Simulizi : Michirizi Ya Damu
Sehemu Ya Tano (5)
Fareed hakujua mahali mwanaume huyo alipokuwa, ila aliambiwa kwamba angepewa maelezo yote kwani yale aliyopewa mara ya kwanza, yalibadilika kwani mtu huyo aliondoka Paris na hakukuwa na aliyejua kama alikwenda Monaco au Marseille.
Baada ya dakika hamsini akapigiwa simu na kuambiwa kwamba mwanaume huyo hakuwa hapo Paris bali alikuwa jijini Marseille katika Hoteli ya Melkizedeki ambapo alikuwa akilala huku kila siku akishiriki katika kikao cha matajiri.
Hilo halikuwa tatizo, haraka sana akaondoka hotelini alipokuwa, akachukua ndege na kuelekea Marseille ambapo ndipo aliambiwa mwanaume huyo alipokuwa. Njiani, alikuwa akimuomba Mungu afike salama kwani alikuwa na hasira kali, asingeweza kumuacha mwanaume huyo akaishi kwani alikuwa miongoni mwa watu waliotaka kumuua kwa nguvu zote.
Walichukua dakika arobaini na tano tu mpaka kufika jiji humo ambapo akateremka na kuchukuliwa kwa gari mpaka katika hoteli moja na kutulia huko. Ilipofika saa mbili usiku, wanaume wawili wakafika hotelini hapo na kuomba kuzungumza naye.
Hilo halikuwa tatizo, alipewa taarifa na Williams kwamba watu hao wangefika mahali hapo, na wao ndiyo ambao wangemwambia kuhusu Belleck ambaye hakujua alikuwa katika hoteli gani.
“Belleck yupo anakula raha, hivi tunavyoongea, keshokutwa anaondoka kurudi Marekani,” alisema mwanaume mmoja aliyejitambulisha kwa jina la De Leux.
“Sawa. Kingine?”
“Huwa anapenda sana kununua malaya mitaani! Tunajua sehemu ambayo hupenda kununua na pia tunajua hoteli anayokaa mpaka chumba alichokuwepo,” alisema De Leux.
“Haina shida! Ningependa nikutane naye na kufanya kazi yangu,” alisema Fareed.
Hakwenda huko kufanya jambo lolote zaidi ya kumuua bilionea huyo na kuondoka zake. Wanaume hao wawili ndiyo walikuwa wachora ramani wakubwa, walikuwa wakienda hotelini hapo, wanaonana na wahudumu wa hapo, wakatengeneza urafiki wa kizushi kwa ajili ya kuwasaidia hapo baadaye.
Hawakujua kama lengo la watu hao ni kumpata mwanaume aliyekuwa ndani ya hoteli hiyo. Wakati mwingine walikuwa wakikaa mapokezini, Belleck alipokuwa akiingia ndani ya hoteli ile na machangudoa walikuwa wakimuona hivyo kuwa kazi nyepesi kwao kufanya kile walichokuwa wakikitaka.
“Cha kwanza ni kupata kadi ya kufungua vyumba vyote,” alisema De Leux.
Hilo ndilo lililotakiwa, kwa kutumia uzoefu mkubwa wa kuzungumza waliokuwa nao, wakajenga ukaribu zaidi na mhudumu aliyeitwa kwa jina la Natalie ambaye bila tatizo lolote lile, naye akaukaribisha ukaribu huo na mwisho wa siku De Leux kumtongoza.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Acha masihara wewe! Mzuri mimi?” aliuliza Natalie huku akitabasamu, japokuwa alipinga kwamba hakuwa mzuri lakini sifa zile zilimfurahisha.
“Wewe ni mzuri sana. Una tabasamu pana, msichana mrembo sana! Umeumbinka kama Mona Liza,” alisema De Leux huku akimwangalia Natalie kwa macho ya nipe nikupe.
Akamsifia usiku mzima, msichana huyo akachanganyikiwa, kila wakati akawa anapandisha juu mpaka katika chumba alichokuwa akilala De Leux na kuingia ndani. Hakutaka kufanya mapenzi na msichana huyo, kitu muhimu kilikuwa ni kuweka ukaribu na mwisho wa siku kuichukua kadi ambayo alikuwa akiitaka mno.
Wakati walipokwenda kuonana na Fareed, walimwambia kabisa kile kilichokuwa kimetokea kwamba kulikuwa na kadi moja muhimu ambayo ingewawezesha wao kuingia ndani ya chumba chochote kile.
Fareed akafurahi kwani urahisi huo ndiyo aliokuwa akiutaka kwa hali na mali. Siku hiyo wakaondoka na kwenda katika hoteli hiyo. Wakachukua chumba kwa ajili ya Fareed ambaye akaingia bila tatizo na uzembe mkubwa ambao waliufanya wahudumu wa hoteli hiyo ni kutokuishikilia passport yake.
Akaingia mpaka chumbani, akajipumzisha na kuambiwa kwamba mtu aliyetakiwa kumuua alikuwa njiani kufika mahali hapo hivyo alitakiwa kusubiri.
De Leux na mwenzake wakarudi mapokezi, wakatulia kochini. Ilipofika saa sita usiku, wakamuona Belleck akirudi hotelini hapo huku akiwa na mwanamke ambaye alivalia hijabu ila kwa nyuma alijazia hasa kiasi kwamba hata wao walipokuwa wakimwangalia walimtamani kupita kawaida.
“Huyo hapo! Subiri!” alisema De Leux.
Wakati mwanaume huyo akiingia ndani na mwanamke huyo, De Leux akamuita Natalie na kuanza kuongea naye. Alimwambia wazi kwamba siku hiyo alitaka kukaa naye na kuzungumza naye mambo mengi lakini iwe baada ya kufanya usafi katika vyumba mbalimbali.
“Haina shida mpenzi! Nitakuja,” alisema Natalie huku akionekana kuwa na furaha tele.
De Leux akaondoka na mwenzake mpaka chumbani kwake, wakakaa huko na kuyapanga kwamba siku hiyo ndiyo ilikuwa mwisho wa mtu huyo ambaye alikuwa adui wa bosi wao kwa kipindi kirefu.
Wakamfuata Fareed na kumwambia kilichokuwa kikiendelea kwamba ni yeye tu ndiye aliyekuwa akisubiriwa kufanya mauaji hayo.
“Haina tatizo!”
“Sawa. Ngoja nimuite huyu msichana alete kadi,” alisema De Leux na hapohapo kuchukua simu ya mezani na kupiga mapokezi ambapo alimtaka Natalie aende huko kuchukua shuka kwenda kulifua.
Msichana huyo hakuchelea, baada ya dakika kadhaa, akawa ndani ya chumba hicho. Alijua fika kwamba hakuitwa kwa ajili ya kubadilisha shuka bali aliitwa kwa sababu kulikuwa na kitu kingine.
Alivaa kimitego na hata alipoingia ndani ya chumba hicho, kitu cha kwanza kabisa ni kuipandisha sketi yake kwa juu, upaja wake ukaonekana, kidogo De Leux akatetemeka.
“Mmh! Leo hatoki!” alijisemea huku akimwangalia msichana huyo kwa matamanio makubwa. Ila akili yake haikuhama kutoka kwenye kadi ile. Ilikuwa ni lazima aipate na kumpelekea Fareed ambaye angefanya kazi hiyo aliyokuwa ameifuata nchini Ufaransa.
Huo ndiyo ulikuwa muda wa kukamilisha alichokuwa akikitaka. Alimwangalia Natalie kwa macho yaliyomaanisha kwamba alimtaka sana kitandani hapo. Msichana huyo pasipo kugundua kwamba kila kitu kilichofanyika kilikuwa ni maigizo, akaanza kumfuata mwanaume huyo.
Hatua zake zilikuwa za taratibu, za mahaba zilizoashiria kwamba alimuhitaji sana De Leux, mwanaume huyo akasimama na kumsogelea, alipomfikia, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kuuwahi mdomo wake na kuanza kubadilishana mate.
Zoezi hilo liliambatanisha na kushikana hapa na pale. Wakati yote yakiendelea, akili ya De Leux ilikuwa kwenye kadi aliyokuwa nayo msichana huyo, hakutaka kupoteza lengo lake kwani aliamini kwamba kama asingefanikisha suala hilo muda huo basi kazi waliyokuwa wakiitaka isingeweza kufanyika.
Wakapelekana mpaka kitandani, wakavuana nguo na kuendelea na zoezi lao. Miguno ya kimahaba ilikuwa ikisikika kila kona na baada ya muda fulani, sauti zile ziliongezeka zaidi.
Kulikuwa na mwanga hafifu, Natalie alichanganyikiwa, muda wote wakati mwanaume huyo alipokuwa juu yake, aliyafumba macho yake, hisia za raha zilikwenda mpaka kwenye ubongo wake, zikamchanganya kiasi kwamba akaona hakukuwa na kitu kilichokuwa na raha duniani kama hicho kilichokuwa kikiendelea kitandani hapo.
De Leux akachukua nafasi hiyohiyo kupekua katika mifuko ya msichana huyo, alichokuwa akikitaka ni kadi iliyokuwa na uwezo wa kufungua milango yote, hilo wala halikuwa zoezi gumu kwani ndani ya sekunde chache, tayari alikuwa na kadi hiyo mkononi mwake.
Akaificha kwenye mfuko wa suruali yake, alipomaliza kufanya mapenzi na msichana huyo, wakabaki wamelala huku wakivuta raundi ya pili iendelee. Muda wote Natalie alikuwa akifikiria ngono, kilipita kipindi kirefu pasipo kufanya mchezo huo na ndiyo maana alipoambiwa aende chumbani kwa mwanaume huyo, hakutaka kujiuliza, haraka sana akaenda tena huku akiwa amejiandaa kikamilifu.
“Una pumzi sana,” alisema natalie huku akiupeleka mkono wake chini ya kiuno cha De Leux.
“Kweli?”
“Yeah! Sijawahi kukutana na mwanaume mwenye pumzi kama wewe. Halafu unajua, kuna wakati nilihisi kama unataka kunivunja kwa jinsi ulivyokuwa ukinikunja,” alisema msichana huyo huku mkono ule ukiwa kulekule.
“Pole sana jamani! Ila nataka tuendelee!”
“Wewe tu! Mimi nipo tayari!” alisema De Leux.
Hata kabla hawajaendelea, De Leux akasimama na kumwambia Natalie kwamba alitaka kwenda kumuona rafiki yake kwamba ikiwezekana asimpigie simu asubuhi sana kwani ilikuwa ni lazima alale na msichana huyo ambaye kwa siku inayofuatia ilikuwa ni ya mapumziko kwake.
Hilo halikuwa na tatizo, akaruhusiwa na kuondoka huku akiwa na kadi ile mkononi. Alipofika katika chumba cha rafiki yake, akagonga mlango, ulipofunguliwa, akampa kadi na kumwambia ampe Fareed ambaye alitakiwa kukamilisha kazi ya mauaji na kuondoka hotelini hapo.
Hilo halikuwa tatizo, kadi ikachukuliwa, De Leux akarudi chumbani kwake kuendelea kufanya mapenzi na msichana huyo. Huku nyuma, rafiki yake akampelekea kadi ile Fareed ambaye aliichukua na kuufuata mlango wa chumba kile.
Fareed hakuwa mikono mitupu, alikuwa na kisu pamoja na dawa kali ya usingizi ya Microphenon ambayo ilikuwa ikitumika sana katika vyumba vya upasuaji. Alipoulikia mlango ule, akaingiza kadi, mlango ukafunguka, akaingia ndani.
Belleck na mpenzi wake walikuwa wamelala, kabla ya kufanya chochote, akaanza kupulizia dawa ile ya usingizi ambapo baada ya kuwaingia wote wawili, wakapitiwa na usingizi mzito, tofauti na ule waliokuwa nao.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kwa haraka sana Fareed akamfuata Belleck pale alipokuwa, akamshusha na kumuweka sakafuni, akanza kumchomachoma visu vya tumbo. Damu zilitoka lakini hakujali, alichoma mara kadhaa, akauacha mwili wa mwanaume huyo chini na kuuburuza kidogo hali iliyoifanya damu ile kutengeneza michizrizi sakafuni pale.
Hakutaka kuondoka hivihivi, akachukua kalamu na karatasi kisha kuandika maneno mafupi yaliyosomeka C'est fait yakiwa na maana ya kukamilika kwa jambo au ‘done’ kwa Lugha ya Kiingereza.
Fareed hakutaka kubaki ndani ya chumba hicho, kwa haraka sana akatoka na kuelekea chumbani kwa rafiki yake, De Leux ambapo akampa ile kadi na yeye kuichukua na kumpeleka mwanaume huyo ambaye bado alikuwa akiserebuka na msichana yule chumbani kwake.
Alipopiga hodi tu, De Leux akafungua mlango, akapewa kadi ile na kisha kurudi kitandani. Mpaka mambo hayo yote yanafanyika, Natalie hakujua kitu chochote kile, alichukulia kawaida, hakujua kama mwanaume huyo alichukua kadi na kwenda kufanya mauaji ndani ya chumba kimoja humo.
Williams akapewa taarifa kwamba kila kitu kilichotakiwa kufanyika, kilifanyika. Moyo wake ulikuwa na furaha kwani hakukuwa na mtu aliyekuwa akimchukia kipindi hicho kama alivyokuwa Belleck. Akampa pongezi zake, hakutaka kuchelewa, kwa kuwa alimuaidi kumpa kiasi cha dola milioni kumi, haraka sana akamuhamishia kiasi hicho mpaka kwenye akaunti yake kwa mategemeo kwamba kama atamuua basi kiasi kile kingeweza kuchukuliwa kirahisi ndani ya saa arobaini na nane.
Ilipofika asubuhi, hawakutaka kuendelea kukaa ndani ya hoteli hiyo, muda wao ulikuwa umefika na hivyo wote kuondoka hotelini humo. Safari yao ilikuwa ni uwanja wa ndege, tayari rubani alikuwa ameandaliwa na alikuwa na taarifa kwamba ilikuwa ni lazima warudi kuelekea nchini Marekani.
Walipofika uwanja wa ndege, wakapanda ndege na safari ya kurudi nchini Marekani ikianza. Huko, Williams akamtumia ujumbe mfupi De Leux kwamba Fareed hakutakiwa kufika nchini Marekani salama, ilikuwa ni lazima auawe njiani na kutupwa katika Bahari ya Atlantiki kitu ambacho kwa mwanaume huyo, jinsi alivyokuwa na ubavu, hilo halikuwa na tatizo lolote lile.
“No problem,” (hakuna tatizo) alijibu De Leux huku akiachia tabasamu. Wakati huo ndege ilikuwa njiani, ndiyo kwanza ilikuwa ikielekea katika anga ya bahari hiyo ambapo mauaji yalitakiwa kufanyika ndani ya ndege. Alichokifanya ni kuwaambia wenzake kwamba piga ua mwanaume huyo alitakiwa kuuawa ili kuficha siri.
Hali ya hewa ilibadilika ghafla, mawingu mazito yakaanza kujikusanya angani kumaanisha kwamba mvua kubwa ingenyesha muda mfupi ujao. Kila mtu alikuwa na hofu kwamba mvua ya siku hiyo ingekuwa kubwa kuliko zote ambazo ziliwahi kutokea nchini Ufaransa.
Watu wa idara ya hali ya hewa nchini Ufaransa walitoa angalizo kabla kwamba siku hiyo mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali ingeweza kunyesha hivyo watu wote walitakiwa kujiandaa.
Miungurumo ya radi ilikuwa ikisikika kila kona, watu wengi waliogopa na kujifungia ndani. Kabla ya mvua hiyo kuanza kunyesha, upepo mkali ukaanza kuvuma. Ulikuwa mkubwa uliosababisha maafa makubwa kiasi kwamba wengine wakasema kwamba upepo kama huo mara ya mwisho ulivuma mwaka 1956 ambapo uliacha madhara makubwa kwa watu kufa na mali nyingi kuharibiwa.
Watu wengi waliogopa, katika viwanja vya ndege, hazikuruhusiwa kupaa kwani hali ilitisha sana na hata kwa ndege ambazo ziliondoka, kila mmoja alikuwa na hofu kwamba zingeweza kuanguka na kulipuka.
Miongoni mwa ndege zilizoondoka ilikuwa ile ndogo binafsi aliyokuwa Fareed na wenzake. Walipanga kumuua ndani ya ndege lakini kabla ya kufanya kile walichoambiwa wakifanye, ndege ikaanza kuyumba huku na kule.
Upepo ulikuwa mkali mno, rubani aliyekuwa akiiendesha ndege ile alichanganyikiwa, alijitahidi sana kuiweka sawa lakini ilishindikana kabisa. Ilikuwa katika usawa wa bahari, upepo mkali uliendelea kuvuma huku mawingu yakiwa yametanda kila kona. Wote wakajua kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wao na hivyo ilikuwa ni lazima wajiokoe.
“Tunakufa…” alisema De Leux huku akionekana kuchanganyikiwa, hata wazo la kumuua Fareed likapotea.
Akaanza kuelekea mpaka kule alipokuwa rubani, akamuuliza juu ya hali iliyokuwa ikiendelea, akamwambia kwamba walikuwa usawa wa bahari, mita mia moja na ilikuwa ngumu kurudi kwani yeye mwenyewe alishindwa kabisa kuiweka sawa ndege hiyo.
“Kwa hiyo?”
“Hatujui tufanye nini! Tusalini sala zetu za mwisho!” alisema rubani, hakuona kama wangeweza kupona kutokana na hali iliyokuwa ikiendelea mahali hapo.
Hakukuwa na mtu aliyejiona kuwa salama, kila mmoja aliona kuwa huo ndiyo ungekuwa mwisho wake. Wakachukua maparachuti yaliyokuwa katika viti vyao kwa ajili ya kurukia baharini ambapo kulionekana kuwa salama kwa maisha yao.
Nje, hakukuwa na mwanga wa kutosha, mawingi mazito yalitanda na upepo mkali uliendelea kuvuma kama kawaida. Chini, hawakuona kitu kwani mawingu yale yalianza kushuka chini kutokana na upepo huo uliokuwa ukiendelea kuvuma kama kawaida.
“Let’s jump,” (turuke) alisema De Leux huku akimwangalia mwenzake, tayari maparachuti yalikuwa migongoni mwao.
“What about me?” (na mimi je?) aliuliza Fareed.
Hawakumjibu kitu chochote zaidi ya kumwangalia. Wakaufungua mlango wa ndege na kutokana na upepo mkali uliokuwa ukiendelea kuvuma, hali ikawa mbaya zaidi, ndege ikayumbishwa kupita kawaida, De Leux na mwenzake wakaruka na maparachuti yale kuelekea chini huku wakimwacha Fareed akiwa na rubani wa ndege ile.
Alichanganyikiwa, hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya, alitamani kuruka lakini alishindwa kufanya hivyo. Haraka sana akamfuata rubani na kuanza kuzungumza naye, alimwambia kwamba lengo lake lilikuwa ni kuruka kwani vinginevyo ndege ile ingepata ajali na kufa humo.
Akamtaka kushusha ndege, kutoka kwenye umbali wa mita mia moja mpaka hamsini ili aweze kujirusha baharini. Kwanza rubani akaogopa, aliijua bahari hiyo, ilikuwa hatari kuliko bahari nyingine kwani baridi lililokuwa likipiga humo, lilikuwa kubwa na ndiyo bahari ileile iliyoua watu katika meli ya Titanic miaka hiyo ya nyuma.
“It’s impossible! You can’t jump,” (haiwezekani! Huwezi kuruka) alisema rubani yule huku akimwangalia Fareed.
Fareed hakutaka kuelewa, alichokitaka kilikuwa ni kuyaokoa maisha yake kutoka katika ndege ile. Alimwangalia rubani, aliangalia mbele ya ndege ile, ni kweli kulikuwa na upepo mkali na mawingu mazito yalitanda kiasi kwamba ilikuwa vigumu sana kuona mbele.
Aliendelea kumwambia rubani yule ashushe ndege kwa kiasi fulani ili aweze kuruka. Baada ya kubembelezwa sana hatimaye rubani huyo akaishusha ndege hiyo kwa umbali wa mita hamsini kisha kumruhusu Fraeed kuruka.
“Una parachuti?” aliuliza rubani.
“Hapana!”
“Boya!”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/-
“Hapana!”
“Hebu subiri!” alisema rubani huyo.
Akaangalia chini ya kiti chake, akaona boya la kuvaa na kumwambia Fareed alivae kwani hapo alipokuwa akirukia palionekana kuwa sehemu ya hatri sana. Hilo halikuwa tatizo, akalichukua boya hiyo, akalivaa, akaufungua mlango na kisha kuruka baharini.
Alikuwa kwenye hali mbaya, wakati mwingine alishindwa kuhema vizuri kutokana na upepo mkali uliokuwa ukiendelea kuvuma. Baada ya sekunde chache akatumbukia ndani ya maji.
Bahari ilichafuka, kulikuwa na mawimbi makubwa yaliyopiga huku na kule. Fareed alipelekwa huku na kule, hakutulia baharini pale, kitu kilichokuwa kikimsaidia kilikuwa ni lile boya tu alilokuwa amelivaa.
Ilikuwa ni mchana lakini kitu cha ajabu, kulionekana kama jioni, hakuweza kuona hata mita kumi na tano kutoka pale alipokuwa. Alikiona kifo, mawimbi makubwa yaliendelea kumpiga na kumpeleka huku na kule mpaka kuona kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wake.
“Mungu nisaidie,” alisema Fareed huku mawimbi yakiendelea kumpeleka huku na kule.
****
Bilionea Belleck alikuwa kwenye kiti chake ofisini kwake, masikio yake yalikuwa kwenye simu yake iliyokuwa mezani. Alikuwa na presha kubwa, alitaka kuona simu kutoka kwa De Leux ikiingia na kumpa taarifa kwamba tayari walifanya mauaji ya Fareed ili moyo wake uridhike.
Muda ulizidi kusonga mbele, dakika ziliendelea kukatika lakini hakukuwa na taarifa yoyote ile. Moyoni mwake akawa na hofu, akahisi kabisa kwamba watu hao walishindwa kumuua au kulikuwa na tatizo jingine ambalo lilitokea.
Aliwaambia kwamba walitakiwa kufanya mauaji hayo haraka sana baada ya ndege kupaa lakini kitu cha ajabu kabisa hakukuwa na simu iliyoingia kumpa taarifa hiyo ambayo aliamini kwamba ingeufanya moyo wake kumtukuza Mungu kwa hicho kilichotokea.
Baada ya kupita saa mbili, akaamua kumpigia mwanaume huyo ili kujua ni kitu gani kiliendelea. Simu haikuwa ikipatikana, ilionekana kuzimwa kitu kilichomuudhi sana Belleck kwa kuona kwamba amedharauliwa.
Alichokifanya ni kumtumia ujumbe wa sauti (voice mail) ili atakapoiwasha simu yake aweze kuipata sauti hiyo na kumwambia kitu kilichokuwa kimeendelea.
“Kitu gani kinaendelea? Kwa nini umekuwa kimya sana? Mmekamisha au bado hamjakamilisha? Hebu ukifungua simu nitafute nijue manake nilishatuma pesa, kama amekufa niambie nizitoe pesa kabla hajathibitisha kuzipata,” alisema Belleck huku simu ikiwa sikioni mwake.
Moyo wake haukuwa na amani hata kidogo, bado aliendelea kuwa na hofu kwamba inawezekana kulikuwa na jambo lililokuwa limetokea huko. Hakutulia, moyo wake ulikuwa na shaka tele kwa kuona kwamba kama Fareed hakuuawa basi kile kiasi alichokuwa amemtumia, kingeweza kuondoka mikononi mwake jumla kama tu mwanaume huyo angethibitisha kukipokea ndani ya siku saba.
Alitaka afe haraka iwezekanavyo! Alifanya kazi aliyoitaka, mtu aliyetakiwa kuuawa aliuawa hivyo alichokuwa akikiangalia kwa sasa ni kupewa taarifa kwamba kazi ile ilifanyika.
Siku ya kwanza ikapita, ukimya ukatawala, siku ya pili nayo ikapita, ukimya ukatawala, siku ya tatu na nne nazo zikaingia lakini hakukuwa na taarifa yotoye ile kama Fareed aliuawa au la, mbaya zaidi hata alipokuwa akimpigia simu rubani, naye hakuwa akipatikana.
Fareed alikuwa akielea juu ya maji, alipelekwa kila kona na kitu kilichokuwa kikimsaidia asizame ni lile boya alilokuwa amelivaa. Aliendelea kuelea mpaka bahari ilipotulia, akaangalia huku na kule na kwa mbali sana akafanikiwa kukiona kisiwa kimoja, hakikuwa kikubwa sana, kilikuwa kidogo hivyo kuanza kupiga mbizi kuelekea kule.
Alichoka, maji yalimchosha, yalimpeleka huku na kule, mikono yote alihisi ikiuma kupita kawaida. Japokuwa kisiwa kile kilionekana kuwa kama umbali wa nusu kilometa lakini alitumia dakika arobaini na tano mpaka kukifikia.
Kilikuwa kisiwa kilichokuwa na miti mingi, hakujua kilikuwa nchi gani lakini kwa jinsi kilivyoonekana, hakukuwa na mtu yeyote aliyekuwa akiishi humo. Akazunguka huku na kule, aliogopa, moyoni mwake alihisi kama angekutana na watu wabaya, au wala wala watu waliokuwa wakipatikana katika nchi nyingine lakini kwa bahati nzuri kwake hakuweza kukutana na mtu yeyote yule.
Alitafuta sehemu chini ya mti na kutulia, macho yake yalikuwa yakiangalia huku na kule kutafuta msaada, pale alipokuwa ilikuwa ni sawa na mtu aliyetengwa, kila kona alipoangalia, hakuona kitu au mtu yeyote yule zaidi ya kisiwa kile kuzungukwa na bahari kila upande.
Alihisi baridi, hicho kilikuwa kisiwa kilichokuwa katika Bahari ya Atlantiki, moja ya bahari zilizokuwa na baridi kali. Alibaki akitetemeka pale alipokuwa kiasi kwamba mpaka akahisi kuwa muda wowote ule angeweza kufa.
Alitulia kwa saa moja, hakuona msaada wowote ule zaidi ya maji yale yaliyokuwa yamezunguka kisiwa kile. Alikaa mpaka usiku, giza likaingia, hakuwa na sehemu salama ya kulala zaidi ya mtini, tena huku akiangalia huku na kule.
Usiku mzima alikesha macho, moyo wake ulimwambia kwamba kungekuwa na msaada kutoka mahali fulani lakini kitu cha kushangaza mpaka inafika asubuhi hakukuwa na msaada wowote ule alioweza kuupata kitu kilichomfanya kukosa tumaini la kuondoka kisiwani hapo.
“Inamaana ndiyo nitakufa hapa?” alijiuliza huku akiangalia huku na kule.
“Labda! Lakini haiwezekani hata kidogo! Siwezi kufa kirahisi namna hii,” alijisemea huku akiteremka kutoka mtini.
Siku hiyo alishinda katika kisiwa hicho, alipokuwa akisikia njaa, aliingia katika pori lililokuwa kisiwani hapo, akachuma makomamanga na kuanza kula. Hayo ndiyo yakawa maisha yake, alipata tabu mno kisiwani humo, alitamani kuondoka lakini ilishindikana kwa kuwa tu hakukuwa na msaada wowote uliotokea.
Alidhamiria kurudi nchini Marekani, ilikuwa ni lazima kwenda kukamilisha kazi aliyokuwa ameiacha. Aliwaua watu wawili ambao walidiriki kumuondoa duniani lakini kutokana na ujanja wake, akanusurika kufa.
Hakutaka kuwaacha watu hao, akawaua na hivyo kubaki mtu mmoja ambaye alikuwa Padri Luke. Naye ilikuwa ni lazima amuue kwa kile alichomfanyia. Moyo wake haukujisikia hukumu wala huzuni, alichokuwa akikihitaji ni kuhakikisha mwanaume huyo anakufa kama walivyokufa wenzake.
Muda ulizidi kwenda mbele, alishindia makomamanga, hakuweza kupata chakula kingine zaidi ya hicho. Aliendelea kuishi kwa mateso makubwa, kila siku akawa anapigwa na baridi kali, alihuzunika mno, aliumia moyoni mwake na wakati mwingine alihisi kwamba huko ndipo ambapo kungekuwa nyumbani kwake milele, hakuona kama angeweza kuondoka mahali hapo salama.
Kila wakati ilikuwa ni lazima kuangalia huku na kule, alitaka kuona kama angebahatika kuona meli yoyote ile ili aweze kuomba msaada lakini hilo halikuwezekana, kila kona alipoangalia aliona kuwa peupe.
“Mungu wangu! Ni nini hiki?” Fareed alishtuka, ghafla tu akaanza kusikia maumivu makali ya tumbo, hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea tumboni mwake, akalishikilia tumbo lake vilivyo, alisikia maumivu mahali ambayo hakuwahi kuyasikia kabla.
Akaanza kusikia kichefuchefu na kuanza kukohoa, madonge ya damu yakaanza kumtoka mdomoni, alishindwa kuvumilia, akalala chini na kuanza kulia. Hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea,
Hakupata msaada wowote ule ule. Baada ya dakika kadhaa, akaanza kutapika, madonge makubwa ya damu yakaanza kutoka. Akahisi kwamba yale matunda ndiyo yaliyokuwa yakimsababishia hali hiyo na kuanza kujitahidi kuyatema.
“Mungu nisaidie,” alisema Fareed huku akiwa kwenye hali mbaya, kwa jinsi tumbo lile lilivyoanza kuuma ghafla, akahisi kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wake.
****CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mauaji ya Bwana Belleck yaliyokuwa yametokea nchini Ufaransa yalimshtua kila mtu, watu hawakuamini kile kilichokuwa kimetokea, ni ndani ya siku tatu mabilionea wawili walikuwa wameuawa na kwa jinsi alama za mauaji zilivyokuwa zikionyesha, kila mtu akagundua kwamba muuaji alikuwa mmoja.
Polisi walichanganyikiwa, wakawasiliana na polisi wa nchini Misri na kuwaomba kuwatumia picha ya mtuhumiwa, hilo halikuwa tatizo, picha ikatumwa na ilipowafikia, wao wenyewe walishangaa.
Alikuwa mtu yuleyule aliyekuwa akitafutwa sana na FBI kwa kosa la kulipua kituo cha treni cha Pennsylvania. Hawakujua sababu ya mwanaume huyo kufanya matukio yote hayo. Wengi walihisi kwamba alikuwa gaidi, lakini gaidi na mabilionea wale kulikuwa na kitu gani kilichokuwa kikiendelea?
Hakukuwa na aliyekuwa na majibu, kila mmoja alikuwa na hamu ya kumkamata Fareed na kuweka wazi kile kilichokuwa kikiendelea mpaka kufanya matukio yote hayo.
“Atafutwe kila kona, wekeni picha zake katika vituo vyote vya televisheni duniani, sambazeni kadiri mnavyoweza mpaka kuhakikisha huyu mtu anatiwa mikononi mwa poli,” aliagiza mkurugenzi wa FBI nchini Marekani, Bwana Sandal Peters.
Mawasiliano yakafanyika kwenda nchini Ufaransa, polisi wa huko hawakujua mahali alipokuwa mtu huyo hivyo kwenda hotelini kwa ajili ya kuangalia kamera za CCTV ambazo waliamini kwamba zilimnasa mwanaume huyo.
Hilo halikuwa tatizo, wakapata picha ya mwanaume huyo, wakafuatilia kumfahamu zaidi mtu huyo, picha zake zikasambazwa kwenda sehemu nyingine, walijua kwamba mwanaume huyo alivyokuwa ameingia nchini Ufaransa alipitia sehemu katika bandari au uwanja wa ndege hivyo kwenda huko.
Walitafuta kila kona, walichukua picha za wasafiri wote waliokuwa wameingia katika sehemu hizo lakini hawakufanikiwa kuipata picha yake. Walipohamia kwa watu walioingia humo kwa ndege binafsi wakafanikiwa kuipata picha ya mwanaume huyo, maelezo yalisema kwamba aliingia ndani ya nchi hiyo kwa kutumia ndege binafsi iliyokuwa ikimilikiwa na bilionea kutoka nchini Marekani, Peter Williams.
“Is this Williams’ jet?” (hii ni ndege ya Williams) aliuliza polisi mmoja.
“Yeah! Why did he do this?” (ndiyo hii! Kwa nini amefanya hiv?) aliuliza polisi mwingine.
“We don’t know! We have to arrest him,” (hatujui! Tumkamateni) alisema polisi huyo.
Kwa msaada wa interpool, Bwana Williams akakamatwa, akawa mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo ya mauaji yaliyotokea nchini Ufaransa. Na kwa sababu alikuwa amemsafirisha mtu aliyehusika katika ugaidi, akapewa kesi hiyo nyingine kwa kuwadhamini magaidi kulipua kituo cha treni cha Pennslyvania.
“Simfahamu kijana huyo,” alisema Williams wakati akiwa katika chumba cha mahojiano.
“Na alifikaje ndani ya ndege yako? Nani alimtafutia vibali? Kwa nini aliingia nchini Ufaransa kwa ndege yako na kuondoka kwa ndege yako?” yalikuwa maswali kadhaa ambayo alishindwa kuyajibu. Kila mtu akajua kwamba alihusika katika mauaji ya Bilionea Belleck lakini pia alihusika katika tukio la kigaidi lililotokea hapo Pennslyvania.
Fareed alikuwa akilia, maumivu ya tumbo yaliongezeka, alijua kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wake. Siku hiyo hakula kitu, hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea tumboni mwake. Mawazo yake yakamwambia kwamba yale matunda aliyokuwa akila ndiyo yaliyomsababishia hali ile.
Siku hiyo ilipita huku akiwa kwenye maumivu makali, aliumia kupita kawaida. Usiku hakulala, alikesha akilia kwa maumivu makali, aliendelea kukohoa na kutoa madonge ya damu.
Ilipofika majira ya saa tano asubuhi ndipo kwa mbali akaiona meli moja kubwa ikielekea kule alipokuwa. Hakuwa na nguvu za kutosha lakini akasimama na kuanza kupunga mikono yake juu huku akijitahidi kutoa sauti ili asaidiwe pale alipokuwa.
Hiyo ilionekana kuwa nafasi pekee ya yeye kuondoka kisiwani pale. Meli ile ikaendelea kusogea, kwa mbali akawaona watu kutoka kwenye meli ileile wakipunga mikono kuashiria kwamba walimuona.
Vijana wawili wakafungua mtumbwi uliokuwa katika meli yao na kisha kupanda, hapohapo wakaanza kuelekea kule alipokuwa Fareed kisiwani ambapo baada ya kumfikia, wakaanza kumuuliza maswali kadhaa kuhusu sababu iliyomfanya kuwa mahali pale.
“Tumbo linauma…” alilalamika Fareed huku akilishika tumbo lake, hata maswali aliyoulizwa akashindwa kuyajibu kabisa.
Wakamchukua na kumpakiza ndani ya mtumbwi na kuelekea naye kwenye meli ile. Alikuwa akiugulia kwa maumivu makali, wakati mwingine aliwaambia watu hao kwamba alikuwa akifa na kitu kilichomuuma zaidi ni kwamba alikuwa akifa hata kabla hajamuua padri Luke ambaye alimbaka badala ya kumuongoza sala ya toba alipokwenda kuungama kwenye kanisa lake.
Hiyo ilikuwa meli kubwa ya wavuvi waliokuwa wakivua samaki katika eneo la kimataifa, walitokea nchini Marekani na miaka mingi kazi yao ilikuwa hiyo, walishinda kwenye meli na ni mara chache sana walikuwa wakitoka na kwenda kuzurura sehemu mbalimbali.
Hawakujua kitu chochote kuhusu Fareed, wakati dunia ikimtafuta kwa mauaji aliyokuwa ameyafanya, wao hawakuwa na habari hata kidogo. Walimkaribisha katika meli yao, wakampa dawa ya tumbo na kuondoka naye.
Kidogo dawa hiyo ikampunguzia maumivu makali. Wakati meli ikiendelea kuvua kama kawaida, alichokuwa akikifikiria ni kutoroka mara baada ya meli kufika nchi kavu.
Fareed akapata nafuu, akawa muongeaji mkubwa, alitaka kuwazoea watu hao ili wasiwe na maswali mengi. Alipoulizwa kuhusu sababu iliyomfanya kuwa mahali pale, hakutaka kuwaambia ukweli, aliwadanganya kwa kuwaambia kwamba alikuwa akisafiri kwa meli na wezake, ghafla bahari ikachafuka, meli ikapasuka na maji kuingia, kilichoendelea ni meli hiyo kuzama.
Ilikuwa rahisi kumwamini kwa kila kitu alichokuwa akikiongea, alizungumza huku akionekana kumaanisha kile alichokuwa akikisema mbele yao. Sura yake ilivyokuwa, ilifanana na maneno aliyokuwa akizungumza hivyo kumwamini kwa asilimia mia moja.
Zoezi hilo la uvuaji liliendelea kwa siku kadhaa na ndipo wakarudi nchi kavu tayari kwa kuuza samaki wao waliokuwa wamewavua katika kipindi walichokuwemo huko.
Japokuwa walimzoea Fareed na waliahidi kumsaidia lakini baada ya meli kufika nchi kavu walishangaa kuona mtu huyo akiwa amewapotea katika mazingira ya kutatanisha. Hawakujua alikuwa wapi, walijaribu kumtafuta kila kona, mwanaume huyo hakuwepo kitu kilichowapa maswali mengi yasiyo na majibu.
Fareed alikuwa njiani akielekea kulipokuwa na mgahawa wa McDonald, alikuwa akitaka kula, kwa kiasi cha pesa alichokuwa nacho mfukoni mwake aliamini kingemsaidia.
Wakati akiwa kwenye mgahawa huo, akiwa ameagiza chakula ndipo macho yake yakatua katika televisheni ambapo kulikuwa na habari iliyokuwa ikizungumzia kuhusu kukamatwa kwa Bilionea Williams.
Alishangaa, alipoangalia sababu ya kukamatwa huko akaona ni kwamba alikuwa akihusika kushirikiana na magaidi katika kulipua kituo cha treni huko Pennsylvannia na pia alihusika kumtuma mtu kwenda kuwaua mabilionea wawili kwa kumtumia mtu aliyeonekana kwenye picha.
Fareed alipoangalia picha ile, alikuwa yeye, alionekana vilivyo alivyokuwa ameingia kwenye piramidi kwenda kumuua Bilionea Keith, alipoingia hotelini kumuua bilionea Bellck mpaka pale alipokuwa akikimbia katika kituo hicho cha treni.
Sura yake ikaanza kuwa maarufu, hapo mgahawani hakutaka kukaa sana, akasimama, akalipia na kisha kuondoka. Alijua fika kwamba ilikuwa ni lazima kukamatwa, hakutaka kuona akikamatwa pasipo kumuuua Padri Luke aliyekuwa amembaka, alitaka kumaliza kila kitu ili pale atakapokuja kukamatwa na kushtakiwa kifo basi afe akiwa na amani moyoni mwake.
“Ni lazima niende kanisani!” alisema Fareed.
Hakutaka kubaki mahali hapo, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kwenda katika kanisa hilo lililokuwa umbali wa kilometa mbili kutoka hapo alipokuwa. Akakodi teksi ambayo ikaanza kumpeleka huko.
Macho yake yalikuwa chini, aliogopa kuonekana na kugundulika, na hata alipokuwa ameongea na dereva wa teksi hiyo alikiinamisha kichwa chake chini.
Safari iliendelea mpaka alipofika kwenye kanisa hilo, akaingia. Kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma ndivyo ilivyokuwa kipindi hicho, kulikuwa na watu wachache sana kanisani humo, akaelekea mpaka katika sehemu ya kuungamia dhambi na kukaa tayari kwa kuzungumza na padri huyo ambaye ndani ya dakika chache, akaingia humo.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nimekuja kuungama dhambi zangu,” alisema Fareed huku akiangalia chini.
Padri Luke hakumgundua kwani alikuwa amebadilika, hakuwa kama vile alivyokuwa kipindi cha nyuma. Alizungumza naye kwa kirefu na kumwambia kwamba angerudi baadaye kwa ajili ya kuzungumza naye.
Akaondoka kanisani hapo, kitu cha kwanza alichokitafuta kilikuwa kisu, akafanikiwa kukinunua katika supamaketi ambayo haikuwa mbali kutoka hapo alipokuwa. Mwanaume aliyemuuzia ndani ya duka hilo alimwangalia kwa makini mno, sura yake haikuwa ngeni, ni kama aliwahi kumuona sehemu fulani.
Fareed akaogopa, akahisi kwamba mwanaume huyo aliliona tangazo la kutafutwa kwake hivyo alichokifanya ni kuondoka harakaharaka huku akiwa na kisu alichokinunua.
Alipofika kanisani, hakuingia katika mlango wa mbele, akapitia katika mlango wa nyuma, ule aliotolewa na padri yule, akafungua nati za kitas, akakitoa na kuingia ndani.
Kulikuwa na giza, akapiga hatua mpaka alipoufikia mlango mwingine ambao ulikuwa ni wa nyuma kuingia katika ofisi ya padri huyo. Akaingia na kutulia katika kochi moja. Padri hakuwepo, alikuwa katika chumba cha kuungamia dhambi akimsikiliza mtu mwingine.
Alikaa hapo kwa dakika ishirini, akamsikia padri huyo akija kule alipokuwa, haraka sana akaelekea nyuma ya mlango na kusimama, padri huyo akaingia. Hata kabla hajafanya kitu, akamkaba kwa nyuma, padri Luke akashindwa hata kupiga kelele, akajikuta akianza kulegea. Hapohapo Fareed akamuacha.
“Do you remember this face?” (unaikumbuka sura hii?) aliuliza Fareed huku akimwangalia padri Luke.
“Please! Don’t kill me,” (usiniue tafadhali) alisema padri huku akipiga magoti.
“Do you?” (unaikumbuka?)
“I saw you a while ago,” (nilikuona muda mfupi uliopita)
“Okey! I came to kill you,” (Sawa! Nimekuja kukuua) alisema Fareed huku akimwangalia padri huyo.
“I’ve done nothing! Please! Have mercy, I have done nothing,” (sijafanya lolote! Tafadhali nihurumie! Sifanya lolote) alisema Padri huyo huku akiwa amepiga magoti.
Fareed akaanza kumkumbusha padri huyo kila kitu kilichokuwa kimetokea kuhusu wao. Alianzia mbali, jinsi alivyokuwa ameathirika kwa vitendo vya kishoga mpaka kufikia hatua ya kwenda kanisani hapo kwa ajili ya kuungama dhambi zake.
Padri Luke akakumbuka, akamwangalia vizuri Fareed, akamkumbuka. Akazidi kulia na kuomba msamaha zaidi kwamba kile alichokifanya ni shetani tu ndiye aliyempitia.
Fareed hakutaka kumuelewa, hapohapo akamchukua na kuelekea naye ndani ya chumba kile cha kuungamia dhambi, kama alimfanyia vitendo hivyo ndani ya chumba kile basi alitaka kumuua ndani ya chumba hicho hicho.
Hakutaka kupoteza muda, hapohapo akamchoma visu vitatu tumboni na kifuani mwake, padri akaugulia kwa maumivu makali, akaanguka chini, akatoka damu nyingi na hapohapo Fareed kumburuza na kuacha michirizi ya damu pale sakafuni.
Hakuishia hapo, alitaka kuijulisha dunia kwamba yeye ndiye aliyefanya mauaji ya watu hao watatu hivyo kuchukua karatasi na kuuacha ujumbe uliosomeka C'est fait yakiwa na maana ya kukamilika kwa jambo au ‘done’ kwa Lugha ya Kiingereza. Hakutaka kupoteza muda, alipoona amekamilisha kila kitu, akaondoka mahali hapo haraka sana.
FBI walishindwa kujua ni kwa namna gani wangeweza kumpata muuaji wa mauaji hayo, walisambaza picha za Fareed kila kona lakini hawakuwa wamefanikiwa. Walijua kwamba kijana huyo alikuwa nchini Marekani lakini kitu cha ajabu kabisa hawakuweza kumuona.
Walichokifanya ni kuweka dau kwamba kwa mtu yeyote ambaye angefanikisha kupatikana kwake basi angezawadia zawadi nono ya dola elfu hamsini, zaidi ya milioni mia moja lakini napo zoezi hilo likaonekana kuwa gumu.
Watu ambao walionekana kufanana nja Fareed walikamatwa na kupelekwa katika vituo vya polisi, kila mmoja alikuwa na uchungu wa kupata pesa hizo ambazo zilikuwa nyingi, pesa ambazo zingeweza kuwatoa katika hali waliyokuwa nayo na kuwapeleka sehemu nyingine kimaisha.
Siku zikakatika, hakukuwa na mtu aliyejua mahali mtu huyo alipokuwa. Walitoa taarifa katika hoteli zote hapo Marekani kuhakikisha kwamba mtu huyo anakamatwa mara baada ya kuingia hotelini lakini zoezi hilo lote lilionekana kuwa gumu kwani bado mtu huyo hakuwa amepatikana mpaka muda huo.
“Where the hell is he?” (yupo wapi?) aliuliza jamaa mmoja, kama walivyokuwa wenzake, hata yeye mwenyewe alikuwa amechanganyikiwa.
“I don’t know! Everyone wants to get the damn money bro,” (sijui! Kila mmoja anaitaka pesa kaka) alisema jamaa mwingine, walikuwa Wamarekani weusi ambao hata kwa kuwasikia jinsi Kiingereza chao walivyokuwa wakiongea, haikuwa ngumu kugundua kama walikuwa wao.
Wakati Marekani ikiendelea kusumbuka kumtafuta Fareed, katika nchi nyingine, zile zilizokuwa na uadui mkubwa na Marekani walikuwa na furaha mno. Walifurahi kuona nchi hiyo ikiwa imeshambuliwa na watu kadhaa kuuawa.
Nchini Urusi, mpaka watu wakawa wanashangilia baa, waliwachukia majirani zao hao na muda wowote ule walitamani kuona nchi hiyo ikipotea katika uso wa dunia.
Uarabuni, katika nchi mbalimbali watu walikuwa wakifurahia, kundi la kigaidi la Al Qaida lilijitangaza hadharani kwamba wao ndiyo walikuwa wamewatuma watu kupeleka mabomu na kulipua kituo hicho, kilichowashangaza ni sababu ya mtu wao mmoja kukimbia kwani lengo lilikuwa ni kuwaua wote.
Maelezo hayo kidogo yakawafanya Wamarekani kufikiria mara mbili kwamba inawezekana mwanaume huyo hakuwa na lengo la kuulipua kituo hicho bali alishinikizwa na watu kufanya hivyo. Walitaka kujua, kama kweli alilipua kituo hicho na kukimbia, ilikuwa ni lazima wamtafute na kumpata ili kujua ni wakina nani walikuwa wamemtuma kushambulia kituo hicho na kwa sababu gani alikuwa akikimbia.
Fareed alichukiwa lakini FBI walikuwa wakimuhitaji kwa nguvu zote. Waliendelea kutangaza dau nono kupatikana kwa mtu huyo lakini ilishindikana ila baada ya siku nne, wakapigiwa simu na kuambiwa kwamba mtu huyo alikuwa katika Hospitali ya Britania Medical Center iliyokuwa hapohapo Pennslyvania hivyo walitakiwa kwenda kumuona huko.
“Hospitali?” aliuliza ofisa mmoja wa FBI.
“Ndiyo! Tumeambiwa yupo huko, hizo ni taarifa za chini, twendeni,” alisema Thomson, mwanaume yuleyule aliyekuwa na jukumu kubwa la kumtafuta Fareed kwa tukio alilokuwa amelifanya.
Akawakusanya maofisa wenzake wanne na kuanza kuelekea huko. Ilikuwa ni lazima wawahi kwani walijua fika kwamba kama wangechelewa basi inawezekana wangekuta ametoroka kwani kwa mtu kama yeye ambaye alikuwa akitafutwa kila kona ilikuwa ni lazima kutoroka ili kujificha asikamatwe.
Hawakuchukua muda mrefu wakafika mahali hapo, haraka sana wakateremka na kuanza kuelekea ndani ya hospitali hiyo. Walitembea harakaharaka kama watu waliokuwa wakiwahi kitu fulani. Walipofika mapokezi, kwanza wakaambiwa kwamba kweli mtu huyo alikuwa hospitalini hapo, alifikishwa baada ya kukutwa barabarani akiwa hoi kwani tumbo lilikuwa likimsumbua.
“Safi sana, hebu tupeleke,” alisema Thomson na nesi kuanza kuwapeleka katika chumba alichokuwepo Fareed.
****
Moyo wake ulikuwa na furaha tele, kitendo cha kumuua Padri Luke kilimaanisha kwamba kile alichokuwa amekihitaji kwa kipindi kirefu hatimaye alikuwa amekifanikisha.
Akaondoka, kila alipopita alikutana na picha zake, alikuwa akitafutwa kila kona huku kiasi cha dola elfu hamsini kimewekwa kama zawadi kwa mtu yeyote ambaye angefanikisha kupatikana kwake.
Moyo wake ukaogopa lakini wakati mwingine hakuona kama kulikuwa na tatizo kaka tu angekamatwa na kufikishwa katika kituo cha polisi. Alikuwa na kiasi kikubwa cha pesa, mwanaume yule, bilionea Williams alikuwa amemuwekea kiasi kingine cha pesa, alijiona kuwa milionea mkubwa ambaye kama angefika nchini Tanzania basi maisha yake yangekuwa katika levo nyingine kabisa.
Hakuwa na pa kulala na aliogopa sana kwenda hotelini, alichokifanya ni kubaki barabarani hapohapo Pennsylvania na kulala na masikini waliokuwa mitaani. Alijisikia amani zaidi kulala humo kuliko hata kulala katika hoteli kubwa huku akiwa na hofu tele.
Alikuwa akijifikiria ni kwa namna gani angeweza kurudi nchini Tanzania. Hakuwa na kibali chochote, kila kitu kilipotea katika ndege ile na mbaya zaidi alishindwa kwenda hata ubalozini kwani kila kona alikuwa akitafutwa.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alilala mitaani na masikini, hakukuwa na mtu aliyejali, kila mmoja alikuwa na mambo yake, ilipofika siku ya nne huku akiwa mtaani na akiendelea kufanya harakati za kutafuta msaada wa siri kuuondoka nchini humo maumivu ya tumbo yakaanza tena.
Yalikuwa ni maumivu makali, alihisi tumbo lake kama likiungua moto, alitapika madonge makubwa ya damu, wakati mwingine mpaka kwenye makalio yake kulikuwa kukitoa damu hali iliyomuogopesha kupita kawaida.
Kilio chake cha maumivu ndicho kilichowashtua masikini waliokuwa mitaani, walipomfuata na kuona tatizo lake, wakaanza kumpeleka hospitalini huku akiwa hoi, kifua chake kilitapakaa damu kutokana na kukohoa madonge ya damu sana.
Akafikishwa katika Hospitali ya Britain Medical Center ambapo moja kwa moja akapelekwa katika chumba kimoja na kuanza kufanyiwa vipimo. Bado Fareed alikuwa akilia kwa maumivu makali, madaktari ambao walikuwa wakimwangalia hawakumgundua kama alikuwa Fareed, mwanaume aliyeua watu wengi kwa kuwalipua katika kituo cha treni.
Akafanyiwa vipimo na kugundulika kwamba alikuwa na kansa katika utumbo wake mkubwa.
Madaktari wakashangaa, hawakujua sababu iliyomfanya mtu huyo kupata tatizo hilo kubwa ambalo mara nyingi lilikuwa likiwapata watu wenye kula vitu vilivyokuwa na kemikali nyingi kupitiliza.
Walitaka kujua chanzo cha tatizo hilo, wakamwambia kwamba alitakiwa kuchunguzwa kwa ukaribu na kugundulika chanzo cha tatizo hilo ili wajue ni kwa namna gani wangeweza kumsaidia.
Uchunguzi ulifanyika kwa saa kadhaa na kugundua kwamba tatizo kubwa lilisababishwa na mapenzi ya jinsi moja aliyokuwa akiyafanya zamani. Kilichomletea matatizo ni mafuta ya vilainishi ambayo yalikuwa yakitumiwa na wanaume waliokuwa wakimuingilia kinyume na maumbile.
Mafuta yale vilainishi yalikuwa yakipenya moja kwa moja mpaka kwenye utumbo mkubwa na kuganda huko, utumbo ukaathiriwa na moja kwa moja kumletea tatizo ambalo lilisababisha utumbo huo kushambuliwa na virusi vilivyosababisha kansa.
Madaktari hawakutaka kumficha, walimwambia ukweli. Fareed alikuwa akilia, moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali, hakuamini kama mchezo ule mchafu aliokuwa ameucheza kwa kipindi kirefu ndiyo ungemletea matatizo hayo.
Hakutaka kufa, hakutaka kuona akiondoka duniani na wakati kulikuwa na mambo mengi ya kufanya. Alifanikiwa kwa kiasi kikubwa, alikuwa na pesa ambazo zilimfanya kuwa na maisha mazuri, leo hii, kwa mchezo uleule wa kufanya mapenzi na wanaume wenzake ukamletea matatizo makubwa kwa kupata kansa ya utumbo mkubwa ambao ndiyo uliunganishwa mpaka nyuma kulipopeleka haja kubwa.
Madaktari walihuzunika, walijua kwamba kwa lile lililokuwa likiendelea mwanaume huyo asingeweza kupona. Wakati wakiendelea kumuhudumia ndipo wakagundua kwamba mwanaume huyo ndiye yuleyule aliyekuwa akitafutwa na FBI kwa kosa la kulipua kituo cha treni na kuwaua mabilionea wawili.
Hawakutaka kumuonyeshea hali ya kugundua kilichokuwa kimetokea bali walichokifanya ni kumchoma sindano ya usingizi, alipolala, wakachukua simu na kuwapigia FBI na kuwaambia kwamba mtu aliyekuwa akitafutwa kwa udi na uvumba, walikuwa naye hospitalini hapo hivyo maofisa hao kuwaambia kwamba ndani ya dakika chache wangekuwa mahali hapo.
Fareed akayafumbua macho yake pale kitandani alipokuwa, alijikuta amezungukwa na watu waliokuwa na suti miilini mwao. Aliwashangaa, hakujua watu hao walikuwa wakifanya nini pale alipokuwa. Alipojaribu kuuinua mkono wake akakuta akiwa amepigwa pingu.
Thomson alikuwa na wenzake, nyuso zao zilikuwa kwenye tabasamu pana, kitendo cha kumpata kijana huyo kilimaanisha kwamba wangefanikiwa kujua mwanzo mpaka mwisho na sababu zilizomfanya kukishambulia kitu kile cha treni na kusababisha watu wengi kufariki dunia.
Hakuwajua watu hao, alijiuliza maswali mengi kwamba walikuwa wakifanya nini mahali pale lakini baada ya kuona vitambulisho vyao akagundua kwamba walikuwa ni maofisa wa FBI waliofika mahali pale kwa ajili ya kumkamata.
Moyo wake alikuwa na huzuni kubwa, hakujua kwamba maisha yake yangeishia kukamatwa na maofisa hao ambao mpaka muda huo hawakuzungumza kitu chochote kile.
Baada ya kumwangalia kwa sekunde kadhaa, wakawaambia madaktari kwamba walitakiwa kuondoka naye kwani kulikuwa na mambo mengi walitaka kumuhoji, mahojiano hayo yalitakiwa kufanyika sehemu maalumu na si hapo hospitali.
Hilo halikuwa tatizo, wakaruhusiwa na kuondoka naye. Ndani ya gari, Fareed alikuwa kimya, tumbo lake liliacha kuuma, kichwa chake kilikuwa kikifikiria mambo mengi kwa wakati huo.
Hawakuchukua muda mrefu, gari hilo likaingizwa ndani ya jumba moja kubwa, lilikuwa na bango kwa nje lililoandikwa Federal Bureau of Investigation (FBI). Liliposimama, wakateremka, wakamchukua na kuelekea naye ndani ya chumba kimoja ambacho kilikuwa na viti viwili, meza moja na pia kulikuwa na kioo kikubwa ambacho wewe haukuweza kumuona mtu wa upande wa pili lakini yeye alikuona vizuri tu.
Thomson ndiye aliyekuwa na wajibu wa kumuuliza Fareed maswali. Kwa jinsi alivyomwangalia, Fareed hakuonyesha dalili za kufanya matukio ya kigaidi, alionekana kuwa mtu mpole sana ambaye hakuwahi kuchinja hata kuku.
Thomson alimwanzia mbali na mwisho kabisa kumuuliza kuhusu kituo kile. Fareed hakutaka kuficha, alitaka kusimulia ukweli juu ya kila kitu kilichotokea.
Simulizi yake ilianza mbali kabisa, tangu alipokuwa ameanza mchezo wa kuingiliwa kimaumbile, alipokutana na Godfrey Kidatu mpaka siku ambayo alianza kujiuza nje ya nchi.
Thomson alikuwa kimya akimwangalia. Fareed hakutaka kuficha kitu chochote kile, alisimulia uchafu wote aliofanyiwa na mabilionea mpaka kufikia hatua ya kutaka kumuua. Alimwambia pia kuhusu magaidi waliokuwa wamemchukua na kumpa bomu na wakati hakuwa akitaka kwenda kufanya tukio lolote lile.
“Kwa nini ulikuwa unakimbia?” aliuliza Thomson.
“Nilikimbia kwa sababu niliacha bomu kule chooni. Sikutaka kufa kwa kuwa kulikuwa na kazi kubwa mbele yangu,” alijibu Fareed.
“Haukujua kama ulibeba bomu?”
“Sikujua! Nilitaka kuuliza lakini maneno yao yalinifanya kubaki kimya. Nilikwenda chooni ili nione kulikuwa na nini kwani begi lilikuwa na uzito usio wa kawaida,” alisema Fareed.
Alieleza kila kitu mpaka Bilionea Williams alivyotaka kumtumia kumuua Belleck. Mahojiano hayo yalichukua saa moja, akapelekwa katika chumba kimoja na kuambiwa kukaa huko.
Fareed alikuwa kimya ndani ya chumba hicho, alikaa katika pembe ya chumba kile, alionekana kuwa na mawazo tele lakini moyo wake ulifarijiwa na kile alichokuwa amekifanya. Alijipongeza kwa kuwa alifanikiwa kuwaua watu wote ambao walisababisha maumivu katika maisha yake.
Baada ya saa moja mlango ukafunguliwa, wanaume wawili wakaingia na kumtaka kuwafuata. Hakubisha, akafanya hivyo na kwenda mpaka katika kile chumba, akawekwa mezani ambapo kulikuwa na karatasi pamoja na kalamu na kuambiwa kwamba alitakiwa kuandika kila kitu kuhusu kile alichokuwa amekutana nacho katika suala zima la ugaidi pamoja na kuwataja watu waliompa bomu na mahali walipokuwa wakiishi hapo Marekani na Uturuki.
“Hii ndiyo nafasi yako,” alisema Thomson.
Hilo halikuwa tatizo, baada ya kuambiwa hivyo, akaanza kuwaambia kila kitu. Hakuwa mgeni nchini Marekani, alizifahamu sehemu nyingi hivyo hata kuwaambia mahali wale watu walipokuwa ilikuwa kazi nyepesi sana.
Huo ulikuwa msaada mkubwa kwa FBI, walifanikiwa kwa kiasi kikubwa kupata majina ya watu hao na mahali walipokuwa wakiishi hapo Marekani na Uturuki.
“Tunashukuru sana!” alisema Thomson.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hakujua hatima ya maisha yake, alishukuriwa lakini watu hao hawakumwambia kwamba alitakiwa kuondoka au kubaki mahali hapo. Hakukuwa na mtu aliyeshughulika naye tena ila baada ya siku tatu akapewa taarifa kwamba kila kitu kilikuwa tayari, magaidi wote walikuwa wamekamatwa tena huku wakiwa na ramani ya Marekani kwa maana ya kutaka kulipua tena.
“So, what about me?” (kwa hiyo vipi kuhusu mimi?) aliuliza Fareed.
Hakukuwa na mtu aliyemjibu, aliendelea kuwekwa ndani ya chumba kile kwa siku kadhaa. Alipofikisha wiki ya pili akaanza kuumwa tena tumbo, akaanza kutapika damu kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma.
Wakati huu hali yake ilikuwa mbaya zaidi, alitapika madonge ya damu kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma. Wakamtoa ndani ya chumba kile na kumpeleka hospitalini ambapo akaanza kupatiwa matibabu.
Hali yake haikutengemaa, utumbo ulishambuliwa sana na kansa kiasi kwamba mpaka madaktari wenyewe walishangaa na kusema kwamba ilikuwa ni vigumu sana kwa Fareed kupona, kwani utumbo wake ulibadilika mpaka rangi, ukawa na rangi nyeusi tii.
“This man is going to die,” (huyu jamaa anakufa) alisema daktari huku akimwangalia Thomson.
Kila mmoja alibaki kimya, utumbo ukapigwa picha, ulikuwa kwenye hali mbaya kupita kkawaida, ulishambuliwa kwa kiasi kikubwa na kusingekuwa na uwezekano wa kufanya muujiza wowote ule labda kama wangempokea kabla ya tatizo hilo kuanza wangemuwekea mpira, ila kwa pale alipofikia, hawakuwa na jinsi.
Siku ya tarehe 26.08/2016 ndiyo siku ambayo Fareed akafariki nchini Marekani huku akiwa kwenye maumivu makali. Ulikuwa msiba mzito kwa marafiki zake lakini hata maofisa wenyewe wa FBI walihuzunika, hawakutaka kabisa kumpoteza Fareed kwani aliwasaidia kupambana na magaidi kwa asilimia tisini.
Taarifa hiyo ikatolewa kwenye televisheni, mawasiliano yakafanyika na FBI wenyewe ndiyo walioshughulikia safari ya kuusafirisha mwili wake kuelekea nchini Tanzania ambapo baada ya kuwakabidhi ndugu, wakawaachia kiasi cha dola laki tano ambazo ni zaidi ya milioni mia tano kama shukrani kwa kila kitu alichokifanya Fareed kwao.
Huo ukawa mwisho wake, mchezo wa kuingiliana na wanaume wenzake ukayagharimu maisha yake, akafa katika maumivu makali. Akaunti yake ilikuwa na pesa nyingi, zaidi ya bilioni ishirini lakini zote akaziacha kwa ndugu ambao kwenye kugawana tu mpaka wengine wakauana, na pesa nyingi zilikuwa zile alizopewa kama zawadi na Bilionea Williams ambaye alikuwa akitumia kifungo cha maisha gerezani kwa kosa la kuhusika na mauaji ya Bilionea Belleck.
Huo ukawa mwisho wake, marafiki zake walimkumbuka, watu aliotembea nao wakamkumbuka, aliacha historia, mbali na mchezo mchafu aliokuwa ameufanya, wema wake, ucheshi na roho yake nzuri viliendelea kuwa mioyoni mwa watu wengi.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment