Simulizi : Mapenzi Yamenifanya Niwe Muuaji
Sehemu Ya Tano (5)
NJIANI nzima roho ilikuwa ikiniuma, baba yangu ameshindwa kuiona nyumba yangu, heri angeingia hata mara moja kwenye nyumba niliyoijenga kwa ajili ya kuwalea wazazi wangu.
Nilisikitika kwa kuwa kitu nilichokipanga kilienda tofauti, niliumia sana, sikupenda kumpoteza baba yangu aliyekuwa mtu muhimu kwenye maisha yangu.
Baba ndiye aliyekuwa taa na dira yangu, siku zote alinipa nguvu sehemu niliyokata tamaa na kujiona ninacho hata kama sina.
Sasa Endelea...
BADO nilitakiwa kumshukuru Mungu kuniachia mama yangu ambaye niliamini ndiye nitayewekeza nguvu zangu zote kwake baada ya kumpoteza baba yangu kipenzi.
Kingine kilichonipa wakati mgumu ni taarifa ya ugonjwa wa baba, kwa kuwa aliugua ghafla kisha kukonda kama mtu aliyeugua kwa kipindi kirefu na baada ya kufa uso wake ukarudi kwenye hali yake ya kawaida.
Kwangu nilijua ule ulikuwa ni mchezo, nimechezewa bila ya kumjua aliyenichezea ni nani.
Roho iliniuma sana kutokana na kufariki kwa mzee Kidereko, kwa kuwa ningejua kila kitu kilichotokea kuhusiana na kifo cha baba yangu.
Moyoni sikumuafiki kabisa mama kutokana na kukubali kirahisi kiasi kile, ingekuwa mimi, mwili wa baba usingezikwa haraka, ungekaa hata mwaka mzima mochwari ili nipate uhakika wa kifo chake.
Niliamini kifo kile hakikuwa cha kawaida na pengine baba yangu hakufa bali aligeuzwa kuwa msukule.
Nilipanga baada msiba kuisha nisafiri kuchunguza kifo cha baba ambacho kwa upande wangu bado sikuwa nikikubaliana nacho.
***
Siku ya pili tulimzika baba, msiba wake ulihudhuriwa na watu wengi sana, wafanyakazi wenzangu walikuwa ni miongoni mwa watu waliokuja kumsindikiza baba yangu na kunipa faraja.
Msibani kulikuwa na minong’ono ya chinichini ikisema kuwa kifo kile si bure lazima kulikuwa na mkono wa mtu.
Mama hakukubaliana kabisa na minong’ono ile pamoja na vitu vya kushangaza vilivyotokea, bado aliamini ni amri ya Mungu.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya mazishi na kukaa siku mbili, nilimuomba mama niondoke naye ili tukamalizie msiba nyumbani kwangu.
Lakini alikataa na kusema msiba ataumalizia palepale nyumbani kwake. Sikuwa na jinsi kwa vile alikuwa ameamua ilibidi niiache familia yangu ikae na mama kipindi chote cha kumaliza msiba wa baba kama alivyotaka mama.
Wiki moja ilikatika na muda wa kurudi kazini ulifika. Nilirudi kwangu na kumuacha mke wangu amtunze mama. Nilirudi nyumbani Jumapili na Jumatatu asubuhi nilikwenda kazini.
Nilianza kazi nikiwa bado na kitendawili kizito kichwani mwangu kutokana na kifo cha baba.
Pamoja na mama kusema kifo kile kilikuwa ni amri ya Mungu lakini sikutaka kukubaliana naye japokuwa nilimkubalia ili kumridhisha.
Nilipanga Ijumaa iliyofuata niondoke na gari la kampuni kwenda Mlalo. Niliamini hata kama nitalala Tewe siku ile na kesho yake Jumapili lazima niwe nimerudi muda wowote ilimradi Jumatatu niwahi kazini.
Wiki nzima niliyokuwa kazini nilikuwa katika dimbwi la mawazo kuhusiana na mazingira ya kifo cha baba yangu.
Wengi walijua kukosa kwangu raha kazini kulitokana na maumivu ya kifo cha baba, ambaye siku zote alikuwa mtu wangu wa karibu.
Kweli kifo cha baba kiliniuma sana kutokana na kipindi kile ndicho nilikuwa nikiwahitaji sana wazazi wangu ili nile nao jasho langu.
Kilichonichanganya zaidi na kuupa moyo wangu wasiwasi kilikuwa ni mazingira ya kifo cha baba. Niliamini utatuzi wake ningeupata kwa mtoto wa mzee Kidereko.
Safari yangu ilibakia kuwa siri yangu, sikutaka kumshirikisha mtu yeyote.
Mwisho wa wiki niliomba gari, nilijifanya kama ninakwenda kumuona mama. Kwa vile nilikuwa nikiivana na bosi, alinikubalia niondoke na gari.
Ijumaa niliondoka kazini saa tano asubuhi, watu wote walijua nimekwenda kumuona mama.
Niliondoka kazini saa tano na nusu asubuhi, nilitumia saa mbili na kufika Chalinze kutokana na mwendo kasi niliokuwa nikiendesha.
Niliunganisha moja kwa moja kuelekea Lushoto, nilifika Tewe saa kumi na mbili jioni. Nilikuta bado mwanga wa jua haujazama vizuri, niliamini kuwa ningeweza kufanya mambo yangu na kama yangekwenda vizuri ningeweza kurudi siku ileile na kuelekea kwa mama kisha ningerudi kazini.
Ugeni wangu wa ghafla uliwashtua wenyeji wangu, baada ya kunipokea walitaka kujua kilichonipeleka pale muda ule kilikuwa nini.
Kwa vile muda ulikuwa bado nilizungumza na mtoto wa mzee Kidereko palepale nje, chini ya mti, wengine wote walitupisha na kutuacha wawili tu.
“Ndiyo ndugu yangu za siku?” mtoto wa mzee Kidereko aliniuliza.
“Nzuri kiasi,” nilimjibu huku nikimtaza na kukutanisha naye macho na kumuona akiwa na shauku ya kutaka kujua kilichonipeleka pale.
“Ujaji wako umenionesha kuna kitu, ehe ndugu yangu tatizo nini tena?”
Nilimuelezea utata wa mazingira ya kifo cha baba yangu. Baada ya kunisikiliza alimwita msaidizi wake, kijana mmoja kati ya wasaidizi wa baba yake mzee Kidereko.
“Hamis.”
“Naam.”
“Njoo, niletee unga wa kutazamia mbali.”
Hamis alikwenda ndani na kurudi na chupa ndogo aliyomkabidhi. Baada ya kumkabidhi aliifungua na kumimina unga mweupe kiganjani kwake kisha aliumwaga kwa kuusambaza na kutulia kuutazama ule unga uliopeperushwa na upepo.
Aliutazama ule unga uliokuwa ukipepea kama vile anaangalia kitu ambacho mimi sikuwa nikikiona. Baada ya kutulia kwa muda alishusha pumzi ndefu na kusema:
“Kuna vita nzito sana.”
“Vita?” nilishtuka kusikia vile.
“Tena nzito, mmh! kuna kazi!”
“Kazi?” nilizidi kushtuka na kutokana na maneno yake.
“Tena nzito, mmmh! hii kwangu sijui!” alinikatisha tamaa bila kujua hiyo ni vita gani na uzito wake ni upi.
“Mbona unanitisha?”
“Sikutishi, ndiyo ukweli wenyewe, vita hii ingenoga kama mzee angekuwepo.”
“Una maana gani?”
“Kifo cha baba yako kina siri nzito.”
“Hebu nieleze tatizo kuliko kunizungusha na kunitisha.”
“Inaonesha hapa kifo cha baba yako kimetokana na kisasi.”
“Kisasi?” nilishtuka zaidi.
“Ndiyo.”
“Kisasi kipi tena?”
“Baada ya kifo cha mgoni wako wa pili, ndugu zake hawakukubali kama kile kifo ni amri ya Mungu. Kutokana na mazingira ya kifo chake, waliamua kufanya uchun-guzi ndipo walipokuona wewe. Hawakukubali kumpoteza ndugu yao, waliamua kulipa kisasi.
“Inavyoonekana waganga wengi wa nchini wamechemsha, hivyo wakaamua kutoka nje ya nchi kuhakikisha wanakulambisha mchanga. Inaonesha uchawi waliotumia kukuroga umetoka mbali sana.
“Naweza kusema mshukuru sana mzee Kidereko kwa kinga aliyokupa. Uchawi waliotumia tungekuwa tumekwisha kukuzika muda mrefu. Unakumbuka siku moja ukiwa kazini uliumwa sana kichwa kisha ulitoka damu puani?”
“Ndiyo nakumbuka.”
Niliikumbuka siku hiyo ambayo katika simulizi hii sikuizungumzia kabisa.
Siku hiyo nikiwa kazini, baada ya kumaliza kazi ya kutoa vifaa ambayo vilikuwa vingi nilisimama kwa muda mrefu.
Nilipokaa chini kichwa kilianza kuniuma kama kinapasuka, kilichofuata ni kutokwa na damu nyingi puani
Nilikimbizwa hospitali ambako nilikutwa na malaria. Baada ya matibabu nilijisikia vizuri na kuruhusiwa kutoka hospitali. Hali ile haikujirudia tena na kuamini yale yalikuwa malaria tu.
“Basi yale hayakuwa malaria ilikuwa ndiyo safari, shukuru kupelekwa kwenye mizimu, uchawi uliofanyiwa mbaya sana. Kutoka damu puani ilikuwa safari isiyo na kwaheri. Lile lilikuwa jini la kutumwa, jini Makata lilikuwa likukate palepale.
“Baada ya kuona kwako ngoma nzito walibadilisha mashambulizi na kuyaelekeza kwenye familia yako. Wameanza na baba yako baada ya hapo atatafutwa mtu mwingine.”
“He! Ina maana wamepanga kuiteketeza familia yangu yote?” nilishtuka kusikia vile.
“Ndiyo.”
“Wanatumia uchawi wa ndizi, wanaroga kwenye mkungu wa ndizi wenye ndizi mbichi, ikiiva ndizi moja na kudondoka, basi katika familia yako anaondoka mtu mmoja.”
“Mungu wangu!” nilishika kichwa kwa mshtuko.
“Mtego wao haukuwasumbua kukunasa kwa vile kilikuwa kisasi cha kuuawa ndugu yao, hivyo ilikuwa rahisi kukupata.”
“Sasa utanisaidiaje?”
“Kazi hii kwa uwezo wangu nzito sana, ila nitakuelekeza kwa mzee mmoja ambaye alikuwa swahiba wa baba, naye yupo vizuri kama mzee Kidereko.”
“Anakaa wapi?”
“Maeneo ya mbele kidogo japo kuna kamwendo kadogo.”
“Tunaweza kwenda leo?”
“Tunaweza kwa vile muda bado.”
“Tunaweza kutumia gari?”
“Hatuwezi kwenda na gari kutokana na eneo lenyewe, lazima tupande kilima na kushuka.”
“Usiku hakuna wanyama wakali?”
“Hakuna.”
Tulikubaliana kwenda kwa mganga mwingine baada ya ngoma yangu kuwa nzito kwake. Tuliongozana wawili kuelekea kwa mganga, ilikuwa safari ya kupanda na kushuka milima mpaka kufika kwa mganga nikiwa nimechoka na kutokwa na jasho chapachapa.
Toka nilipouachia mwili nilikuwa mzembe, safari ya nusu saa ilikuwa kama nimetembea zaidi ya saa sita. Tulipofika kwanza nilikaa chini kupumua, kwani hata kuongea nilishindwa kutokana na kifua kujaa pumzi.
Mtoto wa mzee Kidereko aliniacha nimepumzika kwenye gogo la mnazi na yeye kuingia ndani kwa mganga. Ilionesha pale ni mwenyeji kwa jinsi walivyompokea.
Nilitulia kwenye gogo huku giza likianza kuimeza nuru ya mchana. Baada ya muda alirudi na kunieleza jambo ambalo lilinishtua kidogo.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ndugu yangu tumefeli.”
“Una maana gani?”
“Mzee amekwenda mkoani, kuna watu wamemchukua jana.”
“Atarudi lini?”
“Mmh! Haijulikani.”
“Kwani ndiyo mara yake ya kwanza kusafiri kikazi?”
“Mara nyingi, huwa akiondoka kwenda kufanya kazi za watu mikoani, anaweza kumaliza hata mwezi mzima.”
“Mmh! Sasa itakuwaje, hana msaidizi?”
“Yupo, lakini kazi yako si ya kutumwa mtu mwepesi, unaweza kumpoteza kama mchezo.”
“Kwani ni nzito sana?”
“Hauna tofauti na uliyosababisha ugonjwa kwa baba uliopelekea mauti yake.”
“Mmh! Sasa nitafanyaje, hakuna waganga wengine?”
“Kwa kweli mimi niliyekuleta kwake ndiye niliyekuwa naye karibu pia nina mahusiano mazuri. Hata kazi zao walikuwa wakisaidiana na marehemu baba.”
“Uliniambia uchawi wao ni wa ndizi, kwa hiyo kuna mkungu unaendelea kuiva?”
“Ndiyo, tena uchawi huu ni mbaya sana, unaweza kumaliza ukoo wako kwa muda mfupi.”
“Mungu wangu sasa nitafanya nini ikiwa hakuna mtu wa kunisaidia?” nilijikuta nazidi kuchanganyikiwa.
“Mmh! Hebu turudi nyumbani nataka nikajaribu kutafuta ufumbuzi,” mtoto wa mzee Kidereko aliniambia.
“Ukishindwa?”
“Tumuombe Mungu nisishindwe, shida yangu ni kuzuia, kwani ukifanya mzaha wiki nzima unaweza kuzika familia nzima.”
“Eti?” Kauli ile ilizidi kunitisha.
“Uchawi waliotumia ni mbaya sana, ule haubakizi ukoo.”
Tukiwa katikati ya mazungumzo alitoka kijana mmoja aliyeonekana amevalia nguo za kiganga na kunisalimia.
“Za saizi kaka?”
“Nzuri.”
“Pole sana, nimefuatilia mazungumzo yako na maneno aliyoniambia Maghinde kwa kweli yamenishtua. Wakati nyinyi mkizungumza, niliangalia tatizo lako. Kwa kweli ni vita nzito sana.”
“Jamani badala ya kunisaidia mnazidi kunikata maini,” nilitamani kulia na kuiona kama dunia imeniinamia na hakuna wa kunipa msaada.
“Nia kubwa ni kukusaidia, kuna kitu nimekiona kimenitisha sana.”
“Mungu wangu kitu gani tena hicho?” kauli ya Bwaza ilizidi kunitia hofu.
“Hebu twendeni kwanza ndani, hili si jambo la kulizungumza hapa.”
Tuliongozana ndani huku nikihisi mwili wangu ukipoteza nguvu, moyoni nilijuta kujiingiza kwenye vita ya ushirikina.
Moyo wangu ulijawa na hofu ya kupoteza familia yangu yote kutokana na maelezo ya uchawi wa ndizi unavyoua watu kwa mpigo.
Tulipofika ndani, alichukua unga kama alivyofanya Maghinde mtoto wa mzee Kidereko. Baada ya muda alisema:
“Kama ulivyoambiwa vita hii ni nzito, hali inavyojionesha ni mbaya sana kwa upande wako. Inaonesha wiki hii na ijayo lazima upande watu watatu.”
“Watu watatu?”
“Ndiyo, hapa panaonesha ndizi tatu zimeshaiva tayari zinaweza kuanguka wakati wowote.”
“Ndiziii?”
“Ndiyo, inaonekana imedondoka moja ambayo ni baba yako. Zilizobaki zitadondoka wakati wowote ila moja itadondoka wakati wowote kuanzia sasa.”
“Mungu, sasa nitafanyaje jamani, ina maana na mama anakufa?”
“Hatujajua ila wakati wowote tegemea kupata taarifa za kukushtua.”
“Jamani mbona imekuwa hivi?”
“Mzee angekuwepo nina imani kila kitu kingekwenda vizuri, sasa mtanisaidiaje, Mungu wangu ina maana na mama nitampoteza?” nilianza kulia kwa uchungu.
Mara simu yangu iliita, nilipoangalia ilionesha inatoka kwa mke wangu. Moyo ulinilipuka na jasho kunitoka, moyoni niliomba nisipokee habari mbaya.
Niliipokea huku nikiuliza kwanza hali ya mama kabla ya salam.
“Haloo mke wangu, mama anaendeleaje?”
“Anaendelea vizuri, ndiye uliyemuacha peke yake huku nyumbani?”
“Nisamehe mke wangu, za huko watoto hawajambo?”
“Mwanao mdogo ndiye anaumwa, hapa tupo hospitali tumepewa kitanda.”
“Nini zaidi?”
“Anachemka sana na kuhema kwa shida.”
“Hali hiyo imeanza lini?”
“Hebu subiri kwanza..” mke wangu alisema upande wa pili huku akikata simu.
Nilisubiri maelezo ya mke wangu.
“Vipi?” Maghinde aliniuliza.
“Mke wangu anasema mtoto ameumwa ghafla ila mama hajambo.”
“Ameumwa ghafla yupo wapi?”
“Hospitali.”
Kauli yangu iliwafanya wote watazamane kisha wakashusha pumzi nzito. Kitendo kile kilinishtua sana na kujiuliza kulikoni kufanya vile.
“Kazala, hapa panaonesha ndizi tatu zimeiva ila moja tayari imedondoka.”
“Sijakuelewa si unasema zimeiva ndizi tatu na moja imedondoka?”
“Ndiyo, katika zile ndizi tatu kuna moja imedondoka na kufanya upoteze watu wawili mpaka sasa.”
“Mungu wangu mnataka kuniambia tofauti na baba kuna mtu amekufa?”
“Tena sasa hivi,” Bwaza alinijibu kwa sauti ya upole.
“U...u..nataka ku..kuni..”
Nilikatishwa kauli na mlio wa simu yangu, nilinyamaza na kuiangalia na kuona jina la mke wangu. Huku mapigo ya moyo yakinienda mbio nikaipokea.
“Haloo mke wangu.”
“Mume wangu...maskini mwanangu,” ilikuwa sauti ya kilio ya mke wangu kuonesha mambo yameharibika.
“Mtoto kafanya nini?” niliuliza pumzi zikiwa juu.
“Ame...me...fariki.”
Nilipatwa na mshtuko na kujikuta nikipoteza fahamu, nilipozinduka nilijikuta nimelazwa nje kwenye mkeka huku nikipigwa na baridi kali. Muda huo kiza kilikuwa kimeingia ila mwezi ulikuwa ukiangaza. Pembeni yangu walikuwepo Maghinde na Bwaza.
“Kazala,” Maghinde aliniita.
“Naam,”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Msikilize Bwaza kuna kitu anataka kukuambia cha muhimu sana.”
“Jamani naomba niondoke usiku huu nirudi nyumbani,” kwa kweli baada ya kupata fahamu sikutaka kitu kingine zaidi ya kurudi nyumbani usiku ule ili kuwahi msiba wa mwanangu.
“Sasa kama ulijua hivyo, huku umekuja kufanya nini?”
“Nilichokifuata sijakipata mnafikiri nifanye nini zaidi ya kurudi kusubiri tufe wote,” kwa kweli nilikuwa nimekata tamaa kwa niliyoambiwa na kilichokuwa kikiendelea.
“Sikiliza Kazala ndiyo maana nikakwambia msikilize Bwaza kuna kitu anataka kukueleza.”
“Haya nieleze mbona mwaka huu nitakoma.”
“Ni hivi bwana Kazala, kweli kama tulivyokueleza hali ni mbaya na ndizi kweli zimeonesha zimeiva na moja imeishadondoka muda mfupi na nyingine mbili zitafuata. Katika kuangalia inaonesha nguvu zinazokulinda wewe ni za mizimu na majini ya mti mkuu.
“Naamini kabisa majini na mizimu inakutambua, nina imani kilio chako mbele yao kitaweza kukulinda na balaa linalokuja mbele yako.”
“Sasa jamani, nitawezaje kwenda kwenye mizimu na kuwahi mazishi ya mwanangu?”
“Tulichokipanga tutaondoka usiku huuhuu hadi kwenye mti wa mizimu na mbuzi wawili wenye rangi nyekundu na nyeupe na vitu vingine tutakusaidia kuvitafuta ili kutoa sadaka itakayokusaidia kupata msaada wa haraka wa mizimu na majini.”
“Jamani hao mbuzi usiku huu nitawatoa wapi?”
“Wewe utatoa fedha kila kitu tumekipanga wakati tukikushughulikia ulipoanguka.”
“Kwa hiyo shilingi ngapi mbuzi wote?”
Walinitajia fedha za mbuzi, kwa vile nilikuwa nazo niliwapa. Hatukupoteza muda tuliwachukua wale mbuzi wawili na baadhi ya vitu wanavyovijua wao kwa ajili ya kazi yangu na kuelekea porini. Tulitembea kwa saa mbili mpaka kufika kwenye mizimu.
Tilipofika pale Bwaza, msaidizi wa mganga rafiki wa mzee Kidereko alifanya kama alivyofanya mzee Kidereko siku aliponipeleka pale enzi ya uhai wake.
Alichukua maji yaliyokuwa kwenye chupa na kuyaweka mdomoni kisha aliyapuliza kuelekea kwenye ule mti mkubwa.
Baada ya kumaliza zoezi lile alichukua unga wa dawa na kuurusha pande nne za dunia na kusema kwa sauti.
“Hodi mizimu... hodi majini yote kuanzia Kibwengo na majini yote katika mti huu...hodi tumekuja kutaka msaada wenu... tunajua ninyi mna nguvu, mizimu yote na majini tupokeeni mtusaidie shida zetu,” baada ya kusema maneno yale ulifuatia muungurumo ambao haukudumu muda mrefu ulinyamaza pia haukuwa na tofauti na mwanzo nilipokuja kwa mara ya kwanza Kidereko.
Baada ya hali ile kutulia nilimsikia Bwaza akisema:
“Asante mkuu wa mti huu, asante mizimu yote, asante majini yote.”
Alipomaliza kusema vile alinieleza nikae chini kwenye kichuguu ambacho nilikikumbuka nilikalishwa na mzee Kidereko, mambo mengi yalijirudia.
Baada ya kukaa nilinyoosha miguu kuelekea ule mti mkubwa na kutulia kusubiri maelekezo mengine.
Walichukuliwa wale mbuzi na kuanza kuwatembeza kunizunguka mara saba, kisha walisimama mbele yangu kila mmoja akiwa amemshikilia mbuzi wake kuuelekea ule mti mkubwa.
Bwaza kwa sauti kama anazungumza na mtu alisema:
“Mizimu, amekuja tena mwanadamu huyu ambaye mwanzo aliletwa na mkuu wetu na kumtambulisha kwenu.
Tunashukuru msaada wenu umesaidia, lakini umesahau waliomzunguka wazazi na watoto. Tunavyosema hivi tayari walimwengu wameishachukua vichwa wawili kwenye zizi lake.
“Tumefundishwa na wakuu kuwa tunapopata matatizo tukimbilie huku kuomba msaada wenu. Tunajua ninyi hamshindwi na kitu tunaomba mumsaidie mwanadamu huyu na waliomzunguka. Wakuu ndizi zilizoiva zisidondoke bali wadondoke wao.”
Baada ya kusema vile ulizuka upepo mkali, ulivuma kwa muda kidogo. Safari ile sikushtuka kwani hakikuwa kitu kigeni kwangu. Baada upepo kutulia Bwaza aliniambia ninuie kwa kuwashika wale mbuzi wote kichwani.
“Ninuie nini?” niliuliza kwa vile nilikuwa sijui cha kunuia.
“Chochote kuhusiana matatizo yako ili kukuondolea mabalaa yanayokukabili.”
Nilitulia na kunuia kuiomba mizimu na majini kunilinda mimi na familia yangu. Baada ya kunuia nilimweleza Bwaza nimemaliza. Waliwachukua wale mbuzi na kuwalaza, kisha waliwachinja wote na kuchukua mfuko uliokuwa na nafaka mchanganyiko na kuumimina kwenye ungo uliokuwa pembeni ya ule mti mkubwa. Kisha Bwaza alipaza sauti na kusema:
“Mizimu na majini tumekuleteeni zawadi kubwa ambayo tuna imani mtaipenda. Tunawaahidini kuwaletea ng’ombe mzima kama mtatufanyia kazi nzuri.”
Baada ya kuzungumza vile alimwaga unga wa dawa kwenye damu ya mbuzi na kwenye nafaka kisha tulisimama wote nyuma ya wale mbuzi aliowachinja.
Baada ya kusimama nilishtuka kusikia sauti ikicheka mfululizo kisha vigelegele vikifuatiwa na upepo uliovuma kwa muda kisha ulikoma.
Baada ya muda upepo ulitulia alinieleza nizunguke ule mti mkubwa mara kumi na nne huku nikinuia tena. Nilifanya vile kwa kuuzunguka mara kumi na nne, kisha nilirudi walipokuwa wamesimama. Baada ya muda palitokea mtikisiko wa ajabu kama mti ule mkubwa unataka kung’oka. Sikuwa tena na wasiwasi wa kuangukiwa na mti ule mkubwa.
Baada ya zoezi lile Bwaza alinieleza:
“Nina imani mambo yamekwenda vizuri sana, inaoneka mizimu na majini imefurahi kwa hiyo tuna imani ndizi zilizobaki haziwezi kudondoka tena.”
“Nashukuru sana kwa msaada wetu,” niliwashukuru nikiwa siamini walichonieleza.
“Washukuru mizimu na majini ndiyo yaliyokubali kukusaidia.”
Niliishukuru mizimu na majini kisha tulirudi nyumbani, kwa kumwaga dawa ya unga huku nikisema kwa sauti maneno niliyoelezwa niyaseme. Baada ya zoezi lile nilielezwa shughuli imeisha hivyo tulitakiwa kuondoka kurudi nyumbani.
Nilielezwa sitapewa dawa nyingine kwa vile kazi iliishia kwenye mti mkubwa. Mpaka tunafika nyumbani ilikuwa saa nane za usiku.
Kwa vile nilikuwa nimechoka sana nililala kidogo na saa kumi za usiku niliamka na kuianza safari ya kwenye msiba wa mwanangu nyumbani. Japokuwa nililala kidogo, kitandani muda wote niligeuka moyo ukiniuma familia yangu ikiteketea huku naiona.
Mpaka muda niliopanga kuamka sikupata usingizi hata kidogo. Njia nzima kichwa kilikuwa kizito kutokana na uchovu wa kutokulala.
Niliendesha gari macho yakiwa yamenivimba kwa kukosa usingizi na mwili uliniuma kama kidonda kutokana na kutopumzika kwa siku nzima.
Niliondoka kurudi nyumbani kwa kujilazimisha, mwili ulikuwa hautaki kabisa kwa uchovu wa mihangaiko na kukosa usingizi. Kama isingekuwa msiba wa mwanangu ningelala na kuondoka jioni ya siku ile. Niliendesha gari huku moyo ukiniuma kuona napoteza ukoo kwa ajili ya ushirikina, kuna kipindi nililia peke yangu. Lakini nilijua kulia si dawa zaidi ya kupambana.
Niliyakumbuka maneno ya rafiki yangu Simon kuhusu kumuacha mke wangu kama tabia zake hazibadiliki kuliko kwenda kwa mganga. Niliamini kama ningemsikiliza yote yale yasingenikuta ya kumkufuru Mungu. Lakini bado nilikuwa na haki ya kumpigania mke wangu.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Moyoni niliamini kuwa kama ningekubali kumuacha mke wangu, ningeendelea kuwa mnyonge hadi lini, nilijiuliza ningewaacha wanawake wangapi.
Bado nilikuwa najiuliza kwa nini mtu amfuate mke wangu, nilikuwa tayari nimempoteza baba mzazi na mwanangu wa mwisho na kupewa imani kuwa wawili waliotakiwa kuondoka wiki inayofuata kupitia tambiko lile, wote wamepona.
Nilifika nyumbani majira ya saa tano asubuhi, niliwakuta watu wamekusanyika kuashiria kwamba kulikuwa na msiba.
Mzee Samweli rafiki wa marehemu baba yangu ndiye aliyenipokea. Alinieleza taarifa nyingine iliyozidi kunichanganya na kutaka kunirusha akili.
Mzee huyo aliniambia kuwa mke wangu na mama yangu walikuwa hospitali baada ya kuugua ghafla usiku wa kuamkia siku ile na hali zao hazikuwa nzuri sana.
Nilijikuta nikichanganyikiwa na kuamini kuwa zile ndizi mbili nilizoelezwa kuwa zimeshaiva ni mke wangu na mama yangu.
Nilimuomba Mungu awanusuru maisha yao, kwani ningekuwa mwendawazimu kama ningezika watu watatu kwa mpigo.
Mwili wa mwanangu ulikuwa bado hospitalini, nilimshukuru mzee Samweli na familia yake kwa kusimamia msiba na ugonjwa wa mama na mke wangu.
Nilipofika hospitali nilikuta hali za wagonjwa zimebadilika kwa kiasi kikubwa, hata daktari alishangaa, wagonjwa walipata nafuu haraka tofauti na walivyopelekwa usiku wa kuamkia siku ile.
Kauli ile ilinifanya nikumbuke maneno ya waganga kule kwenye mizimu walipoomba ndizi zilizoiva zisidondoke. Ilionesha wazi kama nisingekwenda kule ningewapoteza mama na mke wangu.
Baada ya matibabu walitoka, jioni ya siku ile tulijiandaa kwa msiba na kesho yake tulifanya mazishi ya mwanangu na baada ya hapo nilipumzika kwa wiki nyingine na kurudi kazini.
Nikiwa kazini muda mwingi nilikuwa mtu mwenye mawazo kutokana na kufikiria jinsi ya kuipukutisha familia yangu.
Moyoni sikukubali kuonewa kiasi kile, nilipanga kwenda popote duniani kutafuta uchawi hata kama ni Nigeria ili kuhakikisha naupukutisha ukoo wao wote.
Kwa uchungu wa kuwapoteza baba yangu na mwanangu, nilikubali hata kufilisika lakini nihakikishe nimelipa kisasi cha mla mbuzi kulipa ng’ombe.
***
Mwezi mmoja baada ya kifo cha mwanangu, katika kuulizia sehemu gani kuna waganga wa uhakika, nilijikuta nikimfuata jamaa yangu mmoja pale kazini yeye alikuwa dereva wa magari makubwa na kumtaka undani.
Jamaa alikuwa akiamini sana ushirikina kiasi kwamba hata alipofanya makosa kazini hakufukuzwa.
Nilimfuata na kumuuliza jeuri yake alikuwa akiipata wapi hadi kufikia hatua ya kujiamini kiasi kile.
“Kazala maisha ni kuhangaika, nimeteseka sana, walimwengu si watu wazuri hata kidogo,” alianza kuniambia Kanyenye na kuongeza:
“Haki yangu mwenyewe ilinifanya nipoteze mke na watoto.”
“Haki yako ipi na tukio hilo limetokea lini?” nilimuuliza.
“Miaka saba iliyopita au miaka miwili kabla ya wewe kufanya kazi hapa, nilidunduliza vijisenti vyangu na kuvipeleka kijijini kwetu kununua shamba, nilifanikiwa na kulikodisha kwa watu ili wanilimie.
“Baada ya muda nililetewa taarifa kuwa jirani yangu kaingia kwenye eneo langu, nilifunga safari hadi kijijini kuonana naye, jamaa alikuwa kama ananitafuta.
“Baada ya kufikishana katika serikali ya kijiji na kumshinda, aliapa kunionesha, kweli bwana baada ya muda nilianza kuandamwa na mabalaa kibao, mara magonjwa na baadaye vifo vya mke na wanangu kwa mpigo.
“Huwezi kuamini nimezika watu watatu kwa mpigo, vifo vyao vilipishana kwa masaa, nilitaka kuwa mwendawazimu lakini nashukuru Mungu alinipa nguvu.
“Hakuishia hapo, nami akanilaza kitandani kwa miezi mitatu nikiwa sijui nini kinaendelea. Nimekwenda kuponea Mlandizi sehemu moja inaitwa Disunyala kwa mtaalamu mmoja ambaye ndiye aliyeninyanyua kutoka kitandani.
“Ila mtaalamu huyo alikataa kuua, alisema yeye anatibu tu. Nilimshukuru kwa msaada wake, baada ya kupona nilitafuta waganga wa kunilipizia kisasi, wengi walichemka, ilionekana jamaa alikuwa amejizatiti mno.
“Ndipo nilipompata jamaa mmoja aliyenielekeza kwenda sehemu moja ndani kidogo ya nchi ya Msumbiji sehemu inayoitwa Silver Makua. Kwa vile nilitaka kulipiza kisasi niliuza sehemu ya shamba langu na kufunga safari kwenda huko.
“Nilipita Mtwara na kuingia boda ya Namoto mpakani mwa Tanzania na Msumbiji. Nilitumia usafiri wa Land Rover za kizamani na kufika kwenye kijiji hicho.
“Nilifanikiwa kuonana na bibi mmoja mzee sana. Baada ya kumueleza shida yangu na yeye kuangalia kitaalamu, aliniambia kuwa atanisaidia.
“Usiku wa siku ile nilichimbiwa shimo na kufukiwa na kubakia kichwa tu. Nilikaa nje peke yangu mpaka asubuhi huku fisi na wanyama wengine wa kutisha wakipita karibu yangu bila kunifanya kitu chochote.
“Bundi walitua juu ya kichwa changu lakini hawakunifanya kitu na kuondoka zao. Kikubwa nilikuwa nimepewa masharti kwamba nisipige kelele kwa chochote nitakachokiona.
“Bila hivyo vitu nilivyoviona usiku ningekufa kwa presha. Kazala uchawi upo na unatisha, shauri yako.
“Alfajiri ya siku ile nilinyweshwa dawa nikiwa bado sijafukuliwa, baada ya hapo ndipo nilipofukuliwa na kuoshwa. Kisha nilipelekwa kwenye makaburi na kupewa kisu nichome katikati ya kaburi moja, nami nilifanya kama nilivyoagizwa.
“Baada ya zoezi lile niliambiwa naweza kuondoka.”
“Huo ndiyo uganga uliofanyiwa baada ya kusafiri umbali mrefu kiasi hicho?”
“Kazala yule bibi aliniambia, hakuna wa kuniua nitakufa kwa amri ya Mungu na kila atakayeshiriki kutaka kuniua au kuigusa familia yangu ni lazima azikwe.
“Nilirudi nyumbani, wiki moja baadaye familia ya jirani yangu ilianguka kama kuku wa mdondo, hivi sasa nyumba na shamba lao limebakia kama gofu wanaishi paka na popo.”
“Aisee naomba na mimi unipeleke,” nilijikuta nikiwa na hamu ya kwenda huko ambako niliamini ndipo pangenifaa sana.
“Ni muda mrefu lakini nitakuelekeza, ukifika pale kijijini jina la yule bibi ni maarufu sana, hakuna asiyemjua, anatambulika kwa jina la Nyangunda.”
“Hakuna tatizo mwisho wa mwezi nikipokea mshahara wangu nitaomba likizo lazima nami niende ili baadhi ya watu nyumba zao zibaki kuwa magofu ya kuishi paka na popo.”
Japokuwa sehemu niliyotaka kwenda ni mbali lakini nilijua ile ndiyo ilikuwa dawa niliyokuwa nikiitafuta kwa muda mrefu.
Baada ya kumaliza msiba, mama alihamia kwenye nyumba yangu mpya na kuishi na mkwewe na wajukuu.
Moyoni nilibakia na siri nzito ambayo sikutaka kumueleza mtu yeyote, kwa vile vita ile ilikuwa ni siri yangu, hivyo niliendelea kuifanya kuwa hivyo bila ya familia yangu kujua kilichokuwa kikiendelea.
Nilijipanga kwenda Silver Makua kutokana na maelezo ya Kanyenye, japokuwa ilikuwa ni safari ya nchi jirani lakini ilikuwa zikihitajika siku tatu.
Siku ya kwanza unaishia Mtwara, siku ya pili unafika unapokwenda tena mapema saa tano asubuhi kama ukiwahi kuondoka alfajiri.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya kila kitu kukamilika, niliomba ruhusa kazini ya wiki nzima, nyumbani niliwaaga nakwenda kuangalia mradi mpya wa kufungua mkoani, walinikubalia. Niliondoka siku ile jioni na mabasi yanayotoka Mwanza na kufika Dar saa nne usiku, nilala kwenye nyumba ya wageni iliyo karibu na kituo cha mabasi cha Ubungo ili alfajiri nipande mabasi ya Mtwara.
Asubuhi ya siku iliyofuata niliondoka na basi kuelekea Mtwara ili niunganishe kwenda Msumbiji kwenye mji wa Silver Makua. Niliwasili Mtwara saa kumi jioni, sikukaa niliunganisha na magari madogo mpaka Namoto ili asubuhi niunganishe kwenda Silver Makua.
Nililala Namoto, asubuhi ya siku ya pili baada ya kuchenchi fedha na kupata za Msumbiji, kutokana na maelezo niliyopewa na Kanyenye lazima niondoke na kijana mmoja pale mpakani anayejua lugha ya kule kunisaidia kuwasiliana na wenyeji.
Nilimchukua kijana mmoja ambaye alikuwa akizungumza lugha zaidi ya moja. Alikuwa akizungumza Kiswahili, Kireno, Kitindiga na Kingereza cha kuungaunga. Tulipanda gari dogo kuelekea Silver Makua. Nilifika Silver Makua saa tano na nusu asubuhi. Bila kuchelewa tulimuulizia Bi. Nyangunda kwa kumtumia mkalimani wangu aliyeuliza kwa lugha ya Kitindiga. Tuliambiwa alifariki muda mrefu zaidi ya miaka miwili iliyopita akiwa mzee sana.
Nilianza kuiona nuksi mbele yangu, mzee Kidereko kabla ya kukamilisha kazi yangu alifariki, naye Bi. Nyangunda alifariki miaka miwili iliyopita. Nilijiuliza nini hatima ya maisha yangu.
Nilimweleza mkalimani wangu aulize kama tunaweza kupata mganga eneo lile.
“Mmh! Kwa hapa hakuna mganga kama yule bibi, baada ya kufa watoto na wakujuu zake walikataa kurithi mikoba yake,” alijibu na mkalimani wangu alinitafsiria.
“Hakuna mwingine?” niliuliza nikiwa nimekata tamaa baada ya safari ndefu, lakini imekuwa haina matumaini.
“Mmh! Hebu subiri,” jamaa aliondoka kwenda kumuuliza mtu wa jirani aliyekuwa akitengeneza bai, baada ya muda alirudi.
“Sikilizeni, kama mnaweza pandeni gari mpaka Msibwa Daplaya, pale muulizieni mzee mmoja anaitwa Ngugude, wanasema ni kiboko kuliko hata marehemu Bi. Nyangunda.”
“Anasema kweli?” nilishtuka.
“Yule mzee kiboko.” Alitujibu yule kijana.
“Amesema yupo wapi?”
“Msimbwa Daplaya.”
“Kuna umbali gani toka hapa?”
“Mwendo wa saa tatu.”
“Kiasi gani?”
“Mnasema mmetokea Namoto?”
“Ndiyo.”
“Nauli yake haipishani sana, kama kuzidi ni kidogo sana.”
Tulimshukuru na kuagana na yule kijana, tulielekea kwenye kituo cha basi kilichokuwa mbele kidogo na tulipokuwa. Haukupita muda ilisimama Toyota Coaster iliyokuwa ikitokea Silver Makua.
Baada ya kuteremka abiria zaidi ya watano kituo kile, tulipata nafasi ya kukaa. Tulifika Msibwa Daplaya saa tisa alasiri.
Niliteremka na kusogea kwenye duka ambalo alikuwa akiuza kijana mmoja, mkalimani wangu alimuuliza na kuelekezwa, alinifuata na kunieleza.
“Itabidi tupande baiskeli tupelekwe kwa mganga aliyekuwa akikaa nje kidogo ya mji.”
“Hakuna tatizo.”
Tulielekezwa sehemu panapokodiwa baiskeli, tulikodi mbili na madereva wake. Safari ya kutoka nje ya mji ilianza. Tulijikuta tukipanda na kushuka milima huku vijana waliotupakia wakionesha uwezo wa kuendesha baiskeli kwa masafa marefu tena kwenye barabara mbovu.
Tuliingia vijiji vya ndani kwa kutumia muda wa zaidi ya saa moja na nusu. Tulifika kijijini kwa mganga Ngugude saa kumi na moja na nusu. Kama kawaida mkalimani wangu ndiye aliyekuwa mzungumzaji mkuu, baada ya kupokewa na binti mrembo wa kike aliyekuwa amejifunga kaniki na kuuacha mgongo nje. Baada ya mazungumzo ambayo mi’ sikuelewa anazungumza nini, alinieleza tumfuate.
Tuliongozwa kuelekea kilingeni, kilikuwa kiko mbele kidogo ya nyumba nzuri za mganga aliyeonekana kajijenga kimaisha, pembeni ya kilinge kulikuwa na zizi kubwa la ng’ombe, mbuzi na kondoo.
Tulifika kwenye kilinge kilichokuwa kumezungushwa uzio wa mimea ya minyaa. Tulipoingia ndani ya uzio tulikaribishwa kwenye vigoda, baada ya kukaa aliyetupeleka aliondoka kurudi sehemu aliyotupokea.
Tulikaa hapo kwa robo saa, kisha alitoka kijana aliyekuwa amevaa rubega la kaniki na kuzungumza maneno ambayo yalikuwa kama ya Kimakonde huku akiashiria kutuita.
Sikusimama nilimsikiliza mkalimani wangu ili kujua yule kijana anasema nini.
“Tunaitwa ndani,” mkalimani wangu alinieleza huku akinyanyuka.
Nilimfuata hadi ndani ya kilinge na kukaribishwa kwenye ngozi ya chui, tulikaa mbele yetu tulimkuta mzee aliyekuwa amekula chumvi nyingi. Kichwa na ndevu zake zilikuwa nyeupe.
Baada ya kukaa alisema neno ambalo sikulielewa, nilimtazama mkalimani wangu ambaye aliuniliuza.
“Anauliza tunatoka wapi? Nimwambie?”
Kabla sijajibu mganga alizungumza kwa lugha ya Kiswahili hali iliyotushtua wote.
“Mnatoka Tanzania?”
“Ndiyo,” nilijibu.
“Karibuni.”
“Asante.”
Mganga alibadili lugha tukawa tunazungumza Kiswahili.
“Mna shida gani?”
Nilimwelezea sababu ya kufunga safari kutoka Tanzania mpaka pale. Baada ya kunisililiza alitoka nje na kuchuma tawi la mnyaa na kuja nalo ndani.
Kisha alikaa kwenye ngozi ambayo sikuijua ni ya mnyama gani.
Baada ya kukaa alinipa tawi la mnyaa na kunieleza ninuie yote yanayonisibu.
Kwa vile nilikuwa nimeishakuwa mzoefu, nililipokea na kunuia, niliyasema yote yanayonisibu.
Baada ya kunuia nilimpa tawi la mnyaa alilichukua na kulibana na mdomo kisha aliziba masikio kwa mikono yake na kufumba macho na kutulia bila kupumua kwa muda, halafu alipumua kwa kasi na kurudia kubana tena pumzi.
Kwangu yalikuwa maajabu kwani alitulia zaidi ya dakika tatu bila kupumua kitu kilichoniogopesha na kuona mambo mapya.
Baada ya muda alitoa mikono masikioni na kubakiza tawi la mnyaa mdomoni na kuwa kama anazungumza na mtu kwa kutikisa kichwa kama kukataa wakati mwingine anakubali kwa kunyanyua kichwa juu.
Alifanya vile kwa zaidi ya robo saa kisha aliutema ule mnyaa na kuuweka kwenye ungo mdogo uliokuwa mbele yake na kusema:
“Kijana umetoka mbali kwa ajili ya mapenzi, kweli?”
“Kweli?”
“Umeua watu kwa ajili ya mapenzi, kweli?”
“Mmh! Kweli,” nilisita kidogo lakini kwa vile jambo lilikuwa wazi nilishindwa kukataa. “Umepoteza mzazi na mtoto kwa ajili ya mapenzi, ni kweli?” yote aliniuliza bila kunitazama, macho yake yaliangalia kwenye ungo.
“Ni kweli.”
“Na safari yako ya kuja hapa kusudio lako kubwa kuua, ni kweli?”
“Ni kweli.”
“Unataka uue watu wangapi?”
“Kivipi?” swali lake sikulielewa.
“Nakuuliza unata uue watu wangapi maana mpaka sasa umeua wanne?”
“Wanne?” nilishtuka kusikia nimeua wanne wakati nalikuwa najua wawili tu.
“Jibu kwanza, unataka kuua wangapi?” Mganga muda wote aliniuliza bila kunitazama.
“Kwa vile wameniulia familia yangu lazima na wao wabakie majina tu,”
“Nani kamuua baba na mtoto wako?”
“Kuna kijana mmoja alitembea na mke wangu, mimi sikukubali nikaamua kulipa kisasi.”
“Kisasi kipi?”
“Nilimuulia mbali.”
“Baada ya hapo?”
“Nilisikia familia yake iliponiendea kona zote za dunia kutaka kuniua, waliponishindwa wakaamua kuimaliza familia yangu kwa kumuua baba na mwanangu wa mwisho.”
“Baada ya hapo?”
“Nilikwenda kwa mtaalamu na kunisaidia kuzuia ndizi zilizoiva ili zisidondoke, lakini bahati mbaya moja ilikuwa imeishadondoka. Mama na mke wangu walikuwa wafe kwa mpigo kwa msaada wake walipona.”
“Unajua kilichoiva kikikaa muda mrefu kinakuwaje?”
“Kinaoza.”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Basi hawajafanya lolote kwa vile ndizi walizozizuia kuanguka muda si mrefu zitaanza kuoza.”
“Na zikioza?” niliuliza kwa mshtuko.
“Zitatoa wadudu.”
“Kwa hiyo?”
“Ile ilikuwa sawa na mgonjwa wa kichwa kumeza dawa ya maumivu, lazima baada ya muda maumivu yatarudi palepale. Kwa hiyo kifo cha pamoja kipo palepale.”
“Mungu wangu, nitafanyaje?” niliuliza nikiweka mikono kichwani.
“Nitakusaidia kuyaondoa maisha yao kwenye ndizi na kuyarudisha katika hali ya kawaida.”
“Nitashukuru sana mzee wangu, lazima niwamalize wote.”
“Ukiwamaliza wote pamoja na familia yako na wewe mwenyewe.”
“Kwa nini?”
“Unajua nani aliyeua familia yako?”
“Mzee si nimekueleza ndugu ya jirani yangu.”
“Hapana, wao hawahusiki,” jibu la mganga lilinishtua.
“Nani sasa muuaji?”
“Wewe mwenyewe.”
“Mimi?” nilishtuka kusikia vile.
“Ndiyo, hapa inaonesha wewe ndiye mhusika wa vifo vyote, kuanzia mgoni wako wa kwanza mpaka mzazi wako na mwanao.”
“Mzee! Mimi?” nilizidi kushtuka na kushangaa.
“Ndiyo.”
“Mzee mimi nitauaje familia yangu kisha nije huku kutafuta msaada?”
“Kumbuka bila wewe kuanza kuua usingewapoteza baba na mwanao.”
“Sasa ningefanyaje kama mtu katembea na mke wangu?”
“Zipo njia nyingi za kutatua tatizo si kuua, waganga wengi wamekuwa na tamaa ya fedha kuliko kutatua matatizo. Uliua ukiamini ndiyo suluhu la matatizo yako lakini bado mkeo aliendelea na tabia zake chafu.Umeua tena kibao kimekugeukia mwenyewe.
“Nataka kukueleza uchawi wa kisasi una nguvu sana, hata kama nitaiteketeza familia yake, bado kuna watu wangebakia na kwenda pande za dunia, lazima wangekumaliza tu, uchawi unazidiana.
“Sasa nifanyeje?” nilijikuta nikihamishwa kwenye dhamira yangu.
“Sikiliza siku zote vita huwa haina kikomo, pia uganga unazidiana naweza kusema mimi ni zaidi kumbe kuna mwingine akawa zaidi yangu na kuweza kukuteketeza kama pamba na moto.”
“Nimekuelewa, sasa nifanyeje mzee wangu?”
“Jiepushe kuchukua uamuzi mkubwa kila wakati bila kujua madhara yake, kama unaweza kuua basi kuna wengine wanaweza kukuua pia. Mfano watu hao wangekuja kwangu kulipa kisasi cha kuuliwa ndugu yao ingekuwaje? Siku hizi waganga tumekuwa tuna tamaa na kuwasilikiza wateja bila ya kuangalia mbele watapatwa na nini. Wengine wanajua kabisa walichokufanyia ni bomu litakalokuripukia mbele lakini kwa vile wana tamaa ya fedha wanafanya tu na kukuacha likuripukie.
Kama mwanamke hatulii mbona zipo dawa nyingi tu za kumfanya atulie. Kwa nini mkimbilie kuua?
Sawa niwaue wabaya wako, umerudi nyumbani mkeo kafanya ujinga wake utaua wangapi?”
“Mzee wangu yaani hata sijui, nahitaji msaada wako,” nilijikuta nikizidi changanyikiwa nilijiuliza yule kweli mganga au ndiyo yamemshinda akaamua kunitisha. Lakini kwa upande mwingine nilikubaliana naye hakuwa tofauti na alivyonishauri Simon.
“Kijana wangu nataka nikuase na waganga wenzangu, tujiepusheni kutoa roho za kiumbe ovyo. Kulipa kisasi ni sawa, lakini hata chuki tu za kibinadamu. Mganga mzuri ni yule anayekushauri madhara ya kitu unachotaka kufanya.
“Mfano tatizo kama lako lililojirudia mara mbili bado unaua watu. Hii ndiyo sababu hata dini zinawaona waganga wa jadi ni chukizo la Mungu, kwa waganga wenye tamaa na wasiozingatia taaluma.
“Wamejisahau na kuendekeza tamaa kumbe kazi yetu ni kutibu na si kuua ovyo. Najua utashangaa mganga kama mimi kukataa kuua?”
“Hapana mzee najua nimefanya makosa naomba msaada wako,” maneno ya mganga yalinibadili na kujiona nimefanya makosa makubwa kutoa roho za watu kwa ajili ya mwanamke. Nilijifikiria kama ningemsikiliza rafiki yangu Simon nisingempoteza baba na mwanangu.
“Sasa hivi umeishakuwa mchawi, najua kwa dhamira yako upo tayari hata kula nyama ya mtu ili kumfurahisha mkeo. Hivi uliposikia mtu uliyemroga amekufa ulijisikiaje?”
“Kwa kweli mzee naomba unisaidie, maneno yako yamenichanganya sana hata sijui nijibu nini, moyo unaniuma sana kwa yote niliyoyatenda.”
“Sishindwi kukufanyia unachotaka, lakini mbele kuna vita kubwa ambayo itakufanya ufe kifo cha aibu. Baada ya kifo cha mwisho cha mwanao, ni baada ya kumzika mama yako na mkeo, ungekuwa chizi na usingepona kwa mganga yeyote mpaka unakufa kifo cha aibu.”
“Mungu wangu!” nilizidi kuchanganyikiwa.
“Usiseme Mungu wangu! Kuna watu katika familia ile hawafi kwa mzizi wala kafara mpaka kwa kudura za Mungu. Lazima nao baada ya tukio la kupukutika kwa familia yao, wangepita juu chini kukumaliza. Siku zote vita haina udogo.”
“Nimekusikia mzee wangu, nifanyeje sasa?”
“Kijana wangu, sawa unampenda mkeo, tatua tatizo la mkeo si kukimbilia kuua, kama nilivyokueleza, zipo dawa nyingi na moja nitakupa hutaamini, kama mkeo akitembea tena nje njoo uvunje mikoba yangu.
“Kama haya ninayokwambia unaona nakudanganya, nenda popote kwa mganga makini utakuta wewe ndiye uliyemuua baba yako na mwanao.
“Waganga wengi tumekuwa tunaangalia tatizo bila kuangalia chanzo chake. Matokea yake tunakimbilia kuua tu. Kama ungekuwa umeonewa kweli, ningekufanyia kazi ambayo hakuna yeyote angeingiza mkono, kila mtu asingekuona. Ningekutengeneza ukawa kiza, watu wangekwenda Mashariki na Magharibi wasingekuona.”
“Mzee wangu nimekusikiliza vizuri na nimekuelewa, utanisaidia vipi?”
“Nitakusaidia kuyaondoa maisha ya mama na mkeo katika ndizi kisha nitakupa dawa ya kumtuliza mkeo. Nina imani ukiondoka hapa utatulia na mpenzi wako najua unampenda, basi tatizo litakuwa limekwisha ila jiepushe kupenda kuua, damu ya watu wengine ni nuksi unaweza kuandamwa na matatizo na kila mganga akawa halioni kwa vile aliyetenda ameisha kufa.”
“Mzee wangu nakuapia kwa Mungu sitarudia tena, nikitoka hapa nakuwa kiumbe kipya.”
“Wapo waganga wanaosifika kwa kuua lakini, mimi nasifika kwa kutibu matatizo kama yako.”
“Nashukuru mzee wangu, nimejifunza kitu, naamini nitakuwa mwalimu mwema kwa wengine.”
“Fanya hivyo ili tupunguze mauaji yasiyo na sababu, kazi ya Mungu tumuachie Mungu, tangu nianze uganga sijawahi kuua na sitaua.”
Baada ya makubaliano mganga alituomba tukapumzike nje ili kusubiri muda wa kufanya kazi yangu.
Tulitoka kwenda kukaa sehemu ambayo tuliletewa maziwa na viazi vya kuchemsha.
Kwa vile tulikuwa hatujala tangu asubuhi tulikishambulia chakula chote. Baada ya kula tulioneshwa sehemu ya kupumzika kwa vile muda ulikuwa umekwenda sana. Kutokana na uchovu wa safari tulilala mpaka siku ya pili.
****CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya kupatiwa kifungua kinywa cha uji wa maziwa na viazi, tuliitwa kilingeni na kukaribishwa kukaa kwenye ngozi ya chui, mzee Ngugude alichukua ungo na kuuweka mbele yake ambapo ndani ulikuwa na ndizi saba. Mbili zilikuwa zimeoza, mbili zilikuwa zimeiva sana na kuanza kubadilika rangi na kuingia weusi kwa mbali na mbili zilikuwa zimeanza kuiva na moja ilikuwa mbichi kabisa.
“Unaziona hizi ndizi?” aliniuliza huku akinisogezea ungo mbele yangu.
“Ndiyo mzee wangu,” nilijibu huku nikizitumbulia macho.
“Umegundua nini?”
“Sijagundua kitu,” nilisema huku nikitikisa kichwa kusisitiza.
“Basi hii ndiyo familia yako.”
“Familia yangu?” nilishtuka kidogo, japokuwa sikumwelewa.
“Ndiyo.”
“Una maanisha nini kusema hii ndiyo familia yangu?”
“Ulipokwenda kwa mganga alikueleza nini kuhusiana na ndizi?”
“Alisema familia yangu imetegewa uhai wake kwenye ndizi.”
“Basi ndizi zenyewe ndizo hizi, nimefanya kazi kubwa kuzivuta, kwa kweli kazi hii ilikuwa ngumu sana. Nimekesha kwa kazi hii lakini nimefanikiwa. Kabla ya kufanya kitu chochote nilitaka uone ili niifanye hii kazi.”
“Kwa hiyo hapa panakuwaje?”
“Kazi iliyopo ni kutoa sumu katika ndizi ili kuyafanya maisha ya familia yako yaondokane na uchawi uliotegwa kwenye ndizi.”
“Sawa mzee.”
“Unaona ndizi hizi mbili zilizooza?”
“Ndiyo.”
“Basi hizi ndiyo baba yako na mwanao waliofariki, unaziona hizi zilizoiva sana?”
“Ndiyo naziona.”
“Hizi ndiyo mkeo na mama yako, si unaona zilikuwa zikiendelea kuiva.”
“Ndiyo.”
“Basi zingeoza lazima ungepoteza watu wawili kwa mpigo japo ingechukua muda kutokana na kinga uliyopewa mwisho, unaziona hizi zilizoanza kuiva?”
“Ndiyo naziona.”
“Hizi ni za wanao waliobakia, nao walikuwa wakiiva taratibu japo wasingedondoka, lakini wangeoza na kufa kwa mpigo.”
“Mungu wangu!” nilishika kichwa.
“Usishike kichwa hapa nakuonesha ubaya wa kisasi, ungeweza kufanikiwa kuongeza idadi ya vifo vya watu, lakini matokeo yake yalikuwa haya, ungeipoteza familia yako na wewe kuwa chizi.”
“Na hii ndizi mbichi?”
“Hii ndiyo wewe, ukweli walikushindwa na kukubali wameshindwa. Unaiona hii ndizi pembeni?”
“Ndiyo.”
“Unaona nini?”
“Kuna mistari myeusi kama chale.”
“Basi haya ni makombora yaliyotumwa kukuozesha. Lakini mwili wako umekuwa imara, kinga uliyofanyiwa chini ya mti mkuu ndiyo iliyokulinda. Kinga yako ingekuwa ya kawaida ya kuchanjwa tu ungebakia jina.”
“Sasa mzee wangu utanisaidiaje?”
“Nitahamisha sumu kutoka kwenye miili ya familia yako huku ukishuhudia kwa macho yako.”
Alizichukua ndizi mbichi nne na kuziweka kwenye ungo mwingine kisha alichukua dawa ya unga mweupe na kuzimwagia zile ndizi taratibu huku akinuiza maneno anayoyajua. Baada ya muda aliuweka ungo wenye ndizi mbichi pembeni ya ungo wenye ndizi alizosema ndiyo familia yangu.
“Unauona ungo huu?”
“Ndiyo.”
“Una nini?”
“Una ndizi mbichi.”
“Ngapi?”
“Nne.”
“Vizuri,” alisema huku akichukua ndizi zilizooza na kuzitupa pembeni na ndizi mbichi akaziweka kwenye kikapu.
“Sasa nataka hizi ndizi ziwe kama hizi na hizi ziwe kama hizi.”
“Sawa mzee wangu.”
Aliuchukua ungo wenye ndizi mbichi na kuuweka pembeni ya ungo wenye ndizi zilizoiva na kutulia.
“Naomba macho yako yasicheze mbali usijesema nimebadilisha ndizi.”
Nilitumbulia macho kwenye ungo wenye ndizi mbichi, kila dakika nilishindwa kuelewa, ghafla nilijikuta nikichanganyikiwa baada ya kuona ndizi zimebadilika na kuhamia ungo mwingine.
“Umeona nini?” mzee Ngugude aliniuliza.
“Sielewi.”
“Huelewi nini?”
“Naona kama ndizi zimehamia huku.”
“Hapana hazijahama bali sumu nimeitoa na sasa ndizi zilizokuwa kwenye ungo huu zimerudi katika hali ya ubichi.”
“Kwa hiyo.”
“Ubichi huo ni uhai, sasa hivi vifo katika familia yako vitatokea kwa amri ya Mungu na si mkono wa mtu.”
Baada ya kusema vile, alichukua unga mweupe na kunyunyizia, alipomaliza alinieleza niende kuoga maji yaliyokuwa na dawa ili kuondoa mikosi ili nijiandae kwa safari.
Nilifanya kama alivyonielekeza baada ya kumaliza zoezi lile, alinipa unga mweupe akaniambia niubwiye kidogo na mwingine niupulize kama kusafisha njia. Nilifanya kama alivyonielekeza kwa kubwiya unga kidogo, unga ulikuwa na ladha kama ya unga wa ngano. Nilipomaliza tulipewa ruksa ya kurudi nyumbani Tanzania.
Tulisafiri salama mpaka Mtwara na kuagana na mkalimani wangu ambaye nilimlipa kiasi tulichokubaliana, kutokana na kazi kubwa aliyofanya nilimuongeza kiasi kingine kama asante. Kwa vile tulifika jioni sikutaka kulala pale Namoto nilikwenda kulala Mtwara mjini ili siku ya pili niondoke na mabasi ya asubuhi.
Siku ya pili asubuhi nilipanda basi kurudi Dar ili niunganishe mpaka nyumbani siku ileile. Nikiwa ndani ya basi bado nilikuwa na maswali kuhusiana na maneno ya mzee Ngugude, niliyaona kama yanajichanganya. Kuna wakati aliniambia anaweza kuua na kuna wakati alisema hajawahi kuua kwa kweli maneno yale yalinishtua na kuona kama uwezo wa yule mzee ni mdogo tofauti na sifa zake.
Moyoni niliamini kama ningemkuta bi Nyangunda ningeweza kuwakomesha wabaya wangu. Pamoja na kukubaliana na yule mganga niliamini bado nilitakiwa kwenda ndani zaidi. Nilifika Dar jioni na kuunganisha safari, nikafika nyumbani saa tano usiku. Nilipowasili nyumba ilikuwa kimya kuonesha wamelala. Nilipogonga mlango nilifuatwa na mke wa jirani yetu aliyenieleza kitu cha kushtushwa kwamba watoto wangu wako kwake. Niliulizia mama yao yupo wapi, niliambiwa yupo hospitali pamoja na mama yangu wapo chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).
“Mungu wangu tatizo nini?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Jana waliugua ghafla, kwa kweli hata hatujui ule ni ugonjwa gani.”
“Wapo kwenye hali gani?” niliuliza macho yakiwa yamenitoka pima.
“Tumuombe Mungu tu hata sijui niseme nini toka jana hatujafanikiwa kuwaona,” alisema kwa sauti ya huzuni.
Nilibakia nimesimama kwa dakika tano nisijue nifanye nini. Bila kujielewa nilijikuta nimekaa chini huku nikiwa na mawazo mengi kuhusiana na hali ile ya kufikia mke na mzazi wangu kurudiwa tena na tatizo.
Wasiwasi wangu mkubwa ulikuwa huenda mabadiliko ya mzee Ngugude ya ndizi ndiyo yaliyosababisha yote yale. Bila kuongeza neno nilinyanyuka mzimamzima na kukimbilia hospitali.
Nilikwenda moja kwa moja kwenye wadi ya wagonjwa mahututi nikaelezwa kuwa wametolewa na kurudishwa wadi ya kawaida. Nilipotaka kuwaona nilikatazwa na kuelezwa nirudi kesho yake kwa vile muda ulikuwa umekwenda sana hivyo wagonjwa kwa muda ule hawakutakiwa kuamshwa.
Kauli ile sikukubaliana nayo nilijua kuwa ni ya kunifariji lakini mama na mke wangu walikuwa wamefariki. Nilijikuta nikiangua kilio mbele ya daktari wa zamu na wauguzi kitu kilichowafanya wanishangae.
“Sasa unalia nini wakati tumekueleza uje kesho?” daktari wa zamu aliniuliza huku akionesha kunishangaa.
“Nije kesho kufanya nini ikiwa mama na mke wangu wamesha fariki?”
“Jamani mbona haya makubwa! Tumekwambia wapo salama ila sasa hivi wamelala. Kutokana na hali waliyokuja nayo ya nusu wafu tumewaacha kuangalia afya zao kwanza, bila hivyo ungewakuta nyumbani.”
“Si kweli, wamekufa ila mnanificha,” niliendelea kulia huku nimekaa chini.
“Kaka hakuna aliyekufa hebu ngoja tukawaamshe uwaone ili uridhike japokuwa si sheria kumuamsha mgonjwa aliyetulia kwa ajili ya mtu kumuona tu.”
Kauli ile ilinifanya ninyamaze kidogo, baada ya muda niliitwa na kuingia wadini. Sikuamini nilikutana na mama na mke wangu wapo kwenye hali nzuri kabisa.
“Umeamini?” daktari aliniuliza.
“Hapa nimeamini, mara nyingi mtu akiingia ICU huwa hatoki salama.”
“Haya baba waache wagonjwa wapumzike njoo kesho.”
Niliagana na wagonjwa wangu na kurudi nyumbani nikiwa na maswali mengi kuhusiana hali iliyowatokea. Nilikumbuka maneno niliyoelezwa na mzee Ngugude kuwa kuna hali itatokea na kuwatisha watu, ni ya kuyabadili mauti kurudi katika uhai.
MWANZO sikuelewa kutokana na kuchanganyikiwa, niliamini nilichoelezwa ndicho kilichotokea.
Baada ya siku mbili walitoka hospitali wakiwa wazima wa afya. Kitendo kile kilinifanya nibadili mawazo na kuona hakuna haja ya kuendeleza vita ya kisasi. Niliyakumbuka maneno ya marehemu baba kuwa hakuna mwanadamu mwenye uwezo kama Mungu hivyo tulitakiwa kumuabudu yeye.
Alinieleza kwa dini yake kisasi ni haki lakini kusamehe ni bora zaidi. Niliamini ule ulikuwa wakati wa mimi kujikabidhi kwa muumba ili nizaliwe upya. Niliendelea na shughuli zangu kama kawaida huku nikiwa nimejifunza vitu vingi katika maisha yangu.
Niliamini hakuna vita ndogo pia moto hauzimwi na mafuta. Siku zote tulihusiwa kusamehe ili kurudisha amani, pia unapolipa jema kwa baya, ubaya hukosa nafasi lakini ukilipa baya kwa baya vita yake haina mwisho. Nilijifunza kitu kimoja kikubwa kuhusu mwanadamu kuingilia kazi ya Mungu, kuua ni kazi ya Mungu kuingilia kazi hiyo ni kujiingiza kwenye dhambi ya kujitakia. Uwezo wa kuumba na kuua ni wake yeye peke yake. Hata unayemuua ukimwacha lazima atakufa tu kwa nini umuue?
Nina imani wengi mmesoma mkasa wangu tokea mwanzo mpaka leo nilipofikia tamati, napenda kuwaomba wote tusikimbilie kuua au kumroga mtu kwa ajili ya mwanamke kwa vile mke au mume bora hutoka kwa Mungu si kwa mapenzi ya mwanadamu.
Kama mwanamke si muaminifu mkanye kama ukishindwa mwache au mtenge, lakini usiue kwa ajili yake. Japo wengi tunaamini waganga wa asili ni wabaya, lakini kama watatokea waganga kama mzee Ngugude dunia itakuwa salama.
Namalizia kwa waganga wa asili, jina lenu linaweza kuwa baya kwa watu kutokana na kuonekana nyie ndiyo chanzo cha matatizo kati ya mtu na jirani yake hata familia kwa familia.
Mganga siku zote anatibu, anayeua au kumroga mtu huyo ni mchawi ni makosa kumwita mganga. Basi chagueni moja kuwa wachawi au waganga. Namalizia kwa kumuomba Mungu anisamehe kwa yote niliyoyafanya kwa ajili ya mke wangu, kwani niliishia kuwa mchawi kamili nilifikia hatua mbaya ya kuroga na kuua pia nilikuwa radhi hata kula nyama ya mtu kwa ajili ya mke wangu. Najua hukumu yake kwangu ni kubwa lakini kupitia ukurasa huu najutia kila nilichokifanya. Nakuombeni katika mkasa huu chukueni mazuri na mabaya muyaache kwa vile kusudio la kuutua mzigo mzito uliokaa moyoni mwangu ilikuwa kuhakikisha makosa yangu hayarudiwi na mtu mwingine.
Namalizia kwa kuwashukuru wote mliokuwa nami mwanzo hadi mwisho wa mkasa huu Mungu awabariki, asanteni.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
MWISHO
0 comments:
Post a Comment