwa vile nilikuwa sijakula, nilinunua chakula pale kituoni kabla ya kuunganisha na usafiri mwingine wa kwenda nyumbani.

    Baada ya kula sikutaka kupoteza muda, nilipanda basi lililokuwa likipita japokuwa halikuwa na siti za kukaa, nilipanda hivyohivyo, tulipofika mbele kidogo abiria mmoja aliteremka nami nilipata siti mpaka nyumbani.

    Saa kumi na mbili na nusu niliteremka kwenye basi na kuchukua usafiri mwingine hadi nyumbani. Mke wangu aliponiona alifurahi sana, alinikimbilia na aliponifikia akanikumbatia, ilikuwa bado kidogo aniangushe.

    “Waawoo mume wangu karibu jamani.”

    “Asante.”

    “Za huko?”

    “Nzuri.”

    Alinipokea vitu na wote tukaelekea ndani, tulipofika kwa vile nilikuwa nimechoka sana baada ya kuoga sikutaka kuzungumza, nilipanda kitandani mpaka siku ya pili ambayo ilikuwa ni Jumanne, niliamka na kujiandaa kwa ajili ya kwenda kazini.

    “Mume wangu hujanijulisha hali ya wazazi nyumbani zinaendeleaje?” mke wangu aliniuliza wakati nikijiandaa kutoka kwenda kazini.

    “Hawajambo na wanakusalimia.”

    “Sasa mbona hukuniambia mpaka nimekuuliza au bado mambo yaleyale hayajaisha kichwani mwako?” mke wangu aliniuliza kwa sauti yake iliyokuwa ikiashiria kutaka kuangusha kilio.

    “Hapana mke wangu, kwangu yalishaisha baada ya kukusamehe, huwa siweki kitu moyoni kwa muda mrefu,” nilimtoa hofu.

    “Sasa kwa nini tangu jana hujanipa habari za nyumbani au sitakiwi kuzijua?”

    “Hapana mke wangu naomba nisamehe, nilijua labda nilishakueleza, hivyo, nilivyoamka nilikuwa nataka kuwahi kazini kwa kuwa jana sikwenda.”

    “Jamani mume wangu baada ya kusalimiana na kukuulizia habari za nyumbani ukasema nzuri na kuniomba ulale kwa vile umechoka hata chakula cha usiku hukutaka kula, tumeongea saa ngapi?”

    “Basi nisamehe lakini nilijua nikirudi kazini tungeweza kuzungumza kwa kirefu zaidi.”

    “Nimekusamehe mume wangu kwa vile nakupenda sana.”

    “Nashukuru kwa kunisamehe niache niwahi kazini.”

    Niliagana na mke wangu na kuondoka huku nikirudiwa na kauli ya mke wangu “eti ni kwa kuwa ananipenda sana”.

    Nilicheka na kujiuliza kama kupendwa ndiko huko basi wasiopendwa wanateseka zaidi.

    Moyoni bado nilikuwa nawaza kifo cha aibu atakachokipata jirani yangu.

    Nilipofika kazini hakuna hata mtu mmoja aliyeniuliza kwa nini jana yake sikuwa nimefika kazini, kila niliyezungumza naye alikuwa akionesha kama vile siku iliyopita tulikuwa wote, hata mtu wangu wa karibu Simon tulipokutana naye aliniuliza habari za nyumbani, hakuniuliza kwa nini jana sikutokea kazini.

    Niliendelea na kazi mpaka jioni, niliporudi nyumbani kupumzika nilipata taarifa kuwa, God amehama pale nyumbani.

    Niliamini kufanya kwake vile alikuwa sawa na mfa maji anayetapatapa lakini lazima afe kwa vile maji hayana rafiki usipojua kuogelea.

    ***

    Siku zilikatika huku nikimuona mbaya wangu akidunda kama kawaida bila kuonesha dalili zozote za mabadiliko.

    Kwa kweli kitu kile kiliniumiza sana na kuona kama niliyoelezwa na mzee Kidereko yalikuwa ya uongo, ilifikia hatua nikahisi hata mgoni wangu wa kwanza inawezekana alikufa kwa amri ya Mungu na si nguvu za mzee Kidereko.

    Kama ingekuwa kweli basi ningesikia kuwa God ameanza hata kukohoa.

    Kwa kweli nilijikuta nikiingia kwenye mateso mapya ya kuumizwa kwa kumuona mbaya wangu akiendelea kudunda. Sikukubali nilipanga safari ya kurudi tena kijijini kwa mzee Kidereko akanijuze ukweli kama amechemsha.

    Niliomba ruhusa ya siku mbili kazini na kufunga safari kwenda Tewe kwa mzee Kidereko ili tukaangalie tumekosea sehemu gani.

    Kama kawaida nilifika kwa mzee Kidereko majira ya saa kumi na mbili jioni, hali ya pale ilinishtua kidogo, mji ulionesha kupooza na kunifanya nijiulize kulikoni.

    Nilipokewa kama kawaida, kwa vile sikutaka kukaa kwa muda mrefu, nilitaka kumuona mzee Kidereko mara moja ili kesho yake alfajiri nirudi zangu nyumbani.

    “Jamani vipi mbona kama hampo katika hali ya kawaida kuna usalama kweli?”

    “Mmh! Upo.” alinijibu msichana aliyenipokea ambaye alikuwa tayari ameshanizoea.

    “Kweli?”

    “Kweli kwani vipi?”

    “Ule uchangamfu niliouzoea umepotea kabisa katika eneo hili.”

    “Ni kweli.”

    “Kuna nini?”

    “Msiba.”

    “Msiba! Wa nani?” nilishtuka.

    “Mzee hatunaye.”

    “Niniii? Hapana..hapana,” sikukubaliana na kauli ile.

    “Kweli kabisa, swahiba wako hatunaye.”

    “Hapana ..hapana, naomba mniambie ukweli.”

    “Kweli kabisa sasa inakimbilia wiki ya pili.”

    “Jamani acheni utani naomba mnieleze ukweli,” bado sikukubaliana na ile kauli.

    “Najua huwezi kuamini, si wewe tu kila mteja wake aliyekuja hakuamini, lakini ukweli utabaki kuwa palepale kuwa mzee Kidereko amefariki dunia.”

    “Mungu wangu, mbona nadhalilika mimi Kazala,” nilijikatia tamaa.

    Kwa kweli sikujielewa nilihisi nguvu zikiniishia, kiza kinene kikitanda mbele yangu, nikashikwa na kizunguzungu na kudondoka chini bila kupenda.

    Sikujua kilichoendelea.

    Niliposhtuka nilijikuta nikiwa katika sehemu yenye kiza kinene, nilipatwa na mshtuko na kuishangaa sehemu hiyo ambayo ilikuwa imetawaliwa na ukimya.



    Nilitulia nikitafakari pale ni wapi, ghafla nilisikia sauti kama mtu akitembea, mara niliona mwanga wa kibatari. Bado nilikuwa njia panda kujiuliza pale ni wapi na nimefikaje.

    “Kaka... Kazala...kaka Kazala.” Iliniita sauti ya kike sikuitikia mara moja mpaka aliporudia zaidi ya mara nne ndipo nilipoitika.

    “Naam.”

    “Amka.”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nilinyanyua nilipokuwa nimelala kisha kukaa kitako na kijishangaa kuhisi baridi, nilipojishika niligundua nipo kifua wazi na mwili ulikuwa umegandiwa na majani.

    “Amka,” yule mwanamke aliyenifuata alinipa mkono kuninyanyua.

    Baada ya kunyanyuka, tulitoka nje na kugundua kumbe nilikuwa nimelazwa chumbani. Nilipewa maji ya kuoga na kuvaa nguo zangu, baada ya kuoga nilikutana na mtoto wa mzee Kidereko ambaye aliandaliwa kwa ajili ya kurithi mikoba ya baba yake.

    “Ndiyo ndugu yangu, pole sana,” alianza kwa kunipa pole.

    “Asante, ni kweli?” nilimuuliza swali ambalo akilini mwangu lilikuwa vigumu kukubalika mara moja kuwa mzee Kidereko anaweza kufa haraka hivyo.

    “Ukweli gani ndugu yangu?”

    “Kuhusu kufa kwa mzee Kidereko.”

    “Ni kweli, mzee amefariki wiki mbili zilizopita.”

    “Mungu wangu, nitakuwa mgeni wa nani?”

    “Unataka kuniambia mke wako bado tu hajatulia?” aliniuliza huku akinikazia macho.

    “Hapana ila yule mtu bado anadunda tena ana afya njema, nilikuja kwa mzee kumuuliza tumekosea wapi?”

    “Hebu nipe mkono,” aliniomba mkono wangu, akaushika na kuutazama kwenye kiganja na kunieleza:

    “Mbona sioni tatizo lolote?”

    “Kwa upande wangu naweza kuwa sawa, kwa huyo mbaya wangu naona kama kuna tatizo.”

    Aliagiza maji kwenye beseni kama alivyokuwa akifanya mzee Kidereko. Baada ya kuletewa, aliingiza mkono na kuwa kama anatafuta kitu kisha alitoa mkono uliokuwa umetapakaa damu na kunifanya nishtuke kuiona hali ile.

    “Mbona hakuna tatizo Kazala.”

    “Na hiyo damu?”

    “Ni uhai wa mbaya wako unapunguzwa kila kukicha.”

    “Mwezi sasa mbona yupo hai wala haoneshi dalili za kuugua?”

    “Kazala ulitaka mbaya wako afe kifo cha mateso, sasa tatizo nini?”

    “Mbona haoneshi dalili zozote za kuugua?”

    “Kazala hujui tu lakini mbaya wako wiki sasa yupo katika mateso mazito, kama angejua ni wewe basi angekuja kukuomba msamaha.”

    “Unanidanganya, mbona anatembea na yupo sawa?”

    “Wiki hii umemuona?”

    “Sijamuona ila yupo anadunda.”

    “Basi hali yake ni mbaya sana, sasa hivi yupo kwenye mateso mazito sana.”

    “Mmh! Sawa, lakini bado siamini,” bado sikuamini maneno ya mganga, niliona ananipa moyo na kwa vile mzee Kidereko amekufa nilijua kila kitu kilikuwa kimekufa.

    “Muulize mtu wa karibu yake atakupa jibu ambalo litakushangaza sana. Mzee angekuwepo angekushangaa sana.”

    “Basi nimekuelewa na nini hasa sababu ya kifo cha mzee?”

    “Ni kifo kama vifo vingine, japo alikuwa na uwezo mkubwa katika karama aliyopewa, lakini alibakia kuwa kiumbe wa kawaida anayeweza kuumwa, kula, kulala na hata kufa kama viumbe wengine.”

    “Lakini naona amekufa haraka sana?”

    “Kwa akili za kibinadamu tutaona amekufa haraka lakini mzee mwenyewe alijua yupo ukingoni katika maisha yake.”

    “Na nini kilichomfanya ajue muda wake wa kuishi umeisha, naona ni wiki tatu toka ajitabirie kifo na kweli mauti yamempata!”

    “Ni kweli kifo chake alikiona na kuomba akifa tulie kama vile wanadamu wa kawaida ameondoka na si kukufuru, pia alisema kama kumlilia ni siku ya kufa tu lakini siku nyingine ni kumshukuru Mungu. Na kweli alipokufa tulilia siku moja baada ya hapo tulimshukuru Mungu.”

    “Kwa hiyo mambo yangu mengine nani atanisaidia?”

    “Kwako nina imani hakuna kazi nzito, nakuahidi kukusaidia kwa muda wote, usihofu niamini nitakufanyia kazi kwa uhakika.”

    “Sawa nashukuru sana, ila nakupeni pole sana kwa kifo cha kipenzi chetu.”

    “Nashukuru sana, ila kifo chake kitabakia palepale kwa kuamini kazi ya Mungu haina makosa.”

    “Kwa mbaya wangu unaniambiaje?”

    “Kazi imefanyika, subiri majibu, ungetaka tumkate mara moja, sasa hivi tungekuwa tumemsahau.”

    Kwa vile muda ulikuwa umekwenda, kililetwa chakula, tulikula pamoja kisha tuliendelea kuzungumza hadi usiku sana nilipokwenda kulala kuisubiri siku ya pili ili nirudi nyumbani. Usiku ulikuwa mrefu kuwaza taarifa ya kifo cha mzee Kidereko.





    Pamoja na kuwa kifo ni haki ya kila kiumbe kinachoishi lakini cha mzee Kidereko bado sikukiamini licha ya kuniambia nisikiogope

    lakini kwa karama zake sikuamini kama kafa kirahisi namna ile.

    Mwanaye pamoja na kunitoa hofu katika matatizo yangu, bado sikumuamini katika kuzifanya kazi zangu.

    Niliamini huenda safari ile iwe ya mwisho kwa miye kurudi tena Tewe kwa kuona hakukuwa na mtu mwenye nguvu baada ya mbuyu kuanguka.

    Lakini kwa upande mwingine nilijiona ni kama mtu niliyetaka kukosa shukrani, kwani kuna baadhi ya vitu nilivyooneshwa na mzee Kidereko nilitakiwa kuvifanyia majaribio.

    Kutokana na kauli ya mzee Kidereko, alinifundisha ili nisisumbuke kwenda kwake mara kwa mara ni kama vile hakupenda kila jambo nilikimbize kwake, labda likiwa zito sana.

    Siku ya pili nilirudi nyumbani na siri yangu moyoni huku nikitafuta taarifa za God ili kutaka kujua ukweli kutokana na kauli za mtoto wa mzee Kidereko.

    Niliamini mzee Kidereko alijua nini kitafuata, pia alionekana kutouamini uwezo wa mwanaye na kuamua kunifundisha silaha za maangamizi pindi nitakapovamiwa niweze kujitetea.

    Taarifa nilizoletewa kuhusiana na mgoni wangu God, nilitakiwa niwe na moyo wa chuma kuzipokea. God alikuwa amemaliza siku nne tangu apelekwe kwao kutokana na kutokwa na damu zisizokata sehemu ya haja kubwa kama mtu wa jinsi ya pili anavyokuwa kwenye siku za kutumikia.

    Ugonjwa wake haukuonekana katika vipimo vya hospitali, ilibidi achukuliwe na ndugu zake wanaoishi Dar ili wampeleke kwa mtaalam Bagamoyo.

    Wiki moja tangu niliporudi kutoka Tewe kwa marehemu mzee Kidereko, nilipata taarifa nyingine ambazo hazikunishtua sana japokuwa zilikuwa zikisikitisha kwamba God alifariki wiki iliyopita akiwa njiani kupelekwa Bagamoyo.

    Mi moyo kwatu baada ya kumtia adabu mbaya wangu na kuapa kila atakayemgusa mke wangu sitakuwa na simile naye. Adhabu yangu niliipanga kuwa ni kifo tu, tena kifo cha mateso.

    Najua msomaji utashangaa kwa kuniona nilikuwa nikitoa hukumu kubwa sana, ni kweli lazima hukumu iwe kubwa kwa vile wanawake wasioolewa ni wengi kuliko walioolewa, hivyo kwa nini mtu amfuate mke wa mtu?

    Kwa hilo mtanisamehe na wala sikuwa tayari kumueleza mke wangu kama bado anaendelea na tabia yake chafu aache japokuwa aliniahidi kutorudia tena huku akibubujikwa na machozi ya uchungu.

    Siku zote niliamini mwanamke huwa hana kosa kwa vile yeye hufuatwa na mtu anayemfuata huwa anajua kabisa mwanamke huyo ni mke mtu, kibaya mtu huyo ananifahamu vizuri.

    Mtu anayekufahamu na kukuchukulia mkeo mpaka kufanya hivyo huwa amekudharau sana, basi mimi kazi yangu nilipanga kumlambisha udongo kila atakayetembea na mke wangu.

    Mzee Kidereko alinikataza kutengeneza tego kwa mke wangu kwani alinieleza kuwa siyo vizuri.

    Aliamini kuwa tego hilo lingeweza kumsumbua hata kumletea madhara anapofanya mapenzi na mtu kama nikiwa nimesafiri.

    Kwa vile nilifundishwa vitu vingi na dawa nyingine zilikuwa zinapatikana kwenye maduka ya dawa za asili ambazo ukizitengeneza kwa kuchanganya na baadhi ya vitu unatengeneza bomu la hatari, sikupata shida sana.

    Namshukuru Mungu baada ya kifo cha mgoni wangu hali ya utulivu ilirudi kwenye nyumba yangu huku mke wangu akijitahidi kuonesha kuwa amebadilika, hata mavazi yake yalikuwa ni yale ya kujiheshimu, aliijali familia yake kuliko kitu kingine chochote.

    Alijitahidi kunifanya niamini makosa aliyoyafanya yalimuumiza sana na kutokuwa tayari kuyarudia tena.

    Kwa upande wangu sikuwa na tatizo lolote, nilimuacha afanye analotaka ila niliamini kuwa kazi kubwa itakuwa ni kwa huyo atakayejaribu kunichukulia mke wangu, huyo ndiye angezipata salamu zangu.

    Siku zilikatika huku nikiwa na siri nzito moyoni ya mke wangu kutoka nje ya ndoa kwa mara ya pili na kuchukua uamuzi wa kuyakatisha maisha ya mpangaji mwenzangu kwa kifo cha mateso makubwa.

    Mke wangu alijua nimemsamehe na suala lile kubakia kuwa siri yetu, kweli ilibakia kuwa siri yetu lakini adhabu niliyoitoa kwa ajili ya mtu aliyetembea naye ilikuwa kubwa sana kwa kuwa niliingilia hukumu ya Mungu, yeye ndiye aliyepaswa kuutoa uhai wa mtu na si mwanadamu.

    Nilimshukuru Mungu siri ile nzito ilibakia kuwa moyoni mwangu, niliamini kama rafiki yangu Simon angesikia alichokifanya mke wangu baada ya kuomba msamaha huku akilia kwa uchungu mbele yake huku akisema kuwa hatarudia tena hakika ingekuwa ni aibu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kama angesikia kuwa amerudia kosa lilelile la kutembea na mpangaji mwenzangu, pia nami kwenda kwa mzee Kidereko na kumuua kwa mateso mpangaji huyo sijui angenishauri nini.

    Kuhusu kifo cha God taarifa zilisema kabla ya kufa aliteseka kwa siku tatu kwa maumivu makali huku damu zikimtoka mpaka akawekewa khanga nzima ili kuzizuia damu.

    Nataka kukuambia kuwa uchawi upo, jiepushe na vitu vya watu, maana mateso yake ni makubwa hasa kama ukitembea na mke au mume wa mtu.

    Kwangu mimi pamoja na kuyafanya yote na marehemu mzee Kidereko huku nikipewa moyo kila nililotaka litatimia, mwanzo niliona ni uongo, hata kifo cha mgoni wangu wa kwanza nilijua ni amri ya Mungu.

    Lakini kifo cha mgoni wangu wa pili na yote niliyoelezwa yakatokea hapo sasa niliamini kuwa kweli uchawi upo, unaua na unatesa.

    Mwaka ulikatika tangu kilipotokea kifo cha mgoni wangu huku ndoa yangu ikizidi kuimarika.

    Wakati huo mke wangu alikuwa ameshika ujauzito mwingine, maisha nayo yalizi kuninyookea, kwani nilikuwa nimepandishwa cheo kuwa mtunza stoo wa vifaa vya ujenzi wa barabara baada ya dawa za mzee Kidereko kufanya kazi.

    Mwili nao ulichukua nafasi yake, kitambi cha juu kilinitoka. Yeyote aliyeniona wakati wa mateso ya ndoa yangu nilipobakia kichwa tu kama kiluilui wa chura angeniona, asingeamini kama nilikuwa mimi.

    Nilipendeza, kazi ilinikubali niliweza kutengeneza fedha kwa kuuza vifaa vya ujenzi kwa kuandika vifaa vingi na vichache tu ndivyo vilivyofanya kazi.

    Vifaa nilivyovizidisha niliviuza na kupata fedha ambazo ziliniwezesha kununua kiwanja na kuanza ujenzi wakati nikiendelea kupanga.

    Baada ya nyumba yangu kuisha nikataka niwachukue wazazi wangu ambao muda ule nami niliona ni muafaka kuwahudumia ili waje wale jasho la mtoto wao.

    Siku zote Mungu akikuandikia ndiyo hakuna kipingamizi, kila mpango nilioupanga uliniingizia fedha.

    Kama nilivyoelezwa na mzee Kidereko kwamba kila atakayenifanyia ubaya basi utamrudia mwenyewe. Mafanikio yangu yalianza kuwaumiza watu pale kazini.

    Mfanyakazi mwenzangu mmoja alikwenda kwa bosi na kunichongea kwamba nilikuwa nikiiibia kampuni.

    Taarifa zile zilinifanya nisimamishwe kazi na uchunguzi ukaanza mara moja.



    Katika hesabu za vifaa vya stoo, ilionekana kila kitu kipo sawa na kufanya aliyekwenda kunichongea kufukuzwa kazi kwa kusa la udanganyifu. Baada ya kukosa ushahidi nilirudishwa kazini.

    Niliamini maisha nimeyapatia kwa kipindi kile, baada ya kukamilisha nyumba yangu, nilitaka kwenda kuwafanyia ‘surprise’ wazazi wangu ya kuwahamisha. Taarifa ya ujenzi wa nyumba niliwapa na kuniombea kwa Mungu isimame haraka. Baada ya kumaliza nyumba yangu nikawaambia ningekwenda kuwachukua japo sikuwaeleza kana ni kuwachukua moja kwa moja au la, hiyo nilitaka kuifanya baada ya kuwachukua.

    Niliazima gari la kampuni aina ya Land Cruser, nililiendesha mwenyewe hadi nyumbani kwa kutumia saa tatu badala ya tano kwa mwendo wa kasi niliokuwa nikitembea nao.

    Nilipoingia eneo la nyumbani nilikuwa na hamu ya kuonana na wazazi wangu. Kila nilipokuwa nikikaribia nyumbani furaha ilizidi mara dufu kuwaona wazazi wangu.

    Lazima niseme ukweli katika vitu nilivyokuwa nikivipenda chini ya jua, walikuwa wazazi wangu ambao kwangu walikuwa kila kitu. Naamini upole na busara ya ndoa nilirithi kwa baba ambaye alinieleza udhaifu wa mwanamke ambao siku zote mwalimu wao ni mmoja.

    Aliniambia kuwa, tulitakiwa tuwavumilie sana na kunieleza kwamba, mwanamke anatakiwa kuacha baada ya ndani kukosekana suluhu pia kushindwa kwa wazazi wa pande mbili.

    Kwangu niliamini kumfumania mke ni talaka isiyo na shaka. Lakini mapenzi yangu kwa mke wangu yalikuwa makubwa sana kiasi cha kushindwa kutoa uamuzi mzito kama ule kwa kuamini mke wangu atajirekebisha. Pamoja na dhambi niliyochuma ya kutoa roho ya viumbe wawili kwa ajili yake, kwangu niliamini walistahili adhabu ile kutokana na wao kujua kabisa waliomshawishi ni mke wa mtu. Duniani wanawake walioolewa ni wachache kuliko wasio na wanaume, mtu kumfuata mkeo ni uchokozi wa makusudi.

    Mtu kuwaacha wanawake wote na kumfuata mkeo, adhabu yoyote utakayompa ni saizi yake. Kwangu niliamini mke wangu hana kosa ila aliyemfuata na kumshawishi akijua ni mke wa mtu huyo ndiye niliyeamini ana makosa na alistahili adhabu.

    Baba yangu alinieleza kuwa, siku zote mwanamke moyo wake huwa mwepesi kushawishika kama mama yetu Hawa alivyoshawishiwa na kusababisha wanadamu tuishi katika shida.

    Kwa udhaifu wa wanawake nilikuwa tayari kumpigania mke wangu, baada ya kuwatia adabu, ndoa yangu ilitulia na kujikuta nikiona matunda ya kumpigania mke wangu ambaye siku zote niliamini ni mwanamke bora.

    Nilipofika nyumbani ambako nilikuwa nimeanzisha ujenzi mpya wa nyumba ambayo nilipanga kuipangisha yote na kuondoka na wazazi wangu kwenda kukaa nao ili wale matunda yangu, sikukuta mtu nje ila mlango ulikuwa wazi, pembeni kulikuwa na vyombo vilivyokuwa vimeanza kuoshwa kuonesha wenyeji wangu hawako mbali.

    Nikaita kwa sauti: “Mamaaa..babaaa, nimefika mwanenu.”

    “Pita ndani baba,” sauti ya mama ilijibu toka ndani.

    Niliingia hadi sebuleni ambako hapakuwa na mtu. Nilijiuliza kauli ya mama inatoka nje au ndani? Nikiwa bado nimesimama, sauti ya mama ilitoka chumbani kwao ikiniita:

    “Kazala.”

    “Naam mama, vipi unaumwa?”

    “Hapana, ila baba yako ndiye simwelewi.”

    “Kafanya nini tena baba?” Nilishtuka.

    “Ingia chumbani.”

    Niliingia chumbani kwa wazazi wangu na kumkuta mama amemlaza baba mapajani mwake ikionyesha anaumwa sana.

    “Mama! Kuna nini?” hali ile ilinitisha.

    “Hii hali hata siielewi, baba yako alikuwa mzima kabisa, muda mfupi uliopita tulikuwa nje wote tukizungumza, mi’ naosha vyombo, yeye akisoma gazeti. Mara ghafla alisema kitu kimemchoma chini ya mbavu kama kichomi na kumfanya ainame kwa maumivu.

    “Nilimsaidia kumuingiza ndani ili apumzike lakini muda ulivyozidi kwenda joto la mwili liliongezeka na jasho jingi kumtoka. Nilichukua maji na kitambaa kumkanda mwili wote, kidogo joto limepungua.

    “Kabla sijatoka nje, akaanza kulalamika kichwa kinamuuma kama kinataka kupasuka. Mpaka baba yako anatokwa na machozi ujue kashikika kweli. Kichwa kilipoanza kumuuma alikuwa akilalamika, lakini kauli ilikata ghafla, kila nikimwita hakufumbua mdomo wala kujigeuza, alitulia tu kama unavyomuona,” mama alisema kwa huzuni.

    “Mmh! Utakuwa ugonjwa gani unaobadilika kama kinyonga?”

    “Ninavyoutazama si wa kawaida, yaani ameanza kuumwa ndani ya muda mfupi lakini ukimuangalia kwa jinsi alivyokonda unaweza kusema kaumwa wiki nzima.

    “Kwa kweli hali inatisha kwani kanifanya na mimi nikose amani kabisa,” alisema mama huku akionekana kama aliyechanganyikiwa.

    “Mmh! Utakuwa ugonjwa gani unaobadilika kama kinyonga?”

    “Ninavyoutazama si wa kawaida, yaani kilichotokea ni muda mfupi, lakini mpaka sasa ukimuangalia baba yako kama kaugua wiki nzima.”

    Niliiangalia hali ya baba kwa kweli ilikuwa mbaya, sikuamini kauli ya mama eti baba kaumwa muda mfupi ndiyo kawa vile. Niliamini ananidanganya kwa vile nimetokea nyumbani ghafla bila taarifa.

    “Mama si kweli, inaonekana baba kaumwa muda mrefu, kwa leo tu ndiyo awe hivi? Haiwezekani ugonjwa wa muda mfupi awe hivi,” sikukubaliana na mama.

    “Mwanangu nikudanganye ili iweje? Kawaulize hata majirani kuhusu hali ya baba yako. Wao nao hawajui kama yupo kwenye hali hii. Nina imani wakimuona hawataamini. Mwanangu hiki ni kitu cha kunishangaza sana.”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Sawa mama nimekuelewa, basi tumuwahishe baba hospitali.”

    “Ngoja nikamuite rafiki yake baba Pasko akusaidie, mimi hata nguvu sina,” mama alionekana kuchanganyikiwa na ugonjwa wa baba.

    “Basi mama wahi.”

    Baada ya mama kutoka nje, nilimsogelea baba na kuushangaa uso wake ulivyokuwa umekonda na midomo kumkauka.

    Hali ile ilionesha baba hakuumwa kwa muda mfupi kama mama alivyosema. Niliamini alikuwa akiumwa kawaida ila siku ile ndiyo alikuwa amezidiwa sana. Nilimwita baba aliyekuwa amekata kauli kwa sauti ya chini.

    “Baba...baba...amka, mimi Kazala mwanao nipo hapa,” lakini baba hakunyanyua mdomo wala kukapua macho.

    Nilijiuliza baba yangu anaumwa nini mpaka kuwa katika hali ile. Mama alirudi na mzee Samweli maarufu kama baba Pasko na kuingia ndani.

    Mzee Samweli alipomuona baba alishtuka na kuhoji.

    “Jamani mzee mwenzangu kapatwa na nini?”

    “Kama nilivyokueleza,” mama alimjibu mzee Samweli, kwa vile mimi nilikuwa sijui chochote juu ya ugonjwa wa baba.

    “Ha! Kazala umekuja saa ngapi baba?”

    “Hata dakika tano sina nimefika na kukutana na hali hii, shikamoo baba.”

    “Marahaba, jamani si nimepita nimewaacha mnazungumza hapo nje?” Ilionesha mzee Samweli naye alishtuka sana kuiona hali ya baba ilivyokuwa.

    “Kama nilivyokueleza,” mama alijibu akiwa amejikunyata kwa hofu ya ugonjwa wa baba.

    “Mama, baba alikuwa akiumwa kabla ya leo?” nilijikuta nikimuuliza mama swali la awali ambalo jibu lake sikukubaliana nalo.

    “Mwanangu muulize hata baba Pasko kama baba yako alikuwa akiumwa hata kidole.”

    “Kazala baba yako alikuwa mzima wa afya njema, asubuhi tulikwenda wote kwenye kahawa na kurudi. Baada ya muda nilipita nikielekea ofisini kulikuwa na kikao cha kata, wakati wa kurudi nimewakuta mama na baba yako wakiwa nje, mama yako akiosha vyombo na baba yako akisoma gazeti na nikamuomba akimaliza kusoma aniazime. Nashangaa kuelezwa anaumwa, tena amekata kauli na la kushangaza zaidi anaonekana kama ameumwa kwa muda mrefu,” kauli ya mzee Samweli ilinishtua sana.

    “Sasa hii itakuwa nini?” niliuliza baada ya kuchanganywa na taarifa ile.

    “Tumuwahishe hospitali tu,” mzee Samweli alitoa wazo.

    Nilitoka kwenda kufungua gari kisha nikarudi ndani kusaidiana na mzee Samweli kumbeba baba.

    Baada ya kumuweka vizuri kwa kumlaza kwenye miguu ya mama, nililiondoa gari kuelekea hospitali. Mzee Samweli alitusindikiza.

    Sikutaka kwenda hospitali ya wilaya, niliamua kwenda moja kwa moja hospitali ya taifa, ambako kulikuwa na rafiki yangu aliyekuwa mkoani na baadaye kuhamishiwa katika hospitali hiyo.

    Tukiwa njiani tulimsikia baba akikoroma kwa muda, kisha alivuta mkoromo mrefu na kutulia.

    Hali ile ilinishtua na kunifanya nimuulize mama.

    “Mama vipi tena?”

    “Hakuna tatizo, twende tu.”

    Niliendesha gari kwa kasi, kidogo nipate ajali lakini nilimshukuru Mungu tulifika salama. Tulipofika tulichukua kitanda haraka na kumchukua baba aliyekuwa amelegea sana. Nilishtuka kumuona mama akizidi kutokwa na machozi. Nilijua ni kutokana na uchungu wa ugonjwa wa ghafla wa baba.

    Baada ya kufanikiwa kumlaza kwenye kitanda cha matairi, tulimuingiza moja kwa moja kwa daktari hata bila kukata cheti.

    Daktari aliacha kazi zote na kumuhudumia baba ambaye ilionesha wazi kuwa alikuwa mahututi.

    Baada ya kumwagalia huku akimpima kwa kumminya baadhi ya sehemu ya mwili wake, baada ya muda alituomba wote tutoke nje.

    Tulitii amri na kutoka nje kumuacha daktari afanye kazi yake. Kilichokuwa kikinishangaza ni machozi ya mama yaliyokuwa yakiendelea kububujika, pamoja nami kuwa na uchungu nilijikaza huku nikimuombea kwa Mungu.

    “Mama usilie baba atapona tu,” nilimsogelea mama na kumliwaza.

    “Tumuombe Mungu lakini...” mama hakumalizia alichotaka kusema, aliinamisha kichwa chini na kuendelea kumwaga machozi na kunifanya nizidi kuwa katika wakati mgumu.

    “Mama nini? Baba atapona tu.”

    Baada ya muda daktari alitoka na kuuliza:

    “Nani mhusika wa mgonjwa?”

    “Wote, mimi mtoto na huyu ni mama yangu mke wa mgonjwa,” nilimjibu.

    “Basi nakuomba wewe ndani mara moja.”

    “Mimi?” niliuliza huku nikijishika kifuani.

    “Ndiyo.”

    Niliingia chumbani kwa daktari ambako baba alikuwa amelazwa kwenye kitanda kilichokuwa kimezungushwa na pazia la kijani.

    Baada ya kuingia ofisini nilikaribishwa kwenye kiti na kutulia kwa muda huku daktari akiandika kwenye karatasi.

    “Samahani ndugu yangu, mzee anaitwa nani?”

    “Hassan Kazala.”

    “Mzee ameumwa kwa muda gani?”

    “Kwa maelezo ya mama, saa moja iliyopita alikuwa haumwi kitu chochote.”

    “Wewe unakaa wapi?”

    “Mkoani.”

    “Umefika lini?”

    “Kama robo saa iliyopita na kukuta hali ya baba imebadilika.”

    “Una ndugu zako?”

    “Nipo peke yangu kama roho kwa wazazi wangu.”

    “Kwa vile wewe ndiye kichwa na mwanaume nataka kukueleza ukweli kuhusu hali ya baba yako,” daktari alinyamaza na kuvuta pumzi na kunifanya nimtazame usoni.

    “Wewe mwanaume, baba yako amefariki.”

    “Eti baba kafanya nini?” nilishtuka kidogo ilikuwa bado kidogo nianguke kwenye kiti.

    “Jikaze ndugu yangu, wewe mtoto wa kiume kwani unatakiwa kumpoza mama anayekutegemea.”



    “DAKTARI kweli baba amekufa?” niliuliza kama vile sikumsikia vizuri alichokisema mwanzo.

    “Kitambo, mmemleta hapa akiwa tayari ameshakata roho.”

    “Nini kimemuua?” nilimuuliza huku nikijifuta jasho la mshtuko.

    “Kwa kweli mpaka tumfanyie uchunguzi wa kitaalamu.”

    “Mmh! Sawa.”

    “Basi mweleze mama vizuri ili asipate mshtuko.”

    “Sawa nimekuelewa, japokuwa najua ni kazi nzito kumwambia, lazima atashtuka mno.”

    “Jitahidi wewe ndiye unayetegemewa kwa sasa baada ya baba yako,” maneno ya daktari yalinijaza nguvu.

    Nilitoka nje huku nikijikaza kiume ili kuhakikisha namwambia mama kwa utaratibu ili asipatwe na mshtuko. Pamoja na kujikaza moyoni nilikuwa na uchungu wa kumpoteza baba yangu kipenzi. Nilikwenda kumweleza mama hali halisi iliyokuwa ndani. Nilishangaa kumkuta mama akiwa ameinama kwenye kifua cha mzee Samweli akionesha kwamba alikuwa akibembelezwa.

    “Mama..mama,” nilimwita huku nikijitahidi kuficha maumivu makali moyoni.

    “Kazala mwanangu kuna mabadiliko?” mama aliniuliza huku akinitazama kwa macho yake yalikuwa yamejaa machozi.

    “Ya nini mama?”

    “Ya hali ya baba yako.”

    “Mama..ba.b..,”

    “Kazala najua.. najua kila kitu, najua mwanangu, nilichokiona najua ndicho ulichokutana nacho ndani, pole mwanangu,” kauli ya mama ilinishtua na kujiuliza inamaanisha nini.

    “Kipi mama?”

    “Hakuna chochote naijua hali ya baba yako ndiyo maana mwanangu unatokwa na machozi.”

    “Ma..ma.m.ma,” kauli ya mama ilinifanya nishindwe kuzungumza na kuhisi maumivu upya.

    Nilikumbatiana na mama na kila mmoja wetu alitokwa na machozi, tulilia kilio cha kimyakimya.

    “Jamani najua tumeumia wote, lakini muda huu tunatakiwa tujue marehemu wetu tunamhifadhi vipi?” mzee Samweli alisema.

    “Wanataka kumfanyia uchunguzi ili kujua kifo chake kimetokana na nini?” nilijibu huku nikiachiana na mama.

    “Hapana mwanangu baba yako alikataa kulazwa mochwali au kufanyiwa uchunguzi wa kifo chake. Aliwahi kusema akifa azikwe tu, kwa vile kila binadamu kifo ni haki yake.”

    “Mama ni ghafla sana, lazima tujue sababu ya kifo chake.”

    “Ukijua ndiyo utamrudisha duniani?” mama aliniuliza swali akiwa amenikazia macho yaliyojaa machozi.

    “Hapana mama, ila ni muhimu kujua.”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Siwezi kwenda kinyume na maagizo ya baba yako, hata mimi nikifa nizikwe siku hiyohiyo, sitaki kulazwa kwenye mafriji au kufanyiwa uchunguzi wa kifo changu.”

    “Sasa tutafanyaje akiwa amefariki muda huu? Hatuwezi kumzika leo, lazima tuwataarifu ndugu na jamaa, mazishi lazima yawe kesho.”

    “Hilo halina tatizo.”

    “Sasa mwili wa baba tutaufanya nini?”

    “Tunatakiwa tuuchukue leo ukalale nyumbani ili uzikwe kesho.”

    “Sawa mama,” nilikubaliana na mama.

    Tuliingia katika chumba cha daktari ambako mwili wa baba ulikuwa umelazwa kwenye kitanda na kuzungushiwa mapazia ya rangi ya kijani. Tulitaka kuutengeneza kabla ya kumchukua. Wote watatu tulisogea kwenye kitanda kilichokuwa na mwili wa baba.

    Kitu kilichotushangaza wote uso wa baba ulikuwa katika hali ya kawaida sana. Uso wake haukuwa na mikunjo yoyote, haukuwa uso uliokonda, alikuwa ni yuleyule baba yangu ninayemtambua.

    Hali ile ilitufanya tutazamane, mzee Samweli hakuvumilia alisema.

    “Hapana hii mpya, sijawahi kumuona mtu akonde akiwa mgonjwa na anenepe akifa.”

    “Hata mimi nashangaa!” mama alisema.

    “Hapa si bure, kuna sababu,” nilichangia.

    “Wee! Koma, maneno gani hayo,” mama alinikomesha, siku zote hakuamini ushirikina, aliuita ni mambo ya kishenzi.

    “Mama hii si hali ya kuiacha ipite hivihivi, lazima kuna kitu baba amefanyiwa, kama ameugua kwa muda mfupi na kukonda uso na anakufa kisha uso wake unarudi kwenye hali ya kawaida, hata ukikataa kuna kitu.”

    “Kazala achana na mawazo ya kijinga, baba yako amekufa tumzike na tumuombee kwa Mungu.”

    “Sawa mama,” nilikuba kwa shingo upande. Baada ya taratibu zote za kuuhifadhi mwili wa baba na kuchukua karatasi ya taarifa ya kifo. Tulikodi gari aina ya Toyota Pick-Up na kuuchukua mwili wa baba.

    Mama na mzee Samweli walitangulia na mwili wa baba mimi niliondoka na gari nililokuja nalo.

    Njiani roho iliniuma sana, baba yangu ameshindwa kuiona nyumba yangu, heri angeingia hata mara moja kwenye nyumba ambayo nilijenga na kuiandaa kwa ajili ya kuwalelea wazazi wangu.

    Lakini nilichokipanga kilienda tofauti, niliumia sana tena sana, sikupenda kumpoteza baba yangu kwani alikuwa mtu muhimu sana kwenye maisha yangu.

    Baba ndiye aliyekuwa taa na dira yangu, siku zote alinipa nguvu sehemu niliyokata tamaa na kujiona ninacho hata kama sina.



    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog